WAULIZE WANAOFAHAMU

WAULIZE WANAOFAHAMU0%

WAULIZE WANAOFAHAMU Mwandishi:
: SHEIKH MUSABBAH SHA'ABANI
Kundi: Misingi mikuu ya Dini

WAULIZE WANAOFAHAMU

Mwandishi: Muhammad Tijani As-samawi At-Tunisi
: SHEIKH MUSABBAH SHA'ABANI
Kundi:

Matembeleo: 51506
Pakua: 5470

Maelezo zaidi:

WAULIZE WANAOFAHAMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 26 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 51506 / Pakua: 5470
Kiwango Kiwango Kiwango
WAULIZE WANAOFAHAMU

WAULIZE WANAOFAHAMU

Mwandishi:
Swahili

10

WAULIZE WANAOFAHAMU

UTENDAJI WA MASAHABA KUHUSU MAAMRISHO YA MTUME (s.a.w.w) BAADA YA KUFARIKI KWAKE

NAMNA WALIVYOIPOTOSHA SUNNA YA MTUME (s.a.w.w)

Bukhari ameandika katika Sahihi yake, juzuu ya kwanza Babu tadh-yius-salah. Imepokewa toka kwa Ghailan, Anas ibn Malik amesema: "Sikioni chochote miongoni mwa mambo ambayo yalikuwepo zama za Mtume (s.a.w.w)." Akaambiwa, "Sala (ipo)" akasema: "Je, hivi hamjaipoteza kwa kuyaacha yaliyomo ndani ya Sala ?" Na amesema: nilimsikia Az-zuhri anasema: "Niliingia kwa Anas ibn Malik alipokuwa Damascus nikamkuta analia, nikamwambia kitu gani kinakuliza? Akasema: sikioni chochote vitu nilivyovifahamu isipokuwa hii sala, na hii sala imekwisha puuzwa ." [12]

Kama ambavyo Bukhari ameandika katika juzuu ya kwanza mlango wa fadhila za sala ya alfajiri kwa jamaa, amesema: "Ametusimulia A'amash, amesema: Nilimsikia Salim, kasema:Nilimsikia Ummud-dar-dai akisema, alikuja kwangu Dar-dai hali yakuwa amekasirika, nikamwambia, Kitu gani kimekukasirisha? Akasema, Wallahi sikioni chochote katika umma wa Muhammad ila ni kwamba wote wanasali tu ."[13] .

Na ameandika Bukhari ndani ya juzuu ya pili Babul-khuruji Ilal-musalla bighair minbar kutoka kwa Abu Said Al-khudri amesema: "Mtume(s.a.w.w) alikuwa akitoka kwenda kusali siku ya Idil-fitri au Al-az'ha, basi kitu cha kwanza alichokuwa akianza ni sala kisha baada ya hapo huwapa mawaidha watu, hivyo basi watu waliendelea kufanya hivyo mpaka siku moja nilitoka na Mar-wan akiwa ndiyo amiri wa Madina, katika sala ya Idul-az-ha au Idid-fitr, basi (Mar-wan) akataka kupanda juu ya Minbar kabla ya kusali, nikaivuta nguo yake naye akaivuta kisha akapanda na akahutubu kabla ya sala, baadaye nikamwambia "Wallahi mmebadilisha.

"Akasema: "Ewe Abu Said yamekwisha toweka uyajuwayo wewe." Nikamwambia "Wallahi niyajuwayo mimi ni bora kuliko yale nisiyoyajua." Akasema: "Hakika watu walikuwa hawakai kwa ajili yetu baada ya sala, ndiyo maana mimi nikaifanya hotuba kabla ya Sala."[14] Ni vipi Masahaba katika zama za Anas ibn Malik na zama za Abud-dardai pia katika zama za Mar-wan zama ambazo ziko karibu mno na zama za uhai wa Mtume(s.a.w.w) , wanabadilisha Sunna za Mtume na kupuuza kila kitu mpaka sala kama ulivyosikia? Si hivyo tu bali wamezigeuza Sunna za Mtume(s.a.w.w) kwa maslahi yao yasiyo na maana na hasa kwa kuwa, Banu Umayyah walijitengenezea Sunna ya kumtukana na kumlaani Ali na watu wa nyumba ya Mtume. Waliwatukana juu ya mimbari kila baada ya khutba, kwa ajili hiyo watu wengi wakawa hutawanyika siku ya Idul-az-ha au Idul-fitr kila inapomalizika sala kwa kuwa walikuwa hawapendi kumsikia Imam wao anamlaani Ali ibn Abi Talib na watu wa nyumba ya Mtume. Kwa sababu hiyo basi, Banu Umayyah wakafanya makusudi hasa kubadilisha Sunna ya Mtume na wakatanguliza hotuba kabla ya Sala katika sikukuu hizo mbili ili wapate fursa ya kumtukana na kumlaani Ali mbele ya Waislamu wote na yote hayo ni kuonesha chuki yao. Kiongozi wa hawa wote ni Muawiyah ibn Abi Sufiyani, yeye ndiye aliyewawekea mwenendo huo ambao waliufanya kuwa ni miongoni mwa sunna tukufu ambayo kwayo wakijikurubishia kwa Mwenyezi Mungu.

Kuna baadhi ya wanahistoria wamesimulia kwamba, mmoja wa Maimamu wao alikamilisha hotuba yake siku ya Ijumaa na akasahau kumlaani Ali akawa anateremka kutoka kwenye mimbari ili aje kusalisha, basi ghafla watu wakawa wanapiga kelele kutoka kila upande, "Umeacha Sunna, umesahau Sunna." Sunna gani hiyo? Naam kwa masikitiko makubwa basi, hii ndiyo Bid'a iliyozushwa na Muawiyyah ibn Abi Sufiyan na ilidumu kwa miaka themanini ikizunguka kwenye mimbari za Waislamu na makovu yake yamebakia hadi leo. Pamoja na yote hayo Ahlus-Sunna Wal-Jamaa wanamuombea radhi Muawiyyah na wafuasi wake, na wala hawawezi kumkosoa wala kumtia kombo kwa madai ya kuwaheshimu Masahaba. Kila sifa njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu, watafiti wenye moyo safi miongoni mwa Umma wa Kiislamu sasa wameanza kufahamu haki kutokana na isiyo kuwa haki, na wengi kati yao wameanza kujinasua kwenye kifungo cha masahaba ambacho hakuna aliyekitebgeneza isipokuwa Muawuya na wafuasi wake na wale wampendao. Sasa hivi Masunni wameanza kuzinduka kutokana na tatizo hili, ingawaje wakati huo wanawatetea Masahaba wote kiasi cha kumlaani mwenye kumkosoa mmoja miongoni mwa Masahaba. Iwapo Masunni utawaambia kwamba "Bila shaka laana yenu hii mnayolaani pia inamkumba Muawiya ibn Abi Sufyaan kwani yeye Muawiya kwa kufanya hivyo alikusudia moja kwa moja kumtukana Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye amesema: Yeyote atakaye mtukana Ali, basi hakika amenitukana mimi basi atakuwa amemtukana Mwenyezi Mungu." Basi hapo utawaona wanachanganyikiwa na kushindwa kujibu na hatimaye husema vitu ambavyo ikiwa vina maana Fulani basi maana hiyo itakuwa ni mawazo duni na ung'anga'nizi wa kipofu ambao unakera.

Kwa mfano baadhi yao husema: Huu ni uongo uliofanywa na Shia, na baadhi yao husema, Ee Bwana hao ni Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) wanao uhuru wa kuwasema Masahaba wenzao namna watakavyo, amma sisi hatuna daraja hata ya kuwakosoa. Umetakasika ewe Mwenyezi Mungu na sifa njema ni zako, kwa hakika maneno yako yamenifahamisha katika Qur'an Tukufu juu ya ukweli ambao ilikuwa vigumu mimi kuufahamu na kuuamini, na kila nilipokuwa nikisoma maneno yako yasemayo kwamba:

وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ لَهُمْ قُلُوبٌ لَّا يَفْقَهُونَ بِهَا وَلَهُمْ أَعْيُنٌ لَّا يُبْصِرُونَ بِهَا وَلَهُمْ آذَانٌ لَّا يَسْمَعُونَ بِهَا أُولَـٰئِكَ كَالْأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ ﴿١٧٩﴾

Na bila shaka tumewaumbia moto wa Jahannam wengi katika majini na wanadamu (kwani) wanazo nyoyo lakini kwa nyoyo hizo hakuna wanachokifahamu, na wanayo macho, lakini hawaoni kwa macho hayo, na wanayo masikio lakini hawasikii kwa masikio hayo. Basi hao ni kama wanyama, bali wao ni wapotofu zaidi, hao ndio walioghafilika" (Qur'ani, 7:179).

Nisomapo maneno hayo nashangaa moyoni mwangu na ninasema ni vipi itakuwa hivyo? Je, inawezekana mnyama asiyesema akawa ameongoka kuliko mtu? Inawezekana mtu akachonga jiwe kisha akaliabudia na kuliomba riziki na msaada? Lakini namshukuru Mwenyezi Mungu, kushangaa kwangu kumetoweka baada ya kupanuka mawasiliano yangu na watu, na niliposafiri kwenda India nimeona maajabu makubwa, nimewaona madaktari katika elimu ya viumbe wanaofahamu umbile la mtu na viungo vyake. lakini bado wanaabudu ng'ombe, lakini lau jambo hili baya lingefanywa na watu wajinga miongoni mwa Wahindu udhuru wao ungekubalika, lakini utamuona mwana taaluma mzuri miongoni mwao anaabudia ng'ombe, jiwe, bahari, jua na mwezi!! Kwa hali hii huna la kufanya baada ya (kuona haya) isipokuwa ukubali na ufahamu maana inayojulishwa na Qur'ani kuhusu watu ambao wao ni wapotevu mno kuliko mnyama.

Ushahidi wa Abud-dharri kuhusu baadhi ya Masahaba Bukhari ameandika ndani ya juzuu ya pili mlango wa Man ud-diyat Zakatuhu falaisa Bikanzin, Imepokewa kutoka kwa Al-Ahnaf ibn Qais amesema: "Nilikaa na watu miongoni mwa Maquraishi, basi alikuja mtu mwenye nywele na nguo zilizochakaa pia na hali yake mpaka akasimama mbele yao akasalimia kisha akasema, Wabashirie kuwa (watachomwa) kwa mawe yaliyochemshwa katika moto wa jahannam, kisha yatawekwa juu ya chuchu ya maziwa ya mmoja wenu na kutokea kwenye sehemu inayoanzia shingo katika bega na kuwekwa (tena) kwenye sehemu inayoanzia shingo katika bega na kutokea kwenye chuchu, kisha (mtu huyo) akageuka na akakaa kwenye nguzo, nami nikamfuata nikakaa naye na hali yakuwa simfahamu kuwa ni nani, basi nikamwambia mimi sioni isipokuwa jamaa wamechukizwa kwa maneno uliyoyasema. Akasema: Bila shaka hao hawafahamu chochote, kipenzi changu aliniambia ndiye aliyeniambia... Mimi nikamwambia ni nani huyo kipenzi chako?

Akasema Mtume(s.a.w.w) aliniambia: Ewe Abudharri wauona (mlima wa) Uhd? Nikaliangalia jua na muda wa mchana uliobakia na hali ya kuwa nahisi kwamba Mtume anataka kunituma kwa shida aliyonayo, nikamwambia, Naam, Akasema: Mimi sipendi kuwa na dhahabu mfano wa Uhud (bali nikiwa nayo) nitaitoa yote isipokuwa dinari tatu. Watu hawa hawana akili, bali wanaikusanya (mali ya) dunia, hapana Wallahi siwaombi dunia yao wala sitaki wanilipie deni mpaka nitakapokutana na Mwenyezi Mungu Mtukufu[15] .

Bukhari pia ameandika katika juzuu ya saba, Babul-haudh Waqaulullahi Taala In-naa A'atainakal-kawthar. Imepokewa toka kwa At'a ibn Yasar kutoka kwa Abu Hurairah kwamba, Mtume(s.a.w.w) amesema: "Kuna wakati mimi nitakuwa nimesimama (siku ya Qiyama), ghafla watafika jamaa, nami nitakapowatambua atatokea mtu kati yangu na wao, atasema Njooni, Mimi nitasema, Waende wapi? Atasema Wallahi motoni, Nitasema Yalikuwaje mambo yao? Atasema, Hakika wao waligeuka baada yako kinyumenyume.

Kisha jamaa wengine watafika mpaka nitapowafahamu, atatoka mtu kati yangu na wao atasema, Njooni, Nitasema waende wapi? Atasema Wallahi motoni, Nitasema Yalikuwaje mambo yao? Atasema: Hakika wao waligeuka baada yako kinyumenyume, Sitamuona miongoni mwao anayesalimika isipokuwa wachache tu." Na imepokewa kutoka kwa Abu Said Al-khudri kwamba: Siku hiyo patasemwa: "Bila shaka wewe hufahamu waliyoyazusha baada yako, basi mimi nitasema na aangamie, aangamie aliyebadilisha baada yangu."[16]

Kama alivyoandika Bukhari katika juzuu ya tano mlango wa Ghaz-watul-Hudaibiyyah na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo, "Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waumini waliofungamana nawe chini ya mti." Imepokewa kutoka kwa Al-alaa ibn Al-musayyab naye kapokea kwa baba yake amesema: "Nilikutana na Al-barra ibn A'zib (r.a) nikamwambia, pongezi wewe ulisuhubiana na Mtume(s.a.w.w) na ukampa baia chini ya mti, akasema, Ewe mtoto wa ndugu yangu hakika wewe hujuwi tuliyoyazua baada yake."[17]

Na huo ni ushahidi mkubwa utokao kwa Sahaba mkubwa ambaye kwa uchache alikuwa mkweli kwa nafsi yake na watu, na ushahidi wake unakuja kutia nguvu maneno aliyoyasema Mwenyezi Mungu kuwahusu Masahaba alipowaambia, "(Muhammad) akifa au akiuawa mtageuka nyuma kwa visigino vyenu." Na unatia nguvu maneno aliyoyasema Mtume(s.a.w.w) , "Nitaambiwa, hakika wao walirudi baada yako kinyume nyume." Huyu Al-barraa ibn Azib ni Sahaba Mtukufu miongoni mwa wale wa mwanzo ambao walimpa baia Mtume(s.a.w.w) chini ya mti, yeye anaishuhudia nafsi yake na za wengine miongoni mwa Masahaba kwamba, wao walizusha baada ya kufa Mtume(s.a.w.w) ili watu wasije danganyika kutokana na Masahaba, na alibainisha wazi kwamba kuwa sahaba wa Mtume(s.a.w.w) na kumpa baia chini ya mti ambako kumeitwa kuwa ni Baia'tur-ridh-wan vitu hivi havizuwii Sahaba kupotoka na kuritadi baada ya Mtume(s.a.w.w) .

Bukhari ameandika katika juzuu ya nane mlango wa kauli ya Mtume(s.a.w.w) isemayo. Mtafuata mwenendo wa watu waliopita kabla yenu. Imepokewa kutoka kwa Ataa ibn Yasar, kutoka kwa Abu Said Al-Khudri naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mtafuata mwenendo wa waliopita kabla yenu hatua baada ya hatua na dhiraa baada ya dhiraa, mpaka hata wakiingia kwenye shimo la kenge nanyi mtawafuata." Tukamwambia Mtume, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu hao ni Mayahudi na Wakristo?" Mtume akasema, "Ni kina nani basi (kama si hao)?" [18] Ushahidi wa historia kuhusu Masahaba Baada ya Qur'ani na Sunna tunao ushahidi mwingine ambao huenda ukawa bayana na wazi zaidi, kwani unatambulikana kwa watu walioishi katika kipindi hicho na wakaushuhudia na kuwa nao sambamba, na hatimaye ukawa ni historia na ni matukio yaliyohifadhiwa. Tutaposoma vitabu vya historia vya Ah-lusunna Wal-Jamaa kama vile Tabari, Ibnul-Athir, Ibn Sa'ad, Abul-Fidai, Ibnu Qutaibah na wengineo tutaona maajabu makubwa na tutafahamu kwamba, wayasemayo Masunni juu ya uadilifu wa Masahaba na kwamba haifai kumkosoa yeyote miongoni mwao ni maneno yasiyoweza kusimamisha dalili,wala akili iliyosalimika haiwezi kukubali isipokuwa (kwa watu) wang'ang'anizi ambao kiza limewazibia mwangaza kiasi ambacho hawawezi kutofautisha baina ya Mtume Muhammad ambaye ni Ma'asum, hatamki kwa matamanio na wala hafanyi kitu isipokuwa ni cha haki tu. Wanashindwa kutofautisha kati yake na Masahaba wake ambao Qur'ani imeshuhudia juu ya unafiki na uovu wao na uchache wa uchamungu walionao, ndiyo maana utawaona Masunni wanawatetea Masahaba zaidi ya vile wanavyomtetea Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) .

Nakupigia mfano kuhusu hilo. Wakati unapomwambia mmoja wao kwamba (maonyo yaliyomo katika) Sura ya Abasa Watawalla hayakukusudiwa kwa Mtume(s.a.w.w) , bali aliyekusudiwa ni mmoja wa Masahaba wakubwa ambaye Mwenyezi Mungu alimlaumu kwa kiburi chake na kuchukizwa kwake alipomuona yule kipofu masikini. Hapo utamuona (Sunni) hakubaliani na tafsiri hii na atasema, "Muhammad hakuwa ila ni mtu tu, kwani ni mara nyingi alikosea na Mola wake akamlaumu mahala pengi tu, yeye hakuhifadhika isipokuwa katika kufikisha Qur'ani. Basi huu ndiyo mtazamo wa Masunni kumhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu. Lakini iwapo wewe utasema kwamba, "Umar ibn Khatab alikosea alipozusha sala ya tarewehe ambayo Mtume wa Mwenyezi Mungu alikataza isisaliwe Msikitini na akawaamuru watu wasali majumbani mwao mmoja mmoja sala ya sunna (yaani isiyo ya faradhi), hapo utamuona Sunni anamtetea Umar ibn Khatab kwa nguvu na hakubali majadiliano bali atasema: "Hiyo ni Bid'a nzuri", na atajaribu kwa juhudi zake zote kumtafutia sababu (ya kumuepushia kosa) pamoja na kuwepo kwa tamko la Mtume(s.a.w.w) inalokataza.

Na ukimwambia kwamba, "Umar alizuwia haki ya Muallafatul-Qulubi haki ambayo Mwenyezi Mungu aliipitisha ndani ya Kitabu chake kitukufu." Pia utamuona anasema, "Bila shaka Bwana wetu Umar alifahamu kwamba Uislamu umekwishapata nguvu, ndiyo maana aliwaambia hao wanaoimarishwa nyoyo zao katika dini kwamba: Hatuna haja nanyi, naye (Umar) alikuwa akifahamu maana za Qur'ani zinavyoeleza kuliko watu wote! Loh! (ewe bwana) halikushangazi jibu kama hili? Kuna mtu mmoja miongoni mwa Masunni kwa hakika yeye amevuka mpaka pale nilipomwambia; "Hebu tuachane na Bid'a nzuri na hao wanaoimarishwa nyoyo zao katika dini, Je, utamteteaje Umar pale alipoanza kutoa onyo kwamba angeliichoma moto nyumba ya Bibi Fatmah pamoja na waliomo, isipokuwa (watasalimika tu) iwapo watatoka kwenda kula kiapo cha utii (kwa Abubakr)?" Huyu bwana alinijibu wazi wazi (bila woga akasema): "Anayo haki (ya kufanya hivyo) kwani lau asingefanya hivyo watu wengi miongoni mwa Masahaba wangejizuwia (kutoa baia) wakabaki kwa Ali ibn Abi Talib na fitina ingetokea." Watu kama hawa kuzungumza nao haisaidii wala kunufaisha kitu, na kwa masikitiko makubwa nasema kwamba, "Wengi wa Masunni wana mawazo ya aina hii, kwani wao hawaitambui haki isipokuwa kupitia kwa Umar ibn Khatab na matendo yake, kwa hiyo wameigeuza kanuni na wakawa huitambua haki kupitia kwa watu, wakati kinachotakiwa ni kuwatambua watu kupitia kwenye haki. Itambue haki utawatambua watu wa haki kama alivyosema Imam Ali(a.s) .

Kisha kanuni hii imeenea kwa Masunni na ikamvuka Umar ibn Khatab mpaka ikawafikia Masahaba wote, na wote ni waadilifu haiwezekani kwa mtu yeyote kuwakosoa au kuwapinga, kwa maana hiyo basi Masunni wameweka pazia zito na kizuwizi kigumu kwa mchunguzi anayetaka kufahamu haki, utamuona hawezi kukwepa wimbi moja mpaka yanapomkumba mawimbi mengi na hawawezi kukwepa hatari yeyote mpaka hatari nyingi zinapozuia njia yake, na masikini hawezi kufikia ukingoni kwa amani isipokuwa atapokuwa miongoni mwa wenye azma, subira na ushujaa. Tukirudi kwenye maudhui ya historia ni kwamba, baadhi ya Masahaba wamevuliwa nguo zao, siri zao za moyoni kukashifika na ulidhihiri ukweli wao ambao walijaribu kwa juhudi zao zote kuuficha mbele za watu, au watetezi wao na wafuasi wao walijaribu kuuficha au unaweza kusema kuwa watawala waovu na mashabiki wao ndiyo waliojaribu kila namna kuficha ukweli huo. Kitu cha kwanza kukitupia macho ni msimamo wa Masahaba hawa juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) waliouonyesha mapema baada ya kufariki kwake, na ni vipi walimuacha na hawakushughulika kumuandaa, kumkosha na wala kumvika sanda na hatimaye kumzika, bali walikimbilia kwenye mashauriano yao katika Klabu ya Bani Saidah, wakagombana na kushindana ni nani aupate Ukhalifa ambao walikuwa wakimfahamu fika muhusika wake kisheria ambaye walikula kiapo cha utii kwake katika zama za uhai wa Mtume(s.a.w.w) .

Kinachotuthibitishia kwamba watu hawa waliitumia fursa ya kutokuwepo kwa Ali na Bani Hashim ambao utu wao haukuwapa nafasi ya kuuacha mwili wa Mtume(s.a.w.w) ukiwa umefunikwa eti tu wakagombee Ukhalifa katika Saqifah, kwa ajili hiyo jamaa hawa wakapitisha haraka haraka maamuzi kuhusu Ukhalifa kabla Bani Hashim hawajamaliza kazi yao tukufu ya kumuandaa Mtume kwa ajili ya mazishi ili hatimaye wawalazimishe kukubali matokeo hayo, na wasiweze kusema chochote wala kutoa hoja hasa kwa kuwa jamaa hao waliokuwa Saqifa walikwisha kukubaliana kumuua yeyote atakayejaribu kutengua kile walichokipitisha, eti kwa madai ya kuwadhibiti wapinzani na kutuliza machafuko. Wanahistoria wanaeleza mambo ya ajabu yaliyotokea katika siku hizo yaliyofanywa na hao Masahaba ambao baadaye walikuwa ndiyo Makhalifa wa Mtume(s.a.w.w) na pia wakawa ndiyo maamiri wa Waumini. Miongoni mwa mambo hayo ni kama vile kuwalazimisha watu kutoa Baia (kiapo cha utii) kwa kuwapiga na kuwatisha kwa nguvu na kuihujumu nyumba ya Bibi Fatmah kisha kuikashifu nyumba hiyo na pia kumbana tumbo lake (Bibi Fatimah) kwenye mlango ambao alikuwa yuko nyuma yake mpaka mimba yake ikaporomoka.

Si hivyo tu bali walimtoa nje Ali hali ya kuwa kafungwa na kumuonya kuwa watamuua iwapo atakataa kutoa Baia, na walimpokonya Bibi Fatmah haki zake ikiwa ni pamoja na zawadi (ya Fadak) na mirathi yake na sehemu ya Qaraba wa Mtume kiasi kwamba, Bibi Fatimah amekufa hali ya kuwa amewakasirikia waliomfanyai hayo na akiwaombea katika kila Sala (waangamizwe), na (Mwana Fatmah) alizikwa usiku tena kwa siri na hao jamaa hawakuhudhuria jeneza lake!! Vile vile jamaa hao wa Saqifah, waliwaua Masahaba waliokataa kutoa zaka kwa Abubakr kutokana na kusita kwao ili tu wafahamu sababu za Ali kutokuwa Khalifa, kwani wakijuwacho wao ni kuwa yeye ndiye waliyempa Baia (ya kuwa Khalifa wao) zama za uhai wa Mtume(s.a.w.w) huko kwenye Bonde la Khum. Pia miongoni mwa mambo waliyoyafanya ni kama vile kuhalalisha mambo ya haramu, kuivuka mipaka ya Mwenyezi Mungu na kuwaua watu wema miongoni mwa Waislamu kisha wakawaingilia wake zao bila kuheshimu kipindi cha Eda. Walibadilisha hukumu za Mwenyezi Mungu na Mtume wake zilizojengeka kwa msingi wa Kitabu Qur'an na Sunnah wakaweka badali yake hukumu za ijitihadi zitakazotumikia maslahi yao binafsi.

Na kama vile kunywa kwao pombe na kudumu kwenye zinaa hali yakuwa ni viongozi wa Waislamu na ni watawala ndani ya Waislamu, vile vile kumuondosha Abudharri Al-Ghifari na kumfukuza kutoka Madina mji wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) mpaka akafa akiwa peke yake (na alifanyiwa hivyo) bila ya kosa lolote alilolitenda, walimpiga Ammar mpaka wakampasua, walimpiga Abdallah ibn Mas-udi mpaka wakamvunja mbavu zake, na pia wakawauzulu Masahaba wema kwenye madaraka na kuwatawalisha waovu miongoni mwa Banu Umayyah ambao ni maadui wa Uislamu. Na (miongoni mwa mambo yao) ni kama vile kuwatukana na kuwalaani watu wa nyumba ya Mtume ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na amewatakasa mno, na pia kuwaua wale wanaowafuata watu wa nyumba ya Mtume miongoni mwa Masahaba wema. Na kama vile kukalia kwao Ukhalifa kwa shinikizo la nguvu, mauaji, vitisho na kumdhibiti yeyote anayewapinga kwa njia mbali mbali kama vile kumuua kwa kumvamia au kumtilia sumu na mengineyo. Na miongoni mwa hayo ni kuushambulia mji wa Mtume kwa jeshi la Yazid. likafanya lilivyotaka bila kujali kauli ya Mtume aliyosema: "Bila shaka mji wangu huu wa Madina ni mji mtukufu, basi yeyote atakayezua ndani yake tukio la uovu laana ya Mwenyezi Mungu na Malaika na watu wote iwe juu yake." Na kama vile kuipiga kwao nyumba ya Mwenyezi Mungu kwa Manjaniq na kuichoma moto nyumba hiyo tukufu ya Mwenyezi Mungu, na ndani yake waliwaua baadhi ya Masahaba.

Na kama vile kumpiga kwao vita Amirul-Muumina Ali ambaye ni Bwana wa Mawasii na ndiye kiongozi wa kizazi kitukufu ambaye mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa na cheo cha Harun kwa Musa, (walimpiga vita) katika vita vya Jamal, vita ya Siffin, na vita ya Nah-rawan (yote hayo) kwa sababu ya tamaa duni na dunia yenye kutoweka. Na kama vile kuwaua mabwana wawili wa vijana wa peponi, Imam Hasan kwa kumtilia sumu na Imam Husein kwa kumchinja, haikuwatosha hali hiyo bali walikiandama na kukiuwa kizazi cha Mtume(s.a.w.w) chote, na hakusalimika isipokuwa Ali ibn Husein, na matendo yao mengine yanayomfanya mtu atoe machozi, nami naiepusha kalamu yangu isiyaandike. Masunni wanayajua mengi miongoni mwa hayo na ndiyo maana huwa wanajaribu kwa juhudi zao zote kuwazuiwia Waislamu kusoma vitabu vya historia na kuchunguza maisha ya Masahaba. Niliyoyataja sasa hivi kutoka katika vitabu vya historia miongoni mwa maovu na machafu hapana shaka ni matendo ya Masahaba, basi haiwezekani kwa mtu mwenye akili baada ya kuyasoma haya akaendelea kuwatakasa masahaba na kuhukumu kuwa wao ni waadilifu ila kama atakuwa hana akili. Pamoja na yote tuliyoyayaeleza sisi tunangalia kwa makini mno na, tunauthamini uadilifu wa baadhi ya Masahaba na usafi wao, uchamungu wao na kumpenda" kwao Mwenyezi Mungu na Mtume wake(s.a.w.w) , na msimamo wao zama za Mtume(s.a.w.w) mpaka walipokufa na hawakubadilisha kamwe, basi Mwenyezi Mungu awaridhie na awape makazi karibu na mpenzi wao na Mtume wao Muhammad(s.a.w.w) .

Masahaba hawa ni watukufu na ni bora, hawezi kuifedhehesha heshima yao mfedheheshaji, au akawazulia mwenye kuzua, na kwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu amewasifu mahala pengi ndani ya Kitabu chake kitukufu, kama ambavyo Mtume ameutukuza usuhuba wao na ikhlasi yao si mara moja. Na kama ambavyo historia haikusajili kwao isipokuwa msimamo Mtukufu uliojaa utu, wema, ushujaa, uchamungu na kujinyima (mambo ya dunia) kwa ajili ya dhati ya Mwenyezi Mungu. Basi pongezi ni zao na marejeo yao ni kwenye mabustani ambayo milango yake iko wazi kwa ajili yao na radhi ya Mwenyezi Mungu kwao ni kubwa na hayo ndiyo malipo ya wenye kushukuru, na wenye kushukuru kama kilivyosema Kitabu cha Mwenyezi Mungu. usisahau kuwa ni wachache mno. Ama wale waliojisalimisha na imani haikuingia mioyoni mwao na wakasuhubiana na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) kwa tamaa (ya mambo fulani) na kwa khofu au kwa haja ya nafsi zao, Qur'ani imewalaumu na kuwaonya, naye Mtume(s.a.w.w) amewahadharisha na amewalaani mahala pengi, na historia nayo imeyasajili matendo yao na misimamo yao mibaya. Watu hawa basi, hawastahiki heshima ya aina yoyote wala cheo chochote, achilia mbali kuwatakia radhi (kitu ambacho kinafanya) tuwaweke daraja ya Mtume na Mashahidi na watu wema. Kwa hiyo basi, huu ndiyo msimamo wa haki ambao unapima mizani kwa uadilifu wala hauchupi mipaka aliyoiweka Mwenyezi Mungu kwa waja wake kwamba, wawatawalishe (viongozi) waaminifu na wawapinge (viongozi) waovu na wajitenge nao mbali. Mwenyezi Mungu anasema:"

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ تَوَلَّوْا قَوْمًا غَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مَّا هُم مِّنكُمْ وَلَا مِنْهُمْ وَيَحْلِفُونَ عَلَى الْكَذِبِ وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿١٤﴾ أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُمْ عَذَابًا شَدِيدًا إِنَّهُمْ سَاءَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٥﴾ اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً فَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ فَلَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿١٦﴾ لَّن تُغْنِيَ عَنْهُمْ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُم مِّنَ اللَّـهِ شَيْئًا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١٧﴾ يَوْمَ يَبْعَثُهُمُ اللَّـهُ جَمِيعًا فَيَحْلِفُونَ لَهُ كَمَا يَحْلِفُونَ لَكُمْ وَيَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ عَلَىٰ شَيْءٍ أَلَا إِنَّهُمْ هُمُ الْكَاذِبُونَ ﴿١٨﴾ اسْتَحْوَذَ عَلَيْهِمُ الشَّيْطَانُ فَأَنسَاهُمْ ذِكْرَ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ حِزْبُ الشَّيْطَانِ أَلَا إِنَّ حِزْبَ الشَّيْطَانِ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿١٩﴾ إِنَّ الَّذِينَ يُحَادُّونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ أُولَـٰئِكَ فِي الْأَذَلِّينَ ﴿٢٠﴾ كَتَبَ اللَّـهُ لَأَغْلِبَنَّ أَنَا وَرُسُلِي إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٢١﴾لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَوْ كَانُوا آبَاءَهُمْ أَوْ أَبْنَاءَهُمْ أَوْ إِخْوَانَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ أُولَـٰئِكَ كَتَبَ فِي قُلُوبِهِمُ الْإِيمَانَ وَأَيَّدَهُم بِرُوحٍ مِّنْهُ وَيُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا رَضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ أُولَـٰئِكَ حِزْبُ اللَّـهِ أَلَا إِنَّ حِزْبَ اللَّـهِ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٢٢﴾

Je, huwaoni wale ambao wamewatawalisha watu aliowakasirikia Mwenyezi Mungu? Hao si miongoni mwenu wala si miongoni mwao, na huapa viapo vya uongo na hali wanajua kuwa ni uongo. Mwenyezi Mungu amewaandalia adhabu kali, kwa hakika waliyokuwa wakiyatenda ni mabaya kabisa. Wamefanya viapo vyao kuwa ngao (yao) wakawazuwia (watu) njia ya Mwenyezi Mungu, basi watapata adhabu ifedheheshayo, mali zao na watoto wao hawatawafaa kitu mbele ya Mwenyezi Mungu, hao ndiyo watu wa motoni watakaa humo milele. (Wakumbushe) siku atakayowafufua Mwenyezi Mungu wote wamuapie (viapo vya uongo) kama wanavyoapa kwenu na wanadhani ya kwamba wamepata kitu! Kwa hakika wao ndio waongo kabisa. Shetani amewatawala akawasahaulisha kumkumbuka Mwenyezi Mungu, hao ndiyo kundi la shetani, fahamuni kwamba bila shaka kundi la shetani ndilo lenye kupata hasara. Hakika wale wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake hao ndiyo miongoni mwa watakaodhalilika. Mwenyezi Mungu amekwishaandika yakuwa bila shaka nitashinda Mimi na Mitume wangu, hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye kushinda. Huwezi kuwakuta watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho kuwa wanawapenda wale wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata kama watakuwa ni baba zao au watoto wao au ndugu zao au jamaa zao, hao ndiyo ambao Mwenyezi Mungu ameithibitisha imani nyoyoni mwao na akawatia nguvu kwa roho itokayo kwake, na atawaingiza katika mabustani yapitayo mito ndani yake, humo watakaa daima, Mwenyezi Mungu amewawia radhi na wao wanamridhia, hao ndiyo kundi la Mwenyezi Mungu, Fahamuni! bila shaka kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufaulu, (58:14-22).

Arnesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Nami siachi fursa kuandika katika makusudio haya kwamba, Mashia ndiyo wako kwenye ukweli, kwani wao hawampendi yeyote isipokuwa ni kwa ajili ya Mtume Muhammad na watu wa nyumba yake na Masahaba waliopita kwenye njia ya Mtume na watu wa nyumba yake, na ( hawa Mashia wanawapenda) waumini ambao waliwafuata hao kwa wema mpaka siku ya mwisho. Amma wasiokuwa Mashia miongoni mwa Waislamu wanawapenda Masahaba wote bila kujali wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mara nyingi hutolea ushahidi kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿١٠﴾

"Ewe Mola wetu! tusamehe sisi na ndugu zetu waliotutangulia katika imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kuwafanyia wale walioamini, Ewe Mola wetu! hakika wewe ni mpole mwenye huruma." (Qur'ani, 59:10).

Na kwa ajili hiyo basi utawaona Masunni wanawaombea radhi Ali(a.s) na Muawiyyah bila kujali aliyoyatenda Muawiyah miongoni mwa matendo ambayo yaweza kusemwa ni kufru na upotofu na ni kumpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na nimetaja katika maelezo yaliyopita habari hizo si vibaya kuzirejea kama ifuatavyo: Mtu mmoja miongoni mwa wacha Mungu alizuru kaburi la Sahaba Mtukufu Hujri ibn Adiyyi Al-kindi, akamkuta kaburini hapo mtu fulani analia sana, akamdhania kuwa huyo ni miongoni mwa Mashia akamuuliza; "Kwa nini unalia?" Yule mtu akajibu, "Namlilia Sayyidna Hujri Radhi yallahu anhu. " akasema: "Ni yepi yaliyompata?" Akasema: "Aliuawa na Sayydna Muawiyah Radhiyallahu anhu. " Akamwambia: "Kwa nini alimuuwa?" Akajibu:"Kwa sababu alikataa kumlaani Sayidina Ali Radhiyallahu anhu.

Yule mtu mwema akamwambia yule aliyekuwa akilia: "Nami nakulilia wewe radhi ya Mungu ikufikie." Basi faida gani ya kupokezana huku kwa kuwapenda Masahaba wote mpaka tunawaona Masunni hawamswalii Mtume Muhammad na kizazi chake isipokuwa wataongeza juu yake Masahaba wake wote. Si Qur'an iliyowaamuru kufanya hivyo wala Mtume wa Mwenyezi Mungu hakuwataka kufanya hivyo wala yeyote miongoni mwa Masahaba hakulisema jambo hilo (ilivyo sawa ni kwamba), sala ya Mtume ilikuwa ni kwa Muhammad na kizazi cha Muhammad kama ilivyoshuka Qur'ani na kama alivyoifundisha Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Kama nitakuwa nashaka juu ya kitu fulani, basi sina na sitakuwa nashaka kwamba, Mwenyezi Mungu amewataka waumini kuwapenda Al-Qurba ambao ni watu wa nyumba ya Mtume na akafanya upendo huo kwao kuwa ni faradhi kama ndiyo malipo ya ujumbe wa Mtume Muhammad, akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

قُل لَّا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا إِلَّا الْمَوَدَّةَ فِي الْقُرْبَىٰ ﴿٢٣﴾

"Waambie sikuombeni malipo (yoyote kwa kazi hii ya Utume) isipokuwa muwapende Qaraba (zangu), (Qur'an, 42:23).

Hapana shaka Waislamu wote wameafikiana bila tofauti kati yao juu ya kuwapenda watu wa nyumba ya Mtume(a.s) , lakini Waislamu wametofautiana juu ya kuwapenda wasiokuwa hao, na Mtume(s.a.w.w) amesema: "Wacha lenye kukutia shaka ufanye lisilokutia shaka. " Kauli ya Mashia juu ya kuwapenda watu wa nyumba ya Mtume na wanaowafuata haina shaka, na (amma) kauli ya Masunni juu ya kuwapenda masahaba wote, ina mashaka ndani yake, basi itakuwaje kwa Muislamu awapende maadui wa watu wa nyumba ya Mtume ambao waliwauwa na eti awatakie radhi maadui hao? Je, huu si utata unaochukiza?

Hebu wachana na kauli za watu waliochanganyikiwa na baadhi ya Masufi ambao wanadai kwamba, mtu hawezi kuutakasa moyo wake wala hawezi kuijuwa imani ya kweli mpaka pale itakapokuwa haikubakia moyoni mwake chembe ndogo ya kuwabughudhi waja wa Mwenyezi Mungu wote miongoni mwao wakiwa ni Mayahudi, Wakristo na Walahidi na Washirikina, na (hawa jamaa) wanazo kauli za ajabu zinazoshangaza kuhusiana na jambo hili ambazo zinaambatana na zile za wabashiri miongoni mwa watu wa Kanisa la Kikiristo ambao wanawadanganya watu kuwa "Mwenyezi Mungu ni upendo na dini ni upendo, basi yeyote mwenye kuwapenda viumbe wa Mungu hana haja ya kusali na kufunga na kuhiji na mengineyo." Mambo hayo kwa hakika naapa ni uzushi ambao Qur'ani na Sunna havikubaliani nao wala akili haikubali. Qur'ani inasema: "Huwezi kuwakuta watu wamuaminio Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho wanawapenda watu wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake." Na amesema tena:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا الْيَهُودَ وَالنَّصَارَىٰ أَوْلِيَاءَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿٥١﴾

"Enyi mlioamini msiwafanye Mayahudi na Wakristo kuwa walinzi wa maslahi (yenu), wao kwa wao ni marafiki, basi yeyote atakayewatawalisha miongoni mwenu yeye atakuwa miongoni mwao, bila shaka Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu." (Qur'an, 5:51).

Na amesema tena Mwenyezi Mungu:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا آبَاءَكُمْ وَإِخْوَانَكُمْ أَوْلِيَاءَ إِنِ اسْتَحَبُّوا الْكُفْرَ عَلَى الْإِيمَانِ وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٢٣﴾

"Enyi mlioamini, msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa walinzi wa maslahi yenu ikiwa watauboresha ukafiri kuliko imani, na yeyote miongoni mwenu atakayewafanya kuwa walinzi wa maslahi yake (yote) hao ndio madhalimu." (Qur'an, 9:23).

Na pia amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا عَدُوِّي وَعَدُوَّكُمْ أَوْلِيَاءَ تُلْقُونَ إِلَيْهِم بِالْمَوَدَّةِ وَقَدْ كَفَرُوا بِمَا جَاءَكُم مِّنَ الْحَقِّ... ﴿١﴾

"Enyi mlioamini msiwafanye adui zangu na adui zenu kuwa walinzi wa maslahi yenu na mukawapenda hali yakuwa wameikanusha haki iliyokujieni." (Qur'an, 60:1).

Naye Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) amesema: "Haikamiliki imani ya Muumini mpaka yawe mapenzi yake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na chuki yake iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ." Pia amesema: "Hayakutani ndani ya moyo wa Muumini, mapenzi ya kumpenda Mwenyezi Mungu na mapenzi ya kumpenda adui wa Mwenyezi Mungu ." Hadithi zinazohusu jambo hili ni nyingi mno, na akili yatosha peke yake kuwa ni dalili, kwani Mwenyezi Mungu ameijaza imani (katika nyoyo za) waumini na akaipamba ndani ya nyoyo zao, na akachukia kwao kufru na uovu na uasi, hivyo basi mtu anaweza kumchukia mwanawe au baba yake au nduguye kwa sababu ya kupinga haki na kudumu katika njia ya shetani, na anaweza kumpenda na kumfanya rafiki mtu baki asiye na uhusiano naye isipokuwa udugu wa Kiislamu.

Kutokana na yote haya basi ni wajibu mapenzi yetu na urafiki wetu uwe kwa wale ambao Mwenyezi Mungu ameamrisha tuwapende, kama ambavyo ni wajibu ghadhabu zetu na chuki yetu na kujitenga kwetu kuwe juu ya wale ambao Mwenyezi Mungu ameamrisha tujitenge nao. Na kwa ajili hiyo basi, ndiyo maana tumemtawalisha Ali na Maimamu ambao ni miongoni mwa wanawe bila ya kuwa sisi tunauhusiano nao hapo kabla ya kuwapenda, na kuwapenda wao ni kwa sababu Qur'ani na Sunna na historia na akili hazikuachia nafasi yoyote ya kuwatilia mashaka ya aina yoyote.

Na kwa ajili hiyo pia kujitenga kwetu na Masahaba ambao walipora haki ya Ali katika Ukhalifa, kumekuja bila ya kuwepo uhusiano fulani uliotangulia wa kuwachukia, na hayo ni kwa sababu Qur'ani na Sunna na historia na akili vimetuachia sisi mashaka makubwa kuhusu wao. Na kwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) ametuamrisha kwa kusema: "Acha linalokutia shaka ufanye lisilokutia shaka ." Basi haifai kwa Muislamu kufuata jambo lolote lenye mashaka, akaacha Qur'ani ambayo haina shaka ndani yake. Kama ambayo ni wajibu juu ya kila Muislamu kujikomboa kutoka katika kifungo alichofungwa na kufuata kwake bila kujua bali aipe akili yake maamuzi bila kujali mawazo ya hapo kabla na chuki iliyojificha ndani, kwani nafsi na shetani ni maadui wa hatari wanaompambia mwanaadamu matendo yake mabaya akayaona kuwa mazuri.

Uzuri ulioje wa maneno aliyoyasema Imam Busairi ndani ya Burdah: "Ipinge nafsi na shetani uviasi (viwili hivi), bila shaka nasaha (yao) wanakudanganya, basi wachukie." Ni wajibu juu ya Waislamu kumuogopa Mwenyezi Mungu kuhusu waja wake wema miongoni mwao, ama wale ambao hawakuwa miongoni mwa wachamungu basi hawana heshima yoyote (wanayostahiki) kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Si uteti kuzungumza habari za mtu muovu " ili Waislamu wapate kuyafahamu mambo yake wasije wakadanganyika kwake na wasijempa utawala. Pia Waislamu wanawajibika leo hii wawe wakweli kwa nafsi zao na waangalie hali yao inavyotia uchungu na huzuni na udhalili walio nao, wasitosheke na kujifaharisha kwa sifa za wakubwa zao waliopita, lau kama viongozi wetu waliopita wangekuwa kwenye haki kama tunavyodhania leo hii, basi sisi tusingefikia kwenye matokeo haya ambayo moja kwa moja yamekuja kutokana na kugeuka ambako kulitokea katika Ummah baada ya kufariki kwa Mtume wake. Roho yangu na roho za Walimwengu ziwefidia kwake.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاءَ لِلَّـهِ وَلَوْ عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالْأَقْرَبِينَ إِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقِيرًا فَاللَّـهُ أَوْلَىٰ بِهِمَا فَلَا تَتَّبِعُوا الْهَوَىٰ أَن تَعْدِلُوا وَإِن تَلْوُوا أَوْ تُعْرِضُوا فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ﴿١٣٥﴾

"Enyi mlioamini kuweni wenye kusimamisha uadilifu, wenye kushuhudia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu japokuwa (ushahidi huo) ni dhidi ya nafsi zenu au wazazi wenu na jamaa zenu, akiwa tajiri au masikini, Mwenyezi Mungu anawastahikia zaidi, basi msifuate matamanio mkaacha kufanya uadilifu, na kama mkipotosha (ushahidi) au mkajitenga, basi Mwenyezi Mungu anajua yale mnayoyatenda." (Qur 'an, 4:135).