14
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
SURA AL-FAJR (ALFAJIRI) (NA. 89)
INA AYA 30
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu
وَالْفَجْرِ ﴿١﴾
1. Naapa kwa Alfajiri.
وَلَيَالٍ عَشْرٍ ﴿٢﴾
2. Na (kwa) masiku kumi.
وَالشَّفْعِ وَالْوَتْرِ ﴿٣﴾
3. Na (kwa) shufwa na witiri.
وَاللَّيْلِ إِذَا يَسْرِ ﴿٤﴾
4. Na (kwa) usiku unapopita.
هَلْ فِي ذَٰلِكَ قَسَمٌ لِّذِي حِجْرٍ ﴿٥﴾
5. Katika hayo mna kiapo kwa mwenye akili.
أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِعَادٍ ﴿٦﴾
6. Je, hujui jinsi Mola alivyoifanya (kabila) ya Aad.
إِرَمَ ذَاتِ الْعِمَادِ ﴿٧﴾
7. Iram wenye nguzo ndefu?
الَّتِي لَمْ يُخْلَقْ مِثْلُهَا فِي الْبِلَادِ ﴿٨﴾
8. Ambayo haikuumbwa mfano wake katika miji.
وَثَمُودَ الَّذِينَ جَابُوا الصَّخْرَ بِالْوَادِ ﴿٩﴾
9. Na (kabila) ya Thamud ambao walikua wakipasua majabali katika (mji wa) waad.
وَفِرْعَوْنَ ذِي الْأَوْتَادِ ﴿١٠﴾
10. Na Firaun mwenye vigingi.
الَّذِينَ طَغَوْا فِي الْبِلَادِ ﴿١١﴾
11. Ambao walipetuka mipaka katika miji.
فَأَكْثَرُوا فِيهَا الْفَسَادَ ﴿١٢﴾
12. Wakazidisha humo mambo maovu.
فَصَبَّ عَلَيْهِمْ رَبُّكَ سَوْطَ عَذَابٍ ﴿١٣﴾
13. Akawateremshia Mola wako namna za adhabu.
إِنَّ رَبَّكَ لَبِالْمِرْصَادِ ﴿١٤﴾
14. Hakika Mola wako ni Mwenye kuotea.
فَأَمَّا الْإِنسَانُ إِذَا مَا ابْتَلَاهُ رَبُّهُ فَأَكْرَمَهُ وَنَعَّمَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَكْرَمَنِ ﴿١٥﴾
15. Ama mwanadamu - Mola wake anapomjaribu, akamtukuza, akamneemesha, husema: Mola wangu amenitukuza.
وَأَمَّا إِذَا مَا ابْتَلَاهُ فَقَدَرَ عَلَيْهِ رِزْقَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَهَانَنِ ﴿١٦﴾
16. Ama anapomjaribu akampunguzia riziki yake husema Mola wangu amenitweza.
كَلَّا بَل لَّا تُكْرِمُونَ الْيَتِيمَ ﴿١٧﴾
17. La, si hayo tu! Bali nyinyi humumtukuzi yatima.
وَلَا تَحَاضُّونَ عَلَىٰ طَعَامِ الْمِسْكِينِ ﴿١٨﴾
18. Wala hamhimizani katika kumlisha maskini.
وَتَأْكُلُونَ التُّرَاثَ أَكْلًا لَّمًّا ﴿١٩﴾
19.Na mnakula mirathi kula kwa pupa.
وَتُحِبُّونَ الْمَالَ حُبًّا جَمًّا ﴿٢٠﴾
20. Na mnapenda mali mapenzi makubwa.
كَلَّا إِذَا دُكَّتِ الْأَرْضُ دَكًّا دَكًّا ﴿٢١﴾
21. Si hivyo! Ardhi itakapo pondwa pondwa!
وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا ﴿٢٢﴾
22. Akaja Mola wako na Malaika (wamejipanga) safu kwa safu.
وَجِيءَ يَوْمَئِذٍ بِجَهَنَّمَ ۚ يَوْمَئِذٍ يَتَذَكَّرُ الْإِنسَانُ وَأَنَّىٰ لَهُ الذِّكْرَىٰ ﴿٢٣﴾
23. Ikaletwa siku hiyo Jahannam! Siku hiyo ndipo mwanadamu atakapokumbuka, lakini kutamfaa nini kukumbuka (kwake)?!
يَقُولُ يَا لَيْتَنِي قَدَّمْتُ لِحَيَاتِي ﴿٢٤﴾
24. Atasema laiti niliyatangulizia (wema) maisha yangu.
فَيَوْمَئِذٍ لَّا يُعَذِّبُ عَذَابَهُ أَحَدٌ ﴿٢٥﴾
25. Basi siku hiyo hapana yoyote atakayeadhibu kama adhabu yake (Mwenyezi Mungu).
وَلَا يُوثِقُ وَثَاقَهُ أَحَدٌ ﴿٢٦﴾
26. Wala hapana yoyote atakayefunga kama kufunga kwake.
يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ ﴿٢٧﴾
27. Ewe nafsi iliyotua!
ارْجِعِي إِلَىٰ رَبِّكِ رَاضِيَةً مَّرْضِيَّةً ﴿٢٨﴾
28. Rejea kwa Mola wako hali yakuwa uradhi (na) mwenye kuridhiwa.
فَادْخُلِي فِي عِبَادِي ﴿٢٩﴾
29. Kisha ingia katika waja wangu (wema).
وَادْخُلِي جَنَّتِي ﴿٣٠﴾
30. Na uingie katika pepo yangu.
UBAINIFU
Katika Sura hii kuna makemeo juu ya kufungamana na dunia kwenye kufuatiwa na kupetuka mpaka na ukafiri, na kuwaogopesha watu wenye mambo hayo na ukali wa adhabu ya Mwenyezi Mungu katika dunia na akhera. Kwa hiyo Sura inabainisha kuwa mtu kwa ufupi wa mtazamo wake na ubaya wa fikra yake anaona kuwa anayoletewa na Mwenyezi Mungu miongoni mwa neema yake ni katika ukarimu wake Mwenyezi Mungu, na yale anayovaana nayo miongoni mwa ufakiri ni utwezo. Kwa hiyo anapetuka mpaka na kuwa mfisadi katika ardhi anapopata na anakufuru anapokosa. Basi yanayompata katika cheo na utajiri na katika ufakiri na dhiki ya maisha, ni mitihani na balaa za Mungu ili adhihirishe kwayo yale atakayoyatanguliza akhera yake kutoka katika dunia yake.
Basi mambo hayako kama vile anavyofikiri mtu na anavyosema, bali mambo yalivyo kama atakavyoyakumbuka itakapotuka hisabu na kuletwa adhabu, kwamba yaliyompata miongoni mwa ufakiri au utajiri na nguvu au unyonge yalikuwa ni mitihani ya Mungu. Ilikuwa inamuwezekania yeye kutangulizia kesho yake kutokana na leo yake, lakini hakufanya na akaathirika na mateso kuliko thawabu. Basi haitapata maisha mema katika akhera isipokuwa nafsi iliyotua kwa Mola wke, isiyoyumba kwa vimbunga vya balaa wala kupetuka mpaka kwa kipato au kukufuru kwa kukosa. Sura hii imeshuka Makka kwa ushahidi wa mpangilio wa aya zake.
Aya Na 1-4
Aya hizo zote ni kiapo. Huenda dhahiri ya neno Alfajiri, Alfajiri yoyote, lakini sio mbali kuwa makusudio yake ni Alfajiri ya usiku wa Ijumaa. Imesemwa ni swala ya Alfajiri na imesemwa ni mchana wote na imesemwa ni kupasuka chemchem katika miamba na mengineyo. Njia zote hizi ziko mbali. Kuhusu masiku kumi huenda makusudio ni masiku kumi ya mwanzo katika mwezi wa Dhulhijja. Imesemwa makusudio ni siku za mwisho za mwezi wa Ramadhan, na ikasemwa ni za mwanzo wake. Pia imesemwa ni siku kumi za mwanzo za mwezi wa Muharram na ikasemwa kuwa ni ibada ya masiku kumi kuchukulia kuwa makusudio ya Alfajiri ni swala ya Alfajiri. Kuhusu Shufwa wa Witiri maana yanakubali kufungamana na kuwa ni siku wa Tarwiya (tarehe 8 Dhul-hijja) na siku ya Arafa (tarehe 9 Dhul-hijja). Imesemwa kuwa makusudio yake ni swala mbili ( rakaa mbilimbili na rakaa moja) katika mwisho wa usiku. Na imesemwa ni swala yoyote, ziko mbili mbili na moja.
Pia imesemwa kuwa Shufwa ni siku ya Idd ya Dhul-hijja wa Witiri ni siku ya Arafa, na imesemwa Shufwa ni viumbe vyote, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema: "Na tukawaumba wanawake na wanaume
" (78:8).
Na Witiri ni Mwenyezi Mungu (s.w.t) Kuna riwaya nyingi zitakazokuja juu ya kauli hizi katika utafiti wa hadith 8 Vile Vile imesemwa makusudio yake ni hisabu ya viwiliviwili na kimojakimoja na kwamba kuapa kwa hisabu, ni kuwa kudhibiti idadi katika kiasi ni katika nema kubwa itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Imesemwa kuwa ni viumbe vyote, kwa sababu vitu vyote ama vitakuwa ni jozi au kimoja. Imesemwa kuwa makusudio ya Witiri ni Adam na Shufwa ni kuwa pamoja na mkewe Hawa.
Na imesemwa Shufwa ni mchana, na usiku, na Witiri ni mchana ambao, hauna usiku nao ni siku ya Kiyama. Imesemwa Shufwa ni Safa na Marwa na Witiri ni Al-Ka'aba, na imesemwa ni siku za kabila la Ad na Witiri ni nyusiku zake. Na imesemwa Shufwa ni milango ya motoni saba. Na zaidi ya hayo mengi yaliyosemwa zaidi ya kauli thelethini na sita (36). Kuhusu kauli yake; Na (kwa) usiku unapopita ni kama Aya Na 33, Sura ya 74 inayosoma: "Na (kwa) usiku unapokucha".
Kwa dhahiri herufi Lam ni ya jinsi yaani usiku wowote, lakini wengine wamesema ni usiku wa Muzdalifa (usiku wa kuamkia Idd) ambao mahujaji wanapita kutoka Arafa mpaka Muzdalifa wanakusanyika Mahujaji kwa kumtii Mwenyezi Mungu kisha wanaamkia kwenda Mina kwa hiyo kama unavyoona itakuwa makusudio ya usiku kumi ni usiku kumi za mwanzo katika mwezi wa Hijja (Dhul-Hijja).
Aya Na 5
Ni ishara ya yaliyotangulia katika kiapo na ni swali la kuthibitisha, maana yake kwa ujumla, ni kwamba, katika hayo tuliyoyatanguliza kuyaapia yanatosha kwa mwenye akili ya utambuzi wa maneno inayopambanua haki na batili. Na Mwenyezi Mungu akiapa naye haapi isipokuwa lile lenye utukufu na daraja linakuwa ni neno la haki lenye kutiliwa mkazo ambalo halina shaka katika ukweli wake. Jawabu la kiapo limeondolewa linafahamika kutokana na yatakayotajwa katika adhabu ya watu waliopetuka mipaka na ukafiri katika dunia na akhera na thawabu ya nafsi yenye kutulia na kwamba kuneemesha kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) juu ya aliyomneemesha na kumzuilia, hakika hayo ni majaribio na mitihani. Kuondoa jawabu la kiapo na kulileta kwa njia ya fumbo, ni kutilia mkazo zaidi katika hali ya kuonya na kutoa biashara.
Aya Na 6
Ni kabila la Aad wa kwanza nao ni kaumu ya Mtume Hud
. Vimekaririka visa vyao katika Qur'an tukufu na imeonyesha kwa wao walikuwa watu wa nchi yenye machunguu ya michanga. Yameelezwa yale yanayopatikana katika visa vyao katika Sur ya Hud (11).
Aya Na 7-8
Neno Imad ni nguzo za nyumba. Kwa dhahiri ya aya mbili hizi, ni kuwa Iram ulikua ni mji uliokuwa wa aina yake wenye majumba marefu na maguzo marefu. Hakika habari zao zimekatika na athari zao zimefutika, kwa hiyo hakuna njia ya ufafanuzi itakayoeleza hali zao kiasi cha kuituliza nafsi isipokuwa yale tu, yaliyohadithiwa na Qur'an tukufu kwa ujumla juu ya kisa chao; kwamba wao walikuwa baada ya kaumu ya Nuh, wakazi wa nchi yenye machuguu ya mchanga, na walikuwa ni wenye umbo kubwa na nguvu kubwa zaidi na walikuwa na maendeleo, miji yenye majengo mengi ardhi za rutuba zenye mabustani ya mitende na mimea na mahali pazuri. Kimeelezewa zaidi kisa chao katika Sura ya Nuh.
Imesemwa kuwa makusudi ya neno Iram ni hao kaumu ya Aad - na sili na neno hilo ni jina la baba yao kwa hiyo wakaitwa kwa jina la baba yao, kama inavyosemwa Quraish kwa kukusudia wanawe au Israil kwa kukusudia wana Israil. Makusudio ya kusema wenye maguzo marefu ni kuwa wao ni watu wenye nguvu, na maana yake ni Je, hujui jinsi Mola wako alivyoifanya (kabila) ya Aad Iram wenye nguvu ambao haukumbwa mfano wao katika miji, au katika dunia nzima, lakini hayo hayaepukani na kuwa mbali na dhahiri ya tamko. Ya umbali zaidi ya yaliyosemwa kwamba makusudio ya kuwa wao ni wenye maguzo marefu, ni vile kuwa wao walikuwa ni watu wa kuazimia kusafiri katika wakati wa maleleji na mimea inaponyauka basi hurudi majumbani mwao. Kisa cha bustani ya Iram kilichopokewa kutoka kwa Wahb bin Manbih na Kaabulahbar, ni katika ngano za watu wakale tu!
Aya Na 9
Yaani walipasua miamba ya milima kwa kuichonga kuwa nyumba. Aya hii iko katika maana ya aya inayosema: "Na mnachonga milimani majumba mkastarehe tu!
" (26:149)
Aya Na 11
Huyo ni Firaun wa Musa, ameitwa mwenye vigingi- kutokana na yaliyo katika baadhi ya riwaya - kwamba yeye alikuwa akitaka kumuadhibu mtu humnyoosha juu ya ardhi na kuipingilia mikono yake na miguu yake kwa vigingi vine katika ardhi, au humnyoosha juu ya ubao na kumfanyia hivyo. Hayo yanatiliwa nguvu na yale aliyoyasimulia Mwenyezi Mungu kuhusu kauli yake Firaun akiwatisha wachawi walipomwamini Musa kwa kusema: "Nitawasulubu katika mashina ya mitende
." (20:71).
Hakika wao walikuwa wakiwamba mikono ya msulubiwa na miguu yake juu ya ubao wa kusulubu.
Aya Na 12
Ni sifa wa waliotajwa, Ad, Thamud na Firaun, maana yako wazi.
Aya Na 13
Ametaja kumimina kwa njia ya fumbo kwa maana ya kufuatana, maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu aliteremsha kwa mataghut wote hawa wenye kukithirisha uharibifu mara tu, baada ya kupetuka kwao mipaka na ufisadi wao, adhabu kali ya aina yake yenye kufuatana mfululizo.
Aya Na 14
Kuwa Mwenyezi Mungu yuko katika kuotea, ni istiara ya kufananisha Mwenyezi Mungu anavyochunga matendo ya waja wake na mtu anayeotea mtu apite amchukue, bila ya kutambua. Basi Mwenyezi Mungu anachunga matendo ya waja wake, wakipetuka mipaka na kukithirisha ufisadi tu, huwaadhibu kwa adhabu kali. Aya hiyo ni sababu ya yaliyotangulia katika mazungumzo ya kuadhibu wanaopetuka mipaka wenye kukithirisha ufisadi. Kuongeza dhamira katika neno Mola na kuwa "mola wako", ni kuonyesha kuwa desturi hiyo ya adhabu ilikuwa ni yenye kupita katika umma wake Mtume(s.a.w.w)
kama ilivyopita katika umati zilizotangulia.
Aya Na 15
Ni mtiririko wa yaliyotangulia, ndani yake mna ufafanuzi kuhusu hali ya mtu anapopewa neema ya dunia au anapozuiliwa, ni kama vile imesemwa: Hakika mtu yuko chini ya ulinzi wa Mungu, anaotewa na Mola wake kuwa je, atatengenea au ataharibika?. Kwa hiyo anamjaribu na kumtahini katika yale atakayompa katika neema yake au kunyima kwake. Ama mtu yeye akineemeshwa huhisabu kwamba huo ni utukuzo wa Mungu kwa hiyo anaweza kufanya vile anavyotaka. Hivyo anapetuka mipaka na kukithirisha ufisadi. Na akimzuilia na kuifanya chache riziki yake, huhisabu kuwa ametwezwa na Mungu, basi hukufuru na kulalamika Makusudio ya mtu ni jinsi ya mtu. Kusema kwake: akamtukuza akamneemesha ni tafsiri ya majarabio yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemtukuza na akampa nema iliamshukuru na amuabudu, lakini yeye mtu mwenyewe anajaalia ni mateso juu ya nafsi yake yanayofuatiwa na adhabu. Kuhusu neno "husema Mola wangu amenitukuza" yaani amenijaalia juu ya ukarimu unaotokana naye kwa neema ambazo amenipa, kwa hiyo ninaweza kufanya lile ninalo taka.
Kusema "Mola wangu amenitukuza" kuko katika mnasaba wa kumzingatia Mungu - hayo hayasemwi na waabudu masanamu na wanaomkanusha Mungu - na ni kwenye kujengwa juu ya kumkubali Mungu kwa kiasi cha maumbile yalivyo ijapokuwa ulimi unajizuia na hilo, vile vile aya inayofuatia.
Aya Na 16
Yaani akifanya mtihani ikawa dhiki riziki yake, basi husema Mola wangu amenidhalilisha. Kutokana na aya hizi (15 na 16) yanadhihirika mambo yafuatayo:
Kwanza
: Kukaririka majaribio na kuthibitika katika sura mbili za neema na kuzuiliwa, ni kwamba kupewa neema na kuzuiliwa vyote ni katika majaribio na mitihani ya Mungu kama alivyosema: "Tutawajaribu kwa (mambo) ya shari na heri
" (21:35).
Pili
: Kupewa neema kwa kuwa ni fadhila na rehema, ni utukufu iwapo wanadamu hawakukubadilisha kuwa adhabu. Tatu: Mtu anaona wema wake katika maisha ya dunia ni kuneemeshwa katika dunia ka neema za Mwenyezi Mungu, hivyo anaona ndio utukufu na kunyima kunakotokana na Mwenyezi Mungu anakuona kuwa ni uovu. Ilivyo nikuwa, utukufu uko katika kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa imani na amali njema, ni mamoja iwe ni utajiri au ufakiri, kupata au kukosa, yote hayo ni mitihani. Wanayo maana nyengine kuhusu aya hizi mbili lakini tumeacha kuyaonyesha kwa kutokuwa na umuhimu wowote.
Aya Na 17
Na makemeo kwa yale wanayoyasema kwamba utukufu uko katika utajiri na kwamba ufakiri na kukosa ni madhila. Basi si hivyo isipokuwa kutoa kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) neema, na kuizuia yote hayo ni mitihani anayojaribiwa mtu. Kusema kwake Mwenyezi Mungu: Bali nyinyi hamumtukuzi yatima, ni kutilia mkazo makemeo kwa kutaja baadhi ya neema ambayo haikusanyi utukufu kabisa, kama kukosa kumtukuza yatima kwa kula urathi wake na kumzuilia nao na kukosa kuhimizana juu ya kumlisha maskini kwa ajili ya kupenda mali. Kuacha kumtukuza yatima ni kumzuilia na urathi wa mzazi wake kama walivyokuwa wakiwazuilia watoto wadogo na kurithi, kama inavyotia nguvu aya inayofuatia.
Aya Na 18
Yaani hamuhimizani kutoa sadaka. Hayo yanatokana na kupenda mali sana kama ilivyo katika aya inayofuatia.
Aya Na 19
Maana ya neno Lamma ni mtu kula fungu lake na la mwengine, na kula chochote anachokipata kiwe kibaya au kizuri. Aya hii ni tafsiri ya kukosa kumtukuza yatima kama iliyotangulia.
Aya Na 20
Aya hiyo nayo inafasiri kukosa kuhimizana katika kumlisha maskini kama ilivyotangulia.
Aya Na 21
Makusudio yake ni kufika siku ya Kiyama. Hilo ni kemeo la pili kutokana na yale anayoyasema mtu katika hali mbili za utajiri na ufakiri. Aya hii inasimamia sababu za makemeo kwa maana ya kuwa, sio kama anavyosema mtu, kwani yeye atakumbuka kitakaposimama Kiyama kwamba maisha ya dunia na vilivyomo ndani yake miongoni mwa utajiri na ufakiri sio makusudio kwa dhati, bali yamekuwa ni majaribio na mitihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) Anapambanua kutokana na mitihani hiyo mwema na mwovu na inamuandalia mtu yale atakayoishi kwayo katika akhera. Hakika mtu ametatizika akadhania kuwa utukufu ndio makusudio kwa dhati akajishughulisha nao na wala asitangulize chochote kwa maisha yake ya Akhera. Kwa hiyo wakati huo atatamani huku akisema: Laiti mimi niliyatanguliza (wema) maisha yangu, lakini matamani hayatatoshelezea lolote na adhabu.
Aya Na 22
Kunasibisha kuja Mungu ni katika mikanganyo ambayo inahukumuliwa na kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) "Hakuna chochote mfano wake
" (42:11). Na yaliyokuja katika alama za Kiyama, ni katika upambanuzi wa kuondoa sababu na mapazia yaliyowaziba na kushihiri kwamba Mwenyezi Mungu ni haki iliyo wazi. Kwa hiyo yale yaliyopokewa katika hadith yanalirudia hilo kwamba makusudio ya kuja kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni kuja amri yake kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na amri siku hiyo ni ya Allah
" (82:19).
Kunatilia nguvu njia hii kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Je, kuna jengine wanalongojea ila kuwafikia Allah katika vivuli vya mawingu na kuwafikia malaika na imekwishapitishwa amri
". (2:210).
Kama tukikikutanisha na kusema kwake. "Je, wanangoja jengine (hawa makafiri) ila wawafikie Malaika? Au iwafikie amri ya Mola wako?
" (16:33). Kwa hiyo basi kuna neno lililondolewa, kukadiria kwake ni: ikaja amri ya Mola wako. Au kunasibisha kuja Mungu ni kwa majazi (fumbo) ya kiakili.
Aya Na 23
Sio mbali kuwa makusudio ya kuletwa Jahannam ni kudhihirishwa, kama ilivyo katika kauli yake. "Basi tumekuondolea pazia yako kuona kwako leo kumekuwa kukali
" (50:22).
Kusema kwake "Siku hiyo atakumbuka mtu" yaani atakumbuka kwa uwazi zaidi kwamba yale yaliyokuwa yakimjia katika maisha ya dunia miongoni mwa heri au shari yalikuwa ni majaribio ya Mwenyezi Mungu na mitihani yake na yeye akapuuza. Hivyo ndivyo unavyofahamisha mpangilio wa maneno. Kusema kwake "wapi kutamfaa kukumbuka" ni fumbo la kukosa kunufaika na kukumbuka isipokuwa kukumbuka kungefaa kama angekuunganisha na kutubia na kutenda amali njema kwa yale aliyoyapuuza, na leo ni siku ya malipo sio siku ya kutubia na kufanya amali.
Aya Na 24
Maisha hapa ni ya akhera au ni maisha ya kihakika ambayo ndiyo hayo maisha ya akhera, kama kulivyozindua kusema kwake: "Na hayakuwa haya maisha ya dunia ila ni upuzi na mchezo; na nyumba ya akhera ndio maisha hasa: Laiti wangalijua
". (29:64) Makusudio ya kuyatanguliza maisha ni kuyatangulizia amali njema.
Aya Na 25-26
Dhamir katika neno adhabu na kufunga inamrudia Mwenyezi Mungu. Yaani siku hiyo hakika adhabu yake na kufunga kwake kutakuwa zaidi ya adhabu ya kiumbe chochote. Wengine wamesoma kwa Fat'ha ya Dhali na Thau. Dhamir kwa kisomo hiki itakuwa inamrudia mtu, yaani hataadhibishwa yoyote siku hiyo mfano wa adhabu ya mtu wala hatafungwa yoyote siku hiyo mfano wa kufunga kwa mtu.
Aya Na 27
Mpangilio wa maneno uonaokubaliana na 'nafsi' hii kutokana na yale yaliyotajwa kabla yake katika sifa zinazofungamana na dunia, upitukaji mipaka, ufisadi na ukafiri na yale yaliyoahidiwa katika mwisho mbaya, unaonyesha kuwa nafsi yenye kutulia ni ile inayotulizana kwa Mola wake na kurudhia kile kinachoridhiwa na Mola wake, inajiona kuwa ni mtumwa asiyejimiliki na chochote katika kheri na inaiona dunia ni nyumba ya kupita, na inayoyakabili katika hiyo dunia miongoni mwa utajiri au ufakiri, manufaa au madhara, ni majaribio na mitihani ya Mungu. Kwa hiyo mtiririko wa neema haumpelekei kupetuka mipaka, kufanya ufisadi mwingi au kujifanya mkubwa wala ufakiri na kukosa kitu hakumuingizi katika ukafiri na kuwacha kushukuru, bali yeye ni mwenye kutulizana, hakosei njia yake yenye kunyooka kwa kupetuka mipaka au kuwapitusha mipaka wengine.
Aya Na 28
Kuisifu nafsi kwa hali yakuwa radhi ni kwamba kutulizana kwale kwa Mola wake kunalazimisha kuridhia kwake yale yaliyokadiriwa na kuhukumiliwa na wala hayamchukizi. Mtu akimridhia Mola wake naye humridhia, kwani Mwenyezi Mungu S.W.T. huchukia sana kutoka mja katika kipambo chake. Basi akilazimiana na njia ya kuwa mja wa Mwenyezi Mungu, litawajibisha hilo radhi ya Mola wake, kwa hiyo ndio maana hali ya kuridhia imefuatishwa na kuridhiwa.
Aya Na 29
Inaungana na aua iliyotangulia inafahamisha kuwa mwenye nafsi yenye kutulia yuko katika kundi la waja wa Mwenyezi Mungu. Hilo ni kwamba alipotulia kwa Mola wake alijiondoa kujiona huru, na akaridhia ile iliyohaki kwa Mola wake, akaona dhati yake, sifa zake na vitendo vyake ni miliki ya Mola wake. Hakupita katika yaliyokadiriwa kuhukumiliwa wala katika yaliyo amrishwa na kukatazwa isipokuwa yale anayoyataka Mola wake. Huko ndiko kudhihiri uja wenye kutimia. Kwa hiyo kusema kwake "ingia katika waja wangu" ni ikrari ya mahali pa uja wake hiyo nafsi. Neno lake "na ingia katika pepo yangu" ni kubainisha kituo chake. Kuitegemeza pepo kwa dhamiri ya mwenye kusema (pepo yangu) ni utukuzo mahsusi wala halipatikani hilo katika maneno yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) isipokuwa katika aya hii tu!.
Utafiti Wa Hadithi Katika Majmau kuhusu kusema kwake "na (kwa) Shufwa na Witiri, imesemwa kuwa Shufwa ni kuumba kwa sababu Mwenyezi Mungu amesema: "Na tukawaumba nyinyi wanaume na wanawake (jozi)
" (78:8). na Witiri ni Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hadithi hiyo imeyoka kwa Atiyal-Aufiy, Abu Saleh, Ibn Abbs na Mujahid, hiyo ni riwAya Na Abu Saad El-Khudriy naye amepokea kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
.
Imesemekana kuwa Shufwa na Witiri ni swala: kuna katika hiyo swala ya Shufwa na ya Witiri. Hiyo ni riwAya Na Ibn Haswin naye amepokea kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
.
Imesemwa kuwa Shufwa ni siku ya kuchinja na Witiri ni siku ya Arafa, kutoka kwa Ibn Abbas Akrama na Adh-Dhah-hak nayo ni riwAya Na Jabir kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
.
Imesemwa kuwa Shufwa ni siku ya Tarwiya (siku ya nane ya mwezi Dhul-Hijja) na Witiri ni siku ya Arafa (siku ya tisa ya Dhul-Hijja), hayo yamepokewa kutoka kwa Abu Jaffar na Abu Abdillah.
Riwaya hizo tatu zimepokewa kwa njia ya Ahli Sunnah. Inawezekana kukusanya kati ya hizo riwaya kwamba makusudio ni Shufwa na Witiri yoyote. Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu "Masiku kumi" amesema ni ya mwezi wa Dhul-Hijja na "Shufwa na Witiri" amesema ni rakaa mbili na moja. Katika hadith Shufwa ni Hassan na Hussein na Witiri ni Amiirul Muuminiin
. Katika riwAya Na Abu Jarud, kutoka kwa Abu Jaffar kuhusu Aya Na tano anasema ni "Mwenye akili". Katika ulal kwa isnadi yake kwa Abana Al-Ahmar amesema: "Nilimuuliza Abu Abdillahi kuhusu kusema kwake Mwenyezi Mungu. Na Firaun mwenye vigingi, kwanini ameitwa hivyo?" Akasema : "Kwa sababu alikuwa anapomwadhibu mtu humtandaza juu ya ardhi na kumnyoosha mikono yake na miguu yake kisha humwamba kwa vigingi vinne. Mara nyengine humtandaza juu ya ubao na kumwamba miguu yake na mikono yake kwa vigingi vine, kisha humwacha mpaka afe, ndio Mwenyezi Mungu akamwita mwenye vigingi."
Katika Majmau kuhusu "Hakika Mola wako ni mwenye kuotea" imepokewa kutoka kwa Ali
kwamba yeye amesema: Hakika maana yake ni kwamba Mola wako ni muweza wa kuwalipa waasi malipo yao. Katika hiyo hiyo Majmau imepokewa kwa Swadiq amesema maana ya neno Mirswad ni korongo kwenye Swirat halipiti korongo hilo mja ambaye hakujiweka kimja. Kutoka kwa Ghawali naye kutoka kwa Aswadiq
katika hadithi ya kutafsiri kauli ya Mwenyezi Mungu (s.w.t): "Na dhun-nun (Yunusi) alipoondoka hali amechukiwa na akadhani ya kwamba hatutamdhikisha." (21:87) Amesema: Husikii kauli yake Mwenyezi Mungu. "Ama amjaribupo, akamdhikisha riziki yake, husema: Mola wangu amenitweza"? Katika Tafsiri ya Qummi katika riwAya Na Abu Jarud, kutoka kwa Abu Jaffar
kuhusu kauli yake "si hivyo ardhi itakapopondwa pondwa' Amesema hilo ni tetemeko.
Katika Durril-Manthur ametoa Ibn Murduwayh kutoka kwa Ali bin Abu Twalib amesema: "Amesema Mtume(s.a.w.w)
he, mnajua nini tafsiri ya aya hii! "Si hivyo ardhi Takapondwa pondwa ikaleta siku hiyo Jahannam" akasema: Kitakapokuwa Kiyama Jahannam itaongozwa kwa hatamu elfu sabini kwa mikono ya Malaika elfu sabini itachomoza mchomozo mmoja, lau Mwenyezi Mungu sikuifunga ingeliunguza mbingu na ardhi. Hadith hii pia ni yenye kupokewa kutoka cha Amali Sheikh kwa isnadi yake kutoka kwa Arridha naye kutoka kwa baba yake naye kutoka kwa Ali
naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
.
Katika Uyun katika mlango wa yaliyokuja kutoka kwa Arridha katika Akhbaru Tawhid kwa isnadi yake kutoka kwa Ali bin Fadh-dhal naye kutoka kwa baba yake amesema: Nilimuuliza Arridha
kuhusu kusema kwake Mwenyezi Mungu "Na akaja Mola wako na Malaika (wamejipanga) safu kwa safu" Akasema: "Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hasifiwi na kuja na kwenda isipokuwa maana ni, na ikaja amri ya Mola wako."
Katika Kafi kwa isnadi yake kutoka kwa Sadiyr Asswayrafiy amesema: "Nilimwambia Abu Abdillah
niwe mkombozi wako ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Je, muumin anachukia anapotolewa roho yake akasema: Hapana, hakika yeye anapojiwa na Malaika wa Mauti kuchukua roho yake hufadhaika, Malaika wa Mauti huwambia: Ewe walii wa Mwenyezi Mungu usifadhaike, ninaapa kwa ambaye amempa utume Muhammad, hakika mimi nitakufanyia wema na upole kuliko mzazi, fungua macho uone.
Hapo atafanishiwa Mtume(s.a.w.w)
, Amirul Muminiin, Fatima, Hassan and Hussein na Maimamu katika kizazi chao
ataambiwa hawa ni marafiki zako. Atafungua macho yake na atanadi mnadi kutoka mbele ya Mwenyezi Mungu atasema; Ewe nafsi iliyotua! Kwa Muhammad na Ahlul Bait wake rudi kwa Mola wako hali ya kuridhia wilaya na hali ya kuridhiwa thawabu, ingia katika waja wangu yaani Muhammad na Ahlul Bait wake na ingia katika pepo yangu. Litakua ni jambo la kupendeza kwake kutolewa roho yake na kumsikia mnadi. Amepokea Qummi riwaya kwa maana haya katika Tafsiri yake na Al-Barqi katika Mahasin.