17
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
SURA LAYL (USIKU) (NA. 92)
INA AYA 21
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu
وَاللَّيْلِ إِذَا يَغْشَىٰ ﴿١﴾
1. Naapa kwa usiku unapofunika
وَالنَّهَارِ إِذَا تَجَلَّىٰ ﴿٢﴾
2. Na (kwa) mchana unapofunuka.
وَمَا خَلَقَ الذَّكَرَ وَالْأُنثَىٰ ﴿٣﴾
3. Na (kwa) mwenye kuumba kiume na kike.
إِنَّ سَعْيَكُمْ لَشَتَّىٰ ﴿٤﴾
4. Hakika matendo yenu ni mbali mbali.
فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ ﴿٥﴾
5. Ama mwenye kutoa akamcha (Mwenyezi Mungu).
وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَىٰ ﴿٦﴾
6. Akalisadiki jambo jema.
فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَىٰ ﴿٧﴾
7. Tutamsahilishia njia ya wepesi.
وَأَمَّا مَن بَخِلَ وَاسْتَغْنَىٰ ﴿٨﴾
8. Ama mwenye kufanya ubakhili akajiona hana haja.
وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَىٰ ﴿٩﴾
9. Akalikadhibisha jambo jema.
فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَىٰ ﴿١٠﴾
10. Tutamfanyia nyepesi njia ya uzito.
وَمَا يُغْنِي عَنْهُ مَالُهُ إِذَا تَرَدَّىٰ ﴿١١﴾
11. Hayatamfaa mali yake atakapopomoka.
إِنَّ عَلَيْنَا لَلْـهُدَىٰ ﴿١٢﴾
12. Hakika na juu yetu kuongoza.
وَإِنَّ لَنَا لَلْآخِرَةَ وَالْأُولَىٰ ﴿١٣﴾
13. Na hakika ni yetu sisi akhera na ulimwengu.
فَأَنذَرْتُكُمْ نَارًا تَلَظَّىٰ ﴿١٤﴾
14. Basi ninawahadharisha na moto unaowaka kwa nguvu.
لَا يَصْلَاهَا إِلَّا الْأَشْقَى ﴿١٥﴾
15. Hatauingia ila mwovu mno!
الَّذِي كَذَّبَ وَتَوَلَّىٰ ﴿١٦﴾
16. Ambaye amekadhibisha akapa mgongo.
وَسَيُجَنَّبُهَا الْأَتْقَى ﴿١٧﴾
17. Na ataepushwa nao mwenye kucha (Mungu).
الَّذِي يُؤْتِي مَالَهُ يَتَزَكَّىٰ ﴿١٨﴾
18. Ambaye hutoa mali yake kwa (kutaka) kujitakasa.
وَمَا لِأَحَدٍ عِندَهُ مِن نِّعْمَةٍ تُجْزَىٰ ﴿١٩﴾
19. Na hali ya kuwa hakuna yoyote aliyemfanyia hisani ili awe anamlipa.
إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٠﴾
20. Isipokuwa ni kwa kutaka radhi ya Mola wake aliye Mtukufu mno.
وَلَسَوْفَ يَرْضَىٰ ﴿٢١﴾
21. Basi hapo ataridhia.
UBAINIFU
Lengo la Sura hii ni kuonya. Inaelezea huko kuonya kwa kufuata njia ya kuonyesha tofauti ya matendo ya watu: Kwamba katika wao, mwenye kutoa, akamcha Mwenyezi Mungu na akalisadiki jambo jema, basi Mwenyezi Mungu atammanikisha katika maisha mema ya milele. Na katika wao mwenye kufanya ubakhili, akajiona hana haja na akalikadhibisha jambo jema, basi Mwenyezi Mungu atamwelekeza kwenye uovu. Sura hii inatilia umuhimu zaidi jambo la kutoa mali. Kulingana na mpangilio wake inawezekana kuwa imeshuka Makka au Madina.
Aya Na 1
Mwenyezi Mungu anaapa kwa usiku unapofunika mchana; kama alivyosema: "Huufunika usiku kwa mchana
" (7:54). Inawezekana kuwa makusudio yake ni kufunika ardhi au jua.
Aya Na 2
Inaungana na Aya Na (1). Maana ya neno Tajallaa ni kudhihiri kitu baada ya kujificha. Amesema katika Majmau ni kudhihiri huo mchana kutoka katika giza. Hili ni neema kubwa, kwani lau wakati wote ungekuwa ni giza, basi watu wasingeweza kutafuta maisha.
Aya Na 3
Pia inaungana na aya iliyotangulia herufi Maa ni kiwakilishi na makusudio yake ni Mwenyezi Mungu Mtukufu. Imekuja ibara hiyo bila ya kumtaja Mwenyezi Mungu kwa kutambulisha utukufu wake; Maana yake; ninaapa kwa kitu cha ajabu ambacho kimeleta kiume na kike ambavyo ni namna moja, lakini vimetofautina. Imesemwa kuwa herufi Maa ni kiarifa chenye kutumika kama jina; Maana yake ni ninaapa kwa kuumba kiume na kike lakini njia hii ni dhaifu. Mukusudio ya kiume na kike hapa ni aina yoyote ya kiume na kike. Imesemwa kuwa ni mtu mume na mke na pia imesemwa kuwa ni Adam na mkewe Hawa, lakini njia iliyo na nguvu zaidi, ni hiyo ya kwanza.
Aya Na 4
Neno Saa'ya lina maana ya kwenda haraka, na makusudio yake hapa ni ketendo kwa vile mtu anajihimu nacho, nalo liko katika maana ya wingi. Jumla hiyo ni jawabu la kiapo na maana yake; Ninaapa kwa vitu hivi vyenye kutofautiana kwa umbo na athari, hakika matendo yenu ni yenye kutofautiana hayo yenyewe na athari zake. Kuna katika hayo ni ya kutoa, kumcha Mwenyezi Mungu na kusadikisha, yana athari inayohusika nayo. Na kuna katika hayo ni ya ubakhili, kujitosheleza na kukadhibisha nayo yana athari inayohusika nayo.
Aya Na 5-6
Ni ufafanuzi wa kutofautiana matendo yao na kutofautiana athari yake. Makusudio ya kutoa ni kutoa mali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kinyume chake ni ubakhili wa kujizuia kutoa mali. Na kusema kwake: "Hayatamfaa mali yake atakapopomoka." Na kusema kwake : "Na akamcha Allah" ni kama anafasiri kutoa, makusudio yake ni kutoa kwa njia ya (taqwa) uchaji Mungu. "Jambo jema" ni sifa yenye kusimama mahali pa chenye kusufiwa, kwa dhahiri kukadiriya kwake ni maandalizi mema ambayo ameyatolea ahadi Mwenyezi Mungu Katika thawabu ya kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) Na huko kutoa ni kusadikisha ufufuo na kuamini Mwenyezi Mungu na kulazimisha imani kwa umoja wake Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika ubwana na kuuamini utume. Hiyo ndiyo njia ya kufikia yale aliyoyatolea ahadi Mwenyezi Mungu kupitia kwenye ulimi wa Mtume wake.
Aya Na 7
Makusudio ya kumsahilishia njia ya wepesi ni kumwafikisha kwa mali njema kwa kuzifanya nyepesi bila ya uzito wowote. Au kumfanya ni mwenye kujiandaa kwa maisha mema mbele ya Mola wake na kuingia peponi kwa sababu ya amali njema anazozifanya. Hii njia ya pili ni karibu na iko wazi zaidi kutokana na yale yaliyotolewa ahadi katika viaga vya Qur'an.
Aya Na 8 -10
Ubakhili ni kunyume cha kutoa. Makusudio ya kukadhibisha jambo jema ni kukanusha mambo mema na thawabu za Mwenyezi Mungu ambazo wamezielezea Mitume. Na hayo yanarudia kukanusha ufufuo. Makusudio ya 'kusahilishiwa uzito' ni kutofanikiwa kwake kwa kukosa kuwafikishwa kwenye amali njema, kwa kuwa nzito na kukosa kukunjuliwa moyo wake na imani au ni kuandaliwa adhabu.
Aya Na 11
Herufi Maa ni swali yaani mali yake itamfaa namna gani atakapokufa na kuangamia. Au ni ya kukanusha, yaani haitamfaa mali yake atakapoangamia.
Aya Na 12-13
Ni sababu ya yaliyotangulia katika kuzungumzia wepesi na uzito Au nikuelezea kwa ufafanuzi zaidi kwamba hakika sisi tunafanya huu wepesi au tunaubainisha ubainifu huu, kwa sababu unatokana na uongofu na ni juu yetu kuongoza na wala hakituzuii kitu chochote. Kwa hivyo kusema kwake "Hakika ni juu yetu kuongoza", kunamaanisha kwamba kuongoza watu alikokupitisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) amejiwabisha mwenyewe kwa mujibu wa hekima, na hilo ni kwamba yeye amewaumba ili wamwabudu; kama alivyosema: "Sikuumba majini na watu ila waniabudu
". (51:56).
Kwa hiyo amefanya kumwabudu ndiyo lengo la kuumbwa kwao na akaifanya hiyo ibada ni njia yenye kunyooka ya kumwendea yeye; kama alivyosema: "Hakika Allah ni Mola wangu na ni Mola wenu, basi mwabuduni hii ndiyo njio iliyonyooka
" (3:51) "Hakika wewe unaongoza njia iliyonyooka
" (42:52).
Mwenyezi Mungu amejihukumilia kuwabainishia watu njia yake na kuwaongoza kwake, kwa maana ya kuwaonyeshea njia, ikiwa wataifuata au wataiwacha, kama alivyosema: "Na Allah ndiye anayesema kweli, naye kuongoa njia (ya uongofu)
(33:4). Amesema tena: "Hakika sisi tumemuongoa njia, basi ama atakuwa mwenye kushukuru au kukufuru
". (76:3).
Hayo yote hayapingi kuwa mtu mwengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu kuweza kusimamia jambo hili kwa idhini yake Mwenyezi Mungu, kama vile mitume; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Hakika wewe (Muhammad) unaongoza njia iliyonyooka
" (42:52). Amesema tena: "Sema, hii ndiyo njia yangu ninailingania kwa Allah kwa ujuzi wa kweli, mimi (ninafanya hivi) na wanaonifuata
" (12:108)
Hayo ni ikiwa uongozi ni kwa maana ya kuonyesha njia. Ama ikiwa uongozi ni kwa maana ya kufikisha kwenye matakwa - na matakwa ni athari nzuri ambazo zinafuatana na kuongoka kwa uongofu wa Mwenyezi Mungu kama maisha mema ya dunia na ya akhera ya milele - basi kwa ubainifu zaidi itakuwa ni kwa upande wa kutengeneza na kupatisha ambako anahusika nako Mwenyezi Mungu (s.w.t) Hayo ni katika yale aliyoyahukumilia Mwenyezi Mungu na kujiwajibishia na kuyasajili kwa kiaga chake cha haki; Mwenyezi Mungu anasema: "Basi atakayeufuata uongofu wangu hatapotea wala hatataabika
." (20:123).
"Mwenye kufanya mema miongoni mwa wanaume au wanawake na hali ya kuwa yeye ni muu'min tutamuhuyisha maisha mema na tutawapa ujira wao mkubwa kwa sababu ya yale mema waliyokuwa wakiyatenda
." (16:97).
Amesema tena: "Na wale waliomaini na wakatenda njema tutawaingiza katika mabustani yapitayo mito chini yake watakaa humo milele. Ndiyo ahadi ya Allah iliyokweli. Na ninani mkweli zaidi kwa usemi kuliko Allah
? (4:122). Kunasibishiwa uongozi mtu mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu, kwa kuingia kati huyo mtu na hayo yanayonasibishwa kwa Mwenyezi Mungu. Hii ikiwa ni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hivyo Mwenyezi Mungu atakuwa ndiyo asili ya uongozi, na mtu huyo ni mfuasi. Maana ya aya, ikiwa makusudio ya uongofu ni kuonyesha njia, ni: hakika sisi tunawabainisha yale tunayoyabainisha, kwa sababu ni juu yetu kuonyesha njia ya kuabudu. Ikiwa ni kwa makusudio ya kufikisha kwenye matakwa, ni: hakika tunawasahilishia hawa wepesi wa amali njema, au na maisha mepesi ya milele na kuingia peponi; kwa sababu hilo ni katika kuvifikisha vitu kwenye lengo lake, na hilo ni juu yetu. Ama kusahilishia njia ya uzito ni kuzuilika na kupata wepesi, "Ili Allah apate kuwapambanua walio wabaya na walio wazuri na kuwaweka wabaya juu ya wabaya wengine na kuwarundika wote pamoja na kuwatupa katika Jahanam
". (8:37).
Mwenyezi Mungu amekwishasema: "Na tunateremsha katika Qur'an (Hayo mafundisho yake) ambayo ni ponyo na rehema kwa wanaoamini wala hayawazidishi (mafundisho hayo) madhalimu ila hasara tu! (kwani hawakubali kufuata)
." (17:82).
Inawezekana kuwa maana ya ungozi hapa - kwa vile tamko 'uongozi' halikutegemezewa sharti yeyote - ni kwamba huu uongozi, pasi na kutajwa katika jambo gani, una maana mapana zaidi kuliko uongozi uliotajwa kama katika mazingatio ya sheria n.k. - kwa hiyo Mwenyezi Mungu ni wake uongozi wa kiuhakika kama alivyosema: "ambaye amekipa kila kitu umbo lake kisha akakiongoza
." (20:50).
Na ni wake uongofu wa kimazingatio, kama alivyosema: "Hakika sisi tumemuongoa (tumembainishia) njia (ya kheri nay a shari) , basi (mwenyewe tena) atakuwa mwenye kushukuru au kukufuru
.(76:3).
Kuhusu Aya Na (13) ni ulimwengu wa mwanzo na ulimwengu wa kurudi; kila kinachohisabika ni kitu basi ni milki yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa milki ya uhakika ambayo inasimamia kupatikana kwa kiti hicho, kisha ndipo inakuja milki wa kimazingatio ambayo katika athari zake ni kujuzu kukifanya lolote.
Kwa hiyo yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamiliki kila kitu kwa kila upande hakuna mpinzani anayempinga wala mzuwiyaji atakayemzuwiya, wala hakuna kitu kinachomshinda, kama alivyosema: "Na Allah huhukumu hakuna wa kupinga hukumu yake
"(13:41).
Na amesema tena: "Na Allah hufanya apendavyo." (14:27).
Na amesema tena: "Na Allah ndiye mwenye kushinda juu ya jambo lake (alitakalo lazima liwe)
." (12:21).
Aya Na 14-16
Ni mtiririko wa yaliyotangulia; yaani ikiwa uongofu ni juu yetu, basi ninawatahadharisha na moto wa Jahannam. Na kwa hilo anauelekeza msemo katika kauli yake (ninawatahadharisha) kutoka katika wenye kusema wengi kwenda kwa mwenye kusema mmoja pekee, yaani ikiwa uongofu ni wenye kupitishwa, basi muhadharishaji wa asili ni Mwenyezi Mungu ijapokuwa ni kupitia kwa ulimi wa Mtume wake. Makusudio ya moto uwakao ni Jahannam kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Lakini wapi! Kwa hakika huo ni moto uwakao
". (70:15).
Makusudio ya mwovu mno ni kafiri yeyote ambaye anakufuru kwa kukadhibisha na kupa mgongo. Kwani yeye ni mwovu zaidi ya waovu wengine. Mwenye kuwa na balaa katika mwili wake amepata uovu, mwenye kupatwa na balaa katika mali yake au mtoto wake pia amepata uovu na mwenye kupata hasara katika mambo yake ya akhera amekuwa mwovu, lakini huyu ni mwovu zaidi ya wengine kwa vile uovu wake ni wa milele hakuna tamaa ya kuepukana nao. Kinyume cha uovu wa mambo ya kidunia, kwa sababu uovu unakatika na ni wenye kutarajiwa kuondoka haraka.
Kwa hiyo makusudio ya mwovu mno hapa ni kafiri mwenye kukadhibisha mlingano wa haki, kama alivyomwelezea Mwenyezi Mungu kwa kusema: "Ambaye amekadhibisha na akapa mgongo." Ama kusema muovu zaidi ni kwa maana ya muovu wa watu wote ni jambo ambalo halisaidiwi kabia na mpangilio wa maneno. Makusudio ya neno Yaswlaaha ni kuufuata huo moto na kulazimiana nao (kuwa nao) kwa hiyo inafahamisha kudumu kwenye huo moto. Hayo ni katika aliyoyahukumilia Mwenyezi Mungu katika haki ya kafiri, kama alivyosema: "Na wale ambao wamekufuru na wakayakadhibisha maneno yetu hao ni watu wa motoni, watakaa milele humo
." (2:39).
Hilo basi linapinga yale yaliyosemwa kwamba maana ya neno: "Hatauingia ila mwovu mno" kwamba mafasiki katika waislamu hawataingia motoni, isipokuwa inaonyesha kuwa asiyekuwa kafiri hatadumu , lakini atauingia.
Aya Na 17-19
Makusudio ya neno Atqaa ni yule mwenye kumcha Mungu zaidi: Wako watu hucha kupotea nafsi kama kwa kifo au kuuawa, na wengine hucha kuharibika mali na wengine hucha ufakiri, kwa hiyo wanajizuia kutoa mali. Na wengine humcha Mwenyezi Mungu tu; kwa hiyo wanatoa mali. Basi huyu ndiye mwenye kucha zaidi ya wote, anatoa mali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Ukipenda unaweza kusema: hucha hasara ya akhera , kwa hiyo anajitakasa kwa kutoa. Yule ambaye hachi kwa kutoa mali anashindwa na huyo anayetoa mali, ijapokuwa hucha mambo ya kidunia au humcha Mungu kwa baadhi ya matendo mema.
Ayah ii inaenea kwa wote na sio mahsusi kwa mtu, kulingana na inavyofahamisha, na kunafahamisha hilo, kumsifu mwenye kucha zaidi kwa aya inayofuatia. "Ambayo hutoa mali yake" hiyo ni sifa ya yeyote yule amayetoa, lakini hili halikanushi kuwa aya au Sura yote imeshuka kwa sababu mahsusi kama ilivyopokewa katika sababu za kushuka. Ama kumuhusisha mbora zaidi mmoja tu! Juu ya watu wote, wabaya au wema katika wote au katika kila zama na iwe maana ni "ataepushwa nao mwenye kucha zaidi ya watu wote, na hatauingia ila mwovu zaidi ya watu wote", ni jambo ambalo halisaidiwi na mpangilio wa aya za mwanzo wa Sura vile vile hakuna maana ya kusema "Ninawahadharisha nyote na moto ambao hatadumu ndani yake ila mmoja katika nyinyi na hataokoka ila mmoja katika nyinyi".
Aya Na (18) ni sifa ya yule mwenye kumcha zaidi yaani ambaye anatoa mali yake hali ya kutaka kwa hilo ziada njema.
Aya Na (19) ni ya kuthibitisha madhumuni ya aya iliyotangulia yaani hana yoyote mbele zake ihsani itakayolipa hiyo ihsani yake isipokuwa anatoa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu. HAya Na natiliwa nguvu na aya inayofuatia.
Aya Na 20
Maana yake ni lakini yeye anatoa mali yake hali ya kutaka radhi ya Mola wake Mtukufu. Maelezo zaidi ya Mola Mtukufu yako katika Sura ya 87.
Aya Na 21
Yaani huyu mchaji zaidi ataridhia yale anayopewa na Mola wake Mtukufu kutokana na malipo mema yaliyo mazuri. Kutaja sifa mbili za Mola na Utukufu, ni kufahamisha kwamba yale malipo anayopewa ni malipo ya neema zaidi na ya utukufu zaidi (juu zaidi) nayo ni yenye kunasibiana na Uungu na Utukufu.
Utafiti Wa Hadith Katika Kafi kutoka kwa Muhammad bin Muslim amesema: "Nilimuuliza Abu jaffar
kuhusu maneno ya Mwenyezi Mungu: "Naapa kwa usiku unapofunika, na naapa kwa nyota zinapoanguka (zinapokuchwa)
" na mifano ya hayo. Akaniambia: "Hakika Mwenyezi Mungu anaweza kuapia chochote anachotaka katika viumbe vyake, lakini viumbe haviwezi kumwapia asiyekuwa Yeye (Mwenyezi Mungu). Imepokewa katika Faqih kutoka kwa Ali bin Mahziyar kutoka kwa Abu Jaffar wa pili
na katika Tafsiri ya Qummi kuhusu Aya Na kwanza anasema: Ni wakati unapofunikwa mchana, na hicho ni kiapo. Kutoka kwa Humayri naye kutoka kwa Ahmad bin Muhammad naye kutoka kwa Ahmad bin Muhammad bin Abu nasr naye kutoka kwa Abul-Hassan Arridhaa
kuhusu tafsiri ya Sura ya Al-layl anasema:
"Hakika mtu mmoja alikuwa na mtende katika ukuta wa Mtu mwengine na huyo mwenye mtende alikuwa akimdhuru huyo mwengine; akamshtakia Mtume akaitwa yule mwenye na Mtume akamwambia nipe mtende wako kwa mtende wa peponi, akakataa. Na kulikuwepo mtu mwengine anayeitwa Abu Dahdaah aliyesikia hayo akamwendea mwenye mtende akamwambia niuzie mtende wako kwa ukuta wangu akamuuzia. Abu Dahdaah akwamwendea Mtume akamwambia nimeununua mtende fulani: kwa ukuta wangu. Mtume akamwambia "utapata badala yake mtende katika peponi ndipo akateremsha Mwenyezi Mungu: "Na mwenye kuumba kike na kiume. Hakika matendo yenu ni mbalimbali. Ama mwenye kutoa (yaani mtende) na akamcha Allah na akalisadiki jambo jema (yaani lililo mbele ya Mtume(s.a.w.w)
mpaka Aya Na 11.
Katika Tafsiri ya Qummi mwenye kucha Mwenyezi Mungu zaidi ni Abu Dahdaah. Hayo ni kwa upande wa Shia kutokana na Maimamu wa Ahlul Bait. Kwa upande wa Ahli Sunna amepokea Tabrasi katika Majmau kwamba kisa hicho kimepokewa kwa Wahidi naye kutoka kwa Akrama naye kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Ansari mmoja alipiga bei na mwenye mtende akaununua kwa mitende arubaini, kisha akampa Mtume naye Mtume akampa mwenye nyumba. Amepokea Tabrasi kutoka kwa Ata kwamba jina la huyo mtu ni Abu Dahdaah. Na amepokea Assuyuti katika Durril Manthur kisa hicho kutoka kwa Ibn Abu Hatim naye kutoka kwa Ibn Abbas, lakini ameifanya dhaifu riwaya hiyo.
Imepokewa tena, katika njia ya Ahli Sunna kwamba Sura hii ilishuka kwa Abu Bakr. Amesema Arrazi katika Tafsiri Kabir: "Wamekongamana wafasiri katika sisi kwamba makusudio katika aya ni Abu Bakr. Anaendelea kusema Arrazi: "Jua kwamba Mashia wote wanakanusha riwaya hii, wanasema imeshuka katika haki ya Ali bin Abu Twalib na dalili juu ya hilo ni juu ya aya inayosema: "Na hutoa zaka na hali yakua wao wanaswali
" (5:55).
Kwa hiyo neno lake Mwenyezi Mungu: "Mwenye kumcha (Mungu) zaidi ambaye hutoa mali yake kwa kujitakasa
" linaishiria kwenye aya hiyo (5:55).
Ama yale yaliyonasibishwa kwa Mashia wote, yenye kutegemewa katika njia zao ni Sahihi ya Al-Himyariyy iliyotangulia kueleza yaliyo katika riwAya Na nayofahamisha kushuka aya kwa Abu-Dahdaah El- Ansari.
Ndio, imekuja riwaya dhaifu kutoka kwa Barqi naye kutoka kwa Ismail bin Mahraan naye kutoka kwa Ayman bin Muhriz naye kutoka kwa Abu Basiyr naye kutoka kwa Abu Abdillah amesema: Ama kauli yake: Na ataepushwa nao mwenye kumcha (Mungu) zaidi, mwenye kumcha (Mungu) zaidi ni Mtume(s.a.w.w)
na wafuasi wake na Ambaye hutoa mali yake kwa (kutaka) kujitakasa, huyo ni Amiirul-Mui'miniin Ali
na ndiyo kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na wanatoa zaka na hali wao ni wenye kuswali
." (5:55).
Na kuhusu aya "Na hali ya kuwa hakuna yoyote aliyemfanyia hisani ili awe anamlipa
" huyo ni Mtume(s.a.w.w)
ambaye hana yoyote wa kumlipa hisani na hali hisani zake ni zenye kuenea kwa watu wote.
Riwaya hiyo ni dhaifu kwa upande wa mapitio yake na kufuatilia kwake bila ya kuangalia tafsir. Dalili iliyowazi ya udhaifu wake ni vile kufuatilia kwake kuwa mwenye kusifiwa ni Mtume na sifa iwe juu ya Ali
kisha aya inayofuatia tena juu ya Mtume. Na kama hilo lingekuwa katika tafsiri ingeliharibika nidhamu yake kabisa. Na huyo Ayman bin Muhriz hajulikani.
Imepokjewa kutoka kwa Al Himyariyy kutoka kwa Ahmad bin Muhammad bin Abu Nasr naye kutoka kwa Abul hassan Arridha
amesema: Niliulizwa kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu: "Hakika Allah humwongoza anayemtaka na kumpoteza anayetaka. Nikamwambia: Mwenyezi Mungu akufanye uwe mwema "Hakika watu katika watu wetu wanadai mwamba maarifa ni yenye kuchumwa na kwamba wao wakiangalia vizuri wanapata heri". Akakanusha hilo na akasema: "Hawa watu hawachumi heri wao wenyewe, hakuna yeyote katika watu isipokuwa ni wajibu kuwa heri inatokana na yule ambaye heri inatoka kwake.
Ama uongofu ambao makusudio yake ni kufikisha kwenye matakwa, huo ni wa Mwenyezi Mungu kwa sababu ni katika mambo ya Mungu. Ama upotevu ambao makusudio yake ni kupoteza kwa upande wa njia na wala sio kupoteza kwa kuanzia ambako hakuegemezwi kwa Mwenyezi Mungu, ni kwa Mwenyezi Mungu pia, kwa kuwa yeye ni mwenye kuzuwiya kushusha rehema na kukosekana uongofu. Ikiwa uongofu unatokana naye basi kuzuilika nako pia kunatokana naye.