13
WAULIZE WANAOFAHAMU
ABUBAKR BAADA YA UHAI WA MTUME (s.a.w.w)
NAMNA ALIVYOMPINGA BIBI FATMAH, KWA KUMNYANG'ANYA HAKI YAKE
Bukhari amethibitisha ndani ya sahih yake juzuu ya tano ukurasa 82 Kitabul-Maghazi Babu Ghaz-watukhaibar amesema: "Imepokewa kutoka kwa Ur-wah naye kutoka kwa Aisha kwamba Fatmah
binti ya Mtume(s.a.w.w)
alituma ujumbe kwa Abubakr akimuomba ampe mirathi yake kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
miongoni mwa mali ambazo Mwenyezi Mungu alimpa Mtume hapo Madina na Fadak na sehemu iliyobaki katika khumsi ya Khaibar.Abubakar akasema: Bila shaka Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Sisi (Mitume) haturithiwi tunachokiacha ni sadaka, hakika watakula kizazi cha Muhammad katika mali hii, na kwa hakika Wallahi sibadilishi chochote katika sadaka ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kutoka katika hali iliyokuwa nayo katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na nitaitumia kama alivyoitumia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w)
. Basi Abubakar akakataa kumpa chochote bibi Fatmah
na ndipo bibi Fatimah alipomkasirikia Abubakar kuhusu jambo hilo na hakumsemesha mpaka alipofariki, na aliishi miezi sita tu baada ya kufariki Mtume(s.a.w.w)
."
Bibi Fatmah alipofariki, mumewe (ambaye ni Sayyidna Ali ibn Abi Talib) alimsalia na akamzika usiku wala hakumruhusu Abubakr kuhudhuria maziko hayo. Katika uhai wa bibi Fatmah
Imam Ali
alikuwa akithaminiwa mno na watu, lakini alipofariki watu wakampuuza Imam Ali, ndipo alipotaka mapatano na Abubakar na akambai, na kabla ya miezi hiyo sita alikuwa hakumbai.
Naye Muslim ameandika ndani ya sahihi yake, juzuu ya pili Kitabul-jihad mlango unaohusu kauli ya Mtume, "La Nuurathu Mataraknahu Sadaqah" Imepokewa toka kwa Ummul-Muuminina Aisha (r.a) kwamba, baada ya kufa Mtume bibi Fatmah
binti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
alimuomba Abubakr, mirathi yake katika alivyoviacha Mtume(s.a.w.w)
na mali aliyompa Mwenyezi Mungu, basi Abubakar akasema: "Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema, Haturithiwi tulichokiacha ni Sadaka
." Basi Fatmah binti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu akakasirika na akakata mawasiliano na Abubakar na alibakia hivyo mpaka akafariki. Na aliishi miezi sita tu baada ya Mtume(s.a.w.w)
, Aisha amesema: "Fatmah alikuwa akimuomba Abubakr ampe sehemu yake iliyoachwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu katika Khaibar na Fadak na sadaka yake iliyoko Madina, basi Abubakar alimkatalia Fatmah na kusema, Siwezi kuacha chochote ambacho Mtume alikifanya ila nami nitakifanya, kwani mimi nachelea ikiwa nitaacha kitu katika mambo yake nitapotea
."
Ama sadaka ya Mtume(s.a.w.w)
ya pale Madina, Umar aliitoa kwa Ali na Abbas, na ile ya Khaibar na Fadak, Umar alizizuwiya na akasema: "Hizo ni sadaka za Mtume wa Mwenyezi Mungu, zilikuwa ni haki yake ambayo inamuhusu yeye na mambo yake, usimamizi wake uko chini ya yeyote atakayetawala, basi zimebakia hivyo hadi leo
."
Pamoja na kuwa Masheikh hao wawili (Bukhari na Muslim) kuikata riwaya hii na kuifupisha ili ukweli usije ukaonekana kwa wale wanaotafiti, lengo lao wamekusudia kulinda heshima ya Makhalifa hawa watatu, na tabia hii (ya kuficha mambo) ni fani yao inayofahamika. Kuhusu (tabia hii ya) Bukhari na Muslim ndani ya maudhui hii, hivi punde Mwenyezi Mungu apendapo tutaifanyia uchambuzi na tutakutosheleza.
Jambo la kuzingatia ni kwamba, riwaya hizi ambazo wao wamezifanyia marekebisho, zinatosha sana kueleza mazingira halisi ya Abubakr ambaye alikanusha madai ya bibi Fatmah, jambo ambalo lilimfanya bibi Fatmah amkasirikie na kumsusa mpaka alipofariki, na mumewe akamzika usiku tena kwa siri kutokana na usia wa bibi Fatmah mwenyewe bila kumruhusu Abubakar (kuhudhuria mazishi hayo). Kama ambavyo tunafaidika kutokana na riwaya hizi kwamba Ali hakumpa baia Abubakar muda wote wa miezi sita ya uhai wa bibi Fatmah baada ya kufariki baba yake, na kwamba Ali
alilazimika kumbai Abubakar pale alipoona watu wamempuuza, basi akataka mapatano na Abubakar.
Na kitu walichokibadilisha Bukhari na Muslim miongoni mwa ukweli ni kuwa madai ya bibi Fatimah
kwamba baba yake ambaye ndiye Mtume wa Mwenyezi Mungu alimpa Fadak katika zama za uhai wake na hiyo siyo katika mirathi, na tujaalie kwamba Mitume hawarithiwi kama alivyoyaeleza hayo Abubakr kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
, na bibi Fatmah akayapinga maelezo hayo na akayalinganisha maelezo ya Abubakr kwenye Qur'ani ambayo inasema kuwa "Na Sulaiman akamrithi Daud
." Basi Fadak haingii katika hadithi hii inayodaiwa, kwani Fadak ni zawadi siyo miongoni mwa mirathi kwa namna yoyote ile. Kwa ajili hiyo basi utawakuta wanahistoria wote, wafasiri na watu wa hadithi wanaeleza kwamba bibi Fatmah alidai kwamba Fadak ni mali yake, na Abubakr akamkanusha na kumtaka alete ushahidi juu ya madai yake, basi akamleta Ali ibn Abi Talib na Ummu Aiman, Abubakr hakuukubali ushahidi wa hawa na akauona kuwa hautoshelezi.
Maelezo kama haya ameyakubali Ibn Hajar ndani ya As-Sawaiqul-Muhriqa pale alipoeleza kwamba bibi Fatimah alidai kwamba, Mtume(s.a.w.w)
alimzawadia Fadak, na hakuleta shahidi juu ya hilo isipokuwa Ali ibn Abi Talib na Ummu Aiman kwa hiyo kiwango cha ushahidi wake hakikukamilika.
Na kama alivyosema Al-Imam Fakhrur-razi ndani ya tafsiri yake kuwa, Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
alipofariki bibi Fatmah
alidai kwamba Mtume alimzawadia Fadak, basi Abubakr akamwambia Fatmah, "Wewe ni mtu muhimu mno kwangu na ni mwenye kupendelewa mno kwangu mimi kuliko wengine, lakini mimi sielewi usahihi wa kauli yako kwa hiyo siwezi kukupa." Anasema. (Bibi Fatmah) akamshuhudisha Ummu Aiman huru wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, lakini Abubakar akamtaka bibi Fatmah alete shahidi ambaye ushahidi wake utakubalika katika sheria, ikawa hakupatikana. Madai ya Fatimah
kwamba Fadak ni zawadi aliyopewa na Mtume(s.a.w.w)
na kwamba Abubakar aliyapinga madai hayo na hakuukubali ushahidi wa Ali na Ummu Aiman, ni jambo linalofahamika kwa wanahistoria na Ibn Taimiyyah amelieleza, na mwandishi wa Siiratul-halabiyyah, na Ibnul-Qayyim Al-jauziyyah na wengineo.
Lakini Bukhari na Muslim wamelifupisha tukio hili na hawakutaja isipokuwa ombi la bibi Fatimah juu ya mirathi peke yake, ili tu wamfikirishe msomaji kwamba bibi Fatmah alimkasirikia Abubakr mahala ambapo hapakustahiki kwani Abubakr hakufanya ila kile alichokisikia kwa Mtume(s.a.w.w)
, kwa hiyo bibi Fatimah alifanya dhuluma na Abubakr alidhulumiwa. Bukhari na Muslim waliyafanya vote haya ili kulinda heshima ya Abubakr bila kutilia maanani uaminifu katika kunakili wala ukweli wa hadithi ambazo zilikuwa zinaumbua aibu za Makhalifa na kuondoa uzushi na vizuwizi vilivyowekwa na Banu Ummayyah na wasaidizi wa Makhalifa, hilo hawakujali japokuwa litakuwa linaharibu heshima ya Mtume mwenyewe(s.a.w.w)
au binti yake Fatmah
(bora tu Makhalifa wao wasalimike).
Ni kwa ajili hiyo tu ndiyo maana Bukhari na Muslim wamemiliki uongozi wa wanachuoni wa hadithi kwa Masunni na hao Masunni wakavizingatia vitabu vyao (Bukhari na Muslim) kuwa ndiyo vitabu sahih mno baada ya kitabu cha Mwenyezi Mungu. Huu ni uzushi usiokuwa na dalili ya kielimu na tutauchambua katika mlango maalum mpaka tuudhihirishe ukweli kwa mwenye kuutaka apendapo Mwenyezi Mungu. Pamoja na hayo sisi tunawahoji Bukhari na Muslim ambao wamezithibitisha fadhila nyingi za Fatmah
kwa mukhtasari, lakini unatosheleza kumkosoa Abubakar ambaye alimfahamu bibi Fatimah na daraja yake mbele ya Mtume(s.a.w.w)
zaidi kuliko walivyomfahamu kina Bukhari na Muslim. Pamoja na hayo Abubakr alimkanusha bibi Fatmah na wala hakukubali ushahidi wake wala ushahidi wa mumewe ambaye Mtume amesema kumuhusu kwamba "Ali yu pamoja na haki, na haki iko pamoja na Ali, haki inazunguka popote azungukiapo. Na hebu tutosheke na ushahidi wa Bukhari na ushahidi wa Muslim kuhusu yale aliyoyathibitisha mwenyewe Mtume(s.a.w.w)
juu ya ubora wa binti yake bibi Fatimah.
Fatmah ni Maa'sum kwa mujibu wa maandiko ya Qur'an Muslim amethibitisha ndani ya sahihi yake juzuu ya saba, mlango wa Fadhail za Ahlul-Bait. Aisha (r.a) amesema: "Mtume(s.a.w.w)
alitoka asubuhi mapema akiwa amejitanda guo la sufi nyeusi, basi akaja Hasan ibn Ali akamuingiza humo, kisha akaja Husein ibn Ali naye akamuingiza pamoja naye, kisha alikuja Fatmah akamuingiza na hatimaye akaja Ali naye akamuingiza kisha akasema: "Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu enyi watu wa nyumba (ya Mtume) na kukutakaseni mno." Sasa basi, ikiwa Fatmah
ni mwanamke pekee ambaye Mwenyezi Mungu amemuondolea uchafu na kumtakasa kwa kumuepusha na kila aina ya dhambi na maasi katika umma huu basi inakuwaje Abubakar anamkanusha na kumtaka ushahidi, ewe bwana unayaona hayo? Fatmah ndiye mwanamke bora miongoni mwa wanawake waumini, na ndiye mwanamke bora katika umma huu.
Bukhari amethibitisha ndani ya sahih yake juzuu ya saba katika Kitabul-isti-idhan ndani ya mlango wa Man Najaa Baina yadain-nas walam Yukhbir Bisirri Sahibih Faidha Maata Akhbara Bih, na Muslim katika Kitabul-Fadhail, Imepokewa kutoka kwa Ummul-Muuminina Aisha amesema: "Sisi wakeze Mtume(s.a.w.w)
wote tulikuwa mbele ya Mtume(s.a.w.w)
hapana aliyekosekana miongoni mwetu, basi Fatmah
akaja akitembea, Wallahi hapakufichikana chochote katika mwendo wake kutokana na mwendo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
, basi Mtume alipomuona Fatmah akasema, karibu binti yangu, kisha akamkalisha kuliani kwake au kushotoni kwake, halafu akamnong'oneza, Fatmah akalia sana. Mtume alipoiona huzuni yake akamnong'oneza kwa mara ya pili, mara Fatmah akacheka, mimi nikamwambia, Mimi ni miongoni mwa wakeze (Mtume) lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu amekuhusisha wewe kwa jambo la siri kati yetu kisha wewe unalia.
Mtume wa Mwenyezi Mungu aliposimama nikamuuliza Fatmah, Ni jambo gani alikunong'oneza? Akasema: Siwezi kutoa siri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume alipofariki nikamwambia Fatmah, Nimekukusudia wewe kwa jambo ambalo nina haki nalo juu yako hujanieleza bado. Bibi Fatmah akasema, Amma sasa ni sawa kukueleza. Akanieleza akasema, Wakati aliponinong'oneza katika jambo la kwanza alinieleza kuwa, Jibril alikuwa akija kumuaridhia Qur'an kila mwaka mara moja na kwamba mwaka huu ameniaridhia mara mbili, na wala sioni isipokuwa muda umekaribia, basi mche Mungu na uwe mvumilivu, kwani mimi ndiye mtangulizi bora kwako wewe, ndipo nilipolia kilio changu ulichokiona, na alipoiona huzuni yangu akaninong'oneza mara ya pili akasema: Ewe Fatmah huridhii kuwa wewe ndiwe mwanamke bora miongoni mwa waumini au mwanamke bora wa umma huu?"
Ikiwa Fatmah
ndiye mwanamke bora kuliko wanawake wa waumini kama yalivyothibiti hayo kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Abubakar anamkatalia Fatmah madai yake ya Fadak na wala hakukubali ushahidi wake, je ni ushahidi gani mwingine utakaokubalika baada yake unaoudhania ewe bwana? Fatmah ndiye mbora wa wanawake wa peponi. Bukhari amethibitisha ndani ya sahihi yake katika juzuu ya nne ndani ya Kitabu bad-il-khalq; Babu Manaqib Qarabatu Rasulillahi, Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
"Fatmah ni mbora wa wanawake wa peponi." Basi kama Fatmah ni mwanamke bora kuliko wanawake wote wa peponi, na maana yake ni kwamba yeye ni mwanamke bora ulimwenguni kwani watu wa peponi siyo ummati wa Muhammad peke yao kama inavyofahamika, sasa vipi Abubakr anamkanusha? Je, hawakudai kwamba laqab ya As-sidiq (ya Abubakr) aliipata kwa kuwa yeye alikuwa akisadikisha kila alilokuwa akilisema sahibu yake ambaye ni Mtume Muhammad, sasa ilikuwaje hakumsadiki Mtume(s.a.w.w)
juu ya mambo aliyoyasema kuhusu bibi Fatmah?
Fatmah ni sehemuya mwili wa Mtume(s.a.w.w)
, na Mtume hukasirika iwapo Fatmah atakasirika. Bukhari amethibitisha ndani ya sahih yake, juzuu ya nne Kitabu Bad-ilkhalq Babu Manaqib Fatmah
Bintun-nabiyyi(s.a.w.w)
amesema: "Ametusimulia Abul-walid, ametusimulia Ibn Uyanah kutoka kwa Amr ibn Dinar kutoka kwa Abi Mulaikha, kutoka kwa Al-Musawar ibn Mukhrimah, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
amesema: Fatmah ni sehemu itokanayo nami, yeyote mwenye kumkasirisha basi kanikasirisha mimi." "Fatmah ni sehemu itokanayo nami kinanikera kinachomkera na kinaniudhi kinachomuudhi."
Ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
anakasirika kwa kukasirika Fatmah na anaudhika kwa kuudhika kwake, basi maana ya maneno hayo ni kuwa yeye Fatmah ni ma'asum hatendi makosa, vinginevyo isingefaa kwa Mtume kusema namna hiyo, kwani mtu atendaye maasi uwezekano wa kumbughudhi na kumkera upo hata kama ana cheo kikubwa namna gani. kwani sheria ya Kiislamu haiangalii aliyekaribu au yule wa mbali, awe ni mwenye heshima (kubwa namna gani) au mnyonge, tajiri au masikini. Na iwapo mambo yatakuwa namna hiyo, iweje basi Abubakr asijali kukasirika kwa Fatmah mpaka akafa hali ya kuwa kamkasirikia, bali alimsusia kabisa na hakumsemesha mpaka alipofariki huku akimuombea dua (ya maangamizo) katika kila sala yake (aliyosali), kama yalivyo maelezo hayo ndani ya kitabu cha historia cha Ibn Qutaibah na wengineo mioneoni mwa wanahistoria.
Naam, hakika mambo haya ni ukweli wenye uchungu na ni ukweli unaouma ambao unatikisa nguzo na kutikisa imani, kwani mchunguzi muadilifu mwenye kujitenga kwa ajili ya kutafuta haki na ukweli hana njia isipokuwa kukubali kwamba, Abubakar alimdhulumu bibi Fatmah na akampokonya haki yake. Jambo hili lilikuwa ndani ya uwezo wake (Abubakr) akiwa ni Khalifa wa Waislamu angemridhia bibi Fatmah na ampe kile alichokidai, kwa kuwa alikuwa mkweli na Mwenyezi Mungu anashuhudia ukweli wake, na Mtume pia ashuhudia ukweli wake, na Waislamu wote akiwemo Abubakr wanashuhudia ukweli wake, ni siasa tu ndio inayogeuza kila kitu kwa hiyo mkweli huwa muongo na muongo huwa mkweli.
Naam, hakika hii ni aina mojawapo ya njama zilizofumwa ili kuwaweka kando Ahlilbait mbali na cheo na daraja ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwapa na zilianza kwa kumuweka Ali ibn AbiTaalib kando mbali na Ukhalifa, na kupokonya zawadi ya bibi Fatmah na mirathi yake, kumfanya muongo na kumnyanyasa ili pasibakie heshima yoyote katika mioyo ya Waislamu. Njama ziliendelea mpaka Ali, Hassan na Hussein, wakauawa. Ama kwa upande wa Hussein aliuliwa yeye pamoja na watoto wake bila huruma, na akina mama waliobakia walichukuliwa mateka. Njama hizo hazikuishia hapo tu, bali Mashia wa Ahlilbait, wapenzi wao na wafuasi wao waliuliwa, na hapana shaka zingali zinaendelea hadi leo na zinafanya kazi yake na zinatoa matunda ya kazi yake. Naam Muislamu yeyote aliyehuru na muadilifu atatambua asomapo vitabu vya historia na kutafiti ukweli na kuiweka kando batili, ataona kuwa Abubakr ni wa kwanza kabisa kuwafanyia dhulma Ahlilbait, na atatosheka na kuisoma sahihi Bukhari tu vile itakapomwekea wazi ukweli endapo atakuwa mtafiti wa kweli.
Bukhari ni huyo (umjuaye) pia Muslimu, wote wanakiri kuwa Abubakar Sidiq alimkubalia sahaba yeyote yule wa kawaida tu kwa dai lake, na akamkatalia Fatuma Zahra na kuudai kuwa ni muongo hali ya kuwa Fatumah Zahra ni mwanamke bora katika wanawake wa peponi na ni yule ambaye Mwenyezi Mungu ameshuhudia kwa kumuondolea madhambi na kumfanya mtakatifu pia Abubakr alimfanya Ali kuwa ni muongo pia Umu Aiman naye akamfanya kuwa ni muongo. Hebu soma sasa uone wayasemayo Bukhari na Muslim. Bukhari ameandika katika sahihi yake juzuu ya tatu kitabu cha Shahadaati mlango wa Man amara bi injazil-waadi. Na Muslim katika sahihi yake ndani ya kitabu cha Al-fadha-il mlango wa Maasuila Rasulullahi shai-an qat, faqala -la, wakathurat a'taihi. Imepokewa kutoka kwa Jabir ibn Abdillah (r.a) amesema: Alipokufa Mtume(s.a.w.w)
, kuna mali ilimfikia Abubakar kutoka kwa Al-a'laa ibn Al-Hadhrami, Abubakr akasema: Yeyote ambaye alikuwa na deni kwa Mtume(s.a.w.w)
au alikuwa na ahadi kwa Mtume basi na aje kwetu, Jabir akasema, Mimi, nikasema, Mtume wa Mwenyezi Mungu aliniahidi kuwa atanipa hivi na hivi na hivi, akakunjua mikono yake mara tatu, basi zikahesabiwa mikononi mwangu mia tano, kisha mia tano, kisha mia tano."
Je, hivi kuna mtu atakayemuuliza Abubakr, "Ni kwa nini alimuamini Jabir ibn Abdallah katika madai yake kwamba Mtume(s.a.w.w)
alimuahidi kumpa hivi na hivi na hivi, kisha Abubakr akaijaza mikono yake mara tatu kwa kiwango cha elfu moja mia tano bila ya kumtaka alete shahidi japo mmoja tu ili kuthibitisha madai yake? Na je Jabir ibn Abdillahi alikuwa mcha Mungu na mtakatifu mno kuliko Fatmah ambaye ni mwanamke bora ulimwenguni? Cha kushangaza kuliko yote ni kwa yeye kuukataa ushahidi wa mumewe Fatmah; Ali ibn Abi Talib ambaye Mwenyezi Mungu amemtakasa mno na akajaalia kuwa ni faradhi kwa Waislamu wote kumtakia rehma (Ali) kama wamtakiavyo rehma Mtume(s.a.w.w)
. Na ni huyo huyo Ali ibn Abi Talib ambaye Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema kuwa, "Kumpenda Ali ni (alama ya) imani na kumchukia ni (alama ya) unafiki.
Zaidi ya hayo ni kwamba, Bukhari mwenyewe amethibitisha katika tukio jingine linalotupatia picha halisi ya dhulma aliyofanyiwa bibi Fatmah na watu wa nyumba ya Mtume(s.a.w.w)
. Bukhari amethibitisha ndani ya sahihi yake Baku maala yahillu liahadin an yar-jia' fi hibatih wasadaqatih, Kitabul-hibat wafadhliha wat-tahridh a'laiha: Amesema kwamba, "Watoto wawili wa Suhaib rum wa Judh'an walidai nyumba mbili na chumba kimoja na kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alimpa vitu hivyo Suhaib, basi Mar-wan akasema: Nani atakushuhudieni juu ya madai yenu? Wakasema, Ibn Umar, Akamwita akashuhudia kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
alimpa Suhaib nyumba mbili na chumba kimoja, basi Mar-wan akaukubali ushahidi wake kwa jamaa hao" Tazama ewe Muislamu matendo haya na maamuzi haya ambayo yanatekelezwa kwa wengine na wengine yanakataliwa, je, hii siyo miongoni mwa dhulma na hila? Na ikiwa Khalifa wa Waislamu anaamua kwa faida ya wanaodai kwa kiasi tu cha ushahidi wa Ibn Umar, basi je, Muislamu anaweza kujiuliza ni kwa nini basi ushahidi wa Ali ibn Abi Talib ulipingwa pia ushahidi wa Ummu Aiman (nao ulikataliwa yeye) pamoja na Imam Ali? (Lakini ni lazima pia ufahamu kwamba) ushahidi wa mwanamume na mwanamke una nguvu kuliko ushahidi wa mwanamume mmoja peke yake ikiwa hatutataka kukifikia kile kiwango ambacho Qur'ani inakitaka.
Au tuseme watoto wa Suhaib ni wakweli mno katika madai yao kuliko Binti wa Mtume(s.a.w.w)
, na kwamba Abdallah ibn Umar ni mkweli mno mbele ya watawala hao wakati ambapo Ali siyo mkweli kwa watawala hao? Ama madai yasemayo kwamba Mtume(s.a.w.w)
harithiwi, nayo ni ile hadithi aliyokuja nayo Abubakar, na bibi Fatmah akaipinga kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu ambacho ni hoja isiyopingika kamwe, kwani imesihi hadithi kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
aliposema: "Itakapokujieni hadithi kutoka kwangu basi ipimeni kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu, ikikubaliana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu itumieni na ikienda kinyume ipigeni ukutani."
Basi hapana shaka hadithi hii inapingwa na aya nyingi katika Quran, je yuko mtu atakayemuuliza Abubakr ni kwa nini ushahidi wa Abubakr peke yake unakubalika katika riwaya ambayo inapinga aya na akili, isitoshe kitabu cha Mwenyezi Mungu kinaipinga hadithi hiyo? (Lakini jambo la kushangaza ni kwamba), ushahidi wa bibi Fatmah haukukubalika hali ya kuwa unaafikiana na nukuu na akili, na haupingani na Qur'an!! Zaidi ya hapo ni kwamba, pamoja na kuwa Abubakr daraja yake ilipanda na wanaomuunga mkono na wanaomtetea wakamtengenezea chungu nzima ya ubora, bila shaka hawezi kufikia daraja ya bibi Fatmah ambaye ni mwanamke bora ulimwenguni, wala (Abubakr) hawezi kufikia daraja ya Ali ibn Abi Talib ambaye Mtume(s.a.w.w)
amemtukuza juu ya Masahaba wote katika kila nyanja, nazitaja baadhi yake kama mfano:
Siku aliyompa bendera na Mtume akamthibitisha kwamba yeye Ali anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Mwenyezi Mungu na Mtume wake nao wanampehda Ali. Na siku hiyo Masahaba waliingojea kwa hamu kila mmoja akitaraji kupewa yeye, basi Mtume hakumpa isipokuwa Ali. Pia Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema kuhusu Ali kwamba, "Bila shaka Ali anatokana nami, na mimi natokana naye, na yeye ni msimamizi wa kila Muumini baada yangu. Na kama watafanya shaka wang'ang'anizi na wenye chuki juu ya usahihi wa hadithi hizi, basi kamwe hawatakuwa na shaka kwamba kumtakia rehma Ali na Fatmah ni sehemu ya sala ya Mtume(s.a.w.w)
, na haikubaliki sala ya Abubakr, Umar wala Uthman na wale waliobashiriwa pepo na Masahaba wote pamoja na Waislamu wote ikiwa ndani ya sala zao hakusaliwa Mtume Muhammad na kizazi cha Mtume Muhammad ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na akawatakasa mno, kama yalivyokuja maelezo hayo ndani ya Sihahi za Masunni zikiwemo Sahih Muslim na Bukhari na Sihah nyinginezo mpaka Imam Shafii amefikia kusema kuhusu haki yao kwamba: "Yeyote asiyekusalieni (enyi watu wa nyumba ya Mtume) mtu huyo hana sala."
Basi ikiwa watu hawa wa nyumta ya Mtume inafaa kusema uongo na kudai madai yasiyo ya kweli basi Uislamu umeingia katika mtihani Ama ukiuliza ni kwa nini ushahidi wa Abubakr unakubalika na ushahidi wa watu wa nyumba ya Mtume unapingwa? .Tawabu ni kuwa, yeye ndiye mtawala na mtawala ana uwezo wa kuamua akitakacho na kwa hali yoyote ile yeye ndiye mwenye haki, kwani madai ya mwenye nguvu ni kama madai ya mnyama mkali kwa meno na makucha aliyo nayo-kwani hiyo ndiyo-hoja yake.
Na ili ukubainikie vema ukweli wa mambo ewe msomaji mtukufu, hebu tuwe pamoja ili uyasome aliyoyathibitisha Bukhari ndani ya sahih yake kuhusu kugongana kwa suala la mirathi ya Mtume ambalo yeye Bukhari alilisema kama alivyolieleza Abubakr kwamba (Mtume kasema) "Sisi Mitume haturithiwi tunachokiacha ni sadaka." Haya ni mapokezi ambayo Masunni wote wanayakubali na kuyatolea dalili ya Abubakr kutokubali maombi ya bibi Fatmah (juu ya mirathi yake kwa Mtume). Jambo litakachokujulisha juu ya kutosihi kwa hadithi hii na kwamba haifahamiki (kwa Waislamu) ni bibi Fatmah
kudai mirathi yake, na isitoshe wakeze Mtume ambao ni mama wa waumini nao walimtumia ujumbe Abubakr wakitaka mirathi yao. Hayo ndiyo aliyoyaandika Bukhari na ndiyo yanayotolewa dalili juu ya kutokurithiwa kwa Mitume, lakini Bukhari anajipinga mwenyewe pale alipothibitisha kwamba Umar ibn Khatab aligawa mirathi ya Mtume kwa wake zake.
Amethibitisha Bukhari ndani ya sahih yake, Kitabul-Wakala, Babul-Muzara'ah Bis-shatri. Imepokewa kutoka kwa Nafi'i kwamba, Abdallah ibn Umar (r.a) alimwambia kuwa, Mtume alimuwakilisha Khaibar kwenye sehemu ambayo kunatoka matunda au mimea, basi alikuwa akiwapa wakeze Mtume mafungu mia moja na mafungu themanini yakiwa ni ya tende na ishirini ya shairi, basi Umar akaigawa Khaibar akawakhiyarisha wakeze Mtume(s.a.w.w)
awakatie sehemu ya maji na ardhi au yeye awaamulie, basi miongoni mwao kuna waliochagua ardhi na kuna waliochagua shehena za tende na shairi, na Aisha alikuwa miongoni mwa waliochaguwa ardhi."
Riwaya hii inajulisha wazi kwamba Khaibar ambayo ndiyo aliyoitaka bibi Fatmah apewe sehemu yake kama mirathi yake kwa baba yake na Abubakar akamkatalia maombi yake kwa kuwa eti Mtume wa Mwenyezi Mungu harithiwi, na riwaya hii inajulisha wazi pia kwamba Umar ibn Khatab aliigawa Khaibar katika zama za Ukhalifa wake kuwagawia wakeze Mtume(s.a.w.w)
na akawakhiyarisha baina ya kumiliki ardhi au shehena, na Aisha alikuwa miongoni mwa waliochagua ardhi. Basi ikiwa Mtume(s.a.w.w)
harithiwi ni vipi Aisha ambaye ni mke anarithi na Fatmah ambaye ni binti asiweze kurithi? Tuelimisheni juu ya mambo kama hayo enyi wenye kufahamu nanyi mtapata ujira (mwema) na thawabu.
Zaidi ya hayo ni kwamba bibi Aisha binti Abubakr aliikalia nyumba nzima ya Mtume(s.a.w.w)
na hakuna mke yeyote wa Mtume(s.a.w.w)
aliyepata hadhi kama aliyopata Aisha, naye Aisha ndiye aliyemzika baba yake ndani ya nyumba hiyo ya Mtume(s.a.w.w)
, na akamzika Umar karibu ya baba yake, na ni Aisha huyo huyo aliyemzuwia Husein
asimzike nduguye Hasan pembeni mwa babu yake. Jambo hili lilimfanya Ibn Abbas aseme kama ifuatavyo juu ya bibi Aisha; "Ulipanda ngamia ukapanda na nyumbu, lau utaishi zaidi utapanda tembo, yako ni sehemu moja kati ya tisa katika thumni (moja ya nane) lakini wewe yote umeitumia."
Iwe iwavyo, mimi sikusudii kurefusha maudhui hii, bali hapana budi kwa wanaotafiti kuirejea historia, lakini si vibaya nikataja sehemu ya khutuba ambayo aliitoa bibi Fatimah
mbele ya Abubakr na Masahaba wengine, ili aangamie mwenye kuangamia miongoni mwao kutokana na ukweli (kama atakataa kuutambua) na aokoke mwenye kuokoka miongoni mwao kutokana na ukweli (iwapo ataukubali).
Bibi Fatmah alisema: "Je, hivi ni kwa makusudi mumekiacha Kitabu cha Mwenyezi Mungu mkakitupa nyuma ya migongo yenu? Kwani Mwenyezi Mungu anasema: Na Sulaiman alimrithi Daudi. Na akasema akisimulia kisa kuhusu habari ya Zakariya: Basi nipe mrithi kutoka kwako atakayenirithi mimi na kuwarithi kizazi cha Ya'aqub na umfanye (mrithi huyo) ewe Mola wangu awe mwenye kukuridhisha. Na amesema Mwenyezi Mungu: Basi nipe mrithi kutoka kwako, atakayenirithi na kuwarithi kizazi cha Ya'aqub na umfanye ewe Mola wangu awe mwenye kukuridhisha. Na amesema tena: Mwenyezi Mungu anakuusiyeni juu ya watoto wenu, mwanamume apate sawa na sehemu ya wanawake wawili.
Na amesema pia kwamba: Na ndugu wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe (katika kurithiana hivyo ndivyo ilivyo) katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na amesema tena: Mmefaradhishiwa, mmoja wenu anapofikwa na mauti, kama akiacha mali, Aiusie kwa wazazi (wake) na jamaa zake kwa namna njema, haya ni wajibu kwa wamchao Mwenyezi Mungu." (Bibi Fatmah anaendelea kusema baada ya aya hizo za Qur'an) Je, hivi Mwenyezi Mungu amekuhusisheni ninyi kwa aya fulani na akamtoa baba yangu katika aya hizo? Au ninyi mnaijua mno Qur'an inapohusisha (kitu maalum) na inapozungumza kwa kuenea kuliko ajuavyo baba yangu na ibn ammi yangu (Ali)? Au mnasema kuwa watu wa mila mbili hawarithiani.