1
DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU
RISALA YA DINI ZA UWONGO
Yapo madhehebu, vikundi, dini, falsafa, na harakati nyingi sana katika hii dunia, zote hizo zikidai kuwa ni njia sahihi na ya sawa au njia ya pekee ya kweli ya Mwenyezi Mungu. Vipi mtu anaweza kutambua ile njia iliyo sawa au ama, kwa hakika, zito ziko sawa?
Njia moja ambayo jibu linaweza patikana ni kuondoa zile tofauti za juujuu katika mafunzo ya wenye kudai kadhaa kwa ukweli wa mwisho na wa msingi, na kutambua malengo ya msingi 'Ibadah wanayo walingania, moja kwa moja au kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja.
Dini zote za uwongo zina fikra moja ya msingi iliyo sawa kwa zote, kuhusiana na Mwenyezi Mungu: ama wanadai kuwa watu wote ni miungu (wenye kuabudiwa), au watu fulani mahsusi walikuwa mungu, au maumbile ni mungu, au kuwa Mwenyezi Mungu ni kitu kilichobuniwa na mwanadamu.
Hivyo, inaweza kusemwa kuwa risala (ujumbe) wa msingi kwa Dini za uwongo ni kuwa Mwenyezi Mungu Anaweza kuabudiwa katika mfumo wa viumbe Vyake. Dini za uwongo zinamuita mwanadamu kuabudu viumbe vya Allah wa kuita viumbe hivyo au sehemu yake kuwa ni mungu. kwa mfano, Nabii Yesu aliwaita wafuasi wake kumuabudu Mwenyezi Mungu, lakini wale wanaodai kuwa wao ni wafuasi wa Yesu leo wanawalingania watu wengine wamuabudu Yesu, wakidai kuwa Yesu alikuwa mungu.
Buddha alikuwa ni mwana-mageuzi aliyeanzisha idadi kubwa ya kanuni za kibinadamu na utu katika dini za India. Hakudai kuwa yeye ni Mwenyezi Mungu wala hakutoa rai kwa wafuasi wake kuwa yeye mwenyewe ni kitu au kiume cha kuabudiwa.
Ilhali kuwa leo Mabuddha wengi wanaoishi nje ya India wamemfanya yeye kuwa mungu na wanasujudia masanamu yaliyotengenezwa, kwa muono wao kwa sura yake. Kwa kutumia msingi na kanuni ya kutambua kitu cha kuabudiwa, tunaweza kwa urahisi na wepesi kuzijua dini za uwongo na kuvumbua maumbile ya asili yake, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani:
مَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِهِ إِلَّا أَسْمَاءً سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّـهِ أَمَرَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٤٠﴾
"Hamuabudu badala yake ila majina tu mliyoyapanga nyinyi na baba zenu. Allah Hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote. Hapana hukumu ila ya Allah tu. Yeye Ameamrisha msimuabudu yeyote isipokuwa Yeye tu. Hiyo ndiyo Dini iliyonyooka. Lakini watu wengi hawajui" (12: 40).
Inaweza kutolewa hoja kuwa dini zote zinafunza mambo mazuri, hivyo kwa nini tujali ni dini gani tunayofuata?
Jibu ni kuwa dini zote za uwongo zinafunza uovu mkubwa sana: kuabudu uumbaji na viumbe.
'Ibadah ya kuhuluku na viumbe ni dhambi kubwa ambalo mwanadamu anaweza kufanya kwa sababu inakwenda kinyume na lengo la uumbaji. Mwanadamu aliumbwa kumuabudu Mwenyezi Mungu peke Yake kama alivyosema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa uwazi kabisa katika Qur'ani:
"Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi"
(51: 56).
Kwa hiyo, kuabudu uumbaji, ambayo ni kiini cha ushirikina ni dhambi la pekee ambalo halisamehewi. Yeyote mwenye kufariki katika hali hiyo ya ushirikina, ameiziba Qadari yake katika maisha ya baadaye (Akhera). Hii si rai, lakini ni Wahyi wa uhakika kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika ufunuo Wake wa mwisho kwa mwanadamu:
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ﴿٤٨﴾
"Hakika Allah Hasamehe kushirikishwa, na Husamehe yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye" (4: 48 na 116).
KILIMWENGU CHA DINI YA MWENYEZI MUNGU
Kwa vile matokeo ya kufuata dini ya uwongo ni makubwa, Dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu ni lazima iwe ni yenye kueleweka kilimwengu na yenye kuweza kufikia kilimwengu hapo awali.
Na ni lazima iendelee daima dawamu kufahamika na kufikiwa katika ulimwengu mzima. Kwa ibara nyengine, dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu haiwezi kuzuiliwa kwa kaumu moja, pahala, au zama fulani. Wala haingii katika mantiki kuwa Dini kama hiyo itaweka masharti ambayo hayana mahusiano yoyote kabisa baina ya mwanadamu na Mwenyezi Mungu, kama ubatizo, au itikadi ya kuwa mwanadamu ni mwokozi, au kipito na wasta ya kuwafikisha.
Ndani ya msingi wa kati wa Uislamu na maana yake (kujisalimisha kwa hiari katika kutekeleza amri za Mwenyezi Mungu) imelala mizizi ya kilimwengu cha Uislamu. Pindi mwanadamu anapofahamu kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja na ni tofauti kabisa na uumbaji Wake, na akanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu, anakuwa Muislamu wa kweli katika mwili na roho na hivyo kustahiki kuingia Peponi.
Kwa hiyo, yeyote kwa wakati wowote anaweza kuwa Muislamu hata akiwa katika maeneo za ndani na mbali katika ulimwengu, mfuasi wa Dini ya Mwenyezi Mungu, Uislamu, kwake yeye tu kukataa kuabudu uumbaji na viumbe na kurudi kwa Mwenyezi Mungu peke Yake. Hata hivyo, inatakiwa ifahamike kuwa ili kunyenyekea na kutii amri za Mwenyezi Mungu, mtu anatakiwa daima na milele awe ni mwenye kuchagua baina ya haki na batili, ukweli na uwongo. Hakika, mwanadamu amepatiwa kipawa, nguvu, uwezo na akili na Mwenyezi Mungu ya kuweza kutofautisha ukweli kutokana na uwongo, lakini pia kuchagua baina yao.
Uwezo huu uliopatiwa na Mwenyezi Mungu inabeba pamoja nayo jukumu muhimu sana, kwamba mwanadamu ataulizwa na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa uchaguzi anaofanya. Kwa hivyo, inafuata kuwa mwanadamu anafaa kujaribu uwezo wa upeo wake kufanya mema na kuepukana na mabaya. Fikra hizi zimeelezwa katika Wahyi wa mwisho kama ifuatavyo:
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَادُوا وَالنَّصَارَىٰ وَالصَّابِئِينَ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَعَمِلَ صَالِحًا فَلَهُمْ أَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿٦٢﴾
"Hakika Walioamini, na Mayahudi na Wakristo, na Wasabai; yeyote atakaye muamini Allah na Siku ya Mwisho na akatenda mema basi watapata malipwa yao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika" (2: 62).
Ikiwa, kwa sababu yoyote ile, wanshindwa kukubali ujumbe wa mwisho baada ya kuwa imeelezwa kwao kinaganaga, basi watakuwa katika hatari kubwa mno. Mtume wa mwisho (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam) amesema:
"Yeyote miongoni mwa Wakristo na Mayahudi atasikia kuhusu mimi, lakini bila ya kuyakinisha Imani yake kwa yale niliyoyaleta na akafa katika hali hiyo, atakuwa miongoni mwa wakaazi wa Moto"
(Sahih Muslim [Tafsiri ya Kiingereza], Mj. 1, uk. 91, Nambari 284).
KUMTAMBUA MWENYEZI MUNGU
Swali linaloibuka hapa ni: Vipi watu wote watatizamiwa kuamini Mwenyezi Mungu mmoja wa kweli, ukitazama usuli zao tofauti, jamii zao na tamaduni? Kwa watu kusualiwa na kubeba majukumu yao kwa kuabudu Mwenyezi Muja wa kweli, wanahitajiwa wawe na fursa na njia ya kuifikia elimu ya kumfahamu na kumjua Yeye.
Wahyi ya mwisho inafundisha kuwa wanaadamu wote wala utambuzi wa Mwenyezi Mungu mmoja wa kweli iliyochapwa katika roho zao kama sehemu ya maumbile yao waliyoumbwa nayo.
Katika Surah ya saba ya Qur'ani, Mwenyezi Mungu Ameeleza kuwa pindi Alipomuumba Adam Alivifanya vizazi vyote vya Adam kuwepo (katika uhai) na Akachukua ahadi kutoka kwao kwa kusema:
أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ قَالُوا بَلَىٰ شَهِدْنَا ﴿١٧٢﴾
"Je, Mimi si Mola Mlezi wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia".(Al-A'raaf, Ayah 172).
Kisha Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anaeleza ni kwa nini Aliwaleta wanaadamu wote washuhudie kuwa Yeye ndiye Muumba na Mwenyezi Mungu, mmoja wa kweli anayestahiki kuabudiwa. Anasema Aliyetukuka:
"Msije mkasema Siku ya Kiyama sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo"
(7: 172).
Hiyo ni kusema, hatuwezi kudai siku hiyo kuwa hatukuwa ni wenye kumjua Allah (Subhaanahu wa Ta'ala), kuwa ndiye Mwenyezi Mungu wetu na kuwa hakuna aliyetuambia kwamba tunafaa sisi kumuabudu Allah peke Yake. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anaendelea kutueleza kuwa:
أَوْ تَقُولُوا إِنَّمَا أَشْرَكَ آبَاؤُنَا مِن قَبْلُ وَكُنَّا ذُرِّيَّةً مِّن بَعْدِهِمْ أَفَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ الْمُبْطِلُونَ ﴿١٧٣﴾
"Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walio shirikisha kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao. Basi utatuangamiza kwa sababu ya waliyo yafanya wapotovu?" (7: 173).
Hivyo, kila mtoto anazaliwa katika maumbile ya kuwa na Imani ya Mwenyezi Mungu na mwelekeo wa asili na silika kumuabudu Yeye peke Yake. itikadi ya kiasili na mwelekeo unaitwa katika lugha ya Kiarabu, "Fitrah". Mtume Muhammad (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam) amenukuliwa akisema kuwa Allah Aliyetukuka amesema:
"Nimewaumba waja Wangu katika Dini ya sawa (na sahihi), lakini Shetani ndiye aliyewafanya kupotea".
Pia amesema Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam):"Kila mtoto anazaliwa katika Fitrah. Baadaye ni wazazi wake ndio wanaomfanya ama awe Myahudi, au Mkristo au Mmajusi"
(Al-Bukhaariy).
Ikiwa mtoto ataachwa peke yake, atamuabudu Mwenyezi Mungu kwa njia yake mwenyewe, lakini watoto wote wanaathiriwa na mazingira. Hivyo, kama vile mtoto ananyenyekea kwa kanuni za kimaumbile ambazo Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amezilazimsha kwa ulimwengu na viumbe vyote, kwa njia hiyo hiyo roho yake inanyenyekea kwa kawaida kwa ile hakika kuwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) ndiye Mola wake Mlezi na Muumba Wake. Lakini, ikiwa wazazi wake watajaribu kumfanya afuate njia nyengine tofauti, kijana huwa si mwenye nguvu za kutosha katika mwanzo wa maisha yake kupingana na kwenda kinyume na matakwa ya wazazi wake. Katika hali hiyo, dini anayofuata mtoto ni ile ya kiada na malezi, na Mwenyezi Mungu Hamuhesabu au kumuadhibu kwa dini hiyo anayofuata mpaka anapofika kipindi cha miaka fulani katika maisha yake.
ISHARA NA MIUJIZA YA MWENYEZI MUNGU
Katika maisha ya wanaadamu wote, kutoka wakati wa ujana na utoto hadi wakati wanapofariki, ishara za Mwenyezi Mungu mmoja peke Yake wa kweli zinaonyeshwa kwao katika maeneo yote ya ardhi, hata katika nafsi zao mpaka ibainike kwao kuwa yupo Mwenyezi Mungu mmoja tu wa kweli (Allah). Mwenyezi Mungu Anasema katika Qur'ani:
سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿٥٣﴾
"Tutawaonyesha Ishara Zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?" (41: 53).
Hapa tunatoa mfano jinsi Mwenyezi Mungu Anavyompatia ishara mtu mmoja kwa upotevu kwa kuabudu masanamu. Katika eneo la kusini mashariki mwa msitu wa Amazon huko Brazil, Amerika Kusini, kabila la asili lisiostaarabika lilijenga kibanda kipya ili kumpatia makazi sanamu-mtu, Skwatch, likiwakilisha mungu mkubwa kabisa wa uumbaji wote. Siku ya pili kijana mmoja aliingia katika kibanda hicho ili kutoa heshima zake kwa mungu. Alipokuwa katika hali ya kusujudu kwa jinsi alivyofundishwa kuwa hilo sanamu ni muumba na mlezi wake, na mwenye kuruzuku, mara aliingia mbwa mzee, hafifu na mwenye upele na aliyejawa na viroboto kwenye kibanda hicho. Kijana huyo alinyanyua uso wake kwa wakati muafaka, wakati tu wakumuona mbwa huyo akinyanyua mguu wake wa nyuma na kulikojolea sanamu hilo. Kijana alimfukuza mbwa huyo katika hekalu kwa ghadhabu kubwa mno; lakini hasira na ghadhabu ilipofifia alitambua kuwa sanamu hawezi kuwa mola wake mlezi wa ulimwengu mzima. Mwenyezi Mungu ni lazima awe kila pahala, alihitimisha. Ajabu kama inavyoonekana, mbwa kulikojolea sanamu ilikuwa ni ishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kijana huyo. Ishara hii ilikuwa na risala ya Mwenyezi Mungu kuwa anachokiabudu ni cha uwongo. Tukio hili lilimuacha huru kijana huyo na utumwa wa kufuata ada alizofundishwa za kuabudu mungu wa uwongo.
Matokeo yake ni kuwa huyu kijana alichaguzishwa: ama kutafuta mungu wa kweli au kuendelea katika upotevu wa njia zake.
Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatutajia kiu aliyokuwa nayo Nabii Ibraahim ('Alayhis Salaam) katika juhudi ya kumtafuta Mwenyezi Mungu kama mfano wa wale wenye kufuata ishara Zake jinsi wanavyoongoka (na hivyo kufuata njia nyoofu na ya sawa).
Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
وَكَذَٰلِكَ نُرِي إِبْرَاهِيمَ مَلَكُوتَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلِيَكُونَ مِنَ الْمُوقِنِينَ ﴿٧٥﴾ فَلَمَّا جَنَّ عَلَيْهِ اللَّيْلُ رَأَىٰ كَوْكَبًا قَالَ هَـٰذَا رَبِّي فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَا أُحِبُّ الْآفِلِينَ ﴿٧٦﴾ فَلَمَّا رَأَى الْقَمَرَ بَازِغًا قَالَ هَـٰذَا رَبِّي فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَئِن لَّمْ يَهْدِنِي رَبِّي لَأَكُونَنَّ مِنَ الْقَوْمِ الضَّالِّينَ ﴿٧٧﴾ فَلَمَّا رَأَى الشَّمْسَ بَازِغَةً قَالَ هَـٰذَا رَبِّي هَـٰذَا أَكْبَرُ فَلَمَّا أَفَلَتْ قَالَ يَا قَوْمِ إِنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ ﴿٧٨﴾ إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ حَنِيفًا وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٧٩﴾
"Na kadhaalika Tulimwonyesha Ibraahim ufalme wa mbingu na ardhi, na ili awe miongoni mwa wenye yakini. Na ulipomuingilia usiku akiona nyota, akasema: Huyu ni Mola Mlezi wangu. Ilipotua akasema: Siwapendi wanaotua. Alipouona mwezi unachomoza alisema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Ulipotua akasema: Kama Mola Mlezi wangu hakuniongoa, nitakuwa katika kaumu waliopotea. Na alipoliona jua linachomoza akasema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Huyu mkubwa kuliko wote. Lilipotua, alisema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayofanyia ushirikina. Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa aliyeziumba mbingu na ardhi, wala mimi si miongoni mwa washirikina" (6: 75 - 79).
Kama ilivyotajwa hapo awali, Manabii walitumwa kwa kila taifa na kabila kuunga mkono itikadi ya kimaumbile ya mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu na mwelekeo wa silica aliozaliwa nao mwanadamu wa kumuabudu Yeye, vile vile kutilia nguvu ukweli wa kutoka kwa mungu. Kwa ishara za kila siku zilizodhihirishwa na Mwenyezi Mungu. Japokuwa mafunzo mengi ya Manabii hawa yaligeuzwa, sehemu zinazoonyesha vifungu zilizoteremshwa na Mwenyezi Mungu zimebaki bila ya waa na zimewatumikia wanaadamu kuwaongoza katika kuchagua baina ya ukweli na uwongo, na haki na batili. Ushawishi wa risala zilizofunuliwa na Mwenyezi Mungu kupitia kwa zama zote zinaweza kuonekana katika "Amri Kumi" za Uyahudi katika Taurati ambazo baadaye zilichukuliwa na kuingizwa katika mafunzo ya Ukristo. Vile vile kuwepo kwa kanuni dhidi ya mauaji, wizi na uzinzi katika jamii nyingi sana kote duniani, katika zama za kale na sasa. Matokeo kwa ishara za Mwenyezi Mungu kwa wanaadamu kupitia kwa zama zote zikichang'anywa na wahyi Wake kupitia kwa Manabii Wake, wanaadamu wote wamepatiwa fursa ya kumtambua Mwenyezi Mungu mmoja tu wa kweli. Kwa hiyo, kila nafsi itahesabiwa kwa itikadi yake kwa Mwenyezi Mungu na kukubali kwake kwa Dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu, Uislamu, ambayo ina maana ya kunyenyekea na kutii amri za Allah (Subhaanahu wa Ta'ala).
HITIMISHO
Maudhui zilizotangulia zinatuonyesha kuwa jina la Dini ya Uislamu, inaeleza msingi wa kati mno wa Uislamu kumnyenyekea na kumtii Mwenyezi Mungu. Ieleweke kuwa jina "Islaam" halikuchaguliwa na mwanadamu lakini na Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa Kitabu kitukufu cha Uislamu. Pia imeonyeshwa kuwa Uislamu peke yake ndio unaofundisha sifa za Mwenyezi Mungu zisio na kifani na unahimiza kuabudiwa kwa Mwenyezi Mungu peke Yake bila ya kuwa na wenye kuwajongeza na kuwaleta karibu Naye. Mwisho, kwa sababu ya mwelekeo wa mwanadamu aliyopatiwa na Mwenyezi Mungu kumuabudu Yeye na ishara zilizoteremshwa na Mwenyezi Mungu kupitia miaka na zama kwa kila mtu binafsi, Uislamu unaweza kufikiwa na watu wote katika zama zote. Kwa muhtasari, umuhimu wa jina Uislamu (kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu), msingi wa Uislamu kukiri kwa ule upweke wa Mwenyezi Mungu na kufikiwa kwake na wanaadamu wote kwa zama zote. Haya yanadhibitisha dai la Uislamu kuwa kuanzia mwanzo wake, kwa lugha yoyote iliyotumiwa kuueleza, Uislamu peke yake ndio uliokuwa, na umebaki kuwa Dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu.
Kuhitimisha, tunamuomba Allah, Aliyetukuka, kutueka na kutubakisha katika njia nyoofu na ya sawa ambayo Ametuongoa nayo, na Utukirimu, Uturidhie na kutupatia rehema, kwani Wewe ni Mwingi wa Kurehemu. Sifa njema zote ni za Allah, Mola Mlezi wa viumbe vyote, sala na salamu zimfikie Mtume Muhammad (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam) na kwa Manabii wote wa Allah ('Alayhimus Salaam) na watangu wema.
SHARTI YA KUCHAPA
Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein
Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini
ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.
MWISHO WA KITABU