1
ASHURA
SHAHADA YA IMAM HUSAYN
HIJRA NA AHLUL BAYT
Mwito wa kwamba hakuna mungu apasae kuabudiwa, ila Allah ulizuwa chuki dhidi ya Mtume kutoka kwa maadui zake, ingawa ni mwito wa kuungana na kujikomboa kutoka katika udhilifu na utumwa ulioathiri utu wa mwanaadamu. Watu wake waliokuwa wakimheshimu na kumtambua kwa cheo kama 'mkweli na mwaminifu' sasa walimgeukia na kumtusi kwa majina ya kila aina. Walimwendea kinyume, kumtupia mawe na kumfanyia fujo katika kila njia na kushindwa kumuangusha ili kumuzuia Mtume. Makafiri wa Makkah hawakuweza kumdhuru kwa kutokana na nguvu na ulinzi aliowekewa na ammi yake Abutalib, ambae alikuwa tayari kupambana na yeyote yule aliyetaka kumdhuru Mtume.
Wathama Bibi Khadija, mkewe Mtume alitumia pesa zake zote alizokuwa nazo katika mchango wake wa kuikuza dini ya kiislamu. Huyu ndiye mwanamke wa kwanza aliyeingia na aliyetetea na kuutukuza Uislamu. Ama utiifu wake haukuwa na mfano. Alipoishiwa na mali yake huyo bibi tajiri mkuu wa waarabu alijitolea na kujimudu kuishi kula majani makavu, alitengana na starehe zote za jamii na marafiki, aliridhika siku zote na sadaka alizotowa na kutakabaliwa na Mwenyezi Mungu , alifurahiya bahati yake yakuwa sehemu na fungu katika kuimarisha ujumbe mtukufu wa Mtume.
Muda wa miaka kumi na mitatu tangu tangazo la Mtume wa Islam, watu wa Makkah walifanya chuki sana juu ya Mtume na ujumbe wake hasa alipoondokewa na wasaidizi wake wote wawili; Abutalib, ammi yake na Khadijah mke wake aliyekuwa msaidizi wake katika kila lililohitajika. Mwaka wa 1 B.H. (621 AD) Mtume alihamia Madina ambako watu wa huko walikuwa wazuri, marafiki wema na wakarimu kwake.
Maadui wa Mtume hao wakazi wa Makkah, hawakutosheka pia na kuhama kwake kutoka Makkah, baadhi ya ma-ammi zake na a'li zao, walimfanyia matata na fujo za kila aina. Mtume alilazimika kupigana vita visivyo pungua 59, vilivyoanzilishwa na wenyeji wa Makkah dhidi ya waislamu katika muda mfupi wa miaka isiyopungua kumi na katika mfululizo wa vita hivi vilivyofwatia moja baada ya nyengine ni Sayyidna Ali, ndiye aliyekuwa kiongozi mwenye ushindi.
Vita vya Badr, Uhud, Khandak na Khaibar ni baadhi ya vita vyenye ushindi wa Mtume na Makka ilitawalwa kwa amani mnamo mwaka 10 B.H (630 AD) juu ya ushindi huo Mtume aliyavunja masanamu 360, yaliyokuwa yamewekwa kama miungu katika Al-Ka'ba. Katika mwaka wa pili 2 B.H. (624 AD) Mtume alimuoza Ali ibn Abutalib binti yake Fatimah kwa sherehe ya arusi iliyofanywa kwa ufupi kabisa ambayo yafaa kuigizwa mfano. Na kutokana na ndoa hii Ali na Fatimah walijaaliwa watoto wanne kama ifuatavyo;
" Hassan, katika mwaka 3 B.H. (625 AD)
" Husayn mwaka wa 4 B.H. (626 AD)
" Zainab mwaka 6 B.H (628 AD)
" Ummukulthum mwaka 8 B.H. (630 AD)
Baada ya kuhamia kwao Madina, palikuwa na tukio jengine la muhimu na la kukumbukwa mbali na vita vilivyopiganwa. Ni katika mwaka 8 B.H. (630 AD) ambapo Mtume alimtembelea binti yake akiwa mgeni wake nyumbani, ambapo alikaa na kujifunika 'utaji' wa nguo, akif'watiwa na binti yake Fatimah na mumewe Ali na watoto wao Hassan na Husayn pia. Wote waliingia ndani ya utaji aliojifunika Mtume. Na katika kikao hiki cha watu watakatifu watano, Mtume aliinua mikono yake na kuomba dua; "Ya Allah, hawa ni watu wa nyumba yangu Ahlul Bait."
Ni watu wanaonihusu na wasaidizi wangu, wao ni nyama yangu na damu yangu. Kwa yeyote yule atakaewasumbua hawa, atanisumbuwa mimi, yeyote atakae waudhi hawa ataniudhi, na mimi nitapigana na yeyote yule atakae pigana nao, na nitakuwa na amani na yule atakae kuwa na amani nao, mimi ni adui wa maadui zao na rafiki wa wale marafiki zao." Hapo aliteremka malaika Jibril na ujumbe huu:
إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا ﴿٣٣﴾
"Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu enyi watu wa nyumba (ya Mtume), na (anataka) kukutakaseni kabisa kabisa." (Qur'ani 33:33).
Vile vile alivyosema Mwenyezi Mungu:
قُل لَّا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا إِلَّا الْمَوَدَّةَ فِي الْقُرْبَىٰ ﴿٢٣﴾
Sema: sitaraji kupata chochote kwako ila mapenzi kwa 'akraba' zangu. (Qur'ani 42:23).
Kadhalika wakati mwingine ilipoteremshwa aya isemayo:
فَمَنْ حَاجَّكَ فِيهِ مِن بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ أَبْنَاءَنَا وَأَبْنَاءَكُمْ وَنِسَاءَنَا وَنِسَاءَكُمْ وَأَنفُسَنَا وَأَنفُسَكُمْ ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَل لَّعْنَتَ اللَّـهِ عَلَى الْكَاذِبِينَ ﴿٦١﴾
Watakaokuhoji (sasa) katika haya baada ya kukufikilia ilimu (hii na kuwafikilia wao), waambie, 'Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu; na wanawake wa kwetu na wanawake wa kwenu, na sisi na nyinyi, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.' (Qur'ani 3:61).
Mtume aliongoza ujumbe wake akiwa na Ali kama Akraba wake, Fatima mwanamke wake na watoto wao Hassan na Husayn kama watoto wake katika pambano lililojulikana kama "Mubahala" (Yamini) dhidi ya watu wa Najran (Yemen). (Neno Mubahala limetokana na Bahala ina maana ya 'kuapiza' au 'kulaani, 'laana. Hivyo lina maana ya kuapizana kati yao).
Ama watu watakatifu hawa "Ahlul Bayt" hawakuwa ni wapenzi wa Mtume(s.a.w.w)
kwa kuwa ni mapande ya nyama yake na damu yake tu, bali ni watu waliokuwa na msimamo imara mbele yake, watu waliokuwa watiifu na waadilifu waliojitolea kumtii kama ilivyoshuhudiwa katika mienendo ya tarikhi zao. Mfano wa watu wa nyumba yangu ni kama vile safina ya Nuhu, yoyote aingiaye humo atapata kuokoka na yule atakaye kupinga na kusita kuingia atatwaliwa na kutoswa na maji. Mtume Muhammad(s.a.w.w).
KHALIFA WA MTUME
Mtume katika rejeo lake Madina baada ya kwenda kuhiji Makkah, katika mwaka wa 10 B.H. (632 A.D.) iliteremshwa aya aliyopokea kama ifuatavyo:
يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ وَاللَّـهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ ﴿٦٧﴾
Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri. (Qur'ani 5:67).
Hapo Mtume aliwakusanya watu wote waliokuwa pamoja nae katika jangwa lilijulikana kama 'Ghadeer' na kuwatolea hotuba moja muhimu kabisa katika ujumbe wake na juu ya hayo, alithibitisha rasmi ukhalifa wa Imam Ali, na suala la uongozi baada ya kuondoka kwake Mtume.
''Mimi ninawaachia nyinyi vitu viwili vizito 'Kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu na watu wa nyumba yangu Ahlul-Bayt' na kwa yeyote yule ambaye mimi ni kiongozi wake, na Ali ni kiongozi wake vile vile. Ewe Allah, na uwe rafiki wa atakaekuwa rafiki yake na adui wa yule atakaekuwa mpinzani wake." Alitangaza, akiwajulisha umati kwamba hii ni safari ya mwisho ya hijja yake na karibuni ataaga dunia. Ama sifa za Ali zilitangaa katika nyanja zote na kutambuliwa na kila mmoja: kwa ujuzi wake wote, kazi yake, Nahjul Balagha, inafwatia Qur'an tukufu isiyokuwa na badili.
Katika Sahih Muslim imeandikwa kwamba Zayd b. Arqam amesema kuwa Mtume(s.a.w.w)
alisema: Enyi watu! Hakika mimi ni binadamu; nami nataraji (hivi karibuni) kujiwa na mjumbe (malaika wa mauti) wa Mola wangu na kuitika (mwito Wake). Kwa hivyo ninawaachia nyinyi vizito viwili; cha kwanza ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu chenye uongozi na mwangaza. Basi shikamaneni na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na watu wa Nyumba yangu (Ahlu Bayt). Ninawakumbusha nyinyi watu wa Nyumba yangu. Ninawakumbusha nyinyi watu wa Nyumba yangu. Ninawakumbusha nyinyi watu wa Nyumba yangu. Kitabu 'Al Fadhail' Mlango wa 'Fadhail Ali'. Kwa Kiingereza ni Vol. 4, Uk. 1286, Hadith 5920.
UTIIFU WAKE
Kulala kwake juu ya kitanda cha Mtume usiku wa Hijra alipohamia Madina, kwathibitisha jinsi alivyojitolea katika dini, nguvu zake na ushujaa aliokuwa nao katika vita alivyopigana, ukweli na uaminifu unyenyekevu na uchaji wake kwa Mungu haufananishwi na yeyote. Mara baada ya tangazo la Mtume, iliteremshwa aya ifuatayo:
الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ﴿٣﴾
" Leo nimekukamilishieni dini yenu na kukutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe dini yenu" (Qur'ani 5:3).
Wanafiki na watesi ingawa hawakufurahishwa na tangazo la Mtume kuhusu Ali, wakati huo walificha chuki zao juu ya 'Ahlul-Bayt' na kuwapongeza. Kinyume na kusikia maoni matakatifu na mithali ya hekima waliyopewa na Mtume kuhusu Ali ibne Abi Talib, kama; mimi ni jiji kuu la elimu na Ali ndie lango la kuingilia; Ali ametokana na mimi na mimi natokana na Ali; Ali kwangu ni kama Harun alivyokuwa kwa Musa; Ali yumo ndani ya ukweli na ukweli umo ndani ya Ali.
Miongoni mwa wafuasi wake na watu ambao hawakukubaliana na maoni matakatifu ya Mtume, walijaribu na kufanya kila waliloweza ili kuvuruga na kutarakanya maneno na kumpinga khalifa wake baada ya Mtume kuondoka. Mtume alifariki Madina baada ya siku sabini tokea alipotoa tangazo lake, aliugua kidogo na kuaga dunia. Walipopokea habari za kifo cha Mtume, wale watu waliokuwa wavunjifu waliondoka mara moja na kukusanyika ili kulazimisha khalifa wa chaguo lao juu ya umma; huku wakiyaondoa mawazo ya waumini katika jambo muhimu kama mazishi ya Mtume.
Imepokewa katika historia kwamba akali ya watu wapatao kumi tu, hivi ndio waliohudhuria katika mazishi ya huyu Mtume mtakatifu wa Mwenyezi Mungu. Hata baadhi ya jamaa zake na wake zake wengine hawakuwa na habari za matayarisho ya mazishi yake hadi waliposikia sauti ya mashepe (wakichimba kaburi). Baada ya kuchagua kiongozi wamtakae hao watu walifululiza moja kwa moja kuelekea nyumba ya Fatimah, wakitaka bay'a yaani kutambuliwa na Ali japo ikibidi kumlazimisha. Namna walivyokwenda kwa vishindo na fujo, waliharibu viamba vya nyumba yake iliyokandikwa na kuitiya moto, mlango wake ulimuangukia Fatimah aliyekuwa amesimama nyuma yake, na kusababisha kifo cha kitoto chake Mohsin aliyekuwa tumboni bado na kusababisha majeraha makali katika mwili wa binti yake Mtume ambaye alisema: "Fatimah ni kipande cha mwili wangu na atakayemdhuru, amenidhuru mimi na atakaye mfurahisha, amenifurahisha mimi."
Ali pamoja na jamii yake walipatwa na fadhaa na huzuni juu ya madhila yaliyowapata hadi Fatimah, alipoomboleza laiti madhila hayo yangeangukia jabali, lingalipasuka na kuvunjika vunjika. Laiti yangeliangukia mwangaza wa mchana, ungeligeuka usiku na kutanda kiza cheusi. Bi Fatimah alifariki baada ya siku sabini tokea alipojeruhiwa na nyumba yake kuvamiwa katika mwaka wa 11 B.H. (632 A.D.) akiwa na umri wa miaka 18 tu, nae alizikwa na vijana wake wawili, Hassan na Husayn ambao Mtume alisema: "Hassan na Husayn ni viongozi wa vijana wa peponi na Husayn ametokana na mimi, na mimi natokana na Husayn," na watoto wawili wa kike; Zainab na Umm-kulthum.
Ali alikaa kando pasi kudai haki yake ya ukhalifa kwa muda wa miaka 25, hadi alipoandamwa na 'kuchaguliwa' kama khalifa wa nne. Na katika wakati wake huo wa ukhalifa alishughulishwa mno na wapinzani wake kutetea uislamu katika vita visivyopungua 40, vilivyozushwa mfululizo kwa miaka 4 ya utawala wake.
UDHALILI NA UGANDAMIZI
Pindi Ali alipochaguliwa kwa wingi wa kura za watu, Muawiya ibne Abu Sufian, alizuka na kujitangazia yeye kuwa ni 'khalifa' wa Islamu katika mwaka wa 36 B.H. (659 A.D.) baada ya kuuliwa Uthman aliyekuwa khalifa wa tatu. Yoyote apendae kumfurahisha mtawala wake, japo kwa kitu kidogo, kitakacho kuwa ni sababu ya kumuudhi Mola wake, huwa ameshaitoka dini ya Allah. Mtume Muhammad(s.a.w.w)
Utawala wake wa dhuluma na ubinafsi uligeuza kila sehemu ya dola ya waislamu wa Hijaz katika upotofu na kuitawala nchi kutoka karibu na mbali na kuendelea kupanua utawala wake pamoja na 'Damascus' (Sham) kama jiji lake kuu. Katika kupuuza kwake si misingi tu ya kiislamu, bali kuendelea kwake na upotofu aliyesambaza machafu na mambo yote maovu yaliyokatazwa katika uislamu kama kuruhusu unywaji pombe, kuendeleza ukahaba na pia kusambaza fitina baina ya waumini na wafuasi wa Mtume pamoja na kuwatesa na kuwadharau 'Ahlul-Bayt' yaani watu wa nyumba ya Mtume.
Mwenendo wa upotofu wa kwenda kinyume cha sharia ya kiislamu kadhalika na kuwatesa watu wa nyumba ya Mtume na kutotambuliwa haki zao tukufu hata kubatilisha sala tukufu ya siku ya Ijumaa kusaliwa siku ya Jumatano na kadhalika, haukukubaliwa katu na wafuasi waadilifu wa Mtume, jambo ambalo lilimkasirisha sana Muawiya na kuwaadhibu wale waliojaribu kumpinga.
Enyi watu, Mtume amesema, kwamba yeyote anaekuta mtawala dhalimu, anaekwenda kinyume na kukiya mipaka mitakatifu na kuvunja shariya ya Allah, kukataa mwendo wa Mtume na kutawala watu kwa ubaya basi asipompinga mtawala huyo kwa maneno na matendo Allah hatompokea na kumueka mahali pema siku ya kiyama.
Imam Husayn ibn Ali
Jambo lingine la upotofu wa Muawiya mtoto wa Abu Sufian lilikuwa kutarakanya maneno ya kinyume cha Ali akiamrisha kutusiwa kwake katika mimbari na kubeza kwamba Mtume ati alimchagua yeye (Ali) kama nafsi yake na kuongeza kwamba Muhammad hakupokea wahyi kamwe. Hatimaye Muawiya alipanga njama ya kumuua Imam Ali wakati alipokuwa akisali ndani ya msikiti wa Kufa katika mwaka wa 40 B.H. (661 A.D.). Hassan ibne Ali, mtoto mkubwa wa Ali pia Imam wa pili vilevile alisumbuliwa, ingawa katika tukio moja la vita Hassan ibn Ali alipigana kishujaa dhidi ya wanafiki walioongozwa na Muawiya na kuandikiana mkataba wa amani.
Mkataba huu wa amani baina ya Hassan na Muawiya ulihusu hifadhi ya ulimwengu wa uislamu kutokana na masharti kadha yaliyotolewa na Hassan, ambayo yalikubaliwa hadharani na Muawiya na kupuuzwa, inamaanisha kwenda kinyume na uislamu. Baadhi ya masharti hayo, ni kuendeleza na kudumisha shariya za kiislamu kulingana na Qur'an tukufu na mwenendo wa sunna ya Mtume Muhammad(s.a.w.w)
, kukomesha mara moja matusi aliyokuwa akitukanwa Ali ibne Abi Talib katika mimbari na Muawiya hatachagua khalifa mwengine baada ya yeke.
Hata hivyo hakuna sharti lolote lililotekelezwa na Muawiya kulingana na mkataba wa amani uliotiwa saini na mali ya wananchi yaliyoporwa na haki zao hazikushughulikiwa wala mwenendo wa Muawiya kinyume cha uislamu haukubadilika bali maonevu na upotovu ulizidi kuendelezwa katika uongozi wake hata kufikilia kiwango cha kutotambulika tofauti kati ya haki na batil, hitilafu baina ya ukweli na urongo au uzuri na ubaya.
Ama kwa kuwapo uhadhiri wa Hassan, muungano wa watu wengi ulikuwa pamoja naye kwa sababu ya ukweli kutawala uongo, ambapo Muawiya na watu wake hawakuridhishwa na msimamo wake Hassan. Walikereka daima na umaarufu wake. Hatimae Muawiya alimshawishi mke wake wa Hassan Jo'ada binti As'ash ambaye alishawishika katika njama ya kumtilia sumu mumewe na matokeo yake yakawa ni kifo cha Imam Hassan, jamaa mwingine wa nyumba ya Mtume "Ahlul-Bayt" katika mwaka 51 B.H. (671 A.D.).
Joa'da aliyehadaiwa na kuahidiwa kuolewa na Yazid mtoto wa Muawiya ambaye alifanywa kuwa mrithi katika utawala, alidanganyika na kuvutiwa na tamaa na ahadi ya urongo ya Muawiya kwamba atakuwa malkia wa pili wa Hijaz, nchi tukufu ya kiarabu, hakuweza kujizuia na matamanio yake ya kutajirika, na kumuua mumewe Hassan ibne Ali, mjukuu wa Mtume. Mara tu baada ya kukamilisha njama yake alivyo-pangiwa na Muawiya, Jo'ada alichukuliwa kama kafiri na alikataliwa kwa kuwa mwanamke asiyekuwa mwaminifu na ahadi aliyopewa ya kufanywa malkia wa Hijaz ikaishilia hapo, na kuharibikiwa na matokeo ya Akhera yake pia.
Husayn ibne Ali ndiye aliyekuwa khalifa wa tatu wa Mtume na wa mwisho katika jamii ya watu wa nyumba, 'Ahlul-Bayt' baada ya Ali ibne Abi Talib na Hassan ibne Ali. Husayn alimzika nduguye Hassan katika maziara ya Madina kuepukana na vita vilivyozushwa na baadhi ya watu waliokuwa na ujamaa kabisa na Mtume lakini hawakuwa katika fungu la watu wa nyumba ya Mtume ambao pia waliamua kumimina mfululizo wa mishale juu ya maiti ya mjukuu wa Mtume ili kuzuia mazishi yake karibu na Mtume. Ndipo nduguye Husayn aliyatenga mazishi ya nduguye kuepukana na umwagikaji wa damu bilashi. Kufa katika utukufu ni bora kuliko kuwa na maisha ya udhilifu.
HUSAYN (a.s) KUHAMA KUTOKA MADINA
Imam Husayn ibne Ali
Mwaka wa 60, B.H. (680 A.D) Muawiya alifariki na kuvunja tena mkataba walioandikiana na Imam Hassan kwa kumchagua mtoto wake Yazid kama Khalifa baada yake. Yazid, ambaye alikuwa ni mbembefu wa wanawake dhahiri hakuwa na maarifa yoyote, wala uhusiano na mwenendo wa waislamu. Hata Uislamu wenyewe hakuutambua, akawa yeye ndiye Khalifa. Nae hakuwa mwenye kusali, alitumia nguvu na kuendeleza ufalme wake kwa kuwatisha watu. Alipendelea sana watu waliokuwa upande wake, aliruhusu vitendo vyote vichafu kama unywaji pombe, uzinifu na kutumia ovyo mali ya mchango wa umma wa Kiislamu kwa njia isiyokuwa haki na maamrisho ya Mwenyezi Mungu yalipuuzwa dhahiri.
Mpotofu huyo Yazid, aliyetokana na ukoo wa Banu Umayya alitafuta bay'a ya watu wote walio chini yake na kuwaapisha juu ya utawala wake. Kadhalika hakuwaacha watu wa Makkah na Madina. Alimtaka na Husayn pia kumpa bay'a kupitia kwa Gavana wake katika Madina, Walid bin Utbah ambae alikuwa ni mjombake Yazid. Walid akiwa na naibu wake, Marwan bin Hakam walitaka kukutana na Husayn katika kasri ya Madina mwezi wa Rajab, ambao ni mwezi wa saba wa kalenda ya kiislamu mwaka wa 60 B.H.
Watu wa Madina kwa jumla walijawa na hofu hasa kwa sababu ya Husayn kuitwa katika kasri ya ufalme. Kinyume cha kutembelewa yeye. Wasiwasi ulisambaa kote na hali yao ilikuwa ya kutishia na kiwewe. Katika mkutano huu, Walid alimjulisha Husayn juu ya kifo cha Muawiya na kutawazwa kwa Yazid kama kiongozi na kwamba sasa Yazid ataka bay'a kutoka kwa watu wa sehemu zote khususan kwake yeye Husayn.
Wasomaji: Hebu tufikirini iwapo tabaka zote za kila sehemu isipokuwa (Husayn na wafuasi wake wachache) wamempa bay'a na kumtambua Yazid, ina maana gani kumsisitiza Husayn na iwapo Husayn amekataa na kutupilia mbali ombi lake, basi angeharibikiwa na nini Yazid aliyekuwa na nguvu zote katika utawala? Ama Yazid, alielewa vyema bay'a ya Husayn haimaanishi kwamba amemkubali kuwa khalifa bali kwa hakika yeye (Yazid) alijiamini nafsi yake kama ndio khalifa wa haki, na kwamba watu wa nyumba ya Mtume Ahlul-bayt wamekubali na kukubaliana na hilo, kungelimaanisha watu wa nyumba ya Mtume na mmoja katika wao wamekubali mwenendo wake wa upotofu kinyume cha uislamu na kuhalalisha unyang'anyi wa haki na mali ya watu. Mtu yeyote mwenye fikira njema asingekubali hilo kwa sababu ingemaanisha ujumbe wa Mtume na dini ya Mwenyezi Mungu haitokuwa na maana yoyote.
Husayn alidhukuru na kulipima suala hilo kwa makini sana katika mizani ya akili yake licha ya kitisho juu ya usalama wa maisha yake na kulitupilia mbali ombi la Yazid. Walid na Marwan, tangu hapo walikwisha panga njama ya kummaliza iwapo Husayn angekataa kumtambua Yazid, kama walivyotarajia, hata kama utakatifu wa nchi ya Madina utaharibiwa na hasa ndivyo ilivyotokea. Baada ya mkutano huo Husayn aliamua kuihama Madina ili kuepukana na uharibifu katika nchi tukufu na uovu wa Yazid. Husayn alitoka na jamii yake isipokuwa Ummi Salma (mke wa Mtume), Fatimah binti Kalebiya (Mke wa pili wa Ali ibne Abitalib na mama wa Abbas ibne Ali) na binti yake Fatima, hawakusafiri pamoja nae.
Msafara huo wa masikitiko na huzuni ulisimamiwa na kutayarishwa na nduguye wa kambo Abbas ibne Ali. Wenyeji wa Madina walipopata habari za kusikitisha za kuhama kwa Husayn, watu wa sehemu zote waliwasili na kumpa pole na hata wengine walimuonya asiende Iraq, kama walivyopokea kutoka kwa Mtume kwamba watu wa nyumba ya Mtume wangeuliwa na kumalizwa Iraq. Abbas, alikuwa ni mtoto wa Ali ibne Abutalib na Fatimah binti Kalebiya mke wa mwisho wa Ali, aliyetamani kuwa na mtoto atakae kumwakilisha katika vita vitakatifu vya Karbala. Na vita hivi vilibashiriwa kitambo na Mtume mwenyewe baada ya mapokeo ya wahyi. Maadamu Mtume atawakilishwa na Husayn, Ali vile vile alipenda awakilishwe na Abbas. Msemo wa Mtume: "Makhalifa wangu watakuwa ni kumi na wawili na wote watatokana na kizazi changu. Mfano wa kwanza ni kama Muhammad, na wa mwisho ni kama Muhammad kila mmoja wa-wao ni kama Muhammad na kwa jumla wote ni kama Muhammad".
Msemo huu, ulidhihirisha ukweli wake katika kila neno. Wakati wakipanda ngamia wao wakusafiria, Husayn alionyesha ulimwengu jinsi wanawake wanavyoheshimiwa katika uislamu kuliko mila ama desturi yoyote nyingine. Yeye mwenyewe alisimamia msafara wakati wakipanda ngamia wao akishuhudiwa na maelfu ya watu ambapo kila mwanamke aliongozwa na maharimu yake akiwa katika vazi lake rasmi la hijab, na vijana wa ukoo wa Hashimia walihakikisha adabu na heshima yao. Taifa linalonunua starehe za maisha kwa kubadilishana na hasira ya muumba halipati kuongoka.
Imam Husayn ibne Ali
HUSAYN KUWASILI KARBALA
Husayn aliondoka Madina siku ya 28, mwezi wa Rajab 60 B.H. (7th May 680 A.D.) na kuwasili Makkah, nchi tukufu yenye usalama kwa watu wote. Hapo mwezi wa Dhulhajj ambao ni mwezi wa ibada ya Hajj katika nchi hiyo tukufu, Husayn aligundua njama ya Yazid aliyetuma majasusi wake wachache na silaha, wakijifanya mahujaji kumbe kusudio lao ni kumuua Husayn akiwa katika ibada hiyo tukufu ya Hijja. Kinyume cha makatazo kwamba hakuruhusiwi kuwinda wala kuua japo kijidudu katika nchi hiyo tukufu wakati wa Hijja.
Yazid alipanga njama za kumuua mjukuu wa Mtume huku akijidai kuwa ni khalifa wa Mtume. Siku ya 9, Dhulhajj, 60 B.H. (13th September 680 A.D.) mahujaji wote wa nyumba tukufu ya Allah wanapoelekea mlima wa Arafat wakiwa na mavazi ya Ehram, Husayn alikatiza hijja yake ambayo ni ibada kuu na kwenda kwenye Umrah na siku hiyo hiyo aliondoka Makkah kwa kusudi la kuhifadhi nyumba tukufu ya Allah, na hiyo ni faradhi yake. Yeye na jamii yake walielekea Kufa, katika mji wa Iraq.
Watu wa Iraq, walikushamuandikia nyaraka nyingi za kumsairi Husayn na kumuita ili aende huko na kuwapa muongozo wake mtakatifu. Na ili kujua undani wa ombi lao Husayn alimtanguliza balozi wake, Muslim ibne Aqeel, ambaye ni binamu yake na mhifadhi wa mafundisho ya sharia za Mtume. Alipokuwa njiani kuelekea Kufa, Husayn alibaini udanganyifu wa watu wa Kufa, ambao walitoroka na kumuacha balozi huyu peke yake kwa kumuogopa Yazid na ubaya wake.
Muslim ibne aqeel, aliyesafiri na watoto wake wawili hawakujulikana mahala walipo. Kuendelea mbele na safari yake Husayn vile vile alipokea habari ya kukatwa vichwa vya watoto hawa, ambao mmoja alikuwa na umri wa miaka minane na mwingine miaka tisa hivi. Msafara wake ulisimamishwa njiani na mlolongo wa majeshi yapatayo elfu moja wapanda farasi walioongozwa na Hurr ibne Riyah ambae aliupendua msafara huo na kuuelekeza upande wa Karbala katika jangwa lililoko kusini mwa Iraq na ambalo limepakana na mto wa Elfurat kwa upande wa kaskazini mwake. Amrisheni mema na kukataza maovu la sivyo waovu watawatawala na mwito wenu kuwa yule aliye bora (anapasa kutawala) hautatiwa maanani Mtume Muhammad(s.a.w.w)
Kufika Karbala Husayn alikita hema lake karibu na ukingo wa mto Elfurat. Kuanzia siku ya pili ya Muharram 61 B.H. - (5th October 680 A.D) majeshi ya Yazid yaliendelea kuongezeka na mara waliwazunguka Husayn na watu wake. Walimlazimisha yeye Husayn pamoja na wenzie waondoshe hema zao kutoka ukingo wa mto na kuzikita mbali kidogo wakiacha nafasi ya uwanja karibu na mto ili kuuzidisha masongamano wa kuteka maji. Hii vile vile ikiwa ni hila moja ya Yazid, kutaka kuwasumbua. Yazid alimtuma kiongozi shupavu wa watu wake, Umar ibne Sa'ad aliyekuwa mjuzi kamili kuhakikisha kwamba viumbe vyote tangu ndege, wanyama na watu wengine wote wapata nafasi ya kuteka maji, isipokuwa watu wa nyumba ya Mtume wasipatiwe maji zaidi.
Siku ya tisa ya Muharram majeshi ya Yazid yaliongezeka na kufikia 'elfu sabini' ambapo Husayn ambae hakujiandaa kivita alikuwa na akali ya watu sabini tu, nao ni pamoja na watoto wadogo. Mara hii tena Yazid alimtuma Umar ibne Saad, akimtaka Husayn amtambue Yazid lakini ombi lake lilikataliwa pia. Na kufikia hali hii, Husayn akijua yatakayompata aliwaita na kuwakusanya watu wake wote akawafahamisha huzuni yake juu ya hali ilivyo na kuwaonya kuhusu yatakayotokea: kukutuliwa kishahidi na wala hakutakuwa na mali itakayotekwa, na kuongeza majeshi ya Yazid yanataka damu yake (Husayn) kwa hivyo yeye yu radhi iwapo wenziwe wangetaka kuondoka na kumuacha yeye peke yake.
Usiku alizima taa zote za kambini ili wapendao kuondoka watoke waende zao wasionekane, lakini hakuna yeyote aliyekubali kuondoka na kumuacha peke yake. Hatimaye watu watatu kutoka kwa jeshi la Yazid walivuka na kumjilia Husayn katika hema lake na kuomba msamaha walipojua vita hivi si vya kupigania ufalme bali ni vita vilivyoanzishwa na Yazid, kutaka kutambuliwa kwake kama Khalifa pasipo haki. Watu hao waliotoka kwa majeshi ya Yazid, ni Hurr bin Riyahi na ndugu yake na mtoto wake. Hurr ndie yule yule aliyezuia na kuuzunguka msafara wa Husayn. Kuambatana na utukufu wa tabia yake ya ukarimu, Husayn hakuukubali msamaha wa Hur tu, bali alimuombea Dua njema. Vile vile alimruhusu kupigana na majeshi dhalimu ya Yazid. Utajiri bora ni kukinai Na ufakiri ni unyonge mbele ya mtu tajiri.
Imam Hassan bin Ali (a.s)
MAUAJI YA KIKATILI YA WATU WA NYUMBA YA MTUME
Ilikuwa jumatano, siku ya kumi, (ashura) ya mwezi wa kwanza wa Muharram kwa kalenda ya kiislamu katika mwaka wa 61 B.H. (13th October 680 A.D.) Husayn alipomwambia mwanawe wa pili Ali Akbar, kuadhini minajili ya sala ya Alfajri ili kuwakumbusha na kuwazindua wale waliomuona na kumsikia Mtume juu ya utakatifu wake Husayn, kwa vile Ali Akber alifanana na Mtume kwa sauti yake na umbo lake pia.
Hili lilikuwa ni lengo la kuwazindua wale waliopotea, ili kuzuia umwagikaji wa damu. Kabla ya kuamkia usiku wa tukio la Ashura (Siku ya tisa maghribi), Abbas ibne Ali ambae ndie aliyekuwa muangalizi mkubwa wa usalama katika kambi ya Husayn, alitokwa na machozi akiona kila mwanamke akiungana na mumewe na watoto wao wakiwahimiza kujitolea kufa kwa kumsaidia Husayn. Huu ndiyo ulikuwa uthabiti wa imani yao kwa Imam. Husayn alipanga vikosi vya usalama, chini ya uongozi wa nduguye Abbas ibne Ali kujitetea mbele ya majeshi dhalimu ya Yazid.
Kama ilivyo, Husayn hakutarajia kupata sifa na ushindi akijitetea na akali ya watu aliyokuwa nao bali alikuwa na lengo la kuwakilisha na kudumisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kutoka kwa Mtume wake aliyemchagua. Alipochoka kuwasairi maadui wake, Husayn aliangua kilio na kuita: "Iwapo dini ya Muhamad, haiwezi kunusurika bila ya ushahidi wangu (kukutuliwa), basi enyi mapanga, njooni mpate kunimaliza".
Kufikia wakati wa adhuhuri nusu ya watu wa Husayn walikwisha kukutuliwa (kuwa mashahidi) na baada ya kumalizika mashujaa wao ikaja zamu ya watu wa ukoo wa Hashimiya ingawa wafuasi hao walipigana na maadui mpaka dakika yao ya mwisho wa pumzi yao, hawakukubali vijana wa Hashimiya waingie vitani. Husayn juu ya fahari ya watu wake alitangaza akisema: "Hakuwa babu yangu wala baba yangu wala ndugu yangu aliyekuwa na watu waaminifu kama hawa wangu." Mmoja baada ya mmoja watu wa Husayn na marafiki zake walimalizwa, akiwamo Habib ibne Mazahir mwenye umri wa miaka thamanini na sita aliyekuwa rafiki yake mpendwa tangu siku zao za utotoni, Muslim ibne Ausajah, Hurr ibne Riyah, John na Wahab na baadhi ya wengine.
Wafuasi hawa hawakutokana na asili moja, kabila, wala nchi. Miongoni mwao mulikuwa na waafrika kumi na watatu waliojitolea kupigania upande wa Husayn wakawa mashahidi minajili ya dini ya Kiislamu na Mwenyezi Mungu. Ilipofika zamu ya vijana wa Hashimiya, waliokuwa baina ya umri wa miaka sita hadi thelathini na nne, hapo Husayn alimtoa kijana wake wa pili Ali Akbar aingie katika uwanja wa vita. Husayn alisema iwapo Mtume angekuwa pamoja nao katika vita hivi, basi yeye Husayn angechukua nafasi badala ya Ali Akbar kuunusurisha Uislamu.
Ali Akbar alifanana na Mtume katika kila njia na fani ya maisha yake hata kwa usemi wake na mwenendo wake wa tabia na umbile na alikuwa mzuri mno katika vijana wa Hashimiya na yeye alishahidiwa katika uwanja wa vita. Habari za kifo cha kijana huyu, zikamfanya Husayn kuomboleza na kujiuliza: "Ni kitu gani kilichobaki ulimwengu huu baada ya kuondokewa na wewe?" Kassim mtoto wa Hassan ibne Ali, ambae ombi lake lilikubaliwa baada ya kunyenyekea sana, alijitolea na kwenda vitani, alikuwa na umri wa miaka kumi na mitatu tu kisha alikuwa ni yeye pekee ukumbusho wa Hassan kaka yake. Kassim, alikanyagwa kanyagwa na kuthinyangwa na mafarasi wa maadui akiwa hai hata akafa.
Bibi Zainab, aliyeandamana na watoto wake wawili, Aun na Muhamad, wenye umri wa miaka sita na saba hivi walijitolea vitani na mara walikutuliwa pia, na Zainab akawachwa pekee. Mmoja baada ya mmoja vijana wote wa Hashimiya waliingia uwanja wa vita na kushahidiwa. Hatimaye kabla ya zamu ya Husayn mwenyewe kufika kwenda kupigania uislamu, ndugu yake Abbas ibne Ali aliyekuwa shujaa mno mwenye nguvu na ujuzi mwingi wa kijeshi, alinyenyekea sana akitaka ruhusa ya kwenda yeye vitani ingawa alikatazwa mara nyingi. Badili yake Abbas akaagizwa akateke maji kwa ajili ya watu wa nyumba kutoka mto wa Elfurat.
Ilikuwa ni siku tatu tangu jamii ya Mtume kuishiwa na maji ya kunywa toka watu wazima hadi mtoto mchanga wa miezi sita hawakuwa na tone la maji. Abbas ibne Ali alijitahidi akafanikiwa kuteka na kujaza mtungi wa maji kutoka mtoni na alipokuwa akirejea huku amebeba mtungi wake, maadui walimshambulia kutoka nyuma wakihakikisha kwamba maji hayakufikia watoto wa kambi ya Husayn bali na kumuua nduguye Husayn aliyekuwa mpiganaji hodari, kiongozi mtukufu wa majeshi yote, akabakia Husayn peke yake Kwa hakika kifo (shahada) cha Husayn kitaamsha mori katika nyoyo za waumini ambao hautapoa milele. Mtume Muhammad(s.a.w.w)
.