TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN12%

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
  • Anza
  • Iliyopita
  • 29 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 43988 / Pakua: 5500
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

DIBAJI YA AL-MIZAN

Katika kazi nyingine alizozifanya mfasiri mkubwa allama tabatabai Al-Mizan inachukuwa nafasi ya kwanza katika kutambuliwa, kwa sababu ya sifa zake zisizokuwa na kifani. Jambo hili si katika vitabu vyake tu bali ni katika vitabu vyote vya Kiislamu vilivyo andikwa kuhusu Dini, Sayansi, Falsafa, na hasa kuhusu aina zote za tafsiri ya Qur'an mpya ama zamani zilizoandikwa na Sunni ama Shia. Maelezo haya hayawezi kueleza kwa urefu mambo yaliyomo lakini yanaweza kuwasaidia wasomaji kwa kuwapa fununu juu ya umaridadi wa Al Mizan. Ninaona kwamba sistahili kuifanya kazi kubwa kama hii kama watu wakubwa mfano Ayatullah Mutahhari ambaye yeye mwenyewe ni mtu mwenye fikra mpya, mjuzi wa Qur'an na mfasiri vile vile, aliposema: "Al- Mizan ni tafsiri kubwa zaidi ya Qur'an iliyowahi kuandikwa tangu kuanza Uislamu; na itachukua miaka sitini ama mia moja mpaka watu wetu kuutambua umuhimu wa Al-Mizan ya Allama Tabatabai. "Wanachuoni wengine, wajuzi na watu walio na busara walitoa maoni kama haya kuhusu kitabu hiki. Majaribio yoyote ya kuonyesha maana ndani ya Al- Mizan hata kama ni kwa njia ya juujuu, katika maelezo mafupi kama haya, ni kama kujaribu kuitia bahari ya Atlantiki katika chungu kidogo.

Hata hivyo ninatarajia kukusanya matone machache katika bahari hii ya elimu ya Kiislamu kulingana na uwezo wangu ili nitosheleze kiu yangu. Nataraji roho njema ya mwandishi mcha Mungu wa kitabu hiki cha milele, itaniwia radhi kwa kazi hii ndogo nitakayoitanguliza.

Historia Ya Al-Mizan Kabla ya kugusia zile alama zinazoipambanua tafsiri hii na nyinginezo, tutaandika historia fupi ya Al- Mizan. Allama Tabatabai, aliyekuja katika hawzah ya Qum mwaka wa 1325 A.H aliandika na akatoa hotuba kuhusu matawi mbali mbali ya elimu za Kiislamu. Tafsiri na maelezo ya Qur'an lilikuwa ni somo moja katika mazungumzo yake, aliyoyafanya na wanachuoni na wanafunzi na "Hawzeh Ilmiyyah" ya Qum. Kuhusu azimio lake la kuandika Al- Mizan, Allama Tabatabai alisema kwamba, alipokuja Qum kutoka Tabriz alijaribu sana kutathmini mahitaji ya jamii ya Kiislamu, na vile vile alzingatia hali iliyokuwapo katika Hawzah Ilmiyyah ya Qum. Baada ya kulizingatia jambo hili, suluhisho lilikuwa, shule ile ilihitaji maelezo ya Qur'an ili waweze kuielewa vyema na kuzifahamu sharia zake na vilevile kuyaelewa maana halisi ya vitabu vyote vya Kiislamu na maandishi yote yaliyo na vipaji vikubwa.

Kwa upande mwingine kwa vile nadharia za mada zilikuwa zikipata nguvu siku hadi siku, palikuwa na haja kubwa ya kupata hoja za kiakili na kifalsafa ili kuiwezesha Hawza kukabiliana na hali mpya na kuchambua misingi ya kifikra na imani ya Uislamu, pamoja na msaada wa hoja za kiakili ili kutetea maoni ya Uislamu. Basi aliona ni jukumu lake kufanya juhudi ili ayatimize mambo haya mawili muhimu kwa msaada wa Mwenyezi Mungu aliye Mtukufu zaidi. Alipanga masomo ya tafsiri ya Qur'an kwa mpango huu. Pengine Alama Tabatabai alitoa masomo ya Qu'ran nzima kwa wanafunzi kwa mara nyingi na huku akiandika yale aliyofundisha. Wakati wa darasa hizi zilizoandaliwa vizuri kwa undani wa fikra, pengine, alitoa vikao hivi vya masomo kwa ufasaha , na baadae yalichapishwa katika mijalada ya vitabu.

Uchapishaji wa kwanza wa Al - Mizan ambao ulikuwa katika lugha ya Kiarabu ulifanyika Iran na ilirudiwa kuchapishwa huko Beirut. Mpaka wakati huu, zaidi ya chapa tatu zimechapishwa huko Iran na Beirut kwa idadi nyingi zaidi. Ni Maktaba chache za watu binafsi na za serkali ambazo hazina seti kamili ya Al Mizan. Vile vile maktaba zote zinayo baadhi ya majalada ya tafsiri hii juu ya rafu zao. Kitabu cha asili cha Al Mizan ambacho kinakusanya majalada ishirini kiliandikwa katika lugha la Kiarabu. Kila mjalada una kurasa mia nne. Ilikusudiwa kwamba watu wote waliyopenda kusoma tafsiri ya Qur'an, wawe watapata faida ya kutosha kutokana na mafundisho ya Quran. Baadhi wa wanafunzi wa Allama Tabatabai walikifasiri kitabu hiki katika lugha ya Kifursi chini ya uongozi na usimamizi wake. Kila mjalada mmoja wa lugha ya Kiarabu ulifasiriwa katika mijalada miwili ya lugha ya Kifursi na idadi ya mijalada hii ikawa arobaini. Jukumu hili lilichukuliwa na Syed Muhamad Baqir Musawi Hamadani. Ili tafsiri ya Al Mizan iliyokuwa katika lugha ya kifursi isionekane tofauti, jambo ambalo lingeharibu usomaji wa kitabu hicho, Allama Tabatabai alimpa mijalada ya mwanzo ya Al Mizan kuifasiri tena.

Ni lengo letu kwamba tafsiri hii ya maneno matukufu ya Qur'an itafasiriwa katika lugha nyengine pia, ili iwe rahisi kwa wale wanaotaka kuondoa kiu ya elimu tukufu na kwa wale wanaotaka kuzijua sheria za Kiislamu zenye kuokoa maisha. Ingekuwa bora tafsiri hii kufanywa na watu na wanachuoni ambao wanaijua vyema lugha ya Qur'an. Ingekuwa ni kazi nzuri kama ujumbe wa Qur'an Tukufu ungetolewa katika njia hii ili uwafikie binadamu na kuwaokoa na mila za makafiri. Elimu ya kumwabudu Mwenyezi Mungu katika Qur'an humwepusha binadamu na aina zote za aibu na utumwa.

Alama Zinazoipambanua Tafsiri Ya Al Mizan: Al Mizan inakusanya aina mbali mbali za elimu: kama vile ya Sayansi, Ufundi, Usanifu na Uzuri. Vile vile Falsafa, Elimu ya Adabu (literature), Historia, Elimu ya Jamii na Elimu ya Hadithi (za Mtume(s.a.w.w) Mambo matatu kati ya haya hayako wazi wakati mengine yanahusiana nayo.

1. Tafsiri Ya Qur'an Kwa Qur'an: Allama Tabatabai katika maelezo yake juu ya Qur'an kwanza anonyesha asili ya kuingiliana kwa aya mbalimbali, na vile vile kusibitisha kwamba, kwa sababu hii ya kuingiliana kwa aya, aya hizi hufasiriana na kujieleza zenyewe. Kwa maneno mengine Allama Tabatabai anaonyesha kwamba baadhi ya sehemu ya Qur'an hufasiri sehemu nyingine.

Ili kuzielewa aya tukufu za Qur'an na Tafsiri zake ni lazima tutafute msaada kutoka katika Qur'an yenyewe. Alizungumzia tatizo la tafsiri ya Qur'an katika kitabu chake " Qur'an dar Islam" (Mahali pa Qur'an katika Uislamu). Baada ya kufafanua jambo hili; Allama Tabatabai alisema ' kwamba tafsiri sawa ya Qur'an inawezekana kupitia kufikiria kwa makini na kushauri aya nyingine kuutazama mwongozo wa aya za Qur'an. Kwa maneno mengine, zipo njia tatu ambapo njia yoyote kati yake iko wazi kwetu kuitumia katika tafsiri ya sawa ya aya.

1.Tafsiri ya aya zozote bila ya kuhusisha maana ya aya nyinginezo; na kwa msaada wa maelezo ya elimu maelezo za Sayanzi tuliyo nayo; au pasi na elimu hizo.

2. Tafsiri ya aya ikiwa na mwongozo na Hadith, ikichukuliwa kutoka kwa mmoja wa Ma'sumin(a.s) , inayofuatia aya.

2. Tafsiri ya aya kwa kufukiria kwa makini maneno na maana ya aya kwa kutumia msaada wa aya zinazohusika. Vile vile kutafuta ushauri katika Hadith mahali inapopasa. Njia ya tatu ndiyo iliyoelezewa katika sura iliyopita (nayo ni mahali pa Qur'an katika Uislamu). Hii ndiyo njia aliyoitumia Mtume(s.a.w.w) na Maimami(a.s) , kama tunavyosoma katika mafundisho yao. Mtume(s.a.w.w) alisema: "Aya nyengine huzungumzia baadhi ya aya nyengine na baadhi yake huzithibitisha nyengine."

Allama huyu mwisho anatukumbusha jambo muhimu; nalo ni kwamba, Qur'an hutafasiriwa kwa Qur'an. Siyo kwa maoni ya mfasiri - njia ambayo imekataliwa na Hadith mushuhuri ya Mtume(s.a.w.w) . Mwisho Allama Tabatabai anazifananisha na kuzieleza njia hizi tatu za tafsiri, kwa urefu. Kisha anasema, njia ya tatu ndiyo njia bora ya kuifahamu Qur'an kulingana na majadilano ya Qur'an na uthibitisho wa hadith. Mwisho wa sehemu hii ya mazungumzo anatuonyesha mfano na tafsiri ya Qur'an kwa Qur'an ambao hatuwezi kuonyesha hapa kwa ajili ya kufupisha. Al-Mizan inaonyesha jambo muhimu la kuzielewa sifa za miujiza ya Qur'an tukufu kufanana na kuingiliana kwa ya zake.

2. Upande Wa Kijamii:

Tafsiri zote za Qur'an kwa uchache ama kwa wingi zimejadili mambo muhimu kuhusu mazingira ya jamii, lakini Al-Mizan haina mfano ikifafanishwa na tafsiri myengine. Mijadala ya kuhusu jamii iliyomo katika Al-Mizan ina kina kikubwa sana cha thamani kwa wingi. Kwa namna alivyoitazama migawanyiko mingi na matatizo ya kijamii, Allama Tabatabai alifaulu kuyatatua kwa kutumia aya za Qur'an. Ametoa mwangaza mpya kuhusu baadhi ya matatizo hAya Na kijamii kwa maoni ya Qur'an, matatizo ambayo mpaka kufikia wakati huu yalikuwa yamepuuzwa. Allama Tabatabai amefungua ukumbi mpya kwa wasomaji walio na ari ya kuvumbua sehemu mpya katika maana ya Qur'an tukufu.

3. Upande Wa Falsafa:

Allama Tabatabai ambaye ni mwanafalsafa mwenye mwelekeo wa mustakbali na usanii nadra na wa asili, alifanya kazi kubwa katika elimu ya tafsiri, kufafanua ughaibu wa Qura'n, jambo ambalo linatupa uoni mkunjufu na wenye faida katika kufahamu bara bara maisha ya ughaibu Aliyakanusha makosa yote yasiyo na msingi yaliyotolewa katika Qur'an. Kwa maoni yake, ughaibu wa Uislamu una mizizi yake katika Qur'an, nayo ni ufafanuzi wa Qur'an kuhusu Mwenyezi Mungu, binadamu na ulimwengu. Allama Tabatabai vile vile anaonyesha kwamba ada ya kuogopa kuzungumzia mambo ya ughaibu (yasiyoonekana), inatokana na ukosefu wa kufahamu mambo hayo na kutokuwa na habari sahihi kuhusu mambo hayo.

Katika vitabu vyake kama vile Usul-e-Falsafa wa Rawish-e-Riyalism (Misingi ya falsafa na utaratibu wa madhehebu ya ukweli), maelezo juu ya kitabu kiitwacho Al-Asfar cha Mulla Sadra, katika makala mbili za (Bidayat, Al-Himah, na Nihayat, al-Hikmah), alieleza na kuyasawazisha makosa yote juu ya asili ya ughaibu. Katik Al-Mizan amezungumza masuala hAya Na a falsafa kadhaa za kifalsafa kutokana na aya hizo. Hili ni jambo ambalo halina mfano katika historia ya tafsiri ya Qur'an. Katika kutafsiri kwake aya za Qur'an na kuelezea uhusiano wake na fikra za ughaibu, alionyesha uthabiti wa Qur'an na vile vile kuonyesha upuuzi na ukosefu wa msingi wa falsafa ya mada. Sehemu hii ya tafsiri yake ni ya asili na vile vile ni mpya katika uwanja wa masomo ya falsafa. Mijadala yake hii ina undani wa maana ulio nadra, usahihi na ustadi ambao utaendelea kuwavutia wasomi katika siku za usoni.

Katika Juzuu Ama masomo mabili mbali ambayo yanazungumzwa kulingana na Sura ni

1. Mazungumzo kuhusu maumbile ya binadamu kutoka katika Qur'an.

2. Mazungumzo kuhusu viapo katika Qur'an orodha ya vitu ambavyo Mwenyezi Mungu anaapia katika kitabu kitukufu.

3. Mazungumzo kuhusu maana ya Roho (Ruh) katika Qur'an.

4. Mazungumzo kuhusu vipi malaika wanafanya kazi kama mawakili katika hali ya maisha.

Mwisho ni lazima nikiri kwamba maarifa yangu machache ambayo huenda yameathiri katika kufahamu undani wa na upana wa fikra za historia zilizomo katika Al-Mizan, yametia kasoro na dosari kubwa. Allah aiweke pema roho ya Allama Tabatabai kwa kazi yake kubwa aliyoifanya.

Abu-Al-Qasim Razzaqi

Kwa Wasomaji Sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa uwezo wa kutafsiri tafsiri hii ya Qur'an iliyoandikwa na mwanachuoni mkubwa Bwana Muhammad Hussein Tabatabai. Ni lazima ieleweke kwamba haikuniwiya rahisi kazi hiyo hasa kwa kuzingatia undani na upana wa fikra za mwanachuoni huyo. Ugumu zaidi ulikuwa pale niliposhindwa kupata maneno ya Kiswahili yatakayotoa maana halisi yaliyokusudiwa jambo ambalo limenilazimisha kuacha baadhi ya ibara hasa zile za kanuni za lugha ya Kiarabu (Nahwu). Hata hivyo nimejitahidi kugusia kila ambacho ni muhimu katika tafsiri hiyo. Kwa vile tafsiri hii imeelezewa kwa undani sana na kwa njia ya kifalsafa, jambo ambalo pengine halikuzoeleka kwa vitabu vya dini vilivyoandikwa kwa Kiswahili, basi ndugu msomaji nawe itakubidi uisome kwa undani na wala sio kuipitia juu juu. Pengine itakubidi urudierudie baadhi ya ibara.

Ndugu msomaji ikiwa macho yako utayafungua kwenye makosa tu, na kuyafumba kwenye usawa na faida, basi ninakwambia Mungu akusamehe na aniongoze mimi na wewe. Hata hivyo sina maana ya kukukataza kunikosoa, bali ninakuomba hasa ufanye hivyo na Inshallah Mwenyezi Mungu atakulipa kwa nia yako. Kwani walikwishasema wahenga : "Binadamu si kamili". Shukrani: Shukrani zangu za dhati ziwaendedd London Islamic Foundation kwa kujitolea kuisimamia na kuigharimia kazi ya kukichapisha kitabu hiki. Pia shukrani nyingi zimwendee Sheikh Islam Khiyar Islam kwa taabu kubwa aliyoichukuwa ya kusahihisha kitabu hiki. Na wengineo ambao kwa namna moja au nyingine wamechangia kukitayarisha kitabu hiki; Mungu awajaze heri ya dunia na akhera (Amin).

Desemba 1988 Hassan Ali Mwalupa

1

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURAT NABA (HABARI)

SURAT NABA (HABARI) (NA. 78) INA AYA 40

Aya ya 1 -16

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

عَمَّ يَتَسَاءَلُونَ ﴿١﴾

1. Ni lipi wanaloulizana?

عَنِ النَّبَإِ الْعَظِيمِ ﴿٢﴾

2. Ni habari kubwa.

الَّذِي هُمْ فِيهِ مُخْتَلِفُونَ ﴿٣﴾

3. Ambayo wao wanahitalifiana.

كَلَّا سَيَعْلَمُونَ ﴿٤﴾

4. Si hivyo! Karibu watajua.

ثُمَّ كَلَّا سَيَعْلَمُونَ ﴿٥﴾

5. Tena si hivo! Karibu watajua.

أَلَمْ نَجْعَلِ الْأَرْضَ مِهَادًا ﴿٦﴾

6. Jee, Hatukuifanya ardhi kuwa ni tandiko?

وَالْجِبَالَ أَوْتَادًا ﴿٧﴾

7. Na majabali kuwa ni vigingi?

وَخَلَقْنَاكُمْ أَزْوَاجًا ﴿٨﴾

8. Tukawaumba nyinyi wanawake na wanaume?

وَجَعَلْنَا نَوْمَكُمْ سُبَاتًا ﴿٩﴾

9. Tukaufanya usingizi wenu ni raha?

وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ لِبَاسًا ﴿١٠﴾

10. Tukaufanya usiku ni sitara?

وَجَعَلْنَا النَّهَارَ مَعَاشًا ﴿١١﴾

11. Tukaufanya mchana ni (wa kutafutia maisha)?

وَبَنَيْنَا فَوْقَكُمْ سَبْعًا شِدَادًا ﴿١٢﴾

12. Tukajenga juu yenu mbingu saba madhubuti?

وَجَعَلْنَا سِرَاجًا وَهَّاجًا ﴿١٣﴾

13. Tukaufanya na taa yenye kung'aa?

وَأَنزَلْنَا مِنَ الْمُعْصِرَاتِ مَاءً ثَجَّاجًا ﴿١٤﴾

14. Tukateremsha kutoka mawinguni maji yenye kububujika?

لِّنُخْرِجَ بِهِ حَبًّا وَنَبَاتًا ﴿١٥﴾

15. Ili kwayo, tutoe nafaka na mimea.

وَجَنَّاتٍ أَلْفَافًا ﴿١٦﴾

16. Na mabustani yenye kushindamana.

UBAINIFU

Sura inakusanya habari za kuja siku ya kupambanuliwa hukumu, na kuitolea hoja kwamba ni kweli, haina shaka. Imeanzia na kuuliza kwao habari yake; kisha ikataja katika mpangilio wa jawabu na kuogopesha kwamba wao watajua. Kisha imetoa hoja ya kuthibiti kwake, kwa kuonyesha nidhamu inayoonekana katika ulimwengu, kutokana na yaliyomo ndani yake, katika mipangilio ya kihekima, yenye dalili waziwazi, kwamba baada ya umbile hii lenye kubadilika na kuzunguuka, kuna umbile lenye kuthibiti na kubakia, na kwamba baada ya nyumba hii yenye kazi bila malipo, iko nyumba yenye malipo bila kazi basi iko siku itakayobainishwa nidhamu hii.

Kisha inasifu siku watakapo hudhirishwa watu, na kugeuka wale wanaopetuka mipaka kwenye adhabu chungu na wenye kumcha Mwenyezi Mungu kwenye neema za kudumu, na yanaishia maneno kwa kuonya. Sura imeshuka Makka kwa ushaidi wa mpangilio wa aya zake.

Aya Ya 1

Kuulizana hapa, ni kwa maana ya kuulizana baadhi yao kwa baadhi nyengine, au ni kuuliza baadhi yao baada ya wengine ijapokuwa mwenye kuulizwa ni mwengine, kwa hiyo ama walikuwa wakiulizana baadhi yao baada ya baadhi nyengine walikuwa wakimuuliza Mtume(s.a.w.w) kuhusu jambo. Ilivyokuwa mpangilio wa jawabu una maonyo zaidi na makamio, inatilia nguvu kuwa wenye kuulizana ni makafiri wa Makka katika wanaomshirikisha Mungu waliokanusha Utume na Marejeo. Kuulizana kwa wanaomshirikisha Mungu, na kukuelezea huko kuulizana kwao, kwa njia ya swali ni kufahamisha udhaifu wake, kwa kuwa jawabu la swali liko wazi.

Aya Ya 2-3

Makusudio ya habari kubwa ni habari ya ufufuo na Kiyama ambayo Qur'an imetilia umuhimu katika Sura zilizoshuka Makka, hasa zile sura zilizoshuka mwanzo mwanzo. Mpangilio huo unatilia nguvu kutokana na maelezo yake ya sifa za siku ya upambanuzi na hoja zilizotangulia kuwa siku hiyo ni kweli kutukia kwake. Imesemwa kuwa habari kubwa ni Qur'an tukufu.

Pia imsemwa habari kubwa ni vile walivyokuwa wakihitalifiana katika kuthibitisha mtengenezaji na sifa Zake, Malaika, Mitume, Ufufuo, Pepo na Moto n.k.

Anayesema haya amezingatia yaliyo katika Sura kuonyesha uhaki wa yote yaliyo katika mlingano wa Kiislamu. Yote hayo yanapingwa kutokana na kuwa ishara ya yote hato ni katika sharti za sifa ya siku ya ufufuo yenye kukusanya mafungu ya itikadi ya haki na amali njema, ukafiri na makosa. Zaidi ya hayo ni kuwa hawa wenye kuulizana ambao ni washirikina wanathibitisha mtengenezaji na Malaika na wanakanusha yaliyotajwa.

Kusema kwake "ambayo wanahitalifiana" Ni kwamba walihitalifiana katika upande wa kukataa, na wanaafikiana kuikanusha. Baadhi yao walikuwa wakiona kuwa ni muhali kama anayosema Mwenyezi Mungu: "Na walisema wale ambao wamekufuru (kuambiana wenyewe kwa wenyewe): "Je, tuwajulishe mtu anayewaambia ya kwamba mtakapochambuliwa vipande vipande (makaburini) kuwa atakuwa katika umbo jipya?! " (34:7)

Wengine walikuwa wakiiweka mbali na kuikanusha. Kama walivyosema: "Je, anawaahidi ya kwamba mtakapokufa na mkawa udongo na mifupa kuwa mtatolewa. Hayawi! Hayawi! Hayo mnayoahidiwa ." (23:35-36). Wengine walikuwa wakiitia shaka na kukanusha: anasema Mwenyezi Mungu: "Kwani imefikia wapi elimu yao (kujua) akhera (hata wanauliza Kiyama?) Bali wao wamo katika shaka nayo, bali wao ni vipofu nayo." (27:66) Na wengine walikuwa na yakini lakini hawaamini kwa inadi tu. Kwa hiyo wanakanusha, kama vile ambavyo hawaamini Tawhid, na Utume, baada ya kutimia hoja; Mwenyezi Mungu anasema: "Bali wao wanaendelea tu katika uasi na chuki ." (67:21)

Maana inayopatikana katika mpangilio wa aya tatu na zinazofuatia, ni kwamba wao waliposikia vile Qur'an inavyowaonya kuhusu jambo la ufufuo na malipo siku ya upambanuzi, waliliona zito hilo, ndipo wakawa wanaulizana kuhusu habari hii ya ajabu ambayo inagonga masikio yao mpaka leo. Walikuwa wakimrudia Mtume(s.a.w.w) na waumini, kuwauliza sifa ya hiyo siku, kwamba kitakuwa lini hicho kiaga mkiwa mnasema kweli? Na huenda walikuwa wakirudiana wao wenyewe katika baadhi ya waliyogonga masikio yao katika hakika za Qur'an. Ameishiria Mwenyezi Mungu katika Sura hii kisa cha kuulizana kwao kwa njia ya swali na jawabu, akasema: "Ni lipi wanaloulizana?" Kisha akasema: "Ni habari kubwa ambayo wao wanahitalifiana." Hilo ni jawabu na maelezo ya kile wanachoulizana. Kisha akasema: "so hivyo! Karibu watajua" na ni hilo ni jawabu la kuulizana kwao.

Wafasiri wana njia nyingi kuhusu tafsiri ya matamko ya aya hizo tatu; tumeziacha kwa kutoafikiana kwake na mpangilio. Yale tuliyoyaleta ndiyo yanayoafikiana na mpangilio wa maneno.

Aya Ya 4-5

Ni kupinga kuulizana kwao; yaani na wakome kuulizana, kwa sababu watafunukiwa kwa kutokea habari hii na wataijua. Katika ibara hii kuna utisho, kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu: "Watajua wafanyao dhuluma ni mgeuko gani watakaogeuka " (26:227).

Kurudia tena maneno hayo katika aya ya (5) ni kutilia mkazo kukataza na utisho. Ufahamisho wa utisho ni kuonyesha kuwa wenye kuulizana ni washirikishaji wanaokanusha ufufuo na malipo, kinyume cha waumini na washirikishaji wengine.

Aya Ya 6

Kuanzia aya hii mpaka aya ya 11 ni mfumo wa kutoa hoja juu ya kuthibiti ufufuo na malipo na kuhakikika habari hii kubwa. Kuthibiti kwa habari hiyo kubwa kunalazimisha usahihi wa neno la Mwenyezi Mungu "Watajua" linaloelezea kwamba wao watashuhudia siku hiyo, hivyo watajua. Uthibitisho wa hoja ni kuwa ulimwengu huu tunaouona, pamoja na ardhi yake na mbingu yake, pia usiku wake na mchana wake, pamoja na watu wanaozaana, nidhamu yenye kupita katika hayo, mipangilio iliyotengenezwa kwa ustadi kabisa, ni muhali kuwa yote hayo ni mchezo usiokuwa na lengo lenye kuthibiti na kubakia. Kwa hiyo ni lazima kwa nidhamu hii yenye kugeuka geuka ifuatiwe na ulimwengu wenye nidhamu yenye kuthibiti na kubakia, ije na kubakia, ije idhihiri athari ya kutengemaa kunakopendelewa na maumbile ya mtu, na vile vile uje udhihiri ufisadi unao katazwa. Kwani katika ulimwengu wetu huu tunaouona, hakudhihiri wema wa wamchao Mwenyezi Mungu uovu wa mafisadi.

Ni uhali kwa Mwenyezi Mungu kutoa umbile linalolingania kufuata silika au kukataza kwenye jambo ambalo haliathari na wala lisitokee. Basi iko siku itakayomfikia mtu na kulipwa katika siku hiyo amali yake, ikiwa ni kheri na ikiwa shari ni shari. Aya hizi ziko katika maana ya aya zinazosema:

"Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake bure. Hiyo ni dhana ya wale waliokufuru. Basi adhabu kali ya moto itawathubutikia wale waliokufuru. Je tuwajaalie wale walioamini na kutenda mema kuwa sawa na wafanyao ufisadi katika ardhi? Au tuwajalie wacha Mungu kuwa sawa na waovu? " (38:27-28).

Kwa ubainifu huu inathibiti kwamba iko siku ya malipo. Kwa hiyo hakuna haja kwa wanaomshirikisha Mungu kuhitalifiana na kutiliana shaka, ikiwa kundi jengine linaona ni muhali, jengine haliamini kwa inadi. Basi siku hiyo ni lazima kutokea na malipo, hakuna shaka. Baadhi wamesema kuwa aya hizi ziko katika mfumo wa kuthibitisha uwezo na kwamba marejeo yanaanzia mwanzo; Mwenye kuweza kuanzisha pia anaweza kurejesha. Hoja hiyo ingawaje ni kamilifu na imetokea katika maneno yake Mwenyezi Mungu, lakini ni hoja ya kueleza uwezekano na sio kutukia. Na mfumo tulionao sisi ni mfumo wa kutokea hasa na wala sio kuwezekana. Hivyo yenye kunasibiana zaidi ni yale tuliyoyatanguliza kuyafafanua.

Vyovyote iwavyo maana ya aya ya (6) ni kuwa: tumefanya ardhi ni kituo chenu cha kutulia na kuitumia.

Aya Ya 7

Huenda yamehisabiwa majabali kuwa ni vigingi kutokana na kuwa majabali yanatokana na kazi ya volcano. Kwa kupasuka ardhi, na kutoka vitu katika ardhi vilivyoyeyuka vinasimama kwa kulundikana kwenye mdomo wa shimo lililopasuka kama kigingi kilichosimamishwa. Chini yake kunakuwa na mchemko wa volcano ambao unanyanyua sehemu ya ardhi kutokana na kutetemeka. Baahi wamesema kwamba makusudio ni kujaalia vigingi ni nidhamu ya masiha ya watu duniani kutokana na manufaa yake na lau si hayo majabali, basi ardhi ingeliwayumbisha yumbisha yaani wasingeliweza kunufaika. Laikini kuiacha dhahiri ya tamko bila dharura hakufai.

Aya Ya 8

Yaani tumewaumba mume na mke ili kizazi kiendelee mpaka atakapotaka Mwenyezi Mungu.

Imesemwa kuwa makusudio yake ni maumbile yaani kila mtu ana umbile la mwenzake.

Pia imsemwa ni aina tofauti, kama weupe, weusi, wekundu, njano n.k. Vile vile imesemwa kuwa ni kuumbwa kwa manii ya aina mbili (ya mume na mke). Hizi ni njia dhaifu.

Aya Ya 9

Kuwa usingizi ni raha ni kwa kuwa unatuliza kiwiwili baada ya kuwa macho katika kutaabika kupitia matumizi ya nafsi. Imsemwa kuwa maana ya "Subata" ni kukata, kwamba usingizi unakata matumizi ya nafsi katika mwili. Maana hiyo iko karibu kuliko iliyotangulia. Imesemwa ni mauti na Mwenyezi Mungu amehisabu usingizi kuwa ni mauti aliposema: "Naye ndiye anayewafisha wakati wa usiku ." (6:60).

Lakini kauli hii iko mbali na maana ya aya hii, imehisabu usingizi kwa kuchukua roho lakini haikuuhisabu usingizi ni mauti kama inavyofafanua Qur'an sehemu nyengine: "Allah huchukua roho wakati wa mauti yake na zile ambazo hazijakufa (pia anazichukua) katika usingizi wake ." (39:42).

Aya Ya 10

Yaani unasitiri. Kutokana na giza lake, na hii ni sababu ya Mungu ya kuwataka watu wa ache harakati zao usiku na kuelekea nyumbani kwa watu wao. Baadhi wamesema makusudio ya kuwa usiku ni sitara nikuwa unasitiri mchana. Na kauli hayo ni kama unavyoina.

Aya Ya 11

Neno maisha linahusika na maisha ya wanyama; haiwezekani kusema maisha ya Mungu au ya Malaika. Maana ya aya nikuwa tumeufanya mchana ni wakati wa kutafuta maisha, kutafuta fadhila kutoka mola wenu.

Aya Ya 12:

Yaani mbingu saba zilizo madhubuti katika mjengo wake.

Aya Ya 13:

Makusudio ya taa yenye kuang'aa ni jua.

Aya Ya 14

Maana ya neno Mu'usirat ni mawingu ya mvua. Imesemwa ni pepo ambazo zinakamua mawingu ili inyeshe mvua.

Aya Ya 15

Nafaka hizo na mimea ni kwa ajili ya chakula cha binadamu na wanyama wengine.

Aya Ya 16

Inaungana na aya iliyotangulia. Kushindana ni kushindana kwa miti.

Utafiti Wa Hadith Katika baadhi ya habari zilizokuja ni kwamba habari kubwa ni Ali(a.s) . Katika Nahjul-Balagha, amesema Ali(a.s) : "Na ameuzuia mtingishiko wa ardhi yake kwa kupiga vigingi kwa majabali ."

Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu aya ya (10) amsema: Usiku unausitiri mcha. Huenda makusudio ya hadithi hiyo ni kuficha yanayodhihiri mchana.

2

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURAT NABA' (HABARI)

SURAT NABA' (HABARI)(NA. 78)

Aya 17 - 40

17. Hakika siku ya upambanuzi imewekewa wakati maalum.

إِنَّ يَوْمَ الْفَصْلِ كَانَ مِيقَاتًا ﴿١٧﴾

18. Siku itakayopulizwa parapanda, mje makundi makundi.

يَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ فَتَأْتُونَ أَفْوَاجًا ﴿١٨﴾

19. Na mbingu zifunguliwe, ziwe milango.

وَفُتِحَتِ السَّمَاءُ فَكَانَتْ أَبْوَابًا ﴿١٩﴾

20. Yaondolewe majabali yawe mlenge.

وَسُيِّرَتِ الْجِبَالُ فَكَانَتْ سَرَابًا ﴿٢٠﴾

21. Hakika Jahannam ni malindilizo.

إِنَّ جَهَنَّمَ كَانَتْ مِرْصَادًا ﴿٢١﴾

22. Ni marejeo kwa wenye kupetuka mipaka.

لِّلطَّاغِينَ مَآبًا ﴿٢٢﴾

23. Watakaa humo karne nyingi.

لَّابِثِينَ فِيهَا أَحْقَابًا ﴿٢٣﴾

24. Hawataonja humo raha wala kinywaji.

لَّا يَذُوقُونَ فِيهَا بَرْدًا وَلَا شَرَابًا ﴿٢٤﴾

25. Isipokuwa maji ya moto na usaha.

إِلَّا حَمِيمًا وَغَسَّاقًا ﴿٢٥﴾

26. Malipo yalitosawa (na makosa yao).

جَزَاءً وِفَاقًا ﴿٢٦﴾

27. Kwa sababu wao walikuwa hawaogopi kuhesabiwa.

إِنَّهُمْ كَانُوا لَا يَرْجُونَ حِسَابًا ﴿٢٧﴾

28. Wakazikadhibisha sana aya zetu.

وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا كِذَّابًا ﴿٢٨﴾

29. Na kila kitu tumekidhibiti kwa kukiandika.

وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ كِتَابًا ﴿٢٩﴾

30. Basi onjeni, hatutawazidishia ila adhabu.

فَذُوقُوا فَلَن نَّزِيدَكُمْ إِلَّا عَذَابًا ﴿٣٠﴾

31. Hakika wanaomcha Allah wana mahali pa kufuzu.

إِنَّ لِلْمُتَّقِينَ مَفَازًا ﴿٣١﴾

32. (Wana) mabustani na mizabibu.

حَدَائِقَ وَأَعْنَابًا ﴿٣٢﴾

33. Na wasichana walio marika.

وَكَوَاعِبَ أَتْرَابًا ﴿٣٣﴾ وَكَأْسًا دِهَاقًا ﴿٣٤﴾

34. Na vikombe vilivyojaa.

لَّا يَسْمَعُونَ فِيهَا لَغْوًا وَلَا كِذَّابًا ﴿٣٥﴾

35. Hawatasikia humo upuuzi wala kukadhibishana.

جَزَاءً مِّن رَّبِّكَ عَطَاءً حِسَابًا ﴿٣٦﴾

36. Wamelipwa na Mola wako kipawa chenye kutosha.

رَّبِّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا الرَّحْمَـٰنِ لَا يَمْلِكُونَ مِنْهُ خِطَابًا ﴿٣٧﴾

37. Bwana wa mbingu na ardhi na vilivyo kati yake, Mwingi wa Rehema Ambaye hawataweza (siku hiyo) kusema naye.

يَوْمَ يَقُومُ الرُّوحُ وَالْمَلَائِكَةُ صَفًّا لَّا يَتَكَلَّمُونَ إِلَّا مَنْ أَذِنَ لَهُ الرَّحْمَـٰنُ وَقَالَ صَوَابًا ﴿٣٨﴾

38. Siku ambayo atasimama roho na Malaika, wamepiga safu hawatazungumza ila aliyepewa ruhusa na (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa Rehema na akasema yaliyosawa.

ذَٰلِكَ الْيَوْمُ الْحَقُّ فَمَن شَاءَ اتَّخَذَ إِلَىٰ رَبِّهِ مَآبًا ﴿٣٩ ﴾

39. Hiyo ndiyo siku ya haki. Basi anayetaka naashike njia ya kurejelea kwa Mola wake.

إِنَّا أَنذَرْنَاكُمْ عَذَابًا قَرِيبًا يَوْمَ يَنظُرُ الْمَرْءُ مَا قَدَّمَتْ يَدَاهُ وَيَقُولُ الْكَافِرُ يَا لَيْتَنِي كُنتُ تُرَابًا ﴿٤٠﴾

40. Hakika sisi tunawaonya nyinyi adhabu iliyo karibu. Siku ambayo mtu ataona kilichotangulizwa na mikono yake, na kafiri atasema: laiti ningelikuwa mchanga.

UBAINIFU

Aya zinasifu siku ya upambanuzi ambayo imetolewa habari kwa ujumla na aya ya 4. Kisha inasifu yale yatakayowapitia wanaopetuka mipaka na wanaomcha Mwenyezi Mungu. Mwisho Sura inamalizia kwa tamko la kuonya, na hilo ndilo kama natija.

Aya Ya 17

Ni kuingilia kusifu yale yanayokusanywa na habari kubwa ambayo imetolewa utisho katika aya ya 4; Kisha Mwenyezi Mungu akasimamisha hoja juu ya hayo kuanzia aya ya 6 na kuendelea. Mwenyezi Mungu ameiita siku hiyo siku ya upambanuzi na akaielezea kuwa ni siku ya kupambanuliwa hukumu. Kuleta ibara ya tamko "kanat" ni dalili ya kuthibiti kwake na kubainishwa kwake katika ujuzi wa Mungu kutokana na hoja iliyotangulia kutajwa. Maana yake hakika siku ya upambanuzi wa hukumu ambayo habari yake ni kubwa, imekua katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu tangu siku aliyoumba mbingu na ardhi na akapitisha katika siku hiyo nidhamu. Yeye Mwenyezi Mungu alikuwa anajua kwamba umbile hili aliloliumba haliwezi kutimia bila ya kukomea kwenye siku ya kupambanuliwa hukumu.

Aya Ya 18

Yamekwisha tangulia maelezo kuhusu maana ya kupuziwa parapanda. Maneno yamekuja kwa njia ya kuambiwa watu kwa kuelezea haki ya kiaga. Kama kwamba aya iko katika mwelekeo wa aya inayosema: "Siku tutakapowaita kila watu pamoja na kiongozi wao ." (17:71)

Aya Ya 19

Utaungana ulimwengu wa watu na ulimwengu wa Malaika. Imesemwa kuwa kukadiria kwake ni: 'zikawa zenye milango.' Na imesemwa ni njia katika hizo mbingu. Lakini njia zote hizo mbili haziepukani na kuangaliwa vizuri.

Aya Ya 20

Kuondolewa majabali na kugongwa kunaishia kwenye kutawanyika vipande na kuondoka umbo lake kama ilivyotokea katika maneno yake Mwenyezi Mungu wakati wa kusifu tetemeko la Kiyama na athari yale alopisema: "Na majabali (yang'oke) yawe yanakwenda mwendo (mkubwa) " (52:10).

Na amesema: "Na ikaondolewa ardhi na majabali ikavunjwa mvunjo mmoja ." (69:14).

Amesema tena "Na majabali ya kawa kama sufi iliyopurwa ." (101:5).

Na amesema: "Na majabali yakasagwasagwa " (56:5).

Amesema: "Na pindi majabali yatakaposagwasagwa ." (77:10).

Ndio kunaishilia kusagwasagwa kwake kwenye kukosekana na kupotea kabisa umbo lake. Majabali yaliyokuwa yamekita kabisa yaliyokuwa yakionekana na nguvu yasiyoweza kutingishwa na kimbunga, leo yana pondwapondwa na kupotea. Aya hii iko katika mwelekeo wa aya inayosema: "Na unayaona majabali unayadhania yametulia, nayo yanakwenda kama mawingu ." (27:88). Yaani hiyo siku ya mtetemeko wa Kiyama.

Aya Ya 21

Mwenyezi Mungu ameita Jahannam ni malindilizo kwa kuwa watu wataipitia. Mwenyezi Mungu anasema: "Wala hakuna yoyote katika nyinyi ila ni mwenye kuifikia (hiyo Jahannam) " (19:71).

Aya Ya 22

Kuihisabu Jahannam ni marejeo, ni kwamba wao walijiandalia wenyewe marejeo walipokuwa duniani. Kisha waliachana na dunia na kurejea.

Aya Ya 23

Maana ya neno Ahqab ni muda mrefu usio na kikomo. Wamehitalifiana kuhusu neno hilo. Baadhi yao wamesema ni miaka 80 au miaka 80 na kitu. Wengine wakaongezea kusema kwamba mwaka katika hiyo Ahqab una siku 360 na kila siku inalingana na miaka elfu. Wengine wamesema ni miaka 40 na wengine wamesema ni miaka 70,000. Wala hakuna dalili yoyote kutoka katika Qur'an inayofahamisha juu ya viwango hivi, wala haikuthibiti katika lugha. Ukweliulivyo ni kuwa neno "Ahqab" ni muda wa wakati usiojulikana.

Kwa dhahiri ni kwamba makusudio ya waliopetuka mipaka ni wale waliofanya inadi katika makafiri.

Hayo yanatiliwa nguvu na aya ya (27) ya Sura hii inayosema; "Kwa sababu wao walikuwa hawachi kuhesabiwa ."

Imesemwa kuwa aya zinazofuatia ni sifa ya hilo neno (Ahqab) maana yake ni kuwa watakaa humo karne nyingi katika sifa hizi nazo nikuwa wao hawataonja raha wala kinywaji isipokuwa maji ya moto na usaha, kisha watakuwa kwenye sifa nyengine kwa muda usiokuwa na kikomo. Kauli hii ni nzuri kama ingelisaidiwa na mpangilio wa maneno.

Aya Ya 24-25

Zinaelezea hali watakayokuwa nayo ndani ya Jahannam.

Aya Ya 26

Ni dalili ya kuwafikiana kwenye kutimia kati ya malipo na amali. Mtu kwa amali yake anataka malipo yaliyo sawa na kazi yake. Mwenyezi Mungu amesema: "Enyi mliokufuru msitowe udhuru leo; Hakika mnapewa malipo ya yale mliyokuwa mkiyatenda ." (66:7).

Aya Ya 27 – 28

Ni sababu ya kufafanua muwafaka wa malipo yao kwa amali yao. Kwamba wao hawakutarajia kuhisabu siku ya upambanuzi wakaona kuwa hakuna maisha ya akhera, wakazikadhibisha aya zinazofahamisha hayo wakakanusha Tawhid na Utume na wakaakiuka kuwa wenyewenyekevu katika amali zao, hivyo wakamsahau Mwenyezi Mungu naye amewasahau na kuwanyima wema wa nyumba ya akhera. Kwa hiyo hawakubakiwa na chochote isipokuwa machukivu na ndio kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Basi onjeni! Hatutawazidishia ila adhabu ".

Aya hii ya (27) ni dalili ya kuafikiana kwenye kutimia kati ya malipo na amali. Mtu hutaka malipo kwa amali yake aliyoifanya. Anasema Mwenyezi Mungu katika aya ya 30 ya Sura hii: "Enyi mliokufuru! Msilete udhuru leo; Hakika mnapewa malipo ya yale mliyokuwa mkiyatenda ." (66:7).

Aya Ya 29

Yaani kila kitu tumekidhibiti na tukakibainisha katika kitabu. Aya hii iko katika mwelekeko wa aya inayosema: "Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari linalobainisha ." (36:12)

Au makusudio yake ni kuwa na kila kitu tumekihifadhi hali ya kuwa ni chenye kuandikwa katika "Lawh Mahfudh" (ubao wenye kuhifadhiwa) au katika karatasi za amali. Na wamejuzisha kuwa maana ya neno "Ihsau" ni kuandika, maana yake itakuwa na kila kitu tumekiandika kitabuni. Kwa vyovyote vile makusudio ya aya ni kutoa sababu ya yaliyotangulia; maana yake; malipo ni yenye kuwafikiana na amali zao, kwa sababu wao walikuwa kwenye hali kadha wa kadha na tumezihifadhi, kwa hiyo tumewalipa malipo yenye kiafiki.

Aya Ya 30

Ni mtiririko wa yaliyotangulia unaoelezea kuwakatisha tamaa ya kutarajia kuokoka. Kuwasemesha kwa kutumia neno "Basi onjeni" ni kwa kutahayariza; Makusudio ya kuwaambia "Basi onjeni hatutawazidishia ila adhabu" ni kuwa mnayoyaonja baada ya adhabu ni adhabu nyengine, hiyo ni adhabu baada ya adhabu na adhabu juu ya adhabu, hamtaepukana na kuongozewa adhabu mpya kwenye ile adhabu ya zamani, basi kateni tamaa katika mnayoyataka na mnayoyapenda. Aya hii haiepukani na kudhihiri kuwa makusudio ya aya 30 ni kukaa milele bila kikomo.

Aya Ya 31-35

Zinaelezea kufuzu kwa wale wamchao Mwenyezi Mungu kwa kupata heri na salama.

Aya Ya 36

Yaani wamefanyiwa wale wanaomcha Mwenyezi Mungu yake waliyofanyiwa hali ya kuwa ni malipo kutoka kwa Mola wako na kipawa chenye kuhisabiwa. Imesemwa kuwa kutegemezwa neno malipo kwa Mola kisha kwa Mtume ni kwa ajili ya kuyatukuza na halikutegemezwa kwa Mwenyezi Mungu neno malipo ya wenye kupetuka mipaka, kwa ajili ya kumtakaza nayo Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwani shari yao iliyowapata imetokana na wao wenyewe. Mwenyezi Mungu anasema: "Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyofanywa na mikono yenu. Na hakika Allah si mwenye kuwadhulumu waja ". (8:51)

Kutokea tamko la hisabu katika mwisho wa malipo ya wenye kupetuka mipaka na wenye kumcha pamoja ni kuthibitisha yale yanayoishiriwa na siku ya upambanuzi yaliyotokea mwanzo wa maneno.

Aya Ya 37

Ni ubainifu wa neno "Mola wako" inakusudiwa kuwa ubwana wake Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni wenye kuenea kwa kila kitu na kwamba Mola ambaye Mtume anamfanya kuwa Bwana na kulingania watu kwake, ni Mola wa kila kitu sio kama walivyokuwa wakisema washirikina kwamba kila taifa lina Mola na Mwenyezi Mungu ndiye Bwana wa mabwana, au kama walivyokuwa wakisema wengine kwamba Yeye ni Mola wa mbingu. Kumsifu Mola kwa kuwa "Mwingi wa Rehema" ni kuonyesha kuenea rehema yake na kwamba hiyo ni alama ya uungu wake hakizuilii chochote na kupata rehema hiyo isipokuwa mtu kujizuilia mwenyewe kwa kuzembea kwake na ubaya wa uchaguzi wake. Na katika uovu wa hao waliopetuka mipaka ni kwamba wao wamejinyima hiyo rehema kwa kutoka katika hali ya unyenyekevu.

Kuhusu "ambaye hawataweza (siku hiyo) kusema naye" kutokana na kuanza aya na "Bwana wa mbingu na ardhi na vilivyo kati yake Mwingi wa Rehema" ni dalili kwamba makusudio ya hawataweza kusema naye ni kumsemesha katika baadhi ya aliyo yafanya kwa njia ya swali kama kusema: kwa nini umefanya hayo? Na kwa nini hukufanya. Kwa hiyo jumla "hawataweza kusema naye" inakuwa katika maana ya neno lake Mwenyezi Mungu: "Haulizwi (Mwenyezi Mungu) anayoyafanya, lakini wao (viumbe) wataulizwa .." (21:23)

Lakini aya inayofuatia baada ya jumla hii inaonyesha kuhusika na Malaika yaani hao Malaika hawatasema na Mwenyezi Mungu katika atakavyopitisha kwa kumwingilia au kuwaombea kama alvyosema Mwenyezi Mungu: "kabla ya haijafika siku ambayo hapatakuwa kujikomboa wala urafiki (wa kusaidiana) wala uombezi ." (2:254)

Aya Ya 38

Makusudio ya roho ni kiumbe kinachohusikana na Mwenyezi Mungu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "sema roho ni jambo linalohusika na Mola wangu ". (17:85)

Imesemwa kuwa ni mtukufu wa Malaika. Imesemwa ni Malaika mwenye kuchukua roho, lakini hakuna dalili juu ya kauli hizi. Imesemwa makusudio ni Jibril, imesemwa ni roho za wanaadamu na kusimama kwao pamoja na Malaika. Katika wakati ulio kati ya mipuzio miwili ya parapanda kabla ya kuingia roho katika viwiliwili hali ya kupiga safu. Na imesemwa ni Qur'an na makusudio ya kusimama kwake ni kudhihiri athari yake siku hiyo katika wema wa waumini na uovu wa makafiri.

Lakini hizi kauli tatu zinapingwa, kwamba ingawaje ametumia Mwenyezi Mungu neno roho katika kila moja yao lakini ni pamoja na kuifunga (kuihusisha) na kitu chengine. Kama katika kauli yake: "Na kumpulizia roho inayotokana na mimi ." (15:29).

Na kauli yake: "Ameyateremsha hayo roho (Jibril) mwaminifu"

(26:193). Na kusema kwake: "....Na tukampelekea roho wetu ." (19:17).

Na kauli yake: "Sema ameiteremsha roho mtakatifu ." (Jibril) (16:102).

Na kauli yake:

"Namna hivi tumekufunulia (Qur'an) kwa roho atokaye kwetu ". (42:52) Kusema kwake "Hawatasema" ni ubainifu wa neno "ambaye hawataweza kusema haya". Dhamiri ni ya kundi lote la roho, Malaika, Watu na Majini kutokana na unavyofahamisha mpangilio wa maneno. Imesemwa dhamiri ni ya roho na Malaika. Na imesemwa ni ya watu lakini kutokea neno hawataweza na hawatasema katika muundo mmoja hakuafikiani na kauli hizo mbili.

Kusema kwake "Ila aliyepewa ruhusa na Allah, Mwingi wa Rehema" ni yule atakayeweza kusema. Jumla hiyo iko katika maana ya kauli yake: "wakati itakapokuja (siku hiyo) kiumbe chochote hakitasema ila kwa ruhusa yake (Mwenyezi Mungu)". (11:105).

Kusema kwake "Na akasema yaliyo sawa " yaani ni neno lililosawa lisiloingiliwa na kosa, ni haki isiyoingiliwa na batili. Kwa hakika jumla ni kuifunga idhini na haki, ni kama vile imesemwa 'wala hatapewa idhini isipokuwa yule atakayesema yaliyosawa." Kwa hiyo aya iko katika maana ya aya inayosema: "Wala hawana uwezo wa uombezi wale wanaowaomba badala yake ila wale wanaokiri (hii) haki, wakaijuwa ." (43:86).

Kuhusu Roho Katika Qur'an Limekaririka tamko la roho katika maneno ya Mwenyezi Mungu, na maana inayofahamika haraka ni kitu ambacho no msingi wa uhai. Na Mwenyezi Mungu hakulitumia neno hili kwa mtu au kwa mtu na mnyama pekee, bali amelithibitisha sehemu nyengine; kama katika kauli yake "na tukampelekea Mariam roho wetu.. " (19:17).

Na kusema kwake: Namna hivi tumekufunulia (Qur'an) kwa roho atokaye kwetu." (42:52) Kwa hiyo roho ina uthibitisho kwa mtu na penginepo, kauli inayoweza kuielezea roho zaidi ni ile ya Mwenyezi Mungu isemayo "Na wanakuuliza habari ya roho. Sema roho ni amri ya Mola wangu". Na ameielezea amri kwa kusema kwake: "Hakika amri yake anapotaka chochote ni kukiambia kuwa kikawa. Ametutuka yule ambaye mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu, na kwake mtarejezwa nyote ." (36:82-83)

Kwa hiyo amebainisha kwamba hiyo roho ni tamko linalofanya kitu kipatikane; hii ikimaanisha kwamba hilo tamko ndiyo kupatikana (kwa kitu) kwa vile kunavyonasibiana na Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anavyosifika na kupatikana huko, na siyo huko kupatikana kunavyonasibiana na ila au sababu za nje. Kwa makusudio haya amemuhisabu Masihi (AS) kuwa ni tamko na roho kutoka kwake aliposema: "Na tamko lake alilompelekea Mariam. Na ni roho iliyotoka kwake ." (4:171).

Hapo ni wakati alipompa Mariam, Isa (AS) kwa njia isiyokuwa ya kawaida. Inakurubia katika makusudio hayo kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hakika mfano wa Isa kwa Allah ni kama mfano wa Adam alimuumba kwa udongo, kisha akamwambia kuwa, basi akawa ". (3:59).

Na Yeye Mwenyezi Mungu ingawaje aghlabu ameitaja hiyo roho kwa kutegemeza au kwa kuifunga na kitu; kama kauli yake "na kumpulizia roho inayotoka na mimi " (15:29).

Na kauli yake: "na akampulizia roho yake " ( 32:9). Na kauli yake:

"na tukamplelekea roho wetu ." (19:17).

"Na ni roho kutoka kwake.. " (4:17)

"Na tukamtia nguvu kwa roho mtakatifu . " (2:87).

Na mengineyo, lakini pia yamekuja baadhi ya maneno yake kwa kutaja roho bila ya kuitegemeza au kuifunga na chochote. Kama kauli yake; "Hushuka Malaika na roho katika Lailatul-Qadri kwa amri ya Mola wao kwa ajili ya kila jambo ". (97:4).

Dhahiri ya aya hiyo ni kwamba roho hapo ni kiumbe kingine cha mbinguni ambacho ni Malaika. Aya hiyo iko katika mwelekeo wa kauli yake: "Malaika na roho hupanda kwake katika siku ambayo muda wake ni miaka elfu hamsini " (70:4). Ama roho yenye kufungamana na binadamu ameitolea taabiri Mwenyezi Mungu kwa mfano wa kauli yake: "Na kumpulizia roho inayotokana na mimi ." (15:29).

Na "na akampulizia roho inayotoka kwake ." (32:9) Na ameleta neno "Min" lenye kufahamisha umwanzo. Na kitendo cha kuleta "umwanzo" akakiita kuwa ni "kupulizia'. Ametaja roho aliyowahusisha waumini kwa mfano wa kauli yake " na akawatia nguvu kwa roho itokayo kwake." (58:22).

Ameleta herufi "Ba" katika aya hiyo yenye kufahamisha sababu na akakiita kitendo hicho 'kutia nguvu'. Ametaja roho aliyowahusisha mitume katika mfano wa kauli yake "na tukamtia nguvu kwa roho mtakatifu" (2:87).

Kwa hiyo akaongezea utakatifu, pia ametaja kuwa ni kutia nguvu.

Kwa kuzikusanya aya hizi pamoja na mfano wa aya, iliyoko katika Sura ya Qadr inadhihiri kwamba mnasaba kati ya roho yenye kutegemezwa kitu ambayo iko katika aya hizi, na roho ambayo haikusasibishiwa chochote ni kama kunavyonasibishwa kumimina na mmiminaji au kivuli na chenye kuleta kivuli. Vinaponasibishiwa na idhini ya Mwenyezi Mungu.

Vile vile roho yenye kufungamana na Malaika, isipokuwa ni kwamba hakusema katika roho ya Malaika kwa kupuzia na kutia nguvu, kama alivyosema kwa binadamu bali ameita roho tu kama katika kauli yake: "Na tukampelekea roho wetu." (19:17). Na kusema kwake: "Sema ameiteremsha roho mtakatifu " (16:102). Kwa sababu Malaika ni roho pekee, kulingana na kuhitalifiana daraja zao katika ukaribu na umbali na Mola wao. Wanavyoonekana na viwiliwili ni kwa kujifananisha tu; kama linavyoonyesha neno lake: "Na tukampelekea roho wetu akajifananisha kwake na (sura ya) binadamu aliye kamili ". (19:17). Kwa sababu hiyo hawakuambiwa roho zao 'zimepuliziwa' tofauti na binadamu ambaye ana sehemu ya kiwiliwili ambacho ni maiti na roho ambayo iko hai, huyu inanasibu kusema amepuliziwa; kama anavyosema Mwenyezi Mungu: "Nikishamkamilisha na kumpulizia roho yangu, angukeni mumsujudie." (15:29).

Kama ambavyo umbile la roho ya mwanadamu ni tofauti na ile ya Malaika, kwa vile katika mwanadamu kuna'kupulizia' na katika Malaika hakuna, hivyo ndivyo tofauti kati ya roho inavyopatikana. Tofauti ya maisha ya roho kuwa mazuri au mabaya, imeleta tofauti katika kuielezea roho inayohusika. Hivyo ndivyo 'kutiwa nguvu' kwa Malaika, na waumini. Miongoni mwa roho, ni roho zenye kupuliziwa kwa mtu anasema "nikapuzia roho itokayo kwangu ". (15:29).

Na roho zenye 'kutiliwa nguvu' ni roho za waumin. Mwenyezi Mungu anasema: "Hao ndio ambao (Mwenyezi Mungu) ameandika nyoyoni mwao imani na akawatia nguvu kwa roho itokayo kwake " (58:22).

Hiyo ni daraja ya juu zaidi katika roho za kibinadamu kama inavyoelezea kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) ambayo iko katika maana ya aya hii tuliyoitaja sasa hivi: "Je aliyekuwa maiti kisha tukamfufua na tukamjaalia nuru, kwa nuru hiyo hutembea mbele za watu, atakuwa sawa na yule ambaye hali yake yuko gizani asiweze kutoka humo ". (6:122).

Kwa hiyo amemuhisabu muumin ni hai mwenye nuru anayotembea kwa nuru hiyo, ni athari ya roho. Na kafiri amemuhisabu kuwa maiti naye ni mwenye roho ya kupuliziwa.

Kwa hiyo inadhihiri kwamba daraja za roho kuna zile zilizo katika mimea kutokana na athari ya uhai. Zinazofahamisha hilo ni aya zenye madhumuni ya kuihuyisha ardhi baada ya kufa. Miongoni mwa aina za roho ni zile wanazotiliwa nguvu mitume nazo. Ama kauli yake: "Hupeleka roho kwa amri yake kwa amtakaye miongoni mwa waja wake, ili kuwaonya siku ya kukutana (naye)" (40:15) Na kauli yake: "Namna hii tumekufunulia roho kwa amri yetu ". (42:52).

Inawezekana kuwa roho zinazozungumziwa katika aya mbili hizo, ni roho ya Imani au roho mtakatifu (Jibril).

Aya Ya 39

Ni ishara ya hiyo siku ya upambanuzi. Kuishiria kwa ishara ya mbali ni kuonyesha uzito wake. Kauli yake "Basi anayetaka naashike njia ya kurejelea kwa Mola wake." ni mtiririko wa habari za siku ya upambanuzi maana yake mwenye kutaka kurudi kwa Mola wake na arudi.

Aya Ya 40

Makusudio ya adhabu hapa ni adhabu ya akhera na kusema iliyokaribu ni kwa kuwa ni kweli hapana shaka kuileta, na kila linalokuja liko karibu. Kuhusu ambacho kimetangulizwa na mikono yake ni amali yake aliyoifanya mwenyewe. Mwenyezi Mungu anasema: "Siku ambayo itakuta kila nafsi mema iliyoyafanya yamehudhurishwa na pia ubaya ulioufanya ". (3:30). Kusema kafiri laiti ningelikuwa mchanga yaani atatamani hivyo kutokana na shida ya siku hiyo kwamba yeye lau angelikuwa kitu kisichokuwa na hisiya yoyote.

Utafiti Wa Hadith Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu aya ya (19) amesema: "Itafunguliwa milango ya peponi " na kuhusu aya ya (20) anasema: yatakwenda majabali mfano wa mlenge ambao unametameta katika jangwa. Katika hiyo hiyo Tafsiri ya Qummi kuhusu aya ya (23) amesema neno "Ahqab" ni miaka na mwaka una siku 360 na siku moja huko ni kama miaka elfu mnayoihisabu. Katika Majmau amepokea Nafi'i kutoka kwa Ibn Umar amesema: amesema Mtume(s.a.w.w) 'Hatatoka motoni mpaka akae humo kitambo cha Huqb nyingi na Huqb moja ni miaka 60 na kitu na mwaka mmoja ni siku 360, kila siku ni kama miaka elfu mnavyohisabu kwa hiyo asitegemee yoyote kutoka katika moto. Riwaya kama hiyo imekuja katika Durril Manthur na imepokewa vile vile riwaya nyengine kutoka kwake(s.a.w.w) kwamba "Huqb" ni miaka 40. Katika hiyo hiyo amepokea Iyashi kwa isnadi yake kutoka kwa Hamran amesema: 'Nilimwuliza Abu Jaffar(a.s) kuhusu aya hii akasema: "Aya hii inawahusu ambao watatoka motoni ."

Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu aya (31) amesema: "Watafuzu ". Na aya (33) ni wake wa watu wa peponi. Katika riwaya ya Abul Jarud kutoka kwa Abu Jaffar(a.s) kuhusu aya (31) amesema ni utukufu. Na aya (33) amesema ni wasichana wenye matiti yaliyosimama. Katika Durril Manthur ametoa Ibn Abu Hatim, Abush Shaykh katika Adhama na Ibn Murdawayh kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Mtume(s.a.w.w) amesema: "Roho ni askari katika askari wa Mungu sio Malaika wana vichwa, mikono na miguu, kisha akasema "Siku atakayosimama Roho na Malaika wamepiga safu akasema: Hao ni askari na hao ni askari ." Imekwisha tangulia riwaya katika aya zinazoelezea roho kutoka kwa Maimamu(a.s) .

Ndio katika riwaya ya Qummi aliyoipokea kutoka kwa Himran ni kwamba Roho ni malaika mkubwa kuliko Jibril na Mikail na alikuwa pamoja na Mtume(s.a.w.w) na yuko pamoja na Maimamu(a.s) . Huenda makusudio ya Malaika ni kwa vile yuko mbinguni au hizo ni dhawa za wapokezi wa hadith katika kunakili maana wala hakuna hali ya kufahamisha kuwa kila kinachopatikana mbinguni ni malaika bali iko dalili ya kinyume cha hilo kama inavyofahamisha kauli yale Mwenyezi Mungu: "Ewe Ibilisi! Kipi kilichokuzuia kumsujudia yule niliyemuumba kwa mikono yangu? Je, umetakabari au umo miongoni mwa wakubwa ". (38:75).

Katika Usul-Kafi kwa isnadi yake kutoka kwa Muhammad bin Al-Fadhil naye kutoka kwa Abul Hassan(a.s) amesema: Nilisoma aya; "Siku ambayo atasimama Roho na Malaika, wamepiga safuu hawatazungumza ila aliyepewa ruhusa na (Allah) Mwingi wa Rehema na akasema yaliyosawa ." Niliposoma aya hiyo akasema: "Wallah sisi ndio tutakaopewa idhini siku ya Kiyama na ndio wenye kusema yaliyosawa ." Nikasema : "Mtasema nini? " Akasema: "Tutamsifu Mwenyezi Mungu na kumswalia Mtume wetu na kuwaombea wafuasi wetu wala hataturudisha Mola wetu ".

Katika Majmau imepokewa hadith hiyo Iyash ikiwa Marfua kutoka kwa Muawiya bin Ammar naye kutoka kwa Abu Abdillah(a.s) . Riwaya hii ni kwa upande wa kuelezea baadhi ya mambo yanayosadikiwa, kwani wako waombezi wengine, katika malaika, mitume na waumini watapewa idhini katika kuzungumza. Na wako mashaidi wa uma watakaopewa idhini ya kuzungumza; kama inavyoeleza Qur'an na hadith.


3

4

5

6

7

8

9

10

11

12

13

14

15

16