UCHUNGUZI JUU YA UWAHABI

UCHUNGUZI JUU YA UWAHABI0%

UCHUNGUZI JUU YA UWAHABI Mwandishi:
: SHEIKH MUSABBAH SHA'ABANI
Kundi: Vitabu mbali mbali

UCHUNGUZI JUU YA UWAHABI

Mwandishi: SHEIKH JA'AFAR SUBHANY
: SHEIKH MUSABBAH SHA'ABANI
Kundi:

Matembeleo: 50940
Pakua: 5274

Maelezo zaidi:

UCHUNGUZI JUU YA UWAHABI
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 24 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 50940 / Pakua: 5274
Kiwango Kiwango Kiwango
UCHUNGUZI JUU YA UWAHABI

UCHUNGUZI JUU YA UWAHABI

Mwandishi:
Swahili

13

UCHUNGUZI JUU YA UWAHABI

KUOMBA MSAADA KWA MAWALII WA MWENYEZI MUNGU KATIKA UHAI WAO

Bila shaka kuomba kitu chochote katoka kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu kuna namna nyingi, nasi tutazionyesha katika mpango ufuatao:

1. Kumuomba mtu aliye hai atusaidie katika ujenzi wa nyumba au kunywesha maji.

2. Kumuomba mtu aliye hai atuombee kwa Mwenyezi Mungu atusamehe.

Namna hizi mbili zinashirikiana kwa kuwa jambo litakiwalo ni la kawaida kimaumbile, na huyo aombwaye anao uwezo wa kulifanya, lakini namna hizi zinatofautiana kwa kuwa ile ya kwanza imefungamana na mambo ya kidunia, na ile ya pili inamafungamano na akhera.

3. Kumuomba mtu aliye hai atufanyie kazi bila ya kutumia sababu za kimaada, kwa mfano kumuomba amponye mgonjwa bila ya dawa, au kumuomba kukirejesha kitu kilichopotea bila kukitafuta, au kumuomba kalipa deni bila ya kufanya kazi ili kaipata mali (ya kulipia deni).

Kwa maelezo mengine, tunamuomba kufanya kazi kwa njia ya muujiza au karama[173] .

4. Kumuomba mtu aliyekufa atuombee kwa Mwenyezi Mungu, na ombi letu kwa mtu huyo litatokana na itikadi yetu kwamba yeye yu hai katika ulimwengu wa Akhera na anaruzukiwa huko.

5. Kumuomba mtu atake msaada kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu (uwezo ambao Mwenyezi Mungu amempa) kumponyesha mgonjwa wetu au aturejeshee kitu chetu kilichopotea au jambo jingine lolote lile. Namna hizi mbili ni kama ile ya pili na ya tatu, lakini tofauti baina yao ni kwamba, kule maombi ni kwa mtu aliye hai katika ulimwengu wa kimaada, na hapa maombi yetu ni kwa mtu aliyekufa kidhahiri lakini kihakika yu hai. Na kwa msingi huu basi, hatuwezi kumuomba mtu aliyekufa atusaidie katika mambo ya kimaada kwa kupitia sababu za kimaada, na hiyo ni kwa sababu ya kutokuwepo utendaji wa kimaada wa maiti katika ulimwengu huu kwa kuwa yeye amekwisha ondoka duniani. Ewe msomaji mpendwa, hizi ni sehemu tano za namna ya kuomba msaada, tatu miongoni mwake zinamuhusu mtu aliye hai ndani ya ulimwengu huu wa kimaada, na mbili zinahusika na mtu aliye katika ulimwengu wa akhera.

Sisi sasa hivi tutazungumzia zile namna tatu za mwanzo na "tunaakhirisha mazungumzo ya kuwaomba msaada Mawalii wa Mwenyezi Mungu walio hai katika ulimwengu wa akhera, jambo hilo tutalizungumzia katika mlango ujao apendapo Mwenyezi Mungu. Na sasa hebu zingatia uchunguzi ndani ya zile namna tatu: Namna ya Kwanza: Bila shaka kuomba msaada kwa watu walio hai ndani ya mambo ya kawaida ambayo yanazo sababu za kimaumbile ni jambo linaloweka msingi wa utamaduni wa binadamu, kwani maisha ya wanadamu duniani kote yamesimama katika msingi wa kusaidiana na kushirikiana na watu wenye akili ulimwenguni wanasaidiana na kushirikiana katika mambo ya maisha. Kwa hiyo, hukumu ya msaada wa aina hii inaeleweka wazi mno kiasi kwamba hapana yeyote aliyeikanusha wala kuipinga.

Na kwa kuwa utafiti wetu umetegemea muongozo wa Qur'an na hadithi, basi bila shaka tutayatatua mas'ala haya ndani ya msingi wa Qur'an, na tunatosheka na aya moja tu. Wakati Dhul-Qar-nain alipotaka kujenga ngome dhidi ya mashambulizi ya "Yaajuju" na 'Maajuju" aliwaelekea wakazi wa sehemu hiyo akawaambia:

"Nisaidieni kwa nguvu (zenu wafanyakazi) nitaweka baina yenu na baina yao kizuwizi kilicho imara." Qur'an, 18:94 Namna ya Pili: Kuomba msaada kwa mtu aliye hai (ndani ya ulimwengu huu wa kimaada) ili aombe maombi ya kheri na kutaka msamaha kwa Mwenyezi Mungu, ni katika mambo ya lazima tena yako wazi wala hapana tofauti katika mambo haya baina ya watu wawili. Qur'an Tukufu inasisitiza jambo hilo mahala pengi na tukitazama haraka haraka katika aya tukufu inatuthibitishia kwamba Manabii walikuwa na kawaida ya kuwaombea watu wao mambo ya kheri na uongofu na mafanikio, au kwamba watu wenyewe walikuwa wakiwaomba manabii wao wawaombee mambo mema na maghfira. Aya za Qur'an ni nyingi mno nazo zimegawanyika (katika vigawo) nasi tunazitaja kwa tarakimu kama ifuatavyo:

1. Mwenyezi Mungu anamuamini Mtume wake Muhammad[s.a.w.w] awatakie maghfira umati wake anasema: "Basi wasamehe na uwaombee msamaha (kwa Mwenyezi Mungu) na upime maoni yao katika mambo". Qur'an, 3:159.

2. "Peana nao ahadi na uwatakie maghfira kwa Mwenyezi Mungu bila shaka Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghfira mwingi wa Rehma". Qur'an, 3:159.

3. "Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa sadaka hiyo na uwaombee, hakika maombi yako juu yao kutawapa utulivu, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia, mwenye kujua ." Qur'an, 9:103.

Na ndani ya aya hii ya mwisho Mwenyezi Mungu anamuamuru Nabii wake Muhammad[s.a.w.w] awaombee waumini na kwamba maombi yake yataleta utulivu ndani ya nyoyo zao. Na wakati mwingine Manabii walikuwa wakiwaahidi wenye madhambi na waasi kuwa watawaombea maghfira katika wakati unaokubalika. Kwa mfano Mwenyezi Mungu anasema: "Ila katika usemi wake Ibrahimu kumwambia baba yake, "Bila shaka nitakuombea msamaha". Qur'an, 60:4.

"Nitakuombea msamaha kwa Mola wangu bila shaka yeye ananihurumia sana ". Qur'an, 19:47.

Na haikuwa kwa Ibrahim kutaka maghfira kwa ajili ya baba yake, ila ni kwa sababu ya ahadi aliyompa. Qur'an, 9:144.

Aya hizi tukufu zinajulisha kwamba Manabii walikuwa wakiwabashiria wenye dhambi kuwaombea msamaha, hata Nabii Ibrahim[a.s] alimuahidi "Aazar" kumuombea msamaha, lakini Ibrahim[a.s] alipomuona "Aazar" anaendelea kuabudu masanamu alibadilisha ahadi yake, kwani miongoni mwa sharti za kukubaliwa maombi ni lazima anayeombewa awe anamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu.

5. Mwenyezi Mungu amewaamuru waumini wenye madhambi waende kwa Mtume[s.a.w.w] na waombe awaombee msamaha, kwani Mwenyezi Mungu atawasamehe kwa baraka ya Mtume kuwaombea msamaha. Mwenyezi Mungu anasema:

وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذ ظَّلَمُوا أَنفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّـهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّـهَ تَوَّابًا رَّحِيمًا ﴿٦٤﴾

"Na lau wangelikuja kwako walipojidhulumu nafsi zao wakaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, mjumbe wa Mwenyezi Mungu naye akawaombea msamaha, bila shaka wangemkuta Mwenyezi Mungu ni mwenye kupokea toba na mwenye kurehemu. Qur'an, 4:64.

Ni aya gani basi iliyo wazi kuliko hii ambayo Mwenyezi Mungu anawaamuru wenye dhambi (katika umma huu) waende kwa Mtume[s.a.w.w] na wamuombe awaombee msamaha? Bila shaka kwenda kwa Mtume[s.a.w.w] na kumuomba kuombea msamaha kuna faida mbili: Ya Kwanza: Jambo hili humfanya mtu kuwa na roho ya utiifu na kumfuata Mtume[s.a.w.w] na hii itakuja kutokana na kuelekea na kuufahamu utukufu wa Mtume[s.a.w.w] na heshima yake mbele ya Mwenyezi Mungu kiasi kwamba kumtaka Mtume aombe msamaha kunaleta maghfira ya Mwenyezi Mungu. Na kwa ujumla kufika mbele ya Mtume[s.a.w.w] na kumuomba aombee maghfira kunawajibisha unyenyekevu kwa Mtume na humuandaa mtu kinafsi awe tayari kufuata kauli ya Mwenyezi mungu isemayo: " Mtiini Mwenyezi Mungu na mumtii Mtume. " Qur'an, 4:59.

Ya Pili: Jambo hili linajulisha wazi wazi daraja ya Mtume[s.a.w.w] mbele ya umma, na kuwabainishia kwamba, matokeo ya kimaada kama ambavyo yenyewe yanategemea sababu za kimaumbile, vile vile matokeo ya kiroho, kwa mfano maghfira ya Mwenyezi Mungu yanakuja kwa kupitia sababu maalum, kama vile dua ya Mtume na Mawalii wa Mwenyezi Mungu kumuombea mtu. Kama lilivyojua, ndiyo asili ya mwanga, nguvu na joto na ikawa neema zinawashukia waja wa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya jua, basi neema za Mwenyezi Mungu na kheri zake zinawashukia waja wa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya jua la utume linalong'ara na kuwaenea kwa kheri na rehma.

Bila shaka ulimwengu huu ni ulimwengu wa sababu na visababishaji na neema za kimaada na kiroho zinakuja kwa kupitia sababu zinazozihusu.

4. Kuna baadhi ya aya za Qur'an Tukufu zinafahamisha kwamba, kuna Waislamu ambao walikuwa wakifika kwa Mtume[s.a.w.w] mara kwa mara na kumuomba awaombee dua na maghfira, na Waislamu hao hao walipowataka wanafiki waende kwa Mtume[s.a.w.w] na wamuombe awaombee dua na maghfira, walikataa kama asemavyo Mwenyezi Mungu.

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا يَسْتَغْفِرْ لَكُمْ رَسُولُ اللَّـهِ لَوَّوْا رُءُوسَهُمْ وَرَأَيْتَهُمْ يَصُدُّونَ وَهُم مُّسْتَكْبِرُونَ ﴿٥﴾

"Na wanapoambiwa njooni ili mjumbe wa Mwenyezi Mungu akuombeeni msamaha, hugeuza vichwa vyao na utawaona wanajizuwia na kujiona wakubwa. Qur'an, 63:5.

5. Na kuna baadhi ya aya za Qur'an zinazoshuhudia kwamba, watu kutokana na maumbile yao matukufu walikuwa wakifahamu ya kuwa, dua ya Mtume inayo athari ya pekee kwao, na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hukubali maombi yao bila ya shaka, na kwa ajili hii basi walikuwa wakimuomba awaombee dua na msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Bila shaka watu kwa maumbile yao yaliyosalimika walikuwa wakijua kwamba neema na rehma za Mwenyezi Mungu huzidi kwa kupitia maombi ya Manabii kama ambavyo uongofu wa watu hukamilika kwa kupitia kwa Manabii. Na kwa ajili hii basi, wakawa wanawakusudia na kuwaomba wawaombee msamaha, kama ilivyokuja katika Qur'an tukufu jun ya kisa cha ndugu wa Nabii Yusufu[a.s] baada ya kulitambua kosa lao na mahusiano yao mabaya kwa ndugu yao Yusuf[a.s] Mwenyezi Mungu anasema:

قَالُوا يَا أَبَانَا اسْتَغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا إِنَّا كُنَّا خَاطِئِينَ ﴿٩٧﴾ قَالَ سَوْفَ أَسْتَغْفِرُ لَكُمْ رَبِّي إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٩٨﴾

"Wakasema, Ewe Baba yetu tuombee msamaha kwa dhambi zetu, bila shaka sisi tulikuwa wenye makosa, akasema (Baba yao) nitakuombeeni msamaha kwa Mola wangu, hakika yeye ndiye mwenye kusamehe na mwingi wa kurehemu." Qur'an, 12:97-98.

6. Ziko aya nyingine ambazo Mwenyezi Mungu anamtahadharisha Mtume[s.a.w.w] kuwaombea dua na msamaha wanafiki ambao wanaendelea kuabudia masanamu, na hii ni kwa sababu ibada yao hiyo siyo ibada ya Mwenyezi Mungu, hivyo basi inazuwiya wao kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu hata kama Mtume atawaombea msamaha. Kuzuwiwa kukubaliwa msamaha kwa watu hao ni jambo linalojulisha kwamba, maombi ya Mtume kuwaombea msamaha (watu) yanakubaliwa isipokuwa kwa wale wanaoendelea na ibada ya masanamu (maombi yao) hayawezi kukubaliwa (japo Mtume ndiye atakayeomba), kwa kuwa ibada ya masanamu inazuwiya kukubalika kwa maombi. Kwa hiyo mfano wa maombi ya Nabii kwa watu hao ni kama maji yanayotiririka juu ya ardhi ngumu isiyoweza kupenya maji ndani yake. Mwenyezi Mungu anasema:

إِن تَسْتَغْفِرْ لَهُمْ سَبْعِينَ مَرَّةً فَلَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَهُمْ ﴿٨٠﴾

"Hata ukiwaombea msamaha mara sabini Mwenyezi Mungu hatawasamehe" Qur'an, 9:80.

سَوَاءٌ عَلَيْهِمْ أَسْتَغْفَرْتَ لَهُمْ أَمْ لَمْ تَسْتَغْفِرْ لَهُمْ لَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَهُمْ ﴿٦﴾

"Ni sawa kwao ukiwaombea msamaha au usiwaombee msamaha, Mwenyezi Mungu hatawasamehe". Qur'an, 63:6.

وَلَمَّا وَقَعَ عَلَيْهِمُ الرِّجْزُ قَالُوا يَا مُوسَى ادْعُ لَنَا رَبَّكَ بِمَا عَهِدَ عِندَكَ لَئِن كَشَفْتَ عَنَّا الرِّجْزَ لَنُؤْمِنَنَّ لَكَ وَلَنُرْسِلَنَّ مَعَكَ بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿١٣٤﴾

"Ilipowaangukia adhabu walisema: Ewe Musa tuombee kwa Mola wako kwa yale aliyokuahidi, kama utatuondolea adhabu bila shaka tutakuamini na kwa yakini tutawapeleka wana wa Israel pamoja nawe." Qur'an, 7:134.

Bila shaka katika aya (hii iliyotangulia) watu wenye madhambi walimtaka Nabii Musa[a.s] awaombee. Na ile sentensi isemayo; "Kwa yale aliyokuahidi Mola wako" inajulisha kwamba watu hao walikuwa wakifahamu kuwa Mwenyezi Mungu anayoahadi aliyomuahidi Musa[a.s] . Ama kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema; "Tuombee kwa Mola wako" ina mielekeo namna mbili:

Mwelekeo wa Kwanza: Kuomba kwao kuondolewa adhabu kuwe ni kwa njia ya muujiza, na hii ni kwa sababu ya imani yao juu ya uwezo wa Nabii Musa[a.s] kwa kusaidiwa na uwezo wa Mwenyezi Mungu juu ya jambo hilo. Pamoja na kusihi kwa muelekeo huu, aya hii inaingia ndani ya ile namna ya tatu ya uchunguzi tuliokwishataja, nayo ni kule kumuomba msaada mtu aliye hai kusimamia kazi ambayo ni ya kimuujiza unaokuwa kinyume na sababu za maumbile ya kawaida, na hapo baadaye utakuja uchunguzi wake Insha-Allah Ta'ala. Mwelekeo wa Pili: Ni kutaka kuomba kuondolewa adhabu wala siyo kwa muujiza unaokhalifu mazoweya. Mwelekeo huu wa pili uko dhahiri kwa sababu Maf-humu ya sentensi isemayo "Tuombee kwa Mola wako" inafahamisha kuwa ni kiasi cha kuwa waombewe ili kuondolewa adhabu. Naam.... katika aya hii hakuna ishara inayoonyesha kuwa Mwenyezi Mungu hatakubali maombi ya Musa[a.s] kuwaombea washirikina na waabudu sanamu, bali ishara hiyo imetangulia katika aya zingine.

7. Kuna baadhi ya aya za Qur'an ambazo zinafahamisha kuwa, wapo baadhi ya waumini ambao walikuwa wakiwaombea msamaha baadhi ya waumini wenzao kama ilivyo katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ ﴿١٠﴾

"Na wale waliokuja baada yao wanasema, Mola wetu tusamehe sisi na ndugu zetu waliotutangulia katika imani". Qur'an, 59:10.

8. Zaidi ya waumini hao wanaowaombea msamaha (waumini wenzao) Malaika wanaochukua Ar-shi nao wanawatakia maghfira waumini kama ilivyo kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:

الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيُؤْمِنُونَ بِهِ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً وَعِلْمًا فَاغْفِرْ لِلَّذِينَ تَابُوا وَاتَّبَعُوا سَبِيلَكَ وَقِهِمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ ﴿٧﴾

"(Malaika) wanaoichukua arshi na wale wanaoizunguka wanamtukuza Mola wao na kumsifu na wanamuamini na wanawaombea msamaha walioamini, (na wanasema) Mola wetu umekienea kila kitu kwa Rehma na Elimu, basi wasamehe waliotubu na wakaifuata njia yako na waepushe na adhabu ya moto." Qur'an, 40:7.

Kwa msingi huu basi, ni uzuri ulioje kwetu sisi kuwafuata hawa katika mwendo huu unaoridhiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu ili tuwaombee msamaha wenye madhambi. Mpaka hapa umekamilika utafiti wa ile namna ya kwanza na ya pili, na sasa hebu angalia namna ya tatu. Namna ya Tatu: Namna ya Tatu ni kuomba msaada kwa mtu aliye hai mwenye uwezo wa kafanya muujiza na kuikhalifu ada (mazowea) ili afanye jambo fulani kwa njia hiyo ya muujiza bila kutegemea sababu za maumbile ya kawaida kama vile kumponyesha mgonjwa na kupasua chemchemi ya maji mahala pakavu na mfano wa hayo. Baadhi ya waandishi wakubwa, wanaiona aina hii ya msaada kuwa inaingia katika ile namna ya pili na wanasema: "Makasudio ya muujiza ni mtu kumuomba Mola wake amponye mgonjwa wake au kumlipia deni lake na mengineyo, kwani vitendo hivi vinamuhusu Mwenyezi Mungu peke yake na hayawi maombi ya Nabii au Imam isipokuwa ni wasila tu kwa Mwenyezi Mungu. Na kwa ajili hii basi kuvinasibisha vitendo hivi kwa Nabii au lmam ni katika mlango wa majazi na siyo hakika."[174] Lakini ndani ya Qur'an ziko aya zinazojulisha wazi wazi kuwa kuomba haja hizi kwa Manabii na Mawalii ni jambo sahihi na siyo majazi, kwani sisi tunapomuomba Maasum yeye mwenyewe (mwenye uwezo wa kufanya muujiza) amponye mgonjwa ambaye kuna uzito wa kupona kwake, basi jambo hilo (la kumponyesha) litathibitika kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na nguvu zake. Ni sawa sawa kwamba, Qur'an inakizingatia kitendo cha kuponya ni miongoni mwa mambo makhsusi ya Mwenyezi Mungu. Anasema Mwenyezi Mungu: "Na ninapokuwa mgonjwa Yeye ndiye aniponyeshaye. " Qur'an, 26:80.

Lakini katika kipindi hicho hicho Qur'an inauhusisha uponyeshaji kwenye Qur'an yenyewe na vile vile asali na inasema:

وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا ﴿٨٢﴾

"Na tunateremsha katika Qur'an mambo ambayo ni uponyo na rehma kwa walioamini." Qur'an, 17:82.

يَخْرُجُ مِن بُطُونِهَا شَرَابٌ مُّخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ فِيهِ شِفَاءٌ لِّلنَّاسِ ﴿٦٩﴾

"Kinatoka katika matumbo yao (nyuki) kinywaji chenye rangi mbali mbali ndani yake kinauponyo kwa watu" Qur'an, 16:69.

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ﴿٥٧﴾

"Bila shaka yamekufikieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu na ni uponyo wa yale yaliyomo katika nyoyo." Quran, 10:57.

Suali lililopo sasa hivi ni Je, namna gani tunaweza kuleta muafaka baina ya aya hizi? Jawabu: Mtazamo wa sawa ili kuziweka pamoja aya hizi, yaani zile zilinazohusisha uponyo kwa Mwenyezi Mungu na zile zinazouthibitisha uponyo kwenye asali na Qur'an na Mawaidha ya Mwenyezi Mungu ni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye mtendaji pekee wa mambo kwa kujitegememea kwa dhati yake mwenyewe katika kila kitu, wakati ambapo asali na Qur'an na mawaidha ya Mwenyezi Mungu, vyote hivi vinaathiri katika vitu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na kutaka kwake. Bila shaka mtazamo wa Uislamu juu ya ulimwengu na maisha unayazingatia mambo yote na watendaji wote kuwa ni wenye kufuata utashi wa Mwenyezi Mungu na uwezo wao wa kutenda, umo ndani ya idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na pia sababu zote na illa zote kamwe hazijitegemei japo kidogo katika athari zake pasina tofauti baina ya sababu za kimaumbile na zile za kiroho.

Na kwa msingi huu basi, hapana kizuwizi chochote kwa mujibu wa Qur'an na akili kuwa, Mwenyezi Mungu ambaye ameweka uponyo ndani ya asali na dawa za mimea na zile za kemikali, hakuna kizuwizi cha kuwapa uwezo kama huo Manabii na Maimamu[a.s] . Hebu watazame watu wanaokaa Riyadha[175] ni vipi wanaweza kufanya baadhi ya mambo ya ajabu, basi kuna kizuwizi gani kwa Mwenyezi Mungu kuwapa Manabii na Maimamu uwezo wa kuponyesha na kuwafanya waweze kutenda mambo yanayoishangaza akili na yenye kukhalifu sababu za kimaumbile ya kimaada? Bila shaka uwezo wa Manabii na Maimamu[a.s] juu ya kuponyesha maradhi na kutenda matendo ya kipekee haupingi kuwa Mwenyezi Mungu ndiye sababu halisi na ya msingi wa matendo hayo, lakini tu amewapa uwezo huo ili kuutumia katika ulimwengu kwa idhini yake kila inapohitajika na kwa maslahi.

Na ukweli ulivyo ni kwamba, ndani ya Qur'an Tukufu kuna aya nyingi zinazofafanua wazi kwamba, watu walikuwa wakiwafuata Manabii na wasiokuwa Manabii vile vile ili wafanye mambo ya kipekee yaliyo kinyume na mazoweya na maumbile. Hebu soma baadhi ya aya hizo:

وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ إِذِ اسْتَسْقَاهُ قَوْمُهُ أَنِ اضْرِب بِّعَصَاكَ الْحَجَرَ ﴿١٦٠﴾

"Na tulimfunulia wahyi Musa pale watu wake walipomuomba maji (tukamwambia) lipige jiwe kwa fimbo yako". - Qur'an, 7:160.

Dhahiri ya aya hii inajulisha kwamba wana wa Israil walimtaka Nabii Musa[a.s] baada ya kupatwa na ukame na maji yakakosekana, awape maji kwa njia ya muujiza na siyo kwa njia za kawaida. Na utaona wazi ndani ya aya kwamba, wana wa Israel hawakumtaka Musa[a.s] amuombe Mwenyezi Mungu wapate maji, bali walimtaka awape maji mara moja na bila kutumia sababu za kimaada na ndipo Mwenyezi Mungu alipomuamuru alipige jiwe kwa fimbo yake ili yatoke maji katika jiwe hilo kwa njia ya muujiza. Mwenyezi Mungu Anasema: "Basi mara ghafla zikabubujika chemchem kumi na mbili. " - Qur'an, 2:60.

Aya nyingine iliyo wazi zaidi kuliko hii ni ile inayozungumzia kisa cha Nabii Suleiman[a.s] wakati alipowataka waliokuwa wamehudhuria mbele yake wamletee kiti cha "Bal-Qiis" bila kujali ugumu na vizuwizi vilivyokuwepo njiani (kwani Nabii Suleiman[a.s] alikuwa akiishi Jordan na kiti cha Bal-Qiis kilikuwa Yemen).

Mwenyezi Mungu anasema, akiisimulia kauli ya Suleiman kwa waliokuwa mbele yake:

قَالَ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَيُّكُمْ يَأْتِينِي بِعَرْشِهَا قَبْلَ أَن يَأْتُونِي مُسْلِمِينَ ﴿٣٨﴾

"Ni nani atakayeniletea kiti chake cha enzi kabla hawajaja kwangu bali yakuwa wamekwisha kusilimu". Qur'an, 27:38.

Bila shaka lengo la Suleiman[a.s] lilikuwa ni kukileta kiti cha Bal-Qiis kwa njia isiyo ya kawaida, na hilo lilitimia kwa vitendo kutokana na kutumika njia isiyo ya kawaida kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

قَالَ الَّذِي عِندَهُ عِلْمٌ مِّنَ الْكِتَابِ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَن يَرْتَدَّ إِلَيْكَ طَرْفُكَ فَلَمَّا رَآهُ مُسْتَقِرًّا عِندَهُ ﴿٤٠﴾

"Akasema yule ambaye anayo elumi kutoka katika kitabu, mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako (kufumba na kufumbua) basi alikiona kimewekwa mbele yake". Qur'an, 27:40.

Bila shaka kiini cha maudhui ni ule mtazamo wa baadhi ya watu kwamba, matendo ya kawaida ndiyo yanayomstahikia mtu na matendo ya kipekee ambayo kwa kawaida watu hawayawezi, hayo yanamuhusu Mwenyezi Mungu peke yake, na mtazamo huu ni wa kimakosa kwa sababu kipimo cha kutenganisha baina ya matendo ya Mwenyezi Mungu na yale ya asiyekuwa yeye ni kwamba Mwenyezi Mungu anafanya kwa kujitegemea na wengine wanafanya si kwa kujitegemea. Matendo ya kiungu ni yale ambayo mtendaji mwenyewe (yaani Mwenyezi Mungu) huyatenda bila ya mwingine yeyote kuingilia kati na bila msaada wa nguvu ya wengine.

Na kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, matendo ya kiungu ni yale ambayo mtendaji anakuwa ni mwenye kujitegemea kikamilifu kuyatenda na wala hamhitajii mwingine kabisa kuyatekeleza. Ama matendo yasiyo ya kiungu, sawa sawa yakiwa ni matendo madogo madogo na ya kawaida tu, au yakawa magumu na yasiyo ya kawaida ni yale ambayo mtendaji wake hawi mwenye kujitegemea katika kuyafanya, bali yanakamilika utendaji wake chini ya kivuli cha uwezo kinachojitegemea na nguvu kutoka kwake, nao ni uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa msingi huu basi, hapana kizuwizi kwa Mwenyezi Mungu kuwapa uwezo Mawalii wake wa kufanya matendo yaliyo kinyume na mazowea na maumbile na ambayo kwa kawaida watu wanashindwa kuyafanya. Mwenyezi Mungu anasema kumwambia Nabii Isa[a.s] :

وَتُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ بِإِذْنِي وَإِذْ تُخْرِجُ الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِي ﴿١١٠﴾

"Unaponyesha vipofu na wenye mbaranga kwa idhini yangu na ulipowatoa wafu (makaburini mwao) kwa idhini yangu...." Qur'an, 5:110.

Basi ni kwa kiasi gani aya hii imefafanua dalili ya maudhui haya? Bila shaka mkusanyiko wa aya hizi unajulisha kwamba, Mawalii wa Mwenyezi Mungu walikuwa na uwezo huu na kwamba maombi ya watu kwa Mawalii ili wawafanyie mambo ya kimiujiza lilikuwa ni jambo lililokuwa likifanyika na kufahamika. Ewe msomaji mpendwa, kwa hakika mpaka sasa tumezizungumzia zile namna tatu za kuomba msaada kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu katika zama za uhai wao kwa mujibu wa Qur'an Tukufu na bila shaka umefahamu kwamba Qur'an imeeleza kusihi kwa namna hizo na imesisitizia katika aya nyingi. Ama kuzungumzia zile namna mbili za mwisho ambazo zinahusiana na kuomba msaada kwa roho takatifu tutakuletea katika mlango ufuatao Insha-Allahu Taala.

Mwenye kukaa Riyadha ni yule ambaye hufanya mazoezi magumu ya kiroho ili kuiwezesha roho kufanya mambo yo ajabu, hasa hasa mambo hayo kuwa ni ya kishetani na sio ya kiungu. kwa hiyo huwa yanaondoka mambo hayo anapoacha mazoezi hayo.