21
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
SURA ALAQ (PANDE LA DAMU) (NA. 96)
INA AYA 19
Kwa jina la Allah Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.
اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ ﴿١﴾
1. Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba
خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ ﴿٢﴾
2. Ameuumba mwanadamu katika pande la damu!
قْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ ﴿٣﴾
3. Soma na Mola wako ni Mkarimu mno.
الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ ﴿٤﴾
4. Ambaye amefunza (kuandika) kwa kalamu.
عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ ﴿٥﴾
5. Amefunza mwanadamu asilolijua.
كَلَّا إِنَّ الْإِنسَانَ لَيَطْغَىٰ ﴿٦﴾
6. Si hivyo! Hakika mwanadamu hupetuka mipaka.
أَن رَّآهُ اسْتَغْنَىٰ ﴿٧﴾
7. Kwa kujiona amejitosha
إِنَّ إِلَىٰ رَبِّكَ الرُّجْعَىٰ ﴿٨﴾
8. Hakika marejeo ni kwa Mola wako.
أَرَأَيْتَ الَّذِي يَنْهَىٰ ﴿٩﴾
9. Je, umemwona ambaye humkataza.
عَبْدًا إِذَا صَلَّىٰ ﴿١٠﴾
10. Mmja, ( wa Mungu) anaposwali?
أَرَأَيْتَ إِن كَانَ عَلَى الْهُدَىٰ ﴿١١﴾
11. Je, inaonaje! Ikiwa yuko katika uongofu.
أَوْ أَمَرَ بِالتَّقْوَىٰ ﴿١٢﴾
12. Au akawa anaamrisha wema?
أَرَأَيْتَ إِن كَذَّبَ وَتَوَلَّىٰ ﴿١٣﴾
13. Je, unaonaje! Akikadhi bisha na akaipa mgongo.
أَلَمْ يَعْلَم بِأَنَّ اللَّـهَ يَرَىٰ ﴿١٤﴾
14. Je, hajui kwamba Allah anaona?
كَلَّا لَئِن لَّمْ يَنتَهِ لَنَسْفَعًا بِالنَّاصِيَةِ ﴿١٥﴾
15. Naakome! Naapa asipokoma, tutamkokota kwa nywele za utosi.
نَاصِيَةٍ كَاذِبَةٍ خَاطِئَةٍ ﴿١٦﴾
16. Utosi wenye kusema uongo, wenye kufanya makosa.
فَلْيَدْعُ نَادِيَهُ ﴿١٧﴾
17. Haya na awaite wanachama wenzake.
سَنَدْعُ الزَّبَانِيَةَ ﴿١٨﴾
18. Na sisi tutawaita Malaika wa adhabu.
كَلَّا لَا تُطِعْهُ وَاسْجُدْ وَاقْتَرِب ﴿١٩﴾
19. Naakome! Usimtii (bali) sujudu (swali) na ujikurubishe ( kwa Mola wako).
UBAINIFU
Amri kwa Mtume kupokea Qur'an kwa Wahyi utokao kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) Hii ni ndio Sura ya kwanza kushuka katika Qur'an na mpangilio wake wa maneno haukatai kwa imeshuka kwa mpigo (mkupuo mmoja) kama tutakavyoeleza - Nayo imeshuka Makka , bila ya shaka yoyote.
Aya Na 1
Amesema Raghib kusoma ni kukusanya herufi na matamko, lakini sio mkusanyiko wowote ni kusoma. Haiwezekani kusema umewasomesha watu kwa kuwa umewakusanya. Kwa vyovyote iwavyo husemwa umesoma kitabu kama ukizikusanya herufi na matamko na kuyachunguza katika bongo hata kama hukuyatamka. Na husemwa umesomea mtu kama ukimkusanyia herufi na matamko katika usikizi wake; vile vile hutumiwa neno Tilawa kwa maana ya kisomo kama alivyolitumia Mwenyezi Mungu neno hilo katika Sura ya (98:2): Naye (ni) Mtume aliyetoka kwa Allah anayewasomea madaftari yenye kutakasika.
Kwa dhahiri maana ya neno Soma ni amri ya kupokea yale anayopewa wahyi na Malaika. Kwa ujuma ni amri ya kusoma kitabu ambayo inatokana na kitabu hichi hicho; kama alivyosema msemaji mmoja katika mwanzo wa kitabu chake kwa yule aliyempeleka "Soma kitabu changu hiki na ukifanyie kazi" kwa hivyo hiyo amri ya kusoma kitabu, imetokana na kitabu chenyewe. Mpangilio huu wa maneno:
Kwanza
: unatilia nguvu yale yaliyopokewa kwamba Sura hii ni ya kwanza kayika Qur'an kwa Mtume(s.a.w.w)
.
Pili
: Kwamba makusudio yake ni kusoma Qur'an au yaliyo katika maana yake, na sio makusudio ya kusoma chochote au kuwasomea watu ijapokuwa hilo ni miongoni mwa lengo la kushuka kwake, kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na Quran tumeigawanya sehemu mbali mbali. Ili uwasomee watu kwa kituo
".(17:106)
Na pia sio makusudio yakuwa lisome jina la Mola wako. Makusudio hasa ni kwamba jumla ya "kwa jina la Moa wako" inafungamana na kitu kilichoondolewa; kukadiriwa kwake ni hali ya kuanza na hali ya kufungua. Hilo halipingi Bismillahi inayoanza katika Sura hiyo, kuwa ni fungu katika Sura, kwani hayo ni katika maneno ya Mwenyezi Mungu aliyoanzia na kuamrisha kuanzia nayo. Kuhusu "Mola wako ambaye ameumba; inaonyesha milki ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe vyote, kwani wanaoamshirikisha Mungu walikuwa wakisema Mwenyezi Mungu kazi yake ni kuumba na kupatisha vitu tu! Lakini hana ufalme wowote juu yake. Mwenyezi Mungu analipinga hilo kwa kusema 'Mola wako ambaye ameumba' kwa kutumia neno Rabb ambalo limaana ya kumiliki na kukiangalia vizuri kile kinachimilikiwa kwa hiyo kuumba na kumiliki ni kwake Yeye peke yake.
Aya Na 2
Neno Alaq lina maana ya damu iliyoganda na makusudio yake ni ile inayogeuka kutoka tone la manii katika mfuko wa uzazi. Hiyo inaonyesha vile Mwenyezi Mungu anavyoangalia vizuri na kupanga mambo ya mtu, tangu anapokuwa pande la damu mpaka anapokuwa mtu kamili kwa namna ya kiajabuajabu kiasi ambacho akili zinakwama kujua hilo. Hivyo mtu hatimii wala hakamiliki ila kwa mipangilio inayotokana na Mungu ambayo ni kutoka umbo moja baada ya jingine. Kwa hiyo mtu hana budi kumfanya Mungu pekee ndiye mlezi. Na maneno haya ni hoja ya kuwa Mmoja Mlezi (Mungu).
Aya Na 3
Amri ya kusoma hapa ni ya kusisitiza ile amri ya kwanza. Imesemwa makusudio yake hapo ni kuamrisha kisomo kwa watu yaani kuwafikishia (Tabligh) kama ilivyosemwa kwamba amri ya kwanza ya kusoma na hii ya pili zote ni kwa ajili ya kuwasomea watu. Lakini njia zote mbili hizi haziko wazi
Aya Na 4-5
Herufi Ba ni yakusababisha, kwa maana ya amemfundisha mtu kusoma au kuandika kupitia kalamu. Maneno haya ni kwa ajili ya kuitia nguvu nafsi ya Mtume(s.a.w.w)
na kumwondoa kiherehere; kwa kuamrisha kusoma na hali ya kuwa yeye ni ummiy haandiki wala hasomi. Kama vile ameambiwa; soma kitabu cha Mola wako anachokufunulia wala usipogope na hali ya kuwa Mola wako ni Mtukufu ambaye amefundisha mtu kusoma kupitia kalamu, kwa hiyo yeye anaweza kukufundisha kusoma maandishi yake na hali ya kuwa wewe ni ummiy (usiyejua kusoma wala kuandika).
Kisha akaeneza Mwenyezi Mungu (s.w.t) neema, akataja kumfundisha kwke mtu asilolijua akasema: Amemefundisha mtu asilolijua. Hilo ni kuzidisha kuutia nguvu moyo wa Mtume(s.a.w.w)
.
Makusudio ya mtu kwa dhahiri ni jinsi ya mtu yoyote. Imesemwa makusudio yake ni Mtume(s.a.w.w)
. Na imesemwa ni Mtume Idris
kwa sababu yeye ndiye mtu wa kwanza kuandika kwa kalamu; Pia imesemwa ni kila Mtume aliyekuwa akiandika. Lakini njia zote ni dhaifu zilizo mbali na ufahamu.
Aya Na 6-7
Makatazo ya kukufuru neema, baada ya Mwenyezi Mungu kumneemesha mtu kwa neema kubwakubwa; mfano kumfundisha kwa kalamu na mengineyo. Ni juu ya mtu kumshukuru juu ya hilo, lakini mtu hukufuru neema zake Mwenyezi Mungu Mtukufu na kupetuka mpaka. Na hiyo ni kutokana na kwamba yeye anajishughulisha na sababu za kidhahir ambazo zinamfikisha kwenye makusudio yake. Kwa hiyo anaghafilika na Mola wake na kuona kuwa hana haja na kumkumbuka na kumshukuru juu ya neema yake, ndipo anamsahau na kupetuka mpaka.
Aya Na 8
Kwa dhahiri maana ya neno marejeo hapa ni kiaga cha mauti na kufufuliwa. Hapa anaambiwa Mtume(s.a.w.w)
na imesemwa anaambiwa mtu. Kauli ya kwanza ndiyo iliyodhahiri zaidi.
Aya Na 9-13
Yanatajwa baadhi ya mambo ya mtu mwenye kupetuka mpaka. Makusudio ya mja anayeswali hapa ni Mtume(s.a.w.w)
kutokana na unavyofahamisha mwisho wa aya za mwisho wakati Mwenyezi Mungu anapomwamrisha Mtume(s.a.w.w)
kusujudu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kumkataza kumtii huyo anayekataza. Mpangilio wa aya hizi kwa kukadiri kuwa Sura ni ya kwanza kushuka na kushuka kwake mara moja, basi unafahamisha kuwa Mtume alikuwa akiswali kabla ya kushuka Qur'an na pia unafahamisha utume wake kabla ya risala yake ya Qu'an. Ama yale waliyoyataja baadhi yao kwamba swala haikufaradhiwa mwanzo wa utume isipokuwa ilifaradhiwa usiku wa Miraj kwa kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Simamisha swala jua linapopinduka mpaka giza la usiku na Qur'an ya Alfajiri
"(17:78).
Hiyo inafahamisha kuwa swala tano za kila siku zilifaradhiwa kwa namna yake hasa rakaa mbili mbili, katika usiku wa Miraji, lakini hakuna linalofahamisha kuwa haikuweko kabla yake. Na zimeshuka Sura nyingi kuwa haikuweko kabla yake. Na zimeshuka Sura nyingi kabla ya sura ya 17 (Israi) zinazotaja swala kama Al- Muddathtir, Al-Muzammil nk. kwa ibara tofauti ijapokuwa namna ya swala yenyewe haikudhihirishwa, isipokua ilikuwa ni namna ya kusoma Qur'an na kusujudu, vile vile zimepokewa baadhi ya riwaya za swala ya Mtume(s.a.w.w)
pamoja na Khadija bin Ali katika mwanzo wa utume, ingawaje haikutajwa namna ya swala yenyewe. Kwa ujumla maana ya aya ni kumfahamisha yule ambaye anamkataza mja anaposwali na huyo anayekataza anajua kuwa Mwenyezi Mungu anamwona yale anayoyafanya. Nifahamishe huyo anaemkataza mja anayeswali aliye juu ya uongofu au anayeamrisha kumcha Mwenyezi Mungu anamwona?, Je, hastahiki adhabu?
Aya Na 14
Kuhusu "Hivi hajui kuwa Mwenyezi Mungu anamwona
". Makusudio ya kujua hapa yamekuja kwa njia ya kulazimsha kujua. Kwa sababu kuitakidi kuwa Mwenyezi Mungu ni Muumba wa kila kitu kunalizimisha kuitakidi kuwa Yeye (Mwenyezi Mungu) ana ujuzi wa kila kitu. Na huyo mkatazaji alikuwa ni mshirikishaji Mungu anayeabudu masananmu, na wanaobudu masanamu wanakubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa kila kitu na wanamtakasa na sifa za upuungufu, kwa hiyo wanaona kuwa Mwenyezi Mungu hapitwi na kitu wala kushindwa na kitu chochote.
Aya Na 15 - 16
Kuusifu utosi wenye kusema uongo ni kwa njia ya fumbo kwa maana ya uongo wa mwenye utosi huo. Maana ya aya kwa jumla ni makemeo na utisho; nikuwa mambo hayako kama anavyotaka yeye. Ninaapa kama hatajizuia na makatazo yake, tutamchukua kidhalili na kumkokota mwenye adhabu ya utosi ambao mwenye utosi huo ni mwongo kwa anayosema na mkosaji kwa anayofanya. Imesemwa maana yake ni tutautia kovu utosi wake kwa moto na kuufanya mweusi.
Aya Na 17-18
Anaeleza Mwenyezi Mungu udhaifu ya huyo mwenye kukataza mja kuswali, kwa kusema: Haya na awaite hao watu wa baraza lake (wanachama wenzake) na sisi tutawaita Malaika wa motoni, wakali wenye nguvu, ambao hawana wa kuwazuyiwa.
Aya Na 19
Ni kusisitiza makemeo. Makusudio ya "Usimtii
" ni usimtii anayekukataza swala. Hii inafahamisha kuwa makusudio ya kusujudu ni swala. Huenda swala aliyokuwa akiiswali Mtume(s.a.w.w)
wakati huo ni tasbih na kumsujudia Mwenyezi Mungu. Imesemwa makusudio yake ni kusujudu kwa ajili ya kisomo cha Sura hi ambayo ni moja ya Sura nne za Azaim ( zenye sijda za wajib). Na kujikurubisha ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Imesemwa ni kujikurubisha kutokana na thawabu za Mwenyezi Mungu.
Utafiti Wa Hadithi Katika Durril-Manthur ametoa Abdurrazzaq, Ahmad, Abdu bin Hamid, Bukhari, Muslim, Ibn Jariyr na Ibn Ambari katika Masahif. Vile vile Ibn Murdawayh na Bayhaqi katika njia ya Ibn Shihab kutoka kwa Urwa bin Zubeir naye kutoka kwa Aisha mama wa waumin amesema "mwanzo wa kudhihirikiwa Mtume(s.a.w.w)
na wahyi ni ndoto njema katika usingizi. Na alikuwa haoti ndoto ila itadhihiri mfano wa Falaq (nyota ya asubuhi).
Kisha akawa anapendelea kukaa mbali na alikuwa akipendelea kwenda Jabal Hiraa na kuabudu huko kwa idadi ya nyusiku kadhaa akiwa amechukua chakula, kisha hurudi kwa Bibi Khadija kuchukua chakula. Alikuwa akifanya hivyo mpaka ilipomjia haki naye akiwa huko Jabal Hiraa. Akamjia Malaika akasema: "Soma" akamwambia "Mimi si msomaji". Mtume anasema: Akanishika na kunikamua mpaka nikafikiwa na kughumiwa, kisha akaniacha, akasema "Soma" nikasema "mimi si msomaji" akanishika tena na kunikamua kama kwanza kisha akaniacha akaniambia "Soma" nikamwambia "mimi si msomaji". Akanishika tena mara ya tatu kisha akaniwacha akaniambia: "Soma kwa jina la Mola wako ambaye ameumba (kila kitu). Amemuumba Mtu kutokana na pande la damu. Soma na hali yakuwa Mola wako ni Mkarimu. Ambaye amemfundisha (mtu) kuandika kwa kalamu".
Akarudi Mtume(s.a.w.w)
kwa Bibi Khadija akiwa anatetemeka moyo wake, akasema: "Nifunikeni, nifunikeni" wakamfunika mpaka ilipomwondokea fazaa, akamuhadithia Khadija habari hiyo na akamwambia 'ninaogopa juu ya nafsi yangu' Khadija akamwambia 'Hapana Mwenyezi Mungu hakukufedhehesha kabisa. Hakika wewe utaunga udugu, utachukua taabu, utawakaribisha wageni na utasaidia upande wa haki'.
Akaondoka Khadija mpaka kwa binamu yake anayeitwa Waraqah bin Naufal bin Asad bin Abdulaziz naye alikuwa ni mkristo katika zama za ujahili na alikuwa akiandika Kiibrania, akawa anaandika Injili kwa Kiibrania; wakati huo alikuwa mzee sana na kipofu. Khadija akamwambia "Ewe binamu nisikilize". Akamwambia "umeona nini?". Akamfahamisha yale aliyoyaona Mtume(s.a.w.w)
. Akamwambia "huyo ni msiri ambaye alimshukia Musa! Natamani ningelikuwa kijana, natamani niwe hai wakati watakapokutoa watu wako!" Akasema Mtume(s.a.w.w)
"hivi watanitoa?" Akasema, "ndio hakuna mtu yeyote aliyekuja na mfano wa uliyokuja nayo wewe ila hupingwa na nikiwahi siku yako hiyo nitakusaidia." Lakini hakuendelea kuishi Waraqah na akafa katika kipindi cha wahyi.
Amesema Ibn Shihab: "Amenifahamisha Abu Salama bin Abdurrahman kwamba Jabir bin Abdillahi El-Ansari amesema: "Amesema Mtume(s.a.w.w)
- akiwa anazungumzia kipindi cha wahyi akasema katika mazungumzo yake mbiguni, nikanyanyua macho yangu, nikamwoma Malaika yule aliyenijia katika Jabal Hiraa kwenye kiti kati ya mbingu na ardhi, nikamwogopa na kurudi nyumbani, nikasema nifunikeni nguo! Nifunikeni! Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha aya: "Ewe mwenye kujifunika maguo, simama uonye (watu) na Mola wako umtukuze. Na nguo zako uzisafishe na mabAya Na puuze
." (74:1-5).
Katika hiyo hiyo Durril-Manthur ametoa Ibn Abu Shaybah, Ibn Jariyr nna Abu Naim kutoka kwa Abdalla bin Shaddad amesema: "Jibril alimjia Muhammad(s.a.w.w)
akasema: "Ewe Muhammad "Soma". Akasema "Nisome nini?" Akamshika kisha akasema ewe Muhammad "Soma". Akasema "nisome nini?" Akasema : "Soma kwa jina la Mola wako ambaye ameumba (kila kitu) mpaka akafikia amemfunza mwanadamu asilolijuwa."
Mtume akaja kwa Khadija akamwambia, "Ewe Khadija naona amenidhuru." Akasema Khadija: "Hapana Mola wako hawezi kukufanya hivyo na wala kukufanyia ubaya wowote". Basi Khadija akamwendea Waraqh bin Naufal, akampa habari hiyo akasema. "Ukiwa unasema kweli, basi mumeo ni Mtume na atapata tabu kutokana na umati wake nakama nikimuwahi nitamwamini."
Kisha akachelewa Jibril kumjia, akasema Khadija naona Mola wako amechukia ndio Mwenyezi Mungu akateremsha: "Naapa kwa mwanzo wa mchana. Na kwa usiku unapotulia hakukuacha Mola wako wala hakukukasirikia
". (93:1-3).
Lakini kisa chote hiki hakiwezi kuepukana na shaka. Miongoni mwa shaka yake ni vile kutia shaka Mtume(s.a.w.w)
kuwa yule aliyoyaona ni wahyi wa Mwenyezi Mungu kutoka kwa Malaika wa Mbinguni, bali hata kudhani kuwa ameshikwa na shetani aliyemtia wazimu. Na shaka zaidi ni vile kumtegemea Mkristo Mtawa kuwa ndiye atakayemtuliza nafsi yake kwa kumfahamisha kuwa yeye ni Mtume, na hali Mwenyezi Mungu amesema: "Sema hii ni njia yangu ninailingania kwa Allah kwa ujuzi wa kweli, mimi na wanaonifuata. (12:108). "Sasa je, ujuzi wa kweli ndio huko kutulizwa moyo na neno la Waraqah? Na amesema Mwenyezi Mungu:
"Sema mimi ninayodalili wazi itokayo kwa Mola wangu
". (6:57)
Sasa dalili gani iliyo wazi katika neno la Waraqah? Na amesema tena Mwenyezi Mungu: "Hakika sisi tumekuletea wahyi kama tulivyowapelekea Nuh na Manabii (wengine) baada yake
." (4:163). Je hao Mitume wengine walikuwa wakitegemea kupata utume wao mfano wa kisa hiki?
Ilivyo ni kwamba wahyi wa utume unalazimisha kuwepo yakini kutoka kwa Mtume mwenyewe kuwa umetokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hayo ndio yaliyopokewa kutokana na Maimamu wa Ahlul Bait. Katika Majmau kuhusu Aya Na tisa; ni kuwa Abu Jahl alisema; "Je Muhammad anaweka uso wake mchangani (anaswali) mbele yenu?" Wakasema "ndio". Akasema "Ninaapa kwa yule anayeapiwa, nikimwona nitaikanyaga shingo yake". Akaambiwa "huyo anaswali". Akawa anakwenda kumkanyaga mara akawa anarudi nyuma huku akijikinga kwa mikono yake wakasema: "Unanini ewe Abul Hakam?" Akasema: "Hakika kati yangu na yake kuna handaki la moto na hawa wenye mbawa". Akasema Mtume: "Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko katika uweza wake, lau angelinikurubia tu! Wangelimchanachana Malaika. Ndipo akateremsha Mwenyezi Mungu Aya Na tisa mpaka mwisho wa Sura. Hayo ameyapokea Muslim katika Sahih.
Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu aya hiyo hiyo nikuwa ilishuka juu ya Walid bin El-Mughira aliyekuwa akiwakataza watu kuswali na kutiiwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ufahamisho wa hayo haupingi kuwa mwenye kuswali ni Mtume(s.a.w.w)
.
Katika Majmau kwenye hadith ya Abdallah bin Masud kwamba Mtume(s.a.w.w)
amesema: "Mja anakuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu anapokuwa amesujudu". Katika Kafi kwa isnadi wa Wash-shai amesema: "Nimemsikia Arridhaa
akisema: "Karibu zaidi anapokuwa mja na Mwenyezi Mungu ni anaposujudu, ndio maana akasema Mwenyezi Mungu "Sujudu na ujikurubishe (kwa Mola wako)".
Katika Majmau amepokea Abdulla bin Sinan kutoka kwa Abu Abdillahi amesema: Al - Azaim (Sura Sajda za wajibu) ni nne (Sura ya 32, 41, 52 na 96), zisizokua hizo katika Qur'an ni sunna tu, kusujudu!.