ADHANA YA USIKU WA MANANE

ADHANA YA USIKU WA MANANE0%

ADHANA YA USIKU WA MANANE Mwandishi:
: S. Muhammad Ridha Shushtary
Kundi: Vitabu mbali mbali

ADHANA YA USIKU WA MANANE

Mwandishi: Ustadh Shahid Murtadha Mutahhari
: S. Muhammad Ridha Shushtary
Kundi:

Matembeleo: 3237
Pakua: 2837

Maelezo zaidi:

Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 2 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 3237 / Pakua: 2837
Kiwango Kiwango Kiwango
ADHANA YA USIKU WA MANANE

ADHANA YA USIKU WA MANANE

Mwandishi:
Swahili

ADHANA YA USIKU WA MANANE

MTUNGAJI: USTADH SHAHID MURTADHA MUTAHHARI

MTARJUMI: S. MUHAMMAD RIDHA SHUSHTARY

KIMETOLEWA WAVUNI NA: TIMU YA AHLUL BAYT DIGITAL ISLAMIC LIBRARY PROJECT

Katika zama za ukhalifa wa Bani Umayyah, kabila Ia Kiarabu ndilo kabila la pekee lililokuwa likitawala na lenye nguvu katika dola kuu la Kiislamu. Lakini katika zama za makhalifa wa Bani Abbasi, Wairani walianza kukabidhiwa madaraka na wakadhibiti nyadhifa na vyeo vingi.

Ingawa makhalifa wa Bani Abbasi walikuwa Waarabu, lakini hawakuwa wakiwapenda Waarabu. Siasa yao ilikuwa ni kuwatoa Waarabu madarakani na badala yake kuwaweka Wairani (Waajemi). Isitoshe, walikuwa wakizuia lugha ya Kiarabu isienee katika miji kadhaa ya Iran. Siasa hiyo iliendelea mpaka katika zama za Ma' muun.

Baada ya kufa kwa Ma'muun, ndugu yake, Mu'tasim, akakalia kiti cha ukhalifa. Ma'muun na Mu'tasim walikuwa ndugu baba mmoja lakini mama zao walikuwa mbalimbali. Mamake Ma'muun alikuwa Mwajemi (Mwirani) na mamake Mu'tasim alikuwa Mturuki. Hii ndiyo sababu iliyowafanya Wairani ambao walikuwa wameshikilia vyeo muhimu - wasiupende uldialifa wa Mu'tasim. Wairani walitaka Abbas mwana wa Ma'muun awe khalifa. Mu'tasim alitambua jambo hili na akawa akiogopa asije mtoto wa nduguye - Abbas bin Ma'muun - akaasi na kwa msaada wa Wairani akamwangusha. Kwa hivyo akapanga njama ya kumwangamiza Abbas na kuvunja nguvu za Wairani ambao walikuwa wakimwunga mkono Abbas. Akamtia jela Abbas ambapo ndipo alipokufa. Ili kuvunja nguvu za Wairani, akafanya mpango wa kuwapa nguvu watu wengine badala yao. Kwa ajili ya kutekeleza mpango huo, akawaleta Baghdad (makao makuu ya ukhalifa) Waturuki wengi wa kabila la mama yake kutoka Uturuki (Turkistan) na Maa Waraun Nahr na akawapa kazi. Haukupita muda mrefu, Waturuki wakashika madaraka na nguvu zao zikazidi kuliko Waarabu na Wairani.

Kwa kuwa Mu'tasim alikuwa akiwaamini sana Waturuki hivyo, kila siku zikipita alikuwa akiwapa uwanja; na kutokana na siasa hiyo Waturuki wakawa ni watu wa pekee wenye nguvu katika dola la Kiislamu. Waturuki wote walikuwa Waislamu, walijifunza lugha ya Kiarabu na walikuwa waaminifu kwa dini ya Kiislamu, lakini ilivyokuwa muda baina ya kuingia kwao katika mji mkuu wa ustaarabu wa Kiislamu na kupata madaraka haukuwa mrefu, hawakuelewa sana mafundisho, adabu na utamaduni wa Kiislamu na hawakuwa na mwendo na tabia ya Kiislamu. Kinyume chake, Wairani walikuwa na uzoefu wa ustaarabu na walijifunza kwa hamu maarifa, maadili na adabu za Kiislamu, mwendo wao ulikuwa wa Kiislamu na walikuwa mbele katika kuutumikia Uislamu. Katika kipindi ambacho Wairani walikuwa na madaraka mikononi mwao, Waislamu wote waliridhika; lakini wakati Waturuki waliposhika madaraka waliwatendea vibaya Waislamu kwa kadiri kwamba walikuwa wakichukiwa.

Askari wa Kituruki wenye kupanda farasi walipokuwa wakipita kwenye mitaa na vichochoro vya Baghdad hawakuwa wakitazama kama yupo mtu mbele ya njia yao. Kwa sababu hiyo, mara nyingi wanawake, watoto, wazee na watu wasiojiweza walikuwa wakikanyagwa na farasi. Watu hawakuweza kustahamili udhalilifu huo. Wakamwomba Mu'tasim ahamishe mji mkuu kutoka Baghdad na afanye mahali pengine. Katika maombi yao walisema kwamba ikiwa khalifa hatohamisha mji mkuu basi watapigana vita dhidi yake. Mu'tasim akawajibu: "Nguvu gani mlizonazo mtakazoweza kupigana dhidi yangu? Mimi nina askari thamanini elfu waliojiandaa kwa silaha." Watu wakamjibu: "Tutapigana kwa mishale ya usiku, yaani tutakupiga kwa laana za usiku wa manane." Mu'tasim akakubali maombi ya watu baada ya kusikia maneno hayo. Akahama Baghdad na akafanya Samarah kuwa ni mji wake mkuu. Baada ya Mu'tasim, Waturuki waliendelea kushika madaraka katika zama za ukhalifa wa Wathiq, Mutawakkil, Muntasir na makhalifa kadhaa wengineo. Waturuki walikuwa wakiwatumia makhalifa hao kwa maslahi yao. Baadhi ya makhalifa wa Bani Abbasi walijaribu kuvunja nguvu za Waturuki lakini walishindwa. Khalifa mmojawapo wa Bani Abbasi aitwaye Mu'tadhid, ndiye aliyeweza kwa kadiri fulani kupunguza nguvu za Waturuki.

Katika zama za Mu'tadhid, alikuwepo mfanyabiashara mmoja mzee ambaye alikuwa akimdai pesa nyingi afisa mmoja wa kijeshi lakini alikataa kumlipa. Mwishowe akaamua amwendee khalifa mwenyewe aingilie kati, lakini kila wakati alipofika kwenye mlango wa kasri ili apate kuonana na khalifa, mabawabu na watumishi wa kasri walikuwa wakimzuia.

Mfanyabiashara maskini alivunjika moyo na hakujua afanye nini. Kwa bahati mtu mmoja akamwelekeza aende kwa mshoni wa nguo katika gulio, na akamwambia kwamba mtu huyo ndiye atakayeweza kumsaidia. Mfanyabiashara akaenda kwa mshoni ambaye alimwamuru afisa huyo wa kijeshi amlipe deni yake. Mfanya biashara akalipwa pesa zake bila ya kukawia.

Kitendo hicho kilimshangaza sana mfanya biashara mzee. Akamshikilia sana mshoni kwa kumwuliza: "Vipi Waturuki hao ambao hawamjali mtu yeyote wanatii amri yako?"

Mshoni akajibu "Mimi nina kisa kimoja ambacho ni lazima nikuhadithie wewe. "Siku moja nilipokuwa nikipita katika njia moja, wakati huohuo mwanamke mmoja mrembo alikuwa akipita hapo. Kwa bahati, afisa mmoja Mturuki ambaye alikuwa amelewa alikuwa ametoka nje ya nyumba yake na akasimama mlangoni akiwatazama watu wanaopita njiani. Alipomwona huyo mwanamke mrembo akapandwa na wendawazimu, akamkumbatia mbele va watu kisha akamvuta kumtia nyumbani kwake. Mwanamke huyo akaanza kupiga mayowe: 'Enyi watu! Nisaidieni! Mimi si mzinzi! Nina heshima zangu! Wallahi ikiwa usiku mmoja nitalala nje, mume wangu atanitaliki! Unyumba wetu utaharibika!'

"Hakuna mtu aliyethubutu kusogelea mbele kumsaidia kwa kuogopa. Mimi nikamwendea na kwa upole sana nikamwomba afisa amwache mwanamke, lakini akanijibu kwa kunipiga kwa nguvu rungu ya kichwa na kunipasua, kisha akamtia mwanamke ndani ya nyumba yake. Mimi nikawakusanya watu wachache, kisha kwa pamoja tukaenda kwenye nyumba ya afisa huyo kutaka amwachie mwanamke, lakini mara afisa Mturuki akatoka nyumbani pamoja na kikundi cha watumishi na watumwa wake na wakaanza kutupiga magongo.

"Sote tukakimbizana na mimi nikarejea nyumbani, lakini kila wakati nilikuwa nikimfikiria mwanamke huyo maskini. Nikafikiri kwamba ikiwa mwanamke huyo atabaki na mwanamume huyo mpaka asubuhi, basi maisha yake yote mpaka kufa kwake yataharibika na hatoweza tena kurejea nyumbani kwake. Nilikaa macho nikifikiri mpaka nusu ya usiku. Mara mpango mmoja ukanijia ubongoni mwangu. Nikasema moyoni. 'Mwanamume huyo amelewa leo usiku na hatambui wakati. Ikiwa nitaadhini sasa hivi, atadhani kuwa ni alfajiri, hivyo atamwachia mwanamke. Mwanamke pia ataweza kurejea nyumbani kwake kabla ya kupambazuka.

"Kwa haraka nikaenda msikitini, nikapanda mnarani na nikaadhini kwa sauti kubwa. Nilipokuwa nikiadhini nilikuwa nikiangalia njiani kuona kama mwanamke ameachiwa ama la. Mara ghafla, niliwaona askari wengi waliopanda farasi na waendao kwa miguu wakimiminika njiani huku wakiulizana: 'Ni nani huyo aliyeadhini wakati huu wa usiku?' Mimi juu ya kuwa niliogopa sana, nikajitambulisha: 'Mimi ndiye niliyeadhini.'

"Wakasema: 'Teremka chini haraka unaitwa na khalifa!' "Wakanichukua kwa khalifa. Nikamkuta khalifa ameketi akiningojea. Akaniuliza: 'Kwa nini umeadhini wakati huu wa usiku?' Nikamwelezea kisa chenyewe tangu mwanzo mpaka mwisho. Papo hapo, khalifa akatoa amri kwamba afisa na mwanamke waletwe mbele yake. Baada ya kuletwa mbele yake na kuwahoji, akatoa amri afisa huyo auawe. Mwanamke akapelekwa nyumbani kwa mumewe na akamtaka asimlaumu bali amwangalie vizuri kwa sababu khalifa ana hakika kwamba mwanamke hakuwa na kosa lolote.

"Kisha Mu'tadhid akaniambia: 'Wakati wowote utakapoona uonevu kama huo, tumia mbinu hiyo mpya uliyoitumia, nami nitachunguza.' "Habari hii ikaenea kwa watu wote. Tangu siku hiyo hao [Waturuki] wakaanza kuniogopa. Hii ndiyo sababu kwamba nilipomwamrisha huyo afisa wa kijeshi akulipe pesa ulizokuwa ukimdai, alitii haraka."

Adhana Usiku wa Manane

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU

YALIYOMO

ADHANA YA USIKU WA MANANE 1

MTUNGAJI: USTADH SHAHID MURTADHA MUTAHHARI 1

MTARJUMI: S. MUHAMMAD RIDHA SHUSHTARY 1

SHARTI YA KUCHAPA 3

MWISHO WA KITABU 3

YALIYOMO 4