4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI
﴿وَمَثَلُ الَّذِينَ كَفَرُوا كَمَثَلِ الَّذِي يَنْعِقُ بِمَا لَا يَسْمَعُ إِلَّا دُعَاءً وَنِدَاءً صُمٌّ بُكْمٌ عُمْيٌ فَهُمْ لَا يَعْقِلُونَ﴾
171.Na mfano wa wale waliokufuru, ni kama mfano wa anayempigia kelele asiyesikia ila wito nasauti tu; ni viziwi, mabubu, vipofu kwa hivyo hawafahamu.
MFANO WAANAYEITAASIYESIKIA
Aya 171
MAANA
Mwenyezi Mungu katika Aya hii anawapigia mfano makafiri ambao wamengangania dini ya mababa, akawafananisha na wanyama na akamfananisha na mchungaji, yule anayewalingania kwenye haki, Kama ambavyo wanyama hawafahamu chochote katika maneno ya mchungaji isipokuwa sauti wanayoizowea baada ya kuzoweshwa; vile vile makafiri hawafahamu haki wala manufaa ambayo wanalinganiwa. Kwa hakika wao ni kama viziwi japo wanasikia; ni kama mabubu japo wanasema, na ni kama vipofu japo wanaona. Aya nyingi za Quran hazimtofautishi kiziwi asiyeweza kusikia kabisa na yule anayeisikia haki wala asiitumie; kama vile Aya hii tuliyo nayo:
Asiyesikia ila wito na sauti tu Na kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿إِنَّمَا يَسْتَجِيبُ الَّذِينَ يَسْمَعُونَ﴾
Wanaokubali ni wale wanaosikia...
(6:36). Na kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ قَالُوا سَمِعْنَا وَهُمْ لَا يَسْمَعُونَ﴾
Wala msiwe kama wale wanaosema: Tumesikia, na kumbe hawasikii.
(8:21)
Unaweza kuuliza kuwa dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewafananisha Makafiri na Mchungaji wanyama sio wanyama; kwa vile amesema:
Na mfano wa wale waliokufuru nikama mfano wa yule anayemwita asiyesikia.
Inavyoelekea nikuwa anayeita ni mchungaji na asiyesikia ni mnyama, sasa imekuwaje? Jibu: Hapa kuna kukadiriwa maneno ambako ni hakika mfano wa wanaowalingania makafiri kwenye haki ni kama mfano wa anayemwita asiyesikia. Hili limefahamika kutokana na mfumo wa maneno ulivyo.
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ وَاشْكُرُوا لِلَّـهِ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ ﴾
172.Enyi mlioamini! Kuleni vizuri tulivyowaruzuku na mumshukuru Mwenyezi Mungu ikiwa mnamwabudu Yeye tu.
﴿إِنَّمَا حَرَّمَ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةَ وَالدَّمَ وَلَحْمَ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ بِهِ لِغَيْرِ اللَّـهِ فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴾
173.Hakika amewaharamishia mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichosomewa kwa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Basi aliyefikwa na dharura bila kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira, Mwenye kurehemu.
KULENI VIZURI
Aya 172-173
MAANA
Baada ya Mwenyezi Mungu kuwaambia watu wote kwa kauli yake kuleni vilivyomo ardhini amerudia kusema tena, lakini akiwahusisha waumini:
Enyi mlioamini! kuleni vizuri tulivyowaruzuku
.
Ili awabainishie kwamba imani sahihi sio kujizuia na vitu vizuri, kama wanavyofanya baadhi ya watawa, makasisi na wengineo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametuhalalishia kustarehe na maisha na neema za kimwili na akatuamrisha kuzishukuru; na maana ya kuzishukuru ni kuzitumia katika njia inayotakikana. Amirul Muminin Ali
anasema:Uchache zaidi wa yanayowalazimu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni kutozitumia neema zake kwa kumwasi
. Huenda wale wenye jaha na utajiri, wakapata onyo kutokana na hekima hii iliyo fasaha ili wasizame katika anasa iliyoharamishwa na kuwa na kiburi na kupetuka mipaka.
Hakika ameharamshia mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilisomewa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
Hakuna mwenye shaka kwamba makusudio ya uharamu hapa ni uharamu wa kitendo ambacho ni kula sio uharamu wa kitu chenyewe. Kwani kitu hakiwezi kutajwa kwa uhalali na uharamu. Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja, katika Aya iliyotangulia, uhalali wa vinavyoliwa, hapa anatupa aina nne ya vilivyo haramu kuliwa:
1. Mfu: Ni kila mnyama aliyekufa bila ya kuchinjwa kisheria.
2. Damu: Makusudio ni damu iliyojitenga na nyama, kwa sababu iliyo pamoja na nyama inasamehewa.
3. Nguruwe: Nyama yake, mafuta yake na mwili wake wote, kinyume na anavyosema Daud Dhahiri aliposema: Ni haramu nyama ya nguruwe tu, sio mafuta yake, kwa kuchukulia dhahiri ya tamko, eti Aya imetaja nyama tu. Ilivyo ni kwamba imetajwa nyama kwa sababu ndio inayotumika zaidi.
4. Kilichochinjiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu: yule aliyetajiwa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni sawa kuchinjwa kwa ajili ya masanamu matambiko, mazindiko au vitu vingine. Hekima ya kuharamishwa aina tatu za kwanza ni kiafya ambayo watabibu wanaijua. Ama hekima ya kuzuia kile kilichotajiwa aisyekuwa Mwenyezi Mungu, ni ya kidini yenye lengo la kuchunga Tawhid na kumwepusha Mwenyezi Mungu na ushirikina. Kwa ujumla ni kuwa ni wajibu kumtaja Mwenyezi Mungu (s.w.t) wakati wa kuchinja. Mwenye kuacha kufanya hivyo kwa makusudi, basi alichoTafsir kichinja ni haramu, ni sawa iwe aliacha kwa kujua au kutojua. Ama akiacha kwa kusahau, basi haiwi haramu. Inatosha kutaja Allahu Akbar au Alhamdulillah au Bismillah au Lailaha illa Ilahu, n.k. Ufafanuzi zaidi unaweza kuupata katika vitabu vyetu vya Fiqh; kama vile kitabu chetu cha Fiqh Imam Jaffar Sadiq
Unaweza kuuliza; Dhahiri ya Aya inafahamisha kwamba hakukuharamishwa isipokuwa aina hizi nne tu za vyakula, kwa sababu neno tu linafaahamisha mambo mawili: Kwanza, kuthibitisha yale yanaelezwa ambayo hapa ni kuharamishwa vitu vinne. Pili: Kukanusha ambako hapa ni kutoharamishwa vitu vingine ispokuwa vitu hivi vine tu; na ilivyo ni kuwa kuna vyakula vingine vilivyoharamishwa; kama mbwa, wanyama wanoshambulia, wadudu, baadhi ya samaki. n.k.
Jibu
: Ndio dhahiri ya Aya inafahamisha hivyo, lakini halitumiwi hilo baada ya kongamano la wanavyuoni na kuthibiti Hadith za Mtume. Hii siyo Aya pekee ambayo dhahiri yake imeachwa na kongamano la wanavyuoni kutokana na Hadith.
MWENYE DHARURA NA HUKUMU YAKE
Basi aliyefikwa na dharura bila kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi.
Mwenye dharura ni yule ambaye anahofia nafsi yake kufa ikiwa hatakula kitu cha haramu, anayehofia kuzuka maradhi au kuzidi maradhi, kuhofia madhara na adha juu ya nafsi nyingine yenye kuheshimiwa; kama vile mwenye mimba kuogopea mimba yake au mwenye kunyonyesha kumhofia mwanawe; au mwenye kulazimishwa kwa nguvu kula au kunywa kitu cha haramu, kwa namna ambayo kama hakufanya hivyo atapata adha ya nafsi yake au mali yake au utu wake. Yote haya na mifano yake ni katika mambo yaliyosamehewa katika kutumia kitu cha haramu, lakini kwa kiasi kile tu kinachoweza kuondoa madhara. Kuanzia hapo ukawa mashuhuri msemo wa mafaqihi: Dharura hupimwa kwa kiasi chake. Hilo linafamishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: Basi aliyefikwa na dharura bila kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Mwenye kutamani ni yule anayefanya haramu bila ya dharura, na mwenye kupitisha kiasi ni yule anayepitisha kiasi cha haja.
﴿إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ مِنَ الْكِتَابِ وَيَشْتَرُونَ بِهِ ثَمَنًا قَلِيلًا أُولَـٰئِكَ مَا يَأْكُلُونَ فِي بُطُونِهِمْ إِلَّا النَّارَ وَلَا يُكَلِّمُهُمُ اللَّـهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلَا يُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴾
174.Hakika wale wafichao aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu katika Kitabu na wakanunua kwacho thamani ndogo, hao hawali matumboni mwao isipokuwa moto: wala Mwenyezi Mungu hatawasemesha siku ya Kiyama, wala hatawatakasa; na wao wana adhabu chungu.
﴿أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ اشْتَرَوُا الضَّلَالَةَ بِالْهُدَىٰ وَالْعَذَابَ بِالْمَغْفِرَةِ فَمَا أَصْبَرَهُمْ عَلَى النَّارِ﴾
175.Hao ndio walionunua upotevu kwa uongofu, na adhabu kwa maghufira. Basi ni ujasiri ulioje wa kuvumilia Moto?
﴿ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ نَزَّلَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ وَإِنَّ الَّذِينَ اخْتَلَفُوا فِي الْكِتَابِ لَفِي شِقَاقٍ بَعِيدٍ ﴾
176.Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameteremsha Kitabu kwa haki, na wale waliohitalifiana katika Kitabu (hiki) wamo katika upinzani ulio mbali.
WAFICHAO ALIYOYATERMSHA MWENYEZI MUNGU
Aya 174-176
MAANA
Hakika wale wafichao aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu katika Kitabu na wakanunua kwacho thamani ndogo.
Inasemekana kuwa Aya hii imewashukia wale walioficha sifa za Muhammad(s.a.w.w)
na Utume wake. Kwa vyovyote itakavyokuwa sababu ya kushuka Aya, makusudio yatakuwa ni kwa kila mwenye kujua kitu chochote katika haki akakificha kwa kuleta tafsiri nyingine au kubadilisha kwa manufaa yake binafsi; awe ni Myahudi, Mkristo au Mwislamu. Kwa sababu tamko ni lenye kuenea na linalozingatiwa ni kuenea tamko si kuhusika sababu za kushuka kwake. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemtisha mpotevu huyu katika Aya nyingi; miongoni mwazo ni zile zilizotangulia (Aya ya 146 na 159) na zitakazofuatia katika Sura Al-Imran, Nisa, Maida na Aya hii tuliyonayo. Zote hizo ni hasira za Mwenyezi Mungu na kiaga kikali cha adhabu na mateso. Kwa sababu ni wajibu haki itukuzwe na kutangazwa kwa kila njia na kuondoa mikanganyo yote ya kutofahamika. Vile vile kumpiga vita mwenye kuipinga kwa nguvu zote na kujitoa mhanga kwayo; Kwani hakuna msimamo wa dini, wala nidhamu au uhai isipokuwa kwa haki.
Hao hawali matumboni mwao isipokuwa moto.
Yaani: adhabu wanayostahili katika moto. Hiyo ni katika kuelezea kinachosababishwa ambacho ni moto na kinachosababisha ambacho ni kula haramu. Ametaja matumbo, ingawaje inajulikana kuwa kula hakufanywi isipokuwa kwa ajili ya tumbo, ili kuonyesha kuwa linalowashughulisha wao ni kujaza matumbo yao tu.
Wala Mwenyezi Mungu hatawasemesha siku ya Kiyama.
Ni fumbo la kuachana nao na kuwakasirikia wala hatawatakasa na madhambi kwa kuwasamehe.
Hao ndio walionunua upotevu kwa uongofu
.
Upotevu ni kufuata matamanio na uongofu ni kufuata kitabu cha Mwenyezi Mungu. Kubadilisha upotevu kwa uongofu ni kuathirika na batili kuliko haki.
Basi ni ujasiri ulioje wa kuvumilia moto?
Huku sio kuelezea ujasiri wao kwa moto wala sio kustaajabu kunakotokana na kutojua sababu ya jambo, hilo haliwezekani kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.), kwani anajua kila kitu. Isipokuwa makusudio hapa ni kuonyesha namna ya kujitia ujasiri kwao kwa kuacha hukumu zake na mipaka yake, na kufuata upotevu na batili. Kwa hiyo makusudio ni kuleta picha ya hali yao hiyo na kufananisha marejeo yao ambayo haiwezekani kuyafanyia ujasiri kwa vyovyote. Razi anasema: Walipojiingiza kwenye lile linalowajibisha moto, wamekuwa kama wenye kuridhia adhabu ya Mwenyezi Mungu na kuwa majasiri wa adhabu hiyo; sawa na kumwambia yule anayejiingiza kwenye lile linalo kasirisha serikali: Ni ujasiri ulioje wako kufungwa jela? Unaweza kuuliza: Tumejua hiyo ndiyo hali ya yule mwenye kuijua haki na akaificha; sasa ni ipi hali ya asiyejua chochote katika yalivyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, lakini pamoja na hayo anasema: Hii ni haramu na hiyo ni halali, na wala hana chochote cha kutegemea isipokuwa dhana na kuwazia tu? Jibu: Huyu ana hali mbaya zaidi kuliko yule anayeijua haki na akaificha. Kwa sababu yeye amejiweka daraja ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na kujifanya ndio msingi wa sharia, wa kuhalalisha na kuharamisha.
MVUTANO KATI YA HAKI NA BATILI
Mwenye tafsir ya Al-Manar amemnakili Sheikh Muhammad Abduh kwamba amesema katika kuifasiri Aya hii: Katika Waislamu kuna wanaoficha yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu kwa kugeuza na kuleta taawili, sawa na wanavyofanya Mayahudi kuficha sifa za Mtume. Waislamu hawa wanatambua mivutano miwili inayopingana mvutano wa haki waliyoijua na mvutano wa batili waliyoizoweya. Hayo yanawatingisha na kuwaathiri, na haya yanawapa kiburi na chuki. Akili zao zimeshinda yale waliyoyajua na nyoyo zao zimeshinda yale waliyoyazowea, wakathibiti kwenye yale waliyoyazua; wakawa katika vita kati ya akili na dhamiri. Wakifikiria kesho (akhera), starehe za sasa (duniani) zinawatokea puani, lakini wanapoonja utamu wa wanayofanya wanasahau yatakayokuja. Je, huku kuhisi kuitweza haki na kuinusuru batili sio moto unaowaka mbavuni mwao? Je thamani ya haki wanayoila si miti ya miba ambayo hainenepeshi wala kuondoa njaa? Hayo ni sahihi kwa upande wa baadhi ya wale wanaojitilia shaka katika dhamiri zao na kujilaumu, wakiwa wanafanya dhambi. Lakini wengine wamezoweya batili mpaka ikawa ni tabia yao, na kuliona adui kila lenye harufu ya haki na utu.
Wakati ninapoandika maneno haya ni mwezi June 1967. Katika mwezi huu ulio na shari, Israil imevamia baadhi ya sehemu za miji ya Waarabu kwa msaada wa Uingereza na Marekani, na wamewatoa watu majumbani mwao, wakawafukuza zaidi ya watu laki mbili na nusu (250,000), wakawachoma wake kwa waume na watoto kwa mabomu ya Napalm. Wengi wameunga mkono fedheha hii na kufurahishwa nayo; wanatamani lau Israil ingeendelea na uovu wake. Mapenzi ya nafsi yamezidi akili na dhamiri zao mpaka zikaisha zote bila ya kubaki athari yoyote, wakawa sawa na wanyama. Ndipo Mwenyezi Mungu akawaita kuwa ni watu wasio na akili; wasiofahamu na kwamba wao ni wanyama, bali ni wapotevu zaidi kuliko wanyama.
Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameteremsha Kitabu kwa haki.
Hayo ni ishara ya adhabu itakayowashukia wale wanaoficha haki. Na, kauli yake Mwenyezi Mungu: Ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameteremsha Kitabu, ni kubainishwa sababu za adhabu ambazo ni kuthubutu kwao kuwa wajasiri wa kuihalifu haki iliyokuja katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Na wale waliohitalifiana katika kitabu wamo katika upinzani ulio mbali.
Wafasiri wamehitalifiana katika makusudio ya kauli hii, Wafasiri wengi, akiwemo mwenye Majmaul Bayan wamesema ni makafiri; na namna ya kuhitalifiana kwao hao makafiri ni kwamba kuna katika wao waliosema kuwa Quran ni uchawi, wengine wakasema ni utenzi na wengine wakasema ni vigano vya watu wa kale. Baadhi ya wafasiri wamesema makusudio ya waliohitalifiana ni Waislamu, kwamba wao baada ya kuafikiana kuwa Quran inatoka kwa Mwenyezi Mungu, wamehitilafiana katika kuifasiri na kuleta taawili; wakagawanyika kwenye vikundi. Ilitakiwa wao wawe na tamko moja kwa vile Quran ni moja. Inawezekana kuwa makusudio ni makafiri, lakini sio kwa kuwa wengine walisema kuwa Quran ni uchawi, utenzi au vigano, bali ni kwamba wao ndio sababu pekee ya kuhitilifiana, kupigana na kuacha kuafikiana na tamko la haki kati yao na wale walioamini Quran.
﴿لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ وَآتَى الْمَالَ عَلَىٰ حُبِّهِ ذَوِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَالسَّائِلِينَ وَفِي الرِّقَابِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُوا وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ﴾
177.Sio wema kuelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi tu, lakini wema ni wa anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na malaika na Kitabu na manabii; na akawapa mali, akiwa aipenda ,jamaa na mayatima na masikini na mwananjia na waombao, na katika ukombozi wa watumwa; na akasimamisha swala na akatoa zaka; na watekelezao ahadi zao wanapoahidi, na wanaokuwa na subira katika shida na dhara na katika wakati wa vita. Hao ndio waliosadikisha na ndio wenye takuwa.
ANATOA MALI AKIWAAIPENDA
Aya 177
LUGHA
Kila amali ya heri ni wema. Mwananjia ni msafiri asiyesafiri kwa maasia, akaishiwa na mali asiweze kurudi kwake. Madhara ni kila linalomdhuru mtu, iwe ni maradhi au kumkosa mpenzi, n.k.
MAANA
Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameyataja mambo aliyoyazingatia kuwa ni nguzo ya wema, uchaji Mungu na imani ya kweli. Mambo hayo kuna yanayofungamana na itikadi, yanayofungamana na kutoa mali, yanayofungamana na ibada na yale yanayofungamana na akhlaq. Kabla ya kufafanua ameanza kwa kusema:
Sio wema kuelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi tu.
Maneno haya waanaambiwa watu wote, hata kama sababu ya kushuka ni mahsusi. Kwa sababu, la kuzingatia ni hayo maneno kwa ujumla sio sababu za kushuka kwa Aya. Makusudio ni kuwaambia waumini na wanaoswali, kwamba kuswali tu upande maalum, sio heri ya dini iliyokusudiwa. Kwa sababu swala imewekwa kwa ajili ya kuwa mwenye kuswali amwelekee Mwenyezi Mungu peke yake na kuachana na wengine. Baada ya utangulizi huu, ameingilia kubainisha misingi ya itikadi ambayo ndiyo nguzo ya wema, na ameikusanya katika mambo matano ambayo yamekusanywa na kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t)
Lakini wema ni wa anayemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na Malaika na kitabu na Manabii.
Kumwamini Mwenyezi Mungu ndio msingi wa amali njema inayo sababisha kumtii Mwenyezi Mungu katika yote aliyoyaamrisha na kuyakataza. Kuamini Malaika ni kuamini wahyi ulioteremshwa kwa Mitume; na kuwakana Malaika ni kuukana wahyi; Mwenyezi Mungu anasema:
﴿ نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الْأَمِينُ ﴿١٩٣﴾ عَلَىٰ قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنذِرِينَ ﴾
Ameiteremsha Roho mwaminifu juu ya moyo wako, ili uwe miongoni mwa waonyaji.
(26: 193-194).
Kuamni Kitabu ni kuamini Quran na Manabii na kuamini sharia zao. Mambo yote haya matano yanarejea kwenye mambo matatu; Kuamini Mwenyezi Mungu , Utume na siku ya mwisho. Kwa sababu kuamini Utume kunachanganya kuamini Malaika na kitabu. Baada ya hayo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaashiria taklifa za kimali kwa kauli yake:
Na akawapa mali akiwa aipenda.
Imesemekana kuwa dhamiri katika kupenda inamrudia Mwenyezi Mungu, kwa vile limetangulia jina lake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika kauli yake: Mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu Na imesemekana kuwa dhamiri inarudia mali na inakuwa kama kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿لَن تَنَالُوا الْبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ﴾
Hamtapata wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda...
(3:92).
Vile vile kauli yake:
﴿وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا ﴾
Na huwalisha chakula masikini na mayatima na mateka na hali ya kuwa wenyewe wanakipenda.
(76:8).
Kauli hii ndiyo iliyo dhahiri zaidi, kwa sababu dhamiri inamrudia wa karibu zaidi, sio wa mbali. Kisha makusudio ya kutoa mali hapa sio zaka ya wajibu, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameunganisha na kutoa zaka na kuunganisha kunahukumilia kubadilika. Aya imetaja aina sita za wale ambao inatakikana kuwapa:
1. Jamaa - Nao ni jamaa wa mwenye mali, kwa sababu wao ndio wenye haki zaidi ya kuwatendea wema. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ﴾
Na wale katika nyinyi wenye fadhila na wasaa wasiape kutoawapa akraba
(24:22).
Ni wajibu kumlisha jamaa aliye karibu, ikiwa ni mzazi na mtoto, ikiwa wanashindwa kujilisha. Ama wasiokuwa hao inakuwa kuwapa ni Sunna sio wajibu, kama wanavyosema Mafaqihi ( [2]
).
2. Mayatima - ambao hawana mali wala mlezi wa kuwatunza. Kwa hiyo itakuwa ni wajibu kwa wenye uwezo kuwalea, ikiwa hakuna hazina ya Waislamu (Baitul-maal).
3. Maskini - wale wenye haja ambao hawawanyooshei watu mkono wa udhalili (hawaombi).
4. Mwananjia - Yule ambaye ameishiwa safarini asiyeweza kurudi kwao bila ya msaada.
5. Wenye kuomba wale ambao wanawa-nyooshea watu mikono ya udhalili. Jambo hilo limeharamishwa kisheria isipokuwa kwa dharura ya hali ya juu; sawa na dharura ya kula mfu. Dalili tosha ya uharamu wake ni kwamba ni udhalili na utwevu, na udhalili huo wenyewe ni haramu uwe umetokana na mtu mwengine au na yeye mwenyewe. Kuna Hadith inayosema: Si halali kupewa sadaka tajiri na mwenye nguvu aliye mzima wa mwili.
6. Watumwa- Yaani kununua watumwa na kuwaacha huru kwa kuwakomboa utumwani. Lakini maudhui haya hayapo siku hizi kutokana na kutokuwepo utumwa. Kwa ujumla aina hizi sita alizozitaja Mwenyezi Mungu ni kwa njia ya mfano, sio kwamba hizo ndio zote. Yako mambo mengi ambayo ni vizuri kuyatolea mali; kama kujenga shule, vituo vya mayatima, mahospitali, kuilinda dini na nchi na mengineyo yanayohusu Umma kwa ujumla. Ikiwa heshima ya mtu itavunjika isipokuwa kwa kutoa mali, basi ni wajibu kuitoa kwa mwenye kuweza; na lolote ambalo wajibu fulani hauwezi kutekelezeka isipokuwa kwa kufanya jambo hilo, basi ni wajibu kulifanya. Mwenyezi Mungu ameashiria nguzo ya kutenda wema ya kiibada kwa kauli yake:
Na akasimamisha Swala na akatoa Zaka
.
Swala ni ya kutakasa nafsi, Saumu ni ya kutakasa mwili na zaka ni ya kutakasa mali. Ameashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwenye nguzo ya maadili kwa kusema:
Na watekelezao ahadi zao wanapoahidi
.
Ahadi inayopaswa kutekelezwa iko namna mbili. Ya kwanza, ni ile inayokuwa kati ya mja na Mola wake; mfano Yamini Nadhiri na ahadi kwa sharti zilizotajwa katika vitabu vya Fiqh. Hayo tumeyafafanua katika Juzuu ya tano ya Kitabu Fiqhul-Imam Jaffar Sadiq
, Ya pili, ni aina ya ahadi ya muamala unaopita kati ya watu. Ni wajibu kuitekeleza; kama vile bei, ajira, deni n.k. Mumini mwema anatekeleza mambo yote yanayomlazimu; hata kama hakuna uthibitisho wa kulazimisha kutekeleza. Ama kutekeleza kiaga sio wajibu kisheria, bali ni Sunna Kifiqh Miongoni mwa tabia nzuri zenye kusifiwa ni subira (uvumilivu) ambayo ni katika nguzo za wema, yenye kuonyeshwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
Na kuwa na subira katika shida na dhara na wakati wa vita.
Shida ni ufukara, na dhara ni maradhi, n.k. Makusudio ya kuvumilia ufukara na maradhi sio kuyaridhia, kwani Uislamu umewajibisha kuhangaika na kufanya juhudi kwa kadri iwezekanavyo, ili kujitoa katika ukata, maradhi, ujinga, na kila linalorudisha nyuma maendeleo. Makusudio yake hasa ni kutosalimu amri kabisa katika shida na kuwa na mshikamano na kufanya kazi kwa uthabiti na bidii ili kujikwamua na yaliyowapata. Baadhi ya wafasiri wanasema: Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja uvumilivu katika mambo matatu: (ufukara, maradhi na vita), pamoTafsir ja na kuwa uvumilivu unatakiwa katika hali zote, kwa sababu hali hizo tatu ni miongoni mwa balaa na mitihani mikubwa. Mwenye kuvumilia hayo, basi anaweza kuvumilia mengine.
Hao ndio waliosadikisha na ndio wamchao Mungu.
Hao ni ishara ya wale ambao wamekusanya mambo yote haya yaliyotajwa - misingi ya itikadi, kutoa mali, kutekeleza ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na tabia nzuri. Hakika hao ni wakweli katika imani yao, wenye kuogopa ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu Yake. Ama wale wanaosema kwa vinywa vyao tu, kuwa tumeamini na wala wasitoe wanayoyapenda wala kutekeleza yanayowalazimu na kuvumilia katika shida. Wote hao wako mbali na wema.
WEMA KATIKA UFAHAMU WA KIQURAN
Aya hii imeonyesha mambo matano: Itikadi, taklifa za kimali, ibada, kutekeleza ahadi na kuvumilia shida. Haya mambo mawili ya mwisho ni katika mambo ya kimaadili. Kwa dhahiri ni kwamba ibada, kama swala na saumu ni athari ya imani na ni alama yake isiyoepukika nayo. Kwa sababu asiyeamini kuwapo Mungu, hawezi kumwabudu. Ama kutoa mali, kutekeleza ahadi na kuvumilia shida, hayo yanapatikana kwa anayemwamini Mwenyezi Mungu au kwa anayemkanusha. Kwani wengi wanaomwamini Mungu wanasema wasiyoyatenda, ni wabahili; hata kwenye nafsi zao na wanasalimu amri mbele ya shida. Lakini mara nyingine mkanushaji Mungu huweza kujitolea mhanga katika kupigania uadilifu na utu, anakuwa imara katika shida na kutekeleza anayoyasema. Kwa hivyo, kidhahiri, inaonyesha kuwa imani hailazimiani na tabia njema wala kufuru hailazimiani na tabia mbaya. . lakini ilivyo hasa hakuna imani bila takuwa (kumcha Mungu).
Lakini Aya hii (sio wema ...). Imezingatia imani kuwa pamoja na tabia njema bila ya kutengana, kwa maana yakuwa sio kumwamini Mungu pekee ndiko kutakakomfanya mtu kuwa mwema; wala tabia nzuri bila ya imani haiwezi kumfanya mtu awe mwema, bali hapana budi kumwamini Mwenyezi Mungu, kuwa na tabia njema na kumwabudu... Kwa hivyo basi mwema anavyoelezwa katika Quran ni Mumin mwenye kufanya ibada, mtekelezaji ahadi, mkarimu na mvumilivu.