1
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA
MWITO WA QURRAN
Mwenye kufuatilia Aya za Quran tukufu, akazingatia maana yake, atazikuta zina mfungamano mmoja tu katika kanuni zake zote na misingi yake. Vile vile katika sura zake na Aya zake. Mfungamano huu ni ule mwito wa kuwapa watu maisha mema yenye uadilifu, ustawi na amani. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ﴾
"Enyi mlioamini mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita katika yale yatakayowapa uhai." (8:24)
MWITO WA MWENYEZI MUNGU NA MTUME
Mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume kwenye maisha, una mfumo wake na nguzo zake maalum zinazousimamia Mwenyezi Mungu ameupanga mfumo wa kulingania kwa kumwambia Mtume wake mtukufu(s.a.w.w)
:
﴿ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ﴾
"Waite kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora." (16:125)
MAKUSUDIO YA HEKIMA NA MAWAIDHA MAZURI
Makusudio ya hekima na mawaidha mazuri ni kuuambia moyo na akili, na kuuonyesha viumbe vya aina yake na vya ajabu. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴾
"Tutawaonyesha ishara zetu zilizo katika upeo wa mbali na katika nafsi zao mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli" (41:53)
Vile vile kuwahadharisha wapinzani na mwisho mbaya, na huwaonyesha mfano wa umma uliotangulia; kama alivyofanya Nabii Shuaib aliposema:
﴿وَيَا قَوْمِ لَا يَجْرِمَنَّكُمْ شِقَاقِي أَن يُصِيبَكُم مِّثْلُ مَا أَصَابَ قَوْمَ نُوحٍ أَوْ قَوْمَ هُودٍ أَوْ قَوْمَ صَالِحٍ وَمَا قَوْمُ لُوطٍ مِّنكُم بِبَعِيدٍ﴾
"Na enyi watu wangu! Kukhalifiana nami kusiwapelekee kuwasibu kama yaliyowasibu watu wa Nuh au watu wa Hud au watu wa Swaleh. Na watu wa Lut si mbali nanyi." (11:89)
Wakiendelea na inadi yao, na ikiwa hakuna dalili zaidi za kutoa, basi achana nao. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿فَإِنْ حَاجُّوكَ فَقُلْ أَسْلَمْتُ وَجْهِيَ لِلَّـهِ وَمَنِ اتَّبَعَنِ﴾
"Na kama wakikuhoji, basi sema nimeusalimisha uso wangu kumwelekea Mwenyezi Mungu na walionifuata (3:20)
﴿فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ﴾
"... Hakika ni juu yako kufikisha na ni juu yetu hisabu."(13:40)
Ama nguzo za mwito wa maisha mema, ni hizi zifuatazo:-
1. Hakika mtu hakupatikana kibahati tu, bila ya makusudio yoyote.
﴿وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ ثُمَّ يَتَوَفَّاكُمْ﴾
"Na Mwenyezi Mungu amewaumba kisha atawafisha" (16:70)
2. Mwenyezi Mungu hakumwacha mtu bure bure tu, ajihukumilie kimapenzi yake, bali amemuwekea njia ya sawasawa, ambayo haijuzu kuikengeuka: Mwenyezi Mungu anasema:
﴿أَيَحْسَبُ الْإِنسَانُ أَن يُتْرَكَ سُدًى﴾
"Hivi anadhani kuwa mtu ataachwa bure bure tu !" (75:36)
﴿فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩٢﴾ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴾
"Naapa kwa Mola wako tutawauliza wote yale waliyokuwa wakiyatenda." (15: 92-93)
3. Amani na kuchunga nidhamu. Mwenye kuiharibu na akafanya uharibifu katika nchi ataadhibiwa adhabu kali duniani, na katika akhera atakua na adhabu. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿إِنَّمَا جَزَاءُ الَّذِينَ يُحَارِبُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَسْعَوْنَ فِي الْأَرْضِ فَسَادًا أَن يُقَتَّلُوا أَوْ يُصَلَّبُوا أَوْ تُقَطَّعَ أَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم مِّنْ خِلَافٍ أَوْ يُنفَوْا مِنَ الْأَرْضِ ذَٰلِكَ لَهُمْ خِزْيٌ فِي الدُّنْيَا وَلَهُمْ فِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ عَظِيمٌ﴾
"Hakika malipo ya wale wanaopigana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kufanya uovu katika nchi, ni kuua-wa au kusulubiwa au kukatwa mikono yao kwa mabadilisho au kuhamishwa katika nchi; hii ndio fedheha yao katika dunia na akhera watapata adhabu kubwa." (5:33)
4. Amani na nidhamu haiwezi kuwako na wala haitakuwako ikiwa kila mtu hatachunga heshima yake na uaminifu wake. Kwa sababu jamii njema, kwa mujibu wa Quran, ni ile isiyokuwa na mbegu ya ufisadi hata moja. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿مَن قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الْأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا﴾
"Mwenye kumuua mtu bila ya yeye kuua mtu au kufanya ufisadi katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote; na mwenye kumwacha hai basi ni kama amewaacha hai watu wote." (5:32)
Hiyo ni kwamba hakika ya utu inakuwa kwa kila mmoja. Mwenye kumfanyia ubaya mmoja, atakuwa amewafanyia ubaya wote na mwenye kumfanyia wema mmoja, atakuwa amewafanyia wema wote.
Kusema kwake Mwenyezi Mungu: Mwenye kuua mtu bila ya yeye kumuua mwingine au kufanya ufisadi katika nchi", ni kuonesha kuwa kila mtu ana heshima yake ya kiutu, mpaka aivunje mwenyewe kwa kufanya kosa litakalovunja heshima yake hiyo.
5. Utangamano kati ya watu unakuwa juu ya misingi ya kuchunga heshima kwa kila mtu bila ya kubagua kati ya mwanamume au mwanamke, mweusi au mweupe na tajiri au maskini, katika mila yoyote aliyo nayo. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameuthibitisha ubainifu huu kwa ibara fupi:
﴿وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ ﴾
"Hakika tumemtukuza mwanaadamu..." (17:70)
Mwenye kuidharau heshima aliyopewa na Mwenyezi Mungu, atakuwa amemdharau Mwenyezi Mungu na sharia yake.
6. Kuamini Mwenyezi Mungu, Utume wa Muhammad(s.a.w.w)
, siku ya mwisho na mengineyo, ni katika misingi ya dini na matawi yake, wala sio kuwa ni bendera ya dini inayopeperushwa na Quran. Kila msingi katika misingi ya Uislamu na kila hukumu katika hukumu zake, zina matunda na amali yenye manufaa. Mwenyezi Mungu amekukutanisha kumwamini yeye na amali njema katika Aya kadhaa. Ama kuamini Utume wa Muhammad(s.a.w.w)
ni kuamini utu na wema wake. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿ وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴾
"Na hatukukutuma isipokuwa uwe rehema kwa walimwengu" (21: 107)
Ama kuingia peponi, kunafungamana zaidi na jihadi na amali njema katika maisha haya. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ ﴾
"Je mnadhani mtaingia peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawajua wale waliopigania jihadi dini ya Mwenyezi Mungu miongoni mwenu na kuwajua waliofanya subira?" (3:142)
﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ﴾
"Enyi ambao mmeamini mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita katika yale yatakayowapa uhai..." (8:24)
Hii ni dalili wazi kwamba mwito wowote ambao hauna muungano wowote wa maisha, basi sio wa dini. Na mwenye kuunasibisha kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atakuwa ameizulia uwongo dini. Kwa misingi hii, ndipo nikajaribu kufasiri Aya za Quran tukufu na kuifafanua kwa ufafanuzi ufuatao:-
Njia Makusudio ya njia hapa ni udhibiti anaokwenda nao mtungaji, bila ya kukengeuka. Kwani kazi yoyote ambayo haina njia ni shaghalabaghala tu, itakayoongozwa na migongano.
Njia niliyofuata katika tafsiri hii, inafungamana na kudhibiti mambo yafuatayo:-
1. Nimeitazama Quran kwa mtazamo kuwa hakika yake na sera yake ni kitabu cha dini na uongozi, kutengeneza na kuweka sharia inayolenga kuwapa watu wote maisha yaliyo katika misingi iliyosalimika, inayoongozwa na amani na uadilifu na iliyojaa furaha na wema.Hayo nimetangulia kuyaeleza.
2. Baadhi ya wafasiri wa kwanza walijishughulisha zaidi na lugha, wakarefusha maneno katika kubainisha siri ya matamko na wakaweka maswali; mfano: Kwa nini imetajwa wau na wala isitajwe fa au kwa nini amesema mafasiki na wala asiseme madhalimu, n.k. Kisha wakajibu majibu yasiyo na umuhimu.Mimi sikuingilia jambo hili.
Ikiwa kila tafsiri imepondokea upande fulani, basi mimi nimepondokea kwenye namna ya kumkinaisha msomaji kwamba dini kwa misingi yake yote na matawi yake pamoja na mafunzo yake mengine, ina lengo la kumpatia mtu heri na heshima na kwamba mwenye kukengeuka lengo hili, atakuwa ameikengeuka hakika ya dini na njia ya maisha yaliyonyooka.
Ili kuweza kulifikia lengo langu hili, nimejaribu kwa juhudi zangu zote kuleta ufafanuzi mwepesi na ulio wazi, atakaoweza kuufahamu msomaji kwa kiwango chochote atakachokuwa. Kwa vile zama walizoishi wafasiri wa zamani hazikuwa zama za kudharauliwa dini, sharia yake na misimamo yake kama ilivyo sasa, ndio maana wafasiri hao walijishughulisha zaidi na fasihi kuliko kumkinaisha msomaji kuwa dini ni msimamo ulio sawa sawa. Kwa hiyo lugha ya tafsiri ya zama hizo sio ya zama hizi.
Hakika tafsiri ni fani kamili inayokwenda na wakati. Ndio maana mimi nimeielekeza tafsiri yangu katika kukinaisha kizazi cha kisasa kuwa dini inakwenda sambamba na maisha. Lakini hiyo haimaanishi kuwa mimi nimeghafilika na upande wenye kunufaisha, ambao umeonyeshwa na wafasiri wakubwa, la! Isipokuwa nimeufupisha upande huo na kuuonesha kwa uwazi zaidi, hata nimeonyesha rai yangu ndani yake hasa katika masuala nyeti ya kifalsafa; mfano: Kulazimishwa watu au kuwa na hiyari, uongofu na upotevu, Uimamu na Isma ya Mitume.
Pia shafaa, mwenye madhambi makubwa, hisabu ya kaburi na mengineyo. Vilevile mara nyingi nimehusisha kifungu maalum cha lugha, kwa ajili ya kutafsiri misamiati ambayo si maarufu. Mara nyingine nimeweka kifungu kingine cha irabu kwa ajili ya kubainisha hukumu za Kinahw (sarufi) kwa tamko lenye utatanishi, ijapokuwa wafasiri wa kisasa hawakujishughulisha nalo, lakini mimi nimeangalia matakwa ya baadhi ya wasomaji wa nahw, ingawaje ni wachache.
Ama usanii wa methali za maneno, elimu ya usemaji, ulinganishaji na uunganishaji, nimemwachia Zamakhshari katika Kash-Shaf, Al-Andalusi katika Bahrul-Muhit, na wengineo. Ili kuthibitisha kuwa lugha ya tafsiri inatofautiana kulingana na wakati, ninataja maneno ya Muhyiddin Ibn El-Arabi katika kitabu Futuhatil Makkiyya, Juzuu ya nne, mlango wa Hadhratul-hikma, kuhusu kuisoma Quran, ambayo yana maana ya undani kabisa na yanayoafikiana na nadharia za kisasa; hasa ile nadharia ya Uwiano (Relativity) ya Einstein, ambaye anazingatia kuwa wakati na mahali ndivyo vinavyosimamisha kitu. Anasema huyo Ibnul Arabi:
Msomaji anasoma alichokihifadhi katika Qur'an, anakuta katika kila kisomo maana ambayo hakuyakuta katika kisomo cha kwanza pamoja na kuwa herufi zinazosomwa ni zile zile, isipokuwa matukio na hali ndivyo vipya.Kwa hivyo hapana budi maana hayo yawe mapya. Kwa sababu, wakati wa kusoma kwa kwanza sio kwa pili.
Hapa aliposema,hapana budi kuwa maana hayo yawe mapya, maana yake ni kuwa, kitu kinakuwa kipya kwa kuwa kipya wakati ule. Amesema kweli mwanafalsafa Rasil, aliposema: Hakika watu wa zamani waligundua nadharia zilizothibitishwa na elimu kulingana na fikra na jitahadi zao; na zilikuwa ni rai za sawa; ambapo katika zama zao hizo hakukuwa na kitu zaidi ya jitihadi ya maoni."
3. Nimeangalia hadith zinazohusu Israil ambazo zimekuja katika baadhi ya tafsiri, nikazikuta ni vigano tu. Kitu kinachofahamisha zaidi uwongo wake, ni kuzinasibisha kwa Waisrail. Vilevile nimejipurukusha na riwaya zilizoelezea sababu za kushuka, isipokuwa chache tu. Kwa sababu, wanachuoni hawakudhibiti mategemezo yake na kupambanua kati ya dhaifu na sahihi; kama walivyofanya kwa riwaya za hukumu. Hata hizo nazo hawakuangalia sana zile za Sunna na kuchunguza kwa makini, isipokuwa katika wajib na haramu.Bali wameweka utafiti mbali katika vitabu vya Usuul.
Vilevile sikujishughulisha na pia kumshughulisha msomaji, kutaja kufungamana au kunasibiana kati ya Aya na Aya nyingine; kama walivyofanya wafasiri
Wengine, Kwa sababu, Quran haikufunuliwa kwa Mtume(s.a.w.w)
kwa mpigo, bali iliteremshwa kwa nyakati maalum, mara nyingine kwa kufuatana na mara nyingine kwa kuchelewa; wala sura au Aya hazikupangwa kama tunavyozisoma hivi sasa.Quran, tuliyo nayo hivi sasa, ilipangwa tangu siku za Mtume(s.a.w.w)
. Mpango huu haukufuata utaratibu wa kushuka sura, wala kuwa sura ni ya Makka au Madina; vile vile hakuna tarehe ya kushuka Aya. Hivyo tunakuta Sura ya Baqarah,Al-Imran na Maida ziko mwanzo wa msahafu baada ya Sura ya Fatiha, pamoja na kuwa zimeshuka Madina. Mara nyingine tunakuta sura iliyoshuka Madina ina Aya zilizoshuka Makka.
Mwenye tafsir ya Al-Manar, akimnukuu mwalimu wake, Sheikh Muhammad Abduh, katika Juzu ya pili, ukurasa 451, chapa ya
Pili: anasema: Quran sio kitabu cha fani cha kuwa na mlango mahsusi na makusudio fulani; isipokuwa ni kitabu cha uongozi na waadhi, inamgurisha mtu kutoka hili mpaka lile. Na mara kwa mara inarudia kwenye utafiti wa kusudio moja, kwa ibara nyingine na namna nyingine ya ubainifu, ili asichoke mwenye kupewa mawaidha na kuongozwa.
4. Kabla ya kitu chochote nimetegemea, katika kutafsiri Aya na kubainisha makusudio, Hadith zilizothibiti kwa Mtume(s.a.w.w)
. Kwa sababu, ndizo zinazofasiri Quran na ni njia ya kujua maarifa yake. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿ وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ﴾
"Alichowapa Mtume kipokeeni na alichowakataza jiepusheni nacho" (59:7)
Ikiwa hakuna hadith, basi ninategemea dhahiri ya Aya na mpangilio wake. Kwa vile, msemaji mwenye hekima, ubainifu wake hutegemea yale anayoyafahamu yule anayemwambia kutokana na dalili zilizo wazi; kama ambavyo mwenye kuambiwa anachukua dhahiri hiyo tu, mpaka pale itakapothibitika kinyume. Kama ikija Aya nyingine katika maana ya Aya ya kwanza na ikawa ina ubainifu na kuwa wazi zaidi, basi ninazitaja pamoja ili zifafanuke zaidi. Kwa vile chimbuko la Quran ni moja, inajitamkia yenyewe na kujiletea ushahidi. Kama ikipingana dhahiri ya tamko pamoja na hukumu ya kiakili, basi ninaitafsiri kwa namna ambayo inaafikiana na akili, kwa kuizingatia hiyo akili kuwa ni dalili na hoja juu ya amali iliyo wajibu.
Ikiwa dhahiri ya tamko inapingana na Ijmai ya Waislamu katika nyakati zote kwenye masuala ya Kifiqh, basi huchukua Ijmai: kama kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿إِذَا تَدَايَنتُم بِدَيْنٍ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى فَاكْتُبُوهُ ﴾
"Mnapowekeana deni kwa muda uliowekwa, basi iandikeni" (2:282)
Ambapo neno iandikeni limefahamisha wajibu, lakini Ijmai imesimamia juu ya kuwa kuandika deni ni sunna. Kwa hiyo hapo nimechukua kuwa ni suna na sio wajibu.
Ama kauli za wafasiri, sikuzifanya ni hoja mkataa na dalili peke yake; isipokuwa kutilia nguvu njia mojawapo, ikiwa tamko linachukua maana nyingi. Hata hivyo wafasiri wamefanya juhudi kubwa sana za kufafanua maana ya Quran na siri zake, na kuonyesha lugha inayofahamika na ngeni. Wamekitafsiri kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa juhudi ambayo haijapatikana mfano wake katika umma wa zamani au wa sasa.
Kwa hakika kuna wafasiri wakubwa na waliobobea katika fani mbali mbali za elimu ya Quran ambao walikuwa ni watu muhimu sana katika historia ya Kiislam. Kwa hiyo ingawaje kauli za mabingwa hao si hoja, kama kauli ya Masum, lakini zinaweza kuwa ni mwangaza juu ya maana yanayokusudiwa na kuuandaa njia ya kufahamu.
Makosa ya Chapa Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa. Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo.Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.
Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa Swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146) Imeandikwa La Yaalamuun, (hawajui) badala ya Yaalamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.
Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya pili, Sura (2:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawmal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile. Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil Makosa ya chapa.
Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbaina sanah badala ya: Hatta idha balagha ashuddahu arbai- na sanah. Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana. Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa, kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.
Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin
:Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu"
. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyoyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani.(Amin).
MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH
NAJILINDA KWA MWENYEZI MUNGU NA SHETANI ALIYEFUKUZWA
Kujilinda na Shetani Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:
﴿فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ ﴾
"Unaposoma Quran jilinde kwa Mwenyezi Mungu na shetani aliyefukuzwa" (16:98)
Amesema tena:
﴿وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ﴾
"Na kama wasiwasi wa shetani ukikusumbua basi jilinde kwa Mwenyezi Mungu. Yeye ni Mwenye kusikia mjuzi" (7:200)
Maana ya kujilinda Kujilinda huku kwa Mungu hakutoshi kwa kusema: Audhubillahi minashshaytwanir rajim tu, isipokuwa linalotakikana ni kumwamini Mwenyezi Mungu, kumtegemea na kumwogopa; hata kama mtu hakutamka hivyo. Mwenye kutenda umuhimu wowote kwa kuitakidi kuwa nyuma yake kuna nguvu inayomsaidia kutenda amali njema; mwenye kupondokea kufanya haramu, lakini twaa ya Mwenyezi Mungu ikamzuia na mwenye kuchanganyikiwa akaifanya sharia ndio kipimo, wote hao ni katika wale wanaojilinda kweli kwa Mwenyezi Mungu na shetani aliyefukuzwa.
Hakuna kitu kinachofafanua zaidi kujilinda kuliko mtu kumtegemea Muumba wake, kuwa na yakini kwamba mja mwingine hawezi kumdhuru wala kumnufaisha na kwamba kabisa hakuna kitu kitakachozidi hifadhi ya Mwenyezi Mungu.
Majaribio yametufundisha kwamba mwenye kumtukuza asiyekuwa Mwenyezi Mungu, amedhalilika; na mwenye kutaka uokovu kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ameruka utupu; na matarajio hayawezi kupatikana kwa kuwakimbilia viongozi, chama, wala kwenye hazina za matajiri, bali Mwenyezi Mungu tu peke yake ambaye hana mshirika.
Shetani ni nani? Sisi hatujamwona Shetani ana kwa ana lakini ametolewa habari zake na wahyi. Kwa hivyo ni wajibu kusadiki kuwa yupo, na si wajibu kujua alivyo. Mwenyezi Mungu amemtaja katika Quran kwa sifa ya kupoteza watu na kuwaepusha na twaa ya Mwenyezi Mungu na amali ya heri. Kwa hiyo kila wazo linalokupitia moyoni au mtu anayejaribu kukuhadaa kukuweka mbali na twaa na kheri ya Mwenyezi Mungu, kukuhadaa kuasi sharia na kuuvika uovu na ubatilifu nguo ya uongofu, basi huyo ni Shetani wa hisia au wa kimaana.
Jambo la kushangaza ni kuwa mashetani watu nao wanaomba walindwe na shetani, hali wao wenyewe ni mashetani lakini hawajijui. Ni sawa na mtu anayesoma Quran na huku inamlaani mwenyewe; kama ilivyoelezwa katika hadith.Quran inamlaani mwongo aliye haini.Kwa hivyo huyo mwongo anapoisoma huwa amejitamkia laana yeye mwenyewe.
Mwenyezi Mungu anasema:
﴿أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُمْ أَنَّ عَلَيْهِمْ لَعْنَةَ اللَّـهِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ ﴾
"Hao malipo yao ni kushukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika na ya watu wote". (3:87)
Hukumu ya Kusoma Audhubillah... kabla ya kusoma Quran ni sunna, wala si wajib; ni kama vile kuosha mikono na kusoma Bismillah kabla ya kula. Lau hiyo Audhubillahi ingelikuwa ni wajibu ingeliwajibishwa katika swala, mahali pa fatiha na Sura.Wanavyuoni wote wamesema kuwa si wajib. Mwenye Miftaahul-Karaama amesema: Hawakuhitalifiana katika hilo isipokuwa Ibn al-Junaid ambaye mafakihi wamemwita: aliyejitenga.
Mantiki ya Iblis Kwa mnasaba wa Audhu (kujilinda na Shetani) tutadokeza vigano alivyonasibishwa navyo Ibilisi. Kwa sababu ingawaje ni vigano, lakini vina picha wazi kwa watu wengi wa zama hizi; hasa wale wanaotaka kujinufaisha bila ya kuangalia maslahi ya wengine, kwa kufanya mbinu za kujaribu kila njia ya kucheza na maneno na kuficha haki. Tutayaonyesha hayo kwa matamko tu; bila ya kudhihirisha madhumuni.
Inasemekana kuwa Ibilisi alimwambia Mwenyezi Mungu (s.w.t):
Haijuzu kuniadhibu kwa kuacha kumsujudia Adam. Mwenyezi Mungu akamuuliza,Kwa nini? Akajibu: Kama ungelitaka hasa nimsujudie ungenifanyisha kwa nguvu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akamuuliza: Wakati gani ulijua kwamba sikukutaka umsujudie Adam? Je ulilijua hilo baada ya kukuamrisha na kuasi amri yangu?Au kabla ya kukuamrisha kusujudu? Akasema: Ni baada ya kuniamrisha.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.).akasema: Basi umejishinda. Kwa sababu ulihalifu kabla ya kujua kuwa Mimi niliyataka yale uliyoacha kuyafanya. Zaidi ya hayo kama ningekufanyisha kwa nguvu, basi isingelikuwa amri. Utaona katika mantiki ya Ibilisi sura iliyo wazi kwamba Mwenyezi Mungu hawafanyishi wenye kuwajibikiwa na sharia kama vile anavyofanya katika kuumba kwa njia ya kun fayakun (kuwa, ikawa). Isipokuwa anawafanyisha kwa njia ya kuongoza matakwa ya mtu kwa sharia inayoelezwa ya kuamrisha mema na kukataza mabaya.
Inasemekana kuwa siku moja Ibilisi alikutana na Mtume Muhammad(s.a.w.w)
akamwambia: Hakika Mwenyezi Mungu amekusifu kwa jina la kiongozi, na mimi amenisifu kwa jina la mpotezaji. Lakini uongozi na upotezaji vyote vinatokana na Yeye, kwa hiyo wewe na mimi hatuna chochote.
Mtume akasema:Hapana! Mimi hubainisha batili na kuikataza na kuitolea kiaga kibaya;hali wewe una unafiki na hadaa ya ubatilifu; na mtu ana uwezo, upambanuzi na hiyari. Kwa hivyo mwenye kufanya hiyari nzuri (akaongoka) anajifanyia mwenyewe, na mwenye kuifanya mbaya (akapotea) pia anajifanyia mwenyewe.
Imesemekana kuwa Ibilisi alimwendea Nabii Isa
akamuuliza: Si unadai kuwa wewe una daraja kubwa kwa Mungu? Basi hebu jitupe kutoka juu tuone,je atakuokoa? Masihi akasema: Hakika Mwenyezi Mungu ndiye anayemjaribu mja wake na sio mja kumjaribu Mola wake.
Imesemekana kuwa baada ya gharika na kukauka maji, Ibilisi alimwendea Nuh
akamwambia: Hakika wewe umenisaidia, kwa hiyo ninataka kukulipa. Nuh
: Akasema: Mungu apishe mbali! kumsaidia na kiumbe kama wewe. Akasema Ibilisi: Ndio hivyo. Nuh
: Akasema kwa nimekusaidia nini? Akasema Ibilisi: Umewaapiza watu wako ili waangamie wakaangamia, na nilikuwa nikijishughulisha usiku na mchana kuwapoteza kwa muda huo. Baada ya kuaangamizwa watu wako, sina kazi ya kufanya; sipati wa kumpoteza. Nuh
akasema: Utanilipa nini?
Akasema: Ninakunasihi usikasirike, kwa sababu hasira ya mtu inarahisisha kunifuata.Wala usihukumu kati ya watu wawili. Kama ukifanya hivyo, basi mimi nitakuwa wa tatu wenu. Wala usikae faragha na mwanamke kwani mimi hukuvutia kwake na yeye humvutia kwako. Kutokana na mantiki hii ya kishetani, inaonyesha kuwa Shetani ndiye mchochezi, na kwamba yeye huzipongeza silaha zenye kuangamiza.
HEKAYA
Inasemekana kwamba Mtume(s.a.w.w)
na sahaba zake walimpitia mtu mmoja akirukuu na kusujudu kwa unyeyekevu. Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni uzuri ulioje wa swala ya mja huyu! Mtume akasema:Huyu ndiye aliyemtoa baba yenu peponi
.
LENGO LA HEKAYA
Lengo la hekaya hii ni kuwa haifai mtu kughurika na kuhadaika kwa zuhudi na ibada ya dhahiri.
Inasemekana kuwa Nabii Musa
alikuwa akienda kuzungumza na Mola wake, ikatokea kukutana na Ibilisi, akamwambia Unakwenda wapi ewe uliyezungumza na Mwenyezi Mungu? Nabii Musa
akasema: Ninakwenda kwa Mola wangu kupokea maneno kutoka kwake na niko tayari kukuombea akusamehe kama utaniahidi kuungoa upotevu wako. Ibilisi akasema: Mimi sina haja ya kuombewa na wewe wala mwingine, bali ni juu Yake Yeye Mungu kutaka radhi yangu.(Mungu apishe mbali). Musa
akamwambia: Kafiri mkubwa we Mwenye laana! Ibilisi Akasema: Kwani nina dhambi gani mimi? Mungu alinitaka nimsujudie Adam, na mimi kwa iIkhlas yangu, siwezi kumsujudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Sasa tangu lini Ikhlas ikawa ni dhambi? Musa
akamjibu: Hii ni kuchezea maneno tu nako hakuwezi kukufaa wewe hata chembe, utaona yatakayokupata Kesho (Kiyama). Ibilisi akasema: Na wewe utaona nitakavyofanya kesho. Akasema: Utafanya nini?
Ibilisi akajibu: Nitamtaka Mwenyezi Mungu atimize ahadi Yake na nitamtolea hoja kwa kauli Yake:
﴿وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ ﴾
"Na rehema yangu hukienea kila kitu" (7:156)
"Nami ni kitu, kwa hiyo ni wajibu rehema Yake inipate (inienee).Kama mimi si chochote, basi sitahisabiwa wala kuadhibiwa.
Akasema Musa
: Hakika rehema ya Mwenyezi Mungu inamwenea yule mwenye mwelekeo nayo, na wewe uko mbali sana nayo. Ibilisi akasema: Basi nitafanya njia nyingine. Nitawaita wafuasi wangu waliopotea na nitamtaka Mwenyezi Mungu (s.w.t.) naye awaite wafuasi Wake waumini, halafu ipigwe kura.Hapo atajulikana nani mshindi mwenye sauti ya wengi. Kama Mwenyezi Mungu akikataa kura, nitafanya maandamano makubwa mpaka nipate ninayotaka.
Kigano hiki kina lengo la kwamba watu wa batili ni wengi zaidi kuliko watu wa haki, kwa sababu haki ni nzito na batili ni nyepesi; kama alivyosema Amirul Muminin, Ali
:Yapasa mwenye akili kutoangalia wingi kuwa ni kipimo cha haki, wala uchache kuwa ni kipimo cha batili.
Katika Nahjul-Balagha, amesema:Hakika kundi kubwa ni watu wa batili hata wakiwa wengi; na kikundi kidogo ni watu wa haki hata wakiwa wachache.
Quran tukufu nayo inasema:
﴿وَأَكْثَرُهُمْ لِلْحَقِّ كَارِهُونَ ﴾
Na wengi wao ni wenye kuchukia haki. (23:70)
﴿وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ﴾
Lakini watu wengi hawajui.(12:21)
﴿وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَشْكُرُونَ ﴾
Lakini watu wengi hawashukuru.(12:38)
﴿وَأَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ ﴾
Na wengi wao hawatumii akili (5:103)
﴿بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴾
Bali wengi wao hawaamini (2:100)
Kuna Hadith inayosema:Wakikutana wasaidizi wa Ibilisi wanaweza kujaza Mashariki na Magharibi
.
Na kwa madondoo haya, na mengineyo mengi, ndipo Shia wakasema: Khalifa wa Mtume ni kama Mtume; huchaguliwa na Mwenyezi Mungu; siye yule anayechaguliwa na watu. Huyo anayechaguliwa na watu ni Mfalme wa watu; si Khalifa wa dini. Ama mkuu wa dini, kwa Shia, ni yule mwenye sifa zilizoelezwa. Sio yule anayechaguliwa na watu wala si yule anayewekwa na kiongozi wa kidunia.
Na kwa nini isiwe hivyo? Je,watu wenye matamanio ya dunia wanaweza kuaminika kuongoza dini ya Mwenyezi Mungu? Basi kama ni hivyo na wawachague na kuwapigia kura Mitume, na walifaradhishe hilo kwa Mwenyezi Mungu. Ametakata kabisa Mwenyezi Mungu na yale wayasemayo madhalimu. Natija ya kimantiki ni kwamba Khalifa wa Mtume hawi, na hatakuwa, isipokuwa kwa usimulizi unaotokana na Mtume mwenyewe, na kwamba mkuu wa dini ni yule mwenye sifa zilizosimuliwa.
Mwenye kujipachika ukuu wa dini bila ya kuwa na sifa zilizotajwa, basi atakuwa amemzulia Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na ameruka patupu mwenye kuzua. Kwa hivyo basi, yote hayo yanafahamisha kuwa suala lolote haliwezi kuwa la kweli mpaka liwe limefuata haki; na kwamba mbinu za kucheza na maneno, haziwezi kuifanya batili iwe haki, au haki iwe batili, wala kisichoingia akilini kiingie akilini; hata kama hizo mbinu zitakuwa za hali ya juu kiasi gani.
Tutakalolifahamu ni kuwa mwenye mbinu hizo ni mwanafunzi hodari wa Ibilisi katika kuificha haki, na kuifunika na moshi wa hadaa.