MAISHA YA BIBI KHADIJA

MAISHA YA BIBI KHADIJA0%

MAISHA YA BIBI KHADIJA Mwandishi:
Kundi: Waheshimiwa wa Kidini

MAISHA YA BIBI KHADIJA

Mwandishi: Syed A .A .Razwy
Kundi:

Matembeleo: 24566
Pakua: 4180

Maelezo zaidi:

MAISHA YA BIBI KHADIJA
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 24566 / Pakua: 4180
Kiwango Kiwango Kiwango
MAISHA YA BIBI KHADIJA

MAISHA YA BIBI KHADIJA

Mwandishi:
Swahili

11

MAISHA YA BIBI KHADIJA

SURA YA KUMI NA TISA

KHADIJA NA UISLAMU

Leo hii Uislamu ni jeshi lenye nguvu kubwa kabisa duniani. Maadui wake hawawezi kufanya lolote. Uislamu ni kama gogo la mti mkubwa, ambalo dhoruba za duniani zimeshindwa kuling'oa. Hata hivyo, kuna wakati ambapo gogo hili kubwa sana lilikuwa mti mchanga, ambao uli- hitaji mtu wa kuulinda kutoka kwenye vimbunga vya waabudu masana-mu na ushirikina ambavyo vilitishia kuung'oa.

Waislamu wanaweza wakasahau lakini Uislamu hautasahau kwamba wakati wa uchanga wake, ilikuwa Abu Talib na Khadija walioulinda. Waliufanya Uislamu usidhurike. Abu Talib aliulinda uchanga wa Uislamu usidhuriwe na tufani ya wasioamini na upagani; na Khadija aliumwagilia Uislam maji ya utajiri wake. Khadija hakuruhusu Uislamu mchanga ufe. Hakika Khadija hakutaka hata kuruhusu Uislamu udhoofike kwa sababu ya uzembe. Kwa Abu Talib na Khadija, kazi yao kubwa sana ilikuwa kuulinda Uislamu. Walipenda Uislamu, na wali-yarithisha mapenzi hayo kwa watoto wao.

Kama Abu Talib na Khadija waliulinda Uislamu usidhuriwe na maadui wakati wa uhai wa Muhammad Mustafa, na wakauimarisha kwa kutumia dhahabu na fedha nyingi, watoto wao na wajukuu wao waliulinda usidhuriwe na maadui baada ya kifo chake, na waliuimarisha kwa kumwaga damu yao. Damu yao ilikuwa Takatifu sana kuzidi yeyote katika Uumbaji wote. Hata hivyo, hiyo ilikuwa damu ya Muhammad Mustafa mwenyewe - Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, wa Mwisho na Mkubwa kuliko Mitume wote.

Khadija alikuwa shahidi aliyeona kwa jicho lake Uilsamu ulipozaliwa. Aliutunza katika kipindi chake cha uchanga, wakati wa matatizo makubwa sana, na wakati wa ukuaji wake. Uislamu ulipewa umbo na sura ndani ya nyumba yake. Kama kuna nyumba yoyote inayoweza kuitwa mtoto mchanga wa Uislamu, basi ni nyumba yake. Aliulea Uislamu. Kama nyumba yoyote ile ingeitwa chimbuko la Uislamu, basi ni nyumba yake. Nyumba yake ilikuwa makazi ya Qur'an Tukufu kitabu cha Allah, na chenye Sheria za Kiislamu, za kidini na za Kisiasa.

Ilikuwa ndani ya nyumba yake Hadija ambayo Malaika Jibril alikuwa anamletea Mjumbe wa Allah (s.a.w.w.) ufunuo kutoka Mbinguni kwa kipindi cha miaka kumi. Khadija amekusanya alama za kwanza nyingi zaidi katika historia ya mwanzo wa Uislamu kuliko mtu mwingine yeyote. Alikuwa mke wa kwanza wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Alikuwa Muumini wa kwanza. Alikuwa binadamu wa kwanza kushahadia kwamba Muumba ni Mmoja tu, na kwamba Muhammad ni mjumbe Wake. Baada ya mume wake alikuwa mtu wa kwanza aliyesikia sauti ya Ufunuo. Alikuwa mtu wa kwanza kusali sala ya Mwenyezi Mungu akiwa na mume wake. Wakati wowote alipokwenda kumsikiliza Mwenyezi Mungu, Khadija alikuwa karibu naye. Alikuwa wa kwanza kuwa Mama wa Waumini. Alikuwa ndiye mke pekee wa Muhammad Mustafa ambaye hakuishi maisha ya uke wenza. Mapenzi yote na urafiki wote wa mume wake, alipewa yeye peke yake.

Wakati Muhammad Mustafa alipotangaza ujumbe wake kuwa yeye ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na kuwaambia Waarabu waache kuabudu masanamu na aliwaita wakusanyike chini ya bendera ya Tauhid, dhoruba ya mawimbi ya huzuni ilimkabili. Washirika walitaka kumuua. Waligundua namna mpya za kumtesa yeye na walijaribu mara nyingi kumnyamazisha milele. Wakati huo wa shida na dhiki, Khadija alikuwa ngome yake. Ilikuwa kwa sababu tu ya Khadija na Abu Talib, washirikina hawakufanikiwa kuvuruga kazi yake ya kuhubiri na kutangaza Uislamu. Katika hali hii alifanya mchango wake muhimu sana kwa uhai na kutangazwa kwa Uislamu.

Khadija aliiwekea misingi viwango ambavyo vilifanikisha kuwepo kwa amani, uelewano, furaha na utimilifu ndani ya nyumba, na sifa hizo alizishikilia na kuonekana katika maisha yake alitoa mfano kwamba, ufunguo wa nguvu na furaha ya familia ni kiwango cha ukaribu wa huba baina ya wahusika wa familia. Alionyesha haki na kazi za waume na wake. Viwango vilivyowekwa na yeye vilikuwa ndio rasimu ya maisha ya familia katika Uislamu. Muhammad Mustafa na Khadija walikuwa pamoja kwa miaka ishirini na tano, na katika kipindi hicho walitunga sheria zinazo yafanya maisha ya ndoa kuwa na mafaniko na yenye fura-ha. Tangu hapo dunia imeshindwa kupata sheria bora zaidi ya hizo, hata za kutumia kwa muda mfupi. Uislamu ulijumuisha sheria hizo katika mpango wake.

Khadija aligeuza mawazo ya dhana na kuyaweka katika hali halisi. Maisha yake na Muhammad ni ushahidi madhubuti wa kweli hiyo. Kile alichokipatia dunia haikuwa mpangilio wa misingi au fikira za kinad-haria bali ni uzoefu wa hali halisi yenye nyakati nyingi za furaha iliy-otakasika, ndani ya Uislamu, miitikio stadi ya kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Kama ilivyotajwa huko nyuma, Waarabu wapagani walijihisi wame-poteza heshima yao yote. Heshima hiyo ilikuwa ile iliyowalazimisha kuua mabinti zao pindi wazaliwapo. Uislamu ulikataza desturi hii ya kishenzi kwa kuifanya dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, na kosa la jinai dhidi ya ubinadamu. Mbali ya kukataza kuua watoto wa kike, Uislamu pia umetoa hadhi, heshima na haki kwa wanawake na kud-hamini haki hizo.

Mwenyezi Mungu alitaka kuonyesha kwamba sheria za Uislamu zinatekelezeka. Kuonyesha utekelezwaji wa sheria hizo, na kuonyesha "Mfumo wa Maisha" ya Kiislamu, Aliteua nyumba ya waja Wake, Muhammad na Khadija. Bila Khadija, sheria za Kiislamu zingekuwa hazina maana. Hakika, inawezekana pia kwamba Muhammad Mustafa hangeweza kuzianzisha sheria hizo bila Khadija. Moja ya Neema kubwa sana Muhammad Mustafa na Khadija waliy-oipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni binti yao Fatima Zahra. Kama ilivyo onyeshwa kwenye kurasa za nyuma, Fatima alizaliwa baada ya kufa kaka zake Qasim na Abdullah. Fatima alikuwa na umri wa miaka mitano tu mama yake alipofariki. Baada ya kifo cha mama yake, Muhammad Mustafa, mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alikuwa baba na mama wa Fatima. Katika kumlea na kumkuza binti yake, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alikuwa anaonyesha jinsi sheria za Kiislamu zitumikavyo. Kwa kuwa yeye ni kigezo cha Waislamu wote, wanatakiwa kumuiga katika matendo yake yote. Aliweka upendo mkubwa sana juu yake, na alionyesha heshima kubwa mno kwa binti yake.

Kote Makka na Madina, watu wengi mashuhuri kama vile watoto wa wafalme na viongozi wa makabila yenye nguvu, walikuja kumuona Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Alikuwa hasimami wakati wa kusalim-iana na watu hao. Lakini kama alisikia kwamba binti yake Fatima Zahra alikuwa anakuja kumuona, alinyanyuka na kwenda kumsalimia, alim-sindikiza na kumuonyesha sehemu ya heshima inayostahili kuketi yeye. Hakupata kuonyesha heshima hiyo kwa mtu yeyote wakati wote katika maisha yake, si kwa mwanaume au mwanamke!

ذَٰلِكَ فَضْلُ اللَّـهِ يُؤْتِيهِ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ ﴿٤﴾

"Hiyo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu anayompa amtakaye; na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kuu. (Quran 62:4).

Mwenyezi Mungu alimpa Fatima Zahra Ukarimu Wake, binti ya kipen-zi chake na Mjumbe Wake, Muhammad Mustafa.

Alikuwa tu binti wa Khadija, Fatima Zahra, ambaye alipata kupokea sifa kuu za Mbinguni kama isemavyo Qur'an Majid, Sura ya 76 Sura Dahr. Kwa hakika, Sura yote inasema habari zake na familia yake pamo-ja na mume wake Ali bin Abi Talib, watoto wake Hasan na Husain, na mtumishi wake Fizza. Pia amekuwa fasili ya maandiko yaliyomo kwenye Sura Kauthar (108) "Mwenyezi Mungu alimpa Khadija mkwe ambaye ni Ali bin Abu Talib aliyeitwa baadaye Simba wa Mwenyezi Mungu; "Mkono wa kuume wa Uislamu;" na ngao na kikingio cha Muhammad Mustafa; na Alimpa wajukuu kama Hasan na Husein ambao walikuwa "Wapanda mabega ya Mtume wa Mwenyezi Mungu", na "Viongozi wa Vijana wa Peponi."

Bila shaka Uislamu unamaanisha matendo ya nyumba ya Khadija, na bila shaka Qur'an Majid ni lugha ya familia yake. Binti yake, Fatima Zahra na wajukuu zake, Hasan na Husain, katika kukua kwao wanazungumza Qur'an Majid. Alikuwa na uhusiano ulio sawa kwa Uislamu na Quran kama vile mwanga ulivyo kwa macho, mng'aro kwa lulu na harufu nzuri kwa ua waridi.

Hata lugha yenye msamiati wa kiwango cha juu hushindwa kuzisema au kuzisifia sifa za Khadija. Lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameahidi zawadi zake kwa wapendwa watumishi wake kama Khadija kwenye Ay a zifuatazo za Kitabu Chake:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ ﴿٧﴾ جَزَاؤُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ذَٰلِكَ لِمَنْ خَشِيَ رَبَّهُ ﴿٨﴾

"Hakika wale walioamini na kutenda wema, basi hao ndiyo wema wa viumbe. Malipo yao kwa mola wao ni mabustani ya daima ambayo mito inapita mbele yake, wakae humo milele; Mwenyezi Mungu amewaridhia, nao wameridhika. (malipo) hayo ni kwa yule anayemuogopa Mola wake." (Qur'ani 98:7- 8).

SURA YA ISHIRINI

KHADIJA NA WANA HISTORIA WA KIISLAMU

Kwenye vitabu vyao vya historia, sifa ya juu sana ambayo wanahistoria wa Kiislamu wamempa Khadija, ni kwamba aliuimarisha Uislamu kwa utajiri wake. Wanampa sifa hii halafu wana endelea na mambo mengine. Ni kweli kwamba ni utajiri wa Khadija ulioufanya Uislamu kuwa na uwezo wa kukua na kuendelea kuwepo; lakini hii ni sehemu tu ya ukweli. Kama kuna uthibitisho uliotolewa na wanahistoria kuhusu mchango wa Khadija kwa Uislamu, ni mdogo sana. Mbali na kukiri huduma nyingi kubwa kubwa alizozitoa Khadija kwa ajili ya Uislamu. Lakini wengi wa wanahistoria ama wameupotosha ukweli au wameu-ficha ukweli au wameunda maneno (maelezo) yao wenyewe, na kuya-toa kama ndiyo ukweli wa historia. Siyo historia yote ya Uislamu ya zama za kale ni taarifa ya kweli; sehe-mu fulani ya historia hii ni "tungo." Historia hii bunifu iliandikwa kwa ajili ya au na makundi fulani yenye mwelekeo maalum, Hadithi nyingi za uwongo zilipata nafasi na kuingizwa kama historia ya Uislamu kwa jinsi hiyo na ukweli ulizikwa kimyakimya.

Kutunga hadithi za uwongo, kuziingiza kwenye mzunguuko wa waso-maji na kuuzika ukweli ilikuwa hila ambayo kwayo viongozi wa sala za jamaa, wahubiri kwenye mimbari misikitini, waalimu shuleni, wasaidizi wa wafalme, masultani na makhalifa, maprofesa wa vyuo, wanafalsafa wa sheria, majaji wa mahakama, wafalme, wote walisaidia. Wanahistoria walikuwa na haki au nafasi ndogo sana ya kuchagua kuhusu jambo hili. Hata kama alikuwa mtu mwenye kuheshimika na mwenye msimamo, hakuthubutu kuupaa changamoto msimamo wa chama. Kama alijaribu kufanya, alihatarisha maisha yake mwenyewe. Kama aliandika historia yenye taarifa ya kweli, aliuawa.

Kwa hiyo ali-fuata mwenendo wa vitendo. Aliacha ukweli na kuandika historia ban-dia (za kubuni) Maulana Shibli Numani, mkuu wa kitengo cha historia ya Uislamu, huko India, ameandika kwenye kitabu chake "Life of the Prophet", Vol. 1 (Azamgarh, India, 1976) kwamba wakati wa utawala wa Khalifa Muawiya (D. A.D. 680), na Waumayya wa baadaye, maelfu na makumi ya maelfu ya Hadith ( I ) zilizalishwa na watengenezaji wa hadithi na ziliingizwa kwenye mzunguko.

Wanataaluma wanahistoria walioko kwenye orodha ya wapokea mshahara wa serikali, waliunganisha pamoja uwongo baada ya uwongo na kuuingiza kwenye vitabu vya historia. Na kwa miaka 90, majina ya Ali bin Abi Talib, na watu wengine wa Bani Hashim walilaaniwa kwenye kila mimbari katika dunia ya Uislamu kutoka Sind huko India hadi Hispania - Ulaya. Watoto waliza-liwa, walikua na walikufa, wakisikia laana hizi na kamwe bila kujua ukweli.

Mnamo A.D. 750, ukoo wa Abbas ulichukua ukhalifa, na kuung'oa utawala wa ukoo wa Umayya. Lakini hata huo ukoo wa Abbas haukuwa na nafuu yoyote katika chuki yao kwa familia ya Muhammad Mustafa kwama ulivyokuwa ukoo wa Umayya. Hakika, baadhi yao waliwazidi Waumayya katika kuwafanyia mateso watoto wa Mtume na wafuasi wake. Tabia moja ambayo koo hizi mbili zilikuwa nayo ni ile chuki ya kinyama waliyokuwa nayo dhidi ya familia na watoto wa Muhammad Mustafa.

Edward Gibbon Watesaji wa Muhammad walipora urithi wa watoto wake; na mabingwa wa waabudu masanamu wakawa ndio viongozi wakuu wa dini yake na himaya. (The Decline and Fall of the Roman Empire) Robet Payne Tena na tena tutaona wafuasi wa Muhammad (yaani, waislamu) kwa ukatili kabisa wanaangamiza kizazi cha Muhammad bila huruma. (uk. 84 - 85) Kwa miaka 350, kizazi cha Abu Sufyan na wale waliodai kwamba wana nasaba na ukoo wa Abbas walipigana vita na kizazi cha Muhammad, (uk. 193). Kipindi chote cha karne za Uislamu, mateso ya kushangaza yalikizun-guka zunguka kizazi cha Muhammad. Ilikuwa kama vile sehemu ile ya dunia ambayo kwa bidii iliukubali Uislamu na Mtume wa Mungu, iligeuka adui wa kizazi chake kiishicho daima milele. (uk. 306). (The Holy Sword (Upanga mtukufu), 1959)

Kampeni ya makhalifa wa ukoo wa Abbas dhidi ya watu wa nyumba ya Mtume au watoto wake, pia ilidumu kama ulivyo dumu ukhalifa wao -miaka 500. Ilikuwa wakati wa ukhalifa wao ndipo historia ya Uislamu ilipoandikwa na hadithi zilikusanywa, zikahaririwa na kuchapishwa. Majaribio yasiyo madhubuti yalifanywa na wasomi makini ambao walitenganisha taarifa zenye ukweli na kuacha taarifa za uwongo, laki-ni kwa mafanikio madogo sana. Vitabu vingi vya historia na Hadithi siku zote vimebebeshwa mizigo ya "ukweli" au "Hadith" ambazo zimepandikizwa humo.

Historia imesemwa kiusahihi kwamba, ni propaganda ya upande ulioshinda. Makundi yaliyoshinda katika historia ya Uislamu, kwanza yalikuwa, ni Banu Umayya na halafu Banu Abbas ambayo yalifaulu, kwa kunukuu maneno ya Gibbon: katika "uporaji wa urithi wa watoto wa Muhammad." Mara walipochukua vyombo vya dola, walikuwa huru kuandika au kupotosha historia ya siku za mwanzo za uislamu jinsi walivyopenda.. Kwa vile vitabu vingi vya historia ya Uislamu vilipewa "msukumo" na kile wakomunisti wakiitacho "watu wenye mamlaka ya dola" nitawatambulisha waandishi wake kama "wanahistoria wa mahakama." Wanahistoria hawa waliwahadaa wasomaji wao juu ya ngano tatu zifu-atazo kwa kulinganisha na maisha ya Hadhrat Khadija, Mwenyezi Mungu na amuwie radhi na amrehemu.

1. Alikuwa na miaka 40 alipoolewa na Muhammad Mustafa.

2. Alikwisha olewa mara mbili kabla ya kuolewa na Muhammad Mustafa.

3. Yeye na Muhammad Mustafa walizaa watoto sita wa kiume wawili na wakike wa nne.

Tutauzungumzia uwongo huu moja baada ya mwingine.

1. Umri wa Khadija.

Wanahistoria wengi wa kiiislamu wanasema kwamba Khadija alikuwa na umri wa miaka 40 alipoolewa na Muhammad Mustafa. Tarakim hii imerudiwa mara nyingi zaidi na wanahistoria hivyo kwamba sasa inaminiwa kama jambo la kweli kabisa. Lakini bado tarakimu hii ina maswali ya wazi kwa sababu zifuatazo:

Hakuna mtaalamu yeyote wa historia anayejua tarehe ya kuzaliwa kwa Khadija, tarakimu "40" ni makadirio tu, na ni makadirio ya juu sana. Ambapo ni kweli kwamba Khadija alikuwa na umri mkubwa kuliko Muhammad Mustafa, hakuwa anamzidi umri kwa miaka 15 kama ambavyo inadaiwa na wanahistoria wengi, lakini anamzidi miaka michache tu.

Bara Arabu ni nchi yenye joto sana, na wasichana wa Kiarabu hubalehe haraka zaidi kuliko wasichana wa nchi zenye baridi au joto la wastani. Hadhrat Aisha inasemekana aliolewa akiwa na umri wa miaka 11. Wasichana wengine wa Kiarabu pia waliolewa mapema sana. Kwenye nchi kama Arabia, mwanamke hangekaa miaka 40 ya maisha yake akingojea kuolewa. Katika umri wa miaka 40, miaka mizuri kwa maisha ya mwanamke itakuwa imekwisha pita - katika Uarabuni au kwingineko popote. Lakini hata kama akiolewa akiwa na miaka 40, hawezi kufikiria kuzaa watoto. Hata kwenye nchi za baridi na joto la wastani, mara nyingi, mwanamke kupita umri wa kutokuzaa ni 40. Arabuni hali hii pengine hutokea mapema zaidi.

Khadija aliishi miaka mingi katika hali ya upekee bila mume. Kama ambavyo imeonyeshwa hapo kabla, alipokea posa nyingi kutoka kwa mamwinyi na watoto wa wafalme wa Arabuni, lakini alikataa. Hawakuweza kumshawishi kwa utajiri wao. Kama walikuwa matajiri, yeye Khadija alikuwa tajiri sana kuliko yule aliyewazidi wao. Na katika sifa za mtu binafsi kama sifa za kichwa mkono na moyo wote walikuwa kama vumbi ya miguu yake. Yeyote aliyejaribu kumshawishi kwa kutumia utajiri wao au mamlaka yao angeonekana mpumbavu kama sio mjinga hasa. Kwa hiyo, alitulia hadi hapo alipojitokeza mwanamume ambaye kweli alipendeza - Muhammad Mustafa na alikubali kuolewa naye.

2. Madai ya ndoa zingine za Khadija.

Khadija hakuolewa kamwe kabla ya kuolewa na Muhammad Mustafa. Ndoa yake na Muhammad Mustafa ilikuwa ya kwanza na ya mwisho. Wanahistoria hao hao ambao wamedai kwamba Khadija aliolewa mara mbili kabla ya kuolewa na Muhamad Mustafa, wameeleza kwamba mamwinyi wote wa Maquuraysh na watoto wa matajiri wa Waarabu, walimposa, lakini alikataa. Kama angekuwa ameolewa mara mbili kabla, hangesita kuolewa mara ya tatu.

3. Watoto wa Khadija:

Imedaiwa na wanahistoria ya mahakama ya Banu Umayya kwamba Khadija na Muhammad walizaa watoto sita na wanatoa orodha ya maji-na yao kama ifuatavyo:

1. Qasim

2. Abdullah

3. Zaynab

4. Ruqayya

5. Ummu Kulthum

6. Fatma zahra.

Muhammad Mustafa na Khadija walizaa watoto watatu si sita. Nao walikuwa:

1. Qasim

2. Abdullah

3. Fatima Zahra,

Miongoni mwa hawa watoto watatu, wawili wa kwanza kuzaliwa - Qasim na Abdullah - walikuwa wanaume, na wote walifariki dunia wakiwa wachanga kama ambavyo imeonyesha huko nyuma. Mtoto wa tatu na wa mwisho alikua binti yao Fatima Zahra. Ni nani hawa watoto wengine watatu wa kike- yaani Zaynab, Rukayya na Umm Kulthum? Swali linajibiwa baadaye kwenye sura hii. Madai haya yote matatu yamepata kuenea kama ya "ukweli" lakini hata hivyo ni ngano za uwongo. "Mng'ao" wa zama umeyafanya "yaheshimike" hivyo kwamba Waislamu wengi wameyaamini (mada hayo) kuwa ya kweli. Lakini hizi sio kwa namna yoyote, ngano pekee ambazo Waislamu wengi wamezipatia hadhi ya ukweli. Kuna ngano nyingine nyingi ambazo "zimefuzhu" kama za ukweli.

Mifano ifuatayo, itaonyesha kwamba hii inaweza kutokea hata kama hakuna nia ya makusudi ya kuupinda ukweli au kuharibu ukweli:

1. Waislamu wengi wanaamini kwamba mhusika anayetajwa kwenye aya 83 na 94 kwenye sura ya 18 ya Quran Majid (Kahf au pango), kama Zul- Qarnain alikuwa Alexander the Great (Alexander Mkuu) wa Macedonia. Hata Abdallah Yusufu Ali anaunga mkono maoni haya. Anasema: "Binafsi, sina shaka kwamba huyu Dhul-Qarnain ni, Alexander the Great, Alexander wa kihistoria, na si Alexander wa hadithi za kale... Na tena, Zul-Qarnain angeweza kuwa yeyote, lakini sio Alexander the Great, Zul-Qarnain alikuwa mteule wa Mwenyezi Mungu, labda alikua Mtume. Alexandaer kwa upande mwengine alikuwa mpagani. Aliwaabudu miungu ya kiume na kike, si tu ya Kigiriki bali pia ya Misri, Babylon na Ajemi. Harold Lamb.

Alexander aliabudu miungu ya ajabu - si Zena tu, bali hata Ammon-Re wa jangwa la Misri, Marduk wa minara ya Babylon, na Anura mlezi wa mahekalu ya Ajemi. (Alexander wa Macedon, New York, 1946) Alexander alifanya makosa mengi pamoja na kuua marafiki zake waw-ili wa siku nyingi na majenerali waliokuwa watiifu, Cleitus na Parmenion. Na alipanga mauji ya Baba yake mwenyewe Philip. R.D.Milns. Hapana shaka kwamba Alexander alipata ufalme kwa kumuua baba yake. (Alexander the Great, New York, 1969)

Wakati wa vita alizopigana, Alexander aliua maelfu ya watu wasio na hatia waume kwa wake bila sababu ya msingi. Labda alielemewa na uchu wa kumwaga damu. Mwana historia wa kisasa anasema kwamba kabla hajafa, alirukwa na akili. Na utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kwamba alikufa baada ya kuwa mzoefu wa kupindukia wa kunywa mvinyo.

2. Jina halisi la Abdul Muttalib, babu yake na Muhammad Mustafa, Mtume wa Mwenyezi Mungu lilikuwa Shaiba. Alipokuwa kijana, siku moja alisaidiwa usafiri na ami yake, Muttalib, kutoka Yathrib ( Madina) kuingia Makka. Watazamaji walisema: "Ohoo angalia! Muttalib amemnunua mtumwa mpya"; Muttalib alikasirika ali-posikia kauli hiyo na alisema: "Mlaaniwe ninyi. Huyu si mtumwa wangu. Ni mtoto wa kaka yangu , Hashim." Lakini jina la "Abdul Muttalib" "Mtumwa wa Muttalib" lilimganda huyo kijana. Anajulikana kwenye historia kwa jina lake la kupanga la kupachikwa -Abdul Muttalib, Jina lake halisi Shaibu limesahauliwa.

3. Mfano huu unatoka kwenye kisa cha Mtume Yusuf. Ay a ifuatayo imo kwenye sura ya 12 ya Qur'an Majid (Sura Yusuf) "Hakika Yusufu na nduguye (yule aliye baba mmoja na mama mmoja naye) wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi hali sisi (watoto wa mama mwingine) ni kundi lenye nguvu. Hakika baba yetu yuko katika upotofu uliyo dhahiri. Qur'ani 12:8. A.Yusuf Ali ameielezea Aya hii ifuatavyo:

"Ndugu kumi hawakuwaonea wivu na kuwachukia wadogo zao Yusuf na Binyamin tu, walimdharau na kutomtiii baba yao kama mzee mjinga mwenye kupungukiwa akili. Katika hali halisi. Yakuub alikuwa na hekima ya kuhakikisha kwamba watoto wake wadogo wasio na hatia walihitaji ulinzi na alitambua Utukufu wa kiroho wa mwanae Yusuf.

Lakini, hekima zake kwao zilikuwa ujinga au kichaa, au kupungukiwa akili, kwa sababu iligusa kujipenda kwao, kama ufanyavyo ukweli mara kwa mara. Na walitegemea juu ya ukatili wa nguvu ya idadi - dhidi ya mzee Yakub, kijana mdogo Yusuf na mvulana Binyamin."Aya nyingine katika muktadha huo huo, inasomeka kama ifuatavyo:

قَالُوا تَاللَّـهِ تَفْتَأُ تَذْكُرُ يُوسُفَ حَتَّىٰ تَكُونَ حَرَضًا أَوْ تَكُونَ مِنَ الْهَالِكِينَ ﴿٨٥﴾

"Wakasema: "Wallahi! Hutaacha kumkumbuka Yusufu ( na kulia) hata utakuwa mgonjwa au utakuwa miongoni mwa wenye kuangamia." (Qur'ani 12:85).

Mfasiri anaifafanua ay a kama ifuatavyo:

"Wakasema" lazima watakuwa watu wa karibu na Yakuub kabla ya nduguze (Yusuf) kuwasili ( kutoka Misri). Ndugu hawa hawa kwa bidii walipanga uzushi kwamba baba yao alikuwa mzee katili aliyepun-gukiwa na akili, na kila mtu aliamini hilo, hata baada ya watunzi wake kuliacha hilo. Hivyo uwongo haufi kiurahisi, mara unapoanzishwa. (A. Yusuf Ali) Ipo mifano mingine mingi kwenye historia ya Waislamu na na wsio Waislamu, ya udanganyifu kugeuzwa kuwa kweli. Hivi ndivyo ilivyotokea kuhusu hizi taarifa za uwongo zilizo husishwa na hadithi ya maisha ya Khadija. Taarifa hizi zilipata kukubalika miongoni mwa Waislamu. Mara uwongo uanzapo, hukataa kufutika.

Pia inawezekana kwamba wanahistoria ambao walikuwa wakikusanya taarifa ili waandike historia ya Uislamu wa siku za mwanzo, waliweza kupata tu visa ambavyo "vilipandikizwa" kwa uhodari kabisa na "taba- ka la watawala" kwenye vyanzo vya mwanzo kabisa. Walishawishiwa kwamba taarifa zinazopatikana kwenye vyanzo hivyo, zilikuwa sahihi, na waliziingiza kwenye vitabu vyao. Madai kuhusu umri, ndoa na watoto aliozaa Khadija, yalichochewa na sababu mbili , ambazo ni: -

1. Khadija alikuwa mama wa Fatima Zahra; na alikuwa mama mkwe wa Ali bin Abi Talib; na bibi wa Hasan na Husein. Kwa hiyo, hangeepuka chuki ambayo Banu Umayya na Banu Abbas walikuwa nayo dhidi ya watu wa familia ya Muhammad Mustafa, hasa zaidi Ali, Hasan na Husain.

Hata waandishi wa historia, kwa sehemu kubwa walikubali kuingia kwenye kundi la wale waliokuwa wanawalipa wakati wanaandika historia, lakini kama wangekataa, wangekosa malipo na pengine hata kuuawa.

Kwa hiyo hawakuwa na jinsi isipokuwa kutunga "ukweli" fulani ambao utapunguza umuhimu wa Khadija. Katika kuchagua "ukweli" ambao wameutunga wao au wenzao waliotangulia, hujiona wako huru kutekeleza busara zao - ushabiki wao. Lakini katika kuyafanya maelezo yao yakubalike, iliwabidi wawe werevu sana vinginevyo chuki yao ingedhihirika kuwa ya wazi mno. Na thamani ya kazi yao ya historia ingekuwa haiaminiki.

2. Wanahistoria mamluki walitaka kuwaambia wasomaji wao kwamba miongoni mwa wake wa Mtume, walikuwepo ambao walikuwa mashuhuri au hata kumzidi Khadija, na kwamba mwanamke huyo ni Aisha. Ilibidi waanze kumtukuza Aisha na si Khadija.

Wanahistoria hawa hawakuwa na hofu na tasnifu ambazo walikuwa wanajaribu kuzikuza kutoka kwa mke mwingine yeyote wa Muhammad Mustafa, lakini walikuwa hawana uhakika kama juhudi zao za kum -wonyesha Aisha kama mke bora kuliko Khadija zingefanikiwa. Lakini watu hawa walikuwa wanabahatisha na wakatengeneza "tungo" kwamba Khadija alikuwa na miaka arobaini na aliolewa mara mbili kabla ya kuolewa na Muhammad. Ni tungo ambayo kwa maoni yao ingeweza kumpinga Khadija. Kwa upande mwingine walidai kwamba Aisha si tu kwamba alikuwa mdogo wa umri na mzuri wa sura bali pia alikuwa bikira.

Kwa matumizi haya ya mantiki za kiholela, wanahistoria wamejenga tasnifu zao za ubora kwa mke mmoja kuwazidi wake wenzake. Lakini, Je Mtume alimuoa Aisha kwa sababu ya ujana wake, uzuri wa sura na ubikira? Abbas Mahmud Ali Akkad, anajibu swali hili kwenye kitabu chake. "Aisha" kama ifuatavyo: Kwa kadiri tujuavyo, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu hakuoa kwa sababu ya kupata watoto. Kwa ujumla alioa kwa sababu mbili, yaani:

1. Wanawake wengine walikua wanahitaji msaada baada ya kufiwa na waume zao. Walikuwa hawana ndugu wa kuwasaidia. Mtume aliwaoa ili wawe na nyumbani kwao.

2. Mtume alitaka kuvunja upinzani wa makabila ya Waarabu dhidi ya Uislamu. Njia mojawapo ya kufanya kwake yeye ni kuoa wanawake wa makabila hayo. Pia palikuwa na sababu nyingine ya tatu kuhusu ndoa nyingine za Mtume, yaani, kama yeye alikuwa mwalimu wa wanaume wa Kiislamu, wake zake walikuwa walimu wa wanawake wa Kiislamu, katika mambo yote ya imani za dini. Waliwapa maelezo wanawake wa Kiislamu maana ya Quran na waliwafundisha jinsi ya kuzitumia she-ria za Kiislamu kwenye maisha yao binafsi.

Ukimuondoa Khadija, Mtume aliwaoa wanawake wengine wote kwa sababu moja au zaidi ya zile sababu zilizotajwa. Ndoa yake na Khadija ilikuwa ndio pekee iliyo tua kwenye huba, mapenzi na urafiki; na kwake yeye, ilitimiza malengo yote ya ndoa. Khadija naye pia aliwafundisha sharia za Uislamu kwa wanawake wa Kiislamu, lakini alifanya hivyo zaidi kwa kuonyesha mifano na kwa maadili kama ilivyoonyeshwa mwanzo. Wanahistoria wa mahakama wamekuwa wakirudia rudia baadhi ya uwongo na nusu ukweli kwa karne nyingi, na kwa marudio hayo wamefaulu kuushawishi Umma wa Waislamu kwamba Khadija aliole-wa mara mbili kabla ya kuolewa na Muhammad Mustafa. Akiandika juu ya suala la ndoa ya Khadija, Mwandishi wa "Raudhatus-Safa" anasema: "Watu wakubwa wa kabila la Quraysh walitaka kumuoa Khadija na walipeleka posa zao lakini hakukubali kuolewa na yeyote yule katika wao." (Volume 2, P. 271).

Na mwandishi wa Raudhatul-hbab" anaandika kama ifuatavyo: "Watukufu wote wa kabila la Quraysh walitaka kumuoa Khadija lakini hakumfikiria yeyote yule katika wao." (Volume1. P. 105) Kwa mujibu wa wanahistoria wala rushwa, wanasema kwamba wakati Khadija anaolewa na Muhammad Mustafa, alikwisha olewa mara mbili; na alikuwa na umri wa miaka 40. Kama hii ni kweli, basi ina maanisha kwamba Khadija alikuwa mwanamke aliyefika umri wa kuelekea uzeeni, au labda, kwenye nchi kama Arabuni alikwisha kuwa na umri wa kati ambapo uzuri wake wa ujana ulikwisha toweka. Kwa nini basi mamwinyi wa kabila la Quraysh na watoto wa familia mashuhuri wa Arabuni walitamani sana kumuoa? Hata hivyo, kuwa tajiri na uwezo kama walivyo kuwa, wangeweza kuwapata wanawake wengine vijana na wazuri wa sura, miongoni mwao wengine wangekuwa mabikira, ili wafunge ndoa nao. Kwa nini basi wakimbilie na kung'ang'ania kumuoa mjane ambaye hata hivyo alikuwa anaelekea uzeeni kiumri? Pia haitakuwa sahihi kusema kwamba wachumba hao waliokataliwa na Khadija walivutiwa na utajiri wake, kwa sababu wachumbiaji wenyewe walikuwa matajiri.

Allama Ali Ahmed Abul Qasim al-Kufi anahoji uthabiti wa hadithi ya ndoa mbili za Khadija kabla ya kuolewa na Muhammad Mustafa. Anaandika ifuatavyo kwenye kitabu chake - Al-Istighatha" "Khadija hakuolewa na mtu yeyote kabla ya kuolewa na Muhammad Mustafa. Waandishi wote wa historia wamekubaliana kwa pamoja kwamba wakuu wote wa kabila la Quraysh walimposa Khadija, kila mmoja kwa wakati wake lakini aliwakataa wote. Hatimaye aliolewa na Muhammad Mustafa. Hali hii iliwafanya wanawake mashuhuri wa Maquraysh kumkasirikia. Walisema kwamba wakati watukufu wakub-wa na watoto wa familia mashuhuri jijini Makka walipomposa ali-wakatalia na kuwabeza. Na halafu, wakati anatokea kijana wa ukoo wa Bani Hashim ambaye hakuwa na utajiri wowote, au mamlaka, alipomposa, alimkubali. Hawa wanawake mashuhuri wa Makka hawakuelewa kwa nini Khadija alidharau maombi ya posa ya watu matajiri na wenye mamlaka katika jamii ya Arabuni, na mwishowe alikubali kuolewa na mtu asiye na kitu wala mamlaka. Huu ni uthibitisho kwamba Khadija hakuolewa na mtu yeyote kabla ya kuolewa na Muhammad Mustafa.

Watu wengine huuliza swali kwamba kama inadhaniwa kwamba Khadija aliolewa mara mbili kabla ya kuolewa na Muhammad Mustafa, na kwamba alikuwa na umri wa miaka 40 wakati wa ndoa yake ya tatu, kuna jambo lolote la kulaumika hapa? Hapana! Kama mwanamume au mwanamke anaoa au anaolewa zaidi ya mara moja au anakuwa na umri, wa miaka 40 wakati wa kuoa au kuolewa, hakuna jambo lolote la kulau- mu hapa. Suala ni kwamba, kama ni kweli au uwongo kama Khadija aliolewa zaidi ya mara moja au kama alikuwa na miaka 40 wakati anaolewa wakati wa ndoa yake ya mwisho. Swali lenyewe ni je, ni ukweli wa kihistoria kwamba Khadija aliolewa mara tatu; au kwamba alikuwa na miaka 40 wakati wa ndoa yake ya mwisho. Hapana. Sivyo hivyo. Kama mtu anakubaliana na waandishi wa historia mamluki kwamba Khadija aliolewa mara tatu, na kwamba alikuwa na miaka 40 wakati wa ndoa yake ya tatu, hakuna kinachopungua kutoka kwenye hadhi yake. Yeye anaendelea kuwa Mtukufu.

Lakini kwa vyovyote vile si kweli kwamba alikuwa mjane wa miaka 40 alipoolewa na Muhammad Mustafa, na, kwa hiyo, si uadilifu kusingizia uwongo kwenye hadithi ya maisha yake, au maisha ya mwanamme au mwanamke yeyote, kuhusu suala hili. Kila mtu anayo haki ya kutoa mawazo yake lakini si kwa taarifa za mambo yahusuyo ukweli wake. Kama mtafiti wa ukweli anataka kutenganisha mambo yaliyo tokea kutoka kwenye dhana, anaweza kufanya hivyo kwa msaada wa kutu-mia akili na mantiki katika kupata mchanganuo ulio sahihi. Utafiti wake wa kuelewa kutoka kwenye misingi isiyobadilika utampa matokeo mazuri ya uzoefu wa hali halisi.

Zainab, Rukaiya na Ummu Kulthum. Kabla Khadija hajaolewa na Muhammad Mustafa, walikuwepo wasichana watatu waliokuwa wanaishi naye nyumbani mwake mjini Makka. Majina yao yalikuwa Zainab, Rukaiya, na Ummu Kulthum. Hawa walikuwa mabinti wa marehemu dada yake. Baba yao alifariki mapema zaidi, na mama yao alipofariki, Khadija aliwachukua na kuanza kuishi nao nyumbani kwake. Baada ya kuolewa Khadija, wasichana wote watatu waliendelea kuwa naye kama wasaidizi wake Inawezekana walimwita Khadija mama yao na Muhammad Mustafa baba yao. Na kufuatana na mila za Kiarabu, walijulikana kama watoto (mabinti) wake kwa sababu waliishi nyumbani mwake, na alikuwa mlezi wao kisheria. Zainab alikuwa ndiye mkubwa kwa umri kuzidi wengine.

Aliolewa na mtu aliyeitwa Abul-As bin erRabi. Mnamo mwaka wa 624 A.D alikuja na jeshi la wapagani wa Makka na alipigana na jeshi la Muhammad Mustafa kwenye vita vya Badr. Alikamatwa kama mateka lakini ali-fidia uhuru wake, na alirudi Makka, baadaye, alisilimu. Wasichana wengine wawili - Rukayya na Ummu- Kulthum waliolewa na Utba na Utayba watoto wa Abu Lahab na Umm Jamil. Wasichana wote watatu waliolewa kabla ya kutangazwa Uislamu, waume wao wote watatu, kwa hiyo, walikuwa waabudu masanamu.

Baaada ya kutangazwa kwa Uislamu, Abu Lahab na mke wake, Umm Jameil, wote walikuwa maadui wakubwa wa Uislamu, wakafanywa kuwa viumbe walio laaniwa katika sura ya 111 ya Qur'an Majd. Hali hii ilichochea hasira zao na waliwamuru watoto wao - Utba na Utayba kuwataliki wake zao na kuwarudisha kwao. Wasichana wote wawili-Rukayya na Ummu Kulthum walipewa talaka, na walirudi nyumbani kwa Khadija. Baada ya muda, Rukayya aliolewa na Uthman bin Affan mtu wa ukoo wa Ummayya wa kabila la Quraysh, na miaka mingi baadaye alikuwa Khalifa wa Waislamu. Alikufa mwaka 624 A.D. huko Madina. Baada ya kifo chake, dada yake Ummu Kulthum, naye pia aliolewa na Uthman bin Affan.

Muhammad Huseyn Haykal Muhammad aliwaoza Rukayya na Ummu Kulthum kwa Utba, na Utaybah, watoto wa ami yake, Abu Lahab. Ndoa hizi hazikudumu, kwa sababu mara tu baada ya kutangazwa kwa Uislaumu, Abu Lahab ali- waamuru watoto wake wawili wawataliki wake zao. Uthman ndie aliyewaoa baadaye mmoja baada ya mwengine. (The Life of Muhammad, Cairo, 1935) Wanahistoria wa Umayya "walitiwa moyo" na Muawiya bin Abu Sufyan, mwasisi wa ukoo wa Ummaya, na warithi wake, walidai kwam-ba Rukayya na Umm Kulthum walikuwa watoto wa Muhammad na Khadija. Hawa mabinti walipoolewa na Uthman aliyetoka ukoo wa Umayya walimwita Dhun-Nurayn, yaani, "mwenye nuru mbili," Rukayya na Umm- Kulthum. Lakini kipindi kifupi kabla ya hapo, "nuru" zote hizi mbili zilikuwa za waabudu masanamu wawili wa Makka. Kila mmoja wa hawa waabudu masanaumu, kwa hiyo, alikuwa mmiliki wa "nuru" moja ambayo baadaye ilikwenda kwa Uthuman. Hata hivyo, "nuru" hiyo au hizo zilibakia hivyo bila mabadi-liko, isipokuwa ni umilikaji tu ndio uliobadilika.

Je, mabinti hawa walikuwa watoto wa Muhammad Mustafa na Khadija kama wasemavyo wanahistoria mamluki? Jibu la swal hili litafutwe

(A) katika Qur'an Majid na (B) ushahidi wa historia. Jibu lake litolewalo hapa chini, ni la dhahiri: A. Ushahidi wa Qur'an Majid. Kama nuru ya mwongozo wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu ina maana yoyote kwa Waislamu, basi hawa mabinti watatu: Zaynab, Rukayya na Umm Kulthum hawakuwa, na hawangekuwa mabinti wa kuzaliwa na Mtume wa Mungu na Khadija. Hawa walikuwa mayatima. Uhusiano wao na Muhammad na Khadija ulikuwa kwamba waliwahi kuishi nyumbani mwao. Khadija alikuwa mlezi wa yatima (na wajane) hata kabla ya kuoliwa.

Kama Muhammad Mustafa na Khadija wangekuwa wazazi wa hawa mabinti, watatu - Zaynab, Rukayya na Umm Kulthum- hawangewaoza kwa waabudu masanamu kama walivyo kuwa waume watatu wa mabinti hawa. Ni kweli kwamba mabinti wote watatu waliolewa kabla ya Uislamu haujatangazwa, lakini hata hivyo, Muhammad hakuvunja amri yoyote ya Qur'an Majid, wakati wowote, kabla au baada ya kufanywa mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Muhammad Mustafa haku-fanya kosa lolote la kipagani wakati wowote maishani mwake. Na Qur'an inaeleza wazi wazi kuhusu kukatazwa kwa ndoa ya mwanamke Mwislamu na mpagani.

Amri ya kukataza ndoa ya mwanamke Mwislamu na mshirikina iliteremshwa katika Aya zifuatazo zilizomo kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu.

"Wala msiwaoze (Wanawake wenu) kwa Wanaume washirikina mpaka waamini (Qur'an 2:221)

"(Wanawake hawa) waumini si halali kwao hao (makafiri wa kiume), wala wao (wanaume makafiri) si halali kwao" Qur'ani 60:10

Zimo aya nyingine ndani ya Qur'ani ambazo ingawaje hazisemi moja kwa moja kuhusu ndoa, zina mfanya Mwislamu asiweze kumwoza au kuwaoza mabinti zake kwa muabudu masanamu. Baadhi ya aya hizo ni:

"Basi laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya makafiri hao Qur'an 2:89 "Enyi mlioamini! Hakika washirikina ni Najisi" Qur'an 9 : 28

"...Mwenyezi Mungu ni adui kwa Makafiri (2:98)

Hakuna Mwislamu ambaye angekuwa mzembe kiasi hicho, hivyo kwamba, angedhani kwamba Muhammad Mustafa alivunja makatazo ya Qur'an kwa kuruhusu mabinti zake waolewe na wanaume ambao Mwenyezi Mungu amewalaani, ambao adui wao ni Yeye na ambao ni najisi. Kwa Mwislamu, Aya za Qur'an Majid zilizonukuliwa hapo juu, zinathibitisha kikamilifu kabisa kwamba Zaynab, Rukayya na Umm Kulthum, wote watatu, wakati fulani waliolewa na waabudu masanamu, hawakuwa watoto wa Muhammad Mustafa na Khadija.

Mwislamu - yeyote - hata yule ambaye yuko pembeni au anafuata mkumbo wa Uislamu atashangaa kama atashawishiwa kumuoza binti yake au binti zake kwa muabudu masanamu au hata kwa Ban Israel au Mkristo. Lakini Mwislamu huyo huyo na hali inanuka uvundo wa kejeli- ataamini, bila kuumwa na dhamira yake, kwamba Mtume wake mwenyewe, Muhammad Mustafa-mfafanuzi na mwenezaji wa Qur'an -aliwaoza mabinti zake watatu kwa waabudu masanamu watatu mjini Makka. B. Ushahidi wa Historia Muhammad Mustafa alikuwa anawapenda sana watoto. Hasa zaidi alikuwa anawapenda watoto wa binti yake Fatima Zahra. Watoto wake Hasan na Husain walikuwa nembo za macho yake. Aliwaendekeza. Watoto hao walikuwa wanapenda kucheza na babu yao hata wakati anaongoza sala ya jamaa. Hata aliingilia kati wakati anatoa hotuba na kuanza kucheza nao kama waliingia msikitini. Walipokuwa na yeye; alisahau matatizo yote ya nchi na serikali. Walimpa furaha kubwa sana nyakati zile walipokuwa naye.

Na inaonyesha kama vile hangeweza kuwapa sifa za juu zaidi wao na mama yao. Kwa hiyo, hili ni jambo la udadisi wa kihistoria kwa nini hakuwataja Zaynab, Rukayya, na Ummu Kulthum wakati wowote ule. Wazazi huwapa watoto wao wote mapen-zi hayo hayo, na hawafanyi ubaguzi wa aina yoyote. Lakini ikiamuli-wa kwa kupitia hadithi na maandishi ya historia ya wakati huo, Mtume wala hakuwa na habari kwamba palikuwepo na wanawake watatu waitwao Zaynab, Rukayya na Umm Kulthum wakiishi.

Kwa upande wa mjumbe wa Mwenyezi Mungu, miaka ya huko Makka baada ya kutangazwa kwa Uislamu, ilijaa hatari. Kila siku ilikuwa na hatari zake na changamoto mpya kwake. Na bado, Rukayya na Umm Kulthum kamwe hawatajwi kama walimtumikia baba yao wakati wowote ule. Kwa upande mwingine, binti yake, Fatima Zahra, alimsaidia yeye, Makka na Madina, kwenye dharura mbalimbali. Wote wawili, Rukayya na Umm Kulthum walimzidi Fatima kwa umri. Wangelazimika kumliwaza baba yao pale alipoonewa na wapagani Mjini Makka au alipoumizwa vitani Madina. Lakini kamwe hawakufanya hivyo. Ukweli uliofanywa udhihirike kwa njia zote mbili kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu na kwa mantiki ya historia, ni kwamba, Zaynab, Rukayya na Umm Kulthum hawakuwa watoto wa Muhammad Mustafa na Khadija.

Suala la umri, madai ya ndoa tatu na idadi ya watoto wa Khadija, si jambo ambalo humo imani ya Uislamu inategemea, sivyo kabisa. Lakini Mwislamu lazima awe na msimamo kuhusu ukamilifu wa historia. Khadija alikuwa mfadhili mkuu wa Uislamu na Waislamu. Kiasi angalau kidogo ambacho Waislamu wanaweza kufanya katika kuthibitisha shukurani zao kwake, si kupindisha ukweli na kusingizia mambo ya historia. Ukweli lazima ushikiliwe kwa gharama yoyote ile, ama iwape faida au iwaumize rafiki na maadui. Mtu anaweza kuwa na yoyote ya kuonyesha utii wake kwa mashujaa wake, na kupenda kufanya hivyo kwa mashujaa, kunaweza kumshawishi kuwatukuza wao. Lakini kama yeye ni Mwislamu, lazima ajizuie kufanya hivyo kwa sababu atavuruga ukweli. Kama akifanya, atastahili kupambana na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ambaye anasema kwenye kitabu chake:

وَلَا تَلْبِسُوا الْحَقَّ بِالْبَاطِلِ وَتَكْتُمُوا الْحَقَّ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٤٢﴾

"Wala msichanganye haki na batili, mkaficha haki, na hali mna-jua." (Qur'ani 2:42).

وَلَا تَكْتُمُوا الشَّهَادَةَ وَمَن يَكْتُمْهَا فَإِنَّهُ آثِمٌ قَلْبُهُ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ ﴿٢٨٣﴾

"Wala msifiche ushahidi. Na atakayeficha basi hakika moyo wake ni wenye kuingia dhambini. Na Mwenyezi Mungu huyajua (yote) mnayoyatenda." (Qur'an 2:283).

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن كَتَمَ شَهَادَةً عِندَهُ مِنَ اللَّـهِ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴿١٤٠﴾

"Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule afichaye ushahidi alio nao utokao kwa Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika na hayo mnayoyafanya" (Qur'an 2:140).

إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَىٰ مِن بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ أُولَـٰئِكَ يَلْعَنُهُمُ اللَّـهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ ﴿١٥٩﴾

"Hakika wale wanaoficha tuliyo yateremsha - nazo ni hoja zetu zilizo wazi na uongozi baada ya sisi kuzibainisha kwa watu kitabuni - hao anawalani Mwenyezi Mungu na wanawalaani (kila) wenye kulaani. (Qur'an 2:159).

Mwenyezi Mungu amewaamuru Waislamu kuthibitisha na kuonyesha shukrani kwa kutendewa fadhili Naye.

وَأَمَّا بِنِعْمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثْ ﴿١١﴾

"Na neema ya mola wako isimulie (kwa kushukuru na kwa kufanya amali njema." (Qur'ani 93:11).

Kama Waislamu ni waaminifu katika kuonyesha shukurani zao kwa Khadija, ni lazima waharibu uwongo, yaani hadithi ya maisha yake. Uwongo huu umekuwa ukisambaa kwa muda mrefu mno. Hakuna njia bora zaidi ya Waislamu kukariri na kutangaza ukarimu wa Mola kama kuheshimu ukweli - kweli yenyewe. Kwa kuheshimu Ukweli, pia wata-fuzu kupata radhi za Mwenyezi Mungu (s.w.t) Khadija alikuwa mtumishi aliye pendwa sana na Mwenyezi Mungu, na alikuwa mke wa kwanza wa rafiki yake na mjumbe, Muhammad Mustafa. Alikuwa wa pekee, hangeweza kulinganishwa na yeyote, na alikuwa maalum kwa Mwenyezi Mungu ambaye alipeleka salaamu zake kwake kupitia kwa malaika mkuu Jibril! Mwenyezi Mungu na amridhie Mtumishi wake, Khadija.

Aya zifuatazo za Qur'an Majid zimeelekezwa kwa watumishi wa Mwenyezi Mungu waaminifu na wapenzi, ambao hutanguliza radhi Zake kabla ya zao. Na wote ambao hutafuta radhi Zake katika kujitoa kumtumikia Yeye na Uumbaji Wake. Khadija alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mstari wa mbele kabisa miongoni mwa watumishi wa Mwenyezi Mungu. (Kwa nafsi ya mtu mwema itasemwa)

يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ ﴿٢٧﴾ ارْجِعِي إِلَىٰ رَبِّكِ رَاضِيَةً مَّرْضِيَّةً ﴿٢٨﴾ فَادْخُلِي فِي عِبَادِي ﴿٢٩﴾ وَادْخُلِي جَنَّتِي ﴿٣٠﴾

"Ewe Nafsi yenye kutua rudi kwa mola wako, hali ya kuwa utarid-hika (kwa utakayopata), na (Mwenyezi Mungu) aridhike na wewe. Basi ingia katika (kundi la) waja wangu (wazuri), uingie katika Pepo yangu. (Qur'an 89:27-30).

Mwenyezi Mungu Amrehemu Khadija na aweze kumnyanyua na kumpa daraja la juu zaidi katika wote wenye mamlaka miongoni mwa watumishi wake wa kweli na rafiki waaninifu.

Mwenyezi Mungu na Amrehemu Muhammad Mustafa na Ahlul-Bayt. Kupitia kwake mwanadamu alipokea neema ya nuru ya Uislamu. Kujitolea mhanga kwa Khadija katika kuutumikia Uislamu si rahisi kulinganishwa. Kujitolea huko kuliingiliana na misingi ya Uislamu. Kujitolea huko kuliimarisha umbo la Uislamu hivyo kwamba haikuwa rahisi kuuharibu. Kujitolea kwa Khadija kumepewa sifa bora na nyingi kushinda za mtu mwengine yeyote ambaye alifanya kitu chochote kwa ajili ya Uislamu. Aliufanya Uislamu uweze kujitegemea kwa kujitolea kwake mno. Kuna uwiano wa wazi baina ya kumuunga mkono mume wake na ushindi wa Uislamu kijamii, kiuchumi na kisiasa. Hapana yeyote ambaye anaweza kuwajibika kwa ustadi, mapenzi, uthabiti, wepesi wa kuelewa na kugun-dua. Kujishughulisha, na kipaji kwa kiwango hicho alichofanya yeye.

Kujitolea kwa Khadija kulileta mafanikio mazuri baada ya kifo chake. Uislamu ulipata ushindi baada ya mapambano na upagani ya muda mrefu. Maadui wa Uislamu waliangamizwa, wakana Mungu wenye kiburi wa ukoo wa Umayya walidhalilishwa na itikadi yao ya kipagani ilivunjwa. Khadija alikuwa miongoni mwa watu muhimu walio fanikisha imani ya kumpwekesha Mungu kushinda ushirikina, imani ya kiroho kushinda tamaa ya mali, na Uislamu kushinda upagani hata pamoja na kwamba historia ya yale aliyo yafanya wakati wa migongano, kwa kipindi kire-fu, imekuwa haifahamiki. Historia hiyo imebakia inaeleweka nje ya dhamira za Waislamu walio wengi. Mwaka A.D. 630 Muhammad Mustafa. aliingia Makka kama mshindi. Yeye na binamu yake, Ali bin Abi Talib, waliingia ndani ya Al- Kaaba wakiwa na nembo ya Amri za Mungu alizompa Ibrahim na Ismail.

وَعَهِدْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ ﴿١٢٥﴾

".Na tulimwusia Ibrahimu na Ismaili (tukawaambia) "itakaseni Nyumba Yangu..." (Quran 2:125).

Muhammad na Ali waliikuta Nyumba ya Mungu katika hali mbaya sana; ilikwisha kuwa nyumba ya masanamu; kwa hiyo, ilibidi itakaswe. Kwa hiyo, kwa kuwaiga Ibrahim na Ismaeli - mitume waliotangulia -Muhammad na Ali waliyavunja masanamu yote na kuharibu mapicha yote ndani ya Al-Kaaba. Waliitakasa nyumba ya Mungu na wakarudisha utakatifu humo. Khadija angelilinganisha tendo hili la kurejesha utakatifu kwenye Kaaba, lililofanywa na mumewe na mkwe wake, kwa kutimia kwa matumaini na ndoto zake, na angefurahi na kujivuna. Na ni kiasi gani Muhammad Mustafa alilazimika kuhisi kwamba mke wake angekuwa naye, akiwa amesimama karibu naye, akaona na kushiriki kupata msisimko wa siku hiyo iliyoneemeshwa ambapo Al-Kaaba ilirejeshwa kwenye wakfu wa matumizi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, baada ya kupita karne nyingi ikiwa mikononi mwa wasioamini.

Tangu wakati Khadija aliposhahadia kwamba Mungu ni Mmoja, na Muhammad alikuwa Mjumbe Wake, aliyaweka maneno, matendo, maisha na kifo chake katika usawa wa mwelekeo mmoja kuafikiana na Radhi na utashi wa Mwenyezi Mungu, alipata Ushindi wa Juu Kabisa wa utakatifu wa maisha yake. Back cover Khadij atul-Kubra Khadija alikuwa mke wa kwanza wa Mtume Mkubwa wa mwisho wa Mungu kwa wanadamu wote - Muhammad Mustafa(s.a.w.w) . Wakati Mtukufu Mtume alipoanzisha harakati itwayo Uislamu, alijipatia sifa ya kuwa Mu'umin na Mwislamu wa kwanza.

Maisha ya Khadija yamejaa utajiri wa mwongozo wa kimungu. Sifa yake kubwa katika maisha yake ya kiutakatifu, ilikuwa ni imani yake isiyo na kifani katika Uislamu. Imani yake ilikuwa kama jabali katika bahari iliyochafuka.

Imani za watu wachache kamwe hazikuwekwa katika mtihani mkali kama ile imani ya Khadija. Imani yake ilijaribiwa kwa njaa, kiu, uhamisho na hatari kubwa katika maisha yake na kwa wapendwa wake. Kusema kweli, wakati wa kwanza wa mika kumi ya Uislamu, maisha yake yalikuwa ya mfululizo wa mitihani isiyo na mwisho. Khadija alifuzu katika mitihani yote. Ufunguo kwenye mafanikio yake ilikuwa ni upendo wake kwa Mungu, mapenzi kwa mume wake na kujituma kwake ili kuufanya Uislamu ufanikiwe.

Khadija aliweka mfano ambao wanawake katika Uislamu wanaweza kuuiga mpka mwisho wa dunia. Wanawake wanweza kuona katika maisha yake vipi mu'mun wa kweli anavyoweza kufanya tabia ya maisha yake kuwa bora sana na ya utukufu.

Mwenyezi Mungu Ambariki Khadija Na Familia Yake.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU