3
MAISHA YA ABU DHARR
Baada ya haya, Abu Dharr na Unais waliketi kwenye nafasi zao wakitazamana uso kwa uso na mtemi, Khafaf. Khafaf alisema kwa sauti ya upole lakini kali, "Ewe Abu Dharr! Ninayo Taarifa kwamba wewe umekuwa na msimamo wa kumuabudu Mwenyezi Mungu Ambaye haonekani. Watu mashuhuri wa kabila letu wamekasirika na msimamo wako huu. Wanasema kwamba Abu Dharr amewatukana miungu yao na anawaita hawana hekima yoyote.
Ewe Abu Dharr! Tunakuheshimu lakini haimaanishi kwamba tupo tayari kustahamili miungu yetu kubezwa. Ninakuomba uache hoja ya mawazo yako ya sasa na urudi kwenye imani ya wahenga wako, au vinginevyo unatakiwa uieleze imani yako kwangu ili niweze kuelewa ukweli wa imani yako. Pia, ninakuhakikishia kwamba nitafikiria kuingia kwenye imani hiyo endapo utathibitisha kwamba imani yako haina shaka zaidi kuliko ya kwetu.
Abu Dharr naye alijibu, "Ewe mtemi wa kabila! Tunakuheshimu na kustahi chochote unacho sema. Lakini, wakati huo huo tunataka kueleza kwamba Mwenyezi Mungu, wa Pekee Ambaye tumeamua kumuabudu na Ambaye tunamwamini, ni huyu huyu ambaye ameumba dunia na mbingu, Ambaye huruzuku viumbe vyote, Ambaye kudhibiti maisha ya viumbe vyote vyenye uhai na Ambaye uwezo wake hauna mipaka.
Masanamu ambayo tumekuwa tunayaabudu hadi sasa, yametengenezwa na mikono yetu kwa kutumia patasi na nyundo. Akili inaweza kuamrisha kwamba yule ambaye ametengenezwa na mikono yetu anaweza kuwa muumbaji wetu, anaweza kuruzuku na tusikiliza dua zetu?
Mwanadamu ni kiumbe bora zaidi kuliko viumbe vya muumbo wote. Inawezekana yeye na heshima yake astahili kuinamisha kichwa chake mbele ya jiwe? Mtemi wangu! Tafadhali tafakari bila upendeleo kuhusu haya ninayosema. Masanamu hayana hata uwezo wa kufukuza adui yao.
Nisikilize, ewe mtemi! Wakati fulani nilikwenda kwa Manat na nikampa sadaka ya kikombe cha maziwa. Nilikuwa bado nipo eneo hilo ambapo mbweha alifika hapo na akanywa maziwa hayo yote na akamkojolea Manat. Tukio hili liliniathiri sana na nilifikiri kwa nini mungu anashindwa kujilinda mwenyewe?
Jambo hili lilinidhihirishia kwamba sanamu haliwezi kuwa mungu. Nina uhakika na kila mtu mwenye akili ataamini kwamba Muumbaji wa mbingu ni bora zaidi kuliko mbingu na muumbaji wa dunia ni bora zaidi kuliko ardhi. Kwa mujibu wa kanuni hii yenye mantiki, masanamu hayawezi kuwa ni bora kuzidi sisi, haina maana sisi kuyaabudu.
Ewe mtemi wangu! Nimekuja kwenye kweli kwamba Mwenyezi Mungu ni Peke Yake Ambaye ni Mumbaji na mwenye kuruzuku ulimwengu, na Muhammad Mustafa ambaye alipelekwa Makkah ni Mjumbe Wake.
"Anazo sifa nzuri kama hizo hivyo kwamba hakuna afananaye Naye hapa duniani. Quraishi ambao ni maadui zake wabaya wanakubali
ukweli wake na uwezo wake. hata wanapojua kuwa Muhammad ni mpinzani mkubwa wa miungu yao na dini yao, wamempatia jina la Sadiq na Amin, kama ambavyo, nimetambua hivi karibuni tu. Sikiliza! Uso wake unang'aa nuru na hekima inatiririka kutoka kwenye maneno yake."
Mara tu Abu Dharr alipomaliza hotuba yake, kelele kubwa ilitoka sehemu zote, "Jinsi gani maneno ya Abu Dharr yalivyo matamu! Kwa hiyo, miungu yetu haisikii na haisemi! Abu Dharr ameidhalilisha imani yetu na anaitukana miungu yetu!"
Kundi moja lilisema kwa pamoja, "Rafiki zangu! Msizungumze mambo yasiyo na mantiki. Kwa uaminifu tunasema kwamba lolote alilosema Abu Dharr linaonekana kuwa sahihi na akili inataka kwamba lazima tukubali ukweli. Tunao uhakika kwamba hatuwezi kupata mwongozo mzuri zaidi kuzidi yale ambayo Abu Dharr ametuletea."
Sauti nyingine ilitokeza: "Nchi ya Arabuni inahitaji muongozaji na inaonyesha kama vile hakuna mwongoaji bora zaidi kuliko huyu ambaye amedhihirishwa na Abu Dharr."
Halafu sauti nyingine ilitokeza, "Hotuba ya Abu Dharr ni ya maana sana." na baada ya hii sauti ya juu sana ilitokeza; kama vile ingetoboa masikio, Ewe Abu Dharr! Ninashahidilia kwamba hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu na ninakiri kuamba Muhammad ni Mtume Wake!"
Alipoona hivi, Khafaf, mtemi wa kabila, baada ya kufikiri sana alinyanyua kichwa chake na akawaambia watu wake: "Wapendwa watu wa kabila langu! Nisikilizeni kwa makini. Mmesikia yote hayo aliyoyasema Abu Dharr. Ni wajibu wetu kutafakari kuhusu hotuba
yake kwa uangalifu sana na kwa makini sana na tuweze kuona inayo kiasi gani cha ukweli.
Uamuzi wa haraka haufai. Si busara kutupilia mbali ushauri wa mtu bila kuchunguza. Rafiki zangu! Mnatambua kiasi cha machafuko yaliopo miongoni mwetu na jinsi uhalifu ulivyo zidi ambao sisi tunahusika. Matajiri wanawanyonya masikini na hakuna mipaka katika kufanya dhambi na maovu.
"Mimi nimeamua kwamba lazima nikubali na kuunga mkono yale anayoyasema Abu Dharr. Sasa ni juu yenu nyinyi kujiamulia wenyewe. Sikilizeni nyinyi nyote. Ninashahidilia kwamba hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wake!"
Mara tu Khafaf alipotamka Kalimah (la ila ha illalah Muhammadan Rasulillah) palitokea kelele kubwa ndani ya kabila, Khafaf amekuwa Muislamu. Khafah ameingia Uislamu!"
Haikupita muda mrefu baada ya Khafaf kuingia kwenye Uislamu, hali ya kabila ilibadilika kabisa. Watu walio wengi walisilimu na kuwa Waislamu hapo hapo, ambapo wengine walingojea kukubali kuwa Waislamu mbele ya Mtukufu Mtume baada ya kuwasili huko Madina.
Kwa ufupi, kwa juhudi kubwa ya Abu Dharr watu wengi wa kabila la Ghifar walikubali kuwa Waislamu na palitokeza ukelele wa "Mungu Mkubwa! na "Mungu ndiye Mwenye Kusifiwa!" na jina la Mtukufu Mtume likaanza kutangazwa mchana na usiku.
Baada ya kujaza moyo wa Uislamu kwenye kabila la Ghifari na kuwasilimisha watu na kuingia kwenye Uislamu, Abu Dharr alielekeza umakini wake Asfan. Alipofika huko alianza kuhubiri Uislamu miongoni mwa watu. Kwa kuwa sehemu hii ilikuwa kwenye njia kuu iliyotumiwa mara nyingi na Quraishi na alijenga hisia dhidi yao kwa sababu ya mateso aliyofanyiwa nao alifanya zoezi la nidhamu kali katika kuwafanya kuwa Waislamu. Kundi la Quraishi lilipopita hapo, aliwaeleza habari ya Uislamu na kwa hiyo idadi kubwa ya Quraishi walikubali kuwa Waislamu.
SURA YA NNE
Abdul Hamid Jaudatus Sahar wa Misri ameandika, Uislamu ulienea Madina kama moto wa mbuga ya majani makavu." Kabila la Ghifar lilifurahishwa sana na hali hiyo. Waislamu walipongezana wao kwa wao kwamba makabila mawili ya Aus na Khazraj, ambao walikuwa wasemaji sana, wapiganaji wazuri sana na waunga mkono wazuri sana walikubali kuingia kwenye Uislamu, na pia kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikwisha ridhika kuinyanyua dini Yake na alinuia kumsaidia Mtukufu Mtume na kutimiza ahadi yake.
Unais alikwenda kwa kaka yake Abu Dharr akiwa na habari za kufurahisha na akasema "Uislamu umeenea Madina na Aus na Khazraj wamekubali Uislamu!"
Abu Dharr akasema, "Mtume wa Mwenyezi Mungu atakwenda na kuhamia huko baada ya kipindi kifupi."
Unais alimwangalia kaka yake kwa mshangao na alisema, "Umepokea habari zozote za aina hiyo?"
Abu Dharr, "Hapana, wala sina taarifa yoyote kuhusu habari hizi, ama kujua kwamba watu wa Yathrib wamekuwa waumini."
Unais, "Vipi sasa ulijua kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu atahamia Yathrib?"
Abu Dharr, "Aliniambia siku hiyo hiyo nilipokutana naye, kwamba alitarajia kwenda kwenye mji wa mitende na nadhani sehemu hiyo ya Yathrib, Mtume alisema kweli."
Unais, "Inawezekana kwamba kabila lake litamruhusu aondoke hapo akiwa na Waislamu, ili kwamba baada ya matayarisho kamili awashambulie?"
Abu Dharr, "Wanaweza wakamruhusu au wasimruhusu, lakini baada ya kipindi kifupi atahamia huko. Kama mambo yalivyo, ni Mwenyezi Mungu tu ndiye anaye jua ni vipi na lini itatokea."
Abu Dharr alisilimisha kabila lake na kuingia kwenye Uislamu baada ya yeye kuwa muumini. Halafu akaelekeza shughuli hiyo Madina. tangu aliporudi kutoka Makkah hadi kuhama kwa Mtukufu Mtume, Abu Dharr alikuwa anashughulika na kuhubiri Uislamu na aliendelea kufanya juhudi kuipeleka dini ya Mungu kwa umma Mtukufu Mtume aliendelea kufanya kazi yake ya kuhubiri Uislamu na Quraishi waliendelea kufanya kazi yao ya kumtesa Mtume. Walimpa mateso makubwa sana hivyo kwamba hakuwa na uchaguzi mwingine isipokuwa kuondoka nyumbani kwake. Kwa ufupi, kwa amri ya Mwenyezi Mungu Jibril alimwambia aondoke Makkah baada ya kumwambia Ali alale kwenye kitanda cha Mtume.
Alifanya alivyoagizwa. Alimwambia alale kitandani pake na akaondoka, hivyo kwamba Quraishi hawangejua kama hayupo kitandani pake. Baada ya kukaa siku tatu kwenye pango la Hira aliondoka kwenda Madina.
Abu Dharr alikuwa anangojea uhamiaji Madina. Watu wa kabila lake pia walikuwa wanangojea na walikuwa wanauliza mara kwa mara habari za Mtukufu Mtume kwa mtu yeyote aliyetokea sehemu hiyo.
Kuanzia Makkah na baada ya kukaa kwa muda wa siku chache pangoni, Mtume aliondoka kwenda Madina. Kabila la Ghifar lilipopata taarifa kwamba alikuwa kati ya Makkah na Madina walifurahi sana. Abu Dharr alihisi wimbi la neema lilikuwa linakuja. Aliungana na kabila kungoja.
Watu walikusanyika na kumzunguka na walimuuliza kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu, mwenendo wake na umbile lake alijibu, "Mtamuona baada ya muda si mrefu.
Yeye ni bora kuliko wote na anamzidi kila mtu kwa sifa." Watu walipongojea kwa kipindi kirefu, Abu Dharr alikuwa anaangalia njia, ili awe mtu wa kwanza kuwataarifu watu atakapo wasili Mtume na kutuliza nyoyo za watu na kuondoa hofu iliyokuwa inawaelemea kwa kungojea kwa kipindi kirefu hivyo.
Muda uliendelea kupita. Watu wa kabila la Ghifar walikuwa na shauku kubwa ya kumpokea Mtume. Abu Dharr alipotupa jicho aliona ngamia anakwenda hapo. Watu wote walikuwa wanaangalia macho ya Abu Dharr. Baada ya muda mfupi, Abu Dharr akasema kwa sauti ya kushangaa, "Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mtume anawasili!"
Allamah Subaiti ameandika, "Uso wa Mtukufu Mtume ulikuwa unatoa nuru. Kwa ufupi watu wote walimfuata Abu Dharr, huku wakisema kwa sauti moja, "Mtume wa Mwenyezi Mungu amekuja! Mtume wa Mwenyezi Mungu amekuja!" Abu Dharr alikwenda mbele haraka na akashika hatamu ya ngamia wake.
Watu walianza kusema, "Allahu Akbar." (Mwenyezi Mungu Mkubwa) huku wakimzunguka Mtume kwa hamu kubwa. Wanawake wote, vijana na vikongwe, wavulana na wasichana walikuwa wanashangilia kwa furaha kubwa. Mtume wa Mwenyezi Mungu amewasili! Mtume wa Mwenyezi Mungu amewasili!"
Baada ya hapo watu wa kabila la Aslam walisema, "Pia na sisi tumekuwa Waislamu kama walivyo fanya ndugu zetu wa kabila la Ghifar." Mtume wa Mwenyezi Mungu alifurahi sana na alinyanyua mikono yake kuelekea mbinguni aliomba, "Ee Mola wa ulimwengu! Wasamehe kabila la Ghifari na uwaweke kabila la Aslam salama."
Baada ya hapo Mtukufu Mtume aliteremka kwenye ngamia na akaanza kukariri Quran. Sauti yake iliingia kwenye nyoyo za watu. Halafu akaanza kuhubiri. Watu walikwenda mbele kwa makundi na kutoa kiapo cha utii kwake. Abu Dharr alisimama kwa maringo karibu na Mtume akiwa amefurahi kupita kiasi.
Watu wa kabila la Ghifari walijitokeza mbele na wakasema, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Abu Dharr alitufundisha yote yale uliyomwambia. Tukasilimu na kuwa Waislamu na tukakiri kwamba wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu."
Baada ya hapo watu walifurahi sana na walikuwa wanaangalia uso wa Mtume mara kwa mara. Abdul Hamid Jaudatus Sahar ameandika, "Watu walianza kuangalia uso wa Mtume kwa makini, waliona kwamba alikuwa mtu mwenye uso unao ng'aa midomo inayo tabasamu na tabia njema kuhusu umbo lake, hakuwa mwembamba au aliye konda ama mnene. Alikuwa na sura nzuri ya kupendeza.
Macho yalikuwa makubwa na meusi, kope za macho zilikuwa ndefu, nyusi zake nyeusi zilizojikunja mfano wa tao, nywele nyeusi, shingo
ndefu na ndevu nyingi. Alikuwa Mtukufu wakati ametulia na alikuwa anatia moyo kwa heshima wakati anasema. Mazungumzo yake yalikuwa matamu. Wala hakuwa mkimya au msemaji. Alikuwa na sura ya kupendeza sana akiwa mbali na mzuri sana akiwa karibu.
Saizi ya umbile lake ilikuwa ya kati, wala hakuwa mrefu sana kiasi cha kutokupendeza kumwangalia, ama mfupi sana kiasi cha kufikiriwa kuwa mtu duni.
Baada ya hapo Mtukufu Mtume aliondoka kwenda Madina na Abu Dharr aliendela kuishi na kabila lake."
Kutoka hapo, Mtukufu Mtume aliondoka kuelekea Madina. Alipofika Madina, watu walimkaribisha kwa moyo mkunjufu. Mara tu baada ya kufika, alianza kuhubiri ujumbe wa Uislamu. Abu Dharr ambaye hakuweza kumsindikiza Mtukufu Mtume huko Madina aliishi mjini kwake kwa kipindi kirefu sana hivyo, vita kuu tatu za Kiislamu (Ghazawat) vita vya Badr, mwaka wa 2, Hijiriya, Uhud mwaka wa 3 Hijiriya, na Ahzab mwaka wa 5 Hijiriya zilipiganwa hadi mwisho.
Baada ya vita ya Ahzab, aya ya Quran Tukufu ilimlazimisha Abu Dharr kuondoka kwenda Madina. Siku moja alikuwa anashughulika na dua baada ya Swala ya jioni kwenye msikiti wa mjini kwake, ambapo alisikia mtu anasoma kwa sauti Aya (61:10)
"Enyi mlio amini! Nikuonyesheni biashara itakayokuokoeni na adhabu iliyo chungu
."(61:10)
Baada ya kutafakari maana ya Aya hii alipata shauku ya Jihadi na akamwambia Unais, "Nitaondoka kwenda Yathrib kesho."
Unais: "Sawa! Nenda. Mwenyezi Mungu na akufikishe huko Salama!"
Abu Dharr, "Sitarudi. Nitatumia maisha yangu yote katika kumtu-mikia Mtukufu Mtume."
Unais, "Ewe ndugu yangu! Umekuwa muumini wa kweli na imani imepenya kwenye moyo na roho yako. Kabila lako na watu wako hapa wanakutaka sana. Patakuwepo pengo kubwa sana ukiondoka hapa. Nadhani ungeacha mpango wa kwenda Madina na uishi hapa hadi mwisho wa uhai wako."
Abu Dharr; "Mtukufu Mtume ni bora zaidi kuliko watu hawa. Chochote ambacho kimetekelezwa kinatosha. Mtukufu Mtume alipigana Badr, Mimi sikuwa naye. Akapigana huko Uhud Mimi si kuwepo. Hadi lini nitaendelea kulitumikia kabila langu na nikose baraka za kufa shahidi. Yote hayo ambayo yamefanyika mpaka sasa yanatosha. Sasa sitakata tama hata kwa dakika moja kuhusu uamuzi wangu wa kwenda Yathrib."
Unais, "Pendekezo langu ni kwamba wewe uendelee kuishi hapa nyumbani kama kawaida. Mtukufu Mtume atakuita yeye mwenyewe atakapokuhitaji. Wewe angalia walikuwepo watu wengi waliokuwa katika miji ya kwao na waliondoka kwenda Madina baada ya kuitwa na Mtukufu Mtume."
Abu Dharr akasema: "muda wa kungojea umepita. Endapo Mtume hajaniita mimi pia nina wajibu. Sitaendelea kungoja, nitakwenda huko bila kuitwa."
Unais: "Vema! Lakini usifanye haraka. Chukua mahitaji ya muhimu kwa safari."
Abu Dharr; "Sihitaji chochote. Vipande vya mikate mikavu vinanitosha."
Abu Dharr aliondoka nyumbani kwake na kuelekea Madina. Alipofika huko alipata heshima ya kukutana na Mtume na akawa naye.
Alikuwa na desturi ya kulala kwenye msikiti wa Mtume usiku na wakati wa mchana alikutana na watu. Alikula chakula pamoja na Mtume na akaiga maisha yake ya kidunia kwa uchaji Mungu na uadilifu. Alifanya bidii sana kujifunza hadithi za Mtume na kuzihifadhi katika kumbu kumbu.
Baada ya kuifika Madina Abu Dharr aliugua kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa. Mtume alipata taarifa ya ugonjwa wake. Akaenda kumuona Abu Dharr na akamwambia; "Abu Dharr! Unatakiwa uishi nje ya Madina kwa muda fulani sehemu ambayo ngamia, kondoo na mbuzi wa taifa huchungwa na uzingatie kwamba usile chochote isipokuwa maziwa wakati wote utakapo kuwa kule."
Mara tu baada ya kupokea amri ya Mtume, Abu Dharr aliondoka kwenda mahali hapo alipoambiwa akiwa na mkewe.
Ugonjwa ulikuwa mkali sana kwa kipindi cha siku kadhaa lakini, ulipungua pole pole akapata afya nzuri hadi akaweza kutimiza tendo la ndoa na mke wake. Sasa, palijitokeza tatizo la upatikanaji wa maji kwa ajili ya josho kubwa la kuondoa janaba kabla ya Swala. Hadi hapo alikuwa hajajua Tayamamu. Kwa hiyo alikuwa hajui la kufanya kwa muda fulani. Hatimaye akili yake ilimwongoza na akaenda kumuona Mtume kwa mwendo wa haraka sana wa ngamia. Mara tu
Mtume alipomuona Abu Dharr alitabasamu na alisema kabla Abu Dharr hajasema, "Abu Dharr! Usiwe na wasiwasi. Maji yametayarishwa kwa ajili yako hapa na sasa hivi. kwa hiyo, msichana aliyekuwa mtumishi wa Mtume alitayarisha maji na Abu Dharr akaoga. Baadaye alikwenda kwa Mtukufu Mtume na aka fundishwa jinsi ya kutumia udongo kwa ajili ya kuchukua Wudhu (Tayamamu)- (Musnad Ahmad bin Hanbal).
Abu Dharr alikuwa anaendesha maisha yake ambapo Vita ya Tabuk ilitokea mnamo mwaka wa 9 Hijiriya. Waandishi wa historia wanasema kwamba Mtume alijua kwamba Wakristo wa Syria walifanya uamuzi thabiti wa kushambulia Madina na wapiganaji elfu arobaini kutoka kwa Harcules, Mfalme wa Roma. Kwa hiyo, Mtume aliamua kuondoka kwenda Syria kama hatua ya tahadhari akiwa na wapiganaji kati ya elfu thelathini hadi arobaini. Alimteua Ali kuwa mbadala wake Madina. Baada ya kutayarisha jeshi lake aliondoka Madina.
Baada ya kuondoka Mtume wanafiki walianza kumdhihaki Ali kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alimwacha ili kupunguza mzigo wake mwenyewe. Katika kuwathibitishia kwamba wanafiki ni waongo aliamua kwenda kwa Mtume.
Kwa kufuatana na Mtume mahali paitwapo Jaraf na akamtaarifu kuhusu dhihaka ya wanafiki.
Mtume akasema, "Wanafiki ni waongo. Nimekuja hapa baada ya kukufanya wewe kuwa kaimu wangu. Ewe Ali hufurahikii cheo chako cha juu zaidi. Uhusiano wako na mimi ni sawa na uhusiano aliokuwa nao Harun na Musa ila tofauti moja tu ni kwamba hapatakuwepo na Mtume baada yangu. Maana yake ni kwamba Musa alipokwenda kwenye Mlima wa Tur alimteua Harun kuwa kaimu (wakili) wake na yeye (Mtukufu Mtume) alifanya namna hiyo hiyo."
Aliposikia hivi Ali alirudi Madina na Mtume aliendelea na safari ya kwenda Tabuk sehemu iliyokuwa kwenye mpaka wa iliyokuwa Falme ya Roma katika urefu wa vituo kumi kutoka Madina na Dameski. Alipofika Tabuk, alikaa hapo kwa muda wa siku kumi. Wakati wa kuwepo yeye hapo, alimtuma Sariys (jeshi la Uislamu linaloongozwa na mtu mwingine na si Mtume) sehemu zote, na alisisitiza kuwaita watu waingie kwenye Uislamu. Hakuna jeshi lililofika hapo kutoka Roma kwa madhumuni ya vita. Kwa hiyo, alilazimika kurudi Madina.
Wakati wa safari hiyo, siku moja usiku wanafiki walitaka kumuua wakati anapita kwenye bonde la Aqaba Zi Fata, kwa kumuogofya ngamia wake, ambaye angeweza kumwangusha chini, lakini Hudhayfah bin Yaman na Ammar bin Yasir walimwokoa. Baada ya Mtukufu Mtume kuvuka bonde, alimwambia Huzayfah bin Yaman majina ya wanafiki waliotaka kumuua kwenye giza, na akamuamuru kuwa majina hayo iwe siri yake. Masahaba maarufu walikuwemo kwenye orodha hiyo.
Kwa mujibu wa Tahzibut Tahzib, watu hao walijaribu kupata majina hayo kutoka kwa Hudhayfah lakini hakufichua.
Hatimaye mmoja wapo wa masahaba hao alikiri mwenyewe, "Uniambie ama usiniambie, kwa jina la Mwenyezi Mungu, mimi nilikuwa miongoni mwa wanafiki hao!" Kwa ufupi, Mtume alirudi Madina wakati wa mwezi wa Ramadhani.
Wakati wa kuondoka kutoka Madina kwa madhumuni ya Vita ya Tabuk, Abu Dharr alikuwa naye. Lakini kwa kuwa ngamia wake alikuwa dhaifu na kukonda, hakuweza kuwa katika msafara. Abu Dharr, hata hivyo, alibaki nyuma ya msafara kwa umbali wa muda wa safari ya siku tatu.
Alijitahidi sana kuwa karibu na Mtume lakini alishindwa. Alihuzunika sana alipotambua kwamba haingewezekana yeye kuwa ndani ya msafara.
Kwa mujibu wa maelezo mengine, alipobaki nyuma, watu fulani walimwambia Mtume kwamba ilikuwa vigumu sana Abu Dharr kuwa naye. Aliposikia hivi, Mtume akasema, "Mwacheni huyo hivyo alivyo. Atafika Inshallah. Kwa hiyo msafara uliendelea na Abu Dharr alizidi kubaki nyuma akiwa amefadhaika na wasi wasi.