TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Juzuu 2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 20444
Pakua: 4036


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 20444 / Pakua: 4036
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Juzuu 2

Mwandishi:
Swahili

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI

﴿ الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ وَإِنَّ فَرِيقًا مِّنْهُمْ لَيَكْتُمُونَ الْحَقَّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴾

146.Wale tuliowapa Kitabu wanamjua yeye kama wanavyowajua watoto wao. Na hakika kundi katika wao wanaificha haki na hali wanaijua.

﴿ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ ﴾

147.Haki ni iliyotoka kwa Mola wako. Basi usiwe miongoni mwa wanaofanya shaka.

WANAMJUA KAMAWANAVYOWAJUAWATOTO WAO

Aya 146-147

MAANA

Wale tuliowapa kitabu wanamjua kama wanavyowajua watoto wao. Yaani: wanavyuoni wengi wa Kiyahudi na wa Kikristo wanajua kwa usahihi na uwazi Utume wa Muhammad(s.a.w.w) ; kama wanavyowajua watoto wao, kwa namna isiyokuwa na shaka yoyote. Kwa sababu Tawrat na Injil zimetoa bishara ya kuja kwake na zikamtaja kwa sifa zake na alama zake ambazo hazikupatikana kwa mwingine yeyote. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ﴾

...Wanamkuta ameandikwa kwao katika Taurat na Injil... (7:157)

﴿ وَإِذْ قَالَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُم مُّصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنَ التَّوْرَاةِ وَمُبَشِّرًا بِرَسُولٍ يَأْتِي مِن بَعْدِي اسْمُهُ أَحْمَدُ فَلَمَّا جَاءَهُم بِالْبَيِّنَاتِ قَالُوا هَـٰذَا سِحْرٌ مُّبِينٌ ﴾

Na aliposema Issa bin Maryam: Enyi wana wa Israil! Mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, nisadikishaye yaliyokuwa kabla yangu katika Tawrat na kutoa bishara ya Mtume atakayekuja baada yangu ambaye jina lake ni Ahmad. Lakini alipowajia kwa hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio wazi (61:6).

Abdallah bin Salam alikuwa ni mmoja wa maulamaa wa kiyahudi; kisha akasilimu. Miongoni mwa maneno aliyosema ni: Mimi ninaujua zaidi Utume wa Muhammad kuliko ninavyomjua mwanangu. Alipoulizwa kwa nini, alisema: Mimi sitii shaka kwamba Muhammad ni Mtume, lakini mtoto wangu, pengine mama yake amefanya hiyana.

Na hakika kundi katika wao wanaificha haki na hali wanaijua .

Ndio! wanaficha, hata kama wangeliona jina la Muhammad katika Lauhul Mahfudh, kwa sababu ya kupupia uongozi wa duniani na maslahi ya kibinafsi. Inadi hii ya kuficha haki haihusiki na Mayahudi na Wakristo tu, Kwani sababu ya kuficha haki ni ya kijumla. Tumekwisha waona baadhi ya Masheikh wanakana sifa za wenzao kwa sababu ya chuki na hasadi tu.

Haki ni iliyotoka kwa Mola wako, basi usiwe miongoni mwa wanaofanya shaka .

Mtume(s.a.w.w) hawezi kutia shaka yale yaliyotoka kwa Mola wake na ni muhali kuyatilia shaka; na Mwenyezi Mungu anajua kuwa Mtume wake Mtukufu hawezi kutia shaka. Lengo la Aya hii ni kubainisha kwamba aliyomteremshia Muhammad hayana shaka wala matatizo yoyote kabisa. Mtu akiyakanusha na kuyapinga basi atakuwa anafanya hivyo kwa inadi na ukaidi tu.

MIMI NA MHUBIRI

Tarehe 15-7-1963 alinitembelea mtaalamu wa mambo ya nchi za mashariki Mkristo kutoka Italia ambaye alikuwa akizungumza lugha ya Kiarabu vizuri. Basi tukawa na mjadala kwa mdomo na kwa maandishi. Miongoni mwa aliyosema ni kuwa: Quran inakiri wazi wazi kuhusu Injil, kwa nini Waislamu wanaikana? Nikamjibu kuwa: Quran inakiri Injil iliyobashiri Utume wa Muhammad(s.a.w.w) ; kama ilivyosema:

﴿ وَمُبَشِّرًا بِرَسُولٍ يَأْتِي مِن بَعْدِي اسْمُهُ أَحْمَدُ﴾

...Na mwenye kutoa bishara ya Mtume atakayekuja baada yangu ambaye jina lake ni Ahmad... (61:6).

﴿ يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ ﴾

...Wanamuona ameandikwa kwao katika Tawrat na Injil... (7:157). Kisha Quran inaendelea kusema:

﴿ إِنَّ مَثَلَ عِيسَىٰ عِندَ اللَّـهِ كَمَثَلِ آدَمَ خَلَقَهُ مِن تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُن فَيَكُونُ﴾

Hakika mfano wa Issa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kwa udongo kisha akamwambia kuwa basi akawa. (3:59)

Injil yenu inasema: Issa ni Mungu, sasa vipi mnatutaka tuiamini na wakati huo huo tuiamini Quran? Ikiwa Wakristo wanakataa kupingana na kukosana katika hukumu ya akili tu, na kukubali kuwa akili inaweza kupingana na kutoafikiana katika dini na itikadi, basi Waislamu wanaliona hilo ni muhali; haliwezekani kiakili na kidini na katika kila kitu. Kwa sababu misingi ya dini kwao inakuwa ndani ya akili tu.

﴿ وَلِكُلٍّ وِجْهَةٌ هُوَ مُوَلِّيهَا فَاسْتَبِقُوا الْخَيْرَاتِ أَيْنَ مَا تَكُونُوا يَأْتِ بِكُمُ اللَّـهُ جَمِيعًا إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴾

148.Na kila mmoja ana mwelekeo anaouelekea. Basi shindaneni kufanya mema. Popote mtakapokuwa, Mwenyezi Mungu atawaleta nyote pamoja. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

﴿ وَمِنْ حَيْثُ خَرَجْتَ فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَإِنَّهُ لَلْحَقُّ مِن رَّبِّكَ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴾

149Na popote uendapo utakako kuwa elekeza uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu; na hiyo ndiyo haki itokayo kwa Mola wako. Na Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika na yale mnayoyatenda.

﴿ وَمِنْ حَيْثُ خَرَجْتَ فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّوا وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَيْكُمْ حُجَّةٌ إِلَّا الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْهُمْ فَلَا تَخْشَوْهُمْ وَاخْشَوْنِي وَلِأُتِمَّ نِعْمَتِي عَلَيْكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ ﴾

150.Na popote utakapotoka utakokuwa elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu, na popote mlipo elekezeni nyuso zenu upande (uliko msikiti) huo ili watu wasiwe na hoja juu yenu, isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Basi msiwaogope, niogopeni Mimi, ili niwatimizie neema Zangu na ili mpate kuongoka.

﴿ كَمَا أَرْسَلْنَا فِيكُمْ رَسُولًا مِّنكُمْ يَتْلُو عَلَيْكُمْ آيَاتِنَا وَيُزَكِّيكُمْ وَيُعَلِّمُكُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُعَلِّمُكُم مَّا لَمْ تَكُونُوا تَعْلَمُونَ ﴾

151. Kama tulivyomleta Mtume kwenu anayetokana na nyinyi, anayewasomea Aya zetu na kuwatakasa na kuwafundisha Kitabu na hekima na kuwafundisha mliyokuwa hamyajui.

﴿ فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ وَاشْكُرُوا لِي وَلَا تَكْفُرُونِ ﴾

152.Basi nikumbukeni nitawakumbuka, na nishukuruni wala msinikufuru.

KILA UMMA ULIKUWA NA QIBLA CHAKE

Aya ya 148-152

MAANA

Na kila mmoja ana mwelekeo anaoulekea . Alipotaja Mwenyezi Mungu Qibla ambacho amewaamrisha Waislamu kukielekea ambacho ni Al Kaaba, na akataja kuendelea kwa Mayahudi na Manaswara kuelekea mielekeo yao, alibainisha kuwa siri ya kungangania huku kwamba kila umma ulikuwa na Qibla chake uliojichagulia kuelekea na wala haukiachi, hata kama ubaya wa mwelekeo wenyewe uko wazi kama jua. Kwa hiyo kauli Yake hii inafanana na kauli Yake:

﴿كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ﴾

...Kila kikundi kinafurahia kilicho nacho (30:32). Hayo ndiyo niliyoyafahamu kutokana na dhahiri ya tamko. Wafasiri wameleta kauli nyingi katika Aya hii; mwenye Majmau ametaja nne.

Basi shindaneni kufanya mema .Popote mtakapokuwa Mwenyezi Mungu atawaleta nyote pamoja, hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu .

Yaani achaneni na watu wa Kitab na washirikina walio wakaidi, na mfanye amali njema. Kwani marejeo yenu kesho ni kwake Mwenyezi Mungu, ambapo atalipwa thawabu mwenye haki na mwenye kufanya wema na kuadhibiwa mwenye batili mtenda maovu. Kama wanavyosema wafasiri maana ya:Popote mtakapokuwa Mwenyezi Mungu atawaleta nyote pamoja, ni ahadi ya thawabu kwa watiifu na kiaga cha adhabu kwa waasi. Ama kusema kwake:Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, ni dalili na sababu ya kuwezekana kufufuliwa viumbe baada ya mauti.

Na popote uendapo elekeza uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu.

Unaweza kuuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu hapa amekariri kuelekea Msikiti Mtakatifu mara tatu na katika Aya ya 149 mara mbili; yaani amekariri mara tano mfululizo?

Jibu : Mwenye Majmaul-Bayan ametaja kauli tatu, na Razi ameleta tano. Miongoni mwa kauli hizo ni lile jibu lililozoeleka linalorithiwa ambalo ni, kutilia mkazo na umuhimu. Nafsi yangu haikutulia kabisa katika kauli hizo. Na mimi sina chochote cha kusema isipokuwa huenda kukariri huku hapa ni kutokana na jambo lililohusu wakati huo ambalo hatulijui. Kuna mambo mengi ambayo hayaingii katika udhibiti na hisabu. Inajulikana wazi kuwa mapokezi ya Aya na sababu zake yako ya kiujumla na mahsusi, na haifai kwa yeyote kutafsiri au kuleta taawili, kwa kutegemea dhana bila ya kupata asili yake yoyote.

Ili watu wasiwe na hoja juu yenu.

Wafasiri wengi wamesema kuwa Mtume(s.a.w.w ) alipokuwa akiswali kuelekea Baitil Maqdis; Washirikina na Waarabu wakasema: Vipi Muhammad anadai kwamba yeye yuko kwenye dini ya Ibrahim, na wala haswali kuelekea Al Kaaba aliyokuwa akiswali Ibrahim na Ismail? Na watu wa Kitab wakasema Yaliyo katika Vitabu vyetu ni kwamba Mtume atakayeletwa katika kizazi cha Ismail ataswali kuelekea Al Kaaba na wala sio Baitul Maqdis, sasa vipi tunaweza kuukubali Utume wa Muhammad. Kwa hiyo wakaifanya kuwa hoja, wanayoitumia kwa dhana yao. Mwenyezi Mungu akambadilishia Qibla kuelekea Al Kaaba na akaifanya ndio Qibla cha kudumu kwa Mtume na Waislamu wote mpaka siku ya malipo, ili hawa na wengine wasibakiwe na hoja yoyote.

Dhahiri ya jumla inafahamisha kwamba: kuswali kuelekea Al Kaaba kunavunja hoja ya wapinzani. Ama kuwa ni kina nani hao wapinzani, Aya haikubainisha. Inawezekana kuwa njia ya kukata hoja ya wapinzani ni kuwa Al Kaaba imejengwa na Ibrahim(a.s) na akaswali hapo. Hilo ni lenye kuafikiwa na wote na Muhammad atafuata mwendo wa Ibrahim.

Isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao.

Yaani hakuna hoja yoyote juu yako ukiswali, isipokuwa kwa mpinzani asiye na haki ambaye hategemei dalili za kiakili katika upinzani wake wala uongozi wa kidini isipokuwa kung’ang’ania, na ukaidi.

Basi msiwaogope,niogopeni Mimi.

Yaani msiogope lawama katika haki, Mimi pekee ndiye ninayewamilikia manufaa na madhara. Ibnul Arabi katika tafsiri yake anasema: Maana ya niogopeni ni; jueni Utukufu Wangu ili makafiri wasijifanye watukufu kwenu. Amirul Muminin(a.s) anasema:Amekuwa mkubwa Muumbaji katika nafsi zao akawa mdogo asiyekuwa yeye katika macho yao .

Na ili niwatimizie neema zangu na ili mpate kuongoka.

Yaani nimewaneemesha kwa Uislamu na nimewatimizia neema kwa kuwapa Qibla chenu kilichowafanyia umoja na kuwakusanya na kinachoelekewa na watu wa mataifa mbali mbali ya pembe zote za dunia, yenye makabila na lugha mbali mbali.

KATIBA YA UISLAMU

Mtaalamu mmoja anasema kuwa katiba ya Uislamu ina vipengele vitatu: Mwenyezi Mungu mmoja, Kitabu kimoja na Qibla nimoja. Waislamu hukusanyika kutoka pembe zote za dunia kila mwaka ili wamwabudu Mwenyezi Mungu mmoja kwa sharia hiyo moja kwenye nchi mmoja, nchi ya mji wa kiroho. Hivi ndivyo ulivyokuwa umoja wa itikadi, sharia na mji, ili wakumbuke Waislamu kwamba wao hata kama wakitofautiana miji, lugha, rangi na nasaba, lakini wanakuwa wamoja kwa dini, wanaabudu Mwenyezi Mungu mmoja na ni wananchi wa nchi mmoja.

Kama tulivyomleta Mtume kwenu anayetokana na nyinyi, anayewasomea Aya zetu na kuwatakasa na kuwafundisha Kitabu na hekima na kuwafundisha mliyokuwa hamyajui.

Wanavyuoni wana maneno mengi na marefu katika maana ya neno hekima. Tunavyofahamu sisi ni kuwa kila kinachowekwa mahali pake panapostahili, kiwe ni kitendo au kauli, basi ni hekima.

Hali yoyote iwayo, maana ya jumla ya Aya hii ni kwamba: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewaneemesha Waarabu kwa Qibla; kama alivyowaneemesha kwa Muhammad(s.a.w.w) ambaye ni katika wao na anatokana na wao. Amewapa umbo jipya; akawatwaharisha na uchafu wa shirk na tabia mbaya. Kwa hiyo, kwa fadhila zake, wakawa ni watu wa dini na sharia ya Mwenyezi Mungu ambayo misingi yake ni uadilifu na usawa; kama ambavyo wamekuwa na dola iliyopanuka, mpaka lugha yao ikawa kubwa na ikaenea kwa sababu ya Quran na fasihi yake.

Hapana mwenye kutia shaka kwamba lau si Muhammad na kizazi cha Muhammad, Waarabu wasingelikuwa na historia wala turathi zozote; wasingekuwa na chochote zaidi ya kuabudu masanamu, ujinga na kuwazika watoto wa kike wakiwa hai, ili kuepuka gharama za kuwalisha. Bali Muhammad(s.a.w.w) , Mwarabu, ni neema kubwa juu ya watu wote. Kwa sababu yake, watu wamepiga hatua za haraka katika nyanja za elimu na maendeleo. Uhakika huu wameukiri na kuusajili wataalamu wa Kimagharibi wale wasiokuwa na ubaguzi, na tumeyanakili baadhi katika kitabu Al-Islam Wal-aql (Uislamu na Akili). Kwa ajili ya neema hiyo aliyowaneemesha Waarabu, ndio Mwenyezi Mungu akawataka wamkumbuke na kumshukuru na akahadharisha wasije wakaikufuru neema na hisani, kwa kusema:

Basi nikumbukeni nitawakumbuka na nishukuruni wala msinikufuru.

Yaani nikumbukeni kwa utii nami nitawakumbuka kwa malipo na thawabu. Na mnishukuru juu ya neema ya Uislamu na Utume kwa Muhammad ambaye anatokana na nyinyi wala msinikufuru. Mahali pengine Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ ﴾

...Kama mkishukuru nitawazidishia, na kama mkikufuru basi adhabu yangu ni kali sana. (14:7).

Amirul Mumini Ali(a.s) alisema:Mwenyezi Mungu hawezi kufungua mlango wa shukrani na akafunga wa malipo . Anaendelea kusema:Mkumbukeni sana Mwenyezi Mungu, kwani huo ndio ukumbusho mzuri, na kuweni na raghba katika aliyowaahidi wanaomcha Mwenyezi Mungu, kwani ahadi Yake ni ya kweli sana .

KUMSHUKURU MNEEMESHAJI

Moja kwa moja akili inafahamu kuwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ni wajibu kwa kila aliye baleghe mwenye akili, hata kama isingeshuka Aya yoyote au kuja Hadith yoyote ya kuwajibisha kushukuru. Kwani Yeye Mtukufu ndiye Muumbaji Mwenye kuruzuku. Maana ya kumshukuru Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kuitakidi kwamba Yeye ndiye mwanzilishi na kwamba Yeye ni muweza wa kila kitu: ni kutii amri Zake na makatazo Yake na kutegemeza mambo kwake peke Yake. Hayo ni kwa upande wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.), Ama mtu akimfanyia wema mtu kama yeye, je inapasa, yule aliyefanyiwa wema kumshukuru aliyemfanyia wema, kiasi ambacho kama hakumshukuru kwa namna fulani atakuwa ni mwasi mwenye kustahiki adhabu? Hapana mwenye kutia shaka kwamba kumshukuru aliyekutendea wema ni jambo zuri, bali hiyo ni alama ya watu wema. Ama kuwa ni wajibu au la, hakuna dalili juu yake. Kwa hiyo kila habari iliyokuja kuhusu kumshukuru mwenye kutoa neema asiyekuwa Mwenyezi Mungu, Mtume au Ahlul Bait wake, ni pendekezo tu ya kuwa ni vizuri; kama alivyosema Ali(a.s) :Ukiwa unammudu adui yako, basi ufanye msamaha ndio shukrani ya uwezo huo wa kummudu.

Kumsamehe aliyekufanyia ubaya sio wajib, lakini ni Sunna kwa Ijmai. Ama msemo unaosemwa sana: Asiyeshukuru kiumbe ndio hamshukuru Muumba, hiyo ni hukumu ya kimaadili tu, siyo ya lazima. Hata hivyo kukanusha neema na kumwambia aliyekufanyia wema: Hukufanya wema ni haramu, kwa sababu ni uwongo; na kumfanyia uovu ndio haramu kabisa, kwa sababu uovu ni haramu kwa dhati yake, hata kwa mtu asiyekufanyia wema. Lakini pamoja na hayo wajibu wa kushukuru ni jambo jingine na uharamu wa uwongo na uovu ni jambo jingine.

﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ﴾

153.Enyi mlioamini! Takeni msaada kwa subira na swala; hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.

﴿ وَلَا تَقُولُوا لِمَن يُقْتَلُ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتٌ بَلْ أَحْيَاءٌ وَلَـٰكِن لَّا تَشْعُرُونَ ﴾

154.Wala msiseme kwamba wale waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni wafu, bali wa hai lakini nyinyi hamtambui.

﴿ وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ ﴾

155.Na hakika tutawajaribu kwa chembe ya hofu na njaa na upungufu wa mali na wa nafsi na wa matunda, Na wape bishara wanaosubiri.

﴿ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ ﴾

156.Ambao ukiwapata msiba, husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na Kwake Yeye tutarejea.

﴿ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ ﴾

157.Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao na rehema, na hao ndio wenye kuongoka.

TAKENI MSAADAKWA SUBIRA

Aya 153-157

SUBIRA

Enyi mlioamini! Takeni msaada kwa subira na swala; hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.

Mwenye Tafsiri ya Al-Manar anasema kuwa: Subira (uvumilivu) katika Quran imetajwa mara sabini. Hiyo inafahamisha umuhimu wake, na Mwenyezi Mungu ameijaalia ni kitu cha kuusiana katika Sura Al Asr kwa kuikutanisha na haki, kwani mwenye kuilingania haki hana budi kuwa nayo.

Mwenye Bahrul Muhit ameiweka mbali sana aliposema: Subira na swala ni nguzo mbili za Uislamu.Ameghafilika na Hadith inayosema: Umejengwa Uislamu juu ya mambo matano: Kushuhudia kuwa hakuna Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, kusimamisha swala, kutoa zaka, kufunga mwezi wa Ramadhan na kuhiji Makka kwa mwenye kuweza njia ya kuendea. Subira haimo katika nguzo hizo. Pia ameghafilika kuwa kuna taklifa za lazima ambazo Mukallaf anatakiwa kuzifanya na ataadhibiwa kwa kuziacha; kama, swala kulipa deni, n.k. Na kuna taklifa nyingine ambazo ni za kimwongozo, zimekuja kinasaha, zinafanana na amri, lakini mukallaf hawezi kuadhibiwa kwa kuziacha; kama usafi, kuosha mikono kabla ya kula, kukatazwa kushiba sana, n.k. Sasa yako wapi haya na nguzo za dini, ambazo mwenye kuziacha anakuwa ametoka katika dini? Kisha subira haisifiwi hiyo yenyewe hasa, isipokuwa inasifiwa ikiwa ni nyenzo ya kufikilia jambo kuu; kama subira katika jihad takatifu, subira juu ya ufukara na uhitaji, subira kwa ajili ya kuipata elimu na subira juu ya matatizo ya familia na kulea watoto. Vile vile subira juu ya kumwokoa mwenye kudhulumiwa, subira juu ya kauli ya mtu mpumbavu kwa kukinga shari, au kufanya subira kwa kumkosa mpenzi asiyesahaulika. Kwani kuendelea kufazaika ni kuzidisha msiba; kama alivyosema Amirul Muminin Ali(a.s) :

Mwenye kuyakuza masaibu madogo,Mwenyezi Mungu humwingiza kwenye makubwa.

Bazar Jamhar aliulizwa: Kwa nini ewe mfalme mwenye hekima husikitiki kwa yaliyokupita wala hufurahi kwa yaliyopo? Akasema: Yaliyopita hayawezi kufutika kwa majonzi wala yaliyopo hayawezi kudumu kwa furaha.

Mwingine alisema: Siwezi kusema kitu kilichokwisha kuwa na tamani kisingekuwa au ambacho hakikuwa natamani kingekuwa. Mara nyingine subira huwa mbaya; kama kusubiri juu ya njaa na uwezo wa kufanya kazi upo, na kusubiri juu ya ukandamizwaji. Katika hali hii subira nzuri ni kumkabili dhalimu.

Unaweza kuuliza, kuna uhusiano gani kati ya swala na subira mpaka zikakutanishwa pamoja katika Aya?

Jibu : Maana ya subira ni kutulizana moyo ingawaje una machungu. Hiyo inahitajia kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuamini kuwa Yeye Yu pamoja na wenye kusubiri. Hakuna mwenye shaka kwamba swala inatilia mkazo mategemeo haya na ni hakikisho la imani hii, kuongezea kwamba kumwomba Mwenyezi Mungu kunapunguza machungu ya masaibu.

Wala msiseme kwamba wale waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni wafu, bali wa hai, lakini nyinyi hamtambui.

Mfano wa Aya hii ni kama nyingine isemayo:

﴿ وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ﴾

Wala usiwadhanie wale waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni wafu, bali wa hai wanaruzukiwa kwa Mola wao. (3:169).

Inajulikana kuwa kila anayefariki hurejea kwa Mola wake, awe mwema au mwovu, shahidi au asiyekuwa shahidi; isipokuwa kwamba mwema anaondoka kwenye maisha ya chini kwenda kwenye maisha ya juu na mwovu inakuwa kinyume chake.

Hapa imehusishwa kutajwa shahidi; ama ni kwa kueleza cheo chake mbele za Mwenyezi Mungu kwa kuhimiza ushahidi; au ni kwa kutokana na yaliyonakiliwa kutoka kwa Ibn Abbas, kwamba Aya ilishuka kwa sababu ya waliouliwa katika vita vya Badr ambao ni Muhajirin kumi na nne na Ansar wanane; ikasemwa ameuawa fulani na fulani; ndipo ikashuka Aya hii. Haya hayako mbali, kwani kauli ya Mwenyezi Mungu: Msiwaite wafu, inafahamiisha hilo. Vyovyote iwavyo, ambalo tunapaswa kuamini ni kwamba mwenye kufa shahidi kwa kuupigania Uislamu au kitu chochote kinachofungamana na haki, uadilifu na utu, atakuwa anahama kutoka ulimwengu unaoonekana kwenda kwenye ulimwengu usioonekana na huko atakuwa na maisha mema. Na kwamba yeye anatofautiana na aliyekufa kifo cha kawaida. Amirul Muminin anasema:Naapa kwa yule ambaye nafsi ya mtoto wa Abu Twalib iko mikononi mwake, kupigwa mapigo elfu ya panga ni bora kwangu kuliko kufa kitandani. Ama hakika ya maisha ya shahidi baada ya mauti na kuhusu riziki anayoneemeshwa ni jambo tusilolijua na wala hatuna haja ya kulifanyia utafiti. Kwa sababu ni jambo tusilokalifishwa kulijua.

THAMANI YA PEPO

Na hakika tutawajaribu kwa chembe ya hofu na njaa na upungufu wa mali na wa nafsi na wa matunda. Na wapashe habari njema wanaosubiri.

Yeyote anayefuata haki ni lazima aigharimie kwa nafsi yake, watu wake au mali yake; na kila haki inavyokuwa kubwa, ndivyo gharama inavyokuwa kubwa, lau kama si hivyo wanaopigania haki wasingelikuwa na fadhla yoyote; na watu wote wasingelifuata haki. Kwa hali hiyo ndiyo tunapata tafsiri ya Hadith hii tukufu:Misukosuko amepewa mumin . na kwamba:wenye misukosuko zaidi ni Mitume; kisha wanaowafuatia . Vile vile misukosuko ya Mitume inakuja kwa kadiri ya daraja zao. Mtume mtukufu(s.a.w.w) amesema:Hakuudhiwa Mtume kama nilivyoudhiwa mimi .

Amirul Muminini amesema:Hakika haki ni nzito lakini nzuri, na batili ni hafifu, lakini mbaya. Inatosha kuwa ni ushahidi kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿مْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِكُم مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاءُ وَالضَّرَّاءُ ﴾

Mnadhani kuwa mtaingia peponi, na hali hamjajiwa na mfano wa wale waliopita kabla yenu? Yaliwapata mashaka na madhara... (2:214).

Aya hii inafahamisha kuwa pepo haipati isipokuwa mwenye kujitolea mhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu, Na kujitolea mhanga hakuwi katika uwanja wa vita vya jihadi na watu wa shirk peke yake, bali machukivu yoyote anayoyavumilia mtu kwa ajili ya kuipigania haki na uadilifu ni kujitoa mhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na ni thamani ya pepo; hata kama kupigania kwenyewe ni kwa neno la kumjibu dhalimu kumsaidia mwenye haki.

Baada ya kuingilia kuandika tafsiri, nimekuwa na yakini isiyo na shaka yoyote kwamba hataingia peponi isipokuwa yule aliyeudhiwa na akavumilia kwa subira, ijapokuwa ni ukandamizwaji na balaa katika njia ya haki na uadilifu. Kwa uchache ni kuifunga nafsi yake na yaliyoharamishwa au kufanya juhudi kwa ajili ya mwingine; hata kama ni mzazi au mtoto. Kipimo cha pepo ni kuvumilia mashaka kwa kumridhisha Mwenyezi Mungu. Ama kuingia peponi kutokana na raha mstarehe ni jambo lililo mbali sana.

Ambao ukiwapata msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye tutarejea.

Maana ya:hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, ni kukiri ufalme na utumwa; na maana ya:kwake Yeye tutarejea, ni kukubali ufufuo baada ya mauti. Kisha kujaribiwa kwa misukosuko ni mtihani ambao unadhihirisha hakika ya mtu. Mumini mwenye akili hayumbishwi na misukosuko; wala hawezi kupayuka payuka na maneno ya ukafiri na ufasiki na ujinga, bali anakuwa na subira; wala misukosuko haiwezi kumwondolea akili yake na imani yake. Ama mwenye akili na imani dhaifu anatawaliwa na shetani, anafuata mwenendo wote wa kufuru na shutuma na hushuka chini kwenye udhalili. Kauli nzuri kuhusu haya ni ile ya bwana wa mashahidi, Hussein bin Ali, siku ya msiba wa Karbala:Watu ni watumwa wa ulimwengu na dini iko kwenye ndimi zao, wanaipeleka kule kwenye maisha yao wakijaribiwa na misukosuko, huwa wachache wenye dini.

Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao, na rehema.

Baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni takrima na ni cheo cha juu; na rehema Yake kwa waja wake ni huruma yake kwao na kuwaongoza kwenye heri na kuwaneemesha.

Katika Hadith imeelezwa:Hakuna Mwislamu yeyote aliyepatwa na masaibu, akakimbilia amri ya Mwenyezi Mungu kwa kusema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake Yeye tutarejea. Ewe Mola wangu Wewe ndiwe unayeyatoshea masaibu yangu, basi nilipe katika masaibu hayo na unipe badali bora, isipokuwa Mwenyezi Mungu humlipa na humpa badali bora.

AINA YA MALIPO YA WANAOSUBIRI

Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewapa wenye kusubiri aina nane za malipo na utukufu:

1. Mapenzi: Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَاللَّـهُ يُحِبُّ الصَّابِرِينَ ﴾

...Na Mwenyezi Mungu anawapenda wanao subiri . (3:146).

2. Ushindi: Mwenyezi Mungu anasema:

﴿إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴾

...Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanao subiri. (2:153).

3. Ghorofa za peponi: Mwenyezi Mungu anasema:

﴿أُولَـٰئِكَ يُجْزَوْنَ الْغُرْفَةَ بِمَا صَبَرُوا ﴾

Hao ndio watakaolipwa ghorofa kwa kuwa walisubiri. (25:75).

4. Malipo mengi: Mwenyezi Mugnu anasema:

﴿إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴾

Hakika wanaosubiri watapewa ujira wao pasipo hisabu... (39:10)

5. Bishara: Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ﴾

Na wape bishara wanaosubiri. (2:155).

6 & 7. Baraka na rehema: Mwenyezi Mungu anasema:

﴿أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ﴾

Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao na rehema. (2:157).

8. Uongofu: Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ ﴾

Na hao ndio wenye kuongoka (2:157)

﴿إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا وَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَإِنَّ اللَّـهَ شَاكِرٌ عَلِيمٌ ﴾

158.Hakika Swafaa na Mar-wa ni katika alama za Mwenyezi Mungu. Basi anayehiji kwenye nyumba hiyo au akafanya Umra,si kosa kwake kuvizunguuka. Na anayefanya heri, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye shukrani (na) Mjuzi.

SWAFA NA MARWA

Aya 158

LUGHA

Swafa na Mar-wa ni vilima viwili vilivyoko Makka karibu na Al Kaaba. Mahujaji na wanaofanya Umra huenda Saay kati ya vilima hivyo.

MAANA

Hakika Swafa na Mar-wa ni katika alama za Mwenyezi Mungu.

Ibada ziko namna mbali mbali na wakati mbali mbali. Kwa kuangalia wakati, kuna zile za kila siku ambazo ni swala, na nyingine ni za kila mwaka ambazo ni kufunga Ramadhani na pia iko ya mara moja tu, katika umri nayo ni kuhiji kwa mwenye kuweza. Hijja ni moja ya nguzo tano zilizojengewa Uislamu, ambazo ni: Shahada mbili, kusimamisha swala, kutoa zaka, kufunga Ramadhan na kuhiji Al Kaaba. Umrah ni ada kama Hijja, lakini katika Umrah hakuna kwenda Arafa, wala kulala Muzdalifa au kutupa mawe Mina. Utakuja ufafanuzi wake Inshaallah katika Aya ya 196 na Sura nyingine zinazozungumzia hilo. Kwa ujumla ni kwamba aina zote za ibada ikiwemo Hijja hazina nafasi ya kufanyiwa Ijtihadi wala kuelezwa sababu yoyote; isipokuwa inatosha nasi (nukuu) ya Quran na Hadith tu na kila ambalo litazidi hayo, Mungu (s.w.t.) hajaliridhia.

Linaloonyeshwa na Aya hii, ni kwamba Swafa na Mar-wa ni sehemu za kufanyiwa ibada kunakoonyeshwa na kauli yake:

Basi anayehiji kwenye nyumba hiyo au kufanya Umra, si kosa kwake kuvizunguka .

Kuzunguka huku ndiko kunakojulikana kwa jina la Saay kati ya Safa na Mar-wa. Ama namna ya kufunya Saay na idadi ya mizunguko yake na kuanzia Safa, utakuja ubainifu wake mahali pake Inshaallah. Unaweza kuuliza: kufanya Saay kati ya Swafa na Mar-wa katika Hijja ni wajibu kwa Ijmai pamoja na kuwa ibara ya: Si kosa, inafahamisha kufaa jambo hilo na wala sio lazima na kwamba hakuna dhambi kuliacha?

Jibu : Kauli yake Mwenyezi Mungu: Si kosa, haikuja kubainisha hukumu ya Saay kuwa ni wajibu au la, isipokuwa imekuja kubainisha kuwa Saay ni sharia na Uislamu unaikubali na kuithibisha. Ama maarifa ya hukumu yake na je, ni faradhi au ni sunna, hayo yanafahamishwa na dalili nyingine.

Zimekuja Hadith mutawatir za Mtume na wamekongamana Waislamu juu ya wajibu wa kufanya saay katika Hijja ya Kiislamu. Katika Majmaul-Bayan anasema Imam Jaffar Sadiq amesema:Waislamu walikuwa wakiona kwamba Swafa na Marwa ni mambo yaliyozushwa wakati wa Jahiliya, ndipo akateremsha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Aya hizi. Yaani anaziondoa dhana hizi na kubainisha kwamba Swafa na Mar-wa vinatokana na Uislamu tangu asili; washirikina wakivizunguukia huwa wanajikurubisha kwa masanamu, lakini Waislamu huwa wanavizungukia kwa kumtii Mwenyezi Mungu na kufuata amri yake.

Na anayefanya heri basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye shukrani (na) mjuzi.

Yaani anayefanya wema kwa kufanya Saay kati ya Safa na Mar-wa baada ya kutekeleza wajibu alionao, basi Mwenyezi Mungu atamlipa wema kwa wema wake. Shaakir (mwenye shukrani) ni katika sifa za Mwenyezi Mungu, na maana ya Mwenyezi Mungu kumshukuru mja wake mtiifu, ni kuwa radhi naye na kumpa thawabu kutokana na shukrani yake na utiifu wake.