5
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِصَاصُ فِي الْقَتْلَى الْحُرُّ بِالْحُرِّ وَالْعَبْدُ بِالْعَبْدِ وَالْأُنثَىٰ بِالْأُنثَىٰ فَمَنْ عُفِيَ لَهُ مِنْ أَخِيهِ شَيْءٌ فَاتِّبَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ وَأَدَاءٌ إِلَيْهِ بِإِحْسَانٍ ذَٰلِكَ تَخْفِيفٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَرَحْمَةٌ فَمَنِ اعْتَدَىٰ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَلَهُ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴾
178.Enyi mlioamini! Mmeandikiwa kisasi katika waliouawa; muungwana kwa muungwana na mtumwa kwa mtumwa na mwanamke kwa mwanamke. Na anayesamehewa na ndugu yake chochote, basi ni kufuatana kwa wema na kulipa kwa ihsani. Hiyo ni tahfifu itokayo kwa Mola wenu na rehema, Na atakeyeruka mipaka baada ya hayo, basi ana yeye adhabu iumizayo.
﴿وَلَكُمْ فِي الْقِصَاصِ حَيَاةٌ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴾
179.Mna uhai katika kisasi, enyi wenye akili, ili msalimike.
KISASI CHAWALIOUAWA MAANAAya
178 - 179
MAANA
Wanavyuoni wa sharia ya Kiislamu wamepanga namna tatu za adhabu:
1. Haddi; kama kukata mkono wa mwizi, kupigwa mawe hadi kufa kwa mzinifu aliye na mke, kupigwa viboko kwa mnywaji pombe, n.k. Utakuja ufafanuzi mahali pake Inshallah.
2. Diya (Fidia): Hiyo ni adhabu ya kimali.
3. Kisasi - kufanyiwa yule aliyefanya jinai kwa makusudi sawa na vile alivyomfanyia yule aliyemuua, au aliyemkata kiungo au aliyemjeruhi. Ama kupiga hakuna kisasi. Mafaqihi wameweka maelezo maalum kwa kila namna ya adhabu hizo tatu, na Aya hii inaingia katika kisasi.
Enyi mlioamini! mmeandikiwa kisasi katika waliouawa.
Wakati wa ujahiliya (kabla ya Uislamu) watu walikuwa hawana sheria yenye mpango; wanauana kidhulma na kiuadui, na kulipiza kisasi kwa watu wasiokuwa na hatia na wala sio kwa yule aliyekosa. Mtu wa kawaida akiuawa, basi watu wake wataua idadi kubwa ya watu wa muuaji. Na, kama mwanamke akimuua mwanamke mwenzake, basi mahali pake patachukuliwa na watu wa ukoo wake au kabila yake; wanaweza kuua hata watu kumi kwa mmoja tu. Dhuluma hii ilisababisha vita vya kikabila; watoto na wajukuu wakarithi uadui na chuki. Ndipo Mwenyezi Mungu akaweka sharia hii ya kisasi ambayo inafahamisha usawa na kisasi kiwe kwa yule aliyeua kwa hali yoyote awayo na wala sio watu wasiokuwa na makosa, na pia kusiweko na ziada au upungufu; kinyume na ilivyokuwa zama za ujahiliya. Na kwa sharti ya kuwa kuua kuwe ni kwa kukusudia sio kwa kukosea au bila kukusudia( [3]
).
Katika maana Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):
﴿أَنَّ النَّفْسَ بِالنَّفْسِ﴾
...Nafsi kwa nafsi...
(5:45).
﴿فَلَا يُسْرِف فِّي الْقَتْلِ إِنَّهُ كَانَ مَنصُورًا ﴾
...Lakini hiyo asipite kiasi katika kuua...
(17:33).
﴿وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِّثْلُهَا﴾
Na malipo ya ubaya ni ubaya ulio sawa na huo...
(42:40).
﴿فَمَنِ اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ فَاعْتَدُوا عَلَيْهِ بِمِثْلِ مَا اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ﴾
...Basi anayewachokoza mchokozeni kwa kadiri alivyowachokoza...
(2:194).
Muungwana kwa muungwana na mtumwa kwa mtumwa na mwanamke kwa mwanamke.
Maana yake yako wazi hayahitaji ufafanuzi. Hiyo ni ibara ya usawa katika kisasi kati ya muuaji na aliyeuliwa katika uhuru, utumwa na jinsia.
Unaweza kuuliza kuwa: Ufahamisho wa mfumo wa tamko unaonyesha kuwa muungwana hauawi kwa kumuua mtumwa. Na kama mwanamume akimuua mwanamke hauawi, Je wameafikiana Mafaqihi? Jibu: Hakika Aya imeonyesha aina tatu tu ambazo ni muungwana kumuua muungwana, mtumwa kumuua mtuwa na mwanamke kumuua mwanamke, na haikueleza aina ya nne ambayo ni muungwana kumuua mtumwa au mtumwa kumuua muungwana na mwanamume kumuua mwanamke au mwanamke kumuua mwanamume. Aya imefahamisha kwa matamko yake kwamba kisasi kimewekwa katika aina tatu za kwanza; na hayo wameafikiana Mafakihi, kwa sababu katika dhahiri ya Quran hakuna kuhitalifiana. Vile vile Aya haikukanusha au kuthibitisha kisasi katika aina nyingine, si kwa kimatamko wala kiufahamu,Kwa hiyo hapana budi kurejea kwenye dalili nyingine ya Hadith au ijmai. Mafaqihi wamehitalifiana katika hilo: Malik, Shafii na Hambal wanasema: Muungwana hauawi kwa kumuua mtumwa. Abu Hanifa anasema: Bali atauawa muungwana kwa kumuua mtumwa wa mtu mwingine, lakini hauawi kwa kumuua mtumwa wake. Wameafikiana wote wanne kwamba mwanamume atauawa kwa kumuua mwanamke na kinyume chake.
Shia Imamia wamesema: Muungwana akimuua mtumwa hauawi, bali atapigwa kipigo kikubwa na kutoa fidia ya mtumwa. Na mwanamke akiua mwanamume, watu wa aliyeuawa wanayo hiyari ya kuchukua fidia, kama huyo muuaji akikubali au kumuua, Kama wakichagua kuua, hapo watu wake hawatatoa chochote. Kama mwanamume ndiye aliyemuua mwanamke, basi watu wake wanayo hiyari ya kuchukua fidia kama muuaji akikubali au kumuua kwa masharti ya kuwapa warithi wa yule aliyeua nusu ya fidia ya mwanamume ambayo ni Dinar mia tano (500).
Na anayesamehewa na ndugu yake chochote, basi ni kufuatana kwa wema; na kulipa kwa ihsani.
Neno: chochote linafahamisha kwamba walii wa aliyeuawa, akisamehe chochote kinachofungamana na muuaji, kama kusamehe kumuua na kuridhia kuchukuwa fidia, basi inatakikana muuaji aukubali msamaha huu kwa wema. Imesemekana pia kuwa neno chochote linafahamisha kuwa, kama warithi wakiwa wengi na mmoja wao akamsamehe muuaji, basi hakuna kisasi, hata kama waliobakia watangangania kutaka kisasi. Vyovyote iwavyo, hakika Mwenyezi Mungu amejaalia kwa walii wa damu iliyomwagwa haki ya kisasi kutoka kwa aliyeua kwa makusudi. Haifai kumlazimisha muuaji atoe fidia ikiwa mwenyewe anataka kuuliwa, wala muuaji hawezi kumlazimisha walii wa aliyeuawa kuchukua fidia ikiwa mwenyewe anataka kulipiza kisasi cha kuua.
Inaruhusiwa kwa wote wawili kuafikiana kwa kufanyiana suluhu ya kiasi cha mali ya fidia, kiwe kichache au kingi, ili kiwe ni badala ya kisasi. Maafikiano hayo yakitimia basi itakuwa ni lazima kutekelezwa na wala haiwezekani kubadilisha. Ni juu ya walii wa aliyeuawa kumtaka muuaji badala ya kisasi kwa wema, bila ya kumtilia mkazo wala kumdhikisha au kuomba zaidi ya haki yake. Na ni juu ya muuaji kutoa mali kwa wema, bila ya kuchelewesha, kupunguza au kufanya hadaa yoyote.
Hiyo ni tahfifu itakayo kwa Mola wenu.
Yaani hekima ya kuwekwa fidia badala ya kisasi ni tahfifu na rehema kwenu.
Na atakayeruka mipaka baada ya hayo, basi yeye ana adhabu iumizayo.
Walikuwa baadhi ya watu wakati wa ujahiliya, wanaposamehe na kuchukua fidia, kisha wanapompata muuaji baadaye humuua. Hapo Mwenyezi Mungu akakataza kupetuka mipaka huku na akamwahidi adhabu iumizayo mwenye kuyafanya hayo. Baadhi ya wafasiri wanasema: Hakimu atamhukumu kuuliwa aliyemuua muuaji baada ya kupita msamaha; hata kama atatoa fidia na kuridhia walii wa aliyeuliwa. Lakini kauli hii ni ya kuonelea uzuri hivyo tu, na wala Aya haifahamishi hilo si kwa karibu wala mbali.
Mna uhai katika kisasi enyi wenye akili.
Hii ni sababu ya kuwekwa sharia ya kisasi na kubainisha hekima, na kwamba katika hukumu hiyo kuna kulinda kufanyiana uadui. Kwani mwenye kujua kwamba yeye atauliwa baada ya kuua, ataogopa. Ama kutoa mali sio kuzuia kuua, kwani watu wengi wangeliweza kutoa mali kwa sababu ya kuwakomoa maadui zao. Wafasiri wamerefusha maneno katika kubainisha ufasaha wa Aya hii na kuilinganisha na msemo unaosema; Kuua ni kinga ya kuua. Baadhi yao wametaja njia sita, Alusi ameongeza mpaka kufikia kumi na tatu na waliokuja baada ya Alusi nao wakaongeza zao. Njia zote hizo zinarudia kwenye utafiti wa matamshi tu.
﴿كُتِبَ عَلَيْكُمْ إِذَا حَضَرَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ إِن تَرَكَ خَيْرًا الْوَصِيَّةُ لِلْوَالِدَيْنِ وَالْأَقْرَبِينَ بِالْمَعْرُوفِ حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ ﴾
180.Mmeandikiwa, mmoja wenu anapofikwa na mauti kama akiacha mali, kuwausia kitu wazazi wawili na akraba kwa namna nzuri inayokubalika. Ni haki haya kwa wenye takua.
﴿فَمَن بَدَّلَهُ بَعْدَ مَا سَمِعَهُ فَإِنَّمَا إِثْمُهُ عَلَى الَّذِينَ يُبَدِّلُونَهُ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴾
181.Na atakayeubadilisha (wasia) baada ya kuusikia, basi dhambi yake ni juu ya wale watakaobadilisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mjuzi.
﴿فَمَنْ خَافَ مِن مُّوصٍ جَنَفًا أَوْ إِثْمًا فَأَصْلَحَ بَيْنَهُمْ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴾
182. Mwenye kuhofia mwusiaji kwenda kombo au dhambi, akasuluhisha baina yao, basi hatakuwa na dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira Mwenye kurehemu.
WASIAKWAWAZAZI
Aya 180-182
LUGHA
Neno: Khayri lina maana ya kinyume cha shari, na makusudio ya neno Khayr hapa ni mali. Inasemekana kuwa kila linapokuja neno Khayr katika Quran linakuwa makusudio yake ni mali; kama ilivyo katika Sura (11:84 ) (24:33), (100:8), , n.k( [4]
).
MAANA
Mmeandikiwa, mmoja wenu anapofikiwa na mauti kama akiacha mali, kuwausia wazazi wawili na akraba kwa namna nzuri inayokubalika.
Aya hii ni miongoni mwa Aya za hukumu, na inaingia katika mlango wa wasia. Kauli za mafaqihi na wafasiri zimekuwa nyingi na kugongana kuhusu Aya hii. Miongoni mwa kauli hizo ni kama zifuatazo:- Ikiwa mtu ana mali na akaona dalili za mauti, basi ni wajibu kwake kuusia kitu katika mali yake kwa wazazi wawili na ndugu wa karibu, hata kama wao ndio watakaoirithi; atawakusanyia urithi na wasia.
Wasia ni wajibu kwa jamaa zake wakiwa sio warithi.
Wasia kwa akraba ni sunna tu, na wala si wajibu.
Kuwausia warithi haki yao na viwango vyao vya kurithi. Kwa hivyo Aya itakuwa inapita mapito ya Aya inayosema:
﴿يُوصِيكُمُ اللَّـهُ فِي أَوْلَادِكُمْ لِلذَّكَرِ مِثْلُ حَظِّ الْأُنثَيَيْنِ﴾
Mwenyezi Mungu anawausia juu ya watoto wenu; fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili.
(4:11).
Wasia utakuwa ni wajibu kwa jamaa ikiwa mali ni nyingi.
Aya ni Mansukh (haitumiki hukumu yake) kwa Aya ya urithi. Na mengineyo zaidi ambayo hayategemewi kabisa.
KUWAUSIAWARITHI
Sunni na Shia wametofautiana katika kuswihi wasia kwa warithi. Wakaafikiana madhebu mane kuwa hauswihi, wakitegemea hadith isemayo: Hakuna wasiya kwa warithi. Shia Imamia wameafikiana juu ya kuswihi wasia kwa warithi na wengineo, kwa kutothibiti Hadith hiyo kwao, na kwamba dalili ya kuswihi wasia inachanganywa kwa ujumla na wasia kwa warithi; kuongezea riwaya mahsusi kutoka kwa Ahlul Bait (a.s.). Dalili yenye nguvu ya kuswihi wasia kwa warithi ni Aya hii tuliyo nayo. Allama Hilli katika kitabu At Tadhkira anasema: Wasia kwa warithi unafaa kwa kauli za wanavyuoni wetu wote, ni sawa warithi wamekubali au la. Hilo ni kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwenye Aya hizi tulizo nazo. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewajibisha kuwausia wazazi wawili, kwa sababu wao ndio akraba (jamaa wa karibu) zaidi wa maiti, kisha akasema kutilia mkazo wajibu huo: Ni haki haya kwa wenye takua yaani anamwambia yule ambaye hayaitakidi haya, kuwa si katika wamchao Mungu. Tena akatilia mkazo kwa mara ya pili kwa kauli yake: Na atakayeubadilisha baada ya kuusikia, basi dhambi yake ni juu ya wale watakaoubadilisha. Mwisho akaitilia mkazo jumla hii kwa kusema: Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mjuzi.
Unaweza kuuliza: Shia wamesema, inajuzu kuusia, na wala hawakusema ni lazima, pamoja na kuwa Aya mmeandikiwa kwa maana ya imesema mmewajibishiwa, kwa hivyo basi Shia wameihalifu Aya kama walivyoihalifu Sunni kwa kusema kuwa hauswihi wasia kwa warithi? Jibu:Wameafikiana Waislamu wote kwamba kutoa hukumu ya sharia katika Quran, hakufai ila baada ya kuangalia Hadith za Mtume, na baada ya kufanya utafiti wa Ijmai vile vile. Kama hakuna Hadith wala Ijmai katika maudhui ya Aya, basi inajuzu kutegemea dhahiri ya Aya. Imethibiti katika Hadith na Ijmai kwamba wasia kwa akraba sio wajibu, kwa hivyo hapana budi kuichukulia Aya kuwa ni Sunna katika wasia na wala sio wajibu, na yanakuwa maana ya: Ni haki kwa wamchao Mungu, kwamba Sunna hii ni yenye kuthibiti kwa haki, kwa sababu maana ya haki ni kuthibiti. Makusudio ya Namna nzuri inayokubalika Ni kuwa kitu chenye kuusiwa kinanasibiana na hali ya mwenye kuusia na mwenye kuusiwa; kisiwe kichache cha kudharaulika, wala kisiwe zaidi kuwadhuru warithi; yaaani kisizidi theluthi ya mali itakayoachwa na marehemu. Kuna Hadith inayosema:Hakika Mwenyezi Mungu amewapa theluthi ya mali yenu wakati wa kufa kwenu. Na atakayeubadilisha baada ya kuusikia.
Yaani atakayebadilisha wasia na kuugeuza na hali anajua. Basi dhambi yake ni juu ya wale watakaoubadilisha; Yaani dhambi ya kubadilisha, itamwangukia yule mwenye kubadilisha, awe ni mrithi, walii, hakimu, wasii au shahidi. Hii ni dalili kwamba mwenye kufanya dhambi ni juu yake mwenyewe peke yake. Ikiwa marehemu alimuusia mtu ambaye anamwamini kuwa atamtekelezea haki ya Mwenyezi Mungu au ya watu aliyonayo,halafu aliyeusiwa akafanya uzembe au hiyana, basi maiti hana dhambi yoyote isipokuwa dhambi iko juu ya yule aliyeusiwa. Razi anasema: Wanavyuoni wameitolea dalili Aya hii, kwamba mtoto mdogo hawezi kuadhibiwa kwa ukafiri wa baba yake. Na haya ni katika mambo yaliyo wazi kiakili ambayo Quran imeyathibitisha kwa mifumo mbali mbali; kama Aya inayosema:
Wala hatabeba mbebaji mzigo wa mtu mwingine.
(35:18). Mwenye kuhofia muusiaji kwenda kombo au dhambi akasuluhisha baina yao, basi hatakuwa na dhambi. Kupata dhambi hapa kuna maana ya kukusudia dhulma. Aya hii inavua hukumu ya Aya iliyotangulia; yaani mwenye kubadilisha wasia atakuwa na dhambi, isipokuwa kama mwusiaji amekosea katika wasia wake. Hapo itajuzu kwa wasii au walii au hakimu kubadilisha batili kuiweka kwenye haki, sio kubadilisha haki. kwenye batili
Hayo ndiyo waliyoyataja wafasiri kuhusu maana ya Aya; nayo ni sahihi hayo yenyewe, lakini yale tunayoyafahamu kutokana mfumo mzima wa Aya, na kuyathibitisha mwenye Majmaul-Bayan, ni kwamba mtu akitokewa na dalili za mauti na akausia mambo ambayo ndani yake mna dhuluma; kama kuwapa wengine na kuwanyima wengine, na katika wasia huo wakahudhuria watu wenye akili na waumini, basi itakuwa hakuna dhambi kwa yule aliyehudhuria kumwonyesha haki mwusiaji na kusuluhisha kati yake na warithi wake, ili wote wawe wameafikiana na kuridhia, wala usizuke baina yao ugomvi na migongano baada ya kufa mwusiaji.
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ﴾
183.Enyi mlioamini! Mmeandikiwa kufunga kama walivyoandikiwa waliokuwa kabla yenu, ili mpate kuwa na takua.
﴿أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴾
184.Siku maalum za kuhisabika. Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi, au yuko safarini, basi atimize idadi katika siku nyingine. Na wale wanaoweza kwa shida, watoe fidia kwa kumlisha maskini. Na atakayefanya heri kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na kufunga ni bora kwenu, ikiwa mnajua.
﴿شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴾
185.Ni mwezi wa Ramadhan ambao imeteremshwa katika mwezi huo Quran, kuwa mwongozo kwa watu na upambanuzi. Basi atakayekuwa mjini katika mwezi huu na afunge; na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyingine. Mwenyezi Mungu anawatakia yaliyo mepesi wala hawatakii yaliyo mazito, na mkamilishe hisabu hiyo, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amewaongoza, na ili mpate kushukuru.
MMELAZIMISHWA KUFUNGA
Aya 183 -185
MAANA
Enyi mlioamini! Mmeandikiwa kufunga kama walivyoandikiwa waliokuwa kabla yenu.
Saumu ni miongoni mwa ibada muhimu, na ni katika dharura za dini, kama ilivyo wajibu Swala na Zaka. Katika Hadith imesemwa: Uislamu umejengwa katika mambo matano: Kushuhudia kuwa hapana Mola anayepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamTafsir ba Muhammad ni Mtume wake (shahada), kusimamisha swala, kutoa zaka, kufunga mwezi wa Ramadhan na kuhiji Makka kwa anayeweza. Mafaqihi wametoa fatwa kwamba yeyote mwenye kukana wajibu wa saumu, basi amekuwa murtadi (si Mwislamu tena) na ni wajibu kumuua. Na mwenye kuamini kuwa saumu ni wajib, lakini akaiacha kwa kupuuza ataaziriwa kutokana na vile anavyoona hakimu wa sharia. Kama akirudia ataaziriwa mara ya pili. Akirudia tena atauawa, wengine wamesema atauawa mara ya nne.
Saumu ni ibada ya zamani aliyoifaradhisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa watu waliotangulia, kwa namna inayotofautiana na yetu sisi Waislamu, kwa kiasi chake namna yake na wakati wake. Kufananishwa hapa kumekuja kwa uwajibu tu, bila ya kuangalia sifa, idadi ya siku na wakati wake. Na kufananisha kitu sio lazima kiwe sawa kwa njia zote. Ili mpate kuwa na takua. Wafasiri wengi wamesema kuwa jumla hii inaonyesha hekima ya saumu ambayo ni mazoezi ya mwenye kufunga kuweza kuthibiti nafsi, kuacha matamanio ya haramu na kuwa na subira (uvumilivu). Hadith inasema: Saumu ni nusu ya subira. Imam Amirul Mumini
anasema:Kila kitu kina zaka (utakaso) na zaka ya mwili ni kufunga
. Amesema tena:Mwenyezi Mungu amefaradhisha saumu kwa majaribio ya ikhlasi ya viumbe...
Kimsingi, ni kwamba kila maamrisho ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake ni majaribio ya ikhlasi ya viumbe, lakini saumu ina taklifa kubwa, kwa sababu kuna kushindana na nafsi na kupambana, kuweza kuidhibiti na mambo inayoyapendelea ambayo ni chakula, kinywaji na matamanio ya kimwili.
Kwa siku maalum za kuhisabika Hizo ni siku za Ramadhan, kwa sababu Mwenyezi Mungui hakutufaradhishia zaidi ya Ramadhan.Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi, au yuko safarini, basi atimize idadi katika siku nyingine.
Na wale wanaoweza kwa shida, watoe fidia kwa kumlisha maskini. Mwenyezi Mungu ametaja katika Aya hii mambo matatu ya kuruhusiwa kufungua Ramadhan ambayo ni Maradhi, Safari na Uzee. Maradhi anayoruhusiwa mtu kufungua ni kuwa mtu ni mgonjwa ambaye kama atafunga maradhi yake yatazidi, au kuzidi siku za ugonjwa. Au pengine ni mzima, lakini anaogopa kama atafunga atazukiwa na maradhi mapya. Ama udhaifu tu, hauwezi kumruhusu mtu kufungua, madamu anaweza kustahmili na mwili wake uko salama. Ikiwa mgonjwa atangangania kufunga pamoja na kuthibitika madhara, basi saumu yake itakuwa batili na ni wajibu kwake kulipa sawa na aliyefungua bila udhuru. Imethibiti kwa upande wa Sunni na Shia kwamba Mtume(s.a.w.w)
amesema ; Si wema kufunga safarini, Katika Tafsir Al-Manar imekuja Hadith mashuhuri iliyopokewa kutoka kwa Mtume mtukufu: Mwenye kufunga safarini ni kama mwenye kufungua akiwa nyumbani.
Katika waliotaja Hadith hii ni Ibn Maja na Tabari. Razi anasema: Wanavyuoni wa kisahaba wamesema kuwa ni wajibu kufungua kwa mgonjwa na msafiri kwa hali yoyote ile kutokana na kutokuwepo amri ya kufunga. Na hiyo ndiyo kauli ya Ibn Abbas na Ibn Umar. Vile vile Daud bin Ali Al-Asfahani. Kutokana na hali hiyo, kufungua safarini ni wajibu na wala sio ruhusa tu, Yaani haifai kufunga kwa msafiri kwa hali yoyote ile kutokana na kutokuwepo amri ya kufunga. Dalilli yenye nguvu zaidi juu ya hilo ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewajibisha kulipa kwa safari kwa namna ile ile aliyowajibisha kwa maradhi, pale aliposema: Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au yuko safarini, basi (atimize) hisabu katika siku nyingine Na wala hakusema ukitaka fungua (utimize) hisabu katika siku nyengine. Na kukadiria hivyo ni kinyume na dhahiri; wala hakuna haja ya kukadiria mambo mengine ikiwa maana yanasimama bila ya kukadiria. Ama ruhusa ya tatu ya kufungua, ni uzee. Mwenyezi Mungu ameonyesha hilo kwa kauli yake: Na wale wanaoweza kwa shida, watoe fidia kwa kumlisha masikini. Hukumu hii inamhusu mzee aliye dhaifu kwa sababu ya ukongwe awe mume au mke. Kuweza kwa shida ni kufanya kitu kwa shida na mashaka sana. Huyu anahiyarishwa kati ya kufunga au kufungua pamoja na kutoa fidia ambayo ni kuwalisha maskini. Kuna Hadith sahihi kuhusu hilo kutoka kwa Ahlul Bait
Na atakayefanya heri kwa kujitolea basi ni bora kwake.
Yaani mwenye kuzidisha kulisha zaidi ya maskini mmoja au kumlisha masikini mmoja zaidi ya kiasi cha wajibu, basi ni bora kwake. Anayo hiari ya kumwita maskini muhitaji amlishe mpaka ashibe au ampe chakula cha unga au nafaka anachokula, kiasi kisichopungua gramu mia nane (800gm). Inaruhusiwa kumpa pesa zenye thamani ya chakula kwa sharti ya kumwambia: Ifanye ni thamani ya chakula chako. Na kufunga ni bora kwenu. Yaani mzee mume au mke walio wakongwe, ingawaje wana hiyarishwa kati ya kufungua na kufunga, lakini wakihiyari kufunga, ni bora mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko kufungua na kutoa fidia. Ni mwezi wa Ramadhan ambao imeteremshwa katika mwezi huo Quran. Mwenye Majmaul-Bayan anasema: Mwenyezi Mungu alipohusisha kufunga katika mwezi wa Ramadhan, amebainisha kwamba hekima katika hili ni kuwa Quran, ambayo juu yake ndio kuna mzunguuko wa dini na imani, iliteremshwa katika mwezi huo.
Kisha akanakili mwenye Majmaul-Bayan kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
kwa njia ya Sunni na Shia kwamba: Sahifa za Ibrahim
ziliteremshwa siku ya tatu ya mwezi wa Ramadhan, Tawrat ya Musa
siku ya sita, Injil ya Isa
siku ya kumi na tatu , Zaburi ya Daud
siku ya kumi na nane na Quran ilimshukia Muhammad(s.a.w.w)
siku ya ishirini na nne. Unaweza kuuliza: Hakika kauli yake Mwenyezi Mungu. Ni mwezi wa Ramadhan ambao imeteremshwa katika mwezi huo Quran kwa dhahiri inafahamisha kuwa Quran imeteremshwa yote katika mwezi wa Ramadhan na inavyojulikana ni kuwa Quran iliteremshwa kwa vipindi katika muda wote wa Mtume ambao ni miaka ishirini na tatu? Jibu: Makusudio ni kwamba kushuka kwake kulianza katika mwezi wa Ramadhan, sio kwamba imeteremshwa yote katika mwezi huo. Na usiku ambao ilishuka Quran unaitwa Laylatul-Qadr, yaani, usiku wa cheo. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:
Hakika sisi tumeiteremsha (Quran) katika usiku uliobarikiwa...
(44:3)
Zaidi ya hayo ni kwamba msahafu unaitwa Quran na sehemu yake pia inaitwa Quran. Ama kauli ya anayesema kwamba Mwenyezi Mungu aliiteremsha Quran kutoka Lawhil-Mahfudh, iliyoko juu mbingu ya saba, na kuileta katika mbingu ya dunia kwa mkupuo mmoja katika usiku wa Laylatul-Qadr, kisha akaiteremsha kwa Muhammad(s.a.w.w)
kwa vipindi, kauli hii haina dalili yoyote. Kuwa mwongozo kwa watu na upambanuzi. Upambanuzi ni kupambanua kati ya haki na batili na kati ya heri na shari.
Tumekwishaeleza maana ya uongozi katika kufasiri Aya ya pili, na kwamba Quran si kitabu cha Falsafa, Historia au elimu ya maumbile, isipokuwa ni ufumbuzi, uongozi na rehma. Na kauli yake Mwenyezi Mungu kuwa mwongozo kwa watu inafahamisha kuwa mawaidha, hekima na viaga na yote ambayo yako katika Quran, yanafahamiwa na watu wote wala hayahusiki na kufahamiwa na mujtahidi au watu mahsusi. Basi atakayekuwa mjini katika mwezi huu na aufunge. Yaani mtu ambaye hayuko safarini katika mwezi huu ni wajibu kwake kufunga, wala haifai kwake kufungua bila ya udhuru wowote. Linalofahamisha kuwa makusudio ya neno shahida ni kuwa mjini, ni kauli yake Mwenyezi Mungu inayofuatia isemayo: Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini basi atimize hisabu katika siku nyingine. Amerudia kutaja ugonjwa na safari kwa kutilia mkazo kwamba katika mwezi wa Ramadhan kunajuzu kufungua, ili kuwajibu wale wanaoshikilia kwamba kufungua hakujuzu kwa hali yoyote.
Kwa dhahiri ya mfumo wa maneno ulivyo, ni kwamba jumla hii ni sababu ya kujuzu kufungua katika hali ya ugonjwa, safari na uzee, lakini kwa uhakika ni sababu ya hukumu zote. Imekuja Hadith isemayo: Wafanyieni wepesi (watu) wala msiwafanyie uzito na wapeni habari za furaha wala msiwafukuze. Mwenye kusema kuwa kufungua ni amri na wala sio ruhusa atakuwa amefasiri kauli yake Mwenyezi Mungu: Anawatakia yaliyo mepesi, kwamba Mwenyezi Mungu anawatakia mfungue katika safari na hataki mfunge. Na mwenye kusema kuwa kufungua ni ruhusa na wala sio amri atakuwa amefasiri kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawataka muwe na wasaa katika mambo yenu na kuchagua lile ambalo ni jepesi kwenu. Ikiwa kufungua ndio wepesi kwenu sawa; au ikiwa kufunga ndio kwepesi sawa. Ikiwa yule ambaye inakuwa wepesi kwake kufunga katika mwezi wa Ramadhan na kuona uzito kulipa, basi kufunga ni bora. Hakuna anayetia shaka kwamba kuzingatia dhahiri ya tamko kunatilia nguvu maana haya. Lau si Hadith sahihi kutoka kwa Ahlul Bait kutokana na babu yao(s.a.w.w)
tungelisema kwamba kufungua katika safari ni ruhusa na wala sio amri. Na mtimize hisabu hiyo. Hii ni sababu ya kulipa alikowajibisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kauli yake: Basi (atimize) hisabu katika siku nyingine. yaani ni juu yenu kulipa saumu kwa idadi ya siku mlizofungua katika mwezi wa Ramadhan, kwa sababu ya maradhi na safari, ili itimie idadi ya siku za mwezi kamili ambazo mara nyingine huwa thelathini au ishirini na tisa.Na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amewaongoza na ili mpate kushukuru.
Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametubainishia hukumu za dini Yake, ili tumtukuze na tumshukuru. Mwenye Majmaul-Bayan anasema: Makusudio ya kumtukuza Mwenyezi Mungu, ni takbira za Idd baada ya swala ya Magharibi ya usiku wa Idd, Isha na Asubuhi, na vile vile baada ya swala ya Idd kwa mujibu wa madhehebu yetu; yaani takbira inayokaririwa baada ya swala ya Idd ambayo husomwa hivi: Allahu Akbar, Allahu Akbar, Lailaha illa llahu Wallahu Akbar, Allahu Akbar wa lillaahilhamd; Allahu Akbar alaama hadaana.
Maana yake ni: Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi, Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi, hapana Mola mwengine isipokuwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu; Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi kwa aliyotuongoza.
﴿ وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ﴾
186. Na waja wangu watakapo kuuliza khabari zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.
NAITIKIA MAOMBI YA MWOMBAJI
Aya 186
MAANA
Inasemekana kuwa Bedui mmoja alimwendea Mtume na kumuuliza: “Mola wetu yuko karibu ili nimnog’oneze? au yuko mbali nimpigie kelele?” Ndipo ikateremshwa Aya hii kuwa ni jawabu la Bedui. Kama ni sawa kauli hii, au sio sawa lakini inanasibiana na maudhui.
Dua ni katika ibada bora na imehimizwa sana katika Qur’an na hadith. Kwa sababu ni dhihirisho la utumwa wa mtu kwa Mwenyezi Mungu na kumhitajia kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Hayo tumeyazungumzia kwa urefu katika kitabu Bainallah wal-insan.
Unaweza kuuliza: kauli yake Mwenyezi Mungu:“anaponiomba”
baada ya kauli yake:“naitikia maombi ya mwombaji”
ni jaribio la kupata ambacho tayari kipo, kwa sababu inafanana na kauli ya mwenye kusema: “Mwangalie mkaaji akiwa amekaa na msikilize msemaji akiwa anasema?”
Jibu
: Makusudio ya“anaponiomba”
, ni dua inayotoka katika moyo wa mwenye ikhlasi na mkweli katika maombi yake, sio dua ya ulimi tu. Hiyo inafanana zaidi na kauli ya mwenye kusema “Mtukuze mwanachuoni akiwa ni mwanachuoni”, akimaanisha mwanachuoni wa kikweli kweli sio mwenye jina tu la wanachuoni.
Swali la pili ambalo ni maarufu na mashuri ni: Dhahiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu “naitikia maombi ya mwombaji”, na kauli yake; “niombeni nitawaitikia” ni kwamba Mwenyezi Mungu anamwitikia kila anayemwomba; wakati ambapo mtu anaweza kuomba sana na kunyenyekea, lakini haitikiwi maombi yake?
Wafasiri wamelijibu swali hilo kwa majibu mbali mbali, baadhi yao wakafikia majibu sita. Wote wameafikiana kwamba Mumin, mtiifu kwa Mwenyezi Mungu, huitikiwa maombi yake, kinyume cha mwingine. Lakini kauli hii inabatilika kwa kuwa Mwenyezi Mungu aliitika maombi ya Iblis:
﴿قَالَ أَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿١٤﴾ قَالَ إِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ ﴾
Akasema: Nipe muda mpaka siku watakapo fufuliwa. (viumbe), Akasema (Mwenyezi Mungu): Utakuwa miongoni mwa walio pewa muhula.
(7:14-15)
Vyovyote iwavyo jibu la swali hilo linahitaji ufafanuzi kwa njia zifuatazo:
1. Mja kumwomba Mola wake mambo yanayopingana na desturi, kama vile kutaka riziki bila ya mihangaiko yoyote, elimu bila ya kujifundisha na mengineyo ambayo ni ya kutaka masababisho bila ya sababu, na kuingia nyumba kwa ukutani wala sio mlangoni. Hiyo siyo dua, au ni dua ya asiyemjua Mwenyezi Mungu na hekima zake na desturi yake. Kwani Mwenyezi Mungu ana desturi kwa viumbe vyake.
﴿ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا ﴾
Wala hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu. (48:23)
2. Kutaka tawfiq na uongofu katika hukumu za dini kwa kufanya amali za heri, kutekeleza wajibu na kuacha maasi na mambo ya haram.
﴿ اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ ﴾
Tuongoe njia iliyo nyooka.
(1:6)
Vile vile dua ya kuomba kujiepusha na shari na maafa:
﴿ قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ ﴿١﴾ مِن شَرِّ مَا خَلَقَ ﴾
Sema: Najikinga kwa Mola Mlezi wa asubuhi, Na shari ya alivyo viumba.
(113:1-2)
Pia kuna dua ya kumwomba Mwenyezi Mungu sababu za kufaulu katika riziki, elimu na afya:
“Ewe Mola wangu! nikunjue kifua changu. Na unifanyie nyepesi kazi yangu.”
Hayo yote ni kwa sharti ya kuwa mwombaji awe na ikhlasi na kumtege- mea Mwenyezi Mungu peke Yake. Hayo ndiyo maombi ya Mitume na watu wema na ndio makusudio ya dua zao.
3. Kabla ya yote inatakikana kwanza tujue na wala tusiipuuze hakika hii ambayo tunaona na kushuhudia kwa macho, nayo ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) humpa anayemwomba na asiyemwomba kwa rehema na ukarimu kutoka kwake. Na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu humpa ufalme anayemtaka na humzuilia ufalme anayemtaka, Humdhalilisha anayemtaka na humwinua anayemtaka na humpa nguvu anayemtaka bila ya dua.
Kwa hivyo basi maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.): “Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba,” sio kwamba Yeye hatoi isipokuwa kwa dua. Wala hakuna maana katika kauli yake:
﴿ إِنَّ رَحْمَتَ اللَّـهِ قَرِيبٌ مِّنَ الْمُحْسِنِينَ ﴾
Hakika rehema ya Mwenyzi Mungu iko karibu na wanao fanya mema. (7:56)
Kuwa rehema ya Mwenyezi Mungu iko mbali na waovu. Hapana si hiyo! Hakika rehema Yake imeenea kila kitu.
﴿وَمَا كَانَ عَطَاءُ رَبِّكَ مَحْظُورًا ﴾
“…Na kutoa kwa Mola wako hakuzuiliki”.
(17:20)
Zimekuja baadhi ya riwaya za dua ya maumivu ya tumbo, nyingine za maumivu ya mgongo, ya jicho, ya meno, n.k. Hadith hizo, ama zitakuwa zimewekwa tu, kwa sababu haziendi na hali halisi wala hazifai chochote; au pengine makusudio ni kujibidiisha kufanya matibabu pamoja na kumtegemea Mwenyezi Mungu.
Inasemekana kwamba Amirul Muminin
alimpitia Bedui, aliyekuwa na ngamia mwenye ukurutu karibu yake, Imam akamwuliza Bedui:“Kwa nini humfanyii dawa?”
Akajibu: “Kwa nini ewe Amirul Muminin! Ninamfanyia,” Imam akauliza:“Dawa gani?”
Bedui akajibu: Dua
Imam akasema:“Pamoja na dua tumia dawa ya utomvu.”
Basi na waniitikie na waniamini.
Razi katika Tafsiri yake anasema: “Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamwambia mja wake: Mimi ninaitikia maombi yako pamoja na kwamba Mimi sikuhitajii kabisa, basi nawe vile vile uwe ni mwenye kuitikia maombi yangu pamoja na kwamba wewe ni mwenye kunihitajia kwa kila hali. Ni ukubwa ulioje wa ukarimu huu!”
﴿أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ هُنَّ لِبَاسٌ لَّكُمْ وَأَنتُمْ لِبَاسٌ لَّهُنَّ عَلِمَ اللَّـهُ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَخْتَانُونَ أَنفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفَا عَنكُمْ فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ فَلَا تَقْرَبُوهَا كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ آيَاتِهِ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ ﴾
Mmehalalishwa usiku wa saumu kuwaingilia wake zenu.Wao Ni vazi lenu na nyinyi ni vazi lao. Mwenyezi Mungu anajua kuwa mlikuwa mkizihini nafsi zenu, kwa hivyo amewatakabalia toba yenu na amewasamehe. Basi sasa changanyikeni (onaneni) naona takeni aliyowaandikia Mwenyezi Mungu. Nakuleni na kunyweni mpaka uwabainikie weupe wa Alfajiri katika weusi wa usiku wakati wa alfajiri. Kisha timizeni saumu mpaka usiku. Na wala msichanganyike nao na hali mko katika itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, msiikaribie. Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha ishara Zake kwa watu ili wapate kumcha.
MMEHALALISHIWA USIKU WA SAUMU
Aya 187
LUGHA
Usiku wa saumu ni ule anaoamkia mtu akiwa amefunga. Kwa asili neno Rafath lina mana ya uchafu makusudio yake hapa ni kumwingilia mke. Vazi ni nguo ya kuvaa, lakini makusudio katika Aya hii ni kuchanganyika.
Mmehalalishiwa usiku wa saumu kuwaingilia wake zenu.
Yaani inafaa kwa mwenye kufunga kumwingila mkewe katika usiku wa kufunga. Usiku wa kufunga unakusanya siku zote za Ramadhan na wala hauhusiki na usiku fulani, au sehemu fulani tu ya usiku! Hilo limefahamika kutokana na kuachiwa neno bila ya kufungwa na kitu kingine.
Mwenyezi Mungu amefumba kuwaingilia kwa neno rafath (uchafu) kwa ajili ya kuitakasa ibara; kama vile ambavyo amefumba katika Aya nyingine kwa maneno kama: Kugusa, kuingiliana na kukurubiana. Ibn Abbas anasema: "Mwenyezi Mungu ni mwenye staha hufumbia anachotaka."
Wao ni vazi lenu, na nyinyi ni vazi lao.
Baadhi ya wafasiri wanasema; vazi hapa ni fumbo la kukumbatiana. Razi anasema: Rabia amesema ni kuwa wao ni tandiko kwenu na nyinyi ni shuka kwao.
Haya ni sawa na tafsiri ya Mustashriqina wanaosema: Wao ni suruali kwenu na nyinyi ni suruali kwao. Ilivyo hasa ni kuwa neno Libas ni matokeo ya neno Labis kwa maana ya kuchanganyika kuvaanas.
Makusudio kwa ujumla ni kubainisha hukumu ya kuruhusiwa kuingiliana na wanawake usiku wa saumu; kwani mke na mume wakiwa pamoja na kutangamana, basi inakuwa uzito sana kwa mume kuvumilia.
Mwenyezi Mungu anajua kuwa mlikuwa mkizihini nafsi zenu, kwa hivyo amewatakabalia toba yenu na amewasamehe.
Msemo unawaelekea baadhi na wala sio wote. Hilo tunalifahamu kutokana na neno hiyana, kutakabali toba na msamaha.
Wafasiri wengi wanasema kwamba Mwenyezi Mungu alimhalalishia mfungaji tangu mwanzo wa sharia, kula na kunywa na kujamiiana na mkewe usiku wa saumu kwa sharti la kutolala au kuswali swala ya Isha. Kwa maana ya kuwa akilala usiku au kuswali Isha, basi ni haramu juu yake kula, kunywa na kujamii mpaka uingie usiku unaofuatia. Na kwamba sahaba mmoja alivunja sharti hili; hivyo akamjamii mkewe baada ya kuamka; kisha akajuta sana na akakiri makosa yake kwa Mtume (s.a.w.w.); ndipo ikashuka Aya hii.
Vyovyote iwavyo ni kwamba: nafsi ina mambo ambayo inakuwa vigumu kujizuwiya nayo. Kwa hiyo mtu huishibisha kwa kujificha au kwa kuasi dini ya Mwenyezi Mungu. Basi lililo bora ni kuhalalisha lile linalopen- delewa ikiwa kuna njia yoyote ya kuhalalisha, ili mtu asivutwe kwenye maasi mara kwa mara, hatimaye kuwa mwenye dharau na kutojali dini na hukumu za Mwenyezi Mungu.
Na takeni aliyowaandikia Mwenyezi Mungu.
Ambayo ni kustarehe na wanawake wakati wa usiku wa saumu, jambo ambalo hapo mwanzo lilikuwa haramu.
Na kuleni na kunyweni mpaka uwabainike weupe wa Alfajiri katika weusi wa usiku.
Yaani mmehalalishiwa kujamiina kuanzia mwanzo wa usiku mpaka machimbuko ya Alfajiri.
Imepokewa Hadith ya Mtume(s.a.w.w):
"Alfajiri ni mbili: Ama ile ambayo iko kama mkia wa mbwa mwitu hiyo haihalalishiwi kitu (swala) wala kuharimishiwa (kula). Ama iliyo katika umbo mstatili ambayo inae- nea pambizoni, hiyo ni halali kuswali ndani yake na ni haramu chakula”.
Kisha timizeni saumu mpaka usiku.
Mwanzo wa saumu ni kuanzia Alfajiri na mwisho wake ni unapoanza usiku. Usiku unaingia kwa kutua jua, lakini kutua kwake hakuwezi kujulikana kwa kufichika machoni tu, bali hujulikana kwa kutoweka wekundu upande wa mashariki kwa sababu mashariki ndiyo inayochomoza magharibi. Kwa hivyo wekundu wa mashariki unakuwa ni akisi ya mwanga wa jua, na kila linavyozidi kujificha zaidi jua ndipo akisi hii inavyopotea
Ama yale wanayotuhumiwa Shia kwamba wao wanachelewesha swala ya Magharibi na futari ya Ramadhan mpaka zitokeze nyota, huo ni uongo na uzushi. Imam Sadiq
aliambiwa kuwa watu wa Iraq wanachelewesha swala ya Magharibi mpaka zitokeze nyota. Akasema."Hiyo ni kazi ya adui wa Mwenyezi Mungu Abul Khatwab."
Na wala msichanganyike nao, na hali mko katika itikafu msikitini.
Katika vitabu vya Fiqh kuna mlango mahsus unoitwa mlango wa itikafu. Aghlabu mafaqihi huutaja baada ya mlango wa saumu. Maana ya itikafu katika sharia ni kukaa mtu katika msikiti wa jamaa sio chini ya siku tatu, kwa masiku mawili, kwa mwenye kufunga; kwamba asitoke msikitini isipokuwa kwa haja muhimu na kurudi mara moja anapomaliza.
Ni haramu kwa mwenye kukaa itikafu kuingiliana na mwanamke usiku au mchana; hata kubusu na kugusa kwa matamanio.
Kukatazwa hapa, kunafungamana na kuvaana na mwanamke kwa hali yoyote; iwe ni ndani ya msikiti au nje. Mwenye kukaa itikafu akitoka msikitini na akajamiiana na mwanamke usiku, hata kama atakoga na kurudi msikitini, atakuwa amefanya haramu; na itamlazimu kutoa kafara ya mwenye kufungua makusudi katika mwezi wa Ramadhan - kumwachia huru mtumwa, au kufunga miezi miwili mfululizo au kulisha maskini sitini.
﴿ وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُمْ بَيْنَكُمْ بِالْبَاطِلِ وَتُدْلُوا بِهَا إِلَى الْحُكَّامِ لِتَأْكُلُوا فَرِيقًا مِنْ أَمْوَالِ النَّاسِ بِالْإِثْمِ وَأَنْتُمْ تَعْلَمُونَ ﴾
Wala msile mali zenu baina yenu kwa batili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi na hali mnajua.
KULA MALI KWA BATILI
Aya 188
MAANA
Wala msile mali zenu baina yenu kwa batili.
Msemo unaelekezwa kwa wote wenye kulazimiwa na sharia. Maana ya msile mali zenu, ni sawa na kauli yake. Mwenyezi Mungu; "Msijiue" yaani msiuane.
Hiyo inafahamisha umoja wa utu, na kwamba utu ni kama kiwiliwili kimoja na watu ni viungo vyake, lilopata kiungo kimoja linafikia kiungo kingine.
Makusudio ya kula, ni kutumia mali iliyopatikana kwa njia isiyo halali. Neno"kati yenu"
katika Aya linahusisha mali iliyotokana kwa mabadilishano ya haramu, kama riba; au mali iliyosimama kwa haramu, kama pombe, nguruwe ambayo hayathibitishwi na sharia.
Mfano wa hayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿ لَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُم بَيْنَكُم بِالْبَاطِلِ إِلَّا أَن تَكُونَ تِجَارَةً عَن تَرَاضٍ﴾
"... Msile mali zenu baina yenu kwa batili, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana...."
(4:29)
Ama uharamu wa mali iliyochukuliwa kwa unyang'anyi, wizi kiapo cha uongo, n.k. hayo yanafahamika kwa dalili nyingine. Kwa ajili hii, ndipo mafaqihi wakatoa dalili kwa Aya mbili hizo juu ya kubatilika kila muamala (mapatano) alioharamisha Mwenyezi Mungu. Aya hii inafahamisha wazi wazi kwamba Uislamu unakubali mtu kumiliki chake. (mali ya mtu binafsi.)
Na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi.
Haya yanaungana na kula. Makusudio ya dhambi hapa ni rushwa, kwa kuangalia mfumo wa maneno ulivyo. Maana yaliyokusudiwa ni kukataza kutoa rushwa kwa mahakimu kwa ajili ya kula mali za watu.
Na hali mnajua.
Yaani msifanye dhambi hii na hali mnajua ubaya wake. Hakuna mwenye kutia shaka kwamba kufanya jambo ovu na huku mtu anajua, ni uovu zaidi kuliko kufanya na shaka shaka.
Kuna hadith isemayo: "Kujizuia na shaka shaka ni bora kuliko kujitia katika maangamizo." Basi itakuwa ni bora zaidi kujizuia ikiwa mtu anajua uharamu.
Rushwa ni katika mambo makubwa yaliyoharamishwa, hata katika hukumu ya haki. Mwenyezi Mungu ameilaani rushwa na mwenye kuitoa, mwenye kuipokea na mwenye kuwaunganisha wawili hao.
Imepokewa Hadith inayofahamisha kuwa rushwa ni kumkufuru Mwenyezi Mungu (s.w.t.), na riwaya nyingine inasema ni shirk.
HUKUMU YA KADHI FASIKI
Hanafi anasema kuwa hukumu ya Kadhi fasiki inafaa, hayo yameelezwa katika kitabu kiitwacho Ibn Abidin chapa ya mwaka 1325 hijriya., mlango wa Hukumu. Ninamnuukuu; "Fasiki ni mtu wa kutoa ushahidi, kwa hiyo anaweza kuwa Kadhi."
Na katika kitabu Fat-hul Qadir J5 uk. 454 mlango wa hukumu amese- ma; "Ilivyo ni kuwa hukumu ya kila mtawala inafaa, hata kama ni mjinga tena fasiki, na hayo ndiyo yaliyo wazi katika madhehebu yetu."
Shia Imamiya wamesema kwa kauli moja kwamba fasiki hawezi kuhuku- mu, na hukumu yake haifai kutekelezwa, hata awe na elimu kiasi gani.
Wamelitilia mkazo hilo kundi la mafaqihi wa Kiimamiya waliposema kuwa mwenye haki haijuzu kupeleka madai yake kwa kadhi asiye mwadilifu, hata kama ikibidi kuwa haki yake hawezi kuipata isipokuwa kwake, kwa namna ambayo lau si kadhi huyo, basi haki yake itapotea.
Akihalifu mwenye haki yake, basi haijuzu kuchukua chochote kilichohukumiwa hata kama ni haki; kwa kuchukulia kauli ya Imam Jaffar As Sadiq
:"Anachokichukua ni haramu, ijapokuwa ni haki yake iliy- omthibitikia."
Mafaqihi wengi wa kiimamiya wamesema kwamba mwenye haki anaweza kumtaka msaada asiyekuwa mwadilifu katika kupata haki yake ikibidi, ikiwa hawezi kupata njia nyingine, bila ya kutofautisha kuwa haki yenyewe ni deni au mali.
Kwa sababu kuzuia madhara ya nafsi kunajuzu, bali mara nyingine huwa ni wajibu, ikiwa hakutimii isipokuwa kumrudia asiyekuwa mwadilifu. Ama dhambi na haramu iko juu ya mwenye kuizuia haki sio mwenye kuchukua haki yake.
Hukumu Ya Kadhi Haibadilishi Uhakika Wa Mambo
Hakimu mwadilifu akiwahukumu watu wawili na akampa haki asiyekuwa na haki kwa kushindwa kutoa ushahidi mwenye haki, basi haijuzu kuchukua alichohukumiwa. Kwa sababu hakimu hageuzi uhakika.
Mtume(s.a.w.w)
anasema:"Mimi ni mtu kama nyinyi isipokuwa napewa wahyi tu, na nyinyi mnapokuja kutaka hukumu kwangu, huenda mwingine akawa fasaha zaidi kwa hoja kuliko mwenzake. Nikihukumu kutokana na niliyosikia, basi ninayemhukumia kitu katika haki ya nduguye, (ajue) nimehukumia kipande cha moto."
Lakini Abu Hanifa amesema kinyume cha hivyo. Akinukuliwa na mwenye Tafsir Al-Manar katika kuelezea Aya hii, Abu Hanifa amesema: "Kadhi akihukumu kuvunjika ndoa kati ya mume na mke kwa ushahidi wa uongo, itakuwa haramu kwao kuishi maisha ya ndoa.
Na kama shahidi akitoa ushahidi wa uongo kwamba fulani amemuoa fulani na hakimu akahukumu kuwa ni sawa, basi ni halali kwa mwanamume kumwingilia bila ya ndoa, kwakutosheka na hukumu ya Kadhi ambayo anajua kuwa sio haki."
﴿يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَهِلَّةِ قُلْ هِيَ مَوَاقِيتُ لِلنَّاسِ وَالْحَجِّ وَلَيْسَ الْبِرُّ بِأَنْ تَأْتُوا الْبُيُوتَ مِنْ ظُهُورِهَا وَلَٰكِنَّ الْبِرَّ مَنِ اتَّقَىٰ وَأْتُوا الْبُيُوتَ مِنْ أَبْوَابِهَا وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ﴾
Wanakuuliza kuhusu ya miezi. Sema: 'Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili ya watu na Hijja. Wala Si wema kuingia majumba kwa nyuma yake, bali mwema ni aliye na takua. Na ingieni majumba kupitia milangoni mwake, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu.
WANAKUULIZA KUHUSU MIEZI
Aya 189
MAANA
Wanakuuliza kuhusu miezi.
Swali hili linawezekana kuwa pande mbili, ikiwa hatukuangalia jibu lake linalofuatia: Kwanza, nikuwa ni swali la kutaka kujua sababu za kisayansi; kutokana na tofauti inayoonekana - kuanzia mwezi mwandamo, kisha mwezi mkamilifu, tena unarudi kama ulivyokuwa. Pili, kuwa ni kuuliza hekima yake, sio sababu za kisayansi.
Tukiliangalia swali pamoja na jibu lake: “Sema: Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili ya watu”, litakuwa ni swali la hekima tu, na wala sio la sababu za kisayansi. Hili ndilo lenye nguvu zaidi.
Ama kauli ya anayesema kuwa wao waliuliza kuhusu sababu za kisayansi na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.). akamwamrisha Mtume wake kuwajibu kwa kubainisha hekima kuonyesha kuwa swali lao haliko mahali pake, kwa sababu wao wameshindwa kufikia kwenye sababu za kisayansi ambazo zinahitaji darasa ndefu na zenye undani na utangulizi mwingi wa kielimu; na ilivyotakiwa wao waulize hekima na faida ya kutofautiana miezi, jambo ambalo wao wanaweza kulifahamu. Kauli hiyo haitegemei dalili yoyote isipokuwa kuonelea kuwa ni vizuri hivyo tu.
Unaweza kusema kuwa dalili iko; nayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):“Wala si wema kuingia majumba kwa nyuma”
.
Kwamba kuuliza kwenu sababu za kisayansi, ni sawa na kutaka kuingia nyumba kwa nyuma; lakini kuuliza kwenu hekima yake, ni kama anayetaka kuingia nyumba kwa mlango wake.
Jibu
: kwanza hiyo ni Ijtihadi ya kuleta taawili ya tamko na wala sio kutafsiri dhahiri ya tamko. Pili, imethibiti kuwa jumla hii imeshuka kutokana na waliyokuwa wakiyafanya wakati wa kijahilia, ya kuingia nyumba kwa nyuma. Ufafanuzi ni kama ifuatavyo.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwamrisha Mtume wake kuwajibu kuwa heki- ma ya kutofautiana miezi ni kuyawekea wakati maslahi yao na mambo yao ya kidunia, kama vile madeni na kukodisha; na mambo yao ya kidini, kama vile Hijja na saumu.
Kwa maneno mengine ni jibu linapitia katika kauli Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t):“ ...Ili mjue idadi ya miaka na hisabu..."
(10:5) Wala si wema kuingia majumba kwa nyuma yake.Bali mwema ni yule anayemcha Mwenyezi Mungu.
“Na ingieni majumba kupitia milangoni mwake”
. Wafasiri wengi wasema wakati wa kijahiliya mtu kuwa anapohirimia Hijja, hutoboa tundu ya kuingilia au hutengeneza ngazi ya kupanda sakafuni; na akiwa ni katika Mabedui hutoka nyuma ya kibanda.
Baadhi ya waislamu nao walikuwa wakifanya hivyo hapo mwanzo mwanzo, ndipo ikashuka Aya kuwabainishia kwamba wema ni kumwogopa Mwenyezi Mungu, kufanya amali za heri na kujiepusha na maasi na machafu, sio kuingia majumba kwa nyuma na mengineyo ambayo hayaingii akilini wala kuwa na lengo la dini na imani.
﴿ وَقَاتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ الَّذِينَ يُقَاتِلُونَكُمْ وَلَا تَعْتَدُوا إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ ﴾
190.Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaowapiga, wala msichokoze. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wachokozi.
﴿وَاقْتُلُوهُمْ حَيْثُ ثَقِفْتُمُوهُمْ وَأَخْرِجُوهُمْ مِنْ حَيْثُ أَخْرَجُوكُمْ وَالْفِتْنَةُ أَشَدُّ مِنَ الْقَتْلِ وَلَا تُقَاتِلُوهُمْ عِنْدَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ حَتَّىٰ يُقَاتِلُوكُمْ فِيهِ فَإِنْ قَاتَلُوكُمْ فَاقْتُلُوهُمْ كَذَٰلِكَ جَزَاءُ الْكَافِرِينَ﴾
191Na wauweni popote muwapatapo na muwatoe popote walipowatoa; na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuua. Wala msipigane nao karibu na Msikiti Mtukufu mpaka wapigane na nyinyi huko. Wakipigana na nyinyi basi nanyi pia wapigeni. Namna hivi ndivyo yalivyo malipo ya makafiri.
﴿ فَإِنِ انْتَهَوْا فَإِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ ﴾
192Lakini kama wakikoma, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira,Mwenye kurehemu.
﴿ وَقَاتِلُوهُمْ حَتَّىٰ لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ وَيَكُونَ الدِّينُ لِلَّهِ فَإِنِ انْتَهَوْا فَلَا عُدْوَانَ إِلَّا عَلَى الظَّالِمِينَ﴾
193Na piganeni nao mpaka kusiwe na fitina, na dini iwe ya Mwenyezi Mungu. Na kama wakikoma, basi usiweko uadui ila kwa madhalmu.
NA PIGANENI KATIKA NJIA YA MWENYEZI MUNGU
Aya 190-193
LUGHA
Neno: Fitna lina maana ya balaa na misukosuko, na makusudio yake hapa ni ukafiri, yaani kuwaharibu watu na dini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ni kutokana na kulinganganisha na neno"Na dini iwe ya Mwenyezi Mungu peke yake."
MAANA
Katika Majmaul Bayan imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Mtume(s.a.w.w)
alipotoka yeye na sahaba zake katika mwaka ambao walitaka kufanya Umra wakiwa watu elfu moja na mia nne (1400), walipofika Hudaybia, Washirikina waliwazuia wasiingie Al Ka'aba. wakachinjawanyama hapo Hudaybia;( [5]
) kisha wakafanya suluh na washirikina kurudi, na waje mwaka ujao.
Mwaka ulipofika Waislamu walijiandaa kutekeleza Umra, lakini wakaogopa kupigwa vita na Washirikina. Mtume(s.a.w.w)
na sahaba zake wakachukia kupigana na washirikina katika mwezi mtukufu tena ndani ya Haram (sehemu takatifu ya Makka).
Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii, na kuidhinishwa kupigana. Baadhi ya jamaa wamesema hiyo ndiyo Aya ya kwanza kushuka kuhusu vita.
UISLAMU UNAPIGA VITA DHULMA NA UFISADI
Baadhi ya ambao wana ghera juu ya Uislamu na kujaribu kuugombea Uislamu kwa kila njia, hata kama itapigana na misingi ya Qur'an, wamesema kuwa Uislamu hauruhusu kupigana na yeyote isipokuwa mchokozi; na vita vya Kiislamu, katika zama za Mtume, vilikuwa ni vya kujikinga sio hujuma na walitoa dalili kwa aya kadhaa miongoni mwazo ni Aya hii tuliyonayo sasa na Aya nyingine inayosema:
﴿وَقَاتِلُوا الْمُشْرِكِينَ كَافَّةً كَمَا يُقَاتِلُونَكُمْ كَافَّةً﴾
"Na piganeni na makafiri nyote kama wao wote wanavyopigana nanyi nyote"
(9:36)
Lililowafanya kuugombea hivyo Uislamu, ni madai ya maadui wa Uislamu kwamba Uislamu ni dini ya vita, sio dini ya amani, kwa kisingizio cha vita vya Mtume(s.a.w.w)
.
Ilivyo hasa ni kuwa Uislamu umeruhusu kupigana kwa sababu zifuatazo: Kujikinga
Kupigana na madhalimu; Mwenyezi Mungu anasema:
﴿ وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ﴾
“Na ikiwa makundi mawili katika waumini yanapigana, basi yapatanisheni, likiwa moja la hayo linadhulumu jengine, basi lipigeni lile linalodhulumu mpaka lirudie kwenye amri ya Mwenyezi Mungu..."
(49:9)
Kumaliza ukafiri wa wanao mkufuru Mungu, Mwenyezi Mungu anasema:
﴿ قَاتِلُوا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَلَا بِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَلَا يُحَرِّمُونَ مَا حَرَّمَ اللَّهُ وَرَسُولُهُ وَلَا يَدِينُونَ دِينَ الْحَقِّ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حَتَّىٰ يُعْطُوا الْجِزْيَةَ عَنْ يَدٍ وَهُمْ صَاغِرُونَ ﴾
"Piganeni na wale wasiomwamini Mwenyezi Mungu wala siku ya mwisho, wala hawaharimishi alivyoviharimisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala hawafuati dini ya haki miongoni mwa waliopewa kitabu,(piganeni nao) mpaka watoe kodi kwa hiari yao,hali wametii."
(9:29)
Mtume amesema:"Nimeamrishwa kupigana na watu mpaka waseme hapana Mungu isipokuwa Allah. Kama wakisema, basi imehifadhika nami damu yao na mali zao."
Lakini kupigana kwa aina hii hakuruhusiwi isipokuwa kwa idhini ya Masum au naibu wake kuepuka vuruga.
Kujuzu kupigana kwa kujikinga, hakuna maana kuwa hakuna idhini ya kupigana kwa malengo mengine, kama vile kumaliza dhulma na ukafiri. Uislamu umeruhusu kupigana kwa ajili ya kupatikana dini ya haki na uadilifu, kwa sababu ukafiri wenyewe ni uadui katika Uislamu. Lakini Uislamu umeharamisha kupigana kwa ajili ya kutawala watu na kuwapokonya uwezo wao na kutawala uchumi wao.
Uislamu umejuzisha kutumia nguvu kumaliza maovu na madhambi na kupigania haki za binadamu, uhuru wake na heshima yake. Wakoloni walianzisha vita wakaleta machafuko na kumwaga damu, wakatafuta elimu kwa ajili ya kuua na kunyonya, na kuiweka juu dhulma na uadui( [6]
)
Hilo ndilo jawabu la wale wanaojaribu kuutweza Uislamu na Nabii wake, kwamba Uislamu ni dini ya vita na upanga. Na kweli Uislamu ni dini iliyokamilika. Inampiga vita kila asiyefuata haki na uadilifu na anayeleta uharibifu na ufisadi katika ardhi. Na kumkufuru Mwenyezi Mungu ni dhulma na ufisadi katika dini ya Kiislamu na sharia yake.
Kulingana na suala hili hatuna budi kudokeza kuwa mafaqihi wa madhehebu zote za Kiislamu wameafikiana kwa kauli moja kwamba mwenye kuvunja miko ya Mwenyezi Mungu kwa kuihalalisha na kwa kumwaga damu na kunyakua mali, basi yeye ni mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu; hata kama akiswali na kufunga na kuhiji nyumba ya Mwenyezi Mungu tukufu; bali huyu ni mwovu zaidi kuliko yule mwenye kukufuru, lakini akazuia umwagikaji damu na kunyakua mali na akijizuia kuwaudhi watu.
Ndio, wote wawili ni makafiri, lakini kafiri mwingine ni mwovu kwa Mwenyezi Mungu na kwa waja wa Mwenyezi Mungu. Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema:"Bora ya watu ni yule mwenye kuwanufaisha zaidi watu, na mwovu zaidi wa watu ni yule ambaye watu wanahofia shari yake."
Tunasema tena kila mwenye kukanusha hukumu ya kisharia iliyothibitika kwa dhahiri ya dini na Waislamu wote, basi huyo ni kafiri hata kama amezaliwa na wazazi Waislamu na akatamka shahada mbili.
Wala msichokoze.
Yaani, msipigane kwa ajili ya manufaa ya kiutu, bali piganeni kwa lengo la heshima ya utu binafsi na kwa lengo la kuihami dini na haki msiwaue watoto, wazee na wagonjwa. Vile vile msiharibu majengo na kukata miti. Mafunzo yote haya na mengineyo yamekuja katika Sunna za Mtume.
Waueni popote muwapatapo.
Yaani waueni makafiri wakati wowote na mahali popote walipo isipokuwa kwenye Msikiti Mtukufu, kwa sababu kupigana hapo ni haramu isipokuwa wakianza humo
Unaweza kuuliza: Katika Aya ya mwanzo kumeamrishwa kupigana na anayepigana na Waislamu, lakini kwenye Aya hii kumeamrishwa kupigana tu, bila ya kufungamanishwa na kitu kingine. Je, Aya hii imefuta hukumu ya hukumu ile?
Jibu
: Hapana kufutwa hukmu. Hivi punde tumeonyesha kwamba kujuzu kupigania nafsi hakufahamishi kuwa hakuna ruhusa ya kupigana kwa malengo mengine; kama vile kumaliza ukafiri na dhulma. Kama ukimwambia mtu 'wewe ni mtu mzuri' haina maana kuwa mwingine si mtu mzuri.
Basi hivyo hivyo kauli yake Mwenyezi Mungu:'Piganeni na wanaowapiga'
haina maana msipigane na wasiowapiga. Ndio, kama angelisema msipigane isipokuwa na wanaowapiga, hiyo ingefahamisha kufunga huko ni kwa kukanusha.
Na muwatoe popote walipowatoa.
Washirikina wa Makka walimtoa Mtume(s.a.w.w)
na sahaba zake hapo Makka, si kwa lolote isipokuwa tu masahaba hao wameamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake na Waislamu wakirudi Makka wakiwa washindi, wamtoe hapo kila asiyemwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; sawa na vile walivyofanywa na washirikina 'malipo yenye kulingana.' Inasemekana Mtume aliwatoa washirikina ulipokuja msaada wa Mwenyezi Mungu na ushindi kwa kuchukulia Aya hii.
Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuua.
Hii ni sababu ya kujuzu kuwaua washirikina. Makusudio ya fitina ni ushirikina. Maana ya kuwa mmeruhusiwa kuwaua washirikina, ni kuwa dhambi ya shirk ni mbaya zaidi kuliko dhambi ya kuua.
Baadhi ya tafsiri zinasema Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekusudia katika kauli yake hiyo, kuwa Washirikina wa Makka hapo mwanzo wa mwito wa Uislamu walikuwa wakimfitini mwenye kusilimu kwa kumuudhi kumwadhibu na kumtoa mjini kwake. Na hiyo ni fitina mbaya zaidi kuliko kuua. Kwa ajili hii ndio kukaruhusiwa kuwaua na kuwatoa mijini mwao.
Vyovyote iwavyo makusudio ya neno Fitna katika Qur'an sio ya kufanya umbeya na udaku kama wanavyofikiria wengi.
Wala msipigane nao karibu na Msikiti mtukufu mpaka wawapige huko.
Hili ni sharti la kujuzu kupigana katika Haram tukufu ambayo ameharamisha Mwenyezi Mungu kupigana ndani yake isipokuwa kama ikivunjiwa heshima kwa kupigana.
Wakipigana nanyi basi nanyi pia wapigeni
. Kwa sababu wao wameanza na wakauvunjia heshima Msikiti mtakatifu na mwenye kuanza hakudhulumiwa, isipokuwa yeye ndiye dhalimu.
Lakini kama wakikoma, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira, Mwenye kurehemu. Kulingana na mfumo wa maneno ulivyo, unahukumia kuwa maana yake ni, basi nanyi jizuieni nao na muwasamehe, kwa vile sababu iliyolazimisha kupigana nao ni kuanza kwao vita; wakijizuia basi sababu imeondoka.
Wafasiri wengi wamesema kuwa maana yake ni, wakitubia kutokana na ukafiri na wakamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa sababu kafiri hawezi kusamehewa na Mwenyezi Mungu kwa kuacha kupigana tu, bali husamehewa kwa kuacha kufuru. lakini huku ni kumuhukumia Mwenyezi Mungu(s.w.t.) kwa sababu Yeye anaweza kumsamehe anayemtaka, hata kama ni kafiri.
Ni kweli kuwa Mwenyezi Mungu hawezi kumwadhibu mwema kabisa, sababu Yeye ni Mwadilifu, lakini anaweza kum- samehe mkosaji kwa namna yoyote ya uovu itakavyokuwa, kwa sababu Yeye ni Karimu, Mwenye huruma.
Na piganeni nao mpaka kusiwe na fitina na dini iwe ya Mwenyezi Mungu.
Yaani Jihadi ni kwa ajili ya imani ya Mwenyezi Mungu. Kumaliza ukanushaji (wa kumkanusha Mwenyezi Mungu) ni wajibu maadam duniani kuna athari ya shirki na ulahidi. Kama yakiondoka haya na watu wote wakaamini, basi wajibu wa Jihadi utakuwa umeondoka.
Kwa ujumla ni kwamba wajibu wa Jihadi kwa ajili ya kuueneza Uislamu una sharti ya kupatikana idhini ya Imam mwadilifu na wala haijuzu kwa hali yoyote bila ya amri yake. Ama Jihadi ya kuihami dini na nafsi, wajibu wake umeachwa bila ya kuwekwa sharti lolote.
Na kama wakikoma basi usiweko uadui ila kwa madhalimu.
Yaani kama wakiacha ukafiri na wakasilimu basi si halali kuwaua isipokuwa kwa sababu zinazowajibisha kuua, ambazo ni moja kati ya mambo matatu: Kukufuru baada ya kuamini, kuzini baada ya kuwa na mke na kuua mtu bila ya haki yoyote.