• Anza
  • Iliyopita
  • 2 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 2630 / Pakua: 2399
Kiwango Kiwango Kiwango
ANAYENGOJEWA

ANAYENGOJEWA

Mwandishi:
Swahili

ANAYENGOJEWA

IMAMU MUHAMMAD AL-MAHDI (a.j)

KIMETUNGWA NA: MAULANA SAYYID 'ALI NAQI SAHEB

KIMETAFSIRIWA NA: SAYYID MUHAMMAD MAHDI EL-MOOSWAWY

UTANGULIZI

Kitabu hiki ni cha mwisho katika mfalulizo wetu huu wa maisha ya Watakatifu Kumi na Wanne wa jamii ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) , nacho kinahusu maisha ya Imamu wa Kumii na Mbili. Watu ambao ni vigumu sana kuwaelewa tuzionapo habari zao na hata tunapoonana nao jicho kwa jicho, hakika itakuwa vigumu zaidi kuwaelewa wanapokuwa hatuwaoni. Kitabu hiki hakikukusudiwa kwa wale wasioyaamini yale yasiyoonekana bali kwa wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu Asiyeonekana.

JINA NA UKOO

Alikuwa ni mwana wa Imamu Hasan Askari, Imamu wa kumii na moja wa ukoo wa Mtume(s.a.w.w) anayetokanana ye kutokana na kizazi cha Husain(a.s) , aliyekuwa mwana wa Fatima(a.s) binti wa Mtume(s.a.w.w) na Bwana Ali(a.s) binamu yake (Imani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao wote). Amepewa jina Ia Mtukufu Mtume(s.a.w. w ) na ana umbo lifananalo na lake. Mama yake ni Bibi Nargis (Narcissus), mjukuu (atokanaye na binti) wa Mfalme wa Urumi na anayotokana na kizazi cha Simon, mwanafunzi wa Nabii Issa(a.s) . Bibi Nargis alipewa mafundisho ya dini na Bibi Halima Umbu wa Imamu Hasan Askari(a.s) kwa amri ya Imamu Hasan Askari(a.s) .

MAJINA YA HESHIMA

Pengine Imamu Mahdi(a.s) ana majina mengi ya heshima na yu wa pili kwa wingi wa majina ya heshima baada ya Imamu 'Ali(a.s) . Majina yake ya heshima yaliyo maarufu sana ni:

1. Al-Mahdi "(Aliyeongozwa)". Jina hili linatumika badala ya jina lake hasa na biashara nyingi za Mtume(s.a.w.w) na Maimamu zimemtaja kwa jina hili. Hii ndiyo sababu kuwa imani ya kuja kwa Mahdi ina msingi katika madhehebu zote za Kiislamu, ijapokuwa zinatofautiana katika maelezo ya jambo hilo.

2. Al-Qa'im "(Wa Sasa)". Jina hii limetokana na hadithi za Mtukufu Mtume(s.a.w.w) zinazosema"Dunia haitafikia mwisho kabla ya mtu mmoja katika ukoo wangu kusimama.

Maana halisi ya Al-Qa'im ni "anayesimama" kuijaza dunia kwa haki.

3. Sahibu Zaman (Kiongozi wa Zama hizi).

4. Hujjatullah (Hoja au Dalili ya Mwenyezi Mungu).

5. Al-Muntadhar, (Anayengojewa).

Si katika Uislamu tu, bali hata katika dini zinginezo, na kwa majina mbali mbali zipo biashara zinazomhusu "Atakayekuja".

KUTABIRIWA KWAKE

1) Kutabiriwa kwake na Mtukufu Mtume(s.a.w. w ) :

Karibuni katika vitabu vyote mashuhuri vya Hadithi (maneno na vitendo vya Mtukufu Mtume(s.a.w. w ) mna bishara zimhusuzo Imamu Mahdi na waandishi kadhaa; walikusanya hadithi zenye bishara hizo. Bwana Hafidh Muhammad bin Yusuf Shaffi katika kitabu chake kiitwacho "Al-Bayan fi Akhbari Sahibi zaman".

Bwana Hafidh Abu Na'im Isfahani amezikusanya hadithi hizi katika kitabu chake kiitwacho "Zikr Ni't Al-Mahdi", Bwana Abu Dawud Sijistani katika kitabu chake kiitwacho "Sunan" chini ya kichwa cha habari maalum cha "Al-Mahdi", Bwana Tirmidh katika kitabu chake kiitwacho "Sahih", Bwana Ibn Majah katika kitabu chake kiitwacho "Sunan" na Bwana Hakim katika kitabu chake kiitwacho "Mustadrak" wameziandika hadithi kadha wa kadha kuhusu jambo hili, mojawapo ikiwa imesimuliwa na Bwana Ibni Abbas, inasema kwamba, Mtukufu Mtume(s.a.w .w ) alisema:"Mimi ni kiongozi wa Mitume na Ali ni kiongozi wa Mawalii. Wa kwanza katika Mawalii wangu kumii na mbili atakuwa Ali na wa mwisho ni Al-Mahdi (a.s) ".

2) Kutabiriwa kwake na Bibi Fatimah(a.s) bint wa Mtukufu Mtume(s.a.w. w ) :

Kufuatana na hadithi katika kitabu kiitwacho "Kafi" cha Bwana Jabir bin Abdullah Ansar alisema kwamba, Bibi Fatimah(a.s) alikuwa na ubao ulioandikwa majina yote ya Mawalii na Maimamu na aliwataja Maimamu wote kumi na wawili kwa majina yao, watatu walikuwa wanaitwa Muhammad na wanne wanaitwa Ali na wa mwisho atakuwa wa kudumu.

3) Na Kutabiriwa kwake na Hadhrat Ali(a.s) :

Sheikh Saduq Muhammad bin Ali ameandika katika kitabu chake kiitwacho "Ikmaluddin" hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Ali Ridha(a.s) kwamba, Hadhrat Ali bin Abu Talib(a.s) alimwambia mwanawe Husain, "Wa tisa katika kizazi chako atakuwa mwenezaji wa dini ya kweli na haki".

4) Kutabiriwa kwake na Imamu Hassan(a.s) :

Imamu Hasan(a.s) amesema katika Hadithi iliyoandikwa katika kitabu hicho "Ikmaluddin" kuwa:"Atakapozaliwa wa tisa katika dhuria wa ndugu yangu Husain, Mwenyezi Mungu atampa maisha marefu katika muda wa ughaibu wake (kutoonekana) na utakapowadia wakati huo atamdhihirisha duniani tena".

5) Kutabiriwa kwake na Imamu Husain(a.s) :

Imamu Husain alisema, "Dhuria wangu wa tisa ni Imamu yule atakayeitetea Haki na Mwenyezi Mungu ataihuisha hii Dunia iliyokufa na kwaye dini ya haki itazishinda dini zote. Muda wake wa ughaibu utakuwa mrefu na katika muda huo watu wengi watapotoka na wachache tu watabaki katika imani nao watateswa. Kwani watu watawaambia, "Kama ninyi ni wakweli, basi tuambieni lini ubashiri huo utatimia". Watavumilia (hao wenye kuamini) na watapata baraka sawa na zile za waliopigana pamoja na Mtume."

6) Kutabiriwa kwake na Imamu Ali Ibnu-ul Husain(a.s) :

Imam Ali Zainul Abidin(a.s) alisema:"Wa mwisho wetu atakuwa yule ambaye kuzaliwa kwake kutakuwa kwa siri kiasi ambacho watu wa kawaida watasema kuwa bado hajazaliwa".

7) Kutabiriwa kwake na Imamu Muhammad al-Baqir(a.s) :

Sheikh Kulini ameandika kuwa Imam Baqir(a.s) alisema: "Wapo Maimamu tisa baada ya Husain, wa tisa wao atakuwa wa kudumu".

8) Kutabiriwa kwake na Imamu Jafari Sadiq(a.s) :

Sheikh Saduq ameandika kuwa lmamu Jafar(a.s) alisema:"Wa tano katika kizazi cha mwanangu, Musa, atakuwa wa kudumu wa ukoo wa Muhammad (s.a.w.w)" .

9) Kutabiriwa kwake na Imamu Musa Kadhim(a.s)

Sheikh Saduq ameandika kuwa Imamu Musa(a.s) alisema: "Mtu mmoja alimwuliza Imam Musa Kadhim, "Wewe ni Qaim bil Haqq" (msimamizi wa haki)? Alimjibu,"Ndiyo, mimi, lakini huyo al-Hasan atakayekuwa Qa'im (wa kudumu) ni yule atakayeisafisha ardhi ya Mwenyezi Mungu kutokana na maadui Wake Mwenyezi Mungu) na ataijaza kwa haki. Atakuwa wa tano katika dhuria wangu. Atatoweka kwa muda mrefu wakati ambao watu wengi watapotea na wachache tu watabakia katika imani" .

10) Kutabiriwa kwake na Imamu Ali Ridha(a.s) :

Mshairi mmoja Bwana Di'bal alipokuwa akisoma shairi lake maarufu Ienye sifa (za Maimamu) mbele ya Imamu Ridha(a.s) , alisoma kifungu kinachosema hivi:

"Na hakika Imamu wetu atakuja.

"Na ataliiamarisha Jina Ia Mwenyezi Mungu na baraka Zake.

"Atatupambanulia baina ya jema na uovu

"Na atawalipa watu wote thawabu na adhabu."

Imamu aliIia na alisema: "Unajua kwamba umeletewa vifungu hivi na Roho Mtakatifu? Unajua ni nani Imamu huyo na lini atadhihirika?" Yule mshairi alijibu kuwa hajui; alichokisikia ni kwamba atakuwepo Imamu katika ukoo wa Mtume(s.a.w. w ) atakayeitakasa dunia na kuijaza haki. Kisha Imamu alisema:"Ewe Di'bal, mwanangu Muhammad atakuwa Imamu baada yangu na baada yake mwanawe Ali, na baadaye mwanawe Hasan, na baadaye mwanawe Al-Qaim, ambaye atangojewa wakati wa kutoonekana kwake na atakapodhihirika, dunia nzima itamwinamia."

Kutabiriwa kwake na Imamu Muhammad Taqi(a.s) :

Imamu Taqi(a.s) amesema, "Wa kudumu katika sisi atakuwa yule Mahdi, atakayekuwa wa tatu katika mfululizo wa kizazi changu".

11) Kutabiriwa kwake na Imamu Ali Naqi(a.s) :

lmamu Naqi(a.s) amesema, Mrithi wangu atakuwa mwanangu Hasan, lakini hali yenu itakuwaje wakati wa mrithi wake? Alipoulizwa aeleze zaidi alisema, "Hamtakuwa salama hata kulitaja jina lake, achilia mbali kutaka kumwona". Aliulizwa, "Basi vipi tukalitaja jina lake?" Alisema, "Itakuwa hivi: "kwa dalili kutoka miongoni mwa ukoo wa Mtume".

12) Kutabiriwa kwake na Imamu Hasan Askari(a.s) :

lmamu Hasan(a.s) aliulizwa, "Masayyidi wako (amani ya Mwenyezi Mungu iwawie wote) walisema kwamba dunia haiwezi kuwa bila ya dalili ya Mwenyezi Mungu na ye yote yule afaaye bila kumjua lmamu wa wakati wake hufa kifo cha kikafiri". Alijibu, "Hakika,hii ni wazi kabisa kama mwanga wa mchana". Tena aliulizwa, "Basi nani atakayekuwa mrithi wako? Alijibu, "Mwanangu, Mwenye jina Ia Mtume atakuwa mrithi wangu na ye yote atakayekufa bila ya kumtambua atakufa kifo cha ujinga. Muda wa kutoonekana kwake utakuwa mrefu hata majahili (wale wasiomjua) watasumbuka hapa na pale na waovu watapata laana ya milele na wale watakaotabiri wakati wake maalum wa kuonekana (wa kudhihiri kwake) watakuwa wanasema uwongo".

Hadithi hizi na tabiri zote hizi zinaonyesha kwamba tokea wakati wa Mtume(s.a.w.w) mwenyewe kumetajwa kuwapo kwa mtu "Aliyeongozwa" katika dini". Si hayo tu, lakini kisa cha shairi la Di'bal kinaonyesha kuwa suala hili ni muhimu sana hata washairi wakaanza kulitungia mashairi. Historia inaonyesha kwamba marafiki na maadui wote kwa pamoja walikuwa na taarifa kamili ya hadithi hizo na daima walijaribu kuzitumia hadithi hizi kwa kuendelezea hoja zao mbaya. Kwa mfano, Khalifa Muhammad wa ukoo wa Bani Abbasi, alijipa jina la Mahdi ili kuwadanganya watu. Katika dhuria wa Imamu Hasan(a.s) , Muhammad mwana wa Abdullah Mahaz vilevile aliaminiwa na baadhi ya watu kuwa yu Mahdi na madhehebu ya Kaisania ilitamka kuwa Muhammdd Hanafiyah yu Mahdi. Lakini dhana ya mtu Mtakatifu kutoka katika ukoo wa Mtume(s.a.w.w) iliyashinda madai ya wale wote waliojifanya Mahdi. Kila mara dhuria wa Mtume(s.a.w.w) wamekuwa wakitoa maelezo kamili kuhusu Mahdi wa kweli na kutoonekana kwake ambayo yalionyesha wazi wazi kuwa Waislamu wamekuwa wakimngojea Mahdi wa kweli. Zaidi ya hapo hadithi za Mtume(s.a.w.w) zinazowataja Maimamu hawa kumi na wawili zinaonyesha uwongo wa madai ya walaghai hawa. Lakini wakati wa Imamu Hasan Al-Askari, Maimamu kumi na moja wa Mtume(s.a.w.w) walishatokea na ulimwengu wa Kiislamu ulikuwa na hamu ya Imamu aliyekuwa akingojewa kabla ya kuzaliwa kwake, na atakayengojewa katika muda wa ughaibu wake baada ya kuzaliwa kwake.

KUZALIWA KWAKE

Wakati ukawadia na mnamo tarehe 15 Shaaban mwaka 255 Hijiriya katika Mji wa Samarah (nchini Iraq) alizaliwa mtoto Mtukufu wakati wa usiku.

Imamu Hasan Askari(a.s) alitoa sadaka ya mikate mingi na nyama nyingi na akachinja mbuzi kadhaa wakati wa sherehe ya "Aqiqah" (kunyolewa kwa nywele za kichwa alizozaliwa nazo).

KUKUA NA MALEZI

Haikuwa kitu kipya kwa ukoo wa Mtume(s.a.w.w) kwa watoto wao kutopata elimu ya nje. Ipo mifano mingine kabla ya 'Anayengojewa'. Kwa mfano, babu yake, Imamu Ali Naqi(a.s) alikuwa na umri wa miaka sita na miezi michache tu alipofariki baba yake Imamu Muhammad Taqi(a.s) ambaye yeye mwenyewe pia alikuwa na umri wa miaka minane tu alipofariki baba yake Imamu Ali Ridha(a.s) .

Ni dhahiri kwamba, muda huo mfupi ukilinganishwa na desturi ya ukuaji wa watoto wa kawaida hautoshi kwa elimu ya nje. Lakini tunapokubali kwamba wamebarikiwa kwa baraza za Mwenyezi Mungu, basi swala la umri halitazuka hata kidogo. Katika mwezi wa Rabiul-Awwal, (Mfunguo Sita) mwaka 260 Hijiriya Imamu Hasan Askari(a.s) alikufa, na huyu mtoto mdogo wa miaka minne na nusu, alichukua nafasi yake ya Uimamu kwa muda mrefu unaokuja.

UPELELEZI WA WATAWALA WA ZAMA ZILE

Kama vile ambavyo Firauni aliposikia kwamba mtoto atazaliwa katika Mayahudi, atakayeangamiza utawala wake hakuacha hata njia moja ya kujaribia kuzuia kuzaliwa kwa yule mtoto na hata ikiwa mtoto huyo keshazaliwa, kujaribu kumwua, vile vile mtawala wa ukoo wa Bani Abbas alijua kwa njia ya hadithi za mara kwa mara zisimuliwazo kuwa atazaliwa mwana wa Imamu Hasan Askari(a.s) atakayekuwa mwangamizaji wa serikali yake hiyo ovu. Hivyo, alijaribu kuzuia kuzaliwa kwa mtoto huyo na akamweka Imamu Hasan Askari(a.s) katika kifungo cha maisha. Lakini, kama vile Nabii Musa(a.s) alivyozaliwa Iicha ya juhudi zote za Firauni, vivyo hivyo, Imamu "anayengojewa" alikuja duniani.

Na kuzaliwa kwake, kufuatana na Maamrisho ya Mwenyezi Mungu na Rehma Yake, kulikuwa siri.

Imamu Hasan Askari(a.s) alipofariki na ulipowadia wakati wa kumswalia sala ya maiti, Mwenyezi Mungu akaliondoa pazia Ia Ughaibu kwa muda mfupi. Watu wote wanaohusiana na jamii ya wafuasi wa ukoo wa Mtume(s.a.w.w) walikuwa wamesimama katika safu kwa ajili ya sala ya maiti na Bwana Jaafar, nduguye Imamu Hasan Askari(a.s) alikuwa kesha simama mbele kuiongoza sala hiyo, alipotokea kwa ghafla kijana mdogo tokea nyuma ya pazia Ia chumba cha wanawake, na akaenda pale aliposimama Bwana Jaafar kupitia katikati ya safu. Akalivuta joho Ia Bwana Jaafar na kumwambia, "Rejea nyuma, Ami: Mimi nina haki zaidi ya kuongoza swala ya maiti ya baba yangu". Bwana Jaafar alirudi nyuma, na Imamu Kijana akaiongoza sala. Baada ya sala Imamu akatoweka tena nuyuma ya lile pazia. Haiwezekani kwa Khalifa wa wakati ule kutofahamu kuwa yule mtoto amezaliwa. Hivyo juhudi za kumtafuta Imamu kijana asiyeonekana zikaanza kwa juhudi maradufu na kila njia ilitafutwa ya kumkamata na kumfunga au hata ya kumwua.

UGHAIBU

Muda wa kazi yake ya Uimamu umegawanyika katika sehemu mbili za Ughaibu. Moja inaitwa "Ghaibat-Sughra" (Ughaibu mfupi) na mwingine inaitwa "Ghaibati Kubra" (Ughaibu mrefu). Yote hayo yamebashiriwa na dhuria wa Mtume(s.a.w.w) , kwa mfano:

(i) Mtume(s.a.w.w) amesema:"Yeye ataendelea katika ughaibu mrefu wakati watu wengi wataingia katika kiza" .

(ii) "Katika muda wa ughaibu wake, wale watakuobakia katika kuamini watakuwa wachache kama kiberiti" .

(iii) Hadhrat Ali(a.s) alisema: "Wa mwisho wetu sisi atakuwa ghaibu kwa muda mrefu. Ninaona jinsi wakati ule marafiki zetu watakavyohangaika kama ng'ombe wafanyavyo wanapotafuta chakula.

(iv) Mahala pengine Imamu Ali(a.s) anasema: "Atadhihirika baada ya muda mrefu sana usiotambulika na ughaibu, wakati ambapo wenye imani kweli kweli ndio watakaoweza kubakia na imani.

(v) lmamu Hasan(a.s) amesema:"Allah atampa umri mrefu wakati wa kutokuwepo kwake".

(vi) Vile vile lmamu Husain(a.s) na Imamu Baqir(a.s) wamesema kwamba:"Muda wa ughaibu wake utakuwa mrefu wakati ambapo wengi watapotea" .

(vii) Imamu Jaffar Sadiq(a.s) amesema:"Mahdi atakuwa wa tano katika kizazi cha mtoto wangu, na ataendelea kufichika kutoka machoni mwenu."

(viii) Mahala pengine lmamu Jaafar(a.s) anasema:"Sahibul Amr kuwa ughaibuni ni lazima wote wawe wanaoamini na kubaki katika njia yao ya unyofu na dini."

(ix) Imamu Musa Kadhim(a.s) amesema:"Uso wake utaondoshwa mbele ya macho ya watu lakini jina litaendelea kukumbukwa na kubakia katika nyoyo za wanaoamini. Yeye atakuwa wa kumi na mbili wetu.''

(x) Imamu Ridha(a.s) amesema:"Atakuwa anayengojewa wakati wa kutokuwepo kwake".

(xi) Imamu Muhammad Taqi(a.s) amesema:"Mahdi atangojewa wakati wa kutokuwepo kwake, na atakapodhihirika ni lazima atiiwe" .

(xii) Imamu Ali Naqi(a.s) amesema:"Wengi watasema kuhusu "Sahibul-Amr" kwamba hajazaliwa bado" .

(xiii) Imamu Hasan Askari(a.s) amesema:"Kutoweka kwa mtoto wangu kutakuwa kiasi ambacho wote watakuwa na shaka isipokuwa wale tu waliorehemewa na Mwenyezi Mungu."

(xiv) Vile vile Imamu Muhammad(a.s) amesema:"Wa mwisho katika sisi atakuwa na vipindi viwili vya ughaibu; mmoja utakuwa mrefu na mwingine utakuwa mfupi" .

(xv) Pia Imamu Jaafar Sadiq(a.s) amesema:"kipindi kimoja (cha ughaibu) kitakuwa kirefu zaidi kuliko kingine" .

Kuwa na elimu ya hadithi hizi zote na ubashiri kuliwaokoa wale walioamini katika kutokuwa na shaka yo yote kuhusu Imamu huyu baada ya Imamu Hasan Askari(a.s) , na hawakumkubali mdai yo yote mwingine kuwa yu Mahdi.

KIPINDI KIFUPI CHA UGHAIBU

Kipindi hiki kilianzia tokea mwaka 260 Hijiriya na katika wakati huo, Imamu aliwachagua manaibu wake kila wakati ili kuchukua maagizo na maswali ya wanaomuamini na kuwapelekea majibu yake, kusimamia mambo ya fedha kwa niaba ya Imamu na wakati mwingine kupeleka maagizo yake ya kimaandishi kwa watu wanaoaminika. Manaibu hawa ni wanne, na ni wata maarufu sana katika zama zao na imani, unyoofu na usimamizi mzuri. Mabwana hao ni:

1. Bwana Abu Amr Uthmaan bin Said Asadi. Yeye alikuwa naibu wa Imamu Ali Naqi(a.s) na Imamu Hassan Askari(a.s) na vile vile aliishikilia kazi hiyo wakati wa Imamu Mahdi (Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao wote) na baada ya kuifanya kazi hiyo kwa miaka kadhaa, alifariki mjini Baghdad (Iraq) ambako alizikwa.

2. Bwana Abu Jaafar Muhammad, mwana wa Bwana Uthmaani aliyetajwa hapo juu, alikuwa amekwisha chaguliwa na Imamu Hasan Askari kushika nafasi ya babie, na babie alipofariki alitangaza kuchaguliwa kwake kwa amri ya Imamu wa sasa. Alifanya kazi mpaka alipofariki huko Baghdad, mnamo Jamadal-Awwal (Mfunguo Nane) mwaka 305 Hijiriya.

3. Bwana Abdul Qasim Husain bin Rauh bin Abi Bahr Naubakhti, Bwana huyu alikuwa mnajimu na falsafa maarufu sana katika zama zake. Yeye ni mtoto wa ukoo maarufu sana wa Naubakht, na yeye mwenyewe alikuwa maarufu na Mwanachuoni Mchamungu sana.

4. Bwana Abul Hasan Ali bin Muhammad Sumri. Yeye alikuwa mjumbe wa mwisho naye alishika mahala pa Bwana Husain bin Rauh, na buda ya kufanya kazi kwa miaka tisa, alifariki mnamo tarehe 15 Shaaban 329 Hijiriya. Alipoulizwa kuhusu mshika nafasi yake alisema, "Sasa Mwenyezi Mungu anataka kufanya utaratibu mwingine na muda wa wakati huo anaujua yeye tu."

Hakuna wasii aliyechaguliwa baada yake. Katika mwaka huo huo, yaani mwaka 329 Hijiriya mwandishi wa kitabu kiitwacho 'Kafi' Bwana Muhammad bin Yaqub Kulini na baba yake Sheikh Saduq Ali bin Babawaihi Qummi vile vile walifariki. Pamoja na hasara hizo, ilionekana idadi kubwa ya nyota zikipita mbinguni mwaka ule hivyo mwaka huo aliuita "mwaka wa kutawanyika kwa nyota", yaani kiza kitafuata. Hii ilikuwa na maana kwamba hakuna mtu aliyebakia ambaye angestahili kuteuliwa kama naibu wa Imamu.

MPINDI KIREFU CHA UGHAIBU

Baada ya mwaka 329 Hijiriya ukaanza muda huu wa kutokuwepo naibu. Maimamu wameacha maagizo ya "kuwafuata wale wenye kuzijua hadithi zetu na wanaopambanua haki na batili (katika mambo ya dini).

Wao watakuwa mawakilishi wetu kati yetu". Ndio sababu wanachuoni (Mujtahidi) wa Kishia wanaitwa 'Manaibu wa Imamu'.

Tunaamini kwamba kwa Rehema za Mwenyezi Mungu Imamu anafanya kazi yote anapokuwa haonekani kama vile alipokuwa anaonekana, na ataendelea kutoonekana mpaka Mwenyezi Mungu atakapoamuru vingine na wakati utafika ambapo atadhihirika na kuifanya dunia kuwa makao ya Uadilifu itakapojaa ufisadi na dhulma. Natuombe kudhihirika kwake na tupate utawala wa furaha.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU

YALIYOMO

ANAYENGOJEWA 1

IMAMU MUHAMMAD AL-MAHDI (a.j) 1

KIMETUNGWA NA: MAULANA SAYYID 'ALI NAQI SAHEB 1

KIMETAFSIRIWA NA: SAYYID MUHAMMAD MAHDI EL-MOOSWAWY 1

UTANGULIZI 1

JINA NA UKOO 1

MAJINA YA HESHIMA 1

KUTABIRIWA KWAKE 2

KUZALIWA KWAKE 4

KUKUA NA MALEZI 4

UPELELEZI WA WATAWALA WA ZAMA ZILE 5

UGHAIBU 5

KIPINDI KIFUPI CHA UGHAIBU 6

MPINDI KIREFU CHA UGHAIBU 7

SHARTI YA KUCHAPA 7

MWISHO WA KITABU 7

YALIYOMO 8