11
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA
AL - BAQARAH (NG’OMBE)
﴿ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَنِّي فَضَّلْتُكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ ﴾
47.Enyi wana wa Israil, ikumbukeni neema Yangu niliyowaneemesha, na nikawatukuza kuliko viumbe wengine.
﴿ وَاتَّقُوا يَوْمًا لَّا تَجْزِي نَفْسٌ عَن نَّفْسٍ شَيْئًا وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا شَفَاعَةٌ وَلَا يُؤْخَذُ مِنْهَا عَدْلٌ وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ﴾
48.Na iogopeni siku ambayo nafsi haitafaa nafsi kwa lolote.Wala hayatakubaliwa kwake maombezi (shufaa), wala hakitapokelewa kikomboleo; wala hawatanusuriwa.
WANAWA ISRAIL TENA!
Aya 47 - 48
MAELEZO
Enyi wana wa Israil ikumbukeni neema Yangu.
Aya hii inatilia mkazo Aya iliyotangulia, na ni maandalizi kwa yatakayokuja baada yake. Tutaonyesha katika sehemu itakayofuatia hekima ya kukaririka. Makusudio ya kukumbuka hapa ni kushukuru; yaani zishukuruni neema zangu kwa usikizi na twaa. Na nikawatukuza kuliko viumbe wengine.
Mwenyezi Mungu aliwafadhilisha kuliko mataifa mengine ya wakati huo. Herufi lam katika neno Alamin ni ya kuenea kwa kawaida, sio kuenea kwa kiuhakika. Inatosha kuwa ubora ni katika upande mmoja na sio pande zote. Upande ambao Waisrail wamepambanuka na watu wengine ni kwamba Mwenyezi Mungu aliwapelekea idadi ya Mitume; kwa mfano Musa, Harun, Yoshua, Zakaria na Yahya na wengineo. Wote hao ni Waisrail. Vyovyote ilivyo, kuwa bora kwao kwa watu wa zama zao kwa upande fulani, hakufahamishi kuwa bora katika kila upande kwa watu wa wakati huo; wala sio kwamba mtu wao ni bora kuliko mtu mwingine. Bali kule kuwa Mitume wengi wamekuja kutokana na kabila lao ni hoja juu yao na wala sio hoja yao, kwa sababu hilo linafahamisha kwamba wao walikuwa katika upotevu sana, ikawa kuna haja sana wapate waonyaji na wahadharishaji. Na ogopeni siku mbayo nafsi haitaifaa nafsi nyingine kwa lolote. Yaani kila mtu na lake hakuna dhahiri wala batini, hakuna kusaidiana wala kuoneana huruma.
﴿ يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ ﴾
Siku ambayo mtu atamkimbia ndugu yake.
(80:34).
Wala hayatakubaliwa kwake (hiyo nafsi) maombezi (shufaa), wala hakitapokelewa kikomboleo; wala hawatanusuriwa. Yaani Kiyama ni sawa na mauti, haufai usaidizi wowote, haitafaa fidiya yoyote, hata ikiwa ghali, wala haitazuia nguvu yoyote hata iwe kubwa kiasi gani. Hakuna chochote isipokuwa Rehema ya Mwenyezi Mungu:
﴿ لَئِن لَّمْ يَرْحَمْنَا رَبُّنَا وَيَغْفِرْ لَنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴾
Kama hataturehemu Mola wetu na kutusamehe, bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliopata hasara.
(7:149)
KUKARIRIKA KATIKA QURAN
Mara ya pili Mwenyezi Mungu anawaku-mbusha wana Israil neema Zake na amerudia baada ya Aya tano. Hiyo siyo Aya peke yake iliyorudiwa katika Quran, zimeka-ririka Aya nyingi hasa zile zinazofungamana na wana wa Israil pamoja na Musa
. Wengi hujiuliza sababu ya kukaririka Aya.Wameafikiana wafasiri kwamba hekima ya kukaririka ni kutilia mkazo. Baada ya kupita siku, wakuu wa vyama, wanasiasa, wafanyibiashara na wenye mashirika wamegundua kwamba, kukar-irika jambo ndio njia nzuri ya kulipendekeza, kulikinaisha na kulifanyia propaganda. Kwa ajili hiyo ndio wakaweka mitindo mbali mbali ya matangazo, kukawa na watu maalum wa kuhusika nayo na yakawa ghali sana.
Gustave Lebon anasema katika kitabu chake kiitwacho The man and his work: Mwenye kulikariri tamko mara kwa mara hulibadilisha kuwa itikadi. Dr Gibson katika kitabu kilichotarjumiwa kwa kiarabu kayfa tufakkir (Vipi utafikiri) anasema Ibara zina sumaku zinapokaririka mara kwa mara mbele ya macho yetu na masikio yetu, zinapumbaza akili zetu kabisa. Kwa hivyo basi Quran inakariri kwa mfumo mwingine pamoja na kuzidisha makemeo na mengineyo kwa kiasi cha hekima inavyotaka.
SHUFAA (UOMBEZI)
Hapana budi shufaa iwe na pande tatu: Mwenye kuombwa, mwenye kuombewa na muombezi ambaye anakuwa kati ya hao wawili, anaomba kwa yule wa kwanza ili amsaidie wa pili ni sawa apate idhini ya yule mwenye kuombwa au la. Hiyo ndiyo Shufaa kwa viumbe. Ama shufaa mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) maana yake ni msamaha na maghufira kwa mwenye dhambi; haitakuwa shufaa mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa idhini yake.
Amesema mwenye Majmaul-Bayan Shufaa kwetu ni yenye kuhusika na kuondoa madhara na kuondoa mateso kwa mumin mwenye dhambi. Muutazila na Khawarij wamekanusha Shufaa ya Muhammad(s.a.w.w)
kwa wenye madhambi makubwa katika umati wake, kwa maana hii tuliyoinakili kutoka kwa mwenye Majmaul-Bayan, lakini Imamiya na Ashaira wameithibitisha kwamba iko.Akili haihukumu kutokea Shufaa au kutotokea, lakini haioni pingamizi yoyote ya kupatikana. Kwa hiyo, kusihi kwake na kuthibiti kwake kutategemea kunakili kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ambaye kumemthibitikia kunakili huko, basi ni wajibu kwake kuamini Shufaa, na kama hakuthibitikiwa basi atasamehewa. Kwa hali hiyo inatubainika kuwa shufaa si msingi wa dini na kwamba mwenye kuikanusha na huku anamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi huyo ni Mwislamu bila shaka.
Tukirudi kwenye Aya za Quran tunakuta nyingine zinakanusha; kama ile inayosema:
﴿ يَوْمٌ لَّا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خُلَّةٌ وَلَا شَفَاعَةٌ ﴾
...Siku ambayo hapatakuwa na bishara wala urafiki wala Shufaa (uombezi)....
(2:254)
Hapo inaonyesha kukanusha Shufaa kabisa.Na Aya nyingine zinathibitisha kwa sharti; kama ile inayosema:
﴿لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ ﴾
....Hautafaa chochote uombezi (shufaa) wao isipokuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia. (53:26)
Tukiziunganisha Aya mbili hizi na tukazikusanya pamoja, natija itakuwa, Mwenyezi Mungu atakubali Shufaa kutoka kwa mwombezi baada ya kumpa idhini. Sio lazima kupatikana idhini ya Mwenyezi Mungu kwa jina la mmoja mmoja, bali inatosha tu kwa Mtume kujua kwamba Shufaa ni halali ikiwa yule mwenye kuombewa si katika wenye kuwakandamiza watu na kunyanganya riziki zao; bali ni katika watu wa kawaida tu, ambao wanafanya madhambi ya kawaida.
Kwa maneno mengine ni kwamba makusudio ya idhini ya Mwenyezi Mungu kwa Shufaa ni kumpa wahyi Mtume wake kwamba Mimi nimekuruhusu kuwaombea uwatakao katika Umma wako ambao wamefanya mad- hambi maalum. Hapo basi mambo ya hao wenye madhambi yatakuwa mikononi mwa Mtume(s.a.w.w)
; naye atamwombea yule mwenye kustahiki kuombewa. Imethibiti kwamba yeye amesema: Nimeuweka akiba uombezi wangu kuwaombea wenye madhambi makubwa katika Umma wangu.
Sisi tuna yakini kuthibiti Shufaa katika Uislamu.Lakini hatujui kwa ufafanuzi; wakati huo huo tunaamini kwa imani ya mkato, kwamba mwombezi bora wa mtu ni matendo yake, na kwamba kitakachowaombea wenye dhambi ni toba. Hakika Mwenyezi Mungu haweki kizuizi kwa mwenye kutaka kuokoka akiwa na ikhlasi na akakimbilia kwenye ukarimu wa Mwenyezi Mungu hali ya kunyenyekea.
﴿وَإِذْ نَجَّيْنَاكُم مِّنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَسُومُونَكُمْ سُوءَ الْعَذَابِ يُذَبِّحُونَ أَبْنَاءَكُمْ وَيَسْتَحْيُونَ نِسَاءَكُمْ وَفِي ذَٰلِكُم بَلَاءٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَظِيمٌ ﴾
49.Na tulipowaokoa kwa watu wa Firaun waliowapa adhabu mbaya; wakiwachinja watoto wenu wakiume na kuwaacha hai wakike; na katika hayo ulipatikana mtihani mkubwa uliotoka kwa Mola wenu.
﴿وَإِذْ فَرَقْنَا بِكُمُ الْبَحْرَ فَأَنجَيْنَاكُمْ وَأَغْرَقْنَا آلَ فِرْعَوْنَ وَأَنتُمْ تَنظُرُونَ﴾
50.Na tulipoitenga bahari kwa ajili yenu na tukawaokoa, na tukawazamisha watu wa Firaun na hali mwatizama.
NA TULIPOWAOKOA
Aya 49 - 50
LUGHA
Neno: Aal, lina maana ya kurudi; kwa hiyo kila mwenye kurudiwa kwa nasaba, rai au itikadi basi yeye ni Aal wa wale wanaomrudia, kisha likawa linatumiwa zaidi kwa maana ya watu wa nyumba ya huyo mtu atakayetajwa, lakini hawezi kuitwa mtu Al mpaka awe na utukufu fulani. Makusudio ya Al-Firaun hapa ni wafuasi wake ambao walikuwa wakiwatesa wana wa Israil kwa amri yake. Abu-Hayan Al-Andalusi (Mhispania) amesema: Katika tafsir yake kubwa Al-Bahrul Muhit; Firaun ni lakabu (msimbo) ya wafalme wa Misri wakati huo; kama vile Kisra wa Fursi, Kaizari wa Roma, Najashi wa Uhabeshi, Tubba wa Yemen na Khaqani wa Uturuki.
Lakini alhamdulillah misimbo hii yote imebakia kuwa ni vigano tu!
MAELEZO
Baada ya Mwenyezi Mungu kuwakumbusha neema zake kwao kwa ujumla, sasa anawakumbusha kwa ufafanuzi. Bora zaidi ya neema aliyoidokeza ni kuwaokoa na Firaun na wafuasi wake ambao waliwapa Mayahudi adhabu kali. Mwenyezi Mungu ameifasiri adhabu hiyo kwa kusema: wakiwachinja watoto wenu wakiume na kuwaacha hai wakike. Yaani wanawaua watoto wanaume na kuwaacha wanawake waje kuwafanya watumishi.
* 18 Mwenye Majmaul Bayan anasema: Firaun aliota mambo yaliyomtisha. Wakamfasiria makuhani kuwa atazaliwa kijana wa kiume kutoka kwa wana wa Israil ambaye atakuja muua, ndipo Firaun akawafanyia hivyo wana wa Israil. Zaidi ya hayo Wamisri walikuwa wakiwadhalilisha Wayahudi kwa kuwatuma kazi za kuvunja mawe, kuchimba mifereji na kazi nyinginezo za sulubu. Msemo umewaelekea Mayahudi waliokuwepo zama za Mtume Muhammad(s.a.w.w)
, kwa sababu wao walikuwa kwenye dini ya mababu zao na waliridhia amali zao. Na,mwenye kupenda amali ya watu wengine anakuwa ameshirikiana nao.
Na katika hayo ulipatikana mtihani mkubwa uliotoka kwa Mola wenu: Yaani, Enyi wana wa Israil, Mwenyezi Mungu amewatahini katika shida na raha, ili ijulikane kuwa je mtapigana jihadi na kuwa wavumilivi katika shida? Na je,mtashukuru raha? Au mtasalimu amri katika shida na mkufuru katika neema? Kwa hakika Mwenyezi Mungu hamtahini mtu ili ajue, la! Yeye anajua lenye kuwa kabla ya kuwa; isipokuwa yeye anamtahini mtu kwa ajili ya kusimamisha hoja juu yake. Kwani hakuna madai kwa asiyekuwa na hoja, hata kama yenye kudaiwa yanathibiti katika elimu ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Mwenyezi Mungu amewaonyesha Waisrail neema ya pili aliposema: Na tulipoitenga bahari kwa ajili yenu na tukawaokoa, na tukawazamisha watu wa Firaun
Yaani tulitenga bahari na tukafanya njia kumi na mbili kwa hisabu ya wajukuu. Wajukuu katika wana wa Israil ni koo katika kizazi cha Yaqub
Kwa ufupi Wayahudi walikuwa katika unyonge na udhalili wa hali ya juu; na adui yao alikuwa na nguvu za hali ya juu. Lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akabadilisha hali hiyo kupitia mikononi mwa Mtume wake Musa
, wao wakawa ndio wenye nguvu; na adui yao akawa dhalili, hilo wakaliona kwa macho yao; kama inavyosema Aya: Na hali nyinyi mnaangalia. Mwenyezi Mungu alimdhalilishia yule aliyewadhalilisha na akamwangamiza yule aliyetaka kuwaangamiza. Kwa hivyo basi wamelazimiana na hoja na imewalazimu kuwaidhika na kuzingatia, wala wasiwafanyie wengine yale waliyofanyiwa na wengine.
Lakini hivi leo mfano ule ule waliokuwa wakifanyiwa na Firaun ndio wanawafanyia Wapelestina. Na waendelee hivyo, lakini wajue hali itakuja wabadilikia tu, na yatawafika yale yaliyompata Firaun. Na waangalie ilivyokuwa kwa Nebukadnezzar na Warumi; na kwamba shujaa huvuma kisha akaisha. Jambo la kustaajabisha sana kwa mtu ni kwamba anapokuwa kwenye shida, kisha akaokolewa na Mwenyezi Mungu, basi hupetuka mipaka akafanya uovu na kusahau kila kitu. Wafasiri wengi wamesema, kwamba bahari iliyotajwa ni Bahari nyekundu (Red Sea).
﴿وَإِذْ وَاعَدْنَا مُوسَىٰ أَرْبَعِينَ لَيْلَةً ثُمَّ اتَّخَذْتُمُ الْعِجْلَ مِن بَعْدِهِ وَأَنتُمْ ظَالِمُونَ﴾
51. Na tulipomwahidi Musa masiku arobaini mkafanya ndama (kuwa Mungu) badala ya Mwenyezi Mungu mkawa madhalimu (wa nafsi zenu).
﴿ثُمَّ عَفَوْنَا عَنكُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴾
52.Kisha tukawasamehe baada ya hayo ili mpate kushukuru.
﴿وَإِذْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَالْفُرْقَانَ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ﴾
53.Na tulipompa Musa kitabu na upambanuzi ili mpate kuongoka.
NA TULIPOMWAHIDI
Aya 51 - 53
LUGHA
Neno: Musa kwa lugha ya Kiarabu lina maana ya: kifaa cha kunyolea nywele kilichotengezwa kutokana na chuma; lakini maana yanayokusuduwa kwa Musa bin Imran siyo ya Kiarabu, bali ni ya Kikibti ambayo ni matamko mawili: Mu lenye maana ya maji na Sa lenye maana ya mti. Kwa hiyo maana ya Musa ni maji ya mti, Ama maana ya kuitwa Maji ya mti, kama ilivyoelezwa katika Majmaul-Bayan, ni kwamba wajakazi wa Asiya(mke wa Firaun), walitoka kwenda kuoga wakakuta sanduku lililokuwa na Musa ndani yake baina ya maji na mti; wakawa naye.
MAELEZO
Baada ya Firaun kuangamizwa na Mwenyezi Mungu na waliokuwa pamoja naye, Waisrail Walipumua, wakarudi Misri wakiwa salama; kama livyoelezwa katika Majmau.Wakati huo, Tawrat ilikuwa bado haijateremshwa, wakamtaka Musa awaletee kitabu kutoka kwa mola wao. Basi Mwenyezi Mungu akamwahidi kumteremshia Tawrat na akamwekea wakati. Musa akawaambia: Hakika Mola wangu ameniahidi kitabu ambacho ndani yake mna ubainifu wa ambayo ni wajibu kwenu kuyafanya na kuyaacha. Akawambia wakati wake ambao ni masiku arobaini, na masiku hayo - kama ilivyosemwa - ni mwezi wa Dhul-Qaada, na siku kumi za mwezi wa Dhul- Hijja.
Musa akenda kwa Mola wake ili awachukulie watu wake kitabu; ndugu yake Harun akawa naibu wake. Kabla ya kwisha muda wa kuja Musa, walianza kuabudu ndama badala ya Mwenyezi Mungu, wakajidhulimu wao wenyewe.
Hiyo ndiyo maana ya dhahiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
Na tulipomwahidi Musa masiku arobaini mkafanya ndama (kuwa Mungu) badala ya Mwenyezi Mungu mkawa madhalimu ( wa nafsi zenu).
Baada ya Musa kurejea kwa watu wake, walitubia na wakarudi kwa Mola wao; Mwenyezi Mungu akawakubali toba yao, na hii ni neema ya tatu ambayo imeelezewa katika Aya:Kisha tukawasamehe baada ya hayo
.
Ama neema ya nne ni; kitabu cha Mwenyezi Mungu:Na tulipompa Musa kitabu na upambanuzi ili mpate kuongoka.
Kitabu chenyewe ni Tawrat; yenye kukusanya kila kitu kwa ajili ya kubainisha haki na batili, na halali na haramu.
Kunganisha kati ya neno, kitabu na kupambanua, ni kuunganisha sifa kwenye kile kinashosifiwa. Kwa muhtasari ni kwamba: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewakumbusha Waisrail katika Aya zilizotangulia, neema nne, Kuwaokoa kuchinjiwa watoto wao wa kiume na kuachwa wa kike wawe watumwa, kuangamia kwa Firaun, kusamehewa na kuletewa Tawrat.
Maelezo mazuri zaidi niliyoyasoma kuhusu maudhui haya, ni kauli ya Abu Hayan Al-Andulusi katika Tafsir Al -Bahrul Muhit; namnukuu: Tazama uzuri wa safu hizi ambazo zimepangika kwa mpango wa mtungo wa lulu na wa sayari katika falaki zake, kila safu katika hizo, yaani neema, imeishia kwa mnasaba wake na ikafikia daraja ya juu ya ufasaha ukitoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia mdomoni mwa Muhammad mwaminifu wake, bila ya kusoma kitabu chochote kabla yake, wala kuandika kwa mkono wake.
Abu Hayan anaonyesha kuwa mpangilio huo wenye kupangika vizuri ni katika miujiza ya Muhammad; kwamba yeye anauelezea bila ya kujifundisha. Mwenyezi Mungu awarehemu wahenga, awasamehe na awape neema nyingi. Kwani hakika wao hawakuona chochote chenye harufu ya kuitilia mkazo dini hii na Mtume wake mtukufu isipokuwa walikinyooshea shingo kwa pupa na shauku; wakafanya haraka kukisherehesha, kukifafanua na kukitolea dalili. Lakini tuko wapi sisi wanavyuoni wa sasa ambao twapupia zaidi dunia; hatuoni umuhimu wowote isipokuwa umuhimu wetu tu; wala matatizo isipokuwa matatizo ya watoto wetu tu! Tuko wapi sisi na hao watukufu waliojitolea kila kitu kwa ajili ya kuutukuza Uislamu na Mtume wa Uislamu? Mwenyezi Mungu awasamehe na awainue, na kila mwenye kuitumikia dini, kwenye daraja ya juu.
﴿وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ يَا قَوْمِ إِنَّكُمْ ظَلَمْتُمْ أَنفُسَكُم بِاتِّخَاذِكُمُ الْعِجْلَ فَتُوبُوا إِلَىٰ بَارِئِكُمْ فَاقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ عِندَ بَارِئِكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ إِنَّهُ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴾
54.Na Musa alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmejidhulumu kwa kufanya kwenu ndama (kuwa ni Mungu). Basi tubuni kwa Muumba wenu na jiueni; hilo ni bora kwenu mbele ya Muumba wenu.Basi akapokea toba yenu.Hakika Yeye ndiye apokeaye toba Mwenye kurehemu.
﴿وَإِذْ قُلْتُمْ يَا مُوسَىٰ لَن نُّؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ نَرَى اللَّـهَ جَهْرَةً فَأَخَذَتْكُمُ الصَّاعِقَةُ وَأَنتُمْ تَنظُرُونَ ﴾
55.Na mliposema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mungu waziwazi.Ukawanyakua ukelele na hali mwatizama.
﴿ثُمَّ بَعَثْنَاكُم مِّن بَعْدِ مَوْتِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴾
56.Kisha tukawafufua baada ya kufa kwenu ili mpate kushukuru.
﴿وَظَلَّلْنَا عَلَيْكُمُ الْغَمَامَ وَأَنزَلْنَا عَلَيْكُمُ الْمَنَّ وَالسَّلْوَىٰ كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ وَمَا ظَلَمُونَا وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴾
57.Tukawatilia kivuli kwa mawingu na tukawateremshia Manna na Salwa: Kuleni katika vitu vizuri tulivyowaruzuku.Na hatukuwadhulumu, lakini wamejidhulumu wenyewe.
MUSA ALIPOWAAMBIAWATU WAKE
Aya 54 - 57
LUGHA
Manna ni kitu fulani kinachonata mithili ya asali, na Salwa ni tombo (aina ya ndege wa jamii ya kware, kama kuku).
MAELEZO
Na Musa alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mumejidhulumu kwa kumfanya kwenu Ndama (kuwa ni Mungu). Basi tubuni kwa Muumba wenu. Maana yoyote inayofahamika kwa kusikia tu haihitaji tafsiri, bali kuifasiri na kuisherehesha ni ufedhuli tu! Na Aya hii iko katika hali hiyo.
Na jiueni Makusudio ya kujiua yako wazi, ni kujitoa roho: wala hapana haja ya kufasiri vingine, kwa maana ya kuhalifu mapenzi na kuidhalilisha nafsi kwa kukiri dhambi na makosa au kumwabudu sana Mwenyezi Mungu; kama ilivyosemwa. Makusudio ya kujiua hapa, ni baadhi wawaue wengine. Kwa hivyo yule ambaye hakurtadi dini yake kwa kuabudu ndama ndio atamuua yule aliyertadi dini yake. Sawa na kusema kwake Mwenyezi Mungu:
﴿فَإِذَا دَخَلْتُم بُيُوتًا فَسَلِّمُوا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ ﴾
...Mnapoingia katika majumba jitoleeni salamu....
(24:61).
Na vile vile kusema kwake
﴿وَلَا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ ﴾
...Wala msijikejeli: yaani msikejeliane
(49:11)
Amesema Tabrasi katika Majmaul-Bayan kwa upande wa Shia, na Razi katika Tafsir Al-Kabir, kwa upande wa Sunni, kuwa Mwenyezi Mungu aliijaalia toba yao ni huko kujiua, sio kwamba wajiue baada ya kutubia. Hukumu hii ina mfano wake katika sharia ya Kiislamu, pale ulipozingatia kuua kuwa ni hadi na adhabu ya kosa la kurtadi.Hilo tutalieleza katika kifungu cha kurtadi kinachofuatia. Zinaendelea Aya kueleza maovu ya Waisrail: Na mliposema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpake tumwone Mungu waziwazi Wakati Musa alipowaendea na Tawrat, baadhi yao walisema: Hatuamini kuwa kitabu hiki kinatoka kwa Mungu mpaka tumwone kwa macho; bila ya kizuwizi chochote kati yetu sisi na Yeye; na atueleze ana kwa ana kuwa Yeye amekutuma na kitabu hiki.
Sijui kama wale wanaokanusha kuwepo Mwenyezi Mungu wakati huu, kwa kuwa tu hawajamuona kwa wazi, wanategemea Waisrail na inadi yao? Au vipi? Mayahudi walimwambia Musa: Hatutakuamini mpaka tumwone Mungu. Hawa wa sasa nao wanasema: Hakuna chochote chenye kupatiana isipokuwa kile tunachoweza kukiona kwa jicho, kukigusa kwa mkono, kukinusa kwa pua au kukionja kwa mdomo. Hivyo ndivyo inavyokaririka historia ya picha ya upinzani wa haki katika kila kizazi.
Yakawanyakua mauti ya ghafla na hali mwalizania Yaani adhabu kutoka mbinguni iliwapata wale waliomwambia Musa hatukuamini mpaka tumwone Mungu wazi wazi, wakaangamizwa mbele ya macho ya wale wasiopinga. Kisha tukawafufua baada ya kufa kwenu ili mpate kushukuru. Baadhi ya wafasiri kama vile Muhamad Abduh, katika tafsiri Al-Manar, amesema: Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuwarudishia uhai mara ya pili baada ya kuchukuliwa na ukelele; na kwamba makusudio ya kufufuliwa kwao ni kizazi chao kuwa kingi. Wengine wakasema kuwa sio hivyo, hayo hayafahamiki kutokana na dhahiri yake ilivyo, na kwamba waliorudishwa ni wale wale waliouliwa na ukelele.Na hii ndiyo sawa, kwani hapana sababu inayolazimisha taawil, madamu kurudishwa kuwa hai kunawezekana kiakili. Na hilo lilimtokea Uzair, kama inavyofahamisha Aya:
﴿قَالَ أَنَّىٰ يُحْيِي هَـٰذِهِ اللَّـهُ بَعْدَ مَوْتِهَا فَأَمَاتَهُ اللَّـهُ مِائَةَ عَامٍ ثُمَّ بَعَثَهُ﴾
Akasema: Mwenyezi Mungu atauhuisha vipi (mji) huu baada ya kufa kwake? Mwenyezi Mungu Akamfisha kwa miaka mia, kisha akamfufua....
(2:259)
Kimsingi,lililotokea haliwezi kuwa muhali. Kwa hakika inaonyesha kwamba makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Yakawanyakua mauti ya ghafla, na kauli yake tukawafufua ni wale waliokuwa wakati wa Musa waliosema: Mpaka tumwone Mungu waziwazi Kwa hiyo, kauli haiwahusu Mayahudi waliokuwa na mtume, msemo umeele-kezwa kwao kwa kuangalia kuwa wanatokana na kizazi kilichosema hivyo.
Tukawatilia kivuli cha mawingu na tukawateremshia Manna na Salwa. Hayo yaliyotokea wakati Waisrail walipotoka Misri wakahangaika katika jangwa la Sinai, kusikokuwa na majengo; wakamlalamikia Musa kwa joto la jua; Mwenyezi Mungu akawaneemesha kwa wingu lililowafunika na kuwakinga na joto la jua kali. Vile vile Mwenyezi Mungu akawaneemesha kwa Manna na Salwa ili wale. Yatakuja maelezo katika tafsiri ya Aya ya 60 kuwa maji yaliwabubujikia kutoka katika jiwe alilolipiga Musa kwa fimbo yake. Inashangaza kuona baadhi ya wafasiri, wakifasiri yale aliyoyanyamazia Mwenyezi Mungu kuyabainisha; kama vile idadi ya waliojiua kwa toba ya kuabudu ndama, kuwa ni watu elfu moja; vile vile walionyakuliwa kuwa ni watu sabini. Ama kuhusu Manna, wanadai kila mtu alikuwa akipata pishi moja na kwamba Salwa ilikuwa ikishuka kutoka mbinguni ikiwa moto moto huku ikifuka moshi, na mengineyo ambayo hayana kauli yoyote iliyopokewa au kudhaniwa.
Imethibiti Hadith kutoka kwa Mtume mtukufu(s.a.w.w)
:Hakika Mwenyezi Mungu amenyamazia mambo si kwa kusahau, ni kwa kuwaonea huruma, kwa hiyo msijikalifishe nayo.
Katika Nahjul-Balagha amesema Imam Ali
:Hakika Mwenyezi Mungu amewafaradhisha faradhi msizipoteze, na amewawekea mipaka msipetuke; na ameyakataza mambo basi msifanye; na ameyanyamazia mambo si kwa kusahau, basi msijikalifishe (nayo).
Na hawakutudhulumu sisi, lakini wamejidhulumu wenyewe
.Kukanusha dhulma kwa Mwenyezi Mungu ni sawa na kukanusha kuwa na watoto na mshirika; yaani kumwepusha kabisa na hilo; sawa na kumwambia mseja kuwa hana mtoto. Ama kujidhulumu kwa Mayahudi ni kwa sababu ya usafihi wao na kuzikanusha neema za Mwenyezi Mungu ambaye hanufaiki na twaa ya mwenye kumtii wala hayamdhuru maasi ya mwenye kuasi na madhara ya uasi yanamrudia mwasi. Anasema Ali bin Abu Twalib (a.s.):Ewe mwanadamu ukiona Mola wako anaendelea kukuneemesha nawe unamwasi, basi mhadhari.
Kwa ufupi Aya hizi zinaonyesha ibada ya Waisrail kwa ndama, kutubia kwao kwa kujiua na kutaka kwao kumwona Mwenyezi Mungu. Vile vile kuangamia kwao na kufufuliwa kwao, kufunikwa na kiwingu na kulishwa Manna na Salwa.. Tutaelezea kisa cha Nabii Musa na Waisrail katika surah ya Maida (5) Inshallah. Waliposema kumwambia Musa:
﴿فَاذْهَبْ أَنتَ وَرَبُّكَ فَقَاتِلَا إِنَّا هَاهُنَا قَاعِدُونَ﴾
...Basi nenda wewe na Mola wako mkapigane sisi tutakaa hapa
(5:24).
Hilo ni tamko linaloonyesha ukhabithi na uduni wa Mayahudi. Wa kwanza waliogundua uhabithi na uduni wao ni watu wa Firaun ambao waliwachinja watoto wao wa kiume na kuwaacha wa kike. Kumwona Mungu Kutokana na Aya tukufu:Mpaka tumwone Mungu waziwazi.
Tutaonyesha mzozo uliopo katika madhehebu ya Kiislamu na tofauti zao kuwa akili inajuzisha kuonekana Mwenyezi Mungu kwa macho au la?!
Wamesema Ashari (Sunni): Hakika kuonekana Mungu kwa macho kunawezekana kiakili, kwa sababu Yeye yupo na kila kilichopo kinawezekana kuonekana.
Imamiya na Mu’utazila wamesema; Haijuzu kuonekana Mwenyezi Mungu kwa macho katika hali yoyote ile, si duniani wala akhera, kwa sababu Yeye si umbo hata akaonekana, wala haingii katika umbo wala upande fulani.
Baada ya akili kuthibitisha kutoonekana, wamechukulia kwamba ataonekana kiakili sio kwa macho na kwa hakika ya imani sio ya viungo vya mwili, kwa mujibu wa alivyosema mwanafalsafa mkubwa na mashuhuri, Muhammad bin Ibrahim Shirazi, maarufu kwa jina la Mulla Sadra. Katika aliyoyatolea dalili Mulla Sadra kuhusu kutoonekana, ni kauli yake: Kuhisi kitu ni hali inayozuka kwa kile kinachohisi kikikutanishwa na kinachohisiwa kilichozuka. Hivyo basi, kulazimisha kitu ambacho hakikuzuka kuwa kinahisiwa ni kama kulazimisha kitu kisicho na upande kuwa kina upande.
Kauli yake hii - kama ninavyoona - ni kwamba jicho haliwezi kuona kitu isipokuwa kwa sharti mbili:
Liwe linaweza kuona na kiwe kile kinachoangaliwa kinaweza kuonekana kwa jicho. Hilo ni jambo la msingi; likikosa jicho uwezo wa kuona, au kikiwa kitu hakina uwezo wa kuonekana; itakuwa kuona hakuko. Jicho ni dogo na duni zaidi kuweza kuona dhati tukufu; kama vile ambavyo, Mwenyezi Mungu ni mkubwa wa kuonekana na jicho. Nilipokuwa nasoma ibara hii, tukufu akili yangu ilienda kwa mwanafalsafa wa Kiingereza John Luk, anayesema kuwa: kitu kina sifa yake ya kwanza yenye kukithibitikia, ambayo haipambanuki nayo, ni sawa mtu aitambue au asiitambue; kama vile vitu vinavyosimamisha kitu hicho.
Vile vile kuna sifa ya pili ambayo haiwezi kuepukana na kuhisiwa au kujulikana; kama rangi, sauti na ladha. Rangi siyo sifa ya kitu, kama inavyoonekana, isipokuwa ni mawimbi ya kimwangaza yanayohusika kati ya kitu na jicho; kama wasemavyo wataalamu. Vile vile sauti ni mawimbi ya kihewa; na ladha isingekuweko kama si mdomo. Kwa hiyo ladha inahitilafiana kwa uzima wa mdomo na ugonjwa.Kwa ufupi anataka kueleza kuwa hakuna rangi bila ya jicho; wala sauti bila ya sikio; au ladha bila ya mdomo. Hakuna mwenye kutia shaka kwamba nuru ya Mwenyezi Mungu imezidi mawimbi ya kimwanga na mengineyo.Kwa hivyo yakikosekana mawimbi haya, ndio kumekosekana kuona.