4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA
AL - BAQARAH (NGO’MBE)
SURA YA PILI
Amesema mwenye Majmaul-Bayan kwamba: sura hii yote imeshuka Madina, isipokuwa Aya ya 281.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
﴿ الم ﴾
1.Alif Laam Miim
﴿ ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ فِيهِ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ ﴾
2.Hiki ni kitabu kisicho na shaka ndani yake; ni uwongozi kwa wamchao Mwenyezi Mungu.
﴿ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴾
3.Ambao wanaamini ghaibu na wanasimamisha Swala na wanatoa katika yale tuliyowapa.
﴿ وَالَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ وَبِالْآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ ﴾
4.Na ambao wanaamini yaliyoteremshwa kwako, na yaliyoteremshwa kabla yako na akhera wana yakini nayo.
Amesema mwenye Majmaul-Bayan kwamba: sura hii yote imeshuka Madina, isipokuwa Aya ya 281.
﴿ أُولَـٰئِكَ عَلَىٰ هُدًى مِّن رَّبِّهِمْ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴾
5.Hao wako juu ya uwongozi utokao kwa Mola wao, na hao ndio wenye kufaulu.
MIANZO YA BAADHI YA SURA
Aya 1- 5
﴿الم﴾
Alif Lam Mim
:
Wamehitalifiana wanavyuoni kuhusu makusudio ya mwanzo huu na ya mianzo ya sura nyingine inayofanana na hii mfano:
Alif Laam Miim Raa, Kaaf Haa Yaa Ayn Swaad na Haa Miim. Imesemekana kuwa herufi hizo ni katika elimu ya ghaibu ambayo Mwenyezi Mungu hakuidhihirisha kwa yeyote.Lakini sidhani kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaweza kuwaambia watu jambo asilotaka walijue. Zaidi ya hayo Mwenyezi Mungu amewakemea wale ambao hawaifikiri vizuri Quran, aliposema:
﴿أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا ﴾
Je,hawaizingatii (hii) Quran au katika nyoyo zao kuna kufuli? (
47:24).
Pia imesemekana mianzo hii ni majina ya sura; vilevile imesemwa ni majina ya Mwenyezi Mungu, aidha ikasemwa kuwa; ni ya Muhammad(s.a.w.w)
nk.. Lakini linaloelekea zaidi ni kauli inayosema kwamba: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kuwaambia wapinzani walete mfano wa Quran, au sura kumi, au moja; na wakashindwa, ndipo akataja herufi hizi. Yaani, kitabu hiki ambacho ni muujiza, hutokana na herufi hizi ambazo hata watoto na wajinga pia wanazitumia, lakini nyinyi mmeshindwa.
Kwa hivyo kushindwa kwenu ni dalili wazi kwamba kuna siri, na siri yenyewe ni kuwa hii Quran ni wahyi wa kidini sio usanii wa kidunia.
QURAN NA SAYANSI
Kauli yake Mwenyezi Mungu:Ni uwongozi kwa wamchao Mwenyezi Mungu
, ni dalili wazi kwamba Quran si kitabu cha elimu ya Historia, wala Falsafa, au elimu ya Fizikia au ya Hesabu; isipokuwa ni kitabu cha elimu ya uongofu wa mwana-adamu katika dunia na akhera, au sema: Quran ni kitabu cha dini, maadili, itikadi na sharia.
Kama utauliza
: Ikiwa Quran ni kitabu cha dini, mbona basi kuna Aya zinazohusu mambo ya kilimwengu; kama vile:
﴿وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَّهَا ﴿٣٨﴾ وَالْقَمَرَ قَدَّرْنَاهُ مَنَازِلَ﴾
Na jua linakwenda mpaka kituoni pake; na mwezi tumeupimia vituo (36:38- 39).
Jibu
: Lengo la Aya hizi sio kutubainishia hali ya maumbile kwa undani wa kielimu - kwani hilo limeachiwa akili na majaribio yake - isipokuwa lengo la kwanza la kutajwa Aya hizo ni kwamba, kujua ulimwengu na nidhamu yake kutatuongoza kujua kuwa kuna Mungu, na kwamba huu ulimwengu haukupatikana kibahati tu bila ya kukusudiwa; kama wanavyodai watu wa kimaada. Bali ulipatikana kwa matakwa ya kihekima. Mwenyezi Mungu amelibainisha hilo katika Aya isemayo:
﴿سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ﴾
Tutawaonyesha ishara zetu zilizo katika upeo wa mbali na zilizo katika nafsi zao mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. (41:53).
Yaani, tutawafafanulia makafiri - kwa vile watakavyoufahamu ulimwengu kutokana na mipangilio mizuri ya Mwenyezi Mungu - kuwa wao wako katika upotevu. Quran inapotoa mwito wa kuangalia ulimwengu, inasema kwa lugha iliyo wazi kuwa dalili za ulimwengu ni hoja ya kweli na ni dalili yenye nguvu zaidi juu ya kuwapo Mungu, kuliko kitu chochote. Baadhi ya wenye hekima wamesema: Mwenyezi Mungu ana vitabu viwili: Kitabu kinachosomwa na kitabu cha akili, ambacho ni ulimwengu.
Ni kweli kuwa Quran inahimiza kusoma sayansi na kila elimu itakayompa binadamu ufanisi. Lakini kuhimiza ni kitu kingine na kuwa ni kitabu cha elimu hiyo ni kitu kingine. Katika ambayo yanatia nguvu na kuunga mkono kwamba Quran ni kitabu cha uongofu, sharia, na maadili mema, na kwamba Quran imeteremshwa kwa lengo hili, ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿هَـٰذَا بَصَائِرُ مِن رَّبِّكُمْ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ﴾
Hizi (Aya za Quran) ni dalili zitokazo kwa Mola wenu na ni uongofu na rehema kwa watu wanaoamini. (7:203).
Amesema tena:
﴿كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ لِتُخْرِجَ النَّاسَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ﴾
(Hiki) ni kitabu tulichokiteremsha kwako ili uwatoe watu katika giza uwapeleke kwenye nuru. (14:1).
Na Mtume mtukufu(s.a.w.w)
anasema:Hakika hapana jingine, nimetumwa kutimiza tabia njema
.
Na amesema Amirul Muminin
katika hotuba ya 174, ya Nahjul-Balagha:
Hakika Quran ni dawa ya ugonjwa mkubwa sana wa kufuru, unafiki na upotevu.
Kwa maneno haya tunapata tafsiri ya Aya isemayo:
﴿وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا ﴾
Na tunateremsha katika Quran yale ambayo ni ponyo na rehema kwa wanaoamini, wala hayawazidishi madhalimu ila hasara tu! (17:82).
Kama utauliza mara ya pili: Unasemaje kuhusu Aya hii.
﴿مَّا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِن شَيْءٍ﴾
Hatukupuuza kitabuni kitu chochote, (6:38)
si inafahamisha kuwa katika Quran kuna elimu zote?
Jawabu
: Kutosha kila kitu huwa ni kulingana na mahitaji. Ukisema: Nyumba hii ina kila kitu; itafahamika kwamba ina mahitaji ya mwenye kukaa humo. Kama ukisema: Kitabu cha Fiqh kina kila kitu, itafahamika kuwa mna masuala yote ya kifiqh. Quran ni kitabu cha dini. Kwa hiyo pale Mungu aliposema. Hatukupuza kitabuni kitu chochote, maana yake ni kila kinachoambatana na heri ya mtu na uongofu wake. Swali la tatu: Unasemaje kuhusu vitabu hivi vyenye majina kama: Quran na Sayansi, Uislamu na tiba ya kisasa, na vingenevyo?
Jibu
:Kwanza
: kabisa, kila anayejaribu kulinganisha kati ya uvumbuzi wa kielimu wa kisasa au wa kizamani na Qurani, atakuwa anajaribu jambo lisilowezekana. Kwa sababu elimu ya binadamu ina mpaka kulingana na nguvu yake ya kiakili; na Quran ni elimu ya Mwenyezi Mungu ambayo haina mpaka. Itakuwaje kitu kilicho na mpaka kiafikiane na kisichokuwa na mpaka?
Pili
: elimu ya binaadamu inaingiliwa na makosa. Kwa sababu inakuwa ni dhana na makisio; inakosea na kupata. Mara ngapi tumewaona wataalamu wakikongamana juu ya nadharia fulani na kudai kuwa ni kweli mia kwa mia; kisha wao wenyewe au wale watakaokuja baada yao wanagundua kuwa ni makosa mia kwa mia? Quran ni yenye kuhifadhiwa na makosa. Itakubalika vipi kuoanisha chenye makosa na kile kisicho na makosa? Kisha je tuendelee kugeuza Quran kila yanapogeuka makisio ya elimu na nadharia zake? Hapana. Ndio! hapana ubaya kujisaidia na ugunduzi wa kielimu katika kufahamu baadhi ya Aya, lakini kwa sharti ya kutoufanya huo ugunduzi kuwa ni kipimo cha ukweli na kusihi Quran, bali hata kutozifanya hizo elimu kuwa ndio nyezo za kufahamu siri ya Quran na kufahamu hekima ya baadhi ya hukumu zake.
Inawezekana kuwa hili ndilo lililowafanya watungaji kutunga vitabu kama: Quran na Sayansi n.k. Vyovyote iwavyo, sisi tuna yakini kwamba tuna hoja zenye nguvu katika dini yetu, na tuna dalili za kutosha juu ya ukweli wake; hatuna haja kabisa na vilivyo kwa wengine. Bali tunaamini kwamba wengine ndio walio na haja kwetu katika hilo. Kwa hakika historia ya binadamu haitapata dini yenye utengeneo zaidi ya dini ya Kiislamu, wala kitabu chenye kunufaisha zaidi ya kitabu chake, au Mtume mtukufu zaidi ya Mtume wake. Na yule ambaye hakuongoka kwa dalili za Quran na mwito wake wa maisha mema, basi hataweza kukinaishwa na ugunduzi wa kisayansi wa sasa au wa zamani.
Kuna kitu nilichokifikiria ambacho huenda kikapunguza machovu ya msomaji kuhusu majibu ya yule anayejaribu kuilinganisha Quran na ugunduzi wa sayansi; kama ifuatavyo:
Uzayr alipita katika mji uliokufa, akiwa na punda wake, chakula chake na kinywaji chake akastaajabu na kusema:
﴿ أَنَّىٰ يُحْيِي هَـٰذِهِ اللَّـهُ بَعْدَ مَوْتِهَا﴾
Mwenyezi Mungu atauhuisha vipi (mji) huu baada ya kufa kwake? (2:259).
Mwenyezi Mungu akataka kuuondoa mshangao wake. Akamfisha miaka mia. Chakula na kinywaji alichokuwa nacho, kilibakia katika hali yake bila ya kuharibika katika muda wote huo. Kisha Mwenyezi Mungu akamfufua na akataka kumwonyesha miujiza yake ya ajabu, akamwambia:
﴿ فَانظُرْ إِلَىٰ طَعَامِكَ وَشَرَابِكَ لَمْ يَتَسَنَّهْ﴾
Tazama chakula chako na kinywaji chako hakikuharibika (2:259).
Hebu angalia msomaji! Je,chakula cha Uzayr kilikuwa katika jokofu (friji)? Swali hili linamhusu mwenye kuilinganisha Quran na elimu ya kisasa.
Hakuna anayetia shaka kwamba jokofu hili ambalo lilihifadhi chakula na kinywaji kwa muda wa miaka mia, pengine linaweza kuwa ni sampuli ya mwaka 2000, na wala siyo ya mwaka 1967. Ndio! Inawezekana kulinganisha sayansi na kufahamu maana ya Quran tukufu; hasa kwa upande wa nadharia ya relativity (uwiano). Kwa vile kufahamu kunahusika na upande fulani katika maana yake, na kunatofautiana na hali ya anayesoma au anayesikiliza.
Kama mtu akisema kuwa tofauti hii haihusiki na Quran peke yake, kwa sababu nadharia ya uwiano ni ya jumla, isiyokubali kuhusishwa, tutajibu: Hiyo ni sawa, lakini maana ya Quran yamejiandaa na hilo. Na hili linatilia nguvu maelezo yetu kwamba mtu mwenye kuganda na kauli za wafasiri bila ya kuongeza kitu, atakuwa na akili ya kusoma tu, lakini sio akili ya mwamko. Basi twamuomba Mwenyezi Mungu azijaalie fahamu zetu katika Aya zake kuwa ni za mwamko na sio fahamu za kunakili.
Wamchao Mwenyezi Mungu Maana ya neno kucha (takua) kilugha ni kujichunga na kitu chochote. Na maana yake kisheria ni kujikinga na hasira za Mwenyezi Mungu na adhabu Yake, kujikinga na kuuacha wajibu na kutenda haram. Amesema Amirul Mumini Ali
:Kumcha Mwenyezi Mungu ndio msingi wa tabia njema.
Wengine wamesema:kumcha Mwenyezi Mungu ni kuwa Mwenyezi Mungu asikuone na lile alilokataza na kutoacha alilokuamrisha.
Kumcha Mungu ndiko kunakomfanya mtu kuwa bora mbele ya Mwenyezi Mungu.Quran inasema:
﴿ نَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴾
Hakika Mtukufu wenu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchae Mungu zaidi. (49:13).
Unaweza kuuliza, ikiwa wenye kumcha Mungu ni wenye kuongoka, basi wana haja gani ya kuongozwa? Je mwanachuoni anahitaji wa kumfundisha? Jibu: Hakika mwalimu hufundisha wanafunzi wote wajinga na wenye akili, lakini wale wanaonufaika na mwalimu ni wale wenye akili wanaojitahidi
ambao mwisho wao utakuwa ni kufaulu. Kwa hivyo ni sawa tukisema kuwa mwalimu ni wa wenye kufaulu. Vile vile Quran tukufu imewaeleza watu wote, lakini wanaonufaika nayo ni wale waumini wenye kumcha Mungu. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿ وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ ﴾
Na wale wanaokubali kuongoka Mwenyezi Mungu anawazidishia uongofu. (47:17)
WANAOAMINI GHAIBU
MAARIFA
Inasemekana kuwa mwanachuoni mmoja mkubwa aliyekuwa na heshima na cheo kikubwa huku watu wakimzunguka kwa kumuuliza maswali na kumnyenyekea, alionewa kijicho na mpinzani wake mmoja. Akamuuliza swali la kutatiza kwa sauti kubwa, ili wote wasikie. Mwanachuoni akasema: Sijui. Muulizaji akasema: Mahali ulipo ni pa anayejua sio pa asiyejua. Akasema mwanachuoni: Ole wako! Hapa ni mahali pa anayejua kitu sio kila kitu; anayejua kila kitu hana mahali.
Ndio! ni muhali kwa mtu kujua kila kitu. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿ وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا﴾
Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu. (17:85).
Hakuna mtu yeyote anayezaliwa na ujuzi, isipokuwa hupata maarifa muda baada ya muda, kutokana na sababu fulani; hata hilo jina lake pia halijui, isipokuwa baada ya kuitwa mara kwa mara. Wajuzi wa fani ya maarifa wametaja sababu nyingi za maarifa ambazo ni:
1. Kujua kutokana na hisia tano: Kujua rangi kwa kuona, sauti kwa kusikia,harufu kwa kunusa, ladha kwa kuonja na ugumu kwa kugusa. Vile vile kuna yale anayoyahisi mtu kwa hisia za kindani; kama njaa, shibe, mapenzi na chuki.
2. Kupata maarifa kutokana na uchunguzi na majaribio.
3. Kujua kwa misingi ya kikawaida; yaani kushirikiana na kukubaliana akili zote; mfano: Moja na moja ni mbili; na chenye kunufaisha ni bora kuliko chenye kudhuru. Au kujua kutokana na majaribio; kwa mfano kuamua kwamba kila kipande cha chuma ni kigumu, baada ya kujaribu kipande kimoja tu. Kwa hiyo hukumu inaenea kwa vyuma vyote lakini maarifa yametokana na majaribio ya kimoja.
4. Kujua bila ya kupata maalumati yoyote ya hisia, majaribio au nguvu ya akili; bali kupata moja kwa moja. Hilo ni baada ya jitihadi ya kuitakasa nafsi na uchafu; kama wasemavyo masufi. Kwa ufasaha zaidi ni kwamba moyo mbele za msufi ni kama akili kwa wengine. Kama ilivyo akili kutambua baadhi ya vitu vingine kwa kujitahidi na kuangalia vizuri, basi hivyo hivyo moyo nao hutambua baadhi ya vitu bila ya jitihadi ya nafsi; kama kuhisi mapenzi, na chuki. Na hutambua vitu vingine baada ya jitihadi ya nafsi; kama kujua kuweko Muumbaji.
Kwa hiyo jitihadi ya akili kwetu sisi inafanana na jitihadi ya nafsi kwa masufi. Wala hakuna yeyote anayeweza kubishana na sufi katika maoni yake na itikadi yake. Kwa sababu ukimuuliza dalili, atakujibu kwamba imani yangu na elimu yangu inatoka katika dhati yangu peke yake. Na kama ukimuuliza: Kwa nini imani na elimu hii haitokei katika dhati za watu wote? Atakujibu: Kwa sababu wao hawakupitia majaribio ya kiroho niliyoyapitia mimi.
Sisi tunajiweka kando na msimamo wa kisufi, bila ya kufungamana na upande wowote. Hatuwezi kuuthibitisha, kwa sababu tuko mbali na tunavyoelewa na tulivyozowea. Pia hatuwezi kuukanusha, kwa sababu mamia ya
wanavyuoni katika kila zama hata katika zama zetu wanaamini kuwako nguvu ya usufi; na kutofautiana kwao kihali, kidini , na hata kilugha.Hatuna hoja yoyote inayokanusha majaribio ya kiutu kabisa. Inawezekana kuwa majaribio ya kisufi yanafanana na vipindi ambavyo anapata ilham (anafunukiwa) mshairi na msanii, lakini jambo hili linamuhusu yeye peke yake; wala hana hoja kwa mwingine.
GHAIBU (YASIYOONEKANA)
Kuna vitu ambavyo hakuna njia ya kuvijua kwa hisia, majaribio au nguvu ya akili, kama vile Lawhin Mahfudh (ubao uliohifadhiwa), Malaika, Iblis, Hisabu ya kaburi, Pepo na Moto.Vile vile miujiza ya Mitume; kama fimbo kugeuka kuwa nyoka, kufufua watu, n.k. Akili haiwezi kugundua mambo hayo wala hatujayaona. Yote hayo ni makusudio ya ghaibu katika neno lake Mwenyezi Mungu: wanaamini ghaibu.
Kwa hiyo ghaibu ni ile ambayo haijulikani isipokuwa kwa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia katika ulimi wa ambaye umethibitika Utume wake. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿ وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ﴾
Na kwa Mwenyezi Mungu ziko funguo za siri hapana azijuaye ila Yeye (6:59)
Kwa hali hii, inatubainikia kuwa kuamini ghaibu ni sehemu ya Uislamu, na kwamba asiyeiamini sio Mwislamu.
Vile vile inabainika kuwa jambo ambalo halijulikani kwa kuona, majaribio au akili; au lisilosimuliwa na Kitabu cha Mwenyezi Mungu wala mapokezi ya Mtume, basi litakuwa ni katika vigano. Na vigano vingi vinatokana na mapokezi ya Mayahudi na mfano wao.