1
WAJIBU WA VIJANA
VIPI TUFAIDIKE KATIKA KIPINDI CHA UBAROBARO
Hayo yote yaliyotangulia ndiyo mambo muhimu na sifa muhimu zinazompambanua barobaro zikiwemo sifa za machimbuko yaliyo hatari pia. Kwa hivyo, imetubainikia kwamba ni kwa miongozo mema na taratibu zilizo salama tu, ndipo itamkinika kufaidika na hivi vipawa na kuvipatiliza katika kuujenga utu wa Kiislamu unaotakikana ili vijana wetu wawe ni mfano halisi wenye kufanana na maisha ya vijana wa Kiislamu waliopigana jihadi kama Ammar bin Yaasir, Mus'ab bin Umayr, Malik Ashtar na Al bin Husayn al-Akbar. Ikiwa tutawapuuza vijana wetu na kutowajali katika wakati huu ulio hatari au tukawatendea vibaya katika sifa zao na vipawa vyao vya kifikra, huenda tukaonjwa kwa kupata umma mpya uliopotoka na kuharibika. Umma huu mpya utapotosha njia na lengo, na vilevile utaubomoa mustakbali wake mwema.
Swali Ietu hivi sasa ni hili: Ni kwa njia gani tutafaidika na wakati huu wa ubarobaro (uvulana)?
Vipi tutavikuza vipawa vyake na kumpangia nyadhifa kwa ajili ya maslahi yake na kuujenga utu wake, ili aweze kuubeba wajibu wa ujumbe huu wa Kiislamu? Haya ni miongoni mwa yale yatakayomfanya kijana awe ni msingi mwema wenye utendaji katika maendeleo ya kijamii na kuuendeleza mbele ujumbe huu wa Kiislamu.
Hapa napendelea kuelezea kwa kirefu kila kipawa cha kipindi hiki cha uvulana, na kuyaelezea mambo yenye kumpangia wadhifa na kumwongoza kwa ajili ya kujenga viongozi miongoni mwa vijana na umma wa Kiislamu unaokuja. Hapo tutaona vipi tutaweza kufaidika na kila kipawa chake, miongoni mwa hizi sifa tulizozitaja wakati atalelewa na kukua katika maongozi sahihi.
Vikwazo vya Matamanio ni Fursa Nzuri ya Kuimarisha Matakwa Ikiwa vijana wa umma wanamiliki irada (matakwa) na nguvu ya nafsi iliyo thabiti ambayo inashinda matamanio ya nafsi, nia na Irada thabiti yenye kupambana na ghururi, hakika umma utakuwa umetukuka na kupata heshima kuu. Tena umma kama huu utakuwa una uwezo wa kukabiliana na maadui na kupambana na wakoloni. Hautaweza kurukuu na kuyaitikia matakwa ya wakoloni, na hautamnyenyekea dhalimu au kuridhia kuwa watumwa wa wadhalimu na wakoloni. Umma ni muundo wa mkusanyiko wa watu. Ikiwa watu wanaounda umma ni watu waliopondokea kwenye uharibifu na maovu, na ni wenye tabia ya ghururi na shahawa, basi msimamo wa umma na muamala wao kwa maadui zao utakuwa ni baridi na wenye kukubaliana na maovu hayo na dhuluma hiyo. Ama ikiwa watu wanamiliki irada (nia thabiti), nguvu ya nafsi na uwezo wa kupambana na vikwazo, hakika umma ukishikana na vijana wake unaweza kukabiliana, kupinga na kusimama kwa ushujaa dhidi ya tamaa za maadui na njama za madhalimu na wakoloni. Wakati huu wa uvulana ni fursa nzuri yenye thamani ya kuikuza irada (matakwa) ya mtu katika umma. Sababu ni kwamba irada ya binadamu haipati nguvu mara moja kwa kuipa mawaidha au kuipa miongozo, bali hupata nguvu kwa kupitia ukinzani na kwa kupambana na ghururi na vikwazo vya kila aina.
Kwa mfano, mtu ambaye ataikuta nafsi yake imezingirwa na mambo yenye udanganyifu na hadaa zenye nguvu, tena ikawa nafsi imebanwa katika vikwazo vyenye shahawa kali, yamkinika kwake kuilelea nafsi yake kwa matendo, kwa kuwa mgumu wa kutoyatii matamanio yake, aikuze kwa kuiviza irada yake kwa majaribio ya kimatendo. Mtu kama huyu anaweza kupata ushindi, hasa pale atakapoitukuza nafsi yake na kuzidharau zile ghururi na shahawa na aikanye nafsi yake kuvinyenyekea vikwazo vya matamanio. Vivyo hivyo, kipindi hiki cha ujana kwa vijana ni kipindi cha kuipa mazoezi irada na kuifanyia majaribio nafsi yake. Kijana akipata miongozo iliyo salama na kupata mafunzo (elimu) sahihi yaliyojaa ubinadamu katika malezi yaliyo mema, ataweza kuyapita majaribio haya kwa ushindi mkubwa, na baada ya mtihani huu atakuwa mwenye irada yenye nguvu na ushujaa. Hakika mara nyingi mabarobaro husumbuliwa na hisia kali za matamanio nafsini mwao, vilevile hupambana na ghururi (hadazi) za aina mbalimbali zenye nguvu, lakini huweza kupata ushindi upesi hasa anapoweza kuitawala nafsi yake, kuuhifadhi utu wake na heshima yake, akaweza kupambana na hadazi zote na akaweza kujiepusha na vitimbi vikubwa vya matamanio yenye kiwi, hasa katika hizi jamii zetu kunakopatikana kwa wingi upondokeaji kwenye uharibifu na ufisadi. Barobaro akiweza kuyashinda hayo yote, yamaanisha kwamba ameimiliki irada yake iliyo thabiti na amemiliki nafsi yenye kutoteteleka. Wakati ambapo umma utamiliki watu pamoja na vijana wa namna hi basi hapo utaweza kuwa na matumaini ya kuwa na mustakbali mwema. Riwaya na hadithi tukufu zilizopokewa katika mafunzo matukufu ya Qur'ani zimeelezea kwamba barobaro anayo sifa tukufu ya kuyapa nyongo mambo yenye ghururi na ya haramu kwa kutubu, kwani toba inadhihirisha kujihifadhi kwake na kulingana kwake.
Mtume Mtukufu amesema: "Toba ni nzuri, na kwa barobaro ni nzuri zaidi.
"
Pia imepokewa kwake kuwa amesema: "Hakuna kitu kizuri kinachopendeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko kumwona barobaro mwenye kutubu.
" Ni kwa nini kitendo hiki kinamfurahisha Mwenyezi Mungu? Sababu ni kwamba barobaro anapojiondoa kwenye maasi na kuyadhibiti matamanio yake huwa amefanya ukinzani mkubwa dhidi ya nafsi yake, vilevile huwa anailelea nafsi yake juu ya misingi ya kupania, kukakamia na kushikamana na imani yake. Tunapoidurusu historia ya viongozi wakubwa wa historia ya binadamu, tunakuta kwamba aghlabu yao walikuwa na jitihada ya hali ya juu sana wakati wa ujana wao katika kuzijenga nafsi zao na kuzielekeza kwenye maongozi matukufu yenye utu na ukamilifu. Na sababu ni kwamba wao walishikamana na mkondo wa matukufu na kulazimiana nayo, na wakakataa kupomoka kwenye lindi Ia matamanio na upotevu wenye kutenganisha na haki, pamoja na kwamba kulikuweko hali zenye kusaidia kuwavuta kwenye matamanio na kuzama zaidi kwenye mambo ya ufisadi. Hebu tujionee baadhi ya kumbukumbu za maisha ya baadhi ya viongozi wakuu ambao wamefaidika kwa kuziviza irada zao katika wakati wa ujana wao, wakazipa nguvu nafsi zao kwa kukakamia kujiepusha na shahawa za nafsi. Kutokana na kufuata njia hii, walizipa nafsi zao nafasi ya kwanza ya kuyavaa matukufu na kuvikwea vilele vya matukufu na ukamilifu.
1. Hebu tuitazame historia ya Nabii wa Mwenyezi Mungu, Yusuf bin Yaakub AS akiwa ameyakosa malezi ya wazazi wake pamoja na huruma yao tokea udogoni mwake baada ya kumpoteza mama yake, ndugu zake walimlia njama na kumtupa kisimani, kisha akanunuliwa na mmoja wa misafara ya Misri kwa thamani ya chini ya dirhamu chache.
Tazama ndugu msomaji, majaaliwa yalitaka aishi katika zama zake za ubarobaro ndani mwa nyumba ya Mfalme wa Misri pamoja na mkewe Zulaikha ambaye alivutwa vilivyo na uzuri wa Nabii Yusuf AS uliojulikana na uliokuwa ukipigiwa mfano. Ashiki ya kumpenda Yusuf ikavama moyoni mwa Zulaikha, na nyumba walimokuwa wakiishi haikuwa na yeyote mwenye kutia zahama, na hali haikuwa na pingamizi yoyote ya kuzuia kutekeleza hila za kishetani. Hebu sawirisha ewe kijana uliye barobaro, kuwa wewe umeingia kwenye mtego wa Nabli Yusuf AS. Pia chukulia kuwa uko katika mazingira yanayosaidia kupotoka, Je, ungefanya nini? Na wajibu wako ungekuwa ni nini katika hali kama hii? Naam, ukweli ni kwamba wengi wa barobaro wetu wa sasa, mara nyingi wanatatizwa na ghururi zilezile ambazo zilimtatiza huyu barobaro mtukufu Yusuf, vilevile wanaishi katika mazingara sampuli ileile aliyoishi.
Kwa hivyo, ni juu ya vijana wetu kumfanya Nabii Yusuf AS kuwa ni kiongozi wao na kugizo chao, wamwige katika kupambana kwake na ghururi kama zile katika kukabiliana kwake na hali kama zile. Hebu tutazame msimamo wake ulikuwa namna gani? Qur'ani Tukufu yatusimulia kwa ufasaha mkubwa ikitumia njia yake ya kimbinguni. Yatutolea baadhi ya visa vinavyoelezea baadhi ya ile mikasa hatari aliyoipata Nabii Yusuf
katika nyumba ya Mfalme wa Misri, pamoja na tukio Ia kurukiwa na Zulaikha. Mwenyezi Mungu asema: "Na akasema yule aliyemnunua huko Misri kumwambia mkewe: 'Mweke pahali pazuri huenda akatufaa au tukamfanya mwana. 'Na hivi ndivyo tulivyommakinisha Yusuf katika ardhi (nchi,) ili tumfundishe taawili (ufafanuzi) za hadithi na Mwenyezi Mungu ni Mshindi juu ya jambo Lake lakini watu wengi hawajui. Na alipofikia ukamilifu wake tukampa hukumu na elimu na vivi hivi huwalipa wonaofanya wema. Na akamtaka [Yusuf kutenda haramu] yule [Zulaikha] ambaye yeye yuko nyumbani kwake nafsi yake, na akafunga milango [ili asikimbie] na akasema: 'Ni toyari njoo [nimejitayarisho kwa ajili yako].' Akasema [Yusuf]: 'Namwogopa Mwenyezi Mungu, Yeye ni Mlezi wangu, ameyafanya mazuri makao yangu. Hakika madhalimu hawafuzu.' " (12:21-23) Qur'ani inaendelea kuyafafanua baadhi ya maelezo ya kisa chenyewe kutokana na umuhimu wake hadi pale ilipomdondoa Zulaikha akisema: Hakika nilimtaka nafsi yake akajizuia (akakataa) na ikiwa hatafanya ninayomwamuru, atafungwa na atakuwa katika wanyonge.' Akasema [Yusuf]: 'Mola wangu, jela ni boro zaidi kwangu kuliko yale wonayoniita kuyafanya, na ikiwa hutaniepusha na vitimbi vyao, nitapondokea kwao na nitakuwa miongoni mwa wajinga.' Basi Mola wake akamjibu, akamwepushia vitimbi vyao; hakika Yeye ni Mwenye kusikia na ni Mjuzi." (12:32-34)
Vivi hivi Yusuf alimwomba Mwenyezi Mungu amsaidie katika kupambana na ghururi za matamanio na hali za upotofu. Naye Mwenyezi Mungu akayajibu maombi yake, na Nabii Yusuf akazishinda zile hali zote za uharibifu na ufisadi ingawa alistahamilia maovu na kwa muda mrefu alibaki jela kwa azma, nia thabiti na nafsi yenye ushujaa. Na hivi ndivyo inavyotakikana kijana mwema awe.
2. Kuna kisa kingine chenye kuvutia na kustaajabisha kama kinachoelezwa katika historia. Kisa chenyewe kinamhusu Sayyid Mir Damad, aliyekuwa mwanachuoni mashuhuri sana nchini Iran. Yaelezewa kwamba Sayyid huyu alifikiwa na kisa hiki wakati akiwa kijana mbichi mwanzo wa kubalehe kwake, naye alikuwa ni mwanafunzi katika madrasa moja ya kidini katika jiji Ia Tehran. Katika usiku mmoja wakati binti wa Shah wa Iran katika zama hizo alipokuwa akitembea mitaani pamoja na vijakazi na watumishi wake, kwa ghafla kukanyesha mvua kubwa na kukavuma upepo mkali na kila mmoja miongoni mwa watumishi wa binti wa Shah akakimbia kutafuta mahali pa kujificha kibinafsi. Binti wa Shah akabakia peke yake mitaani katika lile janga Ienye kutisha na kuhofisha, ikawa naye hana budi kutafuta pahali pa kujificha. Katika kutazamatazama kwake huku na huko iIi angaa naye apate pahali pa kujificha na kujistiri, akauona mlango wa madrasa uko wazi, akaingia madrasani. Kwa bahati akagonga mlango wa chumba cha huyu Sayyid kijana na akamkuta yuko kando ya moto akijiota ili ajiondoshee baridi aliyokuwa nayo.
Binti huyu akamwelezea huyu Sayyid kijana kisa chake, kwamba yeye ni msichana aliyepotea njia na anachohitaji ni msaada, pahali pa kulala na kujistiri usiku ule, hadi hali ya anga iwe tulivu na ipambazuke. Sayyid aliona hana budi kulijibu ombi lile Ia msichana, hivyo akamkaribisha chumbani mwake, yeye akakaa katika kipembe kimoja na msichana naye akakaa katika kipembe kingine. Baada ya kupita muda katika usiku huo, shetani akaanza kucheza mchezo wake mwovu katika hali kama hii, kama ilivyopokewa katika hadithi ikisema: "Mwanamume hakai faragha na mwanamke ila shetani anakuwa wa tatu wao." Shetani akawa anamshawishi Sayyid huyo kijana namna ya kuipatiliza hii fursa na kutenda haramu kwamba mambo yote yako sawa kwa kila njia, mlango umefungwa, wala msichana hana njia yoyote na kujikinga au kujitetea.
Lakini vipi itakuwa? Kwani Sayyid huyo alikuwa ni kijana mwema na mwongofu, anayetambua hila na vitimbi vya Shetani. Akawa anafikiria njia ya kujiepusha kutokana na makucha haya ya shahawa na mtego huu wa Shetani. Mwishowe akafikia kwenye uamuzi mgumu. Akaamua kuitumia njia hii kwa ajili ya kupambana na shahawa zake na kuutatua wasiwasi wa shetani. Uamuzi wenyewe ukawa ni kuweka kidole chake juu ya kaa Ia moto, hadi ashughulishwe na uchungu wa kuchomeka ili asifikirie mambo ya haramu. Naam, aliendelea kujichoma hivihivi usiku kucha, huku akistahmilia uchungu na maumivu na huku akiihutubia nafsi yake: "Onja moto wa dunia ili uuogope moto wa Akhera!"
3. Je, ndugu! Vijana wamewahi kukisikia kisa cha lbn Siriin ambaye alikuwa mwanachuoni mkubwa wa elimu ya nafsi na aliyejulikana kwa kufasiri ndoto? Katika wakati wa ubarobaro wake Ibn Siriin alikuwa mwenye umbo jema, kiwiliwili kizuri, mwenye uso mwangavu na uzuri wa kitabia wenye kuvutia. Alikuwa akifanya kazi kwa mfanya biashara mmoja wa nguo. Siku moja alifika mwanamke dukani kununua vitambaa, alipomaliza kununua mahitaji yake, akamtaka yule mfanya biashara amtume mfanyakazi wake Ibn Siriin ili ambebee mizigo yake aliyonunua hadi nyumbani kwake, kisha ampe ujira. Ibn Siriin akabeba mizigo na kuandamana naye hadi nyumbani, walipoingia nyumbani mwanamke huyo akafunga milango, kisha akamtaka afanye naye kitendo cha haramu, lakini yeye akakataa. Mwanamke alipoona amekataliwa akazidi kutumia hila za kumlazimisha zaidi. Mwisho Ibn Siriin alijiona kuwa ametumbukia mtegoni, na hapana budi kufikiria njia ya kujisalimisha kutokana na mtego huo Alipoigundua hila yenyewe alimwomba huyo mwanamke amruhusu aende chooni kujisaidia. Mwanamke akamruhusu kufanya hivyo, naye alipoingia chooni tu alijipaka mavi mwili mzima, kisha akamtokea mwanamke yule akiwa katika hali kama hii ya kunuka. Mwanamke alipomwona katika hali kama ile, akamkimbia na kumfukuza nyumbani. Na kutokana na hila kama hii lbn Siriin alijiokoa kutoka mtego huu wa matamanio yaliyo na ghururi.
Wajibu wa Vijana katika Jamii Vipawa vingi vya binadamu huchimbuka katika wakati huu wa ujana. Huwa na ukunjufu wa wakati na nafsi. Vilevile huwa anamiliki nguvu, uwezo na nishati. Hivi vyote vinampa nafasi nzuri na kumshajiisha kuwa na wadhifa maalum katika jamii. Hapo mbeleni tuliwahi kuelezea juu ya matakwa ya kijana yenye kiwi ya kutaka kutekelezwa, na kupenda kwake kushiriki katika nyadhifa mbalimbali ili ahisi kwamba yuko huru na awathibitishie wengine uwezo wake na uume wake baada ya kuwa alikuwa mdogo akiishi katika hali ya kuwanyenyekea wengine na kupondokea kwenye matakwa yao. Baada ya kuwa alikuwa akitendewa kama mtoto mdogo, sasa ataka atendewe na jamii kama mtu mkubwa, mwenye heshima yake kamili na mwenye matakwa na irada.
Lau twampa nafasi kijana na kumuacha kutekeleza nyadhifa na wajibu anazoziweza katika jamii, na tukamwelekeza kufanya mambo mema Yenye faida na kumsaidia kuujenga utu wake na kuvikuza vipawa vyake, hakika tutakuwa tumefanya wema kwa kuyajua na kuya pambanua yale yanayoweza kumdanganya katika wakati wa ubarobaro. Na ikiwa hatutashughulika na masiala haya na ikawa hatutampa nafasi barobaro kutoa maoni yake na kutekeleza matakwa yake katika nyadhifa za kijamii kupitia maongozi mema, basi natija itakuwa moja kati ya mambo mawili: Ima vipawa vya barobaro vitafifia, na vitazimika au vitakufa na matumaini yake yatazikika, au atajiingiza katika kutekeleza mambo yaliyopotoka na kufanya mambo maovu ya ufisadi. Na huu ndio mushkili unaoutatiza umma wetu wa Kiislamu. Jamli nyingi hazijajua vipi zishirikiane na vijana wao katika upande huu. Wazee wengi pamoja na viongozi wale wanaoyatawalia mambo ya wananchi na kushikilia hatamu za uongozi, aghlabu yao hawako tayari kuwapa vijana wao fursa ya kutumia ujuzi wao na vipawa vyao, hawawapi nafasi yoyote ya kusimamia jambo lolote la kijamii, na hawawaamini, bali huwazingatia kuwa ni watoto wasiojua kitu na walio dhaifu. Kutokana na sababu hii vijana wetu hukua huku wakiwa na juhudi chache sana na maarifa yao huwa ni ya daraja Ia chini. Hivyo, hupotoka na kuiacha njia ya utukufu yenye utengevu, hasa wanapochukuliwa na makundi mengine ya upotevu na kupewa nyanja za kuziamini nafsi zao na kupewa nyadhifa za kujishughulisha na mambo muhimu yaliyo hatari.
Kitabia, utamwona kijana akivutika kwa urahisi na kujiingiza katika lile kundi ambalo linashughulikia vyema na kumthamini kama mtu mwenye nguvu. Na utamwona mara moja anawaacha wale watu ambao wanaoshughulikiana naye kama mtoto mdogo au kijana dhaifu. Tunasikitishwa sana kuona ya kwamba jamii yetu hadi sasa haijaacha kuwapima watu na kuwapa kima (hadhi na heshima) kupitia kipimo cha umri. Imekuwa kwamba kabla kijana hajakata masafa marefu ya umri, basi jamii ya watu wakubwa hawamwangalii kwa jicho Ia uaminifu na heshima, wala hawampi nafasi ya kutaharaki au kuwa na nishati yoyote.
Mtukufu Mtume ameitangaza wazi rai ya dini ya Kiislamu na akaelezea waziwazi juu ya kukataa kwake kipimo cha umri na miaka, na akafafanua kwamba kipimo cha pekee kilicho sahihi ni kipimo cha ujuzi na matendo, na kwamba kijana mwenye ujuzi na matendo anayestahili na ni bora zaidi na anayo haki ya kutangulizwa kuliko mwingine yeyote. Mtume Mtukufu alimtawalisha Ittaab bin Usaid mjini Makka, juu ya kuwa umri wake wakati huo ulikuwa ni miaka Ishirini na moja. Akamwamuru kusalisha sala ya jamaa na kusimamia shughuli nyinginezo kwa niaba ya Mtume Mtukufu. Kijana huyo alikuwa ni amiri wa kwanza kusalisha jamaa mjini Makka baada ya kukombolewa mji huo. Mtume Mtukufu alimwambia: "Ewe Ittaab! Unajua nimekutanguliza kwa watu gani? Nimekutanguliza na kukufanya mwakilishi wangu kwa watu (waja) wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na lau ningekuwa namjua aliye mbora zaidi kukushinda wewe ningemteua." Baadhi ya wakaazi wa Makka walipopinga uteuzi huo, Mtume Mtukufu alisema: "Mtu asihoji kwa hoja ya udogo wa umri wake, kwani ukubwa si ubora, bali ubora ndio ukubwa." (Jawaan, Sheikh Muhammad Taqi Falsafi; uk. 30).
Vilevile taaluma za Kiislamu zinashajiisha kuvikunjulia vipawa hivi vya vijana chipukizl ili vivie na kuendelea. Kwa mfano, utaona katika vitabu vya fiqihi kuna masiala ambayo yanaruhusu vijana wasiobalighi bado kuwaongoza vijana wenzao katika sala ya jamaa; na hii ni kwa sababu ya kumpa kijana moyo na kumshajiisha ili akulie na hisia ya kuiamini nafsi yake, kwani vijana wanapoona kuwa wana sala yao ya jamaa, watatambua kwamba wamethaminiwa na kwamba wao pia wanaweza kuwa viongozi kama walivyo watu wazima. Wakati tunaposoma sera za viongozi wa Kiislamu na historia ya maisha yao, tunaona wazi kwamba wao wanaamiliana na vijana muamala wa kuwashajiisha na kuwaheshimu. Vilevile huwapa heshima kubwa wale vijana walio na ujuzi, na mara nyingine huwatwisha majukumu mazito zaidi na ya hatari. Angalia jinsi Mtume wetu Muhammad(s.a.w.w)
alivyomchagua Musa'b bin Umair, yule kijana mwenye imani na mpiganaji jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, awe balozi wake mjini Madina, ili auongoze umma wa huko katika njia ya Uislamu, autayarishe mji wa Yathrib kuwa makao ya machimbuko ya Uislamu na makao makuu ya serikali yake changa. Mus'ab alifika mjini Madina akiikuta katika hali nzito kutokana na tofauti iliyokuwepo baina ya makabila ya Aws na Khazraj. Akiwa amebeba ule wajibu mkubwa kuiongoza Madina, Mwenyezi Mungu amemwafikia kufaulu katika kutekeleza wajibu huo kutokana na imani yake ya kweli, ikhlasi aliyovama moyoni na jihadi yake thabiti.
Katika tukio jingine lenye kuthibitisha hakika kama hii katika uhai wake wa mwisho, Mtume Mtukufu aliandaa jeshi kubwa Ia kupigana na Warumi mkiwemo ndani mwake masahaba wakubwa na wazee wa Kiislamu. Uongozi wa jeshi hilo katika vita hivyo alipewa Usama bin Zaid ambaye alikuwa ni kijana asiyefikia hata umri wa miaka ishirini. Na wengine waliokuwemo katika jeshi hilo lenye kunyenyekea uongozi na amri za Usama walikuwa ni Abubakr, Umar na Abu Ubaida ibn Jarraah, Abdul Rahman bin Auf, Talha, Zubair, n.k. Baadhi ya masahaba waliudhika kutokana na uamuzi huo wa Mtume Mtukufu wa kumtanguliza Usama bin Zaid juu yao kutokana na umri wake mdogo, habari hiyo ikamfikia Mtume Mtukufu, naye akaghadhibishwa sana na kitendo hicho cha kumthamini mtu kulingana na kipimo cha umri ambacho kilikuwa kikitumiwa wakati wa Ujahilia. Kitendo hicho kilimfanya Mtume Mtukufu kutoka na kwenda msikitini kuwahutubia watu, juu ya kuwa na shida ya maradhi aliyokuwa nayo na kuumwa kwake. Miongoni mwa yale aliyoyasema katika hotuba yake siku hiyo ni: "Enyi watu! Ni nini haya maneno yaliyonifikia yaliyosemwa na baadhi yenu kwa sababu ya kumtanguliza kwangu Usama? Ikiwa mwapinga kumtanguliza kwangu Usama, hakika mlitangulia kuupinga (uamuzi wangu wa) kumtanguliza baba yake hapo mbeleni. Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba baba yake alikuwa anastahiki uongozi, na hakika mwanawe baada yake naye anastahiki uongozi pia." (an-Nass wal ljtihad, uk. 9).
Naye Imam Jaafar Sadiq
alimkuta kijana Hisham bin Hakam kuwa na vipawa vikubwa na akawa akimdhihirishia mapenzi na heshima yake juu yake kwa kiasi kikubwa mpaka wazee wakaingiwa na wivu mioyoni mwao. Katika kitabu cha Safinatul Bihar imeelezwa kwamba heshima na cheo cha Hisham bin Hakam vimefikilia daraja Ia juu kabisa mbele ya Abu Abdillah Jaafar bin Muhammad Sadiq AS na kwamba Hisham alifika kwa Imam katika Mina, wakati alipokuwa anaanza kubalehe. Katika kikao hicho cha Imam walikuwepo baadhi ya masahaba zake wazee kama Hamraan bin Aayun, Qais al-Maasir, Yunus bin Ya'kub, Abi Jaafar al-Ahwal na wengineo, na Imam akampa Hisham heshima kubwa kushinda wazee wote waliokuwepo hapo. Abu Abdillah alipoona kwamba kitendo hicho kilikuwa kikubwa mbele ya masahaba wake, alisema: "Kijana huyu ametunusuru kwa ulimi wake, moyo wake na mikono yake." (jz. 2, uk. 719) Kauli ya mwisho juu ya maelezo haya yatakikana ifahamike kwamba haiwezikani kabisa kumwacha au kumtenga barobaro huku tukivipuuza vipawa vyake. Haimkiniki kumtupa na kumwacha abakie akiwa hana thamani yoyote au atenganishwe na maisha ya umma. Hakika yatakikana athaminiwe na aheshimiwe na apewe wajibu muhimu azitekeleze na vilevile aongozwe iIi aujenge utu wake. Bila shaka, ikiwa sisi tutamshajiisha na kumpa miongozo yenye kufaa, tutafaidika naye; na hayo yatakuwa ni matayarisho muhimu ambayo yatamjenga na kumfanya awe chimbuko jema lililo muhimu katika siku zijazo. Na ikiwa tutampuuza na kudharau rai zake na uwezo Wake na hatutompa nafasi ya kushughulika na jambo lolote au kumshajiisha na kumtia nishati na kumwongoza katika njia sahihi, tujuwe wazi kwamba atatekwa na wengine na kufaidiwa na wengine, na watamtayarisha kulingana na taratibu zao na miongozi yao miovu yenye kupoteza na kupotosha.
Majaribio mengi yamethibitisha kwamba kijana anapopewa nyadhifa au shughuli za kijamii kuziendesha au kusimamia wajibu wa kidini, huwa yuko tayari kutoa juhudi zake zote kuushughulikia umma wake, tena hushikamana zaidi na kulazimiana zaidi na dini. Ama kule kuwahimiza vijana kusali na kufunga na kuwahimiza kusikiliza hotuba na mihadhara pekee hakutoshelezi hata kidogo kudhamini utengevu wa vijana hao wala uongofu wao, wala hakutoshelezi kuyalelea maadili yao na vipawa vyao. Ni wajibu ulioko juu yetu kuwapa nidhamu na mipango yenye kuwataharakisha na kuwapa nishati. Nidhamu hizo ziwe nzuri ili ziweze kuwatambulisha umuhimu wao katika jamii. Miongoni mwa mambo yanayotia uchungu moyoni ni upinzani unaotoka kwa jamii kuwapinga vijana waumini, au kikundi chema kilichojitolea kusimamia na kutekeleza nishati muhimu za kijamii au za kidini.
Umma huwawekea tuhuma na shaka na huwapinga. Mara ngapi tunayashuhudia makundi ya vijana wema wenye nia safi kwa umma wao, vijana walio na hamasa kwa ddini yao, wanaotaka kusimamia jambo la kidini au la kijamii, au kuunda kamati za maendeleo ya kidini na kijamii, lakini kwa masikitiko utaona jamii hufanya ubahili katika kuwashajiisha na kuwatia moyo. Utaona hawawashajiishi hata kidogo, bali huzuia misaada yao katika pande zote na mara nyingine huwapinga na huwawekea vikwazo. Kwa nini? Je, ni kwa kuwa baba zetu na viongozi wa jamii hawajui tabia ya kipindi hiki cha ujana, wala hawajatambua hatari yake? Au ni kwa kuwa hao wazazi na viongozi hawataki kuwaruhusu vijana washirikiane nao katika kuyaongoza mambo ya kijamii kwa lengo la kuiendeleza hadhi yake? Basi ni kwa sababu gani? Hakika kufanya hivyo ni hiana na makosa makubwa.