UTENZI WA IMAM HUSEN
MWANDISHI: HEMED BIN ABDALLAH BIN SAID
UTENZI WA KISA CHA SAYYIDNA HUSSEIN
1. Bismillahi Aziza, ArRahmani Mweneza, Ndiye wa Kwanza na kwanza, Wa milele na abadi
2. Ndiye Huyu 'lKayumu, Wa milele na dawamu, Ndiye muumba Adamu, Na wote wake waladi
3. Ndiye muumba 'ssamai, Na wote anbiai, Thumma na auliai, Wote ni wake ibadi
4. Jamii ni wake waja, Wala hawati mmoja, Kula atakae haja, Apata wake mradi
5. Kuumba kwake Jalali, Nabiu na Mursali, Aliyeumbwa awali, Tumwa wetu Muhammadi
6. Huyo alitangulia, Kisijawa vitu pia, Vyote vilivyobakia, Vijile yake baadi
7. Nuru yake yalidanda, Na sifaze zikenenda, Jina aketwa Kipendwa, Kipendo chake 'sSamadi
8. Baada ya kudhukuri, Sifa za Mola Jabari, Na za tumwa Mukhtari, Penda nitunge ishadi
9. Natanga tunga utenzi, Usipate nusu mwezi, Ama kwandika siwezi, Macho yametasawadi
10. Macho yamesawidika, Sioni vema kwandika, Kwa kula siku kushika, Karatasi na midadi
11. Macho yangu wanakwetu, Hayafafanui mtu, Natendea kazi yetu, Ya tangu jadi na jadi
12. Na kuiwacha si vema, Taja dhuriwa nakoma, Hata kwamba si mzima, Afadhali jitihadi
13. Na hadithiye kwambile, Nitakayo nitongole, Bajani moyo mkale, Tena mtuze fuadi
14. Mtoe na wasiwasi, Niwatulie nafusi, Baada ya kujilisi, Na roho kutabaradi
15. Ndipo niweleze shani, Ya Maulana Huseni, Dhuria wake Amini, Vita vyao na Yazidi
16. Huyu Yazidi sikia, Babaye ni Muawia, Kutawafukwe Nabia, Na arubaa Sayyidi
17. Wa kwanza Abubakari, Na Maulana Omari, Na Ally Haidari, Na mmoja taradidi
18. Maulana Athumani, Watu hao sikiani, Kuondoka duniyani, Ndipo hayo yakabidi
19. Kuondoka kwao pia, Kutawala Muawia, Miji yote kuzuia, Asibakie biladi
20. Akashika ufalume, Wala pasiwe muume, Na dhuriaze Mtume, Pendo likenda ahadi
21. Akampenda Huseni, Na watotowe nyumbani, Na angawa sultani, Asiweze kutaadi
22. Kakithiri Muawia, Heshima kamwekea, Na pendo kamzidia, Atakalo lisirudi
23. Akazidi muheshimu, Na wote bani Hashimu, Jamii kawakirimu, Akajifanya abidi
24. Baada hayo rafiki, Akenenda Dimishiki, Na dhuriaze sadiki, Asibakie wahidi
25. Kamtukua Huseni, Na dhuriaze Amini, Rijali na nisiwani, Wakubwa hata waladi
26. Dimishiki kenda nao, Muawia kawa nao, Akawaweka kikao, Kizuri kisikyo budi
27. Baada suu wuadhi, Akapatwa ni maradhi, Muawia kiaridhi, Akajua ni ahadi
28. Akajua ni ajali, Ya roho kunakali, Akamwita tasihili, Mtoto wake Yazidi
29. Akamuweka usoni, Wali wao faraghani, Muawia kabaini, Akamba ewe waladi
30. Ewe Yazidi mwanangu, Nitazama hali yangu, Muwili wote matungu, Na uzito wa jasadi
31. Muwili umezuiwa, Sijiwezi kujinua, Na sisi waja twajua, Mauti hatuna budi
32. Twaijua kwa hakika, Ni faradhi kutoweka, Yazidi akatamka, Maneno akaradidi
33. Baba utakapokufa, Nnani nyuma Khalifa, Mtamalaki taifa, Na ezi ikambidi?
34. Akinena Muawia, Khalifa wewe dhuria, Lakini nakuusia, Usije ukafisidi
35. Sikia ewe mwanangu, Ushike wosia wangu, Wepukane na matungu, Hiyo siku ya mnadi
36. Kwanza nikuusiayo, Ezi ni kutunza moyo, Ujue na marikayo, Na walio kukuzidi
37. Na wote raia wako, Ukae nao kitako, Usikithiri vituko, Utakuja jihusudi
38. Na tena uwashauri, Ijiriapo amri, Ukae nao vizuri, Roho zao ziburudi
39. Pindi hayo ukitenda, Tambua watakupenda, Utakalo utatenda, Neno lako halirudi
40. Baada hayo yakini, Nakusikia Huseni, Na watotowe nyumbani, Alla Alla ya Yazidi
41. Alla Alla uwashike, Tangu waume na wake, Na jambo lisitendeke, Shati apende Sayyidi
42. Jambo asilolipenda, Usije ukalitenda, Tambua umejivunda, Hata kwa Mola Wadudi
43. Wala usimkasiri, Hata kwa jambo saghiri, Mpe kuti na uzari, Kabla wote junudi
44. Alla Alla muheshimu, Umzidie makamu, Kwani sisi tu hadimu, Walidio masayidi
45. Ewe Yazidi yashike, Yule asikasirike, Sisi tu watumwa wake, Na babuye Muhamadi
46. Na ukhalifa si wetu, Wala si wa baba zetu, Wake yeye bwana wetu, Sisi kwao tu abidi
47. Pindi atakapokuwa, Siwate kumtukuwa, Umsalimu ulua, Kuko kwao na urudi
48. Alla Alla ewe mwana, Akuapo Maulana, Enenda naye Madina, Na wote wake waladi
49. Umsalimu eziye, Kwamba atatwaa yeye, Au mtu atakaye, Ushike ndiya urudi
50. Atakalo mfanyie, Wala simzuilie, Na kadiri amriye, Ndiyo itayokufidi
51. Umtie mahabani, Dhahiri na faraghani, Siwe na kitu moyoni, Roho yako isafidi
52. Na pindi umpendapo, Hapana budi na pepo, Utakwenda kaa papo, Pa babuye Muhammadi
53. Pindi usipompenda, Kesho huna la kutenda, Ndia utakayokwenda, Na Majusi na Yahudi
54. Muawia kamaliza, Yazidi asikiliza, Maneno kamrudiza, Manenoyo hayarudi
55. Yote uloniusia, Baba nimeyasikia, Si mwenye kuyawatia, Yote uliyoradidi,
56. Baada hayo nakuli, Isipate siku mbili, Akapatwa na ajali, Mauti yakambidi
57. Alipokwisha toweka, Yazidi kafadhaika, Kasimama akazika, Na kuchawanya nakidi
58. Akaliweka tanzia, La babaye Muawiya, Na vitu vikangamia, Vingi visivyo idadi
59. Akavihasiri vitu, Akawakusanya watu, Si siku mbili si tatu, Ikawa hiyo abadi
60. Akawatinda ghanamu, Na wingi wa bahayumu, Na zakula tamtamu, Na sharubati waridi
61. Matanga akiondoa, Nguo mbaya kazivua, Akavaa za uluwa, Nzuri za kusafidi
62. Akajivika na taji, Lawaka kama siraji, Na wengi watundamaji, Majaria na abidi
63. Akajivika libasi, Hudhuri na sandusi, Zawaka kama shamsi, Rihi ambari na udi
64. Akavaa burukhuti, Akakikalia kiti, Cha lulu na yakuuti, Chema cha zabarijudi
65. Akatungika johari, Na thoria mnawari, Vyandarua vya hariri, Siriri na l'wasidi
66. Sayo yakisha tendeka, Akakutubu nyaraka, Kula nti kapeleka, Akamkua junudi
67. Akaweta asibaki, Kula panapo muluki, Wakutane Dimishiki, Wamkiri usayidi
68. Barua zisibakie, Na kula asikiaye, Akaja na kaumuye, Na nyingi mno zawadi
69. Wakaitika amri, Jamii ya ansari, Wakakutana jifiri, Kuja kwake makusudi
70. Walipokwenda timia, Yazidi akawambia, Jambo alilowetia, Ya maishara junudi
71. Mimi nimetamalaki, Aridhi ya Dimishiki, Na jamii ya muluki, Mje kwangu musujudi
72. Mimi ndimi sultani, Niwetapo nitikani, Pasiwe na ushindani, Wala mwenye kukaidi
73. Mimi ni wenu amiri, Ambaye amenikiri, Tamjaza utajiri, Na kula siku nizidi
74. Ambaye amekubali, Tamjaza mangi mali, Yeye na wake ayali, Na wakewe na abidi
75. Ambaye hakuridhika, Kuwa mimi mamlika, Rasiye itaondoka, Kwa saifi ya hadidi
76. Tamkata yake rasi, Nimwangue kama sisi, Semani hima upesi, Nipate kuyafanidi
77. Jamii wakabaini, Wewe ndiwe sultani, Akubishaye nnani?, Hapo mwenye kukaidi
78. Wewe ndiwe bwana wetu, Uliyemiliki watu, Wala hazumbuki mtu, Kuja kwako na taadi
79. Na ambaye atakuja, Kwa harubu au huja, Shauri letu ni moja, Tambua tutakufidi
80. Haya wakishatamka, Yazidi kafurahika, Akawapa twika twika, Jeshi yote ikarudi
81. Kabaki yeye pekee, Na mjini kaumuye, Akampa ampaye, Wengine akawazidi
82. Akaweka mawaziri, Na aribabu amri, Akadirika hamri, Barazani ikabidi
83. Kinyang'anya masikini, Wenye kupita ndiani, Na wajao barazani, Wengine kiwahusudi
84. Kawakataa tariki, Sipitike Dimishiki, Watu wakataharuki, Kwa mambo yake Yazidi
85. Akaitenda jeuri, Kubwa isiyo kadiri, Raia na mawaziri, Wote wakasitajidi
86. Na kula mtu ambaye, Alipendwa na babaye, Yeye kawa hasimuye, Akija kimtaridi
87. Ali akiwasukuma, Wenye haya na huruma, Akakithiri dhuluma, Na kila siku kuzidi
88. Akautupa wosia, Wa babaye Muawiya, Ukazidi utaghia, Mno akatamaridi
89. Na Maulana Huseni, Asimpe nufaani, Wala kwenda barazani, Asipende mshahidi
90. Na mtu amtajaye, Alosimama mbeleye, Yuamkata nyamaye, Na kumpiga jalidi
91. Kamzia Maulana, Asitake kumuona, Pasiwe neno kunena, Ila la kumuhusudi
92. Akashirabu khamri, Na jilasi ikajiri, Na nyama ya hinziri, Akila na kurajidi
93. Kuonakwe Maulana, Vitendo vyake laana, Na babaye alonena, Yote hayakusuudi
94. Kuonakwe tafauti, Kondoka suu wakati, Kenda kwa wake ukhti, Ili kwenda muradidi
95. Akifika akalia, Nduguye akangalia, Sakina akamwambia, Waliza nini Sayyidi?
96. Akatamka Sakina, Una nini Maulana, Ambalo ni kubwa sana, Jambo lililokuzidi?
97. Kilio chako Huseni, Kitawaliza majini, Na malaika mbinguni, Na baharini swayyidi
98. Na nyama wote barani, Watangia kilioni, Hata maji baharini, Pia yatatujamidi
99. Usilie Maulana, Na uliyo nayo nena, Kwa amriye Rabana, Neo lako halirudi
100. Huseni akamwambia, Ewe Sakina sikia, Yaliyonipa kulia, Ni mambo yake Huseni
101. Ametukiwa na siye, Hapendi atusikie, Ni kheri tumuukiye, Si naye tuwe baidi
102. Sikia ewe Sakina, Twenende zetu Madina, Hapa sipataki tena, Hata kwa saa wahidi
103. Twende zetu Yathiribu, Kunako nyumba za Babu, Tumwondokee harabu, Atakayetuhusudi
104. Ni hayo maneno yangu, Nitakayo roho yangu, Wanenaje nduu yangu, Katika suu mradi?
105. Kamaliza Maulana, Akatamka Sakina, Sayyidi unayonena, Mimi ni bora zaidi
106. Huyu ametakabari, Na kumuasi Jabari, Na kushirabu khamri, Na watu kuwajalidi
107. Na babaye Muawiya, Pia alomuusia, Yote hayakutimia, Hata kwa jambo wahidi
108. Afadhali twende zetu, Kunako majumba yetu, Kwani Yazidi si kitu, Amekwisha tamaridi
109. Walakini kamjibu, Umuarifu kitabu, Nenda zangu Yathiribu, Wala huku sitarudi
110. Mpelekee khabari, Ya kumuaga safari, Tusikize madhukuri, Atakayo kuradidi
111. Kwani tutokapo Kofu, Tusipo kumuarifu, Atasema tuna khofu, Haya atayafanidi
112. Sakina kwisha kalimu, Mara Huseni kakumu, Akaagiza kalamu, Na lauhi na midadi
113. Akawandika waraka, Tasihili kwa kikaka, Ila muhibu pulika, Sikia ewe Yazidi
114. Rohoni nimeazimu, Kwenda Madina kukimu, Au kunako Haramu, Hakae nitaabidi
115. Napenda kwenenda Maka, Au Madina hifika, Hatake pa kuniweka, Katika mbili biladi
116. Nami siwezi safiri, Ila unipe amri, Na ambapo hukukiri, Takaa nitabaradi
117. Nipe rukhusa ya kwenda, Au niambie Vunda, Kula utakalopenda, Siwezi kukukaidi
118. Kashilia Maulana, Kaukunda iyo hina, Kamsalimu kijana, Kenda nao kwa Yazidi
119. Ikiwasili barua, Yazidi kaufungua, Jamii makutubua, Yote akayaadidi
120. Hata akisha usoma, Kaupindua kwa nyuma, Aketa kalamu hima, Kumuarifu Sayyidi
121. Maneno akabaini, Akamba ewe Huseni, Kwangu wataka idhini, Ndiyo uliyoradidi
122. Tumia khiari wewe, Hayo ni yako mwenyewe, Mimi sina haja nawe, Sipendi kukushahidi
123. Ukenenda sikutaki, Wala hu wangu rafiki, Na uwapo Dimishiki, Sikupi hata nakidi
124. Sipendi kushuhudia, Kwamba Rabi ajalia, Kuigauza dunia, Ikawa zabarijudi
125. Ningewapa insani, Watu wote duniani, Wewe ukaitamani, Ujapo kujitahidi
126. Kwangu hupati mahaba, Wala kula ukashiba, Nakuwazia msiba, Na 'ladhabu shadidi
127. Na Maka ukiwasili, Majumba yangu ya mali, Nenda kayakae mbali, Usende ukarajidi
128. Sende ukapanda ngazi, Majumba yangu ya ezi, Akimaa matongozi, Waraka kaujadili
129. Kamsalimu risali, Kenda nao tasihili, Hata alipowasili, Kwa Maulana sayyidi
130. Kausoma kauona, Kenda nao kwa Sakina, Akamba tazama mwana, Maneno yake Yazidi
131. Amesema ni khiari, Kukaa na kusafiri, Wanambiaje shauri?, Mwanamke karadidi
132. Mwanamke kadhukuri, Hapana tena usiri, Na watengeze bairi, Wa kuja panda waladi
133. Hima twandame tariki, Tuitoke Dimishiki, Huseni akasabiki, Kamzaini jawadi
134. Twika kazitengeneza, Ngamia akawatwisa, Kula ambaye apasa, Waungwana na abidi
135. Wakalekea safari, Wakamuomba Jabari, Wakaikabili bari, Yenye nondo na asadi
136. Rabi akawanusuru, Kwenda kheri wa sururu, Pasiwe la kuwadhuru, Dhuria za Muhammadi
137. Kawanusuru Rabuka, Kwa maafa na shabuka, Nondo wote na majoka, Wakuja wakisuudi
138. Jamii watu wazima, Hata watoto yatima, Wakiwasili salama, Badari 'lmakusudi
139. Walipofika Madina, Watu walipowaona, Wakafurahika sana, Furaha kubwa shadidi
140. Wakatelea rikabu, Wakangia Yathiribu, Jamii ya Waarabu, Wakamlaki sayyidi
141. Akafikilia dari, Ya babaye Haidari, Ndiyo aliyokhiari, Kuwatia auladi
142. Baada ya kuwasili, Akenenda tasihili, Kaburini kwa rasuli, Kumzuru wake jadi
143. Kimaa yake zuari, Kaburi iketa nuri, Hata juu ya kamari, Nuru hiyo ikazidi
144. Kwishakwe zuru nabia, Roho ikafurahia, Nyumbani akarejea, Nyumbani kwake kurudi
145. Ali yeye na nduguye, Alokwenda zuru naye, Mtakapo ismuye, Jina ketwa Muhammadi
146. Ni mwana wa Shekhe Ali, Kazawa nyumba ya pili, Naye katika kitali, Kama umeme na radi
147. Jamii zote taifa, Wamwita bunu Khanifa, Wala hafikiri kufa, Atokeapo jihadi
148. Ali simba maalumu, Katika nchi ya Shamu, Ambapo ataranamu, Utamboni akabidi
149. Hakiwa akizumbuka, Awezaye kumfika, Wote wenye kutajika, Kwake wakasitajidi
150. Basi wakarejeea, Na Maulana pamoya, Nyumbani wakenda ngia, Kwa baba yao asadi
151. Na wote 'lAnsari, Na jamii Muhajiri, Pasibakie saghiri, Msifurahi fuadi
152. Wale wakamkirimu, Kwa zakula tamtamu, Wakamuweka makamu, Na pendo likashitadi
153. Jamii wakalingana, Kumwambia Maulana, Kula utakalonena, Kwani ni yako biladi
154. Sisitahi bwana wetu, Roho ikataka kitu, Nafasi na mali zetu, Ni yako wewe Sayyidi
155. Sote tumefurahika, Madina unavyofika, Hatupendi kuondoka, Katika zetu fuadi
156. Basi wakasimulia, Hata kiza kikangia, Wakenenda zao pia, Pasibakie wahidi
157. Ila ni wao theneni, Wao wawili nyumbani, Akatamka Huseni, Kamba Ewe Muhammadi
158. Sababu ya kuja zangu, Ni ghadhabu na matungu, Ya hayo asi wa Mungu, Abdullahi Yazidi
159. Alipokufa babaye, Hamtazama haliye, Sikuweza kaa naye, Kwa jeuri na taadi
160. Yote aliyousiwa, Hata moja halikuwa, Aliposhika ulua, Kangia na kufisidi
161. Nami kanizia sana, Asitake kuniona, Haona sina maana, Kukaa yake biladi
162. Haradhiwa kuondoka, Kuja Madina na Maka, Muhammadi katamka, Ahsanta Sayyidi
163. Hasanta bun Ali, Kuja zako afadhali, Mtu kukaa muhali, Wala asipo mradi
164. Miji yao maghasiki, 'lKofu na Dimishiki, kukaa wewe ni dhiki, mashaka hayana budi
165. Na Yazidi bardhuli, Kuwania udawali, Wala si yao asili, Si ya jadi na jududi
166. Huu ulua ni wetu, Wa baba na babu zetu, Wala hazumbuki mtu, Ambaye ametuzidi
167. Wenyewe tukiutaka, Twenenda tukaushika, Na afanyapo dhihaka, Tukamuonya hadidi
168. Na kwamba hatuutaki, Ya nini kwenda jidhiki?, Kheri kufuata haki, Ya Mola wetu Wadudi
169. Nawe sasa Maulana, Keleti hapa Madina, Kula utakalo nena, Neno lako halirudi
170. Na utakapo Makati, Enenda zako kaketi, Na kwamba wataka nti, Takuwali sina budi
171. Utakapo ukhalifa, Sema niwete taifa, Ahadi ni mimi kufa, Ndipo uone taadi
172. Takawali hivi sasa, Utamalaki kabisa, Pasiwe mtenda kisa, Ukate utabaridi
173. Huseni kamrudia, Ya 'lakhi nisikia, Hayo sikupendelea, Kutamalaki junudi
174. Roho yangu naazimu, Nenende hasitakimu, Maka kunako Haramu, Nimuabudu Wadudi
175. Niabudu Subhana, Kwa usiku na mchana, Nitazame kwa Rabana, Atakalo kunibidi
176. Ezi sina haja nayo, Haimo katika moyo, Wakisha kusema hayo, Wakenda wakarajidi
177. Akaketi Maulana, Siku ashara Madina, Khatima wakandamana, Nduguye akamuwadi
178. Maulana akatoka, Akakusudia Maka, Siku haba zikifika, Akawasili biladi
179. Alipokwisha wasili, Wakatoka kabaili, Wanawake na rijali, Kwenda mlaki Sayyidi
180. Katoka bun Zuberi, Abdalla mashihuri, Pasibakie saghiri, Waungwana na abidi
181. Na Abdalla yuani, Ni ndugu yake Huseni, Wa katika ridhaani, Zamani wali wabidi
182. Ni nduguye hana huja, Walinyonya ziwa moja, Akenda akimngoja, Bara katika 'lwadi
183. Na Abdalla pulika, Zamani hizo hakika, Ndiye khalifa wa Maka, Mtamalaki junudi
184. Wakamlaki Huseni, Na ndugu yake Sakini, Wakamtia mjini, Na furaha za fuadi
185. Abdalla akanena, Twende kwangu Maulana, Kwenda pengine hapana, Kwangu ni bora zaidi
186. Kuwasilikwe fahamu, Ikafanyiwa karamu, Ya hubuzi na lahamu, Na vitu vya kusafidi
187. Twenende kwangu nyumbani, Ukae uje makini, Akatikia Huseni, Asiweze kumrudi
188. Kasimama Abdalla, Akafanyiza vyakula, Na wengine kabaila, Wote wakajitahidi
189. Kula mtu katamani, Kumkirimu Huseni, Vitu launi launi, Vya moto na vya baridi
190. Karamu zikafanyiwa, Na kuliwa zikasazwa, Hata kukangia kiza, Usiku ukasawidi
191. Watu wote barazani, Wakarejea nyumbani, Kabaki yeye Huseni, Na mtoto wa asadi
192. Huseni akatamka, Ya Abdalla pulika, Kisa cha kungia Maka, Na Dimishiki kurudi
193. Ni ibnu Muawia, Mambo alonifanyia, Uasi na utaghia, Jeuri na uhasidi
194. Amekithiri jeuri, Uasi na ujabari, Si mwenye kutafakari, Na kwamba yuko Wadudi
195. Amekithiri uasi, Kupita hao Majusi, Nilipoona jinsi, Hushika ndia harudi
196. Babaye akifariki, Akaushika muluki, Yote hakuyasadiki, Aliyokumradidi
197. Yote alomuusia, Jamii hakuridhia, Sikuweza vumilia, Mji wake kurakidi
198. Nimekuja zangu kwetu, Kuliko majumba yetu, Niabudu Mola wetu, Rakaa na kusujudi
199. Abdalla akanena, Hasanta Maulana, Yamenipendeza sana, Kuja Maka kukaidi
200. Kama wewe kuja Maka, Utakalo ni kutaka, Inshalla litatendeka, Kula utaloradidi
201. Ulitakalo twambie, Hapana alibishaye, Twajua bwana ni wewe, Tangu jadi na jududi
202. Utakapo khalafati, Sasa takitoa kiti, Utamalaki Makati, Na jamii ya biladi
203. Nikuwali ukhalifa, Wa babuyo Musitafa, Na mweye kutaka kufa, Ni mwenye kukukayidi
204. Na asemaye hataki, Sharuti tamuhiliki, Na Yazidi Dimishiki, Tapanda mimi jawadi
205. Nitukue farisani, Wazoefu wa vitani, Kama simba ghadhibani, Walio kama asadi
206. Dimishiki nirikabu, Niuonyeshe barabu, Hadi ni kutaadabu, Yeye na wake juhudi
207. Ningie na bildiye, Nitafute asemaye, Nimuondoshe rasiye, Kula aliye hasidi
208. Pasibaki kabaili, Ambaye hatakubali, Huseni kamba ni kweli, Yote unayoradidi
209. Walakini ndugu yangu, Siupendi ulimwengu, Taka abudu Muungu, Ni huu wangu mradi
210. Sitaki usultani, Taka niwe masikini, Wala hayo sitamani, Kwenda wapiga jihadi
211. Nataka niketi Maka, Nimuabudu Rabuka, Wala sipendi kwondoka, Hata ifike ahadi
212. Hapano Maka sondoki, Na ukhalifa sitaki, Kisha sayo kunatiki, Wakenda wakarakidi
213. Baada hayo yuani, Kaketi Make Huseni, Wote walio mjini, Kupenda wakamzidi
214. Wakampenda sikia, Yeye na wake dhuria, Kula siku kuzidia, Mahaba mangi shadidi
215. Wote wakamjamili, Yeye na wake tifili, Na wake namarijali, Wakubwa na auladi
216. Wasitambike nufaa, Wala nguo za kuvaa, Wala nyumba ya kukaa, Tena akataabadi
217. Roho akaituliza, Akaabudu Aziza, Hata usiku wa kiza, Haramuni kisujudi
218. Kaabudu Mola pweke, Kwa kusafi moyo wake, Yeye na msala wake, Pasiwe na kurakidi
219. Akakithiri saumu, Na yake masitakimu, Yali ndani Haramu, Ikwa hiyo abadi
220. Asitake neno tena, Ila dini ya Rabana, Baada sayo nanena, Mambo baidi baidi
221. Nataka niyakutubu, Niyaweke babubabu, Nisije nikaharibu, Haja hambiwa kusudi
222. Nataka nielekeze, Kula kwa sifaze, Na utenzi upendeze, Nilio kuufanidi
223. Baada kupita hayo, Maneno niwambiayo, Sasa ni kutuza moyo, Niwakhubiri Yazidi
224. Kwondoka kwake Huseni, Kashika usultani, Kamiliki buldani, Kwa nguvu na uhasidi
225. Akawadhiki wenziwe, Wageni raiawe, Jamii wasitongoe, Pasi mwenye kuradidi
226. Watu akiwadhulumu, Na kula mna haramu, Na nguzo za Islamu, Zote asitaamidi
227. Wangine kiwadhurubu, Wala pasipo sababu, Akawa mnoa harabu, Kushinda hao Yahudi
228. Ndia zikafungamana, Pasiwe safari tena, Na ambaye amuona, Humwegema kwa hadidi
229. Kiwapoka watu mali, Wangine kiwakutuli, Ndia zote kazidhili, Za karibu na baidi
230. Pasiwe asafririye, Ala mtu enendaye, Kwa vitendo na haliye, Awatendavyo junudi
231. Kisha sayo nitamke, Katika kaumu yake, Mli mtu jina lake, Akitwa bun Ziadi
232. Jinale Abidallahi, Ali adui asahi, Dhuluma na ukabihi, Apita huyo Yazidi
233. Akichecha watu damu, Kwa jeuri na dhulumu, Hali akisha karimu, Ali jabari anidi
234. Yazidi kumuonakwe, Jeuri na hali yakwe, Kampenda yakwe, Pendo lisilo idadi
235. Kawa mtu maarufu, Tena akamsharifu, Akenda muweka Kofu, Akampa na biladi
236. Kampa katamalaki, Tangu Kofu na Iraki, Neno ambalo hataki, Pasiwe mwinua yadi
237. Akenda akaishika, Kakusa watu mashaka, Viumbe wakadhilika, Ikiwa kheri abidi
238. Jamii watu wa Kofu, Roho zikangia khofu, Kwa mambo yake dhaifu, Aliyo kutaahidi
239. Pasiwe mtu mzima, Wala naye heshima, Na mabaye uasema, Mara yamkaidi
240. Hunyang'anywa mali zao, Huuliwa wana wao, Hutwaliwa nyumba zao, Hali ya nguvu shadidi
241. Mali zao hutwaliwa, Na wao wakauawa, Na wasemalo haliwa, Wa sawa na 'kurudi
242. Wakakeleti mjini, Wakawa kama manyani, Mashekhe na madiwani, Nyuso zikawa sawidi
243. Pasiwe mwenye shauri, Wala anye amri, Kwa kushitadi jeuri, Akaptia Namrudi
244. Wa Kofu wakiyatunza, Dhuluma na miujiza, Wakamba hatutawaza, Dhuluma inatuzidi
245. Wakakutana kabili, Wote wazele wazele, Na mashaibu wa kale, Wasizo na 'lmuridi
246. Mashekhe na madiwani, Wakangia faraghani, Wakauzana yakini, Mwaionaje biladi?
247. Mwaonaje wenye nti, Na hakimu mwenye kiti, Tutaweza kuiketi, 'lKofu tukakhalidi?
248. Mwaonaje wenye kaya, Na huyo mwenye ulaya, Na mambo yake ni haya, Atutendayo abadi?
249. Kwa jamii wamwambie, Bunu Ziadi mamboye, Hapana ayawezaye, Yanatuchoma fuadi
250. Hatuwezi siku moja, Kuvumilia miuja, Kupigwa pasipo huja, Kama tunao jihadi
251. Kupigwa kama watoto, Kwa bakora na makoto, Haya ni mambo mazito, Hatuwenepo abadi
252. Kupigwa tukiuawa, Na mali yakitwaliwa, Wala hakutaadiwa, Si kwamba tuna taadi
253. Katungia kwa batili, Akatunyang'anya mali, Kuno akatukutuli, Mambo yanatupa hadi
254. Shauri na tufanyeni, Tuli hapa faraghani, Wangine wakabaini, Walio wana mradi
255. Wangine wakatamka, Yote yaliyotungika, Ya adhabu na mashaka, Tunayataka kusudi
256. Maana tuna yakini, Ezi na usultani, Si wake huyu laini, Wala babaye Ziadi
257. Wala si ya Muawia, Hawa wanajitwalia, Kutamalaki raia, Kampasaje Yazidi?
258. Sisi tu makabaili, Kutoka majitu mbali, Yakaja na ufedhuli, Katika zetu biladi
259. Wakatenda watakayo, Nasi tukaona ndiyo, Twabasa ni kama hayo, Hata yajapo tuzidi
260. Ezi si ya Marijani, Babuye huyo laini, Wala si ya Sufiyani, Babuye huyo Yazidi
261. Twayajua kwa makini, Ezi mwenyewe Huseni, Kwa babu yake Amini, Na baba yake Asadi
262. Twayajua maarufu, Jamii tulio Kofu, Kwondoka kwake Sharifu, Ezi ya wake waladi