4
HIKAYA ZA BAHLUL MWENYE BUSARA
(32). SWALI JUU YA AMIN NA MAAMUN
Siku moja bahlul alikuwa akienda kwa Harun na wakakutana njiani. Harun akamwambi: "Je wakwenda wapi?" Bahlul akamjibu: "Kwako wewe!" Harun akamwambia: "Mimi nakwenda shuleni kujua hali ya Amin na Ma'amun na maendeleo yao. Hivyo iwapo utapenda kuandamana nami, basi tufuatane pamoja." Bahlul alikubali na hivyo walifika shuleni lakini wakakuta watoto hao wawili wametoka nje kidogo. Harun alimwuliza mwalimu hali na tabia za watoto wawili hao. Mwalimu alimjibu: "Amin ni mtoto wa kiongozi wa akina mama na Kiarabu, lakini ni mpumbavu na mwenye akili na fahamu ndogo, na kinyume chake ni Ma'amun ambaye ni hodari mwenye akili na mwerevu! Harun alitamka: "Mimi si yaamini hayo!" Mwalimu akachukua karatasi akaiweka chini ya zulia alipokuwa akikalia Ma'amun na akaliweka tufali chini ya zulia alilokuwa akilikalia amin. Baada ya muda mdogo tu, wote wawili walirejea darasani. Walipomwona tu baba yao, wote wawili walitoa heshima zao, na wakaketi nafasini kwao. Ma'amun alipoketi, hakutulia, aliitazama dari na alitazama kushoto na kulia. Hapo mwalimu alimwuliza: "Ewe Ma'amun mbona unakodoa macho huku na huko? Je umekuwaje?" Ma'amun alimjibu: "Baada ya kutoka darasani na kurejea nahisi kuwa hii ardhi imeinuka kiasi cha unene wa karatasi moja au dari la darasa limeteremka chini kiasi hicho. Yaani kwa kifupi, Zulia langu limeinuka kwa kiasi cha karatasi moja." Papo hapo mwalimu alimwuliza Amin: "Je na wewe wahisi hivyo?" Amin alimjibu: "La! Mimi sihisi chochote kile, nipo sawasawa." Kwa kuyasikia hayo mwalimu alicheka na akawaambia watoke nje ya darasa na akamwambia Harun alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa maneno yake kuthibitika kweli mbele yake.
Hapo Khalifa alimwuliza: "Je nini sababu ya tofauti hizo?" Bahlul akasema: "Ewe Khalifa! Iwapo utanipa ahadi ya amani na kusalimika kwangu kutokana na wewe mimi nitaweza kukujibu sababu zenyewe." "Unayo amani na utasalimika, haya elezea yale uyajuayo kuhusu swala hili." Allimjibu Harun. Hapo ndipo Bahlul alipoanza kuelezea kwa kinaganaga: "Uhodari na uwerevu wa watoto unatokana na sababu mbili - kwanza, wakati mwanamme na mwanamke wanapokutana kimwili pamoja na taratibu njema basi watoto wazaliwao huwa werevu, hodari na wakakamavu. Sababu ya pili, mwanamme na mwanamke wanapotokana na damu na ukoo tofauti basi watoto wao huwa wenye akili, werevu na wenye nguvu. Na vivyo hivyo ndivyo ilivyo katika mimea na wanyama, na hayo yameshakwisha kuthibitishwa, kwa mfano, iwapo kutapandikizwa tawi la tunda aina moja katika aina ya tunda lingine la jinsi hiyo hiyo, basi tunda jipya litakuwa tamu na lenye ladha nzuri kuliko tunda la mti wenyewe. Na iwapo kutakutanishwa kimwili kwa farasi na punda, basi kutazaliwa nyumbu ambaye atakuwa hodari na mwenye nguvu, mwepesi kuliko hao wazazi wake. Kwa kifupi, kasoro aliyo nayo Amin katika kufikiri na fahamu ni kwa sababu ya Khalifa na Zubeidah wanatokana na damu na ukoo mmoja ambapo Ma'amun anaonekana mwerevu, hodari na mwenye akili ni kwa sababu mama yake mzazi ametokana na ukoo na damu tofauti na ile ya Khalifa, na tofauti yake ni kubwa!" Khalifa kwa majibu hayo alicheka na kusema: "Mwehu atasema hayo hayo na wala hawezi kutegemewa kusema kingine cha akili." Lakini mwalimu aliyasadikisha maneno ya Bahlul moyoni mwake.
(33). BAHLUL AMJIBU KHALIFA
Harun Rashid alikuwa akirudi kutoka Hijja na njiani alikuwapo Bahlul aliyekuwa akimsubiri. Alipomuona Harun Rashid, alipaaza sauti yake na akasema mara tatu: "Harun! Harun! Harun!" Khalifa aliuliza "Je ni nani yule aniitaye hivi?" Watu walimwambia: "Si mwingine ila ni Bahlul." Hapo Bahlul aliitwa, na alipokaribia, aliulizwa "Je mimi ni nani?" Bahlul alimjibu, "Wewe ni yule mtu ambaye atatkiwa kutoa majibu ya dhuluma iwapo itafanyika mashariki au magharibi" (Kwani Harun alikuwa Khalifa wa dola nzima hivyo aliwajibika). Harun alipoyasikia hayo aliangua kilio na kusema: "kwa hakika umesema ukweli, sasa niombe ombi lako ili nikutimizie." Bahlul hakuchelewa kusema: "Naomba unisamehee madhambi yangu yote na kuniingiza Peponi." Harun alimjibu: "Deni haliwezi kulipa deni! Kwani wewe mwenyewe unadaiwa na Umma mzima, hivyo warejeshee mali zao Umma wote. Haipendezi wala kusihi kwangu mimi kupokea mali ya watu wengine waliodhulumiwa." Khalifa akasema: "Mimi ninatoa amri ya wewe kupatiwa milki na utajiri kiasi cha kukulisha wewe umri mzima ili uishi kwa raha na mustarehe bila ya kusumbuka." Bahlul alimjibu, "Sisi sote ni viumbe vya Allah s.w.t. na huwa ametupatia sote riziki, sasa itawezekanaje yeye akupe wewe riziki na kunisahau mimi?"
(34). BAHLUL NA SHEIKH JUNAID
Siku moja Sheikh Junaid Baghdadi alitoka nje ya mji wa Baghdad ili kutembea na kutazama mandhari nzuri. Kwa kuwa alikuwa ni Sheikh hodari na maarufu, alifuatwa na wafuasi wake. Sheikh aliwauliza hali ya Bahlul, wao wakamjibu." Yeye ni mtu mwenda wazimu, je unayo kazi gani naye?" Sheikh aliwajibu: "Niitieni kwani ninayo kazi naye." Basi watu walitoka kumtafuta Bahlul, walimkuta upweke. Sheikh alifika mbele ya Bahlul. Sheikh alipomwendea na kumkaribia Bahlul, alikuta ameweka tufali chini ya kichwa akiwa katika hali ya kuwaza. Sheikh alimtolea salaam naye akajibu na akauliza: "Je wewe ni nani?" Sheikh alimjibu: "Mimi ni Junaid Baghdad." Bahlul alimwuliza: "Si wewe ndiye Abul Qasini?" "Naam!" akajibiwa. Bahlul akamwambia: "Je ni wewe mwenyewe Sheikh Baghdad ambaye unawafunza watu ilimu ya kiroho?" Sheikh akajibu: "Naam!" Bahlul akamwuliza: Je wewe wajua namna ya kula chakula chako?" Sheikh alimjibu: "Mimi husema Bismillah, na hula kile kilicho mbele yangu, huchukua matonge madogo madogo na huweka upande wa mdomo wangu, hutafuna pole pole, huwa sitazami matonge ya wengine. Wakati wa kula huwa ninamkumbuka Mwenyezi Mungu na kila tonge nilalo husema Alhamdulillah na hunawa mikono kabla na baada ya kula." Kwa kusikia hayo, Bahlul aliinuka aksimama na kwa kukasirika alisema: "Loh! Wewe wataka kuwaongoza viumbe ambapo hadi sasa hata haujui vile ule chakula chako" akasema hayo na akajiondokea.
Wafuasi wa Sheikh wakasema: "Ewe Sheikh! Huyu mtu ni mwehu!" Sheikh akawajibu: "huyu ni mwendawazimu lakini yupo hofari katika kazi zake. Inatubidi tumsikilize kwa makini kwani huwa anasema maneno sahihi." Naye akaondoka kumfuata Bahlul, akisema "Ninayo kazi naye." Bahlul alipotokezea katika upweke, aliketi. Sheikh alimwendea. Bahlul aliuliza: "Je wewe ni nani?" Sheikh alijibu: "Sheikh Baghdad ambaye hajui hata kula chakula." Bahlul alimwambia: "Iwapo wewe hujui kula chakula,basi je unajua namna ya kuzungumza?" Sheikh alimjibu: "Naam!" Bahlul alimwuliza: "Je unazungumzaje?" Yeye alimjibu:"Huwa ninazungumza kwa sauti ya chini, wala sizungumzi pasipo hitajika na wala sizungumzi kupita kiasi. Huzungumza kiasi cha uwezo wa wasikilizaji kunielewa."
Huwalingania watu dini ya allah (s.w.t) na Mtume(s.a.w.w)
Huwa sizungumzi kiasi cha kuchukiwa na wasikilizaji. Huwa mwangalifu ya yale yaliyo dhahiri na bitini." Kwa kifupi, alielezea taratibu zote zihusianazo na mazungumzo. Bahlul alisema: "Loh! Acha kula usivyojua, hata kuzungumza pia haujui?" Na mara hii tena akaondoka zake baada ya kuyasema hayo. Wafuasi wa Sheikh walisema: "Ewe Sheikh, je umeona kuwa huyu ni mwenda wazimu tu, sasa waweza kutegemea nini kutoka kwa mwendawazimu huyu?" Sheikh Junaid akawaambia "Nina kazi naye. Nyinyi hamuwezi kujua." Tena alimfuata Bahlul, naye akamwuliza: "Mbona unapenda kunifuata niendako, je unanitakia nini? Wewe hujui namna ya kula chakula na wala namna ya kuzungumza, sasa jee wajua namna ya kulala? Naye akamjibu: "Naam" Bahlul akamwuliza: "Je ualalaje?" Sheikh alimjibu: "Baada ya sala ya Isha' na kumaliza shghuli zangu, huanza kuvaa mavazi yaliyotoharika." Alielezea taratibu na desturi zote azijuazo za kulala. Hapo Bahlul akamwambia: "Mimi nimeshaelewa kuwa wewe hata desturi ya kulala pia haujui." Na Bahlul alipotaka kuondoka tu, Junaid alimshika na kumwambia: "Ewe Bahlul! Mimi hayo masuala matatu siyajui, naomba kwa jina la Mwenyezi Mungu unifundishe!"
Bahlul alimwambia: "Mimi nimekuwa nikijitenga nawe kwa sababu wewe ulidai kuwa unajua vyote. Lakini kwa kuwa umekiri mwenyewe kuwa haujui, basi sikiliza "haya yote uliyoyazungumza wewe ni maswala ya matawi tu kwani misingi ni kuwa kila tonge lako liwe tonge halali kwani iwapo utatekeleza desturi zote za kula ambapo tonge lenyewe ni haramu basi hakutakufaidia chochote bali kutaongezea kiza moyoni mwako." Junaid akasema: "Mwenyezi Mungu akujalie malipo mema!" Akaendelea Bahlul: "Katika kuzungumza, kwanza kabisa moyo na nia zinatakiwa ziwe safi na mazungumzo yenyewe yanatakiwa yawe ka ajili ya furaha za Allah (s.w.t) Iwapo utazungumza ufidhuli au upuuzi basi kutakuletea madhara tu kwa hivyo, ukimya utakuwa wenye manufaa. Vile vile ulivyozungumzia desturi za kulala pia ni matawi tu." "Misingi yake ni kuwa unapojitarisha kulala, ni lazima moyo wako usiwe na bughudha, kisasi na husuda dhidi ya Waislamu. Usiwe na tamaa ya mali ya dunia, na unapotaka kulala umkumbuke Allah (s.w.t)" Junaid aliubusu mkono wa Bahlul na akamwombea dua njema. Wafuasi walikuwepo hapo wakidhani Bahlul yu mwenda wazimu, walishangaa kuona busara zake. Kwa hivyo, imetufundisha kuwa iwapo usipojua kitu usiwe na aibu ya kuulizia vile Sheikh Junaid alivyojifunza kwa Bahlul.
(35). BAHLUL NA QADHI
Mtu mmoja alinuia kwenda Hijja msimu huo. Kwa kuwa alikuwa na watoto wadogo wadogo, hivyo alichukua Ashrafi elfu moja akaziweka kwa Qadhi kama amana katika ofisi ya serikali, na akasema: "Iwapo nitakufa huko huko, basi fedha hizi utazisimamia wewe na utakuwa na uwezo wa kuwapatia kiasi chochote utakacho familia yangu amana yangu! Baada ya kutoka Ofisini mwa Qadhi, aliondoka kwenda Hijja. Alifariki bado akiwa safarini. Watoto wake walipokua na kupata fahamu, walimwendea Qadhi kudai amana ya baba yao. Naye Qadhi akawajibu: "Kwa mujibu wa wasiya wa baba yao aliyoitoa mbele ya watu, mimi ninao uwezo wa kuwapa kiasi nikitakacho mimi. Kwa hivyo nitawapa Ashrafi mia moja tu!" Watoto hao walianza kuleta vurugu. Hivyo Qadhi aliwaita wale wote waliokuwako wakati akipokea Ashrafi na kuwauliza: "Je mlikuwapo siku ile ambapo baba watoto hawa aliponiachia amana ya Ashrafi elfu moja na kuniambia kuwa niwape tu kiasi nitakacho mimi." Wale wote waliitikia kuwa hayo ndivyo yalivyokuwa. Kwa hivyo Qadhi alisema: "Basi mimi sintawapeni zaidi ya Dinar mia moja." Wale watoto walijuta mno na walianza kuwaambia watu lakini hakuna mtu aliyeweza kupata ufumbuzi kwani lilikuwa swala la sharia. Pole pole na Bahlul akaja akapata habari. Akawachukua wale watoto hadi kwa Qadhi, na kumwambia: "Je kwanini hauwapatii haki yao mayatima hawa?" Qadhi akamjibu: "Ulikuwa ni wasia wa baba yao kuwa niwape kiasi nitakacho mimi, hivyo sitawapa zaidi ya dinar mia moja." Hapo Bahlul alimnasa Qadhi na akamwambia: "Ewe Qadhi! Wewe unataka Dinar mia tisa na kwa mujibu wa kauli yako, marehemu alikwambia uwape watoto wake kile kiasi utakacho wewe, na hivyo ni Dinar mia tisa ndizo uwape hawa!" Qadhi alishindwa mbinu za kuwababaisha wale watoto na hivyo alilazimika kuwapa wale mayatima Dinar mia tisa.
(36.). SWALI KUHUSU MTUME LUT
Watu walimwuliza Bahlul: "Je mtume Lut
alitokana na ukoo gani?" Alijibu: "Ni dhahiri kwa jina lake kuwa alikuwa ni Mtume wa walawiti na waovu." Watu wakamwambia: "Kwanini wamwaibisha Mtume wa Allah (s.w.t) kwa jibu kama hilo?" Akawajibu Bahlul: "Mimi sikumsema vibaya mtume, bali nimewaambia kuhusu ukoo wake na hayo ni sahihi."
(37). SWALI KUHUSU SHEITAN
Mtu mmoja mwovu kabisa alimwuliza Bahlul: "Mimi nimetamani mno kumwona Sheitan." Bahlul alimjibu: "Iwapo nyumbani kwako hamna kioo cha kujitazama basi tazama kweye maji safi na yaliyotulia, basi utamwona sheitani."
(38). BAHLUL NA MHUDUMU
Mhudumu mmoja wa Harun Rashid alikula jibini na ikabakia kidogo katika ndevu zake. Bahlul alimwuliza: "Je unakula nini?" Mhudumu alijibu: "Nimemla njiwa" Bahlul lalimwambia: "Mimi nilikwishaelewa kabla hata ya wewe kuniambia." Hapo mhudumu alimwuliza: "Je ulitambuaje?" Bahlul alimjibu: Ndevuni mwako kuna mabaki ndiyo yaliyonijulisha. "Mimi nilikwishaelewa kabla hata ya wewe kuniambia" Hapo mhudumu alimwuliza: "Je ulitambuaje?" Bahlul alimjibu: Ndevuni mwako kuna mabaki ndiyo yaliyonijulisha. "(alimaanisha kuwa alichokula na akisemacho ni vitu tofauti na hivyo amesema uongo!)"
(39). BAHLUL NA HARUN WAWINDA
Siku moja Harun Rashid pamoja na kikundi cha watu wake walikwenda kuwinda. Bahlul pia alikuwamo. Katika tafuta tafuta yao, akaonekana swala mmoja, hapo Khalifa alimlenga mshale, lakini haukumpata yule swala. Bahlul akasema: "Vyema kabisa!" Khalifa alinyamaa, na akasema: "Je wanitania? Kwa mzaha huo?" Bahlul alimjibu: "La hasha! Mimi nimemsifu swala huyo vile alivyoukwepa mshale wako!"
(40). BAHLUL NA MWENYE NYUMBA
Siku moja Bahlul alikwenda Basara, na kwa kuwa kule hakuwa na mwenyeji hivyo aliweza kukodi chumba kimoja kwa siku kadhaa. Chumba hicho kilikuwa kikuu mno na kulipokuwa kukivuma upepo basi kulikuwapo na sauti. Bahlul alimwendea mwenye nyumba, akamwambia: "Ewe bwana! Wewe umenipa chumba ambacho kinapovumiwa na upepo basi kuta na dari zake zinaanza kupiga sauti ambazo zinatishia maisha yangu kwani yapo hatarini." Bwana nyumba alikuwa mcheshi alianza kusema katika kumjibu: "Hapana jambo lolote lililo baya. Wewe watambua vyema kabisa kuwa vitu vyote vinamtukuza Mola na Kumsifu na hivyo ndivyo chumba chako kinavyofanya." Bahlul alimwambia: "Hayo ni kweli kabisa kwani kila kitu kinamtukuza Mola na hatimaye huangukia kusujudu pi, hivyo mimi nahofu kule kusujudu kwa chumba chako, hivyo itanibidi nihame haraka iwezekanavyo!" (Kusujudu akimaanishi kubomoka).
(41). KHALIFA NA ULEVI
Siku moja Bahlul alikwenda kwa Harun na akamkuta Khalifa akiwa katika hali ya kuleva vileo, kwa kuona hayo, Khalifa alitaka kuficha aibu yake isije ikatobolewa nje. Kwa hivyo, alianza kumwuliza Bahlul maswali: "Je kula zabibu ni haraam?" Bahlul alimjibu: La, si haram." Khalifa akauliza: "Baada ya kula zabibu, je mtu akinywa maji hukumu yake inakuwa vipi?" Bahlul alimjibu: "Hakuna kitu!" Khalifa aliuliza tena: "Iwapo baada ya kula zabibu na kunywa maji, mtu akakaa juani kwa kitambo, je hukumu yake nini?" Bahlul akamjibu: "Hapo pia hapana kitu." Hapo Khalifa akanena: "Iwapo Zabibu na maji yakiwekwa juani kwa kitambo, basi itakuwaje haramu? Basi Bahlul naye pia alimjibu vivyo hivyo: "Iwapo utamwekea udongo kidogo juu ya kichwa cha mtu, jee itamdhuru?
Khalifa alimjibu: "La! Haitamdhuru." Bahlul aliuliza tena: Iwapo udongo huo huo ukachanganywa na maji, likatengenezwa tofali na hilo tofali akapigwa nalo, je litamdhuru?" Hapo Khalifa akajibu: "Bila shaka tofali litavunja kichwa chake." Bahlul alimjibu: "Iwapo udongo ukichanganywa na maji unaweza kuvunja kichwa cha mtu na kuweza kumdhuru ndivyo vivyo hivyo zabibu na maji ikichanganywa itatengeneza kitu tofauti ambacho kimeharamishwa na sheria za Islam na kusema kuwa si toharifu. Kwa kunywa kinywaji hicho kinamletea mnywaji madhara mengi mno na hustahiki adhabu kali mno katika Islam." Khalifa alistajabishwa mno kwa ufasaha wa Bahlul katika majina yake na papo hapo aliamrisha pombe zote ziondolewe pale.