HADITHI ZA MTUME (S.A.W.W)
KIMETARJUMIWA NA: DUCTOOR A KADIRI
TAASISI YA FIKRA ZA KIISLAMU (ISLAMIC THOUGHT CENTRE)
TEHRAN
Kwa jina Ia Mwenyezi Mungu. Mwingi warehema. Mwenye kurehemu. Sifa zote ni kwa Mwenyezi Mungu Aliyetuokoa na ujahiliya wa zamani. Tunamwomba Atujaalie pia kuutupilia mbali ujahiliya wa kileo. Tuwe ni wenye kufwata barabara maagizo Yake na mafundisho ya Mtume Wake(s.a.w.w)
na tuwe ni katika umati bora uliowahi kutokea kwa watu. Umma wetu wa Kiislamu, kwa kipindi sasa umenyonyorwa mengi: akili, fikra na hata mapato na mwisho kuachiwa mizozo na utengano na kutusahaulisha wajibu wetu. Hivyo, jinsi ya kujua namna ya kujirudishia haki zetu ni kurudi kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Kurani Tukufu) na kwenye mafunzo ya Mtume Wake(s.a.w.w)
ambaye ni kiigizo chema kwetu sisi. Kwake yeye ndiko tutapata ufanisi wetu wa mambo yote: uongofu wa akili, malezi ya kiroho, maelekezo ya kiibada, kijamii, kisiasa, kiuchumi na shifaa ya yaliyo nyoyoni. Kitabu hiki ni mkusanyiko wa baadhi ya mafunzo yake S.A.W. ambayo yanatupa msingi wa yote hayo, kimetarjumiwa kwa Kiswahili kutoka kile cha Kiarabu kilichotolewa kwa mara ya kwanza hapo mwaka 1982 na DAR EL TAWHEED ya huko Tehran, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tunatumai Inshaallah kitakuwa na manufaa kwa sote. Na pia tunataraji kitafaa katika madrassa zetu za Kiislamu huku Afrika Mashariki na hasa kwa watumiao lugha yetu ya Kiswahili.
Na mwisho, tunamshukuru sana Sheikh Abdillahi Nassir kwa kukubali kupoteza masaa yake mengi kupitia mswada wa tarjuma hii na vile vile kwa ushauri wake aliotupa. Mwenyezi Mungu Amjazi heri.
Taasisi ya Fikra za Kiislamu Tehran.
Jamhuri ye KiisIamu ye Iran.
Alisema Mtume Muhammad(s.a.w.w)
: Aliye mbali mno kufanana nami kati yenu ni bahili, mchafu, mwenye mambo ya aibu. Nifikishieni haja ya asiyeweza kunifikishia haja yake. Kwani anayemfikishia mtawala haja ya asiyeweza kujifikishia, Mwenyezi Mungu Atathibitisha (Ataimarisha) miguu yake juu ya Sirati siku ya Kiyama. Mtu mmoja wa ukoo wa Tamimi anayeitwa Abu Umayya, alimjia Mtume(s.a.w.w)
na kumuuliza: Ewe Muhammad, walingania watu kitu gani? Akamjibu: "Ninaita kwa Allah kwa ujuzi wa kweli, mimi (nafanya hivi) na (kila) wanaonifuata." Nawalingania watu warudi kwa Ambaye ukipatwa na dhara ukamwomba, Yeye Hukuondolea. Ukimwomba Akusaidie nawe ukatika dhiki, Yeye hukusaidia. Ukimwomba nawe ufukara, Yeye Hukutajirisha. (Abu Umayya) akasema tena: "Niusie ewe Muhammad" Mtume akamwambia: "Usiwe ukikasirika." Abu Umayya akamwambia: "Niongeze." Akaambiwa: "Waridhishe watu kwa unachokiridhia nafsi yako." Akasema: "Niongeze." Akaambiwa: "Usiwe ukiwatusi watu usije ukajiletea uadui." Akasema: "Niongeze." Akaambiwa tena: "Usiache kutenda mema kwa wenyewe." Akasema: "Niongeze." Akaambiwa: "Wapende watu nao watakupenda, kutana na nduguyo - Mwislamu - kwa uso mkunjufu na usiwe ukinuna kusije kununa kwako kukakukosesha ya dunia na ya Akhera.
Mtu mmoja alimjia Mtume(s.a.w.w)
na kusema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Niusie." Akasema (s.a.w.w): "Usimshirikishe Mwenyezi Mungu na chochote hata kama utateketezwa kwa moto, na hata ukiadhibiwa ila moyo wako uwe mtulivu kwa imani. Wazazi wako walishe, uwatendee hisani wakiwa hai au maiti. Wakikuamuru kumwacha mkeo au kuacha mali yako, basi fanya hivyo. Kwani kufanya hivyo ni katika imani. Sala za faradhi usiziache makusudi, maana aachaye sala za faradhi makusudi hutoka katika dhima ya Mwenyezi Mungu. Na tahadhari sana kunywa pombe na chochote cha kulevya, maana hayo ni ufunguo wa kila shari. Watu walimsifu mtu mmoja mbele ya Mtume(s.a.w.w)
kwa uzuri sana na kumsema kwa mambo yote mazuri. Mtume(s.a.w.w)
akawauliza: "Mtu huyo ana akili kiasi gani?" Wakamjibu: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tunakueleza yanayomhusu kulingana na bidii yake katika ibada na heri zinginezo, nawe unatuuliza kuhusu akili yake!" Mtume(s.a.w.w)
akawajibu: "Mpumbavu hupatwa kwa upumbavu wake, na makubwa kuliko machafu ya mchafu (wa vitendo). Na kesho watu watapanda daraja kubwa na kuwa karibu na Mola Wao kwa kadiri ya akili zao
."
Kipenzi mno wa waja wa Mwenyezi Mungu kwa Mwenyezi Mungu, ni anayewafaa mno waja Wake. Jilindeni na watu kwa kuwadhania mabaya. Ukiona ni kisirani, endelea. Ama ukidhani tu, usiendelee. Na ukifanyiwa husuda, usifanye uovu. Mkimwona mtu asiyejali anayosema au anayosemwa basi huyo ni mwovu au ni shetani.
Umma ukiongozwa na mwovu wao, kiongozi wa umma akiwa ni duni wao na fasiki kuheshimiwa, basi (umma huo) ungojee balaa (kuufika). Mwenyezi Mungu Akiughadhabikia umma na Asiwateremshie adhabu, basi bei ya bidhaa (nchini mwao) hupanda, umri wao ukawa mfupi, biashara zao zikakosa faida, matunda yakakosa kuzaa (ifaavyo), mito ikakosa maji ya kutosha, mvua Akaizuia na Akawasaliti na waovu wao. Umma wangu utakapofanya mambo kumi na matano, watashukiwa na balaa. Akaulizwa: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni yapi hayo?" Akasema: "Wakichukua ngawira kwa noba, amana kuwa ngawira, zaka kuiona ni gharama, mume akamtii mkewe na kumwasi mamake, mamake akamtendea wema rafiki yake na akamtupa babake, sauti zikawa juu misikitini, mtu akaheshimiwa kwa kuogopewa shari lake, kiongozi wa umma akawa ni duni wao, hariri zikivaliwa, tembo (pombe) ikanywewa kwa wingi, wakashughulikia nyimbo na ngoma na wa mwisho katika umma huo kuwalaani wa kwanza wake. Baada ya hayo, wajiandalie kupatwa na matatu: upepo mkali mwekundu, kuondolewa na kutupwa.
Itakapokuwa siku ya Kiyama, guu Ia mtu halitateleza (halitavuta hatua) hadi kwanza aulizwe juu ya mambo manne: umri wake aliumaliza katika nini; ujana wake aliupitisha vipi; mapato yake aliyapata kutoka wapi na aliyatumia katika nini na (alikuwa na kadiri gani ya) mahaba yetu sisi Ahli Bayt. Ikiwa watawala wenu ni wabora wenu, matajiri wenu ni wasamehevu wenu, mambo yenu ni kwa kushauriana baina yenu, basi juu ya ardhi ni bora kwenu kuliko ndani yake. Ama ikiwa viongozi wenu ni wabaya wenu na matajiri wenu, ni mabakhili wenu, basi kuwa ndani ya ardhi ni bora kwenu kuliko (kuwa) juu yake. Ikiwa uzinifu utazidi baada yangu, vifo vya ghafla vitaongezeka. Na pindi vipimo vikipunjwa, Mwenyezi Mungu Atawachukulia hatua kwa njaa na upungufu (wa matunda). Na wakizuia (wakikataa kutoa) zaka, ardhi nayo itafunga baraka zake za mimea, matunda na madini. Na wakipendelea katika maamuzi, watasaidiana katika dhuluma na uadui. Na wakivunja ahadi, Mwenyezi Mungu Atawasaliti na adui yao. Na wakikata jamaa (zao), mali zitawekwa mikononi mwa watu waovu. Wasipoamrishana mema na kukatazana maovu na wasiwafuate Ahli Bayt wangu ambao ni bora, Mwenyezi Mungu Atawasaliti na waovu wao. Wakati huo wema wao wataomba (Mwenyezi Mungu) na hawataitikiwa (dua zao).
Mtu mwovu akisifiwa, Kiti cha Enzi (cha Mwenyezi Mungu) hutingishika na Mwenyezi Mungu kukasirika. Mambo manne ni katika alama za uovu: ukavu wa macho, ugumu wa moyo, wingi wa tamaa katika kuitaka dunia na kukakawana na dhambi. Mambo manne aliye nayo yumo katika nuru ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: Mtu ambaye hifadhi ya mambo yake ni shahada kwa kuwa hakuna mungu ila Allah na kuwa mimi ni mjumbe Wake; na ambaye akipatwa na msiba hunena: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungw na tutarudi Kwake. Na ambaye akipata jema hunena: Alhamdu Lillah. Na ambaye akitokewa na kukosa - hunena Astaghfirullah. Mambo manne humpasa kila mwenye akili na busara katika umati wangu. Akaulizwa: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni yapi hayo?" Naye akajibu: "Kusikiliza elimu, kuihifadhi, kuieneza na kuitumia." Mhurumieni mheshimiwa aliyedhalilika, tajiri aliyefukarika na mwanachuoni aliyepotea katika zama za wajinga. Jilazimisheni siri katika mambo yenu, maana kila mwenye neema huhusudiwa. Shari itakayolipwa haraka mno ni ile ya dhuluma.
Mhusudiwa wa watu wangu kwangu katika umati wangu ni mtu ambaye hali yake si ya makuu, adumishaye vyema sala, amwabuduye Mola Wake vizuri pamoja na kuwa hajawahi kumwona, ainamishaye macho mbele za watu, ambaye riziki yake ni ya kuwania tu lakini akawa na subira mpaka akafa na hali hiyo, warithi wake wakawa wachahce na (pia) wenye kumlilia (baada ya kufa). Mbora wenu wa imani ni aliye mbora wenu wa tabia. Atakayekuwa karibu nami sana Kesho huko Kiyama ni mkweli wenu katika mazungumzo, afikishaye amana, atimizaye ahadi, mbora wenu kwa tabia ujema na wa karibu wenu zaidi kwa watu. Kichache cha kuwepo Akhiri Zamani (mwisho wa dunia) ni ndugu wa kuaminika na pesa za halali. Sameheni kuteleza (au makosa) ya wenye msiba. Kula sokoni ni uanzali (utwevu).
Mkamilifu wa watu kwa akili ni awashindaye katika kumwogopa Mwenyezi Mungu, na awashindaye katika kumtii. Na mpungufu wa watu kwa akili ni awashindaye katika kumwogopa mfalme, na awashindaye katika kumtii. Je niwaelezeni anayefanana na mimi kwa tabia njema? Wakajibu: kwani, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Akasema: Ni mbora wenu wa tabia, mpole wenu sana, anayewashinda nyote katika kuwafanyia watu wake wema na anayewashinda nyote kwa uadilifu katika nafsi yake akiwa amekasirika au ameridhika. Je niwaoneshe bora ya tabia njema za duniani na Akhera? Ni kumwunga anayekukata, umpe anayekunyima na umsamehe anayekudhulumu. Tambueni! Wabaya kabisa wa umma wangu ni ambao huheshimiwa kwa kuogopewa shari zao. Tambueni! Ambaye ataheshimiwa na watu kwa sababu ya kuogopa shari yake, basi huyo si katika mimi (si mfuasi wangu). Nimeamuriwa kuelewana na kuwachukulia watu kama nilivyoamrishwa kufikisha ujumbe (kwa watu). Uaminifu huvuta riziki na hiana huvutia ufukara.
Subira yatokamana na Mwenyezi Mungu na haraka hutokamana na shetani. Kamili wa imani miongoni mwa waumini ni mbora wao wa tabia njema. Kila balaa kubwa hulipwa malipo makubwa. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu Akimpenda mja (Wake) Humpa mitihani. Ambaye moyo wake umeridhia, hupata radhi ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuchukia, hupata chuki. Mwenyezi Mungu Ameharamisha Pepo kwa kila mchafu wa tabia na ulimi, mchache wa haya, asiyejali anayosema au anayosemwa. Mtu aina hiyo hakika ukimweka popote (kumnasibisha) hutomkuta ila tu ni mwovu au ni mshirika wa shetani. Akaulizwa: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, je katika watu kuna mashetani?" Akajibu: "Ndiyo. Je hukusoma neno Ia Mwenyezi Mungu: "Na shirikiana nao katika mali na watoto." 17:64 Mwenyezi Mungu Amewaumba watumwa katika viumbe Wake kwa ajili ya haja za watu. Wanatamani mema na kudhani ukarimu ni heshima. Na Mwenyezi Mungu Hupenda tabia njema.
Mwenyezi Mungu Humchukia mzee mzinifu, tajiri dhalimu, maskini mwenye kuringa na mwombaji mwenye kuchagiza ambaye humharibia mtoaji thawabu zake. Kadhalika Huchukia kiburi, ujuvi na ukedhabu. Mwenyezi Mungu Hupenda Akimneemesha mja kuona ana athari ya neema Zake Alizompa. Na Huchukia shida na kujitia katika shida. Mwenyezi Mungu Humpenda karimu katika haki yake. Mwenyezi Mungu Ana waja ambao hukimbiliwa na watu kwa haja zao. Watu hao ndio wenye kusalimika na adhabu za Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama. Hakika yeyote anayejifunza elimu ili kubishana na wasiojua, au kupata heshima kwa wanaojua, au kuzielekeza nyuso za watu kwake ili wamheshimu, basi na ajiandalie makao yake Motoni. Maana uongozi haustahiki ila kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wanaoustahiki. Na anayejiweka ambapo sipo Mwenyezi Mungu Alipomweka, Mwenyezi Mungu Humkasirikia. Na anayejitukuza kwa kusema 'mimi ndiye mkubwa wenu' hali yeye si hivyo Mwenyezi Mungu Hamtazami mpaka atakapojirudi kwa alilosema na atubu kwa Mwenyezi Mungu kwa alilolidai. Hakika katika (baadhi ya) mashairi mna maneno ya hekima. Na katika maelezo mna uchawi. Muumin hutwaa adabu za Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Akimpanulia riziki, naye hujipanua. Na Akimfungia, hujizuia. Sisi, Mitume sote, tumeamurishwa kuzungumza na watu kwa kadiri ya akili zao.
Nauchelea umati wangu mambo matatu: kutii kukutu, kufuata matamanio na (kumfuata) imamu mpotofu. Hisani hufanyiwa wenye dini au heshima. Jihadi ya wanyonge ni hija, na jihadi ya mwanamke ni kuishi na mumewe kwa wema. Mapenzi ni nusu ya imani. Katu mtu hafukariki akiwa na iktisadi (katika matumizi yake). Na takeni kuteremshiwa riziki kwa kutoa sadaka (kwani) Mwenyezi Mungu Alikataa kuijaalia riziki ya waja Wake waumini kutoka wanapopadhania. Heri zote hupatikana kwa akili, (hivyo) hana dini asiye na akili. Kwa hakika ninaapa kwa Mwenyezi Mungu! Hakuna amali yoyote ya kuwakaribisha na Moto ila nimewaeleza na kuwakanya nayo. Na hakuna amali yoyote ya kuwakaribisha na Pepo ila nimewaeleza na kuwaamurisha muifanye. Kwani Roho Mwaminifu alivuvia moyoni mwangu kwamba hakuna nafsi itakayokufa mpaka riziki yake ikamilike. Mola Wangu Aliniusia mambo tisa: Aliniusia (kuwa na) Ikhlasi kwa siri na dhahiri. Kuwa mwadilifu katika furaha na hasira. Kuwa mwangalifu wa matumizi katika ufukara na utajiri. Nimsamehe aliyenidhulumu, nimpe aliyeninyima na nimuunge aliyenitupa. Kunyamaza kwangu kuwe nafikiri. Uzungumzi wangu uwe ni dhikri (kumtaja Mwenyezi Mungu) na kutazama kwangu kuwe ni kwa kuzingatia.
Mikono ni mitatu: wa kuomba, wa kutoa na wa kuzuia. Na mkono bora ni ule wa kutoa. Imani ni kuitakidi kwa moyo, kunena kwa ulimi na kutenda kwa viungo. Imani ni nusu mbili: nusu moja ni ya subira na nusu nyengine ni ya kushukuru. Ogopeni kujinyenyekesha kiunafiki. Nako ni kuonekana mwili mnyenyekevu, hali moyo si mnyenyekevu. Kuacha shari ni sadaka. Sifa tatu mwenye kuwa nazo amejikamilisha imani: Akifurahi furaha yake haimtii katika batili au makosani; akikasirika hasira zake hazimtoi kwenye haki; na akiwa na mamlaka hatoi kisicho chake. Nyoyo zimeumbwa kumpenda anayezifanyia hisani na kumchukia anayezitendea uovu. Kuketi msikitini kungojea (wakati wa) sala ni ibada (kamili) maadam haijatenguka. Akaulizwa: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni kitu gani kinachotengua?" Akajibu: "Kusengenya."
UZURI (WA MTU) U KATIKA ULIMI
Mtu mmoja alimpelekea Mtume(s.a.w.w)
maziwa na asali anywe. Akasema: "Vinywaji viwili kila kimoja hutosheleza chengine. Mimi sikinywi wala sikiharamishi ila tu namnyenyekea Mwenyezi Mungu kwa sababu anaye mnyenyekea Mwenyezi Mungu Humwinua. Anayemkumbuka Mwenyezi Mungu kwa kumtaja, Mwenyezi Mungu Humpa thawabu
."
Heshima ambazo lazima kila muumin kuzichunga na kuzitekeleza ni: heshima ya dini, heshima ya adabu na heshima ya chakula. Uchangamfu huondoa mfundo. Uzuri wa tabia humfikisha mwenye nayo daraja ya afungaye saumu na kusali sana (usiku wote kila siku). Akaulizwa: "Ni kipawa gani bora alichopawa mtu?" Akajibu: "Tabia njema." Tabia nzuri huimarisha mapenzi. Kutimiza ahadi ni katika imani. Kuuliza vizuri ni nusu ya elimu. Na upole ni nusu ya maisha.
Kuona haya ni namna mbili: kuona haya kwa akili na kuona haya kwa kipumbavu. Kuona haya kwa akili ni elimu na kuona haya kwa kipumbavu ni ujinga. (Kuwa na) haya ni katika imani. Siku moja, Mtume(s.a.w.w)
alitoka na kuwakuta watu wanalivunja jiwe. Akawaambia: "Shujaa mwenye nguvu kuwashinda nyote ni anayejimiliki nafsi yake wakati akihamaki. Na mstahamilivu kuliko nyote ni anayesamehe wakati ana uwezo (wa kuadhibu).
"
Mambo mawili hakuna wema wa juu kuyashinda: kumwamini Mwenyezi Mungu na kuwafaa waja wa Mwenyezi Mungu. Na mambo mawili hakuna shari za kuyashinda: kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kuwadhuru waja wa Mwenyezi Mungu. Vishawishi viwili huwafitini watu wengi: siha na faragha.
Mwema atokana na wema mwenye kuufanya. Na mshari atokana na shari mwenye kuitenda. Bora wenu ni bora wenu kwa tabia njema, wanaozoea (watu) na kuzoewa. Dunia ni duara. Mazuri uliyo nayo yalikujia pamoja na udhaifu wako. Na mabaya yaliyokushukia hukutumia nguvu zako kuyazuia. Anayekata tamaa kwa aliyoyakosa, mwili wake hupumzika. Na anayeridhia alilopewa na Mwenyezi Mungu, jicho lake hutulia. Dunia ni kifungo (jela) kwa muumin na Pepo kwa kafiri. Kichwa cha akili baada ya kumwamini Mwenyezi Mungu ni kuingiliana na watu. Lakini pasi na kuacha haki. Mwenyezi Mungu Amrehemu mja ambaye hunena ya heri akajipatia (fungu), au akanyamaza akasalimika. Umati wangu umeondolewa (kuchukuliwa makosa kwa) mambo tisa: kukosa, kusahau, waliotenzwa nguvu, wasiyoyajua, wasiyoyaweza, waliyolazimika, kijicho, kisirani na kuwadhania watu kwa wasiwasi maadamu ulimi haukutamka (dhana hiyo).
Kuyachukia ya dunia (kwa utawa) ni kuipunguza tamaa, kushukuru kila neema (ya Mungu) na kujiweka mbali na kila Aliloharamisha Mwenyezi Mungu. Aliulizwa (s.a.w.w): "Nani mwenye balaa kubwa zaidi humu duniani?" Akajibu: "Ni manabii, kisha wanaofanana nao (kwa matendo mazuri), kisha wanaofanana nao. Muumin hujaribiwa (na Mwenyezi Mungu kulingana na kadiri ya imani yake na uzuri wa matendo yake. Ambaye imani yake ni sahihi na matendo yake ni mazuri, balaa zake huzidi. Ama ambaye imani yake ni hafifu na matendo yake ni dhaifu, huyo balaa zake hupungua. Ulizeni wanazuoni; zungumzeni na wenye hekima na ketini na mafukara. Mtakuja kuwa na tamaa ya uongozi kisha iwageuke na kuwa hasara na majuto. Mwanzo ni furaha na mwisho ni karaha.