USUULID DIIN
UIMAMU
UTANGULIZI
Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu.
Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote, na rehma na amani ziwe juu ya Bwana wetu Muhammad na Kizazi chake Kitukufu.
"Uimamu" kwa waislamu ni miongoni mwa maudhui ambayo yamezungumzwa sana na kufanyiwa utafiti sana, hadi vitabu vilivyo tungwa kuhusu maudhui haya kufikia maelfu kwa maelfu.
Kisha yakaendelea mazungumzo kuyahusu maudhui hayo, na watafiti kugundua wingi wa kuchipuka kwa matawi yake na upana wa maudhui haya katika utungaji wa vitabu, na kwa hivyo kila kundi kati ya watunzi hao likachukuwa tawi moja wapo kati ya matawi yale au upande mmoja wapo wa maudhui hayo, na matokeo ya kufanya hivyo ukatokea upande ufanyao utafiti na kujihusisha na suala la uimamu ndani ya Qur'ani.
Na upande mwengine ukajihusisha na suala hilo kwa upande wa hadithi za Mtume, na kuna upande uliojihusisha na uimamu kwa mtizamo wa elimu ya akida, au kwa upande wa historia, au kuuangalia uimamu kwa kuzingatia mipaka ya yale yaliyo tokea kwenye Saqifa bani Saida pindi alipo fariki Mtume(s.a.w.w)
, kisha yaliyo husiana na maisha ya Maimamu na historia zao, na kue-ndelea.
Pamoja na vitabu vilivyo tungwa kuwa vingi na idadi kuwa kubwa, hakika vitabu vingi kati ya hivyo, havikuandikwa kwa roho ya kuyatazama maudhui yenyewe tu yakiwa yameepukana na matamanio na ghera (taasubi) juu ya madhehebu fulani, matokeo yake ni kudhihiri utafiti na vitabu vilivyo jawa na taasubi (ghera) iliyo kemewa, na hisia zikaenda kinyume cha ukweli, na kutolewa hukumu zenye kufuata matakwa na mata-manio, na kubeba mambo ambayo akili na mantiki haiyakubali wala kuyaridhia.
Na hapa ikaonekana kuwa maudhui ya uimamu yamezungu-kwa na sura tofauti za kiakili ambazo hazilisogezi karibu lililo mbali na wala haziondoi tofauti iliyopo na hazisaidii kuleta uelewano wala muungano.
Na sura hizi zilizoko akilini hazikuwa na chimbuko lingine tofauti na vitabu hivyo vilivyo tungwa na vilivyo toka kwenye maadili ya utunzi wa vitabu na uandishi wa kimaudhui, na wala si chimbukizi tofauti na picha mbaya iliyotolewa yenye kuchukiza ya mwendo (historia) wa kiislamu kwa karne zote hizo.
Na kwa uwazi kabisa:
Tunapo taka kufanya utafiti wa maudhui ya uimamu hivi leo na baada ya kupita karne kumi na nne tangu lifanyike tukio la "Saqifa" na matukio yake mengine, kwa nini tujaalie kuwa tutatofautiana. Na ikiwa tutatofautiana (na kwa wafanyao utafiti suala la kutofautiana ni la kawaida kwao) kwa nini tunapatwa na ghera (asabiya) ya kupenda kutetea kitu hata kama si cha sawa na kuwa wakali na wenye ghadhabu, wakati ambapo kutofautiana kwa rai hakuharibu mapenzi ya kitu?.
Na je katika utafiti huu kuna jambo limletealo mwanadamu wa leo faida ya mali au kumfikisha kwenye msimamo fulani ambao anaweza kuutumia kwa maslahi yake? Au je kwenye utafiti huu kuna kitu kitakachomtia mtu wa zama hizi gharama au kuleta maudhi yawezayo kumpata huyu au yule katika wana-damu?
Hakika waislamu wa leo, wote kwa ujumla wanakubaliana kutokuwepo kwake kunaweza kupelekea watu kutofautiana katika kumpa baia (kiapo cha utiifu) au kutompa baia, kwa hivyo basi hakuna ugomvi uogopewao au mapigano yenye kuogopewa lau kama mtu fulani atasema maneno yake katika maudhui haya.
Na huenda muulizaji akauliza:
"Ikiwa hali ni hivyo, kwanini -basi- kufanyike utafiti kama huu na juhudi kama hizi"?
Jawabu:
Hakika sisi tunataka kufanya utafiti wa mas'ala haya ili kutoa msimamo wa uislamu (kwa kuzingatia kuwa uislamu ni dini na sheria na ni nidham ya maisha) kwenye maudhui haya hatari, na tunataka kutoa majibu yenye maswali yatatanishayo yenye kiu cha kupata majibu sahihi:
Nini maana ya "Uimamu" katika uislamu?Je "Uimamu" ni lazima kuwepo? Na vipi? Je Uislamu ulifaradhisha kuwepo uimamu, na je ulimteua Imamu au mtu anae faa kuwa Imamu kwa dalili au liliachwa suala hilo kwa ajili ya kufanywa uchaguzi?
Je uimamu kwa kuteuliwa ni fikra ya "kitheokrafia" (theocracy- utawala wa dini) au ya kidikteta au fikra ya kidemo-krasia?
Na pande zingine ambazo ni lazima kuzifanyia utafiti kwa undani na kwa uhuru, huenda kufanya hivyo kukawa na faida au kutuletea ukweli na kutupa msingi na msimamo wa kiislamu kuhusu mas'ala haya yenye msisimko mkubwa.
Na mfumo wa kitabu hiki utawatolea wasomaji natija iliyo salama na utakuwa na muelekeo usio gusa au kuyapa umashuhuri madhehebu haya au yale kati ya fikra na mielekeo ya vikundi mbalimbali vya kiislamu au fikra ya mtu huyu au yule kati ya wanazuwoni wa kiislamu, na nimeuepusha na kuto zungumzia au kutoifanyia utafiti historia ya mambo yaliyo tokea siku aliyo fariki Mtume(s.a.w.w)
kutokana na mgawanyiko na tofauti zilio tokea, ili kuepukana na mambo kadhaa ambayo yaweza yakasa-babishwa na bahthi hiyo, kama vile kuziamsha hisia na mapenzi au kulitonesha jeraha wakati ambapo tunataraji kwa nia safi jambo hili (jeraha hili) litulie na lipone kutokana na usaha wake wenye kuumiza na kusikitisha.
Na matarajio yangu yote ni kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, anisaidie katika njia yangu hii na anisaidie kupita kwenye njia na mipaka niliyo jiwekea na kujifunga nayo na kujilazimisha kuifuata kwenye utafiti nilio tangulia kuufanya, na aiepushe kalamu yangu kutokana na usahaulivu na ukosevu, na auelekeze mkono wangu kwenye kauli aziridhiazo na kwenye matendo ayaridhiayo, hakika yeye ni msaidizi bora na muwafikishaji.
Na maombi ya mwisho, tunasema sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote.
Kaadhimiyya - Iraq
MUHAMMAD HASSAN AALI YAASIN
UIMAMU KWA MAANA YAKE YA UJUMLA
Imam (kama lugha ya kiarabu ilivyo muarifisha), ni mtu mwenye kuwatangulia kaumu yake au watu wake, pia mwenye kufuatwa na mwenye kufanywa kuwa kiongozi na msimamizi wa mambo.
Na uimamu (kwa maana hii) unakuwa na maana ya uongozi na uraisi na kufuatwa na kuwatangulia watu, na kwa hivyo mtu mwenye kuwatangulia watu kwa ajili ya sala atastahiki kuitwa "Imamu" kwa sababu anawatangulia na kuwaongoza wote kwa pamoja.
Na kwa maana hii ya kilugha Qur'ani imekuwa ikilitumia neno "Imam" kama alivyo litumia kwenye kauli yake tukufu:
"Hakika mimi nimekufanya wewe uwe imamu (kiongozi) kwa watu.
"Na kabla yake kulikuwa na kitabu cha Mussa, imamu (kiongozi) na rehma".
"Na utufanye tuwe maimamu )viongozi( wa wachamungu".
"Siku ambayo tutawaita watu wote na imamu wao (kiongozi wao).
Na aya zingine zilizo kuja kwenye Qur'ani tukufu katika matumizi ya neno "Imamu".
Na neno Khalifa (kama ambavyo lugha ilivyo liarifisha vilevile), ni kiongozi na mtawala mkubwa na mwenye kuchukua nafasi ya mtu aliekuwa kabla yake au alie mtangulia.
"Ewe Daudi hakika sisi tumeku-fanya uwe khalifa (mtawala) katika ardhi".
"Yeye ndie aliekufanyeni kuwa watawala kwenye ardhi".
"Na kumbukeni pale alipo kufanyeni kuwa makhalifa (watawala) baada ya watu wa Nuhu"
Na aya zinginezo ambazo ziliyatumia maneno hayo.
Na ikiwa wanazuwoni wa lugha wamekubaliana katika maana hii ambayo ina ashiriwa na neno "imamu" na "khalifa" na wafuasi wao wametofautiana kuhusu maneno hayo mawili ya kwamba je! Yana maana moja au maana mbili tofauti?. Kwa mfano Al-mawridy anatoa taarifa ya uimamu kuwa ni "Umewekwa kwa maana ya khilafa ya kushika nafasi ya mtume (kuchukuwa nafasi baada ya mtume) katika kuilinda dini na kuingoza dunia".
Na Ibnu Khaldun anatoa taarifa ya neno khilafah kuwa "ni kuwaongoza (kuwaelekeza) watu wote kufatana na mtazamo wa kisheria kwenye maslahi yao ya kiakhera na kidunia maslahi ambayo hurejea kwa utawala huo".
Na anatilia mkazo na kusema "Hakika mikakati ya kidini na kisheria huingia chini ya uimamu mkuu ambao ndio ukhalifa.
Na mtu wa tatu kaunganisha "kati ya ukhalifa kwa kuuzinga-tia kuwa ndio uimamu (uongozi) mkuu na swala kwa kuuzingatia kuwa ni uimamu (uongozi) mdogo.
Na maana ya yote hayo ni kuwa maneno haya mawili yanamuelekeo mmoja au makusudio mamoja.
Na huenda "uraisi" au "uongozi" ndio maana zenye kuku-sanya na kutosheleza ambazo zinawezekana kutumiwa kuyatafsiri maneno mawili hayo na kukubaliana juu ya maana hiyo.
Lakini tunapo fuatilia nyanja ambazo uongozi huu au uraisi huu huingia hasa kwenye viwanja vya kazi au sehemu za kazi hakika tunahisi kuwepo tofauti inayo tenganisha kati ya maneno mawili haya au itenganishayo kati ya neno moja na lingine na kuyapambanua kati yake na kuonyesha kutofautiana, tofauti ambayo hulipa kila tamko kati ya matamko mawili hayo ukubwa wake na upana wake.
Basi uimamu (kama ambavyo dalili za dini zinavyo tuonyesha) ni uongozi wa juu wa kidini. Na Khilafa (kama zijulishavyo dalili vilevile) ina maana kuwa ni uongozi wa juu wa dola.
Na,"Imamu kwa wanafikra wa kiislamu, wawe masuni au mashia, amekuwa na maana ya kuwa ni mwenye haki ya kisheria, wakati ambapo tamko khalifa linamuashiria mwenye utawala au nguvu za kiutawala kwa wakati ule"
, na kutokana na haya "Ukhalifa wa Abubakar baada ya Mtume, katika serikali yake au utawala wake ulikuwa ni utawala wa zama hizo na si utawala wa kidini".
Na kwa kuyazingatia hayo kila tamko linakuwa na sehemu zake na nyanja zake maalum na mipaka yake maalum ambapo hufanya kazi ndani ya mipaka hiyo. Na pamoja na tofauti hii iliyopo kwenye nyanja za utekelezaji wa maneno hayo nje, hakika sisi tunaamini (kwa kuzirejelea dalili za kidini) kuwa anwani hizi mbili ni lazima ziungane na zikusanyike kwa mtu mmoja, kwa sababu hatukubali, katika uislamu fikra ya kutenganishwa dini na serikali au dola.
Na ikiwa jamii ya watu wa ulaya ambayo ndio iliyotuletea fikra hii ya kutenganisha dini na serikali wananyudhuru na sababu za kujenga fikra hiyo na waliyoyafanya katika kufanya mapinduzi dhidi ya utawala wa kanisa na kuingilia kwake mambo yote, kwa kuzingatia kuwa ukristo haukuwa na nidhamu ya dola au utawala na mifumo ya kutawala, basi sisi waislamu hatuna udhuru wowote au sababu yoyote iwezayo kutufanya kubeba wito huo au fikra hiyo, maadamu dini yetu kiukweli na uhakika wake ni ujumbe wa dini na ni nidhamu ya dola na utawala.
Kwa hivyo basi, ni lazima kukusanyika uongozi wa dini na wa dola kwa mtu mmoja ili tusije kutumbukia kwenye fikra ya "uwili" ambao athari yake ya mwanzo huwa ni ugonjwa wa kutokuwa na msimamo wa rai moja katika nafsi ya muislamu.
Na ikiwa kati ya wislamu kuna watu wasemao kuwa uimamu ni kitu na ukhalifa ni kitu kingine, hakika waliyapata haya kutokana na historia ya waislamu na matukio yaliyo tokea, wakati ambapo ulitengana ukhalifa na uimamu, na kiongozi wa dini akawa sie raisi wa serikali au dola, na lilikuwa si jambo lenye kuingia akilini, khalifa kama Yazidi bin Muawiya kwa mfano awe ni "Imamu" wa waislamu wakimtegemea na kumkimbilia katika utatuzi wa mas'ala ya dini na mambo ya itikadi.
Hakika Uimamu, kama Shia Imamiyah walivyo ufahamu, ni sehemu ikamilishayo ujumbe wa Mtume na iufanyayo ujumbe huo uendelee kuwepo. Na akili inahukumu ulazima wa kuwepo kwake kwa sababu Uimamu ni huruma ya Mwenyezi Mungu na kila huruma (Lutfu) ni wajibu kwa Mwenyezi Mungu kufatana na hukumu ya akili yenye misingi ya mfumo wa akili katika elimu ya akida.
Ama uimamu kuwa ni Lutfu (Upole au huruma ya Mwenyezi Mungu), ni kwa sababu huruma au lutfu ni kitu kimkaribishacho mja kwenye utiifu wa Mwenyezi Mungu na kumweka mbali na maasi na kumpeleka na kumpitisha kwenye njia ya haki na maana hii huthibitishwa na uimamu kwa uwazi kabisa.
Na kila mmoja anafahamu kuwa kuwepo kiongozi mwenye kusikilizwa na mwenye utawala wenye nguvu, huzuwia dhuluma, na kumpa kila mwenye kudhulumiwa haki yake, na mambo yote ya watu huyawekea nidhamu kwa moyo safi na imani na kuepu-kana na matamanio na ubinafsi na kupenda kujitolea, mambo ambayo humkaribisha mwanadamu kwenye utiifu na kumtenga na maovu na humtia hamasa ya kufuata mfumo ambao Mwenyezi Mungu Ameuchagua.
Na hii ndio maana ya "Lutfu" (upole au huruma ya Mwenyezi Mungu) tuukusudiao kwenye sehemu kama hii.
Na jambo ambalo halihitaji maneno mengi ni kuwa hakika kila jamii ya watu, iwe ya zamani au ya hivi sasa, ni lazima iwe na raisi (kiongozi) mwenye kuyapangilia mambo yake, na nilazima kuwe na katiba na kanuni yenye kuweka nidhamu katika mambo ya jamii hiiyo. Na ikiwa jamii ya leo hii ina hisi kuwepo haja kubwa na umuhimu wa kuwepo raisi na serikali, yaani kuwepo utawala unao simamia mambo ya maisha kwa ajili ya jamii ile kama vile mambo ya kisiasa, ya kijeshi, kiuchumi, ya mahkama na ya malezi na vinginevyo, basi uislamu unamuangalio raisi wa dola kwa mtizamo mpana zaidi na wenye kukusanya vitu vyote, kwa kuwa yeye ni mwenye majukumu na ni mtekelezaji wa mambo yote ya dini na dunia, mambo yale ambayo yamebebwa na sheria au yamo ndani ya sheria kama mifumo ya tabia na mwendo wa mwananchi muislamu, sawa uwe ni mwenendo wa kumuelekea mola wake na mtu yeyote kati ya wanadamu.
Na kwa kuzingatia kuwa katiba nyingi na kanuni nyingi zitumikazo katika jamii za watu zimetungwa na kuwekwa na wanaadamu na zenye uwezekano wa kubadilika na kugeuka kufatana na mahitaji ya wakati na sehemu, na uislamu ukiwa umetoka na uko nje ya kanuni hizo na katiba hizo kwa kuzingatia kuwa ni sheria ya mbinguni ambayo haifai kuguswa au kufanyiwa mabadiliko yoyote, lakini uislamu huo pamoja na kukamilika kwake na kutimia kwake na kuto juzu kuchezewa bado umefungi-ka katika baadhi ya dalili zake na ina kanuni za ujumla na nguzo za msingi katika dalili zake zingine. Na ilikuwa ni lazima, ulazima ambao hauna shaka yoyote, kusema kuwa ni lazima awepo mwenye kutekeleza hukumu na kufafanua na kubainisha na kutoa ufumbuzi na kuelekeza sehemu ya utekelezaji wa kila hukumu. Na hivyo hivyo kila dalili ijulishayo ulazima wa kuwepo utume na wajibu wake itakuwa inafaa kuitumia kama dalili vilevile juu ya ulazima na uwajibu wa kuwepo uimamu, kwa sababu kuwepo utume bila ya uimamu ni sawa na kukatika na kutoendelea kuwepo jambo hilo, na jambo hilo linapingana na uislamu ulio simama kwenye msingi wa kuendelea kuwepo kwa ujumbe wake hadi siku ya kiama.
Kwa hivyo basi utume ni mwanzo wa maisha na uimamu ni kundelea kwa maisha hayo. Na lau kama ingefaa kwetu kukubali utume bila uimamu, ingefaa pia kusema kuwa ujumbe wa Mtume unamtizamo finyu na wenye mipaka maalumu ambao haukuweza kujikadiria umri mrefu hata baada ya kumalizika maisha ya Mtume wake, na haukuweza kuyawekea malengo yake mrithi (au muusiwa) atakae endeleza na kuendelea na kazi yake.
Na kutokana na kuwa uislamu unalenga kwenye dola kubwa ambalo litawajumuisha watu wote pamoja na kuwa wako kwenye nchi tofauti na wenye rangi tofauti, hakuna budi uislamu kuya-andalia malengo hayo uongozi wa kuyatekeleza na kuyafanya hayo, uongozi huo ukionekana wazi kwa mtume katika maisha yake na kwa khalifa wake ambae atakae shika nafasi yake baada ya kufariki kwake.
Na muhtasari wa hayo tuliyoyasema ni kuwa Uimamu kwa hakika ni ukamilisho wa maana ya utume, na kuwepo kwa Mtume na ufanyakazi wake hautasimama madhubuti bila kuwepo Imamu. Na kwa sababu hii Shia Imamiya wanaamini kuwa Uimamu ni wajibu kuwepo au ni lazima kuwepo kama ambavyo ni lazima kuwepo kwa utume, na dharura ya kuwepo uimamu ni sawa na dharura ya kuwepo utume au Mtume. Na haya yana dalili bora ambayo ni hadithi ya mtume iliyo mashuhuri:
"Mwenye kufa hali ya kuwa hamjui Imamu wa zama zake (basi) amekufa kifo cha kijahili". Na ikiwa uimamu ni jambo la lazima ambalo ni lazima kuwepo kwake, kama tulivyo eleza hivi punde, je uislamu uliwaachia watu jukumu la kumchagua Imamu ambae atasimamia kazi za cheo hiki muhimu na cha hatari au suala la Imamu linahusika na dalili (kauli) za Mwenyezi Mungu na Mtume katika kumteuwa na kumthibitisha?.
Shia na Muutazila walio wengi wao wamesema kuwa Imamu ni lazima awe ameelezwa (ametajwa) kwa dalili kutoka kwa mtume na awe amemuainisha yeye mwenyewe.Wamesema haya wakijitegemeza kwenye dalili kuwa, kwa kuzingatia kuwa uima-mu ni kuendelea kwa cheo cha utume, ni lazima kwenye uimamu huo kama ulivyo utume, kuwe na uteuzi na uainishaji maalumu uonyeshao uteuzi wa Mwenyezi Mungu kwa Imamu huyo na kumridhia kwake.
Kama ambavyo hakuna utume au mtume achaguliwae na kuteuliwa kwa kufanya mashauriano, hivyo hivyo, hakuna uima-mu au imamu ateuliwae kwa kufanya shura (kushauriana) na kwa uchaguzi. Na mfumo huu ndio mfumo thabiti ufuatwao na madhehebu hayo mawili katika mas'ala ya uimamu na imamu.
Ama makundi mengine ya kiislamu hayakuchagua mfumo maalum wa utawala katika uislam.
Bali walisema kuwa kila mwenye kushika utawala na kudai kuwa yeye ni imamu basi huyo ndie imamu. Sawa awe amefika kwenye utawala huo kwa njia ya uchaguzi kama ilivyo fanyika kwa Abubakar na Uthumani na Ali na Hassan, na haukufanyika kwa mwingine yeyote kwenye historia ya kiislamu, au amefika kwenye utawala kwa kuwekwa na yule alie mtangulia kama ilivyo tokea kwa Omar Binil-Khattab na makhalifa wengine wa bani umayya na bani Abbasi na Uthmaniyyah, au afike hapo kwa nguvu na kwa kutumia silaha kama ilivyo tokea kwa Muawia bin abi Sufiyani na Abul Abbas Assafah.
Na miongoni mwa dalili walizo zitolea ushahidi mashia juu ya ulazima wa kuwepo dalili inayo onyesha kuteuliwa kwa Imamu ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
"Na Mola wako Ana-umba Akitakacho na Anamchagua Amtakae , hawana hiyari katika hayo
".
Kwani aya hii imetujulisha kwa matamshi yake yaliyo wazi kuwa suala la kuwachagua mitume ambao ni waaminifu juu ya sheria na walinzi wa dini sio katika haki ambazo Mwenyezi Mungu aliwaachia watu wafanye watakavyo, bali suala la kuwachagua watu hao wa nafasi ya utume hufanyika kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na linahusika na Mola pekee.
Ama jibu la mwenye kupinga haya na kusema ya kuwa uteuzi huo unahusiana na suala la Utume tu na aya imeliangalia tu jambo hilo wala haikuligusia jambo lingine, ni maneno yasiyo kubalika, kwani mwanzoni mwa aya au mwishoni mwake hakuna kitu kitujulishacho -hata kama kwa njia ya siri- kuwa aya hii inahusika tu na mitume bali kutofungika kwake na jambo fulani (ujumla wake), na kutokana na uwazi wa matamshi yake, (ujumla huu) una kataa na haukubali kuyafunga maneno yake kwenye utume tu wala kuyafanyia taawili yoyote, na vipi yasikatae taawili wakati ambapo uimamu huzingatiwa kuwa ni kuendelea kwa cheo cha Utume, na kuutimiza ujumbe kunahitajia masharti hayo hayo yaliyo wekwa na kuzingatiwa kwa mtume katika upande huu.
Na ukweli kuwa, lau kama usia usingethibiti kutoka kwa mtume(s.a.w.w)
kwa njia ya riwaya na habari zilizo nukuliwa, hakika akili pekee ni yenye kuhukumu ulazima wa kuwepo usia na kuwa suala la usia lilifanyika. Na kwamba yeyote katika sisi haridhii katika nafsi yake kusafiri na kuziacha mali zake zenye kumalizika au zenye uwezekano wa kutoweka au utawala wake wenye kutoweka na kuviacha vitu vyake kama mali yake chache aliyo nayo bila kuiweka mali hiyo chini ya ulinzi wa mtu aliemuusia na alie muaminifu, atakae iangalia na kuilinda pia kuiangalia isiweze kupotea. Je, inafaa kwa Mtume wa Uislam kuuacha urithi wake ulio mkubwa na urithi huo ukiwa ni kwa ajili ya wanadamu kwa zama zake zote bila kumuacha mtu alie usiwa atakae uchunga urithi huo na kuulinda kama itakiwavyo?
Hakika mazingira na matukio yote yaliyo uzunguka Uislamu wakati wa kifo cha Mtune(s.a.w.w)
yanatufanya tuamini kuwa ni lazima atakuwa alitoa usia, na kwamba mmea wake wenye baraka hakuuacha jangwani hivihivi ukipigwa na upepo mkali au kwenye joto kali liumizalo au jambo lolote lingine liwezalo kujitokeza na kuufanya mmea huo utoweke na usiwepo tena.
Na hakika dini ambayo imefaradhisha kanuni na hukumu na sheria mbali mbali katika kila jambo kati ya mambo ya kidunia na kila upande kati ya pande za maisha na kila kitendo kati ya vitendo vya mwanadamu kama kuuza, kununua, kuhamishwa deni kutoka kwa mdaiwa na kuhamia kwa mdhamini (hawala), na kuchukua dhamana, kukodisha na kuweka wakala, kulima na kumwagilia, kukopa na kuweka rehani, kuoa na kutaliki, kuwi-nda na kuchinja, na kuhusu vyakula na vinywaji, hukumu na kulipa fidia. Hakika dini kama hii haiwezekani kwake kuliacha na kutolitilia umuhimu suala la uimamu, nalo kama lilivyo katika umuhimu wake na nafsi yake katika uwekaji wa sheria na kuongoza dola na majukumu yake ya kuwaelekeza watu kwenye mwendo wa kiislamu, kuelekea kwenye kukamilisha aliyo yaanzisha Mtume(s.a.w.w)
katika ujenzi wa jengo jipya.
Na kuwa uislamu ambao ulilenga katika sheria zake zote kuweka uadilifu na usawa na utulivu kwa ajili ya waislamu na kumpatia amani kutokana na mambo yake yenye kuogopesha, na kumlinda na maovu yote, chini ya itikadi tukufu yenye kumu-unganisha na Mwenyezi Mungu Mtukufu na viungo vyake kutawaliwa na tabia zilizomo ndani ya nafsi yake zimzuwiazo kufanya khiyana na uovu na uharibifu na kutenda mambo mabaya.
Hakika uislamu hauwezi kulithibitisha na kulifikia lengo hilo kubwa -kwa mtazamo wetu mdogo- bila kuwepo Imamu alie teuliwa kwa dalili, na Imamu huyo awe mbali na mambo wayafa-nyayo watu wengine kama kukosea au kutetereka na kuyafata matamanio na kufanya uharibifu, yaani mambo maovu au kusema kauli mbaya na kuathirika na matendo yasiyo ya uadilifu matendo ambayo humfanya hakimu kuwa muovu, na kwa kuhari-bika kwa hakimu na kuwa muovu hupelekea maisha ya watu kuharibika na pia dini yao na nidhamu yao kwa ujumla.
Ni lazima kwa ajili ya kuepukana na maovu yote hayo awepo Imamu alie chaguliwa na Mwenyezi Mungu alie kusanya sifa zote za ukamilifu, alietakasika na sifa yoyote ichukizayo, na kuepuka-na na aina zote za uovu katika matendo na kukosea kwenye makadirio na kwenda kinyume na mafundisho ya sheria na haya ndio tuyaitayo kwa jina la "Ismah". Ni jambo lililo wazi kuwa kumteua mtu aliekusanya sifa zote hizi ni jambo gumu kwa raia wenye kutawaliwa na wenye kuchagua. Kwa hivyo basi ni lazima kuwepo dalili ya Mtume na zikiainishi kuhusu suala hili na kitu cha kuuongoza umma na kuuelekeza katika suala hili.
Na Ismah (yaani kuhifadhika huku kutokana na kutotenda madhambi) kuliko ashiriwa si jambo la kushangaza au kustaaja-bisha kama ionekanavyo kwenye maneno ya baadhi ya watafiti kwenye madhehebu za kiislamu, na hasa kwa mustashrikina, bali si miongoni mwa vitu vya lazima kwa mtawala au hakimu ambae miongoni mwa majukumu yake ni kuitafsiri na kuifafanua Qur'ani tukufu na kutekeleza hukumu zake na kuyatolea ufafanuzi na ufumbuzi mambo yake yaliyo fungika na yasiyo eleweka.
Hakika, Ismah katika maneno ya waarabu ina maana ya kuzuwia
na maana hii ndio tuikusidiayo kwenye istilahi zetu, na Ismah katika istilahi hii ina maana ya uzoefu wa kinafsi kumtawala au kummiliki mwanadamu na kumzuwia kufanya maasi na kuuacha utiifu na kuitawala akili yake na hisia zake na viungo vyake na kumfanya awe ni mwenye kuamka na kuelewa kwa kiasi kikubwa (kwa wakati wote) na kumfanya asiwe ni mwenye kusahau wala kughafilika wala kufanya matendo yasiyo ridhiwa na Mwenyezi Mungu.
Hakika mwenye kufanya maasi ni dhalimu katika istilahi ya Qur'ani.
"Na mwenye kuvuka mipaka ya mwenyezi Mungu hakika hao ndio madhalimu
"
"Na mwenye kuvuka mipaka ya Mwenyezi Mungu hakika amesha idhulumu nafsi yake
".
"Hawa ndio ambao walimsingizia uwongo Mola wao, hakika laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya madhalimu
".
"Kisha tutawaokoa wale ambao walimcha Mwenyezi Mungu na tutawaacha madhalimu humo wakiwa wamepiga magoti
".
Na mfano wa aya hizo ambazo ni nyingi ndani ya Qur'an tukufu.
Na mfanya maasi huyo ambae Qur'ani imemuita "dhalimu" hawezi kuvumilia kubeba majukumu ya sheria yenye kuhusiana na Mwenyezi Mungu Mtukufu na dini yake na sheria yake. Hayo ndio yaliyo tajwa waziwazi na Qur'ani tukufu kwa kusema:
"Na pindi Mola wako alipomfanyia majaribio Ibrahim kwa maneno akayatimiza (Mwenyezi Mungu) Akasema:"Hakika mimi nimekufanya uwe Imamu kwa watu. (Ibrahim) akasema na katika kizazi changu je! (Mwenyezi Mungu) Akasema: Ahadi yangu haiwapati madhalimu
".
Na bwana Fakhru Razi amesema katika kuitafsiri aya hii:"Imethibiti kwamba makusudio ya ahadi kwenye aya hii ni uimamu Na ikiwa aya inajulisha kuwa Imamu hawi muovu, basi aya hii kutujulisha kuwa Mtume haifai kuwa muovu na mwenye kufany a madhambi na maasi ni kwa njia bora zaidi
.
Kwa hivyo inaonekana kuwa maana ya "Ismah" na kuijalia kuwa ni sharti la uimamu na imamu sio fikra ngeni au itikadi ya ajabu, bali hiyo ndio maana inayo wiana na dalili za kisheria zilizo sahihi na ni fikra ya asili ya dini.
Dr Ahmad Mahmoud Subhi katika maelezo yake juu ya mas'ala ya "Ismah" kwa mashia amesema:
"Hakika wanafalsafa wote wa siasa walipo yazungumzia na kuyafanyia utafiti maudhui ya uongozi au utawala wa juu katika dola na serikali au kiongozi wa juu kabisa katika serikali, waliiweka na kuipa nafasi ya juu ya kiwango cha Shubha (kisichokubali kuingiwa na shaka) na wanafalsafa pia wanasiasa wenye kuamini siasa ya kidikteta na wale waliothibitisha kuwa kiongozi wa juu kabisa serikalini ni hakimu (mtawala) walithibiti-sha sharti la ismah hata ingawa walichagua sifa zingine anazota-kiwa kuwa nazo.
Na vilevile wanafalsafa wa mfumo wa demokrasia waliwasifia wananchi au wawakilishi wao au katiba kuwa ni vyenye ismah (yaani wasio fanya makosa). Na inadhihirika kuwa kuhifadhika na kutotenda makosa (Isma) ni lazima kuwe ni sifa ambayo anasifika nayo mwenye jukumu la uongozi wa juu katika dola kama dhamana pekee ya kubakia kwa nidhamu ya utawala na sababu ya kuungwa mkono na wananchi.
Hakika nidhamu zote au mifumo yote ya kisiasa pamoja na tofauti zake, zinakubaliana juu ya ulazima na wajibu wa kuwepo serikali ya juu kabisa ambayo ndio inayo kuwa marejeo ya hukumu zote, na yeyote hawezi kuwa ni mwenye cheo au madara-ka kwenye serikali hiyo vyovyote atakavyo kuwa amemtawala yeyote au utashi wa watu wote au katiba isipokuwa tu atakapo kuwa amepambika na aina fulani ya utakasifu na kusifiwa na sifa ya Ismah (yaani asiwe ni mwenye kufanya makosa).
Kwa hivyo basi, ismah ya Imamu wa kishia si jambo lenye kushangaza, vyovyote neno hili litakavyo onekana kuwa na habari za ghaibu (za mbinguni). Na ikiwa mashia ndio wa mwanzo walianzisha utafiti kuhusu uhakika na undani wa Ismah na mipaka yake lakini si wao peke yao ambao wameshikamana na kauli hiyo.
Na vyovyote mambo yatakavyo kuwa, imekwisha dhihiri kutokana na yaliyotangulia kuwa mashia katika upingaji wao wa kuchaguliwa imamu na watu, hawakutoa upingaji huo kutokana na mwelekeo fulani wenye kutawaliwa na hisia kwa mtu fulani au kutokana na rai fulani ya kisiasa kwa maana inayo eleweka ya kisiasa, bali waliona kutoka kwenye uteuzi kupitia dalili (Qur'ani na Sunna ya mtume) dhamana ya maisha mema na nyenzo salama ya ujenzi,
wao hupata msukumo wa kuiunga mkono rai hii kutokana na roho ya imani ya uislamu na kuwa na ikhlasi ya kufikia lengo (walilo umbwa kwa ajili yake) na kwa kuhisi maslahi yaliyopo. Na hivyo inatuwia wazi kuwa kauli isemayo kuwa ni lazima kuwepo uteuzi:
1- Inaungana moja kwa moja pamoja na hisia za kimaumbile ndani ya mwanadamu, kitu kinacho zaa hisia ya kuwepo mahita-jio ya nguvu ya ghaibu na kuitii kwa mambo yote.
Na uimamu -kama tunavyo fahamu- ndio kichwa cha mambo hayo ambayo humfungamanisha mwanadamu na nguvu hiyo ya ghaibu kwa kupewa hali ya kuhisi utulivu na raha na kusalimu amri kiukamilifu kwenye njia ya salama na mwendo wake kuwa thabiti kwenye njia hiyo.
2- Kauli hiyo inaungana vilevile pamoja na elimu ya nafsi isemayo kuwa ni lazima kung'oa mizizi ya vitu vimpelekeavyo mtu kuwa na hali ya kuchukia na kuwa na wasiwasi na ni lazima kumkataza au kumzuwia asiwe na roho ya kutoitii kanuni.
Na pindi Imamu anapo kuwa ameteuliwa na yule Mwenye wahyi (au Mtume) moja kwa moja, kila mtu atakuwa na matu-maini ya mia kwa mia ya kuenea na kutawala uadilifu na utakasifu na usawa wa kweli na ikhlasi iliyo ya kweli. Na kwa kufanya hivyo mambo yote yasababishayo wasi wasi au kero au uchovu na kutozitii amri yatatoweka.
3:Na pia inaungana na rai waliyo shikamana nayo wanazuwoni wote wa mambo ya jamii kuwa dini ni mfumo wa juu zaidi wa kuunganisha na kuleta mshikamano kwenye maisha ya jamii, na yale yahisiwayo na watu wa dini hizo kama udugu na umoja na kuridhiana kiukamilifu.
Na Imamu alieteuliwa kwa dalili ndie mtu wa juu kabisa na hakuna shaka yeyote katika kazi ya kuunganisha na kuleta mshikamano ulio ungana na chanzo cha juu kabisa (Mwenyezi Mungu) na katika kuhifadhi imani kuwa uchaguzi wake ulikuwa mzuri na uteuzi wake ulikuwa salama.
Na fikra hii haitoweza kudhurika baada ya kuthibiti asili yake kuwa ni ya kiislamu, iliyo chukuliwa kutokana na dalili za Qur'ani na hadithi za Mtume, na baada ya kuthibitika uwiano na muungano wake pamoja na hisia za kimaumbile na misingi ya kielimu ya elimu ya nafsi na elimu ya jamii, hata kama mtu yeyote atajitokeza na kuipinga au kuibeza au kuipa majina tofauti atakayo.
Naam, uimamu hautodhurika baada ya kuthibitika yote hayo yaliyo tangulia kwa kuitwa na baadhi ya waandishi kwa jina la "Theocracy"
(yaani utawala wa kidini). Hakika jina hili likikusu-diwa "Hukumu ya dini" halina matatizo, bali hali ndivyo ilivyo kiukweli wake. Na ikikusudiwa kwa jina hilo kuwatawala "kimabavu" watu kwa jina la dini kwa kulinganisha na utawala mbaya wa kanisa siku za kale, kufanya hivyo ni kinyume na uhakika wa uimamu katika nadharia na katika utekelezaji.
Na kwa kuyazingatia hayo Dr.Majiid khaduri alilipinga jina hilo kwa kutowiana kwake na ukweli ulivyo, na akachagua jina lingine alilo litoa kwenye mifumo madhubuti ya uislamu nalo ni "Nemocracy"
yaani utawala ambao uongozi wake ni wa kanuni.
Na huu ndio ukweli ambao mwenye shaka na mpingaji hawezi kuupinga vyovyote watakavyo zama kwenye shaka na upingaji. Na uimamu vile vile hautadhurika ikiwa baadhi ya waandishi watauita kwa jina la "udikteta". Kwani utawala wa kidikteta ni utawala ambao nafasi ya uongozi wa juu ni ya mtu mmoja au watu kadhaa maalumu, kwa hivyo dola linakuwa ni milki au mali ya watu wale na huzichezea kanuni na sheria kama watakavyo, na haya yana pingana -kiukamilifu- na mfumo wa utawala wa kiislamu ambao unauzingatia uongozi wa juu kuwa ni uongozi wa kanuni pekee, na sio wa kitu kingine. Na nijambo lililo wazi kuwa uongozi wa kanuni kama alivyo utekeleza Mtume na kuonekana kwenye zama zake au utawala wa Imamu wa kwanza Ali bin Abi Twaalib
katika hali ya kawaida na wakati wa vita, uongozi huo na udikteta ni vitu viwili vinavyo pingana.
Kisha uimamu hautodhurika kuitwa kwa jina la "Utawala wa kitabaka" au utawala wa tabaka fulani, kama ulivyo itwa na baadhi ya waandishi. Na ni jambo lenye kueleweka kuwa utawala wa "tabaka fulani" maana yake ni kuidhoofisha sheria yote kwa ajili ya maslahi ya tabaka lile na kuvielekeza vyombo vyote vyenye nguvu kuyaendeleza maslahi makhsusi na ya kibinafsi ya tabaka hilo. Na hayo ni mambo ambayo hayana ukaribu na uhusiano wowote na Uislamu kwa aina yoyote ile na kwa mahusiano ya aina yoyote.
Hakika uongozi wa kanuni ya kuvitawalisha vyanzo vya sheria na kutomruhusu yeyote hata Imamu mwenyewe kubadili-sha dalili (Qur'an na suna) na kuzigeuza hukumu kunakata mahusiano kati ya Uimamu na kila fikra ya utabaka ambayo huenda baadhi wakajaribu kuilinganisha na kuihusisha na nidhamu hii (ya uimamu).
Na mwisho - na sio mwishoni- uimamu hauto dhurika kuitwa kuwa ni mfumo "usio wa kidemokrasia". Kwa hakika thamani ya kimsingi ya demokrasia -ikiwa kama nadharia- hudhihiri katika msemo wake usemao "Utawala wa wananchi"(au utawala wa watu) nayo thamani ya kimsingi ya watu na utawala wao inatokana na kuamini kuwa "watu ndio chanzo cha tawala zote" (au serikali zote).
Na kutokana na ukweli kuwa Mwenyezi Mungu -kwa nadharia ya kiislam- ndie afanyae alitakalo, ilikuwa ni lazima kukiri na kukubali kuwa yeye ndie kauli ya mwisho katika kila jambo kati ya mambo ya utawala na nidhamu.
Na ukizingatia kuwa Mtume ndie mtamkaji pekee kwa jina la chanzo cha tawala na muwakilishi muaminifu wa huyo mwenye kauli ya mwisho (Mwenyezi Mungu) hakika kumteuwa kwake Imamu unakuwa ni uteuzi wenye kuridhiwa utokeao kwenye chanzo hicho cha sheria, na kwa kufanya hivyo atakuwa ameungana na mantiki (fikra) ya kisiasa isemayo kuwa ni lazima kukitaka ushauri chanzo cha tawala zote katika uchaguzi na uteuzi.
DALILI YA KUTEULIWA KWA IMAMU
Muhtasari wa sehemu iliyo tangulia ni kama ifuatavyo:
Hakika uimamu ni lazima kuwepo ili kuendesha na kundeleza mwendo wa kiislam. Na uimamu haupatikani isipo-kuwa kwa kutumia dalili na uteuzi kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
mwenyewe kwa kuzingatia kuwa ni mtu ambae hatamki kwa matamanio au matakwa yake.
Na kwa kumaliza sehemu hiyo ya utafiti kwa muhtasari huo ulio wazi tuna hamia kwenye hatua mpya inayo kusudia kumtafuta imamu alie teuliwa kwa dalili na kuzitafuta dalili tukufu ambazo zimemtaja imamu mwenyewe.
Na kutokana na kuwa dalili za uimamu riwaya zake ni nyingi sana pamoja na wapokezi wake na ni zenye mifumo tofauti ya kutoa ushahidi na ambazo hazihesabiki kwenye sehemu finyu kama hii, sisi tutakomea katika kuzitaja tatu kwa haraka, tukiyaacha mazungumzo marefu na mapana yenye kuelezea pande zake zote kwenye vitabu vikubwa vilivyo jihusisha na maudhui haya.
DALILI YA KWANZA:
Hadithi ya nyumba (Hadithu ddarr)
Ameitoa Ibnu jariir At-twabari kwa upokezi wake kwamba Mtume(s.a.w.w)
pindi ilipo telemka kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
"Na waonye jamaa zako wa karibu"ali-waita wana wa Abdul-Muttwalib kwake, wakiwemo ami zake (baba zake wadogo ), kama vile Abu-Twalib, Hamza, Abbas na Abu Lahab.
Na walipo maliza kula Mtume wa Mwenyezi Mungu akasimama kati yao kwa ajili ya mazungumzo na akasema:"Enyi wana wa Abdul-Muttwalib, ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi simjui kijana yeyote katika waarabu alie waletea kaumu yake (watu wake) kitu bora zaidi ya kile nilicho kuleteeni. Hakika mimi nimekuleteeni kheri ya dunia na akhera. Na Mwenyezi Mungu ameniamuru nikuiteni kwenye kitu hicho, sasa ni yupi miongoni mwenu atanisaidia juu ya jambo hili ili awe ndugu yangu na wasii wangu na khalifa wangu kati yenu? Watu wote wakanyamaza. Ghafla Ali
akasimama na kusema:"Mimi, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nitakuwa waziri wako (msaidizi) juu ya jambo hilo". Mtume(s.a.w.w)
akasema: "Hakika huyu ni ndugu yangu na wasii wangu na khalifa wangu kwenu msikilizeni na mumtii". Watu wale wakasimama huku wakicheka na wakimwambia Abu Twalib:"Hakika amekuamuru umsikilize mwanao na umtii".
Hakika dalili hii ya kihistoria imekusanya sifa tatu za Ali:
1- Waziri (Msaidizi)
2- Wasii (Muusiwa)
3- Khalifa (Mshika makamu)
Na ni haki yetu kujiuliza na kusema:
Kwa nini Mtume alimpa Ali sifa hizo tatu na asiwape wengine? Na ni kwanini alichagua mjumuiko wa kwanza kufanyi-ka baada ya kupewa utume kwa ajili ya kufanya jambo hilo?
Na ikwa usaidizi ni lazima kwake kwa kuzingatia kuwa yeye alihitajia -kwa wakati huo- kuwa na msaidizi na waziri kwa nini basi, aliongeza cheo cha wasii na khalifa kwa matamshi haya mawili? Na kuna uhusiano upi kati ya usia au muusiwa na khalifa katika kuwaonya jamaa zake na kuwaita watu wa familia yake kwenye uislamu?
Na kwa ajili ya kuweka wazi jawabu la maswali haya, ni lazima tusisahau na kughafilika kuwa Mtume(s.a.w.w)
katika mazungumzo haya anatangaza kwa mara ya kwanza mwanzo wa dola jipya na zama mpya na jamii mpya.
Na anatangaza kuwa utawala wowote au jambo lolote ili libakie hai na liwe ni lenye kuendelea ni lazima liwe na raisi au kiongozi wa juu kabisa mwenye kuongoza jambo hilo na kuuelekeza usukani wake na nilazima kuwepo naibu wake ambae watu watamrejelea ikiwa raisi atapatwa na jambo fulani la kumfanya asifanye kazi yake.
Na Mtune(s.a.w.w)
katika mazungumzo na msimamo ule alikuwa akilenga kuwafahamisha watu wale walio hudhuria kwamba mas'ala haya ya kidunia na kidini sio mas'ala ya kutawala tu na kuyatumia kujikingia kwa kivuli chake au ni uraisi anao utumia na kufaidika nao maadamu yuko hai, bali ni ujumbe kutoka mbinguni na ni ujumbe wa milele hautokufa kwa kufariki kwake na hautakwisha kwa kumalizika kwa umri wake bali utabakia kwa muda wote wa kubakia kwa mbingu na ardhi, na baada yake kutakuwa na mtu atakae beba majukumu hayo na kutekeleza mambo yake yote, nae ni kijana huyu ambae anatangaza uwezo wake na maandalizi yake ya kujitolea muhanga na kujitoa fidia na kuwa msaidizi, na si mwingine tumkusudiae, bali ni Ali bin Abi Twalib
.
Na haya yote tunayapata pindi tunapofanya utafiti na kudadisi kwa uwazi kwenye hadithi tukufu ya Mtume tuliyo itaja hapo punde.
Na Imamu Raazi kutokana na kutopata kigezo cha kuto ikubali na kukiri usahihi wa hadithi hii na sanadi (upokezi wake) na kuwa ni dalili iliyo wazi, akafanya haraka kutia shaka kwenye maana ya ukhalifa ulio tajwa kwenye hadithi, akidai kuwa Mtume(s.a.w.w)
angekuwa amekusudia pindi alipo fanya hivyo kumteuwa khalifa baada ya kufariki kwake asinge ishia kusema "na khalifa wangu kwenu", bali ange ongezea kwenye ibara hiyo neno "bada yangu" ili iwe ni dalili iliyo wazi.
Na ukweli ni kuwa sisi hatuoni tofauti kati ya ibara hizi mbili. Na ikiwa "Khalifa wangu kwenu baada yangu" iko wazi katika ushahidi wake, vile vile "Khalifa wangu kwenu" ni hivyo hivyo, kwa sababu maana yake ni kuwa Ali ndie ambae atakaekuwa khalifa wangu na atakae chukua nafasi yangu kwenu ikiwa nitapatwa na jambo lichukizalo (yaani kifo), na hii ni dalili juu ya ukhalifa baada ya kufariki, na maana hii inatiliwa mkazo na neno "wasii" alilo taja Mtume.
Usia katika Uislam unakusudiwa baada ya kifo, kiasi kwa-mba muusiwa (wasii) hufanya aliyotakiwa ayafanye yule alietoa usia. Na jambo hilo kama lingekuwa linahusu mambo yaliyo kabla ya kifo angesema "Wakili wangu" na asinge sema "Wasii wangu", kwa sababu uwakili ndio ibara itumikayo kwenye uislamu kwa anaetakiwa kutekeleza baadhi ya mambo ya mtu aliepo na alie hai.
Kwa hivyo basi, dalili iko wazi kuwa Mtume(s.a.w.w)
tangu siku ya kwanza alichagua mtu atakae kuwa baada ya kufariki kwake kwa ajili ya kuendeleza kazi ya wito na atakuwa ni wasii wake katika kuyalinda mambo ya waislamu, ili jahazi lisiende mrama na kuwa chini ya huruma ya mawimbi na pepo kali baada ya kufariki nahodha wake. Na huu ni mwanzo uliodhihiri na kuchomoza pamoja na sauti ya kwanza iliyo sikika ya wito wa kiislamu, wito ambao nafasi yake ilikuwa ni finyu na katika siku zake za mwanzo, na akaendelea kusisitiza na kutilia mkazo kwenye mwanzo huo hadi siku ya mwisho ya umri wake Mtume wa uislamu.
DALILI YA PILI:
Hadithi ya cheo (Hadithul-manzilah)
Ameitoa Muslim kwa upokezi wake kwamba Mtume(s.a.w.w)
alimwambia Ali:
"Wewe kwangu ni sawa na cheo cha Haruna kwa Mussa, isipokuwa hakuna Mtume baada yangu
".
Hadithi hii tukufu, pamoja na ufupi wa matamshi yake inaashiria kwenye maana nyin gi ambazo huenda zisionekane wazi kwa mtizamo wa haraka haraka, lakini maana hizo zina onekana wazi bila kizuizi pale msomaji atakapo fanya udadisi kidogo kwenye upana wa maneno na maana zake na makusudio yake.
Hakika hadithi ina ashiria kuwa Ali:
A: Ni waziri wa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwani Haruna alikuwa ni waziri wa Mussa, kama aya isemavyo:
"Na uniwekee waziri (msaidizi) kutokana na jamaa zangu
".
B: Ni ndugu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kwani Haruna alikuwa ni nduguye Mussa kama aya isemavyo: "Haruna ndugu yangu
".
C: Ni mshirika wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwani Haruna alikuwa ni mshirika wa Mussa kama aya isemavyo:
"Na mshirikishe kwenye jambo langu".
D: Ni khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwani Haruna alikuwa ni khalifa wa Mussa kama aya ilivyo sema:
"Na akasema Mussa ku-mwambia nduguye Haruna:"Kuwa Khalifa wangu kwenye jambo langu hili".
E: Ni uimamu chimbuko lake kuwa ni utume, kwani dhamiri " anta" iliyo tumika kwenye hadithi inauelezea uimamu na dhamiri ya (yee) kwenye tamko (minniy) ina uelezea utume, na herufi ya jari hapo ina maana ya kuanza na kuwepo, na ili isitumike katika uanzaji huu na chimbuko hili kuwa kuna ulingano kati ya maana zake au vitu hivyo kuwa sawa Mtume akafafanua kuwa kuna tofauti ya msingi ambayo ni utume akasema:"Isipokuwa ni kwamba baada yangu hakuna utume"
Na kutokana na kuwa Mussa alikuwa ame-muo mba Mola wake amuwekee waziri (msaidizi) kutokana na jamaa zake, kama aya ilivyo tujulisha, hakika hilo linatujulisha kuwa ukhalifa na uwaziri kwa ajili ya Mtume unawekwa na kujaaliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu, na sio uchaguzi wa watu au kwa uteuzi wao.
Na hivi ndivyo mtazamo wa udadisi unavyo tuwekea wazi zile maana pana za mbali ambazo hadithi hupanuka na kuzifikia, nazo ni maana zenye kina, ambazo haifai kuzitafsiri kwa msingi tu wa kumtukuza na kumfurahisha Ali
, bali nyuma yake kulikuwa na lengo kubwa, nalo ni kuutanabahisha umma na kuu-fahamisha atakae shika nafasi ya Mtume baada ya kufariki kwake katika suala la kuliongoza dola na kuliongoza jahazi na kuuelekeza usukani wake.
Na ushirika ulio elezwa na hadithi hii, ushirika wa Ali kwa Mtume -Sio ushirikiano wa kibiashara kwenye bidhaa au uundaji au kilimo- unakusudiwa ni ushirika katika kubeba majukumu ya uislamu na kutekeleza mambo muhimu yanayo husiana na dini hii. Na kutokana na kuwa ushirika huenda mipaka yake ikafi-chika na isieleweke kwa msikilizaji wa kawaida (na hasa baada ya kufahamu utume wa Haruna). Mtume akaielezea hadithi ya cheo kwa kueleza mambo yanayo ondoa dhana na kuelezea makusudio ya ushirika huo akapinga kuwepo kwa Utume kwenye ushirika huo moja kwa moja na kuuweka utume nje ya ushirika huo kama tulivyo tangulia kusema.
Na huenda mambo yadhihirishayo wazi umuhimu wa hadithi hii na ushahidi wake na dalili yake na upana wake ni kufahamu kuwa: Sababu iliyo mpelekea Mtume kutangaza cheo hiki ilikuwa ni wakati alipo muacha Ali akiwa naibu wake na mshika nafasi yake kwenye mji wa madina pindi alipo toka kwenda kwenye vita vya Tabuk.
Na Sheikh Ibnu Taimiyya alipinga na kusema kuwa katika mnasaba wa tukio hili hakuna kitu kithibitishacho fadhila yoyote kwa Ali kamwe kwenye hadithi hii kwa sababu Mtume alifuatana na maswahaba wengi na muuminina, na Ali hakumuacha isipo-kuwa na wanawake na watoto, seuze wale ambao hawakwenda vitani na wanafiki na kumuacha mtu kwenye uangalizi wa watu kama hawa hakuna maana yoyote kati ya maana za utukufu na kukirimiwa.
Lakini mwenye kufanya mazingatio na kuelewa mambo atatoka na natija nyingine, tofauti na natija aliyo iona Ibnu Taimiyya anapo soma mazingira ya hadithi hii:
Mji wa madina, ulikuwa ni mji mkuu wa dola na makao makuu ya Utume na Mtume. Na pindi raisi anapo safiri na kuacha mji mkuu na kwenda sehemu ya mbali, kama Tabuuku, na kwa kutumia nyenzo za kizamani na za mwanzo katika mawasiliano na zenye kutumia muda mrefu, na vita havieleweki ni lini vitamalizika, na ni wakati gani watarudi kutoka vitani, bila shaka kuchagua kwa raisi huyu naibu atakae shika nafasi yake kwenye mji mkuu, na hasa mji mkuu ambao ulikuwa umezingi-rwa na hatari mbali mbali na wanafiki na maadui wenye kusubiri fursa yoyote na wakati wowote ili wauchukue mji huo au cheo hicho, mazingira hayo yana tufafanulia kwa uwazi maana kubwa na ya hatari katika uchaguzi huo na uteuzi huo.
HADITHI YA TATU:
Hadithi ya bonde la ghadiir. (Hadithul Ghadiir).
Wameipokea hadithi hii maswahaba wengi sana na taabiina, na maulama na mahufadhi wameipokea pia.
Na kwa ajili ya kufupisha tutachukua kwenye hadithi sehemu ya ushahidi, sehemu ambayo imeungana na hadithi moja kwa moja juu ya uimamu na uteuzi wa imamu. Msimuliaji wa hadithi hii amesema:
Mtume alipokuwa njiani akitokea kwenye hija ya kuaga (ya mwisho) na alipo kuwa amefika sehemu iitwayo Ghadir-Khum, alisimama baada ya sala ya adhuhuri ili kuhutubia kati ya waislamu na miongoni mwa mambo aliyo wambia ni kama ifutavyo:
"Enyi watu! Huenda nikaitwa na kuitika, na mimi nitauli-zwa, nanyi mtaulizwa ni kitu gani mtakacho sema? Wakasema: "Tunashuhudia ya kuwa wewe umefikisha ujumbe na umepigana jihadi na umetoa nasaha. Mwenyezi Mungu akulipe kheri. Mtume akaendelea kuzungumza hadi akasema:"Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtawala (Bwana) wangu, na mimi ni mtawala (Bwana) wa waislamu, na mimi ni bora zaidi kwao kuliko nafsi zao. Kwa hivyo basi yeyote ambae mimi nilikuwa mtawala (Bwana) wake huyu Ali ni mtawala wake. Ewe Mwenyezi Mungu mpende mwenye kumpenda Ali na mfanyie uadui mwenye kumfanyia uadui Ali, na mnusuru mwenye kumnusuru Ali, na ifanye haki, iwe pamoja na Ali popote atakapo kuwa.
Na mtume akamalizia maneno yake nao watu wakamki-mbilia Ali na kumpongeza na kusema: "Hongera! Hongera! Ewe Ali! Umekuwa mtawala wetu na mtawala wa kila muumini wa kiume na wa kike". Kisha akateremka Jibrilu na wahyi wa Mwenyezi Mungu na kusema:
"Hivi leo nimekukamilishieni dini yenu, na nimezitimiza kwenu neema zangu, na nimeridhia kwenu uislamu kuwa ndio dini". Huu ndio ufupi au muhtasari wa hadithi ya Ghadiri Khum na mazingira yake, na haya ndio matamko yaliyotumika kama yalivyo simuliwa na wathibitishaji. Na imekuja ikiwa wazi kabisa katika kuthibitisha fikra ya "Uimamu" yenye utawala wote na majukumu yaliyo mapana na katika kumteua "Imamu" mwenye majukumu baada ya kufariki Mtume(s.a.w.w)
. Na inatutosha dalili moja juu ya uwazi huo nayo ni waislamu kufahamu hivyo na kuharakia kutoa baia, kitendo ambacho kilikuwa ni natija ya kufahamu kwao jambo hilo, na kwenda kumpongeza na kuonye-sha furaha yao kwa mnasaba huu au tukio hili tukufu na zuri.
Na wakajitokeza kwetu baada ya muda fulani, watu wenye kudai kimakosa kuwa ni wenye falsafa, na kusema baada ya kufahamu usahihi wa hadithi hii na kutokuwepo uwezekano wa kuipinga, kuwa haikuwa ni dalili juu ya suala hilo, kwa sababu tamko "maula" katika lugha ya kiarabu linatafsiriwa kwa maana nyingi, kama mfuasi, mwana wa baba mdogo, rafiki, mrithi, na mfano wa hizi, na hatufahamu Mtume alikusudia nini kwa kutumia tamko hilo, na ni maana ipi kati ya maana hizo aliikusudia.
Na huku kujifanya wanafilosofia (wachambuzi) kulitokana na matamanio na malengo fulani, na yaliyo mbali na utafiti wa kina na kimaudhui. Na inatosha katika kubatilisha madai haya kufanya mazingatio ya kina kwenye mambo yafuatayo:
1- Kuteremka kwa aya ya tablighi kabla ya Mtume(s.a.w.w)
kusimama na kutangaza utawala (wilaya). Wanahistoria wamesimulia na mufassirina kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alimle-tea wahyi Mtume wake akiwa ametokea Makka baada ya hija ya kuaga na kusema:
"Ewe Mtume fikisha ulicho teremshiwa kutoka kwa Mola wako, na kama hukufanya utakuwa hukufikisha ujumbe wake na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu
".
2- Mtume(s.a.w.w)
kusimama katikati ya jangwa na kwenye jua kali la adhuhuri kwa ajili ya kutangaza utawala huo.
3- Kuelezwa tawala za aina tatu kwenye maneno ya Mtume(s.a.w.w)
:
A: Mwenyezi Mungu ni Mtawala wangu.
B: Mimi ni mtawala wa waumini.
C: Yeyote ambae nilikuwa ni mtawala wake huyu Ali ni Mtawala wake
.
4: Kumalizia khutuba au mazungumzo yake kwa kumuombea:
"Ewe Mwenyezi Mungu mpende ampendaye na mfanyie uadui mwenye kumfanyia uadui na umnusuru mwenye kumnusuru na muache mwenye kumuacha na ifanye haki iwe pamoja naye popote atakapo kuwa".
Na kwamba dua haiwiani kamwe na jambo au maana nyingine tofauti na utawala wote (mpana) na uongozi juu ya waumini.
5- Kuteremka kwa aya ya kukamilisha dini tuliyo itaja hapo kabla:
Ijulishayo kutokea kwa jambo la hatari na muhimu ambalo Mwenyezi Mungu aliikamilisha dini na kuitimiza neema ya jambo hilo.
6- Na waislam walio kuwepo kwenye tukio hilo kumponge- za Ali kwa mfumo tulio utaja.
Hakika kwa kufanya udadisi kwenye pande zote hizi sita kunatufanya tuamini kwa imani kamili na yakini kamili kuwa makusudio haikuwa kuwazindua waislam kwamba Ali ni mrithi au mfuasi wa Muhammad au ni rafiki yake au kuwa ni mwana wa ami yake.
Na mas'ala ya urithi au kunusuru, lau kama Mtume angetaka kuyazungumzia hayo yalikuwa hayahitajii kuyaelezea kwenye hali na mazingira kama yaliyo kuwepo siku ya tukio la Ghadir Khum, kama vile mazingira yenyewe na kwenye mnasaba ule, pia kuteremshwa kwa aya na Mwenyezi Mungu kati ya aya zilizo wazi, na kutumika mifumo maalumu ya kumpongeza Ali na kumbariki bali yote hayo hayatakuwa na maana yenye kukuba-lika kama usingekusudiwa uimamu na kumteua khalifa na kutoa kiapo cha utiifu (bai'a).
Na huenda Dr Ahmad Muhammad Subhi akawa ameuleta karibu ukweli au ameufikiria, kwa yale aliyo yatolea ushahidi katika kutoa sababu ya kukataa kwa walio kataa hadithi hii pale alipo sema:
"Kwa kuwa Ahlu dhaahiri na Salafiya walikuwa wakimfuata Muawiya kama mtawala hakika hawakuwa na kimbilio tofauti na kuchagua ima kuuacha utawala huo au kuipinga hadithi hii kwa kutumia nyenzo mbali mbali. Na pamoja na kuwa ni wajibu itikadi zetu zifuate dalili, isipokuwa ukweli ni kuwa watu wengi wenye madhehebu, walizifanya hadithi ziwe ni zenye kuyanye-nyekea matakwa yao na madhehebu yao.
Kwa hivyo imethibiti kutokana na yote yaliyo tangulia kwamba Mtume(s.a.w.w)
alitoa dalili juu ya Imamu ambae atachu-kua nafasi yake katika kuuongoza umma huu. Na dalili iliyo ashiriwa, hata kama matamshi yake yatatofautiana na minasaba yake, ilikuwa iko wazi na mafhumu yake yalikuwa bayana.
Lakini: Je kuthibitika dalili juu ya Imamu wa kwanza Ali inatosha kuitumia na kuwateuwa maimamu wengine au ni lazima kuwepo na dalili inayo wahusu wao vilevile?
Kwa hivyo basi vipi umeweza kuthibiti uimamu wa maimamu wengine? Na iliwezekana vipi idadi yao kuifunga kwenye kumi na mbili haizidi wala kupungua?
Hakika ulithibiti uimamu wa maimamu wengine kwa njia mbili:
Njia ya kwanza:
Hadithi nyingi za Mtume(s.a.w.w)
ambazo wingi wake umefikia kiwango cha kuwa mashuhuri sana, kama kauli yake(s.a.w.w)
akimuelezea Hassan na Hussen:
"Nyinyi wawili ni maimamu na mama yenu ana uombezi
".
Na kauli yake(s.a.w.w)
akimuashiria Hussen:
Huyu ni imamu, mwana wa imamu, ndugu wa imamu, baba wa maimamu
".
Na hadithi zenye mfumo kama huu ni nyingi, na ambazo riwaya zake zimo kwenye vitabu vya hadithi na historia na masomo ya juu yaliyo husika na maudhui au bahthi ya uimamu.
Njia ya pili:
Ni dalili ya alietangulia kumthibitisha atakae fuatia. Na dalili au hadithi inayotoka kwa aliyemtangulia mwenzake kumthibi-tisha wa baada yake ni hoja na ni lazima kuifuata na kuifanyisha kazi na kuitii maadamu tuna itakidi uimamu wake uliosimama juu ya msingi wa kuwa yeye ni mkweli na muaminifu juu ya wadhifu wa kuihifadhi dini (uimamu)
.
Ama uthibitisho wa kuwa maimamu ni kumi na mbili hawazidi wala kupungua ni nyingi vile vile.
Na inatutosheleza kwa yote hayo hadithi ya Mtume iliyo mashuhuri ambayo wanazuoni wamekubaliana juu ya upokezi wake, pia mashekhe wa hadithi na mahufadhi wa sunna ya Mtume walio maarufu nayo ni kauli yake isemayo:
"Dini itaendelea kusimama hadi kiama kisamame, na kuwe juu yenu makhalifa kumi na wawili wote watokanao na (kabila la) Makuraishi
".
Na katika hadithi nyingine imekuja kwa matamshi mengine:
"Hakika jambo hili halitamalizika mpaka wapite maimamu kumi na mbili
".
Na pindi tunapofanya udadisi kwenye hadithi hii, ambayo waislamu wote wamekubaliana juu ya usahihi wake, tunaikuta kuwa inaweka wazi mambo mawili:
1: Kuendelea kuwepo dini hadi siku ya kiama.
2: Kuwepo makhalifa kumi na mawili tu, kwa muda wote ambao dini ita kuwepo na ikisimamia na kuyachunga mambo ya waislamu na uislamu.
Na jambo lililo wazi ni kuwa Mtume(s.a.w.w)
aliposema kuwepo kwa makhalifa kumi na mbili hakuwakusudia makhalifa wale ambao waliwatawala waislamu kwa muda wa karne kumi na nne zilizo pita, kwani wao ni zaidi ya "kumi na mbili" kwa mara kadhaa, na kwamba wengi wao walikuwa hawafuati kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna za Mtume, kwa hivyo haiwezekani kuwahesabu kuwa ni makhalifa wa kweli kwa ajili ya ujumbe wa Mwenyezi Mungu na Mtume(s.a.w.w)
, kwa hivyo basi, ni lazima makusudio ya hadithi yawe watu wengine wasiokuwa hawa.
Na hakuna wengine wasio kuwa hawa isipokuwa Ali na wanae kumi na moja ambao waislamu wote wamekubaliana juu ya suala la wajibu wa kuwapenda na kuwatukuza, na kuchukuwa kwao hukumu za dini, na kurejea kwao katika matatizo yatupa-tayo kifikra na kisheria, na kukimbilia au kujitegemeza kwao kila linapo jitokeza tatizo au kila upepo mkali wa zama uvumapo au matukio ya zama yajitokezapo.
Na mwenye kutaka kuelewa zaidi dalili au hadithi za Mtume kuhusu suala la kuteuliwa imamu na kuelezwa idadi yao anaweza kurejea kwenye vitabu vikubwa vilivyo elezea kwa upana zaidi suala hili na masomo yaliyo panuliwa yaliyo jihusisha na maudhui haya.
MAIMAMU (REHMA NA AMANI ZIWE JUU YAO)
Ni lazima kwangu, Ili kuukamilisha mtiririko wa hadithi hii na kukamilisha mfumo wake, kueleza kwa muhtasari, majina ya maimamu watwahirifu na mazingira ya kisiasa yaliyo mzunguka kila mmoja wao, na nina ashiria kwa muhtasari vile vile urithi mtukufu walio tuachia na historia ya maisha yao mema kwa sura ya ujumla, pamoja na kujilazimisha kiukamilifu kufupisha maelezo hayo, ili ukubwa wa kitabu usivuke kiwango kilicho kubaliwa kwenye maudhui yetu na mtiririko wetu huu.
Na yote ninayo yatarajia ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, nae ndie msaidizi na atoae tawfiiq, ni kwamba awe ndie mwenye kunisaidia kuiandika historia ya maimamu hawa watukufu, kwenye vitabu maalumu vyenye kumkusudia kila mmoja wapo kati ya maimamu kumi na wawili, ili vijana wetu wa zama hizi wawe na maarifa kamili ya mwendo na sira za viongozi wa dini yake na urithi wa kielimu walio uacha kwa ajili ya watu wa zama zote zitakazo pita, urithi ambao ni chimbuko la utajiri na nguvu, na ni sababu ya utukufu na kupata daraja za juu, na ndio mwanzo wa utamaduni na maendeleo. Hakika yeye, alie tukuka, ndie Bwana wa usaidizi na tawfiiq.
IMAMU WA KWANZA
ALI BIN ABI TWALIB
Ajulikanae kwa lakabu (sifa) yake maarufu aliyo pewa na Mtume(s.a.w.w)
"Amirul-muumini
"
.
Alizaliwa kwenye mji mtuku-fu wa Makka ndani ya nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu (kaaba) tarehe kumi na tatu (13) mwezi wa Rajab mwaka 30 tokea mwaka wa tembo.
Mtume alimchagua kukaa nae akiwa bado mtoto mdogo, ili kumpunguzia kazi ya malezi Amu yake Abu Twalib, na Mwenyezi Mungu akataka Ali apate hadhi ya kulelewa na Mtume(s.a.w.w)
na kumuelekeza mwenendo mwema tangu utotoni mwake.
Wakati mtume alipo tumwa na kupewa uislamu, Ali alikuwa ndie wa mwanzo kuamini na kusilimu.
Na alipo waita watu wake kwenye uislamu mwanzoni mwa utume, alimteuwa Ali kuwa waziri (msaidizi) na wasii na khalifa, kama tulivyo elezea. Na Mtume alipo kusudia kuhama kutoka Makka kwenda Madina, Ali alijitolea fidia nafsi yake kwa ajili ya Muhammad(s.a.w.w)
akalala kitandani kwa Muhammad ili kuwaonyesha makuraishi kuwa bado yupo kwenye sehemu yake.
Na baada ya kuhamia Madinatul-Munawwara, Ali alishiriki vita vyote vya kiislamu na kubeba bendera ya Mtume kwenye nyanja zote, na hakubakia nyuma kwenye vita vyote vya Mtume isipokuwa vita vya Tabuuk, kwani Mtume alimuacha Madina auhami na kuulinda mji mkuu wa uislamu kutokana na hatari, kama tulivyo eleza.
Mwenyezi Mungu na Mtume walimkirimu kwa kumchagua kwake awe mume wa binti pekee wa Mtume Muhammad ambae ni Fatuma Zahraa.
Na Mtume hakuyamaliza maisha yake isipokuwa tu baada ya kumteuwa Ali kuwa Imamu wa watu kwenye hadithi ya Ghadiri kama tulivyo elezea.
Hata pamoja na matukio yote aliyo yaona na kuishi nayo baada ya kufariki Mtume(s.a.w.w)
hakika hakubakisha nafasi katika kutoa juhudi na nasiha na kutoa nasaha za kuutumikia uislamu na kwa ajili ya kuyatumikia maslahi ya uislamu na kuendeleza mwendo mtukufu ambao ulikuwa ni lazima uendelee na kuuhami usitetereke na kugeuka kutokana na mazingira na hali yoyote itakayo jitokeza.
Waislamu walimkimbilia baada ya kuuliwa Uthumani waki-mtaka akubali ukhalifa akaukubali hali ya kuwa ni mwenye kulazimishwa na akilazimika kuuchukua na kuukubali. Lau kama si kuhudhuria kwa watu wale walio hudhuria na kusimama kwa hoja ya kuwepo kwa wasaidizi, na kuwepo kwa ahadi aliyo-ichukua Mwenyezi Mungu juu ya maulamaa ya kuwa wasikubali shibe ya dhalimu wala njaa ya mwenye kudhulumiwa, angeitupia kamba ya uongozi huo juu ya yule wa mbali na angemnywesha wa mwisho wao kwa glasi ya yule wa mwanzo wao, na watu wangeikuta dunia yao hii kwa Ali kuwa ni kitu duni sana kuliko tembe ya maji ya puwani, kulingana na maneno yake
.
Imam alipata mitihani katika kipindi cha utawala wake kwa kupigana na Naakithiina (waliovunja bai'ah) wafuasi wa ngamia
(As-habu), na Qaasitwini (wenye nyoyo ngumu) wafuasi wa Muawiya, na Maariqina (walio toka kwenye utifu wake) nao ni makhawariji (walio toka kwenye dini).
Alifariki kwenye mji wa Al-kufa kutokana na njama chafu zilizopangwa, katika usiku wa ishirini na moja, katika mwezi wa Ramadhani, mwaka wa 40 Hijiria, na akazikwa sehemu ya juu pembozoni mwa mji wa Al-kuufa sehemu iitwayo "An-najaful Ashraf".