MASIMULIZI (HADITHI) KATIKA QUR'AN

MASIMULIZI (HADITHI) KATIKA QUR'AN0%

MASIMULIZI (HADITHI) KATIKA QUR'AN Mwandishi:
Kundi: Qurani tukufu

MASIMULIZI (HADITHI) KATIKA QUR'AN

Mwandishi: AMIRALY M.H.DATOO
Kundi:

Matembeleo: 8023
Pakua: 2545

Maelezo zaidi:

MASIMULIZI (HADITHI) KATIKA QUR'AN
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 13 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 8023 / Pakua: 2545
Kiwango Kiwango Kiwango
MASIMULIZI (HADITHI) KATIKA QUR'AN

MASIMULIZI (HADITHI) KATIKA QUR'AN

Mwandishi:
Swahili

MASIMULIZI (HADITHI) KATIKA QUR’ANI

MTUNZI: AMIRALY M. DATO0

Maneno Mawili

Bismillahir Rahmanir Rahiim.

Namshukuru Allah (s.w.t) pamoja na Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) pamoja na Ahlul Bayt(a.s) kwa kunijaalia tawfiqi ya kuweza kukitayarisha kitabu hiki.

Mimi binafsi nimekuwa na shauku kubwa ya kusoma hadithi na visa mbalimbali kuanzia utoto wangu na kwa hakika ndiyo maana nimeweza kuwa na faida kubwa kiilimu kwani mafundisho yanayopatikana katika maandiko haya matakatifu na ya wahenga wetu, yanakuwa yamejaa nasiha na mafundisho ambayo si rahisi kuyapata kwengineko. Lakini vitabu vingi vipo ambavyo vinavyo hadithi za uchimvi na vinavyosababisha watu kumomonyoka maadili yao na hivyo kupotoka. Na ndivyo maana inatubidi kujiepusha navyo.

Hadithi hizi nimezitoa kutoka mchanganyiko wa vitabu mbalimbali ili kuwanufaisheni nyinyi wasomaji muvisome na kuwaelezea wananyumba wenu ili nao wafaidike na kuweza kuelewa kuwa Dini na Qur’an Tukufu si kitabu cha kuchosha, bali kama tutasoma ipasavyo, basi sisi tutafaidika mno kwani ndani mwake kuna hazina kubwa ya ilimu na hekima.

Vile kuna vitabu vinginevyo vinavyozungumzia visa, masimulizi kama haya, yaani Visa vya Bahlul, Fadhail na Hukumu zilizotolewa na Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib(a.s) .

Ni matumaini yangu kuwa kitabu hiki na vinginevyo nilivyovikusanya na kuvitarjumu vitawasaidieni nyote. Iwapo utakuwa na maoni yoyote yale nitashukuru iwapo utanitumia ili kuweza kusaidia katika siku za mbeleni.

Wakati huo ninaendelea kutayarisha masimulizi na hadithi nyinginezo za kuongezea hapo mbeleni.

Wabillahi Tawfiq.

MASIMULIZI (HADITHI) KATIKA QUR’ANI

MTUNZI: AMIRALY M. DATO0

MAISHA YA MTUME LUT

Mtume Lut(a.s) alikuwa ni ndugu wa kijamaa wa Mtume Ibrahim(a.s) yaani mtoto wa mamake mdogo na dada yake Mtume Lut(a.s) aliolewa na Mtume Ibrahim(a.s) .

Tendo ovu kabisa lililokuwa katika ukoo wa Mtume Lut (a.s) ni tendo la Ulawiti[1] .

Tabia mbaya

Ulizidi ufisadi katika mji mmoja miongoni mwa miji ya zamani kiasi kwamba atakapoona mtu ufisadi unatendwa na mmoja kati yao basi hakatazwi na mtu mwingine atakapo shuhudia heri inafanywa na ndugu yake basi humkemea mpaka aache heri anayoifanya. Kila mtu katika kijiji hicho alikuwa katika upotevu na uovu na ujinga, hawasikii wala hawasikilizi ilikuwa ni mamoja kwao apatikane mtu wa kuwapa mawaidha wao au mtu wa kuwanasihi wao kulikuwa hakuna tofauti yoyote. Walikuwa ni watu waovu na wabaya zaidi na wenye tabia mbaya miongoni mwa watu, uhai wao (ulikuwa ni khiana na tabia mbaya) na wote hao wakati huo walikuwa ni wenye tabia mbaya sana na nia mbaya. Lakini unaonaje ewe msomaji je walijizuia na maovu yao haya au walizidi katika upotevu na ufijari na madhambi ?

Kuenea mambo ya haramu

Ilikuwa kama kwamba nafsi zao hazikutosheka na kule kusema uongo na kuwa na tabia mbaya na ghadr na mengineyo mengi, wakasababisha na kuleta mambo ya unyama ambayo hakutangulia kufanya yeyote kabla yao. Je ni mambo gani hayo?

Hakika waliacha mambo aliyoyahalalisha Allah (s.w.t) kwao kwa wanawake na wakawa hawaoi wanawake ! Wakawaacha wake zao na kuanza maovu ya kuingiliana na wanaume wenzao. Jambo ambalo Allah (s.w.t) aliliharamisha kabisa.

Na laiti wao wangesitiri haya maovu au wakajaribu kujiepusha kutoka katika maovu haya au kujiweka mbali nayo ingelikuwa afadhali lakini wao walijitumbukiza katika mambo hayo na wakawa wanayatangaza wazi wazi mpaka ukaenea ufisadi na kukaenea mambo ya haramu na zikawa tabia zao mbaya ni rahisi kiasi kwamba zikawa zimefikia daraja kubwa sana na yote hayo yalikuwa ni madhambi na ufisadi wala hawezi mtu yeyote kuyafanya wala kufikiria binaadamu au kupiga picha ya binaadamu katika akili yake.

Mlinganio wa Mtume Lut(a.s) .

Na walipofikia hali yao ya ufisadi kiwango hiki ndipo Allah (s.w.t) alipompa Wahyi mtu mmoja miongoni mwao jina lake Mtume Lut(a.s) . na kukaanza kwake yeye matangazo ya wema na heri. Allah (s.w.t) alimpa Wahyi akamwamrisha kwamba afanye kazi ya kuubadilisha umma wake au kaumu yake na Mtume Lut(a.s) alijibu maombi haya ya Allah (s.w.t) wake na moja kwa moja akaanza kufanya kazi hii ya kuwalingania watu kwenye heri na wema na akawa anasema:

“Enyi watu wangu! Zitoharisheni nafsi zenu na acheni mambo maovu.

Enyi watu wangu! Hakika kitendo chenu hiki ni haramu na Allah (s.w.t) haridhii kuwaacheni nyinyi katika hali hii bila ya kukupeni uongofu basi anayenituma mimi kwenu na mimi ni miongoni mwenu na siwezi kunyamaza juu ya jambo hili la haramu.

Enyi watu wangu! Fanyeni Tawbah ya Allah (s.w.t) na mjiepushe na nia zenu kwa ajili Yake.”

Kiburi

Lakini kaumu ya Nabii Mtume Lut(a.s) ambao uliwazidi wao uovu na ukawafunika wao mambo ya haramu hawakusikiliza maneno ya Mtume Lut(a.s) isipokuwa walizidisha kiburi na wakapinga ‘ibada ya Allah (s.w.t) na kuacha mambo haramu na wala hawakunyamaza kuyafanya maovu yao bali waliendelea kufanya kiburi na wakafanya njama kwamba wamwondoe Mtume Lut(a.s) na watu walioamini maneno ya Mtume Lut(a.s) katika kijiji chao kwa sababu Mtume Lut(a.s) na watu walio mwamini Mtume Lut(a.s) hawafanyi mambo ya uovu kama wanavyofanya wao bila wanajitoharisha. Hivyo wakamwendea Mtume Lut(a.s) huku wakimwonya na wakimtaka kwamba atoke kwenye kijiji chao. Na vile vile walimwahidi kuwa atatoka tu kwani watamfanyia njama na majungu mpaka atoke kijijini humo.

Maonyo

Wakati walipoona Mtume Lut(a.s) njama na kiburi kutoka kwa kaumu yake, akarudia maneno yake kwa kuwaambia wao na kuwaonya na kuwafahamisha matokeo ya njama zao watakavyo fanya na akuwaambia wao

“Enyi kaumu yangu ! Kama hamtafanya Tawbah na kuacha haya maasi basi kwa hakika Allah (s.w.t) atawashushieni adhabu kutoka mbinguni. Hakika Allah (s.w.t) anakuoneni nyinyi na wala hakuathirika na nyinyi na yeye hapendi ukafiri na wala ufisadi na wala hawapendi watu wanaofanya ufisadi.

Rejeeni na mfanye tawbah kwa Allah (s.w.t) na acheni madhambi na mambo mauovu.

Hakika mimi naogopa adhabu ya Allah (s.w.t) na mateso yake yatakayo shuka kwenu”.

Na pamoja na haya hawakusikiliza maneno yake isipokuwa walimfanyia mzaha na kumtania na wakamkemea kwamba atatoka tu pamoja na watu walio mwamiani yeye kwa sababu wao wanajitoharisha wenyewe kwa wenyewe na hawakujali wao kwamba yeye Mtume Lut(a.s) ni mfanya dhambi au makosa yoyote.

Kujibu kwa Allah (s.w.t)

Na hakika Allah (s.w.t) hakumwacha Mtume Lut(a.s) na watu walio mwamini yeye bila ya kuwanusuru na kuwapa ushindi wala hakuwaacha makafiri waliokuwa madhalimu bila ya kuwaadhibu wao.

Ni hawa makafiri ambao wamedhihirisha ufisadi na huyu Mtume Lut(a.s) ambaye anawatahadharisha na kuwazuia wao bila ya kupata majibu yoyote mwisho.

Hatimaye Mtume Lut(a.s) akalazimika kumwomba Allah (s.w.t) awateremshie juu ya watu hawa adhabu na tutanaona kwamba madhalimu hawataweza kumtoa Mtume Lut(a.s) au kuizuia au kuifukuza adhabu itakayowamiminikia juu yao.

Allah (s.w.t) akajibu dua ya Mtume Lut(a.s) na akaishusha !

Malaika wako kwa Mtume Ibrahim(a.s)

Allah (s.w.t) amewatuma Malaika kwenda kwa watu wa mji huu wakapitia kwanza katika nyumba ya Mtume Ibrahim(a.s) na Malaika hawa walikuwa katika umbile la binaadamu (Mtume Ibrahim(a.s) aliwakaribisha na kuwawekea chakula ili wale, lakini wao hawakula, kwani Malaika huwa hawali chakula) Mtume Ibrahim(a.s) akawaogopa wao.

Malaika wakamwambia Mtume Ibrahim(a.s) :

Usiogope hakika sisi ni Malaika kutoka kwa Allah (s.w.t) na tumetumwa kwa kaumu ya Mtume Lut (a.s) watu waovu ili tuwaadhibu wao lakini tumepita kwako ili tukubashirie wewe kwamba utazaa mtoto .”

Mtume Ibrahim(a.s) kwa kuyasikia hayo alifurahi mno yeye pamoja na mke wake (na yeye akiwa ni mwenye umri mkubwa hakuzaa mpaka hivi sasa).

Mtume Ibrahim(a.s) aliwaonea huruma watu wa kaumu ya Mtume Lut(a.s) na akaogopa kwamba yasije yakamfika madhara Mtume Lut(a.s) kwa hiyo Malaika nao wakamjibu kwamba (hakuna hofu yoyote juu ya Mtume Lut(a.s) isipokuwa mke wake alikuwa ni miongoni mwa makafiri………..!

Kwenda kwenye kijiji cha Mtume Lut (a.s)

Wakamwacha Mtume Ibrahim(a.s) na wakaenda zao kwa Mtume Lut(a.s) wakiwa katika maumbo ya vijana wa kiume wenye sura nzuri sana wakaenda moja kwa moja mpaka kwenye kijiji cha watu wadhalimu na wakaingia katika nyumba ya Mtume Lut (a.s), Mtume Lut(a.s) akaogopa kwamba wasije wakamfedhehesha watu wake kwa mambo yao maovu yanayo julikana.

Mtume Lut (a.s) alijaribu kuwaficha hao na habari za wageni wake bila kujua kwamba wao ni malaika lakini wale Kaumu waligundua jambo lile na wakapeana habari wao kwa wao kwamba waanze kufanya uovu wao kwa wale wageni wa Mtume Lut (a.s) Basi ni nani ambaye ametangaza siri ile iliyofichwa kwamba nyumbani kwa Mtume Lut (a.s) kulikuwa na wageni wazuri ?

Hakuna shaka kwamba yuko aliyejua jambo lile na akaenda kwa makafiri kuwapa habari na hakuna shaka kwamba huyu aliyeitoa habari ni kafiri kama wao na kwa sababu hii ndipo akawajulisha wao juu ya jambo hili la uovu.

Mke wa Mtume Lut (a.s)

Hakika mke wa Mtume Lut (a.s) ndiye aliyetoa habari kuwapa wale watu na kuwafahamisha jambo la wageni na kwamba yeye huyo mwanamke alikuwa kafiri na alitangaza ukafiri na akaitoa nje siri na haraka wakaja makafiri katika nyuma ya Mtume Lut (a.s) wakawa wanamtaka Mtume Lut (a.s) awakabidhi wao wageni wake ili wawafanyie mabaya.

Akaogopa Mtume Lut (a.s) na akawaomba wao wajitenge na kujiepusha kabisa na jambo hilo lakini wao walikuwa ni makafiri na watu waovu kabisa ambao wamefikia daraja kwamba hawasikii nasaha ya mtu yeyote na wala hawawezi kujiepusha na maovu.

Mtume Lut (a.s) alifunga milango mbele yao na aliwaghadhabikia sana na katika dakika chache tu wao kwa ujeuri wakaingia kwenye nyumba na wakataka kufanya ulawiti juu ya wageni wa Mtume Lut (a.s)

Ukweli

Alikaa Mtume Lut (a.s) akiwa mwenye kuhuzunika kwa kuingia waovu ndani ya nyumba yake lakini wale wageni ambao walikuwa mle ndani walicheka tu kwa kuingia watu hawa ndani ya nyumba ya Mtume Lut (a.s) na waligeuza nyuso zao kumwelekea Mtume Lut (a.s)na wakamtuliza yeye kwa kumwambia kuwa wao ni Malaika kutoka kwa Allah (s.w.t) na wakamwambia Mtume Lut (a.s) :

“Hakika sisi tumekuja kukuokoa wewe pamoja na waliokuamini wewe. Usituogopa na tunakuomba uiache nyumba yako wakati wa mwisho wa usiku.

Wewe pamoja na wafuasi wako mutajitenga mbali na kutoka katika kijiji hiki ambacho kitashushiwa adhabu kutoka kwa Allah (s.w.t).

Na tunakuomba umwache mkeo kwani yeye ni Kafiri aliye pamoja na watakao adhibiwa naye ni mfano wao anafanya na kuwapa msaada watu waovu.”

Na baada ya hapo alifurahi mjumbe wa Allah (s.w.t) na ikamwondokea hofu moyoni mwake.

Mwisho wa woga

Akatoka Mtume Lut (a.s) na watu wake (isipokuwa mkewe) Mtume Lut (a.s) akakiacha kile kijiji bila ya kukisikitikia mpaka akawa mbali kabisa na kile kijiji na ikaja amri kutoka kwa Allah (s.w.t) ya kushushiwa adhabu. Yakashuka mawe na ikatikisika ardhi na yakapinduliwa majumba na kubomoka na zikaanguka sakafuni na ikawa ardhi yao juu chini na chini juu.

Je nini kimepita ? Hiyo ni adhabu ya Allah (s.w.t) na hayo ndiyo mateso hakika wamekuwa makafiri chini ya kupondwa pondwa na kuharibiwa majumba yao na kubomolewa na mizoga yao kutawanyika yote haya ndio malipo ya kazi yao mbaya ya ukafiri na ubishi wao kwani wao walifanya kiburi na wakapinga uongofu.

Mwisho wa Haki

Na baada ya kufa makafiri je kwa maoni yako nani alibakia ? Ni nani alipata ushindi na akaishi ?

Jibu ni kwamba wale walioamini ( Mtume Lut (a.s) na watu wake ambao walimwamini yeye) ama mke wake ambaye alishiriki na makafiri na hivyo alikufa pamoja na makafiri na hivyo ndivyo ilivyo uongofu siku zote huwa juu na uovu hurudi chini na hali hii ni ya kudumu.

Enyi ndugu zangu kwa hivyo tutakapopigana Jihadi, tukasubiri na kuvumilia magumu, hakika ushindi utakuja kuwa pamoja nasi mwisho wake na Allah (s.w.t) atawagharikisha wale wenye kiburi. Hakika Allah (s.w.t) yu pamoja na wacha Mungu ambao wao ndio wenye kufanya wema.

Na ninataka kukuulizeni enyi vijana mashujaa kabla sijawaageni mwisho wa kisa hiki :

Je mnajua kwa nini tunasoma visa hivi?

Kwa hakika sisi tunasoma visa hivi ili tufahamu haki kutokana na visa hivi na hakika ya sisi tutazichukua nafsi zetu moja kwa moja kufuata haki hii na tutafuata maneno yaliyo mazuri na maana iliyo nzuri na sisi tuko pamoja na Allah (s.w.t) na wanao mcha Allah (s.w.t) na waumini na tunamshukuru Allah (s.w.t) kwa kutoa neema ya imani ya ucha Mungu.

MASIMULIZI (HADITHI) KATIKA QUR’ANI

MTUNZI: AMIRALY M. DATO0

MAISHA YA MTUME SALEH

MTUME SALEH (A.S) ALIITWA:

Mtume Saleh (a.s) bin Abud bin Asif bin Nasikh bin Abud bin Hadir bin Thamud bin Amir bin Sam bin Nuh.

Kabila lake lilikuwa likiishi mipaka ya Kusini ya Syria katika milki iliyokuwa ikijulikana kama Al-hijr au Al-Hajar na ilijulikana kama Wadi-ul-Qura.

Mtume Saleh (a.s) alikuja baada ya Mtume Hud (a.s) na alitokana na kizazi cha tisa cha Mtume Nuh (a.s)

Urithi

Baada ya kuangamiza Allah (s.w.t) Qaum-u-‘Aad ambao hawakuyasikiliza maneno ya Mtume wao Hud (a.s) na baada ya kufa hao wote ikabaki ardhi yao bila majumba wala wakazi wala mimea hata wanyama na baada ya haya yote Allah (s.w.t) aliirithisha ardhi yao kwa Qaum nyingine nao ni Qaum Thamud. Wakaja Qaumu Thamud mahali pakawa Qaum-u-‘Aad Allah (s.w.t) aliwaneemesha neema nyingi kuliko Qaum ‘Aad.

Walijenga Qaum Thamud majumba kati ya majabali na wakalima mabustani na makonde na wakatoboa mito lakini pamoja na masikitiko makubwa hazikuwa akili zoa zina maendeleo kuliko Qaum iliyotangulia.

Ni hao hao ambao waliabudu masanamu na mawe na wakadhani kwamba neema yao haitoondoka na wala haitatoweka.

Ujumbe

Na mbele ya utakafiri huu na ujinga Allah (s.w.t) alimtuma kwao mwanamme miongoni mwao anayeitwa Mtume Saleh (a.s) na yeye miongoni mwa watukufu wao na mwenye akili katika wao ambaye alimuamini Allah (s.w.t) wake na Allah (s.w.t) alimchagua yeye ili awaongoe hawa Majahili waliopotea akawalingania wao kwenye ibada ya Allah (s.w.t) na akatilia mkazo na akawaimiza wao juu ya Tawhid yaani kumpwekesha Allah (s.w.t) na kuacha kumshirikisha Yeye ni Yeye ambaye aliwaumba wao na akawaumbia wao ardhi na akawapa wao miongoni mwa fadhila Zake na neema Zake kisha akawakataza wao kuabudia masanamu ambayo wameyatengeneza wao wenyewe.

Kwani hayo masanamu hayadhuru wala hayanufaishi chochote na wala hayamtoshelezi mtu kutoka kwa Allah (s.w.t) chochote kisha akawakumbusha wao kwamba yeye ni miongoni mwa wao na yeye anapenda kuwanufaisha wao na wanapojipatia maslaha yao na akawaamrisha wao wamtake msamaha Allah (s.w.t) na watubu kwake Yeye kwani yeye ni mwenye kusikia na mwenye kujibu na anakubali toba kwa yule mwenye kutaka msamaha kwake.

Upingaji

Lakini masikio hayakusikiliza wala nyoyo hazikufunguka na macho hayakuona wakapinga na kumpinga Mtume Saleh (a.s) pamoja na ujumbe wake na wakawa wanamfanyia mzaha kwa ujumbe wake na wala hawakusimama kwao ukafiri mpaka kufikia kiwango hiki bali walisema kumwambia Mtume Saleh (a.s):

“Ewe Mtume Saleh (a.s) sisi tumekujua wewe kwamba ni mwenye akili na mwongozi na tulikuwa tunakuuliza wewe na tulikuwa tunakutaka ushauri wewe katika mambo yetu una nini leo unatamka mambo ya upuuzi na upi huu msamaha ambao wewe unatuitia sisi kwao aidha sisi tunaabudu walichokua wanaabudu mababa zetu miongoni mwa masanamu na miungu aidha sisi hivi sasa tupo katika shaka kwa kile unachotuitia sisi kwacho na wala hatutaamini maneno yako na wala hatutosadiki na kuacha itikadi zetu na itikadi za mababu zetu kwa ajili yako.”

Kutahadharisha

Aliposikia Mtume Saleh (a.s) kutoka kwao maneno haya aliwajibu wao kwa hali ya subira na kihekima akisema:

“Enyi watu hakika ambayo nayasema ni haki na hakika ya mnacho kiabudu miongoni mwa mawe ni batili na hakika mimi naogopa kwenu kutokana na nguvu za Allah (s.w.t) ambaye mnamkufurisha baada ya kukupeni nyinyi mali na majumba na mabustani.

“Enyi watu mtakeni msamaha Allah (s.w.t) hakika mimi ni mjumbe wa Allah (s.w.t) kwenu wala sitaki kwa nyinyi mali wala urais hakika si jambo lingine nachotaka mimi ni kukuongoeni nyinyi na kujalieni nyinyi mfikiri na malipo yangu mimi yapo kwa Allah (s.w.t) Bwana wa viumbe wote ambaye amenituma mimi kwenu na yeye ambaye atanilipa mimi Akhera na ataneemesha kwenu neema nyingi ikiwa nyinyi mtajibu na kukubali Da’awa yangu kwa imani na kwa kusilimu.

Wanyonge

Na katika kila kaumu enyi ndugu zangu hupatikana watu wenye akili na ambao wanapenda nasiha na katika Qaumu ya Thamud kulikuwa na kikundi cha watu wachache miongoni mwa watu wanyonge ambao waliona kwamba utajiri haunufaishi chochote mbele ya ujahili wakafikiria kwa akili zao wakaona kwamba hakika anachowaitia Mtume Saleh (a.s) ni cha haki na kuingia akilini.

Hakika Allah (s.w.t) ameumba ulimwengu na masanamu hayanufaishi chochote japokuwa waliabudia hayo masanamu mababa na mababu vikafunguka vifua vya kikundi hiki cha watu wachache na wakaingia katika dini mpya na wakatangaza kusilimu kwao na wakaingia katika imani na kwa hali hii wakawa pamoja na Mtume Saleh (a.s) baadhi ya watu walio amini miongoni mwa kaumu yake walioshudia kwamba hakuna mungu isipokuwa Allah (s.w.t) na kwamba yeye Mtume Saleh (a.s) ni mjumbe wa kutoka kwa Allah (s.w.t)

Subira na Jihadi

Na ama ambao waliofanya kiburi na wakazuia Da’awa ya Mtume Saleh (a.s) kwa vitimbi vyao na wakashikamana kwa ibada zao za kuabudu masanamu na wakamwambia Mtume Saleh (a.s) kwamba hakika Shetani amekutania wewe na ukawa unatamka mambo ya wazimu kisha wakawa wanamzuia yeye kunako dini yake lakini yeye alisubiri na akavumilia kutokana na maudhi yao na vitimbi vyao na akaendeleza tablighi yake na akasema:

Enyi watu hakika mimi sikuacha dini ya haki na nikakufuru kama mlivyo kufuru nyinyi na wala hamtoweza kurudisha kwangu mimi adhabu inayotoka kwa Allah (s.w.t) .”

Lakini ikiwa mmeingia katika Uislam na mkapata uongofu na imani hakika Allah (s.w.t) atakuingizeni nyinyi baada ya kuamini kwenu Jannat (peponi) siku ya Qiyama.

Enyi watu hamkuwa nyinyi isipokuwa ni waongo mnaacha kutumia akili zenu na mkafata matamanio yenu na mkawa miongoni mwa makafiri.

Hofu

Na walipo kutakwamba imani imepata nguvu na subira na mshikamano wenye nguvu waliogopa Mustakbirun kwamba kikundi cha waumini wachache kitazidi na kuwa chenye nguvu hakika waliogopa enyi ndugu zangu juu ya mali zao na maslaha yao na wakaogopa juu ya dola yao na ufalme wao basi vipi wataishi kesho ikiwa idadi ya Muumina itaongezeka.

Hakika hakuna budi ila kuondoa mushkili huu walifikiri makafiri juu ya jambo hili ambalo lilikuwa linawahuzunisha wao na serikali yao wakaona kwamba wamuombe Mtume Saleh (a.s) baadhi ya mambo ayafanye wakidhani kwamba hatoweza kuyafanya hayo mambo na baada ya hapo watajitenga watu ambao walioamini baada ya kudhihiri kushinda kwake na udhaifu wake.

Kuomba muujiza

Na kawaida ya makafiri ambao hawaamini wao hupenda kuwatenganisha watu kutoka kwenye imani ili wawe kama wao na walidhani hawa makafiri kwamba makafiri kutoka kaumu ya Mtume Saleh (a.s) kwamba watakapo mtaka Mtume wao jambo gumu na atakapo shindwa kulifanya hakika wanachomtakia wao kitakuja kuthibitika. Na watakuja hao makafiri kwa Mtume Saleh (a.s) wakizungumza naye kuhusu muujiza wake na wakimtaka awaletee wao huo muujiza ili hiyo dalili juu ya ukweli kwa jambo lake na kwamba yeye ni mtume wa Allah (s.w.t) kama wanavyodai kwake. Na hakika walisema kwamba watakapo taka tukuamini wewe na kuamini ujumbe wako tuletee muujiza ili tukuamini la sivyo sisi tutabaki katika ibada yetu ya masanamu.

Ngamia

Hakika ya Mtume Saleh (a.s) hawezi kufanya jambo lolote isipokuwa kwa idhini ya Allah (s.w.t) na vipi ataweza kufanya jambo na yeye ni mtu kama wao. Hakika Allah (s.w.t) enyi ndugu zangu anajua kwamba makafiri wengi hawaamini hata kama wataona muujiza lakini ili uwe ukafiri wao ni hoja iliyo batilika hakika Allah (s.w.t) alituma kwao Ngamia wa ajabu na muujiza wa Ngamia huyu kwamba yeye anakunywa maji siku moja na kujizuia kunywa maji siku ya pili na akasema Mtume Saleh (a.s) kuwaambia kaumu yake kwamba huyu Ngamia amemtuma Allah (s.w.t) na atakuwa kinywaji chake katika kijiji ni cha kupokezana siku moja ni yenu nyinyi na siku moja ni yake yeye. Jiepusheni na kumuuzi Ngamia huyu na msibadilishe amri na nidhamu hii.

Hofu kutoka kwa makafiri

Na hakika Mtume Saleh (a.s) alijua kwamba makafiri imewaogopesha amri hii ya Allah (s.w.t) kwa hivyo watafanya njama ya kumuua Ngamia.

Kwa sababu hiyo alikwenda Mtume Saleh (a.s) kwa kaumu yake na yeye akiwaambia kwamba (msimfanyie mabaya Ngamia huyu na mtakapo muudhi Ngamia huyu basi Allah (s.w.t) atashusha adhabu juu yenu kwa haraka). Hakika amewafikishia Mtume Saleh (a.s) ujumbe na akawatahadharisha wao na akawaonya lakini makafiri waliona kwamba huo muujiza uko wazi na unajulisha wazi Utume wake, wakaogopa isije ikazidi idadi ya walioamini na wakaongezeka waliokuwa pamoja na Mtume Saleh (a.s), basi wao yaani makafiri hawapendi watu waamini au waamini mwingine zaidi ya walioamini kwa sababu hiyo kwamba wao walifikiri katika njia nyingine kinyume cha Mtume Saleh (a.s) na sasa hawataki tena muujiza mwingine na kwamba wao walikengeuka kwenye kitu kingine.

Njama

Hakika waliangalia makafiri kumwangalia Ngamia mnene wa ajabu wakaogopa juu ya serikali yao kutokana na muujiza huu ulio wazi na wadhahiri na kwamba muujiza huu unavuta nyoyo za watu na unazivutia nafsi za watu. Yote haya yaliwafanya wao wafikirie juu ya muujiza huu nao ni Ngamia kwamba ni muujiza wa hatari na wao hawawezi kuepuka hatari hii ila kwa kumuua Ngamia, wakafikiria mbinu ya kutimiza njama zao na mwisho wakaafikiana kwamba waende baadhi yao mahali anaponywea maji Ngamia na huko huko watamwulia wakati Ngamia anaporejea kutoka mahali anaponywe maji na wao watakuwa wamejiepusha na muujiza huo wa Mtume Saleh (a.s) wenye kutisha na kuogopesha.

Mapambano ya Ngamia

Moja kwa moja kikatoka kikundi cha makafiri kikaenda zake hadi kwa Ngamia wakisubiri marejeo yake kutoka mahali anaponywea maji na wakati alipokuwa akirejea Ngamia, akatupa mmoja wao kumtupia Ngamia mshale ambao ulimchoma na akaanguka Ngamia juu ya ardhi na wala hakutosheka na hayo bali wakamchinja ngamia na kumuua kisha wakarudi kumwendea Mtume Saleh (a.s) huku wakisema kwamba hakika ulitutahadharisha sisi na adhabu ikiwa tutamuua Ngamia, tuletee adhabu ! Haya hatutarudia kukuogopa wewe wala Ngamia wako. Mtume Saleh (a.s) akawajibu fanyeni starehe zenu kabla ya adhabu ya Allah (s.w.t) na mateso, hakika nilikutahadharisheni kwa kutokumuua Ngamia na mkamuua basi subirini adhabu iliyo ahidiwa na Allah (s.w.t)

Maiti zilizoganda

Hakika ahadi ya Allah (s.w.t) ni kweli na adhabu ni karibu, kisha makafiri wakamuomba Mtume Saleh (a.s) afanye haraka au aharakishe adhabu kwao na wao waliyasema haya katika hali ya kumfanyia mzaha Mtume Saleh (a.s) wakaafikiana makafiri upya kwamba wamuue Mtume Saleh (a.s) na watu wake wakiwa wao usingizini usiku, lakini Allah (s.w.t) hakusahau na wala hakumsahau Mtume wake aliye muumin na walioamini pamoja waliomwamini Mtume Saleh (a.s) na ulipoingia usiku ikaja ahadi ya Allah (s.w.t) na adhabu yake ukavuma upepo mkali ulio mkubwa na wenye kutisha ukawafanya makafiri kuwa ni miili iliyoganda haitikisiki abadan, akaamka Mtume Saleh (a.s) na akaona yaliyo pita juu ya makafiri na akajua kwamba Allah (s.w.t) amesha wateketeza na kuwaangamiza wao, na Allah (s.w.t) akamwamsha Mtume Saleh (a.s)

Na yeye akawaamsha wale waliokuwa wamemwanini yeye na akasema:

Enyi watu wangu! Hakika nimekufikishieni nyinyi ujumbe wa Allah (s.w.t) na nikakuonyeni lakini hamuwapendi wenye kutoa nasiha .”

Mwisho

Na sasa je mmeona enyi ndugu zangu vipi kafiri asiyamini vile muujiza usivyomfaa yeye chochote na anavyouogopa ?

Nao waliomba muujiza kutoka kwa Allah (s.w.t) naye akatuma Ngamia na Mtume Saleh (a.s) akawatahadharisha wao wasimwudhi Ngamia na wao wakamwudhi na vile vile wakamwua na Mtume Saleh (a.s) aliwatahadharishia adhabu, wao wakaiomba adhabu na kisha Mtume Saleh (a.s) akawaahidi wao adhabu na wakasema iletwe haraka kwao.

Je walipata faida yoyote kutoka kwa muujiza ?

Jibu ni kwamba wao hawakufaidika chochote.

MASIMULIZI (HADITHI) KATIKA QUR’ANI

MTUNZI: AMIRALY M. DATO0

WATU WA UKHDUD (MAHANDAKI)

Qurani Tukufu inatuambia: Sura Al-Buruj, 85, Ayah ya 4 - 9.

Kuwa walioangamizwa walikuwa watu wa mahandaki. Ya Moto wenye kuni. Walipokuwa wamekaa hapo. Wakitazama yale waliyokuwa wakiwatendea waumini. Wao waliwatesa (hao) si kwa kingine ila hao walimwamini Allah, Mwenye kushinda (na) Mwenye kusifiwa. Ambaye ni Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi; na Allah ni Mwenye kuona kila kitu.

Kuulizia

Imam wa tano, Muhammad ibn-‘Ali Al-Baquir (a.s) anasema kuwa siku moja Imam wa kwanza, Imam ‘Ali ibni Abi Talib (a.s) alimtuma mtu kwenda kwa wakuu wa dini ya Wakristo wa Najran kwa kuwauliza kuhusu watu wa Mahandaki --- na baada ya kupata majibu yao, aliwatumia ujumbe kuwa:

“Kile mukihadithiacho kuhusu watu hao, si hadithi ya kweli na kwa hakika hadithi ya kweli ni kama ifuatavyo.”

Kisa cha kweli

Zu-Nuwas alikuwa ni mfalme wa mwisho wa kabila la Hamir, mwishoni mwa karne ya sita A.D. Yeye alikuwa ni mfuasii wa dini ya Juda ( dini ya Kiyahudi) na hivyo ilikuwa ndiyo dini ya Serikali. Dini hiyo ya Juda ilikuwa imeachwa na watu baada ya kuja Mtume ‘Isa (a.s) Lakini Zu-Nuwas aliendelea kuwaadhibu vikali mno wale wote walioifuata dini ya Mtume ‘Isa (a.s) na alitumia mbinu mbalimbali na hila za kuimaliza dini hiyo katika kila sehemu za ardhi. Yeye alikuwa akiwapendelea mno Mayahudi na kuwatesa vikali mno Wakristo.

Yeye aliwateketeza Wakristo popote pale walipoonekana katika ufalme wake. Yeye alikuwa ameamua kuusambaza Uyahudi katika kila sehemu za dunia huku akizimaliza na kuzifyeka dini zingine zote. Yeye hakubakiza juhudi zake zozote katika kufikia lengo lake hilo. Yeye vile vile alikuwa akizishambulia nchi zozote zile ambazo zilikuwa zikifuata dini mbali na dini ya Juda. Na vile vile alikuwa mwepesi wa kuzishambulia sehemu zozote zile zilizokuwa zikifuata dini mbali na dini ya Juda na hatimaye kuwalazimisha kuifuata dini yake.

Allah (s.w.t) alimtuma Mtume mmoja wa Kihabeshi kwenda kuhubiri watu wa Habeshi. Mtume huyo alipambana sana na mfalme huyo ambaye alikuwa akiipigania dini yake ya Kiyahudi kwa hali na mali.

Katika kuupiga vita Ukristo

Siku moja alipata habari kuwa wakazi wa Najran wamekubalia dini ya Mtume ‘Isa (a.s) isipokuwa Wayahudi wachache tu ndio waliokuwa wamebakia katika dini yao. Habari hizi zilimghasi na kumbughudhi mno huyo Zu-Nuwas kiasi kwamba aliupoteza usingizi wake na kukosa raha kabisa na kufikia uamuzi wa kuishambulia sehemu hiyo kwa haraka iwezekanavyo. Na hivyo alilitayarisha jeshi kubwa mno na kuwapatia silaha nyingi zilizo nzuri na alijitolea mwenyewe kuongoza vita hivyo vya kuishambulia Najran. Kwa hakika alikuwa amewaghadhabikia mno wakazi wa Najran kiasi kwamba alikuwa anataka awarudishe wote kwa pamoja katika dini ya Kiyahudi kwa haraka iwezekanavyo. Alipoukaribia mji wa Najran, aliwataka baadhi ya watu waliokuwa wameheshimika huko kuja kuwawakilisha wakazi wa Najran katika mazungumzo yao pamoja na Zu-Nuwas.

Wakati watu hao walipoletwa mbele yake, yeye aliwaambia:

“Mimi nimekuja hapa baada ya kupata habari kuwa wakazi wote wa mji wenu wameiacha dini ya Kijuda na wamekubali dini ya (Mtume) ‘Isa (a.s) kwa sababu ya kudanganywa na kushawishiwa na Mkristo wa Kikatoliki aitwaye Dus. Hivyo mutambue kuwa mimi nimefika hapa pamoja na jeshi langu hili lililo kubwa sana ili kuirudisha dini ya Kijuda hapa Najran na kuutokomeza kabisa Ukristo. Swala hili la kuwaiteni nyinyi hapa ni kuwatakeni nyinyi murejee kwenu mukaongee na wazee wenu ili wakazi wote wa Najran warudie katika dini ya Kijuda na kuiachilia mbali dini ya Kikristo. Kuna mambo mawili tu yaliyo bayana mbele yenu. Ama mukubali kuingia katika dini ya Kijuda ama sivyo mujiweke tayari kwa adhabu kali kabisa ambayo hayatakuwa chini ya adhabu ya kifo na maangamizo.”

Watu wamkabili Zu-Nuwas

Wawakilishi hawa wa wakazi wa Najran walikuwa ni watu ambao walikuwa na imani thabiti ya dini yao na hivyo wote kwa pamoja walimwelezea wazi wazi mfalme Zu-Nuwas kuwa:

• “Sisi kamwe hatutaki ushauri na uwakilishi wa mtu yoyote yule.

• Sisi tumeshatambua na kuipata njia ya haki na uongofu na hivyo tunafuata mafunzo na maamrisho yake.

• Sisi kamwe hatuogopi mauti.

• Sisi tupo tayari kukabiliana na hali yoyote ile itakayotokezea na tutakabiana nayo ipasavyo na hata kama itabidi kujitolea mhanga, basi tutafanya hivyo ili kuilinda dini na imani yetu.”

Zu-Nuwas alikuwa hakutegemea kupewa majibu makali na yaliyo wazi kabisa kuhusu msimamo wa wakazi wa Najran, na hivyo alizidi kukasirika.

Alifikia uamuzi wa kuwamaliza na kuwateketeza Wakisto wa Najran. Hivyo yeye aliwaamuru majeshi yake kuchimba mahandaki na kuyajaza kwa moto mkali kabisa. Yeye pamoja na majeshi yake walikaa kandoni kwa kuzunguka mahandaki hayo kwa kushuhudia hali mbaya kabisa.

Baadaya ya hapo, alitoa amri ya kuwa waumini wote wa dini ya Kikristo waletwe mbele yake. Kwa kutolewa amri hiyo, majeshi yake yalitoka kuwatafuta Wakristo wote na kuwaleta mbele ya Zu-Nuwas.

Ikatolewa amri ya kuwatupa hao katika mahandaki hayo yaliyokuwa yakiwaka moto mkali sana. Wengi walisukumwa na kuchomwa hivyo na wengine walichinjwa. Vile vile walikuwapo wengine ambao walikatwa viungo vya mwili kama masikio, pua, mikono na miguu. Hivyo ndivyo Najran ilivyotokana na watu ambao waliikuablia dini ya Mtume ‘Isa (a.s)

Inasadikiwa kuwa Zu-Nuwas amewaua watu zaidi ya elfu ishirini (20,000) katika kulazimisha dini ya Kijuda.

Kutorokea Roma

Mmoja wa Wakristo alipoyaona mateso na maagamizo waliyokuwa wakitendewa wafuasi wenzake wa Kikristo, alifanikiwa kutoroka na kwenda mjini Roma akipitia majangwa na milima hadi kwa Czar, aliyekuwa mfalme, na kumpa habari zote zilizowafikia Wakristo wa Najran chini ya amri za Zu-Nuwas na alitoa ombi la kupatiwa majeshi ili kuweza kulipiza kisasi na kumshinda.

Majibu ya Czar

Czar alikuwa Mkristo kwa dini na alihuzunika mno kwa kusikia unyama wa Zu-Nuwas. Yeye alimwambia yule mtu kutoka Najran kuwa:

“Kwa hakika nchi yenu ipo mbali mno na kwetu na hivyo mimi siwezi kuchukua hatua yoyote ile dhidi ya Zu-Nuwas. Hata hivyo mimi ninamtumia risala maalum mfalme wa Habeshi, Najjashi (Negus) ambaye pia alikuwa Mkristo. Ufalme wake upo karibu na Yemen, ufalme wa Zu-Nuwas. Kwa hakika itakuwa rahisi kwa Najjashi kumshinda Zu-Nuwas.”

Mfalme wa Kiroma alimtumia risala maalum Najjashi akimtaka amng’oe Zu-Nuwas na kuwakomboa Wakristo wa Najran. Mtu huyo aliichukua barua hiyo ya Czar na alikwenda Habeshi na akatoa habari zote za ukatili na mauaji wa Zu-Nuwas aliyowafanyia Wakristo wa Najran.

Najjashi alikubali kuishambulia Yemen na kuikomboa kutoka kwa Zu-Nuwas. Zu-Nuwas naye pia alijitayarisha na kujitolea kukabiliana na Najjashi. Hatimaye kulizuka vita vikali mno baina yao ambamo Najjashi alipata ushindi na Zu-Nuwas aliuawa katika vita hivyo. Najjashi aliiunganisha Najran pamoja na ufalme wake na kuirudisha dini ya Kikristo huko ambayo ndiyo ikawa dini ya Watawala.

Habari zaidi ya hayo Vile vile kuna habari ifuatayo nimeipata katika utafiti mwingine

Kulikuwapo na mwanamke mmoja muumini pamoja na mtoto wake aliyekuwa mchanga mikononi mwake. Nao pia walikuwa watupwe ndani mwa mahandaki yenye moto mkali na pale alipoukaribia moto huo, mapenzi ya mtoto wake aliye mchanga, yalimfanya arudi nyuma.

Mtoto huyo aliyekuwa bado yu mchanga, kwa amri za Allah (s.w.t) akamwambia mamake kwa sauti kubwa:

“Ewe Mama yangu ! Ruka ndani mwa mahandaki yawakayo moto mkali pamoja nami kwani moto huu ni mdogo kabisa katika mtihani wa Allah (s.w.t) .”

Kwa hayo mwanamke huyo alijitupa motoni humo pamoja na mtoto wake huyo. Lakini kwa amri za Allah (s.w.t), Mtume, waumini wote, mwanamke huyo pamoja na mtoto wake walikuwa salama u salimini katika mahandaki hayo bila ya kudhurika hata kidogo.

Kwa kusoma kisa hicho kutoka Qur’an tukufu, kwa hakika nyoyo zetu zimejawa na majonzi na masikitiko kwa kuona udhalimu ulivyokuwa katika zama za ujahiliyya. Lakini hata katika zama hizi tunazoziita sisi za maendeleo, bado udhalimu huu unaendelea humu duniani kidhahiri na batini kwa kupitia njama tofauti tofauti. Mfano mmoja wa hivi karibuni ni wa Raisi Saddam wa Iraq, alivyowaua Mashia ambao ndio raia wake.

Kila mtu mwenye akili na busara atakubaliana kuwa ni dhuluma tupu kuwatesa na kuwaua na kuwateketeza watu ambao wamekuwa wakifuata madhehebu kwa mappenzi ya Ahlul-Bait ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) Someni vitabu vya historia na mtaona kuwa Mashia wameuawa kwa mamilioni wakiwemo wanaume, wanawake na hata watoto walio wachanga ati kwa sababu ni Ma-Shia wa Imam ‘Ali (a.s)

Katika Qur’an tukufu kuna mahala pengi panapoelezewa habari za waumini kuhukumiwa adhabu za kuuawa na kuchomwa moto. Wadhalimu watendaji hao wanapofanya hayo hushuhudiwa na watazamaji huku wakiona furaha. Kwa hakika Qur’an kwa uwazi kabisa unawalaani si wadhalimu tu bali hata wale wanaokaa kuyatazama dhuluma wafanyiwao waumini na wale ambao wanaangalia tu bila ya kujitahidi kufanya lolote ili waweze kuzuia hayo yasitokee. Ujumbe huu ni kwa watu wa Makkah ambao walikuwa wakiwahukumu kwa kuwaonea wale wote waliokuwa wameukubali Uislamu, na vivyo hivyo inatumika kwa ajili ya mateso na mauaji ya kikatili dhidi ya waumini ambao wanawafuata kikamilifu Ahlul-Bait (a.s)

Na kwa sababu hii ndiyo maana imesemwa katika Ziyarat:

“La’anallahu Ummatan Zahamatka wa La’anallahu Ummatan Sami’at bidhalika wa radhiat bihi.”

Yaani

“Laana ya Allah (s.w.t) iwe juu ya wale wote wasiotenda uadilifu kwako na walaaniwe wale wote waliosikia haya na wakayaridhia.”

MASIMULIZI (HADITHI) KATIKA QUR’ANI

MTUNZI: AMIRALY M. DATO0

WATU WA RAS

Allah (s.w.t) anatuambia katika Qur’an Tukufu Sura al-Qaaf, 50, Ayah: 12 - 14

Walikadhibisha kabla yao watu wa Nuhu na wakazi wa Rass na Thamudi.

Na Adi na Fir’auni na watu wa Mtume Luti.

Na wakazi wa kichakani, ( watu wa Nabii Shuaibu ) na watu wa Tubba ( Yemen ).Wote walikadhibisha Mitume; kwa hivyo onyo langu likathubutika ( juu yao ).

Watu wa Ras walikuwa ni wale watu ambao walikuwa wakiishi ukingoni mwa mto uliokuwa ukiitwa Ras. Wao waliishi katika zama baada ya Mtume Suleyman (a.s) mwana wa Mtume Da’ud (a.s)

Mto Ras ulikuwa ni mto mkubwa na watu waliitumia ardhi iliyoizunguka katika kilimo. Wao walikuwa wakiishi maisha ya raha na mustarehe na walitosheka na mahitajio ya maisha, vyakula kwa wingi, maji matamu kwa ajili ya kunywa, miti ilijaa kwa matunda, hali ya hewa ilikuwa nzuri, ardhi nzuri na yenye mandhari nzuri ya kuvutia.

Ukingoni mwa mto huo kulikuwa na mti mmoja mkubwa na mrefu kabisa kiasi kwamba unaweza kudhani kuwa ulikuwa ukigusa mawingu, uliota kwa sababu ya hali nzuri ya hewa, ukiitwa msonobari.

Hatimaye Shaytani alifanikiwa kuwapotosha watu hao kuuabudu mti huo kwani ulikuwa wa aina yake pekee wakati huo. Masikini watu waliingia katika mtego huo wa Shaytani na wakaanza kuuabudu mti huo kama ndio mungu wao. Watu walianza kuchukua matawi yake na kwenda kupanda sehemu zao kila mahala na kuanza kuabudu baada ya kukua katika miti kamili. Imani za watu ziliendelea kuwa madhubuti katika mti huu kiasi kwamba ukafika wakati ambapo hawakuwa na imani hata kidogo juu ya Allah (s.w.t) Wao walikuwa wakiusujudia mti huo na walikuwa wakitoa dhabihu hapo.

Ujahili na upagani wao huo kiasi kwamba wakafika wakati ambapo wao walijifanyia maji ya mto huo kuwa haramu kwa ajili yao na wengine wote na badala yake wakawa wanatumia maji kutokea sehemu zinginezo kama mito na chemichemi. Wao walikuwa wakidhani kuwa maisha ya mungu wao huyo, yalikuwa yameunganika na mto Ras na hivyo hakuna mtu yeyote aruhusiwaye kuyatumia maji hayo. Na kama ilitokea kuwa kuna mtu au mnyama yeyote aliyekunywa maji ya mto huo, basi wao walimwua kwa kitali kabisa.

Watu hawa walikuwa wakisherehekea siku moja katika mwaka kama ndiyo siku yao tukufu. Wao walikuwa wakikusanyika karibu na chini ya mti huo huku wakitoa sadaqa zao za wanyama na baadaye kuichoma moto nyama yao. Wakati moshi ulipokuwa ukipaa juu hadi kufikia mawinguni, wao walikuwa wakijiangusha chini kusujudu hapo mtini na walikuwa wakisoma ibada zao kwa sauti. Kwa kuyaona hayo, Shaytani alifurahishwa mno kwani alishuhudia ufanisi wake katika kuwapotosha hawa majaheli kwa kuwazuzua kuuabudu msonobari. Yeye alikuwa daima akiwazuzua kwa kila njia ili mradi watu hao wasirejee katika kumwabudu Allah (s.w.t)

Ikapita miaka huku watu wa Ras wakiendelea na kuuabudu msonobari huo. Hatimaye Allah (s.w.t) alimtuma Mtume wake kuja kuwaongoza katika njia ya Allah (s.w.t) na hivyo kuwaokoa. Mtume huyu alitokana na kizazi cha Mtume Ya’qub (a.s) na kama Mitume (a.s) yote iliyokuwa imetumwa sehemu zote, naye pia alianza kazi zake za tabligh na kuwaita watu katika njia ya Allah (s.w.t). Ili wafanye ‘ibada ya Allah (s.w.t) tu na wala si mwingine (hata si mti huo wa msonobari). Lakini watu hao walitupilia mbali maneno ya Mtume huyo na waliendelea kuuabudu msonobari huo. Ikatokea kuwa siku yao ya maadhimisho ikawadia na Mtume huyo akashuhudia vile watu wao walivyokuwa wamejiandaa kwa matayarisho kamambe kwa ajili ya sikukuu yao hiyo ambayo ilisherehekewa na watu wote.

Wakati Mtume huyo alipoyaona mambo hayo ya ujahili, alimwomba Allah (s.w.t) aukaushe kamili mti huo ili watu hao waweze kuzinduka kutoka ndoto yao hiyo kuwa mti huo haukustahili kuabudiwa.

Kwa hakika dua ya Mtume huyo ikakubaliwa na msonobari huo ukakauka kabisa kwa ghafla, na majani yake yote yakanyauka na kuanza kudondoka ardhini. Lakini watu badala ya kujipatia funzo kutokana na tukio hilo, wao waliukaribia zaidi mti huo na kudhani kuwa Mtume huyo kwa uchawi wake ameudhuru mti wao. Wengi wao walisema kuwa Mtume huyo alikuwa ameudharau na kuukashifu mti huo hivyo kuingiwa na hasira, mti huo umebadilisha hali yake. Hivyo Mtume huyo lazima auawe kikatili kabisa ili mti huo ukifurahi uweze kurudia hali yake ya kawaida. Na hivyo mungu wao huyo (msonobari) utawawia radhi tena.

Kulibuniwa njama za kutaka kumwua Mtume huyo. Wao walichimba shimo kubwa mno na kumtupa Mtume huyo humo huku wakiufunika mdomo wa shimo hilo kwa jiwe kubwa. Kwa muda fulani kulikuwa kukisikika sauti za mlio wa Mtume huyo kutokea shimoni, na hatimaye sauti hiyo haikusika kamwe kwani Mtume huyo alikuwa amejitolea mhanga kwa ajili ya kutaka kuwanusuru watu wasipotee na wala wasiangamie katika adhabu za Allah (s.w.t). Kwa matokeo ni kwamba Allah (s.w.t) alikasirishwa mno na kulianza kutokezea dalili za adhabu za Allah (s.w.t). Kulitokea kimbunga chekundu cha upepo ambacho kiliwateketeza watu wote. Kulitokezea na wingu jeusi kabisa ambalo lilifunika eneo zima kuwa kiza tupu. Hivyo watu wa Ras wamekuwa ni funzo la kujifunza kwa vizazi vilivyofuatia.

WATU WA SABT (SABBATH)

Qurani Tukufu inatuambia: Sura Al-Aaraf, 7, Ayah ya 163 & 164.

Na waulizeni habari za mji ambao ulikuwa kando ya bahari, (watu wa mji huo) walipokuuwa wakivunja (sheria ya) Jumamosi (ambayo waliambiwa wasifanye kazi katika sikuu hiyo, wafanye ibada tu. Na kazi yao ilikuwa uvuvi). Samaki wao walipowajia juu juu siku za Jumamosi zao; na siku isiyokuwa Jumamosi hawakuwa wakiwajia (hivyo). Basi namna hivyo tuliwatia mtihani kwa sababu ya kuasi kwao.

Na (wakumbushe wakati) baadhi ya watu katika wao waliposema (kuwaonya waliovunja hishima ya Jumamosi kwa kuvua, na hali yakuwa wamekatazwa; waliposema): ‘Pana faida gani kuwaonya watu ambao Allah (s.w.t) atawaua au atawaadhibu kwa adhabu kali

( papa hapa)?”

Wakasema:“Tupate kuwa na udhuru mbele ya Allah (s.w.t) wenu (kuwa tumewaonya lakini hatukusikilizwa) na huenda wakaogopa.’

Mtume Musa (a.s) mwana wa Imran aliwahubiri wana wa Isra’il kuwa wawe na siku moja maalum katika juma kwa ajili ya kumwabudu Allah (s.w.t) ili wao wasijishughulishe na kazi zinginezo mbali na ibada ikiwemo kuuza na kununua bidhaa za aina zote.

Siku hiyo ilikuwa makhsusi ya Ijumaa lakini wana wa Isra’il waliiomba siku ya Jumamosi kama ndiyo siku maalumu ya kufanya ibada ya Allah (s.w.t) na hivyo siku ya Jumamosi ikawa ndiyo siku Kuu ambamo biashara za aina zote zilikatazwa. Hivyo kila Jumamosi Mtume Musa (a.s) alikuwa akiwahutubia mkusanyiko maalum wa wana wa Isra’il. Ilipita miaka na watu waliichukulia Jumamosi kama siku njema na maalum kwa ajili ya ibada za Allah (s.w.t)

Baada ya kuaga dunia kwa Mtume Musa (a.s) kulianza kutokea mabadiliko mengi katika jamii ya wana wa Isra’il, hata hivyo wao waliendelea kuiheshimu siku ya Jumamosi kama ndiyo siku maalum kwa ajili ya ibada za Allah (s.w.t). Lakini ulipofika zama za Mtume Daud (a.s), kikundi kimoja cha wana wa Isra’il waliokuwa wakiishi ukingoni mwa bahari, mji wa Ela, walipuuza utukufu wa siku hiyo ya Jumamosi na hivyo wakajishughulisha kuvua samaki.

Habari kamili ya matukio hayo ni kama ifuatavyo

Wakati uvuaji wa samaki ulipokuwa umepigiwa marufuku katika siku za Jumamosi, samaki walibuni njia yao, walikuwa wakijitokeza kwa wingi ufuoni mwa bahari katika siku hizo na kwa siku zilizobakia walikuwa wakiondoka kwenda mbali kabisa katika maji mengi ili wasiweze kuvuliwa na wavuvi. Watu wa Bani Isra’il ambao walikuwa wakitilia maanani maslahi yao ya kidunia, walikusanyika na kulizungumzia swala hili na kutoa kauli yao:

“Sisi hatuna budi kubuni mikakati ya kuweza kudhibiti swala hili la uvuaji wa samaki. Katika siku za Jumamosi, samaki wengi mno huonekana ufuoni kuliko siku zinginezo. Hivyo itatuwia rahisi mno kuvua samaki siku hiyo kwani siku zingine tunambulia kapa kwani wao wanakwenda katika maji yenye kina kikubwa mno hivyo kutuwia vigumu uvuvi.”

Katika kikao hicho kuliafikiwa kuwa wabuni taratibu za kuvulia samaki. Hivyo wakaafikiana kuchimba mito na mifereji midogo midogo ili samaki wanapokuja ufuoni katika siku za Jumamosi waweze kupitiliza katika mifereji hiyo, hivyo kuwawia rahisi katika kuwanasa.

Hivyo wao walitekeleza mpango wao huo na wakachimba mito kutokea baharini. Katika siku za Jumamosi samaki wengi mno walikuwa wakiogelea kwa furaha hadi ukingoni mwa bahari na kupenya katika mito hiyo. Katika nyakati za usiku wakati samaki hao walipokuwa wakitaka kurudi baharini, hao walikuwa wakiziba midomo ya mito hiyo ili samaki hao wasiweze kurudi baharini na badala yake wabakie katika mito hiyo. Siku iliyofuatia wao walikuwa wakiwanasa samaki wote waliokuwa katika mito hiyo.

Hata hivyo watu wenye busara na fahamu waliwakanya watu hao wasijifanye wajanja mbele ya amri za Allah (s.w.t) Wao waliwaonya na kuwabashiria adhabu na maangamizo makubwa yaliyokuwa yakija kwao, lakini haya pia hayakufua dafu.

Hata hivyo watu hao wema waliendelea na juhudi zao za kuwakanya kwa njia mbalimbali kuhusu adhabu na maangamizo ya Allah (s.w.t), lakini walafi hao hawakuwasikiliza na badala yake waliwapuuza na kuwadharau. Hao waovu waliwaondoa wale wenye hekima na busara na badala yake wakaanza kuwafuata wale waliokuwa wakisema:

“Jee kwa nini nyinyi mnawahubiri watu ambao watateremshiwa adhabu kali kabisa za Allah (s.w.t) na hatimaye watateketezwa kabisa ? Hivyo muwaache katika hali yao walivyo.”

Kikundi cha waja wema wakawaambia hao kuwa:

“Sisi tunawahubiria ubashiri mwema hawa watu ambao hawapo katika fahamu zao kamili ili kwamba na Allah (s.w.t) aone kuwa kwa kweli hawa watu ni masikini mbele ya macho ya Allah (s.w.t) .”

Hao wapotofu walikuwa wameshughulika mno na unasaji wa samaki kwa wingi mno bila kujali nasiha za kundi la kwanza la watu wema katika Bani Isra’il na walikuwa wakijionea ufakhari na majivuno juu ya ufanisi wao katika mipango yao hiyo.

Baada ya maonyo ya siku chache, hao wapotofu walipokithiri katika kutotii amri ya Allah (s.w.t) , waliteremshiwa adhabu kutoka kwa Allah (s.w.t) kwamba nyuso zao ziligeuka kuwa za wanyama na baada ya kupita siku tatu, Allah (s.w.t) aliwateremshia adhabuu kali kiasi kwamba wote kwa pamoja wakateketea.