22
WAULIZE WANAOFAHAMU
MLANGO WA NANE
YANAYOZIHUSU SIHAH MBILI, BUKHARI NA MUSLIM
Vitabu hivi viwili ni muhimu sana kwa Masunni kiasi kwamba vimekuwa ni rejea madhubiti na ni misingi ya mwanzo kwa kila mtafiti anayehusika na uchunguzi wa kidini. Imekuwa ni jambo gumu kwa baadhi ya wanaofanya utafiti kuyabainisha wazi wanayoyakuta humo miongoni mwa mambo yanayoidhalilisha dini, kupingana kwa hadithi zilizomo na mambo mengine machafu. Basi wao huyakubali tu kwa kuwa wafanyeje na wala hawawabainishii watu wao kwa kuwachelea watu hao, au kujichelea wao wenyewe kutokana na heshima na utukufu walioutengeneza kuhusu vitabu hivi.
Ukweli uliopo ni kuwa, Bukhari na Muslim hawakupata kuota ndoto hata siku moja kwamba vitabu vyao vitafikia heshima hiyo kwa wanachuoni na watu wa kawaida. Sisi tunapovikosoa vitabu hivi, siyo kwa sababu yeyote ila ni kwa kumtakasa Mtume wetu(s.a.w.w)
ili Ismah yake isije ikavunjwa. Na kama wako baadhi ya masahaba ambao hawakusalimika na jambo hili la kukosolewa kwa lengo lile lile, kwa hiyo basi Bukhari na Muslim siyo wabora kuliko hao Masahaba ambao walikuwa karibu mno na Mtume(s.a.w.w)
.
Na maadam bado tunalenga kumtakasa Mtume(s.a.w.w)
, tunajaribu kwa kadiri ya uwezo wetu kuithibitisha, Ismah ya Mtume na kwamba yeye ndiye mjuzi mno na ni mcha Mungu mno kuliko watu wote kwa jumla. Tunaitakidi kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alimteua ili awe ni rehma kwa viumbe, na akamtuma kwa viumbe wote watu na majini. Basi hapana shaka kwamba Mwenyezi Mungu anatutaka tumtakase na tumuheshimu na tusikubali afedheheshwe. Kutokana na sababu hizo basi, sisi na kila Muislamu tunatakiwa kupinga kila kinachopingana na mwenendo wake Mtukufu, na tukatae kila kinachopingana na Ismah yake ya kutokuwa na makosa au kitu chochote kinachotia dosari heshima yake tukufu ikiwa kinatoka mbali au karibu. Kwa hakika Masahaba, Tabiina (waliowafuatia Mashaba), Maimamu pamoja na Maulamaa wa hadithi na Waislamu wote na hata watu wote wanapaswa kulinda fadhila na heshima ya Mtume(s.a.w.w)
.
Watu wanaopinga (Bukhari na Muslim wasikosolewe) na kung'ang'ania (kila kilichomo vitabuni mwao kuwa ni sahihi) bila shaka watachukia kwa kila watakachokiona kuwa ni kipya kwao. Lakini radhi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiyo makusudio (yetu) na radhi ya Mtume wake(s.a.w.w)
ndiyo matarajio (yetu), na hiyo ndiyo akiba na hazina ya kweli siku ambayo haitamfaa (mtu) mali wala watoto ila yule atakayemfikia Mwenyezi Mungu kwa moyo ulio salimika. Pamoja na yote hayo, sisi tunaridhaa na faraja kwa waumini wa kweli ambao waliufahamu utukufu wa Mwenyezi Mungu na heshima ya Mtume wake(s.a.w.w)
kabla ya kufahamu heshima ya watawala, Makhalifa, na hata Masultani. Nakumbuka wakati fulani nilipambana na upinzani mkali mpaka nikatuhumiwa kuwa nimekufuru na nimetoka katika dini pale tu nilipomkosoa Bukhari kwa kosa lake la kuiandika hadithi isemayo kuwa, "Nabii Musa
alimpiga Malaika wa mauti na kumpofua jicho lake." Matokeo yake niliambiwa, "Wewe ni nani mpaka umkosoe Bukhari?" Jamaa hao walizua zogo na makelele kama kwamba mimi nimeikosoa aya fulani ndani ya kitabu cha Mwenyezi Mungu. Ukweli wa mambo ulivyo ni kwamba, pindi mchunguzi yeyote atakapojinasua kutoka kwenye kifungo cha kufuata kama kipofu na kung'ang'ania ung'ang'anizi usiokuwa na maana, bila shaka atayakuta ndani ya Bukhari na Muslim mambo ya ajabu na ya kushangaza ambayo moja kwa moja yako kinyume cha akili ya Mwarabu (Bedui) wa jangwani ambaye fikra zake bado zimeganda na anaamini kuhusu baadhi ya mambo ya uzushi na ngano za kale, na fikra zake bado zimeelemea kwenye mambo ya ajabu. Hali kama hii sio jambo la aibu, na wala hatumtuhumu kuwa yuko nyuma kimawazo kwa sababu maisha yake ya zama za kale si sawa na zama za mawasiliano ya satellite, simu na rocket.
Jambo la msingi hapa ni kwamba, sisi hatutaki mambo hayo yahusishwe na Mtume(s.a.w.w)
, kwani tofauti iliyopo nikubwa na mwanya ni mpana sana, kwani yeye ni yule ambaye Mwenyezi Mungu alimtuma kutoka kwa wakazi wa Maka ili awasomee aya zake na awatakase na awafundishe kitabu na hekima, na kwa kuwa yeye ndiye Nabii na Mitume mwisho, basi Mwenyezi Mungu amemfunza elimu za watu wa mwanzo na wa mwisho. Kama ambavyo tunamfahamisha msomaji mtukufu ya kwamba, siyo kila kilichomo ndani ya Bukhari basi kinanasibishwa kwa Mtume, kwa hakika Bukhari hupata akaiandika hadithi ya Mtume(s.a.w.w)
kisha akaifuatishia maoni ya baadhi ya Masahaba, kisha msomaji wake hubakia akiamini kuwa rai hiyo au hadithi hiyo ni ya Mtume wa Mwenyezi Mungu wakati ambapo siyo yake.
Ninakupigia mfano wa jambo hilo: Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Kitabul-hiyal Babu fin-nikah juzuu ya nane ukurasa wa 62 amesema: Imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
amesema: "Mwanamke bikra haolewi isipokuwa aulizwe, wala mwanamke mkubwa (haolewi) mpaka ashauriwe." Basi pakaulizwa, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kukoje kukubali kwake?" Mtume akasema: "Atakaponyamaza." Baadhi ya watu wakasema, "Kama mwanamke bikra asipoulizwa na akawa hakuolewa kisha mtu fulani akafanya hila akasimamisha mashahidi wawili wa uongo kwamba yeye amemuoa mwanamke yule kwa ridhaa yake, na kadhi akaithibitisha ndoa yake na hali mume anatambua kwamba ushahidi ule ni wa uongo, basi siyo vibaya kumuingilia nayo ni ndoa sahihi."
Basi hebu iangalie kauli ya Bukhari (baada ya kumalizika hadithi ya Mtume(s.a.w.w)
anasema, "Baadhi ya watu wakasema." Ni kwa nini basi kauli ya baadhi ya watu, tena wasiojulikana isemayo kwamba ndoa ya ushahidi wa uongo ni ndoa sahihi? Mahala kama hapa panamchanganya msomaji na kufikiria kuwa hayo ni maoni ya Mtume kitu ambacho siyo sahihi. Mfano mwingine: Bukhari ameandika ndani ya sahihi yake, Kitabu Bad-il-khalqi Baba Manaqibul-muhajirina wafadhlihim, juzuu ya nne ukurasa wa 203. Imepokewa kutoka kwa Abdallah ibn Umar (r.a) amesema: "Katika zama za Mtume(s.a.w.w)
, tulikuwa hatumlinganishi Abubakr na mtu yeyote (kwa ubora), kisha (hufuatia) Umar halafu Uthman, kisha tunawaacha Masahaba wa Mtume na hatumboreshi (yeyote) baina yao." Bila shaka hayo ni maoni ya Abdallah ibn Umar na wala hawajibiki kwa maoni hayo isipokuwa yeye mwenyewe binafsi, vinginevyo atakuwa wapi Ali ibn Abi Talib ambaye ni mbora wa watu baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, lakini kwa Abdallah ibn Umar hana ubora wowote na amemuweka katika kundi la watu wa kawaida? Na kwa ajili hiyo ndiyo maana Abdallah ibn Umar alikataa kumpa baia Imam Ali na kumtawalisha, na yeyote yule ambaye Ali siyo mtawala wake basi huyo siyo muumini. Ali huyo huyo ndiye yule ambaye Mtume(s.a.w.w)
amesema kuhusu haki ya Imam Ali, "Ali yuko pamoja na haki na haki iko pamoja na Ali." Na huyu Abdallah ibn Umar alimpa baia adui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na waumini aliyekuwa akiitwa Al-hajjaj ibn Yusuf ambaye ni mtu muovu na fasiki.
Lengo letu siyo kurejea kwenye maudhui hizo, lakini tunataka kumdhihirishia msomaji namna alivyo Bukhari na walio mfano wake, yeye anaiandika hadithi hii katika mlango wa sifa za Muhajirina kama kwamba yeye anataka kuwatambulisha wasomaji kwa njia ya kificho kwamba hayo ni maoni ya Mtume(s.a.w.w)
wakati ambapo hayo ni maoni ya Abdallah ibn Umar ambaye alimfanyia uadui Imam Ali
. Tutambainishia msomaji anayetumia akili msimamo wa Bukhari juu ya kila jambo linalomuhusu Ali ibn Abi Talib, na ni vipi alivyojaribu kwa juhudi zake zote kuficha ubora wake ili kumdhalilisha. Kama ambavyo Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Kitabu Bad-il-khalq Bahn Haddathanal-Humcridi amesema: "Ametusimulia Muhammad ibn Kathir, ametueleza Sufiyan, ametusimulia Jami'i ibn Abi Rashid, ametusimulia Abu Ya'ala kutoka kwa Muhammad ibn Al-hanafiyah amesema: "Nilimwambia baba yangu, ni mtu gani bora baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
? Akasema, "Abubakr." Nikasema, "Kisha nani?" Akasema, "Kisha Umar." Basi nilichelea kuwa atasema Uthman nikasema, "Kisha wewe." Akasema, "Mimi si lolote isipokuwa ni mtu miongoni mwa Waislamu."
Naam hadithi hii wameizusha kupitia ulimi wa Muhammad ibn Al-hanafiyyah ambaye ni mtoto wa Imam Ali ibn Abi Talib, na hii hadithi ni kama ile iliyotangulia ambayo imepokewa kwa ulimi wa Abdallah ibn Umar, na matokeo yake ya mwisho ni ya namna moja, japokuwa Ibnul-hanafiyyah alichelea kuwa baba yake angemtaja Uthman kuwa ndiyo watatu. Lakini jibu la baba yake aliposema, "Mimi si chochote isipokuwa ni mtu tu miongoni mwa Waislamu," linatosheleza kwamba, Uthman ni bora kuliko yeye (Ali), kwani hapana mtu yeyote miongoni mwa Masunni anayesema kuwa Uthmani si lolote bali yeye ni mtu miongoni mwa Waislamu tu. Masunni wanasema kuwa, kama ilivyotangulia kwamba wabora wa watu ni Abubakr kisha Umar kisha Uthmani kisha tunawaacha Masahaba wa Mtume(s.a.w.w)
hatumboreshi yeyote baina yao, na baada ya hapo watu wote ni sawa sawa. Je, hamuzishangai hadithi hizi anazozithibitisha Bukhari, ambazo zote zina lengo moja nalo ni kumvua Ali ibn Abi Talib kila namna ya ubora (alionao)? Je, hali hii haifahamishi kuwa Bukhari alikuwa akiandika kila lile linalowaridhisha Banu Umayyah na Banu Abbas na watawala wote ambao walisimama kuwavunja watu wa nyumba ya Mtume? Bila shaka hizo ni dalili tosha kwa yule anayetaka kupata ukweli.
Bukhari na Muslim wanaeleza kila kitu ili kuwatukuza Abu bakr na Umar Bukhari ameandika ndani ya sahihi yake katika Kitabu Bad-il-khalq, Babufadhail Abibakrs-siddiq (r.a).
Imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah amesema: "Mtume alisali sala ya asubuhi kisha akawaelekea watu akasema: Kuna wakati fulani mtu mmoja alikuwa anamswaga ng'ombe basi mara alimpanda kisha akampiga, yule ng'ombe akasema, Sisi hatukuumbwa kwa ajili hii, bila shaka tumeumbwa kwa ajili ya kilimo. Watu wakasema, Sub-hanallahii!! (walishangaa) Ng'ombe anazungumza? Mtume akasema: Mimi naamini jambo hili na Abubakr na Umar. Wakati huo Abubakr na Umar hawakuwepo hapo
.
Na kuna wakati fulani mtu mmoja, alikuwa akichunga mifugo yake, basi ghafla mbwa mwitu alimvamia na kuchukua mbuzi mmoja. Yule mchungaji alimtafuta mbwa mwitu na kumwokoa kondoo kutoka kwa mbwa mwitu. Yule mbwa mwitu akamwambia mchungaji; Umemuokoa kutoka kwangu basi ni nani atakayemuokoa siku ya Qiyama, siku ambayo hapana mchunga ila mimi? Basi watu wakasema, Sub-hanallah!! Mbwa mwitu anazungumza? Mtume akasema, Mimi ninaamini jambo hilo na Abubakr na Umar (nao wanaamini)." Wao hawakuwepo hapo (mahala wakati Mtume anazungumza). Na hadithi hii ni wazi kabisa kuwa ni kuazimisha na ni miongoni mwa hadithi zilizozushwa kuhusu ubora wa Makhalifa hao wawili, vinginevyo ni kwa nini watu wanapinga hali wao ni masahaba wa Mtume, (wanapinga) yale anayowaambia mpaka analazimika kukariri mara ya pili kuwa "Mimi na Abubakr na Umar tunaamini jambo hili."
Kisha hebu angalia msimuliaji wa hadithi hii anavyotilia mkazo kuwa Abubakr na Umar hawakuwepo mahala hapo mara mbili zote, kwa hakika huu ubora wanaopachikwa ni mambo ya kuchekesha na wala hayana maana yoyote. Lakini jamaa hawa ni sawa na mfa maji anayeshikilia majani (kutaka kujiokoa), na hao wazushi wa hadithi walipokosa mambo au matukio muhimu yatakayotajwa kwa ajili ya Abubakr na Umar, basi akili zao zikatunga fadhila kama hizi, na nyingi ya hizo wamezileta kama ndoto za kubuni, hazina dalili ya kihistoria wala kimantiki au kielimu. Kama ambavyo Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Kitabu fadhail As-habin-Nabiyyi(s.a.w.w)
, Babu Qaidin-nabiyyi(s.a.w.w)
Lau kiintii Mut-takhidhan khalilan. Na Muslim ndani ya sahih yake katika Kitabufadhailis-sahabah, Babu min fadhail Abibakr Siddiq (r.a.). Imepokewa kutoka kwa Amr ibn Al-a's kwamba, Mtume(s.a.w.w)
alimtuma kwenye jeshi la Dhatus-salasil, nikamjia nikamwambia, "Je, ni watu gani wapendao mno?" Akasema ni "Aisha", Nikasema, Je, kwa wanaume? Akasema, "Baba yake "Aisha" Nikasema, "Kisha nani?" Akasema "Umar ibn Al-Khatab" Wakawaorodhesha watu wengi."
Riwaya hii imewekwa na wazushi pindi walipofahamu kwamba, historia imesajili ndani ya mwaka wa nane (yaani miaka miwili kabla ya kufariki Mtume(s.a.w.w)
kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alituma jeshi ambalo ndani yake alikuwemo Abubakr na Umar wakiwa chini ya uongozi wa Amr ibn Al-a's kwenda kupigana Dhatis-Salaasil, (walizusha riwaya hii) kwa lengo la kuikata njia ya yeyote atakayesema kuwa, "Amr ibn Al-a's alikuwa akitangulizwa kwa cheo juu ya Abubakr na Umar. Utawaona waliitengeneza riwaya hii kupitia ulimi wa Amri ibn Al-a's mwenyewe ili kuitia nguvu fadhila ya Abubalcr na Umar na wakamuingiza bibi Aisha ili kumuondoa shaka kwa upande mmoja, na ili kumpa hadhi isiyo na mpaka bibi Aisha kwa upande mwingine. Na kwa ajili hiyo utamuona Imam Nawawi ndani ya sharh yake ya sahihi Muslim anasema: "Hii ni kuweka bayana ubora wa Abubakr na Umar na Aisha (r.a) na ndani yake mna dalili iliyo wazi kwa Masunni katika kumboresha Abubakr juu ya Masahaba wote na baada yake ni Umar."
Riwaya hii ni kama riwaya nyingine dhaifu ambazo mad-dajjali (wazushi) hawakuona haya kuzizua hata kwa kupitia ulimi wa Ali ibn Abi Talib mwenyewe, ili tu kwa kupitia riwaya hizo wavunje hoja za Mashia ambao wao wanasema kuwa Ali ibn Abi Talib ni bora kuliko Masahaba wengine, hii ni kwa upande mmoja.
Na kwa upande wa pili wawafikirishe Waislamu kwamba Ali mwenyewe hakuona kuwa alidhulumiwa na wala hakuwalalamikia Abubakr na Umar (kutokana na dhulma aliyofanyiwa).
Bukhari ameandika ndani ya sahihi yake, Kitabu fadhail as-habinnabiyyi(s.a.w.w)
Babu manaqib Umar ibn Khat-taab Abi hafs. Muslim naye ndani ya sahihi yake, Kitabu fadhailis-sahabah Babu min fadhail Umar (r.a). Imepokewa kutoka kwa Ali, kutoka kwa ibn Abbas amesema: "Umar aliwekwa kitandani kwake na watu wakamzunguka wanaomba na kusali kabla hajanyanyuliwa, mimi nilikuwa miongoni mwao na mara kuna mtu fulani akanishika bega langu, kumbe alikuwa Ali, basi akamrehemu Umar na akasema: Hukumuacha mtu yeyote nimpendaye mno ili nitakapokutana na Mwenyezi Mungu niwe na amali mfano wa amali yako, namuapa Mwenyezi Mungu ninaamini Mwenyezi Mungu atakuweka pamoja na Masahaba wako wawili (Mtume na Abubakr) mara nyingi nilikuwa namsikia Mtume akisema: Nilikwenda mimi, Abubakr na Umar, nimeingia mimi, Abubakr na Umar, nimetoka mimi Abubakr na Umar." Naam hadithi hii dhahiri ni ya kubuni inasikika humo harufu ya siasa ilivyofanya kazi yake katika kumuweka mbali Fatmah asizikwe karibu na Baba yake pamoja na kuwa yeye Fatmah ni wa kwanza kumfuata Mtume katika kufa. Na muelezaji wa hadithi hii alisahau kuongeza baada ya kauli yake, Nilikwenda mimi Abubakr na Umar, niliingia mimi Abubakr na Umar na nilitoka mimi Abubakr na Umar, na nitazikwa mimi Abubakr na Umar.
Hivi watu hawa hawaoni ubaya kutolea hoja riwaya kama hizi ambazo zinapingwa na ukweli wa historia na vitabu vya Waislamu vilivyojaa (maelezo yanayohusu) dhulma dhidi ya Ali na Fatmah ambayo ilitendwa na kina Abubakr na Umar muda wote wa uhai wao? Kisha hebu izingatie kwa makini riwaya hii ili umuone mpokezi wa riwaya hii anavyomfanya Ali kuwa ni mtu kutoka mbali amekuja kuangalia maiti ya mtu asiyemtambua. Basi akawakuta watu wamesongamana (kwenye maiti huyo) wanaomba na kumsalia, akamshika Ibn Abbas begani na inakuwa kama kwamba alimnong'oneza sikioni maneno yake hayo na akaondoka, na ukweli wenyewe ni kuwa Ali katika msiba huo awe mbele ya watu na awasalishe na asimuache Umar mpaka azikwe kaburini mwake. Kwa kuwa watu katika zama za utawala wa Banu Umayyah walikuwa wakishindana kutengeneza hadithi (za uongo) kutokana na amri ya Muawiyah ambaye alitaka kunyanyua vyeo vya akina Abubakr na Umar dhidi ya ubora wa Imam Ali ibn Abitalib, basi zilikuja hadithi nyingi zinazozungumzia ubora wao zinazochekesha, na wakati mwingine zinapingana zenyewe kwa zenyewe kufuatana na namna ya matamanio ya msimuliaji anavyotaka. Miongoni mwa hao wasimuliaji wako wale wa Kibanu Taim ambao walikuwa hawamtangulizi yeyote juu ya Abubakr, na wako wengine ni katika Banu Adiyyi ambao hawakuwa wakimtanguliza yeyote juu ya Umar, na Banu Umayyah ambao nao waliathiriwa na Umar ibn Khattab ambaye alikuwa mjeuri na msusuavu asiyejali kufanya lolote wala asiyeogopa kitu. Basi mara nyingi walimsifia na kumtengenezea hadithi ambazo zinamboresha zaidi ya Abubakr.
Hebu angalia baadhi ya mifano hiyo: Muslim ameandika ndani ya sahihi yake katika Kitabu fadhailis-sahabah Babu min fadhail Umar (r.a). Naye Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Kitabul-iiman Babu tafadhul ahlil-iiman fll-a 'atrial Imepokewa kutoka kwa Abu Said Al-khudri amesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema, wakati fulani nilikuwa nimelala niliwaona watu wanaletwa kwangu na wamevaa kanzu, baadhi ya kanzu hizo zimefika vifuani na nyingine hazikufikia hapo, na aliletwa kwangu Umar ibn Khattab akiwa amevaa kanzu anaikokota. (Masahaba) wakasema, Ulifasiri nini juu ya hilo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Mtume akasema: Hiyo ni dini."
Na kama tafsiri ya Mtume kwa ndoto hii itakuwa ni dini, basi maana hiyo itakuwa kwamba, Umar ni bora kuliko watu wote kwa dini, kwa mujibu wao dini haikufika vifuani na haikuingia nyoyoni mwao, wakati ambapo Umari amejaa dini kuanzia kichwani mpaka kwenye nyayo zake na zaidi ya hapo anaikokota dini nyuma yake kama inavyokokotwa kanzu. Sasa basi, Abubakr hapa ana hadhi gani, Abubakr ambaye (inasemekana) imani yake inalinganishwa na imani ya umma wote? Ni kama ambavyo Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Kitabul-ilmi Babu fadhil-ilmi, na Muslim naye ameandika ndani ya sahih yake Kitabu fadhailis-sahabah Babu fadhail Umar.
Imepokewa kutoka kwa ibn Umar amesema: "Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema, Kuna wakati fulani nilikuwa nimelala nikakuta jagi la maziwa, basi nilikunywa mpaka nikaona manukato yanatoka vidoleni mwangu, kisha nikampa Umar ibn Khattab ziyada niliyobakisha, Masahaba wakasema, basi ulifasiri nini (ndoto yako) ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mtume akasema: "Maana yake ni elimu nyingi." Mimi nasema, hivi kweli wako sawa wale wanaojua na wale wasiyojua? Ikiwa ibn Khatab ameuzidi umma wote au watu wote katika dini akiwemo Abubakr, basi ni wazi kabisa ndani ya riwaya hii kwamba Umar pia amewazidi katika elimu na kuwa yeye ndiye mjuzi mno kuliko watu wengine baada ya Mtume(s.a.w.w)
. Sasa imebaki aina nyingine ya ubora ambayo watu hushindana katika kujipamba nayo na kwamba wanahusika nayo, na ubora huo ni miongoni mwa sifa njema ambazo Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanazipenda na watu wote wanaipenda na wanajaribu kuifikia, sifa hiyo si nyingine bali ni ushujaa. Hapana budi kwa watu wanaosimulia hadithi kuzua hadithi ambayo itakuwa ni kwa faida ya Umar ibn Khatab na hawakuacha kulifanya jambo hilo. Bukhari ameandika ndani ya sahih yake katika Kitabu fadhail as-habin-Nabiyyi(s.a.w.w)
, Babu qaulin-Nabiyyi Lau kuntu muttakhidhan khalilan. Pia Muslim ameandika ndani ya sahih yake, Kitabu fadhailis-sahabah Babu fadhail Umar.
Imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah amesema, "Nilimsikia Mtume(s.a.w.w)
anasema: Kuna wakati fulani nilikuwa nimelala, basi niliona niko juu ya kisima, juu yake kuna ndoo nikachota kutoka kisimani kiasi alichotaka Mwenyezi Mungu, kisha akaichukua ndoo ile ibn Abi Qahafah (Abubakr) akachota ndoo moja au mbili na katika kuchota kwake kulikuwa na udhaifu fulani Mwenyezi Mungu amsamehe kutokana na udhaifu wake. Kisha ikageukia upande wa magharibi na akaichukua Ibn Khattab, basi sikumuona mtu hodari miongoni mwa watu aliyechota namna alivyochota Umar mpaka watu walikunywa na kutosheka."
Sasa basi ikiwa dini ni kituo cha Imani, Uislamu, Uchamungu na kuwa karibu na Mwenyezi Mungu Mtukufu, kisha Umar ndiye aliyeizingira kiasi cha kuikokota nyuma yake wakati ambapo watu wengine hawakupata isipokuwa kiasi cha kufikia kifuani na sehemu nyingine za miili yao ikabakia wazi, na pia kama elimu aliyohusishwa nayo Umar ibn Khattab haikuwabakishia watu wengine chochote katika masazo aliyoyasaza Mtume(s.a.w.w)
, kwani yote alimpa Umar naye akayanywa yote bila hata kumkumbuka rafiki yake Abubakr, basi hapana shaka kwamba elimu hiyo ndiyo aliyoimiliki Umar katika kugeuza maamuzi ya Mwenyezi Mungu baada ya kufariki Mtume kwa Ijtihadi yake. Hapana shaka pia kwamba ijtihadi yake ndiyo matokeo ya elimu hiyo. Na kama nguvu zile na ushujaa ule amehusika nao Umar ibn Khattab, vile vile baada ya unyonge uliojitokeza kwa jamaa yake Abubakr na hii ni kweli (alikuwa dhaifu) kwani Abubakr alipata kumwambia Umar, "Bila shaka nimekwisha kukuambia kuwa kuhusu jambo hili wewe ni mwenye nguvu kuliko mimi na hakika umenishinda."
Mwenyezi Mungu na amsamehe Abubakr kwa unyonge wake na kwa kutangulia kwake kushika Ukhalifa kabla ya Umar, kwani wasaidizi wa Umar miongoni mwa Banu Adi na Banu Umayyah hawakustarehe wala kunufaika na kujipatia ngawira na ushindi mbali mbali kama walivyoyapata hayo katika zama za Ukhalifa wa Umar. Naam yote hayo basi ndiyo fadhila na ubora wa Umar ibn Khattab katika maisha ya duniani kwa hiyo ni lazima pia wamdhaminie pepo huko akhera kwa daraja kubwa na ubora mwingi zaidi ya rafiki yake Abubakr, na walifanya hayo ili kumpandisha daraja na kumpa ubora. Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Kitabu bad-ilkhalq Babu majaa fi sifatil-jannah wa an-nahaa mak-khluuqah, na Muslim naye ameandika ndani ya sahih yake katika Kitabu fadhailis-sahabah Babu min fadhail Umar.
Imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah (r.a) amesema: "Wakati fulani sisi tulikuwa mbele ya Mtume(s.a.w.w)
akasema: Kuna wakati nilikuwa nimelala, nilijiona nimo peponi, basi mara alikuja mwanamke akawa anatawadha pembeni ya jumba fulani, mimi nikasema, jumba hili ni la nani? Wakasema, ni la Umar ibn Khattab. Nikaukumbuka wivu wake (Umar), basi nikageuka nikaondoka, Umar akalia na akasema: Nikufanyie wivu wewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?" Ndugu yangu msomaji bila shaka umegundua mfumo wa riwaya hizi, mimi nimeziorodhesha kila moja kwenye ile ibara moja inayofanana katika kila riwaya ambayo inahusika na ubora wa Umar ibn Khattab, ibara hiyo si nyingine ila ni ile kauli ya Mtume (ambayo haiwezekani moja kwa moja kuwa aliisema) kauli inayosema: "Wakati fulani nilikuwa nimelala." Ibara hii utaikuta ndani ya riwaya zote. Wakati fulani nilikuwa nimelala niliwaona watu wakionyeshwa kwangu, wakati fulani nilikuwa nimelala nilikuta jagi la maziwa, wakati fulani nilikuwa nimelala niliona kisima, na wakati fulani nilikuwa nimelala nilijiona nimo peponi. Huenda mpokeaji wa hadithi alikuwa rnwingi wa kuota ndoto na kuchanganyikiwa akawa huzifasiri na kutengeneza riwaya kupitia ulimi wa Mtume(s.a.w.w)
. Ni mara nyingi Mtume amezuliwa zama za uhai wake naye akiwa yupo mbele ya watu hao, basi vipi baada ya kufariki kwake (wamemzulia mengi mno) na kwa hakika watu wa umma huu walikwisha geuka na wakauana wao kwa wao, wakawa makundi na madhehebu mengi na kila kundi wakishangilia na kujivunia mambo waliyonayo.
Sasa kimebaki kitu kimoja ambacho wamekisajili wanahistoria na Masahaba waliokuwa ni mashabiki wa Umar ibn Khattab mwenyewe, kitu hicho si kingine bali ni tabia aliyokuwa akisifika nayo Umar ambayo ni ile tabia mbaya ya ususuavu na ukali kwa watu, na yeyote mwenye tabia hii mara nyingi watu huwa hawampendi. Mwenyezi Mungu anasema:
وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ ﴿١٥٩﴾
"Na lau (wewe Muhammad) ungekuwa mkali na mgumu wa moyo wangekukimbia." (Our'an, 3:159).
Kwa bahati mbaya mashabiki wa Umar wao wanaufanya upungufu na dosari hiyo kuwa ni tendo la kusifiwa, na uovu kuwa ni ndiyo heshima. Kutokana na hali hiyo walifanya makusudi kutengeneza riwaya zinazoonesha udhaifu na udhalili ili kuipaka matope heshima ya Mtume(s.a.w.w)
ambaye Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa Mtume hakuwa mkali wala mgumu wa moyo, bali Mtume ni mpole wa tabia. "Na kwa rehma itokayo kwa Mwenyezi Mungu umekuwa mpole kwao na kwa hakika wewe (Muhammad) una tabia njema ya hali ya juu, na mpole mwenye huruma kwa waumini na ni rehma kwa walimwengu wote." Basi hebu na tuwasikilize wajinga hawa wanasema nini kumuhusu Mtume(s.a.w.w)
. Bukhari ameandika ndani ya sahih yake Kitabu Bad-il-khalq Babu sifati Iblis Wajunudih, naye Muslim ameandika ndani ya sahihi yake, Kitabu fadhailis-sahaba Babu minfadhail Umar.
Imepokewa kutoka kwa Sa'ad ibn Abi Waqqas amesema: "Umar alibisha hodi nyumbani kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
na mbele yake walikuweko wanawake miongoni mwa Maquraish wakizungumza naye na wakimdadisi, sauti zao zikiwa zinapaa juu. Basi alipobisha hodi Umar walisimama na mara moja wakavaa hijabu. Mtume wa Mwenyezi Mungu akamkaribisha Umar hali yakuwa Mtume anacheka. Umar akasema;Mwenyezi Mungu akufurahishe ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume akasema; Nawashangaa wanawake waliokuwa hapa, walipokusikia sauti yako wote wamekimbilia ndani. Umar akasema, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu wewe ndiyo ilikuwa na inastahiki wakuogope. Kisha akasema kuwaambia wanawake hao, Enyi maadui wa nafsi zao mwaniogopa mimi na wala hamumuogopi Mtume wa Mwenyezi Mungu? Wale wanawake wakasema, Ndiyo wewe ni mkali na msusuavu mno kuliko Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema kumwambia Umar, Wallahi namuapa Mwenyezi Mungu ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake kamwe shetani hawezi kukuta unapita njia fulani isipokuwa atapita njia nyingine isiyokuwa njia yako." Ni maneno machafu yatokayo vinywani mwao, hawasemi isipokuwa ni uongo.
Hebu tazama ubovu wa riwaya hii na ni vipi wanawake wale wamuogope Umar na wasimuogope Mtume wa Mwenyezi Mungu na wanyanyue sauti zao juu ya sauti ya Mtume(s.a.w.w)
na wala wasimuheshimu na wala wasiwe na hijabu mbele ya Mtume, na kwa kiasi cha kusikia tu sauti ya Umar walinyamaza na kuharakia kuvaa hijabu. Wallahi nashangazwa na mambo ya watu hawa wajinga ambao hayawatoshi yote hayo mpaka wayanasibishie wazi wazi kwa Mtume kwamba yeye ni mkali na ni msusuavu, kwani Umar ni mkali mno na ni msusuavu mno kuliko Mtume wa Mwenyezi Mungu. Eti hayo ni miongoni mwa matendo yanayopewa ubora kama huu na hayo yaonekane kuwa ndiyo fadhila za Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kama mambo yako hivyo basi Umar ni bora zaidi kuliko Mtume, na ikiwa hizi ni miongoni mwa tabia mbaya, ni vipi basi Waislamu wakiongozwa na Bukhari na Muslim wanazikubali hadithi hizi?
Kisha hayo hayakuwatosha mpaka wakamfanya shetani kuwa anacheza na kufurahia mbele ya Mtume(s.a.w.w)
na wala hamuogopi Mtume. Basi hapana shaka shetani huyu ndiye aliyewafanya wanawake wanyanyue sauti zao na wavue hijabu zao, lakini shetani alikimbia na akapita njia nyingine pale tu Umar alipoingia kwenye nyumba ya Mtume(s.a.w.w)
. Ewe Muislamu mwenye ghera, hivi unafahamu heshima ya Mtume(s.a.w.w)
ni ya kiwango gani kwa watu hao, na jinsi gani wao wanasema hali ya kuwa wanafahamu au hawafahamu kwamba Umar ni bora kuliko Mtume(s.a.w.w)
? Mambo kama haya bila shaka yoyote leo hii ndiyo yanayotokea kila wanapomzungumzia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
, na huwa wanaorodhesha makosa yake wanayoyadai na kulitakasa hilo kwa kuisema (eti) yeye Mtume ni mtu tu ambaye hakuhifadhiwa dhidi ya makosa na kwamba ni mara nyingi tu Umar akimsahihisha Mtume makosa yake, na kwamba Qur'an ilikuwa ikishuka kumuunga Umar mara nyingi tu. Yote hayo wanatolea ushahidi kupitia sura ya A 'basa Watawalla. Na kupitia suala la kuzalisha mtende kwa kutia mbelewele, pia kuhusu mateka wa Badri na mengineyo.
Lakini wewe utakaposema mbele yao kvvamba Umar alifanya makosa kwa kuzuwia sehemu ya wale wanaoimarishwa nyoyo zao, au alipoharamisha mut'aa mbili (yaani mut'atul-hajji na mut'atun-nisai) au pale alipofanya upendeleo katika kugawa kipato, basi bila shaka utaiona mishipa yao ya shingo inafura na macho yao yanakuwa mekundu, bali watakutuhumu kuwa umetoka katika dini na utaambiwa wewe ni nani hata umkosoe Umar Al-faruq ambaye ndiye anayetenganisha baina ya haki na batili? Basi hapo huna jingine la kufanya isipokuwa kukubali na usijaribu kuzungumza nao tena vinginevyo yatakukuta madhara. Bukhari anazibadili hadithi ili kulinda heshima yaUmar. Naam, bila shaka mtu anayechunguza atakapozifuatilia hadithi za Bukhari, nyingi hatozifahamu na itamdhihirikia kama kwamba hazikukamilika au zimekatwa, na kwamba yeye Bukhari huiandika hadithi hiyo hiyo kwa sanadi ile ile, lakini mara nyingi huipatia hadithi hiyo matamko yanayotofautiana katika milango mbali mbali.
Yote hayo huyafanya kwa kumpenda kwake mno Umar ibn Khatab, na huenda jambo hilo ndilo lililo wahamasisha Masunni wampende mno Bukhari mpaka wakamtanguliza mbele kuliko vitabu vingine. pamoja na kwamba Muslim ni bora zaidi kwa udhibiti, na kitabu chake kimepangwa kufuatia utaratibu wa milango. Lakini Bukhari kwa Masunni ndiyo kitabu sahihi mno baada ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na hali hii imechangiwa na mwenendo wa Bukhari katika kuziporomosha kwake fadhila za Ali ibn Abi Talib. Bukhari kwa upande fulani alifanya namna ya kuzikata hadithi na kuzifupisha kila pale zilipogusa (namna fulani itakayoporomosha) heshima ya Umar, kama alivyofanya njia hiyo hiyo (kuzikata na kuzifupisha) hadithi zinazotaja ubora wa Ali. Tutakutosheleza hilo kwa baadhi ya mifano hivi punde Insha-Allah.
Baadhi ya mifano ya mabadiliko ya hadithi zenye uthibitisho unaoiweka wazi hali halisi ya Umar ibn Khattab.
1). Muslim ameandika ndani ya sahih yake katika Kitabul-haidh Babut-tayamum amesema: "Kuna mtu fulani alikuja kwa Umar akasema: Hakika mimi nimepatwa na janaba lakini sikupata maji ya kuoga, Umar akasema, Usiswali, Ammar akasema. Ewe Amirul-Muuminina hukumbuki tulipokuwa mimi na wewe katika jeshi, kisha tukapatwa na janaba na hatukupata maji, amma wewe hukusali, amma mimi nilijigaragaza kwenye udongo na nikaswali. Halafu Mtume(s.a.w.w)
akasema: bila shaka ilikuwa inakutosha upige mikono yako kwenye ardhi kisha upulize na upake uso wako na viganja vyako. Umar akasema, Ewe Ammar mche Mungu, Ammar, akasema ukitaka sitasimulia hadithi hii." Riwaya hii wameiandika kina Abu Dawood ndani ya Sunan yake, Ahmad ibn Hambal ndani ya Musnad yake, Nasai ndani ya Sunan yake, na Baihaqi na Ibn Majah pia.
Lakini Bukhari amefanya khiyana, khiyana ya kutokuwa muaminifu katika kunakili hadithi, kama ilivyo kwa ajili ya kulinda heshima ya Umar. Ameificha hadithi hii kwa kuwa hakupenda watu wafahamu ujinga wa Khalifa Umar kutokufahamu hata kanuni nyepesi za fiqhi ya Kiislamu. Hebu basi ione riwaya hiyo ambayo Bukhari amefanya khiyana ndani yake. Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Kitabut-tayammum hal-yiinfakhu fihimaa. Amesema: Kuna mtu fulani alikuja kwa Umar ibn Khattab akasema, "Hakika mimi nimepatwa na janaba na sikupata maji, basi Ammar ibn Yasir akasema, kumwambia Umar ibn Khattab, hukumbuki kwamba tulikuwa safarini mimi na wewe...? Al-hadithi.
Kama unavyomuona Bukhari ameondoa kwenye hadithi hiyo maneno yasemayo, "Umar akasema usiswali." Maneno haya hayapo. na hapana shaka Bukhari aliyaondoa na kuyaacha ili yasijedhihiri madh-hebu ya Umar kwa watu, madhehebu ambayo yeye alikuwa akiyaona yanamfaa hata zama za uhai wa Mtume, na alikuwa akifanya ijtihadi dhidi ya maandiko ya Qur'an na Sunna, na alibakia kwake kwenye madhehebu yake haya hata baada ya kuwa amekuwa Khalifa na akawa anayaeneza miongoni mwa watu wa kawaida katika Waislamu. Ibn Hajar amesema: "Madhehebu haya ni mashuhuri kuwa yametokana na Umar." Na dalili ya kwamba alikuwa akiyasisistiza madhehebu hayo ni pale Ammar alipomwambia Umar, "Ukipenda sitoisimulia hadithi hiyo." Ewe msomaji soma ushangae."
2). Al-hakim An-nishapuri ameandika ndani ya Mustadrak juzuu ya pili ukurasa 514, nave Dhahabi ameiandika hadithi hiyo ndani ya Tal-khisi yake. Imepokewa kutoka kwa Anas ibn Malik amesema:"Hakika Umar ibn Khatab alisoma kwenye mimbar kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo. "Fa anbatnaa fihaa habban wai 'naban waqadhban wazaitunan wanakhlan wahadaiqa ghul-ban wafakihatan waabbaa."
Kisha akasema yote haya tunayafahamu lakini hii Abbaa ni kitu gani? Basi fuateni yale yaliyobainishwa uongofu wake kwenu ndani ya kitabu na muyatumie, na yale ambayo hamkuyafahamu basi yarejesheni kwa Mola wake." Na riwaya hii wameinakili wafasiri wengi ndani ya vitabu vyao na tafsiri walipokuwa wakifasiri sura ya A'basa, kama vile Suyutti ndani ya Ad-durru manthur, Zamakhshari ndani ya Al-kash-shaf, Ibn Kathir ndani ya tafsiri yake, Ar-razi ndani ya tafsiri yake na Khaazin ndani ya tafsiri yake. Lakini Bukhari kama kawaida yake. hadithi hii ameiondosha na kuikata ili watu wasije wakafahamu kutokufahamu kwa khalifa Umar maana ya Al-abb na ndipo alipoinakili hadithi hii kama ifuatavyo: Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Kitabul-I'ilisam bil-kitabi was-sunnah babu mayukrahu min kalhratatis-sual wa takalafa maalaa ya 'anih wa Qaulullahi la 'ala La las-alu a 'n ash-yaa in-tubda lakum lasn-ukum.
Imepokewa kutoka kwa Anas ibn Malik amesema: "Tulikuwa mbele ya Umar akasema, tumekatazwa kujikalifisha." Naam hivi ndivyo afanyavyo Bukhari kwa kila hadithi ambayo inazo harufu zinazomkosoa Umar. Basi ni vipi msomaji ataufahamu ukweli wa mambo kutokana na hadithi hii iliyokatwa? Bila shaka nia ya Bukhari ni kumsitiri Umar kutokufahamu kwake maana ya Al-abb na akasema tu: Tumekatazwa kujikalifisha.
3). Ibn Majah ameandika ndani ya Sunan yake Juz.2 uk.227 na Al-hakim ndani ya Mustadrak juz.2 uk.59 na Abu Dawood ndani ya Sunan yake juz.2 uk.402 na Bayhaqi ndani ya Sunan yake juz.6 uk. 264 na Ibn Hajar ndani ya Fat-hulbari na wengineo pia wameandika. Kutoka kwa Ibn Abbas kwamba amesema: "Umar aliletewa mwenda wazimu wa kike aliyezini, basi akawataka watu ushauri, kisha akaamuru apigwe mawe. Mara Ali ibn Abi Talib akapita pale akauliza ana nini huyu? Wakasema, Ni mwenda wazimu katika ukoo fulani amezini, na Umar ameamuru apigwe mawe. Ali akasema mrudisheni, kisha (Ali) alimuendea Umar akasema, Hujui ya kwamba kalamu imenyanyuliwa kwa mwenda wazimu mpaka atakaporejelewa na akili. na mwenye kulala naye mpaka atapoamka na motto mpaka atapobalehe? Basi Umar akamuachilia yule mwenda wazimu na akasema, Lau kama si Ali Umar angeangamia."
.
Lakini Bukhari ameivuruga riwaya hii, sasa basi ni vipi watu watautambua ujinga wa Umar namna asivyoweza kuyafahamu mambo yanayohusu adhabu ambazo kitabu cha Mwenyezi Mungu kimeziweka na Mtume kazibainisha? Ilikuwaje akakikalia cheo cha Ukhalifa mtu ambaye hii ndiyo sifa yake? Haiwezakani kabisa kwa Bukhari kuitaja riwaya hii kikamilifu kwa sababu tu ndani yake zimo fadhila za Imam Ali ibn Abi Talib ambaye alikuwa akikesha akiwafundisha watu wasiyoyajua, na pia hawezi kuitaja kikamilifu kwa sababu Umar mwenyewe amekiri kwamba. "Lau kama si Ali Umar angeangamia." Basi hebu tumuangalie Bukhari ni jinsi gani anavyoigeuza riwaya hii na kuificha. Bukhari amethibitisha ndani ya sahih yake katika Kitabid-Muhaaribina min ah-lil-kufri war-riddah Babu la yurjamul-majnunn walamaj-nunah. Bukhari bila ya kutaja sanad yoyote amesema. "Ali alimwambia Umar hujui kwamba kalamu imenyanyuliwa kwa mwenda wazimu mpaka azindukane na mtoto mpaka abalehe na mwenye kulala mpaka aamke?
Naam, bila shaka huu ni mfano hai unaonesha namna ya utendaji kazi wa hadithi ulivyo kwa Bukhari, kwani yeye anaikata hadithi pindi inapokuwa ndani yake kuna fedheha kwa Umar. Na pia huifupisha hadithi kama inafadhila na sifa kwa Imam Ali, basi hawezi kabisa kuiandika hadithi hiyo kikamilifu.
4). Muslim ameandika ndani ya sahih yake katika Kitabul-hudud Babu haddi shaaribil-khamri. Imepokewa kutoka kwa Anas ibn Malik, kwamba Mtume(s.a.w.w)
aliletewa mtu aliyekunywa pombe akampiga kwa fimbo mbili kiasi (mara) arobaini, (Anas) amesema, na Abubakr pia alifanya hivyo hivyo. Amma Umar alipokuwa khalifa aliwashauri watu, basi Abdurrahman ibn A'uf akasema uchache wa adhabu ni bakora themanini, Umar akaamuru hivyo." Na Bukhari kama kawaida yake hataki kudhihirisha kutokujua kwa Umar namna hukmu ilivyo katika adhabu, kwani ni vipi anawashauri watu kuhusu adhabu inayoeleweka ambayo Mtume aliitekeleza kisha baada yake Abubakr aliifanya? Bukhari ameandika ndani ya sahih yake katika Kitabul-Hudud Babu Majaa 'a fi dharbi sharibil-khamr.
Imepokewa kutoka kwa Anas ibn Malik kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
alipiga haddi kuhusu pombe kwa kutumia fimbo na kiatu na Abubakr alipiga mijeledi arobaini.
5). Wanahistoria na wataalamu wa hadithi ambao waliandika juu ya maradhi ya Mtume na kufariki kwake na namna alivyowataka Masahaba awaandikie maandiko ambayo kamwe hawatapotea baada yake, na tukio hilo likaitwa kuwa ni msiba wa siku ya Al-Hamisi. Na wameandika pia namna Umar alivyopinga na akasema kuwa, "Mtume anaweweseka." Mwenyezi Mungu apishe mbali. Na Bukhari ameandika ndani ya sahih yake katika Kitabul-jihad Babu Hal-Yustash-fau' Ila Ah-lid-Dhimmah wamua 'malatihim. Naye Muslim ameandika ndani ya sahihi yake katika Kitabul-wasiyyah Babu Tarkil-wasiyyah Liman laisa lahu shaiun yusii-fihi. Imepokewa kutoka kwa ibn Abbas (r.a) kwamba amesema: "Siku ya al-khamisi, kulikuwa nini siku hiyo ya al-khamisi? Kisha akalia mpaka machozi yake yakalowanisha changarawe. Halafu akasema siku hiyo ya al-Khamisi Mtume (s.a.w.w) maumivu yake yalizidi, akasema, Nileteeni karatasi nikuandikieni maandiko ambayo kamwe hamtapotea baada ya maandiko hayo. Basi watu wakazozana, na haifai kuzozana mbele ya Mtume, kisha wakasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu anaweweseka, Mtume akawaambia, Niacheni kwani hali niliyonayo mimi ni bora kuliko hivyo mnavyodai dhidi yangu. Aliusia wakati wa kufa kwake mambo matatu: Waondoeni washirikina katika bara Arabu, na mtekeleze ridhaa ya wawakilishi kama vile mimi nilivyokuwa nawatekelezea, na lile la tatu nimelisahau
."
Naam, huu ndiyo msiba wa siku ya al-khamisi ambao Umar alichukua nafasi ya ushindi akampinga Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
na akamzuwia kuandika kutokana na maneno yale machafu (aliyoyatamka) ambayo yanapingana na kitabu cha Mwenyezi Mungu. Maneno hayo ni kuwa: "Eti Mtume anaweweseka
." Nao Bukhari na Muslim hapa wameinakili hadithi hii kwa ibara sahihi ambayo Umar aliitamka na hawakuibadili kwa kuwa jina la Umar halikutajwa hapa, na kuihusisha kauli hii mbaya kwa mtu asiyejulikana hapana madhara. Lakini pale linapokuja jina la Umar ndani ya riwaya ambayo inataja kuwa yeye Umar ndiye aliyetamka maneno yale inakuwa vigumu kwa Bukhari na Muslim kuiacha riwaya hiyo kama ilivyo, kwani inamfedhehesha Khalifa na inadhihirisha ukweli wake uliyo wazi na kuumbua kiwango cha yeye kutokuwa kwake na heshima mbele ya Mtume(s.a.w.w)
.
Na Umar ndiye ambaye alikuwa akimpinga Mtume muda wote wa uhai wake katika mambo mengi, na Bukhari na wengine mfano wake walifahamu kwamba neno hili pekee linatosha kuamsha hisiya za kila Mwislamu dhidi ya Khalifa Umar hata hao Masunni wenyewe, hivyo basi wakafanya makusudi kuficha ukweli. Sasa hiyo ndiyo fani yao mashuhuri kuhusu mambo kama haya, na wakabadilisha neno Anaweweseka wakaweka neno lisemalo Maumivu yamemzidia ili waitupilie mbali ile ibara chafu. Hebu basi angalia vile Bukhari na Muslim walivyoandika kuhusu maudhui hii hii ya msiba. Imepokewa kutoka kwa ibn Abbas amesema, "Mtume wa Mwenyezi Mungu alipokaribia kufariki, na watu walikuwemo ndani ya nyumba (yake) na Umar ibn Khattab akiwa yu miongoni mwao, Mtume(s.a.w.w)
alisema: Njooni nikuandikieni maandiko ambayo kamwe hamtapotea baada yake.
Basi Umar akasema, Bila shaka Mtume kazidiwa na maradhi nanyi mnayo Qur'an, kinatutosha Kitabu cha Mwenyezi Mungu, hapo watu waliokuwemo humo ndani wakahitilafiana na kuzozana, miongoni mwao wakasema sogeeni Mtume akuandikieni maandiko ambayo hamtapotea baada yake, na miongoni mwao wakasema alivyosema Umar.
Walipozidisha makelele na kuhitilafiana mbele ya Mtume(s.a.w.w)
, Mtume akawaambia, Ondokeni. Abdallah ibn Mas-ud amesema: Ibn Abbas alikuwa akisema, Msiba mkubwa kuliko yote ni ule uliyopita baina ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na baina ya kuwaandikia maandiko kutokana na kuhitilafiana kwao na fujo zao. Na kwa kuwa Muslim alichukua kutoka kwa mwalimu wake ambaye ni Bukhari, basi sisi tunamwambia Bukhari, "Namna yoyote ile utakavyoipinda ibara na namna utakavyojaribu kuuficha ukweli hakika hicho ulichokiandika kinatosha kuwa ni hoja dhidi yako na dhidi ya bwana wako Umar, kwani tamko la kuweweseka au maradhi yamemzidi, lina matokeo ya aina moja kwa kuwa yeyote mwenye kuzingatia atakuta kwamba watu hadi leo wanasema, "Masikini fulani homa imemzidi mpaka anaweweseka." Na hasa tutakapoongezea juu ya neno hilo, Mnayo Qur'ani, kinatutosha Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na maana ya hilo ni kwamba Mtume(s.a.w.w)
mambo yake ndiyo yamefikia kikomo na kuwepo kwake ni sawa kama hayupo.
Nami nampa changamoto kila mwanachuoni afanye mazingatio katika tukio hili peke yake bila ya mambo mengine yoyote, na bila ya kufuatilia yaliyopita, basi huenda akaamsha hisia zake mbaya mno dhidi ya Khalifa (Umar) ambaye aliunyima umma (wa Kiislamu) uongofu na ikawa ni sababu moja kwa moja ya kupotea kwa umma huu. Hivi ni kwa nini tunaogopa kusema ukweli maadam ukweli huo ni katika kumtetea Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
? Na zaidi ya hapo tunaitetea Qur'ani na mafunzo ya Uislamu kwa ukamilifu wake. Mwenyezi Mungu anasema:"Wala msiwaogope watu, basi niogopeni mimi, wala msibadilishe aya zangu kwa thamani ndogo (ya duniani) na wale wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndiyo makafiri."
Ni kwa nini baadhi ya wanachuoni hadi leo hii katika zama za elimu na nuru (bado) wanajaribu kwa juhudi zao zote kuuficha ukweli kwa kutumia tafsiri za kulazimisha ambazo wanaziunda, tafsiri ambazo hazisaidii chochote? Hebu tazama mambo aliyoyazua mwanachuoni aitwaye Muhammad Fuad Abdul-Baqii ndani na sherehe yake ya kitabu kiitwacho, Al-Lu-ulu-u Wal-mar-jaan fimat-Tafaqa Alayhis-Shaykhain, pale alipoileta hadithi ya msiba wa siku ya Al-khamis amesema akilifafanua tikio hilo. "Nileteeni kitabu, kwa maana ya vifaa vya kuandikia kama vile kalamu na wino, au alikusudia kitabu kwa maana ya kitu ambacho huandikwa ndani yake kama vile karatasi na kombe (mfupa wa begani). Jambo lililowazi hapo ni kwamba, maandiko haya aliyotaka kuandika Mtume, si mengineyo bali alitaka kumthibitisha Abubakr kwenye Ukhalifa, lakini wao walipozozana na maradhi ya Mtume yakawa yamezidia aliacha kufanya hivyo na akatumia kumbainisha kwa msingi alioufanya kupitia (kusalisha) sala."
ameenedelea kusherehesha maana ya neno Hajara (yaani anaweweseka) anasema mwanachuoni huyu, "Hajara, Ibn Bat-tal ameidhania kuwa maana yake ni Amechanganyikiwa, naye Ibn At-tiin amesema maana yake ni Kuweweseka. Na kwa maana hiyo si muafaka kuambiwa Mtume kutokana na daraja yake tukufu, na inawezekana kuwa makusudio yake ni kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu amekuacheni, inayotokana na kuhama ambayo ni dhidi ya kuwepo, kutokana na yaliyomfikia miongoni mwa mambo yenye kufika yanayohusu Uungu, na ndiyo maana alisema: "Fii rafiiqil A 'ala. " Na amesema Ibnul-Athir kwamba, neno Hajara limekuja kwa njia ya kuuliza, na hamza ya kuulizia inayoleta maana ya Je, maneno ayasemayo Mtume yamebadilika na yamechanganyikana kwa ajili ya maradhi aliyo nayo? Imeondoshwa, na ndicho kilicho bora kukisema kuhusiana na maana ya Hajara. Na wala haiwezi kufanywa kuwa ni maelezo yenye kumaanisha ubaya au kuweweseka, na msemaji (wa hilo neno la Hajara) alikuwa ni Umar, na hatudhanii kuwa Umar anaweza kutamka hivyo." (Mwisho wa maneno yake).
Sisi tunakujibu ewe mwanachuoni mheshimiwa kwamba, "Dhana haitoshelezi kitu mbele ya haki, kunatutosheleza kukiri kwako kwamba, msemaji wa tamko hili baya alikuwa Umar. Nani aliyekuambia kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alitaka kuandika juu ya ukhalifa wa Abubakr? Na Je, Umar angelipinga hilo? Je, ni Umar huyo huyo ambaye aliyeziimarisha nguzo za Ukhalifa wa Abubakr na akawalazimisha watu wakubali kwa nguvu mpaka akatishia kuichoma nyumba ya Bibi Fatmah
? Je, yuko mwanachuoni mwingine aliyedai madai kama haya asiyekuwa wewe? Kinachofahamika kwa wanachuoni wa zamani mpaka sasa hivi ni kwamba, Ali ibn Abi Talib ndiye aliyeteuliwa na Mtume awe Khalifa japo tamko linalohusu uteuzi huo hawalikubali. Lakini yanakutosh yale aliyoyaandika Bukhari ndani ya sahih yake katika Kitabul-Wasaya, juzuu ya 3 uk. 186 amesema: "Kuna watu fulani walizungumza mbele ya Aisha kwamba, Ali (r.a) alikuwa ndiyo wasii (wa Mtume), basi Aisha akasema, Ni wakati gani (Mtume) alipousia juu yake na hali mimi nilikuwa nimemuegemeza (Mtume) kifuani mwangu, akaomba aletewe chombo (fulani) nami nikiwa nimempakata miguuni mwangu basi mara punde alifariki, hivyo ni wakati gani aliousia juu yake
?".
Na Bukhari ameiandika hadithi hii kwamba, ndani yake imo dalili inayokanusha wasia, na hili ni jambo linalomfurahisha Bukhari. Lakini sisi tunasema kwamba, "Wale waliozungumza mbele ya mama Aisha kuwa Mtume aliusia Ukhalifa kwa Ali ni wakweli, kwa kuwa Aisha hakuwapinga na yeye mwenyewe hakukanusha wasia ule, lakini aliuliza kama mtu apingaye akasema, Ni lini aliusia? Nasi tunamjibu aliusia mbele ya Masahaba watukufu wakati yeye mama Aisha akiwa hayupo, na hapana shaka kwamba masahaba hao walimtajia mama Aisha wakati Mtume alipousia juu ya Ali kuwa Khalifa, lakini watawala na waliovamia (huo Ukhalifa) walizuia hoja kama hizi kuelezwa (hadharani) kama ambavyo jambo la tatu (miongoni mwa mambo aliyoyausia Mtume) walilisahau. Kwa hiyo siasa zilisimama kidete kuufuta ukweli huu, kwani Umar mwenyewe alipata kutamka wazi kuwa alimzuia Mtume wa Mwenyezi Mungu asiandike yale maandiko pale tu alipofahamu kwamba yanahusiana na Ukhalifa wa Ali ibn Abi Talib. Ibn Abil-hadid ameyaandika majibizano yaliyopita baina ya Umar ibn Khat-tab na Abdallah ibn Abbas, Umar alisema katika majibizano hayo kama ifuatavyo.
"Hivi katika nafsi ya Ali kumebakia kitu kuhusu Ukhalifa?" Ibn Abbas akasema: "Ndiyo." Umar akasema:"Hapana shaka Mtume wa Mwenyezi Mungu alitaka kulibainisha jina lake (Ali) wakati wa maradhi yake, mimi nikamzuia kwa kumuonea huruma na kuulinda Uislamu." Ewe mwanachuoni mtukufu, kwa nini unaukimbia ukweli? Inashangaza mno, badala ya wewe kuchangia kuudhihirisha ukweli baada ya zama za kiza pamoja na Banu Umayyah na Banu Abbas kuondoka, ninyi mnaongezea juu ya giza hilo kifuniko na mapazia ili muwazuie watu wengine wasiufahamu ukweli na kuufikia. Ikiwa wewe uliyasema hayo uliyoyasema kwa nia njema, basi bila shaka mimi namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akuongoze na akufungue fahamu zako.
6). Kama ambavyo Bukhari amefanya mengi kubadilisha na kufuta, na pia kuvuruga hadithi za Mtume ambazo zinaonyesha unyonge na dosari walizonazo Abubakr na Umar. Kwa mara nyingine Bukhari anakusudia kulivuruga tukio mashuhuri la kihistoria ambalo ndani yake Mtume wa Mwenyezi Mungu alizungumza jambo ambalo Bukhari hakulipenda, basi ameipuuza kabisa hadithi hiyo kwa sababu kilichomo kinampa hadhi Ali juu ya Abubakr.
Wanachuoni wa Kisunni wamesimulia ndani ya Sihahi zao na Musnad zao, kama vile Tirmidhi ndani ya Sahih yake, Al-Hakim ndani ya Mustadrak yake, Ahmad ibn Hambal ndani ya Musnad yake, Imam Nasai ndani ya Khasais yake, Tabari katika tafsiri yake, Suyuti ndani ya tafsiri yake iitwayo Ad-Durrul-Manthur na Ibnul-Athir ndani ya tarikh yake, pia Kanzul-Ummal na Zamakhishari ndani ya Al-Kash-Shaf na wengineo wengi, wote wamethibitisha kwamba:
"Mtume wa Mwenyezi Mungu alimtuma Abubakr (r.a) akamuamuru akatangaze maneno haya yafuatayo, Bara-Atun-minallahi Warasulihi, kisha akamfuatisha nyuma yake Ali (r.a) na akamuamuru Ali akatangaze maneno hayo yeye Ali, basi Ali (r.a) akasimama katika siku kumi za mfunguo tatu akatangaza akasema: Hakika Mwenyezi Mungu yuko mbali na washirikina, na pia Mtume wake (yuko mbali nao). Basi nendeni mkizunguka katika ardhi miezi minne, na asihiji mshirikina baada ya mwaka huu. Na yeyote asitufu al-Ka'aba hali akiwa uchi." Abubakr (r.a) alirudi kisha akasema,"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kuna jambo limeshuka kuhusiana na mimi?" Mtume akasema: "Hapana jambo, lakini Jibril amenifikia na amesema, Hawezekani kabisa mtu yeyote kutekeleza amri hii isipokuwa wewe (yaani Mtume) au mtu anayetokana na wewe
."
SHARTI YA KUCHAPA
Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein
Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini
ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.
MWISHO WA KITABU