1
WAULIZE WANAOFAHAMU
(QUR. 16:43 NA 21:7) Bila shaka aya hii Tukufu inawaamuru Waislamu kuwarejea watu wenye kumbukumbu kwa kila linalowatatiza ili wapate kuufahamu muelekeo ulio sawa, kwani Mwenyezi Mungu amewaandaa (wenye kumbukumbu) kwa ajili hiyo baada ya kuwafunza, basi wao ndiyo waliobobea katika elimu na ndiyo wanaofahamu Ta'wili ya Qur'an. Kwa hakika aya hii ilishuka kuwatambulisha Ahlul-Bait
nao ni Mtume Muhammad, Ali, Fatma, Hasan na Husein, na hili lilitendeka katika zama za Mtume. Amma baada ya Mtume(s.a.w.w)
mpaka kitakaposimama Qiyama (wenye kumbukumbu) ni hawa hawa watano waliotajwa ambao ndiyo Ahlul-Kisaa na huongezwa kwa hao, Maimamu tisa kutoka katika kizazi cha Hussein
ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu amewabainisha katika Minasaba mbali mbali na akawaita kuwa ni Maimamu wa uongofu na ni taa ziondoazo kiza na wao ndiyo wenye kumbukumbu, na ndiyo waliobobea katika elimu, Mwenyezi Mungu amewarithisha elimu ya kitabu. Riwaya hizi zimethibiti na ni sahihi tena mutawatir kwa Mashia tangu zama za Mtume(s.a.w.w)
, na wamezieleza baadhi ya wanachuoni wa Kisunni, na wafasiri wao wamekiri kwamba kushuka kwa aya hii kunawahusu Ahlul-Bait
. Ninawataja miongoni mwa wanachuoni hawa kwa kutolea mfano:
1) Im1)Imam Thaa'labi katika Tafsiri yake (alipozunhumzia) maana ya aya hii katika Surat An-NahliNahl.
2) Tafsirul-Qur'an ya ibn Kathir Juzuu ya pili ukurasa 570570.
3) Tafsirut-Tabari, Juzuu ya kurni na nne ukurasa 109.
4) Tasirul-Alusi iitwoyo Ruhul-Maani Juzuu ya kumi na nne ukurasa wa 134.
5) Tafsirul-Qurtubi Juzuu ya kumi na moja ukurasa 272.
6) Tafsirul-Hakim iitwayo Shawa-Hidut-Tanzil, Juzuu ya kwanza ukurasa 334.
7) Tafsir At-Tustari, itwayo Ih-QaaQul-Haq, Juzuu ya tatu ukurasa 482.
8) Yanahi'ul-Mawaddah cha Al-Qanduzi Al-Hanafi ukurasa wa 51 na 140.
Na ilivyokuwa wenye kumbukumbu kwa dhahiri ya aya ni Ahlul-Kitab miongoni mwa Mayahudi na Wakristo, basi imetulazimu juu yetii kubainisha wazi kwamba wao sio waliokusudiwa katika aya hiyo Tukufu.
Kwanza
; Kwa sababu Qur'an Tukufu imewataja (Mayahudi na Wakristo) mara nyingi katika aya nyingi kwamba wao waliyageuza maneno ya Mwenyezi Mungu na wakakiandika kitabu kwa mikono yao, na wakasema kuwa kimetoka kwa Mwenyezi Mungu ili wakiuze kwa thamani ndogo. na (Qur'an) imeshuhudia uongo wao na kuigeuza kwao haki, basi haiwezekani wakati huo huo iwaamrishe Waislamu warejee kwao (Mayahudi na Wakristo) katika Mas-ala wasiyoyajua.
Pili
: Bukhari ameeleza katika Sahih yake ndani ya Kitabus-Shahadah mlango usemao, "Hawaulizwi washirikina". Juzuu ya tatu uk. 163. Kutoka kwa Abuhurairah: Amesema Mtume(s.a.w.w)
: "Msiwaamini Ah-lil-Kitab na wala msiwapinge (kuwaambia kuwa ni waongo) semeni tumemuamini Mwenyezi Mungu na yaliyoteremshwa (toka kwake)
. Hii inafundisha kutowarejea (Ahlul-kitab) katika mas-ala na (lililopo) ni kuwaacha na kuwapuuza, kwa sababu kutowaamini na kisha kutokuwapinga kunakanusha lengo la kuwauliza ambalo linasubiri jawabu sahihi. Tatu: Bukhari ameeleza ndani ya Sahih yake katika Kitabut-Tauhidi mlango wa kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Kila siku yeye yumo katika mambo." Juzuu ya nane ukurasa 208 kama ifuatavyo: Kutoka kwa Ibn Abbas amesema: "Enyi kongamano la Waislamu, vipi mnawauliza Ah-Lul-Kitab na hali kitabu chenu alichokiteremsha Mwenyezi Mungu kwa Mtume wenu(s.a.w.w)
ndicho chenye maelezo halisi ya Mwenyezi Mungu na hakikuharibiwa, Mwenyezi Mungu amekusimulieni kwamba Ah-Lul-Kitab wamekwisha badilisha na kugeuza (yaliyoteremshwa) katika vitabu vya Mwenyezi Mungu (vilivyotangulia) wakaandika kwa mikono yao kisha wakasema hayo ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili wayauze kwa thamani ndogo, je hajakukatazeni yale yaliyokufikieni katika elimu kuwauliza hao? Basi fahamuni, namuapa Mwenyezi Mungu; hatujamuona mtu miongoni mwao akikuulizeni kuhusu yaliyoteremshwa kwenu." Nne: Lau leo hii tutawauliza Ah-Lul-Kitab miongoni mwa Wakristo bila shaka watadai kuwa Isa ni Mungu na Mayahudi wanawapinga (Wakristo kwa madai hayo) na wala hawamkubali (Isa) japo kwa Utume, na kila mmoja wao anaupinga Uislamu na Mtume wa Uislamu, na wanasema kuwa (yeye Mtume) ni muongo na ni mzushi.
Kwa yote hayo basi haiwezekani ifahamike maana iliyomo katika aya kwamba Mwenyezi Mungu ametuamrisha tuwaulize wao, na ilipokuwa Ah-Lud-Dhikr katika dhahiri ya aya ni wao Ah-Lul-Kitab miongoni mwa Wayahudi na Wakristo, basi hapana shaka hali hii haikanushi kwamba aya hii imeshuka kwa watu wa Nyumba ya Mtume kama ambavyo imethibiti kwa 33 Mashia na Masunni kwa njia sahihi. Kwa hiyo inafahamika kutoka katika aya hiyo kwamba, Mwenyezi Mungu ameirithisha elimu ya Kitabu ambacho ndani yake hakuacha kitu kwa hawa Maimamu ambao amewateua kutoka miongoni mwa waja wake ili watu wawarejee katika Tafsiri na Ta'awiili, na kwa kufanya hivyo uongofu wao utathaminiwa iwapo watamtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na hekima yake imetukuka alitaka watu wote wawanyenyekee wateule wanaotoka miongoni mwao, ambao aliwachagua na akawafunza elimu ya Kitabu ili hali za watu ziwe katika nidhamu. Basi lau watu hawa hawangekuwepo miongoni mwa watu, nafasi ingekuwa wazi mbele ya wenye kujigamba (kuwa wanafahamu), na wajinga na hata kila mmoja angefanya kulingana na matamanio yake na mambo ya watu yangevurugika maadam kila mmoja aweza kudai kuwa ni mjuzi zaidi kuliko mwingine. Ili nitoe hoja baada ya mimi kukinaika kwamba Ah-Lul-Bait ndiyo "Ah-Lud-Dhikri" nitauliza maswali ambayo hayana jawabu kwa Ahlis-Sunnah Wal-Jamaa, au yanayo majibu lakini mwenye kujikalifisha kujibu majibu yake hayana hoja iwezayo kukubaliwa na mtu mtafiti mwenye kutaka uthibitisho imara. Ama jawabu lake la kweli, lipo kwa hawa Maimamu watakatifu ambao wameijaza dunia elimu na maarifa na pia wameijaza matendo mema na mafanikio.
MLANGO WA KWANZA: YALE YANAYOMUHUSU MUUMBA MTUKUFU
Swali la Kwanza : Kumuona Mwenyezi Mungu na Kumfanyia Mwili Mwenyezi Mungu katika kitabu chake kitukufu anasema:"Macho hayamfikii (kumuona)
". (Qur 'an, 6:103).
(Hakuna chochote chenye mfano wake
) (Qur'an 42:11). Na anasema Mwenyezi Mungu kumwambia Musa alipotaka kumuona: "Kamwe hutaniona
" (Qur'an 7:143.) Basi ni vipi (enyi Masunni) mnazikubali hadithi zilizopokewa ndani ya Sahih Bukhari na Sahih Muslim kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anajidhihirisha kwa viumbe wake nao watamuona kama wauonavyo Mwezi mpevu? Na kwamba Mwenyezi Mungu anashuka mpaka kwenye mbingu ya dunia kila usiku na ataweka unyayo wake motoni nao utajaa na kwamba ataonesha mguu wake ili waumini wamtambue na kwamba anacheka na kushangaa, na mengineyo miongoni mwa riwaya ambazo zinamfanya Mwenyezi Mungu kuwa ni mwili wenye harakati na mabadiliko, ukiwa na mikono miwili, miguu miwili na ana vidole vitano, ameziweka mbingu kwenye kidole cha kwanza, ardhi kwenye kidole cha pili, mti kwenye kidole cha tatu, cha nne maji na udongo na kwenye kidole cha tano ameweka viumbe vingine vilivyobakia na anayo nyumba anayoishi ndani yake na Muhammad ataomba ruhusa kuingia humo mara tatu. Ametukuka Mwenyezi Mungu kwa Utukufu mkubwa kutokana na hayo (hayuko hivyo) utakasifu ni wa Mola wako Mola aliyetukuka kutokana na sifa wanazomzifu. Jawabu la swala hili liko kwa Maimamu waongofu na Taa ziondoshazo kiza nalo ni kumtakasa kikamilifu Mwenyezi Mungu Mtukufu kutokufanana na umbile na sura na mwili na kumshabihisha na kumuwekea mpaka.
Imam Ali
anasema: "Sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu ambaye wasemaji hawafikii upeo wa sifa zake, wala wenye kuhesabu hawawezi kudhibiti neema zake, wala hawawezi kutekeleza vilivyo haki yake wenye kujitahidi, wala haziwezi kumfikia fikra zozote, na haziwezi kumtambua vilivyo akili mahiri, Mwenyezi Mungu ambaye sifa zake hazina mpaka, wala hasifiki kwa sifa za vilivyopo, na hana wakati unaohesabika wala muda wenye kikomo... Basi mwenye kumsifu Mwenyezi Mungu Mtukufu atakuwa kamfanyia mwenzi na Mwenye kumfanyia mwenzi, kamfanyia wa pili, na Mwenye kumfanyia wa pili kamgawa mafungu, na amgawaye mafungu basi hamjui Mwenyezi Mungu. Asiyemjua hakika kamuashiria na mwenye kumuashiria kamjaalia mipaka, na mwenye kumjaalia mipaka amemuhesabu, na atakaesema yumo ndani ya kitu fulani, basi kamuambatanisha, na atakayesema yuko juu ya nini kamtoa. Yupo siyo kwa kuzuka, yupo siyo kutokana na kutokuwepo, yu pamoja na kila kitu si kwa wenza naye si kila kitu siyo kwa kumfanya si kitu, mtendaji siyo kwa harakati na vifaa, anaona wakati hakuna kinachomuona miongoni mwa viumbe wake
". Kwa hakika nimeyaelekeza macho ya wachunguzi miongoni mwa vijana wenye taaluma kwenye hazina alizoziacha Imam Ali
, zilizokusanywa ndani ya Nah-Jul-Balaghah ambacho ni kitabu madhubuti hakitanguliwi ila na Qur'an, na ni kitabu ambacho kwa bahati mbaya hakifahamiki kwa watu wengi kutokana na kampeni, vitisho na vizuizi vilivyowekwa na watawala wa Banu Umayyah na Banu Abbas dhidi ya kila kile ambacho kina uhusiano na Ali ibn Abitalib. Sitakuwa nimezidisha nitakaposema kwamba ndani ya Nahjul-Balaghah kuna elimu nyingi na mafunzo mengi ambayo watu (wataendelea) kuyahitaji siku zote, na ndani ya Nahjul-Balaghah kuna elimu ya akhlaq, elimu ya jamii, uchumi na miongozo madhubuti katika elimu za dunia na teknolojia na zaidi ya hapo kuna falsafa, tabia, siasa na hekima.
Kwa hakika nimeyathibitisha hayo mimi mwenye we ndani ya Insha niliyotoa kwenye Chuo Kikuu cha Sirbun, Insha ambayo ilijadiliwa juu ya maudhui nne nilizozichagua kutoka ndani ya Nahjul-Balaghah na kutokana na maudhui hizo nilipata shahada ya "Udaktari". Basi lau Waislamu wangeifuata Nahjul-Balaghah kikamilifu wakayachambua mas-ala yote yaliyomo na kila nadharia, bila shaka (Nahjul-Balaghah) ni bahari yenye kina kirefu, kwani kila aizamiapo mtafiti hutoa ndani yake Lulu na Marjan.
Ufafanuzi
: Iko tofauti iliyo wazi kati ya Aqida mbili: Aqida ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa ambayo inamfanya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa na mwili, umbo na sura kama kwamba yeye ni mtu anayetembea na anashuka (kutoka juu) na mwili wake unahifadhiwa na anayo nyumba (anamoishi) na mengineyo miongoni mwa mambo yanayochukiza. Mwenyezi Mungu ametakasika mno, yu mbali na mambo hayo. Aqida ya Mashia ambao wanamtakasa Mwenyezi Mungu na kutomfananisha na kumfanyia mwili, na wanasema kuwa haiwezekani kabisa kumuona (Mwenyezi Mungu) hapa duniani wala akhera. Nami binafsi naamini kwamba riwaya wanazotolea hoja Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa zote ni uchafuzi wa Myahudi katika zama za Masahaba, kwani Kaabul-Ahbar Myahudi ambaye alisilimu katika zama za Omar bin Al-Khatab ndiye aliyeingiza itikadi hizi ambazo Wayahudi wanaziamini (na alifanikiwa kwa) kupitia njia za baadhi ya Masahaba wepesi (wa kuhadaika) kama vile Abu-Hurairah na Wahab ibn Munabbah. Basi ziko riwaya nyingi za aina hiyo zilizopokelewa ndani ya Bukhari na Muslim kutoka kwa Abu-Hurairah, na imekwishatangulia katika uchunguzi uliopita namna gani Abu-Hurairah asivyotenganisha hadithi za Mtume na hadithi za Myahudi Kaabul-Ahbar kiasi kwamba Umar bin Khatab alimpiga na kumzuwia asisiimulie riwaya kuhusu suala la Mwenyezi Mungu kuumba mbingu na ardhi katika siku saba. Na madam Ahlis-Sunnah Wal-Jamaa wanaziamini Sahih Bukhari na Muslim na kuvifanya kuwa ni vitabu sahihi mno, na maadam hawa wanamtegemea Abu-Hurairah kiasi kwamba amekuwa ndiyo tegemeo la wanachuoni wa hadithi (wa Kisunni) na yeye (Abu-Hurairah) kwa Masunni ndiyo mpokezi wa Uislamu (katika hadithi). Basi kwa hali kama hii haiwezekani kwa Masunni kubadili itikadi yao isipokuwa kama watajikomboa kutokana na kufuata kiupofu, na wakarejea kwa Maimamu waongofu (ambao) ni kizazi cha Mtume nao ndio mlango wa mji wa Elimu ambao huendewa. Wito huu hauwahusu Wazee na Masheikh, bali kijana mwenye taaluma miongoni mwa Masunni, pia ni miongoni mwa wajibu alionao (kijana) ni kujinasua kutokana na kufuata kiupofu na afuate hoja na dalili.
Swali la Pili
: Uadilifu wa Mwenyezi Mungu na kutenza nguvu Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema ndani ya Kitabu chake kitukufu:
وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ﴿٢٩﴾
"Na waambie, huu ni ukweli utokao kwa Mola wenu, basi anayetaka naamini na anayetaka naakufuru" (Qur'an, 18:29).
لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ﴿٢٥٦﴾
"Hakuna kulazimishwa katika dini, uongofu umekwisha bainika kutokana na upotofu" (Qur'an 2:256).
فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ ﴿٧﴾ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ ﴿٨﴾
"Na anayefanya wema (hata) kwa kiasi cha chembe ndogo ataona malipo yake, na anayefanya uovu (hata) kwa kiasi cha chembe ndogo ataona malipo yake" (Qur'an 99:7-8).
لَّسْتَ عَلَيْهِم بِمُصَيْطِرٍ ﴿٢٢﴾
"Bila shaka wewe ni mkumbushaji tu, wewe siyo mwenye kuwatenza Nguvu" (Qur'an 88:22).
Basi vipi mnakubali hadithi zilizopokelewa katika Sahih Bukhari na Sahih Muslim kwamba eti Mwenyezi Mungu amewakadiria waja wake matendo yao kabla hajawaumba? Bukhari ameeleza katika Sahih yake amesema: "Walijadiliana Adam na Musa
, Musa akamwambia Adam, Ewe Adam wewe ni baba yetu umetuingiza makosani na umetutoa peponi. Adam akamwambia Musa, Ewe Musa Mwenyezi Mungu amekuteua na akakuandikia (mambo yako) kwa mkono wake, Je, wanilaumu kwa jambo alilonikadiria Mwenyezi Mungu kabla hajaniumba kwa miaka arobaini? Basi Adam akamhoji Musa mara tatu."
Kama ambavyo Muslim amepokea katika Sahihi yake amesema: "Hakika mmoja wenu hukusanywa umbile lake tumboni mwa mama yake kwa siku arobaini kisha katika muda huo anakuwa pande la damu, katika muda kama huo (tena) anakuwa pande la nyama, na katika muda kama huo hutumwa Malaika kupulizia ndani yake roho na huamrishwa mambo manne: Kuandika rizqi yake, muda wake, kazi yake na kuwa ni mwema au muovu, basi naapa kwa ambaye hapana Mola asiyekuwa yeye, hakika mmoja wenu atatenda matendo ya watu wa peponi mpaka pasiwe baina yake na pepo ila dhiraa moja, basi yatamtangulia maandiko (aliyoandikiwa) atatenda tendo la watu wa motoni aingie motoni, na kwamba mmoja wenu atatenda matendo ya watu wa motoni mpaka pasiwe baina yake na moto ila dhiraa moja, basi yatamtangulia maandiko (aliyoandikiwa) atatenda tendo la watu wa peponi aingie peponi.
Ni kama alivyopokea Muslim katika Sahih yake kutoka kwa Bibi Aisha mama wa waumini amesema, "Mtume wa Mwenyezi Mungu aliitwa kwenye jeneza la mtoto mdogo miongoni mwa Ansar, nikasema, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu amefaulu huyu ni ndege miongoni mwa ndege wa peponi hakufanya uovu na wala hakuufikia, Mtume akasema, au kinyume cha hivyo ewe Aisha, hakika Mwenyezi Mungu aliumbia pepo watu wake na akawaumba watu kwa ajili ya pepo hali wakiwa migongoni mwa baba zao, na ameuumbia moto watu wake na akawaumba watu kwa ajili ya moto hali wakiwa migongoni kwa baba zao." Bukhari amepokea katika Sahih yake kwamba, mtu mmoja alisema "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Je, wanafahamika watu wa Peponi kutokana na watu wa Motoni? Mtume akasema ndiyo, (yule mtu) akasema, basi ni kwa nini wanafanya amali? Akasema, kila mmoja anatenda kwa lile aliloumbiwa au kwa lile analorahisishiwa."
Umetakasika Mola wetu, na sifa njema ni zako, utukufu ni wako na umeepukana mno na dhulma hii, basi vipi tuzisadiki hadithi hizi zinazopingana na kitabu chako kitukufu ambacho ndani yake umesema na kauli yako ni ya kweli.?
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ النَّاسَ شَيْئًا وَلَـٰكِنَّ النَّاسَ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٤٤﴾
"Bila shaka Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu chochote lakini watu wanajidhulumu nafsi zao" (Qur'an 10:44).
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ﴿٤٠﴾
"Hakika Mwenyezi Mungu hadhulumu (malipo japo) yenye uzito wa chembe ndogo (Qur'an 4:40).
"Na Mola wako hamdhulumu yeyote
" (Qur'an 18:49).
وَمَا ظَلَمَهُمُ اللَّـهُ وَلَـٰكِنْ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿١١٧﴾
"Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu wao lakini (wao) wazidhulumu nafsi zao" (Qur'an, 3:117).
فَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٧٠﴾
"Basi Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwadhulumu lakini wao wamekuwa ni wenye kuzidhulumu nafsi zao" (Qur'an 9:70, 29:40, 30:9).
وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا هُمُ الظَّالِمِينَ ﴿٧٦﴾
"Hatukuwadhulumu lakini wao walikuwa wakizidhulumu nafsi zao" (Qur'an, 43:76).
ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿٥١﴾
"Hayo (ni malipo) kwa yale yaliyotangulizwa na mikono yake na kwamba Mwenyezi Mungu hakuwa ni Mwenye kuwadhulumu waja." (Qur'an, 8:51).
مَّنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿٤٦﴾
"Yeyote mwenye kufanya wema basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na yeyote (atayefanya) uovu basi ni juu yake na Mola wako si mwenye kuwadhulumu waja" (Qur'an, 41:46).
Na kama alivyosema ndani ya hadithi takatifu, "Enyi waja wangu. mimi nimeiharamisha dhulma juu ya nafsi yangu mwenyewe na nikaifanya kuwa ni haramu kati yenu basi musidhulumiane". Itakuwaje basi Muislamu aliyemuamini Mwenyezi Mungu na uadilifu wake na huruma yake asadiki kwamba Mwenyezi Mungu amewaumba viumbe na akawaamulia baadhi yao (wapate) Pepo na wengine Moto kwa kutaka kwake yeye Mwenyezi Mungu, na akawakadiria matendo yao ikawa kila mmoja amefanyiwa wepesi (kutenda) lile aliloumbiwa kama zilivyo riwaya hizi zinazopinga Qur'an Tukufu na asili ya maumbile ambayo Mwenyezi Mungu amewaumbia watu, na (zinapingana na) akili na ukweli na nafasi ya haki za mwanaadamu! Vipi tutaiamini Dini hii ambayo inaviza akili na kwamba mtu huyu ni kinyago anayeendeshwa na mikono yenye uwezo namna inavyotaka, ili hatimaye imtupe ndani ya tanuru (la moto) - itikadi hii ndiyo ile ambayo inazuia akili ya mtu kuvumbua, kufanya maendeleo na kushindana, mambo ambayo huleta maajabu. (Itikadi hii inamviza) mtu abakie amedumaa mwenye kuridhika katika hali aliyomo na alichonacho kwa madai kwamba anawepesishiwa kwa yale aliyoumbiwa.
Vipi tutayakubali mapokezi haya ambayo yanagongana na akili iliyosalimika na yanatupatia picha kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ni muvimba mwenye kugandamiza na amewaumba waja wake madhaifu kisha awatupe motoni si kwa lolote isipokuwa kwa kuwa yeye anafanya akitakacho! Basi je wenye akili watamuita Mungu huyu kuwa ni mwenye hekima au mwenye huruma au muadilifu? Itakuwaje kama tutazungumza na watu wataalamu na wenye elimu miongoni mwa wasio Waislamu, kisha wakafahamu kwamba Mola wetu anasifa hizi, na kwamba dini yetu imewahukumu watu kabla ya kuzaliwa kwao kuwa ni waovu, basi Je, wataukubali Uislamu na wataingia katika dini ya Mwenyezi Mungu kwa wingi? Ewe Mola umetakasika, bila shaka hizi ni kauli za uongo zilizopandikizwa na Banu Umayyah na wakazisambaza kwa haja zao, na mchunguzi yeyote anafahamu siri ya hayo, kwani ni uzushi mtupu unaopingana na maneno yako, na haiwezekani kwa Mtume wako kukuzulia mambo yanayopingana na ufunuo wako ambao ulimfungulia, hasa kwa kuwa imethibiti kwamba Mtume(s.a.w.w)
amesema:
"Itakapokufikieni hadithi itokayo kwangu, ilinganisheni na kitabu cha Mwenyezi Mungu, ikilingana na kitabu hicho ichukuweni na ikienda kinyume na kitabu cha Mwenyezi Mungu ipigeni ukutani (itupeni haifai)
".
Hadithi zote hizi na nyingine nyingi mfano wa hizi zinapinga Qur'an na zinapingana na akili, basi na zitupwe wala zisishughulikiwe japokuwa zimepokewa na Bukhari na Muslim kwani wawili hawa hawakuwa wamehifadhika kutokana na makosa. Inatutosheleza dalili moja tu kuyapinga madai haya maovu, nayo ni kutumwa kwa Manabii na Mitume kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuja kwa viumbe wake, na kwa muda wote wa historia, ya wanaadamu (Mitume walikuja) kurekebisha maovu ya waja (wa Mwenyezi Mungu) na kuwabainishia njia iliyonyooka na wawafundishe kitabu, hekima na wawabashirie pepo wakiwa wema na wawaonye kuwa, kuna adhabu ya Mwenyezi Mungu motoni kama watakuwa waovu.
Miongoni mwa uadilifu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na huruma yake kwa viumbe wake ni kwamba, hatawaadhibu isipokuwa wale aliowapelekea Mtume na akawasimamishia hoja, anasema Mwenyezi Mungu:
مَّنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ وَمَن ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا ﴿١٥﴾
"Yeyote anayeongoka, bila shaka anaongoka kwa manufaa ya nafsi yake, na anayepotea bila shaka anapotea kwa hasara ya nafsi yake, wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine, basi hatukuwa wenye kuwaadhibu (viumbe) mpaka tupeleke Mtume" (Qur'an, 17:15).
Basi kama riwaya hizi ambazo wameziandika kina Bukhari na Muslim zinazosema kwamba Mwenyezi Mungu amewaandikia waja wake matendo yao kabla hajawaumba na akawaamulia baadhi yao pepo na wengine moto kama tulivyoeleza hapo kabla, na kama ambavyo Ahlis-Sunnah Wal-Jamaa wanavyoamini, mimi nasema, kama riwaya hizo ni sahihi, basi bila shaka kutumwa kwa Mitume na kuteremshwa kwa Vitabu kunakuwa ni aina ya upuuzi!! Na Mwenyezi Mungu ameepukana mno kufanya mambo ya upuuzi, na hawa waaminio hivi hawakumtukuza Mwenyezi Mungu (anavyostahiki kutukuzwa). Kwa hiyo haifai kabisa kwetu sisi kusema maneno kama haya. Ewe Mola wetu umetakasika na huu (usemwao juu yako) ni uzushi mkubwa.
تِلْكَ آيَاتُ اللَّـهِ نَتْلُوهَا عَلَيْكَ بِالْحَقِّ وَمَا اللَّـهُ يُرِيدُ ظُلْمًا لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٨﴾
"Hizo ni aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki, na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu walimwengu." (Qur'an, 3:108).
Amma jawabu la utata huu unaohusu kumtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu kutokana na dhulma na upuuzi, linapatikana kutoka kwa Maimamu waongofu ambao ni taa ziondoazo kiza, na wao ndiyo mwangaza wa Ummah.
Hebu basi na tumsikilize mlango wa mji wa elimu Amiri wa waumini Ali ibn Abi Talib
, anawafafanulia watu itikadi hii ambayo imeendelea kutokutambulika kwa baadhi ya Waislamu ambao wameuacha mlango huo yeye anasema alipoulizwa na mmoja wa wafuasi wake, "Je, kwenda kwetu Shamu kulikuwa kunatokana na Qadhaa (maamuzi) ya Mwenyezi Mungu na Qadar yake?" Anajibu Imam Ali
:
"Ole wako, huenda wewe umedhania kuwa Qadhaa ya kulazimisha na Qadar yenye kuwajibishwa, na lau ingekuwa hivyo thawabu na adhabu vingebatilika, ahadi na maonyo vingetenguka, hakika Mwenyezi Mungu amewaamuru waja wake kwa kuwahiyarisha na akawakataza kwa kuwatahadharisha. Akawalazimisha (kufanya mambo) mepesi na wala hakuwalazimisha (mambo) mazito. Akatoa (malipo) mengi kwa (matendo) kidogo na wala hawakumuasi hali ya kuwa ni mwenye kushindwa na hawakumtii hali ya kuwa ni mwenye kulazimisha. Wala hakuwatuma Mitume kwa ajili ya mchezo tu na hakuteremsha vitabu kwa waja ili iwe ni upuuzi, wala hakuumba mbingu na ardhi na vilivyomo bure bure tu. "Hizo ni fikra za wale waliokufuru basi ole wao waliokufuru kutokana na adhabu ya moto.
" Amesema kweli Imam
basi, ole wao kutokana na adhabu kali ya Mwenyezi Mungu wale wanaomnasibishia Mwenyezi Mungu kufanya upuuzi na dhulma.
Ni vizuri kusema na haki husemwa, ya kwamba Ahlus-Sunna Wal-Jamaa wanamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumuepusha na upuuzi na dhulma, basi iwapo utamuuliza mmoja wao huenda kamwe asimnasibishe Mwenyezi Mungu na dhulma kwa utukufu wake, lakini huenda yeye mwenyewe akajikuta anaona vibaya kuzikataa hadithi zilizotolewa na Bukhari na Muslim na wakati huo huo akaziamini kwamba ni sahihi, kwa ajili hiyo utamuona wakati unamjadili kwa mantiki inayoingia akilini atadai kwamba hiyo kwa Mwenyezi Mungu siyo dhulma kwani yeye ni Muumba, na Muumba anawafanyia viumbe wake vile atakavyo, kwani yeye haulizwi kuhusu ayatendayo nao viumbe wataulizwa. Wakati utakapomuuliza kwa kusema. Ni vipi Mwenyezi Mungu anamhukumu kiumbe kuingia motoni kabla ya kumuumba, eti kwa kuwa amemuandikia uovu na mwingine amemhukumia pepo kabla ya kumuumba kwa kuwa kamuandikia wema? Basi je, hiyo siyo dhulma kwa wawili hao kwa sababu yule atakayeingia peponi haingii humo kwa ajili ya matendo yake bali Mwenyezi Mungu kamchagulia, na vile vile atakayeingia motoni haingii humo kwa makosa aliyoyatenda bali Mwenyezi Mungu amemkadiria. Je, katika hali hiyo siyo dhulma na ni jambo linalopingana na Qur'ani? Jawabu lake atakuambia; "Hiyo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu anafanya atakavyo." Huwezi kufahamu msimamo wake unaopingana; na hii bila shaka ni kwa sababu anampa Bukhari na Muslim daraja ya usahihi kama Qur'an, na anasema kuwa vitabu sahihi baada ya kitabu cha Mwenyezi Mungu ni Bukhari na Muslim.
Ndani ya Bukhari na Muslim kuna maajabu na misiba ambayo Waislamu wamekumbwa na mtihani huo. Hakika Banu Umayyah na baada yao Banu Abbas wamefaulu sana kueneza uzushi wao na itikadi zao ambazo zinaafikiana na siasa zao mbaya, na athari zao zimebakia mpaka leo hii, kwani Wailsamu wanazizingatia kuwa ni urithi bora kwa kuwa (wanaona) ni mkusanyiko wa hadithi sahihi za Mtume kama wanavyodai. Lau Waislamu wangefahamu kiwango ambacho (Banu Ummayah na Banu Abbas) walivyomzulia Mtume(s.a.w.w)
kwa ajili ya kutimiza malengo yao ya kisiasa, basi wasingezisadiki kabisa hadithi hizo na hasa zile zinazopingana na kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Na kwa kuwa Mwenyezi Mungu amechukua jukumu la kuihifadhi Qur'an Tukufu, na Masahaba walikuwa wameihifadhi na wakawa wanaiaridhi kwa Mtume(s.a.w.w)
ndiyo maana (Banu Umayyah na Banu Abbas) hawakuweza kuigeuza wala kuibadilisha, na kwa hali hiyo basi wakaigeukia Sunna takatifu wakaweka waliyoyataka kwa ajili ya yule wamtakaye, khususan kutokana na uadui wao dhidi ya watu wa nyumba ya Mtume(s.a.w.w)
ambao ndiyo walinzi wa Qur'an na Sunna. Walizua hadithi kwa kila tukio wakainasibisha kwa Mtume(s.a.w.w)
na wakairemba kwa Waislamu (na kuwambia) hadithi hizi ni sahihi kuliko nyinginezo, na watu wakazikubali kwa nia njema hali wakipokezana hadithi hizo kwa kurithiana kizazi baada ya kizazi tena kwa uadilifu kabisa. Mimi nasema kwamba Mashia nao ni mateka wa uharibifu na uzushi (uliofanywa) katika hadithi nyingi ambazo zinanasibishwa kwa Mtume(s.a.w.w)
au kwa mmoja wa Maimamu watukufu
.
Uingizaji huo wa hadithi na ufichaji wa ukweli huo hawajasalimika nao Mashia wala Masunni muda wote wa historia (ya Uislamu), lakini Shia wanajipambanua kutokana na Ah'li Sunna Wal-Jamaa kwa vitu vitatu ambavyo vimewapambanuwa Mashia kutokana na makundi mengine ya Kiislamu kwani itikadi yao imejitokeza kuwa salama na yenye kuafikiana na Qur'an, Sunna na Akili. Vitu hivyo vitatu ni hivi vifuatavyo:
Jambo la kwanza
: Mashia wametoshelezwa na (uongozi wa) watu wa nyumba ya Mtume(s.a.w.w)
, hawamtangulizi yeyote juu yao, na kila mmoja wetu anafahamu ni kina nani hawa watu wa nyumba ya Mtume ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na amewatakasa mno.Jambo la Pili
: Idadi ya Maimamu wa nyumba ya Mtume ambao ni kumi na wawili, uhai wao na athari zao viliendelea kwa muda wote wa karne tatu na wameafikiana wao kwa wao katika kila hukumu na hadithi, na hawakutofautiana kwa chochote, jambo ambalo liliwafanya wafuasi wao kuwa ni wajuzi katika kila nyanja za elimu na maarifa kwa uwazi bila ya kupingana katika itikadi na mengineyo.
Jambo la Tatu
: Kukubali na kukiri kwa Mashia kwamba vitabu (vya hadithi) walivyonavyo vinaweza kuwa na mambo yaliyo sawa na mengine yenye makosa , na hawana kitabu sahihi isipokuwa Qur'an ambayo haitofikiwa na batili mbele wala nyuma yake. Basi inakutosha kufahamu kwa mfano kwamba, kitabu kikubwa (cha hadithi) kwao ni Usulul-Kafi wao wanasema kwamba humo kuna maelfu ya hadithi za uongo, na kwa hiyo basi utawakuta wanachuoni wao na Mujtahidina wao ni wenye bidii kutafiti na kuchambua (hadithi) hawachukui katika kitabu hicho ila hadithi iliyothibiti kwa Matni na Sanad na ile isiyopingana na Qur'an wala akili. Ama kwa upande wa Ahlul-Sunna Wal-Jamaa wao wamejilazimisha (kufuata) vitabu walivyoviita kuwa ni Sihah Sita kwa kuzingatia kwamba kila kilichomo humo ni sahihi na wengi wao (Masunni) wanarithishana rai hii bila ya utafiti wala uchunguzi. Hapana shaka kwamba, nyingi kati ya hadithi hizi ambazo zimepokelewa ndani ya vitabu hivi hazisimami kwenye dalili za kielimu na ndani yake mna kufru ya wazi wazi na mambo yanayopingana na Qur'an na mwenendo wa Mtume na matendo yake na yanaitia aibu heshima ya Mtume. Kwa mtu mwenye kutafiti inamtosha asome kitabu cha Sheikh wa Kimisri aitwaye Mahmud Abur-Rayyah kiitwacho, Adh-wau Alas-sunnatil Muhmmadiyyah ili afahamu kikoje kiwango cha Sihahi hizo sita. Al-Hamdulillah leo wapo vijana wengi wanaochunguza na wamejikomboa kutokana na minyororo hiyo, wanatofautisha kati ya (hadithi) dhaifu na yenye nguvu. Kwa hali hiyo basi hata Masheikh wenye kung'ang'ania hizo Sihahi sasa hivi wengi miongoni mwao wanazipinga Sihahi hizo, siyo kwa sababu wamekuta kuwa baadhi ya hadithi ni dhaifu, bali zimekutwa hoja wazisemazo Mashia zinazohusu hukumu za kifiqhi au kuhusu akida za mambo ya ghaibu, basi hapana hukumu au itikadi waisemayo Mashia isipokuwa utaikuta imethibiti ndani ya moja ya Sihahi sita za Masunni.
Katika hali ya majadiliano, mmoja wa baadhi ya wenye ung'ang'anizi aliniambia; "Madamu ninyi (Mashia) mnaitakidi kwamba hadithi za Bukhari siyo Sahihi, basi ni kwa nini mwazitolea hoja dhidi yetu?" Nilijibu, "Siyo kila kilichomo ndani ya Bukhari kinapingwa, ukweli ni ukweli tu na batili ni batili tu nasi tunawajibika kuchekecha ukweli na kuuchuja." Akasema, "Je, wewe unayo darubini maalum ambayo kwayo unafahamu (hadithi) sahihi kutokana na ile ya uongo?" Nikasema, "Mimi sina zaidi kuliko uliyonayo wewe, lakini zile ambazo wameafikiana Masunni na Mashia ndiyo sahihi kwa sababu usahihi wake umethibiti kwa pande zote mbili. Sisi tunawawajibishia kama walivyojiwajibishia nafsi zao, na zile walizotofautiana hata kama zitasihi kwa mmoja wao basi haulazimishwi upande wa pili kuzikubali kama ambavyo siyo lazima kwa mtafiti wa upande mmoja kuzikubali na kuzitolea hoja kama ambavyo mtafiti asiyefungamana na upande wowote halazimiki kuzikubali na kuzitolea ushahidi. Mimi nakupigia mfano mmoja unaohusu hali hiyo ili kusiwe na tatizo katika maudhui hii na ili usirejewe ukosoaji kama huo kwa njia nyingine tofauti". Mashia wanadai kwamba Mtume(s.a.w.w)
alimuweka Ali kuwa Khalifa wa Waislamu huko kwenye bonde la Khum siku ya tarehe kumi na nane Mwezi wa Mfunguo Tatu baada ya Hijja yake ya mwisho na alisema Mtume kuhusu mnasaba huo, "Yeyote ambaye mimi nilikuwa mtawala wake basi huyu hapa Ali ni mtawala wake, Ewe Mwenyezi Mungu msaidie atakayemtawalisha (Ali) na umpige vita atakayempiga vita (Ali)." Tukio na hadithi hii wameinakili wengi miongoni mwa wanachuoni wa Kisunni katika Sihahi zao na Musnad zao na vitabu vyao vya tarekhe, basi hapo inawezekana kwa Mashia kutoa hoja dhidi ya Masunni.
Masunni wanadai kwamba Mtume(s.a.w.w)
alimbainisha Abubakar awasalishe watu wakati Mtume akiwa anaumwa ugonjwa uliopelekea mauti yake na akasema: "Mwenyezi Mungu na Mtume wake na waumini hawamkubali mwingine isipokuwa Abubakar." Tukio hili na hadithi hii haimo ndani ya vitabu vya Kishia, bali wao wanapokea (hadithi isemayo) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alituma ujumbe aitwe Ali
Aisha naye akatuma ujumbe aitwe Baba yake, na Mtume alipotambua hilo alimwambia bibi Aisha, "Hakika ninyi ni kama yule mwanamke aliyemtamani Yusuf
kisha Mtume alitoka ili akawasalishe watu na akamuondosha Abubakr. Basi haiwezekani na wala siyo uadilifu kwa Masunni kutoa hoja dhidi ya Mashia kwa tukio au hadithi waliyopwekeka nayo hasa hasa iwapo riwaya zenyewe zinapingwa na ukweli na historia, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu alimteua Abubakr awe katika jeshi la Usama chini ya uongozi wa Usama, na inafahamika kwamba kiongozi wa jeshi katika jeshi ndiye anakuwa Imamu wa Sala. Imethibiti kihistoria kwamba Abubakr hakuwepo Madina wakati wa kifo cha Mtume(s.a.w.w)
bali alikuwa Sunhi akijiandaa kutoka na kiongozi wake Usama ibn Zaid ambaye alikuwa na umri wa miaka kumi na saba. Basi vipi katika hali kama hii itawezekana kwetu sisi kusadiki kwamba Mtume(s.a.w.w)
alimchagua kuongoza Sala?
Itawezekana tu iwapo tutaisadiki kauli ya Omar ibn Khatab kwamba, Mtume anaweweseka hajui atendalo na alisemalo. Na jambo hili (la Mtume kuweweseka) halina nafasi kabisa kwa Mtume, haliwezekani na wala Mashia hawalisemi kabisa. Hivyo basi kwa mtafiti hapa na amche Mwenyezi Mungu katika utafiti wake wala yasimzuge mapenzi akaiacha haki akafuata mapenzi akajikuta amepotea njia ya Mwenyezi Mungu, bali wajibu wake ni kufuata haki japo haki hiyo anayo mwingine. Na (anawajibika) kuikomboa nafsi yake isiwe yenye kuzolewa na matamanio na ubinafsi, ili awe miongoni mwa wale aliowasifu Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kauli yake aliposema
الَّذِينَ يَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَيَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ هَدَاهُمُ اللَّـهُ وَأُولَـٰئِكَ هُمْ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿١٨﴾
"Wabashirie (wema) waja wangu ambao husikiliza maneno kisha wakafuata yaliyo mazuri hao ndiyo ambao aliowaongoa Mwenyezi Mungu na hao ndiyo wenye akili" (Qur'ani 39:18).
Kwa hiyo haiingii akilini Mayahudi watakaposema "Haki iko kwetu". Na Wakristo nao waseme: "Haki iko kwetu'", Waislamu nao waseme "Haki tunayo sisi" hali ya kuwa wote hawa wanahitilafiana katika itikadi na sheria.
Basi hapana budi kuwa yule anayetafiti achunguze kauli ya dini zote na azilinganishe mpaka haki imbainikie. Na haingii akilini vile vile Masunni waseme kwamba; "Haki iko pamoja nao", na Mashia nao waseme kwamba "Haki iko kwao peke yao". Hali ya kuwa (wawili hawa) wanahitilafiana katika baadhi ya mafundisho na hukumu. Haki ni moja tu haigawiki!! Kwa hiyo hapana budi kwa mtu anayetafiti afanye bidii na achunguze vile vile kauli za pande mbili hizi na azilinganishe na aipe akili yake uamuzi mpaka ukweli umbainikie, na huo ndiyo mwito wa Mwenyezi Mungu kwa kila kikundi kinachodai ukweli pindi aliposema: "Waambie leteni hoja zenu ikiwa ninyi ni wakweli
". (Qur'an 2:111).
Wingi siyo dalili ya kuwa kwenye haki, bali kinyume chake ndiyo sahihi, Mwenyezi Mungu anasema:
وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ ﴿١١٦﴾
"Na kama utawatii wengi wa (hawa) waliomo katika nchi watakupoteza kutoka kwenye njia ya Mwenyezi Mungu" (Qur'ani 6:116)
na Amesema tena
وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ ﴿١٠٣﴾
"Na watu wengi hawatakuwa wenye kuamini hata kama utajitahidi vipi" (Qur'ani 12:103).
(Hali hii) ni kama ambavyo maendeleo ya kielimu na teknolojia na uchumi siyo dalili ya kwamba watu wa magharibi wako kwenye haki na wale wa Mashariki wako kwenye batili. Mwenyezi Mungu anasema:
فَلَا تُعْجِبْكَ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُمْ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُعَذِّبَهُم بِهَا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَتَزْهَقَ أَنفُسُهُمْ وَهُمْ كَافِرُونَ ﴿٥٥﴾
"Zisikufitini mali zao wala watoto wao hakika Mwenyezi Mungu anataka awaadhibu kwa hizo (mali) katika maisha ya dunia na zitoke roho zao hali ya kuwa ni makafiri. (Qur'ani 9:55).
Kauli ya Ahlud-dhikri juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Imam Ali
anasema: "Sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu ambaye anayajua mambo yaliyofichikana, na dalili zilizo wazi zimemtambulisha yeye.
Amefichikana kwa jicho la mwenye kuona, hapana jicho la asiyemuona linalo mkanusha, wala hakuna moyo wa aliyemthibitisha utakaomuona. Ametangulia kwa utukufu hapana cho chote kitukufu kuliko yeye na yu karibu mno. hakuna kilicho karibu kuliko yeye na utukufu wake haukumtenga mbali na viumbe wake na wala ukaribu wake haukuwalinganisha kwake katika daraja. Akili hazikupewa uwezo wa kutambua ukomo wa sifa zake, na wala hazikuzuiliwa ulazima wa kumfahamu. Basi ni yeye ambaye dalili za ulimwengu zinashuhudia juu ya kukiri kwa moyo wenye upinzani. Ametukuka mno Mwenyezi Mungu na yu mbali na yale wayasemayo wenye kumfananisha na wale wampingao." Anaendelea kusema: "Kila sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu ambaye hapana hali yo yote iliyomtangulia na hakuna asemwaye kuwa ni wa pekee ila ni yeye. Na kila mwenye nguvu asiye yeye ni dhalili, na kila mwenye uwezo asiye yeye basi yu dhaifu. Na kila Mfalme ambaye si yeye basi yuko chini ya Ufalme wake. Na kila mjuzi ambaye si yeye ni mwenye kujielimisha. Na kila mwenye kuweza ambaye si yeye huwezwa na hutenzwa nguvu. Na kila asikiaye ambaye si yeye hasikii sauti nyepesi na hufanywa kiziwi kwa sauti kubwa na hasikii kilicho mbali, na kila aonaye asiye yeye haoni aina ya vitu vilivyofichikana na haoni viwiliwili laini, na kila aliye dhahiri asiye yeye basi kafichikana. Kila aliyefichikana asiye yeye yu dhahiri. Hakuumba alivyo viumba ili kuimarisha Ufalme, wala si kwa kuchelea matokeo ya zama, wala kwa kutaka msaada wa mshirika mshauri, wala mshirika mwingi wa fahari wala mpinzani mwenye kuchukiza, lakini wote hao ni viumbe wenye kuchungwa na ni waja wanyonge. Hakuingia ndani ya vitu asemwe kuwa yumo humo, na hakuwa mbali akasemwa kajitenga navyo.
Hakikumshinda kiumbe alichokianzisha wala kuendesha alichokiumba, wala hakupatikana na kushindwa kwa vile alivyoviumba, na wala hakuingiwa na utatanishi ndani ya yale aliyoyahukumu na kukadiria bali ni maamuzi bora. Na elimu iliyothabiti na ni jambo lililosadikishwa, mwenye kutumainiwa pamoja na kuadhibu, na mwenye kuogopewa pamoja na neema. Hana mwanzo wala mwisho, yeye ndiyo wa mwanzo yupo na ni mwenye kubaki bila ya ukomo, zimeinama nyuso kwa ajili yake na midomo yampwekesha. Fikra haziwezi harakati na wala viungo na vifaa. Hasemwi alianza kuwa lini, hakuwekewa kikomo kwa tamko wala mpaka, yu dhahiri hasemwi anatokana na nini. Ametukuka Mwenyezi Mungu kutokana na mwenendo wa wanaomuwekea mipaka miongoni mwa sifa za kukadiria na ukomo wa eneo na asili ya makazi na kumfanyia makao, ukomo kwa waja wake umewekwa na umenasibishwa kwa wasiokuwa yeye. Hakuumba vitu kutokana na asili ya milele wala vyanzo vya milele, bali ameumba alivyoviumba akaviwekea ukomo wake. Na ameumba alivyoumba na akavifanyia maumbile mazuri hapana kinachoshindikana kwake wala haumnufaishi utiifu wa chochote, elimu yake kwa wafu waliokwishapita ni kama elimu yake kwa waliobakia hai na elimu yake kwa vilivyomo mbinguni juu ni kama elimu yake kwa vilivyomo ndani ya ardhi chini kabisa.