MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU0%

MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU Mwandishi:
Kundi: Familia na watoto

  • Anza
  • Iliyopita
  • 9 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 13816 / Pakua: 3622
Kiwango Kiwango Kiwango
MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

Mwandishi:
Swahili

3

MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

SEHEMU YA TATU

CHAKULA BORA NA MANUFAA YAKE KATIKA AFYA YA KIMWILI NA KIAKILI

i. Uislamu na kunyonyesha kwa matiti (maziwa ya mama)

Mtoto anapozaliwa na kuja ulimwenguni, mtu anayemuhitajia na kufungamana naye zaidi ni mama yake, ni sawa kabisa na kusema kwamba nusu ya kitu imeungana na kamili. Mtoto anahitaji kulishwa chakula sawa na kile alichozoea kukila kupitia kwenye damu ya mama yake, wakati alipokuwa kilenge (kitoto tumboni). Chakula hicho alichozoea kukila ndicho huchezea kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, na kuwa maziwa ambayo yana chembechembe zilizo lazima kwa uhai wa mtoto huyo na vitu muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya kukua kwake.

Maziwa hayo hutoka kupitia kwenye matiti, na mtoto kwa uwezo wa Mola, huyahitajia na huyanyonya. Qur ani imeeleza kanuni zinazosimamia uhusiano baina ya mtoto na mnyonyeshaji wa kuajiriwa (yaani wakati mama mzazi anaposhindwa kumnyonyesha mto to wake kwa sababu mahsusi, kisha akakodisha mnyonyeshaji ili amnyonyeshee mtoto wake).

Imetajwa katika Qur ani:

وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ لِمَنْ أَرَادَ أَن يُتِمَّ الرَّضَاعَةَ ٌ ﴿٢٣٣﴾

Na wanawake waliozaa wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili, kwa anayetaka kukamilisha muda wa kunyonyesha. (2:233).

Kutokana na Aya h ii, tunaweza kueleza mambo yafuatayo:

1. Ni wajibu wa mama kumnyonyesha mtoto wake, na si kumnyima haki ya kunufaika na maziwa ya matiti, lakini hii inategemea kama ataweza kumnyonyesha (yaani kutokuwa mgonjwa, n.k.).

2. Muda wa kunyonyesha kwa wale wanaotaka kutimiza muda ni miaka miwili kamili.

3. Kumwachisha mtoto kunyonya kunaruhusiwa kabla ya kutimiza muda (wa miaka miwili) kwa sharti uamuzi huu upitishwe kwa makubaliano ya wawili kati ya baba na mama, tena baada ya kujadiliana kwa pamoja uzuri na ubaya wa uamuzi huo, na jinsi ya kumpa matunzo ya kutosha mtoto wao. Imetajwa katika Qur ani:

فَإِنْ أَرَادَا فِصَالًا عَن تَرَاضٍ مِّنْهُمَا وَتَشَاوُرٍ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا ﴿٢٣٣﴾

Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha kunyonya (kabla ya miaka miwili) kwa kuridhiana na kushauriana, basi hapana ubaya juu yao. (2:233).

4. Ni juu ya baba kumsaidia mama anayenyonyesha, kumweka katika mazingira yafaayo anayohitaji ili kumyonyesha mtoto wake.

Hii inadhihirisha kwamba Uislamu unachukulia kunyonyesha kuwa ni wajibu mkubwa kwa upande wa mama, ambapo haufai kufuatiliziwa na kazi nyingine za ziada. Hivyo basi hii inaonyesha waziwazi jinsi Qur ani ilivyoeleza kwa ufafanuzi juu ya haki za mama anayenyonyesha.

5. Baba atakapokuwa hayuko, ama amefariki, mmoja kati ya watu wa familia atachukua jukumu la kumlisha mtoto na kumtoshelezea mahitaji yake yeye na mama yake, ili aendelee kunyonyesha. Hali mojawapo kati ya hizo zinapotokea huwa zinazingatiwa kwa makini sana na Uislamu, ndipo Uislamu ukaweka kanuni mahsusi kwa waislamu zinazoelezaea mambo haya.

6. Mama anayeweza kumnyonyesha mtoto wake, anakatazwa kuajiri mnyonyeshaji wa kumnyonyesha mtoto wake badala yake.

Uislamu unamlazimisha baba wa mtoto kutoa posho ya pesa kumpatia mama aliyemtaliki (aliyemwacha wakati akinyonyesha), anyonyeshaye mtoto yule. Kwa hali hiyo, Uislamu unahakikisha kwamba mtoto anapata mahitaji yake yote anayopaswa kupewa katika kipindi hiki cha kunyonya. Ni vizuri kutaja hapa kwamba Mwenyezi Mungu ameyatosheleza mahitaji (yote ya lishe) ya mtoto kutokana na maziwa anayoyanyonya kutoka kwenye matiti ya mamake.

Katika siku tatu za mwanzo wa maisha ya mtoto, matiti hutowa majimaji ya kimanjano yajulikanayo kama dangaa (beestings) na ambayo hutoka kwa kiasi kidogo.

Majimaji haya hutosheleza kumpatia mtoto chakula anachokihitaji mwanzo wa maisha, aidha hulis aidia tumbo lake kuanza kupokea na kuyeyusha chakula anachokila. Katika siku ya nne, matiti huanza kutoa maziwa ambayo ni ya muhimu kwa kumlisha mtoto mpaka atakapofikia kuacha.

Mama anayekataa kumnyonyesha mtoto wake bila ya sababu za maana, basi hujinyima yeye na humnyima mtoto wake faida muhimu sana. Kwani kunyonyesha kunamletea mama hisia za mapenzi na humwongezea (moy- oni mwake) hisia za huruma ya umama. Kwa kuongezea tu, kwa yale yaliyotajwa hapo awali ni kwamba, kunyonyesha kunafanya utaratibu wa kuyeyusha chakula kwa mama kuweza kutengeza chakula kinachohitajika, kilicho muhimu kwa mtoto wake na kustawisha hali yake ya kiafya kwa ujumla. Pamoja na hayo, kunyonyesha kunasaidia kurekebisha njia ya uzazi wa mwanamke na kuweza kuirudisha katika hali iliyo sawasawa na ya kawaida baada ya kumalizika kwa zoezi la kuzaa.

ii. Umuhimu wa kunyonyesha kwa matiti

katika Uislamu Qur ani imetilia mkazo umuhimu wa kunyonyesha kwa matiti katika Uislamu ikasema:

وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ أُمِّ مُوسَىٰ أَنْ أَرْضِعِيهِ فَإِذَا خِفْتِ عَلَيْهِ فَأَلْقِيهِ فِي الْيَمِّ وَلَا تَخَافِي وَلَا تَحْزَنِي إِنَّا رَادُّوهُ إِلَيْكِ وَجَاعِلُوهُ مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٧﴾

Tukampelekea mama yake nabii Musa ufunuo (ufahamu w a moyoni - wahyi) kuwa mnyonyeshe, na utakapomhofia, basi mtie mtoni, usiogope, wala usihuzunike kwani sisi tutamrejesha kwako. Na tutamfanya kuwa ni miongoni mwa Mitume (28:7).

Hapa Mwenyezi Mungu amemwamuru mama yake nabii Musa(a.s) kumnyonyesha ili kuleta hisia maalum za kiroho, hisia ambazo zinafanya kunyonyesha kuwa ni mwenendo wenye kusisimua. Wakati mama anaponyonyesha, huwa katika hali ya msisimko mkubwa usiyomithilika, na hisia za umama na huruma zake pia huwa zimeamshwa (huwa na huruma sana). Kwa ajili hii ndipo mama yake nabii Musa(a.s) alipoanza kuhofia kuhusu maisha ya mwanawe. Mwenyezi Mungu alimwamrisha amnyonyeshe, kwani katika muda huo wa kumnyonyesha ndipo njia ya uhusiano inapotokea baina yake na mama yake. Au kwa upande mwingine, mama pia huanza kuunda hisia za moyoni kwa mtoto wake ambaye anazungukwa na pendo na huruma ya hali ya juu. Kumnyonyesha kwa mama yake nabii Musa mtoto wake kulikuwa ni kwa pendo na huruma yake yote. Hii ndiyo ikawa sababu kubwa ya Mwenyezi Mungu kumharamishia (kumfanya akatae kunyonya) maziwa ya mnyonyeshaji wa kukodishwa aliyeletwa na Firauni, kwani nabii Musa alikuwa ameshaonja maziwa ya mama yake, na hivyo kukataa kuonja maziwa ya mwanamke mwingine yeyote.

Amesema Mwenyezi Mungu:

Na tukamharamishia w anyonyeshaji tangu mwanzo (28:12).

Qurani imeeleza tena kuhusu umuhimu wa kunyonyesha na maana yake; na mfungamano imara wa kiakili wa kimoyo kati ya mtoto na mamaye unaotokana na kunyonyesha kwa matiti. Imeelezwa kwamba, hapana mama yeyote awezaye kumt upa mtoto wake mchanga anyonyaye ila awe amepatwa na hofu kuu na hatari itishayo kabisa! Amesema Mwenyezi Mungu:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ إِنَّ زَلْزَلَةَ السَّاعَةِ شَيْءٌ عَظِيمٌ ﴿١﴾ يَوْمَ تَرَوْنَهَا تَذْهَلُ كُلُّ مُرْضِعَةٍ عَمَّا أَرْضَعَتْ وَتَضَعُ كُلُّ ذَاتِ حَمْلٍ حَمْلَهَا وَتَرَى النَّاسَ سُكَارَىٰ وَمَا هُم بِسُكَارَىٰ وَلَـٰكِنَّ عَذَابَ اللَّـهِ شَدِيدٌ ﴿٢﴾

Enyi watu! Mcheni Mola wenu, hakika mtetemeko wa Siku ya Kiyama, ni jambo kubwa (sana). Siku mtakapokiona (Kiyama), kila mwanamke anyonyeshay e atamsahau (mtoto) amnyonyeshaye, na kila mwenye mimba yake. Na utawaona watu wamelewa na wala hawakulewa, lakini (hiyo) ni adhabu ya Mwenyezi Mungu iliyo kali (22:1-2).

Maumbile haya ya dhahiri na ya ajabu, ya uhusiano (wa mtoto na mama) yatageuzwa Siku ya Kiyama kwa mama kumsahau mtoto wake anayemnyonyesha, ambalo hilo kwa hakika ni tukio la kutisha.

Kabla ya ukhalifa wa Umar Ibn al-Khattab, dola ya kiislamu ilikuwa ikitoa posho maalum kwa mtoto anayeachishwa kunyonya. Mpango huu ukawa unatumiwa vibaya na familia maskini, kwani walikuwa wakiwaachisha watoto wao kunyonya mapema sana ili wakajipatie posho hizo. Umar Ibn al-Khattab akalichunguza jambo hilo kwa kina kwa jinsi akina mama walivyowanyima watoto wao haki za kuwanyonyesha kwa muhula wa miaka miwiwli kamili, kama ilivyotajwa katika Qur ani.

Hatimaye tabia hiyo ilidhuru afya na makuzi ya watoto. Kwa sababu hiyo, ndipo Umar (wakati wa ukhalifa wake) akaurekebisha utaratibu huo, akafanya malipo ya posho hiyo yatolewe mara tu mtoto anapozaliwa. Marekebisho haya yakawapa nguvu akina mama ya kuweza kukamilisha kuwanyonyesha watoto wao kwa kipindi cha miaka miwili pasi na kuwanyima haki hii muhimu. Vizazi vya kiislamu vilivyotangulia mara kwa mara vilikuwa vikihimiza kunyonyesha kwa kutambua umuhimu wake katika maisha ya mtoto na familia.

Kwa kuwa Uislamu ni dini ya kimaendeleo na yenye huruma ambayo inafaa kwa wakati wowote na mahali popote, unamtaka kila mtu mwenye busara kufuata na kudumisha vitendo vyema na vilivyo sawa. Ikiwa utaalamu wa kisayansi katika zama zetu hizi za kisasa umetilia mkazo umuhimu wa kunyonyesha, basi ni vizuri kutaja kwamba Uislamu umetilia mkazo jambo hili tangu miaka elfu moja mia nne (1400) iliyopita.

Kwa hivyo Uislamu unampa taadhima baba na mama Muislamu, mtoto na jamii yote ya Kiislamu kwa ujumla, pale unapotuamrisha kufuata vitendo vizuri kama hivyo. Inaeleweka wazi kuhusu athari ya maziwa ya mama kwa afya ya mtoto, tabia yake na maisha yake ya baadaye. Kwa hivyo si ajabu kwa nini Mtume(s.a.w.w) ametukataza tusimpatie kumnyonyesha mtoto mwanamke kahaba au asiye na akili timamu.

Mtume(s.a.w.w) ametuamuru tumlinde mtoto kutokana na jambo lolote litakaloharibu uzuri wa maumbile yake, Amesema:Walindeni watoto wenu kutokana na maziwa ya kahaba na ya mwendawazimu, kwani maziwa yanaambukiza.

Ndani ya maelekezo haya, hapana shaka kwamba Uislamu unahakikisha kabisa kwamba w atoto wanapata malezi na matunzo ya kutosha wanayostahili kuyapata.

iii. Lishe kwa akina mama waja wazito na wanaonyonyesha

Afya ya mtoto aliye tumboni mwa mama yake hutegemea sana utaratibu wa chakula kiletacho afya mwilini wakati mama anapokuwa mja mzito.

Ukosefu wa chakula bora wakati wa uja uzito huwaathiri wote kwa pamoja, kitoto na mama yake.

Tumeshazungumza hapo awali kwamba Uislamu humlinda mtoto hata kabla hajazaliwa ili mtoto azaliwe akiwa na nguvu na afya. Ni kwa sababu hii ndipo mwanamke mja mzito lazima awe mwangalifu sana kwa kuchagua vizuri mchanganyiko wa vyakula wakati huo, kwani kwa kufanya hivyo tu ndipo mtoto wake atakapozaliwa katika hali ya afya njema. Mchanganyiko wa chakula bora wakati wa uja uzito utamwezesha mzazi kuwa na hali nzuri ya kiafya baada ya kujifungua ili kumnyonyesha mtoto wake vizuri. Kutokana na mazingatio ya Uislamu juu ya mambo haya, ndipo ukawaruhusu akina mama waja wazito na wanyonyeshao wasifunge katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani, iwapo wanahofia pengine kufanya hivyo kungemdhuru mtoto aliye tumboni.

Ruhusa hii si ya kudumu, bali inategemea kitambo atakachokitumia mama mnyonyeshaji katika kumnyonyesha mwanawe; ikiwa ni kirefu au kifupi. Ni dhahiri kwamba shabaha ya Uislamu ni kutekeleza utoshelezaji wa mahitaji ya lazima ya mtoto, na kwa jinsi gani unavyoheshimu hisia za huruma za umama. Mtume(s.a.w.w) amesema:Hakika Mwenyezi Mungu amemruhusu mwenye kusafiri asifunge, na apunguze Swala, pia amemruhusu mwanamke mja mzito na anayenyonyesha asifunge.

iv. Mchango wa chakula bora katika kukuza akili timamu

Miongoni mwa mambo yanayozingatiwa sana na Uislamu ni ustawi wa akili na nafsi ya Muislamu. Kula chakula bora ndio ufunguo wa afya nzuri na ustawi wa kiakili na wa nafsi, na yapasa kuanza wakati mama anapokuwa mja mzito na kuendelea katika muda wa maisha ya kila mmoja. Sheria ya Kiislamu inashauri watu wale vyakula mbali mbali vyenye afya ambavyo ni vya lazima kwa mwili wa binaadamu na kuongezeka kwa afya. Mtume(s.a.w.w) amesema:Muislamu mwenye nguvu ni bora na yu karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kuliko Muislamu dhaifu.

Mwili wa binaadamu daima unahitaji chakula bora ili kuweza kurudisha nguvu zilizopotea wakati wa kufanya kazi na harakati nyinginezo, na kuuwezesha kuendelea na kazi zake za kawaida, kwa sababu hizi ndipo Uislamu ukasisitiza kuhusu kula chakula bora bila ya kufanya ubadhilifu. Mwenyezi Mungu amesema: kuleni na kunyweni (vizuri) lakini msifanye ubadhilifu..(7:31).

Amesema tena:

وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ جَنَّاتٍ مَّعْرُوشَاتٍ وَغَيْرَ مَعْرُوشَاتٍ وَالنَّخْلَ وَالزَّرْعَ مُخْتَلِفًا أُكُلُهُ وَالزَّيْتُونَ وَالرُّمَّانَ مُتَشَابِهًا وَغَيْرَ مُتَشَابِهٍ كُلُوا مِن ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَآتُوا حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ وَلَا تُسْرِفُوا إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ ﴿١٤١﴾

Naye ndiye aliyeumba mabustani yanayoegemezwa (yanayokingamana) na yasiyoegemezwa, na (akaumba) mitende na mimea ya aina mbali mbali, na mizaituni, na mikoma-manga inayofanana na isiyofanana, na kuleni matunda yake inapozaa; na toeni haki yake siku ya mavuno yake, wala msifanye ubaadhirifu, hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wafanyao ubadhilifu. (6:141).

Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu ni Mkarimu sana kwa watu wake kwa kuwaumbia ng ombe na wanyama ili kutumia manyoya na kula nyama zao kwa ajili ya kuhifadhi maisha yao. Inakisiwa kwamba ni kwa sababu hii ndipo Mwenyezi Mu ngu akamwamuru Mariam baada ya kumzaa Isa(a.s) kula tende mbivu ili kufidia kiasi cha damu alichokipoteza. Mwenyezi Mungu amesema katika Qur ani:

وَالْأَنْعَامَ خَلَقَهَا لَكُمْ فِيهَا دِفْءٌ وَمَنَافِعُ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿٥﴾

Na amewaumba wanyama katika hao mnapata (vitiavyo) joto, na manufaa mengine, na wengine mnawala. (16:5).

A mesema tena pia katika Aya nyingine:

فِيهِمَا فَاكِهَةٌ وَنَخْلٌ وَرُمَّانٌ ﴿٦٨﴾

Mna (katika hiyo bustani) matunda na hasa mitende na mikomamanga (55:68).

Mwenyezi Mungu (hapa) amezihusisha tende na mikomamanga (mikudhumani) kwa ajili ya ubora wa matunda hayo kushinda mengine. Miongoni mwa faida (za kiafya) zipatikanazo kwenye matunda hayo mawili: Ni kiasi kikubwa cha sukari (Glucose) kilichomo ndani yake ambayo huyeyushwa na kutumiwa na mwili kwa haraka ili kuweza kuzalisha nguvu (Calorie) na joto mwilini. Mwenyezi Mungu amesema:

الْمُلْكُ يَوْمَئِذٍ الْحَقُّ لِلرَّحْمَـٰنِ وَكَانَ يَوْمًا عَلَى الْكَافِرِينَ عَسِيرًا ﴿٢٦﴾

Na litikise kwako shina la mtende litakuangushia tende nzuri zilizoiva na unywe na utulize jicho lako (upumzike) (19, 25-26).

Ama kuhusu koma-manga, imegunduliwa kuwa ina kiasi kikubwa cha Limonic acid ambayo inasaidia kupunguza ukali wa tindikali (acid) katika mko jo na damu pindi inapoyeyuka mwilini. Kwa kuongezea ni kwamba tunda hilo pia lina kiasi kikubwa cha joto ambacho huyeyushwa na mwili kwa urahisi zaidi na hutumika kwa kuupa mwili. Kuhusu asali ya nyuki, imeainishwa kwa kutajwa ndani ya Qur ani:

يَخْرُجُ مِن بُطُونِهَا شَرَابٌ مُّخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ فِيهِ شِفَاءٌ لِّلنَّاسِ ﴿٦٩﴾

..kinatok a katika matumbo yao (nyuki) kinywaji (asali) chenye rangi mbalimbali, ndani yake kina tiba kwa wanaadamu (16:69).

Amesema tena Mwenyezi Mungu:

وَآيَةٌ لَّهُمُ الْأَرْضُ الْمَيْتَةُ أَحْيَيْنَاهَا وَأَخْرَجْنَا مِنْهَا حَبًّا فَمِنْهُ يَأْكُلُونَ ﴿٣٣﴾ وَجَعَلْنَا فِيهَا جَنَّاتٍ مِّن نَّخِيلٍ وَأَعْنَابٍ وَفَجَّرْنَا فِيهَا مِنَ الْعُيُونِ ﴿٣٤﴾ لِيَأْكُلُوا مِن ثَمَرِهِ ﴿٣٥﴾

Na alama (ya rehma za Mwenyezi Mungu) juu yao, ni ardhi iliyokufa (isiyo na rutuba) tunaifufua na tukatoa ndani yake nafaka ambazo wanazila, na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu na kupitisha chemchem ndani yake ili wale matunda yake. (36:33- 35).

Amesema tena Mwenyezi Mungu:

Na katika wanyama kuna wale wabebao mizigo na wanaopandwa. Kuleni katika alivyokuruzukuni Mwenyezi Mungu (6:142).

Amesema tena Mwenyezi Mungu kuhusu maji:

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً لَّكُم مِّنْهُ شَرَابٌ وَمِنْهُ شَجَرٌ فِيهِ تُسِيمُونَ ﴿١٠﴾

Yeye ndiye anayekuteremshieni maji kutoka mawinguni, kw a hayo mnapata ya kunywa na (yanatoa) miti ya kulishia (wanyama). (16:10).

Amesema tena Mwenyezi Mungu kuhusu maziwa kwa ajili yenu:

نُّسْقِيكُم مِّمَّا فِي بُطُونِهِ مِن بَيْنِ فَرْثٍ وَدَمٍ لَّبَنًا خَالِصًا سَائِغًا لِّلشَّارِبِينَ ﴿٦٦﴾

Tunakunywesheni katika vile vilivyomo matumbo mwao (vikitoka) baina ya kinyesi na damu, (nayo ni) maziwa safi mazuri kwa wanywao. (16:66).

Amesema tena Mwenyezi Mungu:

وَكُلُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّـهُ حَلَالًا طَيِّبًا وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي أَنتُم بِهِ مُؤْمِنُونَ ﴿٨٨﴾

Na kuleni katika vile alivyowaruzukuni Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri (5:88).

4

MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

SEHEMU YA NNE

MAONI YA UISLAMU JUU YA MALEZI YA MTOTO

Watoto ni maua yenye kuchanua katika maisha yetu, ni ahadi ing aayo katika mustakbali wetu, na ni kiburudisho cha macho yetu. Wao ndiyo wanaodumisha historia adhimu ya mataifa yao. Watoto na vijana wana jukumu kubwa tena la maana la kufanya wakati wa maisha yao.

Kwanza : wamekadhibiwa ulinzi wa kuhakikisha kuwa kaz i kubwa

inafanyika kwa ajili ya nchi zao.

Pili : wanatarajiwa kutumia uwezo na ujasiri walionao ili nguvu zao ziweze kufaidisha kuinua hali ya maisha ya mataifa yao.

Na kwa sababu hiyo, ndipo Uislamu ukahimiza sana umuhimu wa malezi ya mtoto.

Qur ani ina maagizo na masharti kwa ajili ya kulinda maisha ya mtoto. Pia kumwongoza na kumpangia utaratibu katika maisha yake. Wakati Uislamu unapopanga utaratibu wa maisha ya mtoto, familia na jamii zinazingatia kwamba pana uhusiano wa ndani baina yao unaoonyesha kwamba mabadiliko au uharibifu wowote ukitokea upande mmoja basi utawadhuru wote.

Kwa hivyo fikra za Uislamu zimempangia Mwislamu njia nzuri ya maisha ambayo msingi wake ni ushirikiano, huruma na imani, ili kutoa mchango wake katika kuwatengezea maisha jamii ya kiislamu. Na ili kufanya hivyo, Uislamu unaanza kwa kumpangia mtu mmoja, kwani yeye ndicho kiungo cha mwanzo katika kuunda maisha ya familia na ya jamii ya watu, na mwishowe taifa zima.

Mtu mmoja ndiye msingi wa kitu cha kwanza, na ndipo asili ya maisha ya taifa zima yanapoanzia. Mtu mmoja ndiye chanzo, naye si mwengine bali ni mtoto ambaye huongozwa na maumbile yake ya kiasili na tabia zake alizojifunza kutoka kwa jamii yake kupitia njia ya kuishi pamoja. Kutangamana na watu wengine ndiko kunakotengeneza tabia ya mtu na kumpangia utaratibu wa heshima za kiutu (zinazothaminiwa katika jamii hiyo). Iwapo atakuzwa katika njia bora na yenye nidhamu, basi atakuwa ni nguzo ya mafanikio katika maisha ya familia ambayo ni sehemu ndogo tu ya jamii ya watu.

Kwa hivyo mafanikio katika familia (ambazo zikiungana pamoja zinaunda jamii), mwishowe yataunda taifa imara na lenye nguvu. ii. Mtoto baina ya silika na athari na mazoea ya mazingira, na jukumu la wazazi Maendeleo makubwa sana yamepatikana katika elimu ya saikolojia (nafsi) ambayo kwayo wataalamu wa elimu hiyo huweza kumiliki kutengeneza tabia ya mwanaadamu na kuilezea nguvu ya maumbile ya kudumu ambayo inafanya mtu kutenda jambo kwa njia maalum. Tena, wataalam hao katika utafiti wao, wanachimbua kwa undani zaidi kuhusu nafsi ya mwanaadamu na wamegundua vipengele mbali mbali vya makuzi ya maumbile ya mtoto na tabia zake kiasili.

Tena wakazifafanua silika mbali mbali zinazoongoza mwenendo wa mtoto katika kila hatua ya kukua kwake. Pia wameeleza kwa urefu zaidi kuhusu mahitaji ya watoto na jinsi ya kuwatosheleza. Uislamu umetangulia elimu hiyo katika kupambanua hatua mbali mbali za makamuzi ya mtoto, haki zake, na mahitaji yake. Kazi hii iliyotangulia iliyofanywa na Uislamu inatoa mchango mkubwa katika kuleta ustaarabu wa binaadamu. Kabla hatujaenda mbali zaidi katika kueleza jinsi Uislamu unavyotoa maoni yake kuhusu malezi ya mtoto, hatuna budi kwanza kufafanua mambo muhimu yafuatayo: Kuna baadhi ya watu wanaounga mkono fikra kwamba mtoto huzaliwa mwema kimaumbile. Hii ina maana kwamba mtoto, kiasili, huzaliwa katika hali ya kuwa mwema ila tu ni ulazimishaji wa mazingira ndio unaogeuza na kuathiri mwenendo wake, na ndio unaoamua iwapo atadumisha mwenendo wake mzuri ama la. Kwa upande mwingine kuna wengine wanaoshikilia mawazo yanayosisitiza kwamba, mtoto huzaliwa akiwa ni karatasi nyeupe (yaani si mwema wala si mwovu) ila ni kutokana na mazingira (anamoishi) ndipo huanza pole pole kujizoesha kushika mwenendo na tabia za mazaingira hayo. Mtoto huyo hushika tabia tofauti zinazomfanya kuwa ni sehemu ya mazingira yale anayoishi, mwishowe huunda tabia yake.

Basi kwa vyovyote, aidha iwe maoni ya kwanza ama ya pili ndiyo yenye nguvu zaidi, hapana shaka yoyote kwenye njia zote mbili kwamba, yale mazingira anayoishi mtoto yana mchango mkubwa na wa muhimu katika kuunda tabia, mwenendo, na maisha yote. Miongoni mwa watu wa kwanza katika mvuto wa kitabia wa mtoto, ni wazazi wake. Mtoto huwachukulia wazazi wake kuwa ndiyo kielelezo katika maisha, na ni kwa sababu hii muhimu ndipo wazazi siku zote wanatakiwa wawe mfano bora wa kufuatwa na watoto wao katika jambo walisemalo ama walifanyalo.

Ikiwa ni hivyo, ni dhahiri kwamba maumbile ya kiasili anayozaliwa nayo mtoto na mazingira anayoishi yana athari kubwa katika kumjenga na kumwendeleza awe raia mwema. Kwa sababu hii, ndipo Uislamu kama tulivyoelezwa hapo mwanzo, unamlinda mtoto hata kabla hajazaliwa. Mwenyezi Mungu amewataka watu kuwaangalia vizuri sana watoto wao. Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Wapendeni watoto wenu na muwahurumie, na mtakapowaahidi (kitu) basi watimizieni, kwani wao hawaoni anayewapatia mahitaji yao ila nyinyi. Hadithi hiyo iliyotangulia inafafanua mambo matatu yaliyo adhimu kabisa:

1. Upendo:

Huu ni dhamana inayokusanya watu pamoja kwenye huruma na ihsani, na hasa kwa wale waliofungamana nasi zaidi kushinda jamaa

zetu wote, nao ni kiwiliwili chetu na damu yetu, yaani watoto.

2. Huruma:

Hili ni kimbilio kubwa la binaadamu ambalo hukusanya mapenzi na uaminifu katika ukumbi wake. Mambo mawili haya husaidia kuleta yaliyo bora kwa watu.

3. Kutelekeza ahadi:

Kufanya hivyo kwa baba juu ya watoto wake kunaonyesha namna upendo wa ndani ulio imara na huruma vinavyounganisha uhusiano wao, na hivyo ndivyo tulivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Fikra za mzazi anayemtimizia ahadi mtoto wake baadaye huwa maishani mwake ni moja kati ya kukuza tabia ya kutangamana.

Kutangamana kwa wazazi na watoto wao, humpatia mtoto

sifa na tabia njema na hutengeneza mwenendo wake. Amesema Mtume(s.a.w.w) : Kueni dhamana (mtangamane) na watoto wenu.

Hapa Mtume(s.a.w.w) anakusaidia kwamba watoto wasiachiwe bila ya kupatiwa chakula, wasitupwe, au kuachiwa watu wengine (wasiohusika) kuwaangalia, kwani kufanya hivyo kutawafadhaisha na kuwatia hatarini. iii. Mwalimu aliye mfano bora, na kumfundisha mtoto nidhamu Amesema Utba bin Sufyani wakati alipokuwa akimweleza mwalimu wa mtoto wake: Mfano kwa mtoto wangu uwe ni mfano wako (vile ufanyavyo), kwani macho yao (watoto) siku zo te huwa yanaangalia machoni kwako. Chochote kizuri watakachokiona machoni kwao kitakuwa ndicho kile kizuri ulichokiona wewe, na chochote kiovu watakachokiiga kitakuwa ni kile ulichokionelea.

Amesema Ibn Khaldun akieleza kuhusu Rashid alipokuwa akimwambia mwalimu wa mtoto wake Al-Amin kwamba: Kiongozi amekuamrisha kwa furaha ya moyo wake uwe dhamana kwake (mtoto), na umfanye akutii, uwe kama anavyokutaka uwe: Msomeshe Qurani, mfundishe elimu na bayana, mfundishe namna ya kuhifadhi na kusoma mashairi, mfafanulie kuhusu elimu ya Hadith za Mtume, muonyeshe namna ya kuanza na kumaliza hotuba, asicheke ila kwa sababu. Tena usiache hata saa moja ipite bila kutumia nafasi hiyo kwa kumfundisha jambo lenye faida, na usiache kujihusisha na hivyo kumsumbua na kuichosha akili yake. Usimwache awe goigoi, mfundishe adabu kadri ya uwezo wako lakini kwa uaminifu na huruma.

Wanavyuoni mabingwa wa fikra za kiislamu kama al-Ghazaali, Ibn Khaldun na Ibn Muskawieh, wamesisitiza umuhimu wa malezi mazuri ya mtoto, adabu na mwenendo mzuri. Mtume(s.a.w.w) amesema: Kila mtoto huzaliwa katika maumbile ya kihulka .

Amesema Mwenyezi Mungu:

....ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumba watu.. (30:30). Kufunza adabu ni jambo la kwanza linalotakiwa apatiwe mtoto wakati wa utoto ili ajizoeshe kuwa na mwenendo mwema na tabia nzuri.

Amesema Mtume(s.a.w.w) :Kumfunza adabu mmoja wenu mtoto wake ni bora kwake kuliko kutoa sadaka ya nusu pishi kila siku.

Tunapowafunza adabu watoto wetu, huwa tunasaidia kuweka msingi imara kwa taifa letu na hivyo ndivyo mafunzo ya Kiislamu yanavyotutaka tutekeleze. Uislamu kwa kufuatilia unatutaka tufanye hivyo na kwa njia kama hiyo na ndio maana ukayapita majaribio yote ya kumfunza adabu mtoto. Uilsamu umeunganisha malezi mazuri na zawadi ambayo inatunzwa na kupewa wenye kufunza adabu.

Kwa maana hiyo, Uislamu umewapa moyo wazazi kuwalea vizuri watoto wao.

Mtume(s.a.w.w) amesema:Wakirimuni watoto wenu na muwape adabu.

v. Uislamu na malezi ya kujitegemea kwa mtoto

Wakati Uislamu ulipowapa wazazi ju kumu la kuwalisha watoto wao na kuwaongoza, haukudharau kwa vyovyote vile uwezo alionao mtoto mwenyewe, kwa kufanya hivyo, Uislamu haukusudii kuwafanya wazazi wa mtoto kuyafikiria na kuyapanga maisha yake yote kabisa na wakati huo huo awe akiwategemea wao kabisa. Hata hivyo, Uislamu umekusudia kuwafanya wazazi wawalinde na kuwaongoza watoto wao wadogo, wasiwapotee njia kwa kuingia mashakani na kwenye dhana.

Uislamu umewaamuru wazazi kuwaongoza na kuwalisha watoto wao tu, bila kujiingiza sana katika shughuli zao.

Maoni ya Uislamu kuhusiana na malezi ya mtoto yamefafanuliwa zaidi na Muhammad Rashid Ridha kwa mifano mingi katika tafsir ya Al Manar.

Imethibithishwa katika matukio mbali mbali kwamba kujitegemea kwa mtoto ndiyo mwanzo wa kuunda vizazi vyema na watu barabara wa kutegemewa watakaoweza kuchukua jukumu la kujenga taifa.

Imetajwa katika ushauri kwa mzazi ya kwamba:Cheza na mtoto wako mpaka atakapofikia umri wa miaka saba, kisha mfundishe adabu kwa miaka mingine saba ijayo, kisha uwe suhuba naye kwa miaka mingine saba ijayo, kisha baadaye mwache ajitegemee.

Ni jambo la muhimu sana kumruhusu mtoto ahudhurie katika majadiliano na kutoa maoni yake, japo maoni yake yatakuwa ni ya kijuujuu tu, na ya kuchekesha, au yasiyohusiana na suala linalozungumziw a hapo, inaweza kuwa pia kumdhihaki si jambo la busara, bali ni vizuri wazazi wawe na bidii ya kumfahamisha pale anapokosea wakati wa kutafakari au kuamua. Anapaswa kutiwa moyo kusema kwa kile hasa anachokifikiria kuwa ni sawa. Kwa kufanya hivyo, bila shaka kutanufaisha mambo yafuatayo:

1. Siku zote hataogopa kutoa maoni yake.

2. Ataweza kujisahihisha na kila alilokosea ama kwa kutofahamu vizuri upande wake, na hilo litamfanya kurekebisha maoni yake na kuchukua uamuzi ufaao.

3. Wakati watu wazima watakapopata shauri (juu ya jambo fulani) atajifunza kutoka kwao uamuzi wa sawa, na jinsi ya kukata shauri katika mambo mbali mbali.

4. Atakuwa anafahamu jinsi ya kujadiliana katika mambo na kuweza kupata suluhisho la matatizo, ili asiachwe hivi hivi tu bila ya kuweza kutatua matatizo.

5. Atakuwa ameandaliwa katika kupambana na mikasa ya kimaisha.

6. Hii pia itamsaidia kutojiamulia tu bila ya kufikiri, na itamfanya atambue matatizo, kwa hivyo, atajua jinsi ya kuyaelezea na kuyatatua yatakapomkabili wakati wa maisha yake na hatofadhaika. Mfano ni ule uliotokea kwa Abdalla bin Abbas, wakati Mtume(s.a.w.w) alipowaambia maswahaba zake: Mwenyezi Mungu amemfananisha Mwislamu mwenye imani na mti ambao hautupi ovyo majani yake. Kisha akawauliza: Je mwajua ni mti gani huo? Wote wakanyamaa, kisha Mtume(s.a.w.w) mwenyewe akajibu: Huo ni mtende.

Walipokuwa wakienda nyumbani, Abdallah bin Abbas huku akifuatana na baba yake alimwambia baba yake kuwa alijua jibu la swali alilouliza Mtume(s.a.w.w) lakini aliogopa kusema mbele za kadamnasi ya watu, kwani huenda ikawa ni makosa kufanya hivyo. Baba yake akamwambia:

Lau kama ungelijibu, basi ingekuwa jambo kubwa kwangu kuliko kupata mifugo iliyo bora.

Uislamu na kumuelimisha mtoto Uislamu unawataka waislamu kutafuta elimu. Kutafuta elimu ni wajibu kwa kila Mwislamu awe ni mwanamume au mwanamke. Haikuamrishwa kwa jinsia moja ya watu au nyingine tu, au kikundi fulani cha watu au kingine, kwani (elimu) inaongoza maisha ya watu. Jamii ya watu iliyoundwa kwa elimu na yenye watu walioelimika, ndiyo jamii iliyo bora kushinda zote, kwa kuwa watu wamepata umashuhuri na ufanisi kwa ajili ya elimu. Kwa sababu kama hizo, kanuni za Kiislamu zinapigania sana elimu ambayo itaongoza watu (ya mwenye kuelimika), na itastawisha jamii ya watu wote.

Ili kufikia lengo hili, inasemekana kwamba katika vile vita mashuhuri vya Badr, Mtume(s.a.w.w) aliamuru kila mateka anayejua kusoma na kuandika, aliyeshikwa katika vita hivi, aachiliwe huru iwapo atawafundisha watoto kumi wa kiislamu jinsi ya kusoma na kuandika.

Vile vile Mtume(s.a.w.w) amesema:Wafundisheni watoto wenu kwani, wao wamezaliwa katika zama tofauti na zama zenu.

Amesema tena:Tafuteni elimu hata kama ni (kwenda) China. Uislamu unaagiza kwamba, waislamu wafanye kila wawezalo kutafuta elimu hata kama itawabidi kusafiri mbali kama China kwa ajili ya kutafuta elimu. Ni dhahi ri Uislamu jinsi unavyotetea elimu, hasa tukizingatia kwamba aya yake ya kwanza tu kushuka inazungumzia elimu kama alama ya uongofu. Imetajwa katika Qur ani:

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ ﴿١﴾ خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ ﴿٢﴾ اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ ﴿٣﴾ الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ ﴿٤﴾ عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ ﴿٥﴾

Soma! Kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba mwanaadamu kwa pande la damu. Soma! Na Mola wako ni Mkarimu sana, ambaye amemuelimisha mwanaadamu kwa njia ya kalamu. Amefundisha mwanaadamu mambo aliyokuwa hayajui (96:1-5).

Kisha amesema tena:

الرَّحْمَـٰنُ ﴿١﴾ عَلَّمَ الْقُرْآنَ ﴿٢﴾ خَلَقَ الْإِنسَانَ ﴿٣﴾ عَلَّمَهُ الْبَيَانَ ﴿٤﴾

(Mwenyezi Mungu) Mwingi wa Rehma; amefundisha Qurani, amemuumba mwanadamu, akamfundisha kusema (kwa ufa saha). (55:1-4).

Elimu katika Uislamu haikuwekewa mipaka ya kusoma kitabu maalum au mtunzi maalum tu, bali inahusisha chochote kile ambacho akili inahitajia kusoma na kuongeza mbinu mbalimbali za maarifa. Amirul-Muminin, aliwataka Waislamu kuwafunza wato to wao hata kuogelea, kutupa mishale na kutoa shoti farasi. Kutupa mishale na kupanda farasi ilikuwa ndiyo burudani (kubwa) ya maisha yote ya Waarabu zama hizo, na lau Amirul- Mu minina angeishi hivi leo, basi angeongezea mengine mengi katika hayo aliyoyas ema, (kama kompyuta n.k) ili yaende sambamba na wakati na hali ya mabadiliko ya jamii katika maisha ya kisasa.

vi. Umuhimu wa vidude vya kuchezea watoto (toys)

katika Uislamu Vijidude vya kuchezea na michezo mbali mbali (toys), vinaleta furaha na burudani katika maisha ya mtoto. Vijidude hivyo pia hupanua akili ya mtoto ya kielimu.

Mtume(s.a.w.w) amesema:Mwenye kwenda sokoni, na akanunua kitu cha kuchezea (watoto) akakichukua mpaka kwa watoto wake, huwa ni kama aliyechukua sadaka na kuwapelekea watu wahitaji, basi na aanze kuwapatia watoto wa kike kwanza kabla ya watoto wa kiume.

Umuhimu huu alioupa Mtume(s.a.w.w) kuhusiana na vitu vya kuchezea sijambo la kupuuzwa, kwani kufanya hivyo ni muhimu kama kutoa sadaka kwa wahitaji.

Imeelezwa kwamba watoto wa kike wapatiwe kwanza, ili kuwaridhisha na kuwafurahisha. Haya ndiyo mambo ambayo Uislamu unayapigania ambayo lau tutayatafuta, maisha yetu na ya watoto wetu yatajawa na furaha na Baraka. Nguvu na uzuri wa misingi hii inatoa mfano mzuri kwa jinsi ilivyoamuru kuhusiana na watoto wetu - kiburudisho cha macho yetu.

Mtoto mwema huwa ni mwenye kuendeleza ufanisi wa baba yake, na ni hazina nzuri kwa taifa lake. Mtume(s.a.w.w) amesema:Mtoto mwema ni mrihani (mti wenye harufu nzuri) miongoni mwa mirihani ya Peponi. Mwenyezi Mungu atuangazie na atuongoze katika kuwalea vizuri watoto wetu ambao ni furaha ya maisha yetu. Amin.