1
HIKAYA ZA B A H L U L MWENYE BUSARA
(5). BAHLUL NA FAQIHI
Faqihi mashuhuri kutoka Khurasan alifika Baghdad, alialikwa na Harun Rashid katika Baraza lake na akimkalisha ubavuni mwake. Wakati alipokuwa akizungumza na Harun, alitokezea Bahlul ambaye naye alikaribishwa aketi karibu nao. Huyo mtu alimwona Bahlul yu kama mwehu na hivyo alimwambia Harun: "Nimestaajabishwa na heshima na mapenzi yako Khalifa, kwa kuwa unawastahi hata watu waliwehuka hadi kuwakaribisha karibu nawe?" Alipoyasikia hayo Bahlul, alielewa kuwa alikuwa akisemwa yeye tu na hapo akajikaza akamwambia: "Kwa nini waringia ilimu yako hiyo kidogo, usinidharau kwa udhahiri wangu bali jitayarishe kwa mabishano ili nami nimdhihirishie Khalifa kuwa wewe haujui lolote!" "Mimi nimesikia kuwa wewe u - mwehu na hivyo siwezi kubishana na wehu!" Aliyasema huyo Faqihi. Hapo Bahlul alimjibu akiwa ameghadhabika, "Mimi ninaukubalia uwehu wangu lakini wewe unakataa kuukubalia ujahili wako na kutokuwa na ilimu kamili." Harun alipoyasikia hayo, alijaribu kumtuliza Bahlul, lakini ilishindikana huku akidai kuingia mabishano na huyo Faqihi, iwapo anajiamini kwa ilimu kamili."
Basi Harun alimgeukia huyo Faqihi na kumwambia: "Je kuna kipingamizi gani katika kumwuuliza maswali?" Hapo huyo Faqihi alijibu: "Mimi nipo tayari kubishana naye iwapo atakubaliana na shuruti langu moja nalo ni, iwapo ataweza kunijibu basi nitampa Dinar elfu moja za dhahabu na akishindwa itambidi anilipe hivyo." Bahlul alimjibu: "Kwa kweli mimi huwa sina mali za kidunia na wala sina Dinar wala dhahabu, lakini nipo tayari kuwa mtumwa wake iwapo nitashindwa kumjibu, na iwapo nitamjibu basi nipatiwe hizo Dinar elfu moja za dhahabu ambazo nitazigawa miongoni mwa mafukara." Kwa hayo, huyo mtu alianza kumuuliza swali hivi: "Katika nyumba moja yupo mwanamke aliyeketi na mume wake halali kisheria na humo humo wapo watu wawili ambao mmoja wao anasali na mwingine yupo katika hali ya saumu. Ghafla anatokezea mtu kutokea nje na kuingia ndani ya nyumba hiyo. Kutokezea huku kwa mtu huyo, wale bibi na bwana wanakuwa haramu baina yao na sala na saumu za wale wawili zinakuwa batili. Je unaweza kuniambia huyo mtu aliyotokezea ni nani?" Bahlul bila ya kusita anamjibu: "Huyo mtu aliyeingia nyumbani kwa ghafla alikuwa ndiye bwana wa kwanza wa yule bibi kwani alikwenda safari na baada ya muda mrefu kupita, ilijulikana kuwa amefariki na hivyo huyo mwanamke akaolewa na bwana wa pili (aliyekuwa nyumbani) baada ya kupokea idhini ya hakimu sharia. Wale watu wawili walikuwa wamelipwa kwa ajili ya kusali na kufunga saumu zilizo za qadhaa za bwana wake aliyesadikiwa amekufa safarini.
Na kurejea kwake kutoka safari ndefu aliyosadikiwa amekufa, imebatilisha ndoa ya mke wake na yule bwana kwani yu hai bado, vile vile saumu na sala pia zinabatilika kwani kumsalia mtu aliye hai pia ni batili." Kwa hayo, Harun na wanabaraza wake wote walivutiwa na majibu ya Bahlul na walimsifu sana. Baada ya hapo, ilikuwa ni zamu ya Bahlul kuuliza swali: "Je niulize?" " Uliza tu!" alijibiwa. Bahlul aliuliza: "Iwapo ninayo kasiki moja ya siki (vinegar) na nyingine ya urojo wa sukari, na kwa ajili ya kutengeneza Sikanjabin (kinywaji cha Siki) nimeweka ili kuchanganya katika kasiki ya tatu na hapo tunakuja kumkuta panya amefia humo. Je unaweza kutuambia kuwa huyo panya alitokea kasiki ya Siki au Urojo wa Sukari? Hapo huyo mtu alijaribu kwa uwezo wake wote kumjibu Bahlul, lakini alishindwa. Kwa kuona hali hiyo, Harun alimwambia Bahlul "sasa wewe mwenyewe tujibu hayo." Bahlul alimwambia Harun: "Nitafanya hivyo iwapo huyu mtu atakiri kutoelewa majibu yake." Kwa masikitiko na aibu kubwa huyo Faqihi alikubali kushindwa kwake kwa kuling'amua hilo fumbo. Alianza Bahlul kulijibu: "itabidi sisi kumtoa huyo panya na kumwosha vizuri kwa maji safi halafu tupasue tumbo lake na humo iwapo tutakuta siki au urojo wa sukari, basi itatubidi tumwage kile kitakachothibitika kuwamo tumboni mwake." Wote waliokuwa wamehudhuria, walifurahishwa mno na majibu ya Bahlul na Faqihi alilazimika kutoa Dinar elfu moja za dhahabu ambazo Bahlul alizigawa miongoni mwa mafuqara wa Baghdad.
(6). BAHLUL NA MTUMWA ALIYEOGOPA MAJI
Mfanya biashara mmoja alikuwa akisafiri katika jahazi pamoja na mtumwa wake kuelekea Basrah. Kwa bahati na Bahlul alikuwamo humo pamoja na watu wengineo. Mtumwa huyo alianza kulia palipotokea machafuko hapo majini. Wasafiri wote walikerwa na sauti za kilio cha mtumwa huyo. Hapo Bahlul alimwomba ruhusa mfanyabiashara huyo ili atumie mbinu za kuweza kumkomesha mtumwa huyo, basi bila ya pingamizi alipewa ruhusa. Na hapo Bahlul alitoa amri ya kutupwa majini kwa utumwa na ilitekelezwa hivyo. Alipofikia wakati wa kutaka kufa, alitolewa nje. Baada ya kutolewa nje, mtumwa huyo aliketi kimya akitulia katika kona moja ya jahazi. Hapo baadaye, Bahlul alielezea: "Huyu mtumwa alikuwa haelewi raha na usalama wa jahazi inapokuwa majini. Pale alipotupwa majini ndipo alipotambua kuwa jahazi ni mahala pa raha na usalama."
Fundisho: Amesema mtume(s.a.w.w)
: "Safirini na mutajitajirisha (kwa uzoefu na uelewano).
"
(7). SWALI KUTOKA HARUN
Siku moja Harun alikuwa katika Qasri yake akiangalia mandhari iliyokuwa ikimzunguka na sauti ya mbubujiko wa maji ya mto Tegris. Na mara hapo akatokezea Bahlul, na Harun alimwambia Bahlul: "Ewe Bahlul! leo hii nakuuliza fumbo, iwapo utafumbua vyema basi nitakupa dinar elfu moja na iwapo utashindwa basi nitatoa amri ya kukutosa majini." Bahlul alimwambia Harun: "Mimi sihitaji dinar hizo, bali ninakubali kwa sharti moja." Na alipokubali Harun, Bahlul alisema: "Iwapo nitaweza kulijibu vyema basi itakubidi kuwaachia marafiki zangu mia moja - kutoka Gereza lako, na iwapo nitashindwa basi unao uhuru wa kunitupa majini."
Alianza Harun kulielezea fumbo lake: "Iwapo mimi ninayo mbuzi mmoja, mbwamwitu, na fungu la majani.Je nitawezaje kuvivusha vyote hivyo, kwamba majani hayataliwa na mbuzi na wala mbuzi kuvamiwa na mbwamwitu?" Bahlul alianza kumjibu: "Kwanza utamvusha mbuzi kwenda ng'ambo ukimwacha mbwa mwitu na majani. Baadaye utachukuwa majani uyavushe huku ukirudi na mbuzi upande huu. Utamwacha mbuzi upande huu na utamchukua mbwamwitu ng'ambo.Mwishoni utampeleka mbuzi. Kwa hivi majani hayataliwa na mbuzi wala mbuzi kuvamiwa na mbwamwitu." Harun alifurahishwa mno kwa majibu ya Bahlul. Na hapo Bahlul alimpa orodha ya majini mia moja ya wafuasi na wapenzi wa Ali bin Abi Talib
. Lakini Harun alimgeuka Bahlul. Lakini Bahlul aliendelea kusisitiza, na hatimaye aliwaacha huru watu kumi tu na akimwamwuru Bahlul kuondoka.
(8). BAHLUL AUZA PEPO
Siku moja Bahlul alikuwa ukingoni mwa mto akicheza kwa udongo kwa kutengeneza nyumba na bustani. Hapo alitokea Zubeidah, mke wake Harun, akipita hapo. Alipomkaribia Bahlul, alimwuliza: "Ewe Bahlul! Je wafanya nini?" Bahlul alimjibu: "Najenga Pepo (Jannat) ." Zubeidah alimwambia: "Je wauza hizi Pepo ulizozijenga?" Bahlul alimjibu: "Naam ninaziuza!" Zubeidah alimwuliza: "kwa Dinar ngapi?" Bahlul alimjibu "Kwa Dinar mia moja tu!" Kwa kuwa Zubeidah alikuwa akitaka kumsaidia Bahlul, hivyo aliona hapo ndipo pahala pa kumsaidia na alimwamuru mfanyakazi wake amlipe Bahlul hizo fedha. Nao walimlipa hizo dinar mia moja. Usiku ule Zubeidah aliota ndoto akiwa Peponi ambamo kuna Qasri nzuri mno iliyopambwa mno na wapo wajakazi wamesubiri amri, wao walimwambia hiyo ndiyo Qasri aliyoinunua kutoka kwa Bahlul. Zubeidah alipoamka siku ya pili, akiwa amejawa na furaha, alimwelezea mume wake, Harun. Harun alimwita Bahlul, alipofika, Harun alimwambia, "Ewe Bahlul, chukua hizi Dinar mia moja na uniuzie Pepo mojawapo ya Pepo kama ile uliyomwuzia Zubeidah." Bahlul alicheka na kumwambia: "Zubeidah alinunua bila ya kuona ambapo wewe unataka kununua baada ya kujua ya kuwapo kwake. Hivyo sitakuuzia!"
(9). HARUN RASHID AMKASIRIKIA BAHLUL
Harun alimwajiri jasusi makhususi kwa ajili ya kuchunguza na kuripoti kwake juu ya imani na akida sahihi za Bahlul. Baada ya siku chache huyo jasusi alikamilisha uchunguzi wake na kuripoti kwa Khalifa kuwa Bahlul alikuwa ni mpenzi wa Ahl-al-Bayt ya mtume(s.a.w.w)
na alikuwa mfuasi wa Imam Musa al-Kadhim
. Harun alimwita Bahlul na kumwambia: "Ewe Bahlul! Mimi nimepata habari za kuaminika kuwa wewe ni mmojawapo wa wapenzi na wafuasi wakubwa wa Musa ibn Jaafar na hivyo unafanya kila jitihada za kudhihirisha na hivyo umejidhihirisha u - mwehu ambapo sivyo ulivyo!" Bahlul alimjibu: "Iwapo hivyo ndivyo ilivyo, je utanifanya nini?" Kwa majibu hayo, Harun alighadhibika mno na kumwamuru Masrur, mfanyakazi wake, amvue nguo Bahlul akalishwe juu ya punda na kuzungushwa mjini na hatimaye kukatwa kichwa mbele yake Harun. Masrur, alitekeleza vile alivyoamrishwa na hatimaye kumleta mbele ya Harun katika hali hiyo ili aweze kuuawa. Mara, hapo akatokezea Jaafer Barmaki ambaye kwa kuiona hali hiyo ya Bahlul alimwuliza sababu ya hali yake hiyo: "Ewe Bahlul! Je umetenda kosa gani?" Bahlul alimjibu: "Kwa kuwa mimi nimesema ukweli, kwa hivyo Khalifa akanizawadia mavazi yenye thamani." Harun Rashid, Jaafar, na wote waliokuwepo walichekeshwa mno kwa majibu ya Bahlul, na papo hapo Harun alimsamehe Bahlul na kutoa amri ya kufunguliwa na apewe mavazi mapya na mazuri. Lakini Bahlul hakukubali hayo bali yeye alichukua kifurushi cha nguo zake kuukuu na kuondoka.
(10). BAHLUL NA HARUN KWENDA KUOGA PAMOJA
Ilitokea siku moja Bahlul na Harun Rashid kukutana katika Hammam (majumba ya kuogea). Khalifa alimfanyia mzaha kumwuliza Bahlul: "Je iwapo ningalikuwa mtumwa, ningalikuwa na thamani gani?" Bahlul alimjibu: "Dinar hamsini." Harun Rashid katika kughadhabika alisema: "Ewe Mwehu! itawezekanaje hivyo? Mavazi yangu tu yamezidi thamani hiyo!" Hapo Bahlul alimwambia: "Kwa hakika mimi nimesema kuwa hiyo ni thamani ya nguo zako tu ama Khalifa hana thamani yoyote!"
(11). MABISHANO PAMOJA NA ABU HANIFA
Abu Hanifa alikuwa akiwafundisha wafuasi wake na Bahlul alikuwa ameketi katika kona moja akisikiliza masomo hayo, baina ya mafunzo, Abu Hanifa alisema kuwa yeye hakukubaliana na mambo matatu yaliyoelezwa na Imam Jaafer Sadiq
, nayo ni:
Kwanza
: Imam Jaafer Sadiq
amesema kuwa sheitani ataadhibiwa katika Jahannam (motoni). Kwa kuwa sheitani ameumbwa kwa moto sasa moto utamuumizaje moto huo?
Pili
: Yeye amesema kwa sisi hatutaweza kumwona Allah (s.w.t) ambapo twajua kuwa kile kilichopo ni lazima kionekane. Hivyo Allah anaweza kuonwa kwa macho.
Tatu
: Yeye amesema kila mtenda tendo ndiyo mhusika mwenyewe atawajibika kujibu kwani ametenda mwenyewe. Ambapo sisi (wakina Abu Hanifa) twaamini kuwa kila kitendo kitatokana na Allah na wala mtu hawajibiki. Abu Hanifa alipoyamaliza kuyasema hayo, Bahlul alichukua rundo moja la udongo na kumlenga Abu Hanifa. Alipoutupa, ulimpiga Abu Hanifa juu ya uso wake, ulileta maumivu makubwa mno. Na hapo ndipo Bahlul alipotimua mbio, lakini wanafunzi wa Abu Hanifa waliweza kumshika Bahlul. Kwa kuwa Bahlul alikuwa akipatana mno na Khalifa, alipelekwa mbele yake, ambapo Khalifa alielezwa hali yote. Bahlul alisema: "Aletwe Abu Hanifa ili niweze kumjibu!" Alipoitwa Abu Hanifa, Bahlul alimuuliza, "Je, dhambi gani nililokufanyia? Abu Hanifa alisema: "Kichwa changu chaumwa sana kwa sababu ya wewe kunipiga rundo la udongo." Bahlul alimjibu: "Je waweza kunionyesha maumivu hayo?" Hapo Abu Hanifa alimwambia: "Je na maumivu pia yanaweza kuonyeswa?" Basi Bahlul alianza kumjibu kwa busara: "Wewe mwenyewe umedai kwa kila kitu kilichopo lazima kionekane na umekuwa ukimpinga tena Imam Jaafer Sadiq
na vile vile unadai kuwa itawezekanaje kwa Allah kuwapo na asiweze kuonekana? "Pili madai yako hayafai, kwani itawezekanaje kuwa kitu cha jinsi moja kiwezi kukiumiza kitu cha jinsi hiyo (sheitani hana dhambi wala kuchomwa moto) kwani wewe umeumbwa kwa udongo na udongo niliokupiga ni vitu vya jinsi moja." Tatu, kila tendo linatokana na Allah, hivyo kwanini wewe unilaumu na kunishtaki mbele ya Khalifa na kudai kisasi kwani humlaumu Allah aliyenisababisha mimi kukupiga?" Kwa hayo, Abu Hanifa aliaibika na hakuwa na chaguo lolote isipokuwa kuondoka hapo.
(12). BAHLUL NA WAZIRI
Siku moja Waziri mmoja wa Harun alimwambia Bahlul, "Ewe Bahlul, Khalifa amefanya wewe uwe mtawala na Hakimu wa ufalme wa mbwa, kuku na nguruwe wote." Bahlul alimjibu: "Basi kuanzia hivi sasa, wewe hauna budi kuzitii amri zangu kwani wewe pia upo miongoni mwa raia wangu." Wote waliokuwa pamoja na Waziri walicheka mno na kulimfanya aondoke kimya kwa kuaibishwa.
(13). BAHLUL AMSIHI ABDULLA MUBARAK
Siku moja Abdulla Mubarak alimwendea Bahlul kwa kutaka nasaha. Alipofika kwa Bahlul, alimkuta kichwa wazi na miguu wazi akisema Allah! Allah..... Alimwendea na kumtolea salaam na Bahlul alimjibu. Baadaye Abdulla alisema: "Ewe Sheikh! Naomba unipatie nasaha na naomba unionyeshe njia itakayonionyesha vile niishi maisha yangu pasi na madhambi kwani mimi ni mtu mwenye madhambi ambayo nafsi yangu potofu imenighalibu. Hivyo nionyeshe njia hiyo mwokovu."
Bahlul alimwambia Abdullah: "Mimi mwenyewe nimehangaika mno, sasa wawezaje kunitegemea? Iwapo ningelikuwa mwenye akili, basi watu wasingaliniita mwehu na wewe watambua kuwa maneno ya mwehu hayana athari yoyote yakuweza kukubaliwa na watu. Kwa hivyo, nakuomba umtafute mtu ambaye ni mwenye akili ili akushauri vyema."
Abdullah akasema: "Ewe Sheikh mara nyingi wehu wanatokezea kusema mengi yenye busara." Kwa hayo Bahlul alinyamaza. Hapo tena Abdullah akaanza kumwomba kwa kumbembeleza. "Ewe Sheikh, tafadhali sana usinivunje moyo kwani nimekuja kwa matumaini makubwa."
Bahlul alimjibu: "Ewe Abdullah! Tafadhali sana kwanza kabisa kubali sharti zangu nne ili usiyageukie maneno ya mwehu, ndipo hapo nitakupa nasaha zangu ambazo zitakuokoa.
Abdullah akasema: "Je masharti hayo manne ni yapi ili niweze kuyakubali."
Bahlul akasema: "Sharti la kwanza ni hili: iwapo utatenda dhambi yolote ile, na kupinga hukumu ya Allah, basi uache kula riziki itokayo kwa Allah."
Abdullah akamwambia: "Nisipokula riziki ya Allah, je nitakula riziki ya nani?
Bahlul akasema: "Wewe ukiwa mtu mwenye akili umedai kuwa unafanya ibada ya Allah na kula riziki yake Allah na pepo hapo unafanya maasi ya kutozitii amri zake. Tafadhali sana jaribu kuamua mwenyewe iwapo hii ndio haki ya ibada?"
Abdallah akasema: "Ewe Sheikh wewe umesema kweli na yaliyo sahihi na sharti la pili ni ipi?" Bahlul akasema: Sharti la pili ni kwamba, unapotenda dhambi lolote, basi jitoe katika milki ya Allah." Abdullah akasema: "Ama kusema ukweli sharti hili la pili ni gumu kuliko hata lile la kwanza, kwani kila mahala pana ardhi ya Allah na utawala wake, sasa nitakwenda wapi?" Bahlul alimwambia: "Kwa kweli hili ni jambo baya mno kwani wewe unakula riziki yake na kuishi katika milki yake na papo hapo unakana kutii kwa amri yake. Fanya maamuzi yako wewe mwenyewe kuwa hiyo ndiyo sharti ya ibada?" Hapo Abdullah aliuliza: "Je sharti la tatu ni lipi?" Bahlul alijibu: "Sharti la tatu ni kwamba iwapo wewe wataka kutenda madhambi yoyote, basi uende ujifiche mahala pale ambapo Allah hataweza kukuona, wala kuona hali yako, na hapo ndipo utende vile upendavyo." "Sharti hilo ni gumu zaidi!" alisema Abdullah, kwani Allah anafahamu na kuona kila kitu, yupo kila mahala. Chochote kile akitendacho mja, Allah hukiona na kukielewa."
Bahlul alisema: "Wewe mwenyewe u - mtu mwenye akili. Inakubidi wewe uelewe kuwa Allah yupo kila mahala na kumwona kila mtu. Hivyo ni jambo la kustaajabisha ni kule kutumia riziki yake kuishi katika milki yake na vitendo wazi katika utawala wake ambavyo yeye anakuona na kufahamu. Baada ya yote hivyo unadai kufanya ibada yake. Abdullah alisema: "Kwa hakika umesema ukweli kabisa. Na sharti la nne ni lipi?" Bahlul alimwambia: "Wakati utakapoijiwa na Malakul Maut (Malaika atoae roho) ili kuitoa roho yako, basi umzuie asifanye hivyo hadi hapo utakapokuwa umekwisha agana na ndugu na rafiki zako wote na kuweza kutenda matendo mema ambayo yatakusaidia hapo baadaye." Abdullah alijibu: "Lo! Sharti hili ni gumu zaidi kuliko masharti yote. Huyo Malakul Mauti hatanipa hata fursa ya kupumua!" Hapo ndipo Bahlul alipomjibu: "Ewe mtu mwerevu! Wewe watambua vyema kabisa kuwa mauti hayana hila yoyote, na hauwezi kamwe kujitenga nayo na hautapatiwa muhula wowote ule. Na inawezekana pia ikatokea mauti katikati mwa hali ya madhambi na hautapata hata muhula wa kupumua kama vile Allah (s.w.t) alivyosema. Kwa hiyo ewe Abdullah! Pokea nasiha hata kwa mwehu na uamke kutoka usingizi wako!" Jihadhari na ghururi na ulevi wako na uwazie akhera kwani safari yako ndefu ipo mbele yako na umri wako upo mdogo kabisa. Kazi ya leo usiiweke kesho kwani kesho hiyo labda hautaiona. Muda huu uliopo uthamini. Kazi za Aakhera usizicheleweshe kwani usichokitenda leo utakijutia hapo kesho na kujuta kwako hakutakufaidisha."
Abdullah alipoyasikia hayo alianza kuwaza huku akiwa amekiinamisha kichwa chake. Mara Bahlul alianza kusema: "Ewe Abdullah! Wewe umenitaka nikusihi ili uweze kufaidika nayo kesho, sasa baada ya kuyasikia hayo mbona wainamisha kichwa chini?" Siku ya Qiyama, katika uwanja wa Hisabu na Kitabu, utawajibu nini Malaika watakao kuhoji. Yeyote yule atakayekuwa na hisabu yake safi humu duniani, hatakuwa na khofu yoyote ile hapo Aakhera! Hatimaye,Abdullah alikiinua kichwa chake na kusema: "Ewe Sheikh! Mimi nimeyasikia yote uliyoyazungumza. kwa moyo wangu wote na nimelikubali hili sharti la nne pia, naomba unisihi zaidi na kunifanya niwe mmoja wenu. Bahlul alisema: "Ewe Abdullah! Mwanadamu afanyalo lolote inambidi aweke mbele maamrisho yake Allah (s.w.t) na hata katika hali ya kusema au kusikiliza, kwani kwa kila hali yu mwumba wa Allah (s.w.t)" Bahlul alikuwa ni mtu ameelimika kwa Imam Jaafer as-Sadiq