8
WAULIZE WANAOFAHAMU
MWISHO WA UCHAMBUZI
Kilicho muhimu katika uchambuzi wote uliotangulia japokuwa ni kwa mukhtasari ni kwamba, Ummul-Muuminina Aisha binti Abubakr mkewe Mtume(s.a.w.w)
hakuhesabiwa kuwa miongoni mwa Ahlul-bait ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na amewatakasa sana sana, na kuwahifadhi kutokana na kila dhambi na baada ya utakaso huo wakawani "Maasum". Na itoshe tu kwamba, bibi Aisha siku za mwisho wa uhai wake alizitumia kwa kilio, huzuni na majuto kwa kukumbuka matendo yake hayo, alikuwa akilia na huenda Mwenyezi Mungu Mtukufu atamsamehe makosa yake, kwani ni yeye peke yake ndiye ajuaye siri ya mpepeso wa macho na yaliyofichikana katika nyoyo za waja wake na ndiye ajuaye ukweli wa nia zao. Hakuna kinachofichikana kwa Mwenyezi Mungu ardhini wala mbinguni, wala mtu mwingine yeyote hataweza kuwahukumia pepo wala moto viumbe wa Mwenyezi Mungu, kwani kufanya hivyo ni kujilazimisha usiloliweza au usilolijuwa. Mwenyezi Mungu amesema:
لِّلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَإِن تُبْدُوا مَا فِي أَنفُسِكُمْ أَوْ تُخْفُوهُ يُحَاسِبْكُم بِهِ اللَّـهُ فَيَغْفِرُ لِمَن يَشَاءُ وَيُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٢٨٤﴾
"Vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ni vya Mwenyezi Mungu, na kama mtadhihirisha yaliyomo ndani ya nyoyo zenu au mtayaficha, Mwenyezi Mungu atakuhisabuni kwa hayo kisha amsamehe amtakaye (kwa kuwa katubia) na amuadhibu amtakaye (kwa kuwa hakutubia) na Mwenyezi Mungu ni mwenye uwezo juu ya kila kitu (Qur'an, 2:284).
Hivyo basi, kwa ajili hii si juu yetu sisi kumtakia radhi bibi Aisha wala kumlaani, lakini tunalazimika kutokumfuata wala kuyabariki matendo yake, na tutazungumza yote hayo wazi wazi ili ukweli ufahamike kwa watu, huenda wakaongoka kwenye njia ya haki. Imam Ali
amesema: "Msiwe watukanaji wala wenye kulaani, lakini semeni matendo yao yalikuwa kadhaa wakadhaa ili upatikane ushahidi wa kutosha. Kauli ya Ahlud-dhikr juu ya Ahlul-bait. Imam Amirul-Muuminina Ali
ambaye ni Bwana wa kizazi kitakatifu cha Mtume(s.a.w.w)
anasema: "Namuapa Mwenyezi Mungu, hakika mimi nafahamu vyema namna ya kufikisha ujumbe, kutimiza miadi, kukamilisha maneno na kwetu sisi watu wa nyumba ya Mtume ndiko kwenye milango ya hekima na mwangaza wa mambo.
Wako wapi wale wanaodai kwamba wao ndiyo waliobobea katika elimu kinyume chetu, ni waongo na ni dhulma dhidi yetu (kudai hivyo) kwani Mwenyezi Mungu ametutukuza sisi na akawatweza wao, akatupa sisi na wao akawanyima, na akatuingiza sisi na wao akawatoa, kwetu sisi ndiko huombwa uongofu na huondoshwa upofu, bila shaka Maimamu wanatokana na Maquraish na wamepandikizwa katika tumbo hili la Hashim, basi haufai Uimamu kwa mwingine asiyekuwa wao na wala haukubaliki utawala kutoka kwa asiyekuwa wao. Sisi ndiyo wenyewe na ndiyo tunaostahiki (uongozi) nasi ndiyo hazina na ndiyo milango (ya kuingilia), hayaingiwi majumba isipokuwa kwa kupitia milango yake, basi yeyote mwenye kuyaendea majumba bila kupitia milangoni mwake huyo huitwa mwizi." Kisha Imam Ali
anawataja Ahlul-bait anasema: "Ndani yao Ahlul Bayt ndimo ulimo utukufu wa Qur'an na wao ndiyo hazina ya wingi wa rehma, watamkapo hutamka kweli na wanaponyamaza siyo kwamba wameshindwa.
"
Wao ndiyo uhai wa elimu na ndiyo kifo cha ujinga, subira yao itakuelezeni upeo wa elimu yao, na kujizuwia kwao kutakuelezeni hekima ya mantiq waliyonayo. Hawaendi kinyume na haki wala hawahitilafiani katika haki, wao ndiyo nguzo za Uislamu na ndiyo matumaini ya amani, kwao wao haki imerudi kwenye asili yake na upotofu umeondoka mahala ulipokuwa na hoja zake nazo zimetoweka. Wameizingatia dini kwa mazingatio ya utambuzi na kuilinda na siyo kwa mazingatio ya kusikia na kuelezwa, kwani wapokezi wa elimu ni wengi lakini walinzi wake ni wachache.
Kizazi cha Mtume ndiyo bora ya vizazi, na ukoo wake ndiyo bora ya koo zote, na mti wake (nasaba) ni bora ya miti, umeota mahala patakatifu na ukachanua mahala pema, una matawi marefu na matunda yasiyoweza kufikiwa. Sisi ndiyo mti wa Utume na kituo cha Utume na mahala wapishanapo Malaika, nasi ni kituo cha elimu na ndiyo chemchem ya hekima, mwenye kutuangalia na kutupenda huyo anasubiri rehma, na adui yetu na mwenye kutuchukia anasubiri adhabu. Sisi ni watukufu, na kizazi chetu ni kizazi cha Manabii na kundi letu ni kundi la Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kundi la wenye kutupinga ni kundi la shetani na mwenye kutulinganisha sisi na adui yetu huyo si katika sisi.
Mnakwenda wapi na mnageukia wapi hali yakuwa dalili zimethibiti na ishara zipo wazi na minara imesimikwa, namna gani mnababaishwa? Vipi mnababaika hali yakuwa kizazi cha Mtume wenu kipo miongoni mwenu nao ndiyo walioshikamana na haki, na wao ndiyo viongozi wa dini na ndiyo ndimi za kweli, basi waheshimuni kwa heshima nzuri ya Qur'an na muwaendee kama awaendavyo ngamia mwenye kiu. Enyi watu yachukuweni hayo kutoka kwa Mtume wa mwisho aliposema: "Bila shaka anakufa mwenye kufa miongoni mwetu (watu wa nyumba ya Mtume) lakini yeye si maiti, na anachakaa mmoja wetu lakini si kwamba amechakaa, hivyo basi msiseme msiyoyajua, hapana shaka haki imo ndani ya yale muyapingayo. Mtakaseni ambaye ninyi hamna hoja yoyote dhidi yake nami ndiye huyo, je sikukitumia kati yenu kizito kikubwa na ninakuachieni kizito kidogo na nimeisimika kati yenu bendera ya imani?" Waangalieni watu wa nyumba ya Mtume wenu, mshikamane na kizazi chao na mfuate nyayo zao, hapana shaka hawatakutoeni nje ya haki na wala hawawezi kukurudisheni kwenye maangamizi, wakisimama nanyi simameni, wakinyanyuka nanyi nyanyukeni, wala msiwatangulie mtapotea na wala msiache kuwafuata mtaangamia.
Hizi ni kauli za Imam Ali
kuhusu kizazi kitukufu (cha watu wa nyumba ya Mtume) ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na amewatakasa mno. Na lau tutazifuatilia kauli za Maimamu miongoni mwa wanawe
ambao walikuwa wakizungumza mbele za watu kama vile (kauli za) Imam Hasan, Imam Husein, Zainul-Abidiin, Jaafar As-Sadiq na Imam Riza amani ya Mwenyezi Mungu iwashukie wote, tutawakuta wote wanasema maneno ya namna hiyo hiyo na wanawaongoza watu katika kila zama na kila mahali (wafuate) kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi cha Mtume(s.a.w.w)
kwa lengo la kuwaokoa kutokana na upotevu na kuwaingiza kwenye uongofu. Zaidi ya hapo ni kwamba, historia ndiyo shahidi bora juu ya kuhifadhika kwa watu wa nyumba ya Mtume, kwani haikusajili kwao isipokuwa elimu, uchamungu, utambuzi, ukarimu, upole na usamehevu na kila tendo alipendalo Mwenyezi Mungu na Mtume wake(s.a.w.w)
. Kama ambavyo historia ni shahidi bora vile vile kwamba, watu wema katika umma huu na wachamungu miongoni mwa watu wa Tasawaf, Masheikh wa Tariqa, Maimamu wa madhehebu na wanachuoni wema wa zamani na zama hizi wote hawa wanakiri juu ya ubora wa Maimamu wa kizazi cha Ali na kutangulia kwao kielimu, matendo na kuhusika kwao kwa Mtume
(s.a.w.w)
kiukoo na utukufu. Na kwa yote haya basi si vyema kwa Muislamu yeyote kuwachanganya Ahlul-Bait ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na amewatakasa sana, na ambao Mtume aliwaingiza ndani ya Kisaa, haiwezekani kabisa kuwachanganya na wake wa Mtume(s.a.w.w)
. Je, huoni kwamba Maimamu wa hadithi kama vile Muslim, Bukhari, Tirmidhi, Imam Ahmad, Nasai na wengineo wakati wanapothibitisha hadithi za ubora katika vitabu vyao na Sihah zao, huwa wanatenga mlango maalum wa ubora wa watu wa nyumba ya Mtume mbali na watu wengine miongoni mwa wake wa Mtume(s.a.w.w)
.
Kama ilivyokuja ndani ya Sahih Muslim kwenye mlango wa ubora wa Ali ibn Abi Talib aliposema: "Imepokewa kutoka kwa Zaid ibn Ar-Qam kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
amesema, Fahamuni ya kwamba hakika mimi nakuachieni vizito viwili, kimoja wapo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu, ni kamba ya Mwenyezi Mungu, yeyote mwenye kuifuata atakuwa kwenye uongofu na yeyote mwenye kuiacha atakuwa kwenye upotofu, kisha akasema, na watu wa nyumba yangu, nakukukumbusheni Mwenyezi Mungu kuhusu watu wa nyumba yangu. Sisi tukasema, je wakeze ni miongoni mwa watu wa nyumba yake? Akasema hapana, Namuapa Mwenyezi Mungu bila shaka mwanamke huwa pamoja na mume kwa kipindi fulani, kisha humtaliki na akarejea kwa baba yake na jamaa zake, watu wa nyumba yake Mtume ni wale wenye asili naye na ukoo wake ambao imeharamishwa kwao sadaka baada yake" Kama ulivyokuja ushahidi wa Bukhari na Muslim kwamba Aisha yeye anatokana na kizazi cha Abubakr na siyo katika kizazi cha Mtume(s.a.w.w)
(walipozungumzia) tukio la kushuka aya ya kutayammam. Basi wa nini ung'ang'anizi huu utokanao na baadhi wapinzani ambao wanatumia kila gharama kuihuisha fitina na kuugeuza ukweli ambao hauna shaka ndani yake? Wanawatukana Mashia si kwa lolote isipokuwa kwa sababu wao hawazikubali fadhila hizo za Ummul-Muuminina, lakini ni kwa nini hawavitukani vitabu vyao na wanachuoni wao waliowatoa wakeze Mtume kuwa siyo katika watu wa nyumba ya Mtume?.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾ يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾
"Enyi mlioamini muogopoeni Mwenyezi Mungu na mseme maneno ya kweli. Atakutengenezeeni vizuri matendo yenu na atakusameheni madhambi yenu, na yeyote anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake bila shaka amefanikiwa mafanikio makubwa." (Qur'an, 33:71).
MLANGO WA NNE
YANAYOWAHUSU MASAHABAKWA UJUMLA
ila shaka hukumu zote za kisheria na itikadi za Kiislamu zimetufikia kwa kupitia kwa Masahaba, kwa Waislamu wote duniani hapana yeyote anayedai kwamba, yeye anamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kupitia Qur'an na Sunna (moja kwa moja) isipokuwa Masahaba, wao ndio njia ya kumfikisha kwenye misingi hii miwili muhimu Na kwa kuwa Masahaba walihitilafiana baada ya Mtume(s.a.w.w)
, wakatengana, kutukanana na kulaaniana, wakapigana mpaka wakauwana wao kwa wao, basi kwa hali hii haiwezekani kwetu sisi kuzichukua hukumu (za sheria) bila ya kuzijadili wala kuzichambua, kuzichunguza na (nyingine) kuzikanusha. Kama ambavyo hatuwezi (pia) kuwaunga mkono au kuwapinga bila ya kuzifahamu hali zao na kusoma historia yao na waliyovatenda katika zama za uhai wa Mtume(s.a.w.w)
na baada ya kufa kwake, na tumchuje (miongoni mwao) yule mwenye kutenda haki na yule mwenye kutenda uovu, na kati ya muumini na yule mwenye matendo machafu na mwenye moyo safi na mnafiki, na (pia) tufahamu wale waliogeuka na wale walioshukuru. Na kwa masikitiko mengi ni kuwa, Ahlul-Sunnah hawalikubali jambo hilo na wanalizuwia kwa nguvu zote kuwakosoa Masahaba na kuonesha dosari zao, na wao Ahlul-Sunnah wanawaombea radhi kwa Mwenyezi Mungu Masahaba wote, na zaidi ya hapo wanawatakia rehema kama wamtakiavyo rehma Mtume Muhammad na watu wa kizazi cha Mtume Muhammad(s.a.w.w)
wala hawamtoi sahaba yeyote. Suala wanalotupiwa Ahlul-Sunnah Wal-Jamaa ni kuwa: Je, hivi kuwakosoa Masahaba na kuonesha dosari zao kunasababisha mtu kutoka nje ya Uislamu au maana yake ni kwenda kinyume cha Qur'an na Sunnah?
Kwa kujibu suala hili sina budi kuonesha matendo na kauli za baadhi ya masahaba katika zama za uhai wa Mtume(s.a.w.w)
na baada ya kufariki kwake, na (nitaonesha hayo) kwa kupitia maelezo yaliyotajwa na wanachuoni wa Kisunni ndani ya Sihah zao na Musnad zao na vitabu vyao vya historia, (pia) nitatosheka na (vitabu) vyao bila ya kutaja kitabu chochote miongoni mwa vitabu vya Kishia, kwani wao Mashia msimamo wao kwa baadhi ya Masahaba unaeleweka hauhitaji ziada ya maelezo au ufafanuzi. Na ili nipate kuondoa utata na ili mpinzani asiwe na hoja yoyote atakayoitoa dhidi yangu ninasema: "Bila shaka wakati tutakapokuwa tukizungumza juu ya Masahaba katika mlango huu, basi makusudio ni baadhi ya Masahaba na siyo wote, na huenda baadhi hii wakawa ndiyo wengi au wachache." Basi haya ndiyo tutakayo yafahamu kwa kupitia uchambuzi (huu) Inshaa Allah Taala, kwani wengi wa watu wanaoeneza chuki wanatudhania sisi tuko dhidi ya Masahaba, na kwamba sisi tunawashutumu Masahaba na kuwatukana, na yote haya wanayafanya ili wawatie mashaka wasikilizaji na wawakatize wale wanaofanya uchambuzi kutafuta haki, wakati ambapo sisi tunajiepusha mbali na (suala) la kuwatukana Masahaba na kuwashutumu, bali (ukweli) sisi tunawaombea radhi Masahaba wenye moyo safi ambao Qur'an imewaita kuwa ni "Wenye kushukuru" na vile vile sisi tunajitenga mbali na Masahaba waliorudi kinyume nyume kwa visigino vyao, ambao (waliritadi) wakageuka nyuma baada ya Mtume(s.a.w.w)
, na wakasababisha upotevu kwa Waislamu wengi, na hata hawa (licha ya kugeuka kwao) hatuwatukani wala hatuwashutumu, bali lililopo ni kwamba tunayaweka wazi matendo yao ambayo wanahistoria na wanachuoni wa hadithi wameyataja ili kweli iwadhihirikie wenye kuchunguza, na (kwa bahati mbaya) ndugu zetu Masunni jambo hili hawaliridhii na wanaliona kuwa ni matusi na ni shutma.
Iwapo Qur'ani tukufu ambayo ni maneno ya Mwenyezi Mungu na haichelei kusema ukweli, (yenyewe) ndiyo iliyotufundisha kwamba miongoni mwa Masahaba wamo wanafiki, wengine waovu, wengine madhalimu na wamo waongo, wengine washirikina na wengine waligeuka kinyume nyume na wamo wengine wanamuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Naye Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
ambaye hasemi lolote kwa matamanio yake na lawama ya mwenye kulaumu haimtishi Mtume (atendapo) kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ndiye yeye Mtume(s.a.w.w)
ametufungulia mlango na akatufahamisha kwamba miongoni mwa Masahaba wamo wenye kuritadi, na kuna wenye kutengua ahadi na wengine wenye kutoka katika dini na wamo wenye kuacha njia ya dini na miongoni mwao wataingia motoni na wala usahaba hautawanufaisha kitu, bali itakuwa ni hoja dhidi yao na adhabu yao itakuwa mara dufu katika siku ambayo haitofaa mali wala watoto. Basi itakuwaje katika hali kama hii ambayo inashuhudiwa na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake Mtukufu, wao Masunni wanataka kuwazuia Waislamu wasizungumze na kujadili juu ya Masahaba kwa sababu haki isidhihirike na Waislamu wapate kuwafahamu mawalii wa Mwenyezi Mungu na kisha wawafuate kama ambavyo kwa njia hii watawafahamu maadui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kisha wawapinge?.
Siku moja nilikuwa katika mji mkuu wa Tunisia ndani ya Msikiti mkubwa miongoni mwa Misikiti ya mji huo, baada ya kumaliza kusali sala ya faradhi, Imam alikaa katikati ya mzunguko wa watu waliokuwa wakisali (Msikitini hapo) na akaanza darasa lake kwa kuwatukana na kuwakufurisha wale watu ambao wanawashutumu Masahaba wa Mtume(s.a.w.w)
na aliendelea kwa kusema: "Jihadharini na watu ambao wanawataja kwa ubaya Masahaba kwa madai eti ya utafiti wa kielimu na kutaka kuifahamu haki, watu hao wanastahiki laana ya Mwenyezi Mungu na Malaika na watu wote. Wanataka kuwatia shaka watu katika dini yao, hali ya kuwa Mtume(s.a.w.w)
amesema: "Itakapokufikieni hadithi inayohusu Masahaba wangu basi nyamazeni (msiisimulie) kwani namuapa Mwenyezi Mungu, lau ninyi mtatoa (katika njia ya dini) thamani ya dhahabu kama mlima wa Uhudi msingeweza kufikia sehemu moja ya kumi ya mmoja wao
." Mtu mmoja aliyekuwa kafuatana nami alimkatiza kwa kusema: "Hadithi hii siyo sahihi, na Mtume amesingiziwa" Imamu yule na baadhi ya waliokuwepo walihamaki na wakatugeukia hali ya kuwa wamekasirika, basi mimi nikayaangalia mazingira hayo na kumtuliza Imamu na nikamwambia: "Ewe bwana wangu Sheikh Mtukufu, hivi ni lipi kosa la Mwislamu ambaye atasoma ndani ya Qur'ani kauli (ya Mwenyezi Mungu) isemayo:
وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ أَفَإِن مَّاتَ أَوْ قُتِلَ انقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ وَمَن يَنقَلِبْ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ فَلَن يَضُرَّ اللَّـهَ شَيْئًا وَسَيَجْزِي اللَّـهُ الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٤﴾
"Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume, wamepita kabla yake Mitume (wengi) basi akifa au akiuawa ndiyo mtarudi nyuma muwe makafiri kama zamani? Na yeyote atakayerudi nyuma kwa visigino vyake hatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote, na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaomshukuru, (Qur'an, 3:144).
Je, anakosa gani Muislamu ambaye anasoma ndani ya Sahihi Bukhari na Sahihi Muslim kauli ya Mtume(s.a.w.w)
kuwaambia Masahaba wake kwamba; "Siku ya Qiyama mtachukuliwa muelekezwe upande wa kushoto, kisha mimi nitasema (wanapelekwa) wapi? Nitaambiwa Wallahi (wanapelekwa) motoni, mimi nitasema: Ewe Mola wangu! hawa ni Sahaba wangu, nitaambiwa, hakika wewe hujui ni mambo gani waliyoyazusha baada yako, hakika wao hawakuacha kurudi nyuma tangu ulipowaacha, kisha nitasema atokomee atokomee yeyote aliyebadilisha (dini) baada yangu, nami sioni atakayeokoka miongoni mwao isipokuwa wachache mno.
"
Wakinisikiliza mimi kwa utulivu mno na baadhi yao waliniuliza ikiwa mimi nina hakika na kuwepo kwa hadithi hii ndani ya Sahihi Bukhari. Nami niliwajibu, "Ndiyo, nina hakika kama ambavyo nina hakika kuwa Mwenyezi Mungu ni mpweke hana mshirika na Muhammad ni Mtumwa wake na ni Mtume wake." Yule Imam alipogundua athari yangu kwa waliohudhuria kutokana na kuhifadhi kwangu hadithi ambazo nilizitaja, alisema kwa utulivu: "Sisi tumesoma kwa Masheikh wetu (Mwenyezi Mungu awarehemu) kwamba fitina imelala basi Mwenyezi Mungu amlaani yeyote mwenye kuiamsha."
Mimi nikasema: "Ewe Bwana wangu fitina siku zote haijalala, lakini sisi ndio tumelala, basi na yule aamkaye miongoni mwetu na kufungua macho yake ili aifahamu haki ninyi mnamtuhumu kuwa anaamsha fitina, na kwa hali yoyote ile Waislamu wanatakiwa kufuata Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake(s.a.w.w)
na wala siyo maneno wayasemayo Masheikh ambao wanawatakia radhi kina Muawiyah na Yazid na Ibnul-Aa's. Yule Imam alinikatiza kwa kusema, "Je, hivi wewe humtakii radhi bwana wetu Muawiyah (r.a) ambaye ndiye mwandishi wa Wahyi? Nikasema: "Maudhui hii ni ndefu kuifafanua, na iwapo utataka kufahamu maoni yangu kuhusu jambo hilo, basi mimi nakuzawadia kitabu changu "Thummah-Tadaitu" huenda kikakuamsha kutoka kwenye usingizi wako na kikayafungua macho yako kuhusu baadhi ya mambo ya haki."
Basi yule Imam aliyakubali maneno yangu pamoja na ile zawadi yangu huku akiwa anasita, lakini baada ya mwezi mmoja aliniandikia barua nzuri akimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuongoza kwenye njia yake iliyonyooka na akadhihirisha kuwafuata na kushikamana na watu wa nyumba ya Mtume(s.a.w.w)
, nami nilimuomba niitangaze barua yake hiyo katika chapa ya tatu (ya kitabu changu hicho) kutokana na kuwemo ndani ya barua hiyo mambo ya maana na upendo na roho safi ambayo pindi alipoifahamu haki aliikumbatia, na inaonyesha ukweli kwamba wengi miongoni mwa Masunni huielekea haki kwa kiasi cha kuondoa pazia tu (machoni pao). Lakini Imam huyo alinitaka niizuwie barua yake wala nisiitangaze, kwani inataka muda wa kutosha ili kuwatosheleza (kwa hoja) wale watu ambao wanasali nyuma yake na yeye anapendekeza wito wake uwe wa amani bila ya fitina na vurugu kwa mujibu wa mtazamo wake. Tunarudi kwenye maudhui ya kuzungumzia Masahaba, ili tuudhihirishe ukweli unaouma, ambao Qur'an imeusajili na pia Sunna ya Mtume. Hebu tuanze kwa maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo hayatafikwa na batili mbele yake wala nyuma yake kabla na kwani yenyewe ndiyo uamuzi ulio na uadilifu na ndiyo kauli bayana.
Mwenyezi Mungu anasema:
وَمِمَّنْ حَوْلَكُم مِّنَ الْأَعْرَابِ مُنَافِقُونَ وَمِنْ أَهْلِ الْمَدِينَةِ مَرَدُوا عَلَى النِّفَاقِ لَا تَعْلَمُهُمْ نَحْنُ نَعْلَمُهُمْ سَنُعَذِّبُهُم مَّرَّتَيْنِ ثُمَّ يُرَدُّونَ إِلَىٰ عَذَابٍ عَظِيمٍ ﴿١٠١﴾
"Na miongoni mwa watu wa Madina wapo waliobobea katika unafiki, huwafahamu (kuwa ni wanafiki) sisi tunawafahamu, tutawaadhibu mara mbili kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa". (Qur'an, 9:101).
يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ مَا قَالُوا وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ وَهَمُّوا بِمَا لَمْ يَنَالُوا ﴿٧٤﴾
"Wanaapa kwa Jina la Mwenyezi Mungu (kwamba) hawakusema, na hakika wamekwisha sema neno la ukafiri na wakakufuru baada ya (kudhihirisha) Uislamu wao (wa uongo) na wakaazimia mambo ambayo hawakuweza kuyafikia" (Qur'an, 9:74).
وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللَّـهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٧٥﴾ فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُوا بِهِ وَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ ﴿٧٦﴾ فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَىٰ يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُوا اللَّـهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ ﴿٧٧﴾
"Na miongoni mwao (hao wanafiki) wapo waliomuahidi Mwenyezi Mungu kuwa, akitupatia katika fadhila zake tutatoa sadaka na tutakuwa miongoni mwa wanaotenda mema, lakini alipowapa hizo fadhila zake walizifanyia ubakhili na wakapinga, basi (Mwenyezi Mungu) akawalipa unafiki ndani ya nyoyo zao mpaka siku ya kukutana naye kwa sababu ya kukhalifu kwao waliyomuahidi Mwenyezi Mungu na kwa sababu ya kusema uongo." (Qur'an, 9:75-77).
الْأَعْرَابُ أَشَدُّ كُفْرًا وَنِفَاقًا وَأَجْدَرُ أَلَّا يَعْلَمُوا حُدُودَ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٩٧﴾
"Mabedui wamezidi sana katika ukafiri na unafiki, na wameelekea zaidi wasijuwe mipaka ya yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu juu ya Mtume wake, na Mwenyezi Mungu ni mjuzi na mwenye hekima." (Qur'an, 9:97).
وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَا هُم بِمُؤْمِنِينَ ﴿٨﴾ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَمَا يَخْدَعُونَ إِلَّا أَنفُسَهُمْ وَمَا يَشْعُرُونَ ﴿٩﴾ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ فَزَادَهُمُ اللَّـهُ مَرَضًا وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ ﴿١٠﴾
Na miongoni mwa watu wapo (wanafiki) wasemao tumemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na hali ya kuwa wao si wenye kuamini, wanataka kumdanganya Mwenyezi Mungu na wale walioamini, lakini hawadanganyi isipokuwa nafsi zao hali yakuwa hawatambui, ndani ya nyoyo zao mna maradhi na Mwenyezi Mungu amewazidishia maradhi, basi watapata adhabu iumizayo kwa sababu ya kule kusema kwao uongo." (Qur'ani, 2:8-10).
إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ ﴿١﴾ اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً فَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ إِنَّهُمْ سَاءَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢﴾ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا فَطُبِعَ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَفْقَهُونَ ﴿٣﴾
"Wanapokujia wanafiki husema: tunashuhudia ya kuwa, kwa yakini wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu anajua kuwa wewe ni Mtume wake na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hakika wanafiki ni waongo, wamevifanya viapo vyao kuwa ngao za kujikinga, wakazuwia njia ya Mwenyezi Mungu, hakika ni mabaya waliyokuwa wakiyafanya, na hayo ni kwa kuwa waliamini kisha wakakufuru, basi muhuri ukapigwa juu ya nyoyo zao, hivyo basi hawafahamu chochote" (Qur'ani, 63:1-3).
أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُوا بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَن يَتَحَاكَمُوا إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُوا أَن يَكْفُرُوا بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُضِلَّهُمْ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴿٦٠﴾ وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا إِلَىٰ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَإِلَى الرَّسُولِ رَأَيْتَ الْمُنَافِقِينَ يَصُدُّونَ عَنكَ صُدُودًا ﴿٦١﴾ فَكَيْفَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ ثُمَّ جَاءُوكَ يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ إِنْ أَرَدْنَا إِلَّا إِحْسَانًا وَتَوْفِيقًا ﴿٦٢﴾
"Huwaoni wale wanaodai kwamba wameamini yale yaliyoteremshwa kwako na yaliyoteremshwa kabla yako, wanataka wakahukumiwe kwa Taaghuti (dhalimu) na hali wameamrishwa kumkataa Taaghuti, naye shetani anataka kuwapoteza upotofu ulio mbali, na wanapoambiwa njooni katika yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu na njooni kwa Mtume utawaona wanafiki wanajitenga nawe mbali kabisa, basi itakuwaje utakapowafikia msiba kwa sababu ya yale iliyoyatanguliza mikono yao? Kisha wakakujia wakiapa kwa Mwenyezi Mungu, Hatukutaka ila wema na mapatano" (Qur'ani, 4:60-62).
إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿١٤٢﴾
"Bila shaka wanafiki hutaka kumdanganya (hata) Mwenyezi Mungu, naye atawaadhibu kwa sababu ya kudanganya kwao, na wanaposimama kusali husimama kwa uvivu, wanawaonesha watu (kuwa wanasali) wala hawamkumbuki Mwenyezi Mungu ila kidogo." (Qur'ani, 4:142).
وَإِذَا رَأَيْتَهُمْ تُعْجِبُكَ أَجْسَامُهُمْ وَإِن يَقُولُوا تَسْمَعْ لِقَوْلِهِمْ كَأَنَّهُمْ خُشُبٌ مُّسَنَّدَةٌ يَحْسَبُونَ كُلَّ صَيْحَةٍ عَلَيْهِمْ هُمُ الْعَدُوُّ فَاحْذَرْهُمْ قَاتَلَهُمُ اللَّـهُ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ ﴿٤﴾
"Na unapowaona miili yao inakupendeza, na kama wakisema unasikiliza usemi wao, lakini wao ni kama boriti zilizotegemezwa, wanadhani kila kishindo kiko juu yao, hao ni maadui jihadhari nao, Mwenyezi Mungu awaangamizie mbali, ni vipi wanapotoka kutoka kwenye haki? (Qur'ani, 63:4).
"Bila shaka Mwenyezi Mungu anawajua wale wanaojizuwia miongoni mwenu wasiende vitani, na wale wanaowaambia ndugu zao, njooni kwetu (msiende kwa Muhammad) wala hawaendi katika mapigano ila kidogo tu, wanakufanyieni choyo, lakini inapokuja hofu utawaona wanakutazama, macho yao yanazunguka kama yule aliyezimia kwa mauti, lakini hofu yao inapoondoka wanakuudhini kwa ndimi zao kali wanaifanyia choyo kheri hao hawakuamini, kwa hivyo Mwenyezi Mungu ameviondoshea thawabu vitendo vyao, na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi." (Qur'ani, 23:18-19).
وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً بِقَدَرٍ فَأَسْكَنَّاهُ فِي الْأَرْضِ وَإِنَّا عَلَىٰ ذَهَابٍ بِهِ لَقَادِرُونَ ﴿١٨﴾ فَأَنشَأْنَا لَكُم بِهِ جَنَّاتٍ مِّن نَّخِيلٍ وَأَعْنَابٍ لَّكُمْ فِيهَا فَوَاكِهُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿١٩﴾
"Na wapo miongoni mwao wanaokusikiliza, hata wanapoondoka kwako huwaambia wale waliopewa elimu, (Mtume) amesema: nini sasa hivi, hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewapiga muhuri nyoyoni mwao na wakafuata matamanio ya nafsi zao" (Qur'ani, 47:16).
أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ أَن لَّن يُخْرِجَ اللَّـهُ أَضْغَانَهُمْ ﴿٢٩﴾وَلَوْ نَشَاءُ لَأَرَيْنَاكَهُمْ فَلَعَرَفْتَهُم بِسِيمَاهُمْ وَلَتَعْرِفَنَّهُمْ فِي لَحْنِ الْقَوْلِ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ أَعْمَالَكُمْ ﴿٣٠﴾
"Je, wale wenye maradhi nyoyoni mwao wanadhani kwamba Mwenyezi Mungu hataidhihirisha bughudha yao, na kama tungependa tungekuonesha (watu hao) na ungewatambua kwa alama zao, lakini utaweza kuwafahamu kwa namna ya msemo (wao) na Mwenyezi Mungu anavifahamu vitendo vyenu" (Qur'ani, 47:29-30).
"Watakuambia wale waliokaa nyuma (wasiende vitani) miongoni mwa mabedui (watajidai kutoa nyudhuru) mali zetu na watu wetu walitushughulisha, basi tuombee msamaha, wanasema kwa ndimi zao yasiyokuwamo ndani ya mioyo yao." Kwa hiyo aya hizi zilizobayana kutoka ndani ya kitabu cha Mwenyezi Mungu, maelezo ambayo aya zimeyabainisha kuhusu unafiki wa baadhi yao na miongoni mwao wamo ambao walijificha ndani ya safu za Masahaba wema mpaka ukafichikana unafiki wao hata kwa mwenyewe Mtume lau si wahyi wa Mwenyezi Mungu kumtambulisha. Lakini sisi siku zote kuhusu jambo hili tunapingana na Masunni, kwani wao wanasema; "Tunahaja gani kuzungumzia wanafiki ambao Mwenyezi Mungu amewalaani, na Masahaba siyo miongoni mwa hawa (wanafiki), au husema, wanafiki siyo miongoni mwa Masahaba."Je, wanafiki hawa ni kina nani basi. ambao zimeshuka aya zaidi ya mia moja na khamsini kwa ajili yao ndani ya Surah za At-Taubah na Munafiqiina. " Watakujibu: "Hao ni Abdallah bin Ubai na Abdallah bin Abi Sallul." Na baada ya majina haya hawana jina jingine zaidi. Su-bhanallah!! Ikiwa Mtume(s.a.w.w)
mwenyewe nafsi yake hakuwafahamu wengi miongoni mwa wanafiki, basi itakuwaje unafiki ukomee kwa ibn Ubai na ibn Abi Sallul ambao wanafahamika kwa Waislamu wote?
Ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
aliwatambua baadhi yao na akawabainisha majina yao kwa Hudhaifah ibn Al-yamani kama mnavyosema, na kisha Mtume akaamuru asitangaze unafiki wao, kiasi kwamba Umar ibn Khattab alikuwa akimuuliza Hudhaifah zama za utawala wake Umar juu ya nafsi yake kuwa je, yeye ni miongoni mwa wanafiki? Na je, Mtume alimtaja jina lake? Yote haya ni kwa mujibu wa maelezo yenu ndani ya vitabu vyenu na ikiwa Mtume(s.a.w.w)
alitoa alama za wanafiki ambazo kwazo watatambulikana, nazo ni kumbughudhi Ali ibn Abi Talib, kwa mujibu wa riwaya zilizomo vitabuni mwenu hapana shaka wengi miongoni mwa hawa ni Masahaba ambao ninyi mnawaombea radhi na kuwapandisha daraja (za juu) na wengine licha ya bughudha dhidi ya Ali ibn Abi Talib, bali bughudha hiyo iliwafikisha mahali pa kumpiga vita Ali na walimuua na kumlaani angali hai na baada ya kufa yeye mwenyewe Ali na watu wa nyumba yake na wampendao, na wote waliotenda haya ni masahaba wema kwenu ninyi. Hekima ya Mtume(s.a.w.w)
ilimfanya amfundishe Hudhaifa majina ya wanafiki kwa upande mmoja, na Mtume pia akawapa Waislamu alama za wanafiki kwa upande wa pili, ili asimamishe hoja dhidi ya watu wasijesema baada yake kuwa hakika sisi hatukuwa tunalijuwa jambo hili. Hatuoni maana yoyote wakati Masunni wanaposema "Sisi tunampenda Ali (r.a)."
Sisi tunawaambia Masunni kwamba "Kamwe ndani ya moyo wa Muumini hayakutani mapenzi ya kumpenda Walii wa Mwenyezi Mungu na mapenzi ya kumpenda adui wa Mwenyezi Mungu, kwani yeye mwenyewe Imam Ali
amesema:Hawezi akawa miongoni mwetu yule anayetulinganisha sisi na maadui zetu
."
Ifahamike kwamba Qur'ani wakati ilipozungumzia Masahaba, iliwazungumzia kwa sifa mbali mbali na alama mbali mbali zenye kuthibiti, na inapowatoa miongoni mwao wale Masahaba wema wenye kushukuru, basi bila shaka watakaosalia Qur'an imewataja kuwa ni waovu, au ni wenye khiyana, au ni wenye kujifanya wanyonge, au wenye kutoka katika dini, au ni wenye kugeuka au wanamtilia mashaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na ni wenye kukimbia mapambano dhidi ya makafirina na au wanadhoofisha wenzao kwenye jihadi au ni wapinzani wa haki, au ni waasi wa amri za Mwenyezi Mungu na Mtume wake, au ni wenye kukimbilia upuuzi na biashara na kuacha sala, au ni wenye kusema wasiyoyatenda, au wanajifaharisha kwa Uislamu wao mbele ya Mtume, au nyoyo zao ni ngumu hazikumnyenyekea Mwenyezi Mungu kwa utajo wake na haki iliyoteremka, au watakuwa ni wenye kunyanyua sauti zao juu ya sauti ya Mtume(s.a.w.w)
au ni wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu au ni wenye kuwasikiliza wanafiki. Hebu na tutosheke na kiasi hiki kidogo, kwani kuna aya nyingi hatukuzitaja ili tufupishe maelezo. Lakini ili ipatikane faida, hatuna budi kutaja baadhi ya aya ambazo zimekuja kuhusiana na kuwashutumu Masahaba ambao walisifika kwa sifa hizo, lakini kwa baraka za kisiasa baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
na baada ya wahyi kukatika, wote hawa wakawa ni waadilifu na eti haifai kwa yeyote miongoni mwa Waislamu kuzungumza cho chote kuhusiana nao ikiwa ni kuwakosoa au kutia dosari.