TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN12%

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
  • Anza
  • Iliyopita
  • 29 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 42567 / Pakua: 4763
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi:
Swahili

1

2

3

4

9

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA INSHIQAAQ (KUPASUKA)( NA: 84)

INA AYA 24

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

إِذَا السَّمَاءُ انشَقَّتْ ﴿١﴾

1. Mbingu zitakapopasuka.

وَأَذِنَتْ لِرَبِّهَا وَحُقَّتْ ﴿٢﴾

2. Zikamtii Mola wake na zikafanya ndivyo.

وَإِذَا الْأَرْضُ مُدَّتْ ﴿٣﴾

3. Na ardhi itakaponyooshwa.

وَأَلْقَتْ مَا فِيهَا وَتَخَلَّتْ ﴿٤﴾

4. Ikatupa vilivyomo na ikawa tupu;

وَأَذِنَتْ لِرَبِّهَا وَحُقَّتْ ﴿٥﴾

5. Ikamtwii Mola wake na ikafanya ndivyo.

يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ إِنَّكَ كَادِحٌ إِلَىٰ رَبِّكَ كَدْحًا فَمُلَاقِيهِ ﴿٦﴾

6. Ewe mwanadamu: Hakika wewe ni mwenye kufanya juhudi mpaka (kufikilia) kwa Mola wako; basi ni mwenye kukutana naye.

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ ﴿٧﴾

7. Ama atakayepewa kitabu chake kwa kuumeni kwake.

فَسَوْفَ يُحَاسَبُ حِسَابًا يَسِيرًا ﴿٨﴾

8. Atahisabiwa hisabu nyepesi.

وَيَنقَلِبُ إِلَىٰ أَهْلِهِ مَسْرُورًا ﴿٩﴾

9. Awarejee (atarudi kwa) watu wake huku akiwa na furaha.

وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ وَرَاءَ ظَهْرِهِ ﴿١٠﴾

10. Ama atakayepewa kitabu chake nyuma ya mgongo wake.

فَسَوْفَ يَدْعُو ثُبُورًا ﴿١١﴾

11. Yeye atauita ole wake.

وَيَصْلَىٰ سَعِيرًا ﴿١٢﴾

12. Aingie na motoni.

إِنَّهُ كَانَ فِي أَهْلِهِ مَسْرُورًا ﴿١٣﴾

13. Maana yeye alikuwa kati ya watu wake (ulimwenguni) ni mwenye furaha.

إِنَّهُ ظَنَّ أَن لَّن يَحُورَ ﴿١٤﴾

14. Kwa kudhaani kwamba hatarejea (kwa Mola wake).

بَلَىٰ إِنَّ رَبَّهُ كَانَ بِهِ بَصِيرًا ﴿١٥﴾

15. Kwani? Hakika Mola wake alikuwa akimjua.

فَلَا أُقْسِمُ بِالشَّفَقِ ﴿١٦﴾

16. Naapa kwa mawingu mekundu.

وَاللَّيْلِ وَمَا وَسَقَ ﴿١٧﴾

17. Na usiku na ulichokikusanya.

وَالْقَمَرِ إِذَا اتَّسَقَ ﴿١٨﴾

18. Na mwezi unapotimia.

لَتَرْكَبُنَّ طَبَقًا عَن طَبَقٍ ﴿١٩﴾

19. Mtakutana na hali baada ya hali.

فَمَا لَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٢٠﴾

20. Basi wananini hao hawaamini.

وَإِذَا قُرِئَ عَلَيْهِمُ الْقُرْآنُ لَا يَسْجُدُونَ ﴿٢١﴾

21. Na wanaposomewa Qur'an hawanyenyekei.

بَلِ الَّذِينَ كَفَرُوا يُكَذِّبُونَ ﴿٢٢﴾

22. Bali wale ambao wamekufuru hukadhibishwa.

وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا يُوعُونَ ﴿٢٣﴾

23. Na Allah ni mjuzi wa waliyoyakusanya.

فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٢٤﴾

24. Basi wape habari ya adhabu yenye uchungu.

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ أَجْرٌ غَيْرُ مَمْنُونٍ ﴿٢٥﴾

25. Ila wale ambao wameamini wakatenda amali njema (wao) watapata malipo mema yasiyokoma.

UBAINIFU

Sura inaishiria kusimama Kiyama na inakumbusha kwamba mtu ni mwenye kwenda kwa Mola wake mpaka akutane naye atamuhisabu kwa mujibu wa kitabu chake. Sura hii inatilia mkazo jambo hilo na pia imesisitiza zaidi upande wa maonyo kuliko ule na biashara. Mpangilio wa aya ni wa Makka.

Aya Ya 1

Ni sharti ambalo jawabu lake limeondolewa kukadiria kwake ni: Mbingu zitakapopasuka, mtu atakutana na Mola wake atahisabiwa na kulipwa yale aliyoyatenda. Kupasuka kwa mbingu ni katika alama za Kiyama kama kukunjwa jua, kukutana jua na mwezi, kupuputika nyota, n.k.

Aya Ya 2

Kusikiliza ni fumbo, maana yake ni kutii na kufuata. Kufanya ndivyo: ni kufanya ndivyo huko kumtii na kufuata; yaani zikamtii Mola wake na zikafanya ndivyo kumtii na kumfuata.

Aya Ya 3

Kwa dhahiri makusudio ni kufanywa pana ardhi; Mwenyezi Mungu anasema: "Siku ambayo ardhi hii itabadililishwa kuwa ardhi nyengine ." (14:48).

Aya Ya 4

Yaani itatupa vilivyomo ndani yake katika wafu na kuwa tupu. Imesemwa kuwa makusudio ni kutupa wafu na hazina; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na ikatoa ardhi mizigo yake " (99:2) Imesemwa maana ni kutupa vilivyo ndani yake nakuwa tupu na vitu vilivyo juu yake miongoni mwa majabali na bahari. Huenda maelezo ya kwanza ndiyo yaliyo karibu zaidi na maana.

Aya Ya 5

Dhamiri hapa ni ya ardhi na maana ni kama yaliyotangulia katika mbingu.

Aya Ya 6

Anasema Raghib maana ya neno Kad-h ni kwenda na kufanya juhudi. Na imesemwa maana yake ni juhudi ya nafsi katika amali. Kwa hivyo maana itakuwa ni kwenda, kwa dalili ya herufi ila yenye maana ya mpaka. Kauli ya: "basi ni mwenye kukutana naye" (kuwa katika hukumu yake) inaungana na neno kad-h. Mwenyezi Mungu amebainisha kwa neno hii (Kad-h) kwamba ukomo na mwenendo huu na mahangaiko haya ni kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t), kwa kuwa yeye ndiye Mola Mlezi. Yaani, kwa kuwa mtu ni kiumbe mwenye kulelewa, kumiliki na mwenye akili, daima ni mwenye kuelekea kwa Mwenyezi Mungu kawa sababu yeye ndiye Mola wake mwenye kupanga mambo yake. Mja hajiamulii mwenyewe alitakalo au alifanyalo. Yeye anao uwezo wa kutaka, lakini anafanya tu lile alilolitaka Mwenyezi Mungu na kumwamuru alifanye, sababu yeye ndiye bwana wake. Hivyo mja anachukua jukumu la aliyoyapenda na kuyatenda.

Kwa hivyo hapa yanadhihiri mambo haya:

Kwanza : "Hakika wewe ni mwenye kufanya juhudi mpaka (kufikilia) kwa Mola wako" ni hoja huu ya marejeo ya Kiyama kwa vile ulivyo kuwa ubwana hautimii ila pamoja na jukumu na utumwa, wala hautimii utumwa ila pamoja na jukumu na halimtii jukumu ila kwa kurejea na kuhisabiwa na hakutimu kuhisabiwa ila kwa malipo.

Pili : Kwamba makusudio ya kukutana naye ni kuishia kwake, ambako hakuna hukumu isipokuwa hukumu yake bila ya kuweko kuziwizi chochote.

Tatu : Mwenye kuambiwa ni jinsi ya mtu yeyote, hivyo ulezi wa Mungu ni wenye kuenea kwa kila mtu.

Aya Ya 7

Ni ufafanuzi wa mpangilio juu ya yale yalioelezewa na aya iliyotangulia, kwamba kuna marejeo na maswali juu ya amali na hesabu, na makusudio ya kitabu ni karatasi ya matendo (amali).

Aya Ya 8

Hisabu nyepesi ni ile iliyosahilishwa na ikawa haina malumbano yoyote.

Aya Ya 9

Makusudio ya watu wake hapa ni wale aliomwanadalia Mwenyezi Mungu katika pepo miongoni mwa Hurulaini, watumishi, n.k. Haya ndiyo yanayofahamika kutokana na mpangilio wa aya. Imesemwa kuwa makusudio ni jamaa zake waumini atakaoingia nao peponi, Imesemwa kuwa waumini hata kama sio jamaa zake; kwa sababu waumini wote ni ndugu. Njia zote mbili haziepukani kuwa ziko mbali zaidi na maana.

Aya Ya 10

Huenda ikawa kupewa vitabu vyao nyuma ya migongo yao ni kwa sababu ya kugeuzwa nyuso zao visogoni mwao kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "..kabla hatujazigeuza nyuso tukazipeleka kisogoni. ." (4:47).

Hapana mgongano kati ya kupewa vitabu vyao nyuma ya migongo yao na kupewa kushotoni mwao; kama ilivyo katika kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Ama atakayepewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto. Basi atasema Oo! Laiti nisingelipewa daftari langu ."(69:25).

Yatakuja maelezo zaidi kuhusu maana ya kupewa kitabu nyuma ya migongo katika utafiti wa hadith (Inshallah).

Aya Ya 11

Yaani atakaposema kitabu chake ataita "Oo kuangamia.

Aya Ya 12

Yaani moto wenye joto kali ambao hauna mfano kwa adhabu yake wala hauna kiasi kwa joto lake.

Aya Ya 13

Yalimfurahisha yale aliyokuwa akiyapata katika starehe za dunia na kuvutika na anasa za dunia. Hilo lilimsahaulisha mambo ya akhera. Mwenyezi Mungu anaishutumu furaha ya mtu kutokana na kheri za dunia anazozipata na ameiita furaha pasi na haki. Anasema Mwenyezi Mungu baada ya kuutaja moto na adhabu yake: "Haya (yaliyowapata) ni kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyafurahia duniani pasi na haki na yale mliyokuwa mkijivunia ." (40:75)

Aya Ya 14

Makusudio ni kurejea kwa ajili ya hisabu na malipo. Hakuna kinachomsababisha kudhania hivyo isipokuwa kujiingiza katika dhambi kunakopelekea kuona kufufuliwa ni jambo lisilo wezekana.

Aya Ya 15

Ni jibu la dhana yake; kwamba sio hivyo anavyodhania, kwani hakika Mwenyezi Mungu(s.w.t) ndiye Mola wake na mfalme wake mwenye kuzingatia jambo lake. Anamjua na kuona yote aliyokuwa akiyafanya katika matendo yake. Na matendo yake yana malipo mema au mabaya. Kwa hiyo hapana budi kurudi kwake na amlipe yale yanayostahiki matendo yake. Kwa hali hiyo inadhihiri kuwa kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Hakika mola wake alikuwa akimwona" ni katika kutoa hoja juu ya kupasa marejeo; aya hii ni kama ile iliyotangulia katika kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Hakika wewe ni mwenye kufanya juhudi mpaka (kufikilia) kwa Mola wako."

Vile vile inadhihiri kutokana na mkusanyiko wa aya hizi tisa, kwamba utoaji wa vitabu ni kabla ya hisabu kama kunavyofahamisha kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Na kila mtu tumemfungia vitendo vyake shingoni mwake; na tutamtolea siku ya Kiyama daftari atakayoikuta imekunjuliwa. (Ataambiwa), Soma daftari yako, hii leo nafsi yako inatosha kukuhisabu ." (17;13).

Aya Ya 16

Ni wekundu unaofuatiwa na manjano kisha weupe ambao unatokea magharibi mwanzo wa usiku

Aya Ya 17

Yaani kukusanya vile vilivyotawanyika wakati wa mchana miongoni wa watu na wanyama kwani wao hytawanyika mchana na kurudi katika makazi yao usiku na kutulia. Baadhi wamefasiri neno Wasaq kwa maana ya kufukuza yaani usiku unazifukuza nyota kutoka katika kujificha kwenda kwenye kudhihiri.

Aya Ya 18

Yaani kukusanyika nuru yake na kuwa mwezi mtimilifu.

Aya Ya 19

Ni jawabu la kiapo. Makusudio yake ni mtakutana na hali baada ya hali kwa namna yoyote yatakavyokuwa masafa anayoyakata mtu katika kufikia kwa Mola wake, kutoka katika maisha ya dunia, kisha mauti kisha maisha ya Barzakh, kisha kwenda akhera kisha maisha ya akhera kisha hesabu na malipo. Kiapo - kama unavyoona - ni kutilia mkazo yale yalio katika aya ya 6 na yaliyo baada yake katika hanari za ufufuo Aya hii pia inaonyesha kuwa vipindi anavyopitia mtu ni vyenye kupangwa katika kumfikia Mola wake.

Aya Ya 20 -21

Ni swali la kustaajabu na kutayarisha, kwa hiyo limeoana na mgeuko huu wa ghafla kutoka kwenye mazungumzo ya ana kwa ana na kuwa anamzungumzia mtu mwingine asiyekuwepo; kana kwamba yeye alipowaona kuwa hawaidhiki kwa waadhi wake, aliachana nao na kumwelekea Mtume kwa kumwambia: "wana nini hao hawaamini"

Aya Ya 22-24

Yaani hawakuacha imani kwa sababu ya upungufu wa ubainifu, au kwisha dalili, bali wao wamefuata majadi wao na viongozi wao, wakazama katika kufuru na wakaendelea na kukadhibisha. Mwenyezi Mungu anayajua waliyoyakusanya katika nyoyo na waliyoyaficha katika nyoyo zao, miongoni mwa ukafiri na ushirikina. Imesemwa kuwa makusudio yake ni kuwa wana kitu walichoficha katika nyoyo zao ambacho hakiwezi kuelezwa kwa ibara yoyote: Hakijui isipokuwa Mwenyezi Mungu tu! Lakini maelezo hayo yako mbali na mpangilio wa aya. Kuita maonyo ya adhabu kuwa ni biashara hii ni namna Fulani ya mabezo. Jumla hii ni fungu la (malipo ya) kukadhibisa.

Aya Ya 25

Hapo wanavuliwa na hayo walio amini.

Utafiti Wa Hadithi Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu "mbingu zitakapopasuka" amesema ni siku ya Kiyama. Katika Durril-Manthur ametoa Ibn Abu Hatim kutoka kwa Ali amesema : Itapasuka mbingu hii yenye nyota. Katika Tafsiri ya Qummi: Na ardhi itakaponyooshwa, ikatupa vilivyomo, na ikawa tupu, amesema itanyooshwa ardhi itapasuka wa watatoka watu. Katika Durril Manthur ametoa Hakim kwa isnadi nzuri kutoka kwa Jabir naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) amesema: itanyooshwa ardhi siku ya Kiyama kama inavyonyooshwa ngozi kisha mwanadamu hatakuwa na mahali isipokuwa mahali pa nyayo zake.

Katika Ihtijaj kutoka kwa Ali(a.s) katika hadith amesema: watu siku hiyo watakuwa na sifa na daraja mbali mbali. Kuna katika wao atakayehisabiwa hisabu nyepesi na kurudi kwa watu wake huku akiwa na furaha, na katika wao kuna ambao wataingia peponi bila ya hisabu kwa sababu hawakuvaana na jambo lolote la dunia. Hii ni kwa sababu kisabu huko ni kwa wale waliovaana na dunia. Na muka katika wao watakaohisabiwa hisabu isiyopungua hata chembe na kuwa katika adhabu ya moto mkali.

Katika Maani kwa isnadi yake kutoka kwa Ibn Abu Jaffar(a.s) amesema: Amesema Mtume(s.a.w.w) kila mwenye kuhisabiwa ni mwenye kuadhibiwa akaambiwa: "Basi nini maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) "Atahisabiwa hisabu nyepesi?" Akasema: Hilo ni kwa kusamehe. Imepokewa hadith mfano wa hiyo katika Durril Manthur kutoka kwa Bukhari, Muslim, Tirmidhi na wengineo kutoka kwa Aisha.

Katika Tafsir ya Qummi katika riwaya ya Abul-Jarud kutoka kwa Abu Jaffar(a.s) kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu: "Ama atakayepewa kitabu chake kwa kuumeni kwake" yeye ni Abu Salama Abdulla bin Abdul-Aswad bin Hilal Al-Makhzumi. "Ama mwenye kupewa kitabu chake nyuma ya mgongo wake" ni ndugu yake ambaye ni Al-Aswad bin Abdul-Aswad Al-Makhzumiy aliyeuliwa na Hamza bin Abdul-Muttalib siku ya vita vya BAdr.

Katika Majmau kauli yake Mwenyezi Mungu: "Mtakutana na hali baada ya hali". Amesema: Maana yake ni shida baada ya shida ya uhai kisha mauti, kisha kufufuliwa, kisha malipo. Hadithi hiyo imepokewa marfui. Katika Jawaamiul-Jami kuhusu aya hiyo hiyo, kutoka kwa Abu Abayadah: Mtakutana na desturi ya waliokuwa kabla yenu na hali zao. Na yamepokewa hayo kutoka kwa Imam Sadiq(a.s) .

10

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA BURUJ (BURUJI) (NA. 85)

INA AYA 22

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.

وَالسَّمَاءِ ذَاتِ الْبُرُوجِ ﴿١﴾

1. Naapa kwa mbingu zenye buruji.

وَالْيَوْمِ الْمَوْعُودِ ﴿٢﴾

2. Na siku iliyotolewa kiaga.

وَشَاهِدٍ وَمَشْهُودٍ ﴿٣﴾

3. Na shahidi na chenye kushuhudiwa.

قُتِلَ أَصْحَابُ الْأُخْدُودِ ﴿٤﴾

4. Wamelaaniwa wenye handaki.

النَّارِ ذَاتِ الْوَقُودِ ﴿٥﴾

5. (Lenye) moto wenye kuni.

إِذْ هُمْ عَلَيْهَا قُعُودٌ ﴿٦﴾

6. Walipokuwa pambizoni mwake wamekaa.

وَهُمْ عَلَىٰ مَا يَفْعَلُونَ بِالْمُؤْمِنِينَ شُهُودٌ ﴿٧﴾

7. Na wao, kwa yale wanayowatendea wenye kuamini washuhudia.

وَمَا نَقَمُوا مِنْهُمْ إِلَّا أَن يُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ ﴿٨﴾

8. Wala hapana lililowachukiza kwao ila kwamba walimwamini Allah. Mwenye kushinda Mwenye kusifiwa.

الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿٩﴾

9. Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi. Na Allah ni mwenye kushuhudia kila kitu.

إِنَّ الَّذِينَ فَتَنُوا الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ لَمْ يَتُوبُوا فَلَهُمْ عَذَابُ جَهَنَّمَ وَلَهُمْ عَذَابُ الْحَرِيقِ ﴿١٠﴾

10. Hakika wale ambao wanawaudhi waumini wanaume na wanaumini wanawake, kisha wasitubie watapata adhabu ya kuungua.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْكَبِيرُ ﴿١١﴾

11. Hakika wale ambao wameamini wakatenda amali njema, watapata mabustani yanayopita mito chini yake; huko ndiko kufaulu kukubwa.

إِنَّ بَطْشَ رَبِّكَ لَشَدِيدٌ ﴿١٢﴾

12. Hakika mashiko ya Mola wako ni makubwa.

إِنَّهُ هُوَ يُبْدِئُ وَيُعِيدُ ﴿١٣﴾

13. Hakika Yeye ndiye anayeanza na kurejeza

وَهُوَ الْغَفُورُ الْوَدُودُ ﴿١٤﴾

14. Naye ndiye Mwingi wa kusamehe, Mwenye mapenzi.

ذُو الْعَرْشِ الْمَجِيدُ ﴿١٥﴾

15. Mwenye ufalme mkubwa.

فَعَّالٌ لِّمَا يُرِيدُ ﴿١٦﴾

16. Mwingi wa kutenda alipendalo.

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ الْجُنُودِ ﴿١٧﴾

17. Jee, imekujia habari ya majeshi.

فِرْعَوْنَ وَثَمُودَ ﴿١٨﴾

18. (Ya) Firaun na Thamud.

بَلِ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي تَكْذِيبٍ ﴿١٩﴾

19. Lakini ambao wamekufuru wamo katika kukadhibisha.

وَاللَّـهُ مِن وَرَائِهِم مُّحِيطٌ ﴿٢٠﴾

20. Na Allah kwa nyuma yao amewazunguka.

بَلْ هُوَ قُرْآنٌ مَّجِيدٌ ﴿٢١﴾

21. Bali hii ni Qur'an tukufu.

فِي لَوْحٍ مَّحْفُوظٍ ﴿٢٢﴾

22. Katika ubao uliohifadhiwa.

UBAINIFU

Sura ya maonyo na biashara, ndani yake mna makamio kikali kwa wale wanaowaadhibu waumini wanaume na waumini wanawake kwa sababu ya kumwamini kwao Mwenyezi Mungu; kama walivyokuwa washirikina wa Makka wakiwafanyia hivyo wale waliomwamini Mtume(s.a.w.w) . Wanawaadhibu ili warudie shirki yao ya kwanza. Wakawa katika wao kuna ambao walikuwa wakisubiri wala hawarudi kwa hali yoyote ile na kuna katika wao walikuwa wakirudi na kurtadi nao ni wale wadhaifu wa imani, kama kunavyoonyesha kusema kwake Mwenyezi Mungu:

"Na katika watu kuna wanaosema: tumemwamini Allah lakini wanapoudhiwa katika (njia ya) Allah hufanya vile vituko vinavyowakuta kwa watu kama ni adhabu ya Allah " (29:10).

Na kusema kwake: "Na katika watu wako wanaomwabudu Allah ukingoni. Ikiwafikia heri hutulia kwayo na ikiwafikia fitina (misukosuko) hubwatika juu ya uso wake (akasunukia, hataki kuuna tena uislamu) ." (22:11). Ametanguliza Mwenyezi Mungu S.W.T. ishara hiyo katika kisa cha wenye handaki, kuwahimiza waumini kuwa na subira katika upande wa Mwenyezi Mungu (s.w.t) Na akafuatisha kuishiria habari ya askari wa Firaun na Thamud na hilo ni kuituliza nafsi ya Mtume kwa kiaga cha ushindi na kuwatisha wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu.

Sura hii imeshuka Makka kwa ushahidi wa mpangilio wa aya zake.

Aya Ya 1

Neno Buruj lina maana ya kudhihiri, aghlabu kutumiwa kwa jumba kubwa kwa vile linawadhirikia watazamaji. Na jengo lenye kujengwa juu ya ukuta wa mji kwa ajili ya kujikinga huitwa Buruji. Hayo ndiyo makusudio katika aya hii, kutokana na kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Na hakika tumeweka katika mbingu, buruj (vituo vya nyota) na tumezipamba kwa ajili ya wale wanaozitazama ". (15:16).

Basi makusudio ya Buruj ni mahali pa nyota katika mbingu. Kwa hivyo inadhihiri kwamba kutafsiri Buruj kuwa ni nyota 12 zilizokubaliwa katika elimu ya nyota sio sawa. Katika aya kuna kiapo kwa mbingu yenye kuhifadhiwa na buruji na kiapo hicho kinanasibiana sana na kisa kitakachoelezewa. Pia kunafuatia kiapo cha makamio na kiaga.

Aya Na 2

Inaungana na Aya Na kwanza. Siku iliyoagwa ni siku ya Kiyama ambayo Mwenyezi Mungu ametoa kiaga kwa kuhukumu baina ya waja wake.

Aya Na 3

Pia inaungana na aya mbili zilizotangulia. Viapo vyote hivyo viko juu ya yale yaliyokusudiwa kubainishwa katika Sura, nayo-kama ilivyotangulia kuelezwa - ni makamio kikali kwa mwenye kuwaudhi waumini wanaume na waumini wanawake kwa sababu ya imani yao. Na kiaga kizuri kwa wale waliomini na wakatenda amali njema. Ni kama vile kusema: "Ninaapa kwa mbingu zenye buruji" ambazo kwa buruj hizo Mwenyezi Mungu anazikinga mbingu hizo na mashetani, hakika Mwenyezi Mungu anaikinga imani ya waumini ni vitimbi vya mashetani na marafiki zao katika makafiri. "Na ninaapa kwa siku iliyotolewa kiaga ambayo watalipwa watu matendo yao. Na ninaapa kwa shahidi anayeshuhudia matendo ya hao makafiri na vile wanavyowafanyia waumini kwa sababu ya imani yao kwa Mwenyezi Mungu. Na ninaapa kwa kile chenye kushuhudiwa atakachokishuhudia kila mmoja".

Juu ya hivyo basi inakubalika kuwa "Shahid" ni Mtume kwa kushuhudia kwake vitendo vya umma wake, kisha atavitolea ushahidi siku ya Kiyama. Na inakubalika kuwa chenye kushuhudiwa ni adhabu ya makafiri kwa sababu ya hawa waumini na yale waliyofanyiwa katika maudhi. Ukipenda unaweza kusema ni malipo yake au unaweza kusema juu ya yale yatakayotukia siku wa Kiyama katika mateso na thawabu kwa hao madhalimu na wadhulimiwa. Kuna kauli nyingi juu ya tafsiri ya shahidi na chenye kushuhudiwa; baadhi yao wamefikisha kauli thelathini (30). Kama vile kuwa shahidi ni siku ya Ijumaa na chenye kushuhudiwa ni siku ya Arafa, Siku ya Idd na siku ya Arafa, siku ya Arafa na siku ya Kiyama, kuwa shahidi ni Malaika wanaowashuhudia wanaadamu na chenye kushuhudiwa ni siku ya Kiyama, kuwa shahidi ni ni siku ya Kiyama. Na kuwa shahidi ni wale wanaowashuhudia watu na chenye kushudiwa ni wale wanaoshuhudiwa.

Vile vile kuwa shahidi ni umma huu na chenye kushuhudiwa ni umma wengineo. Shahidi ni viungo vya binadamu na chenye kushuhudiwa ni nafsi zao. Shahidi ni jiwe jeusi (Hajarul-Aswad) na chenye kushuhudiwa ni mwenye kuhiji. Shahid ni Mitume na chenye kushuhudiwa ni Mtume Muhammad(s.a.w.w) ni kwamba shahidi ni Mwenyezi Mungu na chenye kushudiwa ni tamko la Lailah illa llah. Pia iko kauli kuwa shahidi ni Mwenyezi Mungu na chenye kushuhudiwa ni siku ya Kiyama. Shahidi ni Adam na kizazi chake na chenye kushuhudiwa ni siku ya Kiyama. Shahidi ni siku ya Tarwiya na chenye kushudiwa ni siku ya Arafa, siku ya Jumatatu na Ijumaa. Shahidi ni wenye kukurubisha na chenye kushuhudiwa ni illiyuuna. Shahidi ni mtoto ambaye alimwambia mama yake. "Subiri hakika wewe uko kwenye haki" katika kisa cha wenye handaki na chenye kushuhudiwa ni tukio lenyewe na kauli kuwa shahid ni Malaika wanaofuatilia kuandika vitendo, na chenye kushudiwa ni Qur'an ya Al-fajr na kauli nyengine nyingi.

Nyingi katika kauli hizi zinachukulia ushahidi kwa maana ya kutekeleza yale yaliyochukuliwa katika ushahidi na baadhi yake zinatofautisha kati ya shahidi na chenye kushuhudiwa katika maana ya ushahidi na umekwishajua udhaifu wake. Linalonasibu zaidi ni kuchukua ushahidi kwa maana ya kuona ijapokuwa unalazimisha maana ya kutekeleza siku ya Kiyama na kwamba ushahidi unakubaliana kufungamana na Mtume(s.a.w.w) . Vipi isiwe hivyo na hali Mwenyezi Mungu amemwita shaahid aliposema: "Ewe Mtume hakika sisi tumekutuma (uwe) shahidi na mtoaji habari nzuri na mwonyaji ". (33:45).

Na amemwita shaahid aliposema: "ili awe Mtume shahidi juu yenu ." (22:78). Kisha jawabu la kiapo limeondolewa linajulishwa na kusema kwake: "Hakika wale ambao wamewaudhi waumini wanaume na waumini wanawake" mpaka mwisho wa aya mbili. Vile vile hilo jawabu la kiapo linafahamishwa na kusema kwake: "Wamelaaniwa wenye handaki ." na hicho ni makamio cha wale wanaoudhi na ni ahadi kwa waumini wema kwamba Mwenyezi Mungu atawawafikisha kwa subira na atawapa nguvu juu ya kuhifadhi imani yao kutokana na vitimbi vya wachimba vitimbi, ikiwa watafanya Ikhlas (kumtakashia Mwenyezi Mungu amali) kama walivyofanya waumini katika kisa cha handaki.

Aya Na 4

Ni ishara ya kisa cha handaki ili iwe ni mwanzo wa yatayokuja katika kauli yake "Hakika wale ambao wamewaudhi " na sio jawabu la kiapo kabisa. Watu wa handaki ni wale waliochimba handaki na kuwasha moto ndani yake, kisha wakawaumuru waumini waingie ndani yake wakawachoma kwa kuwatesa kwa ajili ya imani yao. Na neno Wamelaaniwa ni dua ua kuwaombea laana. Imesemwa kwa makusudio ya watu wa handaki ni waumini wanaume na waumini wanawake waliochomwa ndani ya handaki na kwamba neno Qutila ni kwa maana ya kuuliwa yaani kuuliwa hao waumini kwa kuchomwa, na wala sio dua ya laana. Lakini hayo yanadhoofishwa na kudhihiri dhamiri katika jumla ya walipokuwa pambizoni mwake, wao kwa yale wayatendayo na hapana lililowachukiza kwao. Dhamiri zote hizo haziwezi kuwarudia waumini.

Aya Na 5

Kuusifu moto wenye kuni ni ishara ya kuonyesha ukali wa moto na mwako wake.

Aya Na 6

Pambizoni mwake ni huo moto yaani hao watu makatili wenye kiburi walikuwa wamekaa pambizoni mwa huo moto.

Aya Na 7

Yaani waumini wanaona na kushuhudia kuunguzwa kwao.

Aya Na 8-9

Yaani walichukizwa na imani yao. Kuanzia mwenye kushinda mpaka mwisho wa Aya Na 9 ni sifa zenye kupita katika jina la Mwenyezi Mungu zinazoonesha kuwa hao waumini. Walikuwa juu ya haki katika imani, wenye kudhulumiwa katika waliyofanyiwa, haijifichi hali yao kwa Mwenyezi Mungu na atawalipa malipo mema na kwamba hao makatili walikuwa kwenye batili wenye kumkosea Mwenyezi Mungu, madhalimu kwa waliyoyafanya na wataonja ubaya wa mambo yao. Hilo ni kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kushinda, mwenye kusifiwa, yaani yeye ni mshindi asiyeshindika kwa hali yoyote, ni mzuri katika vitendo vyake, ni wake peke yake kila utukufuru na uzuri. Kwa hivyo ni wajibu kumnyenyekea na kutompinga. Ikiwa ni wake ufalme wa mbingu na ardhi basi yeye ni mwenye kumiliki hali zote, amri ni yake na hukumu ni yake, Yeye ni bwana wa viumbe vyote. Hivyo ni wajibu kumfanya ni Mola wa kuabudiwa na kutomshirikisha na yoyote. Basi waumini wako kwenye haki na makafiri wako katika upotevu.

Kisha hakika Mwenyezi Mungu- ambaye ndiye aliyepatisha kila kitu- juu ya kila kitu ni mwenye kushuhudia, hakifichiki kwake kitu chochote katika viumbe vyake wala vitendo vyovyote katika vitendo vya viumbe vyake wala haifichiki hisani na mwenye kufanya hisani au uovu wa mwenye kufanya uovu, atamlipa kila mmoja kwa aliyoyafanya. Kwa ujumla, ikiwa Mwenyezi Mungu mwenye kutukuka ndiye mwenye kusifika na sifa hizi tukufu itakuwa ni juu ya hao waumini kumwamini, na ni jambo lisilotakikana kwa hao maharamia kuwaingilia waumini wala kuwafanyia uovu wowte.

Baadhi ya wafasiri wamesema kuhusu makusudio ya kuleta sifa katika aya: Hao watu ikiwa walikuwa ni washirikina, basi jambo liliokuwa likiwaudhi kutokana na waumini halikuwa ni kumwamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, bali lilikuwa ni kukanusha yale yasiyokwuwemo katika ibada zao batilifu. Na kama walikuwa ni wakanushaji wa sifa za Mwenyezi Mungu, basilinalowaudhi ni kuthibitisha Mwenye kuabudia wasiyemzoea. Lakini ilivyokuwa makusudio ya mambo yote hayo mawili (kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kukanusha sifa), ni kumkanusha mwenye kuabudiwa kwa haki mwenye kusifika na sifa za uungu na utukufu, basi ndipo zikaletwa ibara za sifa za Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Katika mghafala waliokuwa nao makafiri ambao ni waabudu masanamu, hawakuwa wakinasibisha kwa Mwenyezi Mungu isipokuwa kutengeneza na kupatisha tu! Ama uungu ambao unawajibisha ibala walikuwa wakitosheka na waungu wao tu! Mwenyezi Mungu kwao alikuwa ni Mungu wa waungu tu! Na sio zaidi ya hapo.

Aya Na 10

Neno Fitna hapa ni kwa maana ya misukosuko na adhabu, na hilo linaenea kwa watu wa handaki na makafiri wa kiquraysh waliokuwa wakiwaadhibu wenye kumwamini Mtume(s.a.w.w) katika waumini wanaume na waumini wanawake kwa aina za adhabu ili warudi katika dini yao. Amesema katika Majmau "pameulizwa vipi kutofautisha kati ya adhabu ya Jahannam na adhabu ya kuungua? Pakajibiwa kwamba makusudio yake ni kwamba wao wana aina za adhabu katika Jahannam ambazo sio kuungua mfano Zakkum(mti wa uchungu), maji ya ushaha na marungu, pamoja na hayo watachomwa kwa moto.

Aya Na 11

Kiaga kizuri kwa waumini cha kuzituliza nafsi zao.

Aya Na 12

Aya hiyo na zinazofuatia mpaka kutimia Aya Na saba ni kuhakikisha na kutilia mkazo yaliyotangulia katika makamio na kiaga kwa makafiri na ahadi ya waumini. Kutegemeza neno "Mashiko" Kwa Mola na kutegemeza neno mola kwa dhamiri ya mwenye kuambiwa ni kuituliza nafsi ya Mtume(s.a.w.w) kwa kumpa nguvu na ushindi na kuonyesha kuwa watu wenye kiburi katika umati wake, vile vile wana fungu katika makamio yaliyotangulia kuelezwa.

Aya Na 13

Neno Yubdiu kwa kulilinganisha na Yuid lenye maana ya kurejeza, lina maana ya kuanza. Wamesema halikusikika neno hilo kwa waarabu, lakini kisomo kiko hivyo. Katika baadhi ya visomo vyengine visivyokuwemo katika istihali husomwa kwa fatha ya yei na dali Yabdau. Kwa vyovyote iwavyo aya iko mahali pa ila (sababu) ya ukali wa mashiko yake Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Hilo ni kwamba yeye Mwenyezi Mungu mwenye kutukuka ni mwenye kuanza. Hupatisha kila anachokikusudia kupatisha kwa kuanza bila ya kumtegemea mwengine. Yeye Mwenyezi Mungu atarudisha kila kilichokuwa vile kilivyokuwa. Yeye Mwenyezi Mungu S.W.T hazuiliki na alilokusudia wala halimpiti. Ikiwa ni hivyo, basi yeye ni muweza wa kumchukulia hatua ya adhabu ya zaidi ya uwezo wake yule mwenye kupetuka mpaka wake, na kumhifadhi juu ya yale aliyo nayo, ili aonje adhabu, Mwenyezi Mungu anasema: "Na wale ambao wamekufuru wana wao moto wa Jahannam, hawatahukumiwa kufa, wala kawatapunguziwa adhabu yake " (35:36).

Yeye nu muweza juu ya kurudisha vile vilivyoharibiwa na adhabu katika hali yake ya kwanza, ili aonje mkosaji adhabu bila ya kwisha; Mwenyezi Mungu anasema: "Hakika wale ambao wamezikanusha aya zetu, tutawaingiza katika moto. Kila ngozi zao zitakapoiva, tutawabadilisha ngozi nyingine ili wawe wanaonja (uchungu wa) adhabu ." (4:56).

Kwa ubainifu huu yanafunuka mamba hAya Na fuatayo:

kwanza : Mpangilio wa kauli yake "Hakika yeye" mpaka mwisho unafahamisha kuwa kuanzisha kupatisha na kurudisha ni kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t), kwa sababu matengenezo na kupatisha kunakomea kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) peke yake.

Pili : Mipaka ya vitu vyote iko kwake Mwenyezi Mungu akitaka kitu kisiwe na mpaka, huwa; au kubadilisha mpaka mwengine. Yeye ndiye ambaye ameweka mpaka (ukomo) wa adhabu ya dunia kuwa ni mauti, na lau asingelitaka kuiweka ukomo angefanya kama ilivyo katika ahabu ya akhera. Tatu: Kwamba makusudio ya mashiko makubwa ni kwamba hakuna wa kumzuia Mwenyezi Mungu na adhabu yake wala haukna wa kuipinga hukumu yake vyovyote vile anavyohukumu.

Aya Na 14

Yaani ni mwingi wa maghufira na mapenzi kwa kuangalia ahadi ya waumini; kama ilivyo katika aya iliyotangulia kwa kuangalia kiaga cha makafiri.

Aya Na 15-16

Arshi ni arshi ya ufalme. Kusema: Mwenye arshi ni fumbo la ufalme yaani Yeye ni mfalme anaweza kufanya vile atakavyo katika mamlaka yake. Mwenye kutenda alipendalo yaani haligeuki analolitaka, si kwa sababu ya ndani kama vile uvivu au kuchoka, wala kwa sababu za nje kwa kizuizi kitakachoingia kati yake na kati ya analolitaka. Kwa hivyo anaweza kuwapa kiaga wale waliowaadhibu waumini wanaume na waumini wanawake kwa moto na kuwaahidi wale walioamini na wakatenda amali njema kwa pepo kwa sababu Yeye ndiye mwenye arshi tukufu, wala hawezi kuvunja ahadi yake, kwa sababu Yeye ni mwingi wa kutenda alipendalo.

Aya Na 17-18

Ni tikrari ya yaliyotangulia katika mashiko yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuwa Yeye ni mfalme mkubwa mwenye kutenda alitakalo. Na hilo nikuituliza nafsi ya Mtume(s.a.w.w)

Aya Na 19

Sio mbali kutokana na mpangilio wa aya kuwa makusudio ya wale ambao wamekufuru ni katika kaumu ya mtume Muhammad(s.a.w.w) . Aya inaonyesha kususiwa mauidha yaliyotangulia, yaani haitakikani kutarajia kwao kuamini aya hizi zilizowazi, kwani wale ambai wamekufuru ni wenye kuendelea na kukabidhisha kwao, hawatanufaika na mawaidha au joha.

Aya Na 20

Nyuma ya kitu ni pambizoni mwake mnamokizunguuka. Inaonyesha kawaba wao hawawezi kumshinda Mwenyezi Mungu Yeye ni Mwenye kuwazuguuka ni muweza juu yao kwa kila upande. Na hilo pia ni katika kuituliza nafsi ya Mtume(s.a.w.w) .

Aya Na 21-22

Ni kupinga kuendelea kwao Kuikadhibisha Qur'an. Maana yake nikuwa sio kama wanavyodai, bali Qur'an ni kitabu kikubwa katika maana yake chenye kushinda katika maarifa yake kiko katika ubao wenye kuhifadhiwa na uongo na batili, na yeye ni yenye kuhifadhiwa kuguswa na shetani.

Utafiti Wa Hadith Katika Durril Manthur ametoa Ibnu Murdawayh kutoka kwa Jabir bin Abdillah kwamba Mtume(s.a.w.w) aliulizwa kuhusu mbingu yenye buruji akasema ni nyota. Akaulizwa kuhusu "ambaye amejaaliwa katika mbingu buruji" akasema ni nyota. Akaulizwa kuhusu Buruujum mushayyadah akasema ni majumba makubwa. Katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Abdu bin Hamid Attrimidhiy na Ibn Abidduniya katika Usuul; Ibn Jariyr, Ibn Al-Mundhir, Ibn Hatim, Ibn Murdawayh na Bayhaqi katika Sunan yake kutoka kwa Abu Huraira amesema: Amesema Mtume(s.a.w.w) : siku iliyoagwa ni siku ya Kiyama na siku yenye kushuhudiwa ni siku ya Arafa na shahidi ni siku ya Ijumaa.

Imepokea hadith mfano wa hiyo kwa njia nyengine kutoka Abu Malik Said Bin Al-Musabbib na Jubayr bin Mut'imu kutoka kwake Mtume(s.a.w.w) ; Shahid ni siku ya Ijumaa na chenye kumshuhudiwa ni siku ya Arafa. Imepokewa kwa tamko hili kutoka kwa Abdurrazzaq, Fariyabiyy, Abdu bin Hamid, Ibn Jariyr na Ibn Mundhir kutoka kwa Ali bin Abu Twalib. Katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Ahmad bin Hamid, Ibn Al-Mundhir kutoka kwa Ali amesema: siku iliyoagwa ni siku ya kiyama, shahidi ni siku ya ijumaa na chenye kushuhudiwa ni siku ya Idd ((Idd-el-Hajj)

Katika Majmau imepokewa kwamba mtu mmoja alingia katika msikiti wa Mtume(s.a.w.w) mara ikawa mtu mmoja anazungumzia Mtume(s.a.w.w) . Amesema: "nikaamuliza kuhusu Shahid na mwenya "kushuhudiwa", akasema: Ndio shahidi ni siku ya Ijumaa na chenye kushuhudiwa ni siku ya Arafa, nikampita na kumfuata mwengine naye pia anamzungumzia Mtume(s.a.w.w) nikamuuliza hilo, akasema: "ama shahid ni siku ya Arafa na chenye kushuhudiwa ni siku ya Idd." Nikawapita wote hao wawili nikaenda kwa kijana uso wake kama Dinar naye anamzungumzia Mtume(s.a.w.w) , nikamwambia: "nifahamishe kuhusu shahidi na chenye kushuhudiwa", akasema: ndio ama shahidi ni Muhammad na chenye kushuhudiwa ni siku ya Kiyama kwani hukusikia kauli yake Mwenyezi Mungu?: "Ewe Mtume hakika sisi tume kutuma (uwe) shahidi na mtoaji habari nzuri na mwonyaji ?" (33:45)

Akaendelea kusema: hiyo siku ya kukusanya watu, ndiyo siky yenye kushuhudiwa. Nikauliza ni nani yule wa kwanza? Wakasema: ni Ibn Abbas, wapili ni Ibn Amr na watu wakasema ni Hasan bin Ali." Hadith hiyo ni yenye kupokewa kwa njia tofauti na matamko yenye kukurubiana. Imetangulia katika tafsir ya aya kwamba aliyoyasema Hasan(a.s) ndiyo yaliyo wazi zaidi kwa kuangalia mpangilio wa aya, ingawaje tamko la shahidi na chenye kushuhudiwa halikatai kufungamana na jambo jengine vile vile.

Katika Tafsir ya Qummi kuhusu "wamelaaniwa wenye handaki" anasema: sababu yake ni kwamba yule ambaye aliitingisha Uhabeshi kwenye vita vya Yaman ni Dhu Nawas naye ndiye mfalme wa mwisho katika ukoo wa Himyar, aliingia katika dini ya Uyahudi na akawakusanya watu wa kabila ya Himyar na kuwafanya kuufuata Uyahudi. Yeye akajiita Yusuf na alidumu hivyo kwa muda mrefu. Akapata habari kwamba huko Najran kuna watu wamebaki kwenye dini ya Unasara (Ukristo) na wanahukumu kwa Injili na kiongozi wa dini hiyo ni Abdallah bin Baryam. Kwa hiyo akachukuwa watu wa dini yake kuwaendea hao Manasara ili wawaingize katika dini ya Kiyahudi. Alipofika Najran akawakusanya wale waliokuwa katika dini ya Kinasara kisha akawelezea dini ya Kiyahudi na kuwahimiza waingie. Akajadiliana nao na akatoa jitahad zake zote lakini walikataa na wakajizulia kuingia dini ya Kiyahudi.

Basi akafanya handaki, akakusanya kuni na akawasha moto. Kuna katika wao waliounguzwa wengine waliouliwa kwa upanga na akawafanyia vya kufanya, ikafikia iadadi ya waliouawa 20,000 (ishirin elfu). Akawaponyoka mtu mmoja anyeitwa Dawshi Dhu Thaalaban na farasi wake, wakamfuata mpaka akawashinda kwa mbio, akarudi Dhu nuwasi kwa askari wake. Ndio Mwenyezi Mungu akasema "wamelaaniwa wenye handaki mpaka mwisho wa Aya Na 8."Katika Majmau amepokea Said bin Jubayr amesema: waliposhindwa watu wa Isfand-han alisema Umar bin Al-Khattab: wao sio wayahudi wala wanasara wala hawana kitabu chochote na walikuwa ni Majusiy, akasema Ali bin Abi Twalib: Hapana wao walikuwa nacho kitabu, lakini kikaondolewa. Sababu ya kuondokwa kitabu nikwamba mfalme wao siku moja alilewa akamwingilia binti yake au dada yake, ulevi ulipomtoka akamwambia: "Itakuwaje kwa nililyoyanfanya? Akamjibu: "Wakusanye watu na mamlaka yako na uwaambie kwamba wewe unapendekeza watu kuonana na mabinti zao na kwamba wewe unawaamrisha walihalilishe hilo."

Kwa hivyo akawakusanya na akawapa habari ya hilo. Wakakataa kumfuata. Akawachimbia handaki katika ardhi na akawasha moto. Ikawa mwenye kukataa humtupa katika moto na mwenye kukubali humwacha. Imepokewa hadith kwa maana haya katika Durril Manthur kutoka kwa Abd bin Hamid kutokana naye Ali(a.s) . Katika Tafsir ya Iyashi, imepokewa kutoka kwa Jabir(a.s) amesema: Alitumwa Ali(a.s) kwa askofu wa kinajrani kumuuliza kuhusu wnye handaki, akamuelezea, kisha Ali(a.s) akamwambia sio kama ulivyosema, lakini nitakueleza: "Hakika Mwenyezi Mungu alimpa utume mtu mmoja wa Kihabeshi, wakamkadhibisha na kupingana naye. Wakawaua wafuasi wake, wakateka nyara na wafuasi wake. Kisha wakamjengea boma wakalijaza moto.

Wakawakusanya watu wakawaambia: "Ambaye yuko kwenye dini yetu na mambo yetu na ajitenge na ambaye tuko kwenye dini ya hawa na ajitupe mwenyewe moto. Wakawa wafuasi wake wanashindana kujitupa katika moto. Akaja mwanamke na mtoto mdogo wa mwezi mmoja. Alipotaka kujitupa aliogopa na akamuhurumia mtoto wake. Mtoto akanadi: 'usiogope nitupe mimi wa wewe katika moto kwani hakika Wallahi adhabu hii kwa Mwenyezi Mungu ni chache'. Akajitupa katika moto pamoja na mwanawe. Na huyo mtoto akawa miongoni mwa waliozungumza uchangani." Imepokewa hadith kwa maana haya katika Durril Manthur kutoka kwa Ibn Murdawayh, naye kutoka kwa Abdillahi bin Naja naye kutokana na Ali(a.s) . Vile vile imepokewa kutoka kwa Ibn Hatim, Ibn Al-Mundhir katika njia ya Hasan kutokana na Ali(a.s) kuhusu "wenye handaki" amesema hao ni wahabeshi.

Sio mbali kufahamika kwamba hadith ya wenye handaki ni matukio mbali mbali yaliyotukia uhabeshi, Yemen na Uajemi. Ziko hadith zinazozungumzia kisa chake bila ya kutaja mahali maalum pa tukio lenyewe. Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu aya "bali hii ni Qur'an tukufu katika ubao uliohifadhiwa" una ncha mbili kuumeni mwa Arshi kwenye paji la Israfil, anaposema Mwenyezi Mungu ambaye umetukuka utajo wake - wahyi, ubao hupiga paji la Israfil naye huangalia kwenye ubao na kuupeleka wahyi kwa Jibril".

Katika Durril Manthur ametoa Abu Shaykh, na Ibn Murdawayh kutoka kwa Ibn Abbas amesema: 'amesema Mtume(s.a.w.w) : ameumba Mwenyezi Mungu ubao kutokana na lulu nyeupe. Umezungushiwa Zabrajad ya kijani, maandishi yake ni ya nuru, huchunguzwa mara mia tatu na sitini (360) kila siku. Anahuisha na kufisha. Anaumba na kuruzuku. Anatukuza na kudhalilisha na anafanya analotaka.' Riwaya kuhusu Lawh ni nyingi zenye kuhitalifiana, nazo ziko juu ya namna ya kufananisha tu!.

7

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA INFITAR (KUPASUKA) (NA. 82)

INA AYA 19

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.

إِذَا السَّمَاءُ انفَطَرَتْ ﴿١﴾

1. Mbingu zitakapopasuka.

وَإِذَا الْكَوَاكِبُ انتَثَرَتْ ﴿٢﴾

2. Na nyota zitakapoputika.

وَإِذَا الْبِحَارُ فُجِّرَتْ ﴿٣﴾

3. Na bahari zitakapofunguliwa na kuchanganyika.

وَإِذَا الْقُبُورُ بُعْثِرَتْ ﴿٤﴾

4. Na makaburi yatakapopinduliwa.

عَلِمَتْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ وَأَخَّرَتْ ﴿٥﴾

5. Nafsi wakati huo itajua ilichokitanguliza na ilichobakisha nyumba.

يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ مَا غَرَّكَ بِرَبِّكَ الْكَرِيمِ ﴿٦﴾

6. Ewe mwanadamu! Ni nini kinachokughuri kwa Mola wako Mtukufu.

الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ ﴿٧﴾

7. Ambaye amekuumba, akakukamilisha, akakulinganisha?

فِي أَيِّ صُورَةٍ مَّا شَاءَ رَكَّبَكَ ﴿٨﴾

8. Akakufanya kwa Sura aliyoipenda.

كَلَّا بَلْ تُكَذِّبُونَ بِالدِّينِ ﴿٩﴾

9. Hapana sio hivyo! Bali mnayakadhibisha malipo.

وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ ﴿١٠﴾

10. Na hakika mna wenye kuwatunza.

كِرَامًا كَاتِبِينَ ﴿١١﴾

11. Watukufu wenye kuandika.

يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ ﴿١٢﴾

12. Wanajua mnayoyatenda.

يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ ﴿١٢﴾

13. Hakika watu wema watakuwa katika neema.

وَإِنَّ الْفُجَّارَ لَفِي جَحِيمٍ ﴿١٤﴾

14. Na hakika watu waovu watakuwa katika moto.

يَصْلَوْنَهَا يَوْمَ الدِّينِ ﴿١٥﴾

15. Watauingia siku ya malipo.

وَمَا هُمْ عَنْهَا بِغَائِبِينَ ﴿١٦﴾

16. Wala hawatakuwa mbali nao.

وَمَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ ﴿١٧﴾

17. Ni lipi la kukujulisha ni ipi siku ya malipo.

ثُمَّ مَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ ﴿١٨﴾

18. Kisha ni lipi la kukujulisha ni ipi siku ya malipo?

يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِّنَفْسٍ شَيْئًا وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ ﴿١٩﴾

19. Ni siku ambayo nafsi haitamilikia chochote nafsi nyengine , na amri siku hiyo ni ya Allah (peke yake).

UBAINIFU

Sura inajulisha siku ya Kiyama kwa kutaja baadhi ya alama zake zenye kulazimiana nayo na zenye kuambatana nayo. Inakisifu hicho Kiyama kwa yale yatakayotukia ndani ya siku hiyo; ambayo ni kukumbuka mtu alilolitanguliza na aliloliacha nyuma katika amali zake njema na mbaya - ambayo yamehifadhiwa na malaika wanaohusika nayo - na kulipwa amali yake. Akiwa ni mwema, basi atalipwa wema na akiwa ni mwovu mwenye kukadhibisha siku ya malipo, basi atalipwa moto atakaouingia hali ya kudumu humo. Kisha inaanzia tena kusifu hiyo siku; kwamba ni siku ambayo nafsi haitamilikia nafsi nyengine kwa chochote na amri siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu. Sura hii imeshuka Makka bila ya ubishi wowote.

Aya Ya 1

Aya hii iko kama aya inayosema: "na mbingu zitapasuka, basi siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa ." (69:16).

Aya Ya 2

Kupukutika nyota yaani kutawanyika kwa kuondoka sehemu zake zilipowekwa. Zimefananishwa nyota na lulu zilizotungwa ushanga, kisha ukakatika uzi wake, zikapukutika na kutawanyika.

Aya Ya 3

Yaani nahari zitafunguliwa kwa kuondoka kizuizi na yachanganyike maji ya tamu na ya chumvi na kuwa bahari moja. Haya ndiyo maana yanayosabiana na tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu. "Na bahari zitakapofurika " (82:6).

Aya Ya 4

Katika Majmau amesema neno Buuthirat lina maana ya kupindua chini juu. Kwa hivyo maana yake ni utakapogeuzwa mchanga wa makaburi na kugeuzwa ndani nje ili kuwatoa wafu na kufufuliwa kwa ajili ya malipo.

Aya Ya 5

Makusudio ya kujua hapa ni kujua kwa upambunuzi matendo yake aliyoyatenda duniani. Na haya sio kuwa yanapatikana kwa kupewa kitabu la! Mwenyezi Mungu anasema: "Bali mtu ni shahidi juu ya nafsi yake ingawa anatoa nyudhuru zake " (78:15).

"Siku atakayokumbuka mtu alichokitenda ". (79:35).

"Siku ambayo kila nafsi itakuta mema iiyoyafanya yamedhuhurishwa na pia ubaya ilioufanya ". (3:30).

Makusudio ya nafsi ni jinsi ya nafsi yoyote, na makusudio ya ilichokitanguliza, ni kile ilichokifanya katika uhai wake. Na kile ilichokibakisha nyuma ni kile ilichokianzia ikiwa kheri au shari na kikafanywa baada ya kufa kwake huandikwa katika karatasi ya amali yake. Mwenyezi Mungu anasema: "..na tunaliandikia kile walichokitanguliza (bila ya kuacha athari) na (kile walichokifnya kikaacha) athari zao ". (36:12) Inasemekana kuwa makusudio ya aya ni kile ilicho kifanya mwanzo wa umri wake na kile ilichokifanya mwisho wa umri wake. Kwa hiyo inakuwa ni fumbo la uchunguzi zimesemwa maana nyengine ambazo hazihitaji kutajwa hapa. Mwenye kuzitaka na ajipatie vitabu vilivyorefushwa tafsiri.

Aya Ya 6-8

Ni lawama na kumkemea mtu. Makusudio ya mtu hapa ni yule mwenye kukadhibisha siku ya malipo kama unavyofahamisha mzunguuko mzima wa maneno unaokusanya "Bali nyinyi mnakadhibisha malipo". Na kuikadhibisha siku ya malipo ni kufuru na kukanusha sheria ya malipo, na kuikanusha kwake ndio kukanusha ubwana wa Mwenyezi Mungu S.W.T. Msemo umeelekezwa kwa mtu kwa kuwa yeye ni mtu ili iwe ni hoja kwa kuthibiti mambo yaliyotajwa ya neema zinazohusikana naye kama mtu. Amefungamanisha kuhadaika na sifa mbili za ulezi wake na ukarimu wake Mwenyezi Mungu (s.w.t), ili iwe ni hoja katika kuelekeza lawama. Kwani hakika mwenye kulewa, akimwasi mlezi wake ambaye anaangalia mambo yake na kumfunika na neema zake ndani na nje, ni ukafiri usiokuwa na shaka katika ubaya wake na katika kustahiki kwake adhabu, hasa akiwa mlezi ni karimu asiyetaka kulipwa chochote katika neema yake na anachokitoa, anayesamehe makosa yanayotukia kwa kutojua. Basi ikiwa hivyo ukafiri wakati huo utakuwa mbaya zaidi, na shutuma na lawama zitakuwa kali zaidi. Kwa hivyo aya ya (6) ni swali la kukemea analokemewa mtu kwa sababu ya ukafiri, hasa usiokuwa na udhuru, nao ni ukafiri wa kukufuru neema ya Mola wake aliyekarimu.

Hawezi mtu kujibu kwa kusoma "Ewe Mola wangu umenihadaa ukarimu wako" kwani Mwenyezi Mungu amekwishayapitisha aliyoyahukumulia na kumfikishia mtu kupitia kwa ulimi wa Mitume yake; kama alivyosema; "Kama mkishukuru nitawazidishieni, na kama mkikufuru, (jueni) kuwa adhabu yangu ni kali sana." (14:7).

"Ama aliyepetuka mipaka. Akapendelea zaidi maisha ya dunia. Basi moto ndio makazi yake ." (79:39).

Zaidi ya hizo kuna aya nyenginezo zinazoelezea kwamba hakuna kuokoka kwa wale wenye kufanya inadi na adhabu; na ukarimu hautawafikia siku ya Kiyama. "Na rehema yangu inaenea kila kitu, lakini nitawaandikia wale wanaojikinga na yale niliyoyakataza ". (7:156) Lau kungemtosheleza mtu mwenye kuasi kusema "umenihadaa ukarimu wako" basi angeliepuka na adhabu kafiri mwenye kufanya inadi, kama itakavyoondolewa kwa muumini aliyeasi. Wala hapana udhuru baada ya ubainifu.

Aya Ya 7

Ni ubainifu wa ulezi wake wenye kuwa pamoja na ukarimu, kwani ni katika kuangalia kwake vizuri kumuumba mtu kwa mafungu yake yote na kumfanya sawa kwa kuweka kila kiungo mahali pake panaponasibiana nacho; kisha akalinganisha baadhi ya viungo vyake na akavitia nguvu kwa baadhi ya viungo vyengine kwa kufanya wizani na ulinganifu kati yao. Kwa hivyo kiungo hakiwezi kukidhoofisha kuingo chengine; kama vile kula kwa kumega tonge ambako ni kwa ajili ya mdomo na mdomo nao unalikata tonge na kulitafuna, hilo linatimia kwa meno tofauti, halafu inahitajika kulipeleka tonge katika pembe za mdomo na kuligeuza, na kazi hiyo inafanywa na ulimi. Na mdomo katika kula unahitaji kuwekewa chakula, hilo linafanywa na mkono na kazi hiyo inatimizwa na kiganja na kufanya kazi kwake ni kwa vidole vyenye manufaa tofauti. Mkono nao unahitaji kuchukua na kuweka mahali na hilo linafanywa na mguu. Ni kama hivyo kazi za viungo vyengine. Ni maelfu kwa maelfu yasiyohisabika katika mipango yake Mwenyezi Mungu, ambaye anayafanya yote hayo bila ya kutaka kujinufaisha au kumzuia yeye mambo ya mtu ya kusahau shukrani na kuikufuru neema. Yeye Mwenyezi Mungu ni Mola Mkarimu.

Aya Ya 8

Ni ubainifu wa kauli yake "Akakulinganisha sawa" yaani katika Surah yoyote aliyopenda akakufanya - wala hataki ila lile lenye hekima - akakufanya mke na mume, mweupe na mweusi, mrefu na mfupi, mzuri na mbaya na mwenye nguvu na mnyonge na mengineo. Vile vile viungo vyenye kushurikiana kati ya watu kwa namna tofauti mfano mikono miwili , miguu miwili na macho mawili. Pia kichwa na kiwiliwili na kulingana sawa kimo nk. Yote hayo ni katika kulinganisha baadhi ya viungo na vyengine. Mwenyezi Mungu anasema: "Hakika tumemuumba mwanadamu katika hali nzuri mno ." (95:4). Yote hayo yanaishilia kwenye mazingatio mazuri yake Mola hakuna utengenezaji wa mtu katika hilo.

Aya Ya 9

Ni kuzuia kughurika mtu na ukarimu wa Mwenyezi Mungu na kulijaalia hilo ni wasila wa kufuru na uasi, yaani msighurike hakutawafaa kughurika.

Aya Ya 10 - 12: Ni ishara ya kwamba amali za mtu zitahudhurishwa na ni zenye kuhifadhiwa siku ya Kiyama kwa njia nyengine isiyokuwa kukumbuka kwake mtu. Njia ambayo ni kwa kuandika waandishi wa amali katika malaika wenye kuwakilishwa kwa mtu kwa kumchukulia hisabu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na tutamtolea siku ya Kiyama daftari (iliyoandikwa amali yake) atakayoikuta imekunjuliwa (aambiwe) soma daftari yako, nafsi yako leo inakutosha kukuhisabu ". (17:13-14).

Kwa hivyo kusema kwake Mwenyezi Mungu : "Na hakika wenye kuwatunza" Yaani hakika mna wenye kuwatunza kutoka kwetu wanaohifadhi amali kwa kuziandika. Kusema kwake "watukufu wenye kuandika" yaani wenye utukufu na enzi mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Imekaririka katika Qur'an tukufu kuwasifu Malaika kwa utukufu, na hilo sio mbali kuwa makusudio yake kwa kusaidiwa na mpangilio wa maneno, ni kuwa wao kimaumbile ni wenye kuhifadhiwa na madhambi na maasi.

Hilo linatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Bali (hao Malaika) ni waja waliotukuzwa. Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri zake ". (21:26-27).

Hilo linafahamisha kuwa wao hawataki isipokuwa analolitaka Mwenyezi Mungu, wala hawafanyi ila waliloamrishwa na Mwenyezi Mungu. Vile vile kauli yake: "Watukufu watenda njema ". (80:16).

Makusudio ya kuandika ni kuandika amali kwa kukutanisha na kauli yake wanajua mnayoyafanya. Kauli yake Mwenyezi Mungu: wanajua mnayoyafanya ni kukanusha makosa yao katika kuihusisha heri na shari kama ilivyotangulia aya ya kuwaepusha na madhambi na maasia, wao ni wenye kuzunguukwa na matendo kama yalivyo na sifa zake, lakini ni wenye kuhifadhiwa nayo. Imekuja katika tafsiri ya aya: "Hakika Qur'an ya Al-Fajiri inashuhudiwa (na Malaika) ". (17:78).

Kwamba waandishi wa amali wa mchana wanapanda nayo, baada ya kutua jua na wanashuka wengine wanaadhika amali ya usiku mpaka Al-Fajiri wanapande na wanashuka Malaika wa mchana na kadhalika.

Aya Ya 13 -14

Ni maelezo yanayobainisha natija ya kuhifadhi amali kwa kuandikwa na waandishi nayo ni kudhihiri siku ya Kiyama. Wema ni wale wenye amali njema na waovu ni wale wenye dhambi.

Aya Ya 15

Dhamiri ni ya moto; yaani waovu watalazimiana nao siku ya malipo.

Aya Ya 16

Inaungana na aya iliyotangulia, inatilia nguvu maana ya kulazimiana nao na moto na kukaa kwao milele. Makusudio ya kutokuwa mbali nao ni kutotoka humo. Aya hii iko katika maana ya aya inayosema: "wala hawatakuwa wenye kutoka motoni ". (2:167).

Aya Ya 17

Ni utisho na kulikuza jambo la siku ya malipo; yaani haiwezi kujulikana nini hakika ya siku ya malipo. Hii ni ibara ya fumbo la kulikuza jambo.

Aya Ya 18

Ni kutilia mkazo ukubwa wake.

Aya Ya 19

Ni ubainifu wa kijumla wa hakika ya siku ya malipo. Hilo ni kwamba athari zote zenye kufungana na sababu za dhahiri ni zenye kukatika, kama kunavyofahamisha kusema kwake Mwenyezi Mungu: "na yatakatika mafungamano yao ". (2:166).

Kuhusu kusema kwake "na amru siku hiyo ni ya Allah" yaani yeye ni mwenye kumiliki amri si mwengine; kama alivyosema: "Leo ufalme ni wa nani" Ni wa Allah mmoja mwenye kushinda " (40:16).

Kusema kuwa neno Amr lina maana ya jambo hakuafikiani. Na mahali hapa.

Utafiti Wa Hadith Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu kusema kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) "Na makaburi yatakapopinduliwa" amesema yatapasuka na watatoka watu. Katika Durril Manthur ametoa Hakim na akaisahihisha kutoka kwa Hudhayfa amesema: "Amesema Mtume(s.a.w.w) : Mwenye kuanzisha heri ikafuatwa atakuwa na malipo mfano wa malipo ya wanaomfuata bila ya wao kupungukiwa. Na mwenye kuanzisha shari ikafuatwa basi atapata dhambi zake na dhambi za mfano wa wanaomfuata bila ya wao kupungukiwa. Akasoma Hudhayfa "Itajua nafsi na ilichokitanguliza na ilichokibakisha nyuma". Katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Abd bin Hamid kutoka kwa Saleh bin Miswar amesema: "Imenifikilia mimi habari kwamba Mtume(s.a.w.w) amesoma aya hii: "Ewe mwanadamu! Ni nini kinachokughuri kwa Mola wako Mtukufu; kisha akasema ni ujinga wake ".

Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu "Akakufanya kwa sura yoyote aliyopenda" anasema: Lau angetaka angekufanya sura isiyokuwa hii. Katika hiyo hiyo Tafsiri kuhusu "na hakika mna wenye kuwatunza" amesema: "Ni Malaika wawili wawakilishi kwa mtu." Kutoka kwa Saad Assu'ud ni kwamba hao Malaika wawili wanamjia Muumin wakati wa swala ya Al-Fajiri wakishuka wale wengine wa usiku huondoka, linapotua jua hushuka wale wa usiku na kuondoka wa mchana. Hiyo inakuwa ni ada yao mpaka anapofikiwa na mauti yake wakati yakifikia mauti yake husema hao Malaika wawili kumwambia mtu mwema: "Allah akulipe uliyosuhubiana nasi kwa kheri, amali ngapi njema umetuonyesha! Kauli ngapi nzuri umetusikilizisha! Na ni vikao vingapi vya kheri umetupeleka! Basi leo sisi tuko juu ya lile unalolipenda na waombezi kwa Mola wako."

Akiwa ni asi (muovu) humwambia: "Mungu akulipe uliyesuhubiana nasi kwa shari, ulikuwa ukituudhi, ni amali ngapi mbaya ulizotuonyesha! Ni kauli ngapi mbovu ulizotusikilizisha! Na ni vikao vingapi viovu ulivyotupeleka! Basi sisi leo tuko juu ya lile unalolichukia na mashahidi mbele za Mola wako." Katika Majmau kuhusu "Na amri siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu" amepokea Amr bin Shamr kutoka kwa Jabir naye kutoka kwa Abu Jaffar(a.s) amesema: "Amri siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu na siku yote ni ya Mwenyezi Mungu. Ewe Jabir siku ya Kiyama mahakimu wote watakomea, hatabakia hakimu isipokuwa Mwenyezi Mungu."

Makusudio yake Imam ni kwamba, kuwa amri ni ya Mwenyezi Mungu, hakuhusika na siku ya Kiyama tu, bali amri ni ya Mwenyezi Mungu milele, na kuihusisha na siku ya Kiyama, ni kwa kuzingatia kudhihiri hiyo amri na wala sio asili yake yaani kudhihiri kwa kuonekana; siku hiyo hakutakuwa na amri ya mwengine yoyote isipokuwa Yake Yeye Mtukufu.

8

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA MUTAFFIFIN (WAPUNGUZAJI VIPIMO) (NA. 83)

Aya ya 1-21

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu

وَيْلٌ لِّلْمُطَفِّفِينَ ﴿١﴾

1. Ole wao wenye kupunguza (vipimo).

الَّذِينَ إِذَا اكْتَالُوا عَلَى النَّاسِ يَسْتَوْفُونَ ﴿٢﴾

2. Ambao wakijipimia kwa watu kwa pishi hujikamilishia.

وَإِذَا كَالُوهُمْ أَو وَّزَنُوهُمْ يُخْسِرُونَ ﴿٣﴾

3. Na wanapowapimia wao kwa pishi au kwa mizani, hupunguza.

أَلَا يَظُنُّ أُولَـٰئِكَ أَنَّهُم مَّبْعُوثُونَ ﴿٤﴾

4. Jee, hawadhani hao kuwa watafufuliwa?

لِيَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿٥﴾

5. Katika siku kubwa.

يَوْمَ يَقُومُ النَّاسُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٦﴾

6. Siku ambayo watu watasimama mbele ya Mola wa viumbe.

كَلَّا إِنَّ كِتَابَ الْفُجَّارِ لَفِي سِجِّينٍ ﴿٧﴾

7. Si hivyo! Hakika maandishi ya watu waovu yamo katika Sijjin.

وَمَا أَدْرَاكَ مَا سِجِّينٌ ﴿٨﴾

8. Ni lipo la kukujulisha nini hiyo Sijjin.

كِتَابٌ مَّرْقُومٌ ﴿٩﴾

9. Ni daftari iliyoandikwa (amali za watu waovu).

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُكَذِّبِينَ ﴿١٠﴾

10. Ole wao siku hiyo wenye kukadhibisha.

الَّذِينَ يُكَذِّبُونَ بِيَوْمِ الدِّينِ ﴿١١﴾

11. Ambao hukadhibisha siku ya malipo.

وَمَا يُكَذِّبُ بِهِ إِلَّا كُلُّ مُعْتَدٍ أَثِيمٍ ﴿١٢﴾

12. Wala haikadhibisha ila kila mpetuka mipaka mwingi wa madhambi.

إِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِ آيَاتُنَا قَالَ أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿١٣﴾

13. Ambaye anaposomewa aya zetu husema: ni ngano za watu wa kale.

كَلَّا بَلْ رَانَ عَلَىٰ قُلُوبِهِم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿١٤﴾

14. Si hivyo! Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao waliyokuwa wakiyachuma.

كَلَّا إِنَّهُمْ عَن رَّبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّمَحْجُوبُونَ ﴿١٥﴾

15. Si hivyo! Hakika wao siku hiyo watazuiliwa kupata rehema ya Mola wao.

ثُمَّ إِنَّهُمْ لَصَالُو الْجَحِيمِ ﴿١٦﴾

16. Kisha wao wataingia motoni.

ثُمَّ يُقَالُ هَـٰذَا الَّذِي كُنتُم بِهِ تُكَذِّبُونَ ﴿١٧﴾

17. Kisha wataambiwa: Hili ndilo ambalo mlikuwa mkilikadhibisha.

كَلَّا إِنَّ كِتَابَ الْأَبْرَارِ لَفِي عِلِّيِّينَ ﴿١٨﴾

18. Si hivyo! Hakika maandishi ya watu wema yamo katika Illiyyin?

وَمَا أَدْرَاكَ مَا عِلِّيُّونَ ﴿١٩﴾

19. Ni lipi la kukujulisha ni nini Illiyyin?

كِتَابٌ مَّرْقُومٌ ﴿٢٠﴾

20. Ni daftari iliyoandikwa (amali za watu wema).

يَشْهَدُهُ الْمُقَرَّبُونَ ﴿٢١﴾

21. Ambayo hushuhudiwa na wenye kukurubishwa.

UBAINIFU

Sura inaanzia kwa kutoa makamio kwa wale wenye kupunguza vipimo katika pishi au mizani na kuwaonya kwamba wao watafufuliwa kwa ajili ya malipo katika siku iliyokuwa kubwa, nayo ni siku ya Kiyama. Kisha inafafanua yale yatakayowapitia siku hiyo waovu na wema. Inavyonasibu zaidi kwa kuangalia mpangilio ni kuwa mwanzo wa Sura unaoelezea makamio kwa wenye kupunguza kipimo, umeshuka Madina. Ama aya zinazofuatia mpaka mwisho wa Sura zinakubali kufungamana na mpangilio wa Makka na Madina.

Aya Ya 1

Ni makamio juu ya wanaopunguza vipimo. Mwenyezi Mungu amelikataza hilo, na ameliita ufisadi katika nchi, kama alivyolielezea katika kauli ya Mtume Shuayb. "Na enyi watu wangu! Timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwapunguzie watu vitu vyao, wala msieneze uovu katika nchi mkafanya ufisadi ." (11:85).

Aya Ya 2-3

Madhumuni ya aya zote mbili ni shutumu ya aina moja; hayo ni kwamba wao wanachunga haki yao tu! Na wala hawachungi haki ya wengine. Kwa maneno mengine, hawachungi haki za wengine, kama vile wanavyochunga haki zao. Jambo hilo linaleta ufisadi katika jamii ya watu iliyojengwa juu ya uadilifu na haki. Haikutajwa mizani katika aya ya 2 kama ilivyotajwa katika aya ya 3 kwa sababu imesemwa kuwa wapunguzaji vipimo aghlabu walikuwa wakinunua nafaka na mazao, kisha wanachuma, kwa kuyauza kidigo kidogo. Desturi yao ilikuwa zaidi ni kunuliwa kwa pishi, sio kwa mizani ndio ikatajwa pishi peke yake katika aya ya pili. Imesemwa kuwa haikutajwa mizani kwa sababu mizani na pishi ni za kununua na kuuza, ikitajwa moja yao, inatosha kufahamisha juu ya nyengine na yale yaliyotajwa katika pishi yanapita pia katika mizani. Njia hiyo haiwezi kuepuka kuangaliwa vizuri. Imesemwa kuwa aya mbili zinaelezea mazoea waliyokuwa nayo wale ambao Sura imetereshwa kwa sababu yao. Walikuwa wakinunua kwa pishi tu! Na wakiuza kwa mizani na pishi. Njia hii ni madai yasiyokuwa na dalili. Mengi yametajwa kwa njia ya kufupisha juu ya pishi ambayo hayaepukani na udhaifu.

Aya Ya 4-5

Ni swali la kukanusha na kustaajabu. Kuishiria wenye kupunguza vipimo kwa neno "hao" nikuishiria kwa umbali, kwa maana ya kuwa kwao mbali na Rehema ya Mwenyezi Mungu. 'Siku kubwa' ni siku ya Kiyama. Kutosheka kutaja ufufuo kwa kudhani tu, pamoja na kuwa ni wajibu kuitakidi kwa kujua na sio kwa kudhani, ni kwamba, kudhania hatari katika amali yoyote kunawajibisha kuepuka kuifanya amali hiyo hata kama haikujulikana. Kwa hiyo kudhania ufufuo katika siku kubwa ambayo atawaadhibu Mwenyezi Mungu watu kwa yale waliyoyachuma kunakataza kufanya dhambi kubwa ambayo itawajibisha adhabu yenye machungu. Imesemekana kuwa dhana hapa ni kwa maana ya kujua. Aya Ya 6: Makusudio ya kusimama ni fumbo la kuwa kwao hai baada ya kufa, ili waende kwenye hukumu yake Mwenyezi Mungu.

Aya Ya 7 -10

Ni kupinga yale waliyokuwa nayo katika kupunguza vipimo na kughafilika na ufufuo na hisabu. Kuhusu maana ya Sijjin mwenye kuangalia vizuri na kufikiri katika mpangilio wa aya nne, kwa kupima baadhi yake na nyengine na kupima mkusanyiko wake na mkusanyiko wa Illiyyin mpaka kutimia aya nne, ni kwamba makusudio ya Sijjin ni mkabala wa makusudio ya Illiyyin na neon Illiyin linatokana na neno Alaa yaani "juu" kwa hiyo Sijjin ina maana ya chini na kufungika; kama inavyoonyesha kauli yake Mwenyezi Mungu: "Kisha tukamrejeza chini ya waliochini (95:5).

Karibu zaidi ni kuwa maana yake ni jela kwa maana ya kufunga. Makusudio ya maandishi ya watu waovu ni yale aliyowakadiria Mwenyezi Mungu katika malipo na kuyathibitisha kwa hukumu yake. Tunayoyapata katika aya, ni kwamba yule ambayo ameyathibitisha Mwenyezi Mungu katika malipo yao au aliyowaandalia yako katika jela ambayo atafungwa mwenye kuiingia kifungo kirefu au milele.

Maana ya neno Marquum kama alivyosema Raghib ni hati nene. Na imesemwa ni kupanga kitabu. Na neno lake Mwenyezi Mungu ni lenye kuchukua njia zote mbili. Maana ya pili ndiyo yenye kunasibiana zaidi. Kwa hivyo inaishia kwamba maana yake ni kuwa, yale waliyoandikiwa ni yenye kubainishwa; yasiyokuwa na utatanishi wowote. Yaani hukumu ni lazima haibadiliki. Na imefahamika kuwa ni yenye kuhukumiwa wao, yenye kuthibitishwa na yenye kufafanuliwa bila utatanishi wowote. Kauli yake Mwenyezi Mungu: "Ole wao siku hiyo wenye kukadhibisha", ni kuwatakia shari waovu. Yaani na waanagamie waovu,- ambao ni wale wenye kukadhibisha siku hiyo yatahakikika yale aliyowaandikia Mwenyezi Mungu na kuwahukumia malipo. Haya ndiyo yanayofahamika kutokana na kuangalia vizuri (Tadabbur) aya hizi nne, nazo zina mpangilio mmoja wenye kuafikiana.

Watu wana kauli mbalimbali katika tafsiri ya matamko na jumla za aya hizi nne kama vile kuwa maana ya neno kitab ni maandishi ya matendo yao. Na imesemwa ni kuandika na kwamba kuna neno lilioondolewa kukadiria kwake ni: 'hakika kuandika amali ya watu waovu ni katika Sijjin. Imesemwa neno " hakika waovu" ni lenye kuenea zaidi kuliko wenye kukadhibisha kwa sababu linakusanya ukafiri na ufasiki. Na wamesema: " makusudio ya Sijjin ni ardhi ya saba chini, huweka maandishi ya watu waovu." Na imesemwa ni bonde katika Jahannam. Pia imesemwa ni shimo katika Jahannam na imesemwa ni jina la kitabu chao. Imsemwa Sijjin ya kwanza ni mbali ambapo panawekwa kitabu chao na Sijjin ya pili ni jina la kitabu chao. Imesemwa ni kitabu chenye mkusanyiko wa amali mbovu za majini na watu. Imesemwa ni hasara na utwezo. Wamesema kuwa aya ya (9) sio tafsiri ya Sijjin bali ni tafsiri ya kitabu kilichotajwa katika aya ya (7). Lakini ukiangalia vizuri utakuta nyingi za kauli hizi ni kujiamulia tu bila ya dalili yoyote.

Aya Ya 11

Ni tafsiri ya aya iliyotangulia. Kwa dhahiri makusudio ya kukadhibisha ni kukadhibisha kwa kauli iliyowazi, kwa hivyo inahusika na kuwatusi makafiri, wala haiwachanganyi mafasiki katika watu wa imani pia haihusiki na yeyote mwenye kupunguza kipimo bali ni makafiri katika wao. Hayo yanatiliwa nguvu na aya inayofuatia. Lakini kama ikikusudiwa kukabidhisha kimatendo, itakuwa inakusanya waovu katika wenye imani, kama vile ambavyo huenda hayo yanatiliwa nguvu na aya ya (4) "Je, hawadhani hao kuwa watafufuliwa?"

Aya Ya 12

Inajulikana kuwa kizuizi pekee cha maasi si kuamini ufufuo na malipo. Na mwenye kung'ang'ania kwenye matamanio, na kuufungamanisha moyo wake kwa kupetuka mipaka katika dhambi, inakataa nafsi yake kusalimika na kujizuia na yanayokatazwa na kuishia kukadhibisha ufufuo na malipo. Mwenyezi Mungu anasema: "Kisha ulikuwa mwisho wa wale waliofanya ubaya ni kuzikadhibisha aya za Allah na walikuwa wakizicheza shere " (30:10).

Aya Ya 13

Makusudio ya aya za Qur'an, kwa kuunganisha na neno "wakisomewa". Maana yake ni wakisomewa aya za Qur'an ambazo zinawahadharisha na maasi na kuwaonya kwa ufufuo na malipo, husema ni ngano za watu wa kale.

Aya Ya 14

Ni kupinga yale waliyoyasema wenye kukadhibisha kuwa ni ngano za watu wa kale. Anasema Raghib: Rana ni kitu inayokuwa juu ya kitu safi. Mwenyezi Mungu anasema: "Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao" yaani hilo limekuwa kama kutu juu ya usafi wa moyo, wakapofuka kujua kheri na shari. Kuwa waliyokuwa wakiyachuma ni kutu juu ya nyoyo zao nikuwa dhambi ni kizuwizi cha kuipata haki kama ilivyo. Katika aya yanadhiri mambo yafuatayo:

Kwanza : Kwamba amali mbaya zina nakshi na picha.

Pili : Kwamba nakshi hizo na picha hizo zinazuiya nafsi kuipata haki kama ilivyo na kuiwekea kizuwizi. Tatu: Kwamba tabia ya mwanzo ya nafsi ni usafi unaotambua haki kama ilivyo na kuipambanua na batili na kupambanua kati ya twaa na maasia Mwenyezi Muungu amesema: "Na (kwa) nafsi na aliyelingamanisha akaifahamisha maasia yake na twaa yake ".(91:7-8).

Aya Ya 15

Ni kukataza kuchuma madhambi yenye kuweka kizuwizi kati ya moyo na kuipata haki. Makusudio ya kuwa wao ni wenye kuzuiliwa na Mola wao siku ya Kiyama, ni kizuiliwa na utukufu wa ukaribu na cheo. Huenda makusudio ni yale aliyoyasema msemaji: "hakika makusudio, ni kuwa wao ni wenye kuzuiliwa na Rehema ya Mola wao". Ama kuondoka kizuizi kwa maana ya kuondoka sababu zenye kuwa kati yake Mwenyezi Mungu na viumbe vyake na maarifa yenye kutimia ya kumjua Mwenyezi Mungu, hilo linapatikana kwa kila mtu. Mwenyezi Mungu amesema: "..na watajua kwamba Allah ni haki iliyodhahiri ."(24:25).

Aya Ya 16

Yaani wataingia na kubaki ndani yake au watafukizwa joto lake kama walivyofasiri wengineo.

Aya Ya 17

Ni kuaibisha. Na mwenye kuyasema hayo ni mtunzaji wa moto au watu wa peponi.

Aya Ya 18-20

Illiyyin ni juu na inafungamana na daraja za juu na vyeo kama vile ambavyo kinyume chake ni Sijjin. Maana ya aya tatu hizi ni mfano wa maana ya aya tatu zilizotangulia ambazo zinakabiliana nazo (aya ya 7, 8 na 9).

Kwa hivyo maana ni kwamba yale ambayo yameandikwa kwa ajili ya watu wema na kuhukumuliwa kuwa ni malipo ya wema wao, yako katika Illiyyin. Ni lipi la kukujulisha nini Illiyyin? Ni jambo lenye kuandikwa na lenye kuandikwa na lenye kupitishwa kwa hukumu ya mkato iliyowazi bila ya uficho. Watu wana kauli nyingi kuhusu aya hizi kama ilivyo katika zile zilizotangulia, isipokuwa miongoni mwa kauli kususu Illiyyin ni kwamba hiyo ni mbingu ya saba chini ya arshi ambako kuna roho za waumini. Na imesemwa ni Sidratul-Muntaha ambako kunaishia amali. Imesemwa ni ubao wa zabarjadi ulioko chini ya arsh, wenye kutungikwa na wenye kuandikwa amali.

Aya Ya 21

Yenye kunasibu zaidi kutokana na maana ya aya zilizotangulia ni kuwa maana ya kushuhudia ni kuona na wenye kukurubishwa ni watu wa peponi, walio na daraja ya juu zaidi kuliko watu wema wote, kama yatakavyokuja maana ya aya ya 28.

Makusudio ya kuona ni kuoneshwa na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amesema mfano wa hayo kuhusu moto. "Si hivyo! Lau mngejua ujuzi wa yakini. (Msingejishughulisha na hayo). Hakika mtauona moto ". (102:56). Katika hilo inadhihiri kuwa wenye kukurubishwa ni watu ya yakini. Imesemwa kuwa kushuhudia ni kuhudhuria na wenye kukurubishwa ni Malaika. Makusudio yake ni kuhudhuria Malaika kwenye maandishi ya amali zao wanapoyapeleka kwa Mwenyezi Mungu. Imesemwa wenye kukurubishwa ni watu wema na Malaika wote. Kauli hizo mbili zina muweko wa kuwa makusudio ya kitabu ni maandishi ya amali. Lakini umekwisha elezwa udhaifu wake.

Utafiti Wa Hadith Katika Tafsiri ya Qummi katika Riwaya ya Abul-Jarud kutoka kwa Abu Jaffar(a.s) amesema: Iliteremshwa Sura ya Al-Mutwaffifin kwa Mtume(s.a.w.w) wakati alipofika Madina, wakati huo wakazi wa hapo walikuwa ni waovu zaidi ya watu wote kwa kipimo na wakawa wazuri. Katika Kafi kwa isnadi yake kutoka kwa Abu Hamza Ath-Thimali amesema: "Nimemsikia Abu Jaffar(a.s) , akisema: "Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametuumba katika watu walio juu zaidi wa Illiyyin. Akaumba nyoyo za wafuasi wetu katika lile tuliloumbiwa sisi isipokuwa viwiliwili vyao. Kwa hivyo nyoyo zao zinapondokea kwetu, kwa sababu zimeumbwa kutokana na lile tuliloumbiwa sisi, kisha akasoma aya hizi (18, 19, 20 na 21). Na ameumba nyoyo za maadui zetu kutoka katika Sijjin na akaziumba nyoyo za wafuasi wao kutokana na lile waliloumbiwa wao isipokuwa viwiliwili vyao, kwa hiyo nyoyo zao zinapondekea kwao kwa sababu zimeumbiwa lile waliloumbiwa wao;" kisha akasoma aya hizi (7, 8, 9, na 10).

Imepokewa hadith mfano wa hiyo katika Kafi kwa njia nyengine kutoka kwa Athimali naye kutoka kwa Abu Jaffar(a.s) .

Na amepokea mfano wake katika Ilalish-Sharaii kutoka kwa Zaid Ash-Shahham kutoka kwa Abu Abdillahi. Na Hadith - kama unavyoona - inatilia nguvu yale tuliyoyatanguliza kuyaeleza katika maana ya aya. Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Hakika maandishi ya watu waovu yamo katika Sijjin", anasema : yale aliyowaandikia Mwenyezi Mungu katika adhabu yamo katika Sijjin. Katika hiyohiyo Tafsiri ya Qummi katika riwaya ya Abul-Jarud kutoka kwa Abu Jaffar(a.s) amesema: "Sijjin ni ardhi ya saba na Illiyyin ni mbingu ya saba ".

Lau riwaya hiyo ni sahihi basi itakuwa pepo na moto ziko pande mbili ya juu na ya chini. Kwa hiyo iko haja ya kuangalia vizuri riwaya hiyo; kama vile kuhisabu kaburi kuwa ni bustani ya peponi au ni shimo la Jahannam, na kuhisabu jangwa la Barhut kuwa ni mahali pa Jahannam. Katika Durril Manthur ametoa Ibn Al-Mubarak kutoka kwa Said bin Al-Musayyib amesema: "Salman alikutana na Abdallah bin Salaam, akasema mmoja wao kumwambia mwenzake ukifa kabla yangu njoo uniambie aliyokufanyia Mola wako nami nikifa kabla yako nitakuja kukupa habari. Akasema Abdalla vipi itakuwa? Akasema ndio hakika roho za waumini zinakuwa katika Barzakh katika ardhi zinakwenda popote zinapotaka na za makafiri zitakuwa katika Sijjin, na Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi."

Katika Usulul-Kafi kwa isnadi yake kutoka kwa Zurara naye kutoka kwa Abu Jaffar(a.s) amesema: "Hakuna mja yoyote ila katika moyo wake kuna doa jeupe, akifanya dhambi kutokea doa jeusi, akitubia huondoka huo weusi, akiendelea na dhambi, huzidi weusi mpaka unafunika weupe. Ukifunikwa weupe, mwenye moyo huo hawezi kurudi kwenye heri milele. Na hiyo ndiyo kauli yake Mwenyezi Mungu: "Si hivyo! Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao waliyokuwa wakiyachuma".

Imepokewa hadith kwa maana haya katika Durril Manthur kutoka kwa maswahaba kadhaa, kutoka kwa Abu Huraira naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) . Katika hiyo hiyo Durril Manthur kwa isnadi yake kutoka kwa Abdalla bin Muhammad Al-Hajjal kutoka kwa baadhi ya maswahaba zetu amesema: "Amesema Mtume(s.a.w.w) kumbushaneni, kutaneni na zungumzeni, kwani mazungumzo ni usafi wa moyo. Hakika nyoyo zinashika kutu kama unavyoshika kutu upanga na usafi wake ni mazungumzo.

Kutoka kwa Rawdhatul-Waidhiya amesema: "amesema Al-Baqir(a.s) : "Hakika kitu kinachoharibu moyo kama makosa. Hakika moyo unapofanya makosa basi huendelea kuwa nayo mpaka uyashinde." Amesema Mtume(s.a.w.w) : Hakika muumin akifanya dhambi kunakuwa na doa jeusi katika moyo wake akitubia na kutka msamaha hukwatuka, akizidi na dhambi nalo huzidi. Hiyo ndiyo kutu aliyoitaja Mwenyezi Mungu aliposema: "Si hivyo! Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao waliyokuwa wakiyachuma ".

Aya 22-36

إِنَّ الْأَبْرَارَ لَفِي نَعِيمٍ ﴿٢٢﴾

22. Hakika watu wema watakuwa katika neema.

عَلَى الْأَرَائِكِ يَنظُرُونَ ﴿٢٣﴾

23. Wakiwa juu ya malili wanatazama.

تَعْرِفُ فِي وُجُوهِهِمْ نَضْرَةَ النَّعِيمِ ﴿٢٤﴾

24. Utaona katika nyuso zao kunyinyirika kwa neema.

يُسْقَوْنَ مِن رَّحِيقٍ مَّخْتُومٍ ﴿٢٥﴾

25. Watanyweshwa mvinyo wenye kufunikwa.

خِتَامُهُ مِسْكٌ وَفِي ذَٰلِكَ فَلْيَتَنَافَسِ الْمُتَنَافِسُونَ ﴿٢٦﴾

26. Mwisho wake (ni) miski na katika hayo nawashindane wenye kushindana.

وَمِزَاجُهُ مِن تَسْنِيمٍ ﴿٢٧﴾

27. Na cha kuchanganyia ni Tasnim.

عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا الْمُقَرَّبُونَ ﴿٢٨﴾

28. Chemchemi ambayo hunywewa na wenye kukurubishwa.

إِنَّ الَّذِينَ أَجْرَمُوا كَانُوا مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا يَضْحَكُونَ ﴿٢٩﴾

29. Hakika wale ambao wamefanya makosa walikuwa wakiwacheka wale walioamini.

وَإِذَا مَرُّوا بِهِمْ يَتَغَامَزُونَ ﴿٣٠﴾

30. Na walipokuwa wakiwapitia wakikonyezana.

وَإِذَا انقَلَبُوا إِلَىٰ أَهْلِهِمُ انقَلَبُوا فَكِهِينَ ﴿٣١﴾

31. Na walipokuwa wakirudi kwa watu wao wakirudi huku wakiona raha.

وَإِذَا رَأَوْهُمْ قَالُوا إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ لَضَالُّونَ ﴿٣٢﴾

32. Na walipokuwa wakiwaona wakisema: "Hakika hawa wamepotea!"

وَمَا أُرْسِلُوا عَلَيْهِمْ حَافِظِينَ ﴿٣٣﴾

33. Wala hawakupelekwa wao kuwatunza.

فَالْيَوْمَ الَّذِينَ آمَنُوا مِنَ الْكُفَّارِ يَضْحَكُونَ ﴿٣٤﴾

34. Basi leo wale ambao wameamini wanawacheka makafiri.

عَلَى الْأَرَائِكِ يَنظُرُونَ ﴿٣٥﴾

35. Wakiwa juu ya malili wanatazama.

هَلْ ثُوِّبَ الْكُفَّارُ مَا كَانُوا يَفْعَلُونَ ﴿٣٦﴾

36. Ja, makafiri wamelipwa kwa waliyokuwa wakiyafanya.

UBAINIFU

Ni ubainifu ulio na baadhi ya ufafanuzi wa utukufu wa cheo cha watu wema na ukubwa wa daraja yao mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) na kwamba wao kwa kuwa walikuwa wakidharauliwa na makafiri na kuchekwa na wao watawacheka na kuangalia adhabu wayoipata.

Aya Ya 22

Neno Naim lina maana nyingi. Yaani hakika watu wema watakuwa katika neema nyingi zisizoweza kusifiwa.

Aya Ya 23

Malili ni viti vya enzi vya kifahari vyenye kupambwa. Kutaja kutazama tu; Bila ya kusema ni kutazama kitu gani, kunatilia nguvu kuwa ni kutazama mandari ya pepo yenye kufurahisha na neema zilizomo. Imesemwa kuwa makusudio ya kutazama hapa ni kutazama yale wanayolipwa makafiri.

Aya Ya 24

Hayo anaambiwa Mtume(s.a.w.w) . Na hukumu ni yenye kuenea kwa wote; kwa maana kila mwenye kuangalia kwenye nyuso zao ataona kwenye nyuso zao kupendeza, kwa neema waliyonayo.

Aya Ya 25

Ni mahali pake kusifiwa kwa sifa ya kufungwa kwa vizibo, kwa sababu huzibwa kitu kisafi ili kisalimike na hadaa yoyote na kuchanganyika na kitu kitakachokiharibu.

Aya Ya 26

Imesemwa maana yake ni kufungwa kwake miski badala ya udongo. Na imesemwa maana yake ni kuwa mwisho wa ladha anayoipata mnywaji ni harufu ya miski. Kuhusu kauli yake "nawashindane wenye kushindana" ni kuvutiwa kuyapata yale yaliyosifiwa katika mvinyo wenye kufungwa. Neno "Na katika hayo" ni kusisitiza kuvutia kwa kuihusisha hukumu baada ya kuieneza. Maana yake: Nawashindane wenye kushindana katika neema ya pepo na katika mvinyo wenye kufunikwa ni watu mahsusi ambao watakunywa.

Aya Ya 27

Tasnim kutokana na inavyofasiriwa na aya inayofuatia ni mto katika pepo ambao Mwenyezi Mungu ameuita Tasnim. Temko Tasnim lina maana ya kunyanyua na kujaza.

Aya Ya 28

Aya hii inafahamisha kuwa wenye kukurubishwa watakunywa Tasnim bila ya kuchanganywa. Hayo yanafahamisha haya yafuatayo:

Kwanza : Kwamba Tasnim ni bora kuliko mvinyo wenye kufungwa ambao unazidi tamu kwa kuchanganywa na Tasnim.

Pili : Kwamba wenye kukurubishwa wana daraja ya juu zaidi kuliko wema waliotajwa katika aya (mbali mbali).

Aya Ya 29

Mpangilio unaeleza kuwa makusudio ya wale ambao wameamini ni wale watu wema wenye kusifiwa katika aya, wametajwa wale ambao wameamini kwa sababu imani yao ndiyo sababu ya kuchekwa na kudharauliwa na makafiri na wametajwa makafiri kwa sifa ya wale ambao wamefanya makosa, kwa kuwa huko kuwacheka wale walioamini ni katika makosa.

Aya Ya 30

Yaani wanakonyeza kwa kuonyesha dharau.

Aya Ya 31

Neno Fakihu lina maana ya furaha iliyozidi kiasi yaani baada ya kuwacheka wenye kuamini wanarudi hali ya kuona raha na kufurahi kwa waliyoyafanya. Au linatokana na Fakaha lenye maana ya mazungumzo ya kupumbaza, kwa maana ya kuwa wakirudi kwa jamaa zao wanazungumzia waliyoyafanya hali ya kupumbazika.

Aya Ya 32

Wanawaona wamepotea kwa njia ya kuona au kuwahukumia tu! Kuwa wamepotea.

Aya Ya 33

Yaani hawakupeleka hao makafiri kuwa wawachunge waumini, na kuwahukumia katika haki yao kwa wanavyotaka wao. Aya hii ni kuwaumbua wenye kuwafedhehesha waumini.

Aya Ya 34

Makusudio ya keo, ni siku ya malipo. Na wale ambao wamefanya makosa kuwaita makafiri ni kurudia hakika ya sifa yao.

Aya Ya 35-36

Neno thawabu kwa asili lina maana ya malipo ijapokuwa linatumiwa zaidi katika kheri. Kwa ujumla maana ya aya ni wake ambao wameamini watakuwa katika vyandarua wakiangalia malipo ya makafiri malipo ya matendo yao waliyokuwa wakiwafanyia katika dunia kama kuwacheka kukonyezana wanapowapitia na kurudi kwa jamaa zao hali yakufurahi baada ya kuyafanya hayo na kusema kwao "Hakika hawa ni wenye kupotea".

Utafiti Wa Hadith Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu kusema kwake Mwenyezi Mungu "Na katika hayo na washindane wenye kushindana" amesema: Ni katika tuliyoyataja miongoni mwa thawabu anazozitafuta Muumin. Katika Majmau kuhusu kusema kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) "Na walipokuwa wakiwapitia wakikonyezana." Imesemwa imeshuka kwa Ali bin Abutwalib(a.s) na kundi la waislamu waliokuwa wakielekea kwa Mtume(s.a.w.w) wakadharauliwa na wanafiki, wakawacheka, na wakakonyezana; kisha wakarudi kwa watu wao wakaambia tumemwona kipara tukamcheka; Ndio ikashuka aya hiyo kabla ya kufika Ali(a.s) na wenzake kwa Mtume(s.a.w.w) . Hadithi hiyo imepokewa kutoka kwa Muqatil na Kalbi.

Imepokewa hadithi hiyo katika Kash shaf. Katika hiyo hiyo Kash shaf ametaja Al-Hakim Abul-Qassim Al-Hasakani katika kitabu Shawahidu tanzil kutoka kwa Abu Swaleh naye kutoka kwa Ibn Abbas amesema: "Hakika wale ambao wamefanya makosa ni wanafiki wa Kiquraish na wale 'ambao wameamini' ni Ali bin Abu-Twalib na wenzake."


7

8

9

10

11

12

13

14

15

16