2
MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU
SEHEMU YA PILI
MAISHA NA MAKAZI YA MTOTO
Mtume(s.a.w.w)
amesema: Yatosha kwa mtu kupata dhambi kwa kutowaangalia wanaomtegemea. Kuna maagizo kadhaa na misingi ya kanuni iongozayo, ambapo Uislamu unaamuru kwa jinsi gani maisha na maendeleo ya mtoto yalivyo lazima, na kwamba uzembe wowote ama kufanya ajizi katika kutimiza misingi hii ya kanuni ni kosa kubwa. Misingi hii imetolewa mfano kama ifuatavyo:
Amesema Mwenyezi Mungu: Wala msijiue. Amesema tena:
وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ ﴿١٥١﴾
..wala msiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha kuuawa ila kwa njia ya haki (6:151).
Amesema tena:
مَن قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الْأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا ﴿٣٢﴾
Mtu atakayemuua mtu bila ya yeye kuua, au bila ya kufanya ufisadi nchini, basi ni kama amewaua watu wote, na atakayeokoa maisha ya mtu, basi ni kama ameokoa maisha ya watu wote (5:32).
Amesema tena:
وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُم ﴿١٥١﴾
Wala ms iwaue watoto wenu (6:151). Amesema tena:
يُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُخَفِّفَ عَنكُمْ وَخُلِقَ الْإِنسَانُ ضَعِيفًا ﴿٢٨﴾
Mwenyezi Mungu anataka kukurahisishieni (mambo mazito) kwani mwanaadamu ameumbwa dhaifu. (4:28).
Amesema tena:
وَلْيَخْشَ الَّذِينَ لَوْ تَرَكُوا مِنْ خَلْفِهِمْ ذُرِّيَّةً ضِعَافًا خَافُوا عَلَيْهِمْ ﴿٩﴾
Na waogope (mawasii kuwadhulumu yatima, na wakumbuke) kama wao wangeacha nyuma yao watoto dhaifu wangekuwa na khofu juu yao. (4:9).
Amesema tena:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا ﴿٦﴾
Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu kutokana na moto. (66:6)
Amesema tena Mwenyezi Mungu:
وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ ﴿١٩٥﴾
Wala msijitie wenyewe katika maangamivu. (2:195).
Amesema Mtume(s.a.w.w)
:Yatosha kwa mtu kupata dhambi kwa kumtupa yule anayemtegemea.
1.
KUISHI KWA MTOTO
Uislamu unamchukulia mtu kuwa ni khalifa wa Mwenyezi Mungu duniani, imetajwa katika Qurani: Hakika nitaweka katika dunia hii khalifa (2:30).
Kwa hivyo, jambo lolote litakalomtia khalifa huyu kwenye aibu, fedheha, ama kudhoofisha uwezo wake, limekatazwa na sheria ya Kiislamu.
Na hii ni kwa sababu ya kuhifadhi heshima na daraja ya mwanaadamu aliyopati- wa akiwa kama khalifa wake duniani. Mwenyezi Mungu amempa uwezo binaadamu kuwa na fahamu za kujua mambo bila ya kufundishwa, nguvu za ulinzi za kuweza kujihami, na kumwezesha kupata kudumu kwa ulimwengu. Pia Mwenyezi Mungu amempa mwanaadamu undani wa maarifa, na amemtukuza zaidi ya viumbe vyote vilivyosalia. Miongoni mwa uwezo aliopewa mwanaadamu ili kukabiliana na vitisho ni uwezo wa kujihami.
Uangalifu wa Uislamu kuhusiana na maisha ya mtoto na ulinzi wake, tayari wenyewe una mamlaka kwenye jamii ya kiislamu kimwili au kiroho, kwa sababu uangalifu huu unazalisha miili imara yenye siha. Kuwa na miili yenye afya katika Uislamu hakuleti natija ya nguvu ya kiakili tu, bali pia uhakika, mafanikio na matumaini katika kushughulika na maisha na watu. Ni kwa sababu hizi ndipo Uislamu umekusanya taratibu zifaazo za kujikinga, ili kuyahifadhi maisha ya waislamu na kuwaongoza katika njia yenye utaratibu na iliyopangwa katika maisha yao yote. Afya ndiyo neema bora kuliko zote alizotunikiwa mwanaadamu baada ya kuwa muislamu, kwani bila ya kuwa na afya huwezi kufanya kazi na kuweza kumtii Mungu sawasawa, kwa hivyo, hakuna chochote kinachoweza kulinganishwa nayo.
Imetajwa na Tirmidhy, kutokana na Abu Huraira ya kwamba Mtume(s.a.w.w)
amesema: Kitu cha kwanza atakachoulizwa mwanaadamu Siku ya Kiyama, kutokana na neema alizopewa ni: Je mwili wako, sikuupa afya? (uliifanyia nini?)
2.
JUKUMU LA WAZAZI HUKO AKHERA, NA MATUNZO YA WATOTO
Inasadikiwa ya kwamba, kulingana na maumbile na hisia za binaadamu, anaweza kuepuka hali zinazotishia (maisha yake). Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu amemuumbia mwanaadamu nguvu ya kiasili inayomlinda kutokana na hatari hizo. Licha ya hivyo, Uislamu umeipa uwezo nguvu hiyo, na umemkumbusha mwanaadamu aitumie kwa kujihami na kwa kuongozea mikakati ya ulinzi kwa ajili ya maisha yake. Kwa hivyo inaonyesha wazi namna gani Uislamu ulivyoupa daraja ulinzi na kuuimarisha. Ulinzi kwa maana hiyo (ilivyotajwa hapa) ungeweza kuwa na maana ya ulinzi wa mwanaadamu hapo Akhera, ambao utamwokoa kutokana na moto na vitisho vya Siku ya Kiyama. Au ungeweza kuwa ni kujilinda kwa mtu kutokana na moto ambako kunamaanisha wakati huo huo, kuilinda familia yake.
Imetajwa katika Qur ani:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ﴿٦﴾
Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu (jamii) yenu kutokana na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe (66:6).
Aya hizo zilizotangulia zinawataka wacha Mungu waumini kujilinda na kujihami wao na jamii zao pia kutokana na Moto ambao kuni zake zitakuwa ni watu waovu. Kujilinda maana yake (hapa) inarejea kwenye kutenda amali njema, na kuwa na mwenendo mzuri, kumtii Mwenyezi Mungu na kujizuia na makatazo yake. Miongoni mwa matendo ya kujilinda kwa Akhera, ni kujizuia na maamrisho yote ya Mwenyezi Mungu, kuhusiana na chakula, kinywaji, mavazi, n.k.
Imetajwa katika Qur ani:
يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ ﴿٥١﴾
Enyi Mitume! Kuleni vyakula vilivyo vizuri (halali) na tendeni mambo mema, hakika Mimi najua yote myafanyayo. (23:51).
3.
JUKUMU LA WAZAZI MAISHANI NA MATUNZO YA MTOTO
Matunzo ya mtoto wakati wa maisha yake yanahusiana na kumkinga kutokana na magonjwa na maradhi yaambukizayo na yote yale yawezayo kumpata mtu kutokana na uzembe, na kutojihusisha. Imesema Qur ani:
Wala msijitie wenyewe katika maangamivu
(2:1 95).
Katika Aya iliyotangulia hapo juu, Mwenyezi Mungu amemkataza mwanaadamu kuchangia maangamivu yake mwenyewe kupitia kwenye vitendo ambavyo angevitenda kulingana na mwenyewe. Ijapokuwa mtu kujidhuru au kujiangamiza kunaonekana kwamba kunapingana na fikra zilizo timamu (yaani haiwezekani), lakini yaelekea kuwa kunaweza kutokea kutokana na uzembe ama kutojihusisha na kuchukua kinga zifaazo ili kuyachunga maisha yake mwenyewe.
Kujiangamiza hapa, haina maana tu ya maangamivu yanayosababishwa na kiu, nja a, au mtu mwenyewe kujitoa mhanga kwa njia moja au nyingine kutokana na madhambi ayatendayo. Kuangamia kwa maana hiyo, kunamaanisha kwamba kufanya ajizi kidogo tu, au kuzembea katika kujikinga, ndiko kujiangamiza. Kwa hivyo hii ni pamoja na mtu kujihatar isha na magonjwa, maradhi yaambukizayo, ukosefu wa chanjo kutokana na maradhi yauwayo, na ukosefu wa uangalifu wakati wa shida na hatari. Vitendo hivyo vyote vilivyotangulia kutajwa vinachukuliwa kuwa ni kumchangia mtu katika maangamivu yake mwenyewe.
Kwa sababu hiyo ndipo Uislamu ukaamuru kuchukua kinga zifaazo, na kutafuta matibabu kwa ajili ya magonjwa yote. Mtume(s.a.w.w)
amesema: Mwenyezi Mungu hakuweka maradhi ila ameleta na dawa ya kuyatibu.
4.
JUKUMU LA WAZAZI NA MAKUZI YA MTOTO
Sheria ya Kiislamu imewaamuru wazazi kuwa ni dhamana kwa maisha ya mtoto na makuzi yake. Kwa msingi wa kwamba, mtoto huchukuliwa kuwa ni dhamana waliyopewa, ambayo inapaswa kutunzwa nao kwani watakujaeleza mbele ya Mwenyezi Mungu (jinsi walivyoitunza amana waliyopewa). Mtoto mwanzoni mwa maisha yake huwa hajui hatari hasa ambazo zingehatarisha maisha yake. Kwa kuongezea ni kwamba yeye hawezi kujilisha na kuchunga maisha yake, kwa hivyo basi, ndipo Mwenyezi Mungu akawafanya wazazi kuwa ni dhamana kwa ajili ya kuwalinda watoto wao kutokana na magonjwa mbalimbali na hatari ambazo zingetishia maisha na makuzi yao.
Imetajwa katika Hadith:Kila mmoja wenu ni mchungaji na kila mmoja ataulizwa juu ya kile akichungacho.
Baba ni mlezi wa jamii yake. Mke ni mchungaji wa mali ya mu mewe na watoto wake, na ndiye atakayeulizwa kuhusu akitunzacho. Mtumishi ni mtunzaji wa mali ya tajiri yake na ndiye atakayeulizwa kuhusu mali aitunzayo. Ndiyo, kila mmoja wenu ni mchungaji na ndiye atakayeulizwa juu ya anachokiangalia. Mbali na kuwa ni d hamana, ni wajibu wao pia kuwalisha watoto wao na kuwatosheleza mahitaji yao, hii inaweza kuwa kwa kuwachagulia kwa njia nzuri chakula chao, na kuwalinda kutokana na maradhi yote yatakayowadhuru.
Miongoni mwa hatari zinazoweza kutishia maisha ya mtoto katika miaka yake ya mwanzoni ni uwezekano wa kupatwa na mojawapo ya maradhi yauwayo watoto kama: Ugonjwa wa kupooza (Polio), Surua (Ukambi), dondakoo (DPT au Diphtheria) n.k. Au upungufu wa maji mwilini uletwao na magonjwa ya kuharisha n.k. Magonjwa hayo yote yanaweza kumshambulia mtoto, kumlemaza na kumhuzunisha maisha yake na ya wazazi wake. Uislamu unatuonya vikali sana tusipuuze matunzo na matibabu ya watoto wetu kutokana na maradhi yauwayo watoto au mengineo. Kwa ajili hiyo, Uislamu unaamrisha waumini wake kuwa wenye nguvu na afya. Mtume(s.a.w.w)
amesema: Muislamu mwenye nguvu ni bora na ndiye apendezaye zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko Muislamu mnyonge.
Kwa kuwa upendo wa wazazi kwa watoto ni sehemu ya maumbile yao (wazazi) ya kiasili, ndipo ikawa hapana haja ya kuagizwa juu ya jambo hilo, kwa hivyo Uislamu umetilia mkazo zaidi umuhimu wa matunzo ya watoto na ukaonya vikali wazazi wasizembee katika jambo hilo, ili familia na jamii ziweze kuishi kwa raha na furaha. Na hii hatimaye huleta muundo wa kizazi ambacho kitategemewa kuweza kubeba mzigo wake barabara na katika hali ya kujitegemea. Imetajwa katika Qur ani:
Wala msijitie wenyewe katika maangamivu. (2:145).
Na je ni maangamivu gani maovu zaidi ambayo mtu anaweza akajifanyia mwenyewe kuliko kuingiza kiwiliwili chake na damu (watoto) wake kwenye hatari ya kifo na adhabu? Imetajwa tena katika Qur ani:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ﴿٦﴾
Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu (jamii) wenu kut okana na moto, ambao kuni zake ni watu na mawe (66:6).
Kujilinda na maangamivu (ya ugonjwa n.k.) kuna maana sawa na kuna daraja moja na kuilinda jamii kutokana na maangamivu ya motoni. Ikiwa kujilinda kunahitajika kwa ajili ya maisha ya akhera, basi kujilinda huko kunahitajika zaidi wakati wa maisha ya duniani kwani kile ukipendacho katika maisha yako duniani ndicho utakachokivuna akhera. Kujilinda kwa maana hiyo, hakumaanishi kujizuia kutokana na kutenda maovu, madhambi na mambo ya fedheha tu, bali ina maana ya ndani zaidi kuhusiana na usawa baina ya mahitaji ya nafsi, kiwiliwili, roho, na kujilinda na maneno ya Mtume(s.a.w.w)
aliposema:Yatosha kwa mtu kupata dhambi kwa kutomjali yule anaemtegemea.
Pia:Nyote ni wachungaji na kila mmoja wenu ataulizwa kutokana na kile anachokichunga.
Tukizingatia, inatudhihirikia wazi kwamba kuwakinga watu wetu kutokana na maradhi ni amri ya kidini na ni wajibu wa jamii na pia ni wajibu wa taifa zima. Mtume(s.a.w.w)
amesema: Mwenye kuitunza jamii na hakuipa nasaha (maonyo), basi mtu huyo atanyimwa pepo. Kuwapatia watoto huduma za chanjo dhidi ya maradhi yauwayo na yalemazayo, humwokoa mtunzaji wa jamii kutokana na kosa la kupuuza jamii yake. Na mwishowe ataokoka Siku ya Kiyama kutokana na vitisho ambavyo vingempat a wakati Mwenyezi Mungu atapomuuliza kuhusu hali ya wafuasi wake (wenye kumtegemea) na sababu ya kuwa mzembe katika jambo hilo. Kwa hivyo basi, iwapo wazazi hawatachukua hatua zifaazo ili kulinda maisha ya watoto wao kuwakinga kutokana na maradhi, kuna uwezekano mkubwa wa kunyimwa pepo akhera.
Chanjo na huduma za O.R.S. (Maji ya dawa ya kurudisha maji mwilini kutokana na maradhi ya kuharisha) hutolewa bure na serikali. Wazazi wanachotakiwa kufanya ni kuzitumia huduma hizi, ili kuwakinga watoto wao kutokana na madhara na hatari ziletwazo na magonjwa. Hata kama watalazimika kulipa ili watoto wao wachanjwe, Uislamu unawapa moyo kufanya hivyo, kwani Mtume(s.a.w.w)
amesema: Bora ya matumizi, ni kutumia (japo) senti kwa ajili ya familia yako.
5.
KUWALINDA WATOTO NI HURUMA, NA HURUMA NI KINGA
Mtume(s.a.w.w)
ametueleza mpango maalum wa kutuwezesha tuwe na huruma na upendo kwa watoto wetu. Ametaja Bukhari katika kitabu chake cha Al-Adab, katika mlango maalum kwamba wahurumieni watoto na pale Mtume(s.a.w.w)
ali posema: Si katika sisi yule mtu asiyemhurumia mdogo, na asiyejua haki ya mkubwa (asiye mheshimu). Akasema tena: Rehemuni (sikitikieni) wenzenu, nanyi mtarehemewa. Ni dhahiri kutokana na Hadith zilizotajwa hapo juu kwamba Mtume(s.a.w.w)
ameeleza jinsi wa le watu ambao hawana huruma kwa wadogo zao wanavyochukuliwa kuwa si waislamu wa kweli na hawako pamoja na Mtume(s.a.w.w)
na ujumbe wake Mtukufu. Inasemekana kuwa hapana yeyote awezaye kuwa na huruma kwa mtoto kama ilivyo wazazi wake (mtoto).
Ikiwa Mtume(s.a.w.w)
amewataka watu wote kwa pamoja kuwa na huruma kwa watoto, basi ni jambo lililo muhimu zaidi kwanza kwa wazazi kuwaonea huruma watoto wao kuliko watu wengine. Sehemu ya huruma yao kwa watoto wao ni kuwapeleka wakapatiwe chanjo na kinga kutokana na magonjwa na maradhi yote yenye kuenea yawezayo kuwashambulia.
Wazazi watakapokuwa na huruma kwa watoto wao, basi huruma hiyo hiyo huwarudia (wazazi) wakati wa uzeeni kwa sababu upendo ni kitu cha kulipana. Mtume(s.a.w.w)
ameeleza kwa ubainifu kuhusiana na suala hili la huruma na kinga, na akaeleza jinsi huruma ilivyokuwa sehemu ya kinga na kinga ni sehemu ya huruma. Amesema: Harehemiwi (haonewi huruma) yule mtu asiyemrehemu mwingine, na hasemehewi yule asiyemsamehe mwingine, wala hapewi toba (na Mwenyez i Mungu) mtu asiyetubu, na wala halindwi yule asiyejilinda.
Katika Hadith hii Mtume(s.a.w.w)
ametilia mkazo ya kuwa huruma ndilo jambo la msingi na akaeleza ya kwamba, yeyote asiyejilinda, basi Mwenyezi Mungu hatamlinda kutokana na maradhi. Ijapokuwa jambo hilo limeelezwa, lakini Mtume(s.a.w.w)
amelielezea kimantiki kwa njia ya maombi. Amesisitiza Mtume(s.a.w.w)
kwamba, yeyote asiyejilinda ama kulinda wengine kutokana na kitakachowadhuru au kuwaingiza hatarini au kwenye ugonjwa, basi Mwenyezi Mungu naye hawezi kumlinda kutokana na mambo hayo. Kwa hivyo basi Mtume(s.a.w.w)
katika maelezo yake hapa anakusudia kuifanya huruma isambae miongoni mwa watu, na anaazimia kuwapa moyo watu kujaribu kupata huduma za kinga zifaazo dhidi ya hii ikiwa ni kukamilisha sehemu ya huruma.
6.
UISLAMU NA UZAZI WA MPANGO
Qur ani imefafanua waziwazi kuhusu muda maalum ufaao kwa kutenganisha baina ya kuzaliwa mtoto mmoja hadi kupata mwingine. Imetajwa ndani ya Qurani kuwa kubeba mimba ya mtoto hadi kumwachisha kunyonya ni kipin di cha miezi thelathini; Amesema Mwenyezi Mungu:
Kubeba mimba ya mtoto hadi kumwachisha ni miezi thelathini
(46:15) Pamoja na hayo, Uislamu unaunga mkono kunyonyesha kwa maziwa ya mama kunakodumu kwa miaka miwili kamili kwa wale wanaotaka kutimiza muda huo kamili. Kwa kufanya hivi, kunamwezesha mama (aliyezaa) kurekebisha afya yake, na kumrudisha nguvu zake za mwilini alizozipoteza katika kipindi cha uja uzito hadi kujifungua.
Muda huu maalum pia utamwezesha mtoto kupata muda wa kutosha wa kunyonya matiti ambapo utaalamu wa utabibu (wa kisasa) umekuja kuunga mkono baada ya kutofaulu kwa muda mrefu, kwa kutumia chupa ya kunyonyea.
Kwa hivyo hapa ni dhahiri namna gani Uislamu unavyopigania uzazi wa mpango ili kuwapatia afya bora mama na mtoto.
Imetajwa katika Qur ani:
وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ إِحْسَانًا حَمَلَتْهُ أُمُّهُ كُرْهًا وَوَضَعَتْهُ كُرْهًا وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا ﴿١٥﴾
Na tumemwusia mwanaadamu kuwatendea wema wazazi wake, mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu, kubeba mimba yake mpaka kumwachisha kunyonya ni (kipindi cha) miezi thelathini (46:15).
Imetajwa pia katika Qurani:
وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ ﴿١٤﴾
Na tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia mema wazazi wake, mama yake amebeba mimba yake kwa unyonge juu ya unyonge, na (kumnyonyesha na) kumwachisha kunyonya katika miaka miwili.
7.
UISLAMU NA KARANTINI ZA AFYA
Uislamu unaonya sana tuwe macho kutokana na maradhi yaambukizayo na unatusihi tujikinge na maradhi hayo. Imepokewa Hadith ya kwamba Mtume(s.a.w.w)
alibaiwa (kuungwa mkono wa uongozi) na mtu mwenye ugonjwa wa ukoma pasi na kupeana naye mkono
, ama kumruhusu kutangamana na watu. Imepokewa kutoka kwa Umar bin Shareed, kutoka kwa baba yake amesema:
Katika ujumbe wa Thaqif uliokuja kum bai (kumtambua kama kiongozi) kulikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa ukoma, basi Mtume(s.a.w.w)
alimrejesha (bila ya kumpa mkono) kwa kusema: Hakika tumekutambua. Na katika Sahih Bukhari, Mtume(s.a.w.w)
amesema: Kaa mbali na mwenye ukoma kama unavyokaa mbali na simba. Mtume(s.a.w.w)
ameeleza wazi wazi kwamba wakati yatapoingia maradhi ya tauni, watu ni lazima wawe macho sana, na wachukue hadhari zote za lazima ili kujikinga na kujiepusha na mtu aliyeambukizwa.
Imetajwa katika Hadith:Tauni (ugonjwa ueneao) ni alama ya adhabu ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu huwajaribu nayo watu miongoni mwa waja wake. Mtakaposikia kuwa umeingia nchini, basi msiingie nchini humo na iwapo utatokea nanyi mko ndani ya nchi hiyo basi msitoke.
Hapa Mtume(s.a.w.w)
anaamuru Karantini na anatukataza kuingia katika nchi iliyokumbwa na ugonjwa wa tauni, ili tujilinde kutokana na kifo, vile vile tumeonywa tusitoke nje ya nchi ambayo tayari imekumbwa na ugonjwa huo, ili tusisambaze maradhi. Na hii pia ni aina nyingine ya kujilinda. Aina hizi mbili za maonyo (zilizotangulia hapo juu) zinachukuliwa kuwa ni aina za hasi (Negative) za kujikinga. Wakati ambapo kuchanja kwa ajili ya kinga za magonjwa na maradhi ya kuambukiza ni aina ya chanya (Positive). Kwa hivyo Uislamu unapigania sana aina hii ya chanjo kwani ndiyo iliyo bora na ni yenye gharama ndogo zaidi kuliko matibabu.