12
WAULIZE WANAOFAHAMU
MLANGO WA TANO
UNAWAHUSU MAKHALIFA WATATU ABUBAKR, UMAR, NA UTHMAN
Bila shaka Masunni kama tulivyotangulia kueleza, hawakubali kabisa kumkosoa Sahaba yeyote kati ya Masahaba wa Mtume(s.a.w.w)
na wanaamini kwamba, Masahaba wote ni waadilifu. Na iwapo kuna mwanataaluma yeyote aliye huru ataandika juu ya kukosoa matendo ya baadhi ya Masahaba, basi Masunni humshutumu, si hivyo tu, bali humkufurisha japo mwanataaluma huyo atakuwa ni miongoni mwa wanachuoni wao. Hali hii ndiyo iliyowapata baadhi ya wanachuoni huru wa Kimisri na wasio Wamisri, na mfano wa wanachuoni hao ni Sheikh Mahmud Abur-rayyah mwandishi wa kitabu kiitwacho Adh-wau Alas-sunnatil-Muhammadiyyah na kitabu kingine kiitwacho, Shaykhul-Mudhirah, na mwingine ni Qadhi Shaykh Muhammad Amin Al-antaki mwandishi wa kitabu kiitwacho, Limadha Ikhtartu Madh-haba Ahlil-Bait na mwingine ni Sayyid Muhammad ibn Aqil, ambaye alitunga kitabu kiitwacho, An-nasaihul-hafiyah liman yatawallaa Muawiyah. Bali zaidi ya hapo, baadhi ya waandishi wa Kimisri walifikia kiasi cha kumkufurisha Sheikh Mahmud Shal-tut, ambaye alikuwa ni Sheikh wa Chuo cha Azhar, pale tu alipotoa fat-wa kuruhusu kufanya ibada kwa mujibu wa Madhehebu ya Ja'afariyyah.
Sasa ikiwa Sheikh wa Azhar na Mufti wa miji ya Misri anashutumiwa kwa kiasi tu cha kuyakubali kwake Madhehebu ya Kishia ambayo yananasibishwa kwa mwalimu wa Maimamu wa Kisunni ambaye ni Imam Jaafar As-sadiq, basi unafikiri atakuwa na hali gani mtu aliyeyakinai (akaingia) ndani ya Madhehebu haya baada ya kuchunguza na kutosheka na akayakosoa Madhehebu ambayo hapo kabla yeye alikuweko na aliyarithi kutoka kwa baba zake na babu zake? Basi jambo kama hili ndilo ambalo Masunni hawalipi nafasi kabisa, na wanaamini kabisa kuwa (kumkosoa Sahaba) ni kutoka katika dini na ni kutoka katika Uislamu, na hali hii inaleta maana kwa mujibu wa madai yao kwamba, Uislamu umo ndani ya Madhehebu manne tu na mengine yote ni batili. Bila shaka fikra hizo ni fikra zilizoganda, zinafanana na akili ambazo Qur'an inatusimulia, akili za watu ambao walipinga wito wa Mtume tena kwa nguvu, pale Mtume alipowaita wampwekeshe Mwenyezi Mungu na waache kuabudia miungu mingi mbali mbali. Mwenyezi Mungu anasema:
وَعَجِبُوا أَن جَاءَهُم مُّنذِرٌ مِّنْهُمْ وَقَالَ الْكَافِرُونَ هَـٰذَا سَاحِرٌ كَذَّابٌ ﴿٤﴾ أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ ﴿٥﴾
"Walishangaa alipowafikia muonyaji kutoka miongoni mwao, na makafiri wakasema huyu ni mchawi tena muongo, hivi kweli anawafanya miungu wengi awe Mungu mmoja, bila shaka hili ni jambo la kushangaza." (Qur'ani, 38:4 - 5).
Kutokana na yote hayo, mimi naamini kwamba kuna mashambulizi mabaya ambayo yataelekezwa kwangu kutoka kwa hao wang'ang'anizi (wa fikra za Kisunni) ambao wamejifanya kuwa wao ndiyo wanaowasimamia wenzao, basi ikawa kwamba hana haki yeyote yule kutoka kwenye mambo ambayo yamezoweleka kwao japo mazowea haya kama yatakuwa hayana uhusiano wowote na Uislamu. Sasa kama si hivyo ni vipi mtu anayewakosoa Masahaba katika matendo yao ahukumiwe kuwa ni kafiri na ametoka katika dini, wakati ambapo misingi ya dini na matawi yake havina kabisa uhusiano na suala la kuwakosa Masahaba? Baadhi ya watu wenye chuki za Kimadh-heb walikuwa wanaeneza uvumi katika mawazo yao eti kitabu changu kiitwacho Thummah-Tadaitu kinafanana na kitabu cha Sal-man Rushdie, ili tu wawazuwie watu kukisoma, bali zaidi ya hayo wakiwahimiza kumlaani mwandishi wake.
Bila shaka huo ni uchafuzi na ni uzushi na uongo mkubwa ambao Mwenyezi Mungu atamuadhibu mtu kwa ajili hiyo, kwani itakuwaje akilinganishe kitabu (changu) Thummah-Tadaitu ambacho kinaligania kwenye kauli ya Isma ya Mtume(s.a.w.w)
na kumtakasa na kuwafuata Maimamu wa nyumba ya Mtume ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na amewatakasa mno? Iweje yeye akilinganishe na kitabu cha Aya za Shetani ambacho mwandishi wake mwenye kulaaniwa anaushutumu Uislamu na Mtume wa Uislamu(s.a.w.w)
ndani ya kitabu hicho, pia anaiona dini ya Kiislamu kuwa ni maneno ya Shetani? Mwenyezi Mungu anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاءَ لِلَّـهِ وَلَوْ عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ ﴿١٣٥﴾
"Ehyi mlioamini kuweni wenye kusimamia' uadjlifu, wenye kushuhudia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu japokuwa (ushahidi huo) ni dhidi ya nafsi zenu." (Qur'an, 4:135).
Na kwa ajili ya aya hii tukufu, mimi sijali isipokuwa (nataka) radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu na siogopi lawama ya mwenye kulaumu maadamu ninatetea Uislamu sahihi na ninamtakasa Mtume wake Mtukufu kutokana na kila kosa japokuwa kwa kufanya hivyo italazimu kuwakosoa Masahaba (waitwao kuwa) watukufu na hata kama watakuwa ni wale Makhalifatur-rashiduna kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
ndiye bora mno anayestahiki kutakaswa kuliko kiumbe mwingine yeyote. Msomaji yeyote mwenye akili iliyohuru atafahamu kutoka katika vitabu vyangu viwili nilivyoandika kwamba, lengo lililokusudiwa ni nini, kwani siyo suala la kuwakosoa tu Masahaba, bali ni kwa kiwango cha kumtetea Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
na Isma yake na kuondoa mashaka ambayo (watawala wa) Banu Umayyah na Banu Abbas wameyaambatanisha kwenye Uislamu na kwa Mtume wa Uislamu katika kipindi cha karne za mwanzoni ambazo waliwatawala Waislamu katika kipindi hicho kwa nguvu na wakaigeuza dini ya Mwenyezi Mungu vile ambavyo yalivyowatuma malengo yao mabaya, siasa zao butu na matamanio yao machafu.
Njama zao hizi kubwa kwa kweli zimeiathiri sehemu kubwa ya Waislamu ambao waliwafuata kwa nia njema na wakakipokea kila kile kilichosimuliwa (katika hadithi) miongoni mwa riwaya ambazo ni zenye kubadilisha (ukweli) na zingine za uongo zikawa ndizo za kweli na kwamba huo ndiyo Uislamu na ni wajibu kwa Waislamu kufanya ibada zao kwa mujibu wa riwaya hizo bila ya kuzihoji. Na lau Waislamu wangetambua ukweli wa mambo ulivyo wasingewathamini kabisa watawala hao na riwaya zao. Kisha lau historia ingetuletea riwaya zisemazo kwamba Masahaba walikuwa wakitekeleza amri za Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
na kuacha makatazo yake" bila ya kumjadili wala kuyapinga maamuzi yake, na kwamba hawakumuasi zama za mwisho wa maisha yake, basi tungewahukumu kuwa ni waadilifu wote na wala tusingefanya uchunguzi juu ya suala hili (la Masahaba) wala tusingesema chochote.
Ama ukweli ulivyo ni kwamba, miongoni mwao (Masahaba) wamo waongo na wanafiki na miongoni mwao wamo mafasiki kwa mujibu wa Qur'ani na Sunna sahihi iliyothibiti. Pia wamo Masahaba waliohitilafiana mbele ya Mtume(s.a.w.w)
na wakamuasi kuhusu amri (yake) ya kuwaandikia maandiko mpaka wakamtuhumu kwamba anaweweseka, na wakamzuwia kuandika (maandiko hayo). Hawakufuata maamrisho yake pale alipompa uamiri wa jeshi Usamah, na walihitilafiana juu ya suala la Ukhalifa baada yake mpaka wakapuuza kumkosha Mtume na kumuandaa na kumzika, na wakagombana kwa sababu ya Ukhalifa, baadhi yao wakaridhia na wengine wakapinga. (Masahaba) walikhitilafiana katika kila kitu baada ya Mtume(s.a.w.w)
mpaka wakafikia kukufurishana wao kwa wao na kulaaniana wao kwa wao na kujitenga baadhi yao kuwatenga wengine.
(Na kutokana nao) Dini ya Mwenyezi Mungu ambayo ni moja ikawa na madhehebu mengi na maoni yanayotofautiana, kwa hali hii hapana budi tufanye uchunguzi juu ya kiini (cha yote haya) na migawanyiko ambayo imeuchelewesha umma bora uliotolewa kwa watu na kuuporomosha chini ukawa ni umma dhalili usiojua kitu na unaodharaulika mno duniani. Leo hii unavunjiwa heshima yake na sehemu zake takatifu kukaliwa (kwa mabavu), mataifa yake kufanywa makoloni na wananchi wake kufukuzwa na kutawanywa (huku na huko) kutoka katikati ya nchi zao, na wala umma huu hauwezi kuwazuwia wavamizi hawa wala hata kujitoa aibu usoni pake. Ufumbuzi pekee ninavyoamini mimi kuhusu tatizo hili sugu ni kujikosoa kikweli kweli, tuache kuridhika na kujitapa kwa yale yasemwayo kufanywa na hao waliotutangulia ambao hawakubaliki na wamechakaa, wamekuwa ni makumbusho ambayo yako tupu hayana faida hakuna hata anaye yazuru. Ukweli unatuita tukafanye uchunguzi wa kina juu ya sababu za maradhi yetu, kubakia kwetu nyuma, kufarikiana kwetu na kushindwa kwetu mpaka tuweze kuugundua ugonjwa na kisha tuutafutie dawa itakayotuponyesha kabla ya kutumaliza sisi na kuwapata wenzetu wanaokuja.
Hili ndilo lengo linalokusudiwa, na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye kuabudiwa naye ndiye mwenye kuwaongoa waja wake kwenye njia iliyonyooka maadamu lengo letu ni sahihi. Basi una maana gani upinzani wa wale wanaopinga na wale wenye kung'ang'ania ambao hawafahamu isipokuwa kutukana na kushutumu eti kwa hoja ya kuwatetea Masahaba? Watu hawa sisi hatuwalaumu wala hatuwachukii, bali tunawahurumia kwa hali yao hiyo, kwani wao masikini kilichowazuwia (kufahamu) ni dhana zao njema kwa Masahaba. Dhana hiyo imewazuwia wasiweze kuufikia ukweli, wamefanana mno na watoto wa Mayahudi na Wakristo ambao wamefanya dhana njema kwa baba zao na babu zao, na hawakuzilazimisha nafsi zao kufanya juhudi ya kuchunguza ukweli wa Uislamu, wamebakia wanaamini tu yasemwayo na viongozi wao waliotangulia kwamba Muhammad ni muongo na wala siyo Nabii. Mwenyezi Mungu anasema:
وَمَا تَفَرَّقَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَةُ ﴿٤﴾
"Na hawakufarakana wale waliopewa kitabu ila baada ya kuwafikia ukweli" (Qur'an 98:3).
Baada ya kupita karne nyingi imekuwa ni vigumu leo hii kwa Muislamu kumtosheleza Myahudi au Mkristo juu ya itikadi ya Kiislamu, basi unafikiriaje juu ya mtu atakayewaambia kwamba Taurati na Injili ambazo wanapokezana (ni vitabu) vilivyobadilishwa na kisha akawatolea juu ya hilo ushahidi wa Qur'an, basi je, Muislamu huyu atampata mwenye kumsikiliza kutoka kwao? Hali ni hiyo hiyo kwa Muislamu wa kawaida ambaye anaamini kuwa Masahaba wote ni waadilifu na akaing'ang'ania fikra hiyo bila ya dalili yoyote, basi je itawezekana kwa mtu yeyote kumkinaisha kinyume cha hivyo? Ikiwa watu hawa (Masunni) hawawezi hata kumkosoa Muawiyah na mwanawe Yazid na wengine wengi kama hawa ambao wameuharibu Uislamu kwa matendo yao machafu, basi utakuwa na hali gani iwapo utakapowasemesha kuhusu Abubakar, Umar na Uthman ambao ni As-sidiq na Al-faruq na yule aliyestahiwa na Malaika, au (ukawasemesha) kuhusu Aisha Ummul-Muuminina mke wa Mtume(s.a.w.w)
na ni binti ya Abubakar, (Aisha) ambaye tumemzungumzia katika mlango uliopita kwa mujibu wa mapokezi yaliyopokelewa juu yake na waandishi wa sihahi zinazotegemewa kwa Masunni? Na sasa imefika zamu ya kuwazungumzia Makhalifa watatu ili tupate kuonesha baadhi ya matendo yao ambayo yamesajiliwa na Sihahi za Kisunni na Musnad zao na vitabu vya historia vinavyotegemeka kwao, kwanza tubainishe kwamba usemi wa kuwa Masahaba wote ni waadilifu siyo sahihi, na kwamba uadilifu haupatikani hata kwa Masahaba (wanaozingatiwa kuwa ni) wema.
Hatimaye tutawaonesha ndugu zetu Masunni kwamba kukosoa (tunakokusudia) siyo kwa kutukana na kushutumu, bali (makusudio) ni kiasi cha kuweza kuondoa pazia ili kuufikia ukweli kama ambavyo (maelezo hayo ya kukosoa) siyo miongoni mwa uzushi na uongo wa wapinzani (wa dini) kama wanavyodai watu wengi bali yote ni kutoka ndani ya vitabu ambavyo (wao Masunni) wamevihukumu kuwa ndiyo vitabu sahihi na wakashikamana navyo. Abubakr Sidiq katika zama za uhai wa Mtume(s.a.w.w)
Bukhari amethibitisha ndani ya sahihi yake juzuu ya sita ukurasa arobaini na sita Kitabu Tafsir Surah Al-Hujurat amesema: "Ametusimulia Nafii ibn Umar, naye amepokea kwa Ibn Abi Mulaikah amesema: Ilikuwa karibu watukufu wawili waangamie, Abubakar na Umar (r.a), walipaza sauti zao mbele ya Mtume(s.a.w.w)
pale ulipokuja msafara wa Bani Tamim, mmoja wao alimuashiria Aqraa ibn Habis ndugu wa Bani Mujashi'i, na mwingine akamuashiria mtu mwingine, Nafii akasema, jina lake silikumbuki, basi Abubakar akasema kumwambia Umar hakuna ulichokusudia ila kunipinga, Umar akasema sikukusudia kukupinga, basi sauti zao zikapaa katika majibizano hayo, Mwenyezi Mungu akateremsha aya isemayo, Enyi mlioamini msipaze sauti zenu, Ibn Zubair amesema basi Umar alikuwa hamsikilizishi Mtume(s.a.w.w)
baada ya kushuka aya hii mpaka Mtume amuulize na hilo hakulieleza toka kwa baba yake yaani Abubakar."
Kama ambavyo Bukhari ameandika ndani ya sahihi yake juzuu ya nane ukurasa wa 145 Kitabul-I'tisami Bil-kitabu Was-sunnah Babu Mayukrahu minat-ta'amuq Wat-tanazu'u amesema: "Ametueleza Waqi'i kutoka kwa Nafii ibn Umar kutoka kwa Abu Mulaikah amesema: Ilikuwa karibu watukufu wawili waangamie (yaani) Abubakar na Umar pale ujumbe wa Bani Tamim ulipofika kwa Mtume(s.a.w.w)
, mmoja wao akamuashiria Aqraa ibn Habis At-tamimi Al-handhali ndugu wa Bani Mujashi'i, na mwingine akamuashiria mwingine, basi Abubakar akasema kumwambia Umar, bila shaka umekusudia kunipinga, Umar akasema, Sikukusudia kukupinga, basi sauti zao zikapaa mbele ya Mtume(s.a.w.w)
, ikashuka aya isemayo: Enyi mlioamini musipaze sauti zenu zaidi ya sauti ya Mtume na wala msiseme naye kwa sauti ya nguvu kama mnavyosemezana ninyi kwa ninyi visije kuporomoka vitendo vyenu na hali ninyi hamjui, kwa hakika wale wanaoangusha sauti zao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, hao ndiyo Mwenyezi Mungu amezisafisha nyoyo zao kwa kumcha Mungu, basi wanayo maghfira na ujira mkubwa."
Ibn Abi Mulaikah amesema, "Zubair amesema: Basi Umar baada ya hapo na hakumueleza hilo baba yake yaani Abubakar, akawa akizungumza na Mtume(s.a.w.w)
humzungumza kama ndugu ampaye siri hakumsikilizisha jambo Mtume mpaka amuulize. Kama ambavyo Bukhari amethibitisha ndani ya sahihi yake juzuu ya tano ukurasa 116 Kitabul-maghazi Wafdu Bani Tamim amesema: "Ametusimulia Hisham ibn Yusuf kwamba Ibn Juraij aliwasimulia kutoka kwa Ibn Abi Mulaikah kwamba, Abdallah ibn Zubair aliwaeleza kuwa ulifika kwa Mtume(s.a.w.w)
, ujumbe kutoka kwa Bani Tamim, Abubakar akasema, Mpe Uamiri Al-Qa'aqa'a ibn Ma'abad ibn Zurarah, Umar akasema Hapana, mpe uamiri Aqra'a ibn Habis, Abubakar akasema huna nia nyingine ila kunipinga. Umar akasema; sikukusudia kukupinga, wakajibizana mpaka sauti zao zikapaa juu ikashuka aya kuhusu tukio hilo isemayo:
Enyi mlioamini, msitangulize kusema lenu mbele ya (neno la) Mwenyezi Mungu na Mtume wake
. Mpaka mwisho wa aya.
Kinachoonekana wazi hapa kupitia riwaya hii ni kwamba Abubakar na Umar hawakufanya heshima mbele ya Mtume(s.a.w.w)
kwa mujibu wa adabu za Kiislamu, na walijitanguliza mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake bila idhini, wala Mtume hakuwaomba watoe maoni yao kuhusu kumpa uamiri mtu yeyote miongoni mwa Bani Tamim, kisha wasitosheke na hali hiyo mpaka wakazozana mbele ya Mtume na zikapaa sauti zao mbele yake bila ya heshima wala kujali mambo yanayowalazimu katika (kuonesha) tabia na adabu (njema) ambazo haiwezekani kwa yeyote miongoni kwa Masahaba kukosa kuzifahamu au kujifanya hazifahamu baada ya Mtume kumaliza muda wa uhai wake akiwalea na kuwafundisha. Lau tukio hili lingekuwa limetokea mwanzoni mwa kuja kwa Uislamu tungewatakia samahani Masheikh hawa wawili juu ya tendo lao hilo, na tungejaribu kupata baadhi ya tafsiri. Lakini riwaya hizi zinathibitisha mambo ambayo hayatoi nafasi ya kuwa na mashaka kwamba tukio hili lilitokea mwishoni mwa uhai wa Mtume(s.a.w.w)
, kwani ujumbe wa Bani Tamim ulifika kwa Mtume(s.a.w.w)
mwaka wa tisa wa Hijra, na baada ya hapo Mtume hakuishi isipokuwa miezi michache, kama ambavyo wanashuhudia pia wanahistoria na wanachuoni wa hadithi ambao wameeleza juu ya kufika kwa ujumbe huo kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Isitoshe hili ni tukio ambalo Qur'ani imelizungumza ndani ya sura za mwisho pale inaposema: "Utakapokuja msaada wa Mwenyezi Mungu na ushindi, utawaona watu wanaingia katika dini ya Mwenyezi Mungu kwa wingi."
Ikiwa mambo yako namna hii, ni vipi wenye kutoa udhuru wanatoa udhuru kuhusu msimamo wa Abubakar na Umar (namna ulivyokuwa) mbele ya Mtume(s.a.w.w)
, na lau riwaya ingeishia kueleza msimamo waliouonesha Masahaba hawa wawili, basi tusingepata nafasi ya kukosoa, lakini Mwenyezi Mungu ambaye hastahi chochote katika haki amelisajili tukio hilo na akateremsha Qur'ani kuhusiana nalo itakayokuwa ikisomwa, na ndani yake yamo maonyo na makemeo kwa Abubakar na Umar kwamba, matendo yao yataporomoka iwapo watarudia tendo kama hilo, kiasi kwamba mpokezi wa riwaya ya tukio hili ameanza maneno yake kwa kusema: "Karibu watukufu wawili waangamie, (akimaanisha) Abubakar na Umar."
Mpokezi wa riwaya inayohusu tukio hili ambaye ni Abdallah ibn Zubair anajaribu kutukinaisha kwamba Umar baada ya kushuka aya hii kuhusu tendo lake kwamba yeye Umar anapomzungumza na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
akawa hamsikilizishi sauti yake mpaka Mtume humuuliza pamoja na kwamba hakumwambia babu yake Abubakar. Lakini historia na matukio ambayo wameyataja wana hadithi yanathibitisha kinyume cha hivyo, na inatosha ukumbuke ile siku ya alhamisi kabla ya kufariki Mtume(s.a.w.w)
kwa siku tatu, tunamkuta Umar mwenyewe alitamka ile kauli yake mbaya akasema: "Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu anaweweseka, kinatutosha kitabu cha Mwenyezi Mungu." Kwa sababu yake watu wakahitilafiana, wapo wanaosema sogeeni kwa Mtume akuandikieni, na wengine wanasema kama alivyosema Umar, basi walipozidisha vurugu na kukhitilafiana, Mtume wa Mwenyezi Mungu akawaambia, Ondokeni haifai kufanya makelele mbele yangu." Maana ya wingi wa fujo, makele, kuhitilafiana na kugombana inajulisha kwamba, wao walivuka kila mipaka ambayo Mwenyezi Mungu aliwawekea katika suratul-huj-rati kama ilivyotangulia.
Haiwezekani kututosheleza kwamba, kutofautiana kwao na vurugu zao eti zilikuwa kwa kunong'ona kwenye masikio, bali inafahamika kutokana na yote hayo kwamba wao walipaza sauti zao mpaka hata wanawake ambao walikuwa nyuma ya pazia na hijabu walishiriki katika fujo na wakasema: "Sogeeni kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
akuandikieni maandiko." Umar akawambia: "Ninyi ndiyo kama wale wanawake waliomfanyia vitimbi Yusuf, anapokuwa (Mtume) mgonjwa mnalia na akipona mnamfanyia vitimbi."
Mtume akasema kumwambia Umar, "Waacheni, kwani wao ni bora kuliko ninyi." Na tunachokifahamu katika yote haya ni kwamba, wao hawakufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu katika kauli yake aliposema: "Enyi mlioamini msitangulize (kusema lenu) mbele ya (neno la) Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wala msipaze sauti zenu zaidi ya sauti ya Mtume." Hawakukiheshimu cheo cha Mtume na wala hawakufanya adabu pale walipomtuhumu kuwa anaweweseka. Hapo kabla Abubakr alikwisha kutamka maneno machafu mbele ya Mtume(s.a.w.w)
pale alipomwambia Ur-wah ibn Mas-oud, "Amsas bibidhril-laab." Na Al-QastaJani ambaye ndiye aliyeisherehesha sahihi Bukhari amesema katika kuifafanua ibara hii kwamba, suala la kufyonza Bidhri ni miongoni mwa matusi makubwa mno kwa Waarabu.
Sasa basi, ikiwa maneno kama haya yanatamkwa mbele ya Mtume(s.a.w.w)
basi nini maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema: "Na wala msiseme naye kwa sauti ya nguvu kama mnavyosemezana ninyi kwa ninyi.?" Na ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ana tabia njema ya hali ya juu kama alivyomsifu Mola wake, na itakapokuwa Mtume ni mwingi wa haya kuliko mwali aliye ndani kama walivyoyathibitisha haya Bukhari na Muslim. Masheikh hawa wawili Bukhari na Muslim wamebainisha wazi kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
hakuwa muovu wala mwenye kueneza maovu na alikuwa akisema: "Hakika mbora wenu ni mzuri wenu kwa tabia." Basi imekuwaje Masahaba wake hao waliokuwa karibu yake mno hawakuathirika kwa tabia hii tukufu? Zaidi ya yote haya ni kwamba, Abubakr hakutekeleza amri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
pale Mtume alipompa uamiri Usamah bin Zaid na Abubakr akawa miongoni mwa askari walio chini ya uamiri wa Usamah (lakini Abubakar hakutii amri hiyo) na Mtume(s.a.w.w)
aliwakemea mno wale waliobakia nyuma (wasiende pamoja na Usamah katika jeshi hilo) mpaka akasema: "Mwenyezi Mungu amlaani yeyote atakayebaki nyuma asitoke na jeshi la Usamah." Haya aliyasema baada ya kumfikia habari yeye Mtume juu ya upinzani wa wapinzani dhidi yake kutokana na kumpa uamiri Usamah ibn Zaid, jambo ambalo wanahistoria wengi wamelitaja.
Hali ni kama hiyo kwamba, Abubakr alikimbilia Saqifah na akashiriki kumtenga Ali ibn Abi Talib kutoka kwenye Ukhalifa, na (yeye Abubakar alipokuwa akikimbilia Saqifah) aliuacha mwili wa Mtume na wala hakuona umuhimu wa kumkosha na kumvisha sanda na kufanya maandalizi (yanayohusika) na hatimaye kumzika, bali aliyaacha yote hayo kwa kugombea cheo cha Ukhalifa na uongozi ambao ndiyo iliyokuwa hamu yake. Kama ni hivyo uko wapi huo usahaba na urafiki unao daiwa (kuwa alikuwa nao Abubakar kwa Mtume)?
Na je, iko wapi tabia njema (anayostahiki kuwa nayo)? Mimi unanishangaza sana msimamo wa Masahaba hawa kuhusu Mtume wao ambaye alimaliza muda wa uhai wake akiwaongoza na kuwalea (malezi bora), na kuwapa nasaha mbali mbali Mtume ambaye "Yanamuhuzunisha yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni na ni mpole na mwenye huruma kwa walioamini." Matokeo yake walimuacha juu ya kitanda cha mauti na wao wakakimbilia Saqifah ili kumchagua mmoja wao awe Khalifa wao. Na sisi leo hii tunaishi katika karne ya ishirini, karne ambayo tunaisema kuwa ni karne mbaya, na kwamba eti tabia za watu zimeharibika na miongozo nayo imetelekezwa. Lakini pamoja na hayo hapana shaka Waislamu (wa leo hii) anapokufa jirani yao hufanya haraka kumshughulikia mpaka wanamsitiri kaburini mwake hali ya kuwa wakitekeleza kauli ya Mtume(s.a.w.w)
aliposema: "Kumkirimu maiti ni kumzika."
Bila shaka Amirul-Muuminina Ali ibn Abi Talib aliyaumbua matukio hayo waliyoyatenda pale aliposema: "Amraa Wallahi, hakika mwana wa Abu Qahafah (Abubakr) aliuvaa (aliutwaa) Ukhalifa hali ya kuwa anafahamu kwamba nafasi yangu juu Ukhalifa ni sawa na mkono (mshikio) ulioko kwenye jiwe la kusagia." Kisha baada ya hapo, Abubakr aliruhusu nyumba ya bibi Fatmah ihujumiwe na kutishiwa kuchomwa moto ikiwa hawakutoka humo kwenda kumbai Abubakr wale wote waliopinga (Ukhalifa wake) na yalitokea yaliyotokea miongoni mwa mambo ambayo wanahistoria wameyataja ndani ya vitabu vyao na wapokezi nao wakayanakili zama hadi zama nyingine. Nasi tutakubainishia ewe msomaji sehemu tu ya hayo, na ni juu ya mwenye kutaka ziyada kuvisoma vitabu vya historia.