• Anza
  • Iliyopita
  • 9 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 15119 / Pakua: 3605
Kiwango Kiwango Kiwango
USUULID DIIN

USUULID DIIN

Mwandishi:
Swahili

3

USUULID DIIN

UIMAMU

SEHEMU YA KWANZA

FIKRA YA KUWEPO KWA MAHDI

Lau kama tutavitupia jicho la haraka vyanzo vya historia, na hasa historia ya dini mbali mbali, tungeweza kuelewa na kuona kwa uwazi kuwa kumuamini au Imani ya "Mahdi" sio jambo lihusikanalo na shia Imamiyya tu na sio katika mambo ambayo haya kuwepo kwenye dini na wao wakalizuwa, kama wasemavyo baadhi ya waandishi, bali jambo hilo sijambo lihusikanalo na waislamu peke yao na kutowahusu watu wengine wafuatao dini mbalimbali za mbinguni. Bali ukweli ni kuwa mayahudi na wakristo wana itakidi kuwepo kwa msuluhishi mwenye kutara-jiwa kuja katika zama za mwisho nae ni Eliya kwa mayahudi na Issa (Yesu) mwana wa Maryam kwa wa Kristo.

Kama ambavyo waislamu kwa ujumla, pamoja na madhehe-bu yao na vikundi vyao tofauti tofauti wanaamini hivyo kwani Shia Imamiyya (Ithina asharia) na kiisaniyya na Ismailiyya, wao wana amini kuwepo kwa "Mahdi" na wanasema wazi kuwa hilo ni katika mambo ya lazima ya madhehebu yao. Nao masunni wameamini vivyo hivyo (kuwepo kwa Mahdi) kwa kushikamana na rai hiyo kupitia maimamu wa madhehebu zao na wapokezi wao wa hadithi na baadhi yao wakadai kuwa wao ni akina Mahdi kama ilivyotokea Morocco, Libya na Sudan.

Na hivi ndivyo dini tatu za mbinguni (Uislamu,Ukristu na uyahudi) zinavyo kutana katika kuamini fikra hii ya Mahdi.

Na hivyohivyo mashia wanakutana na ndugu zao waislamu kwenye suala hili. Na wanaitakidi kuhusu Mahdi, mambo aliyo yasimulia Dr. Ahmad Amiin katika rai za masuni kuhusu huyo Mahdi kuwa" Yeye ni katika alama za kiama, na kwamba ni lazima adhihiri kwenye zama za mwisho mtu atokanae na kizazi cha Mtume, atakae iendeleza dini na kudhihirisha uadilifu na waislamu watamfuata na atayatawala madola ya kiislamu, na anaitwa Al-mahdi".[75]

Na kwamba rai yao kuhusu suala hilo ni kama rai ya Sheikh Abdul-Azizi bin Baaz, raisi wa chuo kikuu cha Kiislamu cha Madina pindi alipo sema:"Hakika suala la Mahdi ni suala lenye kueleweka na hadithi kuhusu suala hilo ni mustafiidha (zimepo-kewa na wapokezi watatu kwenye kila tabaka) bali ni mutawaatir (wapokezi wake ni wengi sana) na zenye kuungana , na zo kwa ukweli kabisa zina thibitisha kuwa kuja kwa mtu huyu alie ahidiwa, ni jambo lililo thibiti na kutokea kwake ni jambo la Haki".[76]

Na kutokana na haya hakika fikra hii (fikra ya kuja kwa Mahdi) yenyewe ni sahihi kama asemavyo muandishi wa Misri wa zama hizi aitwae Abdul-Hasiib Twaha Hamud.[77]

Lakini la kustajabisha na kuchekesha kuhusu suala hili, ni kuwa Abdul-Hasiib huyu hakugundua pale alipo isahihisha fikra hii kama ilivyo tangulia, ya kwamba alijipinga yeye mwenyewe, na alisahau kuwa alishawahi kutoa kauli ya kuwa:"Fikra ya Mahdi ni mojawapo kati ya matunda ya itikadi za (dini ya) Sabaiyyah"[78] , nae kwa kusema hivyo anakusudia kuwa fikra hii imechukuliwa kutoka kwenye itikadi za mayahudi na haina mahusiano yoyote na Uislamu, hata ingawa hakusudii kwenye ibara yake hii isipokuwa kuwatuhumu Mashia ya kuwa wamechu-kua itikadi zao kutoka kwa mayahudi na kuwa hazina mahusiano yoyote na dini ya Kiislamu lakini kwa hakika amewatuhumu waislamu wote bila ya kutambua, kwa tuhuma mfano huo, na akazizingatia na kuzihesabu fikra alizoziita kuwa ni fikra sahihi hapo mwanzo kuwa ni moja wapo kati ya matunda ya itikadi za sabaiyyah, na huku ni kupingana kimaneno na kutetereka. Na ikiwa yatatujulisha juu ya jambo lolote maneno hayo, hapana shaka yanatujulisha nia mbaya na maradhi ya nafsi aliyo nayo, na hasa ukizingatia kuwa utafiti wa kihistoria wa zama zetu hizi umethibitisha kuwa hakuna mtu alieitwa Abdullah bin Sabai na kwamba huyu ni mtu alietengenezwa katika akili na kuundwa na akapambwa na kupewa sifa za kuwa ni mtu muhimu, na ana fikra fulani na ndie muwekaji wa itikadi na rai kadha, na huenda wale watu ambao walikuwa wakilirudia mara kwa mara jina la Abdullah bin Sabai mwanzoni mwa Uislamu walikuwa wakiku-sudia swahaba mtukufu Ammar bin Yaasir, kama wasemavyo baadhi ya watafiti.[79]

Na vyovyote iwavyo hakika natija ipatikanayo kutokana na utafiti wa kina na ulio safi usio na uchafu ni kuwa, Shia hawaku-zua fikra ya Mahdi, na wala hawakufuata itikadi ya dini ya Sabaiyyah au dini nyingine isiyo kuwa ya Sabaiyya, bali ni kwamba fikra ya kuwepo Mahdi ni fikra iliyo bashiriwa na dini tatu za mbinguni (Uyahudi, Ukristo na Uislamu), na kwamba Uislamu ulipotilia mkazo juu ya ukweli wa kielimu wa fikra ya Mahdy waislamu walifanya haraka kuikubali na kuinukulu na kusalim amri mbele ya fikra hiyo kwa kukubali kikamilifu.

Na haiwezekani yote haya yawe ni kunyenyekea kwa kitu kiitwacho kwa jina la "upotovu wa Shia na bidaa zao", bali ni kukubali na kunyenyekea kuliko sahihi kwenye ukweli utokanao na itikadi za Kiislamu na hadithi za Mtume(s.a.w.w) .

Na mwanazuoni mtukufu wa kisuni wa Iraq, alitoa muhtasari wa ukweli huu aitwae Sheikh Swafau ddin Aalu-Shaykh Al-halkah na akasema: "Ama Mahdi mtarajiwa, hadithi zilizopoke-lewa kumhusu zimefikia kiwango kikubwa na ni zenye kutuachia matumaini kwamba huyu atakuwapo zama za mwisho, na ataurudishia Uislamu usalama wake na imani, atairudishia nguvu yake, na dini atairudishia uzuri wake , nazo ni hadithi muta-waatir bila shaka yoyote wala shub'ha, bali inasihi kutumia sifa ya mutawaa tir kwa zinginezo zilizoduni yake, kufuatana na istilahi zote zilizo andikwa kwenye elimu ya Usuul".

Ama athari tuzipatazo kutoka kwa maswahaba, zisemazo wazi kuwepo kwa Mahdi, ni nyingi sana zina hukumu ya Raf'u (kuinuliwa hadithi bila kutaja baadhi ya wapokezi).

Hakika hadithi alizo zitaja Al-barzanji kwenye kitabu cha Al-isha'ah Liasharaatisaa'a, na Aalusi kwenye Tafsiri yake, na Tirmidhy na Abu Dawud na Ibnu maaja na Alhakim na Abu ya'ali na Tabaraan na Abdur-rrazaaq na Ibn Hanbali, na Muslim, Abu Naiim, na Ibn Asakir, na Bayhaqiy, na Al-khatiib kwenye historia yake na Daruqutniy na Rady aany, na Naiim bin Hamad katika kitabu Alfitan na Ibnu Abu Sh'eiba na Abu Naiim Al-kuufiy, na Al-bazzaz, na Dailamiy na Abdul-Jabbar Al-khul'aniy kwenye Kitabu chake cha historia, na Aljuwainiy na Ibnu Habban na Abu Amru Addamiy kwenye sunani zake, katika yote hayo kuna dalili za kutosha.

Kwa hivyo kuamini kutokea kwa Mahdi ni waajibu, na kuitakidi kudhihiri kwake ni kuzikubali na kuziswadikisha hadithi za Mtume(s.a.w.w) .[80] Na wanazuoni wengi wa kiislamu walifanya haraka kukubali na kukiri fikra ya Mahdi na kuzisahihisha habari zake kwa kutunga vitabu na vijitabu vya kutoa fat'wa na kufutu mas'ala katika maudhui hayo ili vizazi vijavyo viweze kufahamu suala hili na ukweli wake kama ilivyo pokelewa kwenye sheria kupitia kwa Mtume Mtukufu(s.a.w.w) na miongoni mwa waandishi hao wa maudhui haya, tukitaja baadhi kwa mfano, walikuwa ni:

1- Ubad bin Yaaqub al-rawajiniy alie kufa mwaka 250 H. Ana kitabu kiitwacho "Akh'baarul-Mahdi".

2- Abu naiim Al-Isbihaaniy alie fariki mwaka 430h. Ana kitabu kiitwacho "Ar-baina hadithan fi amril-Mahdi"[81] na kitabu "Manaaqibul Mahdi"[82] na kitabu "Na'atul Mahdi".

3- Mohammad bin Yuusuf Al-Kanjy Ashaafiiy aliefariki mwaka 658 H, ana kitabu kiitwacho "al-bayaan fi akh'bari Swahib zzamaan", kimechapishwa.

4- Yuusuf bin yahya Assalmy Ashaafiiy alie fariki mwaka 685 H. Ana kitabu kiitwacho "Uqad-Addurar fi Akh-baaril Mahdiyil Muntadhar".[83]

5- Ibnu Qayyim Al-jauziya aliefariki mwaka 751 H, ana kitabu kiitwacho "Al-Mahdiy".

6- Ibnu hajar Al-haitamy Ashaafii alie fariki mwaka 852 H, ana kitabu kiitwacho "Al-qaulul-mukhtasar fi alaamatil Mahdiy-Almuntadhar".[84]

7-Jalaalu ddin Asuyutwiy alie fariki mwaka 911 H, ana kitabu

"Al-urful-wirdiy fi akhabaril-Mahdy" kimechapishwa na kitabu "Alamaatul-Mahdi"

8- Ibnu Kamaal basha Al-hanafi aliefariki mwaka 940 H, ana kitabu "Tal-khisul bayan fi alaamat Mahdiyyi Aakhiriz -zamaan".[85]

9- Mohammad bin tuuluun Ad-damash-qi alie fariki mwaka 952 H, ana Kitabu "Al-muhdi ila ma-warada fil Mahdi".[86]

10- Aly bin Hussaamud-din Al-mutaqiy Al-hindiy alie fariki mwaka 975H, ana kitabu "al-burhaan fi alaamati mahdiy Aakhiriz-zaman" na kitabu "Talkhiisul-Bayaan fi akhbari Mahdiy Aakhiriz-zaman".[87]

11- Ali Al-qaariy Al-hanafiy aliefariki mwaka 1014 H, ana kitabu "Arrad alaa man hakama wa qadha annal Mahdy jaa'a wa madhwa".

Na kitabu "Al-mashrabul-wirdiy fi akh-baril Mahdy".[88]

12- Mar-ii bin Yusuf Al-Karamiy Al-hanbaliy alie fariki mwaka 1031 H, ana kitabu "Faraidu-fawaidul-fikri fil Imamil-Mahdiyil-Muntadhwar".[89]

13- Al-Qaadhi Muhammad bin Ali Ash-shaukani alie fariki mwaka 1250 H, ana kitabu "Ataudhihu fi tawaturi majaa'a fil Mahdiy Almuntadhar wad-dajaali wal-masiih.[90]

14- Rashid Arrashid Atadhafiy Al-halabiy wa zama hizi ana kitabu "Tanwiir Ar-rijaal fi dhuhuril-Mahdy wa dajjal" kime chapishwa.

Hivyo hivyo washairi walikuwa pamoja na "fikra ya mahdi" na "Mahdi mwenyewe", kwani kaswida zao zilikuwa na madhumuni na maana yaelezayo fikra hiyo na ambao ni wengi, na kaswida zao ni zenye kuelezea kutarajiwa kutokea siku yake, na kukiri kuja kwake kusiko na shaka na miongoni mwa washairi hao kwa mfano na kama ushahidi na sio kuwataja wote ni:

1- Al-Kumeit bin Zaid Al-asadi, aliefariki mwaka 126 H, na kuhusu suala hilo anasema:"Ni wakati gani itasimama haki kwenu na wakati gani atasimama Mahdy wenu wa pili.[91]

2- Ismaa'il bin Muhammad Al-himyari alie fariki mwaka 173H, nae anasema kuhusu hilo"Ni kwamba Bwana wa utawala na mwenye kusimama (na kuleta mabadiliko) ambae nafsi yangu inamuelekea kwa kuimba, anayo ghaiba, ni lazima aghibu. Basi Mwenyezi Mungu amrehemu mwenye kughibu, atakaa kipindi fulani kisha atadhihiri kipindi kingine, na kuujaza uadilifu mashariki yote na magharibi".[92]

3- Da'abal a-Khuza'iy aliefariki mwaka 246 H, anasema kuhusu hilo:"Kutoka kwa Imamu hakuna shaka atatoka. Atasi-mama juu ya jina la Mwenyezi Mungu na baraka zake, na atatu-pambanulia haki na batili na atatoa malipo kwa neema na adhabu.[93]

4- Mihyaar-Ad-daylamy aliefariki mwaka 428 H, anasema kuhusu hilo:"Huenda zama za kesho zikaiponya mioyo ya wenye ghadhabu kutokana na wenye kukufanyia uadui.

Huenda ushindi wa haki ukawa juu ya jambo lisilo wezekana, huenda upungufu ukashindwa na utukufu na ubora kwa kusikia kwangu wito wa huyo mtu wenu atakae simama akiitikiwa na kila mwenye kuomba msaada.

5- Ibnu Muniir Attaraabilsiy aliefariki mwaka 548 H, amese-ma kuhusu hilo kwa njia ya mzaha na utani "Nimewatawalisha watu wa kizazi cha umayya walio safi watukufu na walio barikiwa na ninamkadhibisha mpokezi na ninatia ila kwenye kudhihiri kwa Mahadi".[94]

6- Muhammad bin Twalha Ashaafiy aliefariki mwaka 652 H, anasema: "Na alisema Mtume(s.a.w.w) kauli tuliyo ipokea". Akaendelea hadi kusema "Na hakika alimdhihirisha kwa kueleza nasaba yake na sifa zake na kumuita jina lake, na inatosha kauli yake kuwa "anatokana na mimi" kudhihiri uhai na maisha yake na katika pande la nyama yake ni Zahra ndio mahala pake na sharafu yake watakao sema ni Mahdi hawa kukosea kwa hilo walilo litamka".[95]

7- Ibnu Abil-hadiid Al-Mu'utazilii alie fariki mwaka 656 H, amesema kuhusu hilo: "Hakika nimefahamu ya kuwa ni lazima aje Mahdi wenu, na siku ya kuja kwake ninaitarajia. Atahudu-miwa na vikosi vya jeshi la Mwenyezi Mungu, kama mtu mwenye maumivu amekuja akiwa ni mwenye ushindi na kikisonga mbele kizazi cha Abil-hadidi wa kiwa mashujaa na walio mashuhuri na mikuki iliyo inuliwa juu.[96]

8- Shamsud-din Muhammad bin Tuulun Al-Hanafy Ad-damsh-qiy aliefariki mwaka 953H, anasema kwenye kasida yake akiyataja majina ya Maimamu kumi na wawili:"Na Askari Hassan alietwahirika Muhammadul-Mahdi atadhihiri".[97]

9- Abdullah bin Alawi Al-hadaad Attarimy Ashaafi'i, alie fariki mwaka 1132 H, na kuhusiana na hayo amesema: "Muhammad Al-mahdi ni khalifa wa Mola wetu, Imam wa uongofu na dola lake linasimama kwa uadilifu kana kwamba namuona (siku hizo) akiwa baina ya maqaam na nguzo yake (yaani kati ya nguzo ya kaaba na maqam ya Ibrahim) wakimpa baiya kila upande wenye kumpongeza". Na anasema katika sehemu nyingine: "Na kwetu kuna Imam umefika wakati wa kutoka kwake, atasimama kwa amri ya Mwenyezi Mungu kama ipasavyo, na kuujaza ulimwengu kwa haki na uadilifu na uongofu, kama ulivyo jazwa jeuri kwa dhulma ya watu waovu.[98]

SEHEMU YA PILI

MAHDI NI NANI?

Hakika Uislamu uliipinga rai ya mayahudi ya kuwa "Elia" ndie msuluhishaji mwenye kusubiriwa na pia rai ya wakristo isemayo kuwa yeye ni "Issa mwana wa Maryam".Vilevile hali ya wazi ya matokeo ya nje imeipinga rai ya madhehebu ya kiisaaniya ya kuwa huyo mwenye kusubiriwa ni "Muhammadi bin Alhanafiya" na madhehebu ya "Ismaailiyya, ya kuwa huyo ni "Ismaail bin Jaafar" kwani imethibiti kufariki kwa Muhammad na Ismaili na kubatilika fikra ya kubakia kwao. Basi imebaki tofauti na hitilafu kati ya Ahli sunna na Shia Imamiya katika kumuainisha Mahdi ni nani.

Na muhtasari wa itikadi za Ahli sunna ni kuwa Mahdi atadhihiri zama za mwisho na atasimama kwa upanga na kwamba "Habari zake zimekuwa mutawaatiri (nyingi sana na zingine mustafidhi, kwenye kila tabaka kuna wapokezi wawili au watatu" kwa wingi wa wapokezi wake kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) kuhusu kutokea kwake na kwamba yeye anatokana na kizazi chake Mtume, na kwamba atamiliki au kutawala kwa muda wa miaka saba.

Na kwamba ataijaza ardhi na ulimwengu kwa uadilifu, na kwamba atatoka pamoja na Issa(a.s) na kuwa yeye atawaongoza kwenye sala umma huu na Issa atasali nyuma yake.[99]

Na muhtasari wa itikadi ya Shia Imamiyya ni kuwa atadhi-hiri katika zama za mwisho Mahdi atokanae na nasaba ya Ali na atasimama kwa upanga, na kwamba ataujaza ulimwengu uadilifu na usawa na atatengeneza mazingira yawezeshayo kuutekeleza Uislamu kiukamilifu katika ardhi yote.

Kwa hivyo ni sehemu ipi yenye tofauti kati ya kauli mbili hizi?

Hakika kati yao imefungika kwa upande wa masunni kwenye kauli au kwenye itikadi yao ya kuwa, Mahdi huyu atazaliwa katika zama za mwisho, na hivi sasa hayupo, na haijulikani ni wakati gani atakao zaliwa na baba yake ni nani? Kwa msingi huu aliweza Sunuusiy huko Libia na Abdul-Rahmaan wa huko Sudan na wengineo kudai kuwa wao ni akina Mahdi na kusimama kwa upanga (Silaha).

Ama Shia Imamiyya, wao rai yao ni kuwa Mahdi ni Muhammad bin Hassan bin Ali bin Muhammad bin Ali bin Mussa bin Jaafar bin Muhammad bin Ali bin Hussen bin Ali bin Abi twaalib(a.s) na kwamba yupo kwenye dunia hii lakini watu hawamtambui. Na hii ndio nukta yenye tofauti kati ya pande hizi mbili.

Kutokana na ukweli kuwa mwenye kutoa madai ndio huiti-shwa dalili ya madai yake, kama ilivyo katika fiqhi (sharia) ya kiislamu, basi sisi tutatoa ushahidi ambao wana utegemea Mashia kwenye kuthibitisha yale wanayo yaitakidi, na tutaonyesha usha-hidi mwingine walio utumia kuzibatilisha rai za wapingao fikra hii, ili jambo hili liweze kuonekana na kujulikana wazi kwa kila mwenye macho mawili. Na kutokana na ukweli kuwa mashia kama tulivyo eleza mwanzoni mwa maudhui haya kuwa wana amini kuwa uimamu ni cheo cha kupewa na Mwenyezi Mungu na kina hitajia dalili na uteuzi, wame amini kuwa uimamu wa Mahdi, Muhammad bin Hassan kufuatana na dalili zilizopo na kwa kuzitii dalili hizo, na kufuatana na matamshi yake yaliyo wazi kabisa.

Huenda kukawa na mwenye kuuliza, dalili hizo ni zipi na lafdhi zake ni zipi na ni nani alie zisimulia na kuzipokea?

Ili kulifafanua jawabu la swali hilo ni lazima kuashiria kuwa dalili hizo zimhusuzo Mahdi haikuwa ni habari ( hadithi) moja au mbili, bali ni habari nyingi zilizotoka kwa Mtume(s.a.w.w) na zilizo mutawaatir zilizovuka mamia, na zilipokewa na idadi kubwa ya maswahaba, na zikatolewa na idadi kubwa nyingine ya mahuffa-dhi na wapokezi, na kwa wingi wa istifadha (wapokezi watatu kwenye kila tabaka) tawaatur (wapokezi wengi sana) haikuwa tena ni sahihi kufanya mjadala kuhusu usahihi wa hadithi hizi na kuhusu yakini zinazo tuletea katika kuthibitisha swala hilo. Na kwa ajili ya udadisi zaidi na utafiti wa kimaudhui tunasema:

Hakika hadithi hizi kwa sanadi yake na dalili yake zimegawa-nyika kwenye makundi matatu:

Kundi la kwanza:

Zenye sanadi sahihi na dalili yake ni ya dhahiri zisizo na shaka yoyote, na maimamu wa hadithi na mahufadhi wakubwa walithibitisha juu ya usahihi wake au kuwa ni hassan[100] (nzuri) na kuwa baadhi yake ni sahihi kufuatana na masharti ya mashekh wawili, Bukhari na Muslim.

Na hakuna shaka katika uwajibu wa kuzichukuwa hadithi za kundi hili na kuzifanyia kazi na kuyaamini mambo yanayo zungumziwa na kujulishwa na hadithi hizo.

Kundi la pili:

Ni hadithi zisizo sahihi katika sanadi yake hata kama dalili yake (yaani maneno yake) iko dhahiri. Kanuni zilizo kubaliwa kwenye elimu ya hadithi zinatulazimisha kuzichukua hadithi hizo vilevile, kwa kuungana kwake na kusahihishwa kwake na kundi la kwanza na kwa kuwa mashuhuri ya kuwa wanazuoni wame-zikubali, bali wanazuoni wote wamefanya ijmai kuafikiana juu ya madhumuni yake.

Na kundi la tatu:

Limekusanya sahihi na dhaifu, lakini hadithi hizo zinapi-ngana na hadithi zingine zote ambazo ni mustafidhi na zilizo mutawaatir. Basi kitu cha lazima ni kuziacha, na kujiepusha nazo, ikiwa haikuwezekana kuzifanyia ta'awili, kwa mfano zilizosema kuwa jina la Mahdi ni Ahmad au zilizo sema kuwa jina la baba yake linafanana na jina la baba yake mtume(s.a.w.w) au zisemazo kuwa yeye anatokana na watoto wa Abi Muhammad Hassan Az-Zakiy, kwani habari hizi ni habari chache na nadra ambazo wanazuoni mashuhuri wamejiepusha nazo.[101]

Hadithi za makundi mawili la kwanza na la pili hizo ndizo ambazo tumebainisha kuwa ni wajibu kuzichukuwa zilikuwa zikielekeza kwenye lengo kwa ibara tofauti tofauti na zikikusudia kumtambulisha na kumuainisha kwa matamshi tofauti tofauti na tunaweza kuufupisha muhtasari wake kama ifuatavyo:

Baadhi ya hadithi hizo zimethibitisha kuwa Mahdi anatokana na kabila la kikuraishi. Ametoa Ahmad na Al-manwardi ya kuwa Mtume(s.a.w.w) amesema:

"Pateni bishara ya Mahdi, ni mtu atokae kwenye kabila la kuraishi, atokae kwenye kizazi changu. Atatoka watu watakapo hitilafiana na kuwepo mtetemeko, na kuijaza ardhi kwa uadilifu na usawa kama ilivyo jazwa dhuluma na ujeuri".[102]

Na zingine zimethibitisha, kuwa Mahdi ni katika watoto wa Abdul-Mutwalib.

Ametoa Ibn Maaja kwa sanadi yake kutoka kwa Anas bin Maalik, amesema: Nilimsikia Mtume(s.a.w.w) akisema:

"Sisi watoto wa Abdul-Mutwalib ni mabwana wa watu wa peponi, Mimi na Hamza na Ali na Ja'afar na Hassan na Hussen na Mahdi".[103]

Na zingine zimethibitisha kuwa yeye ni katika Aalu Muhammad (Kizazi cha Mtume,(s.a.w.w) . Amesema Mtume(s.a.w.w) :

"Atatoka katika Zama za mwisho mtu atokanae na kizazi changu, jina lake ni kama jina langu, na kuniya yake ni kama yangu (jina la ubaba kwa mfano baba ya fulani) ataijaza ardhi kwa uadilifu kama ilivyo jazwa ujeuri, na huyo ndie M ahdi". Na hii ni hadithi mashuhuri.[104]

Na zingine zimethibitisha kuwa ni katika kizazi chake. Ametoa Abu Daud kwa Sanadi yake kutoka kwa Ummu Salama (Mungu amuwie radhi) amesema:"Nilimsikia Mtume(s.a.w.w) akisema:

"Madhi anatoka katika kizazi changu ".[105]

Na zingine zimethibitisha kuwa yeye ni katika Ahlul bayti. Amesema Mtume(s.a.w.w) :

"Lau kama isingebakia isipokuwa siku moja Mwenyezi Mungu angetuma mtu atokanae na Ahlul-bayti wangu aujaze ulimwengu uadilifu kama ulivyo jazwa ujeuri .[106]

Na zingine zimethibitisha kuwa, anatokana na watoto wa Ali(a.s) , kutoka kwa Said bin Jubair kutoka kwa Ibnu Abbas (Mungu awawie radhi) amesema: "Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu:

"Hakika Ali (a.s) ni wasii wangu na katika kizazi chake atatoka huyo mwenye kusimama (dhidi ya dhulma) na mwenye kusubiriwa (almuntadhar), ambae ni Mahdi atakae ijaza ardhi usawa na uadilifu kama ulvyo jazwa ujeuri na dhulma ".[107]

Na zingine zimethibitisha kuwa ni katika watoto wa Fatima.

Ametoa Muslim na Abu daud na Nasai na Ibnu Maaja na Bayhaqiy na wengine:

"Mahdi ni katika kizazi changu ni katika watoto wa Fatuma ".[108]

Na wengine wamethibitisha kuwa ni katika watoto wa Hussen, Amesema Mtume(s.a.w.w) :

"Haitaondoka dunia mpaka ausimamie umma wangu mtu atokanae na kizazi cha Hussen, aijaze ardhi kwa uadilifu kama ilivyo jazwa dhulma ".[109]

Na zingine zimethibitisha kuwa ni wa tisa katika kizazi cha Hussen. Kutoka kwa Salmani Al-faarisi (Mungu amuwie radhi) amesema:"Niliingia nyumbani kwa Mtume(s.a.w.w) mara nika-muona Hussen akiwa mapajani mwake akilibusu shavu lake na kuulamba mdomo wake na akisema:

"Wewe ni Sayyid mtoto wa Sayyid, nduguye Sayyid, na wewe ni Imam Mtoto wa Imam na ndugu wa Imamu, na wewe ni Hujja mtoto wa Hujja ndugu wa Hujja baba wa Mahujja tisa, wa tisa wao ni yule atakae simama (dhidi ya dhulma) ambae ni Mahdi.[110]

Na zingine zilithibitisha kuwa yeye ni wasii wa kumi na mbili. Na Imamu wa kumi na mbili na khalifa wa kumi na mbili.

"Hakika wasii wangu ni Ali bin Abi twalib na baada yake ni wajukuu wangu wawili Hassan na Hussen watafuatiwa na maimamu tisa watokao kwenye uti wa mgongo wa Hussen(a.s) , akasema:"Ewe Muhammad nitajie majina yao". Akasema: "Aki-ondoka Hussen ni mwanae Ali akiondoka Ali ni mwanae Muhammad, akiondoka Muhammad ni mwanae Jaafar, akiondo-ka Jaafar ni mwanae Mussa, akiondoka Mussa ni mwanae Ali, akiondoka Ali ni mwanae Muhammad, akiondoka Muhammad ni mwanae Ali akiondoka Ali ni mwanae Hassan, akiondoka Hassan ni mwanae Alhujja Muhammad Al-mahdi hawa ndio maimamu kumi na mbili".

Yahya binil Hassan ametaja kwenye kitabu Al-umda kupitia njia ishirini za upokezi ya kwamba makhalifa baada ya Mtume(s.a.w.w) ni kumi na mbili na wote wanatokana na kabila la kikuraishi, katika Bukhari kupitia njia tatu za wapokezi, na katika Muslim kupitia njia tisa na kwa Abi Daud kupitia njia tatu, na katika Tirmidhi kupitia njia moja na katika Al-hamiidi kupitia njia tatu".[111]

Na zingine zimethibitisha kuwa ni mtoto wa Hassan Al-askari.

Katika manaaqib kutoka kwa Jaabir bin Abdillahi al-answary kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) :

"Basi baada yake ni mwanae Hassan aitwae Al-askari, na baada yake ni mwanae Muhammad aitwae Mahdi na mwenye kusimama kwa haki (Al-Qaaim) na Al-hujja, atatoweka na kutoonekana kisha atatokea, na atakapotokea ataijaza ardhi usawa na uadilifu kama ulivyo jazwa ujeuri na dhuluma .[112]

Na hivyo hivyo tunakuta kuwa hadithi hizi kwa wingi huu na tofauti zake zimemuelezea Mahdi wa umma huu, na kusema kuwa ni mtoto wa Hassan Al-askari, nayo ni matokeo au natija thabiti ambayo haina kasoro ndani yake.

Na msomaji ili awe na ujuzi zaidi wa jambo hili tunatoa katika sehemu ifuatayo majina ya wapokezi wa hadithi za Mahdi zilizotajwa hapo kabla na hasa majina ya maswahaba, kwani utafiti wetu huu wa haraka hauna nafasi kubwa ya kuweza kuandika majina ya wapokezi wote kutoka kwenye matabaka mengine:

01- Abu Amama al-baahily

02- Abu Ayyub

03- Abu Said Al khudri.

04- Abu Sulaiman-mchungaji mifugo wa Mtume(s.a.w.w)

05- Abu tufail.

06- Abu Huraira.

07- Ummu Habiba mama wa waumini.

08- Ummu Salama mama wa waumini

09- Anas bin Maaliki.

10- Thubaan-mtumwa wa Mtume (s.a.w.w).

11- Jaabir bin Samrah.

12- Jaabir bin Abdillahi al-Answari.

13- Hudhaifa binil Yamaan.

14- Salman Al-faarisi.

15- Shahr bin Hawhab.

16- Twalha bin Ubaidullah.

17- Aisha mama wa waumini.

18- Abdur-rahmaan bin Auf

19- Abdallah bin Haarith bin Hamzah.

20- Abdallah bin Abbas.

21- Abdallah bin Omar.

22- Abdallah bin Amrubinil Asi.

23- Abdallah bin Masoud.

24- Othmani bin Affan.

25- Ali bin Abitwalib.

26- Ali Alhilaali.

27- Ammar bin Yaasir.

28- Umraan bin Haswiin.

29- Auf bin Maalik.

30- Qurrat bin Iyaas.

31- Mujmau bin Jariyah Al-answari.[113]

Ama ambao walitoa hadithi kuhusu Mahdi kati ya mahufadhi wa hadithi na wenye vitabu vya sahihi na sunanu, ni shekh Abdul-Muhsin Alubad aliwahesabu na kufikia "38" ambao ni mashuhuri na walio wema[114] , na miongoni mwao ni:

01- Abu Daud katika Sunani yake.

02- At-tirmidhi kwenye kitabu chake kiitwacho "Jami'u".

03- Ibnu Maaja kwenye Sunani yake.

04- An-nasai kwenye kitabu chake Alkubra.

05- Ahmad kwenye Musnadi wake.

06- Ibnu Habban kwenye Swahihi yake.

07- Al-haakim kwenye Mustadrak.

08- Abubakar bin Abi Shaiba kwenye "Al-munswif".

09- Naim bin Hamad kwenye Kitabu Al-fitani.

10- Abu Naiim kwenye kitabu "Al-Mahdi wal-hilyah".

11- At-twabaraniy kwenye kitabu "Al-kabiir wal-awsat wa As-swaghiir.

12- Ad-daru-qutni kwenye kitabu "Al-ifrad".

13- Al-baarudy kwenye kitabu "Ma'arifat As-swahaba".

14-Abu Ya'ala al-muuswiliy kwenye Musnad yake.

15- Al-bazzar kwenye Musnad yake.

16- Al-haarith bin Abi Usamah kwenye Musnad yake.

17- Al-khatib kwenye kitabu chake"At-talkhisul-mutashabih" na katika "Almut- tafaq wal-muftaraq".

18- Ibnu Asakir kwenye kitabu cha historia.

19- Ibnu Mundih kwenye kitabu chake cha historia "Taarikh Isbahan".

20- Abul-hassan Al-harbiy kwenye kitabu chake "Al-awwal minal-harbiyaati".

21- Tamam Ar-raziy kwenye "Fawaid".

22- Ibnu Jariri kwenye "Tahdhibul-Athar".

23- Abubakari bin Al-muqri kwenye "Mu'ujam" wake.

24- Abu Amru Addani kwenye Sunani yake.

25- Abu Gharam Al-kuufiy kwenye kitabu chake "Al-fitani".

26- Ad-daylamiy kwenye kitabu chake "Musnadul-fir dausi".

27- Abu Bakar Al-Iskaf kwenye "Fawaidul Akhbaar".

28- Abul-Hussen binil Munawiy kwenye kitabu chake "Al- malaahim".

29- Albaihaqi kwenye "Dalailu An-nubuwah".

30- Abu-Amru Al-muqri, kwenye Sunani yake.

31- Ibnul Jawzi kwenye kitabu chake cha Historia.

32-Yahya Al-hamaniy kwenye Musnad wake.

33- Ar-ruyaaniy kwenye musnad wake.

34- Ibnu Sa'ad kwenye "Twabaqaat".

Imam (Rehma za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) alizaliwa kwenye mji wa Samarra wakati wa Al-fajiri tarehe kumi na tano ya mwezi wa Sha'aban mwaka 255H.[115] na baba yake akamuita Muhammad, na huo ulikuwa ni uthibitisho wa hadithi ya Mtume(s.a.w.w) iliyo maarufu isemayo "Jina lake ni sawa na jina langu"[116] na Kuniyah yake (Jina lake la ubaba) akumuita Abul-Qaasim.[117]

Na wapokezi wa riwaya wa Shia Imamiyya walisalim amri juu ya ukweli huu na wengine wengi wa makundi mengine ya kiislamu. Lakini baadhi ya waislamu pamoja na kuikubali kwao fikra ya kuja mahdi walimkataa Mahdi kwa hoja ya kuwa hakuna mtoto wa Askari, na wakatoa dalili nne kuthibitisha hoja hiyo, na tutazielezea kwa ufupi, kama ifuatavyo:

1- Walisema kuwa Askari alipo karibia kufa alimuweka mama yake (Umul-Hassan) kuwa ndie muusiwa wake wa kuya-angalia yote aliyo kuwa akiyasimamia kama vitu vya wakfu na sadaka na mambo mbali mbali mengine, kama angekuwa na mtoto asingemuacha kumuusia na kumuusia mtu mwingine.

2- Ni kuwa Jaafar bin Ali ami yake Mahdi alipinga kuwepo mtoto wa kaka yake, na ushahidi wa baba mdogo kwenye jambo kama hili ni wenye umuhimu mkubwa.

3- Hakika mashia wanadai kuwa Askari alificha suala la mwanae kwa watu wasio maalumu na wasio wa karibu, kwa nini alifanya hivyo pamoja na kuwa maswahaba wake walikuwa ni wengi katika siku hizo huku wakiwa na nguvu, mali na uwezo wakati ambapo maimamu walio tangulia kwenye zama za utawala wa bani umaya na bani Abbas walikuwa kwenye hali ngumu zaidi na wali banwa zaidi, pamoja na hayo hawakuficha suala la watoto wao kama ufichaji huu.

4- Hakika vitabu vya historia havikumfahamu na kumuelezea mtoto wa Hassan Al-Askari wala havikusimulia habari yake yoyote. Na kwa dalili hizi nne wakapinga wapingaji kuzaliwa kwa Imam Muhammad binil-Hassan.

Tutatowa sehemu ifuatayo kwa ufupi jawabu la dalili hizi ili jambo hili liweze kuwa wazi na iweze haki kudhihiri, na kwa hivyo tunasema:

Ama jawabu la dalili ya kwanza ni kuwa:

Hakika kumuusia mama haifai kuwa ni dalili ya kupinga kuwepo kwa mtoto, na lengo la Imam kutoa usia huo ni kuwafa-nya watu wasimuelekee na kutaka kujua habari za mwanawe na watu kutojishughulisha nae na mazingira kugubikwa na suala lake na kuwajulisha maadui zake kutokuwepo mwanae, bali aliwazidishia dhana hiyo kwa kuwafanya kuwa mashahidi wa Usia huo watu wengi katika wakubwa wa serikali ya wakati huo juu ya usia huu.[118]

Na Imam alikuwa kwenye matendo yake hayo akifuata mfumo wa babu yake Jaafar bin Muhammad As-swadiq(a.s) pale alipojiwekea wausiwa watano baada ya kufariki kwake nao ni Al-mansuril Abbasi na Arrabi'u na Kadhi wa madina ukiongezea mkewe Hamidah, na mwanae Mussa bin Jaafar(a.s) na lengo lake kwa kufanya hivyo ni kuyaweka mbali macho ya watawala na maadui yasimuelekee mwanae Mussa[119] , kwa sababu lau kama angemuusia yeye peke yake, bani Abbasi wangeweza kufanya jambo lolote lingine tangu siku ya kufariki baba yake, na Mansur alipofikiwa na habari za kufariki Imamu Swadiq(a.s) alimuandi-kia gavana wake wa Madina, akimuamuru azidi kumbana wasii wa Jaafar bin Muhammad, yule gavana akamuandikia Mansuur, baada ya kufanya uchunguzi, akimfahamisha kuwa walio usiwa ni watu watano na kuwa wa mwanzo wao na ambae ni muhimu ni khalifa mwenyewe. Na kwa kufanya hivyo ilikuwa ni kumuepu-shia Imamu Mussa bina Jaafar(a.s) maudhi.

Ama jawabu la dalili ya pili ni kuwa:

Hakika Jaafar ni katika watu wa kawaida, na inawezekana kwake kufanya mambo kama wafanyavyo watu wengine wa kawaida kama kukosea na kuasi na kutoa madai ya batili, na inatosha akawa kama mfano wa Kaabiil, pindi alipomuua ndugu-ye au mfano wa watoto wa Yaakub walipomtumbukiza ndugu yao kwenye kisima na wakamuudhi baba yao na kuapa viapo vya uongo ya kuwa ndugu yao ameliwa na mbwa mwitu.

Na Jaafar alidhania, nae akifahamu kufichwa suala la mtoto wa kaka yake kwa watu wasio maalumu kati ya maswahaba wa baba yake, ya kuwa atakuwa Imamu kwa kupinga kule, na kwa-mba mali za kisheria zitakusanywa kwake kutoka kila pembe na kila upande, lakini Irada ya Mwenyezi Mungu ndio yenye kushi-nda, kwani ni haraka sana ulidhihiri uongo na ubaya wa suala lake, kisha akajuta kwa yale aliyoyafanya na akatubia kutokana na uovu alio ufanya hadi kuwa mashuhuri kwa jina la " Ja'afar Attawaab". (Mwenye kutubia)

Na si jambo la ajabu baba mdogo kusimama kidete dhidi ya mtoto wa nduguye. Hapo zamani Abu Lahab na Abbas walikuwa ni viongozi wa kikundi cha maadui dhidi ya mtoto wa ndugu yao, Muhammad(s.a.w.w) kwani walipinga utume wake na kumuhusisha na uchawi na wendawazimu na kuyaongoza majeshi kumpiga vita na wakaweka mipango na mikakati ya kumua.

Ama jawabu la dalili ya tatu ni kuwa:

Hakika jambo lililo mfanya Imamu Askari kuficha suala la mwanae ni kutokana na kufahamika na kuwa mashuhuri ya kuwa Imam atasimama kwa upanga ili kuondoa dola la batili na kusi-mamisha dola la haki, kwa hivyo watawala walikuwa wakimu-ogopa mwana mapinduzi huyo na wakijiandaa na kuandaa mipango ya kumuua kwa aina yoyote ile, lau wangefahamu suala lake na kujua habari zake. Kutokana na hali hii akalazimika Imam Askari kuficha na kutozisema habari za mwanae na kuzihi-fadhi habari zake kwa siri kwa maswahaba wake maalumu. Na jambo linaloweka wazi na kuyaunga mkono maneno haya ni kuwa serikali tawala za wakati huo waliharakisha kuwatuma wapelelezi wao wakati wa kufariki Imam Askari kwenye nyumba yake ili wamkamate mtoto yoyote atakae kuwa ndani ya nyumba hiyo.[120] Lau kama si utashi wa Mwenyezi Mungu ambao ulimfanyia wepesi Muhammad bin Hassan kukimbia na kujificha, wange-muua.

Na Imamu Askari katika ufichaji huu alikuwa na kigezo cha mama yake Mussa bin Imran alipo shushiwa wahyi kuwa ni lazima kumficha na kufanya siri kuhusu suala la Nabii Mussa kwa kumkhofia Fir'auni wa zama zake kama Qur'an tukufu ilivyoelezea kuhusu swala hilo.

Ama maimamu walio tangulia ilikuwa si lazima kwao kusimama kwa upanga, bali suala hilo liliachiwa kulingana na mazingira na mambo ya zama hizo na kufanya kulingana na mahitajio ya kila zama na mazingira yake kwa kujua ni hukumu gani au taklifu ipi inatakiwa, kwa hivyo walikuwa na amani kiasi na uhuru kwa kiwango fulani, hata kama haikuwa ni amani na uhuru kwa maana yake sahihi.

Ama jawabu la dalili ya nne ni kuwa:

Hakika kujulikana utoto au mtoto huyu kuwa ni wa huyu huthibitika katika sheria, kwa kauli ya mkunga au wanawake ambao huwepo kwenye uzazi ule (yaani mama yule anapo jifungua) na kwa kukubali mwenye kitanda (baba mzazi) na kushuhudia wanaume wawili walio waislam juu ya kukiri na kumkubali baba mtoto wake. Na pande hizi tatu zilithibitika na kupatikana kwenye uzazi ule.

Kwa mfano, Sayyida Hakimah binti wa Imam Jawaad(a.s) ndie ambae alisimamia jambo hilo la uzazi na akashuhudia uzazi huo. Na Imam Askari ndie baba na alikubali kuzaliwa kwa mtoto huyo mbele ya maswahaba wake maalumu.[121]

Na waislamu wa zama hadi zama zinginezo zilizo fuatia, wanasimulia habari hizo na wanashuhudia juu ya usahihi wake. Na miongoni mwa waliopokea na kusimulia uzazi huu, ukiongezea juu ya kukubaliana mashia Imamiyya wote juu ya suala hili kati ya wanazuoni wa kiislamu, kuna idadi isiyo chache ya wana historia na waandishi, kwa mfano kuna hawa wafuatao:

01-Muhammad bin Twalha Ashaafii,aliefariki mwaka 652 H.[122]

02- Sibti ibn Jawziy, aliefariki mwaka 554 H.[123]

03- Al-kanji Ashaafi'i , aliefariki mwaka 658 H.[124]

04- Ibnu Khalakaan Ashafi'i, aliefariki mwaka 681 H.[125]

05- Swalahud-dini As-swafadi aliefariki mwaka 764 H.[126]

06- Ibnu Hajar Al-haytami Ashaafi'i aliefariki mwaka 852 H.[127]

07- Ibnu Swabbagh Al-maaliki, aliefariki mwaka 855 H.[128]

08- Ibnu Tuuluum Ad-damashqi, aliefariki mwaka 953[129]

09- Al-Hussen bin Abdallah Assamar qandi, aliefariki mwaka 1043.[130]

10-Mohammad As-swaban Ashaafi'i, aliefariki mwaka 1206.[131]

11- Sulaimani Al-kanduzi'ii, Al-hanafiy aliefariki mwaka 129 H.[132]

12- Mohammad Amin As-suwaydi aliefariki mwaka 1246 H.[133]

13- Mu'umin Ashablanji Ashaafi'i, aliefariki katika karne ya 14 H.[134]