8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA
AL - BAQARAH (NG’OMBE)
﴿وَإِن كُنتُمْ فِي رَيْبٍ مِّمَّا نَزَّلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّن مِّثْلِهِ وَادْعُوا شُهَدَاءَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴾
23. Na ikiwa mna shaka kwa (hayo) tuliyomteremshia mtumwa wetu, basi leteni sura moja iliyo mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnasema kweli.
﴿فَإِن لَّمْ تَفْعَلُوا وَلَن تَفْعَلُوا فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ ﴾
24.Na msipofanya, na hamtafanya, basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, uliowekewa makafiri.
﴿وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ كُلَّمَا رُزِقُوا مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقًا قَالُوا هَـٰذَا الَّذِي رُزِقْنَا مِن قَبْلُ وَأُتُوا بِهِ مُتَشَابِهًا وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴾
25.Na wabashirie walioamini na wakafanya vitendo vizuri, kwamba watapata mabustani yapitayo mito chini yake; kila mara watakapopewa matunda humo kuwa riziki, watasema: Haya ndiyo yale tuliyopewa mwanzo, kwani wataletewa hali yakuwa yamefanana na humo watapata wake waliotakasika; na watakaa milele humo.
LETENI SURA
Aya 23-25
Kama ambavyo Quran imeongoza njia ya kujua kuweko Mwenyezi Mungu Mtukufu vilevile imeongoza njia ya kujua utume wa Muhammad(s.a.w.w)
miongoni mwazo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyomteremshia mtumwa wetu, yaani Muhammad(s.a.w.w).
Basi leteni sura moja iliyo mfano wake.
Makusudio yake ni kushindwa kuleta mazungumzo yaliyo mfano wa Quran, wakiwa wao ndio mabingwa katika fasihi na shughuli yao kubwa ni fasihi, lakini si lazima walete yale yanayolingana nayo kwa idadi na umbo. Walipewa hiyari,wakipenda walete yote; Sura kumi au Sura moja. Vile vile hawakulazimishwa kuleta mfano wa maana yake katika kanuni za tabia, misingi ya sharia na habari za ghaibu, bali walitakiwa walete wanayoyaweza katika maana yoyote na lengo lolote mradi tu ubainifu wake uwe kama wa Quran.
Matakwa haya, kama unavyoyaona yasingeliwashinda kama ingelikuwa Quran haitoki kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu wao hawakutakiwa wainue jabali au wakaushe bahari, isipokuwa walitakiwa maneno tu. Na wala hakuna kitu rahisi kama hicho kwao. Kwa hivyo kulipothibiti kushindwa kwao, imethibiti kwamba kuna siri fulani na wala hakuna tafsiri ya siri hii isipokuwa wahyi na Utume.Vilevile kila linaloshinda kutafsiriwa katika elimu halina budi kutafsiriwa na lile lililo juu ya maumbile. Hakuna kitu chenye nguvu zaidi katika kufahamisha ukweli wa Quran kuliko mkatao huu wa kauli yake Mwenyezi Mungu: Na hamtafanya mpaka hivi leo hajafanya yeyote baada yao. Na mlango bado umefunguliwa kwa anayetaka kujaribu mpaka mwisho.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuwataja makafiri na adhabu ya moto waliyo nayo, amefuatisha kuwataja waumini, neema na thawabu; kama ilivyo desturi ya Quran, kukutanisha mapendekezo na vitisho na ahadi na kiaga kikali, kwa kusisitiza mwongozo na mawaidha. Wafasiri wengi wamesema kuwa dhamiri katika neno,Mfano wake inarudia Quran; yaani mfano wa Quran, kwa maana ya kuwa leteni sura iliyo na sifa za Quran na muundo wake.
Wengine wamesema, bali hiyo dhamiri inarudia mja wetu; yaani mfano wa mja wetu ambaye ni Muhammad(s.a.w.w)
. Kwa maana ya kuwa mleteni Ummiy (mtu asiyesoma),kama Muhammad, aweze kuleta mfano wa Quran hii ambayo ameileta mtu huyu Ummiy.
Maana zipo sawasawa kwa kauli zote mbili ingawaje kauli ya kwanza ndiyo mashuhuri na dhahiri zaidi, ambapo Mwenyezi Mungu amesema: Ikiwa mna shaka kwa tuliyomteremshia...Na wala hakusema; ikiwa mna shaka katika Muhammad(s.a.w.w)
. Hata hivyo kauli ya pili ina maana yenye nguvu, kwani lau yakadiriwa kuwa mtu mwenye uwezo analeta mfano wa Quran lisingelikuwa hilo ni ushindi. Kwa sababu wajihi wa kushinda unakuja kwa kuletwa na asiyesoma (Ummiy) sio kwa mjuzi mwenye uwezo.
Makusidio ya kuni ni chochote kinachowashiwa moto. Watu ni wale waasi, na mawe ni masanamu waliyokuwa wakiyaabudu washirikina.
SIRI YA MUUJIZAWA QURAN
Utume ni ubalozi kati ya Mwenyezi Mungu na viumbe Wake, anamhusisha nao anayemtaka katika waja wake ili awafikishiye yale wasiyoweza kuyajua; Mwenyezi Mungu amempa nguvu kila Mtume kwa ubainifu ulio wazi juu ya ukweli wa utume wake, ili iwe ni hoja kwa wale waliopelekewa Mtume. Sharti la msingi la ubainifu huo, ni kuwa uwe katika namna maalum inayodhihiri katika mkono wa Mtume na sio mwingine. Hiyo ni kwa kuchukuwa hadhari ya kutatizika kati ya Mtume na asiyekuwa Mtume. Muhammad(s.a.w.w)
naye ana ubainifu na dalili juu ya utume wake. Miongoni mwa dalili zake ni hii Quran ambayo nakala zake zimeenea kila mahali na Aya zake zinasikika katika vipaaza sauti na katika idhaa za radio mashariki na magharibi, hata Israel.
Njia inayofahamisha kwamba hiyo Quran imeshinda, ni kuwa kila mkanushaji alishindwa na anaendelea kushindwa kuleta kitu kama Quran au kuleta Sura kama hiyo. Haijanakiliwa habari kuwa kuna mtu aliyeweza kuanzia zamani hadi sasa; ingawaje wapinzani na maadui wa Uislamu na Waislamu ni wengi. Kwa hiyo kimsingi kuthibiti muujiza ndio kuthibiti kwa Utume wa Muhammad(s.a.w.w)
.
Baada ya wanavyuoni kuafikiana kwamba Quran ni muujiza wametofatiana katika njia ya muujiza wenyewe na siri yake. Je, ni maajabu na uzuri wa muundo wake? Au ni madhumuni yake mkusanyiko wa elimu, kanuni za sheria na kutolea habari mambo ya ghaibu, n.k.? Au ni mambo yote mawili pamoja?
Wamerefusha maneno katika kubainisha wajihi wa muujiza na kuweka vitabu mahsusi. Sitaki kurefusha yale yaliyosemwa, nafupiliza yale niliyoyaona yana mwelekeo. Kwa ufupi ni kwamba mtu anaweza kumwiga mtu aliye mfano wake kwa kauli na vitendo. Lakini kumwiga Muumba wake katika athari yoyote miongoni mwa athari Zake, ni muhali. Kwa sababu mtu hawezi kupetuka mpaka wake akiwa kama muumbwa, vyovyote atakavyokuwa na nguvu au mkubwa. Ni vizuri kufafanua kama ifuatavyo:
KUSHINDA
Tumedokeza kwamba Muhammad aliwashinda wapinzani kwa Quran. Hapana shaka kwamba ushindi unatimu na unakubalika ikiwa kitendo chenyewe anakiweza mtu aliyekusudiwa kushindwa; Kama kumtaka mwenye mkono mzima auweke juu ya kichwa chake, au aondoe unyayo ard- hini. Lakini ukimtaka asiyejua kusoma asome na asiyekuwa tabibu atibu au asiyekuwa malenga atunge shairi, haitakuwa ni kushindwa. Muhammad(s.a.w.w)
amewashinda wapinzani jambo wanaloliweza (maneno) likawashinda, na kushindwa kwao huko kumeongezea Quran sifa ya muujiza. Unaweza kuuliza: Je, muujiza wa Quran ni kwa yule fasihi wa lugha ya Kiarabu au asiyejua Kiarabu au mtu dhaifu?
Jibu:Quran ni muujiza kwa kuwa ni maneno ya Mwenyezi Mungu bila ya kumwangalia fasihi na asiyekuwa fasihi, isipokuwa tunajua kwamba ni muujiza kwa kushindwa mwarabu aliye na ufasaha; sawa, na tunapogundua bingwa wa kuogelea anaposhindwa kuogelea kwenye bahari ya mawimbi, kuwa ni kigezo kwamba mwingine asiye bingwa haiwezi bahari hiyo. Yaani ikiwa fasihi ameshindwa basi mwingine ndio kabisa. Kwa maelezo yetu sisi mafaqihi ni kwamba kushindwa kwa fasihi ni sababu ya kujua muujiza wa Quran na wala sio fungu au sharti lake.
JE, MUHAMMAD ANAMUUJIZAMWINGINE ZAIDI YAQURAN?
Wengine wanaona kuwa Muhammad(s.a.w.w)
hana muujiza mwingine isipokuwa Quran Ama mimi niko pamoja na wanaoamini kwamba miujiza yake haina ya idadi. K wa sababu hekima ya kiungu inapelekea kupatikana namna namna za miujiza kwa kutofautiana hali na watu; kama ilivyofanya hekima yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ya kuapizana Mtume wake na Wakristo wa Najran. Hayo ni ikiwa mwenye kutaka muujiza anautaka kwa kusadikisha.
Ama mwongo mkaidi asiyetoshwa na chochote, anatoshewa na Quran tu. Kwa sababu muujiza wa Quran ni msingi wa yote, si wa wakati fulani wala na kundi fulani au mtu fulani. Mara nyingine hekima inataka kutoonyeshwa mtu muujiza kabisa; kama vile kutosheka kwa utambuzi na hisia tu, au kwa kuapa Mtume tu. Imekuja hadith kueleza kwamba mtu mmoja alimwambia Muhammad(s.a.w.w)
: Nina haja gani na muujiza? Apa tu kwa Mwenyezi Mungu, kwamba wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mimi nitakuamini. Mtume Akasema:Naapa kwa Mwenyezi Mungu mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu
. Yule mtu akasema: Nashuhudia kwamba hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Ambalo linatufahamisha kwamba miujiza ya Muhammad(s.a.w.w)
haina idadi, ni kwamba mtu wa dini zamani alikuwa akitoa dalili za Utume wa Mtume Muhammad(s.a.w.w)
kutokana na hadith za kusema na mawe, kujiwa na miti na kuchimbuka maji katika vidole vyake na watu walikuwa wakiyakubali wakati huo. Ama leo ambapo watu wamejitokeza katika maisha bora (na teknolojia), sisi twatoa dalili Utume wake kwamba yeye alisimama pamoja na wanyonge na kuwapiga vita wadhalimu. Na kwa fadhila zake na fadhila za sheria yake yalivuliwa mataji kutoka katika vichwa vya wastakbari na kutupwa chini ya miguu ya wachunga ngamia na zikagawanywa hazina za wafalme kwa mafukara na maskini.
Kwa vyovyote ilivyo ni kwamba miujiza yote ya Mtume mtukufu ni muhimu na mikubwa, lakini muhimu zaidi katika kukadiria kwangu ni mambo mawili:
Kwanza
: sheria ya Quran ambayo imepanga haki za watu na ufungamano wa watu kati yao juu ya misingi ya uadilifu na kusaidiana. Nitaonyesha kila kitu mahali pake Inshaallah.
Pili
: maapizano ya Mtume pamoja na ujumbe wa Najran, ambayo ameyataja Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika Sura ya Al-Imran (3).
Hakika maapizano haya ni dalili mkataa na ni mpaka wenye kupambanua, ambao unamweka mpinzani mbele ya adhabu na maangamizo ana kwa ana Maangamizo atakayoyateremsha Muhammad (s.a.w.) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa tamko moja tu linalotoka katika mdomo wake mtakatifu.
Hakika ushindi huu hauna mfano wake katika historia ya binadamu. Utakuja ufafanuzi mahali pake Inshaallah.Tumerefusha maneno katika msingi wa pili (Utume) ili uwe ni uthabiti wenye kuenea wa kila linaloambatana nao katika Aya. Nimetunga kitabu maalum kuhusu Utume nilichokiita Anubuwa wal-Aql (Utume na Akili), kimechapishwa mara nne.
﴿ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَسْتَحْيِي أَن يَضْرِبَ مَثَلًا مَّا بَعُوضَةً فَمَا فَوْقَهَا فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَيَعْلَمُونَ أَنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ وَأَمَّا الَّذِينَ كَفَرُوا فَيَقُولُونَ مَاذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِهَـٰذَا مَثَلًا يُضِلُّ بِهِ كَثِيرًا وَيَهْدِي بِهِ كَثِيرًا وَمَا يُضِلُّ بِهِ إِلَّا الْفَاسِقِينَ ﴾
26.Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kupiga mfano wowote wa mbu na ulio wa zaidi yake. Ama wale walioamini, wao hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyotoka kwa Mola wao; lakini wale waliokufuru husema: Nini analotaka Mwenyezi Mungu kwa mfano huu? Mwenyezi Mungu huwapoteza kwa mfano huo wengi na huwaongoza kwa mfano huo wengi na hawapotezi kwa (mfano) huo isipokuwa wale mafasiki.
﴿ الَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ اللَّـهِ مِن بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴾
27.Wanaovunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kwisha kuifunga na kuyakata aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu kuungwa, na kufanya ufisadi katika ardhi. Hao ndio wenye hasara.
HAKIKA MWENYEZI MUNGU HAONI HAYA KUPIGA MFANO WOWOTE
Aya 26 – 27
HAYA
Haya ikinasibishwa kwa mtu maana yake ni kubadilika hali yake ya tabia kuwa hali nyingine, kwa sababu fulani.Haya ya mtu inaweza kuwa nzuri au mbaya. Nzuri, ni ile kuona haya mtu kufanya mambo maovu na machafu. Kwa hivyo ndio ikawa inasemwa kwa yule anayefanya uovu bila ya kujali: Kama huoni haya fanya unavyopenda. Imam Jafar Sadiq
amesema;Hana haya asiyekuwa na Imani.
Ama ubaya wa haya, ni mtu kuacha kufanya yale yanayotakikana kwa kuogopa; kama vile mtu kuona haya kujifun-disha, kutafuta maarifa, n.k. Amirul Muminin amesema: Woga uko pamoja na kushindwa; kukosa huletwa na haya, na wakati unapita kama mawingu (ya kiangazi). Ilisemwa zamani: Hakuna haya katika dini.
Hiyo ni haya kwa upande wa binadamu. Ama ikinasibishwa kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.), inakuwa makusudio yake ni kuacha kitendo. Kama ilivyoelezwa katika hadith: Hakika Mwenyezi Mungu anamuonea haya mzee, yaani anaacha kumwadhibu.
Makusudio ya kupiga mfano ni kuiweka wazi fikra na kuondoa mikanganyo. Makusudio ya ahadi ya Mwenyezi Mungu ni hoja iliyosimama kwa waja wa Mwenyezi Mungu; ni sawa iwe matokeo ya hoja hiyo ni maumbile na akili au kunakili kwenye kuthibiti kutoka katika kitabu chenye kuteremshwa au kutoka kwa Mtume.
Makusudio ya kufunga hapa ni kukata na kuhukumu. Ahadi kubwa zaidi ya Mwenyezi Mungu iliyopitishwa ni kumfanya peke Yake na kumfanyia ikhlas jambo ambalo linafahamika kutokana na akili na kuthibitishwa na sharia.
Makusudio ya kukata aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu kuungwa ni maamrisho yake na makatazo yake. Kwa mujibu wa irabu za kinahaw (sarufi) inawezekana kuwa maana yake ni, Hakika Mwenyezi Mungu haachi kujaalia mbu kuwa mfano. Pia inawezekana, kuwa maana yake ni, Hakika Mwenyezi Mungu haachi kujaalia kitu chochote kuwa mfano, hata kama kitu hicho ni mbu.
UONGOFU NA UPOTEVU
Uongofu una maana nyingi; kama ifuatavyo:-
Kubainisha na kuongoza. Aya nyingi katika Quran zina maana hiyo; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
﴿ وَمَا مَنَعَ النَّاسَ أَن يُؤْمِنُوا إِذْ جَاءَهُمُ الْهُدَىٰ ﴾
Na hapana lililozuilia watu kuamini ulipowajia uongofu
(17:94)
Vile vile kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿ وَلَقَدْ جَاءَهُم مِّن رَّبِّهِمُ الْهُدَىٰ﴾
Hakika umewajia uongofu kutoka kwa Mola wao
(53:23)
Yaani; wala hapana ubainifu wa Mwenyezi Mungu isipokuwa ule waliokuja nao Mitume au uliohukumiwa na hukumu ya wazi isiyokuwa na shaka.
Kukubali mtu nasaha na kunufaika nayo; kama asemavyo Mwenyezi Mungu:
﴿ قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَكُمُ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ وَمَن ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا﴾
Sema: Enyi watu! Haki imekwisha wajia kutoka kwa Mola wenu, basi anayeongoka anaongoka kwa nafsi yake na anayepotea anapotea kwa nafsi yake.
(10:108).
Tawfiq na msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia mahsusi; kama anavyosema Mwenyezi Mungu:
﴿ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ﴾
...lakini Mwenyezi Mungu humuongoza amtakaye..
.(2:272)
Na kauli yake:
﴿ وَأَنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يُرِيدُ﴾
...na hakika Mwenyezi Mungu humuongoza amtakaye...
(22:16)
Yaani anamwafikisha kwenye amali kwa uongofu na kumwandalia njia ya kuendea. Kimsingi ni kwamba uongofu kwa maana ya ubainifu tu haulazimishi kuwafikisha kwenye amali; kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.):
﴿ لَّيْسَ عَلَيْكَ هُدَاهُمْ ﴾
Si juu yako uongofu wao.
(2:272)
yaani si juu yako wafanye amali kwa uongofu wako au wasifanye; isipokuwa ni juu yako kubainisha tu Thawabu; kama kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿ إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ يَهْدِيهِمْ رَبُّهُم بِإِيمَانِهِمْ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴾
Hakika wale walioamini na kufanya vitendo vizuri, Mola wao atawaongoza kwa sababu ya Imani yao; itakuwa inapita mito mbele yao katika mabustani yenye neema.
(10:9)
Yaani atawapa thawabu kwa sababu ya imani yao.
Mwenye Kuongoza na mwenye kubainisha, kwa kuangalia kwamba uongofu umepatikana kwa sababu yake.Hayo ndiyo makusudio katika Aya hii tunayoizungumzia. Amesema mwenye Majmaul-Bayan: Kauli yake Mwenyezi Mungu: Huongoza wengi kwa mfano huo,anakusudia wale ambao wameamini. Kwa kuwa uongofu umepatikana kwa sababu ya Mwenyezi Mungu, basi umetengenezwa kwake.
Hukumu; kama kusema: Kadhi amehukumu sawa sawa; yaani amehukumu kwa uadilifu wake. Maana haya yanafaa kuyanasibisha kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Upotevu, nao pia una maana nyingi: Miongoni mwayo ni haya yafuatayo:-
Kutia mashaka, kuingiza katika ufisadi na kuizuilia dini na haki. Maana haya hayategemezwi kwa Mwenyezi Mungu kwa hali yoyote; bal hunasibishwa kwa Iblis na wafuasi wake; kama asemayo Mwenyezi Mungu akimzungumzia Iblis, Firaun na Samiri:
﴿ وَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ﴾
kwa hakika nitawapoteza na nitawatamanisha...
(4:119)
﴿ وَأَضَلَّ فِرْعَوْنُ قَوْمَهُ وَمَا هَدَىٰ﴾
Na Firaun akawapoteza watu wake na hakuwaongoza.
(20:79)
﴿ وَأَضَلَّهُمُ السَّامِرِيُّ﴾
...Na akawapoteza Samiri
(20:85)
ADHABU
Aya nyingi katika Quran zimekuja kwa maana haya; kama vile:
﴿ كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّـهُ الْكَافِرِينَ ﴾
Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu huwapoteza makafiri
(40:74)
﴿ وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ﴾
...Na Mwenyezi Mungu huwapoteza madhalimu...
(14:27)
﴿ كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّـهُ مَنْ هُوَ مُسْرِفٌ مُّرْتَابٌ﴾
Kama hivyo Mwenyezi Mungu humpoteza aliyepita kiasi mwenye shaka
(40:34)
Yaani anawaadhibu waongo, makafiri na madhalimu.
Kukusudiwa jina la mpotezaji,kama kusema Amepotezwa na fulani Ukikusudia kumnasibisha kwenye upotevu na kumzingatia kuwa ni katika wapotevu.
Kujitenga mtu na nafsi yake. Mwenye kumpuuza mtoto wake bila ya malezi yoyote au usaidizi wowote,inafaa kuambiwa amempoteza mtoto wake.
Kupoteza kitu. Husemwa: Fulani amepoteza ngamia wake. Maana haya vile vile hayanasibishwi kwa Mwenyezi Mungu. Majaribio na mitihani, kwa namna ambayo hupatikana upotevu kwenye ubainifu ambao Mwenyezi Mungu humtahini mja wake. Mwenye Majmau anasema: Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu anawatahini kwa mifano hii waja wake, kwa hiyo huwapoteza watu wengi na huwaongoza watu wengi.
MAELEZO
Maana yanayopatikana kutokana na Aya mbili hizi ni kwamba Mwenyezi Mungu haachi kupiga mifano kwa vitu ambavyo wajinga wanaviona ni duni; kama buibui, nzi, mbu na wengineo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Muumba na Mola wa kila kitu; kwake bawa la mbu na ulimwengu mzima ni sawa tu.
Zaidi hayo kupiga mifano kunapatikana katika lugha zote ili kuziweka wazi fikra kwa kuzikutanisha na vyenye kuhisiwa. Kwa hivyo, kila linalohakikisha kupatikana kwa lengo hili linafaa kufanywa ni mfano, liwe dogo au kubwa; na kwalo inatimu hoja kwa kila mpinzani. Mwenyezi Mungu amewatahini watu kwa mifano hii, kama alivyowatahini kwa mambo mengine miongoni mwa dalili na ishara. Wengi wakaitumia na wengi wakapinga. Wale walioitumia ni wale wema walio waumini na waliopinga ni wale mafasiki waliopotea.
Kumesihi kuutegemeza uongofu na upotevu kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kuangalia kuwa Yeye ndiye aliyepiga mifano ambayo imekuwa ni rehema kwa aliyewaidhika na ni mateso kwa asiyewaidhika. Ni vizuri kuleta mfano ili kufafanua fikra hii: Mwanachuoni alipata elimu na ikamwinua, halafu akahusudiwa na hasadi ikadhuru kiwiliwili na akili yake; kama alivyosema Imam Ali
:Siha ya mwili ni husuda kuwa chache
. Inafaa kusema kuwa mwanachuoni huyu ndiye aliyemfanya hasidi kufanya uovu huu; au kama vile unavyosema: Uzuri wa mwanamke fulani umeharibu akili ya mwanamume fulani. Pengine wawili hao hata hawajuani.
Kwa mtazamo huu ndipo umenasibishwa upotevu kwa Mwenyezi Mungu kimajazi. Kwa vile Yeye ndiye aliyebainisha hoja na kuziweka wazi, na mhalifu alipozikhalifu akapotea. Lau Mwenyezi Mungu asingelibainisha, basi kusingekuwepo na suala la utiifu na uasi na asingelikuwako mpotevu na mwongofu. Mwenyezi Mungu amemwita yule asiyepata onyo kwa mifano: Fasiki, mvunja ahadi na mkataji wa yale aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu ya ungwe, ambayo ni kufuatilia mambo ya heri na kuungana na watu wa heri na mengineyo ya kusaidiana kwenye heri.
KUUMBA NA KUWEKA SHARIA
Mwenyezi Mungu ana matakwa mawili: Matakwa ya kuumba ibara yake ni Kun fayakun (kuwa na ikawa).Kwa matakwa haya kinapatikana ambacho hakikuweko. Matakwa ya pili, ni ya kuweko sharia ambayo yanakuwa katika ibara ya kuamrisha na kukataza na kulingania kwenye heri na kuacha shari. Mja akifanya heri huifanya kwa matakwa yake na hiyari yake bila ya kulazimishwa. Vile vile akifanya shari na kuacha heri.
Ikiwa utekelezaji wa hukumu zote za dini unafungamana na matakwa ya wale wenye kukalifiwa na hukumu hizo na hiyari, wala kusiweko mwenye kuwachunga isipokuwa wao wenyewe, basi itakuwa ni kosa kusema kuwa dini imeathiri katika kuanguka wafuasi wake na wenye kunasibika nayo. Ndio, lau wangeliitumia dini na wakaifuata kwa ukamilifu kwenye vitendo vyao, ingelifaa kufanywa dini ni kipimo cha kupanda na kuanguka kwao. Kwa hali hiyo basi ndio inabainika hasadi na chuki dhidi ya Uislamu katika kauli ya aliyesema; Unyonge wa Waislamu ni dalili ya unyonge wa Uislamu na mafundisho yake.
Kutokana na matamko ya mkosaji, inajuzu kwetu kunasibisha katika dini ya Kikristo kila ufasiki, uovu, na kuvunjiana heshima katika Ulaya na Amerika. Vile vile kunasibisha uharibifu wa vita vyote vilivyoathiri dola za Kikristo katika Mashariki na Magharibi ya dunia mpaka kulipuka bomu la Atomiki katika Hiroshima, na mabomu yaliyotupwa Veitnam; na hata kubadili maumbile 9 na kuongezeka idadi ya makosa na maovu siku baada ya siku katika Ulaya na Amerika mpaka kufikia hatua ya kuhalalisha ulawiti katika Uingereza kikanuni na kikanisa.
* 9 Sehemu kubwa ya Hiroshima na Nagasaki zilizopigwa bomu la Atomiki ardhi yake haimei kitu, na watoto wengi hadi leo huzaliwa na kasoro mwilini kutokana na athari ya bomu hilo - Mfasiri Je, yote hayo na mengi mengineyo yanafaa kunasibishwa kwa Masih (a.s.)? Hapana! Ametakasika na uchafu wote huu. Kama tungechukulia uzushi wa huyo mzushi, angelikuwa Myahudi wa Yemen ni sawa na Myahudi wa New York na Mkristo wa Misri ni sawa na wa Paris kimaendeleo.
Kuacha kuendelea miji kuna sababu nyingi sana zisizokuwa za dini; hasa ujinga, Historia ya kubakia katika unyonge na matatizo ya mazingira, na kukosa kuchangayika miji iliyoendelea na ile isiyoendelea.10 Lau kama si kuchanganyika Waislamu wa kwanza na mataifa mengine isingebaki athari yoyote ya maendeleo ya kiislamu. Naam! Uislamu ulikuwa ndio msukumo wa mchanganyiko huo.
Kwa ufupi sababu za kutoendelea hazitokani na tabia ya Uislamu wala ya Ukristo au wasiokuwa na dini, bali ni kutokana na hali za kijamii. Tutarudia kufafanua zaidi tutakapofika kwenye Aya za maudhui ya Jabri na Tafwidh (kutenzwa nguvu na kuachiwa). Na hayo tumeyaelezea kwa ufafanuzi katika kitabu Maalimul Falsafatul Islamiya na kitabu Maashiatul Imamiya.
* 10 Dini ni sawa na baraza la kutunga sharia. Ama utekelezaji ni wa mwingine. Umoja wa mataifa umefeli katika maazimio yake mengi muhimu na baraza la usalama nalo likafeli kuyatekeleza. Vile vile haikufaulu mikutano ya uongozi wa siasa zisizofungamana na upande wowote na wengineo. Mara ngapi wameshindwa, lakini lawama halikuwa lao. Sasa itakuwaje Uislamu ulaumiwe kwa sababu ya wanaoitwa Waislamu.