BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE
KIMEANDIKWA NA: MUHAMMAD IBRAHIM EL-QAZWINIY
Kutokuvaa Hijabu Na Madhambi Ya Ubakaji
Miongoni mwa athari mbaya zinazosababishwa na tabia ya wanawake ya kutokuvaa Hijabu ni yale makosa ya jinai ya kuwabaka wanawake na kuwaingilia kwa nguvu bila hiyari yao. Ni jambo lisilofichikana pindi mwanamke anapouacha wazi mwili wake na mapambo yake, hali hiyo huamsha hisia za kijinsia kwa wanaume. Kwa hakika ni juu ya mwanamke mwenyewe kuulinda mwili wake, mapambo yake na utu wake kutokana na hatari hiyo inayoweza kumkabili.
Hapana shaka kwamba, macho ya vijana wasiokuwa na msimamo wa dini, pindi wanpomuangalia mwanamke ni sawa na macho ya mbwa mwitu anapomuangalia kondoo. Pia tunaweza kuyalinganisha macho hayo na macho ya paka anapomuona panya, au tuseme yanafanana na macho ya mnyama mkali wa porini, anapomuona mnyama mwingine au kitu kimngine ambacho kinamfaa kwa chakula. Siyo ajabu kabisa kwa mazingira kama haya kumkuta mwanamke amenasa ndani ya mtego aliojitegea mwenyewe kutokana na tabia ya kujitangaza mbele ya watu waovu.
Tabia hii ya ubakaji mara nyingi inatokea katika sura ya kutisha huko kwenye nchi za magharibi ambazo zimeporomoka mno katika suala zima la maadili. Katika ripoti moja kati ya matoleo ya gazeti la The Gurdian la nchini Uingereza iliandikwa kwamba: "Takwimu za polisi zinaonesha kuwa, makosa ya jinai ya kubaka yanaongezeka mwaka hadi mwaka. Katika mji wa Washington peke yake kila baada ya dakika kumi na tano huwa kuna tukio la kubaka, na katika mji mkuu wa Uingereza (London) yalitokea matukio 2095 ya kubaka wanawake na wasichana mnamo mwaka wa 1970 peke yake. [13]
"13 Haya ni machache katika mengi ambayo tungeweza kukuorodheshea.
Na miongoni mwa matukio ya kubaka kutokana na wanawake kutokujali kujisitiri kwa mujibu wa sheria na maumbile yao, mimi nimesikia kwamba, kuna rais fulani anayeongoza nchi moja miongoni mwa nchi za Kiarabu, yeye hufanya ziara za mara kwa mara kuvitembelea vyuo vikuu akitafuta mabinti katika vyuo hivyo na kuwachagua wale wazuri na wanaopendeza. Kisha humtoa nje ya msitari binti anayemuona kuwa atamfaa. Baada ya muda mfupi askari wa usalama wa taifa huwa wanakwenda nyumbani kwa binti huyo na kumweleza baba yake kwamba rais wa jamhuri anamtaka binti yake akakeshe naye katika usiku wa siku hiyo!.
Hali kama hii husababisha msiba mkubwa kwa baba, mama, binti huyu na hata familia nzima huingia ndani ya mtihani huu. Msiba huu huwagubika watu hawa kwa sababu wanafahamu wazi kwamba rais huyu ataishi na binti yao kwa usiku huo mmoja tu!! Sasa je, watu hawa watalikataa ombi la rais? Na je, inawezekana kwa watu hawa kuuepuka unyanyasaji unaowasubiri kutoka kwa rais wao? Basi je, matokeo ya jambo hili yatakuwaje? Hapana jambo jingine litakalotokea hapo isipokuwa msichana itamlazimu kuuendea uovu kwa miguu yake mwenyewe. Ataifuata fedheha na aibu hiyo kubwa bila kupenda, na kisha atarudi nyumbani hali ya kuwa amekwishapata hasara ya kuvunjika kwa heshima yake na utu wake pia kagubikwa na kiza la ulimwengu machoni mwake.
Ewe msomaji mpendwa, hapana shaka kwamba watu wanaosoma au kusikia unyanyasaji huu, utawaona wanamlaani na kumshtumu rais huyu muovu. Lakini hebu tufikiri kidogo juu ya misingi inayosababisha mateso haya na tujiulize swali lifuatalo: Je! Ni nani mwenye makosa? Hivi kweli mwenye makosa siyo yule baba ambaye toka hapo mwanzo alimruhusu binti yake atoke ndani hali ya kuwa maungo yake yako wazi na uzuri wake unaonekana kwa kila mtu? Lau binti huyo angekuwa ni mwenye kujisitiri, hivi unadhani yule rais mpumbavu angelimtamani na kumfanya kuwa kiwindo chake? Ni baba ndiyo mwenye kustahili lawama tangu ile siku aliponunua television (ambayo ni adui mkubwa muovu aliyemo ndani) ili kuistarehesha familia yake kwa kuangalia vipndi viitwavyo kuwa ni vya watu walioendelea!! Baba huyo huyo ndiyo mwenye lawama siku zile alipokuwa akiichukua familia yake kwa ajili ya kwenda sinema kuangalia filamu za watu walio uchi. Na mama pia anastahili lawama… Je ! Siyo yeye yule ambaye alikuwa akizifumua nywele za binti yake na kumpamba utadhani siku hiyo ndiyo siku ya harusi yake na kisha akamwacha kwenda shuleni akiwa katika mazingira kama hayo?
Ni huyo mama aliyekuwa akimchagulia binti yake asiyejuwa kitu mavazi mafupi yanayobana mwilini ambayo hayamsitiri inavyopasa? Binti naye anapaswa kulaumiwa kutokana na matokeo hayo yenye kiza kinene cha majonzi kwa kuwa ni yeye mwenyewe ndiye aliyechagua tabia ya kuuweka wazi mwili wake, na pia akachagua kupita njia ngumu iliyojaa miba na mawe. Naam, watu hawa ndiyo tabaka la mwanzo la kulaumiwa, na baada ya hapo ndio mnapaswa kumlaani rais yule!!
Kutokuvaa Hijabu Na Madhambi Ya Utoaji Mimba
Ni vema pia kutaja mambo mengine ambayo yanaletwa na makosa ya jamii inapokuwa imepuuza na kuacha Hijabu. Yapo mengi, lakini yanayotajwa ndani ya kijitabu hiki ndiyo ya msingi. Suala la kutoa au kuharibu mimba ni miongoni mwa athari mbaya ziletwazo na ukosefu wa sitara bora ya kisheria kwa wanawake. Ni mara nyingi inatokea kwa wanawake wasio na Hijabu kuvunjiwa heshima zao na utu wao.
Mwanamke asiyekuwa na sitara bora pindi anapodhihiri mbele ya vijana wenye dhiki ya kukidhi haja zao za kijinsia, hapana shaka vijana hao hushindwa kuyazuwia matamanio yao na hapo ndipo huamua kumbaka. Hapo mwanamke huwa anajikuta ametumbukia mikononi mwao bila hiyari, na huenda ikatokea bahati mbaya mwanamke huyo anaweza kubeba mimba haramu ambayo hakuitarajia. Kutokana na uovu huu aliofanyiwa hulazimika kuitoa au kuiharibu mimba hiyo. Leo hii katika anga la dunia yetu matukio kama haya ni mengi mno. Yako wazi kila mahali na hasa nchi za Ulaya Magharibi na zile zote zinazojaribu kuiga ustaraabu wa magharibi.
Tarehe 28 Februari mwaka 1972. jarida la An Nahaar la Lebanon lilichapisha katika ukurasa wake wa makala maalum kama ifuatavyo. "Katika mji wa London idadi ya utoaji mimba imeongezeka kutoka wanawake hamsini elfu mwaka 1969 hadi kufikia wanawake themanini na tatu elfu mwaka 1970 na idadi inayokaribia laki mbili mwaka 1971. Na huko Ufaransa hali hii imeongezeka na kufikia kutolewa mimba arobaini na sita hadi mia moja arobaini na tatu katika kila mimba mia mbili wanazobeba wanawake kwa mwaka. Ama huko Urusi, kuna mimba zipatazo milioni sita zinazotolewa kila mwaka
.
Kwa hakika takwimu na taarifa hizi zinatisha, na yote haya ni matokeo ya tabia ya wanawake kuyaonesha wazi maumbile yao na uzuri wao mbele ya kila mtu. Hakuna njia ya kuzuwia madhambi haya isipokuwa vazi la Hijabu iwapo litavaliwa kwa mujibu wa sheria na kutunza mipaka ya dini.
Kutokuvaa Hijabu Na Uharibifu Wa Ndoa
Tangu utamaduni wa kutovaa Hijabu ulipokuwa umeenea baina ya wanawake, yapo matatizo mengi yamezuka katika ndoa, na idadi ya matatizo haya inaongezeka siku hadi siku.
Tatizo hili la ndoa wakati mwingine huwa mume ndiyo sababu kubwa inayochangia uharibifu wa ndoa yake. Hasa pale mume huyu anapochukua fursa ya kutoka yeye na mkewe kwenda kwenye sherehe au mahafali mbali mbali zilizo na mchanganyiko wa wanaume na wanawake au kumpeleka mkewe katika majumba ya starehe na sinema. Wakati mwingine mume huyu hupata akaleta nyumbani kwake wageni wanaume na mkewe akaja kuwapokea kwa tabasamu zuri na kupeana nao mikono na chungu nzima ya makaribisho mengine ambayo mke wa bwana huyu huwafanyia wageni wa mumewe, ikiwa ni pamoja nakuwaletea matunda na vyakula vingine mbali mbali. Yote haya yanafanyika bila ya mume huyu kukumbuka kwamba wageni hao ni wanaume na jinsi yao kimaumbile inatofautiana na maumbile ya mkewe, pia pande mbili hizi hazina uhusiano wa kisheria.
Katika kipindi cha kubakia hapo, wageni hawa huendelea kupata kila aina ya makaribisho yasiyokuwa na mipaka ya kisheria. Kutokana na hali kama hii mara ghafla mume huyu humkuta mkewe amekwishaanzisha uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa marafiki zake hao. Hapa ndipo mume huyu huzusha ugomvi na mkewe na kuwasha moto wa volkano dhidi yake, pamoja na ukweli ulio wazi kwamba, yeye ndiyo sababu iliyoleta huzuni hii kubwa na msiba ndani ya nyumba yao. Mume huyu anasahau kwamba, yeye ndiye aliyekuwa kiongozi na muandalizi wa njia ya mkewe kulifikia giza hili na dhambi hii kubwa.
Baada ya tatizo kama hili baina ya mke na mume, hapo hujitokeza moja katika mambo mawili. Ama mume huyu aendelee kubaki na mkewe huyu muovu katika hali ya maisha ya dhiki yatakayokuwa yakiumiza roho yake na kuiadhibu nafsi yake, na kutokuaminiana tena na mkewe. Au pengine aende mahakamani ili akapate kufungua madai dhidi ya mkewe na kudai fursa ya kutoa talaka. Na mara nyingi talaka ndiyo uamuzi ambao mume huuchagua ili atatue tatizo hili. Lakini uamuzi huu unakuja baada ya kutokea fedheha, aibu na unyonge mkubwa katika familia hii. Na mwisho huu mbaya huleta matokeo ya kusikitisha, kwani familia hii hubomoka na maisha mazuri ya ndoa ya wawili hawa huvunjika.
Zaidi ya hapo msiba mkubwa hubaki kwa watoto ambao huwa bado wanahitajia kuwa na mama yao. Kuishi mbali na mama, watoto hawa hukosa huruma na upole wa mama yao, pia hukosa malezi mazuri na mwelekeo mwema. Hapo ndipo mahali ambapo hujitokeza fundo la moyo kwa watoto hawa na kujihisi kuwa na upungufu katika jamii wanayoishi. Watoto hawa hubadilika taratibu katika tabia zao na hatimaye hutokea wakajiunga katika magenge au makundi yenye mielekeo mibaya na kujikuta wamo miongoni mwa wezi na majambazi
.
Mengi ya matukio ya aina hii yamekuwa yakitokea katika nchi zisizo za Kiislamu. Katika moja ya makala zake, gazeti la Kisovieti liitwalo Pravda liliandika kama ifuatavyo: "Asilimia themanini ya makosa ya uvunjaji sheria yafanywayo na vijana wenye umri wa kukaribia balehe (miaka kumi mpaka kumi na tano) yanatokana na kuvunjika kwa familia." Pia likaendelea kueleza gazeti hilo kwamba: "Katika kila matatizo tisa yanayohusu ndoa, moja katika matatizo hayo, matokeo yake huwa mume na mke kupeana talaka." Pravda likaendelea kutoa sababu za matatizo hayo kwa kusema: "Sababu za msingi zinazochangia kuleta hali hii, ni kuharibika kwa mwenendo wa jamii kutokana na ulevi wa kupindukia
.
Sasa basi, ukweli uliopo ni kwamba matokeo ya yote haya yanakuja kutokana na uovu unaosababishwa na kutokujisitiri wanawake kama sheria inavyowataka. Uislamu kwa upande wake haukuharamisha bila mantiki mavazi yasiyowafunika wanawake kwa mujibu wa sheria, isipokuwa ni kwa lengo la kuzuwia maovu haya, na pia haukufaradhisha vazi la Hijabu kwa mwanamke isipokuwa ni kwa nia ya kumuepusha mwanamke asifikwe na maovu haya na mengine mfano wa haya. Kwa hiyo Uislamu unawalazimisha wanawake kuvaa Hijabu ambalo ndilo vazi rasimi kisheria ili kuzuia kuzuka kwa maovu kama yalivyotangulia kuelezwa.
Magazeti na vyombo vingine vya khabari kila mara vinatuarifu habari mbali mbali zinazohusu matatizo ya ndoa na khiyana zinazofanyika baina ya mke na mume, na hali hii husababisha watu kupeana talaka na pengine ikasababisha kutokea mauaji. kila unapofanyika uchunguzi, Sababu za msingi zinarudi kwenye upuuzaji wa Hijabu kwa ile maana yake halisi iliyokusudiwa na Uislamu. Ni mara nyingi tunasoma magazetini au kusikia redioni kwamba mtu kamuacha mkewe na wanawe kwa ajili ya msichana asiye na Hijabu ambaye kakutana naye ofisini au katika mabustani ya mapumziko na au mahali pengine. Au ni mara ngapi tumesikia na pengine kuona mke anamuacha mume wake ili tu akaolewe na kijana aliyekutana naye sinema au pwani wakati wa kuogelea?
Kuna gazeti moja liliandika kama ifuatavyo: "Mtu mmoja alimuua rafiki yake ili amchukue mkewe ambaye alikuwa akijidhihirisha wazi mbele ya bwana huyo bila Hijabu wala aibu. Gazeti liliendelea kueleza kwamba, kuna mwanamke mwingine ambaye yeye alimuua mumewe kwa msaada wa huyo mpenzi wake na kisha wakamkatakata viungo vyake na kuvitupa ndani ya mfereji wa maji machafu. Bibi huyu alifanya madhambi haya ili tu aolewe na huyo bwana mpya." Pia kulitolewa habari na gazeti moja la Kiarabu ambalo liliandika tukio moja miongoni mwa matukio yanayosababisha ndoa za watu kuvunjika, hasa mijini ndiko kwenye matukio mengi ya aina hii. Tukio hilo kwa hakika lilikuwa la kuhuzunisha sana, na cha kuhuzunisha zaidi ni kwa kuwa lilitokea katika moja ya nchi za Kiislamu, lau lingekuwa limetokea katika nchi za magharbi, hali hii ingekuwa ni mahala pake kwa kuwa nchi hizo ndiyo vituo vya kila aina ya maovu, kama vile zinaa na uchafu mwingineo. Lakini ni vipi leo mambo haya yanatokea hata katika nchi takatifu za Kiislamu ambazo hapo kabla zilikuwa zimetakasika kutokana na uchafu huo?
Hapana shaka, hayo ni matokeo ya wanawake kuuwacha utamaduni wao wa Kiislamu katika suala la mavazi, pia mienendo ya Waislamu imebadilika na wameshawishika na utamaduni mbaya wa kimagharibi. Kutokana na kupotea kwa Waislamu na kuacha mwelekeo na utamaduni wao, sasa hivi imekuwa kazi ngumu kuyaepuka maovu na balaa hizi isipokuwa njia pekee ni kurudia utamaduni wetu kama alivyotuamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake(s.a.w.w)
.
Ewe msomaji mpendwa, hebu kaa tayari nikusimulie hicho kisa ili ujionee mwenyewe umuhimu wa Hijabu kwa maana yake kamili na pia ubaya wa kuacha Hijabu: "Naam, wanamichezo wa nchi fulani walitoa mwaliko wa kimichezo kwa mmoja wa wanamichezo mashuhuri wa nchi fulani. Kwa bahati nzuri mwanamichezo mualikwa aliukubali mualiko huo na kufanya safari kuelekea huko akifuatana na mkewe ambaye hakuwa amevaa Hijabu, na kwa sura binti huyo alikuwa kaumbika.
Walipofika uwanja wa ndege wa nchi aliyoalikwa mwanamichezo huyu na mkewe, kwa pamoja walilakiwa na wenyeji wao ambao nao ni wanamichezo. Mwanamichezo huyu mgeni alisalimiana na wenyeji wake kisha akamtambulisha mkewe kwa wenyeji hao nao wakampa mikono mkewe huyu, kitendo ambacho Uislamu umekiharamisha. Wanamichezo hawa wenyeji walionyesha furaha kubwa sana na tabasamu kwa mke wa rafiki yao kiasi kwamba mmoja wao alimtamani mke wa mgeni wao na akafikiria lau angemuoa yeye. Isitoshe alifikiria pia njia za kumuwezesha kutimiza azma yake hiyo. Mwisho wa yote alitumia kila ujanja na mbinu za kishetani za kumhadaa bibi yule na akapata fursa ya kukaa naye faragha. Hapo alimuuliza thamani ya mahari aliyopewa alipoolewa na mumewe, na bila kusita mwanamke yule alitaja thamani ile, k.m. dinari alfu moja. Bwana yule aliendelea kusema: 'Mimi nitakupa dinari elfu tatu kwa sababu uzuri wako unastahiki hivyo, siyo thamani aliyokupa mumeo ni ndogo mno na kwa kweli amekudhulumu.' Kisha akamuuliza mumeo ana kazi gani afanyayo zaidi ya michezo? Yule mama akajibu: 'Mume wangu ni karani katika wizara fulani.' Bwana yule aligutuka na kusema 'Aah!!! Hii ni dhuluma kubwa uliyofanyiwa, hivi kweli pamoja na uzuri wote ulionao unakuwa mke wa karani? Haiwezekani kabisa, wewe thamani yako ni kubwa mno. Napenda kukufahamisha kwamba, mimi ni mhandisi na ninayo shahada ya udaktari na nimemaliza Chuo Kikuu, nataka kukuoa lakini kwanza mumeo huyu akuache.' Na mwisho yule bwana alimuhadaa mke wa rafiki yao na wakaafikiana afanye kila hila adai talaka toka kwa mumewe naye atamuowa. Yote haya wakati yanafanyika masikini mume yule hana habari anandelea na michezo.
Ziyara hiyo ilipokwisha bwana yule na mkewe wakarudi nyumbani kwao. Baada ya safari yao bwana huyu akaanza kuona mabadiliko ya tabia ndani ya nyumba yake. Tabia ya mkewe ikawa si nzuri tena, wakati hapo zamani alikuwa akiliona tabasamu la mkewe ambalo lilikuwa likimsahaulisha taabu ya kutwa nzima kazini, leo ni kinyume chake. Baadaye alimuuliza mkewe sababu ya mabadiliko haya. Mke akajibu, 'Wewe umenidanganya.' Mume akasema, 'Nimekudanganya nini?' Mke akasema, 'Umenioa kwa mahari ndogo ambayo mimi sikustahiki, yuko mtu ambaye anaweza kunioa kwa mahari inayonistahiki na sasa nipe talaka yangu.' Mume huyu akili zilimruka baada ya kusikia majibu ya mkewe. Alipigwa na butwaa la majonzi ambalo yeye ndiye aliyeliandaa siku aliposafiri na mkewe asiye na sitara na kumtambulisha kwa watu wasio maharimu wake. Hata hivyo bwana huyu alijaribu kumpa rai mkewe abadili uamuzi wake, lakini jitihada zake zilishindikana na baadaye akamwacha mkewe kwa uchungu mkubwa hali akiwa bado anampenda. Na yule bibi baada tu ya kuachwa, alisafiri hadi kwa yule bwana aliyemuhadaa akiwa na ushahidi wa talaka mkononi ili akatimize lengo lake la kuolewa upya."
Fikiria ewe msomaji, hili ni tukio katika matukio mengi yanayoharibu ndoa za watu. Hebu tafuta sababu yake, hutapata isipokuwa ni kwa sababu bibi yule alikuwa hakusitiriwa Kiislamu, na lau angekuwa kavaa Hijabu inayositiri maungo yake na uzuri wake, je bibi huyu angetumbukia katika mtego huu? Je, mume huyu naye angeingia katika machungu ya kumwacha mkewe hali ya kuwa bado anampenda kutokana tu uovu aliouandaa mwenyewe kwa kumwacha mkewe bila ya kuwa na sitara ya Kiislamu? Lakini taabu hii na machungu haya aliyataka mwenyewe kwa kutomlea mkewe ndani ya malezi ya Kiislamu. Na haya ndiyo malipo ya mtu anayekwenda kinyume na kanuni za Kiislamu na hukmu za Qur-an.
Wakati huo huo tunajiuliza, hivi kweli mke huyu baada ya kuachwa na yule mume wa kwanza, je ndoa ile kwa huyu mume wa pili ilidumu?
Jawabu la swali hili linasema kuwa: "Mara nyingi ndoa za aina hi huwa hazidumu isipokuwa chache tu miongoni mwa hizo, kwa sababu mume wa aina hii huwa hamuowi mwanamke kwa lengo la kujenga maisha ya ndoa kwa maana ya mke na mume, bali huwa anaowa ili tu atosheleze matamanio yake ya kijinsiya na kuyashibisha matamanio yake ya kinyama. Matokeo yake ni kwamba bibi yule aliachwa na kurudi kwenye mji wao hali ya kuwa ni mwenye huzuni na majonzi tele. Alipata hasara ya kumpoteza mumewe wa kwanza ambaye alikuwa akiishi naye kwa kila aina ya mapenzi na huruma.
Ewe msomaji mpendwa, hili ni tukio moja tu kati ya maelfu ya matukio ya hiyana za ndoa za watu. Lakini hebu fanya uchunguzi juu ya sababu zinazosababisha hali hii. Huwezi kupata sababu isipokuwa ni ile tabia ya wanawake kujidhihirisha na kuyaacha wazi maungo yao. Lau mwanamke yule angelikuwa na Hijabu, akausitiri uzuri wake ipasavyo, hivi kweli angenaswa katika mtego huu? Na je, lau yule mume angejikuta ameanguka ndani ya machungu yale ambayo kwa hakika yeye mwenyewe ndiye aliyeyaandaa? Hapana shaka kwamba haya ndiyo malipo ya mtu yeyote anayekwenda kinyume na kanuni za Uislamu na hukmu za Qur'an.