7
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI
﴿ وَمِنَ النَّاسِ مَن يُعْجِبُكَ قَوْلُهُ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيُشْهِدُ اللَّـهَ عَلَىٰ مَا فِي قَلْبِهِ وَهُوَ أَلَدُّ الْخِصَامِ ﴾
204.Na katika watu kuna ambaye kauli yake inakupendeza katika maisha ya duniani, naye humshuhudiza Mwenyezi Mungu kwa yaliyo moyoni mwake na hali ni hasimu mkubwa kabisa.
﴿ وَإِذَا تَوَلَّىٰ سَعَىٰ فِي الْأَرْضِ لِيُفْسِدَ فِيهَا وَيُهْلِكَ الْحَرْثَ وَالنَّسْلَ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ الْفَسَادَ﴾
205.Na anapotawala hufanya bidii katika ardhi kufanya ufisadi, na huangamiza mimea na viumbe, na Mwenyezi Mungu hapendi ufisadi.
﴿ وَإِذَا قِيلَ لَهُ اتَّقِ اللَّـهَ أَخَذَتْهُ الْعِزَّةُ بِالْإِثْمِ فَحَسْبُهُ جَهَنَّمُ وَلَبِئْسَ الْمِهَادُ ﴾
206.Na anapoambiwa. Mche Mwenyezi Mungu, hupandwa na mori wa kufanya dhambi. Basi Jahannam inamtosha, napo ni makao mabaya mno
﴿ وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْرِي نَفْسَهُ ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِ اللَّـهِ وَاللَّـهُ رَءُوفٌ بِالْعِبَادِ ﴾
207.Na katika watu yuko auzaye nafsi yake kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni mpole kwa waja.
KAULI ZAO ZINAKUPENDEZA
Aya 204 – 207
MAANA
Baadhi ya wafasiri wapya wamejaza kurasa kwa maneno matamu katika kufasiri Aya hizi, lakini hawakuzidisha chochote zaidi ya kuwagawanya watu kwenye wema na uovu. Kwa dhahiri haya yanajulikana na wote, hayahitaji ubainifu wowote, sikwambii tafsiri ndefu tena. Unaweza kuuliza; Ikiwa kugawanyika watu kunajulikana na wote, basi kubainisha kunakuwa ni maelezo ambayo tayari yameshaelezwa na kufafanua lililofafanuliwa na yapasa kuyachukulia maneno ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) vizuri? Jibu: Inawezekana kuwa makusudio ni kuongoza na kuelekeza kwamba mwenye akili anatakikana kutohadaliwa kwa mambo ya nje wala asimwamini mwenye kutegeneza maneno matamu. Kwa sababu wafisadi ni mabingwa wa kazi hiyo na kazi ya ria. Kwa hivyo ni juu yetu kutomtegemea yeyote isipokuwa baada ya kufanya majaribio na kupatikana dalili ya ukweli wake na usafi wake.
Hiyo ndiyo asili ya ujumla inayoenea katika hukumu nyingi za dini na za kidunia; kama kuchagua Hakimu, Kadhi, Naibu, Kadhi, Mufti na kila anayesimamia masilahi ya Umma. Ajabu ya maajabu ni kutakiwa shahada ya kielimu tu kwa mwenye kujitokeza kwa kazi muhimu ya mji au nchi na inayogusa maisha ya watu. Lakini haulizwi uaminifu wake na tabia yake, pamoja na kuwa hayo ndio msingi. Wengi wenye shahada wanazitumia kuwa ni zana za kuibia.
Na katika watu kuna ambaye kauli yake inakupendeza hapa duniani, naye humshuhudia Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo moyoni mwake, na hali ni hasimu mkubwa kabisa.
Yaani wanadhihihirisha mapenzi na heri na hali wao ndio maadui zaidi wa heri na watu wa heri.
Na anapotawala hufanya bidii katika ardhi kufanya ufisadi.
Wamehitaliafiana wafasiri kuhusu neno Tawalla. Je makusudio ni kuondoka na maana yake kuwa ni, anapoondoka kwa yule aliyemdanganya, huhangaika katika ardhi kwa ufisadi. Au kwamba makusudio ni kutawala na usultani, na maana yawe, na atakapokuwa mtawala atafanya wanayoyafanya watawala waovu ya kuangamiza mimea na viumbe? Mwenye Tafsir Al manar amenakili kutoka kwa Ustadha wake Sheikh Muhammad Abduh kwamba ameyapa nguvu maana ya utawala kwa kuunganisha na kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):
"Na anapoambiwa mche Mwenyezi Mungu, hupandwa na mori wa kufanya dhambi."
Kwa maana ya kuwa mtawala mkaidi anakuwa na kiburi kuongozwa kwenye maslahi au kupewa tahadhari ya mambo ya ufisadi, yeye hujiona yuko juu ya haki; kama vile alivyo juu ya watu wake anaowatawala, basi itawezekanaje kwa mtu kumwambia amwogope Mwenyezi Mungu.
Na huangamiza mimea na viumbe.
Mimea ni kilimo na viumbe ni wanyama. Makusudio ni maslahi yote ya kiuchumi katika kilimo, viwanda na ufugaji, mali ghafi, na mengineyo yanayohusika na uhai wa watu na maisha yao. Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja kilimo na ufugaji kwa vile viwanda wakati huo havikuwa na umuhimu wowote kama ilivyo sasa. Uharamu wa mambo hayo kwa mtazamo wa Uislamu ni sawa na uharamu wa kumwaga damu; na mwenye kukusudia ubaya katika vitu hivyo, ndio amekusudia ubaya wa utu hasa; hata kama vitu hivyo ni milki ya adui anayepiga vita Waislamu. Mtume(s.a.w.w)
amekataza kukata miti, kuharibu mimea na majengo na kutia sumu miji ya washirikina siku za vita, n.k. Lau tunailinganisha sharia ya Kiislamu na mambo yanayofanywa leo na dola za kikoloni na vita vyao vya silaha za kemikali kwenye mimea, watu na wanyama, na kuitia sumu anga kwa mabomu ya Atomic na kuyatupa kwa wanawake na watoto, lau hayo yote tunayaunganisha na Uislamu, basi tutajua huruma, uadilifu na utu wa Uislamu na unyama wa dola za Magharibi na jinsi zilivyopetuka mipaka katika dhulma na unyang'anyi.
Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hapendi ufisadi.
Hakuna uharibifu mkubwa zaidi kuliko kuzusha vita na kutumia silaha zenye kubomoa ili kuwatawala watu na kuwanyang'anya chakula na matunda ya jasho lao.
Na anapoambiwa mche Mwenyezi Mungu hupandwa na mori wa kufanya dhambi.
Mtu mwema wenye ikhlasi anakubali masahihisho na nasaha, bali huzitafuta na kuzikaribisha, kwa sababu yeye hana lengo jengine zaidi ya haki, wala hatafuti sifa; kwa sababu amali yake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) sio umashuhuri.
Imam Amirul Muminin
anasema katika maneno anayowasifu wanaomcha Mwenyezi Mungu:"Hawaridhii na amali zao chache wala hawakioni kingi kilicho kingi; wao wanajituhumu na wao ni wenye kunyenyekea katika amali zao."
Katika hotuba yake siku za ukhalifa wake alisema: "Mtu hata kama ana cheo kikubwa katika haki na fadhila kubwa katika dini hawezi kuwa hahitajii kusaidiwa katika aliyobebeshwa na Mungu katika haki zake; wala si mwenye kutaka kujitukuza; wala mtu hata kama nafsi zinamfanya mdogo na kudharauliwa na macho sio kuwa hawezi kusaidia au kusaidiwa... Wala msinidhanie kuwa mimi ni mzito katika haki nitakayoambiwa, kwani mwenye kuifanya nzito haki atakayoambiwa au uadilifu atakaoonyeshwa, basi kwake kuitumia haki na uadilifu ni kuzito zaidi."
Hivyo ndivyo anavyotakikana mwanachuoni mwenye ikhlasi ya kweli. Ama mnafiki mwenye hiana, haki inakuwa nzito juu yake kwa sababu itamfedhehesha; na hununua sifa kwa thamani kubwa ili azibe upungufu wake na uovu wake.
Na katika watu yuko auzaye nafsi yake kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu.
Yaani baadhi ya waumini wanaikabili Jihadi na wanapenda mauti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. sawa na wale wengine wanaopenda uhai. Hawana lengo jengine isipokuwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na thawabu Zake. Razi katika kutafsiri Aya hii anasema kuhusu sababu za kushuka kwake kuwa kuna riwaya tatu; Mojawapo ni kwamba Aya hii imeshuka kwa sababu ya Ali bin Abi Twalib
alipolala kwenye kitanda cha Mtume wakati wa Hijra, alisimama Jibril kichwani mwake, Mikail miguuni mwake na Jibril: Pongezi! Pongezi! ewe Ali akisema: Mwenyezi Mungu anajionea fahari kwako, mbele ya Malalika( [7]
).
﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ﴾
208.Enyi mlioamini! Ingieni katika usalama nyote, wala msifuate nyayo za Shetani. Kwa hakika yeye kwenu ni adui wa wazi.
﴿ فَإِن زَلَلْتُم مِّن بَعْدِ مَا جَاءَتْكُمُ الْبَيِّنَاتُ فَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴾
209.Na kama mkiteleza baada ya kuwafikia ubainifu, basi jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
﴿ هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن يَأْتِيَهُمُ اللَّـهُ فِي ظُلَلٍ مِّنَ الْغَمَامِ وَالْمَلَائِكَةُ وَقُضِيَ الْأَمْرُ وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ ﴾
210.Hawangoji ila kuwafikia (adhabu ya) Mwenyezi Mungu katika vivuli vya mawingu na Malaika, na liishe jambo; na mambo yote hurudishwa kwa Mwenyezi Mungu.
INGIENI KATIKA USALAMA NYOTE
Aya 208 - 210
MAANA
Enyi Mlioamini! Ingieni katika usalama nyote.
Imesemekana kuwa makusudio ya neno Silmi hapa ni Uislamu, na kwamba msemo unawaelekea wanafiki ambao wameificha kufuru na kudhihirisha Uislamu. Na imesemekana kuwa msemo unawaelekea wenye kumwamini Mwenyezi Mungu katika Ahlul Kitab ambao hawakusilimu. Na ikasemekana kuwa unawaelekea Waislamu wote kwa hivyo maana yake yanakuwa ni kumtii Mwenyezi Mungu na kumnyenyekea katika hukumu Zake zote sio baadhi. Na pia imesemekana maana yake ni suluhu kwa maana kuwa ingieni katika suluhu nyote. Tuonavyo sisi ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemwamrisha mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu, kwa imani sahihi kuingia katika lile ambalo lina salama yake ya dunia na akhera. Na njia ya usalama inajulikana na wote, nayo ni kusaidiana, kuungana, na kuacha vita na uhasama. Vile vile kuyashinda matamanio na kuwa na ikhlasi katika kauli na vitendo.
Makusudio ya maneno hayo yanatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu:Wala msifuate nyayo za shetani. Kwa hakika yeye kwenu ni adui wa wazi,
Aliyoileta mara tu, baada ya kusema.Ingieni katika usalama nyote.
Hapo Mwenyezi Mungu amezingatia kuwa nyayo za shetani kinyume chake ni usalama; na amemweka mtu mbele ya mambo mawili tu, hakuna la tatu; Ama kuingia katika usalama au kufuata nyayo za shetani ambazo ndio dhati ya uovu, ugomvi, shari na ufisadi.
Na kama mkiteleza baada ya kuwafikia ubainifu, basi jueni ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye hekima.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuamrisha kuingia katika usalama na kukataza kufuatwa nyayo za shetani, amemhadharisha yule atakayehalifu amri yake na makatazo yake na akatishia kwa kusema: "Basi jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye hekima." Mwenye nguvu, hashindwi katika amri Yake wala hakimzuwii chochote kwa alilokusudia kulifanya. Mwenye hekima, humlipa mema mtiifu na humwadhibu mwasi. Razi anasema: "Huo ndio ukomo wa kiaga kwa sababu ni kuhofisha bila ya kutaja adhabu. Huenda mzazi akamwambia mtoto wake: "Ukiniasi basi wewe wanijua na wajua uwezo wangu kwako", basi maneno hayo yanakuwa ni makemeo ya ufasaha zaidi kuliko kutaja kipigo na mengineyo.
Hawangoji ila kuwafikia (adhabu ya) Mwenyezi Mungu katika vivuli vya mawingu na Malaika. Maana kwa ujumla ni kwamba wale wenye kukadhibisha na wakaasi watajiwa na adhabu kwa ghafla wala hawataokoka. Aya iko katika mwelekeo wa Aya inayosema:
﴿
فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَن تَأْتِيَهُم بَغْتَةً ﴾
"Na hawangoji ila saa ya Kiyama kiwajie kwa ghafla...?"
(47:18).
Na lishe jambo; na mambo yote hurudishwa kwa Mwenyezi Mungu. Mauti ambayo hapana budi nayo, yakija na Kiyama kikija, kila kitu kitakuwa kimekwisha na hapatabakia mbele ya wenye makosa isipokuwa hisabu na mateso.
SIRI NA MATUKIO YA GHAFLA
Hakuna yeyote ajuaye yatakayomtokea mbele na siri ya wakati, heri au shari. Hawezi kuyajua hayo vyovyote atakavyokuwa na elimu au imani:
"Na nafsi yoyote haijui itachuma nini kesho."
(31:34)
Mara nyingi mtu hujiwa na heri kwa ghafla wakati yeye anatazamia kupata shari; na hujiwa ghafla na shari wakati anapotazamia heri. Hakuna kitu kinachotia uchungu kama hicho cha kupata shari wakati wa kutazamia heri; kama vile ambavyo hakuna kitu kitamu kama kupata heri wakati wa kutazamia shari. Mwenye akili hawezi kughurika na alivyo navyo, bali hufikiria mzunguko wa zama; kama vile ambavyo hakati tamaa na lolote linalompata; kwani dunia inageuka milele; ndio maana ikasemwa; "Kudumu hali ni muhali na faraja inakuja kutokana na dhiki." Imam Ali
anasema:"Baada ya dhiki ni faraja.
Anaendelea kusema Imam:"Hakika Musa bin Imran alitoka kuwatafutia watu wake moto akasemeshwa na Mwenyezi Mungu na akarudi akiwa Mtume."
Mwenyezi Mungu anasema:
﴿ إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ ﴾
"...Hawakati tamaa ya rehema ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu makafiri."
(12:87).
Na amesema tena:
﴿ فَلَا يَأْمَنُ مَكْرَ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْخَاسِرُونَ ﴾
... Hawajiaminishi na mipango ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara."
(7:99).
Imeelezwa katika vitabu vya Historia na Sera kwamba Ibn Ziyat alikuwa waziri na mtu wa kutegemewa na Mu'utasim, naye alikuwa ni katika mataghuti wa hali ya juu na dhalimu mkubwa. Alitengeneza tanuri la chuma alilolijaza misumari yenye ncha pambizoni mwake. Anapomkasirikia mtu humtupa ndani, kila anavyojitingisha ndivyo misumari inavyomwingia mwilini mwake. Mutawakkil alipotawala alimshika Ibn Ziyat na akamfunga kwa chuma mikononi mwake na miguuni mwake kisha akamtupa katika tanuri hilo, na baadaye akafa. Kabla ya kufa alisikika akiimba shairi hili: Sifazake tulia, hebu nenda pole pole, Kigeugeu dunia, huenda nyuma na mbele.
﴿ سَلْ بَنِي إِسْرَائِيلَ كَمْ آتَيْنَاهُم مِّنْ آيَةٍ بَيِّنَةٍ وَمَن يُبَدِّلْ نِعْمَةَ اللَّـهِ مِن بَعْدِ مَا جَاءَتْهُ فَإِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴾
211.Waulize wana wa Israil, ishara ngapi zilizo wazi tulizowapa? Na anayezibadilisha neema za Mwenyezi Mungu baada ya kumfikia, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
﴿ زُيِّنَ لِلَّذِينَ كَفَرُوا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا وَيَسْخَرُونَ مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ اتَّقَوْا فَوْقَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَاللَّـهُ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴾
212.Wamepambiwa makafiri maisha ya duniani, na wanawafanyia maskhara wale walioamini. Na wale wenye takua watakuwa juu yao Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila hisabu
WAULIZE WANAWA ISRAIL
Aya 211 – 212
MAANA
Waulize wana wa Israil, ishara ngapi zilizo wazi tulizowapa?
Makusudio ya waulize hapa sio swali hasa la kihakika, kwa sababu Mtume(s.a.w.w)
anajua hali zao, wala makusudio sio kuelezea hali waliyokuwa nayo; kama ilivyo katika Aya ya 49 na inayofuatia. Isipokuwa makusudio hasa ni kuwa Waislamu wazingatie na wapate funzo na hali ya Waisrail. Njia ya kupata funzo ni kuwa Waisrail walijiwa na Mtume Musa
kwa miujiza na hoja ambayo ni mkono kuwa mweupe, fimbo kugeuka nyoka na kupasuka bahari. Vile vile kufunikwa na wingu, kuteremshiwa Manna na Salwa na jabali kutoka maji. Pamoja na hayo yote waliasi na kukhalifu, ndipo Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa madhila na utwevu katika dunia na adhabu iumizayo katika Akhera. Na Waislamu nao wamejiwa na Muhammad(s.a.w.w)
kwa miujiza na hoja zinazofahamisha ukweli wa Utume wake na kuswihi sharia yake; naye akawafikilizia habari kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuwa waaingie katika Uislamu wote, kwani humo watapata heri na utengeneo wao; kama wakiasi kama walivyofanya Waisrail, basi yatawapata yaliyowapata Waisrail.
Na anayezibadilisha neema za Mwenyezi Mungu baada ya kumfikia, basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
Makusudio ya neema hapa ni dalili za haki, kwani hizo ni katika neema kubwa. Kwa sababu ndani yake mna uongofu na kuokoka na kuhiliki na upotevu. Makusudio ya kuzibadilisha ni kuziasi na kuziharibu. Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.)Na anayezibadilisha neema za Mwenyezi Mungu baada ya kumfikia
ni sawa na kauli yake:
﴿ فَإِن زَلَلْتُم مِّن بَعْدِ مَا جَاءَتْكُمُ الْبَيِّنَاتُ﴾
"Na kama mkiteleza baada ya kuwafikia ubainifu..."
(2:209).
Vile vile kusema kwake:
﴿فَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴾
"Basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu"
(2:209) ni sawa na kusema Kwamba:Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye hekima."
Maana ni moja na lengo ni moja.
HAPANA IMANI BILA TAKUA (UCHA MUNGU)
Wamepambiwa makafiri maisha ya duniani.
Hapana tofauti kati ya mwenye kukanusha kuwapo Mwenyezi Mungu na yule mwenye kuamini kinadharia tu, lakini matendo yakawa ni tofauti. Hapana tofauti kati ya wawili hao. Kwa sababu kila mmoja ameathiriwa na dunia na vipambo vyake, ameathirika na kitu cha sasa hivi kuliko cha muda ujao; heri na manufaa ameyapima kwa kiwango cha manufaa yake, wala hakupima na mambo aliyoharamisha Mwenyezi Mungu wala na msimamo wa kibinadamu. Mimi kila ninavyozidi kuzama katika tafsiri ya Qur'an na kuangalia kwa undani Aya zake, basi huwa na yakini zaidi kwamba imani bila ya ucha Mungu haina maana yoyote; na kwamba kila anayeiangalia dunia kuwa ndio makusudio yake yote, basi atakuwa ameiweka mbali sharia ya haki na dini, atake asitake.
Imekuja Hadith Mutawatir kutoka kwa Mtume Mtukufu akisema: "Dunia na akhera zina madhara" yaani zinadhuriana kuhujumu moja yao nikuiacha nyingine( [8]
).
Imam Ali
anasema: "Hakika dunia na Akhera ni maadui wawili wanaotofautiana, na ni njia mbili tofauti. Mwenye kuipenda dunia ataichukia akhera na kuwa adui yake; zote mbili ni kama Mashariki na Magharibi, mwenye kutembea kati yao huwa mbali na nyingine kila anapokaribia moja wapo.
" Na wanawafanyia maskhara wale walioamini.
Ni kawaida wale wanaozichezea Hoja za Mwenyezi Mungu na hukumu zake wakihalalisha damu na mali ya haramu kuwadharau na kuwachezea wale wanaojilinda na maharamisho na kuvumilia tabu na mashaka kwa ajili ya kumridhisha Mungu.
Na wale wenye takua watakuwa juu yao siku ya Kiyama.
Amesema wenye takua wala hakusema wale walioamini, kwa sababu imani bila takua si lolote; kama tulivyobainisha. Maana yako wazi ni kuwa makafiri wakiwadharau waumini hivi sasa, basi mambo yatabadilika kesho. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿قَالَ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ إِنَّ الْخِزْيَ الْيَوْمَ وَالسُّوءَ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴾
"...Watasema walio pewa ilimu: Hakika hizaya na ubaya leo itawafika makafiri."
(16:27).
﴿فَالْيَوْمَ الَّذِينَ آمَنُوا مِنَ الْكُفَّارِ يَضْحَكُونَ ﴾
"Basi leo wale ambao wameamini wanawacheka makafiri."
(83:34)
Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila hisabu.
Riziki ni mbili ya dunia na riziki ya Akhera. Riziki ya dunia inajulikana na riziki ya Akhera, ni neema isiyokatika na isiyokuwa na chembe ya huzuni au hofu. hataipata yeyote isipokuwa kwa imani na amali njema: Anasema Mwenyezi Mungu:
﴿وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴾
"Na wale walioamini na kutenda mema, hao ndio watu wa Peponi, humo watakaa milele."
(2:82).
Kila mtu anaweza kupata riziki duniani, awe ni kafiri au Mumin, mwema au mwovu, na anayehangaika au asiyehan-gaika; kama vile urithi, zawadi, wasiya, n.k. Vile vile inaweza kupatikana kwa njia ya halali, au haramu, kama vile kunyang'anya, kughushi na utapeli. Mwenye Tafsir Al-Manar amenakili kutoka kwa mwalimu wake Sheikh Muhammad Abduh kwamba, amesema wakati wa kutafsiri Aya hii, kwamba riziki bila ya kuhangaika inaweza ikapatikana kwa baadhi ya watu. Ama kwa Umma ni muhali kujitosheleza isipoku-wa kwa kuhangaika na kufanya kazi. Huo ni ukweli ulio wazi kabisa.