BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE
KIMEANDIKWA NA: MUHAMMAD IBRAHIM EL-QAZWINIY
Tofauti Ya Mwanamke Mwenye Hijabu Na Asiye Na Hijabu.
Mmoja wa marafiki zangu alinisimulia tukio la kufurahisha lililomtokea Muumini mmoja wa kiislamu. Tukio hili lilikuwa kama ifuatavyo. Siku moja Muumini huyo alikuwa akitembea pamoja na mkewe aliyekuwa kavaa Hijabu. Matembezi hayo yalimfikisha katika moja ya bustani zinazotembelewa na watu wa aina tofauti.
Ghafla Muumini huyo alijiwa na mtu fulani ambaye naye alikuwa na mkewe. Mke wa mtu huyu hakuwa amevaa vazi la Hijabu na hivyo basi kwa dharau na kejeli alimwambia yule Muumini. "Kwa nini umemvalisha mkeo Hijabu, kwa nini hukumuacha akatoka bila Hijabu kama jinsi alivyo mke wangu? Hijabu ina faida gani?" Jawabu alilotoa Muumini yule lilikuwa la kushangaza na la kishujaa. Alimwambia. "Je unafahamu tofauti ya mwanamke mwenye Hijabu na asiyekuwa na Hijabu? Bwana yule mwenye kejeli akasema "Nini tofauti yake?" Yule Muumini akajibu kwa njia ya kuuliza, je, kuna tofauti gani baina ya taxi na gari ambalo mtu hulitumia yeye binafsi? Yaani kwa matumizi yake pekee yake." Bwana yule akajibu akasema, "Taxi hutumiwa na kila mtu, wakati ambapo gari maalum linamuhusu mwenyewe peke yake. Hii ndiyo tofauti iliyopo." Basi yule Muumini akasema, "Hali hiyo ndio iliyopo baina ya mwanamke aliyevaa Hijabu na yule asiye na Hijabu.
Mwanamke asiye na Hijabu ni sawa na taxi ambayo kila mtu anaweza kuikodisha na kuitumia. Mwili wa mwanamke huyo huwa wazi na kuonesha mapambo yake na uzuri wake, na kuwafanya watu wavutike kutokana naye, jambo ambalo linaweza kusababisha kutendewa maovu, kama ambavyo mara kwa mara hali hii inavyowapata wanawake wa aina hii. Ama mwanamke aliyevaa Hijabu yeye ni bibi aliyemtukufu, ni maalum kwa ajili ya mumewe, mapambo yake na uzuri wake havionekani kwa kila mtu. Pia watu wenye nyoyo chafu na dhaifu hawamuangalii, na uso wake na mapambo yake havikutani na macho yenye khiana, kwa kuwa amehifadhiwa ndani ya Hijabu. Kwa hiyo utukufu wa mwanamke huyu na mwili wake vimo ndani ya hifadhi bora, pia bibi huyu hupendwa na kupendeza mbele ya mumewe na kumfanya mume kuwa na imani na mkewe, kwa sababu ya hifadhi hiyo inayomkinga kuwa na mahusiano na watu wengine kwa njia mbaya." Baada ya maelezo yaliyotolewa na yule Muumini wa kiIslamu, bwana yule mwenye kejeli aliona haya na akaanza kumwambia yule Muumini, "Najuta kwa kukuudhi, kwani maneno yako ni ukweli mtupu, na mifano uliyonipa ni sawa kabisa naomba samahani kwa haya niliyokutamkia na pia natubia kwa Mwenyezi Mungu kwa kitendo nilichokitenda na sasa. Kabla bwana huyu hajamaliza kujieleza mkewe alimkatiza na kusema. "Naam, naapa maneno haya aliyosema bwana huyu ni sawa na mfano aliotoa ni mzuri sana, kwani kabla ya leo nilikuwa sijasikia mawaidha kama haya. Mfano huu umeniingia moyoni nami pia natubia kwa Mwenyezi Mungu."
Baadaye yule mume akarudia kukamilisha usemi wake akasema, "Na mimi sasa naiamini Hijabu na kuanzia leo mke wangu ataingia katika uwanja mtukufu kwa kuvaa Hijabu. Kamwe sikubali mke wangu atoke bila Hijabu, kwani ndiyo vazi la amani na imani. Nafsi yangu haipendi kabisa kumuona mke wangu akidhihiri mbele za watu kama kwamba yeye ni kwa ajili ya kila mtu."
Ni Lipi Lengo La Wanaopinga Hijabu?
Baada ya kuusoma Uislamu kwa undani, maadui wa Uislamu wameandaa mikakati ya kuuangamiza Uislamu na Waislamu kidogo kidogo, bila Waislamu kuigundua hali hii isipokuwa wachache. Na miongoni mwa mikakati yao ya kishetani katika kutilia mkazo kuiondoa Hijabu, wametumia na bado wanatumia kila njia za kuvutia na madai batili kutimiza lengo lao hilo. Kuna mambo mengi machafu wanayoyaeneza katika jamii ya Waislamu, chini ya kiza kinene chenye ibara zinazovutia na kampeni ambazo matokeo yake ni mabaya. Kwa kutumia mbinu za kimaendeleo na utaalamu, wamefaulu kuwapotosha Waislamu, na wakasambaza uovu mwingi. Kwa madai hayo hayo ya maendeleo na kupigania uhuru na haki za binadamu, uchafu wao umeenea ndani ya jamii zetu za kiislamu. Kwa hakika wamefaulu kuzinyang'anya jamii zetu maumbile ya kuwa na haya na heshima. Ibara hizi zimewahadaa Waislamu wengi, wake kwa waume.
Masikini Waislamu hawa wamekuwa wafuasi wa itikadi hizi zenye sumu kali inayovuja kuelekea kwenye maovu na maangamio. Wanawake wa kiislamu na mabinti wa kiislamu wanafanya upinzani hadharani dhidi ya vazi hili la kiislamu. Wametoka katika nyumba ya utukufu na imani na kuingia katika nyumba ya kiza na upotovu. Wanawake wetu na wasichana wetu wameathiriwa na mavazi ya Kiyahudi na Kikristo yatokayo kwa wapinzani wa kimagharibi na makafiri wa mashariki. Maadui na wavamizi hawa wamefanikisha kwa kiasi kikubwa lengo lao, kwa kuwa sasa hivi jamii ya kiislamu imekwisha tumbukia na kuzama katika dimbwi la matendo machafu. Jamiii ya kiislamu ambayo asili yake ni adilifu na yenye muruwa, leo imegeuka na kushika bendera ya maovu ya kila aina.
Matukio ya kubaka,
kupora, udanganyifu, dhulma, kutoa mimba na mengineyo, yameivamia jamii yetu tukufu. Watu hawa wa Ulaya magharibi na mashariki yake, hawali wakashiba wala hawalali wakapata usingizi, ila mpaka watimize lengo lao la kutuachisha utamaduni wetu wa kiislamu.
Ni wazi kabisa kwamba watu hao wanaomtaka mwanamke wa kiislamu avue Hijabu lengo lao wanataka wamuone mwanamke huyu anafanya ufisadi kwa kumlazimisha akae uchi. Nia yao ni kumuangamiza na kuipotosha jamii kwa jumla. Kumtaka mwanamke asivae Hijabu ni kumuondolea heshima yake na uchamungu wake.
Ewe msomaji wangu, iwapo utataka kuyafahamu vizuri maneno yangu, muulize mzee yeyote katika wazee wa makamo na mababu ambao bado wanayo kumbukumbu ya hali ya mambo ilivyokuwa hapo zamani. Waulize kwa kusema, "Hivi maovu haya yaliyopo sasa hivi ya kuwavunjia heshima wanawake na kuwabaka, na watu kudhulumia, mambo haya yakulikuwepo hapo zamani kabla ya miaka ishirini au thelathini iliyopita?" Watakujibu kwa nguvu zao zote, kwa kusema, Hapana kabisa hayakuwako."
Sasa yametoka wapi mambo haya maovu na matukio ya kuhuzunisha? Watakuambia, "Hali hii imetokana na mambo mengi, miongoni mwake ni wanawake wenyewe kutembea mabarabarani bila sitara ya kisheria."
Hili ndilo jibu sahihi kwa matatizo kama haya ya ubakaji ambayo takwimu zake zinaongezeka kila siku. Iwapo utataka uhakika zaidi, waulize wakazi wa miji michache ambayo wakazi wake bado wanashikamana na sheria za kiislamu na imani zao zingali hai na uwaambie, "Hivi katika miji yenu kuna matukio maovu ya kubaka na unyang'anyi kama inavyotokea katika miji mikubwa?" Bila shaka watakujibu hapana. Sababu kubwa ya kutokuwepo maovu kwa wingi katika sehemu hizo, ni kwa kuwa jamii bado inauheshimu na kuulinda Uislamu na kanuni zake zenye hekima.
Maovu mengi zaidi yanajitokeza katika miji au sehemu ambazo zinadai kuwa zimeendelea. Miji hiyo imehusika kwa kiwango kikubwa na ongezeko la maovu ambayo yanakithiri kwa kasi ya kutisha, licha ya serikali zao kutoa adhabu kali kwa wanaohusika kila wanapobainika na kukamatwa
.
Hali hii inaonyesha wazi kwamba kanuni peke yake hazitoshelezi, wala hazinufaishi katika kuirekebisha jamii, bali kinachotakiwa ni kuing'oa mizizi ya maovu kwanza, ili maovu hayo yapate kunyauka yenyewe. Kwa kawaida kila kitu kina asili yake, na asili ya maovu yaliyozikumba jamii zetu sasa hivi, ni hizi picha za video wanazooneshwa vijana wetu, picha ambazo huwa zinaonesha hali ya maumbile ya siri, isitoshe huonesha pia matendo ya jinsiya baina ya mke na mume bila kuona aibu wala huzuni kuuchezea na kuudhalilisha uanadamu ambao ni kitu cha thamani, kutokana na kuwa na uwezo wa kutambua nini cha kufanya na nini si cha kufanya. Kitu kingine kinachochangia ni nchi zetu zinaporuhusu uingizaji wa magazeti na majarida yanayochapisha picha zinazoonesha sehemu za siri na kisha magazeti hayo na majarida yanasambazwa katika jamii. Maadam asili ya maovu bado ipo kama mifano ya picha za video na majarida tuliyoyataja hapo kabla, basi maovu na matukio machafu yataendelea kutokea siku hadi siku, na kamwe hayataondoka kwa kutegemea kanuni hizi za kidunia.
Ni Yupi Mwanamke Bora
Sasa napenda kutoa mifano miwili ya wanawake wawili ambao kila mmoja anao mwelekeo wake na mwenendo tofauti na mwenzake, lakini wote wanaishi katika jamii moja. Wa kwanza ni yule mwanamke mwenye kuvaa Hijabu ambayo ni sitara ya imani na ni vazi la kiislamu, tena ni vazi la heshima na humpa utukufu mvaji.
Kwa kuvaa Hijabu, mwanamke huyu atakuwa amepata radhi za Mola wake na kupata utukufu wa watu wa peponi. Kwa vazi hili mwanamke huyu huvutia mvuto wa ucha Mungu na heshima. Pia dalili za utulivu hujitokeza kwa mwanamke huyu na dhana njema kwake hutawala fikra za kila amuonaye. Amtazamapo mwenye kumtazama, huwa ni shida kutambua, je, mwanamke huyu ni msichana au ni mtu mzima? Sura yake ikoje nzuri au la? Hutatizika wanaomuangalia. Matokeo yake watu humuangalia kwa jicho la heshima, hakuna awezaye kumkabili kwa maneno chafu au maudhi, kwani anafahamu wazi kwamba mwanamke huyo ameshikamana na dini yake na anaheshimu utu wake. Isitoshe mwanamke kama huyu huwa amejitenga na matendo ya aibu na kujiepusha na wanawake wasio na sitara, na kwa ajili hiyo hayuko tayari kuidhalilisha nafsi yake.
Huo ndiyo mfano wa mwanamke mmoja na namna alivyojiweka katika jamii yake. Kwa upande wa yule mwanamke wa pili, ni yule asiyejali kujisitiri uso wake amevua vazi la la stara, hana aibu wala haya. Kwa maana hiyo ameing'oa imani yake, kwa sababu Mtume anasema: "Mtu kuwa na haya ni sehemu ya imani, na mtu asiye na haya hana imani." Kwa mwenendo wake mwanamke huyu, huwa ni mpinzani mkubwa wa muongozo wa Qur'an na huwa anajidhalilisha kwa kuonesha mapambo yakem, kama walivyokuwa wakionesha mapambo yao wanawake wa zama za kijahiliya kabla ya kuja Uislamu. Isitoshe kwa mwanamke huyu, hali aliyo nayo huwa amejifananisha na wanawake wa Kiyahudi na Kikristo, na huwa yuko mbali na heshima yake na utu wake. Kutokana na kuudhihirisha mwili wake na uso wke na mikono yake, pia kifua chake na sehemu nyingine katika maumbile ya kike. Watu waovu na wenye tamaa huyaona wazi wazi maumbile yake na hapo tayari anakuwa mfano wa bidhaa zilizotandazwa sokoni, kwani kila mtu ana uhuru wa kuziangalia bila mipaka.
Matokeo ya uovu wa mwanamke huyu, ni kupata usumbufu toka kwa wahuni ambapo hatimaye wanaweza kumtendea matendo machafu yanayoweza kumharibia tohara yake. Na iwapo itafikia hali ya kuharibiwa tohara yake, basi atakuwa amepoteza heshima yake na utu wake katika jamii. Hii ni kwa sababu ameacha kuulinda mwili wake ndani ya vazi la kisheria.
Baada ya kuwa mmefahamu namna za wanawake hawa wawili sasa tuwe pamoja kaitka kulinganisha hali zao kati yao na tujiulize masuali yafuatayo.
1.Je ni yupi mwanamke bora baina yao?
2.Yupi kati yao ni mtulivu na anayevutia,
3.Mwenye kujilinda au yule anayeuacha wazi mwili wake?
4.Ni yupi mwenye kuheshimika kati yao, mwenye Hijabu au yule asiye na Hijabu?
Bila shaka, mwanamke mwenye Hijabu na ucha Mungu ni bora na ni mtukufu tena ni mwenye thamani kuliko yule mwingine.
Kipindupindu Ndani Ya Jamii
Miongoni mwa maradhi yanayoua haraka ni kipindupindu kwa mujibu wa taarifa ambazo huwa zinatolewa baada ya maradhi hayo kuingia katika kijiji au mji. Kila yanapodhihiri maradhi haya, hutangazwa hali ya hatari katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuwekwa karantini. Kama ilivyo katika kuzuia kipindupindu kisienee katika mji au kijiji, na fisadi nyingine ni hivyo hivyo. Sasa basi mtazamo wa Uislamu katika kuitazama jamii ni mtazamo wenye hekima kubwa, na ni mtazamo ambao lengo lake ni kujenga jamii nzuri na safi isiyokuwa na maovu ndani yake. Miongoni mwa mambo yanayoweza kudhibiti amani na ubora wa jamii ni mavazi. Siyo kweli kwamba kila vazi linaweza kukidhi haja hii, bali Hijabu pekee ndiyo jawabu, kwa sharti ya kuwa mvaaji aivae kwa kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu na siyo kinyume chake
.
Hijabu humlinda mwanamke kutokana na ufasiki na inamzuia kukhalifu maumbile yake aliyopangiwa kuishi ndani yake. Kwa kanuni hii ya Hijabu, Uislamu unakuwa umeisalimisha jamii na kuilinda isije ikajikuta imeteleza na kuvamiwa na maovu. Hali halisi inayojitokeza katika malengo ya msingi kuhusu kanuni hii ya Hijabu, ni kuitakasa jamii na kuisafisha, pindi wanawake watakapofuata sheria ya kuvaa Hijabu. Kinyume chake haitawezekana kabisa kudai kwamba jamii yetu ni safi, wakati wanawake zetu wanatembea bila kujali ni nguo gani wamevaa, kwa kuwa suala la mavazi kwa wanawake linataka litazamwe kwa mapana na marefu isiwe mradi kuvaa tu. Ni mara ngapi tunashuhudia mambo ya aibu na ya kuhuzunisha wanafanyiwa wanawake? Hivyo uchafu unasambaa haraka na kuleta madhara kwa wingi, kama kipindupindu kilichoingia mjini au kijijini. Na kwa ajili hiyo karantini inahitajika kuwekwa na kufuatwa kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu.
Uislamu kwa upande wake unataka kukata na kung'oa mizizi ya fitina na maovu kwa kutumia njia mbali mbali ikiwemo kusisitiza vazi la Hijabu. Pia Uislamu kwa nafsi yake unapinga kwa nguvu uovu na kila jambo linalokuwa ni sababu ya kueneza uchafu ndani ya jamii, miongoni mwa sababu hizo ni mwanamke kutokuwa na Hijabu ambayo ni vazi la kisheria.
Kukosekana Sitara Kunaleta Maovu.
Miongoni mwa maovu na athari mbaya katika jamii, ni wanawake kuacha kuisitiri miili yao ipasavyo, kitu ambacho kimesababisha vijana wetu wa kiume kuteleza na kujikuta wanafanya mambo machafu bila kukusudia. Imam Ali ibn Musa Ar-ridha anasema, "…….Imeharamishwa kuangalia nywele za wanawake, kwani katika kuziangalia nywele hizo kunasababisha kuamsha hisia za wanaume ambazo huwafanya waingie katika maovu na mambo yasiyo halali na yasiyopendeza."
Hapana shaka kwamba, mwanamke anayetoka nyumbani mwake na kwenda sokoni bila kujali ni vazi gani alilovaa, hajali kama limemsitiri vizuri au hapana, ni wazi kabisa huko njiani ataonekana kwa watu wa aina mbali mbali wakiwemo vijana ambao ndiyo kwanza wanaingia katika rika la ujana na nafsi zao bado hazijaweza kujimiliki kuhusu suala la kijinsiya. Hali kama hii ni lazima itaamsha hisia za kimaumbile za vijana hao kutokana na jinsi mwanamke huyo atakavyokuwa amevaa na umbile lake linavyoonekana kwa jumla pindi atakapopita mbele yao. Hisia hizi za kimaumbile ni lazima ziamke kwa kuwa ndivyo ilivyo hali halisi. Kwa hali hii basi nafsi za vijana hawa kwa tabia ya maumbile ya mwanaadamu huanza kuhangaika kutafuta njia za kuyatosheleza maumbile yao.
Suala la kujiuliza hapa ni je, vijana hawa watafanya nini? Ikiwa wao sio watu walioshikamana na mafunzo ya dini wala hawafuati miongozo ya kiislamu, basi watajaribu kutosheleza hamu zao kwa njia ya siri ambayo ni kujitoa manii jambo ambalo ni hasara na aibu. Ama wengine hufanya baya zaidi ambalo ni kinyume cha utaratibu aliotuwekea Mwenyezi Mungu, hawa hufanya liwati. Kundi jingine wao huamua kuzini na katika huko kuzini huwa wanatumia kila njia kufanikisha azma yao hiyo, ikiwa ni kwa hila au hata kwa nguvu ambayo ni kubaka wanawake mitaani. Matokeo ya ubakaji ni kuvunja heshima za watu na kuwadhalilisha wanawake.
Pamoja na matendo haya kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu, pia yanasababisha maradhi hatari na vifo vya ghafla
.
Inakadiriwa kwamba idadi ya hospitali zinazo shughulikia maradhi ya uasherati peke yake inafikia hospitali mia sita hamsini.
Hesabu hii ni kwa nchi ya Marekani peke yake. Chanzo cha balaa lote hili ni kwa wale wanawake wasiojali kutenganisha maumbile yao na ya wanaume mpaka wakawa wanaona miili yao haistahiki kulindwa na kupewa hadhi ya pekee. Lakini kila mwanamke asiyezingatia suala la mavazi kisheria ni lazima atambue kwamba, yeye ni mshiriki mkubwa anayesababisha madhambi na misiba hii, na anayo sehemu yake ya adhabu mbele ya Mwenyezi Mungu.
Yote yaliyotajwa hapa sasa hivi, yanatokana na vijana ambao wao siyo watu wa dini wala hawashikamani na Uislamu. Kwa upande wa pili inawezekana vijana hao wakawa ni watu wa dini na wanaambatana na mafunzo ya kiislamu na sheria zake, basi vijana hao huzuia hisia zao zisivuke mipaka ya Mwenyezi Mungu na hupambana na matamanio ya nafsi zao na kumlaani shetani asije akawahadaa. Vijana hawa huvumilia kero ya maumbile na kubeba mzigo mzito ambao hawakutarajia kuubeba. Kwa mara nyingine tena mwanamke au wanawake wasiojali sheria ya mavazi kama Mwenyezi Mungu alivyoamrisha, wanabeba uzito wa taabu na maudhi yanayowapata watu hawa wa dini.