18
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA
AL - BAQARAH (NG’OMBE)
﴿وَإِذْ جَعَلْنَا الْبَيْتَ مَثَابَةً لِّلنَّاسِ وَأَمْنًا وَاتَّخِذُوا مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى وَعَهِدْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ ﴾
125.Na tulipoifanya ile nyumba (Al-Kaaba) iwe mahali pa kuendewa na watu na mahali pa amani. Na pafanyeni alipokuwa akisimama (Maqamu) Ibrahim ni mahali pa kuswalia. Na tuliagana na Ibrahim na Ismail kuwa: Itakaseni nyumba yangu kwa ajili ya wale wenye kutufu na wenye kujitenga huko kwa ibada na wanaorukuu na kusujudu.
﴿وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ اجْعَلْ هَـٰذَا بَلَدًا آمِنًا وَارْزُقْ أَهْلَهُ مِنَ الثَّمَرَاتِ مَنْ آمَنَ مِنْهُم بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ قَالَ وَمَن كَفَرَ فَأُمَتِّعُهُ قَلِيلًا ثُمَّ أَضْطَرُّهُ إِلَىٰ عَذَابِ النَّارِ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ﴾
126.Na aliposema Ibrahim: Ewe mola wangu! Ufanye mji huu uwe wa amani na uwaruzuku wakazi wake matunda, wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho katika wao. Akasema Mwenyezi Mungu: Na mwenye kukufuru nitamstarehesha kidogo; kisha nitamsukumiza katika adhabu ya moto napo ni mahali pabaya kabisa pa kurejea.
NA TULIPOIFANYA ILE NYUMBA IWE MAHALI PA KUENDEWA
Aya 125-126
LUGHA
Nyumba: ni nyumba yoyote, lakini ikisemwa nyumba tu, basi itakuwa ni Al- Kaaba, kutokana na kutumika sana hivyo.
MAANA
Na tulipoifanya ile nyumba (Al-Kaaba) iwe mahali pa kuendewa na watu na mahali pa amani.
Aya hii inaungana na Aya iliyotangulia (alipomfanyia mtihani Ibrahim). Maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu ameijaalia nyumba yake ni mahali pa kuendewa na watu makundi kwa makundi kwa ajili ya kutekeleza ibada na baadaye warudi makwao; kisha yaje makundi mengine, n.k. Vile vile ameifanya ni mahali pa kupata amani katika akhera. Kwa sababu mtu anapoifikia nyumba hiyo na akatekeleza ibada anajirudi na kutubia. Kwa hiyo nyumba ya Al-Kaaba inakuwa ni nyenzo ya kujitakasa na adhabu na mateso. Kama vile ambavyo ameifanya ni mahali pa amani katika dunia. Kwa sababu mtu mwenye kwenda mahali hapo anakuwa salama wala haingiliwi na yeyote kwa ubaya. Mtu anaweza kumwona mtu aliyemuua baba yake katika Haram (eneo la Al-kaaba) lakini akajitia hamnazo! Desturi hii imerithiwa tangu wakati wa Ismail
mpaka leo.
MKOSAJI KUKIMBILIA HARAM
Katika kitabu cha Al-Jawahir ambacho ni tegemeo kubwa la Fiqh ya Shia Jafariyyah kuna maelezo haya, ninamnukuu: Yeyote aliyekimbilia haram hapigwi haddi kwa kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.).
﴿وَمَن دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا﴾
Na mwenye kuingia humo huwa katika amani
(3:97)
Bali atapunguziwa chakula na atapewa kidogo tu kiasi cha kuzuwia tumbo ili atoke akapigwe haddi nje. Imepokewa riwaya sahihi kutoka kwa Imam Jafar Sadiq
kuhusu mtu ambaye amefanya jinai mahali pengine pasipokuwa Haram kisha akakimbilia kwenye Haram. Akasema Imam:
Hatapigwa haddi, lakini hatalishwa, hatapewa maji wala hatasamehewa, kwani akifanyiwa hivyo, kuna uwezekano wa kutoka nje ya Haram na apigwe haddi. Kama akifanya jinai ndani ya Haram atapigwa haddi ndani ya Haram, kwa sababu hakuihishimu Haram
. Abu Hanifa amesema: Haifai kumwua aliyekimbilia kwenye Haram ametoa dalili kwa kauli ya Mwenyezi Mungu: Na tulipoifanya ile nyumba (Al- Kaaba) iwe mahali pa kuendewa na watu na mahali pa amani. Na pafanyeni alipokuwa akisimama Ibrahim ni mahali pa kuswali. Hiyo ni amri ya kuswali (Maqamu Ibrahim) mahali aliposimama Ibrahim.Mafaqihi wamekubaliana kuwa inatakikana kuswali hapo rakaa mbili za Tawaf ikiwezekana. Maana ya (Maqam Ibrahim) mahali aliposimama Ibrahim ni pale mahali maarufu ndani ya msikiti. Ama mwenye kusema kwamba makusudio yake ni msikiti wote, basi na atoe dalili ya kuthibitisha kauli yake hiyo.
Na tuliagana na Ibrahim na Ismaili kuwa itakaseni nyumba yangu kwa ajili ya wale wenye kutufu na wenye kujitenga kwa ibada na wanaorukuu na kusujudu. Maana yake, tulimwagiza Ibrahim na Ismaili kuiheshimu Al-Kaaba na kuiepusha na kila lisiloelekeana nayo; kama vile masanamu, najisi, upuuzi, uovu, majadiliano n.k. Na wawaamrishe watu hilo Wanye kutufu ni wale wanaoizunguka, wanaojitenga kwa ibada ni wanaokaa humo msikitini au wanaokaa karibu kwa ibada, na wanaorukuu na kusujudu, yaani wanaoswali. Na aliposema Ibrahim Ewe Mola wangu! Ufanye mji huu uwe wa amani. Hii ni dua na matamanio kutoka kwa Ibrahim kwa Mwenyezi Mungu kuijaalia Makka tukufu kuwa ni mji wa amani, yaani watu wake wasiwe na vita, mitetemeko, vimbunga n.k. Kuna kikundi cha wafasiri wamesema kwamba Mwenyezi Mungu ameiitikia dua ya Ibrahim, ambapo hakuna yeyote anayeikusudia Makka kwa uovu ila Mwenyezi Mungu humwangamiza, na mwenye kuikusudia kwa uadui basi uadui wake hauchukui muda mrefu. Na uwape wakazi wake matunda wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Ibrahim alipomaliza kujenga nyumba hiyo katika ardhi kame isiyokuwa na maji wala mmea wowote, alimwomba Mwenyezi Mungu s.w.t. aipe amani ardhi hii na iwe na rizki, wala hakuainisha aina ya riziki wala kule itakapotoka isipokuwa umuhimu ni kufikiwa na riziki vyoyote itakavyokuwa na popote itakapotoka. Mwenyezi Mungu Mtukufu aliitikia maombi ya Ibrahim. Ikawa riziki ya namna namna inakuja Makka kutoka sehemu mbali mbali; ikawa Makka ni kituo cha wasafiri na cha biashara. Katika hali hii ndipo Mwenyezi Mungu akasema katika Aya hii:
﴿أَوَلَمْ نُمَكِّن لَّهُمْ حَرَمًا آمِنًا يُجْبَىٰ إِلَيْهِ ثَمَرَاتُ كُلِّ شَيْءٍ﴾
Je hatukuwakalisha mahali patakatifu na pa amani yanakoletwa matunda ya kila aina.
(28:57)
Ibrahimu aliwahusisha waumini tu katika kutaka riziki, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikwisha mfahamisha kwamba katika kizazi chake kutakuwa watu madhalimu na Mwenyezi Mungu hakuuhaidi Uimamu kwa madhalimu. Akasema (Mwenyezi Mungu s.w.t.):Na mwenye kukufuru nitamstarehesha kidogo
. Yaani Mwenyezi Mungu alimwambia Ibrahim: Mimi vile vile ninawaruzuku makafiri na hata mafasiki. Kwa sababu riziki ni kitu kingine na Uimamu ni kitu kingine, kwani Uimamu ni uongozi wa kidini na wa wakati, nao unahitajia imani, uadilifu na Isma. Ama riziki inakuwa kwa mwema na mwovu; kama vile maji na hewa. Madhambi na maasi hayana dhara yoyote katika umri na riziki katika maisha haya, isipokuwa athari yake itadhirhirika kesho siku ya kiyama ambapo watu watapata malipo yao.
﴿وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴾
127.Na Ibrahim alipoinua misingi ya ile Nyumba (Al-Kaaba) na Ismail (wakaomba): Ewe mola wetu! Tutakabalie;hakika wewe ndiye Msikizi Mjuzi.
﴿رَبَّنَا وَاجْعَلْنَا مُسْلِمَيْنِ لَكَ وَمِن ذُرِّيَّتِنَا أُمَّةً مُّسْلِمَةً لَّكَ وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا وَتُبْ عَلَيْنَا إِنَّكَ أَنتَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴾
128.Ewe mola wetu! Utufanye tuwe ni wenye kusilimu kwako.Na miongoni mwa kizazi chetu pia ufanye umma uliosilimu kwako. Na utuonyeshe ibada zetu na utukubalie toba.Hakika wewe ndiye mwenye kukubali toba mwenye kurehemu.
﴿رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴾
129.Ewe mola wetu! Wapelekee mtume anayetokana na wao, awasomee Aya zako, na kuwafundisha Kitabu na hikima na awatakase.Hakika wewe ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.
NAALIPOINUA IBRAHIM MISINGI YA ILE NYUMBA
Aya ya 127 - 129
HISTORIA YAAL-KAABA
Wafasiri na wanahistoria wametofautiana katika historia ya Al-Kaaba, kwamba je, ilikuako kabla ya Ibrahim, kisha ikaharibika ndipo akaijenga upya yeye na mwanawe Ismail kwa amri ya Mwenyezi Mungu mtukufu; au yeye (Ibrahim) ndiye aliyeanza kuijenga? Wafasiri wengi na wanahistoria wa Kiislamu wamesema kuwa ilikuwako kabla ya Ibrahim kwa miaka mingi. Baadhi wamesema ilianzishwa na Ibrahim
; wengine wamenyamaza na kusema: Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi. Nasi tuko pamoja na hawa. Kwani akili haina nafasi hapa, na njia ya kujua itategemea athari au Aya za Quran au Hadith mkato. Na mimi sikupata kauli yoyote ya watafiti wa athari na uvumbuzi, na Quran haikuelezea waziwazi historia ya Al-Kaaba, bali inaelezea tu kwamba Ibrahim na mwanawe Ismail waliijenga na kusaidiana.Na hii haifahamishi kuwa ilikuwako au haikuako kabla ya Ibrahim.Na Hadithi mkato hakuna isipokuwa Hadithi Ahad (pwekesho). 34 Na Hadithi pwekesho ni hoja katika hukumu ya sheria tu. 35 Kwa vyovyote iwavyo sisi hatutaulizwa na Mwenyezi Mungu mtukufu wala hatuna wajibu wa kuijua historia ya kujengwa Al-Kaaba au kujua wakati ilipoanzishwa.
* 33 Hadithi iliyokubaliwa na wote katika maana na matamshi.
* 34 Hadith ambayo silsila (mfuatano) ya upokezi wake imekatika au Hadith ambayo haikubaliwi na wengi.
* 35 La Kushangaza zaidi ya niliyoyasoma kuhusu maudhui haya ni kauli ya Sayyid Tabatabai katika Tafsir Al-Mizan J1 Uk 196 Kukosekana kusihi mapokezi ya hadith hakuwajibishi kuitupa Hadith hiyo maadamu haihalifu akili au Hadith sahihi Inajulikana wazi kwamba kutohalifu akili na Hadithi thabiti ni sharti la yasiyothibiti, kwa sababu kutothibitika kusihi mapokezi kunatosha kuitupa Hadithi bila ya kuongeza sharti jengine; kama si hivyo basi itabidi kuitumia kila Hadithi isiyokuwa sahihi mpaka itakapohalifu akili au hadithi thabiti. Vile vile hatuna taklifa ya kujua kwamba hiyo ni sehemu ya pepo au ni ya ardhi na kwamba je, Adam na Mitume baada yake walihiji au la! Au kwamba hiyo Al-Kaaba ilipandishwa mbinguni wakati wa Tufani kisha ikateremshwa ardhini.? Pia hatuna taklifa ya kujua kwamba Hajarul-Aswad (jiwe jeusi) lililetwa na Jibril kutoka mbinguni au lilikuja pamoja na Adam kutoka peponi au lilibanduka kutoka Jabal Abu Qubays na kwamba je lilikua jeusi kwa sababu ya kuguswa na wenye dhambi. Na mengineyo ambayo hayana mapokezi yoyote isipokua Hadithi Ahad au visa visivyokuwa na ukweli.
Sisi hatutaulizwa vitu vyote hivyo wala hatuna taklifu yoyote ya kujua si kwa njia ya wajibu, wala sunna; si kiakili wala kisheria.Wala hakuna faida yoyote ya kidini au dunia katika kuifanyia utafiti. Utafiti huu ulikuako kisha ukaenda na upepo; na yeyote anayetaka kuufufua, ni sawa na yule anaejaribu kurudisha nyuma mishale ya saa. Kitu ambacho tutaulizwa na kutakiwa kukifanya kuhusu Al-Kaaba ni kuikusudia kwa ajili ya Hijja na Umra kwa anayeweza kuiendea. Na vile vile kuiheshimu na kuitukuza na kuihami kwa kufuata nyayo za Mtume(s.a.w.w)
Ahlul Bait wake(s.a.w.w),
masahaba, wafuasi, wanachuoni na Waislamu wote. kwani hao wanaamini bila ya tashwishi yoyote kwamba kuiadhimisha nyumba ya Mwenyeezi Mungu ni kumwadhimisha Mwenyezi Mungu, na kuihami ni kuihami dini ya Mwenyezi Mungu. Amirul Muminin amesema: Amewawajibisha Mwenyezi Mungu kuhiji nyumba yake tukufu ambayo ameifanya ni kibla cha viumbe,wanaingia kama wanavyoingia wanyama na wanaingia makundi makundi kama njiwa. Ameijaalia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni alama ya kumnyenyekea yeye (Mungu) na kuukubali Utukufu Wake. Ameijaalia ni alama ya Waislamu, na nikinga ya wenye kutaka hifadhi.
Ewe mola wetu! Tutakabalie.
Hii ni dua kutoka kwa Ibrahim na Ismail ya kutaka thawabu kutokana na amali hii, kwa sababu maana ya kutakabaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kupata thawabu kutokana na amali atakayoikubali, kama vile ambavyo kukosa thawabu kunamaanisha kukataliwa amali. Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu ameitakabali dua yao na amewalipa thawabu kutokana na twaa hii. Kwa sababu yeye ndiye aliyefungua mlango wa dua, na hawezi kumfungulia mja mlango wa dua, hasa mwenye kumcha Mwenyezi Mungu, kisha amfungie mlango wa kutakabaliwa, kama alivyosema Amirul Muminini. Ewe Mola wetu! Utufanye tuwe ni wenye kusilimu kwako. Makusudio ya kusilimu hapa ni kufanya ikhlas katika itikadi na amali (matendo). Hapana mwenye shaka kwamba mwema mwenye kusifiwa, ni yule anayemnyen-yekea Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mambo yake yote.Na miongoni mwa kizazi chetu (pia ufanye) umma uliosilimu kwako.
Ameikubali dua yao na akajaalia katika kizazi chao mamilioni na mamilioni ya waislamu.
SHIA NA MABABU WA MTUME
Shia wamehusika na kauli ya kuwa baba wa Muhammad, na mababu zake, mama yake na nyanya zake wote hawa-kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote na kwamba Muhammad tangu alipoumbwa alikuwa akigura (akihama) katika migongo mitakatifu mpaka kwenye tumbo la mfuko wa uzazi mtakatifu na hadi ilipotimu saa ya kuzaliwa kwake. Sheikh wa Shia mwenye kujulikana kwa jina la Sheikh Al-Mufid amesema katika sherhe ya Aqaid Aswaduq chapa ya mwaka 1371 A.H. uk 67: Hakika mababa wa Mtume(s.a.w.w)
kuanzia baba yake Adam, walikuwa ni watu walio na imani, na Mwenyezi Mungu amemwambia Mtume wake Muhammad: Na mageuko yako kati ya wale wanaosujudu. (26:219) Mtume(s.a.w.w)
amesema: Niliendelea kugurishwa katika migongo mitakatifu kwenda kwenye matumbo matakatifu mpaka Mwenyezi Mungu akanidhihirisha (kwa kuzaliwa) katika ulimwengu wenu huu. Kwa hiyo kauli ya Mtume inafahamisha kwamba mababu zake wote walikuwa wenye imani. Kwani lau baadhi yao wangekuwa makafiri isingelistahiki kusifiwa na utwahara kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:Hakika washirikina ni najisi.
(9:28)
Mtume alipowasifu mababu zake kwa utakatifu imefahamisha kwamba wao walikuwa waumini Utukubalie toba Sio lazima kwa mwenye kutaka msamaha awe na dhambi hasa ikiwa mwenye kutaka ni Mtume au wasii.Kwa sababu watu watukufu hawa wanajiona hawajafikia kuitekeleza haki ya Mwenyezi Mungu sawa sawa kadiri watakavyojitahidi katika ibada ya Mwenyezi Mungu. Kwani wao ndio wanaojua zaidi utukufu wa Mwenyezi Mungu. Na kwamba ibada ya mtu, vyovyote itakavyokuwa haiwezi kutekeleza haki ya utukufu huo usiokuwa na mwanzo wala mwisho. Ewe, Mola wetu! Wapelekee Mtume anayetokana na wao Ombi hili alilikubali Mwenyezi Mungu kwa kuleta Mtume wa mwisho na bwana wa Mitume wote.
Zimekuja Hadith kwa upande wa Shia na Sunni kwamba Mtume amesema: Mimi ni ombi la Ibrahim na ni bishara ya Isa. katika Quran Mwenyezi Mungu amesema: Yeye ndiye aliyemuinua Mtume katika wasiojua kusoma atokaye miongoni mwao anawasomea Aya zake na kuwatakasa na kuwafunza kitabu na hekima.Na kabla ya hayo walikuwa katika upotofu ulio dhahiri.
(62:2) Amirul Muminin Ali
amesema:Alimpeleka Mwenyezi Mungu Muhammad kuwa ni Mtume na hakuna yeyote katika waarabu aliyekuwa akisoma kitabu au kudai Utume wala wahyi.
BISHARA YA MAHDI MWENYE KUONGOJEWA
Kama walivyotoa Mitume bishara ya Muhammad,yeye naye alitoa bishara ya Mahdi kutoka katika kizazi chake. Mimi nimetunga kitabu juu ya suala hilo nilichokiita Al Mahdil Muntadhar Wal-aql (Mahdi mwenye kungojewa na akili) katika kitabu hicho nimenakili Hadith nyingi kutoka upande wa Shia na Sunni; na zimetoka nakala nyingi na kurudiwa na wachapishaji Daarul-malayin pamoja na kitabu Allahu wal-aql, Al-akhira wal-aql na Annubuwwat wal-aql. Vitabu hivyo vinne vimekusanywa kuwa kitabu kimoja kwa jina Al Islamu wal-aql (Uislamu na akili). Kitabu kilichokusanya zaidi kuhusu suala hili katika nilivyovisoma ni kitabu kinachoitwa Muntakhabul-athari fil - Imam thani ashar cha Sayyid Lutfillah Assafi kilichokuwa na kurasa zaidi ya 500, ambacho ni rejea bora zaidi. Baada ya kuchapishwa kitabu Al-Mahdil muntadhar wal-aql nilisoma maneno marefu ya Muhyiddin aliye mashhuri kwa jina la Ibnul Arabi, nanukuu sehemu ya maneno hayo. Mwenyezi Mungu anaye Khalifa atakayetoka ikiwa nchi imejaa dhulma na jeuri ili aijaze uadilifu... na khalifa huyo ni kutoka katika kizazi cha Mtume(s.a.w.w)
kutoka katika kizazi cha Fatima
, jina lake linafanana na jina la babu yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu ...Atafanyiwa baia kati ya rukni na maqam, anafanana na Mtume kwa umbo naye atakuwa na uso mwangavu mwenye pua ndefu... Atawaongoza watu kwa desturi ya Mtume(s.a.w.w)
. Na babu yake alisema kumhusu yeye: Atafuata athari yangu bila kukosea na hiyo ndiyo Isma. Hayo yamo katika kitabu Futuhatil-Makkiyya kilichochapishwa na Darulkutubil- Arabiya uk 327 na kuendelea.
﴿وَمَن يَرْغَبُ عَن مِّلَّةِ إِبْرَاهِيمَ إِلَّا مَن سَفِهَ نَفْسَهُ وَلَقَدِ اصْطَفَيْنَاهُ فِي الدُّنْيَا وَإِنَّهُ فِي الْآخِرَةِ لَمِنَ الصَّالِحِينَ ﴾
130.Na ni nani atajitenga na mila ya Ibrahim isipokuwa anayeitia nafsi yake katika upumbavu? Na hakika sisi tulimtakasa (Ibrahim) katika dunia; na hakika yeye katika akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.
﴿إِذْ قَالَ لَهُ رَبُّهُ أَسْلِمْ قَالَ أَسْلَمْتُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴾
131.Mola wake alipomwambia silimu; akasema Nimesilimu kwa Mola wa walimwengu wote.
﴿وَوَصَّىٰ بِهَا إِبْرَاهِيمُ بَنِيهِ وَيَعْقُوبُ يَا بَنِيَّ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ لَكُمُ الدِّينَ فَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴾
132.Na Ibrahimu akawausia haya wanawe, na pia Yaqub: Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia dini hii; basi msife ila nanyi mmekuwa Waislamu.
﴿أَمْ كُنتُمْ شُهَدَاءَ إِذْ حَضَرَ يَعْقُوبَ الْمَوْتُ إِذْ قَالَ لِبَنِيهِ مَا تَعْبُدُونَ مِن بَعْدِي قَالُوا نَعْبُدُ إِلَـٰهَكَ وَإِلَـٰهَ آبَائِكَ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ ﴾
133.Je, mlikuwapo yalipomfikia Yakub mauti, alipowaambia wanawe: Je, mtaabudu nini baada yangu? Wakasema: Tutamwabudu Mola wako na Mola wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is-haka; Mungu mmoja tu, na sisi tunasilimu kwake.
﴿تِلْكَ أُمَّةٌ قَدْ خَلَتْ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَلَكُم مَّا كَسَبْتُمْ وَلَا تُسْأَلُونَ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴾
134.Huo ni umma uliokwisha pita.Utapata Uliyoyachuma nanyi mtapata mtakayoyachuma; wala hamtaulizwa waliyokuwa wakiyafanya.
NA NI NANI ATAJITENGA NA MILA YA IBRAHIM
Aya ya 130 - 134
MAANA
Na ni nani atajitenga na mila ya Ibrahim isipokuwa anayeitia nafsi yake katika upumbavu?
Haya ni matahayarizo kwa Mayahudi na Manasara na washirikina wa Kiarabu ambao hawakumwamini Muhammad. Siri ya matahayarizo haya ni kwamba Mayahudi wanajifaharisha kwa kunasibika kwao na Israil: Na Israil ndiye Yaqub bin Is-hak bin Ibrahim; Manaswara nao wanajifaharisha kwa Isa na nasabu ya Isa kwa upande wa mama inaambatana na Israil vile vile. Ama washirikina wa Kiarabu wengi wao wanatokana na Adnani nasabu yao inarudia kwa Ismail bin Ibrahim kuongezea kwamba wao walipata heri wakati wa kijahili kwa baraka za nyumba iliyojengwa na Ibrahim. Kwa hiyo wote wanajifaharisha kwa Ibrahim na mila ya Ibrahim na inajulikana wazi kwamba Muhammad(s.a.w.w)
anatokana na kizazi cha Ibrahim na yuko katika mila ya Ibrahim. Kwa hivyo mwenye kumk-anusha Muhammad na mila yake ndio amemkanusha Ibrahim na mila yake. Hapana shaka kwamba mwenye kukanusha matokeo ya utukufu na fahari yake, basi yeye ni safihi (mpumbavu) sawa na mwenye kufanya mambo ya kumwangamiza yeye mwenyewe.
Hakika sisi tulimtakasa (Ibrahim) katika dunia; Yaani tulimfanya safi mwenye kutakata na uchafu; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا ﴾
Mwenyezi Mungu anataka kuwaondolea uchafu enyi watu wa nyumba (ya Mtume) na kuwatakasa kabisa kabisa.
(33.33)
Na hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.Kwa uwazi kabisa ni kwamba yeye katika dunia yuko hivyo; kwa sababu Uislamu unaiunganisha akhera na amali za duniani; ambaye katika dunia atakuwa mwema na mwenye busara, basi huko akhera pia atakuwa hivyo na ambaye katika dunia atakuwa mwovu na kipofu basi huko akhera pia atakuwa hivyo.
Mola wake alipomwambia silimu akasema: Nimesilimu kwa Mola wa walimwengu.
Unaweza kuuliza,Je, Mwenyezi Mungu alimtaka Ibrahim asilimu (anyenyekee) kabla ya kumpa Utume au baada yake? Kwa sababu haiwezekani Mwenyezi Mungu kumpa wahyi asiyekuwa Mtume.Na pia hawezi kuteremsha wahyi kwa mtu ila baada ya kusilimu (kunyenyekea).
Jibu
: Hakika kauli yake Mwenyezi Mungu: Silimu (Nyenyekea) akasema nimesilim ni fumbo la kuwa Ibrahim ni msafi mwenye Ikhlas na kwamba yeye ndiye mwenye kuchukua utume na ujumbe kwa ukamilifu. Kwa hivyo makusudio yake ni kumsifu Ibrahim kutokana na Ikhlasi yake, twaa yake na kufuata kwake amri. Wakati huo huo ni matahayarizo kwa Mayahudi, manaswara na washirikina wa Makka ambao wanajifaharisha kwa Ibrahim, kisha wanamuasi na kumpinga yule aliyekuja kuhuyisha mila ya Ibrahim na kueneza desturi na itikadi yake.
Na Ibrahim akawausia haya wanawe na Yaqub pia: Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia dini hii; basi msife ila nanyi mmekuwa Waislamu. Yaani thibitini juu ya Uislamu mpaka kufa ili mfufuliwe juu ya Uislamu na mumkabili Mwenyezi Mungu kwa huo Uislamu.
HAKI YA MTOTO KUTOKAKWA MZAZI
Aya hiyo iliyotangulia inatambulisha kwamba mzazi ana jukumu kubwa na malezi ya mtoto wake na kumwongoza kwenye dini ya haki. Imam Zaynul- Abidin
Amesema: Ama haki ya mtoto wako ni kujua kuwa anatokana na wewe na kwamba wewe una jukumu la kuitengeneza vizuri adabu yake na kumfahamisha kuhusu Mola wake Mtukufu na kumsaidia kumtii. Basi mwamrishe amali ambayo anajua kuwa atapata thawabu kwa kufanya wema, na kupata dhambi kwa kufanya mabaya.
Je mlikuwapo yalipomfikia Yaqub mauti. Kumfikia mauti ni wakati wa kufa, alipopata alama za kufa. Mwenye Majmau anasema: Mayahudi wanadai kuwa Yaqub alipokufa aliwausia wanawe kushikamana na Uyahudi. Ndio Mwenyezi Mungu akabatilisha madai yao juu ya Yaqub; sasa vipi mnadai mambo ya uongo? Kwa hakika ni kwamba Yaqub aliwaambia wanawe: Je mtaabudu nini baada yangu? Unaweza kuuliza kwamba neno nini hutumiwa kwa kisicho na akili, sasa imekuaje hapa kutumiwa kwa mwenye kuabudiwa kwa haki? Jibu: Wakati huo watu walikuwa wakiabudu masanamu, ndipo likaletwa swali kutokana na vile wanavyoabudu sio kutokana na uhaki wa kuabudu. Kwa hiyo maana itakuwa ni kitu gani mtaabudu? Wakasema: Tutamwabudu Mola wako na Mola wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is-hak, Mungu mmoja tu, na sisi tunasilimu Kwake. Unaweza kuuliza Yaqub ni mtoto wa Is-hak, na Ismail ni ami yake (ndugu wa baba yake) sasa imekuwaje kumwingiza Ismail pamoja na mababa? Jibu: Ami yuko katika daraja ya baba kwa sababu ni nduguye na anaadhimishwa kama anavyoadhimishwa baba.Iko Hadith ya Mtume(s.a.w.w)
inayosema; kuwa Mtume alisema:Nirudishieni baba yangu yaani ami yake Abbas.
Huo ni umma uliokwishapita. utapata ulioyachuma, nanyi mtapata mtakayoyachuma. Aya hii inaashiria kawaida ya mambo, kwamba natija za amali zote na athari zake zitamrudia mwenye kutenda peke yake, hawezi kunufaika nazo mwenye nasaba naye na wala hazitamdhuru mwingine. Uislamu umethibitisha kawaida hii kwa mifumo mbali mbali ya maneno, kama vile anavyosema Mwenyezi Mungu:...Wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine
(6:164)
Na kwamba mtu hatapata ila yale aliyoyafanya.
(53:39) Pia Mtume(s.a.w.w)
amesema kumwambia mwanawe Fatima:Ewe Fatima! Fanya amali wala usiseme mimi ni binti wa Muhammad, kwa sababu mimi sitakutoshea wewe na kitu chochote kwa Mwenyezi Mungu.
Na mengineyo. Kufafanua zaidi maudhui haya kutafahamisha kwamba mpaka leo sisi hatujui mambo yaliyo wazi kabisa.