26
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
SURA MAUN ( MANUFAA) (NA. 107)
INA AYA 7
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.
أَرَأَيْتَ الَّذِي يُكَذِّبُ بِالدِّينِ ﴿١﴾
1. Je, umemwona (unamjua) yule ambaye anakadhibisha dini.
فَذَٰلِكَ الَّذِي يَدُعُّ الْيَتِيمَ ﴿٢﴾
2. Huyo ni ambaye humsukuma yatima.
وَلَا يَحُضُّ عَلَىٰ طَعَامِ الْمِسْكِينِ ﴿٣﴾
3. Wala hahimizi kulisha maskini.
فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ ﴿٤﴾
4. Basi ole wao wenye kuswali.
الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ ﴿٥﴾
5. Ambao wanapuuza swala zao.
الَّذِينَ هُمْ يُرَاءُونَ ﴿٦﴾
6. Ambao wao hujionyesha.
وَيَمْنَعُونَ الْمَاعُونَ ﴿٧﴾
7. Na wakazuilia (watu) manufaa.
UBAINIFU
Sura hii inaelezea kiaga anachopewa yule mwenye kusifika na sifa za kiunafiki kama vile kuipuuza swala kufanya ria na kuzuwiya misaada. Sura hii inawezekana kuwa imeshuka Makka au Madina. Na inasemekana nusu yake imeshuka Makka na nusu yake imeshuka Madina.
Aya Na 1
Neno Araayta lina maana ya kuona kwa macho au kwa kiakili. Makusudio ya dini hapa ni malipo siku ya malipo na kukadhibisha malipo maana yake ni kukadhibisha kufufuliwa. Imesemwa kuwa makusudio ya dini ni kwa maana ya mila.
Aya Na 2
Neno yaduu lina maana ya kusukuma na kufukuza kwa nguvu na jeuri. Hapa ina maana ya yule anayemsukuma na kumfukuza yatima kwa nguvu na jeuri bila ya kujali matokeo ya mabaya hayo ayafanyao. Lau hakukataa siku ya malipo angeliogopa siku hiyo. Na lau aliigopa siku hiyo angelimhurumia yatima.
Aya Na 3
Yaani ni yule ambaye hapendelei watu wawalishe maskini. Imekuja ibara ya kuhimiza, kwa vile kuhimiza kunaenea zaidi kuliko kufanya tu! Inasemekana kuna neno Twaam lina maana ya chakula kama lilivyo, kwa kufahamisha kwamba yule mwenye kupewa ni kama vile anamiliki kile anachopewa, kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na katika mali zao ilikuwako haki ya kupewa maskini aombae na ajizuiae kuomba
." (51:19).
Na inasemwa Twaam katika aya ina maana ya kulisha.
Aya Na 4-5
Wanaopuuza swala ni wale wasiopatiliza swala wala hawajali kukosa swala zote au baadhi, au kuchelewa na wakati wake bora (wa mwanzo). Aya hii inawaunganisha wale wanaopuuza swala na wale wanaokadhibisha malipo, kufahamisha kuwa wao hawaachani na unafiki wao kwa vitendo huku wakijidhihirisha kwa imani.
Aya Na 6
Wanaojionyesha ni wale wanaofanya ibada kwa kujionyesha kwa watu, kwa hiyo wanafanya ibada kwa ajili ya watu na sio kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (s.w.t).
Aya Na 7
Neno Maun lina maana ya msaada wa aina yoyote inayoondoa dhiki au tatizo la aina yoyote kama vile kumkopesha mtu pesa, au kumfanyis wema au kumuazima chombo cha nyumbani.
Utafiti Wa Hadithi. Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu Aya Na 1 anasema ilishuka kwa Abu Jahl na makafiri wa Kiquraish, na kuhusu Aya Na 5 wanakusudiwa wale wanaocha swala na wala sio kusahau, kwa sababu kila mtu anaweza kusahau katika swala. Amesema Abu Abdiallah
: "Ni kuichelewesha swala na wakati wake bila ya udhuru
". Katika Khiswal katika hadith ya mia nne imepokewa kutoka kwa Ali
amesema: "Hakuna amali inayopendeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuliko swala, kwa hivyo kisiwashughulishe chochote na swala kwani Mwenyezi Mungu amewashutumu watu kwa kusema: "Wale ambao swala zao wanazipuuza" yaani wanaopuuza wakati wake.
Katika Kafi kwa isnadi ya Muhammad bin Alfadhil, anasema: "Nilimuuliza mja mwema
kuhusu Aya Na 5 akasema ni kupuuza, na ziko riwaya nyingi katika madhumuni haya haya. Katika Durril Manthur ametoa Ibn Jariyr, Ibn Hatim na Bayhaqai kutoka ka Ali bin Abu Twalib kuhusu neno, wale amabo wanafanya ria ni kufanya ria katika swala. Katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Abu Naim, Dilami na Ibn Asakir kutoka kwa Abu Hurayra naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
kuhusu Aya Na 7 ni vitu wanavyosaidiana watu kama shoka, ndoo, sufuria nk.
Katika Kafi kwa Abu Baswir naye kutoka kwa Abu Abdiallah
amesema: "Na neno lake Mwenyezi Mungu (s.w.t): Na wakazuilia (watu) na manufaa" ni kuzuilia kukopeshana na kufanyiana mema na kuazimana vyombo vya nyumbani na pia kuzuilia zaka. Kilifasiri neno Maun kwa maana ya zaka pia imepokewa kwa njia ya Ahli Sunnah, kutoka kwa Ali
kama ilivyo katika Durril Manthur kuwa tamko Maun ni zaka ya wajibu. Yaani wanajionyesha katika swala zao na huku wanazuia zaka zao.
Katika hiyo Durril Manthur ametoa Ibn Qani kutoka kwa Ali Ibn Abu Twalib
amesema: "Nimemsikia Mtume(s.a.w.w)
akisema: "Muislamu ni ndugu ya muislamu mwengine anapokutana naye humuamkia kwa salam na humpatia kila chenye heri na hamzuilii Maun nikasema, "Ewe Mtume wa Mungu nini maun" akasema Mtume "ni jiwe, chuma, maji nk." Amefafanua Mtume(s.a.w.w)
katika hadith nyengine kuwa chuma ni sufuria za shaba na shoka ya chuma. Na mawe ni nyungu za mawe.
SURA KAWTHAR (HERI NYINGI) (NA. 108)
INA AYA 3
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.
إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ ﴿١﴾
1. Hakika sisi tumekupa kheri nyingi.
فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾
2. Basi mswalie Mola wako na uchinje mnyama.
إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الْأَبْتَرُ ﴿٣﴾
3. Hakika mwenye kukubughudhi wewe yeye ndiye mwenye kuishiwa.
UBAINIFU
Sura hii inaeleza kuneemeshwa kwa Mtume kwa kupewa neema nyingi. Na Sura hii ndiyo Sura fupi katika Qur'an. Mapokezi yamekithalifiana kuwa Sura imeshuka Makka au Madina, lakini inaonyesha kwamba imeshuka Makka. Wengine wamesema imeshuka mara mbili.
Aya Na 1
Imesemwa katika Majmau kwamba neno Kawthar liko katika kipimo cha Faw-al yenye maana ya wingi, kwa hiyo Kawthar ni heri nyingi. Wamehitilafiana kiajabu sana katika tafsiri ya neno Kawthar. Imesemwa kuwa ni heri nyingi, wengine wamesema ni mto peponi, wengine wamesema ni birika ya Mtume katika pepo au katika siku ya kukusanywa watu. Pia imesemwa ni watoto wake, masahaba wake, wafuasi wake mpaka siku ya Kiyama, au wanavyuoni wa umma wake.
Na imesemwa ni Uislamu, Tawhid, elimu na hekima, ubora wake, maqamu yenye kusifiwa, nuru ya moyo wake na zaidi ya hayo yamesemwa mpaka kufikia kauli ishirini na saita (26). Baadhi ya riwaya zimetegemea kwenye kauli mbili za mwanzo (heri nyingi na to katika pepo). Lakini kauli nyingine pia haziwezi kuachwa. Kwa hali yoyote iwayo. Neno abtar kwa dhahiri lina maana ya mwenye kukatikiwa na kizazi. Kwa hiyo makusudio hapa ya kawthar ni kizazi kingi, au heri nyingi kwa maana ya kuwa hicho kizazi ni heri nyingi lau kama si hivyo, basi ingelikuwa jumla ya aya ya haina faida yoyote.
Hadith zimeeleza kwamba Sura hii ilishuka, kutokana na mtu mmoja aliyemtusi Mtume(s.a.w.w)
, kwa kuwa eti amekatikiwa na kizazi chake kutokana na kufa kwa watoto wake wa kiume (Kassim na Abdulla). Kwa hivyo Mwenyezi Mungu akamrudishia majibu kwa kusema huyo mwenye kukubughudhi wewe ndiye abtar aliyekatikiwa na heri zote: Neno "hakika sisi tumekupa wewe", limekuja kwa wingi kwa kuadhimisha tu. Jumla yote hiyo ya maneno inafahamisha kuwa kizazi cha Fatima
ni kizazi cha Mtume(s.a.w.w)
. Mwenyezi Mungu amekifanya kingi sana kizazi hicho kuliko kizazi kingine chochote pamoja na misiba iliyowashukia na kuuliwa kwa makundi katika mauaji ya kuchukiza na ya kinyama.
Aya Na 2
Kushukuru neema ni jambo linalotakikana. Hapa Mwenyezi Mungu anamwamrisha Mtume wake kuwa tumekupa heri nyingi, basi wewe shukuru neema hiyo kwa kusali na kuchinja mnyama. Imesemekana maana ya ayah ii ni kuswali swala ya Idd na kuchinja mnyama. Pia imesemwa maana ya neno wanhar ni kunyanyua mikono miwili katika swala wakati wa kusoma takbira.
Aya Na 3
Imesemwa maana ya neno abtar hapo ni kuepukana na heri au kuepukana na watu wake. Yatakuja maelezo katika utafiti wa hadith. Neon shani ni yule mwenye kubughudhi naye ni Asi bin Wail.
Utafiti Wa Hadith Katika Durril Manthur ametoa Bukhari, Ibn Jariyr na Hakim kwa njia ya Abu Bashar kutoka kwa Said bin Jubayr naye amepokea kutoka kwa Ibn Abbas kwamba yeye amesema: "Kawthar ni heri alizopewa Mtume". Abu Bashar akasema kumwambia Said bin Jubayr: "Hakika watu wanadai kuwa kawthar ni mto katika pepo". Akajibu "mto katika pepo ni katika heri ya Mwenyezi Mungu aliyompa Mtume wake." Katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Ibn Abu Hatim, Hakim, Ibn Murdawayh na Bayhaqi katika hadith zake kutoka kwa Ali bin Abu Twalib
amesema:
"Iliposhuka Sura ya Kawthar, Mtume(s.a.w.w)
alisema kumwambia Jibril: Ni uchinjo gani huu alioniamrisha Mungu? Jibril akasema: "Sio uchinjo isipokuwa anakuamrisha kunyanyua mikono yako katika swala wakati wa kuhirimia, kurukui na wakati wa kunyanyua kichwa baada ya rukui, kwani hiyo ndiyo swala yetu na swala ya Malaika walioko katika mbigu saba, na kwamba kila kitu kina kipambo chake na kipambo cha swala ni kunyanyua mikono miwili kila unaposoma takbira. Katika Majmau imepokewa kutoka kwa Muqatil naye kutoka kwa Asbagh bin Nabata, kisha akasema wamepokea Thaalabi na Wahidi katika tafsiri zao, kwamba imepokewa kutoka kwa kizazi chote kitakatifu cha Mtume kitabu hicho hicho ametoa Ibn Jariyr kutoka kwa Abu Jaffar kwamba maana ya msalie Mola wako, ni swala na maana ya wanhar ni unyanyue mikono miwili unapotoa takbira mwanzo wa swala.
Tena katika hiyo hiyo Majmau ametoa Ibn Murdawayh kutoka kwa Ibn Abbas kuhusu Aya Na 2 amesema: Hakika Mwenyezi Mungu alimpelekea Wahyi Mtume wake kwa kusema : "Nyanyua mikono yako muelekeo wa sehemu ya juu ya kifua hiyo ndiyo nahr". Katika hiyo hiyo Majmau imepokewa kutoka kwa Umar bin Yazid amesema: "Nimesikia Abu Abdillahi akisema? Maana ya wanhar ni kunyanyua mikono yako pambizoni mwa uso wako. Na pia imepokewa kutoka kwa Abdulla bin Sinan mfano wa hadith iliyo karibu na maana hayo kutoka kwa Jamil. Katika Durril Manthur ametoa Ibn Saad na Ibn Asakir katika njia ya Kalabi kutoka kwa Abu Saleh naye kutoka kwa Ibn Abbas amesema: "Alikuwa mtoto mkubwa wa Mtume(s.a.w.w)
ni Kassim kisha Zaynab, Abdulla, Ummu Kulthum, Fatima na Ruqayya. Akafa Kassim, naye ndiye maiti wa kwanza katika kizazi chake, kisha akafa Abdullah. Ndipo akasema Asi bin Wail Assahmi :"Kizazi chake kimekwisha katika, kwa hiyo yeye ni abtar. Basi akateremsha Mwenyezi Mungu; Hakika mwenye kukubughudhi wewe yeye ndiye abtar (mwenye kuepukana na heri zote)".
Katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Ibn Abu Hatim kutoka kwa Assadi amesema. "Walikuwa Maquraish wakisema: mtu anapofiwa na mtoto wa kiume, ni abtar basi alipokufa mtoto wa Mtume(s.a.w.w)
, Asi bin Wail akasema Mtume ni abtar. Tena katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Zubeir bin Bakar na Ibn Muhhamd kutoka kwa baba yake amesema: "Alikufa Kassim mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu huko Makka, Mtume alipokuwa akitoka kuzika akapita kwa Asi Bin Wail akiwa na mtoto wake Amru, akasema alipomwona Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
. "Mimi ninamchukia sana." Akasema Asi: "Achana naye kwani yeye ameshakua Abtar". Mwenyezi Mungu ndio akateremsha Sura hiyo.
Ibn Abi Hatim amepokea kutoka kwa Assadi amesema: "Mtu anapofiliwa na mtoto wa kiume, Quraish walikuwa wakisema: "Fulani ameshakuwa abtar." Basi alipokufa mtoto wa Mtume(s.a.w.w)
Asi bin Wail alisema : "Amekuwa abtar". Wamehitalifiana juu ya aliyembughudhi Mtume(s.a.w.w)
; wengine wanasema ni Walid bin Al-Mughira, wengine wanasema ni Abu Jahl, wengine ni Uqbah bin Abu Muiit na wengine wanasema ni Ka'ab bin Ahsraf. Lakini kauli yenye tutegemewa ni ile inayomtaja Asi nin Wail.
Hayo yanatiliwa nguvu na yale yaliyo katika Ihtijaj ya Tabrasiy kutoka kwa Hasan bin ali
katika hadith anayomwambia Amru bin Al-Asi: "Hakika wewe umezaliwa kutokana na kitanda kilichoshirikianwa, wakabishana juu yako wanaume wa Kiquraish ambao ni Abu Sufyan bin Harb, Walid bin Al-Mughira, Uthman bin Al-Harith, Annadhri bin Al-Harith bin Kaldah na Asi bin Wail. Kila mmoja anadai kuwa wewe ni mtoto wake, ndipo akashinda yule mchafu wao zaidi.
Katik Tafsiri ya Qummi amesema Kawthar ni mto katika pepo aliopewa Mtume badala ya mtoto wake Ibrahim (aliyekufa). Kwa vyovyote iwavyo kutafsiri Kawthar kuwa ni mto katika pepo hakupingani na tafsiri ya heri nyingi, kama yalivyokwisha tangulia maelezo ya Ibnu Jubeir.
SURA KAFIRUN (MAKAFIRI)(NA. 109)
INA AYA 6
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.
قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ ﴿١﴾
1. Sema: Enyi makafiri
لَا أَعْبُدُ مَا تَعْبُدُونَ ﴿٢﴾
2. Mimi siabudu mnachokiabudu.
وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ﴿٣﴾
3. Wala nyinyi hamkiabudu ninachokiabudu mimi.
وَلَا أَنَا عَابِدٌ مَّا عَبَدتُّمْ ﴿٤﴾
4. Wala mimi sitaabudu mnachokiabudu nyinyi.
وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ﴿٥﴾
5. Wala nyinyi hamtakiabudu ninachokiabudu mimi.
لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ ﴿٦﴾
6. Nyinyi mna dini yenu, na mimi nina dini yangu.
UBAINIFU
Katika Sura hii Mwenyezi Mungu anamwamrisha Mtume kudhihirisha kujitenga kwake na dini yao. Dini yake haingilii dini yao wala dini yao haingilii dini yake. Yeye katu haabudu lile wanaloliabudu wala wao katu hawaabudu anachokiabudu. Kwa hivyo wakate tamaa na namna yoyote ile ya kudanganya. Wamekhitalifiana wafasiri kuwa Sura imeshuka Makka au Madina, lakini mpangilio wa maneno unaonyesha kuwa imeshuka Makka.
Aya Na 1
Kwa dhahiri ni watu maalum sio makafiri wote. Hilo linafahamisha kuamrishwa kwake Mtume(s.a.w.w)
kuwambia makafiri kutakasika kwake na dini yao na kujizuilia kwao na dini yake.
Aya Na 2
Makusudio ya kile mnachokiabudu, ni masanamu waliyokuwa wakiyaabudu. Herufi laa hapa ni ya kukanusha kwa muda ujao (mustaqbal) na herufi maa ni ya muda wa sasa hivi. Yaani siabudu milele kile mnacho kiabudu hivi sasa katika msanamu.
Aya Na 3
Pia ni ya kukanusha kwa muda ujao yaani kumpa habari Mtume(s.a.w.w)
kwamba makafiri hawataabudu kile anachokiabudu Mtume(s.a.w.w)
kama walivyokuwa wakidai. Kwa kuunganisha amri iliyo katika mwanzo wa maneno, aya hizi mbili zinaonyesha ya kwamba Mwenyezi Mungu ameniamrisha kudumu kumuabudu Yeye. Halikadhalika ameniamrisha kuwaeleza kama nyingi hamtamuabudu katu. Kwa hivyo hapana ushirikiano wa dini kati yangu na nyinyi. Ayah ii ina maana sawa na ile aya isemayo: "Bila shaka kauli (ya adhabu) imehakikika juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini
." 36:7.
Halikadhalika inakubaliana na aya isemayo: "Hakika wale waliokufuru (Kwa ukaidi na inadi) ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini
". (2:6). Ilikuwa sawa ni kusema: "Wala nyinyi siwenye kuabudu ninayemuabudu". Lakini imesemwa "Ninachokiabudu". Kwa jili ya kufuata mpangilio ulioanzia: "Siabudu mnachokiabudu".
Aya Na 4-5
Ni kutilia mkazo yale yaliyotangulia, kama ilivyo katika Sura ya (102: 3-4); aliposema: "Komeni punde kidogo tu! Mtajua kisha komeni punde kidogo tu! Mtajua
". Na katika Sura (74: 19-29):
"Amelaaniwa, namna gani alivyokadiria (kutia ila Qur'an) kasha amelaaniwa, namna gani aliyokadiria (kutia ila Qur'an)
."
Imesemekana kuwa ma katika neno Abadtum sio mausul yenye maana kurejea kwenye jina, bali ni ya masdariya ya kufanya jina la kitendo yenye maana wa Wala mimi siabudu ibada yenu wala nyinyi siwenye kuabudu ibada yangu. Kwa maana kuwa siwashirikishi wala hamnishirikishi si katika mwenye kuabudiwa wala ibada. Ninayemuabudu mimi ni Mungu na mnayeabudu nyinyi ni sanamu. Na ibada yangu ni ile aliyoiweka Mwenyezi Mungu, lakini ibada yenu ni ile mliyoizusha wenyewe kwa ujinga na uzushi. Yatakuja maelezo katika utafiti wa hadith (Inshallah).
Aya Na 6
Nikuzidi kutilia mkazo kukanusha kushirikiana. Na herufi lam ni ya kuhusisha, yaani dini yenu ya kuabudu masanamu inahusika na nyinyi na hii dini yangu inahusikana na mimi tu! Inasemekana kwamba dini hapa ina maana ya malipo yaani; Mna malipo yenu na nina malipo yangu. Na inasemekana pia kuna kitu kilichoondoshwa yaani, mna malipo ya dini yenu nami nina malipo ya dini yangu. Lakini njia mbili zote hizo, ziko mbali na ufahamu.
Utafiti Wa Hadithi Katika Durril Manthur ametoa Ibn Jariyr, na Ibn Abu Hatim na Ibn Anbari, kutoka kwa Said Ibn maynai Huru (aliyekuwa mtumwa) wa Abul Bakhtari amesema: "Walid bin El-Mughira, Asi bin Wail, sa-wad bin El-Mutwalib na Umayya bin Khalaf, walikutana na Mtume wakamwambia "Ewe Muhammad ! njoo tuabudu kile unachokiabudu na wewe uabudu kile tunachokiabudu na tushirikiane sisi na wewe katika mambo yetu yote, ikiwa haya yetu ni sahihi zaidi kuliko yako, basi utakuwa umepata cha kupata, na kama ikiwa yale unayoyaabudu wewe ni sahihi zaidi kuliko yetu, basi tutakuwa tumechukua la kuchukua". Mwenyezi Mungu ndio akateremsha Sura hiyo yote.
Katika Tafsiri ya Qummi amepokea kutoka kwa baba yake naye amepokea kutoka kwa Ibn Abu Umeir amesema: "Abu Shakir alimuuliza Abu Jaffar El-Ahwal kuhusu Sura ya Kafirun "Jee Mwenye hekima anasema maneno kama haya na kuyarudia mumo kwa mumo? "Abu Jaffar El-Ahwal hakuwa na jibu. Basi akaenda Madina kumuuliza Abu Abdillahi
akasema: :Sababu ya kushuka Sura hiyo na kukariri maneno hayo, ni kwamba Maquraish walimwambia Mtume(s.a.w.w)
: 'abudu miungu wetu mwaka mmoja na tuabudu Mungu wako mwaka mmoja na tena abudu miungu wetu mwaka moja na tuabudu Mungu wako mwaka mmoja".
Mwenyezi Mungu akawajibu kama vile walivyo sema. Akasema juu ya yale waliyoyasema kuwa aabudu miungu yao mwaka alisema: Sema enyi makafiri. Mimi siabudu mwachokiabudu. Na katika yale waliyoyasema kuwa watamwabudu Mungu wake mwaka alisema: Wala nyinyi hamkiabudu ninachokiabudu mimi. Na juu ya yale waliyosema aabudu miungu yao mwaka mmoja alisema: Wala mimi siabudu mnachokiabudu nyinyi.
Na katika yale waliyoyasema wataabudu Mungu wake mwaka mmoja alisema: Wala nyinyi hamtakiabudu ninachokiabudu mimi. Nyinyi mna dini yenu na mimi nina dini yangu. Akarudi Abu Jaffar El-Ahwal kwa Abu Shakir akampa habari juu ya hayo!