1
MAISHA YA BIBI KHADIJA
SURA YA TATU
MUHAMMED MUSTAFA (S.A.W.W) ALIYETEGEMEWA KUWA MTUME WA UISLAMU
Ingawaje nchi ya Arabu haikuwa na serikali yoyote- ya kitaifa, kijimbo au kienyeji - jiji la Makka lilikuwa linatawaliwa na kabila la Qurayishi, kama ilivyotajwa kabla. Kabila la Qurayish lilikuwa na koo kumi na mbili. Koo hizi zilishirikiana majukumu ya kudumisha kiasi kidogo cha sheria na utulivu katika mji wa Makka. Moja ya koo za kabila la Qurayshi ilikuwa Bani Hashim. Kila ukoo ulikuwa na kiongozi wake. Kiongozi wa Bani Hashim alikuwa Abu Talib bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abd Manaf bin Qusayy. Kama walivyokuwa babu zake, Abu Talib pia alikuwa mfanyabiashara. Zaidi ya kuwa mkuu wa ukoo, alikuwa pia mlezi wa Al-Kaaba - Nyumba ya Mwenyezi Mungu - iliyojengwa Makka, karne nyingi zilizopita, na Mtume Ibrahim na Ismaili na wakaitoa wakfu imtumikie Mwenyezi Mungu.
Abu Talib alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Abdullah. Mwaka wa 570 A.D., Abdullah alikwenda Syria na msafara wa biashara. Miezi michache kabla hajasafiri kwenda Syria alimuoa Amina binti Wahab, mwanamke kutoka Yathrib (Madina). Wakati Abdullah alipokuwa anarudi kutoka Syria, aliugua na kufa. Alikuwa na umri wa miaka 17 tu alipokufa. Alipoondoka Makka, mke wake alikuwa mja mzito na alikuwa anaishi nyumbani kwa shemeji yake, Abu Talib. Miezi miwili baada ya kifo cha Abdullah, alijifungua mtoto wa kiume. Babu wa mtoto huyu, Abdul Muttalib, alimpa jina la Muhammad. Muhammad alizaliwa tarehe 8, Juni, 570, nyumbani kwa baba yake mdogo, Abu Talib mjini Makka.
Siku za usoni, mtoto mchanga Muhammed alikuwa ateuliwe na Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa Mjumbe Wake wa dunia yote, na alikuwa abadilishe majaliwa na historia ya binadamu daima milele. Muhammad alikuwa na umri wa miaka sita wakati mama yake, Amina binti ya Wahab, alipokufa baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kutokana na kifo chake hicho, babu yake Muhammad, Abdul Muttalib, alimchukua ili amlee nyumbani kwake. Lakini ilikuwa baada ya miaka miwili tu Abdul Muttalib naye alifariki. Abdul Muttalib alikuwa na watoto wa kiume kumi. Alipokaribia kufa, aliwaita watoto wake wote, na alimteuwa mwanae Abu Talib kama mkuu mpya wa ukoo wa Bani Hashim. Pia alimfanya mlezi wa Muhammad. Wote wawili Abu Talib na Abdullah, baba wa Muhammad, walikuwa watoto wa mama mmoja, ambapo watoto wengine wa Abdul Muttalib walizaliwa na wakeze wengine.
Abu Talib alimpeleka Muhammad nyumbani kwake. Muhammad ali-washinda wote (kwa tabia). Abu Talib na mkewe walimpa Muhammad mapenzi makubwa sana. Walimpenda zaidi kuliko walivyowapenda watoto wao. Muhammad alizaliwa ndani ya nyumba yao. Kuzaliwa kwa Muhammad ndani ya nyumba hiyo ilisababisha nyumba hiyo iwe na neema nyingi; na sasa baada ya kifo cha Abdul Muttalib, alirudi tena ndani ya nyumba hiyo. Muhammad alipokuwa mtoto, hakuonyesha kuvutiwa na mwanasesere na michezo ya watoto. Katika ujana wake, hakuonyesha kupenda michezo na burudani, au kuwa katika makundi ya vijana wa rika lake. Pamoja na kwamba alikuwa kijana, alipendelea zaidi upweke kuliko kuchanganyika kwenye makundi ya vijana wenzake. Kama walivyokuwa watu wengine wa kabila la Qurayish, Abu Talib pia alikuwa akipeleka bidhaa zake Syria na Yemen kila mwaka. Wakati mwingine alikwenda yeye mwenyewe na misafara, na kipindi kingine aliajiri Wakala ambaye aliuza bidhaa zake kwenye masoko ya nchi hizo. Mnamo mwaka wa 582 A.D. Abu Talib aliamua kutembelea Syria akiwa na msafara. Mpwa wake, Muhammad, alikuwa na umri wa miaka 12 wakati huo. Abu Talib alimpenda sana hivyo kwamba alikuwa hawezi kuachana naye hata kwa muda wa miezi michache. Kwa hiyo, alimchukua na kwenda naye Syria.
Akili ya Muhammad ilikomaa upesi, na pamoja na kwamba umri wake ulikuwa bado mdogo sana, alikuwa mchunguzi na mdadisi aliyebariki-wa. Wakati wa safari yake nje na ndani ya Syria, kwa uangalifu sana ali-wachunguza watu na mila zao, desturi zao, namna wanavyo abudu, mavazi yao, hotuba na upembuzi wao wa mambo. Na kila alichokiona, alikumbuka. Aliporudi Makka, aliyakumbuka yote yale aliyoyaona toka mwanzo hadi mwisho na aliweza kukumbuka uchunguzi wake wote bila kubakisha kitu. Hakusahau kitu; kwa hakika, alikumbuka kila kitu. Ingawaje alikuwa mdogo kwa umri, alikomaa kihekima na matumizi ya akili ya kawaida. Abu Talib alitambua kwamba Muhammad alikuwa na hekima na akili iliyopevuka kuliko umri na uzoefu wake. kwa hiyo, hakumchukulia kama mtoto mdogo kwani ilibidi aonyeshe heshima kwake kama ile anayostahili kupewa mtu mzima wa jamii ya Kiarabu.
Haikupita muda mrefu Muhammad alipata umri unaozidi miaka kumi. Ingawa katika rika la kijana aliye balehe, alikuwa bado hakuvutiwa na starehe ambazo vijana wengine huzitafuta. Alijiepusha na purukushani za aina zote na kama ilivyoelezwa huko nyuma, alipendelea kuwa peke yake na tafakuri yake. Alikuwa na fursa ya kutosheleza upendeleo huu alipokwenda kuchunga kondoo wa ami yake. Alikuwa peke yake chini ya anga. Jangwa lililo kimya na kujitandaza hadi upeo wa macho, na ambalo lilimpa matumaini ya kutafakari kuhusu maajabu ya Uumbaji, siri za mbingu na ardhi, na maana na madhumuni ya maisha. Alitazama mandhari ya ardhi kutoka upeo wa macho huu hadi mwingine, na ilionekana kama vile ukubwa wa ulimwengu ulikuwa ndio swahiba pekee "aliyekuwepo" pamoja naye. Upweke kwake ulionekana kuwa "kipimo" kipya cha ulimwengu wake.
Wakati Muhammad alipokuwa amevuka ujana wake, watu wa Makka walikwishaanza kumtambua. Walijua kwamba kamwe hakupotoka kuto-ka kwenye maadili mema na utu mwema na hakufanya kosa kamwe. Aidha walitambua kwamba hakupenda kusema sana na alipofanya hivyo, aliongea kweli tupu, na alitamka maneno ya hekima tu. Kwa kuwa watu wa Makka walikuwa hawajamsikia akisema uongo, walimwita "As-Sadiq" (Mkweli). Katika kipindi cha miaka michache iliyofuata, raia wa Makka walimpa Muhammad cheo kingine. Kwa kutambua kwamba alikuwa makini sana, wengi wao walianza kumpa mali zao ili awatunzie kama vile: fedha taslimu, vito, mapambo, na vitu vingine vya thamani. Wakati mtu yoyote alipotaka mali yake, Muhammad alimrudishia yote. Kamwe hapakutokea kasoro yoyote katika kurudisha mali za watu. Baada ya kuthibitisha kuwa alikuwa na tabia ya namna hiyo, kwa kipindi cha miaka kadhaa watu walianza kumwita Muhammad "Al-Amin". (Mwaminifu) Ni yeye, na yeye peke yake aliyeitwa As-Sadiq na Al-Amin na watu wa Makka. A. Yusuf Ali mtarjumi na mfasiri wa Qur'anTukufu, amelielezea neno "A-Amin" kama ifuatavyo: "Al-Amin Mtu ambaye amana imewekwa kwake, pamoja na maana mbali mbali kidogo zimedokezwa:
1.
Aanyestahiki kuaminiwa;
2.
Anayewajibika kuitoa amana yake, kama Mtume yeye huwajibika kutoa Ujumbe wake;
3.
Anawajibika kabisa kutenda kama ambavyo amana inaelekeza, kama mtume anawajibika kufikisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu tu, na asiongeze chochote cha kwake, na
4.
hatafuti masilahi yake mwenyewe."
Waarabu walioishi kabla ya Uislamu kila mwaka walifanya "Msimu wa maonyesho" sehemu mbalimbali za nchi. Baadhi ya maonyesho haya yalionyeshwa Makka na sehemu nyengine za karibu yake. Maonyesho yaliyojulikana sana ni: Ukkaz, Majanna na Dhul-Majaz. Muhammad aliyatembelea maonyesho hayo pale muda ulipomruhusu kufanya hivyo. Maonyesho yote haya yalionyeshwa wakati wa miezi minne mitakatifu ya Rajab, Dhil-Qaada, Dhil-Hajj na Muharram, kufuatana na mila za Waarabu wa kale. Ndani ya miezi hii minne, mambo yafuatayo yalip-igwa marufuku: vurugu, vita, kuteka nyara na unyang'anyi. Mnamo mwanzo wa "Msimu wa amani" tangazo la kusimamisha vita lilitolewa. Tangazo la kusitisha vita lilitambuliwa na kuheshimiwa na makabila yote ya Waarabu. Wafanya biashara, wakulima na wastadi (wachonga sanamu) waliku-sanyika kwenye maonyesho haya kutoka sehemu za mbali na za karibu (kwa ajili ya) kuuza, kununua na kubadilishana. Walileta pamoja nao mazao yao yaliyo bora kabisa, na kwa fahari waliyafanyia maonyesho. Sanaa nyingine za amani, mashairi yakiwa miongoni mwao, yalikuzwa (na kutukuzwa katika wakati zilipositishwa vurugu (na vita)
Mashairi yalikuwa penzi la kwanza la Waarabu. Kama kipaji cha mashairi kiligunduliwa kwenye kabila lolote, lilikuwa jambo la kush-erehekewa na kila mmoja. Makabila mengine yenye uhusiano mzuri na kabila husika, yalilipongeza kabila hilo kwa kuzalisha kipaji cha namna hiyo. Waarabu walikuwa washabiki wakubwa wa maneno ya Kiarabu na maana yake nyingi. Wao walijiita "watoto wa Kiarabu." Kwenye maonyesho haya washairi walisoma tunzi zao mpya, sifa ambayo Waarabu waliithamini kuwa ya muhimu na maana sana. Mojawapo ya misemo yao ni kwamba uzuri wa mwanamke upo kwenye uso wake; lakini uzuri wa mwanamume upo katika uhodari wake wa kujieleza. Walipenda ustadi wa utunzi na ufasaha wa yale yanayosemwa kwenye mashairi.
Mafumbo yasiyo ya kawaida ya jangwani na watabiri wanaofanana na wanyama pori na waaguzi wa makabila, huwafurahisha asikilizaji kwa hotuba zao za mafumbo hadithi zao za mafumbo na siri za ubashiri, hata hivyo, wachache waliweza kuelewa ishara hizo. Waarabu wengi waliamini kwamba utabiri wa nyota uliamua mwisho mzuri au mbaya wa maisha ya mtu. Kwa hiyo, watu wa nchi nzima waliwaogopa watabiri, iliaminika kwamba walikuwa na uwezo wa kuzungumza na nyota. Waimbaji, wacheza dansi, wachekeshaji, wana sarakasi na wana mazingaombwe wote walishindana ili wapate kusifiwa na watazamaji.
Maonyesho haya yalihudhuriwa na watawa, makuhani na watu watakat-ifu ambao walihubiri imani ya ibada zao. Wote walikuwa huru kueneza itikadi zao na fikira zao bila woga wa kuonewa na mtu yeyote katika kipindi chote cha miezi minne. Amani na sanaa za amani vilishamiri dhidi ya mfululizo wa mambo ya uchangamfu wa binadamu usio na mipaka. Kwenye maonyesho haya, Muhammad alipata fursa ya kuchunguza wakazi wa rasi ya Bara Arabu. Pia alijifunza, kwa mara ya kwanza, mila na imani za watu wa jamii tofauti, na utamaduni na usuli za kijogorafia.
Mnamo majira ya kuchipua ya mwaka wa 595 A.D., wafanyabiashara wa Makka walikusanya msafara wao wa majira ya kiangazi ili wapeleke bidhaa zao Syria. Pia Khadija alitayarisha bidhaa zake lakini alikuwa hajapata mtu mwanamume atakayesimamia msafara wake na kuwa wakala wake. Majina machache yalipelekwa kwake lakini hakupata lililompendeza. Kupitia kwa baadhi ya weza wake wa chama katika wachuuzi wa Makka, Abu Twalib alipata habari kwamba Khadija alikuwa anatafuta wakala ambaye atachukua mizigo yake pamoja na msafara kwenda Syria na kuiuza kule. Ilipita akilini mwa Abu Twalibu kwamba mpwa wake Muhammad ambaye sasa alikuwa na miaka ishirini na tano angelifaa kwa kazi hiyo Alikuwa na hamu kubwa ya kumtafutia kazi mpwa wake. Alijua kwam-ba yeye (Muhammad) hana uzoefu wa kazi ya uwakala lakini pia alijua kwamba yeye (Muhammad) angeweza kazi hiyo kwa sababu ya kipaji chake. Alikuwa na imani na uwezo na akili za mpwa wake na alikuwa na uelewa wa kutosha kufanya kazi yake ya uwakala kwa tajiri yake. Kwa hiyo, pamoja na makubaliano yake ya kimya (na Muhammad), alikwenda kwa Khadija, na alianzisha mazungumzo kuhusu suala la uteuzi wake (Muhammad), kama wakala wake mpya.
Kama ilivyo kwa raia wengine wengi wa Makka, Khadija pia alikwisha sikia kuhusu Muhammad. Khadija alijua kwamba hangehoji kuhusu heshima ya Muhammad. Aliona kwamba angeweza kumwamini Muhammad kwa wazi na kwa siri. Kwa hiyo alikubali kumteua Muhammad kuwa wakala wake. Hakufikiria kutokuwa na uzoefu ingekuwa tatizo kwa Muhammad, na akasema kwamba, kwa jinsi yoyote ile, angempeleka mtumwa wake Maysara, ambaye alikuwa na uzoefu wa kusafiri, awe pamoja naye (Muhammad) amsaidie katika kazi zake.
Khadija alikuwa mwendeshaji mzuri sana na mpangaji aliyekamilika. Lakini pia alikuwa na bahati njema. Kila mara alikuwa na bahati ya kupata mawakala wazuri kwa biashara yake. Hata kama alikuwa na hali ya kufuzu, alistaajabu baada ya kipindi kifupi kugundua kwamba akiwa na Muhammad kama wakala wake, bahati yake iliongezeka kwa kiwango ambacho ilikuwa haijapata kutokea. Kwa Khadija, kamwe palikuwa hapajatokea siku za nyuma, na kamwe haingetokea kwa siku za baadaye kuwa na wakala kama Muhammad. Kama Khadija alikuwa na kile kitu kinachoitwa "mguso wa dhahabu" (golden touch) mkononi mwake, Muhammad alikuwa na "mguso wa baraka" mkononi mwake.
Khadija na Abu Talib walitayarisha vipengele vyote vya mpango mpya. Na Muhammad alipokwenda kumuona tajiri wake mpya kwa madhu-muni ya kukamilisha mkataba, alimwambia mambo yote kuhusu biashara hiyo. Muhammad alielewa haraka sana katika yote Khadija aliyomwambia na hakuuliza swali lolote lile lililohitaji ufafanuzi. Khadija alimwambia Abu Talib kwamba ujira ambao atampa Muhammad kwa kazi yake utakuwa mara mbili zaidi ya ule aliokuwa anawapa mawakala wengine huko nyuma. Jambo ambalo Khadija hakulijua wakati huu ni kwamba ulikuwa ni ule mkono wa majaliwa ndiyo uliokuwa unafanya kazi katika kuusukuma mpango huu. majaliwa yalikuwa na mipango mingine kwake yeye na Muhammad. Mipango hiyo ilivuka mipaka ya ulimwengu huu na masu-ala ya thamani ndogo ya pesa, kama kupata faida kwenye biashara, kama ambavyo hivi punde matukio yatakavyoonyesha.
Kwa wakati huo, "msafara wa kiangazi" wa wafanya biashara wa Makka ulikwisha kamilika, na ulikuwa tayari kuondoka kuelekea kwenye safari yake ndefu. Wafanyabiashara walileta mizigo yao kuto-ka kwenye maghala ili ipakiwe kwenye ngamia. Mikataba ilitayarishwa na kusainiwa. Mahitaji ya njiani yalichukuliwa, na viongozi na wasindikizaji waliajiriwa. Kwa muda uliopangwa, Muhammad na Abu Talib na ami zake wengine walifika. Walisalimiwa na ami yake Khadija ambaye alikuwa anawangojea akiwa na Cheti cha orodha ya Shehena na hati nyingine.. Muhammad aliamua kuhesabu mali ya kuuza huko Syria. Akisaidiana na Maysara, alikagua mali yote na aliona kila kitu kiko sawa sawa. Maysra alifanya kazi ya makaratasi yahusuyo mauzo na manunuzi. Alikuwa mtunza taarifa ya mali.
Abu Talib alitoa maelekezo maalumu kwa Maysara na kwa kiongozi wa msafara kuhusu usafiri wa raha na salama kwa Muhammed. Waliahidi kuhakikisha kwamba Muhammed angesafiri kwa raha na salama. Abu Talib na ndugu zake waliwashukukuru kwa kuonyesha ushirikiano kuhusu safari ya Muhammad. Walimwombea dua apate mafanikio kati- ka kazi yake mpya na kurudi salama. Halafu wakamkabidhi Mwenyezi Mungu amlinde arudi salama, na wakaagana. Wakati wa kiangazi misafara mingi ilisafiri usiku kukwepa joto kali la mchana, na kupumzika mchana. Safari ya mchana ingechosha sana wafanya biashara, ngamia na farasi. Kwa hiyo, misafara mingi iliondo-ka Makka saa za alasiri, kama walivyosema Waarabu, au jua linapokuwa limepita katikati, na joto huwa limepungua.
Msindikizaji mmoja aligonga kengele. Wasafiri wote walijitayarisha na msafara ulikuwa tayari kuondoka. Ngamia waliokuwa wamepumzika walisimama, bila kupenda, walionyesha kutokutaka kuondoka kwa kukataa na kukoroma lakini waliingia kwenye msafara. Takribani saa tatu kabla ya jua kuchwa kiongozi wa msafara alitoa ishara, na msafara ukawekwa tayari kwa kuondoka. Msafara ulielekea Kaskazini. Ndugu na marafiki wa wasafiri walikaw-ia kwa muda fulani huku wakiwa wanapunga mikono na kutazama msafara unavyosonga mbele. Ngamia wa mwisho alipokingizwa na vilima, wasindikizaji nao walisambaa.
Wasafiri wapya walikaa pamoja na wasafiri wazoefu ambao walikuwa wanawaonyesha sehemu za kuvutia walizokuwa wanazijua na walielezea upekee wa sehemu hizo. Maysara alimwonyesha Muhammad sehemu nyingi za kupendeza. Muhammad pia alizitambua sehemu nyingi alizoziona barabarani alipopita humo miaka kumi na tatu iliyopita akiwa na ami yake. Hakuna kilicho badilika wakati wa miaka hiyo 13. Maysara alithibitisha kuwa msafiri mwenza mchangamfu ambaye aliweza kusimulia hadithi nyingi na aliweza kukumbuka matukio mengi sana aliyoyaona wakati wa safari zake za siku za nyuma. Muhammad aligundua kwamba wasafiri wengine pia walikuwa wachangamfu na wenye kufanya urafiki.
Baada ya takribani mwezi mmoja, msafara ulifikia mwisho wa safari yake ulipofika Syria. Mipango ya nyumba ya kupanga ilikwisha tayarishwa kwa ajili ya wasafiri waliochoka kwa msafara, na wote wal-itaka kupumzika baada ya safari ndefu iliyowapitisha kwenye mandhari zilizosababisha safari kuwa ngumu na joto kali. Waliweza kupumzika kiasi cha wiki moja ili kuponyesha sehemu muhimu za mwili zilizo athirika. Wafanyabiashara walipokwisha pumzisha viungo vyao vilivyokuwa vinauma na kupata nguvu upya tena, walikwenda sokoni kuuza mali zao walizoleta kutoka Makka. Kiasi fulani cha mali waliuza kwa fedha taslimu, na iliyobaki walibadilisha mali kwa mali kwa bidhaa za Syria. Iliwabidi pia wanunue bidhaa kwa ajili ya soko la nyumbani, na wal-itafuta na kupata mali nyingi yenye faida. Shughuli za msafara ziliweza kudumu kuanzia miezi miwili hadi minne.
Muhammad pia aliuza na kununua mzigo mpya. Ingawa kwake yeye ilikuwa msafara wa kwanza wa kibiashara, hakusita kwa sababu ya kutokuwa na uzoefu, katika shughuli za biashara. Hakika alimshangaza Maysara kwa werevu wake katika biashara. Aidha Maysara aligundua kwamba Muhammad alikuwa mwepesi kuelewa na kuamua katika mazungumzo ya biashara na upevu wake wa akili na uaminifu wake kama muuzaji. Muhammad alilinda maslahi ya tajiri yake na wateja wake, na bado alipata faida kubwa zaidi katika shughuli hiyo ya Khadija kuzidi mara zote alizokuwa amefanya biashara tangu bibi huyo kurithi biashara ya baba yake. Na bidhaa alizonunua Syria kwa ajili ya biashara ya Khadija zilikuwa safi sana kwa ubora wake na hakika zingepata bei nzuri Makka, na ilitokea hivyo. Huko Syria yeyote aliyemuona Muhammad, alivutiwa naye. Alikuwa na umbo la kuvutia ambalo liliwafanya watu wasimsahau hata kwa kumuona mara moja tu.
Ingawa Muhammad alijishugulisha na kuuza mali, mapatano ya biashara, kuchunguza soko, na kununua, Maysara aling'amua kwamba hata hivyo alipata muda wa kukaa peke yake. Kwa maoni ya Maysara, hivi vipindi vya ukimya wa Muhammed, vilikuwa chanzo cha jambo lililojificha, lakini hakuviingilia kati. Maysara hakuwa anajua kwamba bosi wake mwenye umri mdogo alikuwa na desturi ya kutafakari kuhusu hali na majaliwa ya mwanadamu. Wakati akiwa Syria Muhammad alikutana na Wakristo na Wayahudi wengi. Alidhani kwamba kila kundi kati ya hayo mawili yangekuwa na "imani ya Mungu Mmoja." Lakini alistaajabu alipofahamu kwamba haikuwa hivyo. Makundi yote mawili yaligawanyika katika makundi mengine madogo mengi, na aina ya ibada ya kila kundi ilikuwa tofauti na ile ya makundi mengine. Miongoni mwao kundi lipi lilikuwa sahihi na lipi halikuwa sahihi? Hili lilikuwa swali ambalo lilimsumbua Muhammad. Utafiti wa udadisi wa jibu la swali hili, na maswali mengine madogo madogo yenye kufanana na hili yalimfanya Muhammad asilale usingizi wakati kila mmoja amekwenda kulala.
Hatimaye, shughuli za biashara zilipokwisha, na zawadi za ndugu na marafiki kununuliwa, msafara ulirudi Makka. Kwa wasafiri wakum-bukao sana nyumbani, kurudi nyumbani mara zote ni tukio la kufu-rahisha. Ni tukio lililojaa matumaini kwani mtu atakutana na awapendao ambao mtu hakuwa nao kwa miezi mingi. Wasafiri wachovu hawawezi kungoja kwa muda mrefu kusikia vicheko vya furaha vya watoto wao na wanatambua kwamba wakati mzuri kama huo ukiwadia hawawezi kuzuia na kuficha machozi. Wanajua kutokana na uzoefu wa muda mrefu kwamba pangekuwapo na kulia machozi - machozi ya furaha. Kicheko na Machozi vyenye mchanganyiko ulio huru kabisa katika vipindi vya heri na furaha isiyo na upeo.
Kuwasili kwa msafara mara kwa mara kulisisimua mji. Kwa hakika ulikuwa wakati wa kusherehekea kwa kila mkazi wa Makka na vitongoji vilivyomo pembezoni mwake. Sehemu zilizotengwa maalum kwa ngamia kushushia abiria na mizigo, zilikuwa changamfu mno. Raia walio wengi na hata yale makabila yanayohamahama waliona pilika pilika za kuwasili kwa msafara kwamba yalikuwa mabadiliko ya kutia moyo katika mwenendo wa maisha. R.V.C. Bodley, ameandika katika kitabu chake: "Kuwasili na kuondoka kwa misafara yalikuwa matukio muhimu kwa maisha ya watu wa Makka. Karibu kila mkazi wa Makka alikuwa na aina fulani ya uwekezaji kwenye mali iliyobebwa na maelfu ya ngamia, mamia ya watu, farasi na punda:- bidhaa hizo zilikuwa ngozi, zabibu kavu, vinoo vya fedha, na walirudi na mafuta, manukato na bidhaa zili-zozalishwa viwandani kutoka Syria, Misri na Uajemi, na viungo na dhahabu kutoka Kusini. (The Messenger- the life of Muhammed,1946)
Watu walikuja kuwasalimia wapenzi wao ambao walikuwa wanarudi nyumbani baada ya kutokuwepo kwa kipindi cha miezi sita. Wengi wao walikuja wakiwa na fikira mchanganyiko wa matumaini na woga. Ilipotokea mtu anaondoka mjini kwenda na msafara, hapakuwepo na njia yoyote kwa ndugu zake kujua kama wangemuona akiwa mzima tena. Wasafiri wengine walikufa wakiwa safarini na walizikwa kwenye sehemu ambazo ni njia za ndani ndani sana, na hazipitiki. Ndugu zao kamwe hawakuweza kuyatembelea makaburi yao. Na ilikuwa hapo tu ambapo msafara ulifika ndipo wakazi wa Makka waliweza kusikia habari za dunia nje ya bara Arabu. Waarabu wa siku hizo waliishi katika hali ya upweke sana katika dunia yote. Katika dunia hiyo Waarabu walikuwa na njia moja tu ya kupata habari nayo ni msafara.
Takriban kila raia wa Makka aliwekeza fedha kwenye msafara wa biashara. Watu matajiri miongoni mwao waliweza kutembelea nchi za nje kwa muda mrefu zaidi wa miezi mingi. Lakini watu ambao hawakuwa na uwezo wa kifedha walibaki nyumbani. Hivyo, waliwapa bidhaa zao watu walio waaminifu kuwa mawakala wao wauze kwa niaba yao, na waliwapa wao fedha ya kwenda kununua bidhaa ambazo zilikuwa zinatakiwa Arabuni na ziliweza tu kupatikana kwenye masoko ya Syria, Yemen, Habeshi na Misri. Baada ya mawakala wao kuleta mali za nje Makka, waliuza bidhaa hizo na kupata faida. Ulikuwa ni utaratibu ambao baada ya uzoefu wa muda wa miaka mingi, mpango huu ulionekena unafaa na unatekelezeka.
Wafanyabiashara na mawakala waliokuwa kwenye msafara pia walileta zawadi kutoka nchi za nje na tuzo kwa ndugu na marafiki zao, kufuatana na mila za zamani. Kila mtu alitaka kuona zawadi hizo ambazo ziliwakumbusha utajiri uliopo Syria na anasa za Falme za Ajemi na Roma. Muhammad alipofika Makka, kitu cha kwanza kufanya ni kuzunguka Al-Kaaba mara saba kama ilivyokuwa desturi, na halafu alikwenda kumuona muajiri wake. Alimwelezea tajiri wake kwa kina kuhusu safari na shughuli za biashara alizozifanya kwa niaba yake. Baadae, alimwelezea ami yake Abu Talib, kuhusu matukio ya kuvutia kwenye uzoefu wake kama mfanyabiashara.
Maysara, mtumwa wa Khadija, naye alikuwa na taarifa yake mwenyewe ya kumpa mmilki wake. Alimwambia Khadija kuhusu safari ya kwenda na kurudi kutoka Syria, na faida ambayo Muhammad aliingiza kwenye biashara yake. Lakini kwake yeye (Maysara), kilichompendeza zaidi kuliko kufuzu katika biashara, ni tabia na utu wa Muhammad. Maysara alimwambia Khadija kwamba alipendezwa na kipaji cha Muhammad katika biashara. Aliendelea kumtaarifu Khadija kwamba uwezo wa Muhammad kuona mbali kibiashara ilikuwa kinga; uamuzi wake ulikuwa wa uhakika na uelewa wake haukuyumba. Maysara pia alimwambia Khadija kuhusu bashasha, uungwana na kukubali madaraka yaliyo chini ya uwezo wake, Muhammad.
Khadija alivutiwa na taarifa hiyo, na alimuuliza Maysara maswali kuhusu msimamizi wake mpya, Muhammad. Pengine Khadija hange-shangaa hata kidogo kama Maysara angemwambia kwamba Muhammad alikuwa mtu asiye wa kawaida kulinganisha na watu ambao amewaona katika maisha yake, na alikuwa mtu anayeweza kufanya mambo yasiyo ya kawaida. Siku iliyofuata, Waraqa bin Naufal alikwenda kumuona Khadija. Yeye pia alitaka kusikia habari zilizoletwa na wasafiri kutoka ng'ambo. Habari zilizomvutia yeye sana ni zile za ugomvi wa siku nyingi baina ya Falme za Ajemi na Roma. Kila moja ya hizo Falme ilitaka kuwa na mamlaka kwenye kanda yote iliyojulikana kama "Bara lenye Neema." Pengine pia kama walivyokuwa raia wengine Waraqa aliwekeza fedha kwenye biashara ya Makka ya kusafirisha nje na kuingiza ndani ya nchi bidhaa na alitaka kujua jinsi ambavyo msafara ulifanikiwa kibiashara.
Khadija alimwambia binamu yake habari zote kama alivyozipata kutoka kwa Muhammad mwenyewe na Maysara. Aidha alisema kwamba msimamizi wake mpya alipata faida kubwa ambayo hakuitegemea. Waraqa pia alizungumza na Maysara kuhusu safari na kuhusu Muhammad. Maysara, hata hivyo, alitaka kuzungumzia tu kuhusu Muhammad. Hakuna kitu kingine chochote kilichomvutia, hata hizo shughuli za biashara za kuuza na kuuziwa hakuzitia maanani kabisa.. Waraqa aliposikia taarifa hiyo ndefu inasemekana alipatwa na mawazo mengi sana. Baada ya kipindi kirefu cha kimya, alimwambia Khadija: "Baada ya kusikia yale ambayo wewe na Maysara mmesema kuhusu Muhammad, na pia kufuatana na vile ninavyomjua, mimi ninaona kama kwamba anazo sifa zote, tabia, ishara na uwezekano wa kuwa Mjumbe wa Mungu. Hakika, inawezekana Muhammad atakuja kuwa mmoja wao katika siku zijazo."
Kwa mtazamo wa makini ndani ya giza la upagani wa Arabuni, Waraqa aliwezeshwa labda na ubashiri wake, kuona dalili ndogo za Mwanga wa Uislamu ambazo si muda mrefu zingejitokeza kwenye upeo wa macho na Muhammad ndiye ambaye angeleta Mwanga huo.
Vitabu vingi vinavyoeleza maisha ya Muhammad Mustafa, Mtume wa Uislamu(s.a.w.w)
vimetaja miujiza kadhaa inayodaiwa kufanywa naye wakati wa safari yake ya kwenda na kurudi kutoka Syria. A. Yusuf Ali, mtrjumi na mfasiri wa Qur'an Tukufu, ameandika ifuatavyo: "Hakuna Mtume yeyote aliyeweza kufanya mujiza wowote au kuonye-sha "Alama", bila ridhaa ya Mungu. Ridhaa ya Mungu (Mashiyat) ni Mpango wenye hekima unaohusu dunia yote, mpango huu upo si kwa faida ya kabila, mila, kipindi au nchi moja. Mujiza mkubwa kuliko yote katika historia ni Qur'an. Tunaweza kutambua uzuri wake na utukufu wake leo kama ambavyo walitambua watu wa zama za uhai wa Mustafa, hata zaidi, kwani jumuisho la uelewa wetu kuhusu asili na Uumbaji wa Mungu umeongezeka."
Mahali pengine A. Yusuf Ali anasema: "Dalili zilizopelekwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad, zilikuwa:
(1) Aya za Qur'an na
(2) Maisha na kazi yake,
Ambamo humo mpango na makusudio ya Mungu yalifunuliwa." Inaonyesha kwamba uchangamfu na kipaji cha Muhammad pia vil-imuathiri Khadija. Kama ilivyotokea kwa Maysara, Khadija naye aliin-gia kwenye kundi la watu wanaompenda Muhammad, na ni nani awaye yeyote miongoni mwa watu ambaye angekataa kumpenda. Khadija alimfahamu Muhammad kuwa mtu mpole mwenye staha, mkimya na asiye mpinzani. Aidha Khadija alitambua kwamba watu wa Makka walimpa jina la Sadiq na Amin. Na sasa alionyesha uwezo wake wa kuwa mfanyabiashara. Ustadi na werevu wake vilikuwa sababu ya mtu huyo kuwa na kipaji. Tathmini mpya ya Khadija kuhusu Muhammad, ni kwamba mtu huyu hakuwa mwenye masihara bali alikuwa na uwezo wa kufanya mambo. Tathmini hii ilimshawishi Khadija kufanya uamuzi wa kumwajiri Muhammad kuwa Meneja wa biashara yake kwenye misafara yote ya baadaye.