2
MAISHA YA ABU DHARR
Abu Dharr anasema, "Ali alinipeleka hadi ndani ya nyumba. Niliona nuru katika umbo la mtu inaonekana hapo. Mara tu nilipo muona, nilivutiwa kwake na nikahisi ninataka kubusu miguu yake. Kwa hiyo, nilimsalimia Assalamu Alaykum." (Alikuwa mtu wa kwanza kumsalimia Mtume wa Uislamu kwa desturi ya Kiislamu, kabla ya kusilimu).
Alijibu salamu, akasema, "Waa Aliakum as Salam, wa rahmatullah
wa Barakatuh. Ndio Unataka nini?"
Nilijibu; "Nimekuja kuwako kwa moyo na imani."
Alinielekeza mambo fulani muhimu na akanitaka nikariri Kalimah
(Shahada) yaani (La ilaha illalah Muhammadun Rasulul lah) nilisoma
hivyo, na kwa hiyo nikaingia kwenye Uislamu.
Baada ya hapo, aliondoka kwenda Ka'abah. Alipofika hapo alipoona kundi kubwa la makafiri wa kabila la Quraishi, alisema kwa sauti kubwa, "Sikilizeni enyi Waquraishi nina shahidilia kwamba Mwenyezi Mungu ni Mmoja na Muhammad ni Mtume Wake."
Sauti hii iliwaogofya Quraishi na kuvunja sanamu lao la Lat na Uzza. Hisia za Quraishi kwamba heshima ya masanamu yao imeshushwa iliwatia wasiwasi sana.
Hatimaye watu walimzunguka Abu Dharr wakaanza kumpiga sana hadi akazirai. Ilibakia kidogo afe lakini Abbas bin Abd al-Mutalib alifika hapo ghafla. Alipoona kwamba mfuasi wa Muhammad alikaribia kufa, alilazimika kumlalia Abu Dharr.
Akasema: "Enyi watu! Nini kimewatokea ninyi? Munataka kumuua mtu mkubwa wa kabila la Bani Ghifar. Mmesahau kwamba nyinyi hufanya biashara na Bani Ghifar na huwa mnatembelea huko mara kwa mara. Hamliogopi kabila lake kabisa!"
Baada ya kusikia hayo, watu hao waliondoka hapo na Abu Dharr ambaye alikuwa anatoka damu, alinyanyuka na kwenda kwenye kisima cha zam zam.
Alihisi kiu sana kwa sababu ya majeraha makubwa na kutoka damu nyingi. kwa hiyo, kwanza alikunywa maji halafu akasafisha mwili
wake. Baada ya hapo alikwenda kwa Mtukufu Mtume huku akigumia. Mara tu Mtume alipomuona katika hali ile, alisikitika sana na akasema, "Abu Dharr! Umekula au kunywa chochote?"
Abu Dharr: "Bwana wangu! Nimeona nafuu kidogo baada ya kunywa
maji ya Zam zam."
Mtume: "Bila shaka maji hayo hutoa nafuu."
Baada ya hapo alimliwaza Abu Dharr na akampa chakula. Ingawa
Abu Dharr aliumia sana kwa sababu ya hotuba yake, bado hamasa ya
dini haikumruhusu aondoke kwenda kwao kimya kimya. Imani yake
ilimtaka awafanye Maquraishii waamini kwamba akili ya
mwanadamu hudharau ushirikina wa uchaji masanamu.
Aliondoka hapo akaenda kwenye eneo la Al-Ka'abah tena. Alisimama sehemu iliyoinuka na akaita kwa sauti ya ushupavu imara. "Enyi watu wa Quraishii! Nisikilizeni! Ninashahidilia kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu na ninashahidilia kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu."
Waliposikia hivyo wale wapotovu ambao waliona misingi ya miungu yao inatikiswa na ambao walikasirishwa sana na hotuba yake ya mwanzo, kwa mara nyingine waligutushwa na wakawa katika hali ya wasiwasi na wakageuka kuelekea upande inakotoka sauti na haraka sana walikusanyika na kumzunguka yeye. Walikuwa wanapiga kelele "Muueni huyu Ghifari haraka iwezekanavyo kwani yeye nia yake ni kuwatukana miungu wetu."
Mkusanyiko wote ulisema kwa sauti moja, Mueni Abu Dharr." Kwa hiyo walimpiga Abu Dharr hadi akazirai.
Abbas bin Abdul Muttalib alipoona hivi alijitokeza mbele na kumlalia Abu Dharr kama ilivyofanya jana yake, na akasema; "Enyi Quraishi!
Nini kimewatokeeni kwamba mnamuua mtu wa kabila la Ghifari ingawa mnao uhusiano mzuri na kabila lake na biashara yenu inaendelea vizuri kwa msaada wa kabila lake. Msiendelee kumpiga."
Baada ya kusikia haya, watu wote waliondoka na kumwacha Abu Dharr akiwa amepoteza fahamu. Alipopata fahamu, alikwenda kwenye kisima cha Zam zam! na baada ya kunywa maji alisafisha mwili wake uliokuwa umetapakaa damu.
Abdullah Subaiti ameandika kwamba ingawa Abu Dharr aliteseka sana kwa majeraha lakini hata hivyo aliwalazimisha Quraishi kuwa na maoni kwa mujibu wa ho tuba zake kwamba Uislamu ulikwisha enea kwa watu na uliwavutia sana.
Kwa ufupi Abu Dharr alinyanyuka kutoka kwenye kisima cha Zamzam na kwenda kwa Mtukufu Mtume. Mtume alipomuona Abu Dharr katika hali hiyo alisema, "Ewe Abu Dharr! Ulikwenda wapi na kwa nini umekuwa katika hali hii?" Abu Dharr alijibu, "Nilekwenda kwenye Ka'abah tena. Nilitoa ho tuba tena na nikatapakaa damu kwa kipigo. Sasa nimekuja kwako baada ya kuoga maji ya Zam zam." Mtume akasema; "Ewe Abu Dharr! Sasa ninakuamuru urudi nchini kwako mara moja. Nisikilize! Utakapofika nyumbani kwako, mjomba wako tayari atakuwa amekufa. Kwani hana mrithi mwingine isipokuwa wewe, wewe utakuwa mrithi wake na kuwa mmiliki wa rasilimali yake. Nenda ukatumie mali hiyo kwa kutangaza Uislamu. Baada ya muda mfupi nitakwenda na kuhamia Madina mji wa mitende. Wewe endelea kufanya kazi huko hadi nitakapohamia huko." Abu Dharr alisema, "Ndio! Bwana wangu vyema sana. Nitaondoka hivi karibuni na kuendelea kutangaza Uislamu." Sahih Bukhari, Sura ya Uislamu na Abu Dharr, chapa ya Misri, 1312 Hijiriya.
SURA YA TATU
Baada ya kuingia kwenye Uislamu, Abu Dharr aliondoka Makkah kwenda nchini kwake. Abdullah Subaiti ameandika kwamba Abu Dharr alipoondoka, alikuwa anabubujika imani, kamili, na alikuwa na furaha sana. Alifurahia sana kwamba Mwenyezi Mungu, alimwongoza kwenye imani ambayo imekubaliwa na waliotakasika na dhamira imeridhika nayo na akili inakaribisha kwa ukamilifu.
Aliendelea na safari hadi nchini kwake. Mtu wa kwanza kumsalimia alikuwa kaka yake Unais na pia alikuwa mtu wa kwanza kupata mwamko wa imani yake. Unais alikwenda kubusu miguu ya kaka yake na kusema, "Ewe ndugu yangu! Umepitisha siku nyingi sana Makkah sasa niambie ulichopata huko."
Abu Dharr alisema, "Unais! Nimefanya uamuzi wenye busara. Niliamua baada ya kutafakari sana kwamba lazima nikubali imani ya Muhammad! Ewe Unais! siwezi kukuambia kwamba nilipokutana na Muhammad na kumtazama uso wake, nilihisi kama vile kifua changu kilikuwa kinaongezeka. Moyo wangu ulijaa furaha na akili yangu ililewa imani. Mara nikakariri kalimah-shahada na kukubali Utume wake nilimwomba alifundishe vipengele vya imani. Kwa hiyo alinieleza kanuni za Uislamu. Ewe Unais ninakuomba kwa kweli na kwa moyo safi na nia njema uinamishe kichwa chako kwa unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu na uache kuabudu miungu hii iliyotengenezwa na mikono ya watu yenye asili ya mawe."
Aliposikia hivi, Unais alikaa chini huku akiwa ameinamisha kichwa chake na kuanza kufikiri. Alipatwa na hali kama vile umelewa. Unais alikumbuka mambo hayo yote aliyo yaona huko Makkah. Baada ya muda fulani alisema, "Ewe Ndugu! Akili yangu imethibitisha ukweli
wako na mantiki yangu inanieleza nikutii wewe. kwa hiyo sikiliza! Ninashahidilia kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu na ninakiri kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu."
Abu Dharr alifurahi sana kuona Unais anaikubali imani. Alimwambia: "Sasa twende kwa mama yetu." Wote wawili walikwenda kwa mama yao. Baada ya kumuamkia mama yao, Abu Dharr akasema, "Mama yangu mpendwa! Nakuomba unisamehe! Nimekuwa mbali na wewe kwa kipindi kirefu sana. Lakini, nimepata kitu cha nadra ambacho hakuna mtu aliye nacho hapa."
Mama Akamuuliza, "Kitu hicho ni kipi ambacho kinakubainisha wewe?" Abu Dharr alisema, "Hii ni tunu ya imani mama. Nilikutana na mtu huko Makkah ambaye uso wake uling'aa nuru ya uadilifu, hana wa kumlinganisha kwa uzuri wa tabia yake na ukarimu wake. "Yeye husema kweli tupu. Yeye husema kilicho sahihi. Hutenda haki. Maneno yake yanayo busara. Mama! Maadui zake pia humwita mkweli na mwaminifu. Huwaita watu wamwelekee Mwenyezi Mungu ambaye ni muumba wa mbinguni na ardhi na mpangiliaji wa kuweza kudumu kwa ulimwengu huu.
"Nimekubali kumuamini mtu huyu kwa kuvutiwa na mwelekeo wake, maneno yake na semi zake, na Unais pia amekuwa Muislamu. Tumekubali Upweke wa Mwenyezi Mungu na Utume wa Muhammad."
Mama yake Abu Dharr akasema: "Mwanangu, endapo ndio hivyo, mimi pia nina shahidilia kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, na kukiri kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu."
Abu Dharr alitiwa moyo baada ya kaka yake na mama yake kuingia kwenye Uislamu na sasa alianza kutafakari jinsi ya kuwashawishi
watu wa kabila lake na kuwavuta waelekee kwenye njia iliyonyooka. Baada ya kufikiri sana Abu Dharr alitoka nje ya nyumba yake. Mama na kaka yake pia walikuwa naye. Baada ya kusafiri mwendo mfupi walipiga hema lao karibu na mahema ya watu wa kabila lao.
Usiku uliingia. Wasafiri hawa waliochoka walikuwa wamelala kwenye mahema yao walipohisi kwamba watu wengi wa kabila hilo waliokuwa pale walikuwa wanasimuliana hadithi wao kwa wao na kuelezea matukio mbali mbali. Walikuwa katika mazungumzo mfululizo.
Abu Dharr alipojaribu kusikiliza kwa siri walikuwa wanasema nini, alisikia kwamba walikuwa wanamsema yeye. Baada ya hapo watu waliondoka kutoka kwenye mahema yao na kwenda kwenye hema la Abu Dharr, akamwambia kaka yake, Unais, "Watu wa kabila letu wamekuja karibu na hema letu. Nenda nje ukawaone."
Unais alitoka nje mara moja. Aliwaona vijana wa kabila hilo walikuwa karibu na hema. Walikwenda karibu na hema ili wajue endapo Unais na Abu Dharr walikuwa hapo. Walimsalimia. Baada ya Unais kujibu salamu yao, aliwauliza sababu ya wao kutembelea hapo. Wakasema, "Tumekuja tu kukuona wewe na Abu Dharr."
Unais alirudi ndani na akamwambia Abu Dharr, "Vijana wa kabila letu wamekuja kutaka kujua hali ya safari."
Abu Dharr alisema, "Waambie waingie ndani. Nitazungumza nao. Inawezekana labda nikawasilimisha waanze kumuabudu Mwenyezi Mungu, Aliye Pekee."
Unais alitoka nje na akawaambia, "Ingieni ndani kwani kaka Abu Dharr anawaiteni."
Wote walikwenda kwa Abu Dharr. Mmojawao akasema, "Ewe Abu Dharr! Hatujakuona kwa kipindi kirefu na matokeo yake ni kwamba tunasikitika sana."
Abu Dharr akasema, "Wapendwa wangu vijana! Moyo wangu unayo mapenzi makubwa sana kwenu, na ninawahurumieni."
Mtu mmoja: "Abu Dharr! Ulikuwa wapi kwa muda mrefu hivi? Tumeshindwa kukuona kwa kipindi kirefu."
Abu Dharr: "Nilikwenda Makkah. Nilirudi siku chache zilizopita." Mtu wa pili: "Tunafurahi kwamba ulikwenda Makkah."
Abu Dharr: "Kama mambo yalivyo, nilikwenda Makkah, lakini sikutoa sadaka kwa Hubal wala sikuwasujudia Lat na Uzza. Vijana wangu! Kwa nini nifanye yote haya ambapo ninafahamu kwamba masanamu haya wala hayana uhai, ama kuweza kuumiza au kumnufaisha yeyote? Wala hayawezi kuona ama kusikia, ama kuzuia janga linaloweza kuwapata.
"Sikilizeni! Mimi nimekimbilia kwa Mwenyezi Mungu katika matendo yangu na mambo yangu yote. hakika Yeye ni Peke yake, hana mfano wala mshirika, na ninakiri kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni Yeye peke yake anapaswa kuabudiwa, Yeye ni Muumbaji wa kila kitu na mwezeshaji wa kila kiumbe.
Ninawaomba njooni kwangu tuwe pamoja katika mpango wetu wa utekelezaji na mshahidilie Upweke wa Mwenyezi Mungu kama sisi" Waliposikia hivi, watu wote walianza kutetemeka. Mmoja wao
alisema kwa mshangao, "Ewe Abu Dharr! Unasema nini?" Abu Dharr: "Sikilizeni kwa yale ninayowaambieni ingawa siwezi kumuona Mwenyezi Mungu kwa macho yangu bado ninaweza kumuona Yeye kwa jicho langu la kiroho na sikilizeni! Inawezekanaje kitu chochote kinachotengenezwa na mikono ya mwanadamu kiwe na thamani ya kuabudiwa na binadamu? Si busara kuabudu masanamu yaliyotengenezwa kwa mawe na miti, na kuyaomba ili yatutimizie haja zetu.
"Watu wa kabila langu! mnajua kwamba masanamu haya hayana uwezo wowote. Wala hayawezi kuzuia uovu, ama kuwa na nguvu ya kupata manufaa?"
Baada ya kusikia ushawishi huu wa Abu Dharr, watu walianza kunong'onezana wao kwa wao.
Mmoja wao alisema; "Nimekwisha waambieni kwamba huko Makkah, mtu amejitokeza, anajiita yeye ni Mtume na anawaita watu kumwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja. Abu Dharr amekutana na mtu huyu, na mahubiri ya mtu huyu yamesisimua sana hivyo kwamba fikra zozote anazozitoa Abu Dharr ni za mtu huyo."
Mtu mwingine akasema; "Hali ni mbaya sana. Sasa tupo hatarini ambayo inatujia kupitia kwa Abu Dharr na mahubiri yake. Tunadhani kwamba endapo ataendelea kuhubiri namna hii, tofauti zitajitokeza kwenye kabila letu na maisha yetu yataharibika. Ni vema twende kwa mtemi wetu Khafaf, tumwelekeze hatari zote zinazoweza kujitokeza, na tumsisitizie na alipatie jambo hili kipaumbele ili tuweze kukabiliana nalo."
Vijana wa kabila la Ghifari waliondoka nyumbani kwa Abu Dharr na walikwenda kumwona Khafaf. Wakati wapo njiani walibadilishana
mawazo wao kwa wao. Mmoja wao alisema, "Abu Dharr ameanzisha ghasia kubwa."
Mwingine akasema, "Itakuwa aibu kubwa sana kwetu kama tutaifumbia macho dhambi hii kubwa ya Abu Dharr. Anaifanyia ufisadi dini yetu waziwazi na kukebehi miungu yetu." Mtu wa tatu akasema, "Ni wajibu wetu kumfukuza kutoka kwenye kabila letu bila kuchelewa hata kidogo, kwa sababu kama tukichelewa kumtenga katika kipindi kifupi tu, atawaelemea vijana wetu, wanawake zetu, watumwa wetu na kuwatia mawazo yake maovu akilini mwao. Endapo inatokea hivyo, tutapata hasara kubwa sana."
Mtu wa nne akasema, "Maoni yako ni sahihi. Lakini, nani atamfunga paka kengele? Huyu ni mtu mashuhuri wa kabila na ni mzee wa kaya. Ninaona kwamba hata Unais anayo mawazo haya haya, na yeye pia ni mtu mwenye kuheshimiwa."
Mtu wa tano akasema, "Hakuna haja ya wasi wasi. Njooni tukamtaarifu Khafaf. Tunao uhakika kwamba Khafaf na watu wengine waungwana wa kabila ndio watakao mfukuza kutoka kwenye kabila."
Mtu wa sita akasema, "Ninatafakari kuhusu mawazo yao. Sina uhakika kama wataweza kuwabadili. Inawezekana kwamba wao ndio watakao badilika na kwenda kwenye njia iliyo nyooka tusijisumbue, lakini na tutafakari kuhusu dini yao. Nisikilizeni! Ninaona kuna ukweli kwenye imani yao. Hata hivyo karibu tutafika kwa mtemi Khafaf. Baada ya mazungumzo yetu na yeye, tunategemea kufikia uamuzi wenye msimamo."
Kwa ufupi, wakizungumza pamoja, watu hawa walifika nyumbani kwa mtemi wa kabila la Ghifar na wakamwambia, "Tumetoka kwa Abu Dharr kuja kwako."
Khafaf: "Abu Dharr amerudi kutoka safari yake ya kutoka Makkah?" Mtu mmoja akasema, "Bwana, Abu Dharr ameasi. Aliwabeza miungu wetu. Anasema kwamba yupo mtu ameteuliwa kuwa Mtume. Kazi yake ni kuwaita watu waende kumuabudu Mungu Mmoja na pia kufundisha mambo mazuri. Abu Dharr haridhiki bila kukubali utume wa mtu huyu na kuendelea na msimamo huo, lakini wakati wote anahubiri kwa watu na kuwaita wote wengine waende kwa Mtume huyo na Mungu wake.
Khafaf aliposikia, alisema, "inasikitisha kuona kwamba Abu Dharr, anawaacha miungu wote, na kutangaza kumuabudu Mungu Mmoja. Ni uovu mkubwa sana na kutia kinyaa.
Ninaona kwamba jambo hili litachochea vurugu kubwa katika kabila letu, na matokeo yake kabila litaangamia. Enyi vijana wangu! Msifanye haraka lakini nipeni, muda wa kutafakari kuhusu jambo hili la Abu Dharr."
Baada ya vijana hao kuondoka na kurudi makwao, Khafaf mtemi wa kabila, alianza kufikiri kwa nini wote walikuwa wanasema kwa kumpinga Abu Dharr. Aliendelea kutafakari usiku wote akiwa kitandani kwake. Hali ilimkanganya sana na hakuweza kufanya msimamo hasa. Lakini akili yake ilikuwa na fikra nzito kuhusu maneno yaliyosemwa na Abu Dharr. Saa nyingi zilipita bila kupata usingizi, na alikuwa anafumba macho yake.
Mtemi Khafaf pia alikumbuka hotuba ya mwanafalsafa wa Kiarabu, Qays bin Saidah, pale sokoni. Alisema kwamba Muumbaji wa ulimwengu bila shaka ni Mmoja na ni Yeye tu ndiye anaye stahiki kuabudiwa. Aliunga mkono kikamilifu maoni ya Abu Dharr kwenye hayo mahubri yake ya kusifika na pia alitamka kwamba fikra za Warqa bin Naufal, Zayd binAmr, Uthman bin Hoverath na Abdallah bin Hajash kuelekea kwenye imani ya Abu Dharr.
Alikuwa katika hali hii ya kustaajabisha ambapo akili yake ilimuongoza na akajisemea mwenyewe, 'Naam! Abu Dharr yu sahihi kwa sababu Qays bin Saida amemuunga mkono na ninao uhakika kwamba Qays hawezi akashindwa kuelewa wala kukubali itikadi yoyote ya uongo. Bila shaka, lazima atakuwepo muongozaji wa dunia hii, na lazima pawepo na nguvu yenye uwezo wa kuendesha mpangilio wote wa ulimwengu na ni dhahiri kwamba miungu wetu wa mawe na miti hawana kabisa uwezo kama huu. Ee Mungu wa Abu Dharr! Tuongoze na utukomboe kutoka kwenye uovu huu na utuweke kwenye njia ya haki."
Wakati ambapo Khafaf alikuwa anafanya uamuzi wake muhimu, siku ilipambazuka hadi jua lilionekana angani pamoja na kuenea kwa mwanga wa jua, pia habari zilizidi kuenea kwamba Abu Dharr, kaka yake na mama yake wote wamerudi kutoka Makkah na wamemuabudu Mungu Mmoja tu.
Pamoja na kuenea habari hizi hasira ilichochewa. Watu walianza kumlaani Abu Dharr na kusema, 'Amepata kichaa na hawezi kuelewa kwamba haya masanamu yetu hutuponya maradhi, yanatupatia riziki na kutulinda. Abu Dharr ni mtu wa ajabu ambaye anatuita twende kwa mungu asiyeonekana! Inaonyesha kama vile Abu Dharr anataka kuanzisha vurumai na matatizo miongoni mwa vijana wetu na kuwapotosha watoto wetu na wanawake wetu. Hakika mtu huyu ni muongo na madai yake si sahihi. Lazima afukuzwe kutoka kwenye kabila."
Mmojawao akasema, "Kwa nini! Unawezaje kuelezea wazo la kumfukuza mtu huyu? Itafanyikaje? Hapana , kamwe! Haiwezekani kutokea. Huyu ni mtu jasiri katika kabila letu."
Baada ya mazungumzo haya watu hao waliamua kutaka wasikilizwe na wazee kuhusu suala hili. Kufuatana na uamuzi wao, waliwaendea
wazee wao kushughulikia jambo hili. Wazee wao waliamua kulipeleka jambo hili la Abu Dharr kwa mtemi. Kwa hiyo, wote walikwenda kwa Khafaf.
Mtemi wa kabila alimtuma mtumwa wake haraka aende kumwita Abu Dharr. Mtumwa huyo alipofika nyumbani kwa Abu Dharr alisema, "Abu Dharr! Wewe na Unais mnaitwa na Mtemi."
Abu Dharr akajibu kwamba alikuwa tayari kwenda kwa mtemi. Mtumwa alipoondoka, Abu Dharr alichukua upanga wake na kuhifadhi kwenye mkanda na alimwambia kaka yake, Unais, "Njoo; twende kwa Khafaf!"
Unais: "Ewe kaka! Nimesikia mambo mabaya yanazungumzwa na watu kuhusu wewe. Nina hofu huu mkutano wetu unaweza usiwe na manufaa, jambo lisilotegemewa linaweza kutokea badala ya mategemeo yetu."
Abu Dharr: "Hapana, siyo. Namjua Khafaf vizuri sana. Ni mtu mwenye hekima. Mwenyezi Mungu amempa hekima. Ni mtu mwenye akili sana miongoni mwa kabila letu."
Ndugu hawa wawili waliendelea kuzungumza hadi wakafika kwa Khafaf. Hapo waliona kwamba watu maarufu wa kabila hilo walikuwa wamekaa kumzunguka Khafaf. Akawaamkia wote Abu Dharr akasema, "Salaamu Alaykum " (Amani iwe kwenu).
Waliposikia maamkizi ya Abu Dharr kwa jinsi ya Kiislamu, wazee wa kabila hilo walikasirika na walisema kwa hasira; "Salamu gani hii ambayo hatujawahi kuisikia kamwe." Halafu mmojawao akasema "Inasikitisha. Hatujui Abu Dharr anakoelekea."
Mtu mwingine akasema, "Hebu mtazame. Amekaa na upanga wake, na hana heshima kwa mtemi." Mtu wa tatu akasema, maneno yako ni sahihi. Lakini, huyu ni mpanda farasi wa kabila letu na watu jasiri wakati wote huwa tayari kwa lolote."
Abu Dharr akasema, "Silikizeni! Ninawaheshimu nyinyi kwa sababu ni watu maarufu wa kabila letu, ambao mnastahili kujivuniwa na kuwaenzi. Salaamu niliyo wapeni ni Salamu ya Kiislamu."