• Anza
  • Iliyopita
  • 11 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 4341 / Pakua: 2516
Kiwango Kiwango Kiwango
MASOMO YA KI-ISLAMU 2

MASOMO YA KI-ISLAMU 2

Mwandishi:
Swahili

MASOMO YA KI-ISLAMU

KITABU CHA PILI

DIBAJI

Je, wajua nani Mwislamu? Mwislamu ni ambaye anaamini kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja na Muhammad ni Mtume wake wa mwisho. Kama ukiamini haya, basi wewe ni Mwislamu.

Lakini haitoshi kusema tu kuwa mimi ni Mwislamu; bali ni wajibu juu yako kutenda kwa mujibu wa kanuni za Ki-islamu, ili uwe Mwislamu wa ukweli, na uishi duniani katika raha, na upate utukufu Akhera[1] kwa kuingia peponi na kupata ridhaa za Mwenyezi Mungu.

Basi ni lazima juu yako kujitahidi kufanya hayo.

Na Uislamu una sehemu tatu:

(1) Asili (Mizizi) ya Dini

(2) Matawi ya Dini

(3) Tabia (Mwenendo) ya Dini

Basi anayekubali kwa ukweli Asili ya Dini, na kutumia Matawi ya dini, na akiishajipamba na tabia ya dini, basi yeye ni mbora duniani na akhera (Kiyama[2] ).

Kitabu hiki kimesahihishwa na kimepangwa na Ayatullah Allamah Al-Haj Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, Muasisi na Muhbiri Mkuu wa Bilal Muslim Mission of Tanzania.

MASOMO YA KI-ISLAM

KITABU CHAPILI

1. Somo la Kwanza

Ndugu yangu, Katika kitabu cha kwanza, umeelewa kuwa walikuja maimam (Viongozi wa dini) kumi na wawili baada yake Mtume Mtukufu(s.a.w.w) .

Katika kitabu hiki tunataja, kwa ufupi, hali (maisha) za mabwana hawa, pamoja na hali ya binti wake Mtume(s.aw.w) , naye ni mke wa wasii wake Mtume, na mama ya maimamu wengine.

Basi mimi ninataja hali zao hawa watukufu kwa ajili ya kuthibitisha imani, na kwa kujijulisha kwao ili tupate ugezo mwema katika maisha yetu.

Na yeyote akiwafuata na kutumia vitendo vyao na kufuatisha mwendo wao, basi kawa mtukufu duniani na akhera. Mungu ni msaidizi.

IMAM WA KWANZA

Naye ni Ali bin Abi Talib(a.s) , na mama yake ni Fatima binti Asad, Ibnu Ami Rasulillahi: na mume wa binti wake Mtume(s.a.w.w) . Ndiye Khalifa juu ya watu baada yake, naye ni Amirul Muuminiin (Mkuu wa walioamini), mzazi wa Maimamu wote (juu yao Amani na Rehema).

Kazaliwa bwana huyu Kaabani (ndani ya Kaaba[3] Tukufu) Maka, siku ya Ijumaa, usiku wa mwezi kumi na tatu, mfungo kumi, baada ya kupita miaka thelathini toka kuzaliwa Mtume(s.a.w.w) .

Na akawa shahidi (akauawa kwa ajili ya dini) usiku wa Ijumaa ndani ya msikiti wa Kufa mihirabuni[4] kwa kupigwa upanga na Abdur-Rahman bin Muljimu (Mungu amuweke pabaya), usiku wa mwezi kumi na tisa, mwezi wa Ramadhani Mtukufu; akafa kwa siku ya tatu toka kupigwa. Na umri wake mtukufu ni miaka sitini na tatu.

Akasimamia matengenezo ya mazishi yake Imam Hassan na Hussein(a.s) , na akazikwa katika Najaf (Iraq)alipokuwepo sasa.

Yuna Bwana huyu mwema makuu na fadhila (ubora) zisizo hesabika. Amekuwa ni mtu wa kwanza kuamini; wala hakusujudia sanamu hata kidogo, na hakupata kushindwa vita vyovyote alivyo viongoza, wala hakuwahi kukimbia kunako mashambulizi yoyote ya maadui.

Na katika jumla ya fadhila zake, Mtume(s.a.w.w) kasema: "Kadhi mwenye kuamua vizuri kuliko wote ni Ali (a.s) . "

Na katika uwingi wa elimu yake, Mtume(s.a.w.w) kasema: "Mimi ni Jiji la Elimu na Ali (a.s.) ni mlango wake ."

Basi inatuonyesha kwamba atakaye elimu ya Mtume(s.a.w.w) ni lazima apitie mlangoni na ufunguliwe, na kama hakufunguliwa basi hana elimu, na kufunguliwa kwake ni kumfuata mafunzo yake na mwenendo wake Imam Ali(a.s) .

Na katika kulazimiana na Haki, basi Mtume(s.a.w.w) kasema: "Ali yu pamoja na Haki na Haki ipopamoja na Ali ."

Sina shaka wasemi wamesema kama mtambuzi, tambua wewe mwenyewe.

Na alikuwa mwadilifu kwa raia wake, mgawa kwa usawa, mchamungu katika mshuko wa ulimwengu.

Alikuwa akienda katika idara ya mali (Hazina) na hutazama dhahabu na fedha na husema: "Ee ung'avu wake! Ee uweupe wake! Umkhadaa mwingine, siyo mimi". Kisha hugawa kwa watu.

Alikuwa anawahurumia maskini, hukaanao mafakiri; huwatekelezea wenye shida, na husema ukweli, na huhukumu kwa uadilifu.

Na kwa ujumla, yeye alikuwa kama Mtume katika kila sifa mpaka akamjaalia Mungu Mtukufu, katika aya ya Qur'an, kuwa yeye ni "Nafsi.

MASOMO YA KI-ISLAM

KITABU CHAPILI

2. SOMO LA PILI

BINTI WA NABII(s.a.w.w).

Yeye ni Fatima Zahra; Baba yake ni Rasulullah (Mjumbe na Mtume wake Mwenyezi Mungu) Muhammad bin Abdullah(s.a.w.w) ; na mama yake ni Bibi Mtukufu Khadija Mama wa Waislamu, na mumewe ni bwana wa mawasii Ali Ameerul-Muuminiin, na watoto wake na wajukuze ni maimam watoharifu (juu yao Rehma na Amani).

Alizaliwa Bibi Fatima(a.s) siku ya mwezi ishirini, mwezi wa mfungo tisa, mwaka wa arobaini na tano toka alipozaliwa Mtume(s.a.w.w) .

Na akafa bibi huyo siku ya jumanne mwezi tatu, mfungo tisa, mwaka wa kumi na moja wa Hijiria[5] . Na umri wake ni miaka kumi nanane.

Na akasimamia matendo ya kifo chake Amirul Muminiin Ali(a.s) , akamzika Madina Munawwara (Mji wenye nuru, mji wake Mtume, uliopo katika Saudia Arabia), na akalificha kaburi lake kama alivyo usia mwenyewe Bibi Fatima.

Alikuwa bibi huyo kama baba yake kwa ibada na kumcha Mungu na ubora, na zimeshuka katika sifa zake aya nyingi za Qur'ani al-Hakim.

Alikuwa Mtume(s.a.w.w) akimwita "Bibi wa wanawake wa Ulimwenguni ", na akimpenda mapenzi mazuri mpaka yeye akiwa anaingia kwa Mtume(s.a.w.w) humkaribisha na kusimama na kumkaliza mahali pake, pengine humbusu mikono yake.

Na Mtume(s.a.w.w) akasema: "Mungu huridhika analoridhika Fatima na hukasirika Unalo mkasirisha Fatima ."

Pia Mtukufu Mtume amesema: "Wabora wa wanawake wa peponi ni wanne: Mariam Binti Imrani, na Khadija Binti Khuwailid, na Fatima Binti Muhammad (s.a.w.w) na Aasia Bint Muzaahim .

Mtu mmoja akamwuliza bibi Aaisha "Mtu gani alikuwa mpenzi mno wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w)? Akajibu: Fatima .

Kisha akamwuliza: Ni gani kutokana na wanaume? Akajibu: Mume wake Bibi Fatima, yaani Ali bin Abi Talib(a.s) .

Mtume Mtukufu(s.a.w.w) akasema: "Hakika, Mwenyezi Mungu ameniamrisha mimi nimwoze Fatima kwa Ali (a.s) .

Kazaa bibi huyo kwa Amirul Muuminiin Ali(a.s) : Imam Hassan(a.s) Imam Hussein(a.s) Bibi Zainab(a.s) Bibi Ummu Kulthum(a.s) . Muhsin(a.s) Lakini bwana Muhsin kafa tumboni zama alipopata mama yake msukosuko wa maadui. Kwa hiyo jumla ya watoto wa bibi Fatima ni 5.

Mtume Mtukufu(s.a.w.w) amesema: "Kila mtoto huchukuwa ukoo wa baba yake ispokuwa vizazi vya Fatima, kwani mimi ndiyo walii wao na nasaba wao (yaani, vizazi vya Fatima wote ukoo wao unatokana kwa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) .

Pia Mtume Mtukufu amesema: "Kila ukoo na uhusiano utafatia siku ya qiyama ispokuwa ukoowangu na uhusiano wangu .

MASOMO YA KI-ISLAM

KITABU CHAPILI

3. SOMO LA TATU

IMAM WA PILI

Naye ni Hassan bin Ali bin Abi Talib(a.s) . Mama yake ni Fatima Zahra binti wake Mtume(s.a..w.w ) . Na Bwana huyu ni mjukuu wake Mtume(s.a.w.w) , na ni wapili katika makhalifa wake, na ni Imam juu ya watu, baada ya baba yake Amirul Muuminiin Ali(a.s)

Kazaliwa Madina Munawwara, siku ya Juma nne, nusu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, mwaka wa tatu wa Hijiria.

Na akafariki hali ya kuwa shahidi kwa kupewa sumu, siku ya alhamisi, mwezi ishirini na nane, mwezi wa mfungo tano, mwaka wa arobaini na tisa wa Hijiria.

Na akasimamia maziko yake ndugu yake Imam Hussein(a.s) , na kazikwa Bakii mji wa Madina, mahala palipo kaburi lake sasa.

Alikuwa mwabudu mno katika zama zake, na mwenye elimu mno na mbora sana, alikuwa kamshabihi mno Mtume(s.a.w.w) ; na mkarimu mno katika Ahlul Bayt (Vizazi vyake Mtume) zama zake, na mpole mno kuliko watu wote.

Ni katika jumla ya ukarimu wake kuwa alimjia mjakazi wake na shada la mrehani; akamwambia: "Wewe ni huru kwa lillahi " (kwa ajili ya kupata ridhaa ya Mwenyezi Mungu). Kisha akaseina:- "Hivi hakutufunza Mungu Mtukufu Akisema:

وَإِذَا حُيِّيتُم بِتَحِيَّةٍ فَحَيُّوا بِأَحْسَنَ مِنْهَا أَوْ رُدُّوهَا إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَسِيبًا ﴿٨٦﴾

Na mnapo amkiwa kwa maamkio yoyote, basi nanyi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo, au rejesheni hayo hayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuhisabu kila kitu.

Na katika upole wake, alimwona mtu wa Shami kampanda mnyama, alikuwa anamlaani Imam Hassan(a.s) , lakini Imam hakumrudishia lolote. Alipomaliza laana yake, Imam akamwendea na kumtolea salamu na akamchekea, na akamuuliza: "Ewe! Mzee, ninakudhani kuwa wewe ni mgeni; huenda wewe umekosa kunifahamu, basi lau ungalitaka tungalikutolea shida yako; na lau ungali tuomba tungalikupa, na lau ungali taka kukuongoza tungalikuongoza, na lau ungali taka kukuchukua tungali kuchukua, na lau ukiwa na njaa tutakushibisha na ukiwa huna nguo tutakuvisha, na ukiwa unaona upeke tutakuwa nawe; na ukiwa na haja tutakutekelezea haja yako."

Aliposikia yule mtu maneno yake Imamu, akalia, akasema: "Ninatoa shahada kuwa wewe ni Khalifa wa Mungu katika ardhi yake, na Mungu anajua mahala anapojaalia ujumbe wake."

Na Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mwenye furaha ya kutaka kumwangalia Bwana wa vijana wa peponi amwangalie Hassan(a.s) ."

Na Mtukufu Mtume(s.a..w.w) amesema: "Mwenye kunipenda mimi ampende yeye (yaani Hassan).

Imam Hassan alikwenda hija mara ishirini na tano, na alikuwa anakwenda kwa miguu kutoka Madina mpaka Maka.

Bwana Abu Huraira, Sahaba wake Mtukufu(s.a.w.w) amesema: Akaja Hassan bin Ali, na akatoa salamu na jamaa wakamjibu; na akaendelea na nyendo zake, na Abu Huraira hajuwi aliwasalimu ni nani? kisha akaambiwa kwamba aliyetusalimu ni Hassan bin Ali.

Hapo Abu Huraira akamfuata na akasema: Salaam juu yako, ewe bwana wangu!

Watu wakamuuliza, "mbona unamwita bwana wako?

Akasema Abu Huraira, "Ninakiri kuwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) akasema: "Hakika yeye ni bwana ."

MASOMO YA KI-ISLAM

KITABU CHAPILI

4. SOMO LA NNE

IMAMU WA TATU

Naye ni Hussein bin Ali bin Abi Talib(a.s) , na mama yake ni Bibi Fatima, binti yake Mtume(s.aw.w) , na yeye ni mjukuu wa Mtume(s.a.w.w) , ni wa tatu katika Makhalifa, na ni baba wa maimamu tisa baada yake, na ni Imam wa watu baada ya kaka yake (Imam Hassan) (a.s) .

Kazaliwa Madina Munawwara, mwezi tatu Shaaban, mwaka wa nne wa Hijiria.

Kauwawa hali ya kudhulumiwa kwa upanga katika hali ya kiu, katika mapigano ya Ashura[6] yaliyoko mashuhuri, siku ya Ijumaa, mwezi kumi mfungo nne mwaka wa sitini na moja wa Hijiria, na akasimamia mambo ya mazishi yake baada ya siku tatu mtoto wake Ali Zainul Abediin(a.s) , akamzika mahala lilipo kaburi lake sasa katika mji wa Karbala Mtakatifu.

Fadhila zake hazitajiki. Yeye ni manukato ya Mtume(s.a.w.w.w) , kama alivyo sema Mtume(s.a.w.w) kwa yeye na kwa kaka yake Imam Hassan (a.s) : "Wao ni manukato yangu duniani".

Na akasema Mtume(s.a.w.w) : "Hussein ni katika mimi na mimi ni katika Hussein ." Pia akasema: "Hassan na Hussein ni maimamu ijapokuwa wamesimama au wamekaa ."

Alikuwa mjua mno na mwabudu mno, alikuwa anasali kila usiku elfu rakaa kama baba yake Amirul muuminiin Ali(a.s) .

Alikuwa anabeba siku nyingi mifuko ya vyakula kuwapelekea mafakiri, mpaka ikaonekana alama ya mizigo baada ya kuuwawa kwake; na alikuwa mkarimu, mpole na alikuwa anaghadhibika anapoona mtu akifanya kinyume cha sheria ya kiislamu.

Na katika ukarimu wake kuwa Mwarabu mmoja alimkusudia kwa kutaka haja yake. Akamfanyia mashairi (nashidi), akasema: "Hakurudi utupu ambaye akakutumai na akakusudia mlangoni kwako ."

"Wewe ni mkarimu na wewe mwenye kutegemewa: baba yako alikuwa muuwaji wa fasiki (wale wanaomwasi Mwenyezi Mungu)."

"Lau si ambayo imekuwa kutoka kwa wazee wenu, ingalitufunika moto wa Jahannam."

Imam Hussein(a.s) aliposikia nashid hii akampa dinari elfu nne, na pia akamtaka msamaha kwamashairi haya:-

"Chukua hizi, mimi kwako ninataka msamaha, jua kuwa mimi ni mwenye huruma kwako.

"Lau tungalikuwa na fimbo katika mwenendo wetu wa mapema yangalikuwa mawingu yetu juu yako yenye kunywesha (kama ungalikuwa utawala wa dola ya Islamu mkononi mwetu, tungalikusaidia zaidi).

"Lakini khadaa ya zama ina migeuzo, na kitanga changu ni kichache cha nafaka (matumizi)."

Akahisha(a.s) kwa msimamo wake wa ushujaa (ambao hapana mfano ulimwenguni) sharia za Ki-Islamu na dini ya baba yake Rasulullah(s.a.w.w) , kamwe kuhuisha ulimwengu mzima mpaka siku ya kiyama.

Yeye ni bwana wa mashahidi na mbora mno baada ya kakaye.

MASOMO YA KI-ISLAM

KITABU CHAPILI

5. SOMO LA TANO

IMAMU WA NNE

Naye ni Imam Ali bin Hussein(a.s) , na mama yake Shah Zanan, binti ya Mfalme Yazdajurd. (ShahZanan-Mfalme wa wanawake). Bibi huyo tena anaitwa "Shahr Bano" (Bibi wa Mji). Imam huyu kazaliwa Madina Munnawwara, nusu ya mwezi wa mfungo nane, mwaka thelathini na sita, siku aliyoteka Ali(a.s) Basra. Na kafa hali ya kupewa sumu siku ya Jumamosi, mwezi ishirini na tano, mfungo nne, mwaka wa tisini na tano wa Hijiria. Na umri wake mtukufu ni miaka khamsin na saba. Kazikwa Bakii, mji wa Madina.

Alikuwa bila ya mfano katika elimu, na ibada na fadhila, na uchamungu, na kuwasaidia waliopata shida. Na wamepokea kutoka kwake(a.s) wanachuoni wengi, na yamehifadhiwa kutokana kwake mawaidha, na uradi na Historia na mengineyo.

Alikuwa anatoka usiku anachukua mifuko ndani yake zimo dinari na dirhamu; na wakati mwingine akibeba vyakula au kuni, hata akifika majumba ya masikini na hugonga mlango, kisha huwapa alichonacho. Alikuwa akiuficha uso wake kwa sababu wasimjue masikini. Zama alipokufa ndipo walimjua kuwa yeye ndiye mchukuaji mifuko ya mapesa na vyakula.

Alikuwa anapendeza mno kula nao masikini na viwete na mayatima. Alikuwa mzuri mno wa tabia, alikuwa akiwaita kila mwezi watumishi wake na huwaambia:- "Akiwa yeyote katika nyie anayetaka kuolewa nitamwozesha au kumwuza nitamwuza, au kumwacha huru nitamwacha huru." Alikuwa anasema anapomjia mtu kutaka msaada: "Marahaba kwa mwenye kufikisha akiba yangu akhera."

Na katika uchamungu wake, alikuwa anasali mchana na usiku elfu rakaa[7] ; na utapoingia wakati wa sala hutetemeka mwili wake, na hugeuka uso wake rangi ya njano, na kiwiliwili chake hutetemeka kama kuti. Na alikuwa anaitwa "DHUTH-THAFANATI" yaani mwenye magome. Na sababu yake kuwa kwa wingi wa kusujudu yakamtokea magome katika paa lauso, na vitanga vya mikono na magotini na katika vidole gumba. Kila miezi sita yakikatwa magome haya.

Na alikuwa kila anapomkumbuka Mwenyezi Mungu na neema zake, husujudu, na kila anaposoma aya yenye sijida, husujudu, na kila anapomaliza swala ya faradhi husujudu na huitwa As-Sajaad (yaani mwenye kusujudu sana).

Na wakati ule walikuwa wakisema "Hatukumwona Mquraish mbora kuliko yeye."

Na alitukanwa na mtu katika jamaa zake na kusikia yasiyompendeza, naye alikaa kimya. Baada ya muda mdogo akaenda Imam(a.s) kwake. Wakadhani waliokuwepo kuwa Imam(a.s) anataka akamrudishie, sivyo, laa hasha, alisoma Imam(a.s) maneno ya Qur-an haya:

وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٣٤﴾

Na wavunjao ghadhabu na wanaosamehe watu, na Mungu anawapenda watendao mema.

Kisha Imam(a.s) akasema kumwambia yule aliye tukana: "Ee ndugu yangu! wewe umetushambulia sasa hivi, ukasema uliyoyasema, ikiwa ndivyo ulvyo sema kwangu, basi Mungu anisamehe, na ikiwa ulivyosema sivyo basi Mungu akusamehe ."

MASOMO YA KI-ISLAM

KITABU CHAPILI

6. SOMO LA SITA

IMAMU WA TANO

Naye ni Imamu Muhammad Al-Baqir(a.s) . Baba yake ni Imamu Ali Zainul-Abidiin(a.s) na mama yake ni Fatima binti wa Imam Hassan(a.s) .

Kazaliwa siku ya Jumatatu mwezi wa mfungo kumi, mwaka wa khamsini na saba.

Baba yake alikuwa mjukuu wa Imam Ali bin Abi Talib(a.s) , na vile vile mama yake alikuwa mjukuu wa Imamu Ali bin Abi Talib(a.s) Kwa hiyo, yeye alikuwa mtu wa kwanza aliyekuwa kijukuu wa Imam Ali bin Abi Talib(a.s) kwa pande mbili.

Alikufa kwa kupewa sumu siku ya Jumatatu, mwezi saba, mfiingo tatu, mwaka wa mia moja na kumi na nne wa Hijiria.

Umri wake ni miaka khamsini na saba, kazikwa Bakii-katika Madina Munawwara.

Alikuwa mwenye fadhila kubwa na utukufu na ucha Mungu, na alikuwa na Elimu nyingi na upole mwingi, na tabia nzuri, na ibada na unyenyekevu na ukarimu.

Hadithi hii inaonyesha uzuri wa tabia yake: Siku moja, mkristo mmoja akamwambia Imam(a.s) : "Wewe ni ng'ombe." Imam akamjibu: "Mimi ni Baqir (mchimbua elimu) ." Mkristo akasema tena:-"Wewe ni mtoto wampishi." Akasema Imam(a.s) "Hiyo kazi yake." Akamwambia tena:- "Wewe ni mtoto wa mshenzi." Akamjibu Imam(a.s) "Ikiwa ulivyo sema ni kweli, Mungu amsamehe, na ikiwa ulivyosema ni uongo, basi Mungu akusamehe ."

Kwa alivyoona upole wa Imam(a.s) , akasilimu mkristo yule hapo hapo.

Bwana Jabiri bin Abdillah, Sahaba wake Mtume amesema, "Nilikuwa siku moja kwa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) , huku amempakata mjukuu wake Imam Hussein(a.s) mapajani, anacheza naye. Basi Mtukufu Mtume akamwambia: Ewe Jabir, huyu mwanangu atapata mwana jina lake litakuwa Ali, ikiwa siku ya Qiyama mwitaji atataja: Asimame Sayyidul Abidiin (Bwana wa wenye ibada). Na huko atasimama Ali bin Hussein. na atamzaa kwa huyo mtoto ataitwa Muhammad, basi ewe Jabir, ukimdiriki nisalimie. Na ukikutana naye basi ujue kuwa hutaishi sana baada ya hapo.

Alikuwa bahar ya elimu. Alikuwa anaelezea kila swali analoulizwa pasina kupapasia. Akasema Ibnu Ata Al-Makki: "Sikuona wanachuoni kuwa wadogo mbele ya yeyote isipokuwa akijambele ya Imam Muhammad Al-Bair(a.s) . (Maana yake kuwa mwana chuoni yeyote akifika mbele ya Imam huyu huonekana kuwa anayo elimu ndogo sana). Hakika nimemwona Hakimu bin Utayba (na yeye ana heshima mbele ya watu) mbele ya Imam(a.s) kama mtoto mbele ya mwalimu wake."

Akasema Muhammad bin Muslim: "Hakikupita moyoni mwangu chochote ila nilimwuliza Imam Muhammad Al-Baqir(a.s) . mpaka nilimwuliza thelathini elfu hadithi."

Alikuwa Imam(a.s) anamkumbuka Mwenyezi Mungu daima, hata akasema mwanawe Imamu Jaafar Sadique(a.s) : "Baba yangu alikuwa mwingi wa dhikiri, nilikuwa ninakwenda nayeye, na yeye anadhikiri Mungu, na alikuwa anazungumza na watu, na hali ile ile haachi kumkumbuka Mwenyezi Mungu, na alikuwa anasali tahajjudi[8] kwa kirefu, na alikuwa mwingi wa ibada, alikuwa analia sana kwa mapenzi ya Mungu."

MASOMO YA KI-ISLAM

KITABU CHAPILI

7. SOMO LA SABA

IMAMU WA SITA

Yeye ni Jaafar bin Muhammad, As-Sadiq(a.s) , mama yake ni Fatima (Na jina lake lingine ni Farwah).

Kazaliwa Imam(a.s) Madina, siku ya Jumatatu, mwezi kumi na saba, mfungo sita. siku alipozaliwa Mtume(s.a.w.w) , mwaka wa thamanini na tatu Hijiria.

Amekufa kwa kupewa sumu, siku ya ishirini na tano, mfungo mosi, mwaka wa mia moja na arobaini na nane. Ulikuwa umri wake miaka sitini na tano.

Alikuwa Imam(a.s) ana elimu na ubora na hekima, na ujuzi wa sheria, na uchamungu. na ukweli na uadilifu na ubwana na ukuu na ukarimu, na ushujaa, na mambo mengine matukufu yasiyo hifadhika.

Akasema Al-Mufid: "Hawakuchukua wanachuoni kwa yeyote katika ahlul-bayt kama waliyonakili kwake, wala hajakutana na yeyote katika wanachuoni wa hadithi na historia aliye eneza elimu kuliko Imam Jaafar As-Sadique(a.s) .

Hakika wamekusanya majina ya watu waliopokea elimu kwake yeye (watu waaminifu na wenye imani mbalimbali , walikuwa watu elfu nne.Abu Hanifa, kiongozi wa Masuni, alikuwa mmoja wapo.

Na kwa sababu ya uchamungu wake, alikuwa anakula siki na mafuta na akivaa khanzu nzito si nzuri sana. Na pengine nguo zake zilikuwa na viraka.

Alikuwa anafanya kazi mwenyewe bustanini mwake. Na pengine alikuwa anaghumiwa katika ibada ya Mwenyezi Mungu.

Usiku mmoja Rashidi akampelekea mtu kumwita. Akasema mtumishi wake, "Nilikwenda kwake, nilimkuta katika chumba cha faragha, yamevurugika mashavu yake kwa udongo, kwa unyenyekevu,

anamwomba Mwenyezi Mungu huku akiinua mikono yake, pana alama ya mchanga usoni mwake na mashavuni mwake.

Alikuwa Imam(a.s) mwingi wa kutoa sadaka, mzuri kwa tabia, mlainifu kwa maneno, mzuri kwa kikazi na kushirikiana naye.

Siku moja Imam(a.s) alimwita mtumwa wake aitwae Musaadifu, akampa dinari elfu moja na akamwambia ajitayarishe kwa safari ya kwenda Misri kwa biashara. Kwani watu wa nyumbani wamezidi kuwa wengi, na nilazima kutafuta njia ya maisha.

Musaadifu akanunua vitu vya biashara na akaelekea Misri pamoja na kundi la wafanya biashara. Walipokaribia Misri, walikutana na kundi lingine waliokuwa wanatoka Misri, wakawaeleza, sisi tunavyo vitu fulani, je? vitu hivi vinapatikana kwenye mji?

Wakajibu, "hapana". Wakaahidiana kuwa wasiuze vitu vyao chini ya faida ya mia kwa mia. Wakafanya hivyo; baadae, wakarejea Madina.

Musadifu alikwenda kwa Imam(a.s) akachukua mifuko miwili, na ndani ya kila mfuko mna dinari elfu moja, na akasema:- mfuko huu ni ule wa rasilimali na huu ni faida.

Hapo Imam akamwambia, faida hii ni nyingi mlifanyaje kwenye vile vitu? Akamuelezea namna walivyofanya na namna walivyoapa.

Hapo Imam(a.s) akastaajabu sana na akasema, je mliapa kuwa hamtawauzia umma wa Waislam ila kwa faida ya mia kwa mia?.

Kisha akachukua mfuko mmoja na akasema: "Huu ni rasilmali yangu, na wala hatuna haja ya faida ."

Kisha akasema: "Ewe Musaadifu, kupigana kwa panga ni rahisi kuliko kutafuta maisha kwa njia ya halali ."

MASOMO YA KI-ISLAM

KITABU CHAPILI

8. SOMO LA NANE

IMAMU WA SABA

Naye Imamu Musa bin Jafar, Al-Kadhim(a.s) . Mama yake ni Bibi Hamida Al-Musaffatu. Imam huyu kazaliwa Ab- wa, (Hapo ni mahala kati ya Maka na Madina), siku ya Jumapili, mwezi saba, mfungo tano, mwaka mia moja ishirini na nane Hijiria.

Alikufa Imam, kwa hali ya kupewa sumu, ndani ya gereza la mfalme Haruna. Alikaa humo muda mrefu kwa kufungwa, miaka kumi na nne kwa dhuluma na mateso tu. Alikufa mwezi ishirini na tano, mfungo kumi, mwaka mia moja na thelathini na tatu Hijiria.

Akasimamia mazishi yake mtoto wake Ali Ar-Ridha(a.s) Kazikwa mtukufu katika Kadhimiya, mahala lilipo kaburi lake sasa.

Alikuwa anavunja ghadhabu; kwa hivyo akaitwa Al-Kadhimu' (Maana yake: Mvunja ghadhabu).

Na kwa sababu ya wema wake akaitwa'Al-Abdus-Salih' (Maana yake:- Mja mwema).

Ikaonekana elimu yake katika mambo mbali mbali iliyowashangaza watu. Na hadithi ya mazungumzo yake na Buraina (Mkuu wa wanaswara) ni mashuhuri, alipomshinda Imam(a.s) akasilimu kwa nia halisi.

Maskini mmoja alimwomba Imam(a.s) Dinari mia moja. Imam(a.s) akamuuliza maswali ili kujaribu kiasi cha maarifa yake. Alipomjibu akampa Dirham elfu mbili.

Alikuwa Imam(a.s) mzuri mno kwa sauti kusoma Qur'ani. Na alikuwa mwingi wa ibada na kusoma Qur'an, na alikuwa anasujudu muda mrefu, na alikuwa mwingi wa kulia kwa mapenzi ya Mungu. Kafa Imam(a.s) katika hali ya sijida.

Abu Hamza alimwona Imam Musa Al- Kadhim(a.s) anafanya kazi kwenye shamba akiwa mwenye kujaa jasho kwenye miguu yake. Akamwuliza, wako wapi wafanyakazi?

Akamjibu. Ewe Abu Hamza, amefanya kazi kwa mikono yake aliyekuwa mbora zaidi kuliko mimi na baba yangu.

Abu Hamza akamwuliza, Ni nani huyo?

Akamjibu:- Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t) na Amirul -Muuminiin Ali(a.s) , na wazazi wangu wote walikuwa wafanya kazi kwa mikono yao. Na njia hii ni njia ya Mitume na Mur-saliin na Mawasii na Ma-Saleh wote.

9. SOMO LA TISA

IMAMU WA NANE

Imam Ali bin Musa Ar -Ridha(a.s) . Mama yake ni Bibi Najma.

Kazaliwa Imam(a.s) siku ya Ijumaa, mwezi kumi na moja, mfungo pili, mwaka wa mia moja na arobaini na nane Hijiria, Madina Munawwara.

Kafa kwa kupewa sumu , siku ya mwisho wa mwezi mfungo tano, rnwaka mia mbili na tatu. Akashughulikia mambo ya mazishi yake mtoto wake Al-Jawad(a.s) .Na kazikwa Mash-had mahali palipo kaburi lake sasa.

Elimu yake, na utukufu na ukarimu wake, na uzuri wa tabia na unyenyekevu wake, na ibada zake zinajulikana sana ulimwenguni, na haina haja ya kuzitaja.

Mfalme Mamun alitaka kumtawalisha mambo ya Ukhalifa wa ki-Islamu mahala pake. Lakini Imam(a.s) hakukubali kwa sababu nia yake Mamuni haikuwa safi. Na wakati alipokataa Ukhalifa, Imam(a.s) alilazimishwa na Mamun kukubali awe makamo baada yake. Lakini Imam(a.s) akatoa sharti kwamba hatafanya chochote katika mambo ya dola.

Umedhihiri uwingi wa elimu yake kuhusu dini na madhehebu mbalimbali katika mikutano ya mashindano ambayo aliyoifanya Mamun. Hata wasafiri waliporudi mijini kwao walikuwa wanahadithia habari za elimu yake.

Imam(a.s) alikuwa anakesha kucha kwa ibada, na anasoma (Qur'ani nzima kwa siku tatu. Na wakati mwingine alikuwa anasali mchana na usiku rakaa elfu, na akisujudu kwa muda mrefu. Na alikuwa akifunga mara nyingi.

Alikuwa Imam(a.s) mwingi wa kutoa na kufululiza sadaka kwa siri, hasa katika usiku wa giza. Hakumkatisha Imam(a.s) maneno ya mtu yeyote, wala hakutumia neno chafu, wala hakutegemea chochote mbele ya mtu, wala hakucheka kwa sauti wala hakutema mate mbele ya yeyote.

Na wakati wa kula huwaita jamaa zake na watumishi wake mpaka wakeze na hula pamoja nao.

10. SOMO LA KUMI

IMAM WA TISA

Naye Imam Muhammad Taki bin Ali, al Jawad(a.s) . Mama yake ni bibi Sabika. Kazaliwa Imam(a.s) mwezi kumi, mfungo kumi, mwaka wa mia moja na tisini na tano, Hijiria, Madina Munawwara.

Kafa, hali ya kupewa sumu, Baghdadi mwisho wa mfungo pili, miaka mia mbili na ishirini.

Kazikwa nyuma ya babu yake, Imam Musa bin Jafar(a.s) mahala lilipo sasa kaburi lake katika Kadhimiya.

Alikuwa Imam(a.s) mwanachuoni mno zama zake, na mbora na mkarimu na mtoaji, mzuri mno kwa kikazi, na mbora wa tabia, na alikuwa fasaha mno.

Alikuwa anapopanda mnyama huchukuwa dhahabu na fedha, na kama akiombwa na yeyote njiani humpa. Na akiombwa na Ammi zake huwapa dinari khamsini au zaidi, na akiombwa na mashangazi zake huwapa dinari ishirini na tano au zaidi.

Na elimu yake kubwa imedhihiri waziwazi kwa watu. Mara wanachuoni themanini walikusanyika kwake, baada ya kurudi kwenye hija yao. Walimwuliza maswali mbalimbali akiwajibu Imam(a.s) kwa kumtosheleza kila mtu.

Wakati mmoja watu wengi walikusanyika kwake na kumwuliza maswali thelathini elfu mahala pamoja, akawajibu wote pasi kuzuia wala kukosa. Alikuwa umri wake wakati huo miaka tisa tu, lakini mfano namna hii si kitu cha kustaajabisha kwa Ahlul-bayt.

Na khalifa Mamun Rashid alimwozesha binti wake, baada ya mtihani muhimu, na kisa chake ni mashuhuri.

MASOMO YA KI-ISLAM

KITABU CHAPILI

11. SOMO LA KUMI NA MOJA

IMAMU WA KUMI

Naye ni Imam Ali bin Muhammad, An-Naqii(a.s) . Mama yake ni bibi Samana. Kazaliwa Imam(a.s) Madina Munawwara, mwezi tano, mfungo kumi, mwaka mia mbili na kumi na nane. Kafariki, hali ya kupewa sumu, mji wa Samarra, siku ya Jumatatu, mwezi tatu, mfungo kumi, mwaka mia mbili na khamsini na nne. Kazikwa huko mahala palipo kaburi lake sasa.

Al kuwa Imam(a.s) mbora kuliko watu wote wa zama zake. Alikuwa mwanachuoni mno. Naye ndio makusanyiko ya utukufu na ukarimu, na mlainifu wa mazungumzo. Na alikuwa mchamungu, na mzuri wa mwenendo na tabia na alikuwa mkarimu mno.

Siku moja mfalme alimpelekea thelathini elfu dirham, na Imam akampa mwarabu wa kufa kwa msaada, na akamwambia, "Kalipe deni zako na kwa watoto wako na ahali zako na utusamehe (hatuna zaidi)." Akasema yule Mwarabu, "Ee! Mtoto wa Mtume, nilikuwa ninatumai kupata chini ya kumi elfu, lakini Mungu anajua alipoweka ujumbe wake." Baadaye akachukua mali ile na akaenda zake.

12. SOMO LA KUMI NA MBILI

IMAM WA KUMINA MOJA

Naye ni Imam Hassan bin Ali, Al -Askari(a.s) . Mama yake ni bibi Haditha.

Kazaliwa Imam(a.s) siku ya Jumatatu. mwezi kumi, mfungo saba, mwaka wa miambili na thelathini na mbili.

Amekufa hali ya kupewa sumu, siku ya Ijumaa, mwezi nane, mfungo sita, mwaka 260. Akasimamia mazishi yake mtoto wake Imam Al-Hujjat(a.s) . Kazikwa alipozikwa baba yake katika mji wa Samarra.

'Uso wake na mwili wake ulikuwa mzuri sana. Alikuwa anaheshimiwa sana ijapokuwa umri wake ulikuwa mdogo. Alikuwa anafanana na Mtume(s.a.w.w) katika tabia.

Yaliyosikiwa kwa Ismaili, kasema:- "'Nilikaa njiani kwa kumngojea Imam(a.s) . Alipopita nikamshtakia hali yangu. Akasema Imam(a.s) : Unaapa uongo kwa Mungu, nawe umeficha katika ardhi dinari mia. Sisemi hivyo kwa kuwa nisikupe chochote la, nitakupa." Baadaye Imam(a.s) akamwamuru kijana wake kumpa alicho nacho. Akampa dinari mia.

Mtu mmoja akenda kwa Imam(a.s) aliposikia ukarimu wake. Yeye alikuwa anahitaji dirhamu miatano. Imam(a.s) akampa mia tano dirhamu, na akamzidishia mia tatu dirhamu.

Wanaswara wakashuhudia kuwa Imam(a.s) ni mfano wa Masihi katika fadhila na elimu na miujiza yake.

Alikuwa Imam(a.s) mwingi wa ibada, na mwingi wa sala za usiku-(Tahajjud).

13. SOMO LA KUMI NA TATU

IMAMU WA KUMI NA MBILI

Naye Imam Al-Mahdi Muhammad bin Hassan(a.s) . Na mama yake ni Bibi Narjis.

Kazaliwa Imam(a.s) Samarra, usiku wa nusu ya Shaaban, mwaka mia mbili na khamsini na tano.

Imam huyo(a.s) ndiye wa mwisho na ni hoja ya Mungu ardhini. Na ni mwisho wa makhalifa wa Mtume Mtukufu. Na mwisho wa Maimamu wa Waislamu wa kumi na mbili.

Naye ni hai duniani sasa. Na karefusha Mungu Mtukufu umri wake Mtukufu(a.s) . Naye ni Ghaib (haonekani). Na Atadhihiri Karibu Ya Kiyama wakati itapojaa dunia dhulma na madhambi. Na yeye atajaza dunia uadilifu na haki na usawa.

Kama alivyohubiri Mtume(s.a.w.w ) na ma Imamu(a.s) , kuwa yeye atabaki, hafi.

Atamiliki dunia nzima na kuimarisha na uadilifu, na atawauwa wadhalimu. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu, "Mwenyezi Mungu aishindishe juu ya dini zote ijapokuwa washirikina wachukie."

Ee! Mola, fanya upesi faraja yake na wepesi kutoka kwake, utujaalie miongoni mwa wanusuru wake na wasaidizi wake.

Na kwa sababu kujificha kwake Imam(a.s) kulikuwa nyumbani kwake, wanakwenda Wa-Islamu mahari hapo katika Samarra kwa kumwabudu Mungu hapo. Na nyumba ile inaitwa "Sardab-ul-ghaibat."

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU

YALIYOMO

MASOMO YA KI-ISLAMU 1

KITABU CHA PILI 1

DIBAJI 1

MASOMO YA KI-ISLAM 2

KITABU CHAPILI 2

1. Somo la Kwanza 2

IMAM WA KWANZA 2

MASOMO YA KI-ISLAM 4

KITABU CHAPILI 4

2. SOMO LA PILI 4

BINTI WA NABII (s.a.w.w) 4

MASOMO YA KI-ISLAM 6

KITABU CHAPILI 6

3. SOMO LA TATU 6

IMAM WA PILI 6

MASOMO YA KI-ISLAM 8

KITABU CHAPILI 8

4. SOMO LA NNE 8

IMAMU WA TATU 8

MASOMO YA KI-ISLAM 10

KITABU CHAPILI 10

5. SOMO LA TANO 10

IMAMU WA NNE 10

MASOMO YA KI-ISLAM 12

KITABU CHAPILI 12

6. SOMO LA SITA 12

IMAMU WA TANO 12

MASOMO YA KI-ISLAM 14

KITABU CHAPILI 14

7. SOMO LA SABA 14

IMAMU WA SITA 14

MASOMO YA KI-ISLAM 16

KITABU CHAPILI 16

8. SOMO LA NANE 16

IMAMU WA SABA 16

9. SOMO LA TISA 16

IMAMU WA NANE 16

10. SOMO LA KUMI 17

IMAM WA TISA 17

MASOMO YA KI-ISLAM 18

KITABU CHAPILI 18

11. SOMO LA KUMI NA MOJA 18

IMAMU WA KUMI 18

12. SOMO LA KUMI NA MBILI 18

IMAM WA KUMINA MOJA 18

13. SOMO LA KUMI NA TATU 19

IMAMU WA KUMI NA MBILI 19

SHARTI YA KUCHAPA 19

MWISHO WA KITABU 19

YALIYOMO 20


[1] . Akhera: Ufufuo

[2] . Kiyama: Siku ya kufufuliwa

[3] . kaaba: Nyumba ya Mungu,iliyojengwa na Nabii Ibrahimu (a.s), katika mji wa Maka kwa ajili ya ibada ya Mwenyezi Mungu.

[4] . Mihirabu: Sehemu ya msikiti inayoonyesha kuelekea kibla.

[5] . Hijiria: Chimbuko la tarehe kwa mwaka wa Kiislamu. Inahisabiwa kutoka kuhama kwake Mtume (s.aw.w) Maka.

[6] . Ashura: Mwezi kumi mfungo nne, tarehe kumi ya mwezi wa Muharram.

[7] . Rakaa: Sehemu ya sala. Kila sala inayo Rakaa mbili, tatu au nne.

[8] . Tahajjud: Sala zinazosaliwa baada ya nusu ya usiku. Sala hizi si za faradhi.