12
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
SURA A'ALAA (MTUKUFU) (NA. 87)
INA AYA 19
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.
سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى ﴿١﴾
1. Litakase jina la Mola wako aliye Mtukufu.
الَّذِي خَلَقَ فَسَوَّىٰ ﴿٢﴾
2. Ambaye ameumba (kila kitu) akakiweka sawa.
وَالَّذِي قَدَّرَ فَهَدَىٰ ﴿٣﴾
3. Na ambaye amekadiria (kila kitu) na akakiongoza.
وَالَّذِي أَخْرَجَ الْمَرْعَىٰ ﴿٤﴾
4. Na ambaye ameotesha malisho.
فَجَعَلَهُ غُثَاءً أَحْوَىٰ ﴿٥﴾
5. Kisha akayafanya makavu yenye kupiga weusi.
سَنُقْرِئُكَ فَلَا تَنسَىٰ ﴿٦﴾
6. Tutakusomesha wala hutasahau.
إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ إِنَّهُ يَعْلَمُ الْجَهْرَ وَمَا يَخْفَىٰ ﴿٧﴾
7. Ila anachopenda Allah. Hakika yeye anayajua yaliyowazi na yaliyofichika.
وَنُيَسِّرُكَ لِلْيُسْرَىٰ ﴿٨﴾
8. Tutakusahilishia njia nyepesi.
فَذَكِّرْ إِن نَّفَعَتِ الذِّكْرَىٰ ﴿٩﴾
9. Basi waidhisha ikiwa utafaa waadhi.
سَيَذَّكَّرُ مَن يَخْشَىٰ ﴿١٠﴾
10. Atawaidhika nao mcha (Mungu).
وَيَتَجَنَّبُهَا الْأَشْقَى ﴿١١﴾
11. Na atajiepusha nao asiyemcha.
الَّذِي يَصْلَى النَّارَ الْكُبْرَىٰ ﴿١٢﴾
12. Ambaye atauingia moto mkubwa..
ثُمَّ لَا يَمُوتُ فِيهَا وَلَا يَحْيَىٰ ﴿١٣﴾
13. Kisha humo hatakufa wala hatokuwa hai.
قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّىٰ ﴿١٤﴾
14. Hakika amekwishafaulu mwenye kujitakasa.
وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّىٰ ﴿١٥﴾
15. Akakumbuka jina la Mola wake na akaswali.
بَلْ تُؤْثِرُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿١٦﴾
16. Lakini nyinyi mnapenda zaidi maisha ya ulimwengu.
وَالْآخِرَةُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿١٧﴾
17. Hali akhera ni bora na yenye kubaki.
إِنَّ هَـٰذَا لَفِي الصُّحُفِ الْأُولَىٰ ﴿١٨﴾
18. Hakika hAya Na mo katika vitabu vya kwanza.
صُحُفِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ ﴿١٩﴾
19. Vitabu vya Ibrahim na Musa.
UBAINIFU
Ni amri ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu juu ya yale yanayoelekeana na upande wake Mtukufu na kuitakasa dhati yake tukufu na kutaja pamoja na jina lake Mtu mwengine au kutegemeza kwa mwengine yale yanayopasa kutegemezwa kwake, kama kuumba kuangalia vizuri mambo na kuruzuku. Na nikiaga chake kwa Mtume kwa kumpa nguvu kwa elmu, hifadhi na kummakinisha katika njia ambayo ni nyepesi kwa tabligh na inayonasibiana zaidi na mlingano. Mpangilio wa aya katika mwanzo wa Sura ni mpangilio wa ki Makka. Ama mwisho wake yaani kuanzia Aya Na 14 mpaka mwisho wa Sura, imepokewa katika njia ya Maimamu wa Ahlul Bait vile vile katika njia ya Ahli Sunnah kwamba, makusudio yake ni zaka ya fitr, na swala ya Idd, na ni maalum kuwa saumu na yanayofuatia saumu miongoni mwa zaka ya fitr na swala ya Idd ilianzishwa Madina baada ya Hijra. Hivyo zitakuwa aya za mwisho zimeshuka Madina. Katika hiyo Sura mwanzo wake ni Makka na mwisho wake ni Madina, wala hayo hayakanushi yale yaliyokuja kuwa Sura imeshuka Makka, kwani ilivyo nikuwa haikataliki kuchukulia hivyo mwanzo wa Sura.
Aya Na 1
Ni amri ya kulitakasa jina lake Mwenyezi Mungu S.W.T. na kulitukuza. Na kwa vile hapa kutakaswa Mwenyezi Mungu kumefungamanishwa na jina yake, basi huko kumtakasha kunamaanisha asitajwe yeyote ambaye yeye Mwenyezi Mungu ametakata naye. Kwa sababu jina linatokea katika kusema. Hivyo isitajwe pamoja na jina lake miungu wengine washirikina, waombozi na kuwanasibishia uungu. Na vile vile kama kutaja baadhi ya yanayohusika naye Mwenyezi Mungu (s.w.t) kama kuumba kupatisha, kuruzuku, kuhuisha na kufisha na mfano wake kwa kuyanasibisha kwa asiyekuwa yeye Mwenyezi Mungu Au kama kutaja baadhi ya yasiyofanana na upande wa utakatifu wake, katika vitendo kama kushindwa, ujinga, dhuluma, mghafala na mfano wake katika sifa za upungufu na aibu kwa kuyanasibisha kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t).
Kwa ujumla kulitakasa jina lake ni kuepuka kauli na kutaja yasiyonasibiana kuyataja kwake na jina lake Mwenyezi Mungu (s.w.t), na huko ni kumtakasa katika kiwango cha kauli kwenye kuafikiana na kumtakasa kwake katika kiwango cha kitendo. Hiyo inalazimisha Tawhid (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) iliyo kamili kwa kukanusha kumshirikisha Mwenyezi Mungu kuliko waziwazi; kama ilivyo katika kusema kwake Mwenyezi Mungu:
"Na anapotajwa Allah peke yake nyoyo za wale wasioamini akhera, huchukiwa na wanapotajwa wale walio kinyume naye, mara wanafurahi
". (39:45).
Na pia kusema kwake: "Na unapomtaja Mola wako katika Qu'ran peke yake, basi wao hugeuza migongo yao kwa kuchukia
." (17:46).
Kutegemeza jina Mola kwa dhamiri ya mwenye kusemeshwa (jina la Mola wako) ni kutilia nguvu yale tuliyotangulia kuyataja, kwani maana ni litakase jina la Mola wako ambaye umemfanya ni Mola na wewe unalingania kuwa yeye ni Mola wa waungu, basi isitokee katika maneno yako pamoja na kutaja jina lake kwa uungu wake na kutaja mwengine, kwa kiasi ambacho kitakanusha kumwita Mungu kama alivyojijulisha kwako.
Kusemwa kwake: Mtukufu ni ambaye yuko juu ya aliye juu na kushinda kila kitu, hiyo ni sifa ya Mola wako yaani litakase jina lake kwa sababu yeye ni Mtukufu zaidi. Imesemwa kuwa maana ya aya hii ni kusema "Subhana rabial aala" hayo ni kutoka kwa Ibn Abbas, pia amesema, ni kuswali. Imesemwa makusudio ni jina vile, anavyoitwa yaani mtakase Mwenyezi Mungu S.W.T. na kila sifa na vitendo visivyofanana naye. Imesemwa kuwa makusudio ni kuyatakasa majina yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) na yale yasiyofanana naye wala haitwi asiyekuwa yeye na jina linalomhusu yeye Mwenyezi Mungu, wala halitamkwi katika mahali pasipo nasibiana naye kama chooni n.k. Yale tuliyotanguliza kuyataja katika maana ndiyo mapana zaidi na yenye kukusanya zaidi maana na ndiyo yanayonasibiana zaidi na aya inayosema "tutakusomesha wala hutasahau" na "tutakusahilishia njia nyepesi". Kwa sababu mpangilio ni wa kupewa utume mpaka kwenye ukumbusho na tabligh. Hivyo ikaanzwa kwa maneno yake Mtume(s.a.w.w)
ya kumtakasa na kila linalo tambulisha shirika kwa uwazi au kwa undani. Akamwahidi mara ya pili kumsomesha kiasi ambacho hataweza kusahau chochote katika yale aliyopewa Wahyi na kusahilishiwa njia ya Tabligh.
Aya Na 2
Kuumba kitu ni kukusanya mafungu yake na kuyapanga sawasawa kiasi ambacho huwekwa kila kitu mahali pake panapo nasibiana napo na kukipa haki yake, kama kuweka kila kiungo katika viungo vya binadamu mahali panapo nasibu. Ayah ii mpaka mwisho wa Aya Na nne zinasifu mipangilio mizuri, ya Mungu na hayo ni dalili ya uungu wake Mwenyezi Mungu (s.w.t)
Aya Na 3
Yaani ni kuvifanya vitu alivyoviuumba juu ya kiasi mahususi na mipaka yenye kuonyesha dhati zake na sifa zake na vitendo vyake visivyozidi kipimo chake na akaviandaa na yale yanayonasibiana na yaliyokadiriwa. Kwa hiyo kila mmoja anafuata upande wa yale yaliyokadiriwa kwake, kwa uongozi wa Mungu, kama mtoto kuendea titi la mama yake, kifaranga kutegemea riziki ya mama yake, mwanamume kwa mwanamke na mifano ya hayo. Mwenyezi Mungu anasema:"Na hakuna kitu chcochote ila hazina yake iko kwetu wala hatukukiteremsha ila kwa kipimo maalum
." (15:21).
Amesema tena: "Kisha akamfanyis nyepesi njia
" (80:20). Amesema tena: "Kila mmoja ana mwelekeo wake wa kuelekea
." (2:148).
Aya Na 4 -5
Kutoa malisho kwa ajili ya chakula kisha kuyafanya makavu meusi ni katika usadikisho wa mipangilio ya Mungu na dalili zake; kama ilivyo katika kuumba, kulinganisha sawa, kukadiri na uongozi.
Aya Na 6-7
Amesema katika Mufradati: "Kusoma ni kukusanya herufi na matamko pamoja katika kusoma, lakini sio mkusanyiko wowote ni kusoma, huwezi kusema umewasoma watu, kama ukiwakusanya." Hiyo inafahamisha kuwa hakuwezi kuitwa kusoma kwa herufi moja. Katika Majmau anasema kusomesha ni kuchukua kisomo kwa msomaji kwa kumsikiliza ili usahihishe makosa.
Kumsomesha kwake Mtume, sio kama vile tunavyosemeshana sisi kwa kumsikiliza msomaji kisha kumsahihisha anayoyakosa. Haikuwa kwa Mtume kusoma chochote katika Qur'an akakikosea au asahau wahyi kisha asome ndipo arekebishwe la, bali makusudio yake ni kumwezesha Mtume (SAWW) kuisoma Qur'an kama ilivyoteremsha bila ya kuibadilisha, kwa kuzidisha kitu au kupunguza au kuifanya kombo kwa sababu ya kusahau. Kwa hivyo kauli yake Mwenyezi Mungu tutakusomesha hutasahau ni kiaga kitokacho kwake Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kumuwezesha kuijua Qur'an na kuifikisha kama ilivyoteremshwa, kiasi ambacho hataisahau. Huo ni msingi wa kufikisha wahyi (ufunuo) kama iluvyofunuliwa. Kusema kwake "Ila anachopenda Allah, ni kuvua kunakofahamisha uwezo wa Mungu ulio huru na kwamba kipawa hiki cha kutosahau sio kuwa Mungu amelazimika macho. Yeye anao uwezo wa kukusahaulisha kama akitaka.
Ayah ii kwa mpangilio wake, haiepukani kuwa inatilia nguvu yale yaliosemwa kwamba Mitume(s.a.w.w)
alipokuwa akiletewa wahyi (ufunuo) na Jibril humsomea kwa kuogopa kusahau, ikawa Jibril akimaliza tu naye huanza. Basi iliposhuka ayah ii hakusahau kitu baadaye. Inakurubia kuzingatia kuwa ayah ii tutakusomesha hutosahau ilishuka kwanza ndipo ikashuka aya inayosema: "Usiutikise ulimi wako kwa (kuufanyia haraka) wahyi kwa hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha. Wakati tunapokusomea, basi fuata kusomwa kwake, kisha ni juu yetu kuubainisha
". (75:17-19).
Kisha aya inayosema: Usiifanyie haraka (hii) Qur'an kabla haujamalizika wahyi (ufunuo) wake, Na (uombe) useme. Mola wangu nizidishie elimu" (20:114).
Kusema kwake "Hakika anajua yaliyowazi na yaliofichika" kuwa wazi ni kwa kuona au kusikia kama Qur'an inavyosema: "Wakasema tuonyeshe Mungu waziwazi
". (4:153).
"Hakika yeye anajua kauli iliyo dhahiri
". (21:110) Jumla ya aya iko katika mahali pa sababu kwa maana tutakufanyia uzuri katika kupokea wahyi (ufunuo) na kuuhifadhi kwa sababu sisi tunajua dhahiri na ndani ya hali yako na vile unavyojihimu katika jambo la wahyi na unavyopupia twaa katika yale uliyoamrishwa.
Aya Na 8
Wepesi ni sifa yenye kusimama mahali pa msifiwa yaani njia nyepesi, kwa maana ya kuwa daima tutakufanyia njia ya tabligh ni nyepesi kwa maneno na vitendo utaongoza watu na itatimia hoja kwa wengine na utafanya subira juu ya maudhi yao.
Aya Na 9
Ni mtiririko wa amri iliyotangulia ya kulitakasa jina la Mola wake kuahidiwa kwake kusomeshwa wahyi kiasi ambacho hatasahau, na kusahilishiwa njia nyepesi, hizo ni sharti za kidharura ambazo zinaweza kuzuwia kufaulu mlinganio wa kidini. Maana ni kuwa ukitimiza amri ya kufuata yale tuliyokuamrisha, kukusomesha hutosahau na kukusahilishia njia ya wepesi, basi waidhisha ikiwa utafaa (huo) waadhi.
Imeshartiwa kuwa waadhi uwe wenye kunufaisha. Na hilo ni sharti juu ya uhakika wake. Kwani ikiwa waadhi hautanufaisha basi itakuwa ni upuuzi, naye Mwenyezi Mungu ametakata na kuamrisha upuuzi. Kwa hiyo kumwadhia mwenye kumcha Mwenyezi Mungu kwanza kunafahamisha kupondokea haki na hayo ndio manufaa yake (huo waadhi), vile vile kuwaidhika kama alivyosema: "Atawaidhika anayemcha (Mungu). Na kumwaidhia muovu ambaye haogopi katika moyo wake, kwanza kunafahamisha kutimia hoja juu yake na ndio manufaa yake (huo waadhi) na kunalazimisha kuejiepusha kwake, na kuikataa kwake haki kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na atajiepusha nayo muovu". Waadhi baada wa waadhi haunufaishi na chochote kwa hiyo kukaamriwa kuachana naye. Mwenyezi Mungu amesema: "Basi jiepushe na wale wanaoupa mgongo ukumbusho wetu huu na wala hawataki ila maisha ya dunia
." (53:29)
Imesemekana kuwa sharti ni sharti la kisura tu! Sio la kihakika, kwamba ni kutolea habari kuwa waadhi ni wenye kunufaisha katika kuzidisha twaa na kukoma na maasi, kama inavyosemwa: Muulize inafaa kumuuliza, kwa hiyo ndio baadhi yao wakasema: "Herufi In katika aya ni kwa maana ya (Qad) hakika". Na imesemwa kuwa maneno ni ya mkato kwa kuondoa maneno mengine, kukadiria kwake ni "Basi waidhisha ikiwa utafaa waadhi na hata ukitofaa". Hilo ni kwamba yeye Mtume(s.a.w.w)
amepelekwa kwa waadhi na kuonya. Kwa hiyo ni juu yake kuonya na kutoa waadhi uwe una manufaa au usiwe na manufaa; Kwa hiyo aya inaelekeana na aya inayosema: "Na amewafanyia kanzu zinazowakinga na joto (na baridi)
". (16:81).
Imesemwa kuna ishara ya kuweka mbali manufaa ya hawa wenye kutajwa; Ni kama vile imesemwa: Fanya unayoamrishwa hata kama hayatanufaisha.
Aya Na 10
Yaani atawaidhika na Qur'an yule ambaye moyoni mwake mna kitu cha kumwogopa Mwenyezi Mungu na kuogopa mateso yake.
Aya Na 11
Dhamiri ni ya mawaidha. Makusudio ya neno Ashqa kwa kulinganisha na aya iliyotangulia, ni yule asiyemwogopa Mwenyezi Mungu.
Aya Na 12
Mto mkubwa ni moto wa Jahanam, ni mkubwa kulinganisha na wa dunia. Imesemwa makusudio yake ni daraja ya chini ya Jahanam ambayo ina adhabu kali zaidi.
Aya Na 13
Makusudio ya kutokufa wala kuwa hai, ni kutookoka kabisa kwa maana ya kuwa adhabu haitakwisha wala maisha hayatabadilika kuwa mazuri. Kwa hiyo makusudio ya uhai ni maisha mema; kama alivyosema katika Ardhi; "Si hai wakutarajiwa wala si maiti wakusahauliwa".
Aya Na 14 -15
Makusudio ya kujitakasa hapa, ni kujitakasa na uchafu wenye kufungamana na dunia kwa dalili ya kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Lakini nyinyi mnapendelea zaidi uhai wa kilimwengu." Kurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa kumuelekea yeye Mwenyezi Mungu ni kujitakasa. Kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni kujitakasa na uchafu unaofungamna na mali. Hata udhu wa swala ni mfano wa kujitakasa na yale yaliyochumwa na nyuso, mikono na miguu. Kusema kwake: Akalikumbuka jina la Mola wake akaswali, makusudio yake kwa dhahiri ni kumtaja Mwenyezi Mungu kwa kutamka, na kuswali ni swala ya kawaida ya Kiislamu. Aya mbili hizi kwa dhahiri ufahamisho wake ni kuenea a kila kitu, lakini imepokewa kutoka kwa Maimamu wa Ahlul Bait
kuwa aya hizo zinahusu zaka ya fitri na swala ya Idd. Vile vile hayo yamepokewa katika Ahli Sunnah.
Aya Na 16
Msemo huo unaelekezwa kwa watu juu ya tabia yao ya kiutu inayopelekea kufungamana kabisa na dunia na kujishughulisha na kuiamirisha. Imesemwa kuwa msemo unawaelekea makafiri tu. Kwa hali yoyote maneno ni yenye kuelekezwa kwenye lawama.
Aya Na 17
Imehisabiwa akhera ni yenye kubakia kulinganisha na dunia, pamoja na kuwa yenyewe akhera ni yenye kubaki milele, kwa sababu ya kupima kati ya dunia na akhera.
Aya Na 18-19
Neno haya "Linaonyesha yale yaliyobainishwa kuanzia aya 14 mpaka 17. Imesemwa kuwa ni hAya Na kuwa akhera ni bora na ni yenye kubaki. Imesemwa kuwa kusema vitabu vya kwanza tu. Kisha kuvibainisha kuwa ni vitabu vya Ibrahim na Musa ni kwa ajili ya kutukuza na kukuza jambo.
Utafiti Wa Hadith Katika Tafsiri ya Iyashi kutoka kwa Uqba bin Amir El-Jahaniy amesema iliposhuka aya inayosema: "Litakase jina la Mola wako aliye mkuu" Mtume(s.a.w.w)
alisema ifanyeni katika kurukui kwenu. Na iliposhuka "Litakase jina la Mola wako aliye Mtukufu akasema": Ifanyeni katika kusujudi kwenu. Hadith hiyo pia imepokewa katika Durril Manthur kutoka kwa Ahmad, Abu Dawud, Ibn Maja Ibn El-Mundhir na Ibn Murdawayh nao wamepokea kutoka ka Uqba naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
.
Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu Aya Na kwanza amesema: "utakata ni kwa Mola wangu aliye Mtukufu". Kuhusu na ambaye ameumba akakamilisha na ambaye makadirio ya mwanzo kisha akaviongoza.
Katika Durril Manthur ametoa Ibn Murdawayh kutoka kwa Ibn Abbas amesema: "Mtume(s.a.w.w)
alikuwa anajikumbusha Qur'an kwa kuhofia kusahau akaambiwa tumekutoshea na hilo", na ikashuka aya Tutakusomesha wala hutasahau. Katika Faqih aliulizwa Imam As Sadiq
kuhusu kusema kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) "Hakika amefaulu mwenye kuitakasa
" Akasema: "Ni mwenye kutoa zaka ya fitr". Akaulizwa: na akamkumbuka Mola wake, akaswali? Akasema ni aliyetoa uwanjani akaswali. Amepokea hadith kwa maana hii Hammad, naye kutoka kwa Jarir naye kutoka kwa Abu Baswir na Zurarah kutoka kwake Imam Jaffar As Sadiq
. Katika Durril Manthur ametoa Ibn Murdawayh kutoka kwa Abu Said Al-Khudri amesema: Mtume(s.a.w.w)
alikuwa akisema: "Hakika amefaulu mwenye kujitakasa na akamkumbuka Mola wake akaswali
" Kisha hugawanya zaka ya fitr kabla ya kwenda kwenye mswala siku ya Idd-ul-fitr.
Vile vile kumepokewa kushuka aya mbili hizo katika zaka ya fitri na swala ya Idd kwa njia mbili kutoka kwa Abu Said, vile vile kwa njia mbili kutoka kwa Ibn Umar kwa njia moja kutoka kwa Naila bin Al-Asqa, kwa njia mbili kutoka kwa Abu Aliya na kwa njia moja kutoka kwa Atau. Vile vile kwa njia moja kutoka kwa Muhammad bin Sirin, kwa njia moja kutoka kwa Ibrahim Annakhyi na kutoka kwa Amru bin Awf naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
.
Katika Khiswali imepokewa kutoka kwa Utbah bin Amru Allaythi naye kutoka kwa Abu Dharr katika hadith inayosema: "Nilimuuliza Mtume(s.a.w.w)
ni kitu gani katika dunia alichokuteremshia Mwenyezi Mungu kilichokuwa katika vitabu vya Ibrahim na Musa? Akasema, Ewe Abu Dharr, soma: hakika amefaulu mwenye kujitakasa akalikumbuka jina la Mola wake akaswali. Lakini nyinyi mnapendelea zaidi uhai wa kilimwengu. Hali akhera ni bora na yenye kubaki. Hakika hayo yamo katika vitabu vya kwanza vitabu vya Ibrahim na Musa. Hadithi inatilia nguvu kuwa ishara na neno "haya" ni mkusanyiko wa aya nne kama ilivyotangulia. Katika Baswir kwa isnadi yake kutoka kwa Abu Baswir amesema Abu Abdillah: Tunazo suhuf alizozitaja Mwenyezi Mungu katika Aya Na 19: Nikamwambia ni mbao? Akasema ndio. Amepokea vile vile kwa njia nyengine Abu Baswir kutoka kwake Abu Abdillah
. Kwa dhahiri ni kwamba makusudio ya kuwa Suhuf ni mbao nikuwa ni Taurat yenye kuelezewa katika Qur'an kama mbao; kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t): "Na ukamwandikia katika mbao kila kitu
." (7:145).
Na pia kusema kwake Mwenyezi Mungu:'na akazitupa mbao
.." (7:150). Na kusema kwake "aliziokota zile mbao
" (7:154).
Katika Majmau imepokewa kwa Abu Dharr, yeye amesema: "Nilimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu ni Mitume wangapi? Akasema: Ni laki moja na ishirini na nne elfu (124,000) nikamuuliza ni wangapi walio Mursaal katika wao? Akasema mia tatu na kumi na tatu (313). Nikasema Adam alikuwa Mtume. Akasema ndio Mwenyezi Mungu alimsemesha na amemuumba kwa mkono wake. Ewe Abu Dharr, Mitume waarabu ni Hud, Saleh, Shuayb na Mtume wako.
Nikasema tena: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu ameteremsha vitabu vingapi? Akasema mia moja na nne (104). Kwa Adam mbao kumi, kwa Shiyth hamsini kwa Ukhnun ambaye ni Idris thelathini naye ndiye wa kwanza kuandika kwa kalamu, Ibrahim kumi na Taurat, Injil, Zabur na Qur'an. Yamepokewa hayo katika Durril Manthur kutoka kwa Abd bin Hamid, Ibn Murdawayh na Ibn Asakir nao kutoka kwa Abu Dharr isipokuwa hazikutajwa mbao za Adam na zimetajwa mbao kumi za Musa kabla ya Taurat.