• Anza
  • Iliyopita
  • 2 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 2884 / Pakua: 2723
Kiwango Kiwango Kiwango
MAISHA YA IMAM HADI (A.S)

MAISHA YA IMAM HADI (A.S)

Mwandishi:
Swahili

MAISHA YA IMAM HADI (A.S)

UKWELI KATIKA MINYORORO (IMAMU ALI NAQI AL HADI (A.S)

KIMEANDIKWA NA: MAULANA SAYYID ALI NAQI SAHEB

KIMETAFSIRIWA NA: MAALIM DHIKIRI OMARI KIONDO

KIMETOLEWA WAVUNI NA TIMU YA AHLUL BAYT DIGITAL ISLAMIC LIBRARY PROJECT

IMAMU KATIKA QUR'AN NA HADITHI

Anasema Mwenyezi Mungu: Ewe mwanadamu! ikumbuke siku tutakapowaita kila watu pamoja na imamu wao; basi atakayepewa kitabu chake cha amali kwa mkono wa kulia, hao watavisoma vitabu vyao kwa furaha. (Quran: 17:71)

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) Amesema:

"Ye yote yule afaye pasi na kumjua Imamu wa zama zake, atakuwa kafa kifo cha ujinga ."

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) Amesema:

"Hao (Ulul Amr watajwao katika Qur'ani 4:59) ni Makhalifa wangu na Maimamu wa Waislamu baada yangu. Wa kwanza ni Ali, kisha ni Hassan, kisha ni Husayn, kisha ni Ali bin Husayn, kisha ni Muhammad bin Ali, kisha ni Jaafar bin Muhammad, kisha ni Musa bin Jaafar, kisha ni Ali bin Musa, kisha ni Muhammad bin Ali, kisha ni Ali bin Muhammad, kisha ni Hassan bin Ali, kisha ni Muhammad bin Hassan (Mahdi).. ."

("KifayatuI Athar" na "Rawdhatul Ahbab", vya Hafidh Jamaluddin Muhaddith).

UTANGULUZI

Katika wakati huu wa machafuko kunapokuweko hatari nyingi za kila aina kwa amani yetu, tunahisi kwamba maisha ya hii minara ya Uchamungu na hekima takatifu yatazisaidia akili zetu zilizojaa mataizo. Hapa tunayaelezea maisha ya Imamu wa kumi, Imamu Ali an-Naqi(a.s) .

JINA NA NASABA YAKE

Jina lake ni Ali, Kunyat (jina la utoto) wake ni Abul Hasan, na jina lake la heshima ni Naqi (Mtakatifu). Kwa sababu Imamu Ali bin Abi Talib(a.s) na Imamu Ali Ridha(a.s) nao walikuwa na Kunyat ya Abul Hasan, Imamu Ali Naqi(a.s) anaitwa Abul Hasan wa Tatu. Mama yake ni Bibi Samanah Khatuun.

KUZALIWA NA KULELEWA KWAKE

Imamu Ali Naqi(a.s) alizaliwa mnamo tarehe 5 Rajab, mwaka wa 214 Hijiriya mjini Madina. Aliishi na baba yake kwa muda wa miaka sita tu na kasha ilimbidi Imamu Muhammad Taqi(a.s) kusafiri kwenda Iraq na alifariki huko mnamo tarehe 29 Dhul Qada mwaka 220 Hijiriya. Na kisha Imamu Ali Naqi(a.s) ilimbidi achukue madaraka wa Uimamu. Katika tukio la namna hiyo ni wapi basi ambako tunaweza kupata chanzo cha upeo wa kisomo chake na Uchamungu wake kama si Neema ya Mwenyezi Mungu tu?

MABADILIKO YA KISIASA

Uimamu wa Imamu Ali Naqi(a.s) ulianza katika zama za utawala wa mfalme wa ukoo wa Bani Abbas aitwaye Mu'tasim ambaye alifariki mnamo mwaka 228 Hijiriya na alirithiwa na mfalme Wasiq Billah. Wasiq alifariki mnamo mwaka 236 Hijiriya na alirithiwa na mfalme mshari na mkatili zaidi wa ukoo wa Bani Abbas aitwaye Al-Muttawakil ambaye alifariki mnamo mwaka wa 250 Hijiriya. Baada ya hapo ulifuatia utawala mfupi wa Muntasir Billah ambaye naye alifariki baada ya miezi sita na akarithiwa na Musta'in Billah, lakini mnamo mwaka wa 253 hijirya alipoteza maisha yake pamoja na kiti chake cha enzi na alirithiwa na Mu'tazz Billah ambaye alikuwa mfalme wa mwisho wa zama za Imamu Ali Naqi(a.s) .

SHIDA NA MATESO

Kwa ajili ya matatizo ya kiutawala yaliyokuwa yakisababishwa na vita na kuhamishiwa Baghdad mji mkuu na pia kwa kuwa umri wa Imamu ulikuwa mdogo, mfalme Mutassim hakumsumbua Imamu(a.s) . Baada ya Mutasim, Wasiq naye alimnyamazia Imamu(a.s) . Lakini mara tu Mutawakkil alipokalia kiti cha utawala ulianza wakati mgumu sana kwa Imamu(a.s) . Mutawakkil alikuwa nduguye Wasiq na ni mwanawe Mu'tasim naye alikuwa adui mkubwa wa Nyumba ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) .

Katika muda wa miaka kumi na sita tangu Imam Ali Naqi(a.s) atwae Uimamu, sifa yake ilienea kote katika ulimwengu wa Kiislamu. Watu walikuwa wakimiminika toka pande zote kujifunza lolote lile waliloweza kutoka kwa wakili huyu wa Hekima ya Mwenyezi Mungu (Imamu a.s). Ilikuwa imepita miaka minne tu ya utawala wa Mutawakkil wakati gavana wake wa Madina alipoanza kumsumbua Imamu(a.s) . Alianza kwa kumpa usumbufu wa kila aina na halafu akaanza kumwandikia Mutawakkil akizua kila aina ya uongo juu ya Imamu(a.s) kama walivyofanya wafalme wengine waliomtangulia. Kwa mfano, alimwandikia barua Mutawakkil akisema kuwa Imamu(a.s) amekusanya watu wengi na angeweza kuuvamia utawala wake wakati wowote ule apendapo (Imamu(a.s) kufanya hivyo.

Imamu(a.s) alijulishwa hila hiyo mapema. Hivyo mara moja alimwandikia Mutawakkil akiifichua hila hiyo. Mutawakkil alichukua hatua za kuisuluhishi wa kiserkali alimfukuza kazi gavana huyo wa Madina. Lakini alipeleka kikundi cha jeshi chini ya Uongozi wa Yahya bin Harsimmah kumwomba kirafiki Imamu(a.s) kuutembelea mji mkuu wa Sammarah kwa muda wa siku chache hivi. Imamu(a.s) alijua wazi maana ya ukaribisho huo lakini hakuweza kukataa kwani ukaribisho wenyewe ulionyesha kuwa ni wa kirafiki na vile vile Imamu(a.s) alijua kuwa angelilazimishwa kama akikataa. Hivyo aliondoka Madina (kwenda Sammarah) kwa kusitasita.

Barua ya Mutawakkil kwa Imamu(a.s) ilionyesha heshima yote astahiliyo na kikundi cha jeshi kilipelekwa chini ya kisindikizo cha hila. lakini mara tu Imamu(a.s) alipofika Sammarah, badala ya Mutawakkil kutoka yeye mwenyewe na kumkaribisha Imamu(a.s) au japo kumkaribisha kwenye ikulu yake tu, aliamrisha Imamu(a.s) apelekwe akakae kwenye "Khan-us-Sa'alik" (nyumba ya maskini) iliyokuweko nje ya mji. Ingawa watu wa ukoo wa Mtukufu Mtume[s.a.w.w] walikuwa kila mara tayari kuishi na maskini, madhumuni ya Mutawakkil ni kutaka kumfedhehesha Imamu[a.s] . Imamu(a.s) alikaa huko kwa muda wa siku tatu na baadaye Mutawakkil alimfunga katika nyumba ya mtu moja aitwaye Zarraqi na aliamrisha watu wasiruhusiwe kuonana naye.

Kama vile Uchamungu wa Imamu Musa Kazim(a.s) ulivyoathiri walinzi wa jela alimofungiwa, Zarraqi nae pia katika muda mfupi sana alielewa kuwa mfungwa wake alikuwa mtu apasikaye kuheshimiwa badala ya kumfedhehesha na hivyo alibadilisha tabia yake kwa Imamu[a.s] . Lakini mara tu Mutawakkil alipojua habari hizo, aliuhamishia ulinzi wa Imamu(a.s) kwa mtu mwingine asiyekuwa na huruma naye na ambaye Imamu(a.s) aliishi chini ya ulinzi wake kwa muda wa miaka kumi na miwili. Alikuwa akipitisha siku na mausiku katika sala na ibada. Alifunga mchana na kuswali wakati wa usiku.

Mwili wake ulikuwa jela lakini sifa yake nzuri ilienea Iraq nzima. Kila nyumba ilikuwa ikizungumzia Uchamungu wa Imamu(a.s) na ukatili wa Mutawakkil jambo ambalo lilimfanya mdhalimu huyu achukiwe na raia wake.

Wakati ulifika ambapo Fath-i-Khaqan ambaye licha ya kuwa mfuasi mkuu wa ukoo wa Mtume[s.a.w.w] aliteuliwa kuwa waziri mkuu kwa sababu ya uwezo wake wa pekee. Kwa ombi Ia Ibn Khaqan, Mutawakkil alikipunguza kifungo cha jela kwa Imamu(a.s) na badala yake kikawa kizuizi cha kuwekewa mipaka na alimpa kiwanja cha kujenga nyumba yake mwenyewe chini ya kutotoka mjini Sammarah.

Kuridhika kibinafsi kwa Imamu(a.s) kwa wakati huo kulikuwa mfano wa pekee. Ingawaje alikuwa akiishi mjini, Imamu(a.s) hakuonyesha kutaka jambo loIote Ia raha wala hakumwomba Mutawwakil ampunguzie taabu alizomuwekea. Maisha ya kiibada na uchamungu aliyokuwa akiyaendesha katika jela yaIiendele. Hata hivyo hakuachwa aendelee na mambo yake kwa raha mustarehe: kila mara nyumba yake ilikuwa ikipekuliwa ili kutafuta silaha au barua ambazo zingeweza kuonyesha nia ya Imamu(a.s) kutaka kuipinga serikali. Juu ya hayo siku moja alialikwa kwenye baraza la mfalme ambao wafuasi wema wa mfalme walikuwa wakishughulika kunywa mvinyo na pombe. Mjinga mmoja aliyekosa adabu alithubutu hata kumpa lmamu(a.s) kikombe cha mvinyo. MIinzi wa uadilifu, Uchamungu na sheria (za Islamu) alichukiziwa sana. Lakini kwa utulivu mkubwa alijibu, "Samahani, mwili wangu na damu yangu, na ile ya baba zangu havikuwahi kunajisiwa wa kitu hiki." Kama pangelikuwepo bado wazo la adabu katika kichwa cha mdhalimu huyu alingeliacha kabisa kuendelea na utovu wake wa adabu kwa lmamu[a.s] . Lakini bila aibu alisema, "Haya basi kama huwezi kufanya hivi (yaani kunywa mvinyo), basi tuimbie wimbo wo wote ule." Imamu(a.s) alijibu, "Hata hivyo sijui". Halafu alishikilia kuwa Imamu(a.s) asome aya za Qur'ani Tukufu. Hapo Imamu(a.s) aliona kuwa sasa wakati umefika wa kuigeuzia meza usoni mwa mnafiki huyo. Kwa sauti ya kuchoma moyo alisoma aya chache za Qur'ani Tukufu zilizojaa mawazo mazuri ya uchamungu na udanganyifu wa raha za ulimwengu aliwakumbusha mwisho wa wale waliojitosa katikati ya raha hizo wakiwa wamemsahau kabisa Muumba wao. Mara moja mawazo haya safi yaliyotoka kinywani mwa Imamu(a.s) yaliyojaa Uchamungu yalitoa matokeo yake. Wote wale waliokuwa wakifurahi (tafsiri hiyo walianza kulia kwa uchungu na Mutawakkil mwenyewe alitokwa na machozi. Vikombe vya mvinyo viliwadondoka kutoka mikononi mwao na wote waljiona kana kwamba wamo kwenye ndoto. Mara tu waliporudi katika hali ya kawaida, Mutawakkil alimwambia Imamu(a.s) arudi nyumbani kwake. (Soma nyongeza ya Kwanza).

Mshituko mwingine ambao ilibidi Imamu auvumilie ni Mutawakkil kupiga marufuku kwa mtu yeyote kwenda kuhiji huko Najaf na Karbala na kutishia kuwa wale watakaovunja sheria hiyo watapata adhabu ya kifo. Hakuishia hapo. Aliamrisha kuvunja kwa makaburi ya Najaf na Karbala na kulimwa kwa ardhi yote izungukayo kaburi la Imamu Husain[a.s] . Haikuwezekana kwa wafanya ibada katika kaburi hilo la Imamu Husain(a.s) waonyeshe unyonge wowote ule wa kutokwenda kulizuru kaburi hilo. Matokeo yake ni kwamba damu ya watu wengine wengi wasiokuwa na hatia ilimwagika. Kwa kila mmoja wa Mashahidi hao, moyo wa Imamu(a.s) ulihisi kama vile mtu ahisivyo kwa mwili na damu yake.

lmamu(a.s) alikuwa akiishi katika hali ambayo haikumpa nafasi yoyote ya kuwapelekea maelekezo watu hawa... Mambo hayo yaliendelea mpaka alipokufa Mutawakkil.

Mfano mwingine wa kutokuwa na haya kwa Mutawakkil ni kwamba katika baraza lake ilifanywa miigizo ya kumdhihaki Hadhrat Ali bin Abi Talib(a.s) ambayo hata mtoto wa Mutawakkil alishindwa kuinyamazia miigizo hii na kuona ikiendelea.

AIimwambia baba yake, "Unaweza kusema lolote lile lakini unaposema kuwa Ali alikuwa wa ukoo wa kabila yako usiwaruhusu hawa wachekeshaji waovu kutumia lugha ya matusi kwake". Badala ya Mutawakkil kuwa mpole alimtukana mwanawe na akatunga mashairi yalivokuwa na maneno ya matusi mabaya kwa mwanawe huyo na mama yake na akawapa wachekeshaji wayaimbe ili kuwafurahisha wasikilizaji.

Msiba mwingine wa kuhuzunisha ni ile shahada ya Bwana Ibn-Us-Sakit Baghdadi aliyekuwa mtaalam wa sarufi na elimu ya lugha katika zama hizo. Mutawakkil alimteua Bwana huyu kuwa mwalimu wa watoto wake. Siku moja Mutawakkil alimwuliza "Unawapenda watoto wangu zaidi au Hasan na Husain", "Ibn-Us-Sakit alijibu, "Nampenda zaidi Qambar, mtumwa wa Ali kuliko watoto wako. Mutawwakil alitoa amri ung'olewe ulimi wake na hivyo ndivyo mfuasi huyu wa Imamu Ali(a.s) alivyowahi, kupata Shahada yake.

Misiba hii yote ya kuhuzunisha ilimshtua Imamu[a.s] . Zaidi ya hayo, matendo ya kishari ya Mutawakkil aliyowatendea watu yaliwafanya watu hao kuwa mabaya juu yake na wanawe mwenyewe waligeuka kuwa maadui wake wakuu. Na mwanawe aitwaye Muntasir alimwua Mutawakkil kwa kumtumia mtumwa wa Kirumi aitwae Baghir, na baada ya hapo watu walipata afueni kutokana na mateso yake. Muntasir aliondoa ile amri ya baba yake iliyozuia watu kwenda kuhiji Najaf na Karbala na akayatengeneza kidogo yale makaburi yaliyobomolewa. Hakuonyesha chuki maalum kwa Imamu[a.s] . Lakini Muntasir alifariki mara tu baada ya kutawala kwa muda wa miezi sita. Alirithiwa na Musta'in ambaye naye hakuonyesha chuki yoyote kwa Imamu[a.s] .

Hivyo, tangu hapo Imamu(a.s) aliishi Sammarah; kwa sababu Imamu aIijega nyumba yake huko au kwa sababu watawala wenyewe walikuwa hawataki arudi Madina na katika muda huo hapakuwekwa kizuizi cho chote kilichowekwa na watawala, hivyo wapenda elimu walianza kumkusanyikia Imamu[a.s] . Hali hii ilisababisha wasiwasi kwa Mu'tazz ambaye alirithi kiti cha enzi kutoka kwa Musa'in na alimwua Imamu(a.s) kwa kumpa sumu.

KUFARIKI KWAKE

Imamu(a.s) aIifariki dunia mnamo tarehe 3 ya mwezi wa Rajab, mwaka 254 Hijiriya. Wakati wa kufariki kwake mwanawe Imamu Hasan Askari(a.s) tu ndiye aliyekuwepo na kutayarisha maziko yake na sala, na wakamzika ndani ya nyumba yake aIimokuwa akiishi. Hapo ndipo kaburi lake lisimamapo kuyabariki macho ya mahujaji waendoa kulizuru.

1

MAISHA YA IMAM HADI(a.s)

UKWELI KATIKA MINYORORO (IMAMU ALI NAQI[a.s]

TABIA ZAKE NJEMA

Imamu Ali An-Naqi(a.s) alikuwa na tabia njema kama zile za kila mmoja, wa watu wa ukoo wa Mtukufu Mtume[s.a.w.w] . Akiwa nje au ndani ya jela, tabia ya maisha ya Imamu Ali Naqi(a.s) iliyojulikana sana ilikuwa ni sala, ibada na huruma kwa viumbe vya Mungu.

Popote pale alipoishi alipokuwa jela alitayarisha kaburi na mahaIi alipokuwa akisalia. Alipoulizwa maana yake, alijibu kuwa alitaka kila mara kuliweka wazo la kifo mbele akilini mwake. Hakika hilo liIikuwa jibu la kufaa kwa matakwa ya watawala dhaIimu kwa lmamu(a.s) kuwa aache kuitangazia Imani ya kweli na kuitii serikali ya kiupotovu isiyokuwa na msimamo. Alikuwa akisema kuwa mtu aliye tayari kufa wakati wowote hawezi kutishwa mpaka akatiishwa.

Ingawa milki ya ukoo wa Bani Abbas ilikuwa imezorota sana, lmamu(a.s) hakufikiria kuiangusha na serikali haikuweza kupata kisingizio cha kuyahalalishia mateso waliyompa.

Chuki aliyoionyesha Muntasir na mtumwa wake wa Kirumi aitwaye Baghir aliyempenda kwa baba yake Mutawakkil, kugawanyika kwa utawala na maangamizi ya watu wenye vyeo vya juu srikalini na mwishowe uamuzi wa wanawe Mutawakkil wa kumwondoIea baba yao kiti cha enzi, na wakati wa utawala wa Musta'in kuondoka kwa Yahya bin Ami Alawi, kuanzishwa serikali ya kujitegemea huko Tabaristan na Hasan bin Zaid, maasi ya watumwa wa Kituruki katika mji mkuu wa nchi, kukimbia kwa Musta'in kutoka katika mji huo mkuu na kwenda Baghdad, na mwishowe kulazimishwa kujiuzulu na baadaye kuuawa na Mu'ttaza; na vitendo vya uchochezi vya watumwa wa Kirumi katika zama za Mu'ttazz, Mu'ttazz kutokuwaamini ndugu zake na mwisho wa maisha ya Bani Mu'awiyyah na kufungwa kwa Muwaffaq huko mjini Basrah, matukio yote haya yalimtoa Imamu(a.s) katika hali ya kudhaniwa kuwa anahusika na kitendo chochote cha kisiasa. Je, hii haionyeshi uwezo wa hali ya juu na usio na kifani wa Imamu(a.s) katika kujali zaidi ujumbe wake licha ya majaribu hayo yote ambayo kwa kweli yangeweza kabisa kumwambukiza mtu wa kawaida?

Ustahimilifu uIioonyeshwa na Imamu kwa serikali ambayo alijua kuwa ni ya kidhalimu na haribifu kwa sheria ya Islamu na kwamba imemuwekea taabu nyingi mno, inaonyesha kuwa ni tabia bora mno ya kiakili (inayotokana na Mwenyezi Mungu) ambayo ingeweza kuufanya Mwenge wa Mwanga Mtukufu kuendelea kuwaka.

NYONGEZA YA KWANZA

Mwanahistoria Bwana Mas'ud ananakili tukio ambalo habari zake amezichukua kutoka katika kitabu kiitwacho 'Al-Mubarrad' na ambalo mwanahistoria mwingine Bwana Ibn Khallikan ameliweka katika maelezo (katika Juzuu ya Pili, uk. 214 wa tafsiri ya Kifaransa ya "Tarikh" ya Bwana Ibn Khallikan iliyofanywa na Bwana de Slane) ya Imamu Ali Naqi (Abul Hasan Askari(a.s) lisemalo kuwa, "Habari ya siri ilipelekewa Al-Mutawakkil kuwa lmamu alikuwa na zana na vita, vitabu na vitu vingine ambavyo ilikuwa vitumiwe na wafuasi wake waliyojificha nyumbani mwake, na kushawishiwa kwa taarifa mbaya ili waamini kuwa alikuwa akijitahidi kuipata dola ile. Usiku mmoja Muttawakil alipeleka askari wa Kituruki kuingia nyumbani humo wakati asiotegemea hivyo. Walimkuta akiwa peke yake na akajifungia chumbani mwake akiwa amevaa shati la manyoya na kichwani kwake akiwa amejitanda shuka ya sufu na akielekeza uso wake mjini Makka, akisoma aya za Qur'ani zenye kuonyesha ahadi na vitisho vya Mwenyezi Mungu akiwa hana hata zulia lolote ila kokoto na mchanga tu.

Alichukuliwa hivyo hivyo na kutolewa nje gizani mpaka kwa Al-Mutawakkil ambaye wakati huo alikuwa anakunywa mvinyo. Alipomwona Imamu(a.s) alimpokea kwa heshima na alipoambiwa kuwa hakuna kilichoonekana nyumbani mwa Imamu(a.s) kiwezacho kuthibitisha yale mambo yaliyodhaniwa, alimwambia aketi karibu naye na akampa kikombe cha mvinyo alichokuwa nacho mikononi mwake. Abul Hasan (Imamu[a.s] akasema, "Ewe Amirul-Muuminin", kufuatana na imani ya wanahistoria waandishi wala sio kwa mujibu wa aaminivyo Imamu[a.s] ; pombe kama hii haijachanganywa na mwili na damu yangu, hivyo nisamehe nisiinywe." Mfalme alimkubalia ombi lake lakini alimwomba Imamu(a.s) amsomee beti fulani fulani za Mashairi ambazo zingelimfurahisha. Imamu Abul Hasan(a.s) alimjibu kuwa alikuwa amekariri mashairi machache sana lakini Al-Mutawakkil aliposisitiza kuwa aimbe, aliimba mashairi haya yafuatayo:

"Usiku kucha walikesha katika vilele vya milima,

Wakilindwa na askari shujaa, Lakini hata hivyo maficho yao hayakufaa kitu. Baada ya fahari na madaraka yote waliyonayo,Iliwalazimu wateremke kutoka kwenye ngome zao, ndefu na kuingia mwenye kifungo cha kaburi,O! Mabadiliko hayo ni yenye kuogofya kiasi gani?

Makaburi yao yalikwisha wapokea wakati sauti iliposikika ikisema: Ziko wapi falme zenu na mataji na kanzu zenu za heshima? Sasa ziko wapi nyuso za hao wazuri, zilizofunikwa na maovu na kulindwa na mapazia ya kumbi za wasikilizaji? Kwa ombi hili kaburi lilitoa jibu kamili.

Likasema, sasa mafunza wanazifurahia nyuso hizi (kwa kuzila).

Watu hawa walikuwa wakila na kunywa kwa muda mrefu lakini sasa badala yake wanaliwa.

Kila mtu aliyekuwepo pale alihofia usalama wa Abul Hasan [a]. Waliogopa kuwa Mutawakkil katika hasira yake ya kwanza tu angeweza kuimalizia hasira yake kwake. Lakini badala yake walimwona Mfalme huyo akilia kwa uchungu mwingi sana, machozi yakatiririka kutoka ndevuni mwake hivyo wote waliokuwa pale walianza kulia nao. AI-Mutawakkil aliamuru mvinyo huo utolewe na badala ya hayo alisema: "Niambie Abul Hasan una deni lolote udaiwalo. "Ndiyo", alijibu Imamu(a.s) "Nilikopa dinari mia nne. Mfalme aliagiza Imamu(a.s) apewe fedha hiyo na apalekwe kwake kwa heshima zote."

NYONGEZA YA PILl

Siku moja Mutawakkil alimwomba Bwana Ibn Sukait (Soma maandishi ya kitabu hicho jina hili limeandikwa kitabuni humo lbn-Al-Sakit) kumwuliza Imamu(a.s) maswali magumu sana ambayo yangemshinda kuyajibu. Hivyo alimwuliza maswali yafuatayo:

Ibn Sukait: Mungu alimpa Musa Muujiza wa fimbo na Isa alipewa Muujiza wa kuwaponya wakoma na kuwafufua wafu na Muhammad Mtume wetu alipewa Qur'ani na upanga: Kwa nini hakuwapa mitume hawa wote muujiza wa aina moja?

Imamu[a.s] : Kila muujiza unafaa kwa wakati wake ulipotolewa. Wakati wa Musa wachawi walikuwa mashuhuri sana, hivyo alipewa muujiza huo wa Fimbo na Taa ya mkono. Wakati wa Isa, sayansi ya utabibu ilikuwa imefikia kilele chake, hivyo alipewa muujiza wa kuponya magonjwa na kufufua wafu Na wakati wa Mtakatifu Mtume, ufasaha wa kusema, elimu ya usemaji na ushujaa vilikuwa na sifa zaidi, hivyo alipewa Kitabu (Qur'ani) na Upanga, ili kupambana navyo.

lbn Sukait: Sasa siku hizi wakati ambapo hakuna mwenye muujiza, nini "Hujjah" (Kipomo cha tabia ya watu)?

Imamu(a.s) "Ni akili yao ya kuweza kujua mema na mabaya.

Ibn Sukait: Lakini akili ilikuwepo katika miili tangu awali?

Imamu: Lakini milango ya kupambanua ilikuwa bado haijafunguliwa. Milango hiyo imefunguliwa na Mitume.

Ibn Sukait:Ni nani huyu anayetajwa katika Qur'ani, kwani "... yule aliyekuwa na elimu ya Kitabu... " (Qur'ani, 27:40).

Imamu[a.s] : Asif bin Barkhiya.

Ibn Sukait: Lakini wakati Mtume Suleiman alipowauliza wafuasi wake ni nani kati yao awezaye kumleta Malkia Bilqis (wa Sheba) pamoja na kiti chake cha enzi, haujua kwamba Asif anaweza kufanya hivyo?

Imamu[a.s] : AIijua, lakini alitaka kuhakikisha ubora wa Asif kwao na kuwaambia kuwa atakuwa Mrithi (Khalifa) wake.

Ibn Sukait: Kwa nini Yaaqub alimsujudia Yusufu? Je, ni haki baba kumsujudia mwanawe? Je, mwanadamu anaweza kufanya hivyo kwa mwanadamu mwenzie?

Imamu[a.s] : Kusujudu kule kulikuwa ni utii kwa Mwenyezi Mungu na kumtakia heri Yusuf. Kusujudu huku kulikuwa sawa na kule malaika walikokufanya kwa Adamu. Kusujudu kwa Yaaqub na wanawe kulikuwa ni shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwamba aliwakutanisha tena wakawa pamoja tena baada ya kutengana kwa muda mrefu.

Ibn Sukait: Ni mti gani ule Adamu alioamriwa asiukaribie wala kula matunda yake?

Imamu[a.s] : Ulikuwa ni mti wa Wivu. Mwenyezi Mungu alitaka kawaokoa wana wa Adamu kutokana na wivu.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU

YALIYOMO

MAISHA YA IMAM HADI (A.S) 1

UKWELI KATIKA MINYORORO (IMAMU ALI NAQI AL HADI (A.S) 1

KIMEANDIKWA NA: MAULANA SAYYID ALI NAQI SAHEB 1

KIMETAFSIRIWA NA: MAALIM DHIKIRI OMARI KIONDO 1

IMAMU KATIKA QUR'AN NA HADITHI 1

UTANGULUZI 1

JINA NA NASABA YAKE 1

KUZALIWA NA KULELEWA KWAKE 1

MABADILIKO YA KISIASA 2

SHIDA NA MATESO 2

KUFARIKI KWAKE 5

MAISHA YA IMAM HADI(a.s) 6

UKWELI KATIKA MINYORORO (IMAMU ALI NAQI[a.s] 6

TABIA ZAKE NJEMA 6

NYONGEZA YA KWANZA 6

NYONGEZA YA PILl 7

SHARTI YA KUCHAPA 8

MWISHO WA KITABU 8

YALIYOMO 9