15
UCHUNGUZI JUU YA UWAHABI
KUTAKA UOMBEZI TOKA KWA MAWALII WA MWENYEZI MUNGU
Neno "Shafaa" ni maarufu miongoni mwetu sote, nalo tunalitamka mara nyingi katika ndimi zetu katika nyakati na muhala munamo husika. Kwa mfano: Yanapofanyika mazungumzo kumhusu mtu fulani aliyetenda kosa fulani na mahakama imemhukumu kifo au kufungwa au namna nyingine, kisha akatokea mtu akaingilia kati na kumuokoa tokana na hukumu aliyohukumiwa, basi huwa tunasema mtu fulani kamuombea (kanishufaia) fulani.
MAANA YA SHAFAA (KUSHUFAIA)
Neno Shafaa linatokana na shaf'a kwa maana ya jozi ambalo kinyume chake ni witiri na sababu zilizofanya neno "Shafaa" litumike kwa maana ya kile kitendo cha kuombea na "Shafii" kwa maana ya yule mwenye kuombea ni kwamba, juhudi na bidii zifanywazo na huyu mwenye kuombea zinaoana na juhudi na bidii nyingine za kutaka kujiokoa zinazofanywa na yule anayeombewa, na ndipo yule mwenye kutenda makosa au mwenye kutuhumiwa hupata kuokoka kutokana na kuangamia. Uombezi wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu kuwaombea watu wenye madhambi kunakuja kutokana na ukaribu wao hao Mawalii kwa Mwenyezi Mungu, pia daraja yao na heshima yao mbele yake Mwenyezi Mungu. Basi wao huombea watu wenye dhambi kwa idhini ya Mwenyezi Mungu ndani ya masharti maalum ili Mwenyezi Mungu apate kuwasamehe au kuwapokelea maombi yao. Kwa maelezo mengine ni kwamba "Shafaa" ni msaada wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu kwa idhini yake kuwasaidia watu ambao hawakukata maungamano yao ya kidini kwa Mwenyezi Mungu na Mawalii wake, pamoja na kwamba wao ni wenye dhambi.
Taarifu hii ya "Shafaa" imetoa maana ya kina ambayo inapasa kuizingatia muda wote, na kwa maelezo ya namna ya tatu ni kwamba, Shafaa ni msaada wa mtu mwenye daraja ya juu kwa ajili ya mtu wa daraja ya chini, kwa sharti ya kuwepo maandalizi kupokea Shafaa kwa ajili ya ukamilifu wa mafanikio yake na kupanda kwenye daraja ya juu, na kumbadili kuwa mtu mwema mtakatifu. Baada ya taarifu hizi nyingi tunasema: "Historia inathibitisha kwamba, Waislamu tangu zama za Mtume[s.a.w.w]
na baada yake, walikuwa wanaomba "Shafaa" toka kwa Mawalii wema wa Mwenyezi Mungu, sawa sawa Mawalii hao wawe hai au baada ya kufa kwao, na wala hakuna mwanachuoni yeyote wa Kiislamu aliyeifahamu "Shafaa" kuwa inapingana na misingi ya Uislamu, mpaka alipokuja Ibn Taimiyya katika karne ya nane Hijiriya akiwa na mawazo potofu akayapinga mambo mengi miongoni mwa misingi ya Uislamu na mwenendo wa Waislamu. Na baada ya kupita karne tatu tangu yeye Ibn Taimiyya kuzusha fikra hizo alikuja Muhammad bin Abdul-Wahab kutoka Najdi, yeye aliinyanyua juu bendera ya upinzani dhidi ya Waislamu na akazusha fitna na utengano baina yao, pia akaupa uhai uzushi wa Ibn Taimiyya kwa nguvu kuliko hata alivyokuwa Ibn Taimiyya mwenyewe.
Mawahabi wanaitakidi kusihi kiva "Shafaa" katika misingi yake, lakini tofauti iliyo baina yao na Waislamu ni kwamba wao Mawahabi wanaharamisha kuomba "Shafaa" kutoka kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu hapa duniani, na wao wanaeleza itikadi yao hii kwa maelezo machafu yanayoonyesha dharau kwa Manabii na Mawalii kiasi ambacho inatia woga kuyataja hayo wayasemayo Mawahabi. Miongoni mwa maneno wayasemayo ni kwamba "Mtume wa Uislamu yeye na Manabii wengine na Mawalii na Malaika, wanayo haki ya kushufaia huko Akhera tu, lakini kuomba Shafaa ni lazima iwe kwa Mwenyezi Mungu na sio kwao na isemwe kama ifuatavyo: "Ewe Mwenyezi Mungu mfanye Mtume wetu Muhammad[s.a.w.w]
awe muombezi siku ya Qiyama, au Ewe Mwenyezi Mungu wafanye waja wako wema wawe waombezi wetu au Malaika wako au mfano kama huu miongoni mwa mambo ambayo huombwa kwa Mwenyezi Mungu na siyo kwao Mitume na Mawalii na Malaika hapo haiwezi kusemwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu au Ewe Walii wa Mwenyezi Mungu nakuomba "Shafaa" au kitu kingine miongoni mwa mambo ambayo hakuna ayawezaye isipokuwa Mwenyezi Mungu, basi iwapo utaomba "Shafaa" katika siku zao za kuwa katika Bar-zakh basi tendo hilo litakuwa ni miongoni mwa shirki".
Kwa hali hii unawaona Mawahabi wanavyowatuhumu Waislamu eti kuwa wanafanya shirki kwa kuomba "Shafaa" toka kwa Mtume[s.a.w.w]
na Mawalii wa Mwenyezi Mungu hapa duniani na huko Akhera. Sisi kabla ya kuingia katika majadiliano dhidi ya hoja na dalili za Mawahabi kwanza tunaanza kuyachunguza mas-ala hayo ya "Shafaa" kwa mujibu wa Qur'an Tukufu na Sunna pia sera ya Waislamu kisha tuzilete hizo dalili za Mawahabi na tuzichunguze na kuzijadili.
DALILI ZINAZORUHUSU KUOMBA SHAFAA HAPA DUNIANI
Dalili yetu inayoruhusu kuomba Shafaa hapa duniani imefungamana na mambo mawili, na yatakapothibiti mambo hayo, maudhui ya Shafaa itakuwa imekaa wazi kikamilifu. Mambo hayo mawili ni haya yafuatayo:
1. Kuomba Shafaa ni kuomba dua.
2. Kuomba dua toka kwa watu wachamungu ni jambo Mustahabbu katika Uislamu. Sasa hebu angalia uchambuzi wa mambo haya mawili kama ifuatavyo:
1). KUOMBA SHAFAA NI KUOMBA DUA
Uombezi wa Mtume[s.a.w.w]
na waombezi wengine miongoni mwa watu wema si kitu kingine, bali ni maombi yao kwa Mwenyezi Mungu, kwani wao daraja yao na heshima yao ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa sababu ya daraja yao huwa wananyenyekea mbele ya Mwenyezi Mungu kwa dua na kuwatakia maghfira (msamaha) watu wenye dhambi, naye Mwenyezi Mungu huyakubali maombi yao na kuieneza huruma yake kwa waja wake hao wenye kufanya maasi na kuwasamehe na kuyakosha madhambi yao. Kuomba dua kutoka kwa ndugu muumini Muislamu yeyote ni jambo zuri linalopendekezwa (katika Uislamu) na hapana mtu mwenye shaka juu ya ubora wa jambo hili miongoni mwa wanachuoni wa Kiislamu na Madhehebu mbali mbali hata hao Mawahabi wenyewe, basi itakuwaje hali ya dua ya Mtume na Mawalii wema? Bila shaka haiwezekani kusema kwamba Shafaa maana yake ni ile dua ya siku ya kisimamo cha Kiyama, lakini kinachowezekana kusemwa ni kwamba, katika maana zilizo wazi kuhusu Shafaa ni dua na pia kwamba yeyote anayemsemesha mmoja miongoni mwa Mawalii akasema, "Ewe mwenye cheo mbele ya Mwenyezi Mungu tuombee kwa Mwenyezi Mungu", huwa hakusudii ila maana ya dua.
Amepokea Nidhamud-dini An-Nishapuri, kuhusu tafsir ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat an-Nisa aya ya 85 isemayo: "Yeyote atakayeombea maombezi mabaya atakuwa na sehemu katika mabaya hayo." Yeye Nidhamud-din amepokea toka kwa Muqatil amesema: "Shafaa kwa Mwenyezi Mungu maana yake ni kumuombea Muislamu". Na pia imepokelewa kwa Mtume[s.a.w.w]
kwamba, anayemuombea nduguye Muislamu hali ya kuwa hayupo, maombi yake hukubaliwa, nao Malaika husema (kumuambia aliyeomba) nawe upate mfano wa hayo uliyomuombea nduguyo. Hakika huyu Ibn Taimiyya yeye ni miongoni mwa wale ambao wanaofahamu wazi kwamba, kuomba dua kwa mtu aliye hai (akuombee) ni jambo sahihi, na kwa msingi huu basi kutaka Shafaa hakumuhusu Mtume na Mawalii wa Mwenyezi Mungu peke yao, bali pia inafaa jambo hilo kwa kila muumini mwenye daraja tukufu mbele ya Mwenyezi Mungu.
Al-Imam Fakhrudin Razi, ni miongoni mwa wale wanaoifasiri maana ya "Shafaa" kuwa ni dua na ni Kutawas-sal kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Amesema Fakhrudin Razi katika kufasiri kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً ﴿٧﴾
"Na wanawaombea msamaha wale walioamini (kwa kusema), Ewe Mola wetu umekienea kila kitu kwa Rehema." - Qur'an, 40:7.
akasema kama ifuatavyo: "Aya hii inajulisha kuwepo kwa Shafaa toka kwa Malaika kuwaombea waja wenye dhambi.... Na litakapothibiti jambo hili katika haki ya Malaika (kuwaombea wenye dhambi) basi hali itakuwa ni hiyo hiyo katika haki ya Manabii kuwaombea wenye (dhambi) kutokana na kukubaliana Ijmai kwamba hakuna tofauti yoyote kati ya Malaika na Manabii katika jambo hili.
Na amesema vile vile kwamba: Kadhalika Mwenyezi Mungu amemwambia Mtume Muhammad[s.a.w.w]
"Omba msamaha kwa makosa yako na uwatakie msamaha waumini wanaume na waumini wanawake", (Mwenyezi Mungu) akamuamuru Mtume kwanza aombe msamaha kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe kisha awaombee msamaha wengine." Pia Mwenyezi Mungu anasimulia habari za Nuhu
kwamba, yeye Nuhu alisema: "Ewe Mola wangu nisamehe mimi na wazazi wangu na umsamehe yeyote atakayeingia nyumbani mwangu hali ya kuwa ameamini na uwasamehe waumini wanaume na waumini wanawake".
Ufafanuzi huu wa Fakhrur-razi unashuhudia kwamba yeye anaona maana ya Shafaa kuwa ni maombi ya mwenye kumshufaiya mwenye dhambi na kuomba Shafaa ni kuomba dua kwa huyo mwenye kushufaia.
Pia imekuja katika hadithi nyingi za Mtume[s.a.w.w]
kwamba, dua ya Mwislamu kumuombea nduguye Mwislamu ni kumshufaia. Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas naye kapokea toka kwa Mtume[s.a.w.w]
kwamba, Mtume amesema: "Hapana mtu yeyote Muislamu atakayekufa kisha wakasimama kusalia Jeneza lake watu arobaini wasiomshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote isipokuwa Mwenyezi Mungu atakubali uombezi wao kwa mtu huyo".
Kwa hakika imekuja katika hadithi hii matumizi ya maneno Shafaahumullahu fihi kwa ajili ya wale wanaomuombea ndugu yao mwislamu ili kuonyesha maana ya Shafaa kuwa ni dua. Kwa mujibu wa hadithi, lau mtu atawausia (katika uhai wake) watu arobaini miongoni mwa marafiki zake, wasimame kusalia Jeneza lake atakapokufa na wamuombee, basi mtu huyo atakuwa amewaomba watu hao "Shafaa" na atakuwa ameandaa uombezi wa waja wa Mwenyezi Mungu kumuombea nafsi yake. Naye Bukhari katika Sahih yake ametenga mlango maalum akauita "Watu watakapoomba Shafaa kwa Imam awaombee mvua basi asiwakatalie". Na ametenga mlango mwingine pia ambao ameuita "Pindi washirikina watakapoomba Shafaa kwa Waislamu wakati wa ukame".
Na hadithi zote ambazo Bukhari amezitaja katika milango yote miwili zinajulisha kwamba kuomba "Shafaa" ni kuomba dua na wala haifai kuifasiri Shafaa kwa maana nyingine ila hiyo.
Mpaka hapa tumemaliza kutoa dalili ya Shafaa katika sehemu ya kwanza, na imethibiti kwamba, kuomba Shafaa ni kuomba dua wala siyo kinyume chake. Na sasa hivi tunaanza uchunguzi wa maudhui ya pili ambayo ni kwamba, "kumuomba dua Muumini (akuombee) ni jambo mustahabu basi vipi kuomba dua kwa Mitume na Mawalii wa Mwenyezi Mungu?
2). QUR'AN NA KUOMBA DUA TOKA KWA WATU WEMA
Aya nyingi za Qur'an zinashuhudia kwamba Mtume[s.a.w.w]
anapowaombea msamaha kwa Mwenyezi Mungu baadhi ya waja wake ni jambo lenye manufaa sana. Mwenyezi Mungu anasema:
وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ﴿١٩﴾
1. "Omba msamaha kwa makosa yako na uwaombee waumini wa kiume na waumini wa kike". Qur'an, 47:19.
وَصَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صَلَاتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ ﴿١٠٣﴾
2. "Na uwaombee dua, hakika kuwaombea kwako dua kutawapa utulivu (wafanikiwe). Qur'an, 9:103
Iwapo dua ya Mtume[s.a.w.w]
aombapo inaleta matokeo haya mazuri kwa yule anayeombewa, basi kuna kizuwizi gani kwa mtu kuomba kwa Mtume amuombee mtu huyo hali ya kuwa tunajua kwamba kuomba dua ni kuomba Shafaa kwa Mtume. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذ ظَّلَمُوا أَنفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّـهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّـهَ تَوَّابًا رَّحِيمًا ﴿٦٤﴾
"Na lau wangelikujia walipojidhulumu nafsi zao wakaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na Mtume naye akawaombea msamaha, bila shaka wangemkuta Mwenyezi Mungu ni mwenye kupokea toba na mwenye kurehemu". Qur'an, 4:64.
Maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema, "Wangelikujia" ina maana ya kumjia Mtume[s.a.w.w]
na kumtaka awaombee dua na msamaha, lau kama si maombezi ya Mtume kwao hao watu, basi kuja kwao kusingekuwa na maana ila upuuzi na mchezo tu. Kwa hakika kufika kwao mbele ya Mtume[s.a.w.w]
na kuomba kwake dua awaombee msamaha ni dalili ya kuathirika nafsi zao na kupatikana mabadiliko yanayoandaa njia inayofaa ya kukubaliwa dua. Qur'an inawanakili watoto wa Yaqub
ya kwamba, wao walimuomba baba yao awaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu, naye akaitikia maombi yao na akatekeleza ahadi yake. Mwenyezi Mungu anasema:
قَالُوا يَا أَبَانَا اسْتَغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا إِنَّا كُنَّا خَاطِئِينَ ﴿٩٧﴾ قَالَ سَوْفَ أَسْتَغْفِرُ لَكُمْ رَبِّي ﴿٩٨﴾
"Wakasema, Ee baba yetu tuombee msamaha kwa makosa yetu, hakika sisi tulikosea, akasema nitakuombeeni msamaha kwa Mola wangu..." Qur 'an, 12:97-98.
Aya zote hizi zinajulisha kwamba kuomba dua kwa Manabii na watu wema jambo ambalo ndiyo kuomba Shafaa halipingani na hukumu za kisheria, kanuni na mizani ya Kiislamu. Ewe msomaji Mtukufu, ziko hadithi nyingi zinazohusu kuomba dua kwa waja wema na Mawalii, lakini tumeziacha ili kufupisha maelezo.
3).HADITHI ZA MTUME NA SERA YA MASAHABA
Tirmidhi amepokea ndani ya Sahih yake kutoka kwa Anas kwamba amesema: "Nilimuomba Mtume[s.a.w.w]
aniombee siku ya Qiyama akasema, mimi nitafanya, mimi nikasema, basi nitakuona wapi siku hiyo? Akasema: kwenye Sirat.
Hadithi nyingine ni ile ambayo Sawad bin Qarib alipokuja kwa Mtume[s.a.w.w]
akimtaka amshufaiye akasema katika beti za kishairi alizoziimba: "Uwe wewe Mtume ndiyo muombezi wangu katika siku ile (ambayo) hakuna mwenye kuombea atakayemnufaisha Sawad bin Qarib japo kidogo.
Na yapo maelezo yaliyokuja katika historia kwamba, kuna mtu mmoja aliyekuwa akiitwa "Tub-baa", na aliishi miaka zaidi ya Elfu moja kabla ya kudhihiri Mtume[s.a.w.w]
., pia habari za kudhihiri kwa Nabii wa zama za mwisho kutoka Makka zilikwisha kumfikia, basi aliandika maandiko akayatoa kwa baadhi ya jamaa zake ili wamfikishie Mtume[s.a.w.w]
., ndani ya maandishi hayo alieleza imani yake na Uislamu wake na kwamba yeye ni katika umati wa mjumbe wa Mwenyezi Mungu[s.a.w.w]
. Akasema katika maandiko hayo: "Iwapo sitakuwahi (Ewe Muhammad) basi niombee siku ya Qiyama usinisahau". Bwana huyu alifariki, lakini maandiko yake yakawa yanapokewa toka kwa mtu hadi kwa mwingine mpaka alipodhihiri Mtume[s.a.w.w]
. Na yalipomfikia maandishi haya mikononi mwake, Mtume[s.a.w.w]
alisema, "Karibu ewe ndugu mwema" mara tatu".
Basi iwapo kuomba Shafaa ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu, Mtume asingemwita yule "Tub-baa" kuwa ni 'Ndugu mwema" na wala asingesema mara tatu "karibu". Hizi ni baadhi ya hadithi ambazo zinathibitisha kuruhusu kuomba dua na uponyo toka kwa Mtume[s.a.w.w]
zama za uhai wake.
4). KUOMBA SHAFAA BAADA YA KUFA
Zipo riwaya nyingi zinazofahamisha kwamba Masahaba walikuwa wakiomba Shafaa kwa Mtume[s.a.w.w]
baada ya kufa kwake. Hebu tazama baadhi ya mifano ifuatayo:
1. Ibn Abbas amesema: "Pindi Amiril-Mu'minina Ali
alipomaliza kumkosha Mtume[s.a.w.w]
alisema; "Baba na mama yangu wawe fidia kwako unapendeza ukiwa mzima au umekufa.... tukumbuke mbele ya Mola wako.
"
2. Na imepokelewa kwamba, alipofariki Mtume[s.a.w.w]
, Abu Bakr alimfunua Mtume usoni kisha akaumbusu na akasema: "Baba na mama yangu wawe fidia kwako unapendeza ukiwa mzima au umekufa, tukumbuke mbele ya Mola wako".
Riwaya mbili hizi na nyingine kama hizi zinajulisha kwamba, hakuna tofauti baina ya kuomba Shafaa kwa muombezi katika hai wake, na baada ya kufa kwake, na Masahaba walikuwa wakiomba dua kwa Mtume[s.a.w.w]
baada ya kufariki kwake. Ikiwa kuomba dua kwa Mtume[s.a.w.w]
baada ya kufa kwake ni jambo sahihi basi kuomba Shafaa ambayo ni aina za dua itakuwa ni sahihi pia. Kwa ufupi, kwa kutegemea aya na riwaya pamoja na sera ya Waislamu kwa karne nyingi zilizopita kuomba Shafaa ni jambo litakalozingatiwa kuwa ni sahihi moja kwa moja wala hakuna nafasi ya kufanyia shaka jambo hili kabisa.
DALILI ZA MAWAHABI ZA KUHARAMISHA KUOMBA SHAFAA
Tumetaja ndani ya mlango uliopita dalili zinazoruhusu kuomba Shafaa, zikiwemo hadithi mbali mbali na aya za Qur'an. Sasa hivi umefika wakati wa kutaja dalili za Mawahabi ambazo wanadai kwamba zinaharamisha Shafaa, zikiwemo hadithi mbali mbali na aya za Qur'an. Huu ndiyo ule wakati muafaka wa kutaja zile dalili za Mawahabi ambazo wanadai kwamba zinaharamisha Shafaa na kuzijadili (ili Mwenyezi Mungu aithibitishe haki kwa maneno yake). Mawahabi wametolea ushahidi mambo kadhaa katika kuharamisha Shafaa, nasi tunayataja kama ifuatavyo:
1) WANASEMA: "KUOMBA SHAFAA NI KUMSHIRIKISHA MWENYEZI MUNGU"
Wanachokikusudia Mawahabi katika shirki ni ile shirki ndani ya Ibada, kiasi wanadai kwamba kuomba kwa huyo anayeshufaiya ni kumuabudu. Katika mlango uliopita tumeeleza kwa upana maana ya Ibada na tumetaja kwamba, ombi Ia mtu kuomba Shafaa litakuwa Ibada tu ikiwa litatolewa na muombaji haliya kuwa anaitakidi kuwa huyo mwenye kuombwa Shafaa ni Mola au ni Mungu au yeye ndiye asili ya kupatikana matendo ya Mwenyezi Mungu, na kwamba muombeaji huyo ndiyo msimamizi halisi wa mambo ya ulimwengu na anasimamia yote ambayo (kwa asili na ukweli) yanarejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu (kuwa ndiyo muumba wa mambo hayo).
Hakika (ilivyo ni kwamba) mtu anayeomba Shafaa kwa waombeaji ambao Mwenyezi Mungu amewapa idhini ya kuombea, huwa anaitakidi kuwa wao ni waja wa Mwenyezi Mungu waliokaribu naye na ni watukufu na wenye heshima mbele ya Mwenyezi Mungu.
Hapana itikadi ya kuwa wao ni Miungu au eti wao ndio asili ya matendo ya Mwenyezi Mungu, na hakuna itikadi ya kuwa eti uombezi huo au msamaha wa Mwenyezi Mungu umetegemezewa kwao moja kwa moja bila ya kuhitajia idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hakuna kabisa itikadi za aina hiyo, kwani waombeaji hao wema huwa wanaombea kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kumuombea anayestahiki hiyo Shafaa na hii ni kwa sababu ya kuwepo maungamano yao ya kiroho ambayo hayakatiki. Ukweli unaojitokeza ni kwamba, lau kama kuomba shafaa kwa mtu aliyekufa maana yake itakuwa ni kumuabudu, basi kuomba Shafaa kwa mtu aliye hai pia itakuwa ni kumuabudu.
Katika mlango uliotangulia tumetaja kwamba Qur'an inawataka Waislamu waende kwa Mtume[s.a.w.w]
na wamuombe awaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu, hivyo basi ombi hili kwa Mtume[s.a.w.w]
ni kuomba Shafaa katika zama za uhai wake na haiwezekani tendo hili la kumuomba Mtume Shafaa liwe ni shirki katika wakati fulani na wakati mwingine liwe ni tendo la tauhidi ya Mwenyezi Mungu. Kama ambavyo tumetaja pia katika mlango wa kuomba msaada kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu kwamba, "Iwapo kuomba Shafaa kwa Walii mwema, hakutakuwa kwa kumuitakidia Uungu Walii huyo, basi Shafaa hiyo haitazingatiwa kuwa ni shiriki kabisa. Kwa mfano Mwenyezi Mungu anasema: "
Peke yako tu tunakuomba msaada
". Qur'an, 1:5.
Hapa ina maana kwamba msaada ni jambo linalomuhusu yeye Mwenyezi Mungu peke yake. Baadaye Mwenyezi Mungu anasema: "Tafuteni msaada kwa kusubiri na kuswali
". Qur'an, 2:45.
Basi je mtu anaweza kusema kwamba kutafuta msaada kwa kusubiri ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu? Moja kwa moja jibu lake ni hapana, kwani kutaka msaada kulikoharamishwa ni kule kutakakoambatanishwa na itikadi ya uungu wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, jambo ambalo hakuna anayeliamini miongoni mwa Waislamu.
2) WASHIRIKINA NA UOMBEZI WA MASANAMU
Baada ya kuibatilisha dalili ya kwanza ya Mawahabi inayoharamisha kuomba Shafaa kwa Mawalii, sasa ni wakati mwingine na kuibatilisha dalili ya pili ambayo ni: "Mwenyezi Mungu aliwazingatia wanaoabudu masanamu kuwa ni washirikina kwa kuwa wao walikuwa wakiomba Shafaa kwa masanamu yao, na walikuwa wakilia mbele ya masanamu hayo na kuyaomba uwakala kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ ﴿١٨﴾
"Wanaabudu visivyokuwa Mwenyezi Mungu, vitu ambavyo haviwezi kuwadhuru wala kuwanufaisha, na (walipoulizwa kwa nini wanaviabudu) husema hawa ni waombezi wetu mbele ya Mwenyezi Mungu". Qur'an, 10:18.
Na kwa msingi huu basi, kumuomba Shafaa asiyekuwa Mwenyezi Mungu kwa ujumla kutafahamika kuwa ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu na ni kumuabudu muombezi huyo.
JAWABU LA MADAI HAYO
Kwanza
: Katika aya hii hakuna kabisa dalili yoyote iliyopo wanayoidhani Mawahabi kuwa inawaunga, kwani Qur'an kwa mujibu wa aya hii inapowaona watu hao kuwa ni washirikina siyo kwa ajili ya kuomba Shafaa kwa masanamu bali ni kwa sababu ya wao kuyaabudu Ibada ambayo imewapelekea wayaombe Shafaa vile vile. Na kama ingekuwa kile kiasi cha kutaka Shafaa kwa masanamu ni kuyaabudu jambo ambalo lingewajibisha shirki, kusingekuwa na haja yoyote kwa Mwenyezi Mungu kusema "na wanasema kuwa hawa ni waombezi wetu" bali kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo "Wanayaabudu" ingetosha kuwahusisha watu hao na ushirikina, lakini kuongezeka kwa sentensi ile ya pili baada ya ile ya kwanza ni dalili ya kwamba vitu hivyo viwili ni tofauti na pia kwamba maudhui ya kuabudia masanamu ni tofauti na maudhui ya kutaka Shafaa kwa hayo masanamu. Kwa hakika kuyaabudu Masanamu ni dalili ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, ama kuomba Shafaa kwa jiwe au ubao ni dalili ya ujinga na kukosa akili, pia ni kutokuwa na busara.
Zaidi ya hapo aya hii tuliyoitaja hapo kabla haijulishi kwamba kutaka Shafaa kwa masanamu ni kuyaabudu, basi vipi itawezekana kuzingatia kuwa kuomba Shafaa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni dalili ya kuwaabudu Mawalii hao? Kwa hiyo aya hii haina mafungamano kabisa na maudhui ya Shafaa. Pili: Hebu tukadirie (kama mjadala) kwamba sababu ya shirki kwa watu hao waliotajwa ndani ya aya ni kule kuomba kwao Shafaa kwa masanamu, lakini ieleweke pia kwamba baina ya hao washirikina kuomba kwao Shafaa kwa masanamu na Waislamu kuomba Shafaa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, kuna tofauti kubwa na kuna utengano mfano wa masafa yaliyopo baina ya mbingu na ardhi, hasa kwa kuwa washirikina hao walikuwa wakiamini kuwa, masanamu hayo yanaimiliki hiyo Shafaa na msamaha kama kwamba Mwenyezi Mungu hahusiki kabisa katika mambo hayo mawili, na waliyaona hayo masanamu ndiyo yenye uamuzi wote wa kusamehe na kushufaiya.
Basi ukweli uko wazi kusema kwamba kuomba Shafaa kwa namna hii itakuwa ni kuyaabudu masanamu hayo kwa kuwa Shafaa hii imeambatanishwa na itikadi ya uungu kwa masanamu hayo na vile vile yenyewe kufanywa ndiyo chimbuko la matendo ambayo ni ya Mwenyezi Mungu katika hali ya kuendesha ulimwengu. Kwa hiyo basi Mwislamu huwa anaomba Shafaa na dua kwa huyo mwenye kushufaiya hali ya kumuitakidi kwamba yeye ni mja aliyekurubishwa kwa Mwenyezi Mungu na ni mja mwenye heshima na utukufu aliyepewa ruhusa ya kuombea toka kwa Mwenyezi Mungu. Ewe msomaji, hivi kudai kwamba hakuna tofauti baina ya Shafaa hizi mbili (iliyofanywa na washirikina kwa masanamu yao na ile ifanywayo na Waislamu kwa Mitume na Mawalii) ni kupingana na akili na mantiki na ni kuacha uadilifu? Je, huoni tofauti iliyopo kati ya mambo haya mawili kama unavyoweza kuona tofauti baina ya kiza Ia usika na mwangaza wa mchana?
3).KUTAKA HAJA KWA ASIYEKUWA MWENYEZI MUNGU NI HARAMU
Baada ya kuivunja dalili ya pili ya Mawahabi inayoharamisha kuomba Shafaa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, sasa inakuja dalili yao ya tutu. Nayo ni ile inayokataza kumuomba na kumtaka haja asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kudai kwamba kuomba Shafaa kwa Mawalii ni namna ya kutaka haja, basi jambo hili ni haramu kwani Qur'an inaeleza wazi wazi kama ifuatavyo: Mwenyezi Mungu amesema, "Msimuombe yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu
". Qur'an, 72:18.
Kuikusanya kauli inayoharamisha kumuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu na kauli inayothibitisha kupatikana uombezi wa Mawalii nikumuomba Mwenyezi Mungu awaamuru Mawalii wake wamuombee mwanadamu. Na dalili ya kwamba kumuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni kumuabudu huyo anayeombwa ni kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ ﴿٦٠﴾
"Niombeni nitakubali maombi yenu, hakika wale wajivunao kufanya Ibada yangu wataingia Jahanamu wadhalilike." Qur'an, 40:60.
Pindi tukiifanyia mazingatio aya hii tutaiona imeanza kwa tamko la 'Ad-dawat" kwa maana ya maombi, na imemalizikia kwa tamko la "Ibada". Basi hali hii inatuonyesha kwamba, Maf-humu ya maneno haya mawili ni moja. Imepokewa kwa Mtume[s.a.w.w]
amesema: "Dua ndiyo kiini cha Ibada
".
Jawabu Letu: Kwanza Tunasema: Siyo kweli kwamba makusudio ya kuharamisha kumuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu katika aya iliyotajwa ni kuharamisha maombi kwa ujumla, lakini makusudio yaliyopo kwenye aya hiyo ni kuharamisha "kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu". Ushahidi wa jambo hili uko mwanzoni mwa aya aliposema Mwenyezi Mungu, "Na kwa hakika misikiti yote ni ya Mwenyezi Mungu basi msimuombe (msimuabudu) yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu
".
Kwa hiyo basi mkusanyiko uliomo katika aya unajulisha kwamba dua iliyoharamishwa ni ile inayochanganywa na Ibada na kuitakidi uungu wa huyo anayeombwa na pia kuitakidi uwezo wake wa kuamua katika mambo ya viumbe na ulimwengu. Ukweli ulivyo ni kwamba, itikadi kama hii haipo miongoni mwa Waislamu ambao huomba Shafaa kwa mawalii wa Mwenyezi Mungu.
Pili
: Kwa hakika kinachoharamishwa ndani ya aya hiyo nakukatazwa ni kumuabudu Mwenyezi Mungu pamoja na mwingine na kumfanya huyo kuwa yeye ni sawa na Mwenyezi Mungu katika dua (Ibada), kama inavyojulisha sentensi iliyoko kwenye aya isemayo "pamoja na Mwenyezi Mungu" yaani sawa naye. Basi iko haja ifahamike kwamba, mtu anapomuomba Mtume[s.a.w.w]
. anyenyekee kwa Mwenyezi Mungu kumuombea mtu huyo ili shida yake itatuliwe au asamehewe makosa yake haina maana kwamba mtu huyu atakuwa amemuomba (yaani amemuabudu) Mwenyezi Mungu pamoja na mwingine bali maombi haya ukweli wake ni kumuomba yeye Mwenyezi Mungu peke yake.
Na ikiwa ziko baadhi ya aya za Qur'an zinazofahamisha kuwa, kutaka haja kwa masanamu ni ushirikina, hiyo ni kwa sababu watu hao walikuwa wakiamini masanamu hayo kuwa ni Miungu wadogo wenye kumiliki kikamilifu maamuzi ya matendo ya Mwenyezi Mungu yote au sehemu yake, na ndiyo maana utaiona Qur'an inaikosoa fikra hii potofu. Qur'an inasema:
وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَكُمْ وَلَا أَنفُسَهُمْ يَنصُرُونَ ﴿١٩٧﴾
"Na wale muwaombao kinyume cha Mwenyezi Mungu hawawezi kukusaidieni wala kujisaidia wenyewe nafsi zao"- Qur'an, 7:197.
Pia Qur'an inasema:
إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ عِبَادٌ أَمْثَالُكُمْ ﴿١٩٤﴾
"Bila shaka hao muwaombao kinyume cha Mwenyezi Mungu ni viumbe kama ninyi". Qur'an, 7:194.
Kwa kufupisha maelezo ni kwamba, washirikina walikuwa wakiamini kuwa masanamu hayo ni miungu wadogo na kwamba matendo ya Mwenyezi Mungu yameegemezwa kwao moja kwa moja, lakini kuomba Shafaa na dua kwa mtu ambaye Mwenyezi Mungu amempa cheo hiki na haki hii hatuamini kwamba wao ni Miungu wadogo au matendo ya Mwenyezi Mungu yameegezwa kwao, basi kuna tofauti kubwa baina ya itikadi ya washirikina na itikadi ya utukufu wa walii mwema na mwenye heshima mbele ya Mwenyezi Mungu na kutaka kwake msaada mbele ya Mwenyezi Mungu. Je, Mawahabi hawana uadilifu wala hawatazami vitu kama vilivyo? Je, hawana akili kabisa?
Tatu
: Kwa hakika neno 'Ad-dawah" lina maana pana kiasi kwamba wakati mwingine hutumika kimajazi kwa maana ya "Ibada" kama ambavyo (Mawahabi) walivyolitolea ushahidi katika aya ya 60 sura ya 7 tuliokwisha itaja hapo kabla, na pia katika hadithi ambayo tumeitaja huko nyuma. Lakini tunajua wazi kwamba matumizi haya ya kimajazi hayatoshi kuwa ni ushahidi wa kufasiri maana ya dua kuwa ni ibada kila wakati, au ushahidi wa madai kwamba kuomba haja kwa yeyote ni ushirikina.
4). SHAFAA NI HAKI INAYOMUHUSU MWENYEZI MUNGU TU
Ewe msomaji mpendwa, tumeibatilisha dalili ya tatu ya Mawahabi na sasa tunaitaja dalili yao ya nne ambayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
أَمِ اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ شُفَعَاءَ قُلْ أَوَلَوْ كَانُوا لَا يَمْلِكُونَ شَيْئًا وَلَا يَعْقِلُونَ ﴿٤٣﴾ قُل لِّلَّـهِ الشَّفَاعَةُ جَمِيعًا لَّهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٤٤﴾
"Au ndiyo wamejifanyia waombezi mbele ya Mwenyezi Mungu, waambie: Ijapokuwa hawana mamlaka juu ya kitu chochote wala hawatambui lolote? Waambie uombezi wote uko katika milki ya Mwenyezi Mungu". Qur'an, 39:43-44.
Makusudio ya kutolea ushahidi aya hii, ni kubainisha kwamba Shafaa ni jambo linalomuhusu Mwenyezi Mungu tu, kwa hiyo basi kuna maana gani kutaka Shafaa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu? Jawabu Lake: Mwenyezi Mungu aliposema kwamba "Uombezi wote uko katika milki ya Mwenyezi Mungu" siyo maana yake kwamba Shafaa ni jambo linalo muhusu yeye Mwenyezi Mungu na hakuna mwingine mwenye haki ya kuombea. Na hii ni kwa sababu, hapana shaka kabisa kwamba, Mwenyezi Mungu hamuombei mtu fulani kwa (Mola) mwingine, bali maana iliyokusudiwa hapo ni kuwa, yeye Mwenyezi Mungu ndiye mwenye asili ya mamlaka ya Shafaa wala siyo masanamu, na hiyo ni kwa kuwa muombezi (mwenye kushufaiya) ni lazima kwanza awe na akili na utambuzi, na aweze huko kuombea kwa upande wa pili, kitu ambacho masanamu yamekosa sifa hizi mbili: Na kwa ajili hii Mwenyezi Mungu amesema:
Kwanza
: "Waambie japokuwa hawana mamlaka juu ya kitu cho chote"?
Pili
: "Wala hawatambui lolote?" Kwa hiyo aya inasisitiza kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiyo mwenye mamlaka ya Shafaa siyo masanamu, na pia kwamba Mwenyezi Mungu humpa jambo hili (la Shafaa) mtu ambaye zimetimia sifa zinazostahiki kuwaombea waja wa Mwenyezi Mungu. Hivyo basi aya hii haina uhusiano na maudhui tunayoyazungumzia, hasa inapozingatiwa kwamba Waislamu wanaamini kuwa, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye mamlaka ya Shafaa na wala siyo Mawalii wake, kadhalika Waislamu wanaamini kwamba yeyote ambaye Mwenyezi Mungu amempa ruhusa ya kuombea, basi anao uwezo wa kuombea kinyume cha mtu ambaye hakupewa ruhusa hiyo. Hali hii ya kushufaiya ndiyo ile ile ambayo Waislamu wanayoitakidi kwa kutegemea aya za Qur'an na hadithi kwamba, Mwenyezi Mungu amempa idhini Mtume[s.a.w.w]
yeye na watu wa nyumba yake
ya kuombea, nasi kwa sababu hiyo basi tunaomba Shafaa yao. Kwa hiyo Ewe msomaji imekudhihirikia kutokuwepo uhusiano baina ya aya hizo na uchunguzi huu na kutokuwepo uhusiano bania ya hadithi waliyoitaja na uchunguzi huu.
5). UPUUZI WA KUTAKA SHAFAA KWA MAITI
Dalili ya mwisho ya Mawahabi juu ya kuharamisha Shafaa kwa Mawalii inasema kwamba: "Kuomba Shafaa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu katika maisha haya (ya duniani) ni sawa na kuomba haja kwa maiti asiyesikia". Mawahabi wametolea ushahidi madai yao haya kwa aya mbili zifuatazo:Kwanza
:
إِنَّكَ لَا تُسْمِعُ الْمَوْتَىٰ وَلَا تُسْمِعُ الصُّمَّ الدُّعَاءَ إِذَا وَلَّوْا مُدْبِرِينَ ﴿٨٠﴾
"Kwa hakika huwezi kuwasikilizisha wafu mwito, wala kuwasikilizisha viziwi wanapogeuka wanakwenda zao". Qur'an, 27:80.
Makusudio ya kutolea ushahidi wa aya hii ni kwamba, Qur'an Tukufu imewafananisha washirikina na maiti na aya hii inamwambia Mtume[s.a.w.w]
kwamba yeye hawezi kuwafahamisha washirikina hawa kwani wao nikama maiti hawasikii, kwa hiyo lau maiti wangekuwa wanao uwezo wa kusema na kusikia basi isingefaa washirikina kufananishwa na maiti.Pili
:
إِنَّ اللَّـهَ يُسْمِعُ مَن يَشَاءُ وَمَا أَنتَ بِمُسْمِعٍ مَّن فِي الْقُبُورِ ﴿٢٢﴾
"Bila shaka Mwenyezi Mungu humsikilizisha amtakaye na wewe huwezi kuwasikilizisha waliomo makaburini". Qur'an, 35:22.
Kutolea ushahidi aya hii ni sawa na ushahidi uliotolewa katika aya iliyotangulia kwa kutokuwepo uwezekano kwa maiti kusikia na kusema. Kwa hiyo basi kuwaomba (maiti) Shafaa ni kama kukiomba Shafaa kitu kisicho uhai, kama vile mawe n.k.
Jawabu Letu
: Bila shaka Mawahabi wamelifanya suala la shirki kuwa ndiyo ngao yao kila wanapoyakosoa madhehebu mbali mbali ya Kiislamu na kuwatuhumu Waislamu kwa ukafiri nyuma ya pazia la kutetea Tauhidi ya Mwenyezi Mungu na kuihusisha kwake Ibada. Lakini Mawahabi walipotolea ushahidi aya hizi wamebadilisha usulubu wao wakang'ang'ania usemi wao kuwa "kuomba Shafaa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni jambo la upuuzi wala halina faida, kwa kuwa Mawalii hao wamekwisha kufa". Mawahabi hawa ambao Qur'an hawaifahamu vilivyo, wamejisahaulisha na kupuuza hata zile hoja za kiakili na sheria ambazo zinathibitisha kuwa hai kwa Mawalii hata baada ya kufa. Wanafalsafa wa Kiislamu wamethibitisha kwamba, baada ya roho kujitenga na mwili na kutoutegemea, yenyewe hubakia milele na kuishi maisha yanayohusiana na roho na ufahamu wa kiroho. Wanafalsafa wanaomuitakidi Mwenyezi Mungu wametaja dalili kumi za kiakili kuhusu jambo hili, kiasi kwamba hazikuacha nafasi ya mashaka na wasi wasi ndani yake kwa kila mtu muadilifu na mwenye akili. Zaidi ya hizo dalili za kiakili, Qur'an ambayo ni kitabu cha Mwenyezi Mungu imetangaza wazi wazi kuwepo kwa uhai baada ya kufa, pia ziko hadithi nyingi za Mtukufu Mtume[s.a.w.w]
kuhusu jambo hili. Ili kuthibitisha unaweza kurejea katika Qur'an aya zifuatazo:
1) Aya 169-170 Sura ya 32) " 41 " 4.3) " 45 " 33.4) " 100 " " 23.5). " 46 " " 40.
Zote hizi zinathibitisha juu ya kuwepo uhai baada ya kifo. Basi ina hali gani hoja yenu dhaifu enyi Mawahabi? Na Je, zinamaanisha nini basi aya hizo mbili? Jawabu Lake: Bila shaka aya hizo mbili zinamaanisha kwamba, miili iliyolala makaburini haina uwezo wowote wakufahamu kitu, jambo ambalo linakubalika moja kwa moja, kwani mwili unapotengana na roho kinachobakia ni kitu (kiwiliwili) kisicho na fahamu wala akili. Lakini lazima ieleweke kwamba nukta muhimu tunayozungumzia hapa ni kwamba, wale ambao sisi tunawasemesha na kuwaomba Shafaa kama ambavyo Qur'an inasisitiza "siyo kiwiliwili kilichozikwa katika udongo bali ni roho takatifu zilizo hai ndani ya miili ya Bar-zakh katika ulimwengu wa Bar-zakh." Hivyo basi, ilivyokuwa hakuna uwezekano wa miili iliyozikwa ardhini kufahamu cho chote, hali hii haimaanishi kwamba roho takatifu za miili hiyo ambazo ni hai na zinaruzukiwa huko kwenye ulimwengu wa Bar-zakh eti nazo haziwezi kufahamu kitu. Na ifahamike pia kwamba, salamu, maamkizi na ziyara (zifanywazo na Waislamu kwa Mawalii) ni kwa ajili ya roho zenye nuru zinazobakia milele na ndizo zinazoombwa Shafaa. Na pengine utajiuliza, ni kwa nini Waislamu wanayazuru Makaburi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu? Jawabu: Ni kwa sababu ya mambo yafuatayo:
1. Zimekuja hadithi mutawatiri za Mtukufu Mtume[s.a.w.w]
zinazohimiza kuzuru makaburi ya Mawalii, na katika mstari wa mbele wa hao katika umuhimu, ni Mtume[s.a.w.w]
na watu wa nyumba yake watakatifu (amani ya Mwenyezi Mungu iwashukie), na kuna thawabu nyingi na radhi za Mwenyezi Mungu katika ziyara za makaburi hayo, nasi hapo kabla tumetaja baadhi ya hadithi zilizohimiza kuhyazuru wakati tulipokuwa tukizungumzia kuhusu kumzuru Mtume[s.a.w.w]
.
2. Kuyazuru makaburi yao huwa kunaijenga hali ya kuwepo kwao (miongoni mwetu) na kuziandaa nafsi zetu kuwasiliana na roho zao tukufu, na hali zao za kiroho na wakati tunapowatolea salamu huwa tunajihisi kama kwamba tunaongea nao hali ya kuwa wanatusikiliza, kama ilivyokuja katika moja ya ziyara iliyowekwa na hao maasumin. "Nashuhudia kwamba wewe unashuhudia kisimamo changu na unayasikia maneno yangu, na kwamba wewe ni hai mbele ya Mola wako unaruzukiwa, basi muombe Mola wako ambaye ndiye Mola wangu anikubalie haja yangu.
Kadhalika yemekuja mapokezi yasemayo: "Ewe Mwenyezi Mungu...Mimi nafahamu pia kwamba, Mtume wako na Makhalifa wako
wako hai mbele yako wanaruzukiwa, wanakiona kisimamo changu na wanasikia maneno yangu na wanajibu salamu yangu na wewe Mola wangu umeweka kizuwizi kwangu mimi kutoyasikia maneno yao (lakini) umefungua mlango wa fahamu zangu ili nipate utamu wa kuwazungumzisha".
3. Kuna hadithi tukufu chungu uzima zinazobainisha kwamba miili ya Manabii na Mawalii na wengineo pia hubakia katika udongo hali ya kuhifadhika bila ya kuharibika kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Jambo hili linayo masimulizi mengi na matukio mengi ambayo nafasi hairuhusu kuyaeleza. Tunatosheka kuashiria tukio lililotajwa na wanahistoria kwamba, Waislamu walichimba mifereji ya maji katika ardhi ya Uhdi huko Madina, miaka hamsini baada ya tukio la vita vya Uhdi. Walipokuwa wakichimba wakafukua miili iliyovuja damu ikiwa mizima kabisa kama kwamba imezikwa sasa hivi, kiasi hata sanda zake hazijaharibika. Habari za tukio hili zilipofika mjini Madina, watu walitoka mbio wakiwemo Masahaba na wengineo hata kina mama pia walitoka kwenda kushuhudia na waliitambua miili ya maiti hao kwa majina yao na majina ya wazazi wao na kwamba miili hiyo ilikuwa ya mashahidi wa Uhdi.
Miili hiyo ilibakia katika hali ya usalama ikazishinda zama na mchanga (kutoiharibu) kwa idhini ya Mwenyezi Mungu muweza. Ikiwa miili ya mashahidi hawa imeweza kubakia katika hali hii, basi vipi mwili wa Mtume[s.a.w.w]
na Maimamu watukufu wa kizazi cha Mtume? Hapana shaka miili yao itabakia katika hifadhi dhidi ya kila aina ya uharibufu hasa kwa kuwa miili hiyo inao utukufu mkubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Vile vile sehemu ambayo umezikwa mwili wa mmoja wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, inapata utukufu kwa ajili ya Walii huyo, hivyo basi kufika mahali hapo patukufu huwa panamsababishia mtu kupata rehma na baraka za Mwenyezi Mungu. Mpaka hapa ewe msomaji, imekudhihirikia kwamba, dalili wazitumiazo Mawahabi kuharamisha kuomba Shafaa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni dalili dhaifu, na ukweli ni ule ambao Waislamu wanautenda kwa kufuata Qur'an na hadithi tukufu za Mtume[s.a.w.w]
.