BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE
KIMEANDIKWA NA: MUHAMMAD IBRAHIM EL-QAZWINIY
Ewe Mume Mwema
Jukumu lako ewe mume kuhusu suala la ndoa ni muhimu sana mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani unawajibika kutengeneza na kurekebisha mwenendo na tabia ya mkeo.
Mwenyezi Mungu amekufanya uwe msimamizi wa mkeo na kiongozi wake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:
الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنْفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ.
"Wanaume ni walinzi juu ya wanawake kwa sababu Allah amewafadhilisha baadhi yao kuliko wengine na kwa sababu ya mali zao walizozitoa
." 4:34.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنْفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ.
Na Mwenyezi Mungu anasema: "Enyi mlioamini jiokoeni nafsi zenu na watu wenu kutokana na moto ambao kuni zake ni watu na mawe
" 66:6.
Na ili uweze kutekeleza wajibu wako kisheria na majukumu yako ya dini kama alivyoamuru Allah s.w.t na Mtume Wake, ni lazima uambatanishe mafunzo na maelekezo ya Kiislamu kwa vitendo kama ifuatavyo.
Hijabu liwe ni jambola mwanzo
: Unalazimika kumuamuru mkeo avae Hijabu kama alikuwa havai, na pia umuoneshe dalili za kutosheleza na kukinaisha kuhusu Hijabu. Hii ni kwa sababu atakapovaa awe anafahamu na kuelewa umuhimu wa kanuni hii ya Kiislamu. Endapo utashindwa kumkinaisha kimaelezo basi fuatana naye hadi kwa Sheikh ambaye ataweza kumfahamisha kwa maelezo yatakayoonesha umuhimu wa falsafa inayopatikana katika Hijabu. Na ikiwa kuna njia nyignine ya kumfahamisha kama vile kumtafutia vitabu ajisomee yeye mwenyewe ni bora kumpatia.
Imam Ali
anasema kumuusia mwanawe Muhammad AlHanafiyya: "Umuhimu wa Hijabu ni kitu bora kwako na kwao wanawake, ili muondokane na shaka. Kutoka nje (kwa matembezi ya kawaida) na wanawake siyo jambo baya kuliko wewe kuja na mgeni mwanaume asiyeaminika nyumbani mwako kisha ukamtambulisha kwao (wanawake) na iwapo utaweza kutowatambulisha wake zako kwa yeyote basi fanya hivyo
."
Imam Ali anamaanisha kwamba, mume asimtambulishe mkewe kwa wanaume wasiomuhusu mkewe, kwa kuwa jambo hili husababisha fitna.
Jambo la pili
: Tahadhari na sherehe zenye mchanganyiko: Ewe mume mwema, epukana na mahafali na sherehe zenye mchanganyiko wa wanaume na wanawake. Usimpeleke mkeo sehemu hizo, muepushe mbali kabisa na mikesha ya nyimbo na magoma. Kumpeleka mkeo, katika majumba ya sinema kunachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu mwenendo wa mkeo na pia hali hii itasaidia kumfanya asiwe na aibu na heshima yake itatoweka.
Mume anayempeleka mkewe sehemu zenye sherehe zenye mchanganyiko wa wanawake na wanaume, au anayemuingiza mkewe katika majumba ya sinema, mume huyu ni haini wa kwanza dhidi ya mkewe. Yeye ndiye dhalimu atakayekuwa mfundishaji wa mwelekeo mbaya wa mkewe.
Dhoruba la uovu atakalolianzisha mume huyu dhidi ya mkewe, bila shaka litaanza kumpiga yeye mwenyewe, ili ayaone matunda ya kazi yake hiyo mbaya. Dhoruba hili si jingine, bali ni pale mkewe atakapofanya hiyana ya kuanzisha uhusiano na watu wengine. Hivyo ni wajibu wako wewe mume kumuepusha mkeo kutokana na maeneo ya uovu na mengineyo machafu. Asiyakaribie maeneo hayo licha ya kwenda ili uishi kwa amani na nafsi iliyotulia.
Jambo la tatu
: Usimtii mkeo: Inakulazimu uishi maisha ya muongozo wa dini ya Mwenyezi Mungu na hukumu zake na utahadhari na kila mwelekeo mbaya na wa kupotosha. Kwa kuwa utulivu wa nafsi yako hupatikana toka kwa mkeo, basi huenda akataka umfanyie jambo ambalo Mwenyezi Mungu kaliharamisha. Iwapo hali hii itajitokeaza kwa mkeo, jaribu kumuleza kwa upana hukmu ya Mwenyezi Mungu kuhusu ombi lake hilo ili atambue ubaya wa jambo hilo. Haifai kabisa kumtii mkeo (hata mtu mwingine) katika mambo ya kumuasi Mwenyezi Mungu s.w.t kwani hapana twaa ya kumtii kiumbe katika kumuasi Muumba.
Hivi sasa soma hadithi ifuatayo: Mtume(s.a.w.w)
anasema: "Mwenye kumtii mkewe Mwenyezi Mungu atamuingiza motoni mtu huyo. Mtume(s.a.w.w)
akaulizwa huko kumtii mke ni namna gani? Mtume akasema: Mke kuomba ruhusa kwa mumewe kwenda kwenye starehe na michezo hali ya kuwa kavaa nguo nyepesi (na mume akatoa ruhusa).
"
Kwa hiyo basi, usimruhusu mkeo kuhudhuria sherehe au harusi zenye mchanganyiko na usimkubalie kuvaa mavazi mepesi mbele ya wanaume wengine kwa kuwa yote haya hayamridhishi Mwenyezi Mungu.
Jambo la nne
: Kuwa na wivu kwa mkeo: Huna budi ewe mume kuwa na wivu kwa mkeo, kwani imekuja hadithi kutoka kwa Imam Jaafar Sadiq
kwamba: "Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ana wivu na anampenda kila mwenye wivu, na kwa wivu wake Allah (s.w.t) amekataza maovu yafanywayo dhahiri na yale yafanywayo kwa siri.”
Kwa ajili hiyo basi ni lazima umuhifadhi mkeo na binti zako kitabia, pia mavazi ili msijefikwa na balaa na ghadhabu za Allah (s.w.t). Amesema Imam Jaafar
kwamba: "Pepo imeharamishwa kwa mtu duyuuth (asiye na wivu)." Na amesema tena Imam Jaafar
"Watu wa aina tatu Mwenyezi Mungu hatawasemesha siku ya kiama wala hatawatakasa
1.
Sheikh (mwanachuoni) mzinifu
.
2.
Duyuuth (asiye na wivu)
3.
Mwanamke anayemlaza mwanamume mwingine kwenye kitanda cha mumewe
."
Na katika kuonesha kuwa una wivu, ni kutomwacha mkeo au mmoja kati ya watu wa nyumba yako, wakiwemo mabinti zako wakatoka nje hali ya kuwa wamejitia manukato na madawa ya kujirembesha na mapambo mengine. Hapana shaka kwamba jambo hilo huwa linatishia heshima yako na yao ndani ya jamii, na matokeo ya hali hiyo ni mabaya mno. Mtume(s.a.w.w)
amesema: "Mwanaume yeyote atakayemwacha mkewe ajipambe na kisha mwanamke huyo akatoka nyumbani mwake akiwa katika hali hiyo, basi mume huyo atakuwa ni duyuuth (hana wivu)
.
Na ikiwa mke huyu atatoka nyumbani mwake hali kajipamba na kutia manukato na mumewe akawa radhi, mumewe atajengewe nyumba ndani ya moto kwa kila hatua moja atakayotembea mkewe
. Bwana Mtume(s.a.w.w)
anasema kuwa: "Aina kumi za watu hawataingia peponi mpaka kwanza watubie:…. Miongoni mwa hao kumi Bwana Mtume alimtaja Duyuth, na akaulizwa, ni nani huyo Duyuth? Akasema ni yule mwanaume asiyekuwa na wivu kwa mkewe
.
Imetokea zaidi ya mara moja, kwangu mimi kumuona mtu anakula chakula ndani ya mgahawa au hoteli hali ya kuwa na mkewe na watu wengine wakiwa wanamuangalia mtu huyo na mkewe. Cha ajabu ni kwamba bwana huyo anapokuwa katka mazingira hayo anakuwa yuko huru bila wasiwasi kabisa. Hajali kama kuna sitara yoyote au hapana, na wala hana hata habari juu ya kuwa mkewe kavaa Hijabu au hapana. Kama ambavyo sasa hivi iko wazi kabisa kule kuwako kwa mabustani na maeneo ya matembezi yanayotembelewa na watu wengi wake kwa waume. Kwa hakika jambo hili bila kificho ni jambo baya mno linalohatarisha usalama wa jamii. Kuna Mkurugenzi wa mgahawa mmoja aliniambia kuwa: "Wako baadhi ya watu wanakataa kula chakula ndani ya vyumba maalum vilivyotengwa kwa ajili ya watu wenye familia, na wanaona ni bora wale chakula mahali pa wazi hali ya kuwa wamefuatana na familia zao!" Kama hali ni hii, uko wapi basi wivu wa wanaume kwa wake zao enyi Waislamu?
Mfundishe mkeo Surat An-Nur. Inapendekezwa kwako ewe mume kumfundisha mkeo surat Annur na tafsiri yake, kwa kuwa ndani yake mna Aya nyingi zinazozungumzia mas'ala ya wanawake.
Aya hizo zimedhibiti mambo mengi ambayo yanamlazimu mwanamke ayafahamu ili aishi maisha bora ya Kiislamu na awe mbali na maovu. Mtume wa Mwenyezi Mungu anasema: "Wafundisheni wanawake surat An-nur kwani ndani yake mna mawaidha mengi (kwa wanawake).
Usimuweke mkeo katika chumba cha barabarani. Bwana Mtume(s.a.w.w)
amekataza kuwaweka wawnawake katika vyumba vya barabarani akasema: "Musiwaweke wanawake katika vyumba vya barabarani." Makusudio halisi ya hadithi hii ya Bwana Mtume(s.a.w.w)
ni kuwaonya wanaume juu ya kuwaweka wake zao katika vyumba vinavyotazamana na barabara.
Zaidi ya hapo ni lazima tufahamu hata vyumba vinavyotazamana na masoko na maeneo mengine yenye msongamano wa watu ni hatari kuwaweka wanawake ndani ya vyumba hivyo. Imekuja katika hadithi kwamba, miongoni mwa hatua ambazo Imam Mahdi
atazichukua katika kurekebisha hali ya Umma pindi dola yake itakaposimama, ni kuondosha madirisha yanayoelekea barabarani.
Pengine utajiuliza kwamba ni ipi hekima ya jambo hilo? Jawabu lake ni hili lifuatalo: Hapana shaka kwamba madirisha yanayotazama barabarani ni kichocheo kikubwa katika kuleta uharibifu ndani ya ndoa za watu na pia kuvuruga familia. Na sababu yake ni kwamba dirisha hilo huwa ni nyenzo ya kumfanya mtu aone ni kitu gani kilichomo ndani ya chumba na hasa katika majengo ya ghorofa kadhaa. Majengo haya huwa yanaonesha kila kilichomo ndani ya chumba hicho kwa wapita njia na hata watu wanaoshi mkabala na majengo hayo.
Sasa basi uharibifu wa familia na ndoa za watu unaweza kuja kutoka katika moja ya pande mbili, yaani upande wa mwanamke aliyemo ndani ya jengo hilo au yule mwanaume mpita njia. Kwa mfano mwanamke ikitokezea akachungulia njiani kwa kupitia dirishani na kwa bahati mbaya mmoja kati ya wapita njia akimuona na moyo wake ukaingia namna fulani ya kumpenda huyo mwanamke, basi hapo ndipo unapoanzia ule msiba wa maovu. Na pengine mwanaume naye anaweza kuwa amesimama dirishani na mara akamuona mwanamke kwenye ghorofa lililoko mkabala na ghorofa analoishi yeye, basi kutokana na mazingira ambayo hayapingiki ni kuwa bila ya shaka mwanamke huyo atakuwa hakujisitri kwa kutambua kuwa yumo ndani mwake. Katika hali kama hii tunataraji matokeo gani baina ya wawili hawa ikiwa hawatamuogopa Mwenyezi Mungu? Hapana shaka kwamba Bwana Mtume(s.a.w.w)
amesema kuwa:
"Yeyote atakayechungulia ndani ya nyumba ya jirani yake kisha akaona tupu ya mwanaume au nywele za mwanamke au akaona sehemu yoyote ya mwili wa mwanamke, basi Mwenyezi Mungu atakuwa na haki ya kumuingiza motoni mtu huyo pamoja na wanafiki ambao walikuwa wakifuatilia tupu za wanawake hapa duniani na wala Mwenyezi Mungu hatamtoa ulimwenguni mpaka kwanza amfedheheshe na audhihrishe wazi utupu wake huko akhera.
Hekima inatwambia kwamba: "Kinga ni bora kuliko tiba." Hali inajieleza wazi kwamba, ni mara nyingi tiba imekuwa ni jambo lisilo na mafanikio, wakati ambapo kinga imekuwa ni dhamana yenye nguvu. Kwa hakika miongoni mwa mambo yanayohuzunisha ni kuona kwamba jamii kwa jumla inaishi nje ya mafunzo haya ya Kiislamu yenye ulinzi madhubuti.
Utamuona mwanamke anatoka barazani hali ya kuwa kavaa nguo zinazostahili kuvaliwa ndani, kisha katika hali kama hiyo anaanika nguo kwenye kamba. Au utamkuta mwanamke anachungulia njiani katika hali ile ile huku akiwa amejisahau kwamba kwa kufanya hivyo anajiletea msiba na huzuni yeye binafsi na familia yake. Basi ni juu yako ewe mume mwema uzindukane na ushikamane na mafunzo bora ya Kiislamu, na pia uyatumie ndani ya maisha yako ya ndoa na familia yako kwa jumla mpaka ifikie hali ya maisha yako na familia yako kuwa maisha mema yenye kuepukana na fedheha za duniani na udhalili wa huko akhera.
Mafunzo ya Kiislamu. Ndugu Mwislamu pokea baadhi ya mafundisho ya Kiislamu ambayo Mwenyezi Mungu ametuamrisha kuyatumia katika maisha yetu ya kijamii. Mafunzo haya yanalenga kumhifadhi mtu kutokana na uovu pia kumlinda asiteleze na kuingia makosani.
Kwanza: Usimuangalie mke asiyekuhusu.
Kumtazama mwanamke asiyekuhusu ndiyo hatua ya kwanza kuelekea kwenye uharibifu wa tabia na ndiyo ufunguo wa shari na kutelezesha watu. Katika kumtazama mara moja hutokea ukavutika na kuongeza mtizamo wa pili, na hatimaye watatu na mwisho husababisha nia mbaya katika nafsi.
Mshairi mmoja anasema: Kutazama ndiyo hatua ya mwanzo, tabasamu hufuatia, kisha salamu. Kinachofuata ni mazungumzo, na hatimaye ahadi hufungwa na mwisho wa yote kitendo hutimia.
Kwa sababu kama hizi, Uislamu kwa kutaka kukata mizizi ya fitina umekataza jambo hili.
Mwenyezi Mungu Mtukufu ameharamisha kumtazama mke asiyekuhusu, na akaonya kwa onyo kali. Isitoshe Mwenyezi Mungu amewaamuru Waumini wa kiume wainamishe macho yao wasiwatazame wanawake wasiowahusu Akasema:
قُلْ لِلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ
"Waambie Waumini wanaume wainamishe (chini) macho yao na wazilinde tupu zao, kwani kufanya hivyo kuna utakaso kwa ajili yao. Na hakika Mwenyezi Mungu anafahamu wanayotenda
.
"
Hapana shaka kwamba tabia ya kibinaadamu ni tabia inayopelekea mvuto baina ya jinsiya mbili hizi , yaani ya kiume na ile ya kike kwa sababu tu ya kila mmoja kumtazama mwenzake. Kwa hiyo basi, ni lazima tabia hii iwekewe mipaka kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu, vinginevyo matokeo ya maisha ya jamii ya wanaadamu yataingia ndani ya ufisadi na matokeo ya ufisadi huo ni mabaya. Imam Jaafar As-sadiq
amesema: "Kuangalia kwa kukazaia macho kunapanda mbegu ya matamanio ndani ya moyo, na kwa hakika inatosha kuwa ni fitna kwa mwenye kuangalia namna hiyo." Hapana41 shaka kwamba kuangalia huko kulikoharamishwa na sheria, ndiko kunakoandaa maovu hapa duniani, na kwa ajili hii kumekuja maonyo ndani ya hadithi kama ifuatavyo: "Kuangalia ni mjumbe wa uzinifu.
"Hadithi hii inatufunza kwamba, mwanzo wa uzinifu hupatikana kwa njia ya kuangalia kulikoharamishwa na sheria. Jambo hili liko wazi kwa kuwa, uzinifu haupatikani ila baada ya mwanaume kumkazia macho mwanamke, na ndiyo maana tukaambiwa ndani ya ile hadithi iliyotangulia hapo kabla kwamba:
"Kuangalia kulikoharamishwa ni mjumbe wa uzinifu." Kwa maelezo haya ndugu msomaji, wala hakuna haja ya kuuliza juu ya athari mbaya zinazojitokeza kutokana na uzinifu ikiwemo maradhi mabaya yanayosababishwa na tendo hilo chafu. Isitoshe hali hiyo, bali kuna uharibifu mkubwa mno ndani ya jamii. Na kila ukichunguza utakuta kuwa uzinifu ndiyo chanzo cha misiba hii, na ambayo chimbuko lake ni kumuangalia mwanamke asiyekuhusu kwa mujibu wa sheria. Nabii Yahya ibn Zakariyya
aliulizwa kuhusu chanzo cha uzinifu akasema: "Ni kumuangalia (mwanamke asiyekuhusu) na nyimbo." Siyo jambo la ajabu kuwa, sheria imekuja kuyakataza kwa mkazo sana mambo haya, na wala siyo jambo la kushangaza kuwa, huko akhera kutakuwa na adhabu kali na ngumu kwa watendao matendo haya. Imekuja ndani ya hadithi tukufu ya Mtume(s.a.w.w)
kwamba: "Mtu yeyote atakayeyajaza macho yake kwa kumuangalia mwanamke ambaye ni haramu kwake, Mwenyezi Mungu atayajaza macho yake siku ya kiama kwa misumari ya moto na ataendelea kuyajaza moto macho hayo mpaka watu wote waishe kuhukumiwa ndipo naye aamuriwe kuingia motoni.
"
Hadithi nyingine nayo inasema kuwa: "Yeyote mwenye kuyajaza macho yake kwa kuanglia vitu vilivyoharamishwa, Mwenyezi Mungu atayajaza macho yake siku ya kiyama kwa misumari ya moto, isipokuwa kama atatubia.
"
Miongoni mwa athari za kuwaangalia wanawake wasiyokuhusu ni kujiadhibu wewe mwenyewe nafsi yako na kujisababishia mawazo mengi bila sababu ya msingi.
Imam Ali
anasema:
"Yeyote mwenye kuliachilia jicho lake (likawaangalia wanawake wasiomhusu) mtu huyo hujisababishia majonzi mengi
."
Na kasema tena Imam Ali
:
"Mtu yeyote ambaye macho yake ni yenye kuangalia kwa kufuatilia (wanawake wasiomhusu au mambo ya haramu) mtu kama huyu majuto yake huwa ni ya kudumu
."
Mtu anayeishi maisha yanayoruhusu macho yake kuangalia kila anayemtaka na anachokitaka, hapana shaka kwamba mtu huyu huishi maisha yenye majonzi mengi na huiadhibu nafsi yake mwenyewe, na huwa mwenye mawazo yasiyo na kikomo. Yote haya yatampata kwa sababu moyo wake utakuwa umefungwa kwa huyo aliyemuona na akamtamani kisha asimpate. Akili yake ataishughulisha akifikiria namna ya kumpata, na huwenda akakosa raha na hata usingizi.
Hadithi hii iliyotaja hatari za kuangalia, na kisha kumsababishia taabu na majuto mwenye tabia hiyo, inahusisha mambo mengi ambayo haipaswi kuyaangalia, lakini moja wapo na muhimu ni hili la kuwaangalia wanawake wasiokuhusu, bali tunaweza kusema kuwa hilo ndilo makusudio. Na kwa ajili hiyo basi Imam Jaafar
akibainisha hatari za kumuangalia mwanamke asiyekuhusu anasema: "Kumtazama mwanamke asiyekuhusu ni mshale wenye sumu miongoni mwa mishale ya iblisi, na ni mara nyingi kumtazama mwanamke asiyekuhsu limekuwa ni jambo lenye kuleta majuto ya muda mrefu
."
Ewe ndugu yangu bila shaka unafahamu jinsi mshale unavyoweza kuingia mwilini na kupasua mishipa iliyoko mwilini. Hebu fikiria namna mshale usiokuwa na sumu unavyoweza kuleta madhara pindi uingiapo mwilini, sasa je itakuwaje hali ya mshale wenye sumu ukiingia mwilini?
Bila shaka madhara yake ni makubwa zaidi ambayo yanaweza kupelekea mauaji kwa mtu. Hali ni kama hiyo kwa mtu mwenye tabia ya kuangalia wanawake wasiomhusu, kwani kuangalia huko ni sawa na mshale wenye sumu, mshale huo hujitengenezea njia mpaka ndani ya moyo ili kumnyima mtu huyo raha na utulivu na kumuachia majuto ya muda mrefu. Ewe ndugu yangu mpendwa! Ili uweze kujitakasa na kuwa mbali na mawindo ya shetani, napenda kukufahamisha pia kwamba Uislamu unachukizwa na tabia ya kuwaangalia wanawake. Mimi naamini kwama kuna baadhi ya watu wasiofuata mafundisho ya dini wanapokutana na wanawake, wakishakupishana nao basi huwaangalia nyuma hali ya kuwa wanatizama kwa mtazamo wa kutaka kufahamu namna wanawake hao walivyo au wanavyotembea, pia maumbo yao. Kwa hakika hii ni tabia mbaya mno haifai kabisa. Inasimuliwa kwamba Abu Basir alimuuliza Imam Jaafar
"Ni vipi mtu anapomwangalia mwanamke kwa nyuma? "Imam a.s. akajibu kwa kusema: "Hivi mmoja wenu anapenda mkewe au jamaa yake wa kike aangaliwe namna hiyo?" Abu Basir akajibu: "Hapana." Imam akasema: "Basi waridhie watu kwa kile unachokiridhia kwa ajili ya nafsi yako
.
"
Kuna kisa kimoja kinamuhusu Mtume Musa
katika tafsiri ya neno la Mwenyezi Mungu akimnukuu Binti ya Mtume Shuaibu
aliposema:
قَالَتْ إِحْدَاهُمَا يَا أَبَتِ اسْتَأْجِرْهُ ۖ إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ الْقَوِيُّ الْأَمِينُ
"Ewe Baba muajiri huyu, hakika mbora uwezaye kumuajiri ni mtu mwenye nguvu tena mwaminifu
.
Nabii Shuaibu alipoyasikia maneno ya Binti yake alimuuliza akasema: "Huyu Musa ni mwenye nguvu na hii ni kwa sababu umemuona akilinyanyua jiwe kwenye kisima, sasa je, huu uaminifu wake umeufahamu vipi?" Yule Binti akajibu kwa kusema: "Ewe Baba mimi nilikuwa natembea mbele yake, mara Musa akaniambia, tembea nyuma yangu na iwapo nitapotea njia basi wewe utanielekeza, kwani sisi ni watu tusiyowaangalia wanawake kwa nyuma
.
Katika tafsiri ya neno la Mwenyezi Mungu lisemalo kuwa: "Waambie Waumini wanaume wainamimshe macho yao." Imamu Muhammad Al Baqir
anasema: "Kijana mmoja wa Kiansari alikutana na mwanamke fulani katika vichochoro ya mji wa Madina, na huyu kijana akamkazia macho yule mwanamke. Walipopishana kijana huyu akageuza shingo yake na akaendelea kumuangalia yule mwanamke huku anakwenda hali ya kuwa kageuza shingo yake akimuangalia. Basi ghafla alijikuta amejigonga ukutani na damu zikaanza kumchuruzika. Kijana yule kuona hivyo akasema: Ni lazima niende kwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu nikamueleze juu ya kisa hiki. Kijana yule alipofika mbele ya Mtume(s.a.w.w)
hali damu zikiendelea kumtoka, Mtume alimuuliza umepatwa na nini? Yule kijana akasimulia yaliyomfika, na mara Malaika Jibril
alishuka akiwa na Aya inayowaamuru Waumini wanaume wainamishe macho yao.
"
Kipo kisa kingine kinasimuliwa kuhusu hali kama hizi na kinasema kuwa: "Kuna mtu mmoja ambaye kazi yake ilikuwa kuteka maji na kupeleka ndani ya nyumba ya Sonara fulani kwa muda wa miaka thelathini.
Bila shaka kuna wakati yule hakuwako nyumbani kwa mke wa sonara alikuwa akija kumfungulia mlango yule mchota maji ili apate kumimina maji mahala panapostahili. Kipindi chote hiki yule mchota maji hakuwahi kufanya hiyana yoyote dhidi ya mke wa sonara japo kumuangalia kwa jicho la hiyana.
Siku moja wakati yule mama anamfumngulia mlango yule mchota maji, mara ghafla aliunyoosha mkono wake na kumvuta yule mama na akambusu!! Kwa bahati nzuri mwanamke huyu aliuvuta mkono wake kwa nguvu kisha akapiga makelele na hapo hapo akamfukuza yule mchota maji kutoka mule ndani. Baadaye huyu mama alianza kufikiria huku akishangazwa na hali ile iliyojitokeza. Imekuwaje mchota maji yule kufanya hiyana ile baada ya kuwa muaminifu kwa muda wa miaka thelathini?!! Mumewe aliporudi nyumbani mkewe akamuuliza: 'Je leo kuna jambo gani limetokea huko dukani kwako?' Yule mume akajibu kwa kusema: 'Leo kuna mwanamke alikuja dukani kwangu kununua bangili, basi nilipomfunua mikono yake ili apate kuvaa bangili zile, nilimshika mkono wake kisha nikambusu.'! Basi pale pale mkewe alipiga makelele akasema: 'Allahu Akbaru!'
Baada ya hapo alimsimulia mumewe mambo yaliyotendwa na yule mchota maji."
Naam chochote atakachokifanya mtu kuwafanyia wenziwe na wake wa wenzake, basi na yeye yatamfika hivyo kwa mkewe, mama yake, dada yake na binti yake. Ndani ya hadithul Qudsi inasemwa kuwa: "Vile uwatendeavyo wenzako, basi na wewe utatendewa hivyo hivyo." Maana yake ni kwamba: Iwapo utawatendea wema wenzako basi na wewe utatendewa wema, na iwapo wewe utawatendea ubaya wenzako fahamu wazi kuwa na wewe utatendewa ubaya
.
Ewe msomaji mpendwa: Narudia tena kuzungumzia suala la kumuangalia mwanamke asiyekuhusu na ninasema: Hapana shaka kwamba Uislamu ni dini yenye mafunzo yanayokuhamasisha kutenda mema, na wakati huo huo inayo mafunzo ya kukuonya usiyaendee maovu. Ndiyo maana utaiona Qur'an Tukufu pindi Mwenyezi Mungu anapoitaja pepo na neema zake, hapo hapo hufuatisha kuelezea habari za moto na adhabu zake. Yote haya lengo lake ni kumfanya mtu awe katika mazingira ya kutumainia neema na thawabu, na pia awe na khofu ya moto na adhabu kwa upande wa pili. Hivi punde tu umesoma baadhi ya hadithi tukufu zilizosimulia kuhusu adhabu za kumuangalia mwanamke asiyekuhusu na pia matokeo mabaya yanayoletwa na tabia hiyo mbaya.
Hivi sasa umefika wakati wa kuzungumzia hadithi zinazoelezea malipo mema aliyoyaandaa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ajili ya wale watakaojiepusha na mambo ya haramu. Kadhalika hadithi hizo zitaelezea athari njema zinazopatikana kutokana na tabia njema za kujiepusha na mambo aliyoyakataza Mwenyezi Mungu.
Bwana Mtume(s.a.w.w)
anasema: "Kuyatazama mapambo ya wanawake wasiokuhusu ni mshale miongoni mwa mishale ya ibilisi iliyo na sumu, atakayeliacha jambo hilo kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu (s.w.t) basi Mwenyezi Mungu atamuonjesha ladha ya ibada itakayomfurahisha
.
"Katika hadithi nyingine Mtume(s.a.w.w)
anasema: "Kumtazama mwanamke asiyekuhusu ni mshale miongoni mwa mishale ya ibilisi iliyo na sumu, atakaye acha jambo hilo kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu (s.w.t) basi Mwenyezi Mungu atampa mtu huyo imani ambayo furaha ya imani hiyo ataihisi moyoni mwake
.
"
Bwana Mtume anaendelea kutufunza anasema kwamba: "Yainamisheni macho yenu, kwa kufanya hivyo mtaona maajabu (makubwa)
.
Hapana shaka kwamba Mwenyezi Mungu humfunika mtu huyo kwa wingi wa baraka kutokana na kitendo chake cha kuinamisha macho na kutowaangalia wanawake wasiomhusu. Imam Ja'far Sadiq
anasema: "Mwenye kumuangalia mwanamke asiyemhusu kisha akanyanyua macho yake juu au akayafumba (ili tu asimuone mwanamke huyo), Mwenyezi Mungu humuozesha mtu huyo mwanamke wa peponi kabla hajarudisha macho yake chini.
" Anasema tena Imam Ja'far
: "Hawezi mtu yeyote kujihifadhi isipokuwa kwa kuyainamisha macho yake, kwani macho hayatainamishwa kutokana na mambo aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu, isipokuwa ndani ya moyo wa mtu huyo huwa kumetangulia kuuona utukufu wa Mwenyezi Mungu.
" Sasa hivi kumebakia kitu cha mwisho ambacho ni: Je! Ni namna gani basi mtu anaweza kuepukana na jambo hili la haramu, wakati sote tunafahamu kwamba, gonjwa hili la kansa ya wanawake kuvaa nusu Hijabu na kutokujisitiri kwa mujibu wa sheria limeenea? Na kwa bahati mbaya sana hata katika nchi zetu za Kiislamu gonjwa hili limo. Hivi kweli kwa hali tuliyonayo mtu anaweza tena kuinamisha macho yake na ni vipi ataiona njia?
Jawabu la suali hili ni kama ifuatavyo: Sina shaka umesoma baadhi ya Aya na hadithi tulizozitaja. Kinachotakiwa ni kuinamisha macho siyo kuyafumba, na hii ndiyo maana iliyokusudiwa, yaani uangalie chini.
Anachopaswa mtu kukifanya wakati anapomuona mwanamke asiyemhusu, haraka sana ateremshe macho yake chini au aangalie upande mwingine. Kwa hakika Mwenyezi Mungu hawezi kupoteza malipo yake.
1. Usimpe mkono mwanamke asiyekuhusu: Ndugu Mwislamu, Mwenyezi Mungu ameharamisha kumpa mkono mwanamke asiyekuhusu. Mtume Muhammad(s.a.w.w)
amesema: "Yeyote atakayepeana mkono na mwanamke asiyemhusu mtu huyo hujiingiza katika ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na anayedumisha uhusiano (wa kimapenzi) na mwanamke asiyekuwa mkewe, atafungwa kwa mnyororo wa moto pamoja na shetani kisha wasukumizwe motoni
.
2. Usimtanie mwanamke asiyekuwa mkeo: Miongoni mwa mambo ambayo Mwenyezi Mungu amekukataza na kukuharamishia ewe ndugu Mwislamu, ni kufanya utani na mwanamke asiyekuhusu kisheria, kwani jambo hili mara nyingi hukaribisha uovu na pia husaidia kwa kiasi kikubwa kuamsha hisia za maumbile zilizokuwa zimejificha katika pande mbili hizi. Bwana Mtume(s.a.w.w)
anasema: "Yeyote anayemtani mwanamke asiye na milki naye (asiyekuwa mkewe) Mwenyezi Mungu atamfunga mtu huyo miaka alfu moja (huko akhera) kwa kila neno moja alilomsemesha mwanamke huyo
."
3. Usichelewe kuoa: Ndugu yangu Mwislamu, kuoa ni jambo la lazima kwa Mwislamu anapofikia umri wa kubalehe.
a. Ni lazima Mwislamu aoe ili ailinde dini yake, na ndiyo jambo la kwanza apasalo kufahamu.
b. Jambo la pili: Pindi atakapooa atapata radhi za Mwenye Mungu Mtukufu.
c. Na jambo la tatu: Atakuwa amehifadhi nafsi yake kutokana na mambo ya haramu. Kwa hakika Mwenyezi Mungu amemuumba mtu na akamuwekea matamanio ya kijinsiya, na akayafanya kuwa ndiyo matamanio yenye nguvu kuliko mengine yote. Kwa matamanio hayo Mwenyezi Mungu akafanya kuwa ndiyo njia ya kukidumisha kizazi cha wanaadamu, na akafanya kuoa ndiyo njia ya pekee kuyatosheleza matamanio haya. Kwa hiyo kuoa ndiyo njia nzuri na tukufu na ndiyo ufumbuzi wa pekee uliopo kisheria kuhusu tatizo hili la kijinsiya.
Ukweli ulivyo ni kwamba, kuchelewa kuoa kunamfanya mtu akumbwe na mambo mawili.
1. Kwanza: Katika kushindana na matamanio yake kutamfanya aiumize nafsi yake na kupata taabu kubwa ya kuvumilia katika muda huo.
2. Pili: Huenda hatimaye akaingia katika haramu ikiwa ni pamoja na njia isiyo ya kawaida katika kuyatosheleza matamanio yake, au akajikuta anafanya mambo machafu zaidi ambayo ni kinyume na maumbile. Au huenda akafanya uzinifu na matokeo yake ni kuvunja heshima yake au heshima za watu wengine. Na kutokana na hali halisi ilivyo, kila jambo moja katika hayo lina hatari kubwa kwa mtu yeye mwenyewe na heshima yake na utu wake. Kwani kuzuia matamanio na kuyadhibiti kunasababisha kuiadhibu roho na matokeo yake huleta athari mbaya mwilini na hasa katika akili.
Hali hii husababisha kuingia katika dhambi na hatimaye mtu ndipo hujikuta akifanya ambalo hakulitarajia, hapo utu wake huporomoka na mwisho hupata akahukumiwa kwa kosa la jinai na kuingia gerezani na kuishi humo sawa na wezi na wanyang'anyi.