AL-SAHIFATU AL-KAAMILATU AL-SAJJAADIYYATU

AL-SAHIFATU AL-KAAMILATU AL-SAJJAADIYYATU 0%

AL-SAHIFATU AL-KAAMILATU AL-SAJJAADIYYATU Mwandishi:
: Sheikh Haruna Pingili
Kundi: Imam Ali bin Husein (A.S)

AL-SAHIFATU AL-KAAMILATU AL-SAJJAADIYYATU

Mwandishi: Ali ibn al - Husayn Imam Zaynul al - Abidin (a.s.)
: Sheikh Haruna Pingili
Kundi:

Matembeleo: 19960
Pakua: 4388

Maelezo zaidi:

AL-SAHIFATU AL-KAAMILATU AL-SAJJAADIYYATU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 19960 / Pakua: 4388
Kiwango Kiwango Kiwango
AL-SAHIFATU AL-KAAMILATU AL-SAJJAADIYYATU

AL-SAHIFATU AL-KAAMILATU AL-SAJJAADIYYATU

Mwandishi:
Swahili

12

AL-SAHIFATU AL-KAAMILATU AL-SAJJAADIYYATU

DU'A YAKE SIKU YA JUMANNE

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Sifa njema ni zake Allah na himidi ni haki yake kama anavyostahiki himidi nyingi, na ninajikinga na yeye na shari ya nafsi yangu (Innan-nafsa-la-ammaratun bis-suuin illaa ma rahima rabiy) (12:53)

Hakika nafsi ni yenye kuamrisha uovu isipokuwa Mungu wangu akiirehemu.

Na ninajikinga naye (Mungu) na shari ya shetani ambaye huniongezea dhambi kwenye dhambi zangu. Naomba ulinzi kwake dhidi ya kila fedhuli muovu, na mtawala dhalimu na aduwi mwenye mabavu. Oh Allah nifanye kuwa miongoni mwa askari wako kwa sababu askari wako ndio washindi, nifanye niwe kwenye kundi lako kwa sababu kundi lako ndilo lenye ufanisi, nifanye miongoni mwa Mawaliy wako kwa sababu Mawaliy wako hawatokuwa na hofu wala hawatohuzunika.

Oh Allah niwekee sawa dini yangu kwa sababu ndio hifadhi ya mambo yangu, niwekee sawa ahera yangu kwa kuwa ndio nyumba ya makazi yangu ya kudumu, na ndio kimbilio langu la kuwa jirani na waovu. Ujaaliye uhai uwe ndio zidisho langu la kila kheri, na kifo kiwe raha kwangu kwa kuepukana na kila shari. Oh Allah mrehemu Muhammad na khaataman Nabiyyin na ambaye timizo la idadi ya wajumbe. Na warehemu Aali wake wema walio tahirishwa. Na sahaba wake wateule. Nipe mimi siku ya jumanne mambo matatu: Usiniachie dhambi ila iwe umeisamehe, wala mayonzi ila uwe umeyaondowa, wala adui ila uwe umemsukuma nyuma. Kwa jina la Allah ni jina bora miongoni mwa majina Bismillahi bwana wa ardhi na mbingu najikinga na kila makuruhi mwanzo wake kasiriko lake, na ninaleta kila lipendwalo mwanzo wake ridhaa yake, ni hitimishiye kwa msamaha toka kwako ewe muhisani.

DU'A YAKE SIKU YA JUMATANO

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Kehema Mwenye Kurehemu. Sifa njema ni zake Allah ambaye ameujaalia usiku kuwa ni vazi, na usingizi kuwa ni pumziko. Na ameujaalia mchana kuwa wakati wa kuinuka. Sifa njema ni yako umeniinuwa toka usingizini mwangu. Lau ungependa ungejaalia wa milele. Sifa njema daima haikatiki, idadi yake viumbe hawaiwezi. Oh Allah! zako ni sifa njema kwa kuwa umeumba na ukakadiria. Ulikadiria na kuamuru, umeweka umauti na uhai, umeuguza na umeponya, umetowa afya na umeweka balaa, umetawalia kitanda cha enzi, ufalme ukauzingira, nakuomba ombi la ambaye uombezi wake umedhoofika, ujanja wake umekatika, muda wake umekurubia, matumaini yake duniani yamenywea, mahitaji yake ya rehma zako yameshika kasi, majuto yake kwa kupuuza kwake yamekuwa makubwa, kuteleza kwake na kujikwaa kumezidi, toba yake kwa ajili ya uso wako imekuwa nyofu, mrehemu Muhammad hitimisho la manabiy na warehemu watu wa nyumbani mwake wazuri waliotahirishwa, nitunukiye uombezi wa Muhammad. Oh Allah mbariki yeye na Ali zake, usininyime kuwa pamoja naye, kwa hakika wewe ni mwingi mno wa kurehemu katika wanao rahemu. Oh Allah niamuliye siku ya jumatano mambo manne: Ijaaliye nguvu yangu katika utii wako, na furaha yangu iwe katika ibada yako, upendo wangu uwe katika thawabu zako, kujiepusha kwangu kuwe katika ambalo linawajibisha kwa ajili yangu maumivu ya adhabu yako, kwa hakika umpole kwa umpendaye.

DU'A YAKE SIKU YA ALHAMISI

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Kehema Mwenye Kurehemu Sifa njema ni za Allah ambaye ameuondowa usiku wenye giza kwa uwezo wake, na ameleta mchana wenye mwanga kwa rehma yake, amenivisha mimi mwanga wake na amenipa neema za (mchana). Oh Allah kama ulivyonibakisha kwa huo mchana nibakishe kwa mfano wake. (mchana mwingine). Mrehemu Nabiy Mohammad na Ali zake usinipe mahangaiko humo na katika usiku mingine na mchana kwa kufanya yaliyoharamu na kutenda dhambi, niruzuku kheri zake na kheri zilizomo humo na kheri ya baadaye. Niondolee shari yake na shari iliyomo humo na shari ya baada yake. Oh Allah hakika mimi kwa hifadhi ya Uislam naomba wasila wa kuelekea kwako. Na kwa heshima ya Qur'an isiodhurika nakutegemea. Na kwa Muhammad mteule rehema za Allah zimfikie yeye na Ali zake naomba shafaa kwako. Tambuwa Oh Allah! dhimma yangu ambayo nimeitarajia kukidhi haja zangu. Ewe mwenye rehma nyingi kuliko wote wenye kurehemu. Oh Allah nikidhiye katika siku ya Al-hamisi matano hakuna wasaa kwayo isipokuwa ukarimu wako. Hakuna aya wezae isipokuwa neema zako; usalama unipe nguvu kwa ajili ya utii wako. Ibada ilinistahiki kwa ajili yake wingi wa thawabu zako. Hali ya wasaa kutokana na riziki ya halali. Uniweke katika amani mahali tuwa hofu kwa amani yako. Niweke katika ngome yako dhidi ya mahangaiko na mayonzi, mrehemu Muhammad na Ali wake jaalia wasila wangu kupitia yeye wenye mafanikio siku ya kiyama yenye manufaa kwa hakika wewe ni mwenye huruma zaidi miongoni mwa wenye huruma.

DU'A YAKE SIKU YA IJUMAA

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mnringi 'wa Kehema Mwenje Kurehemu. Sifa njema ni zake Allah wa kwanza kabla ya kuumba na kutoa uhai, wa mwisho baada ya kwisha vitu, mjuzi wa yote ambaye hamsahau mwenye kumkumbuka. Hampunguzi anayemshukuru haachi kumtekelezea amwombaye hakati matumaini ya mwenye kumtumainia. Oh Allah mimi nakuomba ushuhudiye nawe ni shahidi tosha na nawaomba washuhudie malaika wako wote na wakazi wa mbungu zako nawabeba arshi yako na uliowatuma miongoni mwa Manabiy wako na Mitume wako na uliowaumba miongoni mwa sampuli za viumbe wako. Kwamba mimi nashuhudia kuwa hakika wewe ni Allah hapana miungu isipokuwa wewe peke yako huna mshirika wa kulingana. Halishindwi neno lako wala kubadilika na hakika Muhammad ni rehema na amani zimfikie yeye na Ali zake ni mtumwa wako na mjumbe wako. Ametekeleza amefikisha ulilo mtuma kwa waja na amefanya juhudi kwa ajili ya Mungu aliye mtukufu juhudi ya haki na kwamba yeye alibashiri ambayo ni haki miongoni mwa thawabu na ameonnya ambayo ni kweli miongoni mwa adhabu. Oh Allah niimarishe katika dini yako pindi unibakishapo hai, usiupotoshe moyo wangu baada ya kuwa umeniongoza nipe rehema kutoka kwako hakika wewe ni mtowaji sana mrehemu Muhammad na Ali wa Muhammad nifanye mimi niwe miongoni mwa wafuasi wake na Shia wake, nikusanye mimi katika kundi lake ni wafikishe kutekeleza faridha ya Ijumaa zote, na uliyowajibisha humo kwangu miongoni mwa utii, na umegawa kwa watu wake chakutowa siku ya malipo, hakika wewe ni mwenye nguvu mwenye hekima.

DU'A YAKE SIKU YA JUMAMOSI

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Bismillaahi ni neno la wenye kushikamana kwake. Na niusemi wa watakao ulinzi kwake, najikinga kwa Mungu mtukufu na jeuri ya wajeuri na vitimbi vya mahasidi na uchokozi wa madhalimu na ninamuhimidi zaidi ya himidi ya wenye kumuhimidi. Oh Allah wewe ni mmoja bila mshirika na u mfalme bila kutawazwa. Hupingwi katika hukumu yako hushindwi katika ufalme wako nakuomba umrehemu Muhammadi na Ali zake mtumwa wako na mtume wako, niongoze kushukuru neema zako (shukrani) itakayo nifikisha upeo wa ridhaa zako, unisaidie kukutii wewe na kujilazimisha ibada yako ili nistahiki thawabu zako kwa huruma ya uangalizi wako. Nihurumiye na uniziwiye maasi yako kwa kadiri uniwekapo hai, uniwafikishe linaloninufaisha kadiri unibakishapo. Kipanuwe kifua changu kwa kitabu chako, punguza kwa kukisoma kwake mzigo wangu wa dhambi. Nitunukiye salama katika dini yangu na nafsi yangu usinifarakishe na wapenzi wangu timiliza ihisani yako katika umri wangu uliobaki. Kama ulivyofanya ihisani katika umri wangu uliyopita, Oh wee mwenye huruma nyingi kuliko wote wenye huruma.

MNONG'ONO WA IBADA YA WENYE KUJUTA

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Oh Mungu wangu makosa yamenivika nguo ya udhalili wangu, kuwa mbali na wewe kumenifunika vazi la huzuni yangu kuu. Dhambi yangu kubwa imefisha moyo wangu, hivyo basi uhuishe kwa kutubu kwako. Oh we tumaini langu na lengo langu. Oh we ndio utashi wangu na hitajio langu. Kwa uwezo wako, simpati wakusamehe dhambi zangu ambaye si wewe, simwoni yeyote wakuganga vunjiko langu ambaye si wewe. Nimenyenyekea kwa kurejea kwako, nimenyongeka kwa kujiweka chini kwako. Ikiwa utanifukuza toka mlangonni kwako ni kwa nani nitapata kimbilio! Ukinirudisha nyuma toka upande wako ni kwa nani nitajikinga. Huzuni iliyoje kwa kuaibika kwangu na kufedheheka. Oh wee huzuni ni yangu kutokana na matendo yangu maovu na yale niliyoyatenda. Nakuomba ewe mwenye kughofiria dhambi kubwa.

Oh wee mwenye kuganga mfupa uliovunjika, yafumbiye macho matendo yangu yaangamizayo. Na unisitiri siri zangu za kufedhehesha, usinitowe siku ya ushuhuda wa kiyama toka kwenye baridi ya msamaha wako na ghofira yako. Yapeleke mawingu ya msamaha wako juu ya aibu yangu. Mola wangu, harejei mtumwa aliyekimbia isipokuwa kwa bwana wake. Je yeyote aweza kumpa kimbilio toka makasiriko yake asiyekuwa yeye. Mola wangu! Ikiwa kujuta kwa ajili ya dhambi ni toba hakika mimi naapa kwa uwezo wako ni miongoni mwa wajutao. Ikiwa kuomba ghofira kutokana na makosa ni kupunguza, hakika mimi ni mwenye kuomba ghofira kwako, kwako narejea ili uridhike. Oh Mungu wangu kwa uwezo wako juu yangu nikubalie toba yangu. Kwa huruma yako kwangu nisamehe na kwa kunijuwa kwako mimi nifanyiye upole. Mola wangu wewe ndiye ambaye umefunguwa mlango wa msamaha wako kwa waja wako umeuita toba ukasema (tubuni kwa Allah toba ilioimara) ni udhuru gani atakuwa nao mwenye kughafilika kuingia mlango ule baada ya kufunguliwa kwake! Mola wangu! Ikiwa dhambi iko mbaya toka kwa mtumwa wako, msamaha uwe mwema kutoka kwako. Mola wangu mimi si wa kwanza kukuasi ulimkubalia toba yake au aliyejitahidi kutaka mema yako ulimfadhili. Oh we mwenye kumjibu aliye dharurika. Oh we mwenye kuondowa dhara. Oh we mkubwa wa mema. Oh we mjuzi wa yaliyo siri. Oh wee mzuri waa kusitiri! Ninaomba kwako shifaa kwa ukarimu wako na upaji wako. Naomba kwa upande wako na huruma yako nikubalie Du'a yangu kwako usininyime kufanikiwa kwako matumaini yangu. Nikubalie toba yangu. Nifichie makosa yangu kwa huruma yako. na rehema zako ewee mwingi wa kurehemu miongoni mwa wenye kurehemu.

NONG'ONO LA SALA YA MNUNG'UNIKAJI

Kwa Jina la Mwenyezi Mwingi wa Rehema Mwenje Kurehemu. Mola wangu nanung'unika kwako nafsi yenye kuamrisha maovu, yenye kuharakia kwenye makosa inabidii kwenye maasi yako, ikijiweka kwenye hatari ya kasiriko lako, yaipeleka mapito ya kuhilikisha yanifanya mimi mbele yako mwenye kuhiliki rahisi kabisa nyudhuru nyingi. Ikiwa na matumaini marefu, ikiguswa na shari yafadhaika na endapo itaguswa na kheri yazuiya yenye kuelemea sana kwenye mchezo na upuuzi. Imejawa na mghafala na kusahau yaniharakishia kwenye matendo yasiyotakiwa. Yanifanya nichelewe kutubu. Mola wangu nanung'unika kwako adui anipoteza na shetani anipotosha. Amekijaza wasi wasi kifuwa changu ushauri wake umejaa moyo wangu anaunga mkono upuuzi dhidi yangu. Yanipambia kuipenda dunia yazuia kati yangu na utii na ukaribu. Mola wangu kwako nanung'unika moyo mgumu wageuka pamoja na wasi wasi imejivisha kutu na kupigwa muhuri na jicho lisilo lia kwa hofu yako na kwa mambo yanayolifurahisha lina tamaa nayo. Mola wangu, hapana hila wala nguvu ila kwa nguvu zako, wala sina uwokozi kutokana na makuruhi ya dunia ila kwa hifadhi yako kwa hiyo nakuomba kwa umbali unaofikia hekima zako na upenyo wa utashi wako, usiniache nijitose kusiko kuwa na upaji wako, usinifanye nijiingize kwenye fitna kuwa mwenye kunisaidia dhidi ya maadui na mwenye kunisitiri kwenye fedhea na aibu. Na mlinzi kwenye balaa na mhifadhi kwenye maasi kwa huruma yako na rehema zako.

NONG'ONO LA SALA YA MWENYE HOFU

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Mola wangu, waona baada ya kuamini utaniadhibu! Au baada ya upendo wangu kwako utanifurusha. Au pamoja na matumaini yangu rehema zako na msamaha wako uninyime utanitupa pamoja na kukuomba kwangu saana hifadhi. Vipi uso wako mkarimu unifanyie kinyume na matumaini lau ningejua ni kwa ajili ya balaa na udhalili mama yangu amenizaa. Au ili nitaabike amenilea, ni afadhali basi asingenizaa wala asingenilea, afadhali ningejua umenijaalia kuwa miongoni mwa watu wa heri na umenichagua kuwa miongoni mwa wa karibu wako. Ili lifurahiwe kwa hilo jicho langu, na kwalo nafsi yangu iwe na utulivu Mungu wangu, hivi utaziweusisha nyuso ziliporomoka chini zikisujudu kwa utukufu wako, au utazifanya bubu ndimi zilitamka sifa za utukufu wako na enzi yako, au utazipiga muhuri nyoyo ndanimwe mulikuwa na upendo wako, au utayafanya kiziwi masikio yaliona ladha kusikia utajo wako kwa utashi wako, au utaifunga pingu mikono ambayo matumaini yameinyanyuwa kwako ikitazamia huruma yako au utaiadhibu miili imekonda katika juhudi kukutii wewe, au utaiadhibu miguu imefanya bidii katika ibada yako. Oh Mola wangu usimfungie mlango wa rehema zako akupwekeshaye. Usiwazuiye wenye shauku nawe kuangalia uzuri wa mtazamo wako. Mola wangu nafsi uliyoienzi kwa kunena tawhidi yako vipi utaidhalilisha kwa twezo kuiacha kwako. Dhamira imejifunga kwa mapenzi yako vipi utaiunguza kwa joto la moto wako. Mola wangu, nikinge na ukali wa ghadhabu zako na kasiriko lako kubwa, Oh mpendwa Oh mwenye huruma Oh mpole Oh mwenye huruma, Oh jabbar Oh mshindi, ewe msamehevu Oh msitiri, kwa rehema yako niokowe tokana na adhabu ya moto na fedheha ya aibu wajitengapo watu wema kando na washari. Na zibadilikapo sura hali ya kutisha itakapo chukuwa nafasi, wema watakapoletwa karibu waovu wawekwapo mbali (na kila nafsi zitapopewa yoote iliyo ikiyafanya wao hawato dhulumiwa).

NONG'ONO LA SALA YA WENYE MATUMAINI

Kwa Jina la Mwenyezi Mwingi wa Kehema Mwenye Kurehemu. Oh ambaye mja wake amwombapo humpa, akiyatumainia aliyo nayo humpa utashi wake. Akimsogelea humkurubisha na kumleta karibu, akimdhihirishia maasi humsitiri dhambi zake na huifunika, akimtegemea humtosheleza. Mola wangu nani afikaye kwako akiomba takrima yako na usimkarimu, nani ateremkiaye mlangoni kwako akitarajia wema wako na usimwonyeshe, je ni vizuri nirejee toka mlangoni kwako hali nimeondolewa bila ya matarajio yangu nami simjuwi bwana mfadhili mwenye kusifika kwa hisani asiyekuwa wewe. Vipi nimtarajiye asiyekuwa wewe hali yakuwa heri zote ziko mikononi mwako. Vipi nimtumainiye mwingine hali kuumba na amri ni vyako, vipi nitumai wengine.

Nikate matarajio yangu kwako hali ya kuwa umenionyesha ukarimu wako kwa ambalo sikuliomba katika fadhila zako je utanifanya niwe muhitaji kwa aliye mfano wangu, hali nikishikamana na kamba yako! Oh yule ambaye wamekuwa na maisha ya furaha kwa rehema zake wenye juhudi, wala hawakuwa duni kwa kisasi chake waomba ghofira, vipi nikusahau hali ungali wanikumbuka. Vipi nitageuzwa mtazamo mbali na wewe hali wewe wanichunga. Mola wangu kwenye pindo la ukarimu wako nimeangika mkono wangu ili kukifikia ukitowacho nimenyosha matumaini yangu, unipe safi Ikh'laasi kwa kunena tawheed yako, nijaaliye niwe miongoni mwa waja wako wateule. Oh ambaye kila akimbiaye kuelekea kwake hupata kimbilio, ni tumaini la kila mtafutaji, ewe mbora wa atarajiwaye, ewee mkarimu mno wa wenye kuombwa, ewe ambaye hamkatalii mwombaji wake wala hamsitukizi kwa kutomtekelezea amtumainiaye. Oh wee ambaye mlango wake uwazi kwa mwombaji wake, pazia yake imenyanyuliwa kwa mwenye matumaini kwake. Nakuomba kwa ukarimu wako unionyeshe huruma kwa bakshishi yako iwezayo kutuliza jicho langu. Na kwa kukutarajia wewe ambako kutaipa nafsi yangu utulivu, na kwa yakini ambayo itanifanyia wepesi misiba ya dunia, na kuniondolea kifuniko cha upofu toka kwenye ufahamu wangu. Kwa huruma yako ewe mwenye huruma zaidi ya wote wenye kuhurumia.

NONG'ONO LA WENYE KUSIHI SANA

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Mola wangu ikiwa masurufu yangu ni madogo katika msafara wangu kuelekea kwako, basi dhana yangu imekuwa nzuri kwa kutawakali kwako. Ingawaje dhambi zangu zimenihofisha adhabu yako matumaini yangu yamenitambulisha kuwa nitakuwa katika amani bila malipizi yako. Ingawa dhambi zangu zimenichongea kwenye adhabu yako uzuri wa imani yangu umenipasha khabari ya kupata thawabu yako. Ingawaje mghafala umenilaza nisiandae kukutana na wewe maarifa yamenizindu'a kwa ukarimu wako na neema zako japokuwa kutotii na maasi yaliyo kithiri kumefarikisha kati yangu na wewe, bishara ya msamaha na ridhaa zimenifurahisha na kunifanya nihisi ni karibu. Nakuomba kwa fahari ya uso wako na kwa nuru za utukufu wako, nakuomba sana kwa upole wa huruma yako na raufu ya wema wako nithibitishiye dhana yangu ninayoyatumainia, katika wingi wa takrima yako.

Na uzuri wa neema zako kwa ukaribu na wewe na ujirani kwako napendezwa na kukutazama wewe. Mimi ni hapa! Nimejiweka kwenye kibaridi cha upya wako na huruma yako. Nataka msaada wa mvuwa ya ukarimu wako na huruma yako, nikikimbia toka kwenye kasiriko lako kuelekea ridhaa zako. Nakimbia kutoka kwako nikielekea kwako nikitumai kizuri mno kilicho kwako nikitegemea matunzo yako, muhitaji wa uangalizi wako. Mola wangu, fadhila zako ulizozianza zitimize fadhila zako ulizo nitunukia, usiziondowe na ambalo umenisitiri usinifichuwe nalo, ambalo umelijuwa mionngoni mwa matendo yangu mabaya ni ghofiriye. Oh Mola wangu, naomba mwombezi kwako kwa ajili yako ninaomba hifadhi kuja kwako kutoka kwako nimekuja kwako, nikitumai hisani yako, nikitaka wema wako, nikiomba maji ya mvuwa ya fadhila zako, nikiomba mawingu ya mvuwa za fadhila zako, nikiomba ridhaa zako, nikija upande wako, nikija mahali patekwapo maji ya msaada wako, nikiomba mema ya hali ya juu kutoka kwako. Naja kwenye hadhara ya uzuri wako nikitaka uso wako, nikigonga mlango wako, nikijidhalilisha mbele ya utukufu wako na adhama yako. Nifanyie ghofira na huruma ambazo wastahiki, wala usinifanyie ambayo mimi nastahiki miongoni mwa adhabu na malipizi, kwa huruma yako ewe mwenye huruma mno kuliko woote wenye huruma.

13

AL-SAHIFATU AL-KAAMILATU AL-SAJJAADIYYATU

MNONG'ONO WA SALA ZA WENYE KUSHUKURU

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Kehema Mwenye Kurehemu. Mola wangu umenisahaulisha kukushukuru mfululizo wa umbuji wako wingi wa fadhila zako umenifanya nishindwe kuhesabu sifa zako, mtiririko wa mema yako kwangu umenishughulisha nisitaje sifa njema zako. Mfululizo wa nufaisho lako kwangu kumenishindisha kutangaza fadhila zako, hiki ni kituo cha aliyetambua wingi wa neema na akazikabili kwa uzembe ameshuhudia dhidi yake mwenye kutojali na kuzembea, wewe ndio mwenye huruma na mpole, mwema mkarimu, ambaye amvunji moyo amwendeaye. Wala hamfukuzi toka ukumbi wake amtumainiaye, uwanjani kwako kwaishia misafara ya wenye matumaini katika kituo cha uwanjani mwako husimama matumaini ya waomba msaada, usiyakabili matumaini yetu kwa kutotekelezewa na kukatishwa tamaa.

Shukurani zangu zimekuwa ndogo mbele ya ukubwa wa ufadhili wako, himidi yangu na tangazo langu zimenywea mbele ya takrima yako kwangu, neema zako zimenifunika mavazi ya nuru ya iymani, umakii wa wema wako umenifunika pazia la kupendeza. Wema wako umenivika mkufu ambao hauto vulika na umenivika tepe ambazo hazito vunjika, fadhila zako chungu tele ulimi wangu umedhoofika kuzihesabu, neema zako nyingi fahamu zangu zimeshindwa kuzifahamu sembuse kuzitafiti. Hivyo basi vipi nitafanikiwa kushukuru hali yakuwa shukrani yangu kwako yahitaji ishukuriwe kila nikwambiapo Al-hamdulillahi itakuwa wajibu juu yangu nikwambie Al-hamdulillahi!

Mola wangu kama ulivyotulisha kwa upole wako na ukatulea kwa fadhila zako, tukamilishie fadhila nyingi, tukinge na makuruhi za malipizi. Utupe hisa za makazi mawili zilizo juu mno na bora mno zote mbili za papo kwa papo na za baadaye. Nawastahiki sifa njema kwa uzuri wa majaribu yako na wingi wa neema zako sifa njema ziwafikianazo na ridhaa yako na ivutayo wema wako mkubwa na utu wako, yaa adhiim yaa kareem, kwa rehema zako ewee mwingi wa huruma kuliko wote wenye huruma.

NONG'ONO LA WATU WA MUNGU

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Oh Allah tufundishe utii wako, tuepushe maasi yako, tufanyie wepesi kufikia tunayoyatamani miongoni mwa utashi wa ridhaa zako. Tuweke katikati ya janna yako, tanduwa toka kwenye ufahamu wetu mawingu ya shaka, fungua nyoyo zetu zingo na pazia la shaka. Ondoa ubatili toka dhamiri zetu, imarisha haki katika fikra zetu za siri, kwa sababu shaka shaka na dhana ni virutubisho vya fitna na vichafuzi vya usafi wa tuzo na wema. Oh Allah tujaalie tuwe katika safina za uokovu wako, tupe ladha ya sala ya kunong'ona na wewe, tunyweshe vidimbwi vya upendo wako, tuonjeshe utamu wa upendo wako na ukaribu wako, jaalia juhudi yetu kwa ajili yako na hima yetu iwe katika utii wako isafishe nia zetu kwa kazi yako tu. Kwa hakika sisi tupo kwa kuwapo kwako na tu wako, hatuna njia ya kufikia kwako isipokuwa ni wewe. Ewe Mungu wangu niweke mimi pamoja na wateule wema, niunge na wema watawa waliotangulia kuifikia zawadi ya ukarimu wenye haraka kwenye matendo mema watenda mema yenye kubaki wenye juhudi kuinuwa daraja, hakika wewe ni muweza juu ya kila kitu, kwa kujibu ndio wafaa, kwa rehema zako ewe mwingi mno wa wenye kurehemu.

NONG'ONO LA SALA YA WANA MUREEDI

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Kehema Mwenye Kurehemu. Utakatifu ni wako, njia nyembamba zilioje kwa usiyemwongoza! Haki yawazi iliyoje kwa uliye mwongoza njia yake! Mola wangu tupitishe njia za kufika kwako, tuendeshe katika njia ya karibu mno kufika kwako, tufanyie karibu mbali, na turahisishie gumu la taabu. Na utukutanishe na waja wako ambao kwa kuwahi kwako waharakia, daima wabisha hodi mlangoni kwako usiku na mchana wakuabudu wewe tu, nao waiogopa haiba yako, ambao umewasafishia manyweo. Na umewafikishia wayapendayo, umewapa wayatakayo, umewatekelezea kwa fadhila zako, utashi wao, umejaza upendo wako ndani ya dhamira zao, umetosheleza kiuzao kwa kinywaji chako safi, kupitia wewe wamewasili kwenye ladha ya kunong'ona na wewe, kutoka kwako wamefikia malengo yao ya mbali sana. Oh we ambaye kwa wale wamwendeaye huwaendea na huwapa zawadi na huwatunukia fadhila kwa upole, mwenye huruma na mwema kwa walioghafilika kumkumbuka, mpendwa mwenye huruma kwa kuwavuta kuelekea mlango wake.

Nakuomba unijaalie niwe miongoni mwa wenye hisa kubwa mno kubwa, na mwenye daraja ya juu zaidi kwako na miongoni mwa wenye hisa ya mapenzi kubwa kwako na mwenye hisa bora zaidi katika kukutambua, hima yangu imekatika isipokuwa kwako tu, utashi wangu umeelekea kwako tu, wewe tu ndio kusudio langu sio mwingine, kwa ajili yako tu kuamka kwangu na kukesha kwangu, wala si kwa ajili ya mwingine. Kukutana na wewe ndio tulizo la jicho langu. Kuungana na wewe ndio utashi wa nafsi yangu, shauku yangu ni kwako katika upendo wako ndio shauku yangu, kujiambatanisha na wewe ndio bidii yangu, ridhaa zako ni lengo niombalo.

Kukuona wewe ndio haja yangu, ujirani na wewe ndio ombi langu, ukaribu na wewe upeo wa ombi langu, sala ya kunong'ona na wewe ndio pumziko na raha yangu, kwako kuna dawa ya ugonjwa wangu na ponyo la moyo wangu unao unguwa, burudisho la shauku yangu, na kitu cha kuondoa taabu yangu. Kuwa mwenzi wangu katika upeka wangu, tulizo la kujigonga kwangu uwe mwenye kuni ghofiria kuteleza kwangu, mwenye kukubali toba yangu, mwenye kuitikia Du'a yangu, mfadhili wa kunihifadhi na dhambi, mwenye kunitoa toka ufakiri wangu, usikate mawasiliano yangu nawe. Oh we jaha yangu na bostani yangu, Oh we ambaye ndio dunia yangu na akhera yangu, Oh wee mwenye rehema nyingi kuliko wote wenye kurehemu.

NONG'ONO LA SALA YA WAPENZI

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Mola wangu ni nani ambaye ameonja utamu wa mapenzi yako kisha amkusudie mwingine badala yako! Ni nani ambaye umekuwa wa moyoni kwake kwa ukaribu wako naye kisha akamtaka mwingine na kujitoa mbali nawewe! Mola wangu tujaaliye tuwe miongoni mwa uliowachagua kuwa wakaribu na wewe na wapenzi wako, uliyemtakasa kwa upendo wako na mahaba yako, umempa shauku ya kukutana na wewe umemfanya apende maamuru yako, na umemtunuku kuangalia uso wako, na umempendelea ridhaa zako. Umempa kinga ya kutokukuhama na kukukirihi, umemfanyia makazi ya uhakika karibu na wewe, umemteuwa kwa ajili ya ukweli wa kukujua wewe, na kumfanya yu astahiki kukuabudu, umeutiisha moyo wake kwa utashi wako.

Umemchagua ili kukushuhudia, umeuweka tupu mtizamo wake kwa ajili yako, umeweka wazi moyo wake kwa upendo wako, umempendezesha yaliyo kwako umemwongoza utajo wako, umemgawiya shukrani yako umemshughulisha kwa utii wako. Umemfanya kuwa miongoni mwa viumbe wako wema, umemchagua kwa sala ya kunong'ona na wewe, umekata kutoka kwake vitu vyote vimkatavyo kutoka kwako. Oh Allah tujaalie tuwe miongoni mwa ambao mwendo wao ni kukufurahia wewe na upendo na nyakati zao ni kupiga kite na kulia, paji zao za uso zi katika hali ya sijda kwa taadhima yako.

Macho yao yakesha yakiwa chini ya huduma yako, machozi yao yatiririka kwa kukuogopa nyoyo zao zimejitundika kwa upendo wako, viini vyao vyatikisika kwa kukuogopa, Oh we ambaye nuru ya utukufu wake huvuta macho ya wapenzi wake, utukufu wa uso wake huamsha upendo wa nyoyo za wamjuao. Oh we utashi wa nyoyo za wenye shauku, Oh wee upeo wa matumaini ya wapenzi, naomba kwako upendo kwa ajili yako, na kuwapenda wanaokupenda, nakupenda kila tendo linifikishalo karibu yako.Na jaalia umpendwa mno kwangu kuliko mwingine yeyote, na jaalia upendo wangu kwako uwe mwongozo kwenye ridhaa zako, na shauku yangu kwako iwe kinga ya kutokukuasi, niangalie kwa jicho la upendo na huruma, usiugeuze uso wako mbali na mimi, nijalie niwe miongoni mwa watu wenye furaha na wewe na wenye hadhi kwako Oh mwenye kuitikia, Oh we mwenye huruma kuliko wote wenye huruma.

NONG'ONO LA SALA YA WAOMBAO WASILA

Kwa Jina la Mwenyez mwingi wa Rehema Mwenje Kurehemu. Mola wangu sina wasila kufikia kwako isipokuwa matendo ya upole wa huruma yako, wala njia yeyote ya kunifikisha kwako isipokuwa fadhila za upole wa rehema zako, na uombezi wa Nabiy wako Nabiy mwenye huruma, mwokozi wa umma toka kwenye bumbuwazo. Jaalia viwili hivyo kwangu ndio sababu ya kupata ghofira yako, vifanye viwili hivyo kwangu kiungo cha kufuzu ridhaa zako, matumaini yangu yamefika kwenye kitalu cha ukarimu wako, tamaa zangu zimetuwa kwenye ukumbi wa upaji wako. Matumaini yangu yameimarika kwako, hitimisha amali yangu kwa muhuri wa kheri nijaalie niwe miongoni mwa wateule wako ambao umewaweka katikati ya janna yako na umewaweka nyumba ya ukarimu wako uliofurahisha macho yao kwa kukuangalia wewe siku ya kukutana na wewe, uliowarithisha vituo vya ukweli karibu yako. Hawafiki wafikaji kwa mkarimu mno kuliko yeye, wakusudiaji hawampati mwenye rehema zaidi kuliko yeye, Oh mbora wa mwenye kuwa naye peke yake. Oh we mpole wa mwenye kukimbilia ya kwake hali amefukuzwa, nimenyosha mikono yangu kuelekea wasaa wa msamaha wako, kwenye ncha ya ukarimu wako nimetungika mkono wangu, usininyime, wala usinipe balaa la kutofanikiwa na kuhasirika. Oh we msikiaji Du'a, Oh we mwenye kurehemu mno kuliko wote wenye kurehemu.

NONG'ONO LA SALA YA MAFAKIRI

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Kehema Mwenye Kurehemu. Mola wangu mvunjiko wangu haugangwi ila na upole wako na upendo wako, ufakiri wangu hautoshelezi yeyote isipokuwa na upendo wako na hisani yako, woga wangu hautulizi yeyote isipokuw na amani yako. Udhalili wangu hawezi kuuenzi yeyote isipokuwa mamlaka yako, hatonifikisha kwenye matumaini yangu isipokuwa fadhila zako, hawezi kurekebisha ukosefu wangu isipokuwa umbaji wako. Hawezi kukidhi haja yangu asiyekuwa wewe, hawezi kunifariji dhiki yangu isipokuwa rehema yako. Madhara yangu hayaondowi yeyote ila huruma yako, kiu yangu iunguzayo hawezi kuiburudisha yeyote isipokuwa mawasiliano yako, shauku yangu hawezi kuizima yeyote isipokuwa kukutana na wewe. Shauku yangu kwako hakuna wa kuituliza isipokuwa kwa kuangalia uso wako.

Kuwa imara kwangu hakuwezi kufanyika isipokuwa kwa kusogea karibu yako, woga wangu hautulizi yeyote isipokuwa tulizo lako ugonjwa wangu hawezi kuutibu yeyote isipokuwa dawa yako, mayonzi yangu hayatowi yeyote isipokuwa kwa kuwa karibu yako, jeraha langu hawezi liponya yeyote isipokuwa msamaha wako, kutu ya moyo wangu haiondowi yeyote isipokuwa msamaha wako, wasi wasi wa moyo wangu hauondowi yeyote isipokuwa amri yako. Oh we upeo wa matumaini ya wenye kutumaini, Oh we upeo wa ombi la waombaji, Oh we umbali wa utashi wa watakaji, Oh we ambaye ndio juu kabisa wa takwa la watakaji, Oh we mfadhili wa watu wema, Oh we ambaye ni amani ya walio na woga, Oh we mwenye kujibu maombi ya wenye madhara, Oh we ambaye ni bohari ya wasiokuwa na kitu, Oh we ambaye ni hazina ya wanyonge, Oh we mwenye kukidhi haja za mafakiri na masikini, Oh we mkarimu mno wa wakarimu. Ewe mwenye rehema zaidi ya wenye kurehemu, Kunyenyekea kwangu na ombi langu ni kwako, utetezi wangu na ombi langu sana ni kwako nakuomba unipe tulizo la bidhaa yako, udumishe kwangu neema za huruma yako.

Mimi ni huyu! Mwenye kusimama kwenye mlango wa ukarimu wako, nimejiweka kwenye baridi ya wema wako, nimeshikilia kamba yako madhubuti, nimeshikamana na kishiko chako thabiti. Mola wangu muhurumie mja wako dhalili, mwenye ulimi butu na amali (kazi) ndogo, mpe kwa hisani zako nyingi mno, mhifadhi chini ya kivuli chako kikubwa, ewe mkarimu, ewee mzuri, ewee mwingi wa huruma kuliko wote wenye huruma.

NONG'ONO LA SALA YA WAJUZI

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Mola wangu, ndimi zimeshindwa kuifikia sifa yako njema, kwa kiwango kinacholingana na utukufu wako, akili zimeshindwa kuifikia hakika ya uzuri wako, macho yamehasirika bila ya uwezo wa kuangalia utukufu wa uso wako, wala haujamfanyia kiumbe njia ya kukujua wewe, isipokuwa kwa kutoweza kukujua. Mola wangu tujaalie sisi tuwe miongoni mwa ambao imeimarika miti ya shauku yako katika bostani za vifuwa vyao, nguvu ya shauku ya upendo wako imechukuwa mioyo yao yote, wao wakimbilia kwenye viota vya fikra wajilisha katika bostani ya ukaribu na ufunuo. Wanywa kwa glasi ya upendo pamoja na upole wa vikombe vya fadhila, waingia sehemu za maji yenye vuguvugu la upendo, vifuniko vimeondolewa toka macho yao giza la mashaka limewatoka kwenye akida zao na dhamira zao, zimetoweka ingio za shaka nyoyoni mwao na fikra zao za siri.

Vifua vyao vimekunjuka kwa kuthibitisha elimu ya kweli, hima zao zimepanda ili kuwahi maisha ya furaha katika zuhudi kinywaji chao kimekuwa kitamu katika chemchemu ya kazi njema, fikra zao za siri zimekuwa nzuri katika kikao cha moyoni.

Akili zao zimekuwa na amani sehemu za hofu, nyoyo zao zimetakata kwa kurejea kwa bwana wa mabwana, nyoyo zao zimeyakinisha kufaulu na ufanisi, macho yao yamefurahishwa na kumwangalia mpendwa wao, yameimarika makazi yao kwa kupata ombi na kuyafikia matumaini. Biashara yao imepata faida kwa kuiuza dunia kwa akhera, fikra za il-hamu zinaladha ilioje kwa kukukumbuka moyoni, unautamu ulioje msafara wa kifikra kuelekea kwako katika njia isioonekana, wapendeza mno utamu wa upendo wako. Kitamu kilioje kinywaji cha kuwa karibu nawewe, tukinge na fukuzo lako na kuwekwa mbali na wewe, tujaalie tuwe miongoni mwa mahsusi wakujuao, na waja wako wema mno, na wa kweli mno katika waja wako watii na wenye ikhlasi mno katika waja wako wachamungu. Oh we mwenye adhama mwenye ufalme, Ewe mkarimu ewe mtowaji, kwa rehema zako na huruma yako ewe mwngi wa rehema kuliko wenye kurehemu wote.

NONG'ONO LA SALA YA WENYE KUMBU KUMBU

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Kehema Mwenye Kurehemu. Mola wangu lau si wajibu kukubali amri yako ningekutakasa kuwa uko mbali sana na kukukumbuka kwangu wewe, kwa sababu kukukumbuka kwangu wewe ni kwa kadiri yangu si kwa kadiri yako, kadiri yangu haiwezi kufikia mahali pa kukutakasa wewe. Miongoni mwa neema kubwa sana juu yetu kuipitisha dhikri yako ndimini mwetu, na idhini yako kwetu kwa Du'a na kukutakasa na kukusabbihi mungu wangu tia moyoni mwetu utajo wako kando ya watu na katika mkusanyiko. Usiku na mchana, kwa kutangaza na kwa siri wakati wa mafanikio na wataabu, tuambatanishe na utajo wa siri tutumikishe na aamali iliyo safi, na juhudi yenye kuridhiwa na wewe tulipe kwa mizani iliyojaa. Mola wangu!

Nyoyo zenye upendo zafurahiwa na wewe kwa ajili ya kukutambua. Na kwa ajili ya upendo wako zimekusanywa nyoyo zilizotengana. Kutengana nyoyo hazitulii safi isipokuwa kwa kukukumbuka wewe, wala nafsi hazitulii isipokuwa zikuonapo. Wewe ni mwenye kutukuzwa kila mahali, mwabudiwa katika kila zana, upo kila wakati, muombwa kwa kila lugha mwenye kuadhimishwa katika kila moyo, nakuomba unisamehe katika kila ladha imepita bila ya kukukumbuka. Na katika kila raha bila ya kujiambatanisha na wewe, na katika kila furaha bila ya kujikurubisha kwako, na katika kila shughuli bila ya utii wako. Mola wangu! Wewe umesema na usemi wako ni wa haki (o ninyi mlioamini mkumbukeni Mungu sana na mumtukuze asubuhi na jioni) ulisema na usemi wako ni wa haki: (nikumbukeni nitakukumbukeni) ulituamrisha tukukumbuke na ulituahidi kuwa utatukumbuka ili kuinuwa heshima yetu na kututukuza sisi na hao twakukumbuka kama ulivyo tuamuru. Hivyo basi tutekelezee uliyotuahidi, Oh we mkumbukaji mno miongoni mwa wakumbukaji, Oh we mwenye huruma mno miongoni mwa wenye huruma.

NONG'ONO LA SALA YA WENYE KUSHIKAMANA

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Oh Allah Oh we kimbilio la wakimbiliao! Oh we kinga ya wenye kujikinga! Oh we mwokozi wa wahilikio! Oh we mhifadhi wa wanyonge! Oh we mwenye huruma kwa masikini! Oh we mwenye kuwajibu wenye shida! Ewe hazina ya wenye hajja! O we mwenye kuwaganga waliovunjika! Ewe kimbilio la waliokatikiwa! Oh msaidizi wa wanyonge! Oh we mtowa hifadhi kwa wenye hofu! Oh msaidia wenye taabu! Oh ngome ya wakimbizi! Ikiwa sikujikinga na uwezo wako ni kwa nani nitajikinga naye? Endapo sikuomba kimbilio kwa uwezo wako kwa nani nitakimbilia! Dhambi zimenifanya nishike upindo wa vazi la msamaha wako! Makosa yamenifanya niombe kubisha hodi kwenye mlango wa msamaha wako. Maovu yamenifanya niteremke kwenye ukumbi wa utukufu wako. Hofu ya adhabu yako imenichukuwa nishikamane na kishiko cha huruma yako.

Si haki kwa ambaye ameshikamana na kamba yako atupiliwe mbali. Wala haiwi sawa kwa ambaye ameomba hifadhi kwa enzi yako asalimishwe au atelekezwe! Oh Mola wangu usitutowe nje ya himaya yako. Usituvue uangalizi wako. Tulinde kwenye njia za kuangamiza. Hakika sisi tuko machoni mwako. Na tu katika bawa lako. Nakuomba kwa wateule wako miongoni mwa malaika wako na walio wema miongoni mwa viumbe wako. Utujaaliye juu yetu mlinzi atakaye tuokowa kutoka kwenye maangamizi, na utuepushe na maafa. Tufiche kutokana na misiba mibaya. Tuteremshie utulivu wako na funika nyuso zetu kwa nuru ya mahabba yako. Utupe hifadhi kwenye ngome yako. Tukusanye chini ya bawa la uhifadhi wako. Kwa huruma yako na rehema yako. Ewe mwenye huruma nyingi kuliko wote wenye huruma.

NONG'ONO LA SALA YA WATAWA

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Mola wangu umetuweka katika makazi yaliyotuchimbia shimo la vitimbi vyake. Umetuambatanisha kwenye mkono wa umauti katika kamba ya usaliti wake. Kwako twakimbilia toka kwenye vitimbi vya ujanja wake. Kwako twaomba hifadhi ili tusighurike na mng'aro wa mapambo yake. Kwa sababu yenyewe ni yenye kuwaangamiza wayatafutayo, yenye kuwaharibu wakazi wake, yamejaa maafa, misiba. Mungu wangu tushawishi kujiepusha nayo.

Tupe salama mbali nao kwa tawfiki yako na hifadhi yako. Tuvuwe majoho ya kukuhalifu wewe, yasimamie mambo yetu kwa uzuri wa utoshelezaji wako. Tuongezee ziada yetu kutoka wasaa wa rehema yako. Jaalia majazi yetu toka kwenye wingi wa ruzuku zako. Panda mioyoni mwetu miti ya upendo wako tutimiziye nuru ya maarifa yako, tuonjeshe utamu wa msamaha wako na ladha ya maarifa yako, yafurahishe macho yetu siku ya kukutana na wewe kwa kukuomba wewe. Toa kuipenda dunia ndani ya mioyo yetu kama ulivyo wafanyia watu wema miongoni mwa wateule wako, na watu wema miongoni mwa watu wako mahsusi. Ewe mwingi wa rehema kuliko wote wenye kurehemu. Oh wee mkarimu mno kuliko makarimu wote.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU