UKWELI WA SHIA ITHNA ASHARIYA
SEHEMU YA TANO
NDOA YA MUDA
Ndoa ya muda ambayo inajulikama vile vile kama ndoa ya "Mut'a," nayo ni mwanamke kuozesha nafsi yake kwa mwanamme kwa mahari maalumu na kwa muda maalumu, kwa kufunga ndoa iliyotimiza masharti Sahih ya kishariah. Tamko lake ni mwanamke kumwambia mwanaume baada ya maafikiano na maridhiano juu ya mahari na muda: "Zawwajtuka nafsi bimahri qadruhu kadha ilal-ajalil-maalum" (Nimekuoza nafsi yangu kwa mahari kadha kwa muda maalumu), na muda unabainishwa wazi. Na jibu la mwanaume linakuwa haraka "Qabiltu" (Nimekubali).
Na wakala unajuzu katika ndoa hii kama ilivyo katika mikataba mingine. Na kwa kukamilika masharti ya ndoa, mwanamke anakuwa ni mke wa mwanaume na mwanaume anakuwa ni mume wake hadi mwisho wa muda uliopangwa katika ndoa. Na wanaweza kuongeza muda mwingine, na ni wajibu kwa mke akae 'Iddah baada ya kumalizika muda kwa tohara mbili (hedhi mbili) kama anapatwa na hedhi, vinginevyo ni kwa muda wa siku arobaini na tano. Na mtoto wa mut'a awe ni mvulana au binti ananasibishwa kwa baba yake.
Na Waislamu pamoja na khitilafu za madhehebu yao wanaafikiana na aina hii ya ndoa, ndoa hii ni katika mambo yalioanza tangu mwanzo wa Uislamu na kwayo imeteremka Ayah:
فَمَا اسْتَمْتَعْتُم بِهِ مِنْهُنَّ فَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ فَرِيضَةً ﴿٢٤﴾
"Kwa mlio jifurahisha nao miongoni mwao basi wapeni mahari yao
.” (An-Nisaa 04:24)
Na wamefasiri wengi wa wafasiri wa Ahl as-Sunnah Al-Istimtai katika Ayah hii kwa ndoa ya Mut'a na Ibn 'Abbas na 'Ubay bin Kaab na Sa'id bin Jubair walikuwa wanasoma Ayah hii "Fama-stamta'atum bihii minhunna ilaa ajalim-musammaa fa'tuuhunna ujuurahunna."
Amesema Ibn Kathir katika tafsiri yake akielezea hilo "na jambo ambalo liko mbali sana, ni hawa kuamini kupotoshwa kwa Qur'an, hivyo ni lazima kwa lililokusudiwa na wala sio kusoma"
na kuteremka Ayah hii katika ndoa ya Mut'a ni katika ambayo hayapasi kuwa ni maudhui ya mjadala, bali mjadala ni kuwa Ayah hii ni Mansukh au sio Mansukh? yaani imeharamishwa baada ya kuhalalishwa kwake au imebakia katika hali yake?
Mwanzo tunaeleza baadhi ya yaliopokewa katika Hadith zinazothibitisha ndoa ya Mut'a, kuwa ni ya kisheria katika Uislamu miongoni mwa aliyopokea Bukhari katika Sahih yake.
Kutoka kwa 'Abdillah amesema tulikuwa tukipigana vita pamoja na Nabii
na hatukuwa na wanawake basi tukasema Je tufanye ponyeto (tujichue wenyewe)? Akatukataza hilo, akaturuhusu baada ya hapo kuoa mke kwa kumpa nguo - kisha akasema: "Enyi mlioamini msiharamishe mazuri aliyo wahalalishia Allah (s.w.t)."
Na Hadith ifuatayo inathibitisha bila ya shaka yoyote kwamba Mtume amefariki bila ya kuharamisha ndoa ya Mut'a na kwamba aliyekataza ni mtu mwingine baada ya kufariki kwa Mtume Muhammad Mustafa
. Amesema Ayah ya Mut'a imeteremka katika Kitabu cha Allah (s.w.t) na haikuteremka Ayah ya Qur'an ya kuiharamisha na kuikataza mpaka akafariki, Mtu (fulani) akasema kwa maoni yake aliyoyataka.
Na 'mtu' anaye ashiriwa katika Hadith iliyotangulia, si mwingine isipokuwa ni 'Umar al-Khattab, ambaye imethibitika kuwa yeye ndiye aliyeharamisha ndoa hii kama ilivyokuja katika Sharh ya Al-Baari katika Sahih Bukhari - angalia maelezo yake chini kwa tarjuma ya Kiingereza.
Na imekuja katika Sahih Bukhari vile vile katika Babu al-Tamattu' 'alaa ‘ahdi rasulilah
: ametusimulia Musa bin Isma’il, ametusimulia Hamaam kutoka kwa Qatadah amesema, amesimulia Mutarifu kutoka kwa Imran amesema: Tulifanya Mut'a wakati wa Mtume wa Allah
na Qur'ani ilishuka (juu ya hilo), na mtu (fulani) akasema kwa maoni yake anayoyataka.
Ni uwazi ulioje wa vipi mtarjum alivyopiga chenga kwa kuifanya kwake kuwa ni mahsusi kwa Tamattu iliyopokewa katika riwayah ya Imran kuwa ni Haji-Tamattu na wala sio Mut'a ya wanawake. Vyovyote iwavyo kilicho muhimu kwetu ni kile kilichopokewa katika Sahih Bukhari tu, na kuashiria kwetu katika tarjuma haikuwa isipokuwa ni kudhihirisha alicho kinukuu mtarjum kutoka sharh ya Al-Baary katika Sahih Bukhari, na hasa kwa mwanamme asiyejulikana katika riwayah. Na yanatiwa nguvu kwa aliyo mwanamme asiyejulikana katika riwayah. Na yanatiwa nguvu kwa aliyo yapokea Muslim katika Sahih yake kwa Isnad ya Ibnun-Nadhar amesema: “Ibn ‘Abbas alikuwa anaamrisha Mut’a na Ibn Zubeir alikuwa anaikataza basi nikaeleza hilo kwa Jabir.”
Akasema:”Tulifanya Mut’a pamoja na Mtume wa Allah
na alipotawala ‘Umar akasema: “Hakika Allah (s.w.t) anahalaisha kwa Mtume wake anayoyataka, basi timizeni Hijja na Umra na acheni kuoa hawa wanawake, sitoletewa mwanamme aliyeoza mwanamke kwa mwanamme isipokuwa nitampiga kwa mawe.”
Na katika Sahih Tirmidhi kutoka kwa 'Abdallah bin 'Umar aliulizwa na mtu kutoka katika watu wa Sham juu ya Mut'a ya wanawake, akasema: "Ni halali", akasema: "Hakika baba yako alikwishaikataza." Ibn 'Umar akasema: "Unaonaje kama baba yangu amekataza na Mtume
ameifanya, utaacha Sunnah na kufuata kauli ya baba yangu?"
Vile vile katika Sahih Muslim kumepokewa: "Kisha wakataja Mut'a, akasema kweli tulifanya Mut'a wakati wa Mtume wa Allah
, Abubakr na 'Umar."
Na imekuwa mashuhuri kwa hibril-ummah 'Abdallah bin 'Abbas (r.a.) kwa rai yake kuwa Mut'a haikufutwa kama anavyopokea hayo Al- Zamakh'shariy katika Tafsiri yake Al-Kashaaf, ambapo ananukuu kutoka kwa Ibni 'Abbas kwamba Ayah ya Mut'a ni katika Muhkamaati, na vile vile katika Sahih Bukhari kuna yanayotilia mkazo hayo.
Amesema: "Nilimsikia Ibn 'Abbas anaulizwa kuhusu mtumwa wake akamwambia: 'hakika hiyo ni katika hali ngumu na wanawake wakiwa ni wachache au mfano wa hayo?’. Ibn Abbas akasema: “Ndiyo.” [234]
9 Pamoja na uwazi wa dalili hizo ni kama vile uwazi wa jua katikati ya mchana kuhusu kuendelea uhalali wa ndoa ya Mut’a.
Watu wengi katika Ahl as-Sunnah wako kinyume na hayo, lakini Ayah ambayo ni maalumu katika ndoa hii wanadai kuwa imefutwa na wamehitilafiana kuhusu Ayah iliyo ifuta, kati yao wanasema imefutwa na Ayah iliyopo katika Qur'an, na kati yao wanasema iliyofuta ni riwayah zilizopo kati ya Hadith. Tunajibu rai zote mbili kwa Hadith zilizothibiti ambazo zimetangulia, na ambazo zinaonyesha kufariki kwa Mtume
bila ya kukataza, na wale waliosema iliyofuta ni Ayah katika Qur'an nayo ni:
وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾ إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾
"Na wale ambao wanahifadhi tupu zao isipokuwa kwa wake zao au iliyowamiliki mikono yao ya kuume
.”(Al-Mu’minun 23:5-6).
Inatosha kujibu rai yao hii kwa kutazama katika Ayah hii ambayo wanadai kuwa imefuta Ayah ya Mut'a, Ayah hii ni Makki (yaani imeshuka Makkah) na Ayah ya Mut'a ni Madani (yaani imeshuka Madina) na hukumu ya kisheria ya ndoa ya Mut'a ni madani (yaani imeshuka baada ya Ayah ya (na ambao wanahifadhi tupu zao...) na Ayah iliyotangulia haifuti inayokuja baada yake.
Ama aliyesema iliyofuta ni Hadith zilizopokewa kwa Mtume(s.a.w.w)
, hakika Hadith hizo wanazozidai kuwa zimefuta, zinapingana zenyewe kwa zenyewe, baadhi yake zinasema imefutwa katika Khaibar na nyingine katika Autasi, ya tatu inasema ni katika siku ya Fath Makkah, na ya nne katika vita vya Tabuk na ya tano ni katika Umrah ya Qadhaa, ya sita ni katika Hajjat tul-Wida'a.
Kugongana na kupingana kwa riwayah hizo sio kwengine ila ni kuonyesha dalili ya kutokuwa ni Sahih, hayo ni pamoja na kuongezea kuwa riwayah hizo. Haziepukani na kuwa kwake ni Hadith za Ahaad, ambazo hazifai kuwa ni zenye kufuta hukumu ambayo imeletwa na Qur'an, na Shariah yake imethibiti kwa kongamano la Waislamu wote, kwa sababu Naasikhi haipatikani kwa habari ya mtu mmoja kwa ijmai, na Ayah haifutwi isipokuwa na Ayah kwa dalili ya kauli ya Allah (s.w.t):
مَا نَنسَخْ مِنْ آيَةٍ أَوْ نُنسِهَا نَأْتِ بِخَيْرٍ مِّنْهَا أَوْ مِثْلِهَا ﴿١٠٦﴾
"Hatufuti Ayah au kuisahaulisha isipokuwa tutaleta iliyo bora zaidi au mfano wake
.”(Al-Baqarah 02:106)
Na ambacho kinaweza kuwa ni kisingizio cha ijtihad ya 'Umar katika kuharamisha ndoa ya Mut'a ni kwamba, mmoja wa Waislamu jina lake ni 'Amr bin Harith alitumia vibaya Shariah hii, hivyo akachokoza hasira za 'Umar na ikampelekea kuharamisha huku. Na dalili kuhusu haya ni riwayah ambayo ameipokea Muslim katika Sahih yake kutoka kwa Ja'abir: "Tulikuwa tunafanya mut'a kwa kutoa kiasi cha tende na unga wakati wa Mtume(s.a.w.w)
na Abubakr na Umar, mpaka alipokataza kutokana na jambo la 'Amr bin Hurayth.
Na ameitoa Tabarani na Tha'alabi katika tafsiri zao kwa isnad ya Al- Imam 'Ali ibn Abi Talib
amesema: "Kama asingekataza 'Umar Mut’a, basi asingezini isipokuwa mwovu.”
Na katika riwayah nyingine isipokuwa wachache.
Baada ya riwayah zote hizi ambazo zinathibitisha hukumu ya ndoa ya Mut'a, na Mtume Muhammad Mustafa
kutoikataza, na kubaki kwake halali hadi alipoharamisha 'Umar wakati wa ukhalifa wake, hatupati ufumbuzi wa tatizo hili, isipokuwa 'Umar amefanya ijtihad kwa rai yake kwa ajili ya maslahi aliyoyaona - kwa mtazamo wake - kwa Waislamu katika wakati wake na siku zake, yaliyo sababisha kuzuia kufanya Mut'a.
Kuzuia huko ni kwa kijamii na wala sio kwa kidini kwa ajili ya maslahi ya muda, kwa sababu 'Umar ana cheo kikubwa na alikuwa na daraja kitawala, hawezi kuharamisha alichokihalalisha Allah (s.w.t) au kuingiza kitu katika dini naye anajua kuwa halali ya Mtume Muhammad Mustafa
ni halali hadi siku ya Qiyamah, na haramu ya Mtume Muhammad Mustafa
ni haramu hadi siku ya Qiyamah.
Hivyo ni lazima makusudio yake ya kukataza yawe ya muda na ni kuharamisha kwa kijamii na wala siyo kwa kidini. Na msimamo wake huu mkali katika jambo la ndoa ya Mut'a sio wa kwanza katika aina yake kwani amejulikana kwa ukali na ugumu katika mambo yake yote. Anafanya ijtihad katika hilo kwa kutaka kupata maslahi bora zaidi - kwa mtazamo wake - kwa ajili ya Uislamu na kusimamisha Shariah. Na miongoni mwa mifano katika ijtihad ya 'Umar katika hukumu na ukali wake, ni amri yake kwa Waislamu kusali Sala ya Ramadhani (tarawih) katika jamaa baada ya kuwa inasaliwa furada (mmoja mmoja) wakati wa Mtume wa Allah
.
Kutoka kwa Abu Huraira: "Hakika Mtume wa Allah (s.a.w.w.) amesema mwenye kusali Sunnah ya Ramadhani kwa imani na kutaka thawabu anasamehewa yaliyo tangulia katika dhambi zake." Ibnu Shihab amesema: "Mtume wa Allah
amefariki na watu wanafanya hivyo, kisha mambo yalikuwa vivyo hivyo katika zama za Abubakr na mwanzo wa zama za 'Umar (r.a.)."
Akasema (Ibn Shihab): "Nilitoka pamoja na 'Umar Al-Khattab usiku wa mwezi wa Ramadhani kwenda msikitini basi tukakuta watu wametapakaa na wametawanyika, kila mtu anasali peke yake na mtu anasali na kundi linasali nyuma yake, 'Umar akasema mimi naona kama nitawakusanya hawa kwa msomaji mmoja ingekuwa ni bora.
Kisha akaazimia, akawakusanya kwa 'Ubay bin Ka'ab, kisha nilitoka pamoja naye usiku mwingine na watu wanasali kwa sala ya msomaji wao, 'Umar akasema: "Bida'a nzuri ni hii na wale wanaolala (wakasali usiku) ni bora kuliko wanaoisali (sasa), amekusudia mwisho wa usiku na watu walikuwa wanasali mwanzo wa usiku.”
Vile vile amefanya ijtihadi katika Sunnah hiyo ambayo imeitwa sala ya tarawih kwa kuongeza idadi ya raka'a zake hadi kufikia ishirini. Kutoka kwa 'Abdurahman kwamba amempa habari kwamba yeye alimwuliza 'Aisha Sala ya Mtume wa Allah
ilikuwaje katika mwezi wa Ramadhani?" Akasema: "Mtume wa Allah
hakuwa anazidisha katika Ramadhani wala katika mwezi mwingine zaidi ya raka'a kumi na moja."
Lakini baadhi ya walioishi wakati wa khalifa na walio kuja baada yake baadhi ya muhadithin wajinga, waliona ni jambo kubwa mno kuwa ameharamisha alichokihalalisha Allah (s.w.t) na wakalazimika kutoa kisingizio kwa ajili ya hilo. Hivyo hawakupata isipokuwa madai ya nasikh kutoka kwa Nabii baada ya kuhalalishwa, basi wakagongana mgongano huo na kauli zao zikapingana mpingano huo.
Tazama riwayah ifuatayo ili uone upeo wa mgongano na mgawanyiko ambao tunauzungumzia, na mshangao ni kwamba wazushi wa riwayah hiyo wameinasibisha kwa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib
na watoto wake.
Kutoka kwa Zuhri kutoka kwa Hassan na 'Abdillah watoto wa Muhammad bin 'Ali kutoka kwa baba yao: Hakika Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib
aliambiwa kuwa Ibn 'Abbas haoni ubaya wa Mut'a ya wanawake, akasema: 'Hakika Mtume wa Allah
ameikataza siku ya Khaibar, pamoja na nyama ya punda wa nyumbani', na baadhi ya watu wakasema na kama atafanya hila hadi akafanya Mut'a basi ndoa itakuwa ni batil na baadhi yao wamesema: "Ndoa inajuzu na sharti litakuwa batili."
Kama hawa wangefahamu sababu ya khalifa kukataza Mut'a hilo lingewatosha kutokana na mgawanyiko na kutokuendelea.
Hakika mtazamo wa ndoa ya Mut'a uliotangulia ulikuwa ni kwa pande mbili; kidini na kihistoria. Ama mtazamo katika upande wa tabia ya kijamii kuhalalishwa kwake kumekuja kuwa ni rehema kwa wanaadamu na ruhusa kwa walio wengi, na hasa wanaosafiri kwa kutafuta elimu au biashara au wanaopigana jihadi au wanajeshi pamoja na kushindwa kwao kuoa ndoa ya daima, kwa vile mara nyingi kuna vipengele na vitu ambavyo haviendani na hali ya wasafiri, hasa ambao wako katika umri wa ujana na mchemko wa shahawa.
Kwani hali yao haiepukani na mambo mawili, ima subira na kubana nafsi ambako kunasababisha matatizo ambayo yanaleta maradhi ya kudumu na magonjwa ya kinafsi yenye kuangamiza, na mengineyo katika madhara ambayo hayafichikani kwa yeyote, na ima kutumbukia katika zinaa ambayo imejaza dunia kwa ufisadi na madhara. Na imepokewa kutoka kwa Ibn 'Abbas kuhusu suala hilo; " Mut'a haikuwa isipokuwa ni rehema ya Allah (s.w.t) ameuhurumia ‘Ummah wa Muhammed na kama sio kukataza kwake (yaani ‘Umar) asingezini isipokuwa mwovu.”
Na katika yanayotia mkazo dharura ya kitabia na kijamii kwa kuhalalisha aina hii ya ndoa ya muda, ni ambayo baadhi ya Waislamu wametoa Fatwa katika wakati ambao tunao kwa kuruhusu ndoa ya aina nyingine inayomrahisishia msafiri peke yake kutatua matatizo yake katika hali ya kutoweza kuoa ndoa ya daima, na sifa ya ndoa hii ni ya muda kwa upande wa wanaume na ni ya daima kwa upande wa wanawake. Na aliyo kusudia mume katika nafsi yake bila ya yeyote kujua unapomalizika muda, anamshitusha mke wake masikini kwa kumpa talaka.
Hivyo aina hii ya ndoa wameipa jina la "Ndoa kwa nia ya talaka (kuachika)," pamoja na kutambua wale waliozua kuwa huo ni uongo kwa mke na ni udanganyifu na hakuna dalili juu ya hilo katika Kitabu wala Sunnah ya Mtume Muhammad Mustafa
lakini wao wanafanya kwa hoja ya kuwa madhara yake yatabaki yamefichikana kuliko ufisadi wa zinaa. Yote ni kwa kuwa wao wameamini kubatilika kwa ndoa ya Mut'a ambao uhalali wake umekuja katika Kitabu kitukufu na Sunnah za Mtume na kwa kufanya hivyo watakuwa wamebadilisha bida'a walioizua na hukumu ya Allah (s.w.t). "Je mnabadilisha ambacho ni duni kwa kile kilicho bora." Fala haula wala Quwata illa billahi.
Mut'atul Hajj
Mtume amekwisha ifundisha na akaamuru kutokana na kauli ya Allah (s.w.t) Mtukufu: “Basi atakayefanya umrah ya hijja, hiyo ni kwa ambaye familia yake haiko karibu na Msikiti Mtakatifu wa Makkah.” (Al-Baqarah 02:196)
Na makusudio ya hayo ni 'Umrah katika miezi ya hijja kabla ya hijja, nayo ni faradhi kwa ambaye familia yake iko mbali na Makkah. Na imeitwa Tamattu ya hijja kwa yale yaliyomo humo katika kujifurahisha, (yaani raha ya kuhalalishiwa makatazo ya Ihraam katika muda uliopo baina ya Ihraam mbili - Ihraam ya umrah Tamattu na Ihraam ya hijja. Na hayo ni ambayo 'Umar aliyachukia pia, na akayakataza pamoja na kuwa Mtume(s.a.w.w)
alifariki bila ya kukataza.
Kutoka kwa Sa'id bin Mussayib amesema: "Ali
alikhitilafiana na 'Uthman na wao wako katika kuhirimia 'Umrah Tamattu. 'Ali
akasema: 'Hataki isipokuwa kukataza jambo alilolifanya Nabii
.' 'Ali
alipoona hivyo akahirimia zote mbili."
Kutoka kwa Al-Hakim amesema: "Niliwaona 'Ali
na 'Uthman , na (huku) 'Uthman anakataza Mut'a na kuunganisha baina yake, 'Ali
alipoona akapaza sauti kwa vyote viwili: " Labayka bi umrati wa hajjati. " Akasema: 'Sikuwa ni mwenye kuacha Sunnah ya Nabii kwa kauli ya yeyote.”
Ama udhr wa 'Uthman katika rai yake hiyo ni kwa kuwa yeye alikubali sharti kabla ya kupewa bay'a ya kuwa khalifa, Abdulrahman bin 'Auf alitoa sharti kwa wosia kutoka kwa 'Umar, ahukumu kwa Kitabu cha Allah (s.w.t)
Sunnah za Nabii wake na kwa mwenendo wa masheikh wawili kama ilivyo tangulia katika sehemu iliyo tangulia. Na imepokewa kwa tawatur kauli ya 'Umar: "Mut'a mbili zilizo kuwepo wakati wa Mtume wa Allah
mimi nazikataza” [243]
18 na anakusudia kwa kauli yako hiyo Mut’a ya wanawake na Mu’ta ya Hijja.
Na maneno ya 'Umar yanadhihirisha uamuzi wa hukumu hizo ni wake,na wala sio wa mwengine, kwani yeye anakiri kuwa Mut'a mbili zilizokuwa katika wakati wa Nabii
.
Na hakunasibisha kukataza kwake kwa Mtume bali amekataza yeye mwenyewe kwa kauli yake "na mimi nakataza" na Allah (s.w.t) amrehemu aliyesema kuhusu Hadith ya mwisho kuhusu 'Umar "Tumekubali ushahidi wake lakini hatujakubali kuharamisha kwake."