21
WAULIZE WANAOFAHAMU
MTUME ANAJIPINGA MWENYEWE KATIKA HADITHI ZAKE
Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Kitabul-fitan idhal-taqal-Muslimaini bisaifihimaa, juzuu ya 8 ukurasa 92.
Imepokewa kutoka kwa Abdillah ibn Abdil-wahab, ametusimulia Hammad kutoka kwa mtu fulani ambaye hakumtaja, naye kutoka kwa Al-Hasan amesema: "Nilitoka na silaha yangu katika usiku wenye fitina, basi Abubakrih akakutana nami akasema: Unakwenda wapi? Nikasema nakwenda kumsaidia mwana wa ammi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w). Akasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: watakapogombana Waislamu wawili kwa panga zao basi kila mmoja wao ni mtu wa motoni. Akaambiwa basi anakosa gani huyu aliyeuawa? Akasema bila shaka alikusudia kumuua mwenzake. ..." Hammad ibn Zaidi amesema, "Niliitaja hadithi hii kwa Ayyub na Yunus ibn Ubaid nikiwa nakusudia wanifahamishe hadithi hii, basi walisema, hadithi hii ameipokea Al-Hasan kutoka kwa Ah-naf ibn Qais kutoka kwa Abubakrah
."
Kama alivyoandika Muslim ndani ya sahih yake, Kitabul-fitan waashra-tus-sa'ah Babu idha tawaa-jadal-Muslimain bisaifihimaa. Hadithi ya Abibakrah kutoka kwa Al-ahnaf ibn Qais, amesema: "Nilitoka kwa ajili ya kumsaidia mtu huyu, nikakutana na Abubakrah akasema: Unakwenda wapi? Nikasema, kumsaidia mtu huyu. Akasema rudi, hakika mimi nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema: "Wakikutana Waislamu wawili kwa panga zao basi aliyeuwa na aliyeuawa wote wataingia motoni, nikasema, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu huyu muuaji(s.a.w.w)
basi vipi aliyeuawa? akasema: Hakika yeye alikuwa anapupia kumuua mwenziwe."
Kwa kupitia hadithi hii ya kuzushwa msomaji atafahamu vyema sababu zilizopelekea kuzushwa kwake na huyu Abu Bakrah anaonesha wazi uadui wake dhidi ya mwana wa ammi ya Mtume na ni jinsi gani alivyofanya ili Amirul-Muuminina (Ali
) asipate usaidizi. Hakutosheka kwa hayo, bali alianza kukosa azma za Masahaba ambao walitaka kuitetea haki dhidi ya batili. Basi akawatengenezea hadithi kama hii ambayo akili haikubaliani nayo na wala Qur'an haiikubali wala sunna sahihi ya Mtume, kwani kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo kuwa: "Lipigeni lile kundi korofi mpaka lirudi kwenye amri ya Mwenyezi Mungu" Sura Al-hujurat ay a ya 9 ni amri iliyo wazi ya kuwapiga wakorofi na madhalimu, na ndiyo maana utamuona aliyesherehesha sahihi Bukhari mwenyewe ameandika kwenye hamish ya hadithi hiyo ibara ifuatayo. "Tazama, hivi kweli ndani ya hadithi hii kuna hoja yoyote inyoruhusu kuwapiga wakorofi pamoja na kwamba kuna kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo lipigeni lile kundi korofi?" Na inapotokea hadithi kupingana na kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi hadithi hiyo ni ya uongo itupiliwe mbali. Amma Sunna sahih ya Mtume ni ile kauli yake Mtume(s.a.w.w)
kuhusu Imam Ali isemayo kuwa: "Yeyote ambaye mimi nilikuwa kiongozi wake basi Ali ni kiongozi wake, ewe Mwenyezi Mungu muunge atakayemuunga (Ali) na umpinge atakayempinga na umsaidie atakayemsaidia na usimsaidie atakayeacha kumsaidia na uipeleke haki iwe pamoja naye popote atakapokuwa
."
Kwa hiyo kumuunga mkono Ali ni kumuunga mkono Mtume wa Mwenyezi Mungu, na ni wajibu kwa kila Muislamu kumsaidia Amirul-Muuumina (Ali), na kuacha kumsaidia maana yake ni kuacha kusaidia haki na ni kuitetea batili. Lau utafanya mazingatio ndani ya hadithi hii ya Bukhari utakuta kuna mlolongo wa wapokezi, mmoja wao hajulikani hawakumtaja jina lake pale aliposema; "Ametusimulia Hammad kutoka kwa mtu fulani," ambaye hakumtaja jina. Hii ni dalili wazi kwamba huyu asiyejulikana ndiye miongoni mwa wanafiki waliokuwa wakimbughudhi Ali
na wakijaribu kila namna kufuta fadhila zake au zaidi ya hapo kummaliza kabisa yeye na utajo wake kwa njia yoyote watakayoiweza.
Na amesema Sa'ad ibn Abi Waqqas ambaye naye ni miongoni mwa waliokataa kuitetea haki: "Nipeni upanga nikapigane, huyu anasema yuko kwenye haki na huyu anasema yuko kwenye batili." Na kwa mifano kama hii inayochanganya haki na batili na kuzipoteza njia za wazi ili nafasi yake ichukuliwe na njia ya giza. Sisi tunakuta ndani ya vitabu vya Kisunni vinavyotegemewa ya kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
amewabashiria Masahaba wake wengi kuingia peponi, na hasa wale kumi ambao wanaotambulikana mno miongoni mwa Waislamu kwamba wao wamebashiriwa pepo.
Ahmad, Tirmidhi na Abu Dawud wameandika kwamba Mtume(s.a.w.w)
amesema: "Abubakr ataingia peponi, Umar peponi, Uthman peponi, Ali peponi, Talha peponi, Zubair peponi, Abdur-rahman ibn A'uf peponi, Saad ibn Abi Waqas peponi, Said ibn Zaidi peponi na Abu Ubaidah ibn Jarrah peponi. Kuna habari sahihi kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
kuwa amesema: "Furahini enyi kizazi cha Yasir, bila shaka mahala penu ni peponi." Pia kuna kauli nyingine ya Mtume isemayo: "Pepo ina hamu ya watu wanne, Ali, Ammar, Salman na Miqdad."
Naye Muslim amesimulia ndani ya sahihi yake kwamba, Abdallah ibn Salaam amebashiriwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (kuingia) peponi, na imesihi kutoka kwa Mtume aliposema: "Hasan na Husein ni mabwana wa vijana wa peponi
." Kadhalika imesihi habari kutoka kwa Mtume kwamba, Jaafar ibn Abi Talib anaruka peponi pamoja na Malaika, na kwamba bibi Fatmah Az-zahra ndive mbora wa wanawake wa peponi, na kwamba mama yake Fatmah (bibi Khadija) alibashiriwa na Jibril kuwa atapewa nyumba huko peponi.
Pia kuna habari sahihi kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
aliposema kuwa Suhaib ambaye ni mtu wa mwanzo kusilimu kutoka Rumi ataingia Peponi, na Bilal ambaye ni mtu wa mwanzo kusilimu kutoka Uhabeshi naye ataingia peponi pia Salman ambaye ni mtu wa mwanzo kusilimu kutoka Uajemi ataingia peponi.
Ikiwa mambo yako hivi basi ni kwa nini bishara za peponi zinahusika tu na hawa masahaba kumi, hukuti mkusanyiko wala kikao wanapozungumzia pepo isipokuwa kuwataja hawa kumi tu waliobashiriwa pepo.? Sisi hatuna chuki yoyote ile kuhusu jambo hilo, na wala hatuibani rehma ya Mwenyezi Mungu ambayo ni kubwa na imekienea kila kitu. Lakini tunasema tu kwamba, hadithi hizi zinapingana na ile hadithi isemayo, "Wanapokutana Waislamu wawili na panga zao, basi aliyeua na aliyeuawa wote wataingia motoni." Kwani lau tutaikubali hadithi hiyo, basi ile hadithi ya bishara ya pepo itatoweka kwani wengi wa hawa walipigana na wakauana wao kwa wao. Tal-ha na Zubair waliuawa katika vita ya Jamal ambayo kiongozi wake alikuwa Ummul-Muumina Aisha dhidi ya Imam Ali ibn Abi Talib, na panga zao zilichomolewa na zaidi ya hapo walisababisha kuuawa kwa maelfu ya Waislamu.
Kama ambavyo Ammar ibn Yasir aliuawa katika vita vya Siffin ambavyo moto wake uliwashwa na Muawiyah ibn Abi Sufian, na Ammar alikuwa akipigana kwa upanga wake akiwa pamoja na Ali ibn Abi Talib, basi lile kundi ovu likamuua kama alivyotamka hilo Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
. Kama ambavyo Bwana wa mashahidi na Bwana wa vijana wa peponi Imam Husein alipigana kwa upanga wake yeye na watu wa nyumba ya Mtume dhidi yajeshi la Yazid ibn Muawiyah, na (jeshi hilo la Yazidi) liliwaua (watu wote wa nyumba ya Mtume) hakusalimika isipokuwa Ali ibn Husein
. Na kwa mtazamo wa wazushi hawa ni kwamba, wote hawa wataingia motoni wauaji na waliouawa kwa sababu walipambana kwa panga zao. Ukweli ulivyo ni kwamba, hadithi hiyo haiwezi kusemwa kuwa ni ya (Mtume), Mtume ambaye hasemi kwa matamanio isipokuwa kwa ufunuo uliofunuliwa kwake. Na kama tulivyotangulia kusema hapo kabla kuwa inapingana na mantiki na akili, si hivyo tu bali inapingana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume(s.a.w.w)
.
Swali
la kujiuliza hapa ni kwamba: ni kwa kiasi gani Bukhari na Muslim wamegliafilika wasiweze kuufahamu uzushi kama huu na wala wasiweze kuzindukana?
Kupingana katika ubora Miongoni mwa hadithi zinazopingana ambazo utazikuta katika sihahi, ni ubora wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Muhammads.a.w.w
) juu ya Manabii wote na Mitume wengine, na ziko hadithi nyingine zinampandisha Mtume Musa kwa daraja kuliko Mtume(s.a.w.w)
. Mimi naamini kwamba, Mayahudi ambao walisilimu katika zama za Umar na Uthman kama vile Ka'abul-Ahbar, Tamimud-dari na Wahb ibn Munabbih ndiyo walioziweka hadithi hizo kupitia ndimi za baadhi ya Masahaba ambao walikuwa wakiwapenda kama vile Abu Hurairah na Anas ibn Malik na wengineo. Bukhari ameandika ndani ya sahih yake Kitabut-tauhid babu Qaulihi Taala Wakallamallahu Musa Taklima.
Imesimuliwa kutoka kwa Anas ibn Malik kisa kirefu inachosimulia jinsi israi ya Mtume(s.a.w.w)
ilvyokuwa, kisha kupanda kwake mbingu saba mpaka Sidratil-Mnntaha. Kisa hicho kinaeleza pia kufaradhishwa kwa sala hamsini ambazo zilifaradhishwa kwa Mtume Muhammad na umma wake, lakini kwa ubora wa Musa zikapunguzwa na kuwa tano, na mengineyo yaliyomo ndani ya riwaya hizo miongoni mwa uongo ulio wazi kabisa na kufuru mbaya, eti kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu alisogea akateremka akawa karibu mno na Mtume, na mengineyo miongoni mwa uharibifu. Lakini kilicho muhimu kwetu katika riwaya hii ni kwamba, pale Mtume Muhammad alipoomba ruhusa afunguliwe kwenye mbingu ya saba, wakati huo Musa alikuwa katika mbingu hiyo na kwamba Mwenyezi Mungu alimnyanyua kwenye mbingu hiyo ya saba kutokana na ubora wa yeye Musa kumsemesha Mwenyezi Mungu, hapo Musa alisema: "Ewe Mola wangu mimi sikudhani kama kuna mtu yeyote angenyanyuliwa juu yangu." Muslim ameandika katika Kitabul-iman Babu bad-il-wahyi ila Rasuli llah(s.a.w.w)
.
Bukhari ameandika ndani ya sahihi yake Kitabu bad-il-khalqi, babu dhikril-Malaikah
. Yeye ametoa kisa kingine kinachofanana na kile cha kwanza na anaeleza Israi na Mi'iraj, lakini kisa hicho kinasema kwamba, "Musa alikuwa katika mbingu ya sita na Ibrahim ya saba." Jambo la muhimu ndani ya riwaya hii ni hiki kipande kipande kisemacho kuwa: Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
amesema: "Tukafika mbingu ya sita, pakasemwa ni nani huyu? Pakanenwa Jibril, pakasemwa uko pamoja na nani? Akasema, Muhammad(s.a.w.w)
, pakasemwa, ameitwa? Akasema: ndiyo, pakanenewa karibu. Basi nikafika kwa Musa nikamsalimia akasema karibu ewe ndugu na Mtume, basi nilipopita akalia, akaambiwa nini kilichokuliza, akasema, Ewe Mola wangu kijana huyu ametumwa baada yangu katika, umma wake wataingia peponi watu wengi zaidi kuliko wale watakaoingia kutoka katika umma wangu" Kama alivyoandika Muslim ndani ya sahih yake, Kitabul-imaan babit Adnaa Ahlil-jannah Manzilatanfiiha.
Imesimuliwa kutoka kwa Abu Hurairah kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
amesema; ''Mimi ni Bwana wa watu siku ya Qiyama, je, mnafahamu ni kwa nini? Watu watakusanywa wale wa mwanzoni na wa niwisho katika uwanja mmoja atawasikilizisha mlinganiaji na jicho litawafika wote kisha jua litasogea, na kutokana na taabu na shida itafikia hali ambayo watu hawawezi kuvumilia, hapo ndipo watakaposema, Je, mnavaona mambo yaliyokufikieni? Je, hamuangalii mtu wa kukuombeeni kwa Mola wenu? Baadhi ya watu watawaambia wengine nendeni kwa Adam, basi watamwendea Adam
watamwambia wewe ndiyo baba wa watu (wote), mwenyezi Mungu alikuumba kwa mkono wake na akakupulizia roho yake,na akawaamuru Malaika wakusujudie, tuombee kwa Mola wako. Je, huyaoni yaliyotufika? Basi Adam atasema: Leo hii Mola wangu amekasirika kiasi ambacho hajapata kukasirika mfano wake na yeye alinikataza ule mti nami nikamuasi.
Ewe nafsi yangu, nafsi yangu, nafsi yangu, nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Nuh." Riwaya inaendelea na ni ndefu mno (nasi wakati wote tunapenda kufupisha) kiasi kwamba watu watazunguka kwa Nuhu kisha kwa Ibrahim, kisha kwa Musa, kisha kwa Isa na wote wanasema: "Ewe nafsi yangu, nafsi yangu, nafsi yangu." Kila mmoja alitaja kosa lake isipokuwa Issa hakutaja kosa lolote lakini alisema; "Ewe nafsi yangu. nafsi yangu, nafsi yangu nendeni kwa mwingine asiyekuwa mimi nendeni kwa Muhammad.1* Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema, watakuja kwangu mimi nitakwenda chini ya A'rshi nitaanguka hali ya kuwa ninasujudu kwa ajili ya Mola wangu Mtukufu kisha Mwenyezi Mungu atanifungulia baadhi ya sifa zake njema kitu ambacho hajakifungua kwa yeyote kabla yangu. Hatimaye patasemwa. "Ewe Muhammad nyanvua kichwa chako, omba utapewa, omba utakubaliwa." Nitanyanyua kichwa changu na nitasema: "Ewe Mola wangu ummati wangu. Ewe Mola wangu ummati wangu." Patasemwa, "Ewe Muhammad waingize katika ummati wako watu bila ya hesabu katika mlango wa kulia miongoni mwa milango ya peponi, nao watashiriki na watu katika milango mingine miongoni mwa milango, kisha akasema, namuapa Mwenyezi Mungu ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake hakika baina ya milango miwili miongoni mwa milango ya peponi ni kama baina ya Maka na Humair au ni kama baina ya Maka na Basra."
Ndani ya hadithi hizi Mtume anasema kwamba, "Yeye ni Bwana wa watu siku ya Qiyama." Na anasema kuwa, "Musa alisema, Ewe Mola wangu nilikuwa sidhani kwamba kuna mtu yeyote atakayenyanyuliwa juu yangu na pia anasema kwamba, Musa alilia na akasema: Kijana huyu aliyetumwa baada yangu wataingia peponi watu wengi katika ummati wake kuliko wale watakaoingia katika ummati wangu." Tunachokifahamu kupitia hadithi hizi ni kwamba, Manabii na Mitume wote kuanzia Adam mpaka Isa kwa kupitia Nuh, Ibrahim na Musa (amani iwashukie wao na Mtume wetu) hawatawaombea watu mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya Qiyama na Mwenyezi Mungu amemuhusisha kwa jambo hilo Mtume Muhammad(s.a.w.w)
peke yake, nasi tunayaamini yote hayo na tunasema kuwa, yeye Mtume ni bora wa viumbe wote, lakini Waisraili na wasaidizi wao miongoni mwa Banu Umayyah hawakuvumilia ubora huu na heshima hii kwa Muhammad(s.a.w.w)
mpaka wakatengeneza riwaya zinazomboresha Musa juu ya Mtume(s.a.w.w)
. Hilo tumekwishaliona hapo kabla katika kauli ya Musa kwa Muhammad kwenye ule usiku wa Israi na Mi'iraj na pale Mwenyezi Mungu alipomfaradhishia Mtume sala hamsini, Musa akamwambia Mtume, "Mimi nawajua watu kuliko wewe." Hili halikutosha wakatengeneza riwaya nyingine zinazomboresha Musa kuliko Muhammad kwa kupitia ulimi wa Muhammad mwenyewe. Basi hebu ziangalie baadhi ya riwaya hizi zifuatazo.
Bukhari ameandika ndani ya sahih yake katika Kitabut-tauhid babu fil-mashiati wal-iradah Wamaa tashauna Ilia art-Yashaa llahu. Imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah amesema: "Mtu fulani miongoni mwa Waislamu na mwingine Myahudi waligombana, yule Mwislamu akasema, namuapa Mwenyezi Mungu aliyemteua Muhammad juu ya walimwengu. (hiki ni kiapo alichoapia) Basi yule Myahudi naye akasema: Namuapa Mwenyezi Mungu ambaye alimteua Musa juu ya walimwengu. Yule Muislamu akanyanyua mkono wake akampiga yule Myahudi, Myahudi yule akaenda kwa Mtume(s.a.w.w)
akamuelezea yaliyojiri kati yake na yule Muislamu. Mtume(s.a.w.w)
akasema: Msinifanye mie kuwa bora juu ya Musa, kwani siku ya Qiyama watu watazimia nami nitakuwa wa kwanza kuzindukana, basi ghafla Musa amejiangika kwa nguvu pembeni ya Arshi, mimi sifahamu je, na yeye alikuwa miongoni mwa waliozimia kisha akazindukana kabla yangu au alikuwa miongoni mwa wale ambao Mwenyezi Mungu hakuwahusisha (na kuzimia huko)."
Katika riwaya nyingine ya Bukhari amesema: "Myahudi fulani alikuja kwa Mtume(s.a.w.w)
hali yakuwa amepigwa usoni kwake na akasema, Ewe Muhammad mtu fulani miongoni mwa wafuasi wako wa Kiansari amenipiga usoni. Mtume akasema mwite, wakamwita, Mtume akasema, Kwa nini umempiga usoni kwake? Yule mtu akasema, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi nilipita kwa Myahudi huyu nikamsikia anasema;Namuapa Mwenyezi Mungu ambaye alimteua Musa juu ya watu, basi mimi nikasema, na juu ya Muhammad? Hilo likanikasirisha kisha nikampiga. Mtume akasema: Msiniboreshe mbele ya Manabii, kwani siku ya Qiyama watu watazimia nami nitakuwa wa kwanza kuzindukana, mara ghafla (nitamkuta) Musa ameshika nguzo miongoni mwa nguzo za Arshi, sasa sijui amezindukana kabla yangu au alitoshelezwa kwa mzimio ule wa (mlima wa) Tuur."
Kama ambavyo Bukhari amethibitisha ndani ya sahih yake katika Kitabu Tafsiril-Qur-an surat Yusuf
Babu qaulihi falammaa Jaa-ar-rasul. Imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
. "Mwenyezi Mungu amrehemu Lut, kwa hakika alikuwa anakimbilia kwenye pembe iliyo imara, lau ningekaa jela kiasi alichokaa Yusuph ningemwitikia mwitaji. Sisi tunastahiki zaidi kuliko Ibrahim alipoulizwa je, hukuamini? Akasema nimeamini lakini nataka roho yangu itulie. Hawakutosheka na yote hayo mpaka wamemfanya Mtume wa Mwenyezi Mungu kuwa ni miongoni mwa wenye mashaka juu ya hali yake ya baadaye mbele ya Mola wake, hana shufaa wala ile daraja tukufu, na wala hana ubora mbele ya Manabii na Mitume wengine, kwa maana hiyo hana hata ule ubashiri wa pepo kwa Masahaba wake ikiwa yeye mwenyewe hajui hali yake (itavyokuwa) siku ya Qiyama. Hebu tuisome kwa pamoja riwaya hii ambayo ameandika Bukhari, na imma utashangaa au hutashangaa.
Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Babu fil-janaiz, Kitabul-kusufi, juzuu ya pili ukurasa 71. Imepokewa kutoka kwa Kharijah ibn Zaid ibn Thabit, kwamba Ummul-Alai ni mwanamke wa Kiansari ambaye alimpa baia Mtume(s.a.w.w)
. Mama huyu alimuelezea kuwa Muhajirina waligawana hisa katika hisa yetu, akatokea Uthman ibn Madh-u'n nasi tukamkaribisha majumbani mwetu, kisha aliugua maradhi ambayo kwayo alifishwa, alipofishwa na akakoshwa na kukafiniwa katika nguo zake, Mtume(s.a.w.w)
aliingia, basi mimi nikasema: "Rehma ya Mwenyezi Mungu ikushukie ewe Abas-saaib, nashuhudia kuwa Mwenyezi Mungu amekukirimu." Mtume(s.a.w.w)
akasema, ni lipi linalokujulisha kuwa Mwenyezi Mungu amemkirimu?" Nikasema, "Ewe Mtume wa mwenyezi Mungu ni nani basi atakirimiwa na Mwenyezi Mungu?" Mtume akasema: "Amma yeye yaqini imekwishakumfikia, namuapa Mwenyezi Mungu mimi namtakia kheri, namuapa Mwenyezi Mungu, mimi mwenyewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu lakini sijui nitafanyiwa nini? [37]
"
Yule mama akasema:"Namuapa Mwenyezi Mungu kamwe sitamtakasa yeyote baada yake." Wallahi hili ni jambo la ajabu, ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu yeye haujui atakachofanyiwa, basi nini kinachobakia baada ya hili? Na iwapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Bali mtu ni shahidi na nafsi yake
" (Qur.75:14).
na kama Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake:
إِنَّا فَتَحْنَا لَكَ فَتْحًا مُّبِينًا ﴿١﴾ لِّيَغْفِرَ لَكَ اللَّـهُ مَا تَقَدَّمَ مِن ذَنبِكَ وَمَا تَأَخَّرَ وَيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكَ وَيَهْدِيَكَ صِرَاطًا مُّسْتَقِيمًا ﴿٢﴾ وَيَنصُرَكَ اللَّـهُ نَصْرًا عَزِيزًا ﴿٣﴾
"Bila shaka tumekwisha kukupa ushindi uliodhahiri, ili Mwenyezi Mungu akusamehe makosa yako yaliyo tangulia na yanayokuja na kukutimizia neema zake na kukuongoa kwenye njia iliyonyooka na akusaidie Mwenyezi Mungu msaada wenye nguvu kabisa." (Qur'an, 48:1-3).
Na iwapo kuingia peponi kwa Waislamu kunategemea kumfuata, kumtii na kumuamini Mtume(s.a.w.w)
, basi ni vipi tutaisadiki hadithi hii ambayo ni chafu mno?.
Twajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na itikadi za Kibanu Umayyah watu ambao walikuwa hawaamini hata siku moja kuwa Muhammad ni Mtume wa haki wa Mwenyezi Mungu, bali wao walikuwa wakiitakidi kuwa ni Mfalme aliyewashinda watu kwa akili zake na ujanja wake!! Itikadi hii ndiyo ile aliyoibainisha wazi Abu Sufiyan na Muawiyah na wengineo miongoni mwa Makhalifa wao na watawala wa Kibanu Umayyah. Mtume kupingana na elimu ya tiba Bila shaka elimu inathibitisha kwa maelezo ambayo hayana shaka kuwa, kuna baadhi ya maradhi ambayo hupatikana kwa njia ya kuambukiza, jambo hili watu wengi wanalifahamu hata wale ambao hawana kiwango kikubwa cha elimu. Amma wasomi ambao wanasomea elimu ya tiba katika vyuo vikuu, bila shaka watakapoambiwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
anapinga hilo, hapana shaka watamdharau na watapata nafasi ya kumshambulia mno Nabii wa Uislamu. Watu wasioamini dini siku zote wanatafuta mwanya kama huu. Inasikitisha mno kwamba miongoni mwa hadithi ambazo zimethibitishwa na Bukhari na Muslim ziko zile zinazopinga kuwepo kuambukiza, na pia ziko zinazosisitiza kuwa kuna kuambukizana (maradhi).
Sisi hapa tunasajili huku kupingana kwa hadithi hizi chini ya anuani ya kuwa Mtume anajipinga, lakini hatuamini kuwa ilipata kutokea Mtume kujipinga katika maneno yake na matendo yake hata mara moja. Lakini kama kawaida (yetu) na ili kuivutia roho ya msomaji ili apate kuzindukana azitambue zile hadithi za uzushi na za uongo zilizowekwa dhidi ya Mtume(s.a.w.w)
ambaye ni Maasum. Ili msomaji apate kufahamu lengo letu la kuziandika hadithi hizi kuwa ni kwa ajili ya kumtakasa Mtume(s.a.w.w)
na kumpa heshima yake ya kielimu ambayo imeshinda elimu zote za kisasa, kwani hapana nadhariya yoyote ya kielimu inayopingana na hadithi sahihi za Mtume(s.a.w.w)
. Ikiwa zitapingana basi tutajua kwamba Mtume kazushiwa hadithi hiyo kwa upande mmoja na kwa upande mwingine, bila shaka hadithi hiyo itakuwa inapingwa na hadithi nyingine inayokubaliana na nadharia ya kielimu, basi itakuwa wajibu kuikubali hii ya pili na kuiacha ile ya kwanza. Mfano juu ya hilo ninaleta hadithi ya kuambukiza kwani ni ya muhimu katika uchunguzi na itatupatia picha kamili ya kupingana kwa Masahaba na wapokezi (wa hadithi) na wale wazushi na siyo Mtume kujipinga mwenyewe kwani hilo kamwe haliwezekani.
Bukhari ndani ya sahihi yake anataja hadithi mbili, nami nitatosheka naye kwani kitabu chake ndiyo kitabu sahihi mno kwa Masunni, ili tu wenye kugeuza wasije kwenda na njia nyingi pakatokea mwenye kusema kuwa huenda ikathibiti hadithi kwa Bukhari na ikathibiti kinyume chake kwa asiyekuwa yeye miongoni mwa wanachuoni wa hadithi. Msomaji ataona kuwa mimi katika mlango huu nimetosheka na Bukhari peke yake katika hadithi zinazopingana. Bukhari amethibitisha katika sahih yake, Kitabut-tib Babu La Hammah: Imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah amesema: "Nabii(s.a.w.w)
amesema:Hapana kuambukiza wala ugonjwa wa manjano wala ndege mbaya
." Bedui mmoja akasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni vipi kuhusu ngamia aliye mzima kisha akachanganyikana na ngamia mwenye upele na akamuambukiza? Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema: Ni nani aliyemuambukiza yule wa kwanza?" Hebu muangalie bedui huyu, ni vipi anaweza kufahamu kwa kutumia akili yake ya kuzaliwa namna ilivyo tabia ya maradhi ya kuambukiza kupitia ngamia mwenye upele ambaye anaambukiza ngamia wote akichanganyika nao, wakati ambapo Mtume anakosa jibu la kutosheleza suali la bedui na hatimaye yeye Mtume ndiyo anakuwa muulizaji?
Hadithi hii vile vile inanikumbusha daktari mmoja ambaye alimuuliza mama fulani aliyekuja na mwanawe aliyepatwa na shurua, Daktari akasema, "Je, nyumbani mwenu au jirani yenu kuna mtu anayeugua maradhi haya?" Yule mama akasema, hapana." Daktari akasema. "Basi huenda (mwanao) ameupata ugonjwa huu shuleni?" Mama akajibu haraka sana, "Hapana huyu hata shule bado hajaingia umri wake ni chini ya miaka mitano." Daktari akasema: "Kwa hiyo labda kwenye michezo." Mama akasema; "Hapana huyu haendi kwenye michezo." Yule daktari akasema: "Huenda wewe ulienda naye katika matembezi kwa baadhi ya nduguzo au walikutembeleeni baadhi ya ndugu ambao kuna ambaye alikuwa na vijidudu vya maradhi." Yule mama akakanusha, hapo ndipo Daktari alipomwambia yule mama kuwa, "Vijidudu hivyo vimetoka hewani."
Bila shaka hewa inabeba vijidudu na maradhi yanayoambukiza na huenda yakaupata mji wote au kitongoji chote na ndiyo maana kumekuweko kinga ili kuzuia vijidudu vya maradhi mabaya vitakavyobebwa na upepo kama vile kipindupindu, tauni na mengineyo. Basi iweje yote haya yasitambulikane kwa Mtume ambaye hasemi kwa matamanio yake? Bila shaka yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu hakifichikani katika elimu chochote, bila shaka kwa Mwenyezi Mungu hakifichikani chochote kilichoko ardhini wala mbinguni, naye ni msikivu na ni mjuzi mno, na kwa ajili hiyo sisi tunaipinga hadithi hii na wala hatuikubali kamwe, na tunaikubali hadithi ya pili ambayo yeye mwenyewe Bukhari ameithibitisha katika ukurasa huo huo na katika mlango huo huo na ndani ya hadithi yenyewe pale aliposema:
Imepokewa kutoka kwa Abu Salamah, alimsikia Abu Hurairah baadaye akisema, Mtume(s.a.w.w)
amesema: "Muuguzaji asimkurubie mtu mzima (asiyeumwa)." Abu Hurairah akaikanusha hadithi yake ya kwanza sisi tukasema: "Siyo wewe uliye tusimulia kuwa hakuna kuambukizana." Basi Abu Hurairah akazungumza Kihabeshi (kupoteza lengo), Abu Salamah akasema, "Sikumuona akisahau hadithi isipokuwa hadithi hiyo
." Pamoja na kwamba hadithi hizi mbili zinapingana inayosema hakuna kuambukizana, na ile ya mtu anayeuguza asimsogelee mtu asiyeumwa, Muslim naye amezieleza ndani ya sahih yake katika Kitabus- salam, Babu La Ad-wa walaatiirah walaa Hammah wala Safr wala Nau-u, wala Ghaulu, wala yuuridanna Mumaridhun ala musihin.
Na kwa kupitia hadithi hizi, tunafahamu kwamba ile hadithi isemayo, "Muuguzaji asimsogelee mtu mzima (asiyeumwa)" ni hadithi sahihi aliyoisema Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
kwani haipingani na elimu. Amma ile hadithi isemayo, "Hakuna kuambukizana" hiyo ni hadithi ya uongo aliyozushiwa bwana Mtume, kwani hadithi iliyosemwa na mtu asiyejuwa ukweli wa maumbile. Na kwa ajili hiyo basi baadhi ya Masahaba walitambua kupingana kwa hadithi hizi ndipo walipomkemea Abu Hurairah na wakamshangaa kwa hadithi yake ile ya kwanza, na hapo Abu Hurairah hakuwa na njia ya kukwepa mtego huu matokeo yake akaongea Kihabeshi kupoteza lengo. Kinachotuongezea nguvu kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa mbele mno kitaaluma kuliko ilivyothibitishwa na elimu za kisasa hasa kuhusu maradhi ya kuambukiza ni kwamba alikuwa akiwaonya Waislamu dhidi ya tauni, ukoma, kipindupindu na mengineyo. Bukhari ameyaandika hayo ndani ya sahih yake, Kitabul-anbiyai, Babu haddathana Abul-yaman, pia Muslim ndani ya sahih yake Kitabus-salam, Babut-taau'un wat-tirah wal-kahanah waghairiha.
Imepokewa kutoka kwa Usamah ibn Zaid amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
amesema: "Tauni ni maradhi mabaya, yalipelekwa kwa watu fulani katika wana wa Israeli, au kwa wale waliokuwa kabla yenu, basi mkiyasikia yameingia mahala fulani msiende huko, na yakiingia mahala mlipo ninyi msitoke kuyakimbia" Na katika riwaya nyingine "Kisikutoeni kitu isipokuwa kwa kuyakimbia." Na imethibiti kutoka kwake Mtume(s.a.w.w)
kauli yake inayotoa maana hii, "Muepuke mwenye ukoma kama unavyomuepuka simba." Na kauli yake isemayo, "Mmoja wenu anapokunywa (maji au...) asipumulie ndani ya chombo." Na kauli yake nyingine isemayo, "Atakaporamba mbwa ndani ya chombo cha mmoja wenu, basi kikosheni mara saba moja wapo kwa mchanga." Yote hayo ili tu apate kuuelimisha umma wake usafi na njia za afya na kujikinga na maradhi, na siyo kuwaambia (eti) "Nzi akitumbukia ndani ya kinywaji cha mmoja wenu basi amzamishe." Hadithi hii tumekwisha izungumzia unaweza kuirejea. Sisi tunakuta kupingana kuliko wazi hata katika mambo yanayohusu Al-Hammah, kitu ambacho Waarabu walikuwa wakikiona kuwa ni mkosi, na huyo ni ndege mashuhuri anayeruka usiku na inasemekana ni bundi kwa mujibu wa tafsiri ya Malik ibn Anas.
Basi kama Mtume(s.a.w.w)
anasema: "Hakuna Hammah basi vipi anajipinga na anajilinda kutokana naye? Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Kitabu Bad'il-khalq Babu yuzaffuna an-nas-lan fil-Mashyi, juzuu ya nne uk.119. Imepokewa kutoka kwa Said ibn Jubair, naye kutoka kwa Ibn Abbas (r,a.) amesema, "Mtume(s.a.w.w)
alikuwa akiwakinga Hasan na Hussein na husema bila shaka wazee wenu Ismail na Is'haqa walikuwa wakikingwa kwayo - Najilinda kwa maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyotimia kutokana na kila shetani na Hammah na kila jicho baya." Naam, katika mlango huu tulikuwa tunataka kutaja baadhi ya mifano ya hadithi zinazopingana ambazo zinanasibishwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
hali ya kuwa si zake.
Kuna mamia ya hadithi nyingine zinazopingana ambazo Bukhari na Muslim wameziandika ndani ya sahihi zao na tumezitolea mifano kama ambavyo tumemzowesha msomaji wakati wote kumletea kwa mukhtarsari na kumuashiria. Hivyo basi kwa wale watafiti wanalazimika kufuatilia kuyasoma hayo huenda Mwenyezi Mungu akaitakasa Sunna ya Mtume wake(s.a.w.w)
kupitia kwao na kuwalipa malipo makubwa na wao wakawa ndiyo sababu ya kuitakasa haki kutokana na batili na wakaziletea zama hizi mpya utafiti madhubiti kwa kiwango kinachotakiwa na ujumbe wa Uislamu:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾ يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾
Enyi mlioamini, muogopeni Mwenyezi Mungu na mseme maneno ya kweli, Mwenyezi Mungu atakutengenezeeni vizuri matendo yenu na atakusameheni madhambi yenu, na yeyote anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, bila shaka amefanikiwa mafanikio makubwa. (Qur'an, 33:70-71).